Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph Michael Mkundi (82 total)

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe masikitiko yangu kwamba Serikali haina takwimu sahihi ili kuweka kumbukumbu vizuri, Ukerewe tuna zahanati 29 na vituo vya afya vitatu. Kwa kuwa, suala la kupatikana kwa wataalam kwenye kituo cha afya cha Bwisya limekuwa ni la muda mrefu, niiombe sasa Wizara au Serikali kwa ujumla itoe commitment kwa sababu akinamama wengi sana wanapoteza maisha kwenye eneo lile, lini hasa ufumbuzi wa tatizo hilo utapatikana na kituo hiki kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Ukerewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri miaka miwili iliyopita ilijitahidi kujenga kituo cha afya cha Nakatunguru ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, lakini kituo hiki bado hakijaanza. Je, Serikali sasa iko tayari kutoa vifaa na wataalam ili kituo hiki kiweze kuanza kutoa huduma na kwa maana hiyo kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni wazi tunaelewa jiografia ya Ukerewe kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema katika jibu langu la awali ni kweli, jiografia ya Ukerewe ina changamoto kubwa sana na Ukerewe tunaifananisha na Rufiji ambapo kuna deltas mbalimbali kiasi kwamba huduma za kijamii zinakuwa ni ngumu. Mheshimiwa Mbunge najua kwamba, siyo huduma ya afya peke yake, hata huduma ya elimu ina changamoto kubwa katika visiwa vile. Kwa hiyo, Serikali ina kila sababu ya kuangalia ni jinsi gani tunaweka kipaumbele katika visiwa vya Ukerewe ili hali ya kiafya iendelee vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la upatikanaji wa wataalam, naomba nikwambie kwamba sasa hivi tuko katika mchakato na siyo muda mrefu sana tutaajiri wataalam. Niwashukuru sana watu wa Ukerewe. Katika ile hospitali ya Nansio kuna vijana watano pale ambao ni Madaktari graduates wanajitolea na baada ya mawasiliano wameonesha wazi kwamba wale vijana wanataka kubaki kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie hili kwanza, kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tutakapokwenda katika mchakato wa kuwapeleka wale Madaktari watano tutahakikisha wanabaki kule Ukerewe kwa ajili ya huduma ya afya. Kwa hiyo, mchakato wa upatikanaji wa Madaktari tunaufanya kabla hatujatoka katika Bunge hili, wataalam hao watakuwa wameshakwenda siyo Ukerewe peke yake, isipokuwa na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amesema kuna changamoto katika zahanati inayojengwa Nyakatungu. Naomba nimwambie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nitakuwa na hamu sana mara baada ya Bunge hili, niweze kufika Ukerewe nijue jiografia ya Ukerewe na kupanga mikakati tukiwa field kule, kuona tutafanyaje kutatua tatizo la afya la watu wa Ukerewe. Itanipa faida kubwa zaidi siyo afya peke yake, nitaangalia hata sekta ya elimu ambayo siku moja nimeona katika TV watoto wanavuka na boti kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kupata huduma ya elimu.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Baada ya MV Butiama kusita kufanya shughuli zake pale kulikuwa na meli ya MV Clarius ambayo nayo imesimama kufanya kazi na kuna taarifa kwamba itatengenezwa na watu wa MSCL ili iendelee kufanya shughuli zake lakini meli hii imekuwa chakavu, inahitaji matengenezo makubwa. Sasa kwa kuwa wenye jukumu la kutengeneza ni MSCL wenyewe lakini wanatatizo kubwa sana la fedha. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuna haja ya kuwasaidia hawa MSCL kwa kuwapa fedha za kutosha ikiwepo pamoja na pesa za OC ili waweze sasa kutengeneza meli hii iweze kufanya kazi katika mazingira mazuri ikizingatiwa ni ya muda mrefu na katika hali halisi ya sasa kumsafirisha abiria kwa saa tatu majini akiwa amekalia viti vya mbao si kitu kizuri sana?
Swali la pili; ratiba za meli kutoka Mwanza kwenda Ukerewe zina mahusiano ya moja kwa moja na ratiba za vivuko vingine. Kwa mfano, Kivuko cha MV Nyerere kutoka Mgolola kwenda Ukala sasa kumekuwa na matatizo ya kutowiana kwa ratiba kiasi kwamba wasafiri wanakaa muda mrefu. Kwa mfano, akifika Nansio anakaa kwa saa tano ili apate usafiri mwingine wa kumpeleka kisiwa cha Ukala. Je, Serikali haioni sababu za msingi za kuainisha ratiba ya vivuko hivi ili kuondoa gharama kubwa ambazo wasafiri wanazipata wanapokuwa safarini? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza, nakubaliana naye kwamba kuna haja ya kuwaongezea uwezo wa kifedha ikiwa ni pamoja na fedha za OC ili MSCL waweze kutekeleza wajibu wao na hasa katika kuikarabati meli hii ya MV Clarius.
Kwa upande wa pili, ratiba nimepokea ombi lake, nitawasiliana na taasisi hizi mbili zinazohusika, TEMESA pamoja na MSCL waangalie kama kuna uwezekano wa kurekebisha ratiba zao, lakini kwa mazingira ninayoyafahamu, tukirekebisha kutakuwa na tatizo vilevile la kuwasumbua wale wa Ukala wakakaa muda mrefu sana kusubiri MV Clarius ifike, ilete abiria. Tutaangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kutafuta njia nyingine kuweza hili kuliweka sawa ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo mbili za kivuko pamoja na Meli.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Tatizo la
mawasiliano ni kubwa sana kwenye Visiwa vya Ukerewe, hususan kwenye
maeneo ya Bwasa, Kata ya Igala na maeneo ya Bukiko, Kata ya Bukiko. Sasa je,
Serikali iko tayari kutumia wataalam wake kufanya utafiti na kusaidia upatikanaji
wa mawasiliano kwenye maeneo haya ya visiwa vya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko
tayari. Naomba tu nitoe kauli kwamba Mfuko wetu wa Mawasiliano kwa wote
(UCSAF) waifanye kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Jumapili tulikuwa na semina inayohusu mambo ya utalii, na kwenye jarida hili kulikuwa na taarifa ambazo zilikuwa na upungufu juu ya vivutio hivi. Sasa Je, Waziri yuko tayari kutembelea visiwa vya Ukerewe na kushuhudia vivutio hivi ili awe Balozi mzuri na mwenye taarifa zilizo sahihi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, suala la ukuzaji
na uendelezaji wa vivutio hivi mbali na kuvitangaza inategemea zaidi ubora wa miundombinu ya kuvifikia vivutio hivi; na kwa kuwa Halmashauri zetu hazina uwezo wa kutosha wa kuboresha miundombinu hii, sasa Serikali iko tayari kuboresha miundombinu ya kufikia vivutio hivi hasa Jiwe linalocheza la Nyaburebeka la Kisiwani Ukara? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari kabisa kutembelea vivutio hivyo pamoja na Mbunge, Mheshimiwa Mkundi bila wasiwasi wowote na tutapanga safari hiyo mwezi Agosti mwaka huu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vivutio vyote vya utalii vinakuwa vizuri zaidi kama vinafikika na raia na watalii wanaotaka kuvitembelea. Wakati tutakapotembelea tutafanya tathmini ya vivutio hivyo na kuona ni namna gani juhudi hizi zitakamilika ili vivutio hivyo vifikike.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Ukerewe inaundwa na visiwa na kwa kuwa yanapotokea matatizo ya dharura kiafya inakuwa kazi ngumu sana kuwawahisha wagonjwa kupata huduma ya ziada.
Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kutoa ambulance boat kuweza kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wa Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshiniwa Mwenyekiti, najua kwamba tulipeleka ambulance kule ya kawaida katika kipindi cha kati, lakini na mahitaji ya kwamba watu wa Ukerewe wapate ambulance boat, naomba Serikali tuchukue kwa mawazo yenu mapana. Kama Mbunge anavyofahamu tuliongea naye private kwamba tutafika Ukerewe baada ya Bunge hili, tukifika kule tutajadiliana kwa mapana na pamoja nini tutawasaidia wananchi wa Ukerewe. Pia jambo hili tutaangalia jinsi gani tuliweke katika kipaumbele kama Serikali kwa kuweka mawazo ya pamoja kwa upana wake.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo nyingi katika hizi zilizoondolewa si zile zinazomgusa moja kwa moja mvuvi. Wavuvi husasan katika Ziwa Victoria, wanasumbuliwa sana na leseni kwa mfano wanazopaswa kulipa wanapotoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine, kuna ushuru wa uvuvi kwa mfano, na tozo nyingine za SUMATRA na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu nyingi katika hizi ziko chini ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003, Serikali sasa haioni sababu ya msingi kabisa kuleta sheria hii Bungeni ili Bunge liweze kuipitia na kuifanyia marekebisho?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa taarifa nilizonazo Mheshimiwa Waziri wewe ni mtaalam mbobezi kwenye eneo hili la uvuvi na unatoka kwenye eneo la wavuvi, kwa hiyo unaujua vizuri uvuvi na kwa sababu matatizo mengi ya wavuvi, hususan eneo la Ukerewe yanazungumzika, je, uko tayari sasa Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili tuweze kuandamana kwenda katika Visiwa vya Ukerewe upate fursa ya kuzungumza na wavuvi na kusikiliza kero zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anasema kwamba tozo nyingi zilizofutwa sizo zile ambazo ni kero hasa inayowasumbua wavuvi na akatuomba kuleta mabadiliko ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tu kwamba matakwa yake haya tunayachukua na tayari Serikali ipo katika mpango wa kuboresha moja ya Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003, Sheria Na. 22 na kupitia kanuni mbalimbali ambazo zitakwenda kuboresha kwa maana ya tozo hizi zilizofutwa, sawa na majibu yangu ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nimhakikishie; hizi tozo, hasa ile ya movement permit iliyofutwa ilikuwa ni kero kubwa kwa wavuvi wetu na ndiyo maana Serikali hii ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Jospeh Magufuli ikaona iifutilie mbali. Na nataka nimhakikishie ya kwamba kilichobaki ni usimamizi wa kuhakikisha movement permit haiendelei kutozwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni la kwenda Ukerewe; ni kweli mimi ni mvuvi na uvuvi ni maisha yetu. Nataka nimhakikishie rafiki yangu ya kwamba tutafika Ukerewe kwenda kuzungumza na wavuvi na kwenda kuwatoa majaka roho yote yanayowasumbua. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, maeneo ya Kakelege na eneo la uwanja wa ndege Kata ya Nkilizia yapo katikati ya mji wa Nansio. Lakini maeneo haya yamerukwa na huduma ya umeme, jambo linalofanya wananchi wa maeneo haya waone kama wametengwa. na Mheshimiwa Waziri nimekuwa namuwasilishia tatizo hili mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu nataka kujua Serikali imefikia hatua ipi kuhakikisha kwamba maeneo haya yaliyo katikati ya mji wa Nansio yote yanapata huduma za umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika maelezo yangu ya awali Serikali inatekeleza mradi pia wa densification ambao sasa hivi Awamu ya Kwanza na ni kwa Mikoa sita. Baada ya kukamilika kwa mikoa hiyo Serikali itaendelea pamoja na wafadhili wa Norway kutekeleza awamu ya pili. Nia ya mradi huu ni kusambaza umeme katika maeneo kaya, vitongoji na taasisi za umma zilizorukwa. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Awamu ya Pili ya mradi huu itafikiwa katika maeneo ambayo ameyataja.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Matatizo ya upungufu wa Madaktari, watumishi wengine wa afya na vifaa tiba yaliyoko hospitali ya Mkoa wa Geita ni sawa kabisa na yale yaliyoko kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, Hospitali ya Nansio. Serikali iko tayari sasa kuangalia visiwa vya Ukerewe kwa upendeleo maalum na kutusaidia kuondoa tatizo hili ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto visiwa vya Ukerewe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli. Mheshimiwa Mbunge anakiri kwamba, nilipata fursa ya kwenda na tuliweza kufika mpaka kule Ukerewe na ni kweli changamoto ya afya katika visiwa vile imekuwa ni kubwa zaidi. Ndiyo maana katika vipaumbele vyetu sasa hivi hata ukiangalia idadi ya Madaktari ambao juzi tu tumewaajiri, tumeajiri Madaktari takribani 2,058, tumepeleka vijana kule kwa ajili ya kusaidia suala la changamoto inazozipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna fedha vilevile tunaenda kuboresha kile kituo cha afya kama alivyopendekeza Mheshimiwa Mbunge na hatutasita kuendelea. Tunafanya juhudi ya kutosha hasa kwa sababu tunajua kwamba eneo la Ukerewe lazima tuboreshe miundombinu ili hata watumishi tunaowapeleka kule wawe na hamasa ya kufanya kazi baada ya kuboresha mazingira yao. Kwa hiyo, jukumu hili tumelichukua sisi Serikali kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi wa Ukerewe.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mkanganyiko katika utaratibu wa upatikanaji wa vitambulisho kwa wazee ili waweze kupata huduma za afya ambapo baadhi ya maeneo wazee hawa wamekuwa wanatakiwa kuchangia baadhi ya gharama.
Sasa Serikali inaweza kutoa kauli ni upi wajibu wa halmashauri na upi wajibu wa wazee hawa ili waweze kupata vitambulisho ili wapate huduma za afya bure? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni agizo la Serikali kwamba Halmashauri zitoe vitambulisho vya wazee ili waweze kutambulika kirahisi wanapokwenda kutafuta matibabu ya afya. Na hii inaendana na Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inasema kwamba wazee watapata matibabu bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho hivi vinapaswa vitolewe bure kwa sababu halmshauri zinagharamia. Inawezekana kwamba zile gharama ndogondogo kama upigaji wa picha ambazo wanatakiwa wazee nao wazigharamie ambayo sio gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapenda kusema tu kwamba gharama ya kitambulisho ni bure na Halmashauri zinatakiwa zigharamie hilo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na posho za Madiwani, Wenyeviti ya Vijiji na Vitongoji kuwa ndogo, lakini bado halmashauri nyingi zimekuwa zinawakopa viongozi hawa posho hizi kiasi kwamba wana muda mrefu hawalipwi. Sasa Serikali iko tayari kutoa kauli yenye muda maalum kuhakikisha kwamba viongozi hawa wanalipwa madeni yao ya posho zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, juzi nilipokea concern kutoka Buchosa kwamba Madiwani wamekopwa takribani miezi minane, hili halikubaliki hata kidogo. Wakati mwingine utagundua kwamba ni uzembe tu wa usimamizi nzuri. Watu wanafanya collection lakini wakati mwingine katika suala la kuwalipa Madiwani wanaona kama ni hisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitoe maelekezo kwamba halmashauri mbalimbali tunafanya makusanyo, makusanyo yale yanakusanywa na Madiwani ndio wanaofanya maamuzi, lazima mwende mkalipe posho za Madiwani kwa kadri iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani wanafanya kazi kubwa lakini posho zao hazilipwi na wakati huo huo shughuli nyingine zinaendelea ambazo Madiwani hao ndio waliosimamia kupata fedha hizo, haitokubalika. Tutaenda kufuatilia halmashauri moja hadi nyingine. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tuta-cross check na halmashauri mbalimbali ambazo kwa makusudi kabisa wamekataa kuwalipa madiwani either kwa kiburi au kwa jambo lingine lolote.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa kukosa fedha za kuendeshea shughuli za Mabaraza ya Ardhi ya Kata ni kichocheo kikubwa sana cha rushwa kinachopelekea wananchi wengi kunyimwa haki zao za msingi. Sasa Serikali haioni sababu na umuhimu sasa itoe ruzuku kwa Mabaraza haya ili yaweze kuendesha shughuli zake na kuondoa uwezekano wa kuchukua rushwa? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa kesi kubwa nyingi sana kuja kuziangalia hata maamuzi mengine yanakuwa yanasababishwa na baadhi ya wale ambao wako katika Mabaraza ya Kata. Wakati mwingine inaonekana kwamba mtu aliyenacho ndiyo huyo ambaye haki inamwendea, hili ndiyo maana Serikali ilikuwa inafanya tathimini kwa kina sana kuangalia nini kifanyike katika suala zima katika uendeshaji wa Baraza la Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Mheshimiwa Mbunge tunalichukua lakini kuna mchakato mpana tunaufanya kuona jinsi gani tutaboresha haya Mabaraza ya Kata yaweze kufanya kazi vizuri zaidi kulinganisha na hivi sasa kwa sababu haki nyingi za watu zinapotea kwa sababu haki haisimamiwi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wazo hili tunalichukua, lakini tunajumuisha miongoni mwa mambo ya kufanya restructuring tuifanyeje, lengo kubwa la Mabaraza hayo yaweze kufanya vizuri, kwa hiyo, ni wazo zuri tunalichukua kama Serikali kulifanyia kazi kwa mpango.
MHE. MICHAEL J. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inakiri kwamba Ukerewe ni moja kati ya maeneo ambayo watumishi wake wanafanyakazi katika mazingira magumu na kwa kuwa huduma za elimu na afya visiwani Ukerewe hususan kwenye Visiwa vya Ilugwa, Ukara, Bwilo na kwingineko zinaadhirika sana na changamoto zinazowakabili watumishi kwenye maeneo haya.
Je, Serikali iko tayari kutoa fedha na kuwezesha sera hii ya malipo ya mishahara na motisha katika utumishi wa umma kuanza kutekelezwa ili kuokoa maisha na mazingira ya wakazi wa visiwa hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwanzoni mwa mwaka huu Serikali ilisambaza walimu kwenye Halmashauri zetu hasa walimu wa sayansi lakini kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa walimu hawa kuishi katika mazingira magumu sana kwa sababu ya kutolipwa stahiki zao. Je, nini kauli ya Serikali juu ya tatizo hili? Nashukuru sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NAUTWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli ukiangalia si tu kwamba wananchi wa Ukerewe wanaadhirika kutokana na ukosefu wa huduma za elimu na afya, lakini hata watumishi wenyewe walio katika mazingira magumu pia huduma ya elimu katika eneo lile na afya inapokuwa si nzuri inawafanya pia na wenyewe wasivutiwe kufanya kazi katika maeneo hayo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeiona changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kwa ujumla wake mwongozo huu haujaanza kutekelezwa lakini kupitia Bajeti ya Serikali na kupitia bajeti za Halmashauri ambazo zimepitishwa wameshaanza kutekeleza maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu pamoja na afya.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba tutaendelea kulifanyia kazi kama Serikali kutoa msisitizo ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yanayokabiliwa na changamoto hizi basi yanaweza kutengewa fedha za bajeti za kutosha ili kuweza kutekeleza sera hii.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusiana na walimu wa sayansi na hesabu walipangiwa vituo mwaka huu, kwamba hawajalipwa stahiki zao. Kwa kweli ni jambo ambalo limetusikitisha, na haswa ukizingatia katika Halmashauri moja unakuta mtu amepangiwa walimu 12 tu, inakuwaje Halmashauri inashindwa kuwahudumia kwa watumishi wake wapya waliopangiwa katika kituo kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, niseme kupitia hadhara hii natoa tamko au agizo kwa Halmashauri zote zilizopokea walimu wapya wa sayansi na hesabu lakini pia zilizopokea wataalam wa maabara za sayansi zihakikishe ndani ya siku saba zimewalipa watumishi hao stahiki zao zote. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ukerewe ni wazalishaji wakubwa wa matunda hasa machungwa na nanasi. Lakini wananchi wa Ukerewe wamekuwa hawafaidiki sana na matunda haya kwa sababu sehemu kubwa ya matunda imekuwa ikiharibika kwa sababu ya kukosa soko.
Je, Serikali iko tayari kusaidia upatikanaji wa kiwanda cha kusindika matunda haya ili wananchi wa Ukerewe wapate soko la uhakika wa matunda yao?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba bado tunayo changamoto katika usindikaji wa matunda. Na katika mtazamo wetu Tanzania tunajipanga zaidi katika huu ukuzaji wa viwanda hasa katika eneo la kilimo na manasi pamoja na machungwa ni mazao mojawapo ambayo yana changamoto. Jambo ambalo tunaliona sasa hivi ni kwamba iko haja ya kuunganisha taasisi zetu hasa katika kukuza teknolojia zitakazowezesha matunda yanapokuwa yamezalishwa, yasiharibike kiurahisi na kuyaongezea thamani.
Lakini vilevile nikuombe Mheshimiwa Mbunge ukiwa ni sehemu ya uhamasishaji pamoja na Serikali kuendelea kuwahamasisha wadau binafsi kwa ajili ya kuwekeza viwanda katika eneo hilo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara nyingi za mikoa sasa zimeshajengwa na kuna tatizo kubwa sana la barabara Wilayani na vijijini; na TARURA wamepewa jukumu la kujenga barabara hizi, lakini pesa wanazozipata bado hazitoshi. Serikali sasa haioni sababu za msingi za kubadili formula ya ugawaji wa pesa kati ya TANROADS na TARURA ili kuongeza percentage ya pesa zinazoenda TARURA? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kati ya Lugezi na Kisorya kuna kivuko ambacho ni mbadala wa daraja, lakini katika kivuko kile kuna tatizo kubwa la utozaji wa nauli, hususan mizigo ambayo inaleta kero sana kwa wananchi kwa mizigo iliyo chini ya kilo 20. Inategemea busara ya mtozaji kama kilo moja atatoza kiasi gani? Kilo mbili kiasi gani?
Sasa Serikali haioni sababu kuweka kiwango maalum, kwa mfano, chini ya kilo 20 wananchi wasitozwe tozo zozote za nauli ya mizigo ili kuondoa migogoro ambayo imekuwa inajitokeza mara kwa mara kati ya vivuko vya Kisorya na Lugenzi na Bugorora na Ukara? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunaendelea na ujenzi wa barabara na kipaumbele kilikuwa kwenye barabara kuu. Barabara kuu zina urefu wa zaidi ya kilometa 8,000 na kwa sasa hivi tumeshavuka nusu ya urefu huo. Kwa maana hiyo, sasa ni fursa ambayo itawezesha Serikali kuelekeza fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza barabara ambazo zinaunganisha mikoa na hatimaye pia kwenda kuunganisha barabara ambazo ziko chini ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba utambue hivyo, pamoja na wapiga kura wa Ukerewe kwamba tumejipanga vizuri. Mara baada ya kukamilisha sehemu kubwa ya barabara kuu, nguvu kubwa ya Serikali itaelekezwa katika eneo la barabara ambazo ziko kwenye Mikoa na Wilaya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwamba tunachukua hatua gani kwa ajili ya gharama ya kivuko hiki cha MV Ujenzi?
Mheshimiwa Spika, ninatambua, nasi upande wa Serikali tumelichukua hili, lakini tumeshaanza kufanya utafiti wa kuhakikisha kwamba suala la bei hii ya vivuko tunaliangalia kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, iko hoja kwamba gharama ya ubebaji wa mizigo iko chini kwenye baadhi ya maeneo, lakini yako maeneo yanaonesha kwamba gharama ni kubwa. Kwa maana hiyo sasa, tunafanya utafiti ili tuweze kuja na bei ambayo itakuwa rafiki kwa watumiaji wa vivuko hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Ukerewe tuvute subira. Nawaomba na wenzetu wa upande wa TEMESA waharakishe hili zoezi la kufanya utafiti ili tuweze kuchukua hatua ambayo itafanya usafiri huu uwe rafiki kwa watumiaji wa vivuko. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa zoezi hili la kuzuia uvuvi haramu linatumiwa sasa na vikosi vya doria kunyanyasa, kudhalilisha na kupora wananchi hasa wavuvi kwenye Visiwa vya Ukerewe kwa kuwadai pesa na malipo mbalimbali yasiyo halali. Nataka kujua Serikali iko tayari kutoa kauli kuzuia unyanyasaji huo lakini na Mheshimiwa Waziri kufika Ukerewe kukaa na wavuvi na kupata ushahidi wa haya yaliyotokea ili Serikali iweze kuchukua hatua kwa wahusika? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe. Naomba kusema kwamba kama kuna changamoto yoyote ambapo watendaji wetu kwa namna ile wameenda kinyume na misingi na taratibu tulizowapa, watendaji wetu wote wanapoenda doria wanapewa mwongozo wa makosa gani ambayo yanatakiwa kuchukuliwa hatua na kwa kiasi gani. Mheshimiwa Mbunge kama anayo hiyo orodha ya watu ambao anasema kwamba hawakutendewa haki atuletee sisi tutalishughulikia mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mimi kwenda Ukerewe…
MHE. JOSEPH MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mahakama ya Mwanzo ya Bukindo, Bukonyo na Ukara zina hali mbaya sana kimiundombinu, achilia mbali upungufu wa watumishi. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira haya ili haki ya wananchi wa Visiwa vya Ukerewe iweze kupatikana kwa haraka?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wilaya ya Ukerewe, imepangiwa kujengewa Mahakama ya Mwanzo katika eneo la Ilangala katika mwaka wa fedha unaoanza sasa wa 2018/2019.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo ambapo shughuli nyingi za uvuvi zinafanyika kunapatikana athari za kijamii za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kama ilivyo kwenye maeneo zinapofanyika shughuli za uchimbaji wa madini ambapo maeneo yanayozunguka migodi hii yanapata mrahaba kama sehemu fulani ya ku-recover athari hizi.
Je, Serikali haioni sababu sasa sheria hii iweze kutumika kwenye maeneo ambako shughuli za uvuvi zinafanyika na kusababisha athari mbalimbali za kijamii kwa ajili ya ku-recover sehemu ya athari hizi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameulizia suala la kupata service levy kutokana na uvuvi katika Ziwa Victoria. Naomba niseme tu suala la uvuvi haliko katika Sheria ya Madini ambayo tunaisimamia sisi. Nadhani ni vema Mheshimiwa Mbunge akaifuatilia Sheria ya Serikali za Mitaa kuona kama kuna stahiki ambayo unaweza ukaipata kutokana na masuala ya uvuvi. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa baada ya operesheni nyavu zinazotumika sasa ni mbovu sana, hazina kiwango na wala hazistahili kutumika kwa uvuvi, zinawatia hasara sana watumiaji. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kupata nyavu zinazostahili, zinazoweza kukabiliana na mazingira ya Maziwa Viktoria, Tanganyika na mengineyo ili wavuvi wetu mbali na kupata hasara za kuchomewa nyavu wasiendelee kupata hasara za kununua nyavu kila siku chache zinapokuwa zinapita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, juu ya suala linalohusu ubora wa nyavu, ni kweli Wizara yangu imepokea malalamiko kutoka kwa wavuvi kutoka pande zote za nchi yetu hasa wavuvi wa Ziwa Viktoria na tumekwenda kujiridhisha. Tupo katika utaratibu wa kuendelea kufanya tathmini ya hali hii. Nataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tunashirikiana vyema na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya kuweza kupata viwango halisi vya ubora wa nyavu zetu zinazozalishwa nchini.
Mheshimiwa Spika, pale itakapobainika kwamba liko tatizo juu ya ubora huu, la kwanza tutawataka ama tunawataka wazalishaji wetu waongeze viwango vyao vya ubora, lakini ikibidi sisi kama Wizara tuko tayari kutafuta mpango mwingine wa kuweza kuwanusuru wananchi wetu ili waweze kuendelea na shughuli hii ya uvuvi bila ya tatizo lolote.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa fursa ya kuulizwa maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na umuhimu wa huduma za ugani na upatikanaji wa pembejeo lakini bado huduma hizi haziwafikii wananchi kwenye maeneo ya chini kule ambako ndiko kwenye uzalishaji. Nini sasa mkakati wa Serikali ili kuondoa tatizo hili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo kwa zao la pamba, zao la muhogo ambalo limekuwa muhimu sana kwa wananchi wa Visiwa vya Ukerewe kiuchumi, lakini hata kwa chakula limekuwa linakabiliwa na matatizo mengi sana ya magonjwa, lakini hata tatizo la ardhi kwenye eneo la Visiwa vya Ukerewe. Je, Serikali ina mkakati wowote wa kutuma timu ya wataalam kufanya utafiti ili basi Visiwa vya Ukerewe vitumie ardhi yake hii ndogo kwa tija zaidi katika kuzalisha zao hili la muhogo? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kujibu maswali la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kuhusu mikakati ya Serikali tuliyo nayo kwa ajili ya pembejeo na Maafisa Ugani. Kwanza tumezielekeza Halmashauri zote nchi ni kutenga asilimia 20 ya mapato yao ya ndani kwa maagizo ya Serikali kupitia Waziri Mkuu kwa ajili ya kupeleka kwenye sekta ya kilimo ili Maafisa Ugani hawa waweze kuwezeshwa kwa ajili ya kuwafikia wakulia kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, viongozi wote wa Serikali katika ngazi mbalimbali, hasa wale wanaosimamia sekta ya kilimo tumewaambia lazima washiriki katika kilimo ili mashamba yao pia yaweze kuwa mfano kwa wakulima wale ambao wapo wanazunguka. Tunafahamu pia kwamba tuna upungufu mkubwa wa Maafisa Ugani nchini, mahitaji ni zaidi ya 20,000 lakini tulio nao ni 6,800. Tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Utumishi kwa ajili ya kuongeza Maafisa Ugani nchi nzima ili wawafikie wakulima wetu kwa ajili ya kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu zao la muhogo kukubali kule Ukerewe pamoja na vituo vyetu vya utafiti, tuko tayari kama Serikali na tunawaagiza kituo chetu cha utafiti cha pale Ukiruguru, Mwanza pamoja na Ilonga kufika maeneo hayo ya Ukerewe kwa ajili ya kufanya utafiti wa udongo kuona namna gani zao hili linaweza kulimwa katika Visiwa Vya Ukerewe.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa takwimu zinaonesha ni takribani asilimia 30 tu ya akina mama wajawazito ndio wanaohudhuria kliniki.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa akina mama wajawazito ili wahudhurie kliniki na waweze kuepuka matatizo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; umbali kutoka mahali ambapo akina mama wajawazito wanapata huduma ni moja kati ya sababu zinazosababisha matatizo hayo. Kwa mfano, kwenye Jimbo la Ukerewe ambalo linaundwa na visiwa vingi, Visiwa kama Zeru, Kamasi, Bulubi, Gana vyote vile vinatumia zahanati moja.
Sasa kama Serikali ilivyofanya kwa Kituo cha Bwisya, tunashukuru, je, Serikali iko tayari kushirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Afya ili ama kituo hiki cha Kamasi kiweze kupandishwa na kupata pesa za kutengeneza miundombinu kuweza kutoa huduma zilizo bora kwa kina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu za hali ya utoaji huduma za afya mwaka 2015 akina mama ambao wanakwenda kliniki angalau mara moja tuko asilimia 90, lakini tunataraji kina mama waende kliniki angalau mara nne katika kipindi chao cha ujauzito, na sasa hivi tuko kwenye zaidi ya asilimia 60 katika kiwango cha kitaifa. Kwa hiyo, rai yangu bado naendelea kutoa kwa wanawake wote wajawazito katika nchi yetu kuhakikisha kwamba wanapokuwa wajawazito angalau kufika katika vituo vyetu vya kutolea (Anti-Natal Clinic) angalau mara nne ili iweze kuwasaidia kupata ushauri na jinsi gani bora ya kuweza kuhudumia ujauzito waliokuwa nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameongelea suala la umbali. Serikali inatambua hilo na tumekuwa tunaendelea kuboresha huduma za afya na hivi vituo 208 ambavyo tumeviboresha hivi karibuni na kuweza kutoa huduma nzuri za ujauzito na upasuaji pamoja na kujifungulia ni moja ya mkakati wa Serikali. Kuna mkakati wa kuongeza Hospitali za Rufaa za Wilaya, tuna mkakati wa kuongeza Hospitali za Rufaa za Mikoa na kadri tutakapokuwa tunaona mahitaji katika hivyo visiwa vingine vya Ukerewe ambavyo umevisema hatutasita kukaa na wenzetu wa TAMISEMI na kuangalia jinsi gani ya kuboresha huduma katika maeneo hayo husika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mradi wa maji wa Bukindo, Kagunguli Visiwani Ukerewe unatekelezwa kwa ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais na kusimamia na MWAUWASA. Mradi ule kwa sehemu kubwa umekamilika lakini haujaanza kutoa huduma kwa sababu ya kukosa pesa za kuunganisha umeme. Je, Serikali iko tayari kuwasiliana na MWAUWASA ili waweze kusaidia uunganishaji umeme mradi huo uweze kutoa huduma uweze kuwasaidia wananchi wa Kata za Bukindo, Kagunguli na Mtungulu ambao watafaidika na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari kufanya mawasiliano na Mkurugenzi wa MWAUWASA na ikatakapobidi tufanye jambo hili la haraka ili wananchi wake waweze kupata umeme ili mradi uweze kutekelezeka na wananchi waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. MICHAEL J. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali bado kuna matatizo makubwa sana kwenye utendaji katika ngazi hizi za chini zinazotokana na ama na kutokuelewa wajibu wa kila upande katika kusimamia utendaji kwenye maeneo haya. Je, bado Serikali haioni sababu ya msingi kabisa kutoa elimu pamoja na majibu haya yaliyotolewa bado kuna tatizo kubwa sana kwenye usimamizi hasa nyakati za uchaguzi ambapo kumekuwa na migogoro mingi inayotokana na watendaji wanaosimamia chaguzi hizi kufanya au kutoa maamuzi kulingana na maelekezo yanayokuwa yametolewa na viongozi wa juu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na migogoro hii, Serikali haioni kwamba kuna sababu ya msingi kabisa kutokana na mapendekezo ya Katiba iliyopendekezwa kuwepo na umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ili kuondoa kabisa migogoro hii inayotokea nyakati za uchaguzi kwenye ngazi mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimhakikishie kwanza uzoefu wangu kwamba kati ya mwaka 1996 mpaka mwaka 2000 mwenyewe nilikuwa Ofisa Mtendaji wa Kata, kwa hiyo nina uzoefu mkubwa na kile ninachokielezea na kata yenyewe ilikuwa ni Kata ya Manzese pale Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chaguzi za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa sheria na kama atatokea Msimamizi Msaidizi yeyote akatenda kinyume cha sheria, mdau yeyote anao uhuru wa kulalamika katika vyombo vinavyohusika ikiwemo kulalamika kwa Msimamizi wa Uchaguzi na hatua zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya watu ambao wanatenda kinyume cha utaratibu wa sheria ya uchaguzi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, ameuliza kwamba kuna mapendekezo kwenye Katiba iliyopendekezwa. Sasa kwa sababu Katiba iliyopendekezwa bado hatua zake hazijakamilika, nashauri Bunge lako Tukufu kwamba tusiwahishe mambo, tusubiri kwanza huo mjadala wa Katiba Mpya Iliyopendekezwa ukamilike na mambo yaingizwe kwenye sheria basi hapo tutatekeleza baada ya sheria kuwa imekamilika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Kwanza nishukuru kwa majibu yenye kutia matumaini ya Serikali kupitia kwa Naibu Waziri. Lakini kwa kuwa usanifu wa awali ulionesha chanzo cha maji kwa ajili ya miradi hii ambacho sasa si cha kuaminika, Serikali sasa iko tayari kupitia usanifu ule ili chanzo cha maji kwa ajili ya mradi huu ukiwa ni Ziwa Victoria?

