Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deo Kasenyenda Sanga (10 total)

MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali ilichukua eneo kubwa kwa ajili ya kujenga Soko la Kimataifa, Makambako na iliahidi kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo; na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kuwalipa fidia hiyo:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa mpango wa kujenga Soko la Kimataifa la Makambako ni wa muda mrefu na suala la wananchi kulipwa fidia limechukua muda mrefu pia. Sababu zilizosababisha kuchelewa ni ufinyu wa bajeti na hivyo kusababisha kurudia kufanya tathmini ya mali na mazao ya wananchi waliotoa maeneo ya kupisha mradi huu. Tathmini ya kwanza ilifanyika mwaka 2011 na kurudiwa mara ya pili mwaka 2015 baada ya muda wa kulipa fidia kisheria kupita.
Mheshimiwa Spika, tayari Mthamini Mkuu wa Serikali amepitisha tathmini hii mpya na hivyo, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Makambako itatenga fedha kwa ajili ya malipo ya fidia katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kwa hiyo, wananchi waliotoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Kimataifa, Makambako watalipwa fidia katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali imeshaweka Mkandarasi ambaye kwa sasa yuko site anaendelea na kazi ya Mradi wa umeme katika Vijiji vya Mawande-Utengule, Luhota, Ngamanga, Ikwata, Mlowa, Mkolanga, Ibumila, Mahongole, Manga Usetule, Kifumbe, Mtanga, Kitandililo, Ibatu, Nyamande, Mtulingala na Mbugani;
Je, ni lini mradi huo wa umeme katika vijiji hivyo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyanda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Ni kweli kwamba Serikali imeweka Mkandarasi Lucky Exports ambaye kwa sasa anatekeleza mradi wa REA awamu ya pili Mkoani Njombe. Mkandarasi huyo amepewa Vijiji vya Ikwata, Kifumbe, Luhota, Manga, Mlowa, Mwande, Ngamanga, Usetule pamoja na Utengule, ambayo amepatiwa kama kazi ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kazi ya usanifu tayari imekamilika na kwa sasa Mkandarasi anasubiri kusaini Mkataba kati yake na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kabla ya mwezi Machi mwaka huu, ili aanze utekelezaji wa mradi. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi unajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomiti 38.8, lakini pia ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 51, ufungaji wa Transfoma 19 ambapo transforma nne za ukubwa wa kVA 25 na transfoma 15 za ukubwa kwa kVA50. Hii ni pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,875. Kazi hii itachukua miezi sita kukamilika na itagharimu shilingi bilioni 3.3.
Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Mahongole, Manga, Mbugani, Mtanga, Mtulingala, na Nyamande vimewekewa umeme kwenye Mradi wa awamu ya tatu, (REA phase III) inayoanza utekelezwa hivi karibuni. Kazi ya kupeleka umeme kwenye Vijiji hivi inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33, yenye urefu wa kilomita 73, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 36, ufungaji wa transfoma 14 ambapo transfoma tano za ukubwa wa kVA 25 na transfoma tisa za ukubwa wa kVA 50. Hii ni pamoja na kuwaunganishia umeme wateja awali 1493. Kazi hii itaanza Julai mwaka huu na itagharimu shilingi bilioni 4.05.
Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Ibatu, Ibumila na Kitandililo tayari vimefanyiwa tathmini ya gharama za kupeleka umeme na kazi inatakiwa kufanyika kwenye kazi za nyongeza lakini kutokana na gharama kuwa kubwa itajumuishwa kwenye mradi wa awamu ya tatu.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka kwenye vijiji hivi inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu kilomita 11, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo kilovoti o.4 yenye urefu wa kilomita 13 pamoja na ufungaji wa transfoma tano ambapo transfoma ambapo transfoma moja ina ukubwa wa kVA 50 na transfoma Nne za ukubwa kVA 100.
Hii pia itaunganisha pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 589. Kazi hii itaanza Julai, 2016 na itagharimu takribani shilingi milioni 885.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Miradi ya Maji Manga pamoja na Kijiji cha Mutulingara inasuasua tu mpaka sasa.
