Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Grace Victor Tendega (19 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata fursa ya kuchangia kwa maandishi kuhusu Wizara hii. Kwa masikitiko makubwa nalaani kitendo cha kutokuwa na uhuru wa tasnia ya habari kama inavyotekelezwa na Bunge lako Tukufu. Kwa sisi akinamama na vijana katika nchi hii tumekuwa tukipambana na maisha na mara nyingi tulikuwa tunasahaulika. Uhuru wa vyombo vya habari ulifanya wanawake wengi waingie kwenye tasnia ya siasa kwa kuwa wamekuwa wakiwaona wenzao waliotangulia wakifanya uwakilishi wao Bungeni vizuri na hii ilihamasisha wanawake wengi kuona kuwa wanaweza.
Mheshimiwa Spika, akina Getrude Mongela, Asha Rose Migiro, Spika aliyestaafu Mheshimiwa Anne Semamba Makinda, Mheshimiwa Halima Mdee, Mheshimiwa Pauline Gekul na wengine walionesha mfano kuwa wanawake tunaweza. Kwa namna hii inaonesha kuwa, Bunge hili linataka kudidimiza kufikisha 50 kwa 50 kwani wengi wanawake waliogombea wameweza kushinda Ubunge wa Majimbo na waliaminiwa na wananchi wao kwa kuwa walionekana wakitetea maslahi ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, nashauri Bunge hili lirushwe live ili wanawake tupate fursa ya kuonekana ili kuondokana na kuwa Wabunge wa Viti Maalum.
Mheshimiwa Spika, suala la Zanzibar. Nchi yenye utawala bora haina woga wowote, lakini nchi yetu imeonesha ufinyu wa demokrasia kwa suala la uchaguzi wa Zanzibar. Serikali inapaswa kutumia busara zaidi na si ushabiki kuhakikisha Zanzibar inakuwa tulivu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Watumishi hewa; naunga mkono hotuba ya (KRUB) iliyofafanua jinsi udhibiti wa wafanyakazi utakavyokuwa kwa kuunganisha mfumo, mfano, mfumo wa Utumishi wa Umma uunganishwe na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama vile NSSF, PSPF, LAPF, GEPF na kadhalika. Kwa wale wahusika wote pia wachukuliwe hatua za kisheria.
Mheshimiwa Spika, nimeshukuru na naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KRUB).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata fursa hii ya kuchangia kwa maandishi na nitajikita katika kilimo. Nashauri Serikali ijikite katika kutoa elimu juu ya uzalishaji wa mazao bora ya kilimo. Kwa mfano, Mkoa wangu wa Iringa una Kiwanda cha Nyanya chini ya mwekezaji kiitwacho DARSH kwa ajili ya kusindika nyanya. Iringa huzalisha karibu zaidi ya 50% ya nyanya inayozalishwa Tanzania lakini kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa nyanya. Wakulima wamekuwa wakilima nyanya zisizokidhi ubora unaotakiwa kiwandani kwa kukosa elimu ya kilimo bora cha nyanya.
Pia wakulima hawa hawajaandaliwa kwa kilimo hicho kwani wengi wao hulima kienyeji. Mahitaji ya kiwanda ni zaidi ya tani 200 kwa siku ambapo mara nyingi hazipatikani na wengine husafirisha kwenda Mkoa wa Dar es Salaam. Hivyo, uzalishaji wa kiwanda hicho hauna tija kwa kuwa wakulima hawajaandaliwa. Nashauri Serikali iwaandae wakulima kuzalisha kwa ubora na uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu au changamoto nyingine ni gharama ya mbegu. Mfano, hybrid seed (Eden na Asila) gramu 30 kwa ekari moja ni Sh. 210,000. Ni gharama kwa wakulima wetu walio wengi, nazungumzia (hot culture). Vile vile hakuna Maafisa Ugani wa kutosha kupita kwa wakulima vijijini hasa katika Wilaya ya Iringa, Jimbo la Kalenga, Kilolo na Isimani. Nashauri Waziri anapojibu hoja hizi atueleze ni lini wananchi wa Wilaya ya Iringa watapatiwa Maafisa Ugani wa kutosha?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri mkulima awezeshwe bajeti ya mbegu, mbolea na viatilifu (pesticides). Wakulima ambao wanatumia madawa hayo kwenye mazao mara nyingi magonjwa hayaishi mfano ugonjwa wa kantangaze kwa sababu madawa haya wakati mwingine ni feki. Makampuni mengi yanauza madawa yasiyofaa, Waziri afuatilie na kuzingatia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbolea zinazotumika ni za gharama kubwa mfano yara. Mbolea hii mfuko mmoja ni Sh. 90,000 wananchi wa kawaida hawawezi kumudu kutumia na hivyo kusababisha kuzalisha mazao yasiyo na ubora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha umwagiliaji ni suluhu kwa uzalishaji mazao mbalimbali. Wizara ihamasishe kilimo cha matone lakini wakulima wawezeshwe kwani hawataweza kumudu drip lines. Serikali itoe mitaji kwa wakulima na pia iwe na Benki ya Wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kiwanda cha Chai kilichopo Wilaya ya Kilolo, mpaka leo hii kimefungwa na kinakatisha tamaa wakulima wa chai wa wilaya hiyo. Naomba Serikali itoe majibu ni lini kiwanda hiki kitaanza kuzalisha ili wakulima wa chai waweze kujikwamua kiuchumi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia REA inafanya kazi ya kusambaza umeme vijijini, pamoja na kufanya kazi hiyo katika Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Iringa Vijijini kuna substation iliyopo katika Kijiji cha Tagamenda ambapo umeme umeanza kusambazwa kwenda mikoa mbalimbali ikiwemo Shinyanga na mingine
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kushangaza, wanakijiji wanaofanya kazi ya kulinda umeme huo, hawajapata umeme hata huo wa REA. Swali kwa Wizara, hivi hawaoni kuwa hawawatendei haki wananchi wa Vijiji vya Tagamenda, Wangama, Ikuvilo na vingine ambao huishi karibu na kituo hicho substation kuunganisha umeme huo au hata wakapata umeme wa REA na wasiwe walinzi tu wa kituo na nyaya hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, anapohitimisha naomba kupata majibu ili tuweze kuondokana na adha hii kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda kukushukuru kwa kupata nafasi hii na pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kupata fursa hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani kwa asilimia 100. Ninavyounga mkono, naomba ninukuu maneno ya Hayati Baba wa Taifa katika kitabu chake cha Binadamu na Maendeleo alipokuwa akizungumzia faida ya elimu katika nchi. Naomba ninukuu baadhi ya mistari, anasema:- “Tunatumia fedha nyingi sana zisizolingana na uwezo wetu kuwasomesha watu wachache ili baadaye na wao walete faida kubwa kiasi hicho hicho katika nchi. Tunatumia fedha nyingi kutafuta faida katika akili ya mwanadamu kama vilevile tunavyotumia fedha kununua trekta na kama vilevile ambavyo tukinunua trekta tunatarajia kufanya kazi kubwa zaidi kuliko kazi ya mtu na jembe la mkono”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaona elimu ni gharama tujaribu ujinga, walikwishazungumza watu wengi. Elimu ya nchi hii imewekwa rehani. Watanzania walio wengi hawaoni umuhimu wa kupeleka watoto wao katika shule zetu za Serikali kwa sababu ya matokeo ambayo tunayaona sasa hivi. Watoto wengi wamekuwa wakimaliza shule bila hata kujua kusoma na kuandika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri wa Elimu aweze kunisikiliza kwa makini. Hakuna elimu bora bila kujali Walimu. Walimu ndiyo wanaofanya elimu hii ikawa bora zaidi hata kama shule ikiwa haina madawati mengi, haina miundombinu mizuri zaidi lakini Walimu wakawa wameboreshwa vizuri wanaweza wakafanya elimu hii ikawa bora hivyo vingine vinasaidia kuwa bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii imewatelekeza Walimu. Tumesema tunahitaji Walimu wa Sayansi katika nchi hii lakini tuna vyuo vya