Primary Questions from Hon. Halima James Mdee (20 total)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Serikali ilitoa kauli kuwa itapanga gharama za karo elekezi kwa shule zote za binafsi hapa nchini:-
(a) Je, Serikali imegundua kiwango cha gharama kwa kila mwanafunzi (unit cost) kwa shule za bweni na za kutwa ni kiasi gani?
(b) Je, kiwango hiki hakitasababisha kuporomoka kwa ubora wa elimu ambayo ilikuwa ikitolewa hapo awali na shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imefanya utafiti kuhusu gharama za kumsomesha mwanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari. Kupitia utafiti huo, imebainika kuwa ada zinazotozwa katika shule za binafsi zinatofautiana kwa kiasi kikubwa kulingana na huduma zinazotolewa, aina ya shule na miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utafiti huo, Wizara yangu ilifanya mazungumzo na baadhi ya taasisi zinazosimamia shule zisizo za Kiserikali na kukubaliana namna ya kufikia viwango vya ada elekezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi ambazo tumefanya nazo mazungumzo ni pamoja na Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Kamisheni ya Huduma za Jamii za Kikristo (CSSC) na Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA). Kutokana na tofauti za ubora na idadi ya huduma zinazotolewa na shule, Wizara sasa imeanza zoezi la kupanga shule hizi kwa makundi ili kuweka viwango vya ada kwa kuzingatia ubora na huduma na hivyo kutoathiri kiwango cha elimu inayotolewa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatarajia kuwa utaratibu wa ada elekezi hautaathiri ubora wa elimu katika shule binafsi kwa sababu ada hiyo itapangwa kulingana na ubora na huduma na miundombinu iliyopo shuleni.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Serikali iliwaahidi wananchi wa Jimbo la Kawe kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba na barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill – Madale:-
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba pamoja na barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill - Madale Goba ni kati ya barabara ambazo zimo kwenye mpango wa Serikali wa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ambao utekelezaji wake ulianza mwaka 2010 na unagharamiwa na Serikali za Tanzania kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo ujenzi wa kiwango cha lami umekamilika ni Ubungo Bus Terminal - Kigogo Roundabout ambayo ni kilomita 6.4, Ubungo Maziwa - Mabibo External kilomita 0.65 na Jet Corner - Vituka - Davis Corner ambayo ni kilomita10.3. Aidha, barabara zinazoendelea kujengwa ni pamoja na Tangibovu - Goba kilomita 9, Kimara Baruti - Msewe - Changanyikeni kilomita 2.6, Kimara - Kilungule - External kilomita 9 na Tabata Dampo - Kigogo kilomita 2.25.
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu wa kina wa barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill -Madale - Goba na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi umekamilika. Aidha, usanifu wa kina wa barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba utafanyika sambamba na ujenzi wa barabara hiyo yaani design and build.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara za Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba na Tegeta Kibaoni - Wazo Hill - Madale - Goba umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Jimbo la Kawe ni miongoni mwa Majimbo ambayo (baadhi ya maeneo) yamekuwa yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama kwa kipindi kirefu ambayo ni Kata ya Mabwepande (Mtaa wa Mbopo, Mabwepande na Kinondo), Kata ya Makongo (Mtaa wa Changanyikeni na baadhi ya maeneo ya Mtaa wa Makongo Juu), Kata ya Wazo, Mbweni na Mbezi Juu; na changamoto hii sugu ilitarajiwa kupungua na kumalizika kabisa baada ya mradi mkubwa wa maji wa Ruvu chini kukamilika ambao kwa sasa tayari umeshakamilika:-
(a) Je, mikakati ya usambazaji maji pamoja na Mabomba (katika maeneo ambayo hayana mtandao wa mabomba) ikoje ili kutatua kero husika?
