Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji (57 total)

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni aibu na fedheha kwa Serikali kwa jinsi ilivyowatelekeza wastaafu wake. Ukiangalia nchi ya Kenya na Rwanda, wastaafu wana hali nzuri. Serikali mmepandisha pensheni kutoka shilingi 50,000/= mpaka shilingi 100,000/=, wastani wa shilingi 3,300/= kwa siku, fedha ambayo hata chai haitoshi! Serikali inasemaje sasa? Kuna mkakati wa ziada angalau kuwaongezea pensheni wastaafu kwa shilingi 250,000/= kwa mwezi? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, kwa mujibu wa Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, miaka kadhaa, miaka mbalimbali, imekuwa ikiripoti kupunjwa, kudhulumiwa kwa mafao ya wastaafu na Serikali imekuwa ikisema kwamba wataalamu wake ndio wanaokosea. Tunataka tuelewe, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuweza kutoa mafao stahiki kwa wastaafu wetu?
Pale ambapo wastaafu wanafariki, Serikali imekuwa ikitoa risala za kutoa machozi na kulia, uwongo mtupu! Tabia hii mbaya lini mtaacha? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba niseme, siyo sahihi kwamba imekuwa ni fedheha kwa Serikali. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi ni kwamba tumekuwa tukiongeza kiwango hiki cha pensheni kwa wastaafu kulingana na uchumi unavyoimarika na tumekuwa tukiliangalia kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa wazi wa kuongeza shilingi 250,000/= kwa mwezi kama pensheni; kama nilivyosema mwanzo, tunaangalia kiwango cha uchumi wetu, uchumi utakakaa vizuri kuturuhusu kulipa shilingi 250,000/= tutalipa hiyo shilingi 250,000/=.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mkakati wa kutoa mafao sahihi kwa wastaafu kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge katika swali lake la pili; naendelea kusisitiza kwamba uchumi utakapokuwa umeimarika vizuri; na kama mlivyoona kwa speed ya Serikali ya Awamu ya Tano, tunakusanya mapato kwa kiasi kikubwa na tunatarajia kuongeza tax base ya kukusanya kodi ambayo tunazingatia. Moja ya watu wa kuwaangalia ni Wastaafu wetu, wamelitumikia Taifa na tuna uhakika tutaweza kuwahudumia. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, ulipaji wa kodi ili kuiwezesha Serikali kuweza kutoa huduma nzuri kwa wananchi ni wajibu wa kila raia wa nchi hii na kwa kuwa kumekuwa na matatizo mengi katika mfumo wa ulipaji wa kodi katika Serikali Kuu na Halmashauri, kodi usumbufu mkubwa kwa walipa kodi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mfumo wa ulipaji kodi ili uwe wazi zaidi na kuwawezesha wananchi kuweza kulipa kodi zile zinazotakiwa kulipwa?
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa wananchi wengi hawajui umuhimu wa kulipa kodi, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi na hasa walipa kodi ili waweze kuzijua aina zote za kodi na kuweza kulipa kama inavyotakiwa.ambazo zimekuwa zikileta
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza mpango gani wa kurekebisha mfumo wa ulipaji kodi. Sasa hivi kama mlivyoona na kwa kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya „SASA KAZI TU‟ tumeimarisha mfumo wa ulipaji kodi kuanzia katika ngazi ya Taifa mpaka Halmashauri zetu na mmeona jinsi ambavyo sasa tunaweza kukusanya kodi kwa kiasi kikubwa.
Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuimarisha na Mamlaka yetu ya Mapato Tanzania imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba hilo linafanyika katika ngazi ambayo wanafanyia kazi wao na pia mpaka Halmashauri zetu kule wanakokusanya uimarishaji wa ukusanyaji kodi utakuwa wazi kabisa na kila mmoja ndani ya Halmashauri mwenye jukumu hilo anayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu kutoa elimu, mpaka sasa hivi tayari tuna kitengo cha utoaji elimu ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na elimu hii huwa inatolewa moja kwa moja kupitia televisheni zetu mbalimbali tuna vipindi ndani ya wiki na pia utoaji huu wa elimu ya kodi pia hufanywa kwa semina mbalimbali na warsha zinazofanywa na watoa elimu wetu kutoka Mamlaka ya Kodi Tanzania.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali imebaki katika kuweka mazingira mazuri, lakini naona kwamba mazingira mazuri hayo si kweli sana kwa sababu hayaonekani maana wananchi wanalalamika sana. Kwa sababu ukienda Bureau de Change hii ina rate hii, ukienda Bureau de Change nyingine ina rate tofauti na zimetapakaa sehemu zote kama sisimizi. Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha rates hizo zinalingana? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kuwa Serikali imejitoa katika biashara hii ya kumiliki Bureau de Change lakini huo ulikuwa ni uamuzi wa zamani na tujue kwamba sasa hivi dunia imebadilika, ni dunia ya sasa. Je, atakubaliana nami kwamba sasa umefika wakati wa Serikali kumiliki huduma hii ili kuwaondolea wananchi wake matatizo ambayo wanakabaliana nayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru kwa kuuliza maswali mazuri ya nyongeza ambayo yanakidhi haja na yanaakisi kinachoendelea katika maduka yetu ya kubadilisha fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu la swali lake la kwanza kwamba rates ni tofauti sana kutoka duka moja kwenda duka lingine, nakubaliana naye na hii yote ni kuonesha kwamba tuko ndani ya soko huria na kila mtu anatakiwa ku-charge anavyoona inafaa. Pia kiuchumi, sisi wachumi tunafahamu kwamba bei ya bidhaa yoyote ile hutegemea na demand na supply. Kwa hiyo, kama demand ya bidhaa hiyo ni kubwa bei zitakuwa tofauti kutoka kwa muuzaji mmoja kwenda kwa muuzaji mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Serikali iweze kurudi kwenye kuendesha biashara kama hizi na kwamba huo ulikuwa ni uamuzi wa zamani, naamini uamuzi ule ulikuwa ni sahihi na bora. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba tangu mwaka 1991 Serikali ilishajitoa kuendesha mabenki haya. Tunaendelea kusisitiza, sisi kama Serikali tutaendelea kutunga sera na sheria mbalimbali za kusimamia maduka haya ili yaweze kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wetu.
MHE. CONCHESTER L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Msingi wa swali langu ni malalamiko ya wastaafu wanaopokea pensheni kwamba hawajawahi kuongezewa fedha hizi. Kwa kuwa kuna malalamiko hayo na kwa kuwa Serikali sasa imetoa tangazo hili kupitia swali langu, je, inasema nini kuhusu wale wastaafu ambao hawajalipwa kiwango hicho kipya na wanaelekezwa vipi namna ya kudai fedha zao hizo pamoja na arrears? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Rwamlaza. Alichokisema na Serikali inafahamu kipo, lakini naomba niseme yafuatayo:-
Katika ongezeko hili ni Mfuko wa PSPF pekee ambao umeweza kulipa sh. 100,000 kwa mwezi mpaka leo. Mifuko mingine iliyobaki kwa mujibu wa vifungu vya 25 na 36 vya Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya mwaka 2008 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2012, kima cha chini cha pensheni kwa mifuko yote inatakiwa kupandishwa na Mamlaka hii ya SSRA. Kwa sasa Mamlaka hii inamalizia kufanya actuarial valuation kwa Mifuko yote hii na Bodi za Mifuko hii pia zipo katika mchakato baada ya actuarial valuation kukamilika ili waweze kuanza kulipa rasmi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kulipa arrears zao, wastaafu wote watalipwa arrears zao baada ya actuarial valuation kukamilika na Bodi za Mifuko hii kukamilisha mchakato huu kuanzia Julai 2015. Kwa hiyo, wasiwe na wasiwasi watalipwa arrears zao zote.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Pamoja na majibu ma… yasiyoridhisha sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwa na malalamiko mengi sana ya hawa wastaafu. Mmetutangazia kwamba hapa kazi tu, unaweza ukatuambia ni lini hawa wastaafu watapewa hizo hela kwa sababu sasa ni muda mrefu umepita? Tunataka tupate muda kwa sababu kwa kweli wanakuja kwenye maofisi yetu na wanatusumbua. Naibu Waziri ametangaza kwamba wamelipwa lakini hawajalipwa wakati waliahidiwa? Ni lini sasa Serikali hii ambayo inasema hapa kazi itatoa hizo pesa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Peter Msigwa kwa swali zuri lakini kwa kukiri japo ameishia njiani kwamba kwa majibu yangu mazuri, nakushukuru sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimesema kwamba bodi hizi zinaendelea na mchakato ili waweze kutangaza baada ya SSRA kumalizia actuarial valuation. Leo hii mchana nitakuwa na kikao na Mkurugenzi Mkuu wa SSRA kuhusu suala hili. Naomba niwaahidi wastaafu hawa kwamba pale tu tutakapomaliza, Serikali imeshaji-commit kwamba tutalipa malipo yao yote kuanzia Julai 2015.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu yaliyotolewa na Wizara ambayo hayakidhi viwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wastaafu zaidi ya idadi iliyotolewa na hasa walimu, hata Jimboni kwangu Buyungu idadi kubwa ya walimu waliostaafu inaweza ikaakisi idadi ya watumishi walistaafu katika nchi hii. Sababu zilizotolewa za wastaafu hao kutolipwa moja kubwa ni kukosa fedha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo Serikali haijataja.
Swali la kwanza, naomba Serikali ikiri ni lini italipa wastaafu wote kwa kupeleka fedha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili wasiendelee kuteseka sambamba na kuwarudisha nyumbani kwao mara baada ya kustaafu? (Makofi)
Swali la pili, wapo wastaafu wa aina mbili, wapo wanaolipwa pensheni na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na wapo wanaolipwa pensheni na Hazina. Wale wa Mifuko wa Hifadhi ya Jamii wanapata monthly pension wale wahazina wanalipwa kwa miezi mitatu (quaterly pension) hali hii inawasumbua na kuwatesa wastaafu wetu. Naomba wastaafu wote walipwe monthly pension kama ilivyo kwenye mkataba wa kazi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naomba uulize swali, naona unaleta ombi.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Swali la pili dogo, ni lini Serikali itaanza kuwalipa wastaafu wote pensheni ya kila mwezi badala ya miezi mitatu? Ahsante!
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumhakikishia data nilizompatia ni za kweli na za uhakika, kwa hiyo naomba aamini hao ndiyo wastaafu ambao tunajua wamestaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili sababu nilizozitaja ndizo zinazosababisha wastaafu hao wachelewe kulipwa siyo upelekaji wa fedha. Serikali imekuwa ikipeleka fedha kwenye Mifuko hii ili waweze kulipwa wastaafu hawa na hizi sababu nilizozileta ndizo ambazo tunazifahamu kama Serikali na Mifuko yote imeendelea kupokea fedha kutoka Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, wastaafu wanaolipwa Hazina kulipwa kwa miezi mitatu mitatu. Naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba uamuzi wa Serikali kuelekea kulipa miezi mitatu mitatu lilifikiwa baada ya maombi ya wastaafu hawa kuomba walipwe miezi mitatu mitatu. Kama itaonekana sasa wataomba tena walipwe mwezi moja moja, Serikali haioni ugumu wowote kurejea kule tulikotoka.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wastaafu ambao wanapitia Mfuko PSPF hivi karibuni Serikali iliongeza kiwango, lakini wastaafu hawa wanakuwa hawalipwi kwa wakati na kwa kiwango ambacho Serikali ilitangaza.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kuwalipa wastaafu hawa kwa kiwango sahihi na kwa wakati muafaka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu tatizo hili lilkuwepo PSPF, lakini kuanzia Disemba 2015 mpaka leo wastaafu hao wamekuwa wakilipwa pesa zao inavyostahili. Kuanzia Disemba hiyo tumeanza kulipa hao wastaafu shilingi 100,000/= kama ambavyo Serikali iliongeza kiwango hiki kupitia Mfuko wa PSPF na arrears zao mpaka kufikia mwisho wa mwezi huu wa nne wote watakuwa wamelipwa zile arrears za kutoka Julai hadi Disemba.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshmiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekuwa na tabia tata ya kuchukua fedha kwenye Mashirika ya Umma kama NSSF, LAPF na Mashirika mengine na kutokuzirudisha kwa wakati, ama kuwekeza katika miradi mfu kama mradi wa Machinga Complex na miradi mingine ambayo imekuwa haina tija Serikalini.
Ni lini Serikali itakoma mchezo huu wa kuchukua fedha ambazo zinawaathiri wachangiaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imekuwa ikichukua fedha na hii ikifuata taratibu zote na Mifuko hii kuingia katika Mikataba ili Mifuko hii iweze kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itasitisha utaratibu huu, siamini sana kwamba ni sahihi sana Serikali kusitisha, kama Mifuko inaweza kuwekeza na wakaingia katika mikataba ambayo tunaita ni Win Win Situation kati ya Serikali na Mifuko naamini ni sehemu nzuri ya uwekezaji kwa mifuko yetu hii. Kwa hiyo, naomba tuendele kufanya hivyo.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:
(a) Kwa vile Naibu Waziri ameeleza kwamba kuna database maalum ambayo TRA wanayo na kule Zanzibar inatumika, je, huu mfumo una tatizo gani, kwa sababu mizigo yote ambayo inapitia Zanzibar kuja Bara asilimia 100 ya mizigo ile inatozwa kodi inapoingia Tanzania Bara, wakati sheria inayotumika ni hiyo moja, na mamlaka ambayo inasimamia kodi na Kamishna ni huyo huyo mmoja?
(b) Mheshimiwa Naibu Waziri, alieleza katika jibu lake kwamba endapo vitu vinatoka Zanzibar kuja Bara wanaagalia tozo la awali ambalo lilitozwa Zanzibar na kuangalia ile tofauti ambayo kwa mujibu wa database zao wanam-charge yule mtu. Sasa je, kwa mtu ambaye ana tv moja anapopita bandarini pale kutokea Zanzibar hana entry…
NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali Mheshimiwa Jamal,
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Ahsante Mheshimiwa NAibu Spika, je, mtu ambaye kwa vitu ambavyo ni item moja moja kama tvna redio anapotoka Zanzibar kuja Bara wanatumia mfumo gani wa kukokotoa hiyo kodi?
NAIBU WAZIRI WA FEHDA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kodi inazotozwa kwa bidhaa zinazotika Zanzibar kuja huku kwetu, kwanza naomba nisahihishe, mfumo huu wa Import Export Commodity Database unaotumika Tanzania Bara kule Zanzibar hautumiki. Ndiyo maana inaonekana kule ambako hawatumii mfumo huu, bidhaa kule tathmini inapofanyika mara nyingi huonekana ipo chini ya thamani ya kiwango ambacho kinatakiwa kulipiwa kodi inapokuja Tanzania Bara.
Hivyo ndiyo maana bidhaa zinazotoka Zanzibar kuja huku zinatozwa tena kodi. Siyo kodi mara mbili lakini ni kuangalia utofauti wa kodi wa thamani, zilizothaminiwa kutoka Zanzibar na ambazo zimethaminiwa huku Tanzania Bara. Hivyo, tunaomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waweze kufanya haraka kujiunga na mfumo huu, ili kwa pamoja hili tatizo wanalopata wafanyabiashara wetu wasiweze kulipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bidhaa hiyo moja moja, mfumo ni huohuo mmoja, inapofika kama haikuzalishwa Zanzibar, inapofika Forodhani inatakiwa ichajiwe utofauti ule wa kodi ambao utaonekana ilichajiwa Zanzibar na huku Tanzania Bara. Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kilichokuwa hasa kinatakiwa kipatiwe ufafanuzi, pamoja na majibu mazuri, tunafahamu namna ambavyo mapato ya Serikali yanapatikana kutoka Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Sasa tunachouliza hapa, miradi mingi ambayo imekuwa ikianzishwa kutoka kwenye Halmashauri inayotegemea fedha kutoka Serikali Kuu, fedha hizi haziji kwa wakati na badala yake miradi mingi sana inakuwa mwaka unaisha, miradi inakaa miaka mitano haikamiliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunataka tu kufahamu, miradi hii mingine ambayo kwa kweli ingekamilika ingekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi; kwa mfano, kwenye Jimbo la Nyamagana, uko mradi wa maji wa Fumagila, una zaidi ya miaka mwili sasa na umebakiza fedha kidogo sana kutoka Serikali Kuu, kiasi cha shilingi milioni 256 hazijapatikana mpaka leo. Ni lini fedha hizi zitapatikana ili maji yanayokadiriwa kusaidia watu zaidi ya 16,000 yaweze kuwasaidia kwa wakati na kupunguza mzigo kwa akina mama? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba upungufu wowote unaotokana katika vyanzo viwili vya kuchangia katika bajeti yetu hupelekea tatizo hilo, lakini Serikali imejipanga na kwa pamoja tumeona kwamba fedha hizi sasa zimeanza kutolewa. Miradi yote ambayo haijakamilika, Serikali imedhamiria kuendelea kupeleka pesa ili miradi hii iweze kukamilika. Pamoja na mradi wake wa maji alioutaja wa Nyamagana uliobakiza shilingi milioni 200, ninamwahidi kwamba Serikali itapeleka fedha hizo ili kukamilisha mradi huo pamoja na miradi mingine yote ambayo imefikia katika hatua nzuri za utekelezaji.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Miradi mingi ya maendeleo imekuwa haifanyiki, sababu kubwa pia ni kutokana na baadhi ya gharama za uendeshaji na Halmashauri zetu kutokupelekewa fedha, kwa mfano gharama za kusimamia mitihani. Je, Serikali inajipangaje kulipa madeni hayo kabla mwaka huu wa fedha wa 2015/2016 haujaisha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na katika jibu la swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula, Serikali imejipanga vizuri, mapato yanaongezeka na miradi yote itapelekewa pesa ili iweze kukamilika kwa wakati.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu baadhi ya maeneo ambayo Mkaguzi Mkuu wa Muungano amekuwa akiyafanyia ukaguzi. Kwa nini mpaka sasa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo wa Jimbo, haujawahi kufanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema ukaguzi wa Mfuko wa Jimbo hufanywa na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa pamoja huwa wanashirikiana kufanya ukaguzi huu na Mkaguzi wa Zanzibar, kwa upande wa Zanzibar. Kwa swali lako la kwa nini, nina imani kuwa Mfuko huu utafanyiwa ukaguzi pale muda utakapofika na ukaguzi huo utafanyika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Mkaguzi Mkuu huwa anakagua mashirika mengine, lakini ningependa kujua au kwa niaba ya wengine pia, yeye huwa anakaguliwa na nani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkaguzi Mkuu naamini yeye pia hujikagua mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kwa kuwa, ulipaji wa kodi ni suala la kizalendo na kwa kuwa, suala la ulipaji wa kodi ni wajibu wa kila mwananchi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile kwa kuwa Wabunge, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaji, ni wanufaika kutokana na mishahara na faida mbalimbali tunazozipata kutokana na kodi ambazo wananchi wanalipa.
Je, ni lini Serikali sasa italeta marekebisho ya Income Tax inayompa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Rais wa Zanzibar msamaha wa kodi kwenye mishahara yao? Pia ni lini Serikali italeta marekebisho kwenye sheria inayowapa Majaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania misamaha ya kodi kwenye mishahara yao ili wote kwa pamoja tutimize wajibu wa kiraia wa kulipa kodi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyokiri yeye mwenyewe kulipa kodi ni haki ya kila mtu na ni wajibu wa kila mtu. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Upendo pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, muda sahihi utakapofika wa kuleta marekebisho ya Sheria hii tutaileta hapa Bungeni na marekebisho yatafanyika na watu wote watalipa kodi kwa msingi sahihi unaotakiwa. Pia naomba nimkumbushe kuwa, siyo kwamba Mheshimiwa Rais halipi kodi! Mheshimiwa Rais analipa kodi. Nashukuru.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi kuuliza swali la nyongeza. Ili misamaha ya kodi iweze kupungua kufikia asilimia moja ni pamoja na kuhakikisha kwamba sheria zilizopitishwa na Bunge hili zinatekelezwa kikamilifu. Kumekuwa na parallel system, mfano TIC kumekuwa na kikao cha TIC na TRA ambapo TIC ikipokea maombi ya wale wanaoitwa
Strategic Investors wanakaa kikao na wanachagua baadhi ya bidhaa wanazipa msamaha wa kodi. Jambo hili litakoma lini kufanyika? Kwa sababu, pia, linawaweka katika mtego wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato ambao wakishiriki kikao hicho ambacho kinatoa msamaha…
Mheshimiwa Naibu Spika, lini Serikali itahakikisha kwamba, Sheria za Kodi zinatekelezwa kama zilivyopitishwa na Bunge? Kusiwe kuna parallel system?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia kwamba, sheria hizi zinatekelezwa kama ambavyo zimepitishwa na vikao hivi huwa vinafanywa kwa pamoja kati ya wataalam wetu waliopo kwenye TIC na wale wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Inapofikia sehemu ya discussion kuhusu kodi wataalam hawa hukaa pamoja kuona ni jinsi gani ya kutoa misamaha hii ya kodi. Hakuna sehemu ambako Wataalam wa upande mmoja hukaa peke yao katika kufikia maamuzi haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalithibitishia Bunge lako sheria zetu kama zinavyopitishwa na Bunge zinatekelezwa kama tulivyopitisha.
