Supplementary Questions from Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji (4 total)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa, mpaka sasa hivi kuna baadhi ya makampuni ya watu binafsi na wafanyabiashara wanaendelea kutoza na kupanga bei kwa kutumia dola badala ya Tanzanian shillings.
Je, Serikali haioni hiyo inaidhalilisha shilingi yetu na kuonesha kwamba, hawana imani na shilingi ya Tanzania?
Swali la pili, kwa kuwa moja ya eneo ambalo linatumia fedha nyingi sana na kusababisha kutokuwepo kwa urari mzuri wa nchi ni uagizaji wa vyakula mbalimbali kutoka nje ya nchi wakati vyakula hivyo vinaweza kuzalishwa ndani ya nchi, maeneo kama mafuta ya kula, sukari na mazao mengine ambayo yanaweza kuzalishwa hapa nchini. Kwa mwaka tunatumia zaidi ya shilingi trilioni 2.8 kwa ajili ya kuagiza mazao yanayotokana na vyakula vinavyoweza kuzalishwa hapa na kutoa ajira kwa wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuzuia uagizaji wa baadhi ya vyakula kutoka nje ya nchi ili kuinua ualishaji wa ndani ya nchi na kuokoa shilingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kwamba katika watu ambao wanaweka bei kwa kutumia dola wanaidhalilisha shilingi yetu, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tulipitisha sheria katika Bunge lako Tukufu kwamba siyo kosa kuweza kuweka bei kwa currency ambayo siyo ya Tanzania, kosa ni ni kukataa pesa shilingi ya Tanzania pale ambapo mteja anataka kulipa na yule mwenye duka akakataa kupokea hilo ndio kosa, lakini siyo kosa katika kuweka bei hiyo kwa currency ambayo sio shilingi yetu ya Tanzania, kama Taifa tuliona inafaa na ndiyo maana tunaendelea kutekeleza sheria hii tuliyopitisha mwaka 1992.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuzuia ku-import bidhaa ambazo zinazalishwa hapa nchini. Napenda kulijibu Bunge lako Tukufu kwamba, ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza kwamba uchumi wa viwanda ili tuweze kuzalisha bidhaa zetu za kutosheleza ndani ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumeweza kuzalisha bidhaa hizi kwa kiwango ambacho kinatosheleza hatuna sababu ya kuendelea ku- import na tutaweza kurekebisha sheria zetu ili tuweze sasa kutumia bidhaa zetu, lakini kusema sasa tupige marufuku wakati bado kuna uhitaji wa bidhaa hizi, haitakuwa sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika kuiendea Tanzania ya Viwanda, tuna uhakika ndani ya miaka mitano mpaka kumi tutakuwa tumeweza kujitosheleza kwa bidhaa zetu ndani ya Tanzania. (Makofi)
MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahitimisha mahojiano na Waziri akatuambia kwenye utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu vijiji vyote vinakwenda kupata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachoendelea kwenye vijiji vyetu na majimbo yetu ni mchakato ambao haueleweki kwa wananchi kwa sababu walimsikia Waziri akisema kila nyumba, kila kijiji na kila kitongoji kinakwenda kupata umeme. Kinachoendelea kwa wakandarasi walioki site sasa wanafanya survey wanasema kila kijiji wanapelekea nyumba 20 tu, sasa hii imeleta changamoto kwetu sisi Wabunge hasa tunaotoka vijijini.
Ni nini kauli ya Serikali wao ili wawaeleze wananchi ni nyumba zote vijiji vyote au tunakwenda awamu kwa awamu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ashatu Mbunge wa Kondoa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata umeme nyumbani kwake, lakini haiwezi kuwezekana kufanya hivyo kwa siku moja na tunapotoa kazi kwa mkandarasi kulingana na bajeti na fedha tuliyonayo tumekuwa tukianza na wale tunaowaita wateja wa awali kwa hiyo mkandarasi tunampa kazi ya kupeleka umeme katika eneo fulani, na kwenye mkataba wake tunampa labda wananchi 100 au 500 au 700 kulingana na wigo wa lile eneo lilivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mkandarasi akikamilisha hao watu 500 sisi tunafunga mkataba wa mkandarasi kwamba tunamaliza.