ualimu visivyo na maabara. Nitavitaja baadhi muone kama vyuo vya ualimu ambavyo vinafundisha Walimu wa Sayansi havina maabara unategemea nini huko? Kuna Chuo cha Ualimu Vikindu, Chuo cha Ualimu Singa Chini, Chuo cha Ualimu Mpuguso, Chuo cha Ualimu Kitangali na vinginevyo hivi navitaja ni baadhi havina maabara na hakuna vifaa vya maabara. Sasa tunatarajia nini na tunajenga maabara nchi nzima tukitarajia kwamba tutapata Walimu bora ambao watakuja kufundisha watoto wetu lakini kule tunakoandaa Walimu wetu hakuna maabara. Serikali hii inafanya masihara na elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu hao hao wa Sayansi waliahidiwa kupewa mikopo, hapa ninavyozungumza Walimu hao wa Sayansi hawajapata fedha za mikopo mpaka dakika hii. Nina ushahidi nitakuletea orodha ya Walimu Mheshimiwa Waziri kama utahitaji, wengi hawajapata mikopo katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kuzungumzia katika suala la mitaala. Naomba ni declare interest mimi ni Mwalimu na pia nilikuwa mkuzaji wa mitaala kabla sijaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kabisa tunapozungumzia elimu bora tunahitaji mitaala iliyo bora na mitaala ili iwe bora ina process zake za uandaaji. Zile hatua zikipindishwa ndiyo tunapata matokeo haya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatakiwa tufanye research ili kujua Serikali yetu au nchi yetu inataka Watanzania wawe na elimu ya namna gani ili kuwanufaisha hao Watanzania, ile sera kwanza haipo vizuri. Tulikuwa tuna falsafa ya elimu ya kujitegemea huko nyuma lakini sasa hivi haieleweki na haitafsiriki vizuri kwenye mitaala kwamba tunakwenda na falsafa ipi sasa hivi. Je, bado ni elimu ya kujitegemea mpaka sasa hivi ama tuna nini ambacho kipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya process nyingine zinarukwa, tunatakiwa tuite wadau ili tukubaliane nao ni yapi ambayo tunatakiwa kuyaweka kwenye mitaala. Mheshimiwa Waziri alikuwa ni Mjumbe wa Bodi katika Taasisi ya Elimu Tanzania anaelewa matatizo yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tulikuwa tukiomba fedha Wizara ya Elimu lakini fedha za kufanyia mambo hayo mengi zinakuwa hakuna, unatarajia upate nini? Unatakiwa ufanye utafiti, uitishe wadau lakini kwa kiasi kikubwa wadau wa nchi nzima unaweza ukaita wadau 60 au 100, hao watasaidia kuweza kujua kwamba nchi hii inahitaji twende katika mrengo upi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika suala hilohilo kuna masuala ya vitabu. Mheshimiwa Waziri amezungumza katika hotuba yake, amezungumzia masuala mengi yanayohusu masuala ya vitabu. Kulikuwa na bodi iliyokuwa inaitwa EMAC ambayo walikuwa wanashughulikia vitabu vyetu, ilivunjwa wakarudisha Taasisi ya Elimu Tanzania iweze kufanya kazi hiyo. Hivi ninavyozungumza hapa shule zetu kule hazina vitabu, Wizara imeandaa masuala ya KKK lakini sijui huo usambazaji TAMISEMI unakwenda vipi. Walimu wanakwenda wanafundisha bila vitabu na vitabu vyenyewe vilivyokuwa vimetolewa kwa masomo mengine vinatofautiana, hii ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 80 kulikuwa na ushindani baina ya shule za Serikali na shule za watu binafsi. Leo hii mnaleta bei elekezi, hivi hawa wenye shule binafsi wangekuwa hawakuweza kuwekeza hivyo wale watoto wetu waliokuwa wanaachwa wangekwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, badala ya kukaa tukaboresha elimu yetu katika shule zetu za Serikali ndipo sasa tuanze kuona kwamba tunaweka bei elekezi baadaye, kwa nini tunaanza kubana watoto wetu wasiweze kusoma katika hizo shule kwa sababu huku waliachwa katika nafasi ya shule za Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu shule za Serikali zinawachukua wale ambao ni bora na hawa shule binafsi zinawachukua wale ambao siyo bora ilivyokuwa zamani. Sasa hivi hata wazazi hawaoni umuhimu huo kwa sababu kule shuleni tunakuta hakuna Walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano katika Mkoa wangu wa Iringa kuna baadhi ya shule ina Mwalimu mmoja shule nyingine zina Walimu wawili, shule ya sekondari wanatakiwa wafundishwe masomo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kimoja Mheshimiwa Waziri lazima mtambue utahini wa mitihani. Shule X ambayo ina Walimu wa masomo yote na shule Y ambayo kwa mfano ina Mwalimu mmoja au wawili lakini mwishoni mwa utahini mnatahini mitihani sawa. Hii siyo sawa hata kidogo!
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwaangalie wale ambao wamefundishwa na Mwalimu mmoja somo moja tutahini kwa kile walichofundishwa! Kwa nini mnawafelisha watoto wetu wakati mwingine wakati siyo makosa yao kwa sababu…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyikiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia katika Bunge hili. Kwa sababu ni mara ya kwanza na mimi kuchangia katika bajeti napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kuweza kuja humu kuwakilisha akina mama wa Mkoa wa Iringa. Napenda pia kushukuru chama changu ambacho pia kimeniwezesha kuwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nichangie kwa kuanza na kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 89, ukatili wa kijinsia. Kumekuwa na matatizo mengi, kumekuwa na ukatili wa kijinsia ambao unafanyika katika nchi yetu na hasa waathirika wa tatizo hilo ni wanawake na watoto. Tumeona wanawake wengi wanafanyiwa ukatili wa kinyama, tumeona watoto wetu wanafanyiwa ukatili wa kinyama, tumeona watoto wanachomwa moto, tumeona watoto wanamwagiwa maji ya moto, tumeona madhara mengi kwa watoto wetu wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri ameeleza katika hotuba yake kwamba wataendelea kusimamia sheria, sheria zipo Mheshimiwa. Kama zipo na matukio yanaendelea kuna tatizo kubwa katika nchi hii la usimamizi wa sheria. Nikuombe Waziri unapokuja kuhitimisha hoja zako uweze kutueleza usimamizi huo utakuwaje tofauti na mazoea ya siku za nyuma ambayo yalikuwa yakiendelea ambapo akina mama wengi wananyanyasika, watoto wengi wananyanyasika, watoto wamekosa kabisa wa kuwasemea, tumeona watoto wanafichwa kabisa ndani kwa miaka kadhaa. Inatia uchungu kwa sisi wazazi ukiona matukio yale yanaendelea katika nchi hii ambayo tunasema ina amani na utulivu. Mheshimiwa Waziri tunaomba uweze kulisimamia na kwa sababu ni mwanamke mwenzetu basi uchungu huu najua unao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende katika masuala ya afya kwa ujumla. Tukiangalia bajeti ambayo imetengwa kwa Wizara hii, asilimia ambazo waliomba 100 wao wamepewa asilimia 11, hivi tutatekeleza kweli haya yote? Ndiyo maana wenzangu waliotangulia wanasema wanamuonea huruma Waziri kwa sababu matatizo ni mengi, mahitaji ya afya ni mengi huko kwenye Wilaya na majimbo yetu kuna matatizo lukuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikizungumzia katika Wilaya ya Iringa, Jimbo la Kalenga, tumekuwa na shida kubwa ya huduma za afya. Zahanati wananchi wamejenga, ukienda Wasa wamejenga zahanati lakini hakuna madaktari na manesi wananchi wanatoka kule kuja hospitali huku Ipamba ambapo ni mbali. Watu wanatoka Kata ya Magulilwa na kata mbalimbali kwa sababu hakuna hospitali za kuwahudumia na wakifika pale wanapata shida kwa sababu dawa lazima wanunue na dawa ni gharama na wakati mwingine hazipo. Kwa hiyo, kumekuwa na changamoto kubwa sana katika hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri aweze kutupa majibu hizi changamoto zitatatuliwa lini, huu upungufu wa madaktari na wataalam katika maeneo yetu utakwisha lini? Hawa wananchi wameweza kujitolea kujenga majengo lakini mengine yamekaa kama magofu hakuna madaktari wala dawa. Serikali hii mnasema ni sikivu lakini watu wanapotea na tunasema afya ndiyo mtaji wa kwanza kwa jamii yetu. Sasa kama Serikali hii ambayo mnasema ni ya viwanda kwa sasa hivi, je, hivyo viwanda vitaendeshwa na watu wasio na afya bora. Tunahitaji kuwekeza kwenye afya ili tupate Watanzania wenye fikra bunifu za kuweza kuwekeza huko kwenye viwanda. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri uweze kuja na majibu ya masuala hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa upande wa wazee, huko ndiyo kabisa. Tunashuhudia wazee wetu wakipata shida hospitalini. Hii Sera ya Wazee kupata huduma ya afya bure haitekelezeki, hawapati dawa. Wazee wanakwenda hospitalini wale wahudumu wetu madaktari na manesi wanatoa maneno ya kashfa kwa wazee wetu, inatia uchungu. Wazee hawa wameifanyia kazi kubwa nchi hii, wameweza kufanya mambo mengi kwa nchi hii lakini sisi hatuwalipi hata fadhila ya kupata dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta ni rahisi kwa nchi yetu na Serikali hii ya CCM kuitisha mkutano wa wazee Dar es Salaam, lakini mara nyingi haiwezi ikawatimizia ahadi zao. Ni rahisi sana wakawa wamewekwa sehemu wazee wasikilize lakini kutimiza ahadi zao inakuwa ni ngumu. Tukuombe Mheshimiwa Waziri uweze kutuambia hawa wazee matibabu bure yatapatikana lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa huduma za afya kwa watu wenye ulemavu. Mara nyingi tupo nao, tukiwa kwenye foleni hospitalini mnawaona hawa watu hawapewi kipaumbele kama inavyotakiwa. Hawa watu wanahitaji kuhudumiwa kwa ukaribu. Mimi nikuombe tu Mheshimiwa Waziri kwenye hitimisho lako hawa watu ikiwezekana wapewe bima ya afya ili waweze kutibiwa kwa bima ya afya. Kwa sababu wanapata shida sana, wengine hata hawajiwezi, hawajui wapate wapi pesa ya matibabu, hawajui wataendaje hospitalini lakini hawahudumiwi! Tunaomba wapate bima ya afya kwani itawaokoa wao kuweza kutibiwa na kuweza kuwa kama watu wengine kwa sababu na sisi ni walemavu wa kesho, hakuna ambaye sio mlemavu, ikitokea itakuwa ni bahati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa katika Mfuko wa Bima ya Afya. Mfuko wa Bima ya Afya huko ndio kabisa, ukimgusa mwananchi huko kijijini ukamuelimisha anakuelewa lakini anakuja na swali tukienda hospitalini watu wenye kadi za bima ya afya wanatengwa, hawapati huduma haraka, wananyanyapaliwa sana, hii adha itaisha lini? Unakuta mtu ana bima ya afya lakini akienda pale wanasema tunahudumia kwanza wanaolipa cash wengine mtasubiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na WAVIU wale Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niweze kumshukuru Mwenyenzi Mungu aliyenijalia afya na pia niwashukuru sana wote waliochangia kuhusu Wizara hii ya Afya kwa sababu bila afya hatuna hiyo Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza kwa huzuni sana kwa sababu bajeti ya Wizara hii kwa kipindi hiki ambacho tumebakiza muda mfupi sana haijatekelezeka kwa asilimia 60; japokuwa tuna Mawaziri ambao kwa kweli wanajitajidi kufanya kazi, lakini hawapati fedha za kutosheleza bajeti yao, na tunaona afya za Watanzania zinazidi kudorora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinga ni bora kuliko tiba, nilikuwa natengemea Mheshimiwa Waziri pia aje na jinsi ambavyo tutazungumzia jinsi ya kuwakinga Watanzania kutokupata maradhi mbalimbali, ukija ukaangalia katika maendeleo ya jamii ambako ndiko wako vijana wetu wafanyakazi ambao wanaweza wakaenda na wakawasaida Watanzania, bajeti yao ni ndogo na huko tunakotoka kwenye Halmashauri hawajaliwi, wako kama wanyonge ukiwakuta kule utawaonea huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri vijana wetu kule wananyanyasika hawako vizuri kabisa katika hii sector, ninaona kwa mfano, kuna masuala ya afya ya mazingira ambayo unaweza ukashirikiana na Wizara ya Mazingira, mkaanza kuona ni jinsi gani mnaweza kupunguza masuala ya maabukizi mbalimbali. Kwa mfano, Dar es Salaam asilimia 90 ni vyoo vya shimo, asilimia tisa tu ndiyo ina vyoo vya kuvuta, hizi ni takwimu ambazo zimetolewa na mashirika mbalilmbali waliopita na kufanya tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaona kipindi cha masika jinsi ambavyo mtiririko wa maji taka unavyosambaa katika Jiji lile. Hii inakwenda kuleta maambukizo mbalimbali. Tunaambiwa kwamba Watanzania asilimia kubwa tuna kawaida ya kutonawa baada ya kwenda sehemu za kujisaidia na sehemu mbalimbali na hizi zinasababisha maradhi mbalimbali ambayo tunayapata na magonjwa mbalimbali. Kwa mfano, UTI ambao inafikia mahali sasa umekuwa ni ugonjwa wa kawaida lakini pia unaua. Mheshimiwa Waziri uweze kulitizama hilo na kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika makubaliano ya Abuja (Abuja Declaration) makubaliano yalikuwa asilimia 15 ya bajeti mzima inaweza kutatua changamoto za afya, lakini asilimia hii imekuwa haitolewi kwa muda wote wa bajeti. Ukianzia mwaka 2015/2016 zilitengwa shilingi trilioni nne zikaidhinishwa shilingi trilioni 1.5 tu. Ambayo ilikuwa ni asilimia saba hatukuweza kufikia hata hapo. Kwa hiyo, hii inaonesha jinsi ambavyo hatuwezi kutekeleza baadhi ya mipango ambayo tumeipanga ili iweze kutekelezeka kwa Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala hili la kutokupeleka fedha vizuri ambalo linaanzia ngazi ya sera tunavyotunga sera katika Wizara ya Afya tunakwenda katika mikoa, halmashauri mpaka vijijini, jinsi ambavyo mtiririko mzima unavyochanganya. Huu mchanganyiko wa kiutendaji katika Wizara hii unatuletea shida katika utekelezaji na ufuatiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati tumependekeza mara zote kwamba ingewezekana Wizara ya Afya kama ilivyo Wizara ya Elimu, kuwe na mtiririko kutoka sera mpaka utendaji wake. Unakuta katika Halmashauri baadhi ya masuala hayatekelezeki tunaambiwa hii iko TAMISEMI, hii iko Wizara ya Afya, basi unakuta ni mchanganyiko na fedha zinakuwa hazifuatiliwi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Waziri aweze kumshauri Rais jinsi juu ya Wizara hii nyeti ambayo itatengeneza Watanzania ambao wenye akili timamu na nzuri, wenye afya bora wa kuweza kuendeleza na kuleta maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Menyekiti, nizungumzie kule kwangu japokuwa kuna baadhi ya mambo ambayo yalitakiwa yazungumzwe kwa TAMISEMI, kwa sababu sikupata nafasi lakini pia kwa sera yakwenda. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa waliomba shilingi milioni 150 waliidhinishiwa shilingi milioni 35 na hawakupata hata shilingi moja, unategemea hawa watafanyaje kazi zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia OC ilikuwa ni shilingi milioni 25 badala yake wamepelekewa shilingi milioni sita tu. Ukija katika Halmashauri ya Kilolo kwanza Halmashauri ile ina upungufu wa watumishi asilimia 51, waliopo ni asilimia 49 na hao tumepata wenye vyeti fake 13 bado kuna upungufu wa watumishi katika Halmashauri hiyo ya Kilolo.
