Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joseph Michael Mkundi (37 total)

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Wilaya ya Ukerewe inajumuisha visiwa 38 na kati ya hivyo, visiwa 15 hutumika kwa makazi ya kudumu lakini huduma za kijamiii hasa afya siyo nzuri:-
(a) Je, Serikali inachukua hatua zipi za makusudi za kunusuru maisha ya watu hasa akinamama wajawazito na watoto wanaokufa kutokana na ukosefu wa huduma bora za afya katika visiwa hivyo?
(b) Je, ni lini Maabara katika kituo cha afya Bwisya katika Kisiwa cha Ukara itakamilika na kupewa wataalam ili kutoa huduma ya upasuaji kunusuru maisha ya wananchi wa kisiwa hicho na visiwa vya jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya utoaji wa huduma za afya Ukerewe zinatokana na jiografia ya eneo lenyewe kuwa linazungukwa na maji. Kwa kutambua hali hiyo, Serikali imejenga Hospitali ya Wilaya katika kisiwa cha Nansio, vituo vya afya viwili na zahanati 17. Hata hivyo, Serikali inatambua bado zipo changamoto ambazo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi kupitia bajeti za Halmashauri kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa wananchi wa kisiwa hiki hupelekewa huduma za afya kwa njia ya mkoba pamoja na kliniki ambazo huratibiwa na Madaktari pamoja na Wauguzi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto, Serikali imejenga jengo la upasuaji katika kituo cha afya cha Bwisya. Tayari kituo hicho kimepatiwa Daktari Msaidizi na Mtaalam wa dawa za usingizi ili kuanza huduma za upasuaji. Changamoto inayoendelea kushughulikiwa ni upatikanaji wa vifaa na nishati ya umeme na maji ambapo mpaka sasa shughuli za kuweka umeme katika kituo hiki zinaendelea.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI (K. n. y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Ni zaidi ya miaka mitano sasa tangu Meli ya MV Butiama isitishe huduma zake katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Nansio (Ukerewe) hali inayosababisha shida na usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa Ukerewe.
(a) Je, ni lini meli hiyo ya MV Butiama itatengenezwa na kuendelea kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta meli mpya sasa ikizingatiwa kuwa meli ya MV Clarius imechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, meli ya MV Butiama ambayo ilikuwa inatoa huduma ya usafiri majini kati ya bandari ya Mwanza na bandari ya Nansio - Ukerewe ilisitisha huduma hiyo mwaka 2010 baada ya engine yake kupata uharibifu mkubwa na kukatika muhimili wake (crankshaft). Kufuatia uharibifu huo tathmini ilifanyika na kubaini kuwa injini hiyo isingefaa tena kutumika kwa ajili ya usafirishaji wa aibiria na mizigo na kwamba inabidi iununuliwe engine mpya pamoja na gear box yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ya huduma za meli MSCL ilikamilisha mchakato wa kupata engine stahiki kwa ajili ya meli hiyo na gharama elekezi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli imetenga kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya matengenezo ya meli ya MV Butiama. Aidha, kulingana na tathmini iliyofanyika matengenezo ya meli hiyo yanategemewa kukamilika ndani ya miezi wa kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mipango thabiti ya kujenga meli mpya zitakazotoa huduma ya usafiri na usafirishaji katika Ziwa Victoria na maziwa mengine makuu ya Tanganyika na Nyasa. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi bilioni 21.0 ikiwa malipo ya awali ya asilimia 50 kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria.
MHE. JOHN W. HECHE (K.n.y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Ni miaka mitatu sasa tangu barabara ya Bunda – Kisorya - Nansio iwekwe katika mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami lakini ujenzi huo unasuasua tu.
(a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika?
(b) Je, Serikali ina kauli gani juu ya ujenzi wa daraja kati ya Kisorya (Bunda) na Lugezi (Ukerewe)?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nyamuswa (Bunda) - Kisorya - Nansio yenye urefu wa kilometa121.9 inaunganisha Mikoa ya Mara na Mwanza.
Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika awamu ya tatu; Nyamuswa - Bunda - Bulamba (kilometa 55); Bulamba – Kisorya (kilometa 51) na Kosorya - Nansio (kilometa 15.9) ikihusisha pia ujenzi wa daraja kubwa kati ya Kisorya na Lugezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hii umekamilika isipokuwa sehemu ya Kisorya - Nansio (kilometa 15.9). Ujenzi wa kiwango cha lami umeanza kutekelezwa Disemba 2013 kwa sehemu ya Bulamba - Kisorya (kilometa 51) na unaendelea. Hadi sasa ujenzi wa sehemu hii ya barabara umekamilika kwa asilimia 14. Hata hivyo, ujenzi wake umekuwa ukisuasua kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya mkandarasi. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha ili kukamilisha ujenzi wa barabara hii.Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeanza mipango ya ujenzi wa daraja kati ya Kisorya na Lugezi linalounganisha Mikoa ya Mara na Mwanza ambayo imekamilisha upembuzi yakinifu na kwa sasa usanifu wa kina unaendelea.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Ni zaidi ya miaka mitano sasa tangu Meli ya MV Butiama isitishe huduma zake katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Nansio (Ukerewe) hali inayosababisha shida na usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa Ukerewe.
(a) Je, ni lini meli hiyo ya MV Butiama itatengenezwa na kuendelea kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta meli mpya hasa ikizingatiwa kuwa meli ya MV Clarius imechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.6 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ili kufanya matengenezo makubwa ya meli ya MV Butiama iliyositisha kutoa huduma zake tangu mwaka 2010 kutokana na hitilafu kubwa ya injini zake. Zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo zilikwishatangazwa na sasa kazi ya uchambuzi wa kina inaendelea. Matarajio yetu ni mkandarasi kuanza ukarabati huo mwezi Machi, 2017 na kumaliza mwezi Novemba, 2017 (b) Kuhusu mpango wa kujenga meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuimarisha huduma ya usafiri wa majini katika eneo hilo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI alijibu:-
Kisiwa cha Ukerewe kina vivutio vingi vya utalii vinavyoweza kuiingizia nchi yetu pesa nyingi za kigeni vikiwemo mapango ya Handebezyo, Makazi ya Mtemi Rukumbuzya, Jiwe linalocheza la Nyaburebeka huko Ukara na kadhalika.
Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuimarisha na kujenga mazingira na kuvitumia vivutio hivyo ili kuongeza pato la Taifa na wananchi wa Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sura ya Nne aya ya 4.2.7 ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 - 2020/2021) unasisitiza pamoja na mambo mengine upanuzi wa wigo wa vivutio vya utalii na utalii utokanao na vivutio vya urithi wa utamaduni (The heritage tourism)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kuzihusisha Halmashauri husika inakamilisha orodha ya vivutio vyote vya utalii ikiwa ni pamoja na vivutio vya malikale nchini ili kuweka utaratibu wa kuvisajili, kuviboresha na hatimaye kuvitangaza na kuviuza kwa watalii wa ndani na wa nje. Zoezi hili linatengemea kukamilika mwaka wa 2017/2018. Vivutio vya mapango ya Handebezyo, Makazi ya Mtemi Rukumbuzya na Jiwe linalocheza la Nyaburebeka vilivyoko katika kisiwa cha Ukara katika Halmashauri ya Ukerewe ni miongoni mwa vivutio hivyo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Serikali imeondoa tozo mbalimbali zilizokuwa kero kwa wananchi katika sekta ya uvuvi lakini bado kuna mkanganyiko ni tozo zipi zimefutwa na zipi zinaendelea.
(a) Je, Serikali inaweza kuainisha aina ya tozo zilizoondolewa katika sekta ya uvuvi?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa mwongozo kwa watendaji wa Halmashauri juu ya mabadiliko hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na kutekeleza Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuweka mazingira mzuri katika kuwezesha wavuvi na wawekezaji kuendesha biashara ya uvuvi kwa ufanisi.
Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 katika hotuba yake alielekeza kupitia na kuangalia tozo zote ambazo ni kero kwa wananchi ili ziondolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inaelekeza kuwezesha wavuvi wadogo kwa kuwaondolea kero mbalimbali zikiwemo tozo zisizo na tija. Ili kutekeleza maelekezo haya, wizara yangu katika Bunge la Bajeti ya mwaka 2017/2018 ilitangaza kuondoa ada na tozo mbalimbali ambazo zilionekana kuwa kero katika sekta ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada na tozo zilizoondolewa katika sekta ya uvuvi ni kama ifuatavyo:-
• ushuru wa kaa hai (waliozalishwa na kunenepeshwa) wanaouzwa kwenda nje ya nchi.
• Tozo ya cheti cha afya baada ya kukagua mazao ya uvuvi shilingi 30,000.
• Ada ya ukaguzi wa kina wa kiwanda/ghala kila robo mwaka shilingi 100,000.
• Tozo ya usafirishaji samaki yaani movement permit kuanzia kilo 101 hadi kilo 1000 shilingi 5,000; kilo 1001 hadi kilo 5000 ni shilingi 10,000; kilo 5001 hadi kilo 9999 shilingi 30,000; zaidi 10,000 na zaidi shilingi 50,000.
• Ada ya usajili wa chombo cha uvuvi chini ya mita 11 kwa wavuvi wadogo shilingi 20,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha mabadiliko ya tozo katika sekta ya uvuvi inatekelezwa na watendaji wa Halmashauri, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wizara ya TAMISEMI imeshatoa maelekezo kwa Halmashauri husika kusitisha mara moja tozo ambazo zimefutwa na Serikali. Aidha, Wizara Wizara inafanya marekebisho katika Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 ili kuendana na mabadiliko hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kupitia Halmashauri zetu kuhakikisha kuwa maagizo haya kuhusu tozo zilizoondolewa na Serikali yanatekelezwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Watumishi walio maeneo ya pembezoni mwa nchi ikiwemo Wilaya ya Ukerewe wanafanya kazi katika mazingira magumu, mfano walimu wa watumishi wa afya.
Je, Serkali ina mpango gani wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa maeneo ya pembezoni?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba watumishi walio katika Halmashauri zilizo katika maeneo ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Ukerewe hufanya kazi katika mazingira magumu na upungufu mkubwa wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010 Serikali ilipitisha Sera ya Malipo ya Mishahara na Motisha katika utumishi wa umma ambayo miongoni mwa malengo yake mahsusi ni kuwavutia, kuwapa motisha na kuwabakiza watumishi katika utumishi wa umma. Lengo ni kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi katika Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza sera hii mwaka 2012/2013 Halmashauri 33 za Wilaya, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ziliwezeshwa kuandaa miongozo ya kutoa motisha kwa watumishi wake. Kutokana na zoezi hilo Halmashauri 29 ziliandaa na kuwasilisha katika ofisi yangu miongozo iliyoabainisha aina za motisha zinazohitajika kwa ajili ya watumishi wake. Utekelezaji wa miongozo hiyo kwa Halmashauri zote 29 ulikadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 331.087 kwa mwaka, ambapo kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 314.372 kilihitajika kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni 16.761 kilihitajitaka kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miongozo hii ulitarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2013/2014. Hata hivyo, utekelezaji wa miongozo hii haujaanza kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Uwepo wa mawasiliano ya uhakika kati ya Visiwa vya Ukerewe na Mkoa wa Mara ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe na hatua kadhaa zimeshachukuliwa kuhakikisha daraja kati ya Lugezi na Kisorya linajengwa. Je, ni hatua ipi inachukuliwa na Serikali kuhakikisha daraja hilo linajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali, naomba uniruhusu nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumshukuru Mungu kwa kukurejesha na afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha mawasiliano kati ya visiwa vya Ukerewe na mikoa mingine, imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara yote ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya – Nansio (Ukerewe) yenye urefu wa kilometa 118.
Aidha, usanifu umejumuisha madaraja mawili ya Lugezi yenye urefu wa mita 600 na mita 450 yanayounganisha Kisorya na Nansio pamoja na maandalizi ya nyaraka za zabuni. Kazi ya usanifu imekamilika na ujenzi kwa kiwango cha lami kati ya Bulamba hadi Kisorya katika barabara hii unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo, pamoja na madaraja mawili kati ya Kisorya na Nansio ili kuunganisha Kisiwa cha Ukerewe na Mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza.
MHE. PAULINE P. GEKUL (K.n.y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka umeme katika Vijiji vya Kakerege na Nkilizya vilivyopo Nansio Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Nkilizya kina vitongoji saba (7) na kati ya vitongoji hivyo vitatu (3) vya Magereza, Kenonzo na Lwocho, vilipata umeme mwaka 2005 kupitia utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme Nansio Wilayani Ukerewe kutoka Wilaya ya Bunda ambapo wateja 60 waliunganishiwa umeme. Vitongoji viwili (2) vya Namalebe na Chamatuli vilipatiwa umeme mwaka 2012 kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na jumla ya wateja 47 wameunganishiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, vitongoji vingine viwili (2) vya Mumakeke na Bubange vya Kijiji cha Nkilizya visivyokuwa na umeme, pamoja na Kijiji cha Kakerege vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa kwa sasa. Kupitia utekelezaji wa mradi huu, jumla ya vijiji 35 katika Wilaya ya Ukerewe vitapatiwa umeme. Kampuni ya Nipo Group Limited aliyepewa kazi za Mradi wa REA III katika Mkoa wa Mwanza anaendelea na utekelezaji mradi huo na mradi unatarajiwa kukamilika Juni, 2019.
Mheshimiwa Spika, kazi za Mradi wa REA III Ukerewe zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 78.32; njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 156; ufungaji wa transfoma 78 za KVA 50 na 100; pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 2,640. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 9.28.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Nansio) inakabiliwa na msongamano wa Wagonjwa; Mwaka 2002 Halmashauri ya Wilaya ilitumia zaidi ya shilingi milioni 200 kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Nakutunguru kama njia ya kupunguza msongamano huo. Hata hivyo, ujenzi huu haujakamilika kutokana na ukosefu wa fedha:-
Je, Serikali ipo tayari kuondoa upungufu uliopo ili Kituo hicho kianze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kupitia fedha za Ruzuku ya Maendeleo kwa Serikali za Mitaa yaani (Local Government Development Grant) mwaka 2012 kwa ajili ya kuanza kwa awamu wa kituo cha Afya Nakatunguru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo hilo OPD ulikamilika mwezi Aprili, 2015 na lilizinduliwa rasmi tarehe 18 Februari, 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Mpaka sasa kituo hiki kinafanya kazi kwa kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) na huduma za Mama, Baba na Mtoto (Reproduction and Child Health (RCH).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa Fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imeidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi wa Kituo hiki. Kwa sasa Serikali ipo katika awamu ya nne ya utekelezaji wa mpango wa ukarabati wa Vituo vya Afya nchini, hivyo tutakiingiza Kituo cha Afya Nakutunguru katika awamu zijazo ili kuhahakisha kinakamilika na kutoa huduma zote ikiwemo huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji wa Miyogwezi uliopo katika Kijiji cha Igongo, Ukerewe ni tarajio kubwa la suluhu ya upungufu wa chakula, zaidi ya miaka mitano sasa toka kufanyika uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 700 bado mradi huo umetelekezwa:-

(a) Je, kwa nini Serikali imetelekeza mradi huo?

(b) Je, nini kauli ya Serikali kuhusu uendelezwaji wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali haijautelekeza Mradi wa Kilimo cha Umwagilia wa Miyogwezi, bali mradi huo umesimama kutokana na muda wa utekelezaji wa mradi wa DASIP uliokuwa unafadhili mradi huo kumalizika kabla ya Mradi wa Miyogwezi haujakamilika. Mradi wa Miyogwezi ulitekelezwa kupitia mradi wa District Agriculture Sector Investment Project yaani (DASIP) ambao jumla ya shilingi 695,784,852.50 zilitumika. Utekelezaji wa mradi huo ulihusisha ujenzi wa mabanio mawili na mifereji mikuu yenye urefu wa kilometa 3.15 ambapo kilometa 1.1 zilisakafiwa. Ujenzi wa mabanio mawili katika mto wa kudumu yaani perennial river wa Miyogwezi na katika mto wa msimu wa Mriti. Hadi kukamilika kwa muda wa Mradi wa DASIP mwezi Disemba, 2013 ujenzi wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 76. Aidha, uendelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na Serikali kujipa muda wa kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa miradi yote ya DASIP ili kupima ufanisi wake ulivyotekelezwa.

(b) Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mradi wa Miyogwezi na miradi mingine ya umwagiliaji nchini inakamilika, Serikali imekamilisha mapitio ya mpango kabambe wa umwagiliaji wa mwaka 2002 kwa kuzingatia mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali maji yaani (Integrated Water Resource Management) ili kubaini maeneo yanayofaa kwa uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji yakiwemo mabwawa, visima vifupi na virefu vya chini vya ardhini, pamoja na hali ya skimu zote za umwagiliaji nchini.

