Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edward Franz Mwalongo (42 total)

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Njombe Mjini halimo kwenye mpango wa REA limo kwenye mpango wa umeme unaoenda Songea, hiyo kazi hiyo haijaanza.
Je, ni lini kazi hiyo itaanza ili kusudi wananchi wa Njombe na wenyewe waweze kunufaika na umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Njombe siyo kwamba hawatapata umeme wa REA wataendelea kupata umeme wa REA kama kawaida, lakini chanzo cha umeme kwa wananchi wa Njombe, Ludewa, Songea Mjini, Songea Vijijini, Namtumbo ni pamoja na ule umeme wa Makambako - Songea ambao ni wa Kilovoti 220.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge, nakushukuru kwamba kwa sababu hujaona chini, watu nguzo wanaweka chini lakini kazi imeshaanza. Kazi za awali za upembuzi yakinifu zimekamilika na taratibu za Mkandarasi za kuanza kazi zimekamilika, kufikia Januari mwaka unaokuja kazi rasmi za kutifua na kuweka nguzo zitakuwa zimeshaanza kabisa.
MHE. EDWARD F. MWALONGO:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, naomba nimuulize Naibu Waziri je, katika suala la ruzuku hiyo ambayo inakuja Serikali inaonaje sasa ikatoa upendeleo kwa wakulima kwamba mkulima awe ndio mwenye kuchagua mbolea anayoihitaji kwa ajili ya mazao anayolima badala tu ya kulazimisha kwamba mkulima ni lazima achukue mbolea ya kupandia mahindi, ama ni lazima achukue mbolea ya kupandia mpunga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kabisa kwamba kumekuwepo na changamoto ya utaratibu wa kuwalazimisha wakulima wote kuchukua mbolea inayofanana na ruzuku nyingine zinazofanana. Nimhakikishie tu kwamba kwa sababu pendekezo lake linakuja katika wakati muafaka, wakati tunajaribu kurejelea utaratibu huu, tutahakikisha kwamba tunaweka utaratibu wa kuwafanya wakulima vilevile waweze kuwa na uchaguzi kutegemeana na kitu wanacholima.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema tusiweke karakana kwenye shule za msingi lakini kuna vituo vya shule za msingi ambavyo vina ufundi, watoto huwa wanachaguliwa darasa la saba wengine wanakwenda sekondari wengine ufundi na vituo hivi vipo kwenye shule za msingi na vina fani za useremala. Je, Serikali iko tayari kusaidia kituo kama cha Shule ya Msingi Uwemba ili kusudi kiweze kutengeneza madawati kwa ajili ya Jimbo la Njombe Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna shule zingine zina karakana na hii nadhani ni kutokana na maelekezo kwamba tuwafunze wanafunzi wetu masomo ya ufundi. Kama shule ina kiwanda cha ufundi maana yake hata kiwanda chake kimewekwa kwa minajili kwamba hakitaathiri mazingira ya shule. Miongoni mwa zile shule ambazo tutazibainisha ni shule ambazo ndani yake zina karakana. Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni jukumu lake kubwa kuangalia shule hizi sasa zinashiriki vipi, siyo kuziwezesha peke yake, isipokuwa kuona kwamba programu hii inakuwa endelevu ili vijana watakaotoka hapo wawe na ufundi bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba na mimi nitatamani sana nikifika Jimboni kwake anipeleke katika shule hiyo ili kwa pamoja tubadilishane mawazo kuhusu kuisaidia shule hiyo. Lengo likiwa ni kuongeza stadi za kazi kwa wanafunzi wetu lakini kurahisisha mambo mengine ambayo yanaweza kufanyika katika Halmashauri husika yaweze kwenda vizuri.
mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutoa majibu mazuri juu ya barabara hii ya Njombe - Makete, lakini pamoja na barabara hii ya Njombe - Makate ndani ya Mkoa wa Njombe tuna barabara nyingine zinazounganisha na Mkoa; iko barabara ya Itoni - Ludewa inayopitia kwenye kata za Uwemba, kata ya Luponde, kata ya Matola. Na sasa hivi kule Ludewa wanaanza kulipa fidia kwa ajili ya kuanza uchimbaji wa madini, barabara hii imekuwa ikiharibika sana haioneshi kwamba kuna fedha inayotosheleza kujenga hii barabara. Je, Mheshimiwa Waziri anatuambiaje sisi wana-Njombe juu ya barabara ya Ludewa - Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, alishiriki katika kuipitisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, na anafahamu katika bajeti hiyo tuliongea kabla na tukahakikisha tunatenga kilometa 50 za kujenga katika mwaka huu wa fedha. Na kwa sababu, bajeti imeshapitia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kazi yetu ni moja tu, kutekeleza eneo hilo ambalo bajeti imeipitisha.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni kwa nini sasa katika yale madarasa ya awali ukiangalia fungu lile la elimu bure wanapotoa ile fedha, wale watoto wa madarasa ya awali hawapati ile fedha na inawafanya wazazi waendelee kuchangia yale madarasa ya awali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema katika majibu yangu ya msingi, ukija kuangalia maeneo mbalimbali ambapo watoto wale wa awali waliokuwa wakienda shuleni, mara nyingi sana walimu waliokuwa wanafundisha utakukuta ni walimu waliokuwa wanachukuliwa mtaani, waliomaliza form four, darasa la saba ambaye anaweza akafundisha. Katika maelekezo ya utaratibu wetu wa elimu, wale watu wote wanaomaliza grade „A‟ wanakuwa na component ya elimu ya awali. Kwa hiyo, utakuja kuona kwamba, wakati mwingine watoto walikuwa wakienda shule wanalazimishwa walipie fedha kwa ajili ya mwalimu wa awali, jambo lile tumesema kwamba, walimu wote sasa hivi wanaomaliza grade „A‟ walimu wale wanaopelekwa mashuleni, kuna mwalimu anayefundisha darasa la awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yetu kama Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ni kuhakikisha Wakurugenzi, wanahakikisha katika allocation ya wale walimu katika shule mbalimbali, wawapeleke walimu ili kusaidia kuondoa ule utaratibu wa wazazi kuwa wanachanga kwa ajili ya kumchukua mtu mtaani kuja kufundisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili tumeenda mbali zaidi, ndiyo maana watu walioshudia mwaka jana hapa katika Chuo chetu cha UDOM, tulipeleke takribani walimu wapatao 17,000 katika somo la KKK. Lengo ni kuwawezesha watoto wanapoingia shuleni kuanzia awali na watoto wa darasa la kwanza waweze kujua kusoma na kuandika.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ni kweli Serikali tunajua changamoto ni nyingi kutokana na suala la elimu bure, lakini Serikali inaangalia jinsi gani tutatatua matatizo mbalimbali. Mara baada ya kufanya jambo hili tumegundua jambo changamoto nyingi zimeweza kujitokeza, changamoto hizi ni kutokana na hii fursa sasa, Serikali ya Awamu ya Tano iliweza kufungua sasa na kupitia hizi changamoto, ndiyo tunaenda kuhakikisha kwamba tunalijenga Taifa la kupata elimu bora. Changamoto hizi, tutakuwa tunazitatua awamu kwa awamu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri Jafo, ninataka kuongezea kwenye swali alilokuwa analijibu hivi punde kwamba, isichukuliwe kwamba watoto wanaojiunga kwa darasa la awali ni tofauti na watoto wanaoanzia darasa la kwanza mpaka la saba. Wote ni wanafunzi isipokuwa tu wale wana special treatment, lakini fedha inayopelekwa kwa ajili ya uendeshaji wa shule, ndiyo hiyo itumike katika kuendesha na mahitaji ya wale watoto wa awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa tunafahamu Serikali kwamba mahitaji ya watoto wa awali ni maalum sana. Jitihada kubwa itakayokuwa inafanyika ni kuona namna gani tutaongeza hii bajeti, pia kutafuta facilities kwa ajili ya watoto hawa wa awali kwa sababu namna yao ufundishwaji ni tofauti na hawa wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii tu kuwaomba Walimu Wakuu wa shule na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya kuhakikisha kwamba hawatenganishi zionekane kwamba kuna shule ya awali na shule ya msingi inayoanzia darasa la kwanza. Hii shule ni moja na ndiyo maana hata walimu wake ni walewale, kwa sababu wale walimu wanaomaliza grade „A‟ wanakuwa wana component ambayo wamefundhishwa namna ya kufundisha watoto hawa wa madarasa ya awali.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri, kwa kuwa suala hili linawagusa karibu Watanzania wote na mimi nitajitahidi kwenda polepole kama alivyoenda yeye polepole. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nyumba nyingi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwalongo naomba usiende polepole kwa sababu muda wetu unakimbia sana na watu wana maswali mengi. (Makofi/Kicheko)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nyumba nyingi katika Mji wa Njombe zimewekewa alama ya kijani. Serikali haioni ipo haja ya sasa kufuta alama hizo ili kuwapa fursa wananchi wamiliki wa nyumba hizo kufanya ukarabati wa nyumba zao na kuzitumia nyumba zao kama dhamana katika taasisi za fedha? (Makofi)
Swali la pili, je, Serikali haioni sasa upo ulazima kuleta Sheria Namba 13 ya mwaka 2007 tuifanyie marekebisho ili ibainike bayana kwamba, maeneo ya mjini yawe na upana wa mita 42 badala ya 60 za sasa. Hii itasaidia kutunza historia za miji katika nchi yetu, lakini vilevile itaipunguzia gharama Serikali pamoja na wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka „X‟ ya kijani kama ishara kwamba hilo eneo haliruhusiwi kuendelezwa, haliruhusiwi kujengwa nyumba mpya kwa sababu ni eneo la hifadhi ya barabara kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 2007. Kwa hiyo, kusema wafute na ianze kutumika kama dhamana siyo sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Watanzania wote wakati tunapitisha sheria hii tulikuwa na malengo ya kuiendeleza nchi yetu kimiundominu, tupate fursa ya kupanua barabara na hatimaye zitupeleke katika karne ya viwanda, tuwe na maendeleo makubwa na huko ndiyo tunakoenda hatuwezi kurudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, suala la kubadilisha sheria, kwanza mimi binafsi na niliongea na Mheshimiwa Waziri wangu naongea kwa niaba yake kwa kweli tulitaka tupanue zaidi kwa sababu sasa hivi tunaenda kwenye miundombinu, sehemu za mijini kuna flyovers na highways lazima tuwe nazo ambazo zinahitaji ardhi kubwa zaidi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Naibu Spika kama ifuatavyo:- (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, alama ya kijani ama nyekundu, maana yake nyumba hiyo haitakiwi kuwepo hapo kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 2007. Tunachotaka, wale ambao walijenga kabla ya mwaka 2007 haki yao inayoongelewa hapa ni ya kufidiwa, siyo kuendelea kukaa, ila hatuwaondoi mapema mpaka pale tutakapokuwa na mahitaji ndipo tutakapowafidia. Ila tutakachokifidia ni kile kilichofanyika kabla ya mwaka 2007. Chochote kitakachokuwa kimefanyika baada ya mwaka 2007 kitabomolewa bila fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hiyo ya kubadilisha sheria mimi binafsi siiungi mkono lakini tumechukua ombi lako na tutaliwasilisha Serikalini likajadiliwe ili maamuzi ya Kiserikali yatolewe.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri watu wengi wamesimama, lakini nadhani swali la msingi hapo ni kwamba hawa watu wenye kijani umesema mpaka mtakapohitaji barabara. Kama jibu ni hilo, hawa watu waendelee kusubiri? Kama utaihitaji barabara baada ya miaka kumi, wao inabidi waendelee kusubiri wasifanye chochote kwenye hayo maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Naibu Spika kama ifuatavyo:- (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, alama ya kijani ama nyekundu, maana yake nyumba hiyo haitakiwi kuwepo hapo kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 2007. Tunachotaka, wale ambao walijenga kabla ya mwaka 2007 haki yao inayoongelewa hapa ni ya kufidiwa, siyo kuendelea kukaa, ila hatuwaondoi mapema mpaka pale tutakapokuwa na mahitaji ndipo tutakapowafidia. Ila tutakachokifidia ni kile kilichofanyika kabla ya mwaka 2007. Chochote kitakachokuwa kimefanyika baada ya mwaka 2007 kitabomolewa bila fidia.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kabla hujatoka, alama nyekundu ni kwamba wale watu wanatakiwa kubomoa wasiwepo; alama ya kijani maana yake sheria imewakuta. Sasa ndiyo anauliza Mheshimiwa Mwalongo wanatakiwa kusubiri muda gani hao wenye alama ya kijani ambao sheria imewakuta?
Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hii alama ya kijani, hili tutalichukua na tutaliangalia tuone tutafanyaje.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tukiachana na hayo ya huko Ndembela, naomba sasa maswali ya nyongeza nielekeze Njombe kwa maana hii nafasi ni fursa kwangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imesema kwamba, Shule zote za Kata ambazo zinakidhi vigezo vya kuwa shule za bweni iko tayari kuzichukua na kuzifanya kuwa shule za bweni. Je, baada ya kuzichukua hizi shule kuwa za bweni zitakuwa zinachukua wanafunzi kutoka ndani ya eneo la kata kama ilivyo sasa ama zitachukua kama shule za Kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali iko tayari kutuma wakaguzi kwenda kukagua Shule ya Sekondari Uwemba na Shule ya Sekondari Matola zilizoko ndani ya Jimbo la Njombe Mjini ili ziweze kuwa shule za Kitaifa na kupata hiyo keki ya Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika harakati za ujenzi wa miundombinu ya shule za sekondari toka ilipoanza Awamu ya Nne changamoto kubwa ilikuwa ni suala zima la kuwasaidia vijana jinsi gani waweze kufikia elimu ya sekondari. Mchakato huu umefanyika kwa jitihada kubwa sana ndiyo maana tunaona shule nyingi za sekondari za kata zimejengwa. Baada hapo, tumekuja kugundua kuna changamoto kwamba vijana wa sekondari za kata wanakosa kwenda Form Five and Six kwa kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanafaulu lakini nafasi ni chache. Sasa tumetoa maelekezo kwamba shule hizi sasa zipanue wigo na kuzifanya sekondari hizi kuwa na mabweni ili baadaye ziwe na Form Five na Form Six.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake specific lilikuwa linasema ni jinsi gani zile shule za sekondari za kata zilizokuwa na mabweni zitahuishwa rasmi ili ziwe sekondari za bweni za kitaifa. Naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa shule ambazo zitakidhi vigezo zitajadiliwa katika vikao husika vya Halmashauri na kupelekwa Wizara ya Elimu. Wizara ya Elimu itafanya tathmini ya kina ili kuona kama shule husika ina hadhi ya kupandishwa daraja na ikijiridhisha itapandishwa daraja rasmi na kuwa shule ya sekondari ya bweni. Hata hivyo, naomba niseme kwamba Serikali haiwezi kupandisha shule zote za kata kwa mara moja kuwa sekondari za bweni kwa sababu jambo hili vilevile lina changamoto ya kibajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili aliuliza ni jinsi gani hizi shule mbili za Uwemba pamoja na nyingine aliyoitaja zitapandishwa rasmi daraja. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya awali kwamba tufanye mchakato ule wa kawaida baada ya mchakato huo, Wizara ya Elimu itaangalia na wataalam watafika watafanya tathmini kama vigezo vitakuwa vimefikiwa Serikali itaona jinsi gani ya kufanya.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niulize swali dogo tu la nyongeza kwa maslahi ya Polisi wa Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi limekuwa likijishughulisha sana na kusaidia polisi, lakini hali ya polisi katika Mkoa wa Njombe ni mbaya sana. Mkoa huu umeanza mwaka 2012 na mpaka leo hawana nyumba hapa moja.
Je, Mheshimiwa Waziri atanihakikishia kwamba katika nyumba hizo 4,136 zipo zitakazo jengwa katika Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uanzishwaji wa mikoa mipya ikiwemo Njombe, Geita, Simiyu na Mkoa mpya wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba, Wizara yangu itahakikisha kwamba katika huu mpango kabambe tunaouzungumza mikoa mipya itapewa kipaumbele na nimhakikishie kwamba Njombe, makazi ya askari wetu pamoja na vituo vyetu vitaimarishwa.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Ulebwe ni chuo ambacho kina eneo linalozidi hekta 94 na kwa sasa hivi ninavyoongea, kina wanafunzi 64 tu.