Swali la pili, kwa sababu mbali na Bonde hili la Miyogwezi, kuna Bonde la Bugolola lakini na maeneo mengine ambayo ni potential kwa ajili ya uzalishaji wa chakula kwenye Visiwa vya Ukerewe. Lakini yote haya tunaweza tukayatumia kwa ufanisi kama Mheshimiwa Waziri anaweza kufika pale akapitia na tukaweza kufanya maamuzi yenye maslahi.

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuandamana na mimi ili tuweze kufika katika Visiwa vya Ukerewe tuweze kupitia mambo haya? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyotumia muda mwingi kufuatilia na kuwapigania watu wake wa Ukerewe.

Pili, nimesikiliza ushauri wake na kwa niaba ya Serikali tunauchukua ushauri huo na nichukue nafasi hii kuwaelekeza Wahandisi wetu wa Kanda ya Umwaliaji, Kanda ya Mwanza kufika Ukerewe kuanza uchambuzi wa awali kuangalia hiko chanzo kipya na cha zamani ili kuja kutushauri kitaalam kuutekeleza mradi huo upya.

Swali lake la pili, kutaka kwamba kwenda kuambatana na mimi kufika katika eneo hili, Mheshimiwa Mbunge niko tayari baada ya Bunge hili likimalizika tarehe 8 Februari tuoanane ili tupange siku gani tunaweza kutembelea huko maeneo yake.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Tatizo la kukatika kwa umeme limekuwa linajitokeza sana kwenye Visiwa vya Ukerewe hali inayoathiri shughuli za kiuchumi na hasa shughuli za utoaji wa huduma za afya kwenye hospitali yetu ya Wilaya ya Nansio.

Ningependa kupata kauli ya Serikali, ni mkakati gani uliopo kuondoa tatizo hili na kufanya Visiwa vya Ukerewe vipate umeme bila shida ya kukatikakatika kwa umeme kwenye maeneo hayo. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi Mbunge wa Ukerewe kupitia Chama cha Mapinduzi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge aliwasilisha hilo leo asubuhi kwamba kuna tatizo hilo katika Visiwa vya Ukerewe na hapa nilipo nishatoa maelekezo kwamba kwa sababu umeme wa Ukerewe unatokea katika maeneo ya Bunda na kwa changamoto ambayo nimeipata hivi asubuhi baada ya kuwasiliana na Meneja kwamba kuna tatizo la changamoto ya nguzo, ndiyo maana Serikali imefanya maamuzi ya kuhama sasa itumie nguzo za zege.

Kwa hiyo, tumetoa maelekezo ifanyike utafiti wa kina changamoto ni nini ili ifanyiwe kazi, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kutoka hapa tufanye mazungumzo ili kuweza kumpa mikakati ambayo Serikali imepanga. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nitumie fursa hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake na nimshukuru kwa ushirikiano ambao amekuwa anautoa kwa masuala ya uvuvi. Nina maswali mawili ya nyongeza; la kwanza uvuvi wa dagaa wanavuliwa kwa kuchotwa, kwa hiyo isitegemee kwamba wategemee dagaa wale wanase kwenye nyavu, ndio maana ni muhimu angalau matundu yake yawe madogo kidogo. Sasa kwa kuwa dagaa wanaopatikana Ziwa Victoria hawatofautiana sana na dagaa wanaopatikana Bahari ya Hindi na natambua kuna mchakato wa kufanya utafiti kwenye Bahari ya Hindi ili dagaa wanaovuliwa kwenye Bahari ya Hindi wavuliwe kwa nyavu za milimita sita na kuendelea. Je, Serikali haioni sababu sambamba na utafiti utakaofanyika Bahari ya Hindi ufanyike vilevile na uvuvi utakaofanyika Ziwa victoria kwa dagaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wavuvi wa Ukerewe wa samaki aina ya gogogo au ngere wanapata bugudha sana wakati wanavua samaki wale kwa kisingizio kwamba sheria hairuhusu, lakini mazingira ya uvuvi wa samaki wale na aina yake ni tofauti sana na samaki wengine. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa tamko ili wavuvi wa ngere kwenye Visiwa vya Ukerewe na maeneo mengine wasibughudhiwe ili wafanye shughuli zao za uvuvi wa samaki hawa bila shida yoyote. Nashukuru sana?
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mkundi na timu ya Waheshimiwa Wabunge katika eneo la Ziwa Victoria kwa namna ambavyo mara kadhaa wamekuwa wakisimamia maslahi mapana ya wapigakura wa eneo hili ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za nchi yetu kupitia sekta hii ya uvuvi. Sasa swali la kwanza la Mheshimiwa Mkundi linahusu juu ya ya Serikali kuwa tayari kufanya utafiti katika eneo la Ziwa Victoria kama ambavyo tunafanya utafiti kwenye maji ya bahari ili kuweza kuruhusu nyavu ya chini ya milimita nane kuweza kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kuwa, kwa upande wa bahari bahari zilizokuwa zikitumika ni milimita 10 na zimekubalika kuonekana na maoni ya wadau kuwa milimita 10 zimeshindwa kukamata dagaa na ndio maana Serikali tukaielekeza Taasisi yetu ya Utafiti (TAFIRI) kufanya utafiti na kujiridhisha ya kwamba tufanye mabadiliko ya kanuni kwa haraka ili ikiwezekana tuweze kutumia nyavu za milimita nane ili kuweza kuwabnufaisha wavuvi wa upande wa bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa rai hii ya kutaka tutumie njia hiyo ya utafiti kwa upande wa Ziwa Victoria, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mkundi na Waheshimiwa Wabunge wote wavuvi wa kutoka Ziwa Victoria tunaichukua rai hiyo na tutawaelekeza TAFIRI waweze kufanya utafiti na kuweza kujiridhisha bila ya kuathiri sekta hii ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mkundi linahusu uvuvi wa samaki aina ya gogogo, ngere na ningu. Samaki hawa ni samaki wenye kupendwa sana katika eneo la Ziwa Victoria naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge katika mabadiliko ya kanuni tunayoyafanya hivi sasa tumezingatia kwamba tufanye makubaliano ya kuweza kupitisha kanuni rasmi sasa ya kuweza kuvua na kutumia rasilimali hii ya samaki hawa aina ya gogogo, ningu na ngere ambao wameonekana katika kanuni zilizopita kuwa hawakutajwa moja kwa moja. Naomba niwahakikishie wavuvi wote wa eneo la Ziwa Victoria Serikali inalifanyia kazi jambo hili na muda si mrefu watapata matokeo ili waweze ku-enjoy na kufurahia rasilimali za Taifa lao.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini ukweli ni kwamba pamoja na maelekezo yanayoelekezwa kule chini, viongozi hawa wa Mitaa na Vijiji, Vitongoji hawalipwi posho zao; na kwa kuwa Serikali kwa namba ya viongozi hawa kuwa kubwa inashindwa kuongeza posho zao:-

Serikali haioni umefika wakati sasa kufikiria uwezekano wa kuwalipa kiwango fulani cha pesa viongozi hawa pale wanapomaliza muda wao wa Uongozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona Waheshimiwa Wabunge wanazungumzia posho za Madiwani na posho za Wenyeviti wa Mitaa; naomba nitumie nafasi hii kusema tu kwamba wakati tunamalizia hoja yetu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, suala la posho za Madiwani zile ambazo zilikuwa zimezungumzwa, Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo kwa Madiwani wote wa Halmashauri watapata Waraka wa maelekezo kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuondoa sintofahamu ya posho za Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali alilouliza Mheshimiwa Mkundi, tulipokee; ni kweli kwamba Wenyeviti wa Mitaa baada ya kustaafu kuna kiwango cha fedha wanapaswa kulipwa. Sasa maoni ya Mbunge ni kwamba tuangalie namna ya kuongeza kiwango hiki (lump sum amount) kama watasema ni shilingi 500,000/= au shilingi 1,000,000/= kwa mkupuo itaweza kuwasaidia. Jambo hili tunalipokea, tunalifanyika kazi, kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu, tutalitekeleza kwa sababu ni jambo jema kwa ajili ya viongozi wenzetu hawa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Baada ya ajali ya Kivuko cha MV Nyerere tarehe 20 Septemba, mwaka jana pale Ukala, Serikali iliahidi kutengeneza kivuko kipya kwa ajili ya kusaidia wananchi eneo lile. Hivi sasa kuna kivuko cha muda cha MV Sabasaba ambacho kimekuwa na changamoto nyingi sana. Nataka kujua kutoka Wizara, ni hatua ipi imefikiwa ya ujenzi wa kivuko kipya kitakachofanya kazi kati ya Bugolora na Ukara? Nashukuru.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHATA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ile ajali Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshatangaza tenda na Mkandarasi amepatikana na mkataba umeshasainiwa na sasa hivi tunaendelea kununua engine haraka ili kitakapokamilika kifungwe, lakini pamoja na Kivuko cha Nyamisati, Mafia.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kumekuwa na tatizo kubwa sana la kukatika kwa umeme wakati mwingine kwa siku nzima au hata zaidi ya siku kwenye visiwa vya UKerewe kila wakati mvua inaponyesha. Ningeomba Mheshimiwa Waziri awaambie wananchi wa Ukerewe ni lini tatizo hili litakoma ili wafurahie huduma ya umeme kama yalivyo maeneo mengine nashukuru sana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo la Ukerewe kwa mwezi mmoja uliopita umeme ulikuwa umekatika sana umesababishwa na sababu moja tu, wavuvi wanaovua kutoka eneo la Kisolia ambapo ni mwanzo wa kuingilia kutoka Bunda kuelekea Lugenzi wamekuwa mara nyingi sana wakikata nyaya wakati wa uvuvi. Lakini nyaya zile zimekuwa zikitikiswa pia wakati wa mvua inapoambatana na upepo, kwa hiyo, ni kweli maeneo ya Ukerewe yamekuwa yakipata changamoto kwa kukatika kwa umeme kipindi hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua tulizochukua kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge na wananzegwa wananchi wa Ukerewe ni kwamba kwanza tumeanza kujenga kebo ya kutoka Kisolia kwenda Lugenzi ambapo ni kilomita nne na tume-commit shilingi bilioni 375 na ujenzi umeanza tutafunga kebo tutaipitisha juu ili wavuvi waache kuzigusa na hivyo kutakuwa na umeme muhimu sana kwa maeneo hili. Kwa hiyo, wananchi wa Ukerewe wavumilie kipindi cha wiki mbili zinazofuata mradi utakamilika ili umeme uwe ni uhakika zaidi kwa maeneo ya UKerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipe nafasi kidogo kwa sababu ni suala la Ukerewe nitoe tangazo kwa wananchi sio wa Ukerewe peke yake ingawa Mheshimiwa Mbunge hajaliuliza, kumekuwa na changamoto kwa wananchi wa Ukerewe hasa watumiaji wadogo wa umeme kutozwa shilingi 2500 kwa unit kinyume na utaratibu na sheria ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe tangazo kwa wananchi wa Ukerewe wasikubali kutoa shilingi 1000 kwa unit kwa sababu wananchi wote wa Ukerewe ni sawa na Watanzania wengine ambao wanatumia unit 75 ambao wanatakiwa walipe shilingi 100 per unit badala ya 2500 per unit.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe tangazo hili Mheshimiwa Mbunge anifikishie, lakini nimuombe Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe alisimamie na Meneja wa TANESCO alisimamie ili mwananchi yoyote atakayepatikana akitozwa hivyo kupitia kwa mkandarasi basi atoe taarifa mara moja na Serikali ichukue hatua dhidi ya watu ambao sio wazalendo kwa kitendo hicho ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini napongeza vile vile hatua zilizofikiwa za kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na kwamba utafiti bado unaendelea, lakini tatizo la msingi tayari limepatikana kwamba kuna kiwango kidogo cha mboji, lakini pH vilevile ya udongo wa Ukerewe iko chini. Sasa swali langi, Wizara iko tayari kuijumuisha Ukerewe katika maeneo yanayopata ruzuku za pembejeo itakayoambatana na ushauri wa aina ya mazao yanayopaswa kulimwa kwenye maeneo yetu ya Ukerewe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Ukerewe tuna fursa kubwa sana ya matunda, lakini tatizo kubwa, matunda yetu yamekuwa yanaharibika kwa kukosa soko. Tumejitahidi kupata wawekezaji kwa ajili ya kujenga viwanda, lakini tumekuwa tunakwama ama kutokana na kiwango cha malighafi inayozalishwa au aina ya matunda tunayoyazalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iko tayari kuwasaidia wananchi wa Ukerewe ambao wanalima matunda ili aina ya matunda yanayotakiwa iweze kulimwa, lakini sambamba na hilo, kusaidia kuwepo kwa kiwanda cha kusindika matunda haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN MOHAMED BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mkundi kwa kazi kubwa anayofanya Jimboni kwake. Kuhusu suala la kupewa ruzuku kama ni special case, suala la ruzuku kwenye mbolea, hatuwezi kutoa commitment kama Serikali kwamba tutawapa watu wa Wilaya ya Ukerewe peke yao. Suala la ruzuku ama mabadiliko ya sera juu ya suala la kutoa ruzuku katika Sekta ya Kilimo, litatazamwa kwa ujumla wake kwa kuwa sasa hivi Wizara inapitia upya Sera yetu ya Kilimo ya Mwaka 2013 ili kuona mahitaji na namna gani tunaweza kutatua changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua za awali, tunaendelea kusisitiza wananchi wa Wilaya ya Ukerewe, watumie mbolea za minjingu na mbolea nyingine ambazo zinaweza kuongeza uzalishaji katika eneo lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la matunda, siyo suala la Ukerewe peke yake, mazao yote ya horticulture sasa hivi kama Wizara tunafanya baseline study ya kuangalia ni namna gani tunaweza kufanya zoning ya kila eneo ili tuweze kutambua ni mazao gani ya high value yatokanayo na horticulture yanaweza kuzalishwa. Wizara sasa hivi iko katika hatua za awali kuangalia ni namna gani sekta ya horticulture inaweza kupewa kipaumbele na namna gani mazao ya matunda na mboga mboga yanaweza kupewa kipaumbele kama zao la muhimu kwa ajili ya export katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwaombe Waheshimiwa Wabunge watupe muda, kabla ya mwaka wa fedha ujao tuta-unveil Sera ya Wizara ambayo itafanya diversification katika sekta nzima ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri limeonesha wavuvi na wadau 520 wamepata elimu hiyo lakini pamoja na kuwapa elimu watu hawa 520 hakuna mfumo rasmi unaoweza kusaidia hii elimu waliyoipata ku-disseminate kuwafikia wadau wengine ambao ni sehemu kubwa ya wakazi wa Jimbo la Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka jana alitembelea Jimbo la Buchosa akatumia mfumo mzuri sana kutoa elimu kwa wavuvi wa eneo lile. Swali la kwanza, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuja Ukerewe ili kwa pamoja tushirikiane kuwapa elimu wadau wetu hawa wavuvi waweze kujua hasa nini kinachopaswa kufanyika kwenye eneo la uvuvi kuwaondolea adhabu wanazopata bila kuwa na elimu ya msingi kujua wajibu wao ni upi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hatua iliyofikiwa na kikundi hiki cha Bugasiga ni nzuri na ilipelekea kupata mkopo wa shilingi milioni 250 na nina kila sababu ya kuipongeza Serikali kuwezesha jambo hili. Changamoto zilizopo ni kwamba mkopo huu unatolewa kwa ushirika unaolazimisha sasa dhamana inayotakiwa iwe ni kwa mtu mmojammoja na matokeo yake sasa mkopo unaonekana kama ni wa mtu mmoja na sio ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali kwa nini isitengeneze mfumo kwamba wadau hawa kupitia ushirika wapewe mikopo lakini sasa wao wenyewe waunde SACCOS ili SACCOS zile zikopeshe mdau mmoja mmoja na wawajibike kwa SACCOS halafu SACCOS ndio iwajibike kwenye ushirika? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukrani kwa Mheshimiwa Mbunge kutupongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri tuliyoifanya katika eneo la Kanda ya Ziwa ya kutoa elimu na akatolea mfano wa Jimbo la Buchosa ambalo hivi sasa tunacho Chama cha Ushirika cha Zilagula Fisheries Cooperative ambacho na chenyewe kimeomba mkopo wa shilingi milioni 300 na kitakwenda kupata kupitia TADB lakini na vyama vingine takribani milioni 50 kila chama shilingi milioni 10. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi la utoaji elimu ni endelevu na sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tupo tayari tutakwenda Ukerewe mara tu baada ya kuahirishwa kwa Bunge hili kwenda kutoa elimu ile kwa wavuvi wa pale Ukerewe ili waweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili linahusu juu ya mfumo wa mikopo kupitia ushirika na SACCOS. Naomba tulichukue wazo lake hili ni ushauri mzuri ambapo Wizara tutaufanyia kazi. Kwa kuwa tayari tunalo Dawati letu la Sekta Binafsi linalofanya kazi nzuri sana ya kuratibu mikopo hii na kuratibu namna ya kuweza kuwasaidia vyama vya ushirika, nataka nimhakikishie kwamba ushauri huu tunauchukua na tunakwenda kuufanyia kazi kwa maslahi mapana ya wadau wetu wa uvuvi ili waweze kusonga mbele. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Jimboni Ukerewe mwaka jana tarehe 5 Septemba, 2018, alitoa maelekezo ya ujenzi wa km 14 za lami kutoka Lugeze - Nansio mjini. Nataka kujua ni hatua ipi imefikiwa ili ujenzi huo uweze kuanza? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii ameifuatilia muda mrefu na matokeo yake niseme kwamba usanifu wa barabara hii umeshaanza ukikamilika tutajenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na matatizo makubwa ya kijiografia yaliyoko katika Visiwa vya Ukerewe yanayoathiri utoaji wa huduma za afya lakini tuna madaktari 3 pekee kati ya 10 wanaotakiwa, tuna waganga wasaidizi 5 pekee kati ya 43 wanaotakiwa na tuna wauguzi 80 pekee kati ya 289 wanaotakiwa. Nini kauli ya Serikali wanayoweza kuwaambia wananchi wa Ukerewe juu ya kuboresha huduma za afya kwa kutoa wahudumu wa afya kiasi kinachotakiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yana upungufu mkubwa wa watumishi, wakati tunaajiri hao 550 tutazingatia. Naamini na Ukerewe nao hatutawasahau, ipo nia kubwa kuhakikisha kwamba tunapunguza hilo pengo la upungufu wa watumishi. Naomba nimhakikishie Mbunge tutazingatia katika mgao.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza maswali ya nyoneza. Kwanza nipongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nitakuwa na maswali mawili, la kwanza kwa mujibu wa maelezo ya waziri, Wizara inafungua Ofisi za Kanda Mwanza pale zikijumuisha Idara ya Utalii pamoja na kodi ya utalii, lakini kuna taarifa kwamba TANAPA imegawa shughuli zake Kikanda, na moja ya Kanda hizo ni Kanda ya Kaskazini Magharibi na kwa mujibu wa taarifa tulizonazo ni kwamba uongozi wa bodi umeelekeza Ofisi za Kanda ziwe Bunda eneo ambalo ni jarani sana na Serengeti. Lakini ili kusaidia ukuzaji wa utalii kwenye maeneo ya Ukerewe, Saanane, Lubondo nakadhalika. Ni kwa nini Ofisi za TANAPA za Kanda hizi, Kanda ya Kaskazini Magharibi isiwe Mwanza ziliko Ofisi za Utalii pamoja na Bodi ya Utalii badala yake zipelekwe Bunda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kama Mheshimiwa Waziri alivyosema Wizara tayari imetambua uwepo wa vivutio vya utalii na sasa inahitaji kuviendeleza na kuvitangaza. Sasa ili kufanikisha hili ni kwa nini wizara sasa isiwekeze pesa pale Ukerewe kwa ajili ya maandalizi ya miundombinu lakini pamoja na ku-train wadau mbalimbali wakiwemo hizi local groups ambazo zimekuwa zikibainisha vivutio hivi ili kama maandalizi sasa ya kukuza na kutangaza utalii ulioko kwenye Visiwa vya Ukerewe? Nashukuru sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru kwa pongezi zake, kwa wizara ambazo amezitoa na kulidhika na majibu yake ya maswali ya msingi. Lakini Mheshimiwa Mkundi ameomba kufahamu kwamba TANAPA katika juhudi za kuboresha shughuli za kukuza na kusimamia uhifadhi na utalii wamefungua Ofisi Kaskazini Magharibi, lakini Ofisi hiyo wameipeleka Bunda badala ya Mwanza na ameshauri kwa nini Ofisi hiyo isikae Mwanza ambapo kuna Ofisi za TTB na Ofisi za utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge nitawasiliana na TANAPA na kuona sababu za msingi zilizowapeleka Bunda, lakini ninaamini kwamba ushauri wake ni wa msingi kwa sababu Mwanza bado ni kitovu cha Kanda ya Ziwa ambapo ingelikuwa rahisi zaidi kuwahudumia wateja kuliko Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wake wa pili swali langu la msingi limejibu kwamba baada ya kuziimarisha vituo hivi vyote vya mali kale tunajielekeza sasa kwenye kushirikiana na taasisi zetu mbalimbali ambazo tutazikabidhi kwenye maeneo mengi ili ziweze kuviambatanisha vituo hivi pamoja vivutio mbalimbali vya utalii kama nilivyosema Saanane na Lubondo. Kwa hiyo, nimuhakikkishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya vituo ambavyo tutahakikisha kwamba vinapata pesa kwa ajili ya uendelezaji na kwa ajili ya kuviimarisha itakuwa ni Ukerewe ili kuhakikisha kwamba Kisiwa cha Kirewe kinatumika kama Kisiwa cha utalii katika Ziwa Victoria.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, Serikali ilitoa maelekezo kwamba kwamba wananchi vijijini waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 bila kujali kama ni kupita REA au TANESCO, lakini agizo hili bado halitekelezwi na wananchi maeneo mengi wanapata shida kwa kutakiwa kulipa gharama ileile ya zamani. (Makofi)

Je, nini kauli ya Serikali juu ya jambo hili? Nashukuru.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa
Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kuanzia tarehe moja Mei mwaka huu tumetoa maelekezo nchi nzima kwamba pamoja na kwamba katika baadhi ya maeneo ambako REA ilikuwa haijafika, kuunganishwa umeme ilikuwa ni tofauti na 27,000; lakini ili tuweze kushambulia, vijiji vyote vipelekewe umeme haraka iwezekavyo Serikali imetoa maelekezo kwamba vijijini umeme wataunganishiwa kwa 27,000 na si vinginevyo, iwe anapeleka TANESCO, iwe anapeleka REA, iwe anapeleka mkandarasi yeyote aliyepewa kazi na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwape taarifa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kote, hakuna mahala ambapo umeme utapelekwa tofauti na 27,000 ili mradi ni vijijini. Kwa hiyo, maagizo haya nimeyatoa na Serikali imeyatoa na tutaendelea kufuatilia hilo. Tupe ushirikiano Mheshimiwa Mbunge ikibidi tutatembelea jimbo lako ili tuwafafanulie vizuri wananchi. Hayo ndiyo maelekezo ya Serikali. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nishukuru vilevile kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kuwezesha vijana katika maeneo mengi, lakini bado kuna Sekta ambayo inaajiri vijana wengi sana kama vile sekta ya uvuvi na kilimo lakini hasa kwenye sekta ya uvuvi vijana wengi wameajiriwa maeneo haya lakini wanakutana na vikwazo vingi sana vinavyowafanya washindwe kufaidika na shughuli zao hizi za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba vijana wanaojiajiri na kuajiriwa kwenye sekta kwa mfano ya uvuvi wanaondolewa vikwazo wanatambuliwa na kuwezeshwa ili waweze kufanya shughuli hizi na kufaidika na shughuli hizi za uvuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Lakini, swali la pili kilimo ni sekta muhimu sana inayoweza kuwasaidia sehemu kubwa sana ya vijana, lakini bado sioni kama Serikali imefanya juhudi za kutosha za kuweza kuwatambua vijana walio na mahitaji ya kuweza kujiajiri kwenye sekta hii ya kilimo na kuwawezesha kwa kuwapa mtaji ili wafanye shughuli za Kilimo zenye ufanisi, nini mpango wa Serikali kutumia Kilimo kama sehemu kubwa inayoweza kuajiri vijana wengi kwenye nchi hii?

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza Serikali inatambua ya kwamba moja kati ya sekta ambayo inachangia katika kutoa nafasi za ajira ni pamoja na sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Spika, mpango uliopo hivi sasa na ambao tumeanza kuutekeleza ni kuendelea kuwaweka vijana wote wanaofanya shughuli za uvuvi katika ushirika na vikundi mbalimbali ili waweze kupata fursa kukopesheka kupitia Mifuko ya Mendeleo ya Vijana lakini vilevile Mifuko ya Uwezeshaji na hivi sasa tumeshafanya kazi hiyo katika baadhi ya Mikoa ikianzia Mkoa wa Geita kwenye Wilaya ya Chato, lakini vilevile na Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Pangani tumeanza kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua na tupo katika mkakati wa kuhakikisha kwamba tutaishirikisha na Benki ya TADB ili waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusu kilimo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo tunatekeleza kwa pamoja mpango wa kuwashirikisha vijana kwenye kilimo ambao una lengo la kuwafanya vijana hao kutumia fursa ya kilimo kama sehemu ya ajira.