(b) Je, ni miradi gani inayotarajiwa kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Chini umekamilika na umeanza kutumika rasmi tarehe 23 mwezi Machi, 2016. Mradi huu ulihusu upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa Bomba kuu kutoka Ruvu Chini kwenda Dar es Salaam. Hivi sasa uzalishaji wa maji kutoka Ruvu Chini ni mita za ujazo milioni 270 kwa siku ikiwa ni ongezeko la mita za ujazo milioni 90 kwa siku. Kutokana na kukamilika kwa mradi huu, kumekuwa na ongezeko la upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa hayapati maji licha ya kuwa na mabomba ya DAWASCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Kwanza, Serikali inatekeleza mradi wa uboreshaji na usambazaji wa maji unaogharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 32.772 kutoka Benki ya Exim-India. Katika Jimbo la Kawe la Mheshimiwa Mbunge, mradi huu utatekelezwa katika maeneo ya Changanyikeni, Makongo, Salasala, Wazo, Tegeta, Ununio, Bunju na Mabwepande. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kusukumia maji katika Kata ya Mabwepande na matanki ya kuhifadhia maji katika Kata za Makongo na Wazo pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA).
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Barabara mpya ya Mwenge - Tegeta kwa kiwango fulani imesaidia kupunguza tatizo la foleni ingawa ina changamoto kadhaa kama kukosekana kwa taa za kuongoza magari kunakosababisha ajali za mara kwa mara; nyakati za mvua barabara hujaa maji sababu ya udogo wa mapokeo na matoleo ya maji ya mvua hususan eneo la Makonde - Mbuyuni hali inayohatarisha uhai wa wananchi na barabara yenyewe; kuna maeneo hatarishi sana ambayo Serikali inatakiwa ama kuweka matuta au vivuko vya waenda kwa miguu ili kuzuia ajali, miongoni mwa maeneo hayo ni eneo la Bondeni (Jeshini Kata ya Mbezi Juu) karibu na njia panda ya kwenda Kawe:- Je, ni lini changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu wa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara zetu ili kusaidia kupunguza ajali hususan barabara ya Mwenge -Tegeta. Mkandarasi wa ujenzi wa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya Afrikana tayari amepatikana na anatarajia kuanza kazi wakati wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu udogo wa mapokeo na matoleo ya maji ya mvua yanayosababisha kero katika eneo la Makonde hadi Mbuyuni, Serikali inakamilisha taratibu za kusaini mkataba wa ujenzi wa mtaro mkubwa eneo la Mbezi Samaki Wabichi ambao utatatua kero ya barabara kujaa maji nyakati za mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Kawe Bondeni hadi Jeshini, Kata ya Mbezi Juu na Kawe tayari limeshapatiwa ufumbuzi. Serikali itajenga daraja la juu kwa ajili ya kivuko cha waenda kwa miguu (Over- Head Pedestrian Bridge) eneo la Kawe Bondeni. Kwa sasa mkandarasi wa kujenga daraja hilo yupo kwenye hatua za maandalizi (mobilization) kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu sana unaohusu eneo lenye ukubwa wa ekari 357.5 Boko Dovya – Kawe – Kinondoni baina ya wananchi na watu wanaojitambulisha kuwa wamiliki halali wa eneo hilo maarufu kama SOMJI; wananchi katika hatua mbalimbali wamepeleka malalamiko Serikalini kuanzia ngazi ya Wilaya, Wizara ya Ardhi na hata kwa Waziri Mkuu lakini mpaka sasa hakuna utatuzi uliofanyika.