MHE. ESTER N. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza Naibu Waziri wa Fedha kwa makini, kwa jinsi alivyojibu ametutajia figure kubwa sana ambazo zimeenda katika sekta ya kilimo, lakini ni wazi na Waheshimiwa Wabunge wanajua bado wakulima wetu kilimo chao ni cha kusuasua na wanalima katika mazingira magumu. Hata wale ambao wanajitokeza katika kilimo cha umwagiliaji wakiwemo watu wangu wa Tamau, Nyatwali na maeneo mengine wanakosa vifaa. Mna mkakati gani wa kuhakikisha hizi figure zinaendana na hali halisi ya mkulima mmoja mmoja?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru kwa kuelewa kwamba kiasi hiki nilichokitaja ndicho ambacho kimetoka Benki ya TIB (Tanzania Investment Bank) kwenda katika miradi ya kilimo na miradi mingine niliyoitaja. Mimi kama Naibu Waziri wa Fedha na Mipango jukumu langu ni kuhakikisha pesa hizi zinafika kwa wale wanaomba pesa hizi. Kwa hiyo, naamini tutafanya kazi kwa ushirikiano mzuri mimi na Waziri wa Kilimo, mtani wangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ili tuhakikishe sasa pesa hizi zinawanufaisha walengwa na zinaweza kukidhi mahitaji yale waliyoomba.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni takribani miaka 13 toka Wilaya hii ya Kilindi imeanzishwa. Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, pana umbali mkubwa sana kati ya Wilaya ya Handeni iliko ofisi ya Mamlaka ya Mapato na Kata mbalimbali za Jimbo la Kilindi hususani katika Kata ya Pagwi. Je, ni lini sasa utafiti huu utakamilika ili wananchi wa Kilindi waweze kunufaika na huduma hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ametaka kujua ni lini utafiti huu utakamilika. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba pamoja na utafiti huu kukamilika pia tunaangalia potentials ya ukusanyaji yaani cost and benefit analysis ya kuanzisha ofisi hizi kila Wilaya. Kwa sasa hivi nguvu nyingi tunazielekeza katika kuanzisha ofisi za Mamlaka za Mapato katika mikoa mipya ambayo imeanzishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naendelea kusema kwamba namwomba Mheshimiwa Kigua aendelee kuongea na wananchi waendelee kulipa kodi kupitia Wilaya yao ya mwanzo kabla ya Kilindi kuanzishwa. Pia tutakapokamilisha utafiti huu na tukaona kwamba kuna potential kubwa ya kupata mapato ya kutosha Wilaya ya Kilindi, basi hatutasita kuanzisha ofisi hii katika Wilaya ya Kilindi na wilaya nyingine zote za Tanzania ambazo hazina Ofisi.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa benki nyingi hapa Tanzania zinatoa mikopo kwa riba kubwa sana na zinafanya wafanyabiashara ama wananchi wa Tanzania kukopa lakini kutokurudisha mikopo hiyo kwa wakati kutokana na riba kubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha benki hizo zinapunguza riba hizo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa hivi sasa kumejitokeza taasisi nyingi ambazo zinatoa mikopo, lakini hazifuati taratibu za kitaalamu je, Serikali inalijua hilo na kama inalijua hilo inazichukulia hatua gani taasisi kama hizo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Faida Bakar kwa umakini wake wa kufuatilia masuala ya kifedha hapa nchini. Hili ni swali lake la pili katika Bunge hili nalijibu akiulizia masuala haya, hongera sana Mheshimiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kumekuwa na riba kubwa, lakini naomba tufahamu kuwa kufuatia mabadiliko ya mfumo wa kifedha hapa nchini kuanzia mwaka 1991, Serikali ilijitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kifedha hapa nchini, ili kuruhusu ushindani huru na kuboresha huduma katika sekta yetu ya fedha. Hivyo, viwango vya riba na mikopo zinazotozwa na benki zetu na taasisi nyingine za kifedha zinapangwa kutokana na nguvu ya soko huria ambalo tuliamua wenyewe kuingia katika soko hilo.
Mheshimiwa Spika, pia napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba katika upangaji wa viwango hivyo vya tozo mbalimbali na riba benki pia na taasisi zetu za kifedha huzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, pia gharama za uendeshaji na sifa alizonazo mkopaji katika kuliendea hilo. Hivyo Serikali pia tunaendelea kuwasisitiza mabenki yetu pamoja na taasisi zetu za kifedha kutumia takwimu za credit reference bureau ili kuweza kujua taarifa halisi na historia za wakopaji na pia ushindani uliopo ili tuweze kushusha riba hizi, lakini kama Serikali hatuwezi kuingilia tena katika soko hili.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Faida Bakar, amependa kujua kwamba kumekuwepo na taasisi nyingi za kifedha na je, zile ambazo hazifuati utaratibu je, Serikali ina mpango gani wa kuzitambua na kuzirasimisha?
Napenda kumjibu Mheshimiwa Faida Bakar kwamba Serikali inafahamu tatizo hili la Taasisi zilizopo za binafsi ambazo zipo na zinasumbua sana wananchi wetu. Katika kulitambua hilo Serikali kwa sasa iko katika mpango wa kuandaa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2016 ambapo sasa hivi ipo katika hatua nzuri, itapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri na hatimaye tutaweza kuwa na Microfinance Act itakayoweza kudili na tatizo hili moja kwa moja. Nashukuru.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSA: Mheshimiwa Spika, napenda nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kutokana na mfumo wa mabenki mengi, utitiri wa mabenki mengi hapa nchini, Serikali imejipanga vipi kuyasimamia mabenki yale na kuyawezesha ili iweze kuwakopesha wateja na kuleta tija kwa Taifa letu?
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwamba Serikali kupitia mabadiliko ya mfumo uliotokea mwaka 1991 ilijitoa katika kuendesha moja kwa moja sheria za kifedha hapa nchini, lakini hayajaachwa huru, Benki Kuu inayasimamia na ndiyo maana nimesema hata hizi taasisi ndogo ndogo tunaandaa Sera ya Taifa ya hizi taasisi ndogo ndogo za fedha ili zote tuweze kuzisimamia kiuhakika, lakini siyo kuingilia katika uendeshaji wa huduima hizi. Nina imani kubwa taasisi zetu hizi za kifedha zinafanya kazi kwa ajili ya Watanzania na kwa ujumla zinatenda vizuri ndiyo maana watu wengi wanaweza kuzifikia na kupata mikopo pale wanapohitaji.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka kujua ni lini Serikali itasambaza mashine za EFD katika Mikoa yote ya Tanzania, ili mwananchi aweze kulipa kodi kihalali na kuweza kulipatia Taifa mapato? (Makofi)
Swali la pili; kuna changamoto katika mtandao, changamoto hii ya mtandao inapelekea kukatika kwa mawasiliano kati ya mashine hizi na TRA. Mfano mnunuzi yupo kituo cha mafuta X akiwa safarini kuelekea Mkoa Y na ikatokea kuna changamoto hiyo, je, mnunuzi anatakiwa afanyeje ikiwa juzi tu tumepitisha sheria kwamba lazima mtu achukue risiti?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba nia ya Serikali yetu ni kusambaza mashine hizi nchi nzima. Kama tunavyofahamu jambo lolote lina gharama na mashine hizi pia zina gharama, kwa sasa Serikali imeanza kugawa mashine hizi za EFD katika Mkoa wa Dar es salaam kwa wafanyabiashara wadogo wenye mauzo ghafi kati ya shilingi milioni 14 hadi milioni 20. Katika awamu ya kwanza Wizara yangu imepanga kugawa mashine za EFD 5,703 na mpaka leo tayari wafanyabiashara 118 wameshachukua mashine zao. Naomba pia niwashajihishe wafanyabiashara wote wa Dar es salaam ambao waliainishwa kuchukua mashine hizi sasa waende wakachukue mashine, kama ambavyo tumesikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba mashine hizi zipo lakini wafanyabiashara hawataki kujitokeza kwenda kuchukua mashine hizi. Nawaomba wafanyabiashara wafike na wachukue mashine hizi katika Mamlaka yetu ya Mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Neema ameuliza changamoto katika mtandao. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba Serikali yetu pia imefanya jitihada ya kusambaza mkongo wa Taifa nchi nzima. Kwa hiyo, changamoto hii ya mtandao naamini haina muda mrefu itafika mwisho na pia naomba niseme na niwaombe wafanyabiashara, wamekuwa wakisingizia changamoto ya mtandao kumbe hakuna tatizo la mtandao. Naomba niwaambie ni vizuri wakaweza kutumia sasa fursa hii ya kuenezwa kwa mkongo wa Taifa na kuweza kutumia mashine hizi katika kutoa risiti pale ambapo wanauza au wanatoa huduma yoyote kwa wananchi. Nimekuwa nikiongea na wafanyabiashara nikiwauliza swali na Waheshimiwa Wabunge naamini ninyi ni mashahidi nani amewahi kufika katika mabenki ya biashara akaambiwa mtandao upo chini, hakuna. Kwa hiyo, hii pia ni danganya toto ya wafanyabiashara, naomba niwaambie sasa Serikali tumeingia vizuri na tunaanza kazi kila mmoja aweze kutoa risiti hizi za mashine ya EFD.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kupata taarifa za wafanyabiashara ili waweze kulinganisha na maandalizi ya kumbukumbu zao za hesabu. Sasa katika uhasibu kuna marekebisho ya kiuhasibu, inatokea mtu anatoa kitu kinaitwa credit note au debit note ili kufanya masahihisho. Lakini kwa sasa mfumo huu wa electronic signature device hauchukui marekebisho ya kiuhasibu. Je, ili kuondoa hali ya sintofahamu na kulinganisha kumbukumbu za TRA na wafanyabiashara, Serikali ipo tayari kubadilisha mfumo wake na kuingiza hizi credit note au debit note katika marekebisho ya kiuhasibu ili ziweze kusomeka katika mtambo wa TRA na kurahisisha kazi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi; lengo la mashine hizi ilikuwa ni kupata taarifa na kumbukumbu sahihi za wafanyabiashara na mauzo yao, lakini kama kuna jambo lolote ambalo litaweza kuboreshwa zaidi Serikali yetu iko wazi kabisa, naomba tushirikiane ili tuweze kuhakikisha kumbukumbu zote zinaingia katika mfumo huo. Kwa sasa, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba tumeanza na hizo kumbukumbu za mauzo na mapato ya wafanyabiashara ila haya mengine yote pia tunaendelea kuboresha mfumo wetu, nina imani kubwa yote yataingizwa kwenye mfumo huu.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ni kutaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia akina mama walioanzisha VICOBA kwa kuongezewa mtaji wao? Pia Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha taasisi binafsi zinazotoa mikopo kuacha kunyanyasa akina mama wanapochelewa kulipa mikopo yao kwa kuwanyang‟anya vifaa vyao vya matumizi na vinavyowaendeshea maisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itashawishi mabenki kutupelekea benki kwenye Wilaya ya Mafia na Jimbo la Utete? Kwa sababu Makao Makuu ya Wilaya ya Rufiji ni Utete lakini mpaka leo hapo Utete hakuna huduma inabidi waende Kibiti kufuata huduma. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili japo yameonekana kama manne ya Mheshimiwa Zaynabu Vulu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni akina mama kuongezwa mtaji kwa kuwa wameanzisha VICOBA. Kwanza kabisa naomba niwapongeze akina mama wote nchini kwa kuonesha ujasiri wao katika kuungana katika vikundi na kuanzisha VICOBA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba Serikali imeweka mazingira mazuri na tayari taasisi za kifedha au benki za jamii zinaanzishwa hivyo nawashauri akina mama hawa na mimi nitashirikiana nao kama mama kuhakikisha kwamba tunaanzisha taasisi au benki yetu ya kijamii ya wanawake sehemu yoyote ile. Naomba nitoe nafasi hiyo, tushirikiane kwa pamoja Wabunge wanawake ili tuweze kuungana na akina mama hawa kuanzisha benki ya wanawake ya kijamii sehemu yoyote ile ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ya swali hili la kwanza ilikuwa ni taasisi za kifedha zinazokopesha ziache kuwanyanyasa akina mama. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba kama nilivyojibu wiki moja iliyopita Serikali inaanzisha rasimu ya sera kwa ajili ya taasisi hizi ndogo za fedha ili sasa kuweza kuzikagua na kuziwekea sheria na taratibu ya kuweza kufanya kazi na kuacha kuwanyanyasa akina mama. Sera hii itakapokuwa tayari, nina uhakika kabisa taasisi hizi zitaacha kuwanyanyasa akina mama. Pia naomba niwashajihishe taasisi zote hizi zinazotoa mikopo kwa akina mama ziache utaratibu huu wa kuwanyanyasa akina mama. Tufuate taratibu zote za utoaji wa mikopo kama vile kuangalia uwezo wa mlipaji anayekopa kabla hujamkopesha kuliko kumkopesha tu kwa kuonekana wako kwenye kikundi halafu baadaye unakuja kuwanyanyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nilisema ameuliza maswali mawili lakini yanaonekana kama manne, kwa hiyo, kulikuwa na sub-questions. Napenda kulijibu swali hili, kwamba ni lini Serikali itaweza kuzishawishi benki kupeleka matawi yao Mafia na Rufiji?