Sasa kinachokuwa kimebakia ni kwamba wananchi wa maeneo yale sasa waendelee kufuatilia na kuomba umeme kutoka taasisi yetu ya umeme yetu ya TANESCO ili waendelee kuunganishiwa kwa sababu sio watu wote wanakuwa tayari kuunganishiwa umeme katika siku moja ambapo mkandarasi anakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa maelezo mafupi ni kwamba mkandarasi anakuwa na wateja wa awali wa kuanza nao na akikamilisha wale aliopewa wateja wengine wanaendelea kupewa umeme na TANESCO na tutahakikisha kwamba kila Mtanzania anapata umeme nyumbani kwake. (Makofi)
MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Pori la Hifadhi la Akiba la Mkungunero ni tatizo kubwa ambalo limegharimu maisha wa wananchi wetu limegharimu maisha hata ya wanyama pori wenyewe.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kondoa wangependa kujua ni lini ripoti ya Mawaziri ambayo ilikuwa ni taarifa ni timu iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ikaenda timu ya Mawaziri nane kwenda kufanya kazi na kuzunguka kwenye mapori yote likiwepo Pori la Hifadhi ya Mkungunero. Sasa ni lini ripoti ile itatolewa kwa wananchi na mipaka ikajulikana ili matatizo ambayo wananchi wameyaishi kwa miaka 50 na zaidi yaweze kufika mwisho sasa? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili nilisaidia kuchangia na nikasema kwamba tumekubaliana tutapita kwenye maeneo haya yote ya migogoro ili kuhakiki kwa pamoja kwa kutumia idara inayohusika na upimaji wa ramani ambayo ipo chini ya Wizara yangu, kwenda kuhakiki maeneo yote haya yenye migogoro ili tuweze kuchukua hatua. (Makofi)
Lakini nataka kumpa taarifa katika eneo hilo la Mkungunero timu ya Wizara yangu ipo huko wiki hii, kwa maombi ya Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, lengo ni kwenda kuhakiki mipaka ya Mkungunero kulinganisha na GN iliyoanzisha pori na ndicho kilichoombwa na Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, kwamba yeye hapingi pori, lakini anataka kujua ana mashaka pori lina mipaka tofauti na ile ya GN kwa hiyo timu ya wataalam wa Wizara yangu na Wizara ya Maliasili wako Mkungunero hivi sasa kwenye pori hilo hilo wanafanya hiyo kazi ya uhakiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini juu ya matokeo ya ile timu ambayo iliagizwa na Serikali tulikuwa tumeshasema hapa kwamba tuliomba fedha mwaka huu na tumepewa kwenye bajeti hii, tunakwenda sasa kuwajulisha na Wakuu wa Mikoa wanajua.
Mheshimiwa Spika, lakini tunakwenda kutelekeza sasa uamuzi wa Baraza la Mawaziri yale maeneo ambayo wananchi wameachiwa tutakwenda kuwaonesha na yale maeneo ambayo yanaondoshwa ndani ya hifadhi tutakwenda kuwaonesha na yale maeneo ambayo yanakaa ndani ya hifadhi tutawaonesha na tutaweka mipaka inayoonekana.
Kwa hiyo shughuli hiyo hatujaifanya katika maeneo yale lakini mwaka huu Wizara ya Maliasili na ya kwangu tumepewa fedha tunakwenda kufanya kazi hiyo rasmi baada ya bajeti hii. (Makofi)
MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Naomba niulize swali moja tu la nyongeza nalo ni hili lifuatalo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utekelezaji wa maamuzi wa maelekezo na kazi nzuri iliyofanywa na mawaziri hawa nane bado hayajafanyika, na kwa kuwa bado maelekezo yaliyotolewa wakati timu hiyo inaundwa kwamba wananchi waachwe maeneo yao wakiendelea na shughuli za maendeleo bado halijavunjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa je, ni kwa nini wananchi wa vijiji 11 wanavyozunguka pori la Akiba Mkungunero bado mifugo yao inakamatwa? Na wananchi bado wanapigwa na maaskari hawa wakiwa kwenye maeneo yao hayo. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ashantu na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Kaimu Naibu Waziri wa Maliasili nilitaka nimpe maelezo Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepata maelekezo maalum ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu, kwamba sasa tuunde timu kwenda kufanya uhakiki wa maeneo hayo kama Mkungunero ambalo anahangaika nalo na mimi nalijua sana. Na ilikuwa lazima Mheshimiwa Rais mwenyewe atoe idhini na maelekezo hayo na ametoa maelekezo ya huruma kabisa kwamba pamoja na maelekezo yale ya awali, lakini nendeni mkafanye uhakiki kabisa ili tuone namna ya kumaliza jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kumhakikishia timu ya watalaam itakuja Mkungunero mwezi wa kumi na maeneo mengine yenye migogoro kama hii kwa sababu inajulikana. Tumeagizwa tufanye kazi hiyo ya uhakiki ili kukomesha kabisa migogoro hii kwa kadri itakavyowezekana. Uamuzi umetolewa na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tutakuja kushirikiana pamoja na wewe na viongozi wengine na viongozi wa mkoa katika kuhakikisha mambo haya yanakwisha.
Mheshimiwa Spika, tunajua yapo mengi huyu ameuliza katika mengi mengine na wewe hata leo uliunda kamati fulani niende kule nimewaambia kidogo, lakini nataka kukuhakikishia kwamba haya maneno Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo maalumu.