Je, ni lini miradi hii itapatiwa fedha ili iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi ya Maji ya Manga na Mutulingara, ni miongoni mwa miradi ya Vijiji 10 inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Makambako. Kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Manga inaendelea na hadi kufikia mwezi Machi, 2016, utekelezaji wake ulifikia asilimia 90. Serikali tayari imemlipa mkandarasi kiasi cha shilingi milioni 235.08 kati ya shilingi milioni 491.9 anazodai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Mradi wa Mutulingara, bado haujaanza kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi huu katika awamu ya pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 992.8 kwa ajili ya miradi ya maji katika Halmashauri ya Mji wa Makambako.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Makambako kuwa Hospitali lakini tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa vifaa tiba na kufanya watu wengi kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula.
Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa hivyo ili watu wasipate taabu ya kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupandisha hadhi Kituo cha Afya Makambako kuwa Hospitali, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya umeme chumba cha upasuaji, kitanda cha kufanyia upasuaji na seti tatu za vifaa vya upasuaji akina mama wajawazito na seti mbili za upasuaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo, tukiri kwamba bado upo upungufu wa vifaa kama vile X-ray, Ultrasound, ECG machine na mashine ya dawa za usingizi, pulse oxymeters, monitors, seti ya mashine ya kufulia nguo na vifaa vya meno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 20.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kupitia vyanzo vya mapato ya ndani. Aidha, Halmashauri imepanga kukopa shilingi milioni 154.2 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Kutoka Kijiji cha Mutelewele kwenda Makambako ni kilometa tano wakati kwenda Halmashauri ya Wanging‘ombe ni kilometa 65; kutoka Kata ya Soja kuja Makambako Mjini ni kilometa 25 na kwenda Halmashauri yao ya Wanging‘ombe ni kilometa 88 na kutoka Kijiji cha Nyigo kuja Makambako ni kilometa 8 wakati kwenda Halmashauri ya Mufindi ni kilometa 88 na huduma zote zikiwemo matibabu wanazipata Makambako; kutoka Kijiji cha Igongolo ni umbali wa kilometa 6 kwenda Makambako wakati kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni kilometa 54.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kugawa mipaka upya ili wananchi wapate huduma karibu na Halmashauri yao ili iendane na kauli mbiu ya kusogeza huduma karibu na wananchi?
(b) Je, ni lini sasa Serikali itapima upya mipaka hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, Vijiji vya Mutewele na Saja viko katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging‘ombe na Kijiji cha Nyigo kiko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa vijiji hivyo kijiografia viko karibu na Halmashauri ya Mji wa Makambako kwa maana ya huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia njema ya Mheshimiwa Mbunge ya kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi vipo vigezo na taratibu zinazozingatiwa katika kusajili au kubadili mipaka ya vijiji. Mapendekezo haya yanapaswa kujadiliwa kwanza katika Mikutano Mikuu ya Vijiji, Kamati za Maendeleo ya Kata, Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri zote, Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC) na Kamati za Ushauri za Mikoa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mabadiliko ya mipaka hiyo yataathiri mipaka ya utawala ya Mikoa ya Iringa na Njombe ambapo lazima wadau wa pande zote wakubaliane kuhusu maamuzi hayo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, napendekeza haya yapitishwe kwanza kwenye vikao vilivyotajwa na endapo vitaridhiwa, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itayafanyia kazi mapendekezo hayo sambamba na maombi yaliyowasilishwa kutoka maeneo mengine.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga Vyuo vya VETA kwa kila Wilaya ili kuwasaidia vijana
kujifunza stadi za kazi mbalimbali:-
(a) Je, hadi sasa ni Vyuo vingapi vya VETA vimeshajengwa katika nchi
nzima?