Namuomba Mheshimiwa Zaynabu Vulu tushirikiane tuone ni jinsi gani ya kuongea na benki zetu na hasa benki yetu ya NMB na CRDB, nina uhakika wakienda ku-access mazingira ya Mafia wataenda kufungua tawi lao sehemu hii. Naomba tukae na Mheshimiwa Zaynabu Vulu tuone ni jinsi gani ya kushughulikia suala hili.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa niulize swali la nyongeza. Wafanyakazi wamekuwa wakikatwa fedha zao na kupelekwa kwenye huu mfuko wa PSPF. Lakini wafanyakazi hawa wanapokuwa wamemaliza huo muda wanacheleweshewa kupewa mafao yao. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuona kwamba, wafanyakazi hawa wanapomaliza muda wao wawe wanaandaliwa cheque zao mapema ili kusudi ziweze kuwasaidia katika kufanya shughuli zao wanazokuwa wamejipangia kuliko hivi sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, je, Mheshimiwa Waziri amejibu amesema wameshaanza kulipa; anaweza sasa akanisaidia mimi orodha ya Mkoa wa Tanga, hususan Korogwe, wale ambao wamekwishalipwa ili wasiendelee kunieleza kwamba wanadai? Nipate ile orodha ili iweze kunisaidia.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa swali lake la kwanza alilouliza kuhusu kucheleweshewa malipo, kama ambavyo Serikali imekuwa ikitoa majibu humu Bungeni ni kwamba kucheleweshewa huku hakutokani na Serikali, kunatokana na waajiri ambao wanachelewesha kufikisha nyaraka za wastaafu hawa katika Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii. Hivyo, nitoe tu wito wangu kwa waajiri wote wajitahidi kupeleka nyaraka zote zinazostahili kwa wastaafu miezi mitatu au sita kabla mstaafu hajastaafu ili tuweze kulipa mapema iwezekanavyo. Wakiweza kufanya hivyo, Waheshimiwa Wabunge tunaweza kabisa mstaafu anapokuwa amestaafu nyaraka zake zimekamilika na cheque yake itaweza kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, Mheshimiwa Mbunge naomba nifanye kazi mimi na wewe kuhusu wastaafu wote wa Wilaya ya Korogwe wanaolipwa na Mfuko wetu wa PSPF, tunapomaliza Kikao hiki cha Bunge naomba tushirikiane ili upate orodha halisi ya waliostaafu na orodha halisi ya waliolipwa katika kipindi hiki. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Naomba kuuliza swali la nyongeza, Serikali ina mkakati gani sasa kwa watumishi ambao wamestaafu kwa hiyari ama wengine wamebadilisha kazi kwa mfano kuwa Wabunge, ili kuendelea kuchangia Mfuko huu wa PSPF badala ya kuwaondoa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliopo kati ya Serikali na watumishi hawa, nadhani ni ndani ya mtumishi yeye mwenyewe kwamba kama anaona anaweza kuendelea kulipa anaweza kuongea na watumishi wa mfuko huu, Wakurugenzi wetu wote na wote wako tayari na wanapenda kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mussa Sima nikwambie mimi ni mmoja wa waliokuwa watumishi wa Serikali na sasa naendelea kuchangia malipo yangu baada ya mimi kwenda kuongea na Mkurugenzi wa Mfuko wa PSPF na sasa mimi naendelea kuchangia.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, Waheshimiwa Watumishi wote na Watanzania kwa ujumla wanaoona wanaweza kuendelea kulipa basi waende wafike kwenye mifuko hii na wataweza kuendelea kulipa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa niwapongeze Waheshimiwa Naibu Mawaziri wote wawili kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama tu kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sheria hizi za malipo ya pensheni na mifumo ya kuchangia katika mifuko ya pensheni zimehuishwa na sasa kila mtumishi wa umma ama mtumishi katika sekta binafsi anapohama kiajira kutoka ajira moja kwenda ajira nyingine ama anapotaka kuhamisha mafao kutoka mfuko mmoja kwenda katika mfuko mwingine kwa mujibu wa sheria sasahivi anaruhusiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni suala tu kila mtu kufikiria na kuona ni namna gani anataka kuendelea kuhuisha mafao yake na anaweza kuhusiaha katika mfuko wowote kwa kuhamisha kutoka mfuko mwingine kwenda mwingine kama anabadilisha ajira ama anaamua kufanya hivyo na sheria sasa hivi zinaturuhusu. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kwa pensioners ambao hawalipwi kupitia Hazina moja kwa moja kwamba, vile viwango vipya vya malipo hawajaanza kulipwa mpaka hii leo. Na haya malalmiko yamekuwa ni ya muda mrefu sana. Naomba commitment ya Serikali ni lini wastaafu hawa wataanza kulipwa viwango vyao vipya pamoja na arrears zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekuwa nikiliarifu Bunge lako Tukufu ni kwamba watumishi wote ambao wanalipwa kupitia Hazina walianza kulipwa fedha zao za nyongeza tangu mwaka jana mwezi wa saba, 2015. Kwa mifuko ambayo haijaanza kulipa kama ambavyo nilisema mwanzo, nyongeza hizi, sasa hivi Bodi za Mifuko hii zinamalizia kufanya maamuzi, ili waweze kuanza kulipa nyongeza ambayo ni ya 50,000 kama ilivyotangazwa na Serikali.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kuniruhusu kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Kagera enzi hizo ukiitwa Ziwa Magharibi baada ya kupata uhuru ilikuwa ni miongoni mwa mikoa minne ambayo ilikuwa na utajiri na pato kubwa ikiwa ni Kilimanjaro, Dar es Salaam pamoja na Mbeya, na wakati huo ikiwa na Chama cha Ushirika (BCU) ambacho kilikuwa na nguvu kubwa kiasi cha kuikopesha hata Serikali, sasa maswali yangu.
La kwanza, je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba miongoni mwa mambo ambayo yamesababisha umaskini kwanza ni vita ya Kagera ambayo hata baada ya kualizika na Serikali ya Uganda kulipa fidia, wananchi hawakupewa fidia yoyote?
Pili, ugonjwa wa UKIMWI, lakini tatu Chama cha Ushirika cha KCU ambacho kimesambaratika na hususan kutokana na mambo mengi ya kisiasa badala ya kutetea zao la kahawa. Lakini pia Reli ya Kati ambayo kimsingi imesambaratika na haifiki Kemondo na hivyo wananchi wa Mkoa wa Kagera kupokea bidhaa kwa njia ya barabara ambayo inawagharimu vibaya sana.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja pamoja na mambo aliyozungumza ambayo kimsingi bado yanaeleaelea na hayana mashiko, kuweka mkakati mahsusi wa kuyaweka katika utekelezaji na hata kuyaweka katika mpango wa BRN (Matokeo Makubwa Sasa), lakini sambamba na hilo kwa kupitia Mpango wa TASAF, kama Serikali imetathmini kwamba mkoa ni maskini na kaya ni maskini kwamba bajeti ya TASAF iongezeke ili kaya ziweze kupokea pato zaidi na kaya ziweze kuongezeka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kufuatana na sababu zilizotolewa na takwimu zilizotolewa, je, hizi takwimu zinatoa takwimu sahihi ambayo inaashiria ni kwa Wilaya zote au ni kwa baadhi ya wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Kagera ndiyo zenye umaskini wa namna hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nakubaliana na sababu alizozisema na ndiyo maana Serikali iko kwenye mpango mkakati wa utekelezaji wa mpango wetu ambao tumeuwasilisha humu Bungeni kama alivyosema tuje na mpango mahsusi wa utekelezaji kupeleka kwenye BRN, Serikali iko kwenye mchakato wa kuja na utekelezaji wa maazimio yote na malengo yote yaliyopo ndani ya BRN.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo utakumbuka ni kwamba tayari sasa hivi mchakato wa kutengeneza Reli ya Kati kwa standard gauge unaanza mwezi Disemba tunaanza utekelezaji na ambayo inaelekea upande huohuo wa Mikoa ya Magharibi na Kagera ikiwepo ili tuweze kufungua uchumi wa Mkoa wa Kagera na uchumi wa mikoa mingine ya upande wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu takwimu hizi, naomba niliambie Bunge lako Tukufu, takwimu hizi ni sahihi na zinaashiria Mkoa mzima wa Kagera kwamba upo katika kiwango cha umaskini wa asilimia 39 kama nilivyosema.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo yaliyopo kwenye Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Mwanza pia ni moja kati ya mikoa iliyotajwa kuwa mikoa maskini, sasa ningependa kujua mikakati ya Serikali mbali ya majibu mazuri na mipango ya miaka mitano na mwaka mmoja, ina mkakati gani wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ili kuwa sehemu ya kuhakikisha na wao wanakuwemo kwenye mpango wa kuhakikisha umaskini huu unatoweka wakiwa wana nafasi nzuri ya kufanya biashara zao kwa uhuru?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema na kama tulivyoainisha kwenye mpango wetu wa mwaka mmoja na mpango wa miaka mitano kwamba sasa hivi tunaangalia jinsi ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo vidogo pamoja na viwanda vikubwa vikubwa, vya kati pia ili tuweze sasa kutengeneza ajira kwa watu wetu. Na hii ni pamoja na kuwawezesha wafanyabiashara hao wadogo na wa kati ili waweze kupata bidhaa zao kwa bei nafuu na pia tuangalie pia wafanyabiashara ambao wako katika sekta ya kilimo kwa sababu tumesema viwanda vidogo, viwanda vya kati na vikubwa vitatumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwa hiyo ni mpango wa Serikali yetu kuweza kuwawezesha watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu tunakuja na Microfinance Act mwezi huu au mwezi wa 11 ni uhakika kwamba watu hawa, wafanyabiashara wadogo na wa kati watapewa elimu ya ujasiriamali na jinsi gani ya kuendeleza biashara zao pamoja na kuwezeshwa mitaji ni moja ya mikakati ya Serikali yetu.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa mujibu wa takwimu ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri ametupatia, Deni la Taifa sasa mpaka Juni mwaka huu limefikia shilingi trilioni 51 na bilioni 40. Kiwango hiki cha fedha ni almost mara mbili ya bajeti ya Taifa. Wakati huo huo ukigawanya deni hili kwa Watanzania milioni 45 kila Mtanzania leo atakuwa anadaiwa shilingi 1,134,222.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kukopa ni muhimu katika wakati mwingine ili kuweza kusukuma mbele shughuli za kimaendeleo, lakini ulazima wa kukopa kwa kiwango ambacho tunaweza kukilipa kwa wakati ili Taifa liondokane na mzigo wa riba pamoja na kulimbikiza madeni liweze kujielekeza mapato yake zaidi katika kushughulikia mipango ya maendeleo, ni vyema tuwe na kiwango cha ku-control ukopaji wa Serikali.
Sasa swali langu la mwisho ni hili, tutakumbuka wakati wa Awamu ya Tatu, wakati wa Mheshimiwa Mkapa, Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi zilizokuwa zimepata sifa ya kuwa miongoni mwa nchi zilizosamehewa madeni kupitia mpango wa HIPC (Heavily Indebted Poor Countries) ambapo Deni la Taifa liliweza kusamehewa na likashuka chini ya dola bilioni 10 na almost tulikuwa tunamaliza Deni la Taifa.