Kwa hiyo, katika mgawanyo wenu wa watumishi wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maadili na utamaduni wa Mtanzania; maadili na utamaduni wa Mtanzania yameendelea kuporomoka siku hadi siku kutokana na mambo mengi ikiwemo ukuaji wa teknolojia. Watu walio wengi, hasa vijana, wamekuwa wakikosa maadili mema kwa kuangalia au kuiga mila na tamaduni za nje ya nchi. Baadhi ya watoto wamekosa heshima kwa wakubwa.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kutunza mila nzuri na tamaduni zetu kwa kuchukua hatua pale panapotokea ukiukwaji wa mila na desturi, wazazi pia wanapaswa kuangalia maadili ya watoto wao. Elimu kuhusu utunzaji wa mila na desturi itolewe katika jamii. Tunahitaji Tanzania yenye Watanzania walio na maadili mema.

Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa viwanja vya michezo; viwanja vingi katika mikoa mbalimbali havikidhi vigezo vya kuwa viwanja vya michezo, hasa vile vinavyomilikiwa na CCM. Katika Mkoa wa Iringa, Uwanja wa Samora Machel umejengwa maghala ndani yake na kusababisha uharibifu pamoja na kuharibu lengo la kuwa na uwanja huo. Napendekeza kuwa Serikali, kupitia Wizara, iwashirikishe Sekta Binafsi ili kuendeleza viwanja hivyo hasa Uwanja wa Samora Machel Mjini Iringa ili kuweza kuinua kiwango cha michezo. Serikali pia ijenge viwanja vipya vya michezo.

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Sanaa Bagamoyo; wananchi walio wengi, hasa vijana, wamekuwa wakijishughulisha na sanaa. TASUBA ni chuo kinachotoa mafunzo ya sanaa lakini miundombinu yake haikidhi mahitaji. Katika fedha waliyotengewa Bajeti 2016/2017, milioni 300, wamepata milioni 100 tu, sawa na 5.6%. Nashauri Serikali iweze kuwamalizia kiasi cha fedha kilichobakia kwani chuo hiki ni tegemeo la vijana wengi kupata ujuzi ili wajitegemee kimaisha.

Mheshimiwa Spika, uhuru wa kupata habari; kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kuwa wananchi wanao uhuru wa kupata habari, Serikali imezuia wananchi kupata habari za Bunge Live. Naishauri Serikali isiwe na woga wa kukosolewa kwani ni afya kwa Taifa na watajipanga kuweza kutekeleza majukumu yao. Niiombe Serikali iruhusu uhuru wa vyombo vya habari ili wananchi wapate haki yao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika hotuba hii. Naomba niungane na wenzangu kwa kuwapa pole wafiwa wote wa watoto waliopata ajali Mkoani Arusha, Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na maneno ya wanazuoni ambayo yanasema ukitaka Taifa bora, boresha elimu; ukitaka kuboresha elimu boresha walimu na ukitaka Taifa la watu wanaojiheshimu, heshimu walimu. Ninazungumza hivi kwa sababu walimu wetu kwa kweli wamekuwa na kinyongo cha kufanya kazi yao, wengi wamekuwa na malalamiko mengi na wamekuwa hawapati haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu zamani walikuwa wakipata posho ya mazingira magumu ya kazi na hasa wale wa vijijini ili yawavutie, lakini sasa hivi hakuna posho hizo. Napenda kusema kwamba mimi pia ni mwalimu, wakati huo tukifundisha kulikuwa na posho, wale walimu wa sayansi walikuwa wana posho ya ziada ya walimu wengine wa masomo ya arts na biashara, maslahi hayo yalikuwa yanatia moyo na mwalimu anafundisha kwa nguvu kubwa sana na wanafunzi walikuwa wakifaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile unaona kwamba kada hii ni kada inayofanyakazi kwa saa 24. Mwalimu anaandaa somo, mitihani na anasahihisha, mwalimu anapanga matokeo, muda wote wa siku mwalimu anafanya kazi hizi, lakini Serikali hii imekuwa haiwalipi posho ya kufundishia walimu ambayo ilikuwa ni kilio chao cha siku nyingi na walimu wamekuwa hawapati hizo posho. Tunaomba Serikali iangalie suala hili ili walimu wetu waweze kupata posho ya kujikimu na waweze kufanya kazi vizuri, hasa walimu wanaokaa kwenye mazingira magumu. Tumeona wengine wakifuata mishahara yao wanafunga shule kabisa. Mimi nina shule yenye walimu wawili kutoka mkoani kwangu, wakati wa kufuata mishahara mmoja anabaki, mwenzake anakaa na darasa la kwanza mpaka la saba. Kwa kweli, hii ni kazi kubwa kwa walimu, tuwatizame kwa jicho lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi hawapo, tunaomba Waziri alitizame suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie sasa suala la vitabu. Vitabu ndiyo moyo wa mwalimu katika kufundisha, tuna mitaala, vitabu na vilevile tuna masuala mengine ambayo yapo katika ufundishaji. Mwalimu akikosa kitabu, akipata kitabu ambacho kinamwongoza mwanafunzi vibaya Taifa zima litakwenda kwenye fikra hizo na tutatengeneza Watanzania wenye fikra ambazo zimepotoshwa. Vitabu hivi kama tulivyokwisha kuviona na wenzetu wamevionesha hapa asubuhi vimekuwa na mapungufu mengi, hivi Serikali inataka tuende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu, alikuwa kwenye Bodi ya Taasisi ya Elimu na amefanya kazi anajua jinsi ya kuandaa vitabu anafahamu kabisa. Baada ya kumaliza kazi hii inatakiwa watu wa kuhakiki, kuna panels za masomo ambazo zinatakiwa zipitie. Kweli kama panel zile zilipitia na makosa haya yakatokea basi hawa waliofanya kazi hiyo wachukuliwe hatua, kwa sababu hii ni hasara kubwa kwa Taifa letu, Watanzania na watoto wetu wanakwenda kufundishwa vitu ambavyo vitawapoteza na vitawapotosha. Kwa sababu wanasema unapopata elimu ya msingi bora ndiyo itakayokuongoza mpaka kwenye maendeleo ya baadae. Hivyo, ukimkosea mtoto hapa toka kwenye msingi kwa kweli utamfikisha mahali ambapo siyo panakotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala sasa la ufundishaji hasa kwa watoto wa kike na masuala ya mazingira ya watoto wa kike katika elimu. Tumeona kwamba kuna changamoto nyingi…

(Hapa kengele ililia kuashiria muda wa mzungumzaji kuisha)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo ambayo ni muhimu kwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja, kwanza kabisa ni bahati mbaya sana sekta hii ya kilimo imekuwa haipewi kipaumbele. Asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania ni wakulima na napenda niseme katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati akiwasilisha ukomo wa bajeti alisema kwamba katika bajeti ya mwaka 2018/2019 bajeti hii imetoa kipaumbele katika mambo yafuatayo, nitayasema machache. Alisema kwanza kulipa deni la Serikali; pili, kugharamia ujenzi wa miundombinu pamoja na reli na viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka kipaumbele katika vitu na si watu na ndiyo maana watu wanajiuliza, hivi mnavyosema uchumi umekua, umekua wapi? Mifukoni mwa watu hawana pesa, wakulima wanalima hawapati masoko ya mazao yao. Hawa wakulima sijui itakuwaje, mtawajibu nini mwaka 2020 kwa sababu mmewatelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika Mkoa wangu wa Iringa wananchi wanalima mahindiambayo ndiyo zao lao la chakula na ndiyo zao lao kuu la biashara pamoja na mazao mengine yakiwemo alizeti, ngano, karanga, viazi na vitu vingine. Haya mahindi yalikuwa yanauzwa mpaka shilingi 80,000 kwa gunia mpaka shilingi 100,000 mwaka jana. Sasa hivi gunia la mahindi ni shilingi 25,000, debe moja ni shilingi 5,000 mpaka shilingi 4,000. Huyu mkulima amenunua mbolea kwa gharama kubwa sana mwishoni anakuja kuuza gunia la mahindi kwa bei ambayo hata nusu ya mfuko wa mbolea haifikii, hii haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukijigamba hapa tunakwenda kununua ndege ili wananchi wapande, wananchi wangapi wanaopanda ndege? Katika Mkoa wangu wa Iringa ukitaka kuhesabu wanaopanda ndege asilimia zaidi ya 90 hawapandi ndege. Tunaomba mkae mliangalie suala hili ili wananchi hawa waweze kupata fedha kwa kuwapatia masoko ambayo yatakuwa yanawasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala la mbolea. Mbolea zimekuwa haziji kwa wakati, sisi kule kilimo chetu msimu wetu unaanza Novemba amabo ndiyo mvua za kupandia zinaanza lakini inapofika Februari au Machi ndiyo mbolea zinakuja, hii mbolea itamsaidia nani? Tumewatupa watu wetu na hatuwapi mambo yanayostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijawa Mbunge nilikuwa nasikia masuala haya ya kulalamikia bajeti ya Wizara ya Kilimo, ya kulalamikia jinsi ambavyo mawakala wanapata shida. Nimekuja nipo Bungeni mwaka 2015 hivyo hivyo, mwaka 2016/2017 hivyohivyo, naingia hii mwaka 2017/2018 bado suala la kulalamikia bajeti ndogo ya Wizara ya Kilimo iko vilevile. Tunaenda wapi na nchi hii? Tunakwenda wapi na Watanzania wanakwenda wapi? Mmesema tunataka tuwe na nchi ya viwanda, viwanda hivi vitapata malighafi kutoka wapi? Wakulima wamekata tamaa kabisa, hawana matumaini na Serikali yao... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia bajeti hii ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya uhai kuweza kuwa mahali hapa kufanya kazi hii ambayo ni kwa ajili ya wananchi. Nitajielekeza moja kwa moja katika kuchangia bajeti hii. Namheshimu sana Mheshimiwa Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake lakini katika majibu ya mwezi Mei mwaka 2017 kuna hoja ambazo tulikuwa tukiuliza kuhusu afya ya mama na mtoto na jinsi ambavyo wanaweza wakakinga akinamama kutopata vifo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu haya tuliambiwa kwamba, Wizara na Serikali kwa ujumla imejipanga kuhakikisha kwamba wanapunguza katika vizazi hai 100,000 watafikia wanawake 292 angalau watakaokuwa katika hilo. Hata hivyo, sasa hivi mmeona wanawake katika vizazi hai 100,000 wanaopatwa na vifo ni 556, imepanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo naomba majibu Mheshimiwa Waziri atuambie ni mkakati gani ambao wanaenda kufanya akinamama hawa wasiweze kupoteza maisha yao wakati wa uzazi. Tunaomba mkakati madhubuti wa Serikali ambao utakwenda kupunguza ama kumaliza tatizo hili la akinamama pamoja na kazi kubwa ambayo inafanyika ya kupeleka vifaa na kadhalika nini kilichopo hapo kinachopelekea ongezeko hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni bajeti kutotoka kwa wakati. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kama alivyokwishasema mwenzangu tunatenga bajeti, lakini utekelezaji wake unakuwa ni mdogo sana. Waziri atuambie nini kinafanya hivyo, tumekwenda katika ziara katika Mkoa wa Iringa, tumekwenda Mkoa wa Mbeya, tumeona wenyewe, inafika mahali mnaona aibu kama Wabunge, mnakwenda kukagua miradi ambayo pesa hatukupeleka. Tunawaweka katika mazingira gani hawa Watendaji ambao tunasema tunakuja kukagua pesa ambazo zilitumwa, tuliidhinisha mwaka wa fedha huu wa 2017/2018 halafu mnakwenda pale hakuna hata shilingi moja iliyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda Chuo cha Rungemba cha Maendeleo ya Jamii, hakuna fedha iliyokwenda. Tumekwenda Chuo cha Uyole Maendeleo ya Jamii, hakuna fedha iliyokwenda. Tumekwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambayo inahudumia mikoa saba lakini hakuna fedha iliyotengwa iliyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli wale Wakurugenzi wanafanya kazi kubwa sana. Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ameweza hata kuajiri wafanyakazi kwa kutumia own source, kazi ambayo ilikuwa ifanywe na Serikali hii lakini amekwenda kufanya hiyo kazi. Tunampongeza kwa sababu wananchi waliweza kupata huduma. Tunaitaka Serikali ipeleke pesa wananchi waweze kupata huduma kama tunavyopitisha bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka 2017/2018 iliongezeka kwa asilimia 35 kutoka bajeti ya 2016/2017, lakini bajeti hii ambayo tunaijadili sasa imepungua kwa asilimia
20. Hii maana yake nini? Ni kwamba tunakwenda kuwahangaisha wananchi tena kule, hawatapata madawa, hawatapata huduma bora inayotakiwa, vifaa tiba na kadhalika, hii inakwenda hadi kwenye Mkoa wangu wa Iringa, ukiangalia Mkoa wa Iringa Wilaya ya Kilolo ambako…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja hotuba ya Kambi ya Upinzani na ile ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zetu huko vijijini zina matatizo mengi. Hakuna mabweni kwa ajili ya wanafunzi wala walimu wa kutosha. Watoto wa kike wanapangiwa vyumba vya kulala kwa kukosa mabweni, huko wanarubuniwa na kushawishiwa kwa kuwa hukosa pia fedha za kujikimu kwani wazazi wakati mwingine hawawapi kutokana na umaskini walio nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa kike huweza kubakwa na kupata mimba, hivyo ninashauri Serikali ione namna ambavyo mtoto huyu anayepata mimba atakavyoweza kupata elimu baada ya kujifungua. Imekuwa kama adhabu kwa sababu tu ya kuwa ni wa jinsi ya kike kwani kama kijana aliyempa ujauzito huendelea na masomo hata kama sheria ipo hatujaona utekelezaji wake. Tunaomba Wizara ione hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la VETA tunaomba lipewe kipaumbele pamoja na FDCs ili wale watakaopewa kipaumbele kwa sehemu hizo wapate mafunzo na kuweza kujiajiri pindi watakapomaliza na hasa kupunguza wimbi la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee katika Mkoa wa Iringa. Wazazi wameweza kujenga ama kuhamasisha ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wasichana hasa shule ya sekondari Lyandembela Ifunda Mkoa wa Iringa na sekondari ya Mseke. Tunaomba Wizara iweze kushirikiana na TAMISEMI kuweza kusaidia katika umaliziaji wa majengo haya pamoja na kugaiwa walimu wa masomo ya sayansi, walimu watakaokuwa walezi wa wanafunzi kwa ajili ya kufundisha unasihi. Mheshimiwa Waziri utakapohitimisha uweze kutueleza mkakati wa kuwa na walimu wa ushauri nasihi mashuleni hasa shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa niweze kutoa pole kwa Mheshimiwa Heche kupotelewa na ndugu yake, Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi, Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naenda moja kwa moja katika kuchangia na naomba nianze na maneno yafuatayo ya aliyekuwa Rais wa Marekani Abraham Lincoln ambaye alishawahi kusema naomba ninukuu; “The philosophy of the school room in one generation