Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Grace Victor Tendega (7 total)

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kuwa REA III imeanza Machi, 2017. Kwa kuwa wananchi katika vijiji hivyo vya Wangama, Ikuvilo, Tagamenda, Lupembelwasenga pamoja na Lyamgungwe ni wakulima na wanajihusisha na kilimo cha umwagiliaji na kuna wawekezaji ambao wameonesha nia ya kujenga viwanda na tunasema tunahitaji Tanzania ya viwanda lakini umeme haupo. Naomba commitment ya Serikali ni lini watapata umeme kwa sababu imekuwa ni muda mrefu kutopatiwa umeme katika maeneo hayo ili wanufaike na viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika kipengele
cha kwanza majibu ya Waziri ni tofauti kabisa na hali halisi ya eneo hilo la Malulumo kwa sababu mimi natokea eneo hilo na wanasema utekelezaji umefanyika kwa 90%. Je, Waziri yuko tayari kuongozana na mimi akaone huo utekelezaji wa 90% uliopo maeneo yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na swali la pili, niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Grace kwenda kwenye eneo lake ili kuangalia utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Grace tukimaliza Bunge tu mguu mmoja mimi na wewe Iringa tukamalize kazi hiyo, lakini kwa ruhusa yako Mwenyekiti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Grace na Wabunge wote wa Mkoa wa Iringa kwa jinsi ambavyo wanafuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme. Niwahakikishie kwamba tarehe 21 Machi, 2017 tulizindua rasmi utekelezaji wa Mradi wa Umeme Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Iringa na eneo la Iliwa kwa Mheshimiwa Mwamoto ndipo tulipofanyia uzinduzi kwa niaba ya mkoa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie kabisa Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Iringa pamoja na Mufindi, Kilolo, Njombe, tumeshawakabidhi wakandarasi wawili, NACROI na NAMIS na wameshaanza utekelezaji wa kazi hiyo. Kwa hiyo, kuanzia Machi tumeshaanza kutekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji ambavyo amevitaja Mheshimiwa Grace vya Wangama, Lupembelwasenga, Tagamenda na Mseke pamoja na vijiji vingine ambavyo amevitaja na kwa Mheshimiwa Mwamoto vitapatiwa umeme katika awamu hii ya mradi. Nimeenda kwa Mheshimiwa Mwamoto na Waheshimiwa Wabunge wengine, nimeenda Nang’uruwe, Kihesa Mgagao na huko tumeshawapelekea umeme. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba utekelezaji wa mradi huu umeanza na utakamilika mwaka 2020/2021.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nitoe masikitiko makubwa sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, ambapo tarehe 8 Juni, 2016 niliuliza swali kuhusu vijiji na kata hizo hizo na aliyekuwa Naibu Waziri na sasa ni Waziri mwenye dhamana TAMISEMI alinipa majibu ambayo yalikuwa yanaeleza kwamba vijiji hivyo vimetengewa bajeti ya shilingi milioni 49.5 ambayo itatekelezwa mwaka 2016/2017. Mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea, ni Bunge hili hili ambalo linatoa majibu hayo na leo tena nimepewa asilimia hiyohiyo 49.5 kwamba itatekelezwa 2018/2019. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa wananchi hawa, toka mwaka 1995 mpaka leo ni upembuzi yakinifu unafanyika, ni lini hawa wananchi watapata maji? (Makofi)
MheshimiwaMwenyekiti, swali la pili, ni kwa nini hawakufanya upembuzi wa kina wakati bajeti ilitengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, ni kweli kwamba usanifu wa kina haukufanyika ule wa zamani, lakini kwa sasa tunatarajia usanifu kina utafanyika mwaka 2018/2019 kwa ajili ya utekelezaji wa kumaliza kabisa matatizo ya maji kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ambalo lilikuwa ndiyo la kwanza, ni kwamba kazi ambazo zimefanyika kuanzia 2016 mpaka Desemba, 2017 nimesema hapa kwamba tumejenga visima sita katika Kata za Magulilwa, Luhota, Maboga na Mgama. Hii kazi imefanyika na taarifa hizi zimetoka kule kule kwenye Halmashauri yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taarifa za kina zaidi namuomba sana tushirikiane naye baada ya kikao hiki ili tuweze kushauriana vizuri namna bora ya kuhakikisha kwamba tunamaliza matatizo ya wananchi kwenye maeneo hayo.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kabisa yanaonyesha jinsi ambavyo walimu wetu wamekuwa wakikosa nyumba za kuishi, walimu wa sekondari 52,000 hawana mahala pa kuishi na walimu 130,300 wa shule za msingi hawana nyumba za kuishi. Tumesema tunataka kuwa na elimu bora katika nchi yetu na hatufahamu walimu wanaishi wapi.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka sasa wa kuamuru Jeshi la Polisi liweze kujenga nyumba hizi za walimu kama walivyofanya kwa Mererani kuzuia ile migodi yetu, tatizo hili ili liweze kuisha kwa haraka?
