Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji (34 total)

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:-
Hali ya maisha ya wastaafu wetu ni mbaya sana na Serikali imeshindwa kuongeza pensheni zinazolingana na gharama halisi za maisha kwa sasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha pensheni za wastaafu hao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni kwa ajili ya kuwapunguzia wastaafu makali ya ongezeko la gharama za maisha. Ili kukabiliana na changamoto za ugumu wa maisha kwa wastaafu, Serikali imekuwa ikiongeza pensheni kwa wastaafu pale ambapo hali ya uchumi inaruhusu.
Kwa mfano, mwaka 2004 pensheni ilikuwa shilingi 21,606.05 ambayo iliongezwa hadi shilingi 50,114.43 kwa mwezi wa Julai, 2009 sawa na ongezeko la 132%. Mwezi Julai, 2015 Serikali imeongeza pensheni hadi kufikia Sh. 100,125.85 sawa na ongezeko la 100%.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za kiuchumi zilizopo kuanzia mwaka 2004 hadi 2015 kiwango cha pensheni kimeongezeka mara tano na Serikali itaendelea kuboresha pensheni za wastaafu kwa kadiri uchumi wa nchi utakavyokuwa unaimarika.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 inalenga kuwapunguzia wafanyakazi kodi ya mapato (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi kufikia tarakimu moja.
Je, Serikali imejipangaje kutekeleza jambo hilo muhimu kwa ustawi wa wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mfumo wa kodi ya wafanyakazi uliopo sasa una viwango vya kodi kwa kuzingatia kipato cha mfanyakazi ambapo kiwango cha kodi hupanda kadri ya kipato cha mfanyakazi kinavyopanda. Kwa sasa, kima cha chini kisichotozwa kodi ya mfanyakazi ni kipato cha mshahara kisichozidi shilingi 170,000/=. Watumishi Waandamizi wanalipa kodi kubwa kutokana na mishahara yao mikubwa na kwa asilimia kubwa zaidi ya wale watumishi wa hali ya chini.
Mheshimiwa Spika, watumishi wa ngazi za chini wataendelea kuboreshewa maslahi yao kwa kupunguza kiwango cha chini cha kodi. Kiwango cha chini cha kodi kinachotozwa kwenye kipato cha zaidi ya shilingi 170,000/= ni asilimia 11; na cha juu zaidi ni asilimia 30. Serikali imekuwa ikishusha kiwango cha chini cha kuanzia kutoza kodi kwa mfanyakazi hatua kwa hatua, kutoka asilimia 18.5 mwaka 2006/2007, asilimia 15 mwaka 2008/2009 na kufikia asilimia 14 mwaka 2010/2011. Mwaka 2012/2013 tumefikia asilimia 13; asilimia 12 kwa mwaka 2013/2014 na sasa kufikia kiwango cha asilimia 11. Lengo la kuendelea kushusha kiwango hiki ni kufikia kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufikia kiwango hicho cha asilimia 10 Serikali itaendelea kujadiliana na Vyama vya Wafanyakazi kwa lengo la kupunguza kodi hii ya Pay As You Earn (PAYE) hadi kufikia tarakimu moja kutegemea na hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika mwaka hadi mwaka.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO aliuliza:-
Mwaka 2013 Serikali iliuza hatifungani ya thamani ya Dola za Kimarekani milioni mia sita (USD 600m) kupitia benki ya Standard yenye tawi hapa nchini (Stanbic); Shirika la Corruption Watch la Uingereza kwa kutumia vyanzo kama IMF imeonesha kwamba hatifungani hiyo imeipa Serikali ya Tanzania hasara ya Dola za Kimarekani milioni themanini (USD) 80.m) na Serikali imelipwa faini Dola za Kimarekani milioni sita (USD Six Million) tu.
Je, kwa nini Serikali haiichukulii hatua Stanbic Bank ili walipe faini zaidi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Ruyagwa Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mahitaji yaliyofanywa na serious fraud office ya Uingereza dhidi ya Standard Bank Group, Serious Fraud Office ilitambua kiasi cha Dola za Kimarekani milioni sita, sawa na asilimia moja ya mkopo ambao Tanzania haikupaswa kutozwa. Tozo (arrangement fee) iliyotakiwa kulipwa kwa Standard Bank Group ni asilimia 1.4. Badala yake tozo iliyoingizwa kwenye mkataba ni aslimia 2.4, na ilithibitika kwamba tozo ya asilimia moja ya ziada haikuwa halali.
Katika hukumu iliyotolewa na Mahakama huko Uingereza Standard Bank Group iliamriwa kulipa faini ya Dola za Kimarekani milioni thelathini na mbili nukta mbili. Kati ya hizo kiasi cha Dola milioni saba zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania, Dola za milioni sita zikiwa ni fidia na Dola milioni moja ikiwa ni riba.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia taarifa ya hasara kwa Serikali ya Tanzania ya Dola za Kimarekani milioni themanini iliyotajwa na Mheshimiwa Zitto Mbunge wa Kigoma Mjini na hatukupata usahihi wake. Hata hivyo, taarifa ya hasara ya dola milioni themanini imetajwa katika taarifa yenye kichwa cha habari How Tanzania was Short Changed in Stanbic Bribery Payback iliyochapishwa katika gazeti la The Guardian la tarehe 16 Disemba, 2015, likinukuu taarifa ya Corruption Watch ya Uingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taarifa haikutoa maelezo ya namna hasara ya dola milioni themanini ilivyopatikana na kwa kuwa, taarifa iliyonukuliwa kutoka corruption watch pia haielezi jinsi hasara hiyo ilivyokokotolewa, Serikali inashauri Mheshimiwa Mbunge awasilishe taarifa alizonazo tuone iwapo ina vigezo vya kutosha kuisaidia Serikali kujenga hoja ya madai ya hasara hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo hayo napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Benki Kuu imeiandikia Benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni tatu kwa kosa la kufanya miamala inayokiuka sheria na kanuni za benki na taasisi za fedha. Aidha, sheria inaitaka Benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambacho kimekwisha tarehe 30 Januari. Kwamba Stanbic imewasilisha taarifa ya utetezi wao Benki Kuu na utetezi wao unafanyiwa kazi kwa sasa. Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi huo Benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kwa muda mrefu uchumi wa Nchi yetu umekuwa ukikua kwa asilimia saba kwa mwaka:-
Je, mapato ya Serikali yamekuwa yakiongezeka kwa asilimia ngapi kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, uchumi wa nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita 2010-2015 umekua kwa wastani wa asilimia 6.74. Ukuaji halisi wa asilimia katika kipindi hicho ulikuwa asilimia 6.4 mwaka 2010, asilimia 7.9 mwaka 2011, asilimia 5.1 mwaka 2012, asilimia 7.3 mwaka 2013 na asilimia saba mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho mapato ya Serikali ambayo yanajumuisha mapato ya kodi na mapato yasiyokuwa ya kodi ya Serikali Kuu pamoja na mapato ya Halmashauri yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 17.8 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010/2011 mapato yalifkia shilingi trilioni tano nukta saba tatu na kuongezeka hadi Shilingi trilioni saba nukta mbili mbili mwaka mwaka 2011/2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.9, mwaka 2012 mapato yakafikia shilingi trilioni nane nukta tano moja, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.9. Mwaka 2013/2014 mapato yalifikia shilingi trilioni kumi nukta moja mbili ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.6 na mwaka 2014/2015 mapato yakafikia shilingi trilioni kumi nukta tisa tano, sawa na ongezeko la asilimia 7.6.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha na kumiliki Bureau de Change zake yenyewe badala ya kuacha huduma hiyo kuendelea kutolewa na watu au taasisi binafsi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbuge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mkakati wa kufungua au kuanzisha Bureau de Change zake kwa sababu imejitoa kuhusika moja kwa moja na biashara ya fedha kama vile benki na Bureau de Change kutokana na mabadiliko ya mfumo katika sekta ya fedha nchini unaotekelezwa kuanzia mwaka 1991. Sekta binafsi imeachiwa jukumu la kuanzisha na kuendesha biashara ya fedha nchini chini ya usimamizi wa Benki Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imebaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri na salama ya uwekezaji katika sekta zote, ikiwemo sekta ya fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kuanzisha, kuendesha na kutoa huduma bora za kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka sheria na taratibu za kusaidia nguvu na juhudi za wananchi katika kuanzisha benki au taasisi za fedha katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.
