Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lathifah Hassan Chande (4 total)

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, mpango huu wa REA upo kwa ajili pia ya Mkoa wa Lindi hadi Lindi Vijijini, lakini mpaka sasa hivi maeneo mengi ya Mkoa wa Lindi bado hayana umeme. Je, ni vijiji vingapi katika Mkoa wa Lindi ambavyo vinatarajia kupewa umeme wa REA katika bajeti ya mwaka 2016/2017?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vinavyotarajiwa kuunganishwa umeme katika Mkoa wa Lindi kupitia REA Awamu ya III ni 117. Ahsante sana.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na kwamba Serikali inanunua ndege na kuikodisha ATCL, hata hivyo umiliki huu wa ndege uko kwa Wakala wa Ndege za Serikali. Kwa maana hiyo basi, ATCL inakodisha hizi ndege. Sasa je, ATCL inatoa malipo yoyote kwa Serikali kwa ajili ya kukodisha ndege hizi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwamba mpaka sasa hivi Serikali inaisimamia management pamoja na Bodi ya ATCL, kwa maana hiyo ATCL haina mamlaka huru ya kutekeleza shughuli zake za utawala. Sasa swali langu ni kwamba, Serikali ina mpango gani wa kuiachia management na Bodi ya ATCL ili iweze kufanya mamlaka yake kwa uhuru na kuweza kufanya shughuli za kibiashara kwa ajili ya kuipatia Serikali mapato ambayo itakuwa ni faida endelevu? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna malipo yanayolipwa na ATCL kwa mmiliki wa ndege, lakini nadhani Mheshimiwa Lathifah anafahamu, mmiliki wa ndege, TDFA, inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali na kwa upande mwingine mwendesha ndege au mkodishaji wa ndege hizo ni ATCL ambaye naye anamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Hiyo haifanyi ATCL apunguze nguvu katika kuhakikisha kwamba anafuata shughuli za biashara na hatimaye analipa gharama za kukodisha ndege hizo. Kwa hiyo, zinalipwa na takwimu tu bahati mbaya sina, ukizitaka nitakuletea uone hadi sasa ATCL wameshalipa kiasi gani kwa TDFA ambao ndege zao wamezikodisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhuru wa bodi na management, nimhakikishie Mheshimiwa Lathifah, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ni moja kati ya Wizara zinazohakikisha taasisi zake zinazofanya shughuli za kibiashara zinafanya shughuli kibiashara na haziingiliwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi hizo zikiwa ni pamoja ATCL, haiingiliwi, bodi ina mamlaka kamili ingawa tu wanalalamika kuna vikao vingi sana vya taasisi za Kiserikali na taasisi za Bunge, lakini hizi zote ni kwa mujibu wa sheria. Sheria za Bunge zinawataka wao wawajibike Bungeni kila wanapotakiwa kuwajibika na Sheria za Msajili wa Hazina zinawataka wao wawajibike kwa Msajili wa Hazina kila wanapoona kwamba wanahitaji kuwajibika, lakini huko siyo kuingilia uhuru wao. Taasisi hizi zinatekeleza wajibu wao kwao, wao wanaendelea kuwa huru katika kufanya maamuzi yao.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na kwamba demand ya Soko la Dunia ni ufuta mweupe, lakini Tanzania tumekuwa tukilima ufuta wa brown ambao bei yake inakuwa haina thamani kubwa kama ilivyo ufuta mweupe: Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kuwasaidia wakulima wa ufuta nao waweze kuanza kulima ufuta mweupe ili kuweza kuongeza kipato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni juu ya Kiwanda cha Korosho kilichopo Lindi, Kiwanda cha TANITA ambacho kilikuwa kinaendeshwa na Serikali na kiliweza kuwapatia ajira wananchi wengi. Sasa hiki Kiwanda cha Korosho, TANITA, kimebinafsishwa ambapo hamna shughuli yoyote inayoendelea baada ya ubinafsishwaji huu na kupelekea wananchi kukosa ajira. Je, Serikali ina mpango gani juu ya kukifufua kiwanda hiki kutokana na kwamba Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ni Tanzania ya viwanda? Ina mpango gani juu ya kufufua hiki kiwanda na viwanda vingine vingi vilivyoko Mkoani Lindi? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lathifah ameuliza swali lake la kwanza wakati muafaka; bajeti ya Wizara ya Kilimo inafuata nami nitamhimiza Waziri wa Kilimo kwamba tulete mbegu zinazozalisha ufuta mweupe ambao una soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kiwanda cha korosho, Serikali ina mpango gani? Mpango wetu ni kuhakikisha kwamba viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi. Hatuendi kwa kasi inayotakiwa kama nitakavyoeleza kwenye bajeti yangu kesho kutwa, ni kwa sababu viwanda vingine vina matatizo ya mikataba ya kisheria, lakini dhamira yetu ni hiyo na tutahakikisha viwanda vyote vinafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na viwanda hivi, wako wawekezaji wanakuja na nitahakikisha Mheshimiwa Mbunge tunashirikiana kwamba Waheshimiwa Wabunge wanaokuja waende Lindi na nimeshazungumza hata na ndugu yangu, viwanda vingi vitakwenda vitaanzishwa ikiwemo na kufufua vile vya zamani.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali ilisema kwamba itagawa sulphur bure na matokeo yake sulphur iliyogaiwa, nyingi ilikuwa ni feki na nyingine ilikuwa imeshapitwa na muda, yaani ime-expire. Hii inaweza kupelekea kuharibu zao hili la Korosho. Sasa Je, Serikali ikiwa kama mdhibiti, ilikuwa wapi mpaka hii sulphur ikaweza kuingia nchini na hadi kumfikia mkulima?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba, sasa hivi Mkoa wa Lindi wamelima kwa wingi zao la choroko na mbaazi ambalo wamekosa soko hadi kupelekea gunia moja la kilo 100 kuuzwa kwa Sh.15,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo miaka ya nyuma, Bunge hili lilipitisha Sheria ya Exchange Commodity ambapo ilikuwa na mpango wa kuanzisha Exchange Commodity Market na mpaka dakika hii tayari Ofisi kwa ajili ya Exchange Commodity Market imepatikana na hadi savers zimekuwa set up lakini hakuna operation zozote zinazoendelea; kitu ambacho soko hili la Exchange Commodity lingeweza kuwasaidia wakulima waweze kupata soko la uhakika kwa ajili ya mazao mbalimbali. Sasa je, Serikali ina mpango wa kuanza lini operations katika Commodity Exchange Market? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na viuatilifu au sulphur feki au iliyopitwa na wakati, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba hakuna sulphur feki wala iliyopitwa na wakati ambayo imesambazwa kwa wakulima. Naomba yeyote mwenye ushahidi wa mkulima mmoja tu ambaye ameuziwa au amepewa sulphur feki au ambayo imepitwa na wakati anipe ushahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawahakikishia kwamba hakuna sulphur feki wala ambayo imepitwa na wakati ambayo imesambazwa kwa wakulima. Kilichotokea katika taarifa zile mlizoona kwenye vyombo vya habari ni kwamba kulikuwa na sulphur ambayo iko kwenye maghala ambayo imepitwa na muda, ime-expire lakini haikuwa kwa ajili ya kugawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la commodity exchange, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa commodity exchange hautafuti soko, yaani siyo kwamba ukishatumia commodity exchange basi unakuwa na uhakika wa soko. Kama soko halipo ni kwamba halipo tu. Commodity exchange haina tofauti kimsingi na utaratibu wa sasa tunaotumia wa stakabadhi ghalani. Tofauti yake kidogo tu ni kwamba yenyewe inatumia teknolojia zaidi, lakini kama hakuna mnunuzi hutapata kwa kutumia commodity exchange.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimhakikishie kwamba Serikali kwa sasa imejiwekeza zaidi katika kuimarisha utaratibu tulionao wa stakabadhi ghalani kwa sababu ili tuweze kufikia kwenye commodity exchange tunahitaji vitu vingi. Tunahitaji kuwa na maghala ambayo ni ya kisasa zaidi, tunahitaji teknolojia, tunahitaji kuweza kuzalisha kwa utaratibu unaotakiwa na masoko ya nje lakini vilevile tunahitaji wakulima wetu waweze kuzalisha kwa viwango vile ambavyo vinahitajika. Kwa hiyo, kwa sasa jitihada ya Serikali siyo kwenye commodity exchange, tutaelekea kule, lakini kwa sasa tunaweka nguvu nyingi kwenye utaratibu wa stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta soko kwa ajili ya mazao ya mikunde. Changamoto iliyotokea ni kwamba India ambayo ndiyo nchi inayonunua mazao ya mikunde, kwa mwaka huu wana ziada ya asilimia 30 na ndiyo maana mbaazi zetu, dengu zetu na choroko zimepata changamoto. Hata hivyo kwa kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kununua mbaazi za wakulima, lakini huko mbele ya safari tunagemea tuanze kuuza zao hilo la mbaazi kwa utaratibu wa stakabadhi ghalani tukiamini kwamba kuuza kwa pamoja kutasaidia bei iwe nzuri zaidi. (Makofi)