Je, hatua gani zimeanza kuchukuliwa ili kero hiyo ya muda mrefu imalizike?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali namba 17 la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali shamba hili lililokuwa na ukubwa wa ekari 366 Mbweni maarufu kama Somji Farm lilipimwa na upimaji namba E7/37F na kupewa namba ya upimaji 10,917 ya tarehe 15 Agosti, 1959. Baada ya upimaji shamba lilimilikishwa kwa Ndugu Hussein Somji pamoja na Ndugu Munaver Somji mwaka 1961 na baadae kuandaliwa hati iliyosajiliwa kwa namba 14,573 ya kipindi cha miaka 99.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya shamba hilo, ekari 5.8 zilitwaliwa kwa matumizi mahususi ya Serikali mwaka 1975 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 670 la tarehe 30 Mei, 1975. Aidha, sehemu iliyobaki yenye ekari 357.5 ilitwaliwa na Serikali tena mwaka 2002 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 617 la tarehe 27, Septemba, 2002 kwa ajili ya kutumika katika mradi wa viwanja 20,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo eneo hilo halikuingizwa kwenye mradi kutokana na sehemu kubwa kuwa imevamiwa na wananchi. Pamoja na uvamizi huo, wamiliki wa awali walifungua mashauri mahakamani dhidi ya Serikali kupinga eneo lao kutwaliwa; shauri la Kikatiba namba moja la 2003 na shauri la Kikatiba namba 40 la 2010. Uwepo wa mashauri haya ulikwamisha juhudi za Serikali kushughulikia mgogoro huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni mara kadhaa imekaa na wahusika kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha wamiliki wa awali kulipwa fidia stahiki kwa fedha iliyopatikana kutokana na wanachi ambao watatakiwa kurasimishiwa maeneo waliyojenga.
Hata hivyo changamoto iliyopo ni katika kumilikisha makubaliano haya kwa wananchi kupitia kamati yao waliyounda, kutokuwa tayari kuchangia gharama za kurasimisha eneo hilo. Jitihada zaidi za wadau wengine akiwemo Mbunge zinahitajika katika kuwaelimisha wananchi kupitia Kamati yao kuwa tayari kushiriki katika upatikanaji wa ufumbuzi wa suala hili.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Baadhi ya maeneo katika Jimbo la Kawe yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama kwa kipindi kirefu. Maeneo kama Kata ya Mabwepande (Mtaa wa Mbojo, Mabwepande, Kinondo); Kata ya Makongo (Mtaa wa Changanyikeni na baadhi ya maeneo ya Mtaa wa Makongo Juu); Kata ya Wazo, Mbweni na Mbezi Juu na changamoto hii sugu ilitarajiwa kupungua na kumalizika kabisa baada ya mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Chini kukamilika ambao kwa sasa tayari umeshakamilika.
• Je, mikakati ya usambazaji maji pamoja na mabomba katika maeneo ambayo hayana mtandao wa mabomba ikoje ili kutatua kero husika?
• Je, ni miradi gani inayotarajiwa kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam hususan maeneo ambayo hayakuwa na mtandao wanaondokana na kero ya kutopata huduma ya maji, Serikali katika awamu ya kwanza kupitia DAWASA inakamilisha ujenzi wa matanki na mabomba makuu ya kupeleka maji katika maeneo ya miinuko ya Changanyikeni, Wazo na Salasala. Aidha, awamu hii pia itahusu ujenzi wa mtandao wa maji Kata ya Kiluvya na Mbezi Luisi. Mradi huu unatekelezwa chini ya ufadhili wa mkopo wa masharti nafuu kutoka India kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 32.772. Hadi sasa utekelezaji wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 82 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya utekelezaji itahusu ujenzi wa mabomba madogo madogo ya kusambaza maji na kuunganisha wateja katika maeneo yote kuanzia Changanyikeni, Bunju hadi Bagamoyo. Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanzia mwezi Julai, 2018 na unatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya dola za Marekani milioni 45. Mradi huu utatekelezwa kwa miezi 15. Zabuni ya ujenzi wa mradi huo itatangazwa hivi karibuni baada ya kupata kibali kutoka Benki ya Dunia.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Mwezi Novemba, 2018, Rais aliutangaza ulimwengu kwamba Serikali yake itanunua korosho zote kwa bei isiyopungua shilingi 3,000/= kwa kilo.
(a) Je, mpaka sasa ni kiasi gani kimetumika na kimetoa chanzo kipi na je, tani ngapi zimenunuliwa?
(b) Je, Wakulima/Vyama vya Msingi vingapi vimelipwa na vingapi bado havijalipwa?
(c) Je, zoezi hilo linatarajiwa kukamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, makadirio ya uzalishaji wa korosho msimu wa 2018/2019 ni zaidi ya tani 240,000 za korosho ghafi. Hadi kufikia tarehe tarehe 30 Januari, 2019, Serikali imekusanya jumla ya tani 214,269.684 za korosho ghafi zenye thamani ya Sh.707,089,957,200 sawa na asilimia 89.3 ya lengo la uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, ununuzi wa korosho unafanywa na Taasisi ya Serikali ya Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko ambapo malipo yaliyolipwa na kuingizwa kwenye akaunti za wakulima hadi tarehe 30 Januari, 2019 ni kiasi cha Sh.424,849,405,110 zilizotokana na korosho za wakulima kiasi cha tani 134,535,904. Aidha Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko ni Taasisi ya kibiashara yenye lengo la kupata faida na mtaji wake unatokana na ruzuku kutoka Serikali na mikopo kutoka Taasisi kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), NMB, CRDB na Benki zinginezo.
(b) Mheshimiwa Spika, jumla ya wakulima laki 390,466 wamekwishalipwa hadi kufikia tarehe 30 Januari 2019. Aidha Vyama vya Msingi 603 vimelipwa kati ya Vyama vya Msingi 605 vilivyohakikiwa.
(c) Mheshimiwa Spika, zoezi la operesheni korosho linaendelea vizuri na linatarajia kukamilika ifikapo tarehe 15 Februari, 2019.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo sugu la uchimbaji mchanga na uchafu uliokithiri;
Je, Serikali ina mikakati gani ya muda mfupi na muda mrefu kukabiliana na kero hiyo sugu na hatarishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako naomba kwanza nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa George Simbachawene kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini pia Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Maziringira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna changamoto kubwa ya uchimbaji wa mchanga Dar es Salaam. Aidha, yapo machimbo ya mchanga yaliyoruhusiwa kisheria na kupata vibali kutoka mamlaka husika kama Serikali za Mitaa (Halmashauri za Jiji na Manispaa), Ofisi za Mamlaka ya Mabonde na Wizara ya Madini. Hata hivyo, upo uchimbaji holela hususan katika maeneo ya mito na machimbo mengine ya mchanga ambayo si rasmi yanayoanzishwa na wananchi katika maeneo mbalimbali. Uchimbaji wa madini ya mchanga usio rasmi ni kosa kwa mujibu wa Kifungu 6 (1) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji huu huleta athari ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa kingo za mito, uharibifu wa maji na miundombinu, mwingiliano wa maji ya bahari katika nchi kavu (sea water intrusion), kubadilika kwa mkondo wa mto kutoka uelekeo wa asili, kuharibika kwa uimara wa mto (channel instability), uharibifu wa mimea ya asili ambayo husaidia kupunguza mmomonyoko na uharibifu wa mazalia ya viumbe hasa wakati kina cha maji kinapoongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hili hatua zifuatazo zinachukuliwa:
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kuelimisha wananchi kuhusu athari za uchimbaji holela wa mchanga na kuzuia uchimbaji holela. Aidha, mamlaka mbalimbali zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mamlaka za Mabonde na Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Madini Mkoa wa Dar es Salaam zimekuwa zikifanya ukaguzi wa mara kwa mara na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria
huchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, Serikali inaandaa mkakati wa muda mrefu utakaotokana na Mapendekeo ya Kamati Maalum ya Wadau iliyoundwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuwa na uchimbaji endelevu wa mchanga usiokiuka sheria za nchi; na kufanya tafiti na kuendeleza teknolojia za ujenzi zinazoweza kutumia mchanga kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchafuzi wa mazingira uliokithiri, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu 139(1) imetoa mamlaka kwa Serikali za Mitaa kuzuia au kupunguza taka ngumu, taka vimiminika, gesi taka na taka zenye madhara. Serikali itaendelea kuelimisha wananchi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia programu ya Elimu kwa Umma inatoa elimu kuhusu usimamizi na udhibiti wa taka kuanzia ngazi ya jamii, viongozi na wadau hasa katika eneo la urejelezaji wa taka ngumu. Natoa wito kwa Serikali za Mitaa kuwajibika kwa kuweka mipango endelevu na usimamizi wa taka kama ilivyobainishwa katika Kifungu 139(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
(a) Je, ni nini sababu ya kuweka tozo ya ada ya tathmini ya asilimia moja kwa mkopaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambapo asilimia 50 inalipwa kabla ya kuanza kufanya tathmini na asilimia 50 inalipwa baada ya mkopo kuidhinishwa?
