Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Edward Franz Mwalongo (11 total)

MHE. JORAM I. HONGOLI (K.n.y. MHE. EDWARD F. MWALONGO) aliuliza:-
Uchafuzi wa Mazingira unaosababishwa na mifuko ya plastiki ni mkubwa mno nchini:-
(a) Je, Serikali haioni sasa umefikia wakati wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwawezesha wadau wa mazingira kwa kuwanunulia mashine kwa mkopo ili waweze kuchakata plastiki hizo kuzifanya kuwa ngumu na bora zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini. Katika kutekeleza hatua hii Serikali imepitia upya kanuni ya kuzuia uzalishaji, uagizaji, uuzaji, ununuzi na matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa inapiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki iliyo chini ya makroni 30 ambazo zilionekana kuwa na changamoto katika utekelezaji wake. Hivyo Serikali iliandaa Kanuni mpya ya matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2015. Kanuni hizi zinaifuta kanuni ya mwaka 2006 na kuweka viwango vipya vya mifuko na vifungashio vya plastiki kuwa na unene usiopungua makroni 50 ambayo ina uwezo wa kuoza kirahisi kwenye mazingira ukilinganisha na ile ya makroni 30.
Pamoja na kuongeza unene wa mifuko ya plastiki, kanuni hii inapiga marufuku uanzishwaji wa viwanda vipya vya kutengeneza mifuko, vifungashio vya plastiki na pia inapiga marufuku uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki ambayo ipo chini ya kiwango vilivyobainishwa na Kanuni. Hatua hii ni mwanzo wa kuelekea katika lengo la kupiga marufuku kabisa (total burn) uzalishaji na matumizi ya mifuko na vifungashio vya plastiki nchini kwa kuzingatia maoni ya wadau.
(b) Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uwekezaji katika sekta ya mazingira na kuhamasisha uwekezaji katika teknolojia rafiki wa mazingira, Serikali inaandaa kanuni na taratibu za nyenzo za kiuchumi zitakazotoa ruzuku, makato na punguzo la kodi kwa wawekezaji ili kuendeleza na kuimarisha utunzaji wa mazingira. Hatua hii itasaidia wadau wa mazingira kuwekeza katika viwanda vidogo na vikubwa vya uchakataji wa taka ikiwemo taka za plastiki.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana na fasaha ya Naibu Waziri ningependa kuongeza na kulitaarifu rasmi Bunge lako Tukufu kwamba ndani ya Serikali tunafanya mazungumzo pamoja na kuwahusisha wadau mbalimbali na naamini wakati wa bajeti ya Wizara yetu tutakuwa tumefikia muafaka, dhamira ni kwamba tarehe 1 Januari, 2017 iwe mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini, lakini tutafika pahala ambapo uamuzi huo utakapofikia basi tutalitaarifu Bunge lako Tukufu.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Serikali imeweka alama ya “X” ya kijani na nyekundu katika nyumba za wakazi wa Jimbo la Njombe Mjini kikiwemo na Kituo cha Polisi cha Njombe.
Je, Serikali inasema nini juu ya tafsiri sahihi ya alama hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na Sheria ya zamani ya Barabara ya mwaka 1932 ambayo ilirekebishwa mwaka 1967 (The Highway Ordinance CAP. 167) upana wa eneo la hifadhi ya barabara kuu na barabara za mikoa ulikuwa ni mita 45 yaani mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii naenda taratibu kwa sababu najua watu wengi sana wana-interest nalo na wananchi wasikie. Sheria mpya ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 (The Road Act, No. 13 of 2007) na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009 (The Road Management Regulations of 2009) ziliongeza upana wa eneo la hifadhi ya barabara kuu na barabara za Mikoa kuwa mita 60, yaani mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande, hivyo kuna ongezeko la mita 7.5 kila upande wa barabara kulingana na Sheria mpya ya Barabara ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na maelezo ya utangulizi napenda kutoa ufafanuzi kwamba, nyumba zilizo ndani ya eneo la mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande zipo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara kinyume cha sheria, hivyo zimewekewe alama ya “X” nyekundu na zinatakiwa kubomolewa bila malipo yeyote ya fidia.
Aidha, nyumba zilizojengwa katika eneo la kutoka mita 22.5 hadi mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande kabla ya Sheria mpya ya Barabara ya mwaka 2007 zimewekewa alama ya “X” ya kijani katika baadhi ya Mikoa kwa ajili ya utambuzi ili maeneo hayo yakihitajika kwa ajili ya ujenzi au upanuzi wa barabara wamiliki walipwe fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wananchi kutofanya uendelezaji mpya wa nyumba kwenye eneo la hifadhi ya barabara ili kuepuka hasara ya kuvunjiwa nyumba zao bila kulipwa fidia.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Baada ya ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya FDC – Njombe na kile cha Ulebwe kilichopo Wanging‟ombe.
(a) Je, ni fani zipi zitaanza kutolewa katika vyuo hivyo?
(b) Je, ni wananchi wangapi wanatarajia kufaidika na vyuo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) Njombe na kile cha Ulebwe kilichopo Wanging‟ombe, Serikali itaendelea kuimarisha na kutoa mafunzo yale yale yaliyokuwa yanatolewa hapo awali, yaani mafunzo ya ufundi stadi katika fani za ufundi magari, ufundi chuma, useremala, uashi, umeme wa majumbani, ushonaji, kilimo na mifugo katika Chuo cha Njombe na fani za useremala, ushonaji, uashi, umeme wa majumbani, kilimo na mifugo katika Chuo cha Ulebwe.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na uwezo na vyuo hivyo, Chuo cha Mendeleo ya Wananchi Njombe kina uwezo wa kunufaisha wananchi 180 wa kukaa bweni na wananchi 70 wa kutwa, wakati Chuo cha Wananchi Ulebwe kina uwezo wa kunufaisha wananchi 80 wa kukaa bweni na 40 wa kutwa na hivyo kufanya jumla ya wananchi wanufaika 370 kwa mwaka.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Kumekuwa kukitokea taarifa juu ya kuanza kazi ya uchimbaji katika Migodi ya Liganga na Mchuchuma.
(a) Je, ni lini kazi hiyo itaanza?
(b) Je, nini mazao ya migodi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi unganishi ya Mchuchuma na Liganga inatekelezwa na kampuni ya ubia kati ya NDC na Sichuan Hongda Group Limited ya China inayojulikana kwa jina Tanzania China International Mineral Resources Limited. Kampuni hii imekamilisha uchorongaji na upembuzi yakinifu wa miradi hiyo. Uchorongaji umeonesha kuwepo kwa tani milioni 428 za makaa ya mawe eneo la Mchuchuma na tani milioni 126 za chuma eneo la Liganga. Upembuzi yakinifu umeonesha Mgodi wa Chuma Liganga una uwezo wa kuzalisha tani milioni 2.9 kwa mwaka na Mgodi wa Makaa ya Mawe ulioko Mchuchuma una uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka; lakini pia uwezo wa kufua umeme wa megawati 600.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, gharama za uwekezaji katika miradi hii ni dola za Marekani bilioni tatu ambapo dola bilioni 600 ni mtaji wa mwekezaji na mkopo utakuwa dola bilioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni imekwishapata leseni maalum za uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na vibali vya mazingira mbalimbali. Pia imepata maeneo katika eneo la Katewaka pamoja na Mchuchuma na Lupali. Kazi ya uthamini na makazi na mali ya wananchi walio ndani ya maeneo ya miradi wanaotakiwa kupisha shughuli za mradi, zimekamilika na hivi sasa tathmini ya fidia iko kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na mwekezaji. Mradi huu utaanza mara baada ya kukamilisha fidia na wananchi waliopisha mradi pia na Government Notice kwa ajili ya incentive za mradi itakapotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hiyo unganishi itawawezesha kuchimba makaa ya mawe kiasi cha milioni tatu na chuma ghafi tani milioni 2.9 kwa mwaka. Aidha, sehemu ya makaa ya mawe itatumika kuzalisha umeme na nyingine kwa ajili ya matumizi ya viwandani. Vilevile sehemu ya chuma itatumika kwenye Sekta ya Ujenzi, Viwanda, Kilimo, na kadhalika, lakini madini ya vanadium yatatumika kwa ajili ya matumizi kwenye viwanda vya kemikali pamoja na magari, lakini kadhalika madini ya titanium kwa ajili ya matumizi kwenye viwanda, ndege, meli, pamoja na magari.
MHE. EDWARD F. MWALONGO Aliuliza:-
Jimbo la Njombe lina Mahakama ya Mwanzo moja tu iliyopo Njombe Mjini. Je, Serikali ipo tayari kukarabati Mahakama za Mwanzo za Mahenye na Igominyi ili wananchi waweze kupata huduma hiyo jirani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Sheria na Katiba, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Mahakama ni uhaba na uchakavu wa miundombinu. Sehemu nyingi nchini hazina majengo ya Mahakama na baadhi ya majengo yaliyopo ni chakavu na ni ya muda mrefu. Aidha, ni kweli kwamba Mahakama za
Mwanzo za Igominyi na Mahenye ni chakavu sana kiasi cha kushindwa kuendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, mpango uliopo ni kujenga majengo mapya na siyo kukarabati yaliyopo, hasa ikizingatiwa kuwa majengo haya yapo kwenye hifadhi ya barabara. Ni kweli Mahakama hizi zinahitajika sana na ni moja ya miradi ya kipaumbele katika ujenzi wa Mahakama
za mwanzo katika Wilaya ya Njombe. Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017 kipaumbele ni ujenzi wa Mahakama ya Mkoa na kwa mwaka 2017/2018 imepangwa kujengwa Mahakama ya Mwanzo Mahenye-Uwemba; na Mahakama ya Mwanzo Igominyi imepangwa kujengwa katika mwaka 2019/2020 kulingana na upatikanaji wa fedha.
Pamoja na hayo, Mahakama imeshapata nafasi katika Ofisi ya Kijiji cha Uwemba kwa ajili ya kuendesha shughuli za Mahakama ya Mwanzo Mahenye ili huduma iendelee kutolewa wakati mipango ya ujenzi inaendelea.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ujuzi wa kufanyia matengenezo vifaa tiba kutokana na ukosefu wa watu wenye utaalam huo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwa na chuo maalum kwa ajili ya kufundisha wataalam wa vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mafunzo ya wataalam wa matengenezo ya vifaa tiba yanatolewa kwenye Vyuo viwili ambavyo ni Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) pamoja na Arusha Technical College (ATC). Mafunzo haya yalianza hapa nchini mwaka 2011 kwa kufundisha Stashahada (Diploma) za matengenezo ya vifaa tiba kwa miaka mitatu, jumla ya wanafunzi 32 walihitimu mwaka 2014 ambapo wahitimu 17 walitoka DIT na 15 walitoka ATC. Wahitimu wote hao walipata ajira sehemu mbalimbali nchini. Mwaka 2015, jumla ya wataalam wengine 32 walimaliza mafunzo yao na sasa wanasubiri ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wahitimu wa fani ya ufundi wa vifaa tiba kuanzia mwaka 2016 ni 60. Idadi hii itaongezeka na kufikia wahitimu 85 mwaka 2019. Idadi ya wahitimu wote ifikapo mwaka 2025 inakadiriwa kuwa 1,107 ambayo ni sawa na asilimia 24 ya mahitaji yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho ya utoaji wa huduma za kibingwa hapa nchini kufanywa na sekta ya umma lakini pia na sekta binafsi, hasa katika kuongeza vituo vya utambuzi wa magonjwa ni dhahiri kuwa mahitaji ya wataalam hawa yataongezeka maradufu na hivyo uzalishaji wa wataalam hawa ni kipaumbele kwa Serikali na hivyo, mipango ya kuongeza vyuo vya mafunzo iko bayana.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Elimu ya ufundi ni muhimu ili kuwawezesha vijana kuajiriwa na kujiajiri:-
• Je, nchi yetu ina vyuo vingapi vya Ufundi Stadi vya Umma?
• Je, kuna vyuo vingapi visivyo vya Umma?
• Je, hivi vyote vina uwezo wa kudahili vijana wangapi kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kwa mwaka wa 2016/2017 ilikuwa na jumla ya vyuo vya ufundi stadi 127 vya umma na vyuo 634 visivyo vya umma vilivyokuwa vinatambulika na kusajiliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Vyuo 501 kati ya 761 vilipata ithibati ya VETA na viliweza kudahili jumla ya wanafunzi 56,420 kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo vya ufundi stadi vina umuhimu mkubwa wa kuandaa nguvukazi ya kutosha, mahiri na yenye ujuzi unaotakiwa ili iweze kushiriki katika kujenga uchumi wa viwanda wakati tunaelekea kwenye nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa 2016/2017 - 2020/2021 imelenga kuongeza idadi ya wahitimu katika vyuo vya ufundi stadi kutoka 150,000 kwa mwaka 2015 hadi kufikia 700,000 ifikapo mwaka 2021 ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana wenye ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itakamilisha ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi ngazi ya mkoa katika mikoa mitano na ngazi ya wilaya katika wilaya sita. Aidha, itakamilisha ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi katika wilaya mbili. Mkakati uliopo ni Serikali kuendelea kutenga bajeti ya maendeleo kila mwaka pamoja na kutafuta wafadhili mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuweza kujenga vyuo vingine.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
• Je, Serikali inatumia pesa kiasi gani kuhudumia mfungwa mmoja kwa siku kwa huduma ya chakula tu?
• Vitendo kama kulala chini, kulala bila blanketi au shuka, kulala bila neti vimekuwa vya kawaida kabisa katika Magereza yetu nchini; je, hii nayo ni sehemu ya adhabu ambayo wafungwa wanapewa kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza katika kutekeleza jukumu lake la kuwapokea na kuwahifadhi wahalifu kisheria, pia hutoa huduma ya chakula kwa wahalifu kupitia bajeti inayotengwa na Serikali kila mwaka wa fedha. Gharama ya chakula kwa mfungwa mmoja kwa siku ni wastani wa shilingi 1,342.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za wafungwa na mahabusu Magerezani kwa kununua vifaa mbalimbali vya malazi ikiwemo magodoro, shuka, mablanketi na madawa ya kuua wadudu kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa msingi huo inapotokea ukosefu wa huduma hizo, inakuwa siyo sehemu ya adhabu kwa wafungwa bali hutokea kutokana na idadi kubwa ya wafungwa gerezani.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Watendaji wa Vijiji ni kada muhimu sana katika kuwahudumia wananchi walio vijijini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara watumishi hawa ili kuboresha utumishi wao na utoaji huduma kwa wananchi walioko vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji wa Vijiji kama walivyo watumishi wengine wa umma wanapaswa kupewa mafunzo mara kwa mara ili kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi. Mafunzo yanayotolewa kwa Watendaji wa Vijiji hujumuisha masuala ya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya UKIMWI mahali pa kazi, maadili ya utumishi wa umma pamoja na majukumu yao katika utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia ruzuku ya maendeleo kwa Serikali za Mitaa ambayo inajumuisha Mpango wa Mafunzo kwa watumishi wa kada mbalimbali, Watendaji wa Vijiji 1,840 walipewa mafunzo katika mwaka wa fedha 2016/17. Kuanzia Julai 2017 hadi Aprili 2018 kwa mwaka huu unaoendelea, Watendaji wa Vijiji 1,543 wamepewa mafunzo. Mpango huu ni endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuziagiza halmashauri zote nchini kuweka kipaumbele na kutenga bajeti ya mafunzo kwa kada hii muhimu na kuanzia mwakani tutaanza kufuatilia utekelezaji wa agizo hili ili kuhakikisha kuwa limezingatiwa na halmashauri zote wakati wa bajeti.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Hospitali ya Kibena ni kongwe sana na imechakaa sana:-
Je, ni lini Serikali itaifanyia ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuifanyia maboresho Hospitali ya Kibena katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2018/2019. Kwa sasa Serikali inafanya upanuzi wa jengo la radiolojia ili kusimika mashine mpya ya X-Ray. Ujenzi huu utagharimu jumla ya Sh.39,750,000. Vile vile upanuzi wa jengo la upasuaji unaendelea chini ya ufadhili wa Shirika la UNICEF.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe katika eneo la Wikichi ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali ilipeleka kiasi cha Sh.3,234,787,370 ambazo zimeweza kutumika katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambao umekamilika kwa asilimia 95.
Mheshimiwa Spika, vile vile, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo kwa kujenga majengo ya X-Ray, upasuaji, uchunguzi wa maabara na kichomea taka hatarishi. Sanjari na hilo, kupitia fedha za Global Fund, hospitali itajengewa jengo la huduma ya mama na mtoto na hivyo kuifanya hospitali hii kuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu za afya katika Mkoa wa Njombe.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwahudumia wagonjwa wa akili wanaozurura mitaani katika masuala ya matibabu, mavazi na makazi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kuimarisha huduma za afya nchini ikiwemo huduma ya afya ya akili. Uimarishaji wa huduma ya afya ya akili umekwenda mpaka katika ngazi ya afya ya msingi ambapo ndipo jamii ilipo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuongezeka kwa wagonjwa wa akili wanaorandaranda barabarani, Sheria Afya ya Akili ya mwaka 2008 inawataka ndugu na jamii kuibua wagonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma ili wapate matibabu. Wagonjwa wakishapata nafuu huruhusiwa kwenda kukaa na familia zao kwenye jamii wanazotoka. Jukumu la kwanza la kulinda afya ya jamii huanzia ngazi ya familia lakini jamii zetu zimekuwa zikiwanyanyapaa, kuwabagua na kuwatenga wagonjwa wa akili na kupelekea wagonjwa wa akili kurandaranda mtaani.

Mheshimiwa Soika, kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, Sehemu ya Tatu, kifungu cha sheria namba 9(1)(3) imeeleza wazi kuwa Afisa Polisi, Afisa Usalama, Afisa Ustawi wa Jamii ngazi ya Wilaya pamoja na viongozi wa dini, Afisa Mtendaji wa Kata, Afisa wa Kijiji wana jukumu la kubainisha mtu yeyote anayerandaranda kwa kutishia amani au vinginevyo na kumfikisha kwenye sehemu ya uchunguzi wa magonjwa ya akili na ikithibitika taratibu za kumpatia matibabu huanza kama ilivyoainishwa kwenye Sehemu ya Tatu ya Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, kifungu namba 11(7)(12) cha sheria hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa rai kwa jamii kuibua watu wanaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo cha afya ili waweze kupata matibabu kwani huduma hii ipo na inatolewa bila gharama yoyote. Magonjwa ya akili yanatibika, hivyo, nitoe rai kwa jamii waache kuwanyanyapaa wagonjwa wa akili na badala yake wawafikishe kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuwa ugonjwa wa akili hauna uhusiano na imani za ushirikina.