will be the philosophy of the government in the next.” Ana maana kwamba falsafa ya elimu inayotolewa darasani kwenye kizazi cha leo ndiyo itakayokuwa hatma ya Serikali ya kesho. Tunaona jinsi ambavyo elimu yetu inakwenda ICU. Elimu yetu haiko katika muafaka kabisa, watoto wengi wanamaliza wakiwa hawana ujuzi, maarifa na ubunifu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika ripoti ya Kamati jinsi ambavyo shule binafsi zinaongoza kuanzia mwaka 2016. Mwaka 2016/2017 shule 10 bora zote za kitaifa zilikuwa za private na watoto bora wote wa kitaifa walikuwa wanatoka shule za private na ukiangalia kidato cha pili hivyo hivyo. Hii maana yake nini, maana yake kwamba kama kungekuwa hakuna shule zisizo za kiserikali division one, two na three zingekuwa hazipo kabisa. Sasa tufanye nini? Mimi naumia sana ninavyosikia kwamba mnazuia kukaririsha katika shule za private. Shule za private wanakaririsha kwa sababu wanataka wapate vijana wenye ujuzi, wenye maarifa, wasiende kama taburarasa, waende wakiwa wanaelewa nini wanachokifanya kwa kila kidato, kuanzia darasa la nne, saba, form one, two mpaka form four, sisi tunataka walingane, ama mnataka kutekeleza ule usemi wa Mheshimiwa Rais aliyosema kwamba matajiri wanataka waishi kama maskini. Kwa sababu wanapeleka watoto kule ili waweze kujikwamua katika elimu ninyi mnataka walingane wote tupate ma-zero, hili halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala la Bodi ya Walimu ambayo itakuwa ni independent board. Naomba hili lifanyike, Mheshimiwa Waziri unapokuja utuambie ni lini Bodi hii itaanza, kwa sababu itawianisha na kupima shule za private zinakaguliwa na kupewa masharti lukuki, lakini shule za Serikali hakuna masharti yoyote yanayotolewa. Iwe haina choo, iwe ina choo ni kuendelea, hii haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda sasa katika suala la walimu. Walimu wamekata tamaa, asilimia 37.8 ya walimu ndio wenye hamasa ya kufundisha, lakini asilimia 60 ndio hawana hamasa kabisa ya kufundisha. Ina maana hawa walimu kama mlivyosema kauli zile zinazotolewa mara kwa mara kwamba asiyetaka kazi aache.

Sasa walimu wameacha kazi wamebaki na utumishi. Mheshimiwa Waziri walimu wameacha kazi, wako na utumishi. Wamekata tamaa kwa sababu hawana motisha kama ambavyo wanapewa shule za private, walimu hawa unakuta anafanya bora liende, shule hakuna discipline, mwalimu anaenda anasoma anaweza akawa anafundisha au asifundishe, haya yanatokea Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, tukuombe Mheshimiwa uliangalie kwa jicho la ndani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la lugha ya kufundishia; kiingereza na kiswahili. Wamezungumza wenzangu hapa lugha za kufundishia ni jambo muhimu sana katika elimu. Usipokuwa na lugha ambayo umeamua ifundishiwe tunakuwa na mchanganyiko. Tumeona katika shule za private wanafundisha kwa Kingereza. Wanaaanzia darasa la tatu kiingereza wanakwenda nacho na shule za government ni Kiswahili lakini darasa la nne wanakutana na mtihani wa pamoja, sijui kusudi na maudhui yake mnataka wapate nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakienda kufika darasa la saba wanamaliza, wakienda sekondari hawa waliotoka shule za government wamesoma Kiswahili, wanaenda kukutana na lugha ya Kiingereza wanapata taabu, matokeo yake unakuta wanaanza kuibia. Kwa hiyo, kunakuwa na kazi kubwa sana watoto wanaibia wanasema wanapiga chabo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa toka form one mpaka form four, anakwenda form five mpaka form six anapiga chabo; unatarajia huyu mwanafunzi akija kupata kazi atapiga chabo wapi sasa wakati anafanya kazi? Kwa hiyo, hii ni changamoto Mheshimiwa Waziri uangalie kama

hakuna lugha maalum ya kufundishia muone jinsi mtakavyofanya. Mimi ni mwalimu by profession, lugha ya kiingereza unakuta zile phonetics watoto wadogo wanasoma kwa sauti, unajua sauti ndiyo inaingia na inakaa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa mchango wangu katika Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai, bila maji maisha hayawezi kwenda mbele. Naishauri Serikali iongeze tozo ambapo asilimia 70 ielekezwe vijijini na asilimia 30 iwe mijini, kwa kuwa kuna vijijini ndiyo kuna shida sana ya maji. Wanawake wa vijijini wamekuwa wakipata adha kubwa kwa ukosefu wa maji safi na salama. Wanashindwa hata kufanya shughuli za kiuchumi na maisha kuwa duni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka nyingi za maji zinadaiwa bili za umeme kwa kushindwa kulipa na wao pia wanazidai taasisi nyingi za Serikali, hivyo kufanya wananchi wanaolipa bili za maji kukosa maji. Naishauri Serikali iweze kulipa madeni ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa yenye Majimbo mawili ya Kalenga na Isimani imekuwa na shida kubwa sana ya maji safi na salama wakati kuna vyanzo mbalimbali vya maji kama vile Mto Mtitu, Ruaha pamoja na chanzo kinachoitwa Ibofwe. Maombi mbalimbali ya fedha yametolewa, lakini utekelezaji wake haupo na inakatisha tamaa sana kwa wananchi ambao ni wapiga kura.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iweze kutoa fedha ili maji yapatikane katika majimbo haya. Kuna maji ardhini ambapo pia, Serikali inaweza kuwekeza kwa kuchimba visima na maji yapatikane. Kwa hiyo, fedha ziwe zinatolewa kwenda kwenye Wizara hii ili waweze kufanya kazi ya kufumbua tatizo la maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali pia, ihimize uvunaji wa maji kwa kushauri kila anayejenga nyumba yenye bati kibali kitolewe tu kama ataweka na mfumo wa uvunaji maji, uchimbaji wa mabwawa na malambo hasa wakati wa masika ili kuvuna maji yatakayowasaidia wananchi; ni jambo la kutiliwa mkazo kwa Wizara hii. Naitaka Serikali/Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha aniambie utekelezaji wa haya niliyoeleza ukoje?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 (The Public Finance Act, 2001 No.4) inaitaka Serikali kuleta Bungeni bajeti ya nyongeza kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha za awali hazikutosha. Kwa sasa kuna baadhi ya miradi ya maendeleo inatekelezwa nje ya bajeti na hatujaona Serikali ikiomba bajeti ya nyongeza, mfano, ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ujenzi wa barabara za juu Dar es Salaam, ni baadhi tu. Kitendo cha Serikali kuamua kufanya matumizi bila kupata idhini ya Bunge ni uvunjaji wa Katiba na sheria na kitendo hicho kinaweza kuruhusu mianya ya rushwa na ubadhirifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo ya elimu ya juu, katika mwaka wa fedha 2016/2017 wanafunzi waliopata mikopo walikuwa 20,183 na wanafunzi takribani 27,053 walikosa mikopo. Mheshimiwa Rais katika kampeni za mwaka 2015 alisema yeye atakuwa muarobaini wa mikopo ya elimu ya juu. Utolewaji wa mikopo umekuwa na ubaguzi na usumbufu mkubwa, ni vyema Serikali katika Mpango wake iweke commitment ya kuandaa mfumo bora wa utoaji mikopo ili kuondokana na tatizo hili. Vilevile kumekuwa na tatizo au hakuna mfumo mzuri wa urejeshaji mikopo kwani sheria iliyopo inawaumiza sana waliopo katika ajira kukatwa asilimia kubwa kulingana na kipato wanachopata na kushindwa kuhimili maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haionyeshi uwezo katika kuziwezesha sekta binafsi kukua ili ziweze kuipunguzia Serikali mzigo wa walio wengi kukosa ajira. Wafanyabiashara walio wengi wamefunga biashara zao au kupunguza wafanyakazi kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji, kushuka kwa mapato kwa baadhi ya makampuni, mfano, viwanda vya vinywaji, makampuni ya kitalii, nyumba za starehe zikiwemo baa na hoteli. Mfumo huu unaangamiza kabisa sekta binafsi. Sekta binafsi ndiyo inayochangia mapato ya Serikali kupitia kodi inayokusanywa kwa bidhaa na waajiriwa. Vilevile kumekuwa na tabia ya kuwatishia wafanyabiashara kufunga makampuni kiholela, hii inaongeza umaskini kwa Watanzania walio wengi. Hivyo, nashauri Mpango huu uzingatie na uweke kipaumbele katika kuwezesha sekta binafsi kufanya kazi bila bughudha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda, kama Tanzania ya viwanda ni uhalisia na siyo ndoto basi suala hili lisingekuwa ni la matamko kwani hivi karibuni Waziri wa TAMISEMI amenukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa kila mkoa kujenga viwanda 100 ambapo hadi Desemba, 2018 katika Mikoa yote Tanzania Bara inatakiwa kuwa na viwanda 2,600. Kama miaka yote iliyopita imeshindikana kufufua tu viwanda vilivyokuwepo hii leo ya mwaka mmoja itawezekana? Kwa Mkoa wangu wa Iringa tu kulikuwa na viwanda vifuatavyo:-

1. Kiwanda cha Vifaa vya Nyumbani kama masufuria kiliitwa IMAC;

2. Kiwanda cha Nyuzi na Nguo (COTEX);

3. TANCUT Almasi;

4. Kiwanda cha Magurudumu ya Magari (VACULUG);

5. Kiwanda cha Tumbaku;

6. Kiwanda cha Coca cola; na

7. SIDO

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyote hivyo havipo tena. Maelekezo hayo ya viwanda 100 yanashangaza kwa sababu kama mikopo kwa sekta binafsi imepungua na kama Serikali haifanyi biashara hivyo viwanda vitajengwa na nani? Serikali inabidi ijipambanue ili kujua mfumo upi inaufuata kama ni uchumi wa kijamaa au uchumi wa kibepari au soko huria ili ijikite madhubuti katika mfumo itakaoamua kuufuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ndicho kinachotoa ajira kwa Watanzania zaidi ya asilimia 70. Katika Mpango huu bado sekta hii inaendelea kupuuzwa na matokeo yake ni kudorora kwa uchumi na hiyo Tanzania ya viwanda inaendelea kuwa ndoto. Kuna changamoto kwenye kilimo kwani wakulima hawapati pembejeo kwa wakati, kilimo cha umwagiliaji hakitiliwi mkazo, Maafisa Ugani hawako wa kutosha, baadhi ya mabenki kutokopesha wakulima kwa madai kwamba mikopo katika sekta ya kilimo huwa haina uhakika wa kurudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu Serikali inatakiwa kubuni utaratibu maalum wa kuziwezesha benki za biashara kuweza kutoa mikopo hiyo. Wanawake na vijana wakiwezeshwa hasa katika mikopo ya kilimo na ufugaji ukosefu wa ajira utapungua.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima walipata ari ya kujihusisha katika kilimo hususan kilimo cha mahindi na alizeti katika Mkoa wa Iringa japo gharama za pembejeo ni ghali na wakafanikiwa kupata mazao hayo kwa wingi. Kitu cha kushangaza ni kutolewa kwa maagizo toka Serikalini ya zuio au uuzaji mazao yao hasa mahindi nje ya nchi na kuathiri wakulima hao kujipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iweze kuruhusu wakulima hao kufanya biashara hiyo ya kutafuta namna ya kuwafanya wakulima hawa waweze kuendelea na kilimo kwani zuio hilo limeshusha bei ya mahindi hadi kufikia sh.6000 kwa debe moja gharama ambayo haitoshelezi hata ununuzi wa mfuko mmoja wa mbolea kwa gunia moja la mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa wanashughulika pia na kilimo cha nyanya na mbogamboga. Changamoto kubwa katika kilimo hiki ni ukosefu wa elimu hasa kwa wakulima kuhusu kilimo cha kisasa. Hii husababisha uzalishaji mdogo usio bora kwa zao hilo. Aidha, changamoto ya pembejeo na magonjwa ya nyanya, Serikali itoe elimu ya kilimo cha mazao haya na iyape kipaumbele. Itengwe bajeti ya kutosha kuwezesha shughuli za tafiti kwa ajili ya namna ya kutibu magonjwa ya nyanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Wakulima walio wengi wanashindwa kukuza kilimo kwa kukosa mitaji. Benki ya Kilimo, (TADB) iliomba shilingi bilioni 800 lakini hadi Desemba, 2017 walikuwa na mtaji wa bilioni 66.7 tu. Hivi ukijiuliza watawafikia wananchi wangapi kwa fedha hiyo tu? Naishauri Serikali iweke msisitizo katika upelekaji wa fedha katika benki hiyo kwani itawafikia wakulima walio wengi na kusaidia kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji. Serikali iweze kutoa kipaumbele katika kilimo cha umwagiliaji kwani ndio utatuzi hasa pale ambapo kunakuwa na uhaba wa mvua. Ni asilimia ndogo sana inatumika kwa kilimo hiki, Serikali ikiweza kujenga mabwawa ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia katika suala la kazi na wafanyakazi hasa Watendaji wa Vijiji ambao wameondolewa kazini kwa sababu ya kiwango chao cha elimu, yaani darasa la saba. Wafanyakazi hawa wamelitumikia Taifa letu wakati likiwa kwenye uhaba mkubwa wa watumishi na wengine walishindwa kujiendeleza kwa sababu ya mazingira halisi ya maslahi yao. Kuwaondoa bila hata kupata marupurupu siyo haki kwao. Nashauri Serikali itazame upya suala hili, kwani linaleta chuki kwa Serikali yao, kama hawatarudishwa kazini, basi wapewe stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la viwanda. Viwanda 3,000 ambavyo inasemekana vipo, ni vema vikaainishwa ili Watanzania waweze kutambua vipi ni viwanda vikubwa, vya kati na viwanda vidogo. Vilevile tujulishwe viko wapi kwa ajili ya utambuzi. Nashauri pia Serikali iweke mazingira tulivu ya uwekezaji ili kupata wawekezaji wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee kuhusu suala la walemavu. Pamoja na kwamba hatua mbalimbali zimekuwa zikifanywa kuwawekea mazingira mazuri watu wenye ulemavu, bado kuna tatizo la tengeo la fedha hasa kwa ajili ya vifaa tiba vya albino (mafuta) pamoja na huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ifanye utafiti wa kina ili kubaini watu wenye ulemavu wasio na uwezo wa kujitibu wapatiwe matibabu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa ushauri kwa Serikali kwamba suala la kuhamisha Walimu wa Shule za Sekondari kwenda Shule za Msingi liangaliwe kwa jicho la kipekee, kwani kuna changamoto katika utekelezaji wake. Walimu hao wapewe fedha za uhamisho, wapatiwe mafunzo ya kufundisha elimu ya msingi (child psychology), saikolojia ya mtoto ili wakafundishe kwa ufanisi. Vinginevyo, badala ya kujenga, tutabomoa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Michezo, imekuwa ikikumbwa na changamoto ya gharama kubwa ya vifaa vya