(b) Je, ni kigezo gani kilisababisha tozo kuwa asilimia 1 na si vinginevyo?
(c) Je, mkopo usipoidhinishwa hiyo asilimia 50 ya asilimia moja iliyolipwa inarudishwa ama la?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ada ya tathmini ya mikopo inayotozwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania ni kwa ajili ya kulipia gharama za uchambuzi wa maombi ya mkopo ambayo ni pamoja na shajara, uhakiki wa mradi pamoja na dhamana ya mkopo.
(b) Mheshimiwa Spika, kigezo kinachotumika kutoza ada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo ni gharama halisi za uchambuzi wa maombi ya mkopo zinazotokana na nguvu ya soko kwa wakati husika. Aidha, utaratibu huu ni wa kawaida kwa taasisi za fedha kutoza ada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo.
(c) Mheshimiwa Spika, endapo mkopo hautaidhinishwa, asilimia 50 ya asilimia moja iliyolipwa huwa hairejeshwi kwa mwombaji wa mkopo kwa kuwa kiasi hicho kinakuwa kimetumika kulipia gharama za uchambuzi wa mkopo.
MHE. FELISTA D. NJAU K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Je, nini kimepelekea mkwamo wa mkakati wa ujenzi wa Mji mpya wa Kawe kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na lini mradi huo utaendelea?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwezi Agosti, 2013, Baraza la Mawaziri kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, hususani thamani ile ya ardhi katika eneo la Kawe, ilitoa kibali kwa Shirika la Nyumba la Taifa ili eneo hilo ambalo lilikuwa eneo la Kiwanda cha Tanganyika Packers liendelezwe kuwa mji wa pembezoni (satellite town) na uendelezaji huo ufanyike kwa njia ya ubia kati ya NHC na Kampuni ya Al Ghurair Investments. Kazi zilizoanza kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa miradi miwili ya makazi na biashara yani Golden Premier na Kawe 711 ambayo kwa sasa imesimama ikiwa imefikia asilimia 43 kwa Golden Premier pamoja na asilimia 38 kwa mradi wa Seven Eleven (711).
Mheshimiwa Spika, mkwamo wa utekelezaji wa miradi ya Golden Premier pamoja na Kawe Seven Eleven (711) umesababishwa na uhaba wa fedha uliotokana na Shirika la Nyumba la Taifa kufikia kikomo cha idhini ya kukopa iliyotolewa na Serikali kabla ya mradi wake kukamilika. Hali hii ilitokana na Shirika kuwa na miradi mingi sana kwa wakati mmoja ambayo yote ilitegemea vyanzo vilevile vya mkopo kwa ajili ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, ili kuikwamua miradi hii, Shirika limefanya juhudi mbalimbali ili kupata fedha kupitia vyanzo vingine zaidi ya mikopo. Hata hivyo, Shirika tayari limeanza mpango huu wa kukwamua kwa kumalizia Mradi wa Morocco Square, ambao unakadiriwa kukamilika kufikia mwisho wa mwaka huu 2021. Ukamilishaji wa ujenzi wa mradi wa Golden Premier pamoja na Kawe Seven Eleven (711) unategemea kuanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Je, uwepo wa Kiwanda cha kuua mazalia ya Mbu (Tanzania Biotech Product Limited) umesaidia vipi mapambano dhidi ya Malaria nchini?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hawapo, inakuwa shida sana kuwaona mpaka uvae miwani ya x-ray. (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lilikuwa linauliza je, uwepo wa kiwanda cha kuua mazalia ya mbu kimesaidia vipi mapambano dhidi ya malaria nchini? Tangu Kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited kuanza uzalishaji mnamo mwaka 2016, jumla ya lita 340,520 za viuadudu zimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 ambazo ni wastani wa shilingi 13,200/= kwa lita. Lita hizi za viuadudu zilisambazwa katika Mikoa 28 na kuzifikia Halmashauri zote 185 nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi hizi ziliungana pamoja na utekelezaji wa afua zingine za udhibiti wa malaria zikiwemo matumizi ya vyandarua, kupulizia viatilifu - ukoko ndani ya nyumba hasa kwenye maeneo yenye kiasi kikubwa cha maambukizi ya malaria na uwepo wa vipimo na dawa zenye ubora kwenye kutibu wagonjwa watakaothibitika kuwa na malaria. Hivyo, matokeo ya juhudi hizi ni kuwa, zimefanikisha kupungua kwa idadi ya Mikoa yenye hatari kubwa ya maambukizi ya malaria kutoka Mikoa 11 mwaka 2017 hadi Mikoa