Je, ni kwa nini Serikali sasa hivi, kwa sababu bado mpango wa HIPC upo chini ya World Bank na IMF, ni kwa sababu gani Serikali isione uwezekano tena wa kufanya initiative ya kurudishwa katika Mpango HIPC ambao unasimamiwa na World Bank na IMF ili tupunguze mzigo huu wa madeni na hizo pesa tuzielekeze zaidi kwenye shughuli za kimaendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijaondoka kwenye mpango huo wa kusamehewa madeni na bado tunaendelea na mchakato huu kwa kushirikiana na IMF pamoja na World Bank. Zipo nchi ambazo zilikuwa katika mpango wa kuhakikisha tunasamehewa madeni kama nchi yetu lakini zilisitisha kutokana na migogoro ambayo ipo ndani ya nchi hizo, moja ya nchi hizo ilikuwa ni Iraq, Iran pamoja na nchi nyingine zenye migogoro ambazo zilisitisha sasa kusamehewa madeni. Hivyo bado tunaendelea na mchakato huo kuendelea kuwashawishi wadau hao wa maendeleo ili waweze kutusamehe madeni haya.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa ya kitaalam, lakini nilitaka kuongezea nyongeza tu na kuwatoa hofu Watanzania kwenye kile alichosema Mheshimiwa Mbowe kwamba ukiligawa deni hilo kwa kila Mtanzania.
Kwanza hakuna siku Watanzania watagongewa mlango wakigawanywa Deni hilo la Taifa na wala katika Taifa lolote hakuna utaratibu wa kupima deni kwa kuangalia mgawanyo wa ujazo wa watu bali Deni la Taifa linapimwa kufuatana na uwezo wa nchi kimapato inavyokusanya na inavyoweza ku-service deni hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tunapoangalia kukua kwa deni tutakiwa pia tuangalie miundombinu ya nchi yetu imekuwa kwa kiwango gani kwa sababu wazo hilo linafuatana na uamuzi wa nchi inayochukua kwenye miundombinu, hata hivi sasa Waheshimiwa Wabunge tunavyoongelea standard gauge ya reli, tunavyoongelea miradi mikubwa mikubwa kama ya bandari tutakuwa tunaongelea uwezo wa nchi yetu kuweza kuendesha miradi, lakini ujenzi wake utategemea njia hizo hizo za kuweza kukopa. Ndiyo maana hata mataifa makubwa ambayo yameendelea leo hii yana madeni makubwa lakini yana uwezo wa kulipa madeni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimoja tu ambacho natakiwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbowe ambacho Serikali inakifanya, haikopi kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Serikali inapokopa kwa mara zote inakopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo itazalisha kulipa deni hilo. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Naipongeza Serikali kwa kuweka mfumo huu wa EFDs kwa ajili ya kukusanya kodi ili kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato stahiki kulingana na biashara zinazofanyika ndani ya nchi yetu, huo ni upande mmoja wa shilingi katika kukusanya mapato.
Upande wa pili, je, ni lini Serikali sasa itaweka bei kwa kila bidhaa inayoingia nchini ili wafanyabiashara wetu wanaoingiza mali kutoka nje ya nchi ajue hasa kwamba nikiingiza gari aina fulani ya mwaka fulani inalipiwa kiasi fulani ili asikwepe kodi lakini na kumfanya mtu wa TRA kuwa na negotiation ya kodi ili Pato la Taifa liongezeke kwa mfanyabiashara wetu kujua hasa kwamba nikileta kitu hiki nakilipia ushuru huu? Kwa hiyo, yeye mwenyewe hakuna negotiation ili kuondoa mambo ya rushwa na mambo ya manung‟uniko kwa wafanyabiashara wetu. Ahsante. (Makofi)anajijua na
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, bei anazosema kwa ajili ya bidhaa zote zinazoingia nchini tunazo na ndiyo ambayo inakuwa ni base ya kuweza kufanya tax assessment kwa bidhaa zote zinazoingia. Kwa hiyo, tunazo bei hizo ambazo zinakuwa zimetumika kwa bidhaa hizo kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, miezi sita, miezi sita ndani ya nchi yetu bidhaa hizo ziliingia kwa kiasi gani. Kwa hiyo hizo taarifa na database tunazo katika Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba tunazo hizo lakini pia Mamlaka ya Mapato huwasiliana na mamlaka za masoko mengine nje ya nchi yetu kuweza kujua bidhaa kama hizo zinauzwa kwa shilingi ngapi ili tunapofanya tax assessment kwa ajili ya wateja wetu, tuwe tunawatendea haki wateja wetu. Kwa hiyo, tunatumia njia zote hizo na database hiyo Mheshimiwa Mbunge ipo kabisa na tunaitumia.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali madogo tu ya nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kwanza, je, wanatumia vigezo gani vya usajili wa hivyo VICOBA?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakiwa wanakopesha wanaanzia na kiwango gani cha hiyo mikopo, ili wananchi nao waweze kukopa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza vigezo vinavyotumika ni kuangalia kikundi husika kinajishughulisha na nini na kama kina wadau muhimu katika kikundi hicho, pamoja na aina ya shughuli kinachotaka kujishughulisha kikundi hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na swali lake la pili, ameuliza ni shilingi ngapi wanakopeshwa, hapa kinaangaliwa tu kikundi husika kina mtaji kiasi gani na kimeomba kiasi gani na hivyo, kuangalia kama wanaweza kukopesheka, kuangalia viashiria hatarishi ndani ya kikundi kile kama waliwahi kukopa na uwezo wao wa ku-manage biashara walianza lini. Kwa hiyo, tunaangalia mtaji wao endelevu na sustainability yao katika biashara wanayofanya.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Wizara ya Fedha kwa kufanya mipango mizuri na niishukuru sana kutangaza Kariakoo kuwa Mkoa wa TRA.
Mheshimiwa Waziri, leo tumesoma kwenye magazeti yanasema kwamba, kuna mdororo wa uchumi, mpaka kufikia mahali ambapo mabenki hayakopeshi tena wananchi na wameanza kuuza bond zao. Ni nini Wizara ya Fedha inazungumza kuhusu haya mabenki kutokuwakopesha wawekezaji au waanzishaji biashara mpya ili waendelee kuuimarisha huu uchumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Fedha itoe msimamo wake. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ajali, swali la msingi linahusu VICOBA, sasa maelezo ya jumla kuhusu uchumi, hayo yatamtaka Waziri alete hoja hapa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tutaendelea.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kero hii inalalamikiwa sana na wafanyabiashara wetu na hufikia hatua kupoteza wafanyabiashara hawa kuendelea na biashara. Je, ni lini Wizara hii itaanza utatuaji wa kero hii kwa wafanyabiashara wote?
Swali la pili, Wizara itamaliza lini kero hii ya kutatua suala hili la kodi ya wafanyabiashara wanaotoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, utofauti huu unatokana na tatizo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokutumia mfumo nilioutaja kwenye jibu langu la swali la msingi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuishawishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kujiunga na mifumo inayotumika ndani ya Idara ya Forodha ili kuondoa changamoto hii inayowakumba wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba, progress ni nzuri na kwa kuanzia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika bajeti yake ya mwaka 2016/2017 imeridhia kutumia mfumo wa Import Export Commodity Database kwa bidhaa ya magari yatakayoingia Zanzibar ili kuweza kuondoa changamoto hii. Kwa hiyo, naona huu ni mwanzo mzuri. Tunaendelea kuishawishi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iweze kujiunga moja kwa moja kwa bidhaa zote zinazoingizwa Zanzibar na hatimaye kuletwa Tanzania Bara.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Wilaya ya Lushoto ina Mjimbo matatu na Ofisi ya TRA ni moja tu kwa Majimbo yote matatu; je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi Ofisi ya TRA, Lushoto na kutoa TIN Number, Motor Vehicle na License za udereva ili wananchi wasipate taabu ya kwenda mpaka Tanga Mjini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunajua Wilaya ya Lushoto ina Majimbo matatu na tuna Ofisi moja ya TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Mbunge atakumbuka ndani ya wiki mbili zilizopita, nilijibu kuhusu ufunguzi wa Ofisi za TRA, lakini kwa kuwa tuna Ofisi ya TRA Lushoto, kinachohitajika ni kupandishwa hadhi; namuomba Mheshimiwa Mbunge tuonane ili tuweze kukaa pamoja na tuone ni jinsi gani sasa tutaweza kuipandisha hadhi ofisi hii ili huduma hizi muhimu ziweze kupatikana kwa ajili ya wafanyabiashara wetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa iliyokuwa NBC, Benki iliyokuwa inamilikiwa na Serikali ilikuwa na tawi pale mlalo na ilikuwa inahudumia wakazi wa Mlalo, Mbaramo, Mtae mpaka Mlola; je, kwa nini NMB iliyochukua nafasi ya NBC isitekeleze wajibu huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri amesema sehemu ambazo zina mzunguko mkubwa wanaweza wakaongeza ushawishi wa kutengeneza Community Bank; na Jimbo la Mlalo lina mzunguko mkubwa wa fedha; je, ni lini kwa kushirikiana na SACCOS ya Kumekucha Mwamko SACCOS Ltd. wanaweza wakawajengea uwezo ili tuweze kuanzisha hiyo Community Bank? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Serikali ilijitoa moja kwa moja kuendesha shughuli hizi, lakini Serikali kupitia Wizara yangu itaendelea kuhimiza mabenki kuendelea kusambaza huduma zao kwa wananchi wa vijijini likiwepo na Jimbo la Mlalo. Pia nitalifikisha ombi hili katika Benki yetu ya NMB na kuwashauri kuhusu ombi hili la Mheshimiwa Rashid Shangazi ili tuone sasa NMB inaweza kurejesha huduma ambayo mwanzo ilikuwa ikiendeshwa na Benki yetu ya NBC. Kwa hiyo, nitakaa nao, nitaongea nao na namwomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane naye ili tuweze kuongea na Menejimenti ya NMB ili kurejesha huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ipo tayari kabisa kutoa ushauri wa kitaalamu na namna ya kuanzisha benki za kijamii. Ninafahamu pale Mlalo hasa maeneo ya Lukozi, maeneo ya Rangwi, Mlalo yenyewe, Shume na Mlola kuna huduma nyingi za kiuchumi, hivyo niko tayari kabisa kuishauri Benki Kuu kwamba sasa tukatoe huduma hizi za kitaalamu kwa wajasiriamali wetu hawa ili waweze kuanzisha Benki ya Kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kuna society nzuri pale ambayo tukishirikiana nao na mtaji unaotakiwa kuanzisha Community Bank ni shilingi bilioni mbili tu, kwa taarifa nilizonazo, taasisi hii iliyopo pale ina zaidi ya shilingi bilioni moja sasa. Kwa hiyo, wamebakiza sehemu ndogo tu waweze kuanzisha Community Bank. Mheshimiwa Rashid Shangazi tushirikiane ili tuweze kuanzisha Community Bank pale Mlalo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba niulize swali lingine la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile huduma hizi za kibenki ni suala la kisera; na kwa vile ni haki ya kila Mtanzania kupata huduma hizi; na kwa vile imebainika kwamba mabenki yetu ya kibiashara hayawezi kufika yale maeneo ambayo hayana tija sana kibiashara; ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba Benki ya Kilimo inayafikia maeneo hayo ambayo hayana tija kwa wafanyabiashara wa kibenki likiwemo Jimbo la Madaba na Jimbo la Mlalo kama ilivyoulizwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mhagama kama ulivyosikia wakati tunaweka Mezani bajeti yetu ya Wizara ya Fedha, moja katika benki ambazo tunategemea kwamba zitafungua matawi yake zaidi, ni hiyo Benki yetu ya Kilimo. Kwa hiyo, tunaendelea kuijengea uwezo na muda siyo mrefu Benki hii itafungua matawi yake katika maeneo yenye wakulima wetu ili waweze kufaidika na huduma za Benki yetu ya Kilimo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa kuna mtazamo kwamba kila kundi kufungua benki ndiyo jibu la huduma ya benki, siyo jema; na kwa kuwa hapa tulipofikia, huko nyuma tulikuwa na Benki ya Posta ambayo iko kila mahali na watumiaji wa benki ni hao hao wananchi wa eneo lile; je, ni kwa nini sasa Serikali isiipe uzito Benki ya Posta ikasambaa kote?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika benki ambazo zinakuja juu sasa ni Benki yetu ya Posta. Tumeiwezesha vizuri, Menejimenti yake imekaa vizuri sasa, imezindua huduma nyingi ambazo hata benki nyingine kubwa za kibiashara zimeshindwa kuanzisha huduma hizo. Kwa hiyo, ni imani yangu kubwa Benki ya Posta ndani ya muda mfupi ujao itarejesha hadhi yake ndani ya nchi yetu ya Tanzania.
Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kuiunga mkono Benki yetu ya Posta, tufungue akaunti kule, tuiwezeshe sisi kama shareholders muhimu ili Benki ya Posta iweze sasa kurejea. Tuko vizuri na inakimbia Mheshimiwa Shally, itafungua matawi yake sehemu zote nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa pamoja na upungufu uliopo katika kodi hii, lakini pia baadhi ya wananchi ambao sio waaminifu walikuwa wanatumia mwanya huo kutengeneza sticker ambazo ni feki: Je, Serikali ina mpango gani wa kuja na sticker madhubuti ambazo siyo rahisi kufojiwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wapo wananchi ambao wanatenda vitendo viovu vya kufoji sticker hizi. Kama nilivyosema, lakini naomba pia tufahamu kwanza Waheshimiwa Wabunge, katika sehemu ambako tumeboresha kwa kiasi kikubwa ni utoaji wa sticker hizi ambapo kwa sasa hivi mwananchi yeyote anaweza kulipia gari yake popote alipo na akaenda kuchukua risiti yake katika Ofisi zetu za Mamlaka ya Mapato popote pale alipo huku akiwa amepewa control number. Kwa hiyo, tumeweza kutoka katika manual work na sasa tunatumia teknolojia katika kutoa huduma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maboresho hayo, kama nilivyosema, tusubiri Finance Bill itakapokuja, tutaona sasa kutakuwa hakuna mkono wa mtu yeyote kuingia katika ukusanyaji na utoaji wa sticker hizi kwa sababu itakuwa ni mfumo wa automatic ambao hakuna yeyote atakayeweza kuuingilia na kuweza kutoa sticker ambazo ni feki.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Serikali ya Awamu ya Tano katika matendo yake imeonekana inasimamia haki. Nataka kujua kama pato la kodi hii Serikalini kwa magari yaliyosimama kwa muda mrefu kwa sababu za msingi, lina tofauti yoyote na pato analolipata mwananchi au mtumishi hewa kutoka Serikalini?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni ushauri. Kwa kuwa magari yanayotozwa kodi hii hutumia mafuta na kwa kuwa kodi hii imekuwa na adha katika ukusanyaji wake na ni kero pia kwa wananchi: Je, Serikali inapokea ushauri kwamba, kodi hii ihamishiwe kwenye mafuta ili kurahisisha ukusanyaji wake na kuondoa kero kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kodi hizi hutozwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge letu Tukufu. Kwa hiyo, kuifananisha na watumishi hewa siyo sahihi kabisa na ndiyo maana nimesema Serikali ina nia na imeanza maboresho ya sheria hii ili kuweza kuondokana na adha hii wanayoipata watumishi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuifananisha kwa sababu ni ngumu kwa sababu ya jiografia ya nchi yetu. Huwezi tu kusema gari hii imesimama bila kujiridhisha kweli imesimama. Kama ilitolewa mjini na ikapelekwa Vijiji ambavyo hatuwezi kuvifikia, inakuwa ni tatizo kusema gari hili limesimama. Ndiyo maana nasema, naomba tuvute subira, tutakapoleta Finance Bill ya mwaka huu 2016/2017 anachokipendekeza Mheshimiwa Mbunge kitaonekana na adha hii itaondoka kabisa wala haitakuwepo tena kwa wananchi wetu.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nisikitike tu kwamba jibu lake haliendani na uhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhalisia uliokuwapo Lindi ni kwamba takwimu za watu wanaokadiriwa 100,000 ni wa Jimbo la Lindi Mjini. Vilevile nimkumbushe Naibu Waziri katika mchakato wa bajeti iliyopita ya mwaka jana kwamba maafisa wa Halmashauri walishakaa vikao tofauti na maafisa wa Wizara yake katika kuangalia uwezekano wa kubadili bajeti kutokana na idadi ya watu. Sasa anaposema kwamba idadi ya wakazi wa Lindi na akitumia takwimu za wapiga kura ni sahihi nakataa kukubali jibu lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali ya nyongeza kama tu Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara yake walikubali kwamba idadi ya watu wa Lindi ni kidogo na hivyo watafanyia kazi mchakato wa kuongeza bajeti katika bajeti inayokuja, je, yuko tayari kuthibitisha hilo au kulifanyia kazi hilo kwa bajeti inayokuja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kutokana na idadi ya watu kutotumika idadi stahiki katika Jimbo la Lindi imepelekea huduma za afya kupelekwa katika kituo kimoja tu cha afya katika Lindi Mjini na hivyo kupelekea shida kubwa kwa watu wa Lindi.
Je, Mhehsimiwa Waziri anayehusika yuko tayari kuiboresha hospitali inayotoa huduma ambayo inaendeshwa na Jeshi la Polisi Lindi ili kuweza ku-accommodate matatizo ya afya ya wananchi waJimbo la Lindi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiiwa Mwenyekiti, kwa swali la kwanza ambalo anasema kwa bajeti inayokuja, naomba nilikumbushe Bunge lako tukufu kwamba Bunge hili lilipitisha sheria ya takwimu Machi, 2015 ambayo inatoa mamlaka kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuratibu takwimu zote rasmi. Na kwa Serikali tunachofahamu ni kwamba idadi ya watu wa Lindi Mjini ni ambao wametajwa na kwa makadirio ya mwaka 2016, idadi ya watu Lindi Mjini ni 85,871 hiyo ndio takwimu rasmi inayotambulika na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu swali la pili, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge swali hili tutakaa pamoja na Waziri wa Afya na Waziri wa TAMISEMI tutalifanyia kazi kuona hospitali hii inaboreshwa.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, kumekuwa na ubadilishanaji wa fedha kiholela sana hasa katika sehemu za mipaka yetu na nchi jirani. Mfano, kama kule Tunduma ambapo ubadilishanaji huu huwa kama vile tunagawiana njugu yaani holela. (Makofi)
Je, Serikali ina mkakati gani wa kurasimisha kazi hii inayofanywa na watu wa kawaida na kuweza kuchukuliwa na Serikali ili kuwaondoshea hata wale watu wanaofanya kazi hiyo, inawezekana hata wakapoteza maisha yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali haioni kwamba inapata hasara na haipati mapato mengi ikiachia biashara hii iendeshwe isivyo halali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar kwa umakini wake katika ufuatiliaji wa masuala ya kifedha na uchumi wa Taifa letu. Serikali inakiri uwepo wa watu wanaojihusisha na biashara hii kiholela hasa katika mipaka mbalimbali ya nchi yetu na nchi jirani, kwa mfano, kule Tunduma kama alivyosema, Namanga, hata pia katika Miji yetu mikubwa kama Arusha na Mwanza, lakini Serikali yetu haipo kimya katika kulishughulikia tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kupitia Sheria yetu ya Fedha za Kigeni ya Mwaka 1992 na Kanuni tulizozipitisha mwaka 2015, Serikali inaendelea kushughulikia tatizo hili. Pia, tunakiri kwamba, mapato ya Serikali yanapotea ndiyo maana Benki Kuu pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamekuwa wakiendesha operation na warsha mbalimbali katika sehemu hizi nilizozitaja ili sasa kuwasaidia wananchi wetu hawa kuwa na uelewa wa hatari ya biashara wanayofanya, pia na kuonesha kwamba, ni kwa jinsi gani Taifa letu linapoteza mapato katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, tunatambua hili na tumeendelea kutoa warsha katika maeneo haya na kwa watu hawa tunafanya jitihada za hali ya juu kuhakikisha sasa watu hawa wanarasimishiwa biashara zao hizi wanazozifanya, ili kwanza kama alivyosema Mheshimiwa Faida, kupunguza hatari ya maisha yao na pia kuhakikisha Serikali yetu inapata mapato ambayo tumekuwa tunapoteza.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa fursa hii na nimshukuru Mheshimiwa Faida kwa swali zuri alilouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi linahusu matumizi ya dola, hivi sasa kumekuwa na kilio cha wanafunzi wengi wa vyuoni kulipishwa ada kwa malipo ya dola na baadhi ya taasisi, ikiwemo taasisi hii ya TRA inayoongozwa na Waziri na Naibu Waziri wa Fedha. Je, kuna Sheria yoyote iliyopitishwa humu kuhusu suala hili na amesema tokea 1992 hakuna utaratibu huo? Je, hatua gani zinazochukuliwa kwa taasisi hizi zinazolipisha ada ya dola kinyume na sheria?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekiri na nimesema kwamba, tunafahamu zipo taasisi zinazotumia dola katika kufanya transaction. Nimesema pia, ni mojawapo ya chanzo cha Serikali yetu kupata fedha za kigeni moja ya faida ni hiyo, lakini kama nilivyosema ni asilimia 0.1 tu ya transaction zinazofanyika nchini zinazotumia dola ya Kimarekani. Kama nilivyosema Sheria ilipitishwa na Kanuni zake zimepitishwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba tunawachukulia hatua gani, bado hatuoni kwamba, inahatarisha na kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, siyo sababu inayopelekea thamani ya pesa yetu kupungua.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yasiyotosheleza sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Swali la kwanza; kwa kuwa kutunza dhahabu kwenye hazina ya nchi yoyote ni kuashiria utajiri wa nchi hiyo; kwa mfano, nchi ya Marekani ina dhahabu zaidi ya tani 8,100 kwenye hazina yake, lakini nchi ya Ujerumani 3,300 na nchi ya Italia ina tani 2,450. Kwa nini Tanzania tunachelea chelea kutunza dhahabu wakati sisi sasa hivi ni wazalishaji wa dhahabu duniani?
Swali la pili, kwa kuwa Tanzania ni nchi inayozalisha dhahabu kama Ghana, ina tani nane kwenye ghala yake, lakini Afrika ya Kusini ina tani 125. Na kwa kuwa kwa kipindi cha muda mrefu dhahabu imekuwa ikipanda thamani. Miaka ya 1900 dhahabu ilikuwa zaidi ya dola 200, miaka ya 2000 ilikuwa zaidi ya 500; sasa hivi ni zaidi ya dola 1000. Kwa nini Serikali inachelea kwamba dhahabu inatelemka bei. Kwa nini sasa Serikali isifanye utafiti ikaangalia nchi zingine zinafanyaje na ikatunza dhahabu kwenye hazina yake kwa ajili ya kupandisha uchumi wa nchi yetu? Ahsante sana.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza, sababu kubwa ya msingi ya Benki Kuu ya nchi yoyote kuweka akiba yake katika dola ni kujiwekea akiba (reserves), hiyo ndiyo sababu ya msingi ya Mataifa yote. Hata katika historia wakati wa vita, dhahabu ilichukuliwa kama mkivamia nchi moja kitu cha kwanza mnachokimbilia kuchukua kwa wale mliowashinda mnachukua ile dhahahu kwa sababu ina hesabika ndiyo inabeba thamani ya vitu. Kwa hiyo, sana siyo kuonesha kiwango cha utajiri katika nchi kama sababu ya msingi ya kuweka akiba yako katika dola. Vilevile tunachelea kuweka akiba yetu katika dola kwa sababu ya msingi….