Kwa hiyo, Serikali inategemea kuwa wananchi watatumia fursa hii ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini na kuanzisha huduma za kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo yenye uhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kusimamia kwa ukaribu zaidi maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ili yaweze kutoa huduma bora na inayokidhi matakwa ya sheria na kanuni za biashara ya fedha. Hivi karibuni Benki Kuu imetoa kanuni mpya kwa lengo la kuimarisha usimamiaji wa maduka hayo. Maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni yanatakiwa kufunga mashine za EFDs ili kuiwezesha TRA na BoT kupata taarifa za moja kwa moja juu ya miamala inayofanywa kwenye maduka hayo.
MHE. CONCHESTER L. RWAMLAZA aliuliza:-
Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 Serikali kupitia Waziri wa Fedha iliahidi kupandisha pensheni kwa wastaafu wanaolipwa Sh.50,000 ili walipwe Sh. 100,000/=.
Je, Serikali imetekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchester L. Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumfahamisha Mheshimiwa Rwamlaza na Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali ilitekeleza ahadi yake ya kuongeza kima cha chini cha pensheni kutoka Sh.50,114.43 kwa mwezi hadi kufika Sh.100,125.85 kwa mwezi, kuanzia Julai 2015 ikiwa ni ongezeko la asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kabla sijaruhusu swali langu kujibiwa naomba marekebisho madogo kwenye majina yangu yaliyo kwenye majibu ya Waziri. Jina langu Samson halina (iiI kule mwisho na jina langu Bilago halina N katikati halisomeki Bilango linasomeka Bilago.
MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wastaafu kutolipwa mafao yao baada ya kustaafu:-
(a) Je, kuanzia Januari hadi Disemba, 2015 ni watumishi wangapi wa umma wamestaafu utumishi?
(b) Je, kati ya hao ni wangapi wamelipwa mafao yao?
(c) Kama kuna ambao hawajalipwa, je, ni kwa sababu gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Idadi ya watumishi wa umma waliostaafu, kati ya Januari, 2015 na Disemba, 2015 ni 7,055
(b) Kati ya watumishi 7,055 waliostaafu, watumishi 5,057 wamelipwa mafao yao.
(c) Jumla ya watumishi waliostaafu 1,998 hawajalipwa mafao yao kutokana na sababu zifuatazo:-
(i) Upungufu wa baadhi ya nyaraka muhimu katika majadala ya wastaafu.
(ii) Waajiri kuchelewa kuwasilisha nyaraka muhimu zinazotakiwa kuthibitisha uhalali wa utumishi wa wahusika kabla ya mfuko kuanzishwa Julai, 1999.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Je, ni utaratibu gani unaotumika kukokotoa kodi katika forodha zetu zinazopokea bidhaa na vitu mbalimbali vinavyotokea Zanzibar, wakati vitu vilevile vinavyozalishwa Zanzibar ni vilevile vinavyotoka nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini na ukokotoaji wa ushuru au kodi ya bidhaa mbalimbali kutoka nje, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazopitia Zanzibar kuja Bara, unafanywa kwa kutumia mfumo ujulikanao kama Import Export Commodity Database. Mfumo huu unatunza kumbukumbu ya bei ya bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka nje na kutumiwa na Mamlaka ya Mapato kama kielelezo na rejea wakati wa kufanya tathmini na ukokotoaji wa kodi au ushuru wa forodha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyaraka za bidhaa zinapowasilishwa Central Data Processing Office, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazotoka nje ya nchi kupitia Zanzibar, bei au thamani ya bidhaa husika huingizwa kwenye mfumo wa Import Export Commodity Database, ili kuhakiki uhalali wa bidhaa na bei husika na kukokota kiwango cha kodi anachotakiwa kulipa mteja. Endapo bei au thamani ya bidhaa iliyopo kwenye nyaraka itakuwa chini ya ile iliyopo kwenye mfumo wa wetu, mfumo utachukua bei iliyopo kwenye database na kukokotoa kiwango halali cha kodi. Hata hivyo, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kusafirishwa kuja Tanzania Bara hazilipiwi kodi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Fedha za miradi ya maendeleo kutotolewa kwa wananchi kwa wakati jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara na miradi ya maendeleo kuchelewa kukamilika:-
Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Bunge lako Tukufu linavyofahamu, muundo wa bajeti yetu unavyopitishwa na Bunge, una vyanzo viwili vya mapato; mapato ya ndani na mapato kutoka nje. Wakati wa utekelezaji wa bajeti, kiwango cha mgao hutegemea zaidi mapato halisi kutoka vyanzo vyote viwili. Hivyo basi, mapato pungufu au chini ya malengo kutoka kwenye chanzo chochote kati ya hivyo vilivyotajwa, yataathiri mgao wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia pekee na muafaka ya kukabiliana na changamoto hiyo ni Serikali kuongeza mapato yake kutoka vyanzo vya ndani. Hatua kadhaa za kuongeza mapato ya ndani tayari zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na kubana na kuziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuhakikisha kuwa kila anayestahili kulipa kodi, analipa kodi stahiki na kupanua wigo wa kodi kwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuweka mazingira rafiki au wezeshi kwa mlipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la hatua hizi ni kuongeza mapato ya Serikali na hatimaye kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ambayo inaambatana na masharti kadhaa, baadhi yake yakileta usumbufu na hasara kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wanatambua hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli katika kudhibiti suala la kukwepa kodi na kuongeza mapato ya Serikali. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge waunge mkono hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali yetu.
MHE. KHATIB SAID HAJI (K.n.y. KHAMIS MTUMWA ALI) aliuliza:-
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inafanya ukaguzi katika Taasisi za Tanzania Bara na Zanzibar:-
Je, Ofisi hii inashirikiana vipi wakati wa kufanya ukaguzi wa Taasisi za Muungano na Ofisi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mtumwa Ali, Mbunge wa Jimbo la Kiwengwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inafanya ukaguzi katika Taasisi zote za Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 143 (2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977. Ibara hiyo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, mamlaka ya kufanya ukaguzi wa hesabu za mihimili yote mitatu ya dola, Serikali, Bunge na Mahakama na kutoa ripoti ya ukaguzi angalau mara moja kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mipaka ya kufanya kazi baina ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Jukumu la ukaguzi wa Taasisi za Muungano lipo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Wakati jukumu la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ni kukagua Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mipaka hiyo ya kazi, kumekuwepo na ushirikiano katika kufanya ukaguzi wa pamoja kati ya Ofisi hizi kuu mbili kwa lengo la kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu. Kwa mfano ukaguzi wa ujenzi wa Ofisi za Wabunge kwenye Majimbo, ukaguzi wa bahari ya kina kirefu na mradi wa kupambana na UKIMWI Zanzibar. Ukaguzi wa miradi hii ulifanywa kwa ushirikiano wa pande zote mbili.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupunguza misamaha ya kodi kufikia asilimia moja (1%) ya GDP?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ya kupunguza misahama ya kodi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa ni mkakati unaotekelezwa kwa awamu na kwa kuzingatia mazingira ya kiuchumi, kijamii na sheria zilizopo. Juhudi za kutekeleza azma ya kupunguza misamaha ya kodi zilianza kufanyika mwaka 2010/2011 baada ya kubaini kuwa, kwa wastani misamaha yetu ilikuwa imefikia takribani asilimia 3.2 ya pato la Taifa kwa mwaka, katika kipindi cha mwaka 2006/2007 hadi 2009/2010.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009/2010 Serikali iliamua kupitia upya sheria zinazohusu misamaha ya kodi ili kuondoa misamaha ambayo haikuwa na tija katika Taifa letu. Katika mapitio hayo Serikali ilibaini kuwa takribani asilimia 60 hadi asilimia 64 ya misamaha yote ya kodi ilikuwa inatokana na kodi ya ongezeko la thamani – VAT. Baada ya kubaini hali hiyo, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilifanya maboresho ya Sheria ya VAT, Sura ya 148 na kuondoa misamaha ambayo haikuwa na tija kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa, hususan za kurekebisha upeo wa misamaha inayotolewa chini ya Kituo cha Uwekezaji – TIC na Sekta ya Madini, zimesaidia kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia 1.9 ya pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015. Katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016 kiasi cha kodi kilichosamehewa ni shilingi milioni 564,106.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwenendo huu ni matarajio yetu kuwa kiasi cha msamaha wa kodi katika Mwaka wa Fedha 2015/2016 kitakuwa ni shilingi milioni 752,141.9 sawa na asilimia 0.84 ya pato la Taifa. Kutungwa upya kwa Sheria ya VAT ni eneo moja ambalo limeleta ufanisi mkubwa katika kutimiza azma yetu ya kupunguza misamaha ya kodi, hadi kufikia asilimia moja ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, baadhi ya misamaha ya kodi haiepukiki katika mifumo ya kodi hapa nchini na popote duniani. Suala la msingi ni kuwa Serikali itahakikisha kuwa misamaha yote ya kodi inatolewa kwa mujibu wa Sheria za Kodi zilizopo.
Katika siku za usoni usimamizi wa misamaha utajengwa katika mifumo imara ya udhibiti inayozingatia matumizi ya teknolojia. Lengo la muda mrefu ni kuweka mfumo wa misamaha ya kodi unaokubalika Kimataifa, pia misamaha hiyo iwe ni ile inayochochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Kwa miaka mingi sasa Tanzania Investment Bank na TADB imekuwepo ila mchango wake katika kupunguza umaskini haufahamiki zaidi hata kwa Waheshimiwa Wabunge. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Benki za TIB na TADB zinajielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa sababu ndiyo mkataba wa mpango kazi wa maendeleo ya nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya kuanzishwa kwa Benki ya TIB na TADB kama benki za maendeleo ni kutoa mikopo ya muda wa kati na muda mrefu kwa lengo la kufadhili miradi ya kimkakati. Katika kutimiza azma ya kufadhili miradi ya kimkakati ya kufungua fursa za kiuchumi na kupunguza umaskini, TIB imetoa mikopo katika maeneo yafuatayo:
Mradi wa Maendeleo ya Makazi (Temeke na Kinondoni); Mradi wa Maendeleo ya Miji kupitia NHC; Viwanda vya Kubangua Korosho; maghala; mabomba ya maji; sukari na kilimo cha miwa; kukoboa na kusindika kahawa; kusindika matunda; mifuko ya kuhifadhia mazao; nyaya za umeme; vinu vya pamba na uzalishaji wa mafuta yatokanayo na mbegu za pamba; na mahoteli. TIB umewekeza katika mashirika ya umma kama vile Shirika la Reli (TRL), imeiwezesha TPDC katika mradi wa gesi na kuipatia TANESCO mkopo kwa ajili ya fidia kwa wananchi ili kuweka njia mpya ya kusafirisha umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mwaka jana (2015), TIB imewawezesha Watanzania wengi kupambana na umaskini kwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 550 katika sekta mbalimbali za kiuchumi. Katika sekta ya kilimo, TIB imewasaidia wananchi wengi kwa kusimamia mikopo iliyotolewa na Serikali kupitia Dirisha la Kilimo inayofikia shilingi bilioni 58.8 hadi mwishoni mwa mwaka 2015. Mikopo hii ilitolewa kupitia makampuni binafsi yapatayo 121, taasisi ndogo ndogo za fedha zipatazo 11 na SACCOs 78.
Mheshimiwa Naibu Spika, TIB pia imetoa mkopo wa shilingi bilioni 489.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 181 ya kusambaza umeme vijijini kupitia REA na kaya 257,000 zimenufaika na mradi huo. Aidha, vikundi 17 vya wachimbaji wadogo wadogo vimenufaika na mikopo ya jumla ya shilingi bilioni nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya TIB kwa sekta na taasisi mbalimbali imesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira mpya na kuendeleza zilizopo. Pia mikopo ya TIB imetumika kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje kama vile maua, kahawa na dhahabu. Pamoja na Benki ya Kilimo kuchelewa kuanza kutoa mikopo ni wazi kabisa kuwa Benki ya TIB imejielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo kama vile Dira ya Taifa (2025), Mpango wa Pili wa Maendeleo na Maendeleo Endelevu 2020 pamoja na Ajenda ya Afrika 2063.
MHE. OMAR M. KIGUA aliuliza:-
Ulipaji kodi ni chanzo kikuu cha mapato ya nchi kwa ajili ya maendeleo na Serikali inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria na ili Serikali iweze kukusanya kodi kwa ufanisi mkubwa ni lazima kuwe na Ofisi za TRA katika maeneo mbalimbali nchini:-
(a)Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Ofisi ya TRA katika Wilaya ya Kilindi?
(b)Kwa kutokuwa na Ofisi za TRA Serikali haioni kama inadhoofisha maendeleo ya Wilaya hususani katika suala la mapato?
(c)Kwa kuweka Ofisi za TRA Wilaya ya Handeni na kuacha Wilaya ya Kilindi, Serikali haioni kama inawajengea wananchi tabia ya kukwepa kulipa kodi kutokana na umbali uliopo kati ya Wilaya hizo mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufungua Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Wilayani Kilindi kama ilivyo katika Wilaya zingine. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina mpango wa kufungua ofisi za Mamlaka ya Mapato katika Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Kilindi baada ya kukamilisha zoezi la utafiti na uchambuzi wa kina kuhusu fursa za mapato ya kodi zilizopo katika Wilaya zote ambazo hazina ofisi za TRA.
(b)Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha ofisi za Mamlaka ya Mapato katika Wilaya ni fursa mojawapo ya kuleta maendeleo katika eneo husika. Aidha, uamuzi wa kufungua ofisi ya Mamlaka ya Mapato unazingatia zaidi gharama za usimamizi na ukusanyaji wa mapato. Kwa msingi huo, Serikali haidhoofishi maendeleo ya Wilaya ya Kilindi isipokuwa ni lazima tufanye utafiti kwanza kubaini gharama za usimamizi na ukusanyaji wa mapato kabla ya kufungua ofisi.
(c)Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Kigua kuwa uwepo wa ofisi za Mamlaka ya Mapato katika maeneo yetu unaongeza ari ya wananchi kulipa kodi kwa hiari. Napenda kutoa rai yangu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilindi na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa mujibu wa sheria. Aidha, wananchi wasiache kulipa kodi kwa kutumia kisingizio cha maeneo yao kukosa ofisi za Mamlaka ya Mapato kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamevunja sheria na kuikosesha Serikali yao mapato ambayo yangetumika kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Benki ya Wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao (wajasiriamali) kupata huduma iliyo bora kupitia benki yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu na Mchango wa wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kufungua benki mpya za wafanyabiashara wakubwa na wadogo, isipokuwa inafanya jitihada za kuimarisha benki zake zilizopo ikiwemo Benki ya Kilimo na Benki ya Wajasiriamali.
Mheshimiwa Spika, ni vema tukaimarisha benki za Serikali zilizopo kwa sasa kuliko kuanzisha benki zingine. Tukianzisha benki mpya tutaipunguzia Serikali uwezo wa kifedha wa kuziimarisha benki zilizopo. Mfano, Benki ya Posta ni benki ya Serikali na imeenea nchi nzima kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wetu, hususani wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati. Kama Serikali, tutaimarisha benki hizi zilizopo na pia kuipa sekta binafsi fursa ya kuanzisha benki zaidi kwa kadri soko litakavyoruhusu, ni imani yetu kubwa kwamba wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo watapata huduma husika.
MHE. NEEMA W. MGAYA (K.n.y. MHE. SUSAN C. MGONOKULIMA) aliuliza:-
Mfumo wa mashine za EFDs hauchanganui kwa uwazi fedha ipi ni mapato ya kodi na ipi ni faini au ni gharama za uendeshaji:-
Je, ni lini kutakuwepo ushirikishwaji kati ya waandaaji mfumo wa TRA na viongozi wa wafanyabiashara ili kodi inayotozwa iwe halali na isiwe inayoua mitaji ya wafanyabiashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Chogisasi Mgonokulima, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa matumizi ya mashine za kutunza hesabu za kodi za kielektroniki ulianzishwa kwa lengo la kurahisisha na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za biashara za walipa kodi. Mfumo wa EFD ulianzishwa ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya utunzaji kumbukumbu za mauzo na utoaji wa risiti za mauzo zinazoandikwa kwa mkono. Mfumo huu umerahisisha usimamizi na ukadiriaji wa kodi kwa kuwa kumbukumbu zote za mauzo na manunuzi huhifadhiwa na kutunzwa kirahisi kwenye mashine za EFD na taarifa za mauzo ya mlipa kodi hutumwa kwenye saver ya Mamlaka ya Mapato moja kwa moja kwa njia ya mtandao kupitia mashine husika ya EFD kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa EFD haukuundwa kwa ajili ya kutoa mchanganuo wa fedha kwa mapato ya kodi, faini au gharama za uendeshaji wa biashara. Mfumo wa EFD ni kwa ajili ya kutunza kumbukumbu sahihi za mauzo na manunuzi ya mfanyabiashara pamoja na kutoa risiti. Mchanganuo wa mapato ya kodi na gharama za uendeshaji hufanywa kwa njia ya kawaida ya kiuhasibu kwa kutumia kumbukumbu za mauzo na manunuzi ya biashara zinazotunzwa katika mashine za EFD.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania ina jukumu la kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya Serikali yanayotokana na kodi, ada, na tozo mbalimbali pamoja na kusimamia sheria zote za kodi zilizotungwa na kupitishwa na Bunge lako Tukufu. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango ina utaratibu wa kushirikisha wadau mbalimbali wakati wa maandalizi ya bajeti ambao hutoa michango yao na ushauri kwa kupitia kikosi kazi yaani task force kilicho chini ya Idara ya Sera ambacho kazi yake ni kuchanganua maoni na ushauri uliotolewa na kuainisha mambo muhimu ya kuingiza katika bajeti ya Taifa. Utaratibu huu hutoa fursa kwa viongozi wa wafanyabiashara na wengine kutoa maoni na ushauri ili ufanyiwe kazi na kuingizwa katika mipango ya Serikali. Hakuna kodi inayotozwa kwa nia ya kuua mitaji ya wafanyabiashara wetu, kwani kiwango cha juu cha kodi ya mapato ni asilimia 30 ya mapato baada ya kuondoa gharama za biashara yaani net profit. Pale ambapo mfanyabiashara hakupata faida, hakuna kodi ya mapato itakayotozwa. Hivyo basi, kodi zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato ni halali na haziui mitaji ya wafanyabiashara wetu.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE) aliuliza:-
Wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii huko vijijini lakini pia hawana mafunzo maalum ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kufikia huduma hiyo ya kukopeshwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma ya benki kwenye vijiji ili wanawake wa huko waweze kupata mikopo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa akina mama hao mafunzo maalum yatakayowasaidia katika kujipanga kukopa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mipango ya Serikali kupeleka huduma ya benki kwenye vijiji ili wanawake waweze kupata mikopo, napenda ikumbukwe kwamba kufuatana na mabadiliko ya mfumo wa kifedha nchini unaotekelezwa tangu mwaka 1991, Serikali imejitoa katika kuhusika moja kwa moja na uendeshaji wa shughuli za benki na badala yake Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya utoaji huduma za kibenki ili huduma hizi ziwafikie wananchi wengi. Kupitia Benki Kuu ya Tanzania, Serikali imefanya msukumo wa kuhakikisha kuwa huduma za kibenki zinawafikia wananchi ili kurahisisha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi mijini na vijijini. Benki kadhaa zimeanzisha huduma za kibenki kupitia mawakala na huduma za kifedha kupitia simu za mkononi ambazo zimewasaidia sana wananchi sehemu ambako hakuna matawi ya benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Benki Kuu inaendelea kuweka mazingira wezeshi na taratibu rafiki ili kusaidia nguvu za wananchi na sekta binafsi kuanzisha benki au taasisi za fedha. Juhudi hizi zimesaidia wananchi kuanzisha benki za kijamii na taasisi ndogondogo za fedha katika maeneo yao. Ni matarajio ya Serikali kuwa wananchi watatumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hapa nchini kuwekeza wao wenyewe au kuzishawishi benki kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo yao. Aidha, Serikali pia itaendelea kushawishi benki nchini kupanua shughuli zao ili ziwafikie wananchi wengi hasa wale wa vijijini wakiwemo akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikishirikiana na Benki Kuu ipo tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo akina mama. Benki Kuu kupitia Kurugenzi yake ya Utafiti na Uchumi ina mpango wa kuelimisha umma (consumer literacy program) kuhusu utumiaji wa huduma za kifedha nchini ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa huduma za kifedha ikiwemo taratibu zinazohusu mikopo.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE aliuliza:-
Kufuatia taarifa zilizotolewa na vyombo vya Serikali vinavyohusika na masuala ya utafiti na takwimu, Mkoa wa Kagera ulikuwa miongoni mwa mikoa mitano maskini ya mwisho Kitaifa.
(a) Je, ni mambo gani yametumika kama vigezo vya kuingiza Mkoa wa Kagera katika orodha ya mikoa mitano maskini Kitaifa?
(b) Je, ni jitihada gani za makusudi zinazochukuliwa na Serikali kuunusuru Mkoa wa Kagera na umaskini huo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Bukoba Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vilivyotumika katika kubainisha Mikoa na Wilaya maskini ni uwezo wa kaya kukidhi mahitaji ya msingi kama vile chakula chenye kiwango cha kilo kalori 2,200 kwa siku, mavazi na malazi. Kwa kutumia vigezo hivi uchambuzi wa kina wa takwimu zilizotokana na utafiti wa mapato na matumizi katika kaya wa mwaka 2011/2012 na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ulibaini kuwa Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha umaskini wa asilimia 39.3.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kunusuru Mkoa wa Kagera na umaskini, Serikali inafanya jitihada na kuchukua hatua mbalimbali kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama ifuatavyo:-
(i) Kuendeleza maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda kwa kujenga miundombinu ya msingi ili kuwezesha uwekezaji na ukuaji wa viwanda vidogovidogo na vya kati katika Mkoa wa Kagera.
(ii) Kuendelea kuhamasisha wananchi wote ikiwemo Mkoa wa Kagera kutumia fursa na rasilimali mbalimbali zilizopo katika mikoa husika.
(iii) Kuendeleza Sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo, utafiti, na masoko ya mazao.
(iv) Kukuza sekta ya viwanda, hususan vya kusindika mazao ya maliasili, kilimo na uvuvi.
(v) Kuendeleza viwanda vya nyama vilivyopo Kanda ya Ziwa ikiwemo Mkoa wa Kagera, viwanda hivyo vitasaidia kuendeleza ufugaji utakaoinua kipato cha mtu mmojammoja pamoja na kuendeleza uchumi wa mkoa husika.
(vi) Uendelezaji wa viwanda vya nguo katika mikoa inayozalisha pamba ambapo Kagera huzalisha kwa asilimia 2 ya pamba yote katika Ukanda wa Magharibi.
MHE. FREEMAN A. MBOWE (K.n.y MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Nne ilikopa fedha kwenye Benki za Nje na zile za biashara kwa mfano mwaka 2011 Serikali ilikopa shilingi trilioni 15 na kufanya Deni la Taifa kufikia shilingi trilioni 21, kabla ya mwaka 2015 ilikopa tena kiasi cha shilingi trilioni 9 na kufanya Deni la Taifa kuongezeka kufikia shilingi trilioni 39.
(a) Je, mpaka sasa Deni la Taifa linafikia kiasi gani?
(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya makusudi ya kudhibiti ongezeko hilo la Deni la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali ilipokea mikopo ya nje yenye masharti nafuu na ya biashara kiasi cha shilingi bilioni 1,333.28 na mwaka 2014/2015 Serikali ilipokea mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 2,291.6. Mikopo hiyo haikufikia kiasi cha trilioni 15 kwa mwaka 2011 na trilioni tisa kabla ya mwaka 2015 kama ilivyotafsiriwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Juni, 2016, Deni la Taifa lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 23.2 ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni 19.69 mwezi Juni, 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 20.5 na deni la sekta binafsi lilikuwa dola za Kimarekani bilioni 2.7.
Aidha, deni la Serikali lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja nchini, mradi wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafishia gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na mradi wa maji Ruvu Chini na Ruvu Juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya makusudi kabisa ili kudhibiti ongezeko la deni hilo. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa miradi yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa Pato la Taifa, kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa wakandarasi na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mikataba inayoweza kusababisha mzigo wa madeni kwa Serikali. Aidha, Serikali inaendelea na mchakato wa kukamilisha zoezi la nchi kufanyiwa tathmini (sovereign rating) kwa lengo la kupata mikopo nafuu.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Serikali imeanzisha mfumo ambao wafanyabiashara wanapouza au kutoa huduma wanatoa risiti kupitia mashine za EFD na mfumo huu umeelekezwa na Sheria na Kanuni za kodi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka utaratibu ambao utawezesha TRA kupata rekodi za moja kwa moja ambayo inapata kupitia mfumo wa EFDs kwa mauzo ya huduma ambayo yanafanyika kwa njia ya Electronic Commerce.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitunga Sheria na Kanuni za matumizi ya mashine za EFDs ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa takwimu sahihi za miamala ya mauzo ya kila siku kutoka kwa wafanyabiashara. Lengo ni kurahisisha ukokotoaji na ukadiriaji wa viwango vya kodi ikiwa ni hatua ya kuhakikisha kuwa Serikali inapata kodi stahiki na mlipa kodi analipa kodi stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu wa matumizi ya EFDs unaiwezesha Mamlaka ya Mapato kupata taarifa zote za mauzo yanayofanyika ndani ya nchi, hata kama mauzo ya bidhaa au huduma yatakuwa yamefanyika kwa njia ya mitando (E- Commerce). Ili kufanikisha azma ya Serikali ya kupata takwimu sahihi za mauzo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na jitihada ya kuhakikisha wafanyabishara wote wenye sifa za kutumia mashine za EFDs wanafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za kiteknolojia, hususan teknolojia ya kufanya manunuzi kupitia mitandao. Hatua tunazochukua ni pamoja na kuongezea wafanyakazi wa mamlaka uwezo wa kukusanya kodi kwenye biashara zinazofanyika kwa njia ya mitandao. Aidha, mamlaka inaendelea kuingia kwenye makubaliano ya kubadilishana taarifa mbalimbali na taasisi na mashirika mbalimbali (Third Party Information) ili kuweza kupata taarifa za miamala ya mauzo, hususan zile zinazofanyika nje ya upeo wa kawaida tunaoweza kuona kupitia mitandao.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Zanzibar vipo vikundi vya VICOBA ambavyo usajili wake ni lazima waje Tanzania Bara kufanya usajili:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha Ofisi Tanzania Zanzibar ili kuweka unafuu kwa wananchi wa Zanzibar?
(b) Je, gharama za usajili wa VICOBA ni kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, VICOBA ni vikundi ambavyo vimekuwa vikiundwa na wananchi ili kupambana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya kifedha, hususan wananchi wa kipato cha chini na wale waishio mbali na huduma rasmi za kifedha. Vikundi hivi kwa sehemu kubwa vimekuwa vikiundwa na kusimamiwa na taasisi zisizo za Serikali kama vile NGOs, CBOs na kadhalika. Kwa maana hiyo, taratibu za uratibu, uhamasishaji, usajili na malezi ya vikundi hivyo hufanywa na NGO‟s au CBO‟s.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mwongozo maalum kwa sasa kwa usajili wa vikundi vya VICOBA. Hivyo basi, baadhi ya vikundi vya VICOBA kutoka Zanzibar hufuata usajili Tanzania Bara ili kukidhi matakwa ya taasisi zinazowaongoza, hususan NGOs na CBOs. Aidha, kwa kutambua mchango mkubwa wa vikundi hivyo katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na huduma za kifedha katika baadhi ya maeneo na makundi maalum, Serikali imetoa fursa kwa vikundi hivyo kusajiliwa BRELA pamoja na Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar Ofisi za Ushirika zinasajili VICOBA kama Vyama vya Kuweka na Kukopa vya Awali kwa makubaliano kwamba, VICOBA hivyo vitakua na hatimaye kubadilishwa kuwa SACCOS kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha mapitio ya marekebisho ya Sera ya Huduma Ndogondogo za Kifedha na Sheria yake Tanzania Bara na Sera ya Huduma Ndogondogo za Kifedha kule Zanzibar zinazotarajiwa kuweka mwongozo rasmi wa usajili wa VICOBA na uendeshaji wake. Mapendekezo ya marekebisho ya sera yanasubiri kupangiwa tarehe ya kujadiliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia sasa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za usajili wa vikundi vya VICOBA zinatofautiana kutegemeana na mamlaka zinazowasajili. Mfano, ada ya usajili chini ya NGOs ni sh. 150,000 na Halmashauri za Wilaya ni kati ya sh. 30,000 na sh. 70,000. Viwango vya ada ya usajili chini ya Halmashauri za Wilaya vinatofautiana kwa kuwa hakuna mwongozo maalum, kama nilivyosema hapo awali, unaopaswa kuzingatiwa na Halmashauri zote.Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa upande wa BRELA ada za usajili zinatofautiana kulingana na mtaji wa kikundi husika. Mfano ada ya usajili kwa kikundi chenye mtaji usiozidi sh. 5,000,000 ni sh. 10,000; kati ya sh. 5,000,000 na 10,000,000 ni sh. 20,000 na kati ya sh. 10,000,000 na sh 50,000,000 ni sh. 50,000.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Wafanyabiashara wanaotoa bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara hutozwa kodi Zanzibar na wanapofika Tanzania Bara hutozwa kodi tena; vilevile, wafanyabiashara wanaotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar, hutozwa kodi tena Zanzibar. Hali hii husababisha wafanyabiashara kushindwa kuendelea na biashara kwani wanatozwa kodi mara mbili:-
(a) Je, Serikali inatambua uwepo wa utaratibu wa kutozwa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi na wa kudumu kutatua suala la wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa utaratibu wa kutozwa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara wanoingiza bidhaa za nje Tanzania Bara kupitia Zanzibar kwa sababu Tanzania Bara inatumia mfumo ujulikanao kama Import Export Commodity Database, ambao hautumiki kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, Import Export Commodity Database ni mfumo unaoweka kumbukumbu ya bei ya bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu ya bei za bidhaa mbalimbali zilizopo kwenye mfumo wa Import Export Commodity Database hutumiwa kama msingi wakati wa kufanya tathmini ya kodi ya bidhaa zinazoingizwa nchini pale thamani ya bidhaa husika inapoonekana kuwa hailingani na hali halisi. Hivyo basi, tofauti ya kodi inayotokana na kutotumika kwa mfumo wa Import Export Commodity Database kuthamini kiwango cha kodi kwa upande wa Zanzibar hukusanywa Tanzania Bara ili kuweka mazingira sawa ya ushindani kibiashara kwa bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara.
Mpango wa muda mfupi, muda mrefu na wa kudumu wa kutatua changamoto ya wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili, ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuridhia matumizi ya mifumo ya uthaminishaji wa kodi inayotumika ndani ya Idara ya Forodha ili kuondoa tofauti zilizopo za ukadiriaji wa kodi kati ya sehemu mbili za nchi yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itashawishi Benki za Biashara kuwekeza katika Jimbo la Mlalo ambalo mzunguko wa fedha ni mkubwa sana kutokana na magulio ya mboga mboga na matunda?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo huduma za kibenki katika sehemu zenye shughuli za kiuchumi kama kilimo cha mboga mboga na matunda kama Jimbo la Mlalo. Kwa sababu hiyo, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya utoaji huduma za kibenki ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na miundombinu ya umeme ili kuchochea zaidi shughuli za uzalishaji na hatimaye kuvutia mabenki kufungua matawi sehemu hizo. Ikumbukwe kuwa uanzishaji wa huduma za kibenki hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia uwezo wa kupata faida pande zote mbili yaani benki na wananchi. Hii pia hutegemea na uchumi wa eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya kuendesha mfumo wa kifedha nchini unaotekelezwa kuanzia mwaka 1991, Serikali imekuwa ikitekeleza azma ya kujitoa katika kuhusika moja kwa moja na biashara ya mabenki. Kwa hiyo, Serikali imebaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuiwezesha sekta binafsi kuanzisha benki na kutoa huduma bora za kifedha kwa wananchi wetu, hususan pale ambapo huduma hizo zitaweza kujiendesha. Serikali inaendelea na ushauwishi wake wa Benki za Biashara na taasisi nyingine za fedha kuanzisha huduma za kibenki na kifedha popote ambapo kuna mzunguko mkubwa wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ushawishi wa Serikali, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Serikali yetu, kuwashauri wananchi wa Mlalo kujiunga na kuanzisha Benki za Kijamii (Community Banks) na taasisi ndogo za kifedha (Micro Finance Institutions) zinazozingatia mazingira ya mahali husika ili kukidhi mahitaji ya kibenki ya Jimboni Mlalo.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Wizara ya Fedha katika juhudi zake za kukusanya mapato ya Serikali, imeweka Sheria ya Kukusanya Kodi ya Magari inayoitwa Motor Vehicle au Road License. Kodi hiyo imekuwa ikilalamikiwa sana na wananchi kwa kuwa imekuwa ikidaiwa hata kwa magari mabovu au ambayo yamepaki kwa muda wote bila kujali kipindi ambacho gari lilikaa bila kufanya kazi:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuitazama upya sheria hii?
