Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Deo Kasenyenda Sanga (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wachangiaji wenzangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu; Waziri Mkuu; Makamu wa Rais; Mawaziri na Waziri mwenye dhamana hii ya afya, pamoja na Naibu na Watendaji wake wote, kwa namna ambavyo wameonesha vizuri mwelekeo wa bajeti hii kwa mwaka wa 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli. Unajua wakati fulani vijembe hivi! Hivi kweli pale Muhimbili hakuna mabadiliko! Muhimbili ukienda sasa hivi pana mabadiliko makubwa kabisa. Duka la MSD Mheshimiwa Rais alisema litakuwa pale, Waziri mwenye dhamana amesimamia liko pale. Vitu vingine, kuna mabadiliko makubwa! Kwa kweli tuwatie moyo kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kuna mchangiaji mmoja alizungumzia lugha fulani iliyokuwa inagusa akinamama. Akinamama wametuzaa; kalipuka! Ni mama zetu hawa, wametuzaa, lakini mmoja vile vile siku ya nyuma yake pia naye alidhalilisha akinamama hawa hawa! Alitamka kwamba alipokwenda huko wakapigwa, wakakatiwa shanga zao. Hivi ndiyo vya kuzungumza hapa vitu nyeti kama hivyo? Eeh! Sasa niseme, kama Mwenyekiti wa CCM mwenzangu kwa yule kijana ambaye Mbunge alizungumzia lugha ambayo CCM hatukumtuma, mimi namwombea radhi kama Mwenyekiti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tuliopo hapa, kila mmoja ana akili; na wakati fulani tuliopo hapa wote ni vichaa, lakini vichaa vinatofautiana. Ukienda upande wa elimu na ndiyo maana sekondari, shule za msingi na kadhalika huwa kunakuwa na shule za watu wenye vipaji maalum. Maana yake hawa wana akili kuwazidi wenzao. Sasa baadhi ya Wabunge hapa walizungumzia habari ya viti kumi ambavyo Mheshimiwa Rais anawateua kwa kazi maalum, kwa vipaji maalum. Ndiyo maana alimteua Mheshimiwa Tulia, Naibu Spika kwa kazi maalum. Kwa hiyo, tusimwingilie Mheshimiwa Rais, kazi ambazo anawateua watu, zile nafasi kumi amemteua Waziri wa Fedha, ameteua na wengine, tusimwingilie nafasi zile kumi. Hata Mheshimiwa Mbatia amewahi kuteuliwa kupitia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie habari ya Jimbo la Makambako. Nilimwandikia Mheshimiwa Waziri ile ahadi ya Mheshimiwa Rais. Ndugu zangu, naishukuru Serikali, miaka miwili, mitatu iliyopita mmepandisha hadhi Kituo cha Makambako kuwa hospitali na mmetuletea Madaktari wa kutosha, tunao. Tatizo kubwa nimekuwa nikisema hapa na niliseme tena kwa Mheshimiwa Waziri, tuna jengo la upasuaji, tulichokikosa ni vifaa vya upasuaji. Gari letu la wagonjwa limekuwa likipeleka watu Njombe kila siku, mara saba, mara tano mpaka mara nane. Ni gharama kubwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha na nilimltea, akaniambia Daktari anipe orodha ni vitu gani vidogo vidogo ambavyo vimekosekana. Nilimpa! Atakapohitimisha aniambie wamejipangaje kuona sasa tunapeleka vifaa vya upasuaji pale Makambako ili kuwaokoa akinamama na watoto, gari lisiwe linakimbia kwenda Njombe na Ilembula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo hospitali yetu ya Makambako tuna wodi ya akinamama na watoto. Wodi nzuri iliyojengwa zaidi ya miaka miwili, vimebakia vitu fulani fulani havijakwisha; miaka miwili tume-invest pale hela ya Serikali. Nawaomba Wizara waone uwezekano wa kuona tunamalizia jengo hili ili liweze kufanya kazi iliyokusudiwa. Chonde chonde, ili kuokoa hela ya Serikali ambayo imeendelea kukaa kwenye majengo hayo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kufungua maduka ya MSD katika hospitali zetu za mikoa na wilaya, naomba sana, Mkoa wetu wa Njombe ni mpya. Mkoa huu ndiyo Mkoa ambao sasa una kitega uchumi kikubwa ambacho kitaanzishwa, Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, naomba sana tuhakikishe tunapeleka Duka la MSD la Madawa pale Mkoani Njombe ili kuwasaidia wananchi wetu wa Wilaya na Mkoa wa Njombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Mji wa Makambako tumejenga zahanati tisa katika vijiji tisa; na karibu zahanati saba tumeshazipaua. Naomba Serikali ione upo umuhimu sasa wa kutenga bajeti ya kumalizia kuwaongezea nguvu wananchi hawa wa Mji wa Makambako. Hili linawezekana na ni kwa nchi nzima. Yako majengo ambayo yamejengwa hayajamalizika, tunaomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kumalizia haya majengo ambayo yalishajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna Kituo cha Afya ambacho kilijengwa katika Kata ya Lyamkena. Kituo hiki cha Afya kina zaidi ya miaka miwili. Kilishapauliwa na kadhalika, bado hakijamaliziwa, kimeendelea kukaa pale. Jengo hili la kituo cha afya, inawezekana kabisa na majimbo mengine vituo vya afya kama cha Makambako, vipo! Tutenge fedha kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya ili kazi iliyokusudiwa iweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwa kasi anayokwenda nayo ambapo yuko nyuma ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imani yangu na imani ya Wabunge hawa, atatufikisha salama. Nampongeza sana kwa dhati pamoja na Watendaji wake. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema, atakapokuwa anahitimisha, basi ni vizuri atueleze kwa ujumla wake ili tuweze kuwa kitu kimoja na CCM ahadi ambazo iliahidi, tunamtegemea yeye kupitia Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya, nisiwachukulie muda wenzangu, niseme tu naunga mkono hoja ya Waziri wa Afya kwa asilimia mia moja. Nawashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru na mimi kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana Wizara hii, watendaji wote na Waziri na Naibu Waziri, wamefanya kazi nzuri na bajeti hii ina muelekeo mzuri; wapate fedha, sisi tunasubiri maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja alikuwa anachangia jana hapa, anasema daraja la Kigamboni halina faida, hivi kweli halina faida daraja la Kigamboni, kweli? Ila amesema amekwenda mara nane, mara ngapi, anakwenda na kurudi, si ndio faida yenyewe. Kama daraja halipo angekwendaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ni kwa ajili ya watu wa chini. Na watu wa chini kule, hivi tunakwenda kuwaambia leo mambo hayo watu wa Kigamboni kweli? Eeh, wanatembea kwa mguu, si ndio wana faidi daraja hili. Songa mbele Waziri, usirudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumzia habari ya kuuza zile nyumba. Nyumba ziliuzwa Waziri Mkuu alikuwa Mheshimiwa Sumaye. Mheshimiwa Sumaye ndiye aliesimamia mambo hayo, ndiye alieuza zile nyumba, lakini na nyumba zile na nyumba…
MHE. DEO K. SANGA: …mnanijua, wee!
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nyumba zile…
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nyumba zile walionunua ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni Mheshimiwa Sumaye, si athibitishe!