Mheshimiwa Spika, mapitio ya mpango huo pia yamebaini miradi yote ya umwagiliaji ambayo haifanyi kazi na ambayo ujenzi wake haujakamilika katika kipindi kilichopita ikiwemo Mradi wa Miyogwezi. Aidha, Mradi wa Umwagiliaji wa Miyogwezi ni miongoni mwa miradi ya umwagiliaji itakayotekelezwa katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2023.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na.22 ya mwaka 2003, Dagaa wanapaswa kuvuliwa kwa wavu wenye matundu mm 8 – mm10, lakini sheria hii haijazingatia aina tofauti za dagaa:-

Je, kwa nini Serikali isifanye utafiti utakaoainisha matumizi ya nyavu kutegemea aina ya dagaa wanaopatikana kwenye Ziwa husika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina jukumu la kulinda, kuhifadhi na kuendeleza na kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi hapa nchini zinavunwa kwa busara ili ziwe endelevu kwa manufaa ya kiuchumi, kijamii na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria na kanuni zinazosimamia uvuvi nchini zinalenga uvuvi unaofanyika uwe endelevu ambapo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) hufanya tafiti ili kubaini athari za matumizi ya dhana na mbinu mbalimbali za uvuvi kwa rasilimali za uvuvi na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 66(1)(k) cha Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 kinaeleza kuwa nyavu za dagaa zenye ukubwa wa machi chini ya milimita nane zimakatazwa kutumika kwa uvuvi wa dagaa katika maji baridi ikiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Aidha, tafiti zilizofanyika katika Ziwa victoria zinaonesha kuwa aina moja tu ya dagaa anayejulikana kwa jina la kitaalam Rastrineobola argentea. Utafiti pia unaonesha nyavu zenye macho kuanzia milimita nane zikitumika kuvua dagaa hawa Ziwa Victoria zitavua dagaa waliopevuka na matumizi ya nyavu zenye matundu chini ya milimita nane zikitumika zitavua dagaa wachanga na hii itaathiri uvuvi wa dagaa katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Uvuvi na Kanuni zake imezingatia aina ya dagaa katika maji baridi na maji bahari. Aidha, TAFIRI itafanya utafiti ikiridhika kuna haja ya kufanya hivyo katika Ziwa Victoria kuhusiana na uvuvi wa dagaa. Serikali inaendelea kusisitiza wavuvi kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Kutokana na ufinyu wa ardhi na ongezeko la watu kwenye visiwa vya Ukerewe, pamoja na ardhi kutokuwa na rutuba, kumesababisha Kilimo kisicho na tija:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya utafiti wa kisayansi ili kuwashauri wananchi wa Ukerewe aina ya mazao yanayopaswa kulimwa na jinsi ya kutumia eneo dogo la ardhi kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ni kufanya utafiti wa tabaka na afya ya udongo katika kanda zote saba za kiikolojia za kilimo nchini, ikiwemo kanda ya Mwanza. Utafiti huo wa kisayansi unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo mbalimbali pamoja na kubaini mimea na mazao yanayostawi kwenye udongo husika ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Ukerewe ambayo wananchi wengi hulima mihogo, mpunga, mtama, mahindi, viazi vitamu na machungwa, utafiti wa awali unaonyesha kwamba, udongo wake una mboji kiasi kidogo cha asilimia 1.3 ukilinganisha na kiwango cha asilimia 2.5 ambacho ndicho kiwango cha mboji katika udongo wenye rutuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile utafiti umeonyesha kwamba kiwango cha tindikali kwa maana ya pH ni 5.4 ukilinganisha na pH ya 6.6, kiwango ambacho kinafaa kwa mimea ya kufyonza virutubisho kutoka kwenye udongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa kiasi hicho cha tindikali katika maeneo hayo kunaashiria kwamba kuna upungufu wa virutibisho vya nitrogen, phosphorus, potassium, sulphur, calcium na magnesium. Aidha, kulingana na matokeo hayo, inashauriwa kutumia mbolea zenye virutubisho vya nitrogen, potassium, phosphorus, sulphur, calcium na magnesium, ambazo ni pamoja na Minjingu, mazao ya ramila, samadi na CAN, UREA na DAP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sampuli za udogo zimechukuliwa katika kanda na mkoa mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Mwanza unaojumuisha Wilaya ya Ukerewe kwa lengo la kubaini viwango vya virutubisho vilivyopo katika sampuli hizo ambapo kwa sasa tathmini ya kina inaendelea kufanyika katika maabara ya TARI, Selian.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kukamilika kwa tathmini hiyo kutasaidia kushauri wakulima kuweka viwango vya mbolea vinavyohitajika kulingana na virutubisho stahiki kwa mazao husika na aina ya mazao na yanayopaswa kulimwa katika maeneo husika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, ni vikundi au wavuvi wangapi katika Kisiwa cha Ukerewe wamepewa elimu na mitaji ili waweze kufanya uvuvi wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa wavuvi wa Kisiwa cha Ukerewe juu ya uvuvi endelevu, matumizi ya zana na mbinu bora za uvuvi zinazokubalika kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na madhara yatokanayo na uvuvi haramu. Lengo la elimu hiyo ni kuwawezesha wavuvi wadogo wa kisiwa cha Ukerewe kufanya uvuvi endelevu na hivyo kunufaika na rasilimali za uvuvi zilizopo katika maeneo yao. Zaidi ya wavuvi wadogo na wadau wengine wa uvuvi wapatao 520 kutoka visiwa vya Ghana, Kunene, Lyegoba na Hamukoko katika Halmashauri ya Kisiwa cha Ukerewe walipatiwa elimu hiyo kwa njia ya mikutano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kuwezesha wavuvi kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kununua zana bora za uvuvi wakiwemo wavuvi wa Kisiwa cha Ukerewe. Ili kuwezesha wavuvi kunufaika na fursa hiyo, Serikali imeendelea kuwahamasisha wavuvi wadogo nchini wakiwemo wa Kisiwa cha Ukerewe, kuunda na kujiunga katika Vikundi vya Ushirika vya Wavuvi na Vyama vya Akiba na Mikopo ili kuwasaidia wavuvi kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Aidha, hadi sasa jumla ya shilingi million 250 zipo katika hatua ya mwisho ya kutolewa kwa wavuvi wa Kisiwa cha Ukerewe kama mkopo kupitia Chama cha Ushirika cha Bugasiga kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhamasishaji huo umewezesha kuanzishwa kwa Chama cha Ushirika cha Wavuvi katika Kisiwa cha Ukerewe, visiwa vidogo vya Ghana, Kunene, Lyegoba na Hamukoko ambacho kipo katika hatua za usajili. Uanzishwaji wa chama hiki utawezesha wavuvi kutoka Kisiwa cha Ukerewe kupata mikopo kwa urahisi kutoka Taasisi za Kifedha na hivyo kufanya uvuvi wenye tija.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Visiwa vya Ukerewe bado havitumiki ipasavyo kama eneo mahsusi kiutalii ingawa vimo vivutio vingi vya utalii ikiwemo jiwe linalocheza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na vikundi kama vile vya mila na desturi Ukerewe (KUMIDEU) katika kukitangaza Kisiwa cha Ukerewe kama eneo la utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua kuwa Ukerewe ni miongoni mwa Visiwa vichache nchini vyenye rasilimali mbalimbali ikiwemo fukwe nzuri, utalii wa utamaduni pamoja na jiwe linalocheza. Vivutio hivi kwa miaka ya hivi karibuni vimekuwa vikivutia wageni wengi kutembelea maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wizara inaendelea na zoezi la kuainisha vivutio vya utalii kwa dhumuni la kuviendeleza pamoja na kuvitangaza. Katika mwaka wa Fedha wa 2019/2020 tunatarajia kutekeleza zoezi hilo hilo katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza. Kazi hiyo hutekelezwa kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa, Wilaya, Vijiji na wadau wa Sekta ya Utalii katika maeneo hayo, hivyo nimjulishe Mheshimiwa Mbunge, zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa katika Mkoa wa Mwanza, Wataalam wangu watapita katika Kisiwa cha Ukerewe ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na kikundi cha Mila na Desturi cha Ukerewe cha (KUMIDEU)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hilo ni juhudi za makusudi za Wizara yangu za kupanua wigo wa mazao ya utalii kwa kubainisha vivutio vya utalii wa asili sehemu mbalimbali nchini. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa kusimamia na kuendeleza Sekta ya Utalii Kanda ya Ziwa, Wizara ilifungua Ofisi ya Kanda iliyohusisha Idara ya Utalii na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika Jiji la Mwanza. Lengo likiwa ni kusogeza kwa karibu huduma kwa wadau wa Sekta ya Utalii walio katika Kanda ya Ziwa na maeneo jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake za kuhakikisha Sekta ya Utalii inazidi kuendelea na kukua hususani katika Kisiwa cha Ukerewe na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla. Ifahamike kwamba Sekta ya Utalii ni Mtambuka na hivyo kazi ya uendelezaji sekta hii inahitaji juhudi za pamoja za wadau wa Sekta hii, Umma na Binasfsi. Hivyo, Wizara yangu itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa Sekta ya Utalii kuendeleza utalii nchini ahsante.
MHE. JOSESPH M. MKUNDI aliuliza:-