(b) Kwa kuwa kodi hudaiwa hata kipindi ambacho gari halifanyi kazi: Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo inawaibia wananchi wake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi ya Motor vehicle Annual License inasimamiwa chini ya Sheria ya Road Traffic Act, 1973 pamoja na kanuni zake (The Road Traffic na Motor Vehicle Registration Regulations). Sheria hii imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara kulingana na mahitaji ya wakati husika. Kodi hii ni moja ya kodi zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini na kutoa huduma mbalimbali. Hivyo hatuwaibii wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa The Road Traffic Motor Vehicle Registration Regulations ya mwaka 2001, Sura ya Pili, Kifungu cha (4) na (5) hakuna msamaha wa leseni ya gari kwa mtu yeyote na inataka ada hiyo kulipwa kila mwaka tangu gari husika liliposajiliwa. Hivyo, sheria haitoi unafuu wowote kwa gari lililosimama kwa muda mrefu bila kutembea barabarani. Ni kweli utekelezaji wa sheria hii unaleta adha kwa wamiliki wa magari na hasa pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kwamba gari husika limesimama kwa muda mrefu na kwa sababu za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa adha hii, Mamlaka ya Mapato imeanza mchakato wa kuboresha sheria hii ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuhudumia wamiliki wa magari ambayo yatakuwa yamesimama kwa kipindi kirefu bila kutembea barabarani kwa sababu za msingi. Aidha, baada ya taratibu zote kukamilika, mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hii yataletwa Bungeni ili kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa kadri itakavyoonekana inafaa.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inasema kuwa idadi ya watu katika Jimbo la Lindi Mjini ni takribani 78,000, lakini takwimu za watu waliojiandikisha NIDA inafika 100,000 na sensa iliyofanywa kupitia Serikali za Mitaa inaonyesha kuwa wakazi wa Lindi Mjini ni zaidi ya 200,000 na Serikali inaendelea kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kutumia takwimu za watu 78,000 hivyo kuathiri huduma stahiki za maendeleo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuangalia upya takwimu hizo ili wananchi wa Lindi Mjini wapelekewe huduma za maendeleo stahiki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya watu kwa Manispaa ya Lindi (Jimbo la Lindi Mjini) ilikuwa ni watu wapatao 78,841. Kwa madhumuni ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, eneo la Manispaa ya Lindi ni lile linalojumuisha kata 18 za Ndoro, Makonde, Mikumbi, Mitandi, Rahaleo, Mwenge, Matopeni, Wailes, Nachingwea, Rasbura, Matanda, Jamhuru, Msinjahili, Mingoyo, Ng’apa, Tandangongoro, Chikonji na Mbanja. Hivyo basi, tunapozungumzia idadi ya watu 78,841 tuna maana ya idadi ya watu katika kata nilizozitaja hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilitoa makadirio ya idadi ya wapiga kura kwa kila jimbo hapa nchini. Katika makadirio hayo, Jimbo la Lindi Mjini linakadiriwa kuwa na wapiga kura 47,356. Katika zoezi hilo hilo la uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi nayo ilikadiriwa kuwa Jimbo la Lindi Mjini lina wapiga kura wapatao 42,620. Makadirio haya yalizingatia idadi ya watu kwa Lindi Mjini kama ilivyotolewa na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura, Jimbo la Lindi lilionyesha kuwa na wapiga kura 48,850 idadi ambayo ni karibu sawa na ile iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Matokeo haya yanadhihirisha usahihi wa takwimu za sense zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya watu wapatao 100,000 waliojiandikisha NIDA ni kwa Wilaya nzima ya Lindi, ambayo inajumuisha Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na sio Manispaa ya Lindi au Jimbo la Lindi Mjini pekee kama ilivyohojiwa katika swali la msingi la Mheshimiwa Hassan Kaunje.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Matumizi ya dola katika maeneo mengi nchini ndiyo sababu kubwa ya kushuka kwa thamani ya fedha yetu:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha matumizi ya fedha yetu kwa wananchi wake pamoja na wageni nchini ili kukuza thamani ya fedha yetu na maendeleo ya nchi kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakari, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sarafu ya shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo hapa nchini na hakuna sarafu nyingine yoyote iliyowahi kuidhinishwa kisheria kutumika kwa malipo hapa nchini badala ya shilingi. Hakuna sababu ya kuhamasisha matumizi ya shilingi kwa sababu Watanzania wote wanajua fedha halali kwa malipo ni shilingi na si vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanyika mwaka 2013 ulionesha kuwa, malipo ambayo hufanyika kwa dola ya Marekani hapa Tanzania ni asilimia 0.1 tu ya malipo yote na haya hufanyika zaidi katika maeneo yanayohusisha wageni kama vile mahoteli ya kitalii, mashirika ya ndege, shule za kimataifa na nyumba za kupanga kwenye baadhi ya maeneo mijini. Sababu mojawapo ya maeneo haya kuwa na bei kwa dola ya Kimarekani ni kurahisisha uelewa wa bei hizo kwa wageni na kuwarahisishia malipo. Pamoja na mambo mengine malipo kwa fedha za kigeni yanachangia upatikanaji wa fedha za kigeni hususani pale wazawa wanapouza bidhaa na huduma kwa wageni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya dola nchini Tanzania siyo sababu kuu ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu. Mfano, wakati Tanzania haijafanya mabadiliko yoyote katika kanuni ya fedha za kigeni tangu mwaka 1992 thamani ya shilingi ilikuwa ikishuka na kupanda kama zilivyo thamani za sarafu nyingine duniani. Aidha, kutokea mwezi Desemba, 2011 hadi Desemba, 2014 thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilikuwa imara zaidi ya sarafu nyingine za washirika wetu kibiashara kama vile Rand ya Afrika ya Kusini, Yen ya Japan, Euro ya Jumuiya ya Ulaya na Paundi ya Uingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kuu zinazopelekea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni ni tofauti ya mfumuko wa bei kati ya Tanzania na nchi tunazofanya nazo biashara. Nakisi ya biashara ya nje ya bidhaa na huduma ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na mabadiliko ya mara kwa mara ya kiuchumi duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kanuni zilizotokana na sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 na tamko la Serikali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni la mwaka 2007, sarafu ya shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo. Aidha, Benki Kuu ikishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza usimamizi katika maduka ya fedha za kigeni ambapo miamala yote ya fedha za kigeni inatakiwa kuoneshwa. Pia, Benki Kuu imechukua hatua za kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa na mabenki ni kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, kidiplomasia na kijamii pekee.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Moja kati ya jukumu la Benki Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 51(2)(a) cha Sheria ya Benki Kuu, 2016 ni kutunza dhahabu safi.
Je, kwa nini Serikali imekataa kutunza dhahabu safi katika Benki Kuu wakati Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha dhahabu safi na kwa wingi Afrika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuwa na utulivu wa bei kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa. Ili kufanikisha azma hii, Benki Kuu inadhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali zikiwemo kuuza dhamana na hati fungani za Serikali na kushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki ambayo ni Interbank Foreign Exchange Market.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu lake la msingi, Benki Kuu hutunza hazina ya rasilimali za kigeni zinazotosha kuagiza bidhaa nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne. Hazina ya rasilimali za kigeni inaweza kuwa dhahabu-fedha yaani monetary gold au fedha za kigeni. Uamuzi kuhusu hazina itunzwe vipi unazingatia vigezo mbalimbali vikiwemo vile vya kudumisha thamani, wepesi wa kubadilisha yaani convertibility na faida inayopatikana kwa kuwekeza hazina hiyo.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu kwa muda mrefu haijaweka dhahabu kama sehemu ya hazina ya rasilimali za kigeni kutokana na bei ya dhahabu katika soko la dunia kutokuwa tulivu na hivyo kusababisha uwezekano wa kupunguza thamani ya hazina ya rasilimali ya nchi. Mfano, tumeshuhudia bei ya dhahabu ikishuka kutoka dola 1,745 za Kimarekani kwa wakia moja Septemba, 2012 hadi dola za Kimarekani 1,068 Disemba 2015. Aidha, ununuzi na uuzaji wa dhahabu unahitaji ujuzi maalum ambapo kwa kuzingatia jukumu la msingi la Benki Kuu ambalo tumelieleza hapo juu, Benki Kuu haijajijengea uwezo katika eneo la biashara ya dhahabu.
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
Riba kubwa katika benki zetu nchini imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake na vijana kupata mikopo.
(a) Je, Serikali ipo tayari kuandaa utaratibu maalum wa riba elekezi itakayowawezesha wanawake na vijana kupata mikopo benki kwa riba nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuziagiza benki za biashara kulegeza masharti ya dhamana kwa vijana na wanawake ambayo yanarefusha mchakato wa upatikanaji wa mikopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye kipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mabenki na Taasisi za Fedha nchini ya mwaka 1991, Serikali iliruhusu benki binafsi kutoa huduma za kibenki hapa nchini kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo huduma hizo zilikuwa zinatolewa na vyombo vya fedha vya Serikali tu. Hatua hii ilikusudia kuongeza ushindani katika sekta ya fedha na kuhakikisha kwamba huduma za kibenki zinatolewa kwa ufanisi na kwa kutegemea nguvu na mfumo wa soko huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maombi mbalimbali juu ya kupunguza viwango vya riba ikiwa ni pamoja na Benki Kuu kuweka ukomo wa riba au riba elekezi ya mikopo. Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, Benki Kuu imepewa dhamana ya kusimamia sekta ya fedha na usimamizi wa mabenki hapa nchini. Kama msimamizi wa mabenki, Benki Kuu kuweka ukomo wa riba sio tu inapingana na jukumu lake la msingi la kusimamia mabenki hayo, bali pia inapingana na mfumo wa uchumi wa soko huria. Kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, Benki Kuu haina mamlaka kisheria ya kuweka ukomo au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya riba katika mabenki na taasisi nyingine za kifedha hupangwa kwa kutegemea nguvu ya soko, sifa za mkopaji, ushindani katika soko, gharama za upatikanaji wa fedha, mwenendo wa riba za dhamana za Serikali, gharama za uendeshaji na matarajio ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Benki Kuu imeendelea na jukumu lake la msingi la kuhakikisha kuwa mfumo huu unaendeshwa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ili kulinda maslahi ya Taifa na uchumi kwa kusimamia na kudhibiti mambo yafuatayo:-
(i) Kuhakikisha kuwa ingezeko la ujazi wa fedha linaenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko kuhakikisha kuwa ongezeko la ujazi wa fedha linaenda sambamba na mahitaji halisi ya uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei;
(ii) Ongezeko la mikopo ya mabenki haliathiri uzalishaji mali na linalingana na malengo ya ujazi wa fedha;
(iii) Soko la dhamana za Serikali linaendeshwa kwa ufanisi ili liweze kutoa riba elekezi kulingana na hali ya soko na uchumi kwa ujumla; na
(iv) Mwisho kuhimiza mabenki na taasisi zote za fedha kutumia takwimu za Credit Reference Bureau.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Kituo cha Biashara cha Taifa - Tanzania Trade Center kilichopo London, Uingereza kimeripotiwa kuwa kinakabiliwa na uhaba wa fedha za kukiendesha na kulipa watumishi wake kutokana na kukosa fedha kutoka Hazina jambo ambalo linasababisha kuzorota kwa kazi za kituo hicho na kukabiliwa na mzigo mzito wa madeni.
(a) Je, Serikali inaweza kueleza hali ya kituo hicho kwa sasa ikoje?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hali ya kifedha na kiutendaji ya kituo hicho ambacho kimesaidia sana kutangaza Tanzania nje ya nchi inakuwa imara na kufanya kazi zake kwa ufanisi?
(c)Je, ni kiasi gani cha fedha kinachodaiwa na kituo hicho na watu mbalimbali nchini Uingereza na hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Biashara cha London kilianzishwa mwezi Oktoba, 1989 kufuatia uamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais mwaka 1989. Lengo la kituo hicho lilikuwa ni kuhamasisha biashara baina ya Tanzania na nchi za Ulaya, hususan Uingereza kwa kutangaza fursa za biashara na uwekezaji na kuvutia wawekezaji kutoka Tanzania na Ulaya kuchangamkia fursa hizo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwake kituo kimefanikiwa sana katika kutekeleza majukumu yake licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zitokanazo na ufinyu wa bajeti na upungufu wa rasilimali watu. Changamoto hizo zimefanya kituo hicho kushindwa kuendana na kasi inayotakiwa ya mabadiliko duniani yanayotokana na matumizi ya teknolojia katika mifumo ya uenezaji wa taarifa na habari ulimwenguni. Ili kulinda heshima ya Taifa na watumishi waliokuwepo katika kituo hicho, Serikali imeamua kukifunga rasmi kituo hicho na kuhamisha majukumu yake kutekelezwa na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Mjini London.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kituo kimefungwa na majukumu yake kutekelezwa na Ofisi yetu ya Ubalozi Mjini London, Serikali itaangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya Ubalozi wetu ili kukidhi majukumu ya ziada yaliyoongezeka.
(d) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Novemba, 2016 Wizara ilipokea na kulipa deni la jumla ya shilingi 129,896,360 kutoka kituo hicho cha London ikiwa ni madai ya pango, maji, simu, umeme na gharama za kufunga kituo hicho.
MHE. ENG.ATASHASTA J.NDITIYE aliuliza:-
Nchi yetu bado ina upungufu mkubwa sana wa sukari na kwa kuwa Wilayani Kibondo kuna ardhi oevu kwenye Bonde la Mto Malagarasi na Lupungu ipatayo ekari 52,000 na wananchi wako tayari kutoa ushirikiano kwa matumizi ya ardhi hiyo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta mwekezaji wa kiwanda cha sukari katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kuwa katika Nchi yetu kuna upungufu wa sukari kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge. Viwanda vyetu vyote kwa pamoja vina uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari ya mezani na hakuna uzalishaji wa sukari ya viwandani ilihali mahitahi ya Sukari kwa matumizi ya nyumbani na viwandani ikikadiriwa kuwa tani 610,000 hivyo uhitaji wa uwekezaji katika sekta hiyo ya viwanda vya sukari ni mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa upungufu huo, Serikali imeshatambua na inaendelea kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Mara, Pwani, Songwe na Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Bonde la Mto Malagarasi lililopita katika vijiji kumi vya Kasaya, Kibuye, Kigina, Kukinama, Kumsenga, Kumshwabure, Magarama, Nyakasanda, Nyalulanga na Nyarugusu ni moja ya maeneo ambayo Serikali imeyaainisha kwa ajili ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari. Tayari Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwa kushirikiana na Wananchi na Kampuni ya Green Field Plantations imefanya vikao vya uhamasishaji katika vijiji vyote kumi na hivi karibuni wataanza taratibu za upimaji wa ardhi. Mradi huu utahusisha jumla ya hekta 25,000 sawa na ekari 61,776 ambapo Kampuni ya Green Field Plantations italima hekta 20,000 na itawasaidia wakulima wadogo pembejeo na teknolojia ili waweze kulima hekta 5,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimshukuru Mheshimiwa Mbunge na Mkuu wa Wilaya ya Kibongo kwani barua walizotuma Wizarani ziliongeza kasi hii, tuendelee kushirikiana.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:-
Miradi mingi ya maendeleo inashindwa kumalizika kwa wakati kutokana
na Serikali Kuu kutokuleta fedha za miradi kwa wakati:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa wakati kwenye Halmashauri ili miradi
ya maendeleo itekelezwe kwa kipindi kilichopangwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suzana Chogisasi Mgonukulima, Mbunge
wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa
kutumia fedha za makusanyo ya ndani, mikopo ya ndani na nje, misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo pamoja na makusanyo ya Mamlaka ya Serikali za
Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapato ya fedha za ndani (tax revenues and
non tax revenues) hupelekwa katika Wizara, taasisi na idara mbalimbali za Serikali
pamoja na Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kulingana na upatikanaji wa fedha kutoka
katika kila chanzo. Aidha, asilimia 60 ya makusanyo ya Mamlaka ya Serikali za
Mitaa hubakishwa katika Halmashauri husika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha
za mikopo ya ndani au nje, pamoja na fedha za washirika wa maendeleo, fedha
hizo hupelekwa kwenye Halmashauri zetu mara tu zinapopatikana. Hivyo basi,
uhakika wa mtiririko wa fedha kutoka vyanzo vyote vya mapato ndiyo msingi wa
kupeleka fedha kwenye Halmashauri zetu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wetu Waheshimiwa Wabunge
kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani katika Halmashauri zetu kupanga
mipango stahiki, kuainisha vyanzo vya mapato na kusimamia ukusanyaji na
matumizi ya mapato hayo ipasavyo ili kuziwezesha Halmashauri zetu kujenga
uwezo wa kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hivyo
kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali isidhibiti matumizi holela ya dola nchini ili kupunguza
utakatishaji wa fedha na kuimarisha ukuaji wa uchumi kama zinavyofanya nchi
nyingi duniani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa
Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti matumizi holela ya fedha za
kigeni, Benki Kuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza
usimamizi katika maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambapo taarifa za kila
muamala wa fedha za kigeni unaofanywa zinapaswa kuoneshwa. Hatua
zimechukuliwa pia kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa
na mabenki ni ile inayohusu shughuli za kiuchumi tu ili kulinda thamani ya shilingi
yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tamko na mwongozo uliotolewa na
Serikali mwaka 2007, ulieleza kuwa bidhaa na huduma zinazowalenga watalii au
wateja wasio wakazi wa Tanzania, bei zake zinaweza kunukuliwa kwa sarafu mbili
yaani shilingi ya kitanzania na sarafu ya kigeni na malipo kufanyika kwa sarafu
ambayo mlipaji atakuwa nayo. Pia, mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe
kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa kuruhusu soko huru la fedha za kigeni
hapa nchini ni hatua ya makusudi ambayo ilichukuliwa na Serikali yetu ili
kuiwezesha nchi kuondokana na hali ya kuadimika kwa fedha za kigeni. Mfano,
kufikia Desemba, 2015 akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Kimarekani milioni
4,093.7 wakati amana za fedha za kigeni za wakazi wa Tanzania zilikuwa dola za
Kimarekani milioni 2,933.1 na rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi
cha dola za Kimarekani milioni 1,021.1.
Mheshimiwa Naibu Spika, utulivu wa urari wa biashara ya nje umetokana
na sera huru ya fedha za kigeni ambayo imechangia kuimarisha uchumi kwa
zaidi ya miaka 10 iliyopita. Wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita ulikuwa ni asilimia saba ikiwa ni wastani wa juu sana
ikilinganishwa na nchi zingine duniani. Mfano, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 5.4 katika kipindi hicho, wakati
ule wa nchi zinazoibukia kiuchumi ulikuwa ni asilimia 5.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia zinazotumika kutakatisha fedha ni pamoja
na kuziingiza fedha haramu kwenye taasisi za fedha na kuziwekeza katika
rasilimali halali kama ardhi na nyumba. Baadhi ya mambo yanayowapatia
wahalifu fedha haramu ni pamoja na biashara ya dawa za kulevya, rushwa,
ujangili, ujambazi, ukwepaji kodi na kadhalika. Fedha zinazotokana na shughuli
za kihalifu zinaweza kuwa shilingi za Kitanzania, dola za Kimarekani au fedha
nyingine yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kanuni ambazo zinafuatwa na vyombo vya
fedha ili kuzuia utakatishaji wa fedha zote zilizopatikana kutoka vyanzo haramu
na siyo dola tu. Benki Kuu kupitia jukumu la usimamizi wa taasisi za fedha
hufuatilia mabenki ili kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinafuatwa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Kuna ongezeko kubwa la maduka ya kucheza kamari yanayotaitwa Jack Pot katika miji nchini ikiwemo Dodoma; maduka hayo huchezesha kamari mchana na usiku na wateja wengi ni vijana ambao hutumia mbinu mbalimbali kupata fedha ndani ya familia ili wakacheze kamari hali ambayo husababisha uvunjifu wa maadili:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mchezo wa kamari ambao huwakosesha amani wazazi na jamii nzima?
(b) Je, Serikali haoni kuwa kuna uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya vijana inapotea kwa kucheza kamari badala ya kushiriki katika uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo yote ya kubahatisha ikiwemo kamari inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Namba 4 ya mwaka 2003, Sura 41 pamoja na kanuni zake. Kwa mujibu wa sheria, hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendesha biashara ya michezo ya kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na vibali vingine vinavyotolewa na mamlaka zingine za biashara. Pia, sheria inakataza watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote atakayeruhusu mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la mchezo wa kubahatisha anahesabika kufanya kosa na anastahili kulipa faini ya sh. 500,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja. Aidha, endapo kosa hili litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi ina mamlaka kisheria ya kumfutia leseni. Hivyo basi, wajibu wa Serikali ni kuzuia watoto na vijana walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha. Hata hivyo, natoa rai kwa wazazi na walezi kuwazuia vijana wao kucheza michezo ya kubahatisha pale wanapoona kuwa uchezaji wao unakuwa na matokeo hasi.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ya kubahatisha ni moja ya shughuli za kiuchumi inayoendeshwa kwa mujibu wa sheria kama shughuli nyingine zozote. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa, wote wanaoendesha michezo ya kubahatisha wanazingatia sheria na kanuni zilizowekwa. Pili, ni wajibu wetu kama wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa vijana wetu wanazingatia mila na desturi zinazolinda maadili ya Kitanzania pindi wanapokuwa wanajishughulisha na shughuli halali za kiuchumi.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya wananchi, watumishi wa umma na wafanyabiashara juu ya riba kubwa inayotozwa na benki zetu kwa wale wanaochukua mikopo hali ambayo inarudisha nyuma juhudi zao za kupunguza umaskini na kwa kuwa Benki Kuu ndiyo inayosimamia mabenki yote nchini.
(a) Je, ni lini Serikali kwa kupitia benki zetu nchini itaweka utaratibu wa kupunguza riba ya mikopo walau kufikia 10% -12% badala ya riba ya sasa ambayo ni 17% - 20%?
(b) Kwa kuwa mikopo inayotolewa kwa watumishi wa umma ni salama zaidi kwa mabenki, je, benki hizo haziwezi kuweka riba maalum?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na gharama zingine za huduma za kibenki. Viwango vya riba za mikopo na riba za amana, pamoja na riba za mikopo kati ya benki na benki hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, gharama za uendeshaji, riba za dhamana za Serikali, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo, pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, Serikali haina mamlaka kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha hatari ya kutolipa mkopo ni miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa na mabenki katika kupanga viwango vya riba za mikopo. Aidha, kwa sehemu kubwa gharama za riba za mikopo hutegemea zaidi gharama za upatikanaji wa fedha pamoja na gharama za uendeshaji.
Pili, ni muhimu kutambua kwamba kadri riba za mikopo zinapokuwa juu, ndivyo riba za amana zinapokuwa juu pia. Mfano; wastani wa riba za kukopa kwa mwaka mmoja mwezi Juni, 2016 ulikuwa ni asilimia 13.67 wakati wastani wa riba za amana za mwaka mmoja ulikuwa ni asilimia 11.52 ikiwa ni tofauti ya asilimia 2.25
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu yanayotolewa na wachongaji wa vinyago hasa pale wanunuzi wa vinyago hivyo kutoka nje wanaponyang’anywa bidhaa hiyo wafikapo airport kwa madai mbalimbali ikiwemo kutolipa kodi.
(a) Je, vinyago hivyo ambavyo ni biashara ya wanyonge baada ya kuzuiliwa hupelekwa wapi?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kufanya hivyo kunawapotezea wateja na soko kwa wanaofanya ujasiriamali wa aina hiyo lakini pia kuwaingizia hasara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, vinyago sio miongoni mwa bidhaa zinazotozwa kodi au ushuru kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi. Ikiwa vinyago vilizuiliwa uwanja wa ndege au mpakani, sio kwa sababu ya kutolipiwa kodi au ushuru wa forodha. Utaratibu unaotumika kimataifa ikiwemo nchi yetu katika kushughulikia bidhaa zozote zinazokamatwa kwenye sehemu za kuingia au kutokea nje ya nchi kama viwanja vya ndege na mipakani ni wa aina mbili:-
Moja, kuziharibu au kuziteketeza bidhaa hizo au kuzipiga mnada. Bidhaa zinazoharibiwa au kuteketezwa ni zile ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi au kwa afya ya binadamu, kwa mfano, silaha, vyakula au kemikali zilizobainika kuwa si rafiki kwa matumizi ya binadamu na mazingira. Bidhaa nyingine ambazo haziangukii kwenye kundi hilo, ikiwa ni pamoja na vinyago hupigwa mnada na baada ya kuondoa gharama zozote za uhifadhi, mapato yake huingizwa Serikalini. Kwa kuwa swali la Mheshimiwa Tauhida halijabainisha ni lini na ni wapi vinyago hivyo vilikamatwa, idadi yake au taasisi au mamlaka ipi ilikamata vinyago hivyo ni vigumu kueleza vinyango hivyo vilipelekwa wapi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia vinyago au bidhaa nyingine yoyote inaposafirishwa nje ya nchi, hufanyika tu baada ya kubainika kuwa kuna ukiukwaji wa sheria na kanuni. Kwa hiyo, lengo la kufanya hivyo ni kujiridhisha kuwa wadau wote wa biashara au bidhaa hiyo wanafuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili asiwepo yeyote mwenye kupoteza mapato yanayotokana na biashara au bidhaa hiyo ikiwemo Serikali yetu.