Mheshimiwa Mwenyekiti, walinunua nyumba zile ni Watanzania, ndio walionunua zile nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri mwenye dhamana, pale mjini…
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Waziri katika bajeti aone namna ya kutafuta fedha hata kilometa moja na nusu Makambako Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, katika kupandisha daraja barabara za Halmashauri kwenda TANROADS, kuna barabara ya kutoka Makambako - Kifumbe, kutoka Usetule kwenda Kitandililo, tafadhali sana. Lakini vinginevyo Rais wa Awamu ya Tano…
MWENYEKITI: Ahsante! Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Wanasema ukiona watu wanasema wewe una tatizo, wewe songa mbele, wewe ni jembe unafaa kutumikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea bajeti nzuri yenye mwelekeo na kwa kumteua Waziri Mpango pamoja na Naibu Waziri. Naipongeza Wizara ya Fedha na Watendaji wote kwa kutupa bajeti yenye mwelekeo mzuri kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mategemeo yetu Watanzania ni kwamba matatizo ya maji, elimu, afya, barabara, umeme yatapungua. Hii ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ahadi alizozitoa Mheshimiwa Rais kwa Watanzania ikiwemo Mji wa Makambako ambapo aliahidi maji, vifaa tiba, lami kilomita sita, umeme na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu bajeti hii hata waliotoka humu ndani nao wanahitaji maendeleo kwenye Majimbo yao. Rais wetu alishasema maendeleo hayana chama, peleka maendeleo hata huko katika Majimbo waliyotoka utakuwa unawatendea haki Watanzania. Ingawa wenzangu watasema, aah, aah, ndugu zangu tunawapelekea maendeleo Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala hili ambalo limeleta mkanganyiko mkubwa juu ya mageti ambayo yalishatangazwa kwamba yanaondolewa kwenye Halmashauri zetu yanayohusiana na ushuru. Waziri atakapokuwa anahitimisha hapa atuambie jambo hili limekaaje maana tayari linaleta mkanganyiko kuhusiana na kuondoa mageti haya ya ushuru wakati Halmashauri zilishaweka bajeti na wananchi wameshapata kauli ya kwamba ushuru sasa umeondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri kwa kuondoa tozo mbalimbali kwa wakulima. Jambo hili limeleta faraja kubwa sana kwa Watanzania na wakulima wetu. Nirudie tena kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kumteua Waziri huyu Mheshimiwa Dkt. Mpango sasa tunaona mipango itakwenda vizuri, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napingana na hawa watu ambao wametoka hapa na wamekuwa wakipinga kwamba hii bajeti haina mwelekeo na kadhalika, ndugu zangu uchaguzi ulishakwisha, Rais sasa ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu, Waziri Mkuu ni Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa pamoja na Mawaziri wote walioteuliwa, naomba chapeni kazi ya maendeleo kwani watu wanasubiri maendeleo katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wamezungumzia sana suala la kiinua mgongo. Mimi niseme tu kwamba suala la kiinua mgongo linagusa Watanzania wote hasa watumishi. Watumishi pamoja na Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukikatwa kodi mbalimbali lakini kodi hii ya kiinua mgongo kwa watumishi nadhani iangaliwe upya. Kwa sababu watumishi hawa wametumikia nchi na wamekatwa kodi mbalimbali. Kwa hiyo, naomba suala la kiinua mgongo kwa watumishi wote kwa ujumla liangaliwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali imesikia kilio cha Wabunge ambao wamezungumzia sana suala la manunuzi kwamba lilikuwa ni tatizo kubwa katika Halmashauri zetu na wenzangu wengi wamesema hapa. Suala hili la manunuzi ilikuwa hela zikipelekwa kwenye Halmashauri zinaliwa tu na baadhi ya watendaji ambao siyo waaminifu. Naishukuru sana Serikali, Waziri alisema hapa unaletwa Muswada wa kubadilisha Sheria ya Manunuzi na mimi naafiki kwamba utaratibu huu ukibadilishwa utaleta tija na maendeleo katika Halmashauri zetu na hizi fedha zote zinazojadiliwa hapa sasa zitakwenda kutumika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wetu wa Makambako sasa tunazungumzia suala la kujenga viwanda, watu wanahitaji kuwekeza viwanda katika mji wetu lakini tatizo kubwa ni upatikanaji wa maji. Niipongeze sana Wizara ya Maji ambayo tayari imetenga fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la maji katika Mji wa Makambako. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ya Fedha ipeleke haraka fedha hizi ili ziweze kuleta maji ili wawekezaji waweze kuanzisha viwanda katika Mji wetu wa Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, hili nimelisema mara nyingi sana, naomba nirudie, Serikali imewekeza fedha kwenye hospitali yetu pale kwa miaka zaidi ya minne sasa, tumejenga wodi mbili kubwa za akina mama na watoto imebaki tu kumalizia, miaka minne imebaki magofu. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu liangalie suala hili zinahitajika hela kidogo sana ili wodi hizi ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwani fedha ya Serikali imekaa pale kwa muda mrefu. Namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha aone ni namna gani atatatua tatizo hili la kumalizia wodi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba hospitali ile ya Mji wa Makambako imeshapandishwa hadhi na kuwa hospitali kamili na kwa miaka mitatu tunakwenda vizuri. Tatizo ambalo lipo katika Mji wetu wa Makambako, nilimueleza hata Waziri wa Afya na Waziri wa TAMISEMI, tayari tuna jengo pale la upasuaji ambalo limeshakamilika lakini tunakosa tu vifaa tiba vya upasuaji. Tuna gari letu la ambulance kwa siku mara saba linapelekea wagonjwa Njombe kwa ajili ya upasuaji. Fedha inayohitajika ni kidogo sana hata shilingi milioni 30 hazifiki ili tuweze kununua vifaa vya upasuaji vilivyobakia ili shughuli za upasuaji ziweze kuendelea. Mmetuletea Madaktari wazuri wako pale wamekaa tu hawawezi kufanya kazi kwa sababu shughuli za upasuaji hakuna. Namuomba Waziri wa Fedha atakapokuwa anahitimisha aone namna ya kutatua tatizo la kununua vifaa vya upasuaji ili kuweza kutatua tatizo la Makambako. Vifaa vinavyohitajika ni kifaa cha kuchanganyia dawa ya usingizi na vitu vidogo vidogo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Waziri Dkt. Mpango chapa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mpango huu ambao umeletwa mbele yetu. Mpango huu ni mzuri sana, una mwelekeo mzuri na dira nzuri ya kuhakikisha shughuli zote ambazo zimepangwa hapa zinakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua hata vitabu vitakatifu vinasema unapotaka kwenda peponi au mbinguni ni lazima ukeshe ukiomba. Sasa kazi ya kukesha na kuomba si ndogo, ni kubwa sana, kazi ya kukesha na kuomba na ukishakesha na kuomba ndio unaweza kufika peponi au mbinguni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano kazi kubwa ambayo ilikuwa ikiifanya ni kuturudisha kwenye mfumo, kuachana na ule utaratibu tuliouzoea kwa hiyo, ilikuwa inaturudisha kwenye mfumo. Turudi tujenge nidhamu katika Serikali na kazi hiyo imefanywa na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, amefanya kazi nzuri sana. Hata wakati anawaambia Watanzania anaomba ridhaa aliyasema haya kwamba, nipeni nitafanya moja, mbili, tatu; leo anayafanya haya tunasema aahhaa, anafanya vibaya! Lakini mtu mmoja amewahi kusema ukiona mtu anakusifia jiangalie mara mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayofanywa na Serikali kupitia Mawaziri waliopo na huyu ambaye ameleta mpango huu ni kazi nzuri sana. Sasa kwamba Serikali imeturudisha kwenye mfumo, imedhibiti mambo ya pesa, Mheshimiwa Mpango baada ya kudhibiti sasa peleka kwenye Halmashauri ili zikafanye kazi, maana kwanza alikuwa anaturidisha kwenye mfumo na sasa tumerudi kwenye mfumo, kwa hiyo fedha sasa zianze kwenda kwenye Halmashauri ili zikafanye kazi iliyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu waliozungumzia habari ya Liganga na Mchuchuma. Na mimi napata ukakasi, hivi kuna tatizo gani linalofanya shughuli ya Liganga na Mchuchuma ikwame? Kwenye mpango imekaa vizuri, tunaomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana suala la Liganga na Mchuchuma hebu sasa liweze kusonga mbele kadri ambavyo lilikuwa limepangwa ili liweze kusaidia Tanzania, tuweze kupata ajira nyingi kwa vijana wetu wa Tanzania kama ambavyo mpango upo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua napata taabu kitu kimoja kidogo sana! Mambo mengi amenimalizia yuko pale, ambayo nilikuwa nimeyaweka hapa kwa sababu...! Sasa naomba niseme! Eeh, ndio mwenyewe! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani wote ni Wabunge sawa, kila mmoja ana hadhi yake ameingia hapa, tunahitaji kuheshimiana. Tunapomnyooshea mtu, Mbunge mwenzako kwamba eti wewe huoni uchungu kwa sababu uliteuliwa, tena huyu ndiye anaheshima kubwa sana kuliko wewe, kwa sababu kama alivyosema Mbunge mwenzangu pale kwamba kila mmoja amepata kura kwa idadi tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nani aliyepata humu ndani kura nyingi kama za Mheshimiwa Magufuli, nani? Sasa zile zote si ndio amepewa yule kwa heshima ya Watanzania? Ndugu zangu tuheshimiane, aliyeteuliwa, ambaye hakuteuliwa wote ni Wabunge. Wakati fulani ninyi wenyewe ndio mnatoka huko mnakwenda pale, Waziri eeh, moja, mbili, tatu! Ni Waziri huyu, apewe heshima yake kama ambavyo Wabunge wengine tuko hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kudhibiti mambo yote sasa peleka fedha Halmashauri zikalipe na fidia zile pamoja na Makambako ikiwemo. Kuna fidia kule wananchi wangu wanadai kule ili zikaweze kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla mpango huu nauunga mkono vizuri, ni mpango mzuri ambao sasa peleka fedha zikaanze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sina la ziada. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwanza nizungumzie suala linalohusiana na maji. Kwenye bajeti ya kipindi kilichopita kuna miradi mikubwa ambayo tuliipitisha hapa. Kwa mfano, kuna miradi mikubwa ya maji ya miji ya Makambako, Njombe na Wanging’ombe ambapo ilionyesha fedha zinatoka Serikali ya India. Kwa hiyo, ni vizuri Waziri atakapokuwa anasimama atuambie Serikali imejipangaje juu ya kutatua tatizo la maji kwa mradi mkubwa huu wa Makambako, Njombe na Wanging’ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la pembejeo hizi za ruzuku ambapo Mkoani kwetu Njombe zinachelewa sana. Sisi tunaanza kupanda kuanzia mwezi wa 11 na kuendelea. Kwa hiyo, Serikali ijipange vizuri msimu huu tunaokwenda sasa kuona kwamba pembejeo hizi zinafika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, kuna hawa wasambazaji ambao mpaka sasa wanaidai Serikali na mpaka sasa wako watu ambao wamefilisika, wako watu wanauziwa nyumba zao. Ni lini Serikali italipa deni hili ambalo wananchi hawa walisambaza pembejeo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne, ni suala la lumbesa kwa wakulima, nadhani Serikali ijipange vizuri suala hili lipigwe marufuku kwa nchi nzima ili kusudi isiwaumize wakulima.
Mheshmiwa Mwenyekiti, jambo la tano ni mifugo. Suala la mifugo limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wafugaji na wakulima na watu wanapoteza maisha. Aidha, Kamati au ninyi Serikali muone namna ambavyo nchi ya Sudan wana mifugo mingi kuliko sisi lakini hakuna tatizo la wakulima na wafugaji, waende kule wakajifunze wenzetu kule wanafanyeje mpaka hakuna migogoro ambayo ipo kama huku kwetu kila wakati mara watu wameuawa na kadhalika. Kwa hiyo, nadhani Serikali ijipange kuona namna ya kuondoa tatizo hili la mifugo na wakulima kwa sababu limekuwa ni kubwa sana, siyo kitu kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sita, hapa kuna watu wamezungumzia Wizara hii ya Kilimo. Mimi niseme ndugu zangu, Waziri huyu Tizeba na Naibu wake wakati fulani tunawalaumu bure tu, sasa watachukua wapi fedha kama hawana fedha? Nadhani sisi tuungane kwa pamoja kuona namna ambavyo tunaiambia Serikali ili bajeti ya msimu huu tunaokwenda iwe nzuri kuliko bajeti iliyokwisha ambapo ilitengwa shilingi bilioni 20 tu ambazo hazijatosha kitu chochote.
Kwa hiyo, nilikuwa nadhani sasa badala ya kumlaumu Waziri na Naibu wake na Wizara kwa ujumla, tuone namna ambavyo sasa Serikali inajipanga kuona msimu huu tunakuwa na bajeti ya kutosha kwa sababu ndiyo uti wa mgongo kwa wakulima wetu. Nadhani tukifanya hivyo, Serikali ikiongeza bajeti tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi lakini kwa sababu na mimi nipo kwenye Kamati hii nirudie tena kuzungumzia hili suala la maji, Waziri utakaposimama uwaambie wananchi wa Makambako wataondokana lini na tatizo kubwa hili la maji na uwaambie fedha za kutoka nje wananchi wale wa Njombe, Wanging’ombe wanazipataje na mpango huu sasa unaendeleaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. DEO K. SANGA:Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naipongeza sana Serikali kwa kuleta muswada huu ambao Wabunge wameelezea kwa muda mrefu sana ili kuleta tija na mabadiliko makubwa ambayo huko nyuma lilikuwa ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kupitia Waziri wa Fedha, Naibu na watendaji wote wa Wizara hii ya Fedha ikiongozwa na Mheshimiwa Mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli lilikuwa tatizo kubwa sana tulifika mahala unakuta bati moja lilikuwa linaweza kununuliwa kwa shilingi 35,000; simenti shilingi 22,000; mimi ninasema hivyo iko haja ya kipindi kilichopita mimi kama Mbunge, Mfuko wa Jimbo tulinunua simenti kwa shilingi 22,000 na bati la geji 28 kwa shilingi 35,000; ukiuliza wanasema Sheria ya Ununuzi. Jamani mbona huko madukani wanauza bei chini? Sheria ya Ununuzi. Kwa hiyo nadhani sasa imeletwa wakati muafaka kabisa kwamba sasa tutaangalia soko linasema nini. Kwa hiyo mimi nadhani tutawatendea haki watanzania walipakodi na kadhalika.
Lakini pamoja na marekebisho hayo, nivizuri marekebisho hayo bado Serikali iendelee kuangalia mapungufu madogo madogo ambayo yataendelea kujitokeza ili waendelee kukaa na kuona namna ambavyo waweze kurekebisha uendelee mpango mzuri zaidi kadri ambavyo itakavyokuwa inakwenda. (Mkofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu Kamati ya Mipango na Fedha za Halmashauri, mimi nishauri na niombe sana, sijaona kama wameleta amendment hapa; lakini ni vizuri Kamati hizi hasa Kamati ya Mipango na Fedha ya Halmashari iendelee kama ilivyokuwa ni lazima angalu ipitie kwa sababu Kamati hizi zinakaa kila mwezi mara moja ili kuona kwenye Halmashauri yao ni kitu gani ambacho kimejadiliwa kwenye Bodi ya Zabuni. Sasa tukiondoa kabisa Kamati hii ya Mipango na Fedha na wao ndio wenye fedha za Halmashauri na bajeti hii ambayo tumeendelea kuijadili na kuimalizia sasa Serikali imetenga fedha nyingi kwenda huko, haki ya Mungu zitakwenda kuliwa, tutakuwa tulichokifanya hakipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana kwamba waone uwezekano kabisa wa Kamati hii ya Mipango na Fedha kama alivyo Mpango mwenyewe Waziri wetu aone uwezekano wa kwamba Kamati hii ni vizuri ikapitia, itakuwa tumeitendea haki kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiuangalia muswada huu umelenga pia kuwa hudumia walemavu, jamii mbalimbali, akina mama, watoto na kadhalika, tumeutendea haki kabisa muswada huu nadhani umefika mahala pake ambapo sasa maelekeo ni mazuri.
Mimi niombe tu Waziri Mpango tunakuamini sana, Bunge hili linakuamini sana, wewe, Naibu wako pamoja na Wizara nzima, tuombe sana, Kamati ya Mipango na Fedha, niombe sana ishiriki kwenye mambo hayo ambayo wao watakuwa wamepitisha kule hawa wanapitia kuangalia kilichomo kwenye Halmashauri yao tutakuwa tumeitendea haki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vinginevyo naunga mkono hoja, ahsante sana, nakushukuru.