Kituo cha Afya Bwisya kimekarabatiwa na kuongezewa miundombinu muhimu kufikia kiwango cha hospitali:

Je, kwa nini Serikali isipandishe hadhi kituo hicho na kuwa Hospitali ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa visiwa vya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuanzia Julai, 2017 hadi Machi, 2020 Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 800 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya Bwisya na Muriti. Vilevile Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, alielekeza baadhi ya kiasi cha fedha za maafa ya ajali ya Kivuko cha Ukerewe kiasi cha shilingi milioni 860 zitumike kupanua na kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya Bwisya. Hivyo kituo hicho kimejengwa na kukarabatiwa kwa jumla ya shilingi bilioni 1.26.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha taratibu za kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Bwisya kilichopo kwenye Kisiwa cha Ukara ili kiwe na hadhi ya Hospitali ya Halmashauri.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza: -

Pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya kusambaza umeme vijijini kupitia Mradi wa REA bado kuna shida kubwa katika maeneo ya vitongoji kwenye vijiji hivyo.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa umeme unasogezwa kwenye maeneo ya vitongoji ambavyo havijapata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji visivyokuwa na umeme kupitia mzunguko wa pili wa mradi jazilizi (Densification IIA) katika mikoa tisa ya Mbeya, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na Mwanza kwa kupeleka umeme katika vitongoji 1,103 kwa kuunganisha umeme wateja wa awali wapatao 69,079. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 197. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2021. Kazi hii ni endelevu inayofanyika pia kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Mheshimiwa Spika, ili kutimiza Azma ya Serikali ya kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji, Serikali kupitia Mradi wa Densification IIB unaotarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2021 utaendelea kupeleka umeme katika vitongoji vya mikoa kumi ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Morogoro, Njombe, Simiyu, Songwe, kwa kupeleka umeme katika vitongoji 1,686 na kuunganisha umeme wateja wa awali wapatao 95,334. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 230. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2022.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza:-

Je, ni lini Daraja la Kisorya – Lugezi litakalounganisha Wilaya za Bunda na Ukerewe litajengwa ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa daraja litakalounganisha Wilaya ya Bunge na Ukerewe ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba – Kisorya – Nansio yenye urefu wa kilomieta 121.6 ambao utekelezaji wake umeanza na uko katika hatua mbalimbali. Kazi ya upembuzi yakinifu na usaniifu wa kina wa barabara ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba hadi Kisorya yenye urefu wa kilometa 107.1 ilikamilika Machi, 2013. Aidha, usanifu wa kina wa sehemu ya barabara ya Kisorya – Rugezi – Nansio (Ukerewe) yenye urefu wa kilometa 14.5 pamoja na Daraja la Rugenzi – Kisorya ulikamilika Aprili, 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu umegawanyika katika sehemu tatu, yaani Lots tatu, ambazo ni Nyamuswa – Bunda – Bulamba (Lot I) yenye urefu wa kilometa 56.1; Lot II bulamba – Kisorya yenye km. 51 na Lot III Kisorya – Lugezi – Nansio yenye urefu km. 14.5 inayojumuisha na daraja la Kisorya – Rugezi yaani daraja lina urefu wa mita 1000. Hadi sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Bulamba – Kisorya ambao ni Lot II umekamilika. Ujenzi wa sehemu ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba Lot I kwa kiwango cha lami unaendelea na umefikia asilimia tano. Aidha, ujenzi wa sehemu ya Rugezi – Nansio Pamoja na daraja la Kiisorya – Rugezi utaannza baada ya fedha kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa sehemu ya Kisorya – Rugezi – Nansio ikiwemo ujenzi wa daraja Serikali kupitia wakala wa ufundi na umeme TEMESA inaendelea kutoa huduma ya kuvusha wananchi wa maeneo haya kupitia kivuko cha MV Ujenzi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Bulamba – Bukonyo hadi Masonga yenye urefu wa kilometa 32.23 kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri ya Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bulamba – Bukonyo hadi Masonga yenye urefu wa kilometa 32.23 ni barabara ya mkoa inayounganisha mji wa Nansio na Ziwa Viktoria kupitia vijiji vya Murutunguru - Bukonyo hadi Masonga. Barabara hii inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inaendelea kuiimarisha kwa kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka ili kuhakikisha kuwa inapitika kipindi chote cha mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga jumla ya shilingi milioni 757.94 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii. Kazi za matengenezo hayo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hii kila mwaka ili kuhakikisha kuwa inaendelea kupitika wakati wote kabla ya kuijenga kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka ujao wa fedha wa 2021/2022, barabara hii imeombewa shilingi milioni 219.159 kwa ajili ya matengenezo ya vipindi maalum na shilingi milioni 510 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya Daraja la Nabili lililopo katika barabara hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni lini Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio itatambuliwa rasmi na kuanza kuwahudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tangazo la kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio lilitolewa tarehe 1/10/2007 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Wilaya Sheria Na. 7 ya mwaka 1982 kifungu cha 16 na 17.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Serikali iliunda timu ya wataalam kwa ajili ya kuchukua maoni ya wananchi kuufanya Mji Mdogo wa Nansio kuwa Halmashauri ya Mji. Wananchi wa kata kumi zilizopendekezwa kuunda Halmashauri ya Mji Nansio waliridhia Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio kupandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji na mapendekezo hayo yaliwasilishwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilipokea mapendekezo hayo na kutuma timu ya wataalam kwenda katika Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio ili kujiridhisha kama vigezo muhimu vinavyotakiwa ili kupandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio vimefikiwa. Timu ilibaini kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio bado haikidhi vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji.