Saba mwaka 2020. Aidha visa vipya vya malaria vimepungua kwa asilimia 35 kutoka wagonjwa 162 kwa kila watu 1000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 106 kwa watu 1000 mwaka 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kutumia bidhaa za Kiwanda chetu cha Kibaha kwa ajili ya kuchangia jitihada za Serikali kufikia kumaliza Malaria (elimination) ambapo tumedhamiria kuwa ifikapo 2025 kiwango cha malaria kiwe kimepungua hadi kufikia asilimia 3.5 kutoka asilimia 7.5 ya mwaka 2017. Aidha, Serikali itahakikisha kila Halmashauri inaendelea kuwajibika kwenye kuhakikisha kuwa inatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya utekelezaji na hapa wanafanya vizuri. Mwaka huu wa fedha tunaoenda kuuanza mpya wametenga bilioni 2.7 lakini ilikuwa milioni 600 mwaka 2020/2021. Kwa hiyo tunaenda vizuri. Ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
(a) Je, tangu janga la Corona lianze ni Watanzania wangapi wamepata maambukizi; wangapi wamekufa; na wangapi wamepona?
(b) Je, ni fedha kiasi gani zimetengwa na Serikali na zimefanya nini na wapi katika kukabiliana na janga hili?
(c) Je, nini kinapelekea gharama za kupima Covid- 19 kuwa kubwa na ni dawa gani zilizofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa zina uwezo wa kuzuia au kutibu Covid-19?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika na mlipuko wa Ugonjwa wa Covid-19. Hadi kufikia tarehe 25 Oktoba 2021, idadi ya Watanzania 26,164 ndio waliothibitika kuwa na maambukizi. Kati ya hao, 725 walifariki na 25,330 walipona.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani kiasi cha shilingi bilioni 158 zimetumika kununua vifaa mbambali ikiwemo mitambo 19 ya kuzalisha hewa ya oxygen yenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 hadi 300 ambapo mitambo saba tayari imeshasimikwa na 12 ipo katika hatua ya usimikaji. Fedha nyingine zilinunua PPE, dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na magari 105 ya kubebea wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Sekta ya Afya imepokea kiasi cha shilingi bilioni 466.78 ambazo zitatumika katika kupambana na Uviko-19 ikiwemo kujenga na kusimika vifaa katika majengo ya matibabu ya dharura (EMD) 115, ujenzi wa wodi za uangalizi maalum (ICU) 67, ununuzi wa magari 253 ya kubebea wagonjwa, magari nane ya damu salama, usimikaji wa mitambo 10 ya kuzalisha hewa ya oxygen, vitanda 2,700 kwenye vituo 225 vya kutolea huduma za afya, kununua na kusimika mashine 95 za X-Ray, CT-Scan 29, mashine 4 za MRI pamoja na kufanya tafiti sita kuhusu tabia za virusi vya korona.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama halisi ya kumpima mgonjwa mmoja ni Dola 135 na Serikali sasa inatoza Dola 50. Hivyo Serikali inachangia Dola 85.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti mbalimbali zimefanyika duniani kuhusu dawa, ila hadi sasa dawa zilizopo zinatumika kutibu tu madhara yatokanayo na virusi. Hata hivyo kilichothibitika kwa sasa kusaidia kuondoa vifo ni chanjo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali italipa madai ya shilingi trilioni 7.91 ya watoa huduma kama yalivyoripotiwa kwenye ripoti ya CAG 2021?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, deni la shilingi trilioni 7.91 linajumuisha madeni ya wafanyakazi na watoa huduma kwa mashirika ya umma 71. Ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa na kudhibiti uzalishaji wa madeni mapya, mashirika yote ya umma yameelekezwa kuendelea kulipa kwa haraka iwezekanavyo na kuandaa mkakati wa kukabiliana na madeni na kuwasilisha Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkakati huo, kila taasisi inatakiwa kuonesha namna itakavyodhibiti uzalishaji wa madeni mapya na kulipa madeni yaliyopo. Lengo ni kuhakikisha kuwa kiwango cha madeni kinafikia asilimia mbili ya jumla ya bajeti ya mashirika ya umma ifikapo mwaka 2025. Aidha, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali itatumia mkakati huo katika uchambuzi na uidhinishaji wa mapato na matumizi ya kila mwaka. Ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, Serikali ina kauli gani juu ya ushuru mkubwa wa bidhaa za ngozi unaotozwa bandarini na vikwazo vya kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya ushuru wa kusafirisha ngozi ghafi na ngozi iliyosindikwa kiwango cha kati kwa maana ya Wet blue nje ya nchi ni makubaliano ya Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliokubaliana kuainisha viwango vya ushuru kwa lengo la kuhakikisha viwanda vya ndani vinapata malighafi ya kutosha na kuzalisha bidhaa za ngozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushuru wa kusafirisha ngozi ghafi nje ya nchi kwa maana export levy ni asilimia 80 ya mzigo ukiwa bandarini kwa maana FOB au Dola za kimarekani 0.52 kwa kilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ngozi zilizosindikwa kwa kiwango cha kati kwa maana ya Wet blue zinatozwa ushuru wa asilimia 10 ya FOB ili kutoa motisha kwa wasindikaji. Ngozi zilizosindikwa hadi kufikia hatua ya mwisho kwa maana ya finished leather hazitozwi ushuru wowote ule, ni 0%. Jitihada hizo zimesaidia kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kusindika ngozi na kuzalisha bidhaa za ngozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna vikwazo vyovyote katika kusafirisha zao la ngozi, kwa kuwa takwimu zinaonyesha kiwango cha usafirishaji wa ngozi ghafi kimeendelea kupanda kutoka kilo 513,201 mwaka 2015/2016 hadi kufikia kilo 7,370,533 mwaka 2020/2021.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, ni makundi gani yamenufaika na mkopo wa shilingi trilioni moja iliyoahidiwa kutolewa na Serikali katika sekta ya kilimo na kwa masharti gani?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua hatua za ziada za kisera, ikiwemo kuanzisha dirisha la mkopo maalum la shilingi trilioni moja kwa benki na taasisi za fedha nchini ili kuchochea mikopo nafuu kwa sekta binafsi, hususan sekta ya kilimo. Masharti ya mkopo maalum ni kuchochea mnyororo wa thamani katika kilimo cha mazao, miundombinu ya umwagiliaji, mifugo, uvuvi na ununuzi na usindikaji wa mazao kwa wakulima wadogo na wa kati pamoja na kampuni ndogo ndogo na za kati. Aidha, benki na taasisi za fedha zinatakiwa kutoa mkopo usiozidi shilingi bilioni moja kwa kila mkulima kwa riba ya asilimia chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Spika, masharti mengine ni Benki Kuu kuzikopesha benki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia Tatu ili taasisi hizo kukopesha wakulima na kampuni zinazojishughulisha na mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10. Aidha, hadi tarehe 31 Desemba, 2022, jumla ya mkopo wa shillingi billioni 164.9 umetolewa kwa sekta ya benki na taasisi za fedha na kuwanufaisha wakulima wadogo na wakulima wa kati zaidi ya 5,385 na AMCOS 21.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kutengeneza Bajeti kwa jicho la jinsia?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/2024 umetoa maelekezo kwa Maafisa Masuuli kuzingatia masuala ya jinsia, wakati wa uandaaji, uwasilishaji, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Mpango na Bajeti zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelekezo hayo, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake - UN Women inaendelea kushirikiana na Serikali kujenga uwezo katika maandalizi ya nyaraka za sera kwa kuzingatia masuala ya kijinsia. Aidha, katika mwaka 2022/2023, Wizara ya Fedha na Mipango imeunda kikosi kazi kwa ajili ya kuboresha Mwongozo wa maandalizi ya mipango na bajeti ya Serikali kwa jicho la kijinsia, ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, tangu kuanzishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kiasi gani cha fedha kimewekezwa na nini faida na hasara za uwekezaji huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2022 kwa hesabu zilizokaguliwa na CAG, thamani ya uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilikuwa imefikia jumla ya shilingi trilioni 14.4 ambapo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi trilioni 6.03, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi trilioni 7.49 na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Workers Compensation Fund ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi bilioni 521.94.