Mheshimiwa Spika, tunachelea kuweka akiba yetu katika dhahabu kwa sababu ya tabia ya bei ya dhahabu katika miaka ya karibuni kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyoeleza.
Mheshimiwa Spika, hata huko Ghana ambako ni kweli wana akiba ya dhahabu ya tani 8.4 ambayo siyo sehemu kubwa sana ya akiba yao ya reserves na wamekuwa na akiba hiyo toka mwaka 2000, kiasi hicho hakijabadilika. Hali kadhalika Afrika ya Kusini toka mwaka 2016 wamebakiwa na tani 123.8 tu na kiasi hicho kimeteremka na kufikia tani 183.1, lakini ni wasiwasi huo wa mwenendo wa bei ya dhahabu katika soko la dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali inafanya uchambuzi kuona uwezekano kama tunaweza tukaweka sehemu yetu ya akiba katika Tanzanite badala ya dhahabu lakini hii ni kazi ambayo inaendelea.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini swali langu la msingi niliuliza ni utaratibu gani mtaweza kuwasaidia makundi maalum ya wanwake na vijana ili waweze kupata mikopo kwa riba nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili nilitaka kuuliza, kwa kuwa kuna ugumu na sheria zinazoibana Serikali kusimamia riba hizi. Ni lini sasa Serikali itatusaidia kutimiza ile ahadi ya shilingi milioni 50 kila kijiji na mtaa ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu na kinamama wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi; kwa mujibu wa Sheria Benki Kuu haiwezi kutoa maelekezo ya kuleta riba elekezi ili kuweza kusimamia mabenki haya yaweze kufanya vizuri katika soko letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu shilingi milioni 50 kama ambavyo Serikali imekuwa ikisema; tunaendelea kuandaa utaratibu na kwenye bajeti yetu ya fedha ya mwaka 2016/2017 tumetenga bajeti hii na tutaweza kuitekeleza kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa jibu la msingi la Mheshimiwa anasema Benki Kuu haiwezi kuingilia kutoa bei elekezi, tunawezaje kusaidia Benki ya Wanawake iweze kutoa riba ndogo kwa kupata ushauri kutoka kwenye Wizara yake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo, kwa mujibu wa sheria Benki Kuu haiwezi kutoa hiyo riba elekezi na napenda niseme kwamba riba hizi zilizopo ni kwa mujibu wa Sera ya Riba ya mwaka 1992. Kwa hiyo, lazima tuendane na sera tuliyoipitisha humu Bungeni ili kuweza kuhakikisha kwamba sekta ya fedha inafanya vizuri ndani ya uchumi wetu na kwa Benki ya Wanawake naamini Mheshimiwa Waziri wa Afya anaweza kulisimamia hili na kuweza kutoa riba ambayo ni nzuri, lakini hawezi kukiuka misingi ile iliyowekwa na Sera ya Riba ya mwaka 1992.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia leseni za kufanya biashara katika Manisapa mbalimbali zinatolewa baada ya kupatikana kwa tax clearance, lakini ukweli ni kwamba sio biashara zote hasa biashara ndogo zinahitaji wakati mwingine tax clearance, haioni ni wakati muafaka kuweka categories za biashara ambazo wanaweza kupewa leseni bila hata tax clearance badala ya kinachofanyika sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hili ni swali la kutoa leseni ambalo ni swali jipya ambalo tumeondoka katika riba, kwa hiyo naomba niseme tu tuna viwango ili kuweza kutoa leseni katika biashara zote zinazoendeshwa ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, kama hawajafikia ndani ya kiwango kile kinachohitajika mfanyabiashara huyo wala hatozwi na wala hapewi leseni lakini akishavuka yale malengo ya biashara yake tayari anatakiwa apewe leseni na tunasimamia kama moja ya njia za kukusanya mapato yetu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwezesha elimu bure, upatikanaji wa madawati na pia watumishi hewa kuondolewa, naomba kufahamu, kwa sasa Watanzania wengi hasa akinamama katika SACCOS zao wamekuwa na hamu kubwa ya kufanya biashara. Je, Serikali inachukua hatua gani kuwezesha SACCOS za akinamama katika halmashauri zote zipate hela za kutosha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ikumbukwe kwamba sote humu ndani Waheshimiwa Wabunge sisi ni Wajumbe katika Mabaraza yetu ya Halmashauri, hivyo tunatoa asilimia tano katika mapato ya halmashauri na hayo ni katika kuimarisha vikundi vyetu vya VICOBA pamoja na SACCOS zilizopo ndani ya halmashauri zetu. Nitoe wito tu kwa Waheshimiwa Wabunge, tusimamie kwa ufasaha asilimia hizo tano za mapato ndani ya Halmashauri zetu ili ziweze kuwafikia wananchi wetu hasa akina mama na vijana ili kuweza kuinua uchumi wao.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kituo hiki kilipoanzishwa mwaka 1989 tayari Tanzania ilikuwa na Ubalozi Mjini London ambao ulianzishwa mwaka 1961, na moja ya jukumu la kituo hiki ni kuvutia uwekezaji na hasa suala la utalii ambao unachangia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa. Je, nini kilionekana kimeshindikana wakati huo kufanywa na Ubalozi na ambacho sasa kinaweza kufanywa na Ubalozi huo?
(b) Kwa kuwa kituo kimefungwa na miongoni mwa madai makubwa ambayo Serikali ilikuwa inadaiwa ni posho za wafanyakazi wa kituo waliopo London, mishahara ya wafanyakazi na kodi za nyumba za wafanyakazi wetu waliopo London.
Je, Serikali inaweza kutoa tamko gani juu ya madai ya wafanyakazi wa kituo hiki waliopo London kama wameshalipwa fedha zao na kama wamerejeshwa nchini, je, wamelipwa fedha zao za kujikimu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema yalikuwa ni maagizo ya Mheshimiwa Rais lakini pia naomba ikumbukwe kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imesema na inatekeleza sasa kuboresha na kupeleka watumishi wote katika balozi zetu zote duniani ili kuhakikisha wao wanafanya kazi husika na zinazostahiki kufanywa na balozi setu.
Kwa hiyo agizo lile halikuwa la makosa na sasa Serikali ya Awamu ya Tano imerejesha jukumu hili ndani ya Ubalozi ambalo ni moja ya majukumu yake na Ubalozi wetu unaendelea kufanya vizuri.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, niseme kama Naibu Waziri wa Fedha, madai tuliyoyapata ni shilingi 129,896,000 na ndiyo ambayo tunayalipa kama kuna watumishi ambao wanadai posho zao na haki zao zozote naomba watuletee ili tuweze kuhakiki na tutaweza kulipa kama ambavyo tumelipa deni lililotangulia.
MHE. ENG. ATASHASTA J.NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana, jina langu ni Atashasta Justus Nditiye au Engineer Nditiye inatosha. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wazawa Green Field Plantations walianza mchakato wa kufuatilia eneo hilo toka mwezi wa pili mwaka jana na tuliwapa ushirikiano namshukuru sana Mkuu wa Wilaya pamoja na wananchi wa Jimbo la Muhambwe, lakini ilipofika mwezi wa nane ameondoka mpaka sasa hivi ninapoongea hajarudi. Tunadhani ni muhimu sana tupate mwekezaji competitor kwa ajili ya ku-speed up suala la yeye kuja kufanya shughuli za uwekezaji kama tunavyotarajia ili wananchi wasije wakakata tamaa. Ni lini Serikali inafikiria kutafuta mwekezaji mwingine ikiwezekana hata wa kutoka nje ili kuweza kuwekeza katika Kiwanda cha sukari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika kuelekea kwenye sera ya viwanda katika nchi yetu tuna wabunifu wengi sana na katika Wilaya yetu ya Kibondo kwa mfano, kuna kijana amebuni magodoro yanayotumia mifuko ya plastic na kila alipojaribu kuwasiliana na COSTECH kwa ajili ya ushauri wamekuwa hawampi ushirikiano wa kutosha. Ni lini Serikali inajipanga kuwaongezea uwezo COSTECH ili wanapopata maswali kutoka kwa wabunifu wadogo wadogo waweze kuwatembelea na kuwapa ushauri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata taarifa kwamba hapa mwekezaji aliondoka na hajarejea na kama alivyosema Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda. Tutamleta mwekezaji mwingine kama alivyosema na siyo mmoja bali wawili, watatu kuongeza competition na ufanisi hilo nimelichukua na Serikali inalifanyia kazi, watakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubunifu na COSTECH; kwanza nikiri kwamba huyo mwanafunzi na nimwambie Mheshimiwa Mbunge mwanafunzi huyo ni mwanafunzi wangu niliyemfundisha Masters Chuo Kikuu Mzumbe. Namfahamu na tulimfundisha na sasa anaendelea na ubunifu huo na COSTECH pamoja na Chuo Kikuu Mzumbe tumepanga kumuendeleza mwanafunzi huyo pamoja na wabunifu wote wanaoibuka ndani ya Nchi yetu.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Niongezee kwa hoja ya msingi iliyozungumzwa. Mwekezaji huyo katika Bonde la Malagarasi aliyeko Muhambwe pia yuko mwekezaji mwingine anaitwa Kigoma Sugar yuko Bonde la Malagarasi upande wa Wilaya ya Kasulu. Wote hawa inaonekana wameshindwa na kama sisi Kasulu tunataka ardhi yetu ekari 100,000 tumnyang‟anye sasa tuweze kutafuta mwekezaji mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naomba basi juhudi hizo za kutafuta mwekezaji zifanyike kote Muhambwe na Wilaya ya Kasulu kwa sababu wote wako kwenye Bonde hilo la Malagarasi. Kwa hiyo, swali langu ni kuomba tu Serikali wawekezaji wote hao wa zamani wameshindwa, hawapo.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme siyo kwa Wilaya ya Muhambwe na Kasulu tu, niseme kwa Wilaya zote na maeneo yote ya uwekezaji na hasa uwekezaji kwa ajili ya kilimo cha miwa pamoja na viwanda vya sukari. Naomba tupatiwe taarifa ili Serikali tuchukue hatua mara moja kama walipewa ardhi basi naamini Waziri wa Ardhi yupo makini tutaichukua ardhi hiyo na kumpa mwekezaji mwingine.