Mheshimiwa Spika, vigezo zilivyokosekana ni pamoja na kutokuwa na idadi ya watu angalau 150,000, kutokuwa na eneo lenye ukubwa wa walau kilomita za mraba 300, kutokuwa na kata walau 12 na mitaa 60. Hivyo, Ofisi ya Rais- TAMISEMI iliishauri Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuendelea kuilea Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nansio mpaka itakapokidhi vigezo. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la mawasiliano ya simu katika maeneo ya Bukiko, Chabilungo, Kitale na maeneo mengine yenye tatizo hilo Visiwani Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo la Bukiko lina mnara wa Halotel uliojengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Eneo la Chabilungo linapata huduma za mawasiliano kupitia watoa huduma ambao ni Tigo, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) pamoja na Vodacom.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini kwa mara nyingine katika maeneo ya Chabilungo, Bukiko, Kitale na maeneo mengine katika Jimbo la Ukerewe ili kubaini mahitaji halisi ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo, Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni vivutio gani vya utalii vimetambuliwa Wilayani Ukerewe na hatua zipi zimechukuliwa kuendeleza na kuvitangaza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara katika kipindi cha mwaka 2020/2021 kwa kushirikiana na maafisa wa Mkoa wa Mwanza walitekeleza zoezi la kubaini na kuvitambua vivutio vya utalii vilivyopo katika Kisiwa cha Ukerewe. Vivutio hivyo ni pamoja na utalii wa ikolojia, utalii wa fukwe, utalii wa kiutamaduni na kihistoria.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati ya kuvitangaza na kuviendeleza vivutio hivyo vya utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii hapa nchini. Sambamba na hilo Serikali inaendelea kuimarisha Ofisi ya Kanda ya Utalii iliyopo Jiji la Mwanza na kuanzisha Chuo cha Utalii cha Taifa katika Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kusogeza huduma za Kanda ya Ziwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Serikali kukifanyia ukarabati Kituo cha Polisi cha Nansio?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi Nansio kilichopo Ukerewe. Tathmini kwa ajili ya ukarabati imeshafanyika mwaka huu wa 2022 na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 68,000,000 zinahitajika ili kugharamia ubadilishaji paa, dari, mfumo wa maji na maji taka, pamoja na kuziba nyufa, kurekebisha sakafu pamoja na kupaka rangi. Ukarabati huu utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni lini Chuo cha VETA Ukerewe kitaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Ukerewe ili kiweze kutoa mafunzo yatakayowezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa chuo hiki upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji ambapo ujenzi umefikia asilimia 97. Aidha, tayari Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hiki ili kianze kutoa mafunzo ya muda mfupi ifikapo mwezi Aprili, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Vituo vya Abiria vya Bugorola, Ukara na Kisorya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika mwaka wa fedha 2022/2023, umetenga fedha kiasi cha shilingi 332,220,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Abiria vya Bugorola, Ukara na Kisorya katika Wilaya ya Ukerewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TEMESA imeingia makubaliano na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA - Mwanza) kwa ajili ya kufanya usanifu wa miundombinu ya majengo na mchanganuo wa makadirio ya gharama husika. Taratibu za kumpata Mkandarasi atakayejenga miundombinu hiyo zitatekelezwa baada ya usanifu kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/2023, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, kwa nini Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nansio haifanyi kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika inaonesha kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio bado haijakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mamlaka nyingi zilizoanzishwa bado zina upungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali kuvifanya vivutio vya mapango ya Handebezya na jiwe linalocheza kuwa na tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza, kukuza na kutunza vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza vinavyopatikana katika Kisiwa cha Ukerewe. Mikakati hiyo ni pamoja na kutangaza vivutio hivyo kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalan, Wizara kupitia TTB iliratibu ziara ya Kituo cha Televisheni cha ITV kwenda kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na jiwe linalocheza kwa ajili ya kuandaa documentary ambayo itakapokamilika itaonyeshwa katika kipindi cha ITV cha Chetu ni Chetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mafunzo yanaendelea kutolewa kuhusu uanzishwaji wa utalii wa utamaduni ambapo hadi sasa kuna vikundi vya utalii wa utamaduni vikiwemo Ukerewe (Ukerewe Cultural Tourism Enterprises) na Nansio (Nansio Cultural Tourism Enterprises).

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kushiriki katika maonesho na matamasha mbalimbali yakiwemo Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki na Tamasha la Bulabo yanayofanyika katika Kanda ya Ziwa kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo katika ukanda huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa miundombinu inayoelekea katika maeneo yenye vivutio vya utalii, ujenzi wa huduma za malazi zenye hadhi pamoja na kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo maji, umeme, huduma za kibenki na mawasiliano.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali katika kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa walimu ili kuwaongezea morali ya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa kupeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya mafunzo kwa walimu ambapo shilingi bilioni 1.9 zimetumika. Aidha, vitendea kazi kama vile kompyuta, printa, photocopy na projector vimenunuliwa kwa ajili ya walimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa vishikwambi kwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari ili waendane na dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.03 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na taratibu za ununuzi zinaendelea. Vilevile, Serikali imetenga shilingi bilioni 5.04 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo 252 vya walimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuviimarisha vituo vya Walimu kwa ajili ya wao kukutana na kujengeana uwezo utakaowaimarisha katika shughuli za ufundishaji na ujifunzaji na itaendelea kuboresha maslahi ya Walimu kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, upi mpango wa Serikali kumaliza kero ya upatikanaji wa maji safi na salama Wilayani Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ukerewe ina jumla ya vijiji 76, kati ya vijiji hivyo 37 vinapata huduma ya maji safi na salama. Aidha, katika mwaka 2022/2023, Serikali inatekeleza miradi katika vijiji vingine 26 na inatarajia kukamilisha miradi hii mwezi Julai, 2023.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itajenga miradi ya maji kwenye vijiji 13 vilivyobaki ambapo ni Bugula, Kameya, Halwego, Chamuhunda, Mukunu, Bugorola, Kamasi, Busumba, Kaseni, Bukonyo, Busagami, Msozi na Kweru. Kukamilika kwa miradi hiyo kutaondoa kero ya maji Wilaya ya Ukerewe na wananchi wote watapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO K.n.y. MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, lini kipande cha barabara cha Kisorya hadi Nansio kitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inajenga barabara ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya – Nansio yenye urefu wa kilometa 121.9 kwa awamu. Ujenzi kwa kiwango cha lami awamu ya kwanza sehemu ya Bulamba – Kisorya kilometa 51 umekamilika. Kwa sehemu ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba kilometa 56.4 ujenzi umekamilika na upo kwenye kipindi cha matazamio huku Mkandarasi akimalizia kazi ndogo ndogo zilizobaki. Kwa sehemu iliyobaki ya kutoka Kisorya hadi Nansio ambayo ina urefu wa kilometa 12.8 Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwezesha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki katika Wilaya ya Ukerewe?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchumi unaozingatia misingi ya Sera ya soko huria ujenzi wa viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya kuchakata samaki unafanywa na sekta binafsi. Jukumu la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Kwa kuzingatia sera hiyo Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuhamasisha wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje kuja kujenga viwanda vya kuchakata samaki katika Wilaya ya Ukerewe pamoja na maghala ya kuhifadhia na kugandisha mazao ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi, maghala ya kuhifadhia na kugandishia mazao ya uvuvi katika maeneo ya uvuvi yenye mavuno mengi hapa nchini ikiwemo Wilaya ya Ukerewe. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati au kujenga Mahakama mpya ya Wilaya ya Ukerewe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mahakama inaendelea na utekelezaji wa mpango wa kujenga na kukarabati majengo katika ngazi mbalimbali. Aidha, katika ngazi ya Mahakama za Wilaya, bado tuna Wilaya ambazo hatuna majengo na hivyo, kulazimika kutumia majengo ya kuazima kwenye taasisi nyingine kama Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe kwa sasa inafanya kazi kwenye majengo ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Hata hivyo, katika mpango wetu wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, tumepanga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe katika mwaka wa fedha 2024/2025. Naomba nitumie fursa hii kuishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa kutupatia kiwanja kwa ajili ya kujenga jengo hilo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza:-

Je, lini mradi wa ujenzi wa Feri ya MV Buyagu utakamilika ikizingatiwa kuwa mkataba wa ujenzi umekwisha muda wake Aprili, 2024?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajenga kivuko kipya kitakachokuwa kiunganishi muhimu kati ya Wilaya ya Sengerema na Wilaya ya Misungwi kupitia eneo la Buyagu lililoko Sengerema na eneo la Mbalika lililopo Misungwi. Mkataba wa ujenzi wa kivuko hiki ulisainiwa mwezi Aprili, 2023 kati ya Serikali kupitia TEMESA na mkandarasi Songoro Marine Transport Mwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za ujenzi wa kivuko hiki zimepangwa kukamilika mwezi Agosti, 2024 baada ya muda wa awali kuongezwa, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, kwa nini ujenzi wa Barabara ya Bukiko hadi Bwisya kupitia Katende inayosimamiwa na TARURA haukamiliki kwa zaidi ya miaka miwili sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo ndio siku ya kwanza nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza kama Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nichukue dakika moja kutoa maneno ya utangulizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na siha njema mpaka wakati huu. Kipekeee naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniteua katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Namuahidi Mheshimiwa Rais nitafanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu mkubwa ili kumsaidia majukumu yake na kutimiza maono yake kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kukushukuru wewe kama mlezi wetu sisi Wabunge, kwa nasaha zako, kwa mafunzo yako ambayo yamenijenga mimi kiuongozi, lakini pia katika maisha yangu binafsi, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano mkubwa ambao wamenionesha. Kwa heshima kubwa na unyenyekevu niwaombe ushirikiano zaidi sasa ili kwa pamoja tuweze kushirikiana kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutimiza maono yake kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii adhimu pia kuwashukuru akinamama wote na wapigakura wangu wa Mkoa wa Kigoma kwa kuendelea kunipa ushirikiano mkubwa unaonipa utulivu katika kazi zangu. Baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini ilifanya matengenezo ya kufungua upya Barabara ya Bukiko hadi Bwisya kupitia Katende kilometa 7.54 kwa gharama ya shilingi milioni 141.2. Fedha hizo zilitekeleza kazi za ufunguzi wa barabara na kuunda tuta la barabara kilometa 7.54, ujenzi wa madaraja madogo matatu na ujenzi wa mistari minne ya madaraja madogo. Kazi zote zilikamilika kwa mujibu wa mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali imeweka katika mipango yake ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, kufanya matengenezo ya kawaida na kujenga madaraja madogo mawili kwa gharama ya shilingi milioni 30.16 ili barabara iweze kupitika wakati wote. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaongeza nguvu ya mnara katika Kata ya Bukiko kutoka 2G hadi 3G na kuweka generator kwa kuwa kata hiyo ina shida kubwa ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itaijumuisha kata ya Bukiko katika mradi wa kuboresha huduma za mawasiliano kwa kuongeza teknolojia za 3G na 4G na pia mradi huu utaimarisha miundombinu ya nishati ikiwemo ya kuweka generator. Utekelezaji wa mradi huu utaanza katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, upi mkakati wa kuondoa kero ya kutokuwa na umeme wa uhakika na wa gharama kubwa kwenye Visiwa vya Ukara na Ilugwa – Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ili kuondoa kero ya kutokuwa na umeme wa uhakika na kupunguza gharama ya umeme katika Visiwa vya Ukara na Ilugwa, Serikali kupitia Mradi wa Gridi Imara unaotekelezwa na TANESCO imeanza kujenga njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 132 pamoja na kujenga kituo cha kupokea na kupoza umeme chenye mashineumba mbili zenye uwezo wa MVA 120 katika eneo la Nansio Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa kituo hicho, visiwa vya jirani kikiwemo Kisiwa cha Ukara vitaungwa na umeme wa Gridi ya Taifa. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutoa ruzuku kwa wazalishaji binafsi wa umeme wanaohudumia visiwa hivyo ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji. Kupitia ruzuku hiyo wazalishaji hao wataweza kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika visiwa hivyo na kuweza kupunguza bei ya kuuza umeme kwa wananchi wanaowahudumia, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, nini husababisha kuchelewa kubadilishiwa Muundo wa Utumishi kwa Walimu mara baada ya kujiendeleza kitaaluma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuchelewa kubadilishiwa Muundo wa Utumishi kwa Walimu mara baada ya kujiendeleza kitaaluma husababishwa na changamoto mbalimbali ikiwemo:-

(i) Walimu husika kuchelewa kuwasilisha vyeti vya taaluma kwa wakati mara baada ya kuhitimu;

(ii) Baadhi ya Walimu kujiendeleza kitaaluma bila mwajiri kuwa na taarifa hali inayosababisha kutoingizwa kwenye Bajeti na Ikama kwa ajili ya kubadilishiwa miundo ya utumishi kwa wakati; na

(iii) Walimu kutowasilisha vyeti vya taaluma kwa kuhofia kutumikia cheo kimoja chenye mshahara ule ule kwa muda mrefu kabla ya kupandishwa daraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, walimu 4,917 kati ya watumishi 5,110, sawa na 96% wamebadilishiwa muundo baada ya kujiendeleza kitaaluma. Aidha, walimu 156,162 kati ya watumishi 227,290 sawa na 69% wamepandishwa cheo. Ninashukuru.