Mheshimiwa Naibu Spika, faida ya uwekezaji huu ni kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuhakikisha Mifuko inakuwa endelevu ili kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulipa mafao. Aidha, uwekezaji huu huchangia na kuongeza ajira, mapato ya Serikali kupitia kodi na kuchochea shughuli za uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo katika uwekezaji wowote kuna vihatarishi (risk) ambavyo vinaweza kusababisha hasara kwa baadhi ya uwekezaji. Hasara zilizojitokeza kwa uwekezaji uliofanywa na Mifuko ni pamoja na kutolipwa kwa wakati kwa mikopo iliyotolewa kwa wanufaika mbalimbali na baadhi ya miradi kutofanya vizuri ikilinganishwa na matarajio yaliyokuwepo wakati wa kubuni miradi hiyo, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa maji Mitaa yote ya Kata za Mbezi Juu, Wazo na Mabwepande katika Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo ya Kawe, Kata za Mbezi Juu, Wazo na Mabwepande. Hadi kufikia mwezi Desemba, 2022, kazi ya ulazaji wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji umbali wa kilometa 391.306 ilikamilika kupitia mradi mkubwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayoendelea sasa ni ulazaji wa mabomba ya maji umbali wa kilometa 64.3 kuanzia ulipoishia mradi mkubwa kwenda maeneo ya Mpiji Magohe, Mbopo, Mbopo Chekanao na Kinondo na itakamilika mwezi Desemba, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, maeneo yote katika Kata za Mbezi Juu, Wazo na Mabwepande yatakuwa yamepata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Bunju B – Mabwepande – Kibamba utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Bunju B – Mabwepande – Kibamba yenye urefu wa kilometa 24.4 imeanza na inatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2024. Baada ya kazi ya usanifu kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -
Je, Serikali inadaiwa fedha kiasi gani ilizokopa Mifuko ya Hifadhi za Jamii na kiasi gani cha madeni kimelipwa na kwa utaratibu gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikopa fedha kutoka katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na deni la michango ya wastaafu waliokuwa katika utumishi kabla ya mwaka 1999. Mchanganuo wa madeni na kiasi kilicholipwa ni kama ifuatavyo: -
(i) Mfuko wa PSSSF shilingi bilioni 506.88 na imeshalipwa shilingi bilioni 500 kwa utaratibu wa kibajeti; na deni la michango ya wastaafu waliokuwa katika utumishi kabla ya mwaka 1999 shilingi trilioni 4.46 na shilingi trilioni 2.17 zimeshalipwa kwa utaratibu wa hatifungani maalum. Aidha kiasi kilichobaki cha deni la Mfuko wa PSSSF shilingi bilioni 6.88 na shilingi trilioni 2.29 zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023.
(ii) Mfuko wa NSSF shilingi bilioni 292.59 zilizokidhi vigezo baada ya uhakiki wa deni la shilingi bilioni 490.16 zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023; na
(iii) Mfuko wa NHIF shilingi bilioni 80.68 zilizokidhi vigezo baada ya uhakiki wa deni la shilingi bilioni 209.72, zitalipwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itaendelea kuhakiki sehemu iliyobaki ya deni la Mfuko wa NSSF na NHIF ili yaweze kujumuishwa katika mpango wa malipo.