Kwa hiyo, niombe Waheshimiwa Wabunge tupate taarifa ya wawekezaji wote wanaonekana ni wababaishaji na wameshindwa kufanya kazi, tushirikiane na Tanzania ya viwanda inawezekana.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri. Pamoja na Tanzania kwamba tuna maeneo mengi mazuri kwa ajili ya kilimo cha miwa na viwanda tulivyonavyo vya sukari na pamoja na mbwembwe nyingi za Serikali ya Awamu ya Tano iliyonazo kukuza uchumi, lakini bado bei ya sukari katika nchi yetu ni kubwa sana na uwezo wa wananchi wetu ni mdogo. Je, ni lini Serikali itaangalia sasa uwezekano wa kupunguza bei ya sukari ili ifikie angalau pale tulipokuwa na tatizo la sukari wananchi wetu waweze kumudu kununua sukari?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikanushe Serikali ya Awamu ya Tano siyo ya kibabaishaji tunafanya kazi na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa tathmini ya mwezi Januari viwanda vyetu vya ndani vimeshazalisha asilimia 86 ya uhitaji wa sukari ndani ya nchi yetu, kwa hiyo, ninauhakika kwa demand na supply nguvu hii tayari tukishaweza kuzalisha asilimia mia moja bei ya sukari itashuka. Tukumbuke tu Waheshimiwa Wabunge nchi hii ni huru na inafuata soko huria, hatuwezi kuingilia hilo na turuhusu sasa Viwanda vyetu viweze kuzalisha asilimia mia moja na bei ya sukari itashuka na wananchi wetu watafurahia Serikali yetu ya Awamu ya Tano utendaji wake.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na
majibu ya Waziri, Manispaa ya Iringa ina miradi mikubwa ya Machinjio ya Kisasa
ya Ngelewala, Soko la Ngome, Sekondari ya Mivinjeni, Nyumba za Waganga na
Wauguzi wa Zahanati ya Njiapanda na Nduli. Katika Baraza la Madiwani, kupitia
bajeti ya mwaka 2016/2017, Manispaa ya Iringa ilikadiria kukusanya mapato ya
ndani Sh. 4,532,000,000 ili kuweza kumalizia miradi midogo iliyokuwa inaikabili
Manispaa hiyo. Manispaa ya Iringa, vyanzo vikuu vya mapato vinatokana na
kodi ya majengo, Serikali ikaamua kodi hizi za majengo zikusanywe na TRA, je, ni
lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka hela za miradi hii kwa wakati ili kuweza
kumalizia miradi ambayo haijamalizika hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika,
napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaona umuhimu wa
miradi yote ya maendeleo kama ilivyopitishwa katika bajeti yetu mwezi Juni.
Hivyo, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kinachopelekea kupeleka
fedha hizi ni upatikanaji wa fedha hizi. Kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge
ameongelea kuhusu kodi ya majengo, naomba nimwambie kwamba TRA
imekusanya kodi ya majengo mwezi wa Kumi, baada ya quarter ya kwanza
kupewa Halmashauri zenyewe kukusanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge,
anapuhudhuria Baraza la Madiwani aweze kusimamia mapato yaliyopatikana ili yaweze kutumika katika miradi aliyoitaja. Serikali yetu baada ya kukusanya
kuanzia mwezi wa Kumi, fedha zote tulizoahidi zitarejeshwa katika Halmashauri
husika kutokana na bajeti zilizopitishwa.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo hayatoshelezi kwa
sababu niliwahi kuuliza swali hili lakini nimepata majibu yale yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi, ni kwa nini tuendelee
kutumia dola katika kununua, siyo uhuru wa soko. Sasa swali la kwanza, kwa nini
Tanzania isitumie utaratibu wa nchi zingine kama Zambia, South Africa, Ghana,
Dubai na Ulaya? Wote tumesafiri tumeona ukifika tu kwenye nchi hizo
unaachana na matumizi ya dola lazima ubadilishe na ukalipe kwa hela yao.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa nini au ni lini Serikali sasa
itakagua haya maduka ya fedha ambayo kwa kweli kuna taarifa za ki-intelijensia
zinasema wanatumika kutorosha fedha zetu? Wakaguliwe, mapato yao
yajulikane na ijulikane pia ni jinsi gani wanazitumia hizi fedha na kuziweka kwenye
soko letu la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la
kwanza, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi Sheria yetu ya Benki Kuu ya
mwaka 2006, Sehemu ya Tatu, kipengele cha 26 kimeweka wazi kabisa kwamba
fedha halali kutumika ndani ya nchi yetu ni shilingi ya Kitanzania. Pia Sheria ya
Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 inaruhusu mtu yeyote kupokea na
nimeeleza kwa nini Serikali yetu imepitisha sheria zote mbili, dhamira ikiwa ni
kukuza uchumi wetu na kuwa na fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Dokta Kafumu
kwamba nchi nyingine hufuata utaratibu kutokana na mazingira ya nchi yao.
Kwa nchi yetu hatujaona athari kubwa ya kuruhusu wageni wetu kutumia fedha
hizi ndani ya uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni lini Serikali itakagua, naomba
nimwambie kwamba, Serikali yetu inakagua siku hadi siku. Kama nilivyosema
katika jibu langu la msingi Serikali yetu haijalala, Benki Kuu kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Mapato zinakagua siku hadi siku na sasa miamala yote ya maduka
haya ya kubadilishia fedha yanakuwa monitored na Benki Kuu kupitia TRA. Pia
tunaendelea kuimarisha mifumo yetu ili kuhakikisha fedha na uchumi wetu uko
salama kabisa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mashaka ya vijana wetu yamekuwa yakizidi siku kwa siku, vijana wanajihusisha katika michezo hii ambapo muda mwingi unapotea hata muda wa masomo, muda wa kufanya kazi …

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Maadili yamepotea, kuna masuala ya betting ambayo yanachukua muda mwingi wa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waziri kuniambia kwamba kuna Sheria Namba 4 inayoruhusu mambo hayo lakini udhibiti wake ukoje? Je, mpaka sasa ni wafanyabiashara wangapi wamekamatwa na maduka yao kufungwa ambao hawakuzingatia taratibu za kuzuia vijana wenye umri mdogo kuingia sehemu hizo na je, wamepelekwa kwenye vyombo husika na kuchukuliwa hatua?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza aliuliza udhibiti wake ukoje, kama nilivyosema sheria yetu imeweka wazi na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha iko makini kusimamia michezo hii yote ndani ya nchi yetu ili kuhakikisha sheria hii iliyotungwa na Bunge letu Tukufu inafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, ni watu wangapi na maduka mangapi yamefungwa, naomba nilichukue swali hili tuweze kulifanyia kazi kwa sababu linahitaji data mahsusi ili tuweze kumjulisha Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda na mimi nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa hii michezo ya kamari imekuwa ikichezwa kwenye stendi kubwa na sehemu za starehe na kupelekea watu kufilisika na wengine kufikia hatua hata ya kujiua. Je, hamwoni sasa ni wakati muafaka wa kukataza michezo hii isichezwe na wale wanaochezesha michezo hii wachukuliwe hatua?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema michezo hii ipo kisheria, sisi kama Wizara hatuwezi kuisitisha. Tutafanya utafiti ili tuone kama inahitajika kuleta sheria mpya Bungeni ili tufanye hivyo. Hata hivyo, tusisahau kama nilivyosema michezo hii ni sawa na michezo mingine pale inaposimamiwa vizuri na sisi tuna uhakika inasimamiwa vizuri. Kwa mfano, kwa mwaka jana 2016 mchezo huu ulichangia zaidi ya shilingi bilioni 2.1 katika mapato yetu. Hivyo, niombe tu kama jamii na kama Taifa tuweze kuwasimamia vizuri vijana wetu ili yale madhara hasi yasiweze kupatikana.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba kutokana na kwamba hii Sheria ya Fedha ipo kwa muda mrefu tangu mwaka 1991, na kutokana na mabadiliko ya kidunia ya uchumi na baadhi ya nchi jirani kubadilisha sheria hizi katika nchi zao; je, haaoni kwamba umefika wakati kwa Serikali kubadilisha sheria hii?
Na la pili, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba riba katika mwezi wa Juni, 2016 ilikua kwa kiwango cha 13.46 lakini ukweli halisi ilikuwa ni kati ya 16 mpaka 18. Katika swali langu niliuliza je, haoni kwamba Serikali inahitaji ichukue juhudi maalum kwa wafanyakazi wa Serikali kwa sababu fedha zao kulipwa ni rahisi na zina dhamana zaidi, anaonaje Mheshimiwa Waziri?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anauliza utayari wa Serikali kubadilisha sheria, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu, tuko katika soko huria na tunafuata soko huria hivyo haiwezekani kurudi katika kuelekeza mabenki yetu. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Benki Kuu ikifanya hivyo itakosa mamlaka sasa ya kuyasimamia mabenki hayo pindi yatakapopata hasara kutokana na riba elekezi iliyoyatoa. Hivyo nashauri tu tuendelee na mfumo uliopo kwa sababu tupo katika mfumo wa soko huria na hii pia ni global practice hivyo siamini kwamba ni njia njema kwa nchi yetu kuweza kurejea katika maelekezo kwa ajili ya riba zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, naomba niseme kwamba kuhusu kutoa riba elekezi kwa wafanyakazi pia haiwezekani kwa sababu riba tunazoziona zinakuwa ni wastani wa riba ambazo zimetolewa kutoka katika sekta na makundi mbalimbali, hivyo tukisema wafanyakazi tuwape riba nafuu itapelekea makundi mengine ambayo hasara yake au vihatarishi ni vya juu kupata riba kubwa sana na hivyo tutakuwa tumewaumiza.
Kwa hiyo, niliombe Bunge lako Tukufu na Wabunge kwamba tukubaliane na wastani huo ambao hutolewa na Benki Kuu baada ya kupata sasa riba zote kutoka katika mabenki yetu yote.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wajasirimali wadogo wadogo hasa mama lishe na wamachinga na ambao wengine wana vipato vya chini wamekuwa wakikopa mikopo kwa ajili ya biashara zao na kutozwa riba kubwa na kushindwa kurejesha mikopo ile na kufilisiwa.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inatafuta fedha kwa ajili ya Wajasiriamal wadogo wadogo na kuwatoza riba ambayo inaendana na biashara zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nilikumbushe Bunge lako tukufu kwamba tayari Serikali imeshatunga sera ya huduma ndogo za fedha za mwaka 2016 na sasa tupo katika hatua nzuri kuja na sheria katika Bunge lako tukufu ili kuwalinda wajasiriamali wadogo wanaokopeshwa kwa riba kubwa. Ni imani yangu sheria hii itakapokuwa imepitishwa watakopa katika viwango halisi ambavyo viko sokoni na sivyo ambavyo wanaonewa kwa sasa.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu aliyonipa Mheshimiwa Waziri lakini sikuridhika na majibu haya.
Mheshimiwa Waziri katika majibu yake ya msingi anasema kwamba kati ya bidhaa ambazo hazitozwi kodi pamoja na vinyago, lakini katika swali hilo hilo la msingi anabainisha kwamba kati ya vitu vinavyokamatwa na kupigwa mnada ni pamoja na vinyago. Mheshimiwa Waziri katika suala hili ulivyolijibu huoni kwamba umejichanganya? Kama vinakamatwa na kupigwa moto, vinakamatwa kwa kosa lipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuuliza swali la pili, je, Serikali imetoa elimu yoyote kuhusiana na suala zima la uuzaji wa vinyago kwa wajasiriamali wadogo wadogo ukizingatia Mheshimiwa Rais ameondosha kodi ndogo ndogo kwa wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, naomba nikiri kwamba sijamchanganya, vinyago tunafahamu ni bidhaa zinazotokana na maliasili za nchi yetu hivyo inawezekana watu wa Wizara ya Maliasili wanatozo zao ambazo wanazitoza. Mimi nimekanusha utozaji wa kodi ambao tunatoza sisi kama Wizara ya Fedha kwamba hizi hazipo katika orodha ya bidhaa tunazozitoza kodi (extport duty). Kwa hiyo, ndiyo maana katika jibu langu la sehemu ya pili nilisema yawezekana zilikuwa zinatakiwa kulipiwa tozo mbalimbali kutoka katika Wizara ya Maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, elimu ya ujasiriamali tunaendelea kuitoa, kuna kitengo ndani ya Wizara yangu ya Fedha na tunaendela kuifanyia kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wajasirimali wote nchini wakiwepo wafanyabiashara wa vinyago.