Je, Serikali haioni kwamba sasa kutokana na mazingira mazuri ya Ulebwe kuna ulazima wa kubadilisha mifumo katika chuo kile na kuimarisha fani za kilimo na mifugo ili kusudi vijana wa Njombe waweze kunufaika na chuo kile? (Makofi)
Swali la pili, vijana wengi wamekuwa hawasomi hivi vyuo kwa sababu ya mfumo wanautumia kufundishia ambao ni wa VETA ambao sasa unatumia zaidi lugha ya Kiingereza katika mitaala pamoja na mafunzo yote na vijana wengi hawana uwezo wa lugha hiyo ya Kiingereza; je, Serikali iko tayari kuandaa mitaala ya Kiswahili ili iweze kuwasaidia vijana wadogo wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari waweze kunufaika na haya mafunzo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kubadilisha mafunzo katika chuo hicho, napenda tu kumfahamisha Mheshimiwa Mwalongo kwamba kwa mujibu wa Katiba yetu kifungu cha 9(i) kinazungumzia kwamba utajiri wa nchi na rasilimali utaelekezwa zaidi katika kuhakikisha kwamba unatoa umaskini, maradhi na ujinga katika maeneo yetu yote. Vilevile inaendelea kwa kusema kwamba haki ya kupata mafunzo au elimu ni ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo hivi vya FDC vilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi wote hata wale ambao hawajafika kidato cha nne au darasa la saba wanapata mafunzo na kuweza kuwasaidia kukimu katika maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni mtazamo wangu kuona kwamba vyuo hivyo viimarishwe ili kuweza kutoa mafunzo kwa wananchi wengi zaidi ambao bado tunao katika maeneo yote. Sio wote kwamba wamefika darasa la saba au kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la kufanya mafunzo haya lazima yafanane na VETA, Wizara inaona kwamba iko haja ya kuona kwamba mafunzo yanayotolewa katika vyuo hivi vya FDC yanakidhi uwezo wa wananchi hao kuweza kuyatumia kikamilifu kwenye kazi zao na hivyo siyo lazima yafundishwe kama ilivyo Vyuo vya VETA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo, naona kwamba kwa siku za nyuma kulitokea na mkanganyiko kidogo wa kuona kwamba Vyuo vya VETA ni bora kuliko FDCs, lakini tungependa kuona kwamba FDCs zifanye kazi kwa malengo yake na VETA zifanye kazi kwa malengo yake, lakini vyuo vyote viimarishwe na kuweza kutoa mafunzo stahiki kwa walengwa wanaohusika.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, imeshajionesha kwamba katika machimbo mbalimbali ya madini, wananchi wanaozunguka maeneo hayo huwa wanaathirika sana na pia wanakuwa hawana shughuli ya kufanya katika ile migodi. Sasa kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Njombe ni wananchi wanaojituma sana kwenye kilimo, je, Serikali iko tayari sasa kuanza mchakato maalum wa kusaidia wananchi wanaozunguka maeneo yale hasa Jimbo la Ludewa na Njombe Mjini, waweze kuwa tayari kuzalisha bidhaa za chakula kitaalam, pindi migodi hii itakapoanza waweze kunufaika na soko litakalokuwepo pale migodini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Mwalongo kwa jinsi anavyofuatilia kwa ukaribu suala hili kwa manufaa ya wananchi wa Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za Serikali zinazochukuliwa kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika hasa katika masuala ya local content kwa maana ya ushirikishwaji, Serikali imechukua hatua kadhaa; mojawapo ni pamoja na kuitaka kampuni itakayowekeza kutoa elimu pamoja na mikopo ili kuwawezesha wananchi hao kunufaika na rasilimali hiyo. Katika kazi hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nimshukuru sana, vijiji vya Itoni pamoja na Nanundu ambayo ipo katika maeneo yale, vimeshapewa elimu kwa ajili ya ulimaji wa mboga mboga, lakini pia katika shughuli za kufuga kuku pamoja na kufuga nguruwe. Kwa hiyo, wananchi wataweza kufanya kazi kwa ajili ya kujiwekeza kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze tu kwamba Serikali kwa kushirikiana na kampuni, kampuni itaanza kutoa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wanaozunguka mgodi ule kufanya shughuli ndogo ndogo za kiuwekezaji ili pia sasa waanze kushiriki mara baada ya mradi kuanza kwenye shughuli za kibiashara na za kiuchumi katika maeneo yale. Inatoa elimu, lakini inatoa mikopo ya masharti nafuu ili wananchi waanze kufanya hivyo. Utaratibu huu ulianza tangu Oktoba, 2012 na unaendelea hadi sasa.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika ahsante kwa kunipa nafasi. Nashukuru kwa majibu mazuri
ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza:-
Pamoja na Mahakama hiyo lakini liko tatizo kubwa sana la Mabaraza ya Kata. Mabaraza ya Kata yamekuwa ni
mwiba mchungu sana kwa wananchi katika maeneo mbalimbali na hasa hasa katika Jimbo la Njombe. Kinachosababisha, moja; ni kukosa weledi. Je, Serikali sasa ipo tayari kuajiri mtaalam mmoja mmoja katika Mabaraza ya Kata ili asaidiane na wale wananchi wanaokuwa wajumbe wa Mabaraza haya ili kupunguza matatizo
yanayojitokeza kwa kukosa utaalam?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali ipo tayari kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Mabaraza haya ya Kata ili
kusudi wanapofanya kazi zao za kusuluhisha migogoro mbalimbali kwa wananchi wawe na uelewa? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuhusiana na kuongeza idadi ya watumishi katika mabaraza ya kata. Nimhakikishie tu kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa ikifanya kazi nzuri katika kuyasimamia mabaraza haya na lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba Mabaraza haya ya Kata pamoja na Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya pamoja na mahakama zetu zote zinasogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kuwa na miundombinu, vitendea kazi, lakini pia kuwa na watumishi wa kutosha kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tunalipokea, tutalifanyia kazi na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, kwamba, endapo Serikali tupo tayari kutoa mafunzo kwa watendaji
hawa katika Mabaraza ya Kata; nimhakikishie ndiyo na Ofisi ya Rais TAMISEMI imekuwa ikifanya hivyo kila mara ili
kuhakikisha kwamba wanaenda na wakati, wanafahamu sheria na masuala mengine wanayosimamia.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa hitaji la vyuo vya ufundi kwenye nchi yetu liko juu sana na uwezo wa Serikali unaonekana kwamba ni mdogo kuwezesha kujenga vyuo vya VETA nchi nzima kwa wakati mmoja. Je, Serikali iko tayari kutumia fursa tulizonazo kwenye shule zetu za sekondari kujenga karakana ya fani angalau moja kila shule ya sekondari ili kuwezesha vijana wengi kupata elimu ya ufundi na kurejesha elimu hiyo katika shule za sekondari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kupitia Sera yetu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya Mwaka 2014, Wizara inaangalia kwa umakini uwezekano wa kuongeza nafasi za udahili kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata fursa hizo. Kisera ni kwamba tungehitaji kuona mwanafunzi akisoma moja kwa moja mpaka kidato cha nne na kwa misingi hiyo kuna mambo mbalimbali ambayo yanaangaliwa ili kwa pamoja tuone kwamba ni jinsi gani tutaweza kuangalia mafunzo ya kawaida na vilevile mafunzo ya ufundi ili kuwezesha fursa hizo kupatikana.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Hospitali ya Wilaya ya Njombe, Kibena ni hospitali ambayo sasa inasomeka kama Hospitali ya Mkoa na inahudumia watu wengi sana. Pale kuna tatizo kubwa la watoto njiti na hakuna chumba cha kutunzia watoto hawa njiti. Je, Serikali iko tayari kutusaidia kupata chumba cha watoto njiti pale ili tuweze kuokoa maisha ya hawa watoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuchukue concern hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anafahamu tulikuwepo pale Hospitali ya Kibena. Tutajadili kwa pamoja ili tuone nini tufanye ili eneo lile ambalo ni Makao Makuu ya Mkoa pale sasa, japo katika hospitali ile angalau tuweze kupata centre maalum kwa ajili ya watoto njiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa pamoja kujadili nini tufanye kwa ajili ya Hospitali ya Kibena pale iweze kutoa huduma kwa ajili ya wananchi wetu.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza ninalo. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwasaidia vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi kama hao wa Makete kupata angalau vifaa tu vya kuanzia kazi?
Swali la pili, Halmashauri ya Mji Njombe ina shule za sekondari 22 na zoezi hili la kujenga Vyuo vya Ufundi linaonekana sasa kwa Serikali limekuwa gumu sana na linakwenda pole pole sana.
Je, Serikali ipo tayari kupokea ushauri, sasa ianze kuzibadilisha baadhi ya shule za sekondari kuwa shule za ufundi ili kusudi vijana wetu walio wengi watakaokuwa wanahitimu Kidato cha Nne waweze kuwa mafundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kimsingi ni kwamba VETA imekuwa ikifanya hivyo baada ya kumaliza mafunzo ya ufundi kwa baadhi ya wanafunzi wanaohitimu wamekuwa wakipewa vifaa kwa ajili ya kuanzia shughuli zao za kiufundi, pia kusaidia kutengeneza clusters za hao wanaokuwa wamehitimu pamoja na wengine ambao wamekuwa wamehitimu mafunzo ya ufundi siyo tu kupitia VETA hata kupitia kwa wananchi wa kawaida, tunawatambua na kuweza kuwapa vifaa, vilevile kuwatambua rasmi na kuweza kuwapa vyeti.
Swali la pili la kuweza kubadilisha shule ziwe za ufundi, Wizara tayari tumeshaliona hilo na tunafikiria kubadilisha baadhi ya shule za sekondari hasa zilizokuwa shule za ufundi kama Ifunda, Mtwara, Tanga, Bwiru na shule ya Musoma ili ziweze kuwa vyuo vitakavyoweza kutoa mafunzo kwa ajili ya technicians.
Kwa hiyo, muda ukikamilika tutafanya hivyo na kwa mwaka huu tunategemea tuanze kujenga shule mbadala kwa sababu shule hizi zinachukua wanafunzi wa sayansi kwa kidato cha tano na sita na form one mpaka form four tunawajengea shule yao ili hayo majengo ambayo ni muhimu sana kama workshops yaweze kutumika kwa Vyuo vya Ufundi.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali moja tu la nyongeza, lakini naomba nitoe na ushauri kwa Serikali. Kwanza kabisa nitoe ushauri kwamba kuongeza vyuo haitakuwa msaada mkubwa sana, niombe sana sasa Serikali ione umuhimu wa kuboresha mafunzo katika hivi vyuo viwili. Dar es Salaam Institute pamoja na Arusha Technical kwa kuongeza vifaa vya kufundishia vijana hawa na kuboresha ufundi. Kwa sababu Serikali inaposema asilimia 24 itakuwa imefikiwa mwaka 2015 maana yake hali ni mbaya sana. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iliangalie hilo iboreshe mafunzo katika vyuo hivi vilivyopo na wafundishe mpaka level ya degree.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na wataalam hawa kutengeneza vifaa vya tiba, lakini wako wataalam wa kupima kwa kutumia hivi vifaa wajulikanao kwa jina la Radiologists, Halmashauri ya Mji wa Njombe katika Hospitali yake ya Kibena ina wataalam hawa wawili lakini ni wa daraja la pili. Je, Serikali iko tayari kutuletea Radiologist Grade One ili aweze kutumia mashine ambayo Halmashauri tumeinunua pale katika Hospitali yetu ya Kibena?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ushauri wake tumeupokea, lakini kwa sasa tupo katika jitihada za makusudi za kuongeza idadi ya wadahiliwa kwenye fani mbalimbali za Uhandisi wa vifaatiba, lakini pia Serikali kupitia vyuo vyake vikuu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) kwa ajili ya kutengeneza mtaala ambao utatumika kufundisha hao wanafunzi wa uhandisi kwenye eneo la vifaatiba kwa sababu tunakoelekea teknolojia ya vifaatiba itaendelea kuongezeka, kukua kwa kasi na tunaendelea kuingiza nchini kama nilivyotoa maelezo yangu hata jana hapa. Kwa msingi huo, mafundi hawa lazima tuwe nao wa kutosha. Kwa hiyo, tumeona tuanzishe degree ya Uhandisi wa Vifaatiba kwenye Vyuo Vikuu vya Muhimbili pamoja na kile cha Dar es Salaam. Malengo ni hayo ya kukabiliana na mahitaji ambayo yanajitokeza nyakati na nyakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia swali lake la pili kuhusu kupeleka mtaalam wa kupima mionzi (Radiologist) pale Kibena, naomba nilichukue ombi lake na pindi tutakapokuwa tunaajiri wataalam na kuwatawanya kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu tutazingatia ombi la Mheshimiwa Mbunge.(Makofi
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA imepokea kazi hizi za barabara katika Halmashauri zetu, sasa katika masuala haya ya barabara katika Halmashauri tulikuwa tunakarabati barabara hata katikati ya msimu, inaweza ikatokea mvua nyingi ikasomba barabara, Halmashauri ikatoa lori, wananchi wanashiriki kujenga ile barabara.
Je, katika kipindi hiki cha TARURA, wataendelea kufanya hiyo Kazi? Kwa sababu sasa TARURA haina malori, Halmashauri ina malori haina mafungu ya barabara, lakini TARURA wana mafungu hawana malori. Hapa huu utaratibu wa kurekebisha hizi barabara utakuwaje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo wala kwanza halina mashaka, kwa sababu jukumu hili sasa liko chini ya TARURA. Lakini ufahamu siyo Halmashauri yako peke yake, kuna Halmashauri mbalimbali wengine wana greda. Nafahamu magreda haya au malori haya sio kwamba yatakuwa yanafanya kazi peke yake lakini inawezekana ni kitega uchumi cha kwenu ninyi kama Halmashauri. Wakati TARURA inafanya kazi yake, wakati inatekeleza kupitia Meneja wa TARURA katika ngazi husika lazima kama utaratibu wa kukodi malori utafanywa katika utaratibu ule usiokuwa na kikwazo. Kwa hiyo, kama mna malori yenu, mna magreda yenu ambayo nanyi ni sehemu ya kitega uchumi kwenu barabara zitakapokuwa zinajengwa katika maeneo yale kama mtakuwa na utaratibu wa kukodisha jukumu kubwa ni kwamba TARURA itemize wakibu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mwalongo naomba usihofu kila kitu kitaenda vizuri, ni kipindi cha mpito tu kina mashaka kwa sababu ni jambo jipya lakini jambo hili litakuwa halina matatizo ya aina yoyote, tutafika muda mtaona kila kinaenda vizuri katika Halmashauri zetu.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kalenga pamoja na kazi nzuri inayofanyika wakandarasi hawa wanapeleka umeme lakini hawafikishi kwenye Taasisi za umma kama zahanati shule.
Je, Serikali inatoa msisitizo gani na kuwafariji hawa wanchi wa Kalenga juu ya utekelezaji wa mradi huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika Jimbo ya Njombe Mjijini yupo mkandarasi anayetekeleza mradi wa Makambako - Songea. Mradi hule ulikuwa-designed miaka mingi sana, matokeo yake ni kwamba mitaa imepanuka na maeneo yamepanuka na yule anatumia mchoro wa miaka mingi iliyopita.
Je, Serikali inatusaidiaje sasa ili kusudi mradi ule wa Makambako - Songea inaopisha umeme katika vijiji, umeme ule uweze kufika vitongoji vyote na taasisi za umma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza lilijielekeza kwenye taasisi za umma ambazo hazifikiwi na Mradi wa REA unaoendelea. Ningependa kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye Mkoa wa Iringa kuna mradi wa densification unaotekelezwa kwa ajili ya maeneo ambayo yalirukwa kwenye Awamu wa Pili. Inaangalia maeneo ya umma, taasisi mbalimbali, iwe hospitali, ziwe shule za msingi na kadhalika. Kwa hiyo nimuhakikishie kwamba mradi wa densification unafanya hiyo kazi katika Mkoa wa Iringa na mkandarasi anaendela na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, aliulizia juu ya mradi wa Makambako - Songea. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwamba katika mradi huu wa Makambako Songea ujenzi wa laini wa msongo wa KV 220 kwanza kazi inaendela vizuri lakini pia swali lake alikuwa anauliza je maeneo ambayo vijiji vinavyopitiwa na msongo huo usambazaji wa umeme ukoje. Nimthibitishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ya kusambaza umeme itaendelae na maeneo ambayo yataachwa REA III itaendelea kuya-cover kwasababu mpango wa Serikali ya Awamu Tano ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata umeme ifikapo 2020/2021. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali iliahidi kwamba maeneo yenye vyuo vya wananchi (FDCs) itaviongezea uwezo ili viweze kutoa elimu ya ufundi kwa ufanisi zaidi. Je, ni lini Serikali sasa itatimiza hiyo azma katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Njombe Mjini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ujenzi wa Vyuo vya VETA nchini unasuasua sana na Jimbo la Njombe Mjini lina shule 11 za sekondari, kuanzisha fani ya ujenzi ama umeme gharama yake ni nusu ya gharama ya kujenga maabara ya kemia ama ya baiolojia. Je, Serikali ipo tayari kuzifanya Shule za Sekondari Mgola na Luhololo kuwa shule za Sekondari za Ufundi kwa fani mbili kwa majaribio (pilot project)?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu jitihada za Serikali katika kuboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs); naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara tayari imepata ufadhili wa kuweza kukarabati vyuo 30 kati ya 55 tulivyonavyo vya wananchi. Lengo ni kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinarudi katika utendaji bora zaidi, vilevile ikiwezekana waendelee kutoa elimu ya ufundi kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Chuo chake cha Njombe Mjini nimweleze tu kwamba ni fursa imejitokeza kwamba tayari tumepata dola milioni 120 kwenye mradi unaoitwa Education and Skills for Productive Jobs (ESPJ), fedha hizi zinapatikana lakini kwa ushindani. Kwa hiyo hata Chuo chake cha Njombe Mjini inabidi washindane kuomba fedha hizi ili Wizara iweze kuja kufanya tathmini na kuangalia kama ni chuo ambacho kinahitaji kukarabatiwa, ni fursa ambayo ipo. Kwa hiyo nimweleze tu kwamba fedha zipo tutatangaza muda sio mrefu ili waweze kuziomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kurejesha vyuo vyote 55 vya wananchi virudi katika hali yake ya zamani, viwe vyuo vizuri ili viendelee kusaidia kutoa mafunzo katika maeneo mbalimbali ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana…
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Shule zake za Sekondari za Mgola na Luhololo kuruhusiwa kuwa shule za ufundi hili linajadilika. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama wao kama Njombe Mjini wanakubali zibadilike kuwa shule za ufundi sisi tuko tayari kama Wizara tufanye majadiliano na kwa hakika itawezekana. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niulize kwamba, kuna vijiji katika Kata ya Matola na Kata ya Uwemba katika Jimbo la Njombe Mjini; Kijiji cha Mtila na Kijiji cha Kilenzi. Vijiji hivi vinazalisha maji kwa ajili ya vijiji vya jirani kwa sababu vyenyewe viko juu ya mwinuko lakini vyenyewe kama vijiji havina maji kabisa. Je, Serikali iko tayari kutuchimbia visima virefu katika vijiji hivi viwili ili kusudi wananchi hawa wanaozalisha maji na kutunza mazingira waweze na wao kufaidi maji hayo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJ: Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu tu kwamba, Serikali ipo tayari, ndiyo maana imemtengea bajeti, ni suala la yeye Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri yake kuweka kipaumbele ili waweze kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo maji yanatoka, basi wao wawe wa kwanza kupata maji, waweke vipaumbele, wachimbe visima, watakapokuwa wamefikia, bajeti mwakani inaanza; huu ndio mwaka wa kwanza tunaanza na tutaendelea kutenga bajeti, kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata maji.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Wananchi wa Vijiji vya Kitulila, Mwatola, Luponde, Njomlole, Lusitu na Uwemba walichanga fedha kama asilimia 10 ya mradi wa maji ya mtiririko kutoka katika milima ya Igongwi
Ludewa: Je, ni lini mradi huu sasa utaanza kutekelezwa ili wananchi hawa waweze kupata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulivyoanza mradi wa WSDP tulisema kwamba mradi huu ni shirikishi na wananchi ilibidi wachangie, lakini sasa tumeamua kwamba fedha zile ambazo wanachangia wananchi hazitatumika wa kujenga miradi ila watazitumia katika kuiendesha miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, asilimia ambayo vijiji wameweza kujenga, watatumia katika kuendesha ile miradi itakapokamilika. Lini miradi ile itaanza? Tumetoa program na bajeti tumepitisha, tumeeleza utaratibu. Kwa hiyo, kila Halmashauri ilileta vijiji vya kipaumbele, kwa hiyo, naamini vijiji anavyovisema, Halmashauri yake iliviweka kwenye kipaumbele, tutaanza katika mwaka wa fedha wa 2016 /2017.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Kibena katika Jimbo la Njombe Mjini ndiyo inayotumika kama Hospitali ya Mkoa wa Njombe lakini haina kipimo cha x-ray.
Je, Serikali ipo tayari kutuwezesha wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini mashine ya x-ray ili iweze kusaidia wananchi wote wa Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba amehamisha goli, goli limehama kutoka katika swali la msingi, hii ni kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anaguswa na wananchi wa Njombe. Ni kweli pale hakuna x-ray na tulivyofika pale ilibainika kweli changamoto kubwa pale ni x-ray. Hata hivyo, tulitoa maelekezo kwa Halmashauri katika mipango yao ya bajeti kuhakikisha wanapata x-ray, aidha, kwa kupata mikopo kutoka NHIF au kutumia mikakati yoyote kupata funds.
Napenda nimtaarifu Mbunge kwamba suala hili tumelichukua na tutakaa pamoja naye kuangalia tufanye nini ili tuwaokoe wananchi wa pale Njombe wanaohudumiwa na Hospitali ya Kibena kupata x-ray kwa sababu mtu akiumia inakuwa shida. Tunatambua eneo hilo imepita barabara kubwa ya magari yanayotoka Songea, kwa hiyo, ajali zikitokea pale lazima waweze kupimwa na vipimo hivyo vya x-ray. Kwa hiyo, nitaomba tukae pamoja kuona ni jinsi gani tutakuwa na mpango mkakati, Halmashauri na Serikali tubadilishane mawazo ya jinsi ya kupata x-ray katika Hospitali ya Njombe.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niiulize Serikali, je, ni lini uwanja wa ndege wa Njombe utawekwa lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Njombe ni kati ya viwanja 11 ambavyo viko kwenye utaratibu wa kuboreshwa. Kulikuwa kuna changamoto kidogo pale ya wale majirani kwenye uwanja Mheshimiwa Mbunge anatambua, kuna watu wameendelea kuweka majengo marefu kandokando ya uwanja huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na mawazo ya kuuhamisha ule uwanja ili uwe nje ya sehemu hiyo uliopo. Kwa hiyo, zoezi hilo tuliwaachia wataalam waendelee kuliangalia itakapokuwa imekamilika au itakapokuwa imeonesha tofauti basi tutaendelea na hatua ya kuujenga huu uwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu changamoto zilizokuwepo na Mheshimiwa Mbunge tumekuwa tukizungumza nae, lakini nasi tumelichukulia hatua tumewaagiza wataalam wa upande wa TAA na Mkoa waweze kukaa na kuona kama tutauhamisha huu uwanja basi tusichelewe kuchukua hizo hatua ili tuweze kufanya ujenzi wa uwanja huu.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza ninalo. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwasaidia vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi kama hao wa Makete kupata angalau vifaa tu vya kuanzia kazi?
Swali la pili, Halmashauri ya Mji Njombe ina shule za sekondari 22 na zoezi hili la kujenga Vyuo vya Ufundi linaonekana sasa kwa Serikali limekuwa gumu sana na linakwenda pole pole sana.
Je, Serikali ipo tayari kupokea ushauri, sasa ianze kuzibadilisha baadhi ya shule za sekondari kuwa shule za ufundi ili kusudi vijana wetu walio wengi watakaokuwa wanahitimu Kidato cha Nne waweze kuwa mafundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kimsingi ni kwamba VETA imekuwa ikifanya hivyo baada ya kumaliza mafunzo ya ufundi kwa baadhi ya wanafunzi wanaohitimu wamekuwa wakipewa vifaa kwa ajili ya kuanzia shughuli zao za kiufundi, pia kusaidia kutengeneza clusters za hao wanaokuwa wamehitimu pamoja na wengine ambao wamekuwa wamehitimu mafunzo ya ufundi siyo tu kupitia VETA hata kupitia kwa wananchi wa kawaida, tunawatambua na kuweza kuwapa vifaa, vilevile kuwatambua rasmi na kuweza kuwapa vyeti.
Swali la pili la kuweza kubadilisha shule ziwe za ufundi, Wizara tayari tumeshaliona hilo na tunafikiria kubadilisha baadhi ya shule za sekondari hasa zilizokuwa shule za ufundi kama Ifunda, Mtwara, Tanga, Bwiru na shule ya Musoma ili ziweze kuwa vyuo vitakavyoweza kutoa mafunzo kwa ajili ya technicians.
Kwa hiyo, muda ukikamilika tutafanya hivyo na kwa mwaka huu tunategemea tuanze kujenga shule mbadala kwa sababu shule hizi zinachukua wanafunzi wa sayansi kwa kidato cha tano na sita na form one mpaka form four tunawajengea shule yao ili hayo majengo ambayo ni muhimu sana kama workshops yaweze kutumika kwa Vyuo vya Ufundi.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa vijana wanaohitimu elimu ya sekondari katika nchi yetu ni kama 400,000 hivi na wanaokwenda kidato cha tano ni kama vijana 90,000, zaidi ya vijana 300,000 wanabaki. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuanzisha kambi maalum ili kusudi sasa vijana hawa waweze kupata misaada ya kutosha ya utaalam wa kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo ni zuri, hata hivyo Serikali imesha-take initiatives za kutosha katika eneo hilo, ndiyo maana Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali, na hivi sasa mikoa mbalimbali wameshaanzisha kambi za vijana katika jitihada za kujenga ujasiriamali, ujasiri na uzalendo. Jambo hilo limetokea katika Mkoa wa Tabora pamoja na Pwani na mikoa mingine na zoezi hilo linaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuwashukuru wenzetu wa taasisi binafsi hasa shirika la Plan International ambalo kupitia mikoa mbalimbali kama vile Mkoa wa Morogoro, Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani na mikoa mingine wameanza kupitisha programu maalum ya vijana kwa ajili ya kuwawezesha katika fani mbalimbali za ufundi. Hili limetoa mafanikio makubwa, zaidi ya vijana 9,500 wamepata skills hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba Serikali itawatumia wadau mbalimbali na nguvu za Serikali lakini na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nawashukuru sana, wameshaanza ku- take hiyo initiative kwa kufanya mabadiliko hayo makubwa; naamini tukifanya hivi tutawasaidia sana vijana wetu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kipengele kimoja tu cha swali na kipengele kinachofuata hajakisoma. Kwa kuwa nimepewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza nafikiri atakisoma atakaporudi kwenye jukwaa.
Mheshimiwa Spika, Gereza la Njombe lina msongamano mkubwa sana na katika msongamano huu wako akina mama wenye watoto wadogo mle ndani ya Gereza.
Je, Serikali sasa iko tayari kuwapa chakula maalum watoto wale ili kutokuwaathiri makuzi yao na kuwafanya wakue wakiwa na afya bora? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Gereza la Njombe, yuko Mahabusu anaitwa Erick Mgoba. Mahabusu huyu amepelewa Hospitali ya Rufaa kwa kushirikiana na Gereza la Njombe ili apatiwe matibabu. Alivyofika Hospitali ya Rufaa Mbeya akatakiwa kulipa shilingi 300,000 ili atibiwe na akarudishwa Njombe bila kutibiwa na afya yake ni mbaya.
Je, Serikali iko tayari kumtibu mahabusu huyu ili kuokoa maisha yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mbali ya upungufu wa fedha ambazo tunatumia kwa kumlisha chakula mfungwa, ambayo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba ni shilingi 1,342; lakini tunahakikisha kwamba chakula ambacho anakula mfungwa ni chakula chenye kiwango cha kutosha. Tunapima hivyo kulingana na calories ambayo nadhani ni 2,200 na kitu kwa kila mfungwa; 2,200 kwa mfungwa mwanaume na 2,500 kwa wafungwa wanawake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la watoto na wafungwa wa kike na wa kiume kwa ujumla, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wanapata chakula chenye ubora na chenye kiwango cha kuridhisha, juu ya upungufu wa fedha, lakini kiwango tunahakikisha kwamba kinakuwa kwa maana ya lishe, inakuwa ni lishe ambayo iko sawa kabisa kitabibu.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na matibabu ya mfungwa ambaye amemzungumza amesema kama tuko tayari, naomba baada ya Bunge hili mimi na yeye tukutane tuone jinsi gani tunalishughulikia hili jambo. Ni lazima tuhakikishe kwamba mfungwa huyu anapata matibabu. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Sisi Wabunge wa Mkoa wa Njombe kwa ujumla wetu tumekuwa tukilalamika sana juu ya upatikanaji wa mbolea katika mkoa wetu; na wananchi wetu ni wakulima ambao hawatumwi na mtu kwenda kufanya kazi ya kilimo. Je, ni lini sasa TFC watakuwa na godowns za kutosha ili ku-supply mbolea katika Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wa Njombe kwa jitihada kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na kilimo kinachotosheleza katika ulishaji wa Taifa na kuweza kuuza nje. TFC imekuwa na maghala karibu katika kila Mkoa na hata sasa bado kuna mazungumzo yanayoendelea ya kuona kwamba pengine iweze kuwa moja kwa moja chini ya Wizara ya Kilimo ili sasa masuala hayo yaende vizuri zaidi.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe, Hospitali ya Kibena ndiyo hospitali inayotumika kama Hospitali ya Mkoa, lakini imechakaa sana na haina wodi ya wanaume wala x-ray.
Je, ni lini Serikali itatusaidia watu wa Njombe kupata wodi ya wanaume na x-ray?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala zima la kuchakaa Hospitali ya Wilaya ya Njombe ambayo kimsingi ilijengwa miaka ya zamani sana, tunakiri na tunatambua juu ya uchakavu huu. Kwa kadri bajeti itakavyoruhusu, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunazikarabati Hospitali za Wilaya ili zifanane na hadhi ya sasa hivi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika zile Hospitali ambazo zitakarabatiwa wakati bajeti ikiruhusu na Njombe nao hatutawasahau.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majibu ya Serikali ni dhahiri kwamba mafunzo haya hayafuatiliwi ndiyo maana sasa wanaagiza. Katika mafunzo yanayotolewa hayahusu mafunzo ya ukakamavu, je, Serikali iko tayari kuweka mpango wa kuwapeleka baadhi ya Watendaji wa vijiji kupata mafunzo ya JKT ili kusudi kuwaimarisha kiutumishi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika kutekeleza majukumu yao, Watendaji wa Vijiji wamekuwa wakipata madhara ikiwemo kudondoka na pikipiki na wengine kuumizwa na wananchi. Ni nani anayewajibika kuwalipa fidia pale wanapokuwa wamepata madhara hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwalongo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, napenda kumpongeza sana kwa sababu anahitaji sana Watendaji wetu wawe wakakamavu. Napenda kumpa taarifa na kulipa taarifa Bunge lako Tukufu kwamba wale Watendaji wote ambao walipitia JKT kwa mujibu wa sheria kabla utaratibu huo haujasimamishwa kwa muda, hao hawahitaji kupatiwa mafunzo tena kwa sababu tayari hao ni service girls and women. Kwa hiyo, wale ambao hawakupitia mafunzo hayo, tumepokea wazo lake zuri, tutaandaa utaratibu siyo lazima kuwapeleka JKT bali wanaweza wakahudhuria mafunzo ya mgambo ambayo huendeshwa na Washauri wa Mgambo katika wilaya zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili kuhusu fidia, zipo Sheria za Utumishi zinazoelekeza kuhusu fidia. Kwa hiyo, suala hili kwa sababu ni la kisheria, naomba sana watumishi wote ambao wanapata ajali au kuumia kazini sheria zipo zitumike. Ahsante sana.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Njombe ni Mji unaokuwa kwa kasi sana na upo katika Miji 17 ambayo imeahidiwa kutengenezewa miradi mikubwa ya maji na Mji wa Njombe unategemea kupata maji kutoka Mto wa Gafilo.
Je, ni lini huu mradi sasa utaanza ili kusudi wananchi wa Njombe waweze kupata maji safi na salama?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji na tunatambua kabisa katika Mkoa wa Njombe ni moja ya Mikoa ambayo ina changamoto kubwa sana katika suala zima la maji. Wizara yetu ina miradi zaidi ya 17 kwa maana ya mkopo nafuu katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo lolote kubwa ambalo lina mafanikio makubwa, lazima linakuwa na taratibu zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuko katika taratibu za manunuzi. Pindi manunuzi yatakapokuwa yamekamilika, tutampata Mkandarasi katika kuhakikisha mradi ule unakamilika kwa wakati kwa wananchi wake wa Njombe. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Njombe una uwanja wa ndege lakini wa nyasi; lakini katika ule uwanja kuna wananchi wana nyumba pembezoni mwa ule uwanja. Hakuna mipaka ya uwanja na hawaruhusiwi kuendeleza maeneo yao. Je ni lini Serikali itaenda kufanya utambuzi na kuwalipa fidia wale wananchi ili wapishe ule uwanja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwalongo jirani yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua changamoto zilizokuwepo kwenye Uwanja wa Ndege wa Njombe na hata hivi karibuni Mheshimiwa wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amefika Njombe kwa ajili ya kuona namna bora ya kuweza kukamilisha na kuweka mipaka katika eneo hili. Kilichokuwa kimetuchelewesha ilikuwa pia ni wazo la Mkoa kuweza kuomba kuhamisha uwanja katika eneo hili. Hata hivyo baada ya mazungumzo nafikiri sasa tuko tayari kuweka mipaka hiyo ili na ukarabati wa uwanja huu kati ya viwanja 11 uweze kufanyika.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Itoni – Manda kuanzia eneo la Nundu kupitia Kata za Uwemba, Luponde na Matola, ni barabara ambayo imeahidiwa miaka mingi sana na Serikali kwamba itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Nataka kufahamu, ni lini hasa kazi hii itaanza kutekelezwa? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kuhusiana na Barabara ya Itoni – Manda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile tayari tumeshaanza kuitekeleza na ndiyo barabara pekee ambayo inajengwa kwa kiwango cha zege kilometa 50 kutoka Lisitu - Mawengi. Tumeanza na hilo eneo tukaacha kilometa 50 ambazo zinaingia kwenye jimbo lake, lakini nimhakikishie kwamba na hizo 50 nazo tuko kwenye hatua ya kukamilisha taratibu tuweze kuzitangaza ili iweze kuunga sasa kutoka kwenye lami kwenda barabara ya zege.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa sasa wa kutumia VETA na vyuo vya FDC kutoa mafunzo ya ufundi stadi umekuwa ni wa polepole sana na idadi kubwa ya vijana wanamaliza shule za sekondari hawana ujuzi kabisa. Je, Serikali inaonaje sasa ikaanza kubadilisha baadhi ya shule za sekondari ambazo tumezijenga katika Halmashauri zetu kuwa shule za ufundi ili kusudi zisaidie vijana hawa kupata elimu ya ufundi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwalongo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba Serikali tayari imeshaona hiyo changamoto na ndiyo maana zile shule za ufundi ambazo awali zilikuwa zimebadilishwa mafunzo ya ufundi yaliondolewa tayari Serikali imeshachukua jukumu la kuzikarabati zile shule saba za ufundi za Kitaifa na kuziimarishia vifaa vya kufundishia na karakana zake zote zimeimarishwa. Nitoe wito kama alivyosema Mheshimiwa Mwalongo, Serikali itafurahi sana kama kuna Halmashauri ambayo ina shule na wanaona kwamba inakidhi vile vigezo vya kutoa mafunzo ya ufundi tuko tayari watuambie ili twende kuikagua na tutapenda tu kuongezea idadi ya wanaofanya mafunzo ya ufundi.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Katika Jimbo la Njombe Mjini kuna kilimo cha umwagiliaji wa zao la viazi, kilimo hiki ni maarufu kwa jina la kipalila, wananchi hawa wamekuwa wakilima kwa kujitegemea hawana mbinu bora za umwagiliaji na wala hawana scheme yoyote. Je, Serikali sasa iko tayari kuja Jimbo la Njombe na kusaidia wananchi hawa kujengewa miundombinu bora kabisa ya umwagiliaji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa asili yake kilimo cha vinyungu kinakwenda kulimwa kwenye maeneo oevu na kwa mujibu wa taratibu za kimazingira tunasema kwamba maeneo haya hayafai kulimwa kwa sababu yanaharibu eco system ya mtiririko wa maji. Tuko tayari na tumeshaanza kulifanyia kazi, wananchi hawa hawawezi kuacha kulima vilimo vya vinyungu. Lakini tutaweka utaratibu ambao watalima vinyungu, lakini siyo kwenye maeneo oevu ya mabonde yale ambayo yanatunza maji.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naishukuru Serikali kwa kutupatia fedha milioni mia tano kujenga Kituo cha Afya cha Ihalula, lakini naomba kuiuliza Serikali; je, lini sasa watatupatia fedha kwa ajili kukarabati Hospitali ya Halmashauri ya Mji Njombe Kibena?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mwalongo kwa sababu juzi nilienda kukagua kituo kile wamejenga vizuri sana. Nilipokuwa Mkoani Njombe nilitembelea vituo mbalimbali, miongoni mwa kituo ambacho wametumia taaluma vizuri ya Force Account, Mheshimiwa Mwalongo mmefanya vizuri. Hata hivyo tunafahamu katika ujenzi, hasa changamoto ya miundombinu, kama Serikali, tunachukua hili tunaweka katika mipango yetu. Lengo kubwa ni kwamba isiwe kwa hospitali yako peke yake, lakini hospitali mbalimbali za Wilaya ambazo zinachangamoto lazima tulirekebishe ili wananchi wapate huduma vizuri. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Utaratibu wa Serikali wa kutekeleza miradi ya maji ni ule ambao unamtaka Mkandarasi atekeleze alete madai na aweze kulipwa. Lakini utaratibu huu umeonesha kwamba Wakandarasi wengi hawana uwezo matokeo yake miradi mingi inachelewa sana kutekelezwa na mingine inaharibika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha utaratibu wa utekelezaji wa miradi wa maji inayoanza kuanzia tarehe 1 mwezi wa 7 ukiwemo huu mradi wa maji wa Makambako?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkopo nafuu kutoka Serikali ya India unahusu pia vilevile Mji wa Njombe ambao upembuzi yakinifu umefanyika kwa ajili ya kupata maji kutoka chanzo cha Mto Hagafilo na kusambaza katika Mji wa Njombe na sasa huu ni mwaka wa tatu, kila mwaka Serikali inatuambia kwamba mradi huu unaanza. Je, Serikali inatoa majibu gani ya uhakika sasa kuwahakikishia wananchi wa Mji wa Njombe kwamba mradi huu wa maji kutoka Mji wa Hagafilo unaanza kutelekezwa? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya Wizara yetu ya Maji katika kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi, salama na yenye kutosheleza, lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo la Wakandarasi.
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona haja sasa Wahandisi wote wa maji kutoka Halmashauri waje kuweka katika Wizara yetu ya Maji ili tuwe na usimamizi wa ukaribu na majukumu ya pamoja katika kuhakikisha tunatatua matatizo hayo. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali ni kuanzisha sasa Wakala wa Maji Vijijini katika kuhakikisha Watanzania waliokupo vijijini wanafikiwa na asilimia 85 ya upatikanaji wa maji.
Mheshimiwa Spika, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha, kama nilivyomhakikishia kwamba tumeshasaini mkataba ule wa kupata fedha, niwahakikishie wananchi wa Njombe kwamba watapata maji hayo safi, salama na yenye kuwatosheleza. Sisi kama viongozi wa Wizara tutasimamia kwa ukaribu ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. imeuliza kuhusu Hospitali ya Kibena; nimepewa majibu kidogo sana juu ya Hospitali ya Kibena lakini zaidi majibu yamejikita kwenye hospitali mpya ya mkoa inayojengwa. Hospitali ile ya Kibena ni hospitali chakavu, ina wodi moja tu ya akinababa. Wanaopata ajali na wanaougua maradhi mbalimbali wote wanalazwa katika wodi moja. Hospitali hii haina fence tangu wakati imerithiwa kutoka Kampuni ya TANWART. Naomba sasa commitment ya Serikali, ni lini Serikali itatusaidia kuboresha hospitali ya Kibena kwa maana ya wodi ya wagonjwa na fence?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imetusaidia tumepewa fedha kujenga Kituo cha Afya Ihalula, lakini hata sisi katika halmashauri yetu kwa kushirikiana na wananchi katika Kata ya Makoa wamejenga kituo cha afya, Kata ya Kifanya wanaendelea na ujenzi wa kituo cha afya, ndiyo wanakamilisha. Naomba pia commitment ya Serikali, je, ni lini itatusaidia sasa vifaa kwa ajili ya vituo hivi vya afya ambapo viwili vimekaribia kukamilika na kimoja kinakaribia kukamilika?.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi nimeeleza kwamba na bahati nzuri nimepata fursa ya kutembelea hospitali zote mbili, hii ambayo ni Hospitali ya Kibena pamoja na hospitali mpya ya rufaa ambayo tunaendelea kujenga. Sisi kama Wizara, msukumo wetu sasa hivi ni kuweka nguvu kwa kuhakikisha kwamba ile Hospitali mpya ya Rufaa ya Njombe inakamilika.
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto na mimi binafsi nimeona katika Hospitali ile ya Kibena na ndiyo maana sasa hivi maboresho makubwa ambayo tunayafanya ni kupanua ule wigo wa utoaji huduma. Kwa hiyo nataka nimhakikishie tu kwamba sisi kama Serikali tunataka tukamilishe ile hospitali kubwa na ya kisasa ili huduma za msingi kwa wananchi wa Njombe Mjini ziweze kupatikana pamoja na Mkoa mzima wa Njombe.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vifaa kwa vituo vipya vya afya ambavyo tunaendelea kuviboresha, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) inaendelea kununua vifaa hivyo na kadri inavyofika kutoka kwa Washitiri tutakuwa tunavisambaza, ikiwa ni pamoja na vituo hivi ambavyo viko Njombe Mjini.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Ili watoto wa kike waweze kufanikiwa katika masomo ya sayansi wanahitaji uwepo wa walimu. Tuna tatizo kubwa sana kama nchi ya walimu wa sayansi na hasa hasa physics. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakisha shule zetu zinapata walimu wa kutosha wa physics?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwalongo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba ili watoto wa kike waweze kufanikiwa kuchukua masomo ya sayansi ni lazima kuwa na walimu na ndiyo maana Serikali imekuja na mikakati thabiti ya kuhakikisha kwamba walimu wanapatikana. Wote tunakumbuka kwamba Serikali ilipeleka wanafunzi wale waliokuwa UDOM kwenda kusoma masomo ya sayansi na tunategemea wataanza kuingia sokoni kwa ajira za hivi karibu. Pia katika vyuo 35 ambavyo tunavyo, Serikali imeamua sasa kutenga vyuo vichache kati ya hivyo vinakuwa ni vyuo vinavyofundisha sayansi. Kwa hiyo, tunaendelea kuongeza fursa na udahili katika vyuo vya elimu vinavyotoa walimu wa sayansi.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tatizo la wagonjwa wa akili wanaorandaranda limekuwa sasa ni tishio kwenye jamii. Kwa mfano, wiki iliyopita tu mama mmoja Wilaya ya Nzega ameua watoto sita na amejeruhi watoto wengine wanne lakini katika jitihada za kumdhibiti na yeye mwenyewe ameuawa. Tunaona tena pia wagonjwa hawa wa akili wakiwa wamebeba mizigo na madudu chungu nzima na wanatishia usalama wa watu wengine.

Je, Serikali iko tayari sasa kuwaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Franz Mwalongo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tunaendelea kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na masuala haya ya magonjwa ya afya ya akili. Tunachokifanya sasa hivi tumeweka Waratibu katika ngazi za Mikoa na Halmashauri zote. Kwa hiyo, katika masuala yanayohusiana na masuala ya afya ya akili, majukumu ya msingi yapo kwa Waratibu wa Afya ya Akili ngazi ya Mkoa na Halmashauri na tutaendelea kuwahimiza na kuwasimamia kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao huo.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe, Kibena, ina kituo cha watoto njiti, lakini kituo kile kina mazingira duni sana na kinahudumia mkoa mzima. Na sasa hali ya hewa inakwenda kuwa ya baridi sana kuanzia mwezi wa tano. Je, Serikali iko tayari kutusaidia Wananchi wa Njombe kupata huduma haraka iwezekanavyo katika kituo cha watoto njiti cha Kibena Hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali na kupitia hospitali zetu za rufaa za mikoa kwa sasa, moja ya msisitizo mkubwa ambao tumeuweka ni pamoja na kuboresha huduma za watoto wachanga, ikiwa ni pamoja na njiti. Sijajua, hususan, jambo gani ambalo analiongelea pale, lakini katika Mkoa huu wa Njombe sasa hivi tuko katika hatua za mwisho kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa na lengo letu ni kwamba, baada ya hapo ile Hospitali ya Kibena tuirudishe katika ngazi ya halmashauri. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mikakati yetu ambayo tunayo kama Wizara ni kuhakikisha kwamba, huduma za watoto wachanga, ikiwa ni pamoja na njiti katika Mkoa wa Njombe itapewa kipaumbele.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Njombe Mjini ni wafugaji wa ng’ombe wa maziwa. Tatizo kubwa tunalokabiliwa nalo katika Jimbo la Njombe ni upatikanaji wa ng’ombe bora wa maziwa. Hivi sasa tunapokezana ng’ombe mpaka imefikia mahali sasa ng’ombe wa maziwa anatoa lita moja kiasi ambacho anasababisha hasara kwa wafugaji kwa kuwa hatupati maziwa ya kutosha.

Je, Serikali ina mpango gani sasa kutuwezesha sisi wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wa Jimbo la Njombe Mjini kupata ng’ombe bora wa maziwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wetu katika Serikali wa kupatikana kwa ng’ombe bora, tunayo mipango kadhaa ya kuhakikisha tunaongeza idadi ya ng’ombe bora wa maziwa kwa kupitia mfumo wa uhimilishaji (artificial insemination) kwa kuuza mitamba ya kutoka katika mashamba yetu likiwemo shamba la ng’ombe wa maziwa la Kitulo lililoko Makete katika Mkoa huu wa Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachowaomba wafugaji wa Njombe na wafugaji wengine wote nchini wajiunge katika vikundi ili iwe rahisi kuweza kuwasaidia kama tulivyowasaidia kupatikana mitamba ya ng’ombe wa maziwa wafugaji wa Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa pale Tanga kwa maana ya Chama Kikuu cha Ushirika cha TDCU ambacho kimepata mkopo kutoka Benki ya Kilimo ya Zaidi ya shilingi bilioni moja na kununua mitamba ya maziwa ya zaidi ya 300 kwa ajili ya kuweza kulisha katika kiwanda cha Tanga Fresh.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la wakulima wa Njombe ni udongo kuwa na tindikali nyingi zaidi na wataalaam wanajua hilo. Je, Serikali inatusaidiaje wakulima wa Njombe Mjini kutuletea chokaa ya kilimo ili kupunguza tindikali kwenye udongo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Wizara inafanya mobile sampling kwa nchi nzima kuangalia udongo na kuweza kuja na study ya wazi kujua kwamba wapi kuna tatizo gani na tuweze kupata solution. Tumuombe Waheshimiwa Wabunge watuvumilie wakati tunamaliza study hii tunaamini kufika mwisho wa siku huu tutakuwa na sample ya nchini nzima na kujua eneo gani linafaa kulima nini na eneo gani linahitaji mbolea gani ili tuweze kuwapitia huduma sahihi wakulima wetu badala ya kulima kwa kubahatisha. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote niipongeze sana Serikali kwa jitihada ambazo zinaendelea, niombe basi speed iongezeke kuwaandaa walimu, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ufundi ni ujuzi wa jambo lolote lile. Je, Serikali inaonaje sasa ikabadilisha mtizamo wa kuanza kujenga vyuo vya ufundi vikubwa na vyenye gharama kubwa badala yake iende kwenye fani ambazo zinahitaji fedha kidogo na kazi za mikono kwa vijana wa Tanzania kama vile kilimo na ufugaji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Njombe tuliahidiwa kukarabatiwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Chuo kile ni kichakavu sana kinachukua wananfunzi wachache sana. Je, Serikali imefikia wapi katika ahadi yake ya kukarabati Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Njombe Mjini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kujielekeza zaidi kwenye vyuo vidogo badala ya vile ambavyo vina gharama kubwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendesha vyuo vya aina zote; vidogo, vya kati vilevile vikubwa. Yeye mwenyewe ni shahidi kwamba Serikali kwa sasa imeweka fedha nyingi katika kukarabati Vyuo vya Wananchi lengo lake ni ili wananchi waweze kupata kozi ambazo zinaendana na shughuli ambazo wanafanya. Kwa hiyo, kwenye maeneo ya kilimo kunakuwa na vyuo ambavyo viatoa elimu ya ufundi wa masuala ya kilimo au shughuli nyingine yoyote ambayo wananchi wanafanya. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba wazo lake hilo siyo baya na tayari Serikali inalifanyia kazi na ndiyo maana kuna vyuo vya aina mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la Chuo chake cha Wananchi kwamba ni lini kitaanza kukarabatiwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tumeanza na ukarabati wa vyuo 20 kati ya vile vyuo 55 na tunategemea vile vingine vilivyobaki ukarabati utaanza mwezi ujao. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba yeye na wananchi wake wawe tayari kwa sababu ukarabati unakwenda kuanza.