Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji (1 total)

MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itaelekeza kwa wananchi maamuzi ya Timu ya Mawaziri iliyozunguka kwenye maeneo yenye migogoro kati ya wananchi na mapori ya hifadhi?

(b) Je, ni lini Serikali kwa kushirikiana na wananchi itaweka mipaka kati ya mapori ya hifadhi na vijiji vinavyoyazunguka ili kupunguza migogoro iliyopo na kuwezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi bila usumbufu?
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Kondoa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Serikali imeandaa mpango kazi kwa ajili ya kuwaeleza wananchi juu ya uamuzi wa Serikali kuhusu migogoro kati ya wananchi na hifadhi. Katika kutekeleza mpango kazi huo, timu ya Mawaziri wa Kisekta itapita katika mikoa husika kwa lengo la kutoa elimu na ufafanuzi kwa viongozi wa mikoa pamoja na wilaya.

Zoezi hilo litaenda sambamba na timu ya watalaam itakayojumuisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Uongozi wa Mikoa, Wilaya na Vijiji.

(b) Mheshimiwa Spika, zoezi la uwekaji wa mipaka kwenye maeneo yote yenye migogoro litafanywa na timu ya wataalam kutoka katika sekta za Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maliasili na Utalii. Timu hii, itapita katika maeneo yote ili kufanya tathmini, uhakiki na kuweka mipaka kulingana na uamuzi wa Serikali. Aidha, katika zoezi hilo wananchi watashirikishwa ili kuondoa uwezekano wa kujitokeza migogoro mingine. Ahsante.