Mheshimiwa Spika, mpaka ninapozungumza hivi sasa tayari mpango huu umeanza kutekelezwa na vijana wengi hivi sasa wameshaanza kubadili mtazamo na kukichukulia kilimo kama pia ni sehemu ya ajira tofauti na pale awali ambako kilimo ilikuwa ni last resort. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mpango huu unatekelezwa kwa pamoja na tumeanza hivi sasa katika Mpango wa Kitalu Nyumba ambao utashirikisha vijana 18,800 nchi nzima, lakini vilevile kampuni za vijana zinazofanya kilimo pia zimeanza kushiriki moja kwa moja katika kuhakikisha kwamba wanaanza kutoa msukumo na mtazamo kwa vijana wengine wengi kuingia kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatambua jambo hilo na Serikali tunaendelea kulifanyia kazi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa dhati kabisa nitambue kazi nzuri na kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi nchini, lakini majibu haya haya hayaakisi hali halisi iliyopo kwenye maeneo yetu kule. Magari mengi ya Polisi yanapoharibika hutegemea zaidi hisani ya wadau mbalimbali hasa Wabunge kuweza kuyatengeneza. Jambo hili linaathiri sana utendaji wa Jeshi letu la Polisi.

Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha utaratibu huu unatekelezwa na magari ya Polisi yanatengenezwa katika mazingira mazuri kama utaratibu ulivyoelekezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri?

Swali la pili; kama ilivyo kwa tatizo la magari vituo vyetu vya Polisi vinakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa vitendea kazi vya kila siku kama mafuta ya magari, karatasi, wino na kadhalika. Jambo hili linaathiri sana utendaji wa kila siku wa Jeshi letu la Polisi lakini hata kuchelewesha haki za wananchi wa kawaida kule kwenye vituo vyetu vya Polisi.

Nini sasa Mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inawezesha Jeshi letu kupata vifaa vya utendaji kazi vya kila siku kama hivi ili waweze kutimiza wajibu wao wa kila siku?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo inagusa maeneo yote mawili aliyozungumza ni ufinyu wa bajeti. Uwezo wa Jeshi letu la Polisi kutengeneza magari kwa maana ya kiutalam tunao lakini wakati mwingine magari haya wanapohitaji kutengeneza yanahitaji ununuzi wa vipuli na matengenezo makubwa ambayo yanahitaji fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza wadau wote mbalilmbali ikiwemo Waheshimiwa Wabunge ambao wameona changamoto hii na wameona umuhimu wa kusaidiana na Serikali kukabiliana na changamoto ya ubovu wa magari yetu katika Jeshi la Polisi. Ninawatia moyo waendelee hivyo nasi Serikali pamoja na Jeshi la Polisi mbali ya kuwa na Serikali inaendelea kuongeza bajeti la Jeshi la Polisi kadri ya hali inavyoruhusu lakini tumekuwa tukibuni mbinu mbalimbali za kuweza kuyarekebisha magari haya yaweze kuwa bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna magari katika Mikoa mbalimbali ambayo tumefanya matengenezo kwa njia hii za ushirikishaji wa wadau. Hii inakwenda sambamba na hoja yake ya pili ambayo inahusu vitendea kazi kwa ajili ya Jeshi la Polisi nami nikuhakikishie kwamba kama ambavyo sote tunatambua jinsi ambavyo uchumi wetu unavyoendelea kukua vizuri hivyo Serikali kuongeza uwezo wa kuhudumia taasisi zake ni imani yangu kwamba changamoto hizi zitaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na miundombinu mizuri iliyopo katika Kituo cha Bwisya, kuna upungufu mkubwa wa watumishi pale kituoni na kuathiri utoaji wa huduma.

Mosi, je, ni lini Serikali itapeleka madaktari na wahudumu wengine wa afya Bwisya?

Pili, Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Nansio), Vituo vya Afya na Zahanati Jimboni Ukerewe vina upungufu mkubwa wa watumishi (chini ya 50%): Ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha na hasa ikizingatiwa ugumu wa jiografia ya visiwa vya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imepata kibali cha kuajiri madaktari 610 na kuwapanga kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kutoa kipaumbele kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa. Hivyo baadhi ya Madaktari hao watapangwa kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya Wilaya ya Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuajiri wataalam wa huduma za Afya kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, katika vitongoji 514 vilivyoko Jimboni Ukerewe vitongoji 238 bado havina umeme, lakini hata vile vitongoji 276 ambavyo tayari vina umeme, umeme wake unakuwa una matatizo makubwa, umeme unakatika mara kwa mara kwenye Jimbo la Ukerewe na hii inatokana na cable inayosafirisha umeme kutoka Kisorya kwenye Lugezi kuchoka.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua sasa Serikali ina mpango gani ili kuweka cable nyingine mpya iliyo sahihi ili kurekebisha hali hiyo na kusababisha wananchi wa Ukerewe kupata umeme wa uhakika?

Lakini swali langu la pili, kupitia mradi huu wa REA Serikali iliingia mkataba na makampuni binafsi kusambaza umeme kwenye maeneo ya visiwa, baadhi ya makampuni yalifanya kazi muda mfupi lakini hayakukamilisha kazi kwenye baadhi ya visiwa kwa mfano Visiwa vya Ghana, Visiwa vya Bulubi; makampuni yalisimika nguzo lakini wananchi hawakuweza kupata umeme. Lakini baadhi ya visiwa makampuni yalitowa umeme kwa mfano Kisiwa cha Ukala, Kisiwa cha Ilugwa lakini umeme ule ukawa unauzwa kwa bei ghali na baada ya Serikali intervene gharama ile ilishuka lakini wananchi wakawa wanapata umeme kwa mgao.

Nini kauli ya Serikali sasa ili iweze kutoa faraja kwa wananchi wa maeneo haya ya Visiwa vya Ukerewe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jimbo la ukerewe ni moja wapo majimbo ambayo yako katika miradi ni jimbo linalopata umeme kwa miradi ya TANESCO ya Gridi na miradi ya off grid. Kwa hiyo ni kweli kwamba kuna tatizo la umeme ambalo linafahamika katika maeneo ya Ukerewe na hasa shida ni kama alivyosema kwamba hiyo kebo inayopeleka umeme kule imekuwa ikipata matatizo.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ukerewe linapata umeme kutoka sub station yetu ya Kibara iliyopo pale Bunda na umeme ukitoka pale unasafirishwa kwa waya za kawaida kuelekea kisolia baada ya Kisorya unaenda kupitia kwenye maji kwenda Igongo na baada ya Igongo unaingia Lugezi ambacho ni kisiwa chenyewe cha Ukerewe. Kutoka Bunda kwenda mpaka Igongo siyo shida tena, lakini kutoka Igongo kwenda mpaka Lugezi kuna mita 700 ambapo ndiyo sasa ile cable inayopitisha umeme inapita majini na imekuwa ikipata shida kwa sababu siyo ile cable ambayo inatakiwa kupita kwenye maji.

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali kupitia TANESCO imeshaanda mazingira ya kufanya njia ya muda mfupi na njia ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba basi inawekwa sub-marine cable kwa hizo mita 700 kuhakikisha kwamba sasa umeme utakuwa ni wa uhakika kwa Jimbo la Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, shida nyingine iliyokuwepo ni kwamba nguzo ambazo zimekuwa zikishikilia umeme kwenye eneo la Igongo nguzo zinazotembea kwa kilometa angalau moja zimekuwa zikijaa zikiingia kwenye maji kwa hiyo zinaharibika kwa hiyo mradi wa muda mfupi tutaweka pale nguzo za zege kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi wa umeme unaweza kuwa wa uhakika kwenye jimbo letu la Ukerewe. Lakini njia ya muda mrefu inayotarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Januari mwakani itakuwa ndiyo hiyo hiyo ya kuweka marine cable ambayo itaanzia kutoka Jimbo la Bunda pale kwenda mpaka Ukerewe itakuwa ni mradi wa uhakika ambao utafikisha sasa umeme kwenye jimbo letu la Ukerewe bila wasiwasi wowote na tunatarajia labda mwakani ndiyo serikali itajipanga kutekeleza mradi huo ambao utagharimu takribani bilioni 12.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili kuhusiana na wale wanaopeleka umeme ambao walikuwa siyo wa TANESCO. Serikali kupitia REA ilipata watu wakandarasi mbalimbali wa kupeleka umeme kwenye maeneo ambayo Gridi ya Taifa haijafika na umeme wa jua tunaita nishati mbadala, nishati jadidifu. Ni kweli kwamba maeneo ya ukerewe na maeneo mengine ya visiwa vilivyopo Muleba na Geita vimekuwa vikipata shida ya bei na shida kubwa ya bei ilisababishwa na wakandarasi waliotengeneza hiyo miradi kuwa na gharama kubwa ya uuzaji wa umeme kuzidi kile kiwango ambacho TANESCO inakielekeza.

Mheshimiwa Spika, TANESCO inauza unit moja kwa shilingi mia moja lakini wenzetu walikuwa wanauza unit moja hadi kufikia shilingi 3,500 na Serikali Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza mwaka jana kwamba gharama hizo zishuke kuja kwenye gharama ambazo ni za kawaida ili kuepusha kuwa na gharama ya double standard kwenye maeneo yale yale ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, tunavyofahamu ni kwamba maelekezo hayo yalitelekezwa kama alivyosema Mheshimiwa Mkundi lakini yale maeneo mbayo bado maelekezo hayo hajatekelezwa basi tunaomba taarifa hizo zifikishwe ili tuweze kuchukuwa hatua.

Mheshimiwa Spika, lakini pia wazabuni hawa ambao walikuwa wanatoa umeme huo tumekuwa tukizungumza nao na majadiliano yanaendelea na tutahakikisha kwamba wanaendelea kupeleka umeme wa uhakika kwa gharama nafuu na kuwafikia wateja wote muda wote ili adhima ya Serikali ya kufikisha umeme kwa ajili ya maendeleo ya viwanda kuwa salama yaweze kufikiwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu la Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua jitihada za Serikali kuboresha usafiri kati ya Rugezi kwenda Kisorya. Hata hivyo, kutokamilika kwa hili eneo la Lot III na hasa barabara ile ya kilometa 14 kutoka Rugezi – Nansio inaathiri sana uchumi wa wananchi wa Ukerewe, na ndiyo maana tarehe 04 Septemba, 2021 Hayati Dkt. John Magufuli akiwa Ukerewe, kwa kutambua changamoto hizi alitoa maelekezo eneo hili lifanyiwe kazi mara moja. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa Ukerewe alisisitiza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwanini sasa Wizara isione umuhimu wa jambo hili ikatenga pesa kwa haraka ikaufanya kama mradi wa haraka ili Lot III, hasa wakati wanasubiri pesa za kujenga daraja basi barabara km. 14 kati ya Rugezi kwenda Nansio iweze kukamilika kwa haraka?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi Mbunge wa ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Lakini Mheshimiwa Mbunge yeye pia atatambua kwamba Serikali inafanya jitihda kubwa sana kuhakikisha kwamba inatengeneza barabara na ndiyo maana imegawanywa kwenye Lot III. Lot ya pili imeshakamilika, lot ya kwanza mkandarasi yuko site na Serikali imeahidi kwamba inatafuta fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja tunaloliongelea urefu wake unafanana na daraja karibu lile linalojengwa la pale Surrender Bridge, ni takriban kilometa moja. Kwa hiyo Serikali lazima ihakikishe kwamba inajitahidi kupata fedha ya kutosha ili kuweza kujenga daraja hilo; na ndiyo maana tayari usanifu wa kina umeshafanyika. Tayari Serikali imeonesha jitihada za makusudi, kwamba kwanza ni ahadi ya Hayati Rais, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa hiyo Serikali kama nilivyosema kwenye jibu la msingi inaendelea kutafuta fedha na fedha ikipatikana nina uhakika kipande hiki cha Lot ya tatu kitajengwa. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa Kituo cha Afya cha Nakatunguru pale Ukerewe kilishakamilika kujengwa na kukamilika kwake kutasaidia sana kupunguza mzigo kwenye Hospitali yetu ya Wilaya; ni lini sasa Serikali itapeleka wataalam na vifaa tiba ili Kituo hiki cha Afya cha Nakatunguru kianze kufanya kazi na kusaidia kutoa huduma kwa wananchi wa Ukerewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Jimbo la Ukerewe, Wilaya ya Ukerewe, tayari kituo cha afya kimeshajengwa na kimekwishakamilika na hatua iliyobaki sasa ni kupeleka watumishi na vifaa tiba ili huduma za afya zianze kutolewa katika kituo kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe kwamba Serikali inatambua na tumeshaweka mipango kwanza kuhakikisha katika Halmashauri ya Ukerewe tunapata watumishi wachache kwa maana ya internal redistribution ya watumishi waliopo na vifaa tiba kwa uchache vilivyopo kwa ajili ya kuanza huduma.

Lakini pili, mpango uliopo katika mwaka wa fedha ujao ni kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba, lakini pia kadri tutakavyoajiri watumishi, tutawapangia katika Halmshauri ya Ukerewe na katika kituo kile cha afya ili kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tumelichukua, tunalifahamu na tunalifanyia kazi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe, inasaidia wananchi wanaoenda Kivuko cha Bugorora kwenda Ukara ambako kuna hospitali mpya sasa ya Wilaya ya Bwisya; barabara hii inasaidia wananchi wanaoenda Kakukuru ambapo ndiyo msingi wa uchumi wa Ukerewe, pia inasaidia wananchi wanaoenda Mliti mpaka Lubya kwenye msitu wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa hizi za matengenezo ya kawaida zinazotengwa zimekuwa hazisaidii sana kwa sababu inakuwa nzuri kwa muda mfupi, lakini inakuwa haipitiki kwa muda mrefu. Ni kwa nini sasa Serikali isianze kuifanyia Barabara hii upembuzi na hatimaye upembuzi yakinifu ili hatimaye sasa ianze kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo kimsingi siyo swali, ni ushauri; kwenye Kivuko cha Bugolola kwenda Ukara kumekuwa na shida ya kivuko kile na inaweza kusababisha ajali hata gari kutumbukia majini. Kinachohitajika ni kuweka Moorum au trip kadhaa za mawe ili kutengeneza gati lile ili wanananchi waweze kuvuka kwa usalama. Kwa hiyo, nitoe ushauri kwa Wizara, kwa haraka na kwa dharura, ifanyie kazi jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali lake la kwanza Mheshimiwa Mkundi ameomba barabara yake hii ifanyiwe upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe Mkundi kwamba tumepokea ombi, tutalifanyia kazi ili tufanye tathimini ya kina halafu tuweze kujua gharama ambayo inahitajika kuwekwa kiwango cha lami ili barabara iweze kutengenezwa na kupitika kwa wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili tumepokea ushauri ambao naomba nimwelekeze Mkurugenzi wa vivuko Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kwa kuwa amesema kuna hali hatarishi ya maisha katika eneo hili, afanye tathmini, aangalie hali halisi, halafu tuweze kuchukua hatua ya dharura ili kuweza kuokoa maisha ya watu wetu katika eneo hili. Ahsante.
MHE. MKUNDI M. JOSEPH: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pale Ukerewe tuna kiwanja kidogo cha ndege na kama kitaboreshwa kitasaidia sana kuchochea vivutio vya utalii na kuvitangaza vilivyopo Ukerewe, lakini na kuchochea uchumi wa Ukerewe na wananchi wa ukanda ule kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini mkakati wa Serikali kukiboresha kiwanja kidogo cha ndege kilichopo kwenye visiwa vya Ukerewe? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Ukerewe ni eneo la kisiwa na kwa sababu hiyo usafiri pekee ambao unatumika ni aidha, kutumia anga au kupita majini. Mheshimiwa Mbunge nampongeza kwa kuombea wananchi wake wameshapata kivuko inafanya kazi katika eneo lile na hili wazo tunaomba tulipokee.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni ya kuboresha viwanja vyetu vya ndege na hasa eneo kama Ukerewe ambalo kuna mambo ya kiutalii, wageni wanaweza wakatua pale, kuna shida ya kiusafiri, hili tunalipokea tunalifanyia kazi, tukipata fedha za kutosha Mheshimiwa Mbunge nakuhakikishia eneo lako litaboreshwa zaidi ya hapo lilipo ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru na nishukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ni kweli TAMISEMI walituma timu ikaja kufanya mapitio lakini tokea wakati ule tayari vile vigezo vyote viwili vilivyoonekana havijafikiwa kwa maana ya idadi ya kata ziko kata 12 na idadi ya watu ambacho ni kigezo namba mbili tayari mamlaka ile ina watu zaidi ya 200,000 ni zaidi ya kigezo ilichowekwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali langu sasa, je, Serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI, wako tayari sasa kuridhia kuifanya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nansio kuwa halmashauri ya mjini? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi kwamba kwa wakati huo wakati tadhimini inafanyika Nansio ilikuwa haijafikia vigezo vilivyokuwa vinahitajika, lakini kwa taarifa ya Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa tumeshafikia vigezo hivyo naomba tulichukue jambo hili kama Serikali tukalifanyie tathimini, lakini pia tukajiridhishe kama vigezo hivyo vimefikiwa ndipo tuweze kuona hatua zinazofuata kwa ajili ya kufanya maamuzi. Nakushukuru.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na Kisiwa kikubwa cha Ukerewe kuwa kwenye matatizo ya umeme kwa takribani wiki tatu sasa, wananchi kwenye Visiwa vidogo vya Ilugwa na Ukara wamekuwa wananunua umeme, lakini hawapelekewi token. Je, nini kauli ya Serikali juu ya changamoto hii? Nashukuru sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe. Kesi ya wananchi wa Ukerewe inafanana sana na maeneo mengi ya visiwa, ambapo wakandarasi binafsi ambao wanapeleka umeme kwa wananchi wanaozalisha, kwanza wanauza umeme kwa bei kubwa tofauti na maelekezo ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wameanza pia mchezo, wanapopeleka kwa bei ya Serikali hupeleka kwa kiwango kidogo. Naomba nitoe tamko mbele ya Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe na Waheshimiwa Wabunge, mara baada ya Bunge tutatembelea maeneo yote yenye kero ya namna hiyo na kutoa maelekezo kwa mameneja wetu kuwasimamia wakandarasi wa namna hiyo ili kupeleka umeme kwa bei elekekezi ya Serikali ya Sh.100 kwa unit na kuendelea kutoa umeme kwa wananchi kulingana na mikataba yao inavyowaelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitakwenda kwa Mheshimiwa Mkundi, Ukerewe. Pia nitatembelea Maisome na maeneo mengine ili kutoa maelekezo ya Serikali na namna ya kuyasimamia. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwanza kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini eneo la Bukiko ni kweli kupitia UCSAF, ulijengwa mnara wa Halotel lakini kuna shida kubwa; ule mnara unategemea umeme jua, kiasi kwamba nguvu ya umeme inapopungua kunakuwa hakuna mawasiliano, lakini vile vile kuna shida kubwa ya Internet kwa sababu mtandao ulioko pale ni wa 2G; Sasa naiomba Serikali niweze kujua, ni lini sasa Serikali itapeleka jenereta kwenye eneo lile? Vile vile iwasiliane na watu Halotel ili kuweka mtandao wa zaidi ya 2G kwa maana ya 3G na vyovyote itakavyowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwenye majibu, ni kweli kuna shida kubwa ya mawasiliano kwenye maeneo mengi, kwenye visiwa vya Ukerewe; na Serikali imejibu kwamba itaenda kupitia maeneo yote yenye shida: Ni lini sasa kazi hii itafanywa na Serikali ili timu iende kule, ifanye uchunguzi na hatimaye marekebisho yafanyike ili kuwe na mawasiliano mazuri kwenye eneo lile? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu jenereta; kwanza kabisa ile site ya mawasiliano iwe imekamilika, haijalishi kama ni umeme wa TANESCO au ni wa Solar, ni lazima site iwe na backup generator. Kwa vile Mheshimiwa Mbunge amelifikisha hili, basi Serikali inalipokea na tutalifanyia kazi ili kujiridhisha na changamoto ambayo ameiongea.

Mheshimiwa Spika, vilevile ni azma ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba, maeneo mengi nchini yanapata huduma ya internet, yaani kutoka katika huduma ya zamani ya 2G kwenda 3G. Hapo kabla Wizara tayari ilishatoa maelekezo kwa watoa huduma ili kuhakikisha kwamba, minara inayojengwa kuanzia sasa basi iwe na huduma ya 3G.

Mheshimiwa Spika, tuna minara ya aina mbili; minara ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali, lakini vilevile kuna minara ambayo inatokana na wawekezaji wenyewe. Ile ambayo inatokana na ruzuku ya Serikali tayari Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeshaanzisha mchakato wa ku-up grade minara yote ambayo itakuwa ina 2G kwenda kwenye 3G. Pia Serikali imeelekeza kwa watoa huduma wengine katika minara ambayo sio ya Serikali, ihakikishe kwamba, inaona umuhimu sasa wa kuelewa kwamba, sasa teknolojia ya 3G inahitajika kwa Watanzania wote. Ahsante.
MHE. MICHAEL J. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na sinto fahamu kubwa juu ya kiwango gani kitozwe kwa wananchi ili kuweza kuvutiwa umeme kwenye maeneo mbalimbali wakiwemo wananchi wa eneo la Nasio Wilaya Ukerewe. Nilitakakujua ni vigezo gani vinavyotumika kujua ni kiwango gani cha pesa kinatakiwa kulipwa na mwananchi ili aweze kuvutiwa umeme kwenye eneo lake la nyumba.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mkundi kwa swali lake nzuri Mbunge wa Ukerewe ambaye pia amekuwa akifuatilia sana mambo ya umeme katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka tulikuwa tume standardize gharama za upatikanaji wa umeme lakini baadaye tulimuomba Mheshimiwa Rais atukubalie tufanye marekebisho katika baadhi ya maeneo ili kuweza kufanya kazi hii kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumerudi kwenye vile viwango ambavyo tulikuwa tunavitumia hapo awali ambapo maeneo ya mijini yanapata umeme kwa gharama ambazo wenzetu wa EWURA ndiyo wa simamizi wa gharama wameziweka zinaanzia laki tatu na kuendelea. Lakini maeneo ya vijijini yanapata umeme kwa gharama ya shilingi elfu saba kwa line ya njia moja na gharama nyingine zile za kawaida kwa njia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango na vigezo ambavyo tunavitumia viko katika sheria ya mipango miji ile ndiyo inayosema hapa ni jiji hapa ni mji hapa ni Kijiji na hapa ni nini. Kwa hiyo, kwa kutumia sheria hiyo ambayo inatumiwa na wenzetu wa TAMISEMI na watu wa ardhi tunaitumia hiyo sasa ku-decide kwamba hapa itakuwa 27 hapa itakuwa zile gharama za mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajipanga kuendelea kutoa elimu kubwa Zaidi ili wananchi waweze kuelewa kwamba kiwango gani kinatozwa wapi na kwa sababu zipi kwa mfumo huo niliousema kwa hapo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru; Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina upungufu wa watumishi zaidi ya 1,700 wa kada ya ualimu. Kwa sababu za kijiografia watumishi wengi wamekuwa wakipangiwa wanaripoti baadaye wanaondoka.

Sasa Serikali haioni sababu za msingi na kwa sababu maalum kutoa kipaumbele kwa watu wenye taaluma ya ualimu, wazawa wa Ukerewe wakaajiriwa na wakapangiwa eneo la Ukerewe kuweza kuwasaidia watu wa jamii ile? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watumishi hasa wanaoajiriwa katika maeneo ya Halmashauri za vijijini kuomba uhamisho mapema mara baada ya kuajiriwa. Lakini mambo mawili yamefanyika Serikalini; la kwanza, katika ajira zilizopita tulihakikisha kila anayeomba ajira anaomba ajira kwa maana ya shule husika na Halmashauri husika. Tulikubaliana katika mikataba kwamba lazima wakae angalau miaka mitatu katika vituo vyao vile ambavyo wameajiriwa.

Kwa hiyo, suala hilo litakuwa endelevu tutahakikisha kwamba mtumishi yeyote anayeajiriwa, akishaajiriwa katika Halmashauri na shule hiyo lazima akae angalau miaka mitatu ili kuepusha wimbi la kuhama kwa maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala la kuwa na watumishi wazawa ni jambo jema na tumeendelea pia kuwapa kipaumbele. Lakini pia tunapenda utaifa kwa maana ya kwamba, waalimu wanaotoka Ukerewe waende maeneo mengine, lakini wanaotoka maeneo mengine waende pia Ukerewe ili kujenga utaifa wa nchi yetu, badala ya kuwa na watu wa aina moja katika eneo lile. Lakini tutaendelea kuhakikisha kwamba waalimu wanaopangiwa maeneo hayo, wanabaki na pia tunaendelea kudhibiti sana uhamisho katika maeneo hayo, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Wilaya ya Ki- TANESCO ya Ukerewe inapata umeme kutoka kwenye kituo cha kupoza umeme kilichoko Bunda, ambako ni umbali mrefu, hali inayosababisha kutokuwa na umeme wa uhakika. Na kwa kuwa Serikali ina mpango wa kujenga vituo kadhaa vya kupoza umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini sasa Serikali isiweke Ukerewe kama moja ya maeneo ambayo yatajengewa kituo cha kupoza umeme, ili kurahisisha umeme wa uhakika kwenye eneo la Ukerewe? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kulichukua jambo hili, ili wataalam waende wakachakate na kuona economic feasibility ya kuweka kituo pale Ukerewe na uwezo wa kukitumia katika mahitaji tuliyonayo, ili kuweza kuboresha huduma ya umeme katika eneo la Ukerewe.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Nitambue kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii, pamoja na kutambua mikakati hii ambayo itasaidia kutangaza na kuviendeleza lakini bado sisi tulioko kwenye maeneo yale ikiwa ni pamoja na wataalam wa halmashauri hawana uelewa wa mikakati hii.

Sasa Mheshimiwa Waziri yupo tayari baada ya Bunge hili kuja Ukerewe ili kwa pamoja sasa wao na sisi pamoja na wataalam wa halmashauri tuweze kushirikishana mikakati hii ili iweze kuwa na tija?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; moja kati ya vivutio vilivyoko Ukerewe ni pamoja na beach ya Rubya ambapo pia kuna msitu ulio chini ya TFS. Lakini kwa kuwa Ukerewe tuna upungufu wa madawati karibu 6,000; Mheshimiwa Waziri kupitia CSR, TFS wako tayari kutusaidia kuondoa upungufu huo wa madawati 6,000? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari kuambatana na Mbunge kwenda katika Kisiwa cha Ukerewe kuibua vivutio vilivyopo, lakini pia kuvitangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala hili la pili la kuhusu beach ya Rubya ni kweli tuna hifadhi ya Rubya ambayo ni hifadhi ya msitu unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na tumekuwa tukitoa CSR katika maeneo hayo na hivi karibuni tunakwenda kuzindua Kituo cha Polisi ambacho kimejengwa kutokana na hii Hifadhi ya Rubya. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo tunayahifadhi wananchi walioko kwenye maeneo hayo wanafaidika na rasilimali iliyoko pale. Kwa hiyo, suala la madawati tutakwenda kulishughulikia na tutakwenda kuzungumza na wananchi ili waone umuhimu wa kuendeleza hifadhi hiyo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nilitaka kujua, ni lini meli ya MV. Kaliasi itaanza tena safari zake kutoka Bandari ya Mwanza, Kwenda Bandari ya Nansio Visiwani Ukerewe? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna meli katika Ziwa Victoria ambayo ilipata shida katika mifumo yake ya kuongozea meli, na tulishaagiza kifaa hicho nje ya nchi; na ndani ya mwezi wa Kumi mwanzoni tunategemea kitakuja, kinaitwa mouse controller. Kwa hiyo, mwishoni mwa mwezi wa Kumi meli hii itaanza kufanya kazi zake ndani ya Ziwa Victoria. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bandari ya Nansio ina hali mbaya na inaweza kuleta matatizo muda wowote, Mheshimiwa Waziri uko tayari baada ya Bunge hili utembelee Jimbo la Ukerewe ili uone umuhimu wa kuharakisha matengenezo ya bandari ile ya Nansio? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari mara baada ya Bunge wiki ijayo tutembelee bandari hii ya Nansio na kujionea; na nitaambatana na wataalam ili washauri vizuri zaidi. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Miradi mingi ya maji ikiwemo ya Jimbo la Ukerewe inasuasua kukamilika kwa sababu ya mchakato mrefu wa kupata msamaha wa kodi. Nini mkakati wa Serikali kupunguza urasimu kwenye kupata misamaha ya kodi ili miradi hii ya maji iweze kukamilika haraka? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli na hivi sasa Serikali inaendelea na jitihada, Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kufanya utaratibu wa kuhakikisha kwamba misamaha yote ya kodi inayohusu sekta ya maji iweze kupitiwa na kupatikana suluhu mapema ili kuweza kuwanufaisha wananchi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nitumie fursa hii kutoa pole kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ukerewe, kwa msiba wa askari uliopatikana jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada hayo, nina maswali mawili ya nyongeza, la kwanza; kwa kuwa tathimini tayari imeshafanyika, lakini miundombinu iliyoko pale hasa mifumo ya maji safi na maji taka pamoja na mapaa ya kituo chenyewe na nyumba za watumishi ni mbovu sana, sasa Serikali haioni sababu kuchukua jambo hili kama la dharura na ikalifanyia kazi kwa haraka kadri inavyowezekana ili kujenga mazingira mazuri ya utendaji kwa watumishi wetu pale?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri haoni sababu, namwomba ikiwezekana twende naye pale ili aangalie mazingira kwa uhalisia tuweze kujadiliana tuone namna njema ya kuboresha mazingira ya utendaji kwa watumishi wetu wa Ukerewe? Nashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza alikuwa anaomba tuchukue jambo hili kama dharura; basi kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anakifahamu vizuri kituo hiki naomba nikubaliane naye kwamba tunalichukulia hili jambo kama la dharura. Kwa hiyo nitatoa maelekezo kufuatilia, kuona jinsi gani ambavyo tunaweza tukafanya ili yale mambo ya dharura tuweze kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu suala la mimi kwenda kwenye Jimbo lake, hilo halina tatizo, tutapanga ratiba baada ya Bunge hili kumalizika ili tuweze kwenda kutembelea jimbo lake kuona wenyewe jinsi ambavyo tunaweza kusaidiana kutatua changamoto za kidharura ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa Chuo cha VETA kinachojengwa pale Mhula Jimboni Ukerewe kipo kwenye hatua za mwisho kabisa za ukamilishaji, ni lini Chuo hiki kitaanza kutoa huduma? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali dogo la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilikuwa imeanza ujenzi wa vyuo 25 katika wilaya 25 pamoja vile vinne vya mikoa na ujenzi ule upo kwenye hatua za mwisho. Hivi sasa tuko katika ukamilishaji wa vifaa vya kufundishia pamoja na samani ambazo tutapeleka mle madarasani. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka ujao wa 2023 vyuo hivi 25 vya Wilaya na vile vinne vya mikoa vitaanza kutoa mafunzo rasmi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe ina tatizo kubwa sana la mashine ya X-Ray ni lini Serikali itapeleka mashine yakisasa ya X-Ray kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vifaa tiba zikiwemo X-Ray za kisasa ni moja ya vipaumbele ambavyo Serikali imeviweka na tunakwenda kwa awamu. Ninafahamu kwamba Hospitali ya Ukerewe ina X-Ray ya zamani ambayo imekuwa inaharabika mara kwa mara na Mheshimiwa Mbunge amekuwa mara kwa mara akikumbusha na kuomba Serikali iweze kupeleka X-Ray hiyo.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba tunaendelea kutafuta fedha na ni kipaumbele tukipata fedha tutahakikisha tunapeleka X-Ray katika kituo cha afya hicho.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Je, ni lini Serikali itajenga kilometa saba kwa kiwango cha lami za barabara kati ya Nasio-Mutunguru- Masonga ili kuondoa shida zilizopo kwenye barabara ile? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hiyo aliyoainisha Nansio Mutunguru yenye urefu wa kilomita saba ipo kwenye mpango mkubwa wa kujenga barabara ya lami. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango bado upo, utaanza tu pale ambapo fedha tutakuwa tumeipata na ujenzi huu tutaanza na kukamilisha hizo kilomita saba za lami katika Kisiwa cha Ukerewe.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kutoa mikopo ya zana za kisasa za uvuvi kama boti pamoja na pesa kwa ajili ya kufanya uvuvi wa kuvua samaki kwa njia ya vizimba kama njia ya kuzuia uvuvi haramu. Je, ni lini sasa mikopo hii itawafikia wavuvi wetu? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joeseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti katika kuondoa uduni na kero ya Wavuvi kutumia vyombo hafifu na kwa hivyo kupelekea kupatikana kwa vyombo vya kisasa sasa ni lini tunawapitia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari hatua za kimanunuzi zimekalika. Tunazo boti takribani 160 za kisasa zitakazogawiwa kwa wanufaika Wavuvi waliotimiza viwango ambavyo viliwekwa na Serikali na miongoni mwa Wavuvi hao wapo wa kule Ukerewe. Boti hizo zitakuwa ni za kisasa zenye fish finder, kwa maana kifaa maalumu kinachoelekeza wapi samaki alipo lakini pia vilevile kitakuwa nae neo la kuhifadhia samaki lisilopungua tani moja, kitakuwa na GPS na vifaa vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa pesa takribani bilioni 20 kwa ajili ya zoezi la ufugaji wa samaki kuongeza uzalishaji wa samaki aina ya sato. Walengwa ni pamoja na vikundi vya vijana na akinamama.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa hatua kubwa iliyofikiwa ya ujenzi wa chuo hiki cha VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dhamira ya Serikali kujenga vyuo vya VETA ni kusaidia vijana wetu kupata taaluma itakayowasaidia kujiajiri au kuajiriwa kulingana na mazingira yao, nataka kujua, ni kozi zipi au aina ipi ya mafunzo itakayotolewa kwenye chuo hiki cha VETA ukerewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza kwenye majibu ya msingi kwamba mafunzo tutaanza mwezi wa Nne na tutaanza kwa kozi fupi; na tuliwaelekeza Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, katika Mabaraza yetu ya Madiwani waweze kuamua au ku-detect na aina ya kozi ambazo tunatarajia kuanza nazo; ziko zile kozi za jumla ambazo tunatarajia kuanza nazo kama za ufundi umeme wa majumbani, uchomeleaji na ufundi wa mabomba; hizo ni kozi muhimu ambazo tunatarajia kuanza nazo katika kipindi hicho kifupi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Je, ni kwa nini Serikali isipeleke pesa za miradi hii ya TARURA kwa meneja wa wilaya badala ya mkoa ambako mara nyingi zimekuwa zinasababisha urasimu kwenye utekelezaji wa miradi hii ya barabara zilizo chini ya TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba fedha za matengenezo ya barabara zimekuwa zikipelekwa katika ngazi ya mikoa na siyo ngazi ya Mameneja wa Wilaya na sababu ya msingi ilikuwa muundo wa TARURA uliweka watendaji wengi zaidi kwenye ngazi ya mkoa kwa maana ya wataalam; Wahasibu, wataalam wa manunuzi na wengine. Kwa hiyo ilikuwa ni vyema sana kupeleka fedha kwenye ngazi ya mkoa ambayo ina watendaji wengi kuliko halmashauri. Utaratibu huu tunaendelea kuutekeleza, lakini pale tutakapoona tuna sababu ya kupitia upya tutafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Daraja la Mto Nabili linalounganisha Kata ya Bukindo, Kata Nkilinzia ni muhimu sana kwa mawasiliano ya wananchi wa maeneo haya.