michezo inayotokana na kodi inayotozwa hasa vifaa vinavyotolewa kama msaada kwa mfano kulikuwa na nyasi bandia ambazo hadi sasa sijui suala hilo limefikia wapi kwani zilizuiliwa bandarini. Waziri atupe majibu ya suala hilo. Kuna uvamizi na kubadilishwa kwa matumizi ya viwanja vya michezo. Serikali itupe majibu na pia kuna uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa burudani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ni biashara, hivyo ni lazima tufanye uwekezaji kama biashara yoyote inavyotakiwa ifanyike. Uwekezaji lazima uanzie katika ngazi ya chini kwa kutayarisha watoto wetu kuwa wachezaji wazuri kwa michezo mbalimbali au sanaa na utamaduni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za michezo na utamaduni katika halmashauri zinakuwa chini ya Idara ya Elimu msingi ambayo ina majukumu mengi ya kushughulikia elimu na sehemu kubwa ya bajeti yake matumizi ya kawaida inatoka Serikali Kuu. Kitengo cha michezo kinamezwa na shughuli za elimu, hivyo kushindwa kutimiza wajibu na majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri zile asilimia 10 za wanawake na vijana ziwekezwe kwa kuwapa mafunzo vijana na wanawake katika vyuo mfano, TASUBA ili wapate ujuzi na wawekeze katika sanaa. Halmashauri zinaweza kusomesha hata vijana wawili kila mwaka. Hii ni sawa na
kuwapa ndoano badala ya kuwapa samaki. Tusiwape fedha tu, mafunzo ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Kilimanjaro Marathon. Michezo hii ilianza kufanyika Mkoa wa Kilimanjaro lakini pia Mkoa wa Mwanza wameanzisha marathon. Mapendekezo au ushauri wangu ni kuwa; Serikali iangalie namna watakavyogawa mikoa na shughuli mbalimbali na tofauti ili iweze kuwa tulivu. Mfano, Mikoa ya Kusini wanaweza kuwa na mashindano ya vifaa vya majini kama vile mashua na boti na mikoa mingine itafutiwe michezo kulingana na mazingira yake kama vile mashindano ya magari na kadhalika hii itasaidia wananchi kujua na kutilia maanani sehemu ambayo mchezo anaoutamani na mahali atakapokwenda kufanyia ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa masikitiko makubwa sana kwa ukosefu wa maji katika majimbo ya pembezoni ya Mkoa wa Iringa. Wananchi wanapata adha kubwa sana. Katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 271 namba 63, 65 na 66 jinsi ambavyo Wizara na watendaji wake wamefanya kazi ya ku–copy and paste kwani wameonesha visima hivyo vipo katika Mkoa wa Iringa wakati visima hivyo vipo Mkoa wa Njombe na si Iringa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya makosa yanasababisha adha kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa hasa Wilaya ya Iringa, Jimbo la Kalenga na Isimani ambapo kuna changamoto kubwa sana ya maji. Kuna shida kubwa ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagliaji ya vijiji vya Ibumila na Mgama ambavyo vipo kata ya Mgama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kalenga kumekuwa na uchakavu wa miundombinu ya maji yote, hivyo tunaiomba Serikali itoe pesa wananchi wapate maji. Vivyo hivyo kata za Kihorogota na Kisinga vilivyopo Jimbo la Ismani vipatiwe maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na watendaji wenzake kwa kazi kubwa wanayofanya katika Wizara hii. Hata hivyo, napenda kushauri yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ugatuaji wa madaraka D by D halitekelezwi inavyopaswa kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara hii, ningependa kufahamu ni wapi wanapokutana kuweka masuala ya elimu sawa? Hizo hati idhini walizonazo zinawakutanisha kwenye masuala gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano suala la Walimu wa Shule za Sekondari kuhamishiwa katika Shule za Msingi ni mambo gani wamejadiliana na Wizara ya Elimu, hususan, suala la mafunzo (Induction Course) kwa Walimu hawa? Nani atatoa mafunzo ya Child Centered Psychology ambayo ni kipaumbele kwa Walimu hawa kwa kuwa, tunafahamu kwamba, Wizara ya Elimu ndio mtoaji wa mafunzo? Je, Wizara imeshawaandalia fedha zao za uhamisho au posho ya usumbufu? Mheshimiwa Waziri anapohitimisha atuambie ni nini watakachokitekeleza kwa Walimu hawa hasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa Walimu shule za msingi na Walimu wa sayansi kwa shule za sekondari. Tatizo hili ni kubwa, katika Mkoa wa Iringa hadi 2017 kulikuwa na upungufu wa Walimu shule za msingi 785, kwa Walimu wa sekondari sayansi mahitaji yalikuwa 1,290, waliopo 619, upungufu Walimu 671. Tatizo hili ni kubwa, hivyo nashauri Wizara iajiri Walimu wa kutosha na wapelekwe hasa shule zilizopo vijijini na wapewe motisha ya mazingira magumu ya ufundishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya; kuna tatizo ama upungufu wa watumishi katika sekta hii, hasa kwa Mkoa wa Iringa katika zahanati na vituo vya afya, Wilaya ya Kilolo na Iringa Vijijini hasa. Naiomba Serikali iajiri watumishi hawa na kupelekwa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Barabara, TARURA. Hiki ni chombo muhimu sana, lakini kina changamoto ya uhaba wa fedha. 30% wanayopata ya fedha ni kidogo sana kukamilisha miradi. Naungana na maoni ya Kamati kuongeza hadi angalau 50% ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba barabara inayounganisha Wilaya toka Iringa Manispaa kupitia Jimbo la Kalenga, Kata ya Luhota na Magulilwa kwenda Wilaya ya Kilolo ambazo ni kilometa chache tu zitengewe bajeti na kujengwa kwa kiwango cha lami kwani kuna wafanyabisahara na wakulima wa mazao mbalimbali kama vile matunda, mahindi, njegere. Miti ambayo inazalisha mbao hupata tabu kupita katika barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na maoni ya Kamati kuhusu suala la kuwasilisha Bungeni Muswada wa kusudio la kutunga sheria itakayosaidia kusimamiwa utengaji, utoaji na urejeshaji wa fedha zinazotokana na 10% ya mapato ili kuwezesha wanawake na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala la kuondoa kodi au kupunguza kodi kwa taulo za kike ili kuwezesha watoto wa kike hasa kutoka katika familia maskini kumudu gharama hizo na kuweza kuhudhuria masomo kikamilifu na ikiwezekana wapewe bure kama ilivyo katika nchi za Kenya, Shelisheli na nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utawala bora. Kumekuwa na kawaida katika Awamu hii kutoongeza mishahara kwa wafanyakazi wakati maisha kila siku yanapanda kwa gharama za bidhaa. Wafanyakazi wengi hawana raha kwa kutokuweza kukidhi mahitaji na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi. Serikali iweze kupandisha au kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukiukwaji wa sheria na taratibu. Mfano Mkurugenzi kutotii mamlaka ya Waziri mwenye dhamana mfano Mkurugenzi wa Tunduma Mkoa wa Songwe, Mkuu wa Wilaya na wengineo wateule wa Rais kutofuata taratibu. Hii ni kinyume kabisa na utawala bora tunaotarajia, Serikali ilifanyie kazi suala hili ili wananchi wapate haki yao ya kupata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.