Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jesca David Kishoa (5 total)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kutoka Benki Kuu inaonesha kwamba kuanzia mwaka 2006 mpaka 2015 takribani miaka kumi kila mwaka nchi imekuwa ikitumia gharama ya takribani wastani wa dola milioni 900 ambayo ni sawa sawa na shilingi trilioni mbili katika fedha hizi zinatumika kwa ajili ya kununulia bidhaa kutoka nje. Katika fedha hizi, fedha dola milioni 120…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca uliza swali.
MHE. JESCA D. KISHOA: Nauliza swali Mheshimiwa Mwenyekiti, dola milioni 120 zinatumika kununulia mafuta ambayo ni sawa na takribani shilingi bilioni 250.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali iliyoko madarakani itawakumbuka wananchi wa Singida ambao wamepuuzwa wametelekezwa, lakini wamesahaulika hata katika hili la mafuta? Ninaomba Waziri aje anipe majibu.
MHE. JESCA D. KISHOA: Ni lini bodi itaundwa kwa ajili ya mafuta?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue umuhimu wa maswali haya kwa logic, kwa maana ya kwamba Wizara na Serikali, tukishirikiana na Wizara ya Viwanda, tumedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunajitegemea kwenye sekta hii ya mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Mheshimiwa Mwijage, ameshazindua mkakati ambao utatuondoa katika tatizo hilo. Mheshimiwa Jesca mdogo wangu ambaye tuligombea naye Jimbo moja, wananchi wa Mkoa wa Singida hawajapuuzwa, isipokuwa tunalotaka kufanya kama Serikali na Wabunge wote wanaotokea mikoa hii tuwahamasishe na sisi tulisema kwenye hotuba yetu kila familia iwe angalau na ekari moja ya alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kigoma na Mheshimiwa Jesca amewagusa watu wake wote, kaanzia Singida kwa wazazi wake halafu kaenda swali la michikichi kwa wakwe zake alipoolewa kule na Mheshimiwa Kafulila. Tuwahamasishe, hamasa hii ambayo inatoka kwenye alizeti ambayo Mheshimiwa Allan Kiula, Mheshimiwa Kingu na Mheshimiwa Mlata na Aisharose wanafanya pamoja na akina Mheshimiwa Nkamia na Mheshimiwa Ashatu, tuhamasishe walime alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kule Kigoma, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyojibu ya michikichi 137 kwa kila ekari tuwahamasishe walime, baada ya hapo hatua zitakazofuata za Serikali zitakuwa zile za kisera za kuhakikisha kwamba tuna-discourage mafuta kutoka nje na yatumike yale yanayotoka ndani. Tukianza kwanza kwa ku-discourage mafuta ya nje kabla hatujahamasisha watu kulima kitakachofuata bei zitapanda na watu watakosa hiyo bidhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linalohusu bodi na lenyewe sasa hivi alizeti itakuwepo kwenye Bodi ya Mazao Mchanganyiko kwa sababu uzalishaji wake haujawa mkubwa, wananchi hawa tusije tukawawekea mzigo ambao wamekuwa wakibeba wengine kwa ajili ya kuhudumia bodi hizi ile hali wao hawajajitosheleza na kuvutiwa zaidi kwa ajili ya zao hilo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa mujibu wa jarida la The Citizen la tarehe 23, Oktoba mwaka huu, 2016, imeonyesha kwamba miongoni mwa mikopo iliyokopwa kutoka China mwaka 2015 ni pamoja na Dola za Kimarekani milioni 132 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 300 za Kitanzania kwa ajili ya mradi wa umeme wa upepo Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iwaeleze wananchi wa Singida fedha hizi zimekwenda wapi? Kwa sababu mpaka hivi sasa hakuna kinachoendelea, hakuna hata nguzo moja halafu tunaambiwa bado majadiliano yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa sababu mazingira kama haya ambapo mikopo inaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini fedha zinaelekezwa maeneo yasiyohusika. Ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa kumwagiza CAG akague mikopo inayoagizwa katika nchi hii? Kwa sababu katika deni la Taifa, inawezekana kuna ujanja ujanja unafanyika kwenye suala zima la mikopo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mradi wa upepo wa Singida ambao unazalisha Megawatt 100 hautokani na fedha za mkopo, ni wawekezaji binafsi, niweke wazi. Kadhalika, kuhusiana na masharti ya mikopo, ni Makampuni yenyewe yanakopa na kuja kuwekeza kwa ajili ya kufanya biashara na TANESCO inanunua umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la CAG, ni taratibu za Kiserikali. CAG ana utaratibu wa kukagua na Mashirika na ofisi za Serikali zina utaratibu wa kuwasilisha taarifa za kukaguliwa. Tutaendelea kupeleka taarifa kwa mujibu wa CAG ili hesabu zote zikaguliwe. Kwa hiyo, hakuna suala la kuficha kwenye ukaguzi; CAG ana ratiba ya kukagua na Serikali tuna wajibu wa kupeleka takwimu ili zikaguliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kupeleka takwimu zikaguliwe.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa ya uhaba wa maji katika Mji wa Singida, lakini pia kuna changamoto kubwa ya miundombinu mibovu kwa maana miundombinu yake ni ya muda mrefu sana. Ni lini sasa Serikali itatatua changamoto hii kwa sababu ni ya muda mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunatakiwa kutenga fedha za maintenance. Mnapoleta bajeti Waheshimiwa Wabunge kupitia kwenye Halmashauri zenu kama ambavyo wamefanya watu wa Rungwe, tunatakiwa pia kutenga bajeti kwa ajili ya matengenezo ili hii miundombinu ifike mahali kwamba isichakae kabla hatujafanya ukarabati. Pia sasa hivi kama miundombinu imeshachakaa, basi tunaomba muainishe kwenye Halmashauri mtuletee ili tutenge fedha kwa ajili ya ukarabati.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Singida Jimbo la Iramba Magharibi kuna Mradi wa World Bank ambao ulijengwa mwaka 1978 wa matenki ya maji ambayo mpaka leo yamekaa kama sanamu. Naomba Mheshimiwa Waziri aseme ni lini au Serikali ina mkakati gani wa kumalizia mradi huu kwa sababu ni muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa maelekezo, tumeandaa bajeti ya mwaka uliopita kwamba katika bajeti hiyo tuhakikishe kwamba tunatekeleza miradi ile ambayo bado haijakamilika; na tunaendelea hivyo na mwaka huu pia tumeandaa bajeti. Kwa hiyo katika halmashauri yake kama kuna miradi ambayo ilikuwa haijakamilika basi fedha katika mpango kazi wao wahakikishe kwamba wanaielekeza kwenda kukamilisha miradi ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano anaouzungumzia Mheshimiwa Mbunge nimeukuta Nanyamba ambapo Mheshimiwa Mbunge alinifuata na tukaenda kukaa na halmashauri. Kulikuwa na matenki yamejengwa lakini hayana maji. Sasa hivi Nanyamba tayari wananchi ile fedha ya mwaka jana wameshaitumia vizuri, wameelekeza kwenye miradi ambayo ilikuwa haijakamilika, wananchi wanapata maji. Naomba na Mheshimiwa Mbunge afanye hivyo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mikopo isiyolipika (non performing loans) imekuwa kwa kikubwa sana tangu miaka 1990, na sababu kubwa ni mbili, ya kwanza ni mazingira magumu ya biashara na ya pili ni riba kuwa juu.
Swali, ni kwanini, Serikali haioni haja ya kuwasaidia wafanyabiashara kwa kuwapa riba yenye mikopo nafuu kama njia ya stimulus package?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu Serikali yetu imekuwa ikijinadi kuwa yenyewe ni Serikali ya Kijamaa, na misingi na Sera ya Serikali ya Kijamaa ni pamoja na kuwa ukomo wa riba. Je, ni lini Serikali itaweka ukomo wa riba kama ambavyo nchi ya kibepari ya Kenya imeweka ukomo wa riba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kutokana na mfumo wa mwaka 1991 na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha, Benki Kuu au Serikali haiwezi kutoa mwelekeo au ukomo wa riba kwa ajili ya benki na taasisi za kifedha. Nchi yetu ni nchi huru inayofuata liberalization of the economy na hilo haliwezi kufanyika kwa sababu nimesema ni sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, nchi ya Kenya iliweka ukomo huo lakini imeingia katika matatizo makubwa ya kiuchumi kwa benki na taasisi za kifedha. Hivyo nchi yetu kama nchi huru inayofuata liberalization of the economy hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu ni sheria iliyopanga hivyo.