Swali la pili, walimu wamekuwa wakikosa udhamini katika mabenki mbalimbali kwa kutokuwa na mali za kudhaminiwa na taasisi alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri ni hizo ambazo huwezi kudhaminiwa kama huna dhamana ya vitu visivyohamishika kama viwanja, magari na vitu vingine na tunatambua hali za walimu wetu zilivyo.
Je, sasa Serikali haioni haja kwamba ni wakati muafaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iweze kuwa dhamana kwa walimu wetu wakati bado wakiwa kazini na siyo baada ya kustaafu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nisisitize kwamba katika jibu langu la msingi ile takwimu niliyoitaja kwa faida ya Bunge lako tukufu haikumaanisha kwamba walimu hao hawana makazi kabisa. Nimesema kwamba walimu hao wanaishi katika aidha, nyumba za kupanga au nyumba zao binafsi, hilo ndilo jibu langu la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ya swali lake kwamba kwa nini Serikali isiamuru Jeshi la Polisi kujenga nyumba za walimu nchi nzima, hilo ninaomba sana majeshi yetu yana kazi zake maalum ambayo yamepewa kufanya na waliojenga ukuta wa Mererani siyo Jeshi la Polisi ni Kitengo cha Ujenzi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Tumekuwa tukiwapa kazi nyingi sana, SUMA JKT kujenga nyumba za walimu kujenga nyumba za walimu katika mahali pengi. Hata kwake kule Iringa tumewapa sehemu nyingi tu SUMA JKT kujenga nyumba na tutaendelea kuwapa mikataba ya kujenga nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kwamba ujenzi wa nyumba ambao unafanywa na Serikali utaendelea kuwa kidogo kidogo kwa sababu unategemea sana bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, napenda nimuondoe wasiwasi kuhusu dhamana. Karibu mabenki yote na taasisi zote zinazokopesha hakuna dhamana zaidi ya mshahara wa mtumishi. Kinachotakiwa tu ni kwamba mtumishi asiwe anadaiwa mikopo mingine hilo ndiyo jambo la msingi, kama mtumishi hadaiwi mikopo mingine anao uwezo wa kukopa na ataamua mwenyewe, je, akope kwa kurejesha miaka mitatu au akope kwa kurejesha miaka 10 au akope kwa kurejesha miaka 25 ni yeye mwenyewe katika makubaliano ya fomu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuwasisitiza watumishi wote nchi nzima na Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wako chini yangu nataka niwaambie kwamba mikopo hiyo ya watumishi ipo, waingie makubaliano maalum na hizo taasisi na mabenki ili kusudi watumishi waweze kukopesha waweze kujenga nyumba zao binafsi. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Ibofwe uko Mkoani Iringa ambao unahudumia vijiji 10. Nilikwishauliza swali la msingi nikajibiwa kwamba shilingi milioni 49 zitatolewa baada ya kutoka certificate. Certificate ilishatolewa pesa hazijapatikana toka mwaka jana, naomba kujua ni lini pesa hizo zitatolewa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitumie nafasi hii kumjibu Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa maji ni uhai na sisi kama Wizara ya Maji hatupo tayari kupoteza uhai wa wana Iringa, namuomba Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge tukae na wataalam wetu tuangalie namna ya kuzipeleka fedha hizo wananchi wapate maji.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nasikitika Waziri anavyojibu, anaingiza suala la Mbunge wa Jimbo wakati mimi niliuliza swali langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, majibu ya Waziri hayajaniridhisha kabisa. Kuna vijiji vya Kimala, Idete, Uluti, Nyamuhanga, Ibofwee na Itimb. na vingine ambavyo sijavitaja wanajihusisha sana na kilimo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzalisha zao la mbao, ambayo yote haya yanahitaji mawasiliano kwa ajili ya kupata soko. Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa wananchi hawa wanapata mawasiliano ili waweze kuuza mazao yao na kupata masoko wanayoyahitaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Waziri amesema minara hiyo imejengwa na inatoa huduma kama kawaida, yuko tayari twende akaone hiyo minara anayosema inatoa huduma ili ahakikishe mwenyewe kwamba huduma hiyo haipatikani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Tendega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuondoe masikitiko kwa sababu hizi shughuli tunazifanya kwa kuwa tunazijua na tumeshatembelea na kufanya survey ya kutosha nchi nzima kujua maeneo gani yana shida ya mawasiliano critical na eneo gani ambalo lina shida ya mawasiliano ya kawaida ambayo yanahitaji kuongezewa coverage na ni maeneo gani ambayo yana shida za mawasiliano kwa vipindi tu vifupi kutokana na kufungiwa solar badala ya umeme wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujibu maswali yake kuhusu eneo la Kimala, Kidete na vijiji vinavyohusiana, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya ziara baada ya Bunge hili la bajeti kwenye maeneo yote pamoja na maeneo ya Kata nzima ya Kising’a najua kuna changamoto za mawasiliano, lakini nitafanya ziara kwenye Kata ya Mahenge, maeneo ya Magana na Ilindi ambako kuna shida kabisa ya mawasiliano, vilevile nitafanya ziara kwenye Kata ya Ibumu kwenye Kijiji cha Ilambo kuangalia kuhusu changamoto ya mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nitakuwa tayari kuongozana naye pamoja na Mbunge wa Jimbo kuangalia maeneo hayo. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda Serikali isikwepe wajibu wake wa kuhudumia watu wasiojiweza. Natambua kabisa kuwa kuna walemavu wenye uwezo lakini watu wengi wenye ulemavu wana matatizo mengi; kuna wale ambao ni yatima, kuna wengine ambao wametelekezwa na kuna wengine ambao kaya zao ni maskini sana. Ni kwa nini Serikali isiwajibike kuwahudumia watu hawa wenye ulemavu hasa kwa kuwatambua na pili kuwapatia bima ya afya bure? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema wagonjwa kuna wagonjwa wengi sana wa msamaha ambao wako katika hospitali zetu. Sawa wako wagonjwa wengi lakini ni lini Serikali sasa itatekeleza wajibu wake wa kutoa ruzuku katika hospitali zetu za mikoa au hospitali zetu za rufaa kwa sababu hawa wagonjwa ambapo wengine ni watu wenye ulemavu, watoto umri chini ya miaka mitano na wazee wanakwenda katika hospitali hizi kutibiwa na hizi hospitali zinakuwa na watu wengi ambao wanatakiwa kupata vifaatiba na vitendanishi? Ni lini Serikali itatoa ruzuku katika hospitali zetu ili ziweze kujikimu na kutoa huduma bora? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kutoa huduma za afya na haijawahi kusitisha kutoa huduma ya afya kutokana na sababu eti kwamba mtu anashindwa kugharamia matibabu. Hilo lipo vizuri ndani ya Sera yetu ya Afya na kuna makundi ambayo tumeyaainisha katika sera ambapo watu wanapata matibabu bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la walemavu kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, si kila mlemavu hana uwezo wa kupata matibabu, nataka niweke msisitizo. Ndiyo maana nimesema katika Sera hii Mpya tutaweka utaratibu mzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya sasa kati ya asilimia 60 - 70 ya wagonjwa ambao wanafika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya wanapata matibabu bure. Sasa hivi tunataka tuweke mfumo mzuri na kuhuisha na mifumo mingine kama ile ya TASAF kuhakikisha kwamba tunawatambua tu wale ambao kweli hawana uwezo na wanahitaji kupata matibabu. Tutakapokuja na huu utaratibu wa bima ya afya kwa wananchi wote tutakuwa na kundi dogo sana ambalo limebaki ambalo litakuwa linagharamiwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza kwa nini Serikali haipeleki ruzuku. Nimthibitishie Mheshimiwa
Mbunge na bahati nzuri naye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na analijua na hivi karibuni tumetoa taarifa ya utekelezaji ya nusu mwaka, Serikali inapelekea mishahara hatujashindwa kupeleka mishahara, dawa na hela ya uendeshaji. Hakuna hospitali ya rufaa ya mkoa ambayo haijapata huduma zote hizo ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna vyanzo vingi vya mapato ndani ya hospitali. Pamoja na ruzuku ya Serikali tuna fedha za papo kwa papo, fedha za bima na nyingine zinapata basket fund. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ninapozungumza watoto njiti nina maana wanazaliwa kabla ya miezi tisa haijatimia:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; dawa ya kusaidia mtoto ili aheme vizuri inayoitwa surfactant inauzwa shilingi laki sita kwa dozi moja na inategemea hali ya mtoto ambayo amezaliwanayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama una mtoto mmoja shilingi laki sita, kama umejifungua watoto wawili ni shilingi 1,200,000/=. Na watoto walio wengi wanatoka katika familia zenye hali duni na kipato cha hali ya chini, kama wanashindwa tu kwenda nao kliniki itakuwa na hii shilingi laki sita. Je, sasa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, dawa hizi zinatolewa bure, ili kunusuru maisha ya watoto hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba, likizo ni siku 84 kwa mtoto mmoja na siku 100 kwa watoto mapacha, lakini hawa ni watoto njiti. Kama amejifungua kabla ya miezi tisa tusema miezi saba ina maana kuna miezi miwili ambayo iko kabla ya miezi ile tisa. Sasa je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, wazazi wote wawili, baba na mama, wanapata likizo yenye malipo kwa miezi hiyo iliyopo kabla ili waweze kutunza hawa watoto njiti? Asante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Grace tendega kwa swali lake zuri. Na nianze kwa kutoa tafsiri ya mtoto njiti, watoto njiti wako katika makundi mawili; kuna wale ambao wamezaliwa kabla ya wiki 37 na kuna wale ambao wanazaliwa na uzito mdogo kuliko ule ambao tunatarajia, kwa maana ya kilo 2.5 kwa hiyo, wote hawa tunawaweka katika group hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, watoto ambao wanazaliwa njiti mara nyingi wanazaliwa na changamoto mbalimbali, hususan wale ambao wamezaliwa kabla ya umri wa wiki 37. Na moja ya changamoto ambayo wanayo ni matatizo ya kupumua, mapafu yanakuwa hayajakomaa na wanahitaji dawa ambayo ni surfactant kukomaza yale mapafu. Na nikiri kweli, gharama za surfactant ni kubwa na sisi kama Seriakali tumeliona hilo, tunajaribu kuliangalia utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, tunatoa afua kwa akinamama ambao wamezaa watoto njiti. Hatutaweza kuitoa bure, lakini tutaweka utaratibu ambao unaweza ukapunguza gharama katika utaratibu ambao tunao sasa hivi wa kuagiza dawa moja kwa moja kutoka viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linahusiana na kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa wazazi ambao wana watoto njiti:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, watoto njiti wanazaliwa wakiwa na changamoto nyingi pamoja na matatizo ya kupumua, wengine wanazaliwa na viungo bado havijakomaa, ikiwa ni pamoja na ubongo na wengine wanaweza wakapata matatizo mengine endapo hawatapata matunzo ya karibu. Lakini jiwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, sasa hivi kwa mujibu wa teknolojia watoto ambao wanazaliwa hata akiwa na wiki 22 kwa maana ya miezi mitano, wana uwezo mzuri sana wa kuweza kukua na kuishi vizuri. Na mtoto ambaye ameweza kuzaliwa na…

MWENYEKITI: Muda, muda.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalotaka kulisema kwa kifupi tu kwamba, Serikali inaweza ikaliangalia suala hili kwa maana ya kuwa, pale kama mtoto ana matatizo mzazi anaweza akawa anapewa ruhusa kwa mujibu wa kanuni na taratibu ambazo tunazo.