Ni lini Serikali itatupatia pesa kujenga daraja hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimwondoe tu hofu kwamba tumepokea hiki kilio chake na tutakifanyia kazi, kwanza tutawatuma watu wetu wakafanye tathmini na kuona fedha kiasi gani zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina upungufu wa watumishi kada ya ualimu zaidi ya 1,700 ambayo ni karibu asilimia 40 na watumishi karibu 170 ambao ni karibu asilimia 56 kwenye kada ya afya. Je, Serikali iko tayari sasa kwenye ajira zinazokuja hivi karibuni kutoa kipaumbele kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathimini kuona maeneo yenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi wa elimu, afya na watumishi wa kada nyingine ikiwemo Ukerewe na maeneo haya ndiyo yatakayopewa kipaumbele cha juu zaidi kuliko yale maeneo ambayo yana watumishi wa kutosha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tutatoa kipaumbele Ukerewe, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Serikali iliwekeza zaidi ya milioni 700 kwenye Bonde la Miogwezi lililoko kwenye Kijiji cha Igongo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, lakini mradi ule umesimama.

Je, Mheshimiwa Waziri huu nao ni kati ya miradi itakayotekelezwa kwenye mwaka wa fedha 2022/ 2023?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi linaloendelea hivi sasa ambapo ni maelekezo wamepewa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika kuhakikisha kwamba miradi yote hii inafanya kazi. Tumewapa jukumu la kupitia miradi yote nchi nzima kujua status yake, tuone ipi inafanya kazi, ipi inahitaji marekebisho na ipi inahitaji over whole, kwa maana ya kuanza upya katika mradi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba katika bajeti yetu ambayo tutaisoma wiki inayokuja tutaainisha miradi ambayo itatekelezwa na imani ni kwamba katika mradi aliosema tutaingiza katika utaratibu wa utekelezaji katika bajeti inayokuja.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mhesimiwa Spika, nashukuru, ni, lini Serikali itakamilisha usambazaji umeme kwenye visiwa vidogo vilivyoko nje ya Gridi ya Taifa Jimboni Ukerewe? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa ya Mheshimiwa Joseph Mkundi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumeshatangaza zabuni tayari kwa ajili ya wapelekaji wa umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na Gridi na kinachofanyika sasa ni mchakato wa kubaini bei na uhalisia wa huduma yao ili tuweze kufikisha umeme katika maeneo ambayo Gridi ya Taifa haijafika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi yanayohusu huduma mbalimbali za wazee ikiwemo tiba na mengineyo. Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuleta Sera ya Wazee Bungeni ili kwa ujumla wake tuangalie mapungufu na yale ambayo yanaweza kufanyika kuweza kujenga mazingira mazuri ya wazee wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze kwa swali zuri ambalo limeendana kabisa na mpango wa Serikali ambao tunaufanya hivi sasa. Katika vituo hivyo vya wazee, na katika utaratibu uleule wa kuangalia makundi ambayo yanahitaji msaada zaidi, hasa katika masuala ya chakula, malazi, mavazi, matibabu na welfare yao kwa ujumla, tayari Sera ya Wazee ipo na iko katika hatua za kwenda kufanyiwa marekebisho ili kuweza kuhakikisha tunawasaidia wazee hawa, ikiwa ni pamoja na kuunda mabaraza ya wazee katika ngazi za halmashauri huko mpaka ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji ambayo tayari imekwisha kuanza kufanya kazi na zinafadhiliwa na halmashauri zetu kote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nishukuru kwa majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa kituo cha Bukimwi kinachopokea abiria kutoka Kayenze nacho vile vile hakina Banda kwa ajili ya abiria kusubiri usafiri. Je, ni sehemu ya vituo vitakavyofanyiwa ujenzi kama ilivyo Bugorola, Kisorya na Ukara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Kivuko cha kutoka Kitale kwenda Ilugwa na kingine kutoka Kakukuru kwenda Ghana ni vivuko vilivyoko kwenye maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2020 - 2025. Je, Serikali ina mpango gani kuanza ujenzi wa vivuko hivi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi kwenye eneo hilo? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwa awamu. Nikiri hivi vivuko alivyovisema viko kwenye ilani, lakini katika Ziwa Victoria tunajenga vivuko vipya vinne na katika Vituo vya Bukimwi – Kayenze vituo hivi kwa sasa haviko kwenye mpango wa kuvijenga kwa mwaka huu wa fedha labda kwa mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vituo alivyovitaja vya Kitale – Ilugwa, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu na tuna uhakika kadri idadi ya watu inavyoongezeka kuna haja kubwa sana ya kuongeza vituo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa visiwa hivi kwamba Serikali inafahamu na tunalifanyia kazi kutafuta fedha kuhakikisha kwamba tunakuwa na mawasiliano katika vile vivuko alivyovitaja vya Kitale, Ilugwa hadi Ghana, ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa sababu tatizo hili limekuwa kubwa karibu katika Wilaya zote nchini, kuna mlundikano wa kesi nyingi, lakini Wenyeviti hao wa Mabaraza ni wachache sana. Kwa nini Serikali isiwe na mkakati maalum kuhakikisha kwamba mabaraza yote ya ardhi katika Wilaya zetu yanapata Wenyeviti hawa? Swali la pili, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina mlundikano mkubwa wa kesi, ina migogoro mingi inayohusu ardhi: Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi atakayekaa pale kwa ajili ya kuondoa migogoro na kutatua kesi zilizopo zinazohusu masuala ya ardhi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia jibu la msingi ambalo nimelitoa, ni kwamba sasa hivi tunaendelea na michakato kama nilivyoeleza, ya kuziba pengo la Wenyeviti 57 ambao utaratibu wake ukikamilika, tutakuwa tumekamilisha Wilaya zote hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ukerewe, kutokana na mlundikano wa kesi, hili tutaliangalia kwa umuhimu wake na tutalifanyia kazi, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa ni zaidi ya miezi mitano sasa tokea Serikali imepeleka x-ray machines kwa kwenye Vituo vya Afya vya Muriti, Bwisya na Hospitali ya Wilaya ya Nansio, lakini mpaka sasa vifaa hivi havijaanza kutoa huduma kwa wananchi; nini kauli ya Serikali? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada za Serikali zimekuwa ni kubwa sana kupeleka vifaa tiba maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Muriti na Bwisya kule Ukerewe. Nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuagiza timu yetu ambayo inazunguka mikoani kutoa mafunzo kwa wataalam wetu kutumia vifaa hivi vya kisasa, wahakakikishe wanafika Ukerewe mara moja na kutoa mafunzo kwa watumishi hawa wa Muriti na kule Bwisya.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa taratibu kama hizo kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri zipo, lakini utekelezaji wake wakati mwingine unaleta changamoto;

Je, ni kwa nini Serikali sasa isifuatilie kujua hatma ya yale mazungumzo yanakuwaje ili mwisho wa siku wananchi wapate huduma wanazozitarajia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili. Kituo cha Afya cha Nakatunguru Jimboni Ukerewe ni muhimu sana, kinahudumia watu zaidi ya 10,000 kwenye Mji wa Nansio pale lakini kina upungufu mkubwa wa miundombinu;

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa miundombinu kwenye kituo kile cha afya cha Nakatunguru ili kiweze kutoa huduma zinazostahili kwa wananchi wa ukerewe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika majibu yangu ya msingi kwamba utaratibu upo wa kamati hizi za kitaalamu za kushauri katika ngazi ya mkoa. Kuna timu ya mkoa, kuna timu ya halmashauri na mashirika ya kidini ambayo yanamiliki hospitali hizi. Kwa hiyo nipende kuchukua nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kuwataka waganga wote wakuu wa mikoa hapa Tanzania kuhakikisha wanakaa vikao hivi ambavyo vipo kisheria na wenzetu wamiliki wa hospitali hizi ambao ni taasisi za kidini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kweenye swali lake la pili la kituo cha Nakatunguru kule Nansio Ukerewe, kwamba ni lini Serikali itapeleka fedha kumalizia. Serikali itapeleka fedha kumalizia kituo hiki kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ni lini Serikali itapeleka majokofu kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti kwenye vituo vya afya vya Muriti na Bwisya Jimboni Ukerewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya majokofu haya katika vituo vya afya kule Ukerewe alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge kadri ya upatikanaji wa fedha na tutaangalia katika bajeti hii tunayoenda kuitekeleza ya 2023/2024, kama imetengwa fedha tutahakikisha inafika mara moja kwa ajili ya kupunguza changamoto hii iliyopo katika Wilaya ya Ukerewe.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, wakati wa hotuba ya Bajeti Kuu mwaka 2023/2024, Bunge hili lilipitisha Tozo ya shilingi 100 kwa kila kilo moja ya samaki wakavu aina ya dagaa wanaosafirishwa kuingia nchini au Kwenda nje ya nchi. Jambo hili limetafsiriwa vibaya Jimboni Ukerewe, jambo ambalo limefanya watumishi wanatoza wananchi shilingi 100 kwa samaki wanaosafirishwa ndani ya Wilaya jambo ambalo limeleta taharuki kubwa Jimboni Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kupata kauli ya Serikali juu ya jambo hili ili kujenga amani kwa wananchi wa Jimbo la Ukerewe. Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze, jambo hili amekuwa akilifuatilia sana kwenye Wizara ili kuhakikisha wavuvi waliopo katika ukanda huo wa Ziwa Victoria na pale Ukerewe wananufaika zaidi na biashara wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha marekebisha ya tozo, awali tozo ilikuwa kuanzia kilo 0 - 500 ilikuwa haitozwi chochote, lakini kilogramu kuanzia 501 na kuendelea ilikuwa inatozwa shilingi 100. Kwa kuzingatia kwamba ile ni biashara ya ndani na nje (import and export business) haiwezi kuwa na masharti sawa na ufanyaji wa biashara ndani ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ni kosa la kitafsiri la kanuni na sheria, hivyo natumia fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi kumwagiza Katibu Mkuu awasiliane na Mheshimiwa Mbunge ili kwenda kurekebisha changamoto hiyo inayowapata wavuvi wa hapo Ukerewe, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru na nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa miradi mingi inayotekelezwa na TARURA, kumekuwa na changamoto ya ubora wa wakandarasi wanaotekeleza miradi hii.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha katika miradi hii, pamoja na Serikali kutenga pesa nyingi lakini wakandarasi wanaopatikana wawe na ubora wa kuhakikisha barabara zile zinakuwa vizuri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwenye Jimbo la Ukerewe barabara inayounganisha Kata ya Nkilinzya na Kata ya Bukindo kuna daraja pale linaleta shida kubwa sana. Je, ni lini Serikali itatusaidia kupata pesa za kujenga daraja linalounganisha Kata ya Bukindo na Kata ya Nkilizya? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kusisitiza kwa Mameneja wote wa TARURA wa Mikoa na Wilaya, kwamba Serikali ilikwishatoa maelekezo kwamba kila tunapotekeleza miradi ya Barabara, kwanza lazima tupate wakandarasi wenye sifa na uwezo wa kujenga barabara kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha, lakini kukamilisha kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, pili, tulishaelekeza kuchukua hatua kwa wakati kwa wakandarasi ambao wataonesha kutokuwa na uwezo mzuri wa kujenga barabara hizo. Pia, kuhakikisha kwamba ikiwezekana tunavunja mikataba hiyo kwa kufuata taratibu za kisheria na kupata wakandarasi ambao wana sifa hiyo. Kwa hiyo, naomba nisisitize kwenye eneo hili, kwamba ni wajibu wa Mameneja wa Mikoa, pia wa Wilaya lakini na halmashauri zetu na Mabaraza ya Madiwani kuhakikisha kwamba wanajiridhisha na ubora wa barabara kabla mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na daraja linalounganisha Kata ya Bukindo na Nkilizya ambalo liko katika halmashauri ya Ukerewe, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunahitaji kufanya tathmini na hivyo meneja wa TARURA Wilaya afanye tathmini, watuletee gharama. Tutaona kama Serikali Kuu inahitaji kutoa fedha ama mapato ya ndani yanaweza kujenga daraja hilo, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Natumia nafasi hii kuipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa jitihada zinazofanywa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Napongeza Wizara kwa kutumia TTB na kuratibu ziara ya waandishi wa habari kwa ajili ya kubaini vivutio hivi. Hata hivyo, huwezi kutenganisha utalii na rika mbalimbali kwenye eneo husika kwa maana ya watu wazima, wazee, rika la kati na watoto katika kubaini na kuendeleza utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziara hii imefanikiwa, lakini bahati mbaya sana kuna rika la watu wazima, kuna kikundi cha KUMIDEU na vinginevyo ambavyo vinafahamu zaidi utamaduni, mila na desturi za watu wa Ukerewe, walitakiwa kuhusishwa. Nini sasa mkakati wa Serikali ili wakati mwingine vikundi kama hivi vishirikishwe ili kupata uhalisia wa vivutio vya utalii vilivyopo pale Ukerewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali, lakini tunakosa kiungo kinachoweza kuratibu mambo haya ya utalii. Halmashauri zetu zingeweza kutoa msaada mkubwa sana, lakini bahati mbaya sana hazina watu specific wanaoshughulika na utalii zaidi ya utamaduni. Je, ni nini mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha Halmashauri zetu zote zinakuwa ama na idara au na vitengo vinavyohusika na utalii ili kuweza kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais katika kukuza Sekta ya Utalii? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ulimwenguni kote, custodian wa mila na desturi ni Machifu wakienda sambamba na wazee wa mila na desturi. Kwa bahati mbaya kwenye halmashauri zetu kumekuwa na upungufu wa kubaini makundi haya ya wazee wa mila na desturi. Natoa rai kwa halmashauri zetu, ziwe na mikakati ya kuwatambua wazee wa mila na desturi ambao ndio custodian wa tamaduni zetu ili tunapofanya jukumu la kutambua na kutangaza vivutio vilivyopo kwenye maeneo yetu, basi wazee hawa waweze kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa halmashauri zetu, zijielekeze kwenye kutambua maeneo yote yenye sifa za kiutalii, wawasiliane na Wizara ili maeneo haya yaweze kusajiliwa tuweze kuweka mpango mkakati wa pamoja wa kutangaza maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili la uhaba au kukosekana kwa kiungo, kwa kukosekana wataalam kwenye halmashauri zetu. Mamlaka ya ajira ya watumishi kwenye ngazi ya halmashauri, ni Wizara ya TAMISEMI. Naomba sana halmashauri zetu zijielekeze kwenda kuomba vibali vya ajira kwa TAMISEMI ili jambo hili liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa kutambua gap lililopo, Wizara ya Maliasili inao wataalam kwenye kanda zetu. Kwa mfano, kwenye Kanda ya Ziwa Victoria, tunao wataalam wetu wawili walioko Mwanza, Kanda ya Kusini, tunao wataalam watatu wapo Iringa, Kanda ya Kaskazini, tunao wataalam sita wapo Arusha, Kanda ya Pwani, tunao sita wapo Dar es Salam lakini vilevile hapa Makao Makuu tunao wataalam. Tunaomba halmashauri zetu ziwatumie wataalam hawa wakati wakijiandaa kupata vibali vya ajira kutoka TAMISEMI.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, pamoja na jitihada kubwa za Serikali kuboresha miundombinu na kutoa vifaa, nini mpango wa Serikali sasa kutoa posho ya kufundishia (teaching allowance) kwa Walimu wote nchini ili kuongeza morali ya kazi?

Swali la pili, nini mkakati wa Serikali sasa kutoa posho ya mazingira magumu kwa watumishi hasa Walimu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu kijiografia kama ilivyo Ukerewe na Mafia? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu hii posho (teaching allowance) Serikali itaendelea kuangalia suala hili na kadri ya uwezo wake wa kibajeti tutaendelea kuliona ni namna gani tunaweza tukalitekeleza. Vilevile kuna Halmashauri ambazo Wakurugenzi wao wenyewe kupitia mapato yao ya ndani wamekuwa wakitoa motisha kwa Walimu hasa wale ambao wanaenda kuripoti kwa kuwapa magodoro na vifaa vingine vya kwenda kuanzia maisha.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la posho ya mazingira magumu. Hili tunalipokea kama Serikali na tutaendelea kulifanyia analysis na kuona ni namna gani tunaweza tukapata fedha ya kuweza kulitekeleza hili lakini kwa sasa bado tutaendelea katika mazingira yote kuwa-treat watumishi wetu sawa na haki sawa katika maeneo yote.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nitumie nafasi hii kwanza kutoa pongezi na shukurani kwa Wizara pamoja na Serikali kwa ujumla kwa hatua mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha Visiwa vya Ukerewe vinapata maji safi na salama. Swali langu, Serikali sasa iko tayari kutoa maelekezo ili wakati wa usambazaji wa maji wataalam wazingatie mtawanyo kuhakikisha kwamba kila kitongoji kinafikishiwa mtandao huu wa maji? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Mkundi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza napokea shukrani zako na wewe nakupongeza kwa sababu umekuwa mfuatiliaji na tumekwenda Ukerewe zaidi ya mara mbili mimi na wewe na kazi nzuri unaifanya.

Mheshimiwa Spika, suala la usambazaji maji kwa kila kitongoji, hiyo ni moja ya mipango ya Wizara. Nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo tumeweza kutatua changamoto ambayo ilikutesa kwa muda mrefu, suala la usambazaji maji pia tunakuja kulifanyia kazi na nitoe wito kwa Mameneja wote wa Wilaya ambao wananisikiliza waweze kuhakikisha wanafika katika vitongoji vyote na maji yanasambazwa kadri ya miradi ilivyosanifiwa. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kuwa suala la magugu maji limekuwa ni tatizo kubwa, ni kwa nini Serikali isifanye utafiti kuona kama kuna eneo ambalo magugu maji haya yanayotumika kama raw material ili yaweze kuvunwa kirahisi zaidi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelishauri ni jambo jema na kwa sababu tumegundua kwamba hata nchi jirani wameshaanza hivyo na ndio maana unakuta changamoto ya kuenea kwa magugu maji inakuwa kubwa sababu sisi tukiyatoa, kwa wenzetu yanakuwepo na kwa sababu Ziwa ni moja yanarudi.

Mheshimiwa Spika, wenzetu Uganda wameshaanza kulifanyia hilo, wanatengeneza mikeka na mambo mengine na sisi tumo kwenye kufanya utafiti, nini ambacho tunaweza tukatengeneza. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutahakikisha na sisi tunatumia magugu maji kama raw material kwa ajili ya kuinua vipato vya wananchi, nakushukuru.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Serikali inajenga hospitali pale Ukerewe ambayo ikikamilika itakuwa na hadhi ya Mkoa na ikikamilika itakuwa inahudumia cases kubwa za rufaa. Sasa nataka kuiuliza Serikali haioni umuhimu sasa kuimarisha kituo cha afya cha Nakatungulu ambacho kitasaidia kuhudumia wagonjwa magonjwa ya kawaida na kikikamilika kitahudumia Kata zaidi ya Sita kwenye eneo la Mjini pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumekuwa tukiboresha vituo vya afya ambavyo vimekuwa na idadi kubwa ya watu na zile ambazo zinahudumia Kata nyingi ikiwemo katika hii Kata ya Nakatundu ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Kwa hiyo, bado iko katika mipango yetu na sisi tutaendelea kuziboresha kuhakikisha tunapeleka huduma za afya karibu na watu.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa pesa nyingi kwa ajili ya miradi ya barabara hizi zinazosimamiwa na TARURA, bado miradi mingi kwenye maeneo imesimama au inasuasua ikiwemo Jimbo la Ukerewe kwa sababu wakandarasi ama kutokuwa na uwezo au kuwa na mrundikano wa kazi nyingi.

Nini kauli ya Serikali juu ya hali hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali katika maeneo yote ambayo wakandarasi hawafanyi vizuri ni kuhakikisha kwamba wanamaliza ndani ya muda kwa sababu tumetoa muda kamili wa kufanya ile kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kama kuna maeneo ambayo wakandarasi wamekuwa hawatekelezi kabisa wajibu wake tunaomba maeneo hayo mtuletee sisi ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia TARURA, ili tuweze kuchukua hatua zikiwemo kuvunja mikataba kwa sababu wanachelewesha hizo kazi. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru; mradi wa maji wa Nansio Jimboni Ukerewe ulishakamilika na kuanza kutoa huduma, lakini bado maji hayajaweza kuwafikia wananchi wote zinahitajika bomba takribani kilometa kama 67 ili kuweza ku-cover eneo lote na maji yawafikie wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari sasa kusaidia mamlaka hii ya maji bomba hizi ili huduma ya maji iweze kuwafikia wananchi wote kwenye Mji wa Nansio? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema mradi umekamilika tunahitaji kuona maji bombani, hivyo kama tumeshakamilisha mradi wa fedha nyingi hili suala la usambaji wa mabomba kuwafikia wananchi ndiyo jukumu letu kubwa. Hivyo nipende kukutoa hofu Mheshimiwa Mbunge tutafika na tutafanya kwa pamoja na wananchi wanakwenda kunufaika na maji bombani.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kutokana na matatizo mbalimbali wanayopata wananchi wanaotumia umeme nje ya Gridi ya Taifa, mwezi wa Pili mwaka huu Wizara iliunda timu ya wataalam ikiongozwa na Mheshimiwa Naibu Waziri kuzungukia maeneo haya kusikiliza wananchi na baadaye kutoa uelekeo nini utatuzi wa changamoto zile, lakini tokea wakati huo mpaka sasa Wizara imekuwa kimya. Wananchi, wakiwemo wananchi wa Jimbo la Ukerewe Visiwa vya Gana na Ukara wanataka kusikia nini maelekezo na uelekeo wa Serikali juu ya changamoto hizi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mimi mwenyewe nilifika Nansio, Ukerewe; nilifika Ukara, Gana, Kamasi, Irugwa katika visiwa vyote vya Ukerewe ili kuangalia changamoto ambayo wananchi wanaipata. Maeneo haya yapo mengi zaidi. Yalikuwepo mengine katika Mkoa wa Kagera na mengine katika maeneo ya Buchosa. Zoezi lile linaendelea na tunatarajia litakamilika mwishoni mwa mwezi huu. Litakapokuwa limekamilika, taarifa ya Serikali na maelekezo ya Serikali yatatolewa kwa maeneo yote ambayo yalikuwa na changamoto ya bei ya umeme na wananchi wataendelea kupata umeme kwa gharama ambazo ni nafuu ili Serikali iweze kuwahudumia vizuri.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, wananchi wanaoishi Visiwa vidogo vidogo Jimboni Ukerewe wanalazimika kusafiri kwenda Makao Makuu ya Wilaya kufuatilia vitambulisho vya NIDA jambo linalopelekea usumbufu na gharama kubwa.

Nini mkakati wa Serikali kuwapelekea huduma lakini wakati huo huo ikiwaondolewa usumbufu wa wananchi hao? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuwapunguzia usumbufu hawa wananchi wanaokaa mbali na makao makuu wakiwepo hawa wa visiwani, vitambulisho hivi vimepelekwa mpaka ngazi ya Kata ili maofisa wetu kwenye ngazi ile aweze kuwagawia wananchi wao, nadhani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza usumbufu wa wananchi. Naomba niwaelekeze wenzetu wa Ukerewe kama lipo tatizo la kuwataka wananchi wote wasafiri kwenda Nansio warekebishe ili vitambulisho hivi wavipate kwenye Makao Makuu ya Kata zao. Nashukuru.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Baadhi ya vijiji kwenye Jimbo la Ukerewe umeme umesogezwa mpaka kwenye transfoma lakini kwa zaidi ya mwaka mmoja umeme huu haujaweza kusambazwa kwenye makazi ya wananchi.

Nataka kujua mpango wa Serikali kuweza kusambaza umeme huu kwenye makazi ya watu. Nashukuru.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwa na changamoto hiyo ya kufikisha umeme katika maeneo ambayo watu wanaishi katika Jimbo la Ukerewe na napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zimepangwa, manunuzi yamefanyika ya vifaa vya kuweza kusogeza umeme katika makazi ya watu. Katika mwaka ujao wa fedha tutaongeza kasi ya kuwaunganishia umeme wananchi wa Jimbo la Ukerewe na kote nchini.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa bado uhamasishaji unaendelea, lakini wavuvi wetu wengi hawa wadogo wanakosa elimu na zana kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao, lakini vilevile wanakosa taarifa za kutosha za masoko yanayoweza ku-determine bei ya bidhaa zao wanazozalisha. (Makofi)

Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanasaidia jamii hii hasa kwenye eneo la Ukerewe ili wavuvi wetu waweze kunufaika na shughuli zao za uvuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuzingatia mazingira ya Ukerewe kama eneo maalum la uvuvi; nini sasa mkakati wa kujenga mwalo kwenye eneo la Kakukuru kwenye Wilaya yetu ya Ukerewe? Nashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili kwa pamoja ya Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango mkakati wa namna ya kuwasaidia wavuvi wetu hapa nchini ili kuwasaidia wawe na zana bora, lakini pia waweze kuongeza uzalishaji wa mazao ya samaki hapa nchini. Mojawapo ya mkakati ni kwenye bajeti ya mwaka ujao tuna mpango wa kununua boti 320 kwa nchi nzima ili tuweze kuzikopesha kwa wavuvi wadogo wadogo na wavuvi wa kati waweze kuwa na uwezo wa kuvua katika maji marefu upande wa bahari, lakini pia upande wa maziwa yetu. Lakini pia tuna mpango wa kuboresha mialo yetu yote na kuijenga katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha masoko madogo madogo ya wavuvi wetu kwa kujenga vichanja ili mazao yale yanayotolewa baharini au ziwani yaweze kupata mahali pa kuanikwa vizuri, lakini yaweze kuwa bora na kuweza kupata bei iliyo nzuri kwenye soko letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili, Serikali imepanga kukarabati mwalo wa Kakukuru kwenye Wilaya ya Ukerewe ili kwamba mwalo ule uwe bora, ili kwamba wavuvi wa Wilaya ya Ukerewe wapate mahali ambapo wanaweza wakashusha mavuvi yao vizuri na kwa urahisi zaidi. (Makofi)