(b) Je, ni lini Chuo cha VETA kitajengwa katika Wilaya ya Njombe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa
Makambako, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Serikali kupitia Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA imeshajenga na kumiliki vyuo 29 vya
ufundi stadi vya ngazi ya Mkoa, Wilaya na vyuo maalum vya ufundi. Vyuo hivyo
orodha yake ni Mikoa ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Moshi,
Manyara, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Iringa, Mwanza, Kihonda na Tabora. Vyuo
vya Wilaya ni Dakawa, Mikumi, Singida, Songea, Mpanda, Shinyanga, Kagera,
Mara, Makete, Ulyankulu na Arusha ambapo vyuo maalum vya ufundi ni pamoja
na Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro, Chuo cha Mafunzo ya TEHAMA
Kipawa na Chuo cha Mafunzo ya Hoteli na Utalii -Njiro.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haina mpango wa
kujenga chuo cha ufundi stadi katika Wilaya ya Njombe, badala yake
itaviboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi - Njombe na Ulembwe na
kuvijengea uwezo ili viweze kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na mafunzo ya
maendeleo ya wananchi. Aidha, Mkandarasi wa ujenzi wa Chuo cha VETA cha
Mkoa wa Njombe ameshapatikana ambaye anaitwa Herkin Builders Limited na
yupo katika eneo la kazi, Kijiji cha Shaurimoyo Wilaya ya Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo hicho kinajengwa katika eneo hilo
kimkakati kutokana na miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Mchuchuma na
Liganga. Vilevile, Wizara kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga fedha kiasi
cha shilingi milioni 450 kwa ajili ya kujenga bweni katika chuo cha VETA Makete ili
kuongeza udahili kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Mwaka 2014 Rais wa Awamu ya Nne alipokuja Makambako aliahidi kutoa Sh.600,000,000/= ili zisaidie kuboresha au kuchimba bwawa la maji Makambako litakalotoa huduma ya maji kwa wananchi wa mji huo:- Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili zifanye kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi wa maji Makambako. Mradi huu utahusisha ujenzi wa bwawa eneo la Tagamenda, chujio la kutibu maji, matanki ya kuhifadhi maji na ulazaji wa bomba kuu na mabomba ya kusambaza maji. Mradi huu unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 38. Serikali imepata mkopo wa gharama nafuu kutoka Serikali ya India kwa ajii ya utekelezaji wa mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali wakati inasubiri utekelezaji wa mradi huo mkubwa imechukua hatua za dharura za kuboresha hali ya huduma ya maji mjini Makambako kufuatia ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Mji wa Makambako. Mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 654. Kazi zitakazotekelezwa kwa mradi huu ni pamoja na ujenzi wa kitekeo, tanki, bomba kuu, pampu ya maji na nyumba ya pampu. Kiasi cha shilingi bilioni mbili kimetengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 na zabuni imetangazwa tarehe 4/1/2017 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Bomba la mafuta la kwenda Zambia limepita katikati ya Mji wa Makambako na barabara ambayo ipo juu ya bomba hilo hairuhusiwi kutengenezwa hivyo kuwa na mashimo mengi na kuhatarisha maisha ya watu wanaoitumia barabara hiyo.
(i) Je, ni lini Serikali italihamisha bomba hilo?
(ii) Je, kwa nini barabara hiyo isitengenezwe, ili wananchi waendelee kupita kwa urahisi wakati Serikali inajipanga kulihamisha bomba la mafuta?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua usumbufu wanaopata wananchi wa Makambako kutokana na bomba la mafuta kwenda Zambia (TAZAMA) linalopita katika Mji wa Makambako. Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inawasiliana na Kampuni ya Tanzania na Zambia ya kusafirisha mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia (TAZAMA Pipeline Limited) kuainisha hatua stahiki zitakazochukuliwa kuondoa tatizo hilo. Wakati mawasiliano yanafanyika pamoja na kuainisha hatua za gharama zitakazotumika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania itatengeneza maeneo yaliyoharibika, ili wananchi waweze kutumia barabara hiyo bila matatizo.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA (K.n.y. MHE. DEO K. SANGA) aliuliza:-
Serikali iliahidi kufuta Ushuru mdogo mdogo unaokusanywa na Halmashauri ili wajasiriamali wadogo wakiwemo akina mama lishe waweze kuongeza kipato kupitia shughuli zao.
Je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwa Halmashauri zetu nchini ili wasikusanye tena ushuru huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyanda Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefuta ushuru na tozo ambazo zilikuwa zinatozwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi mfano Mama Lishe, wauza mitumba wadogo wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo wadogo kama mboga mboga na ndizi na matunda isipokuwa biashara za migahawa na maduka na wale ambao wako kwenye maeneo rasmi. Vilevile wafanyabiashara wadogo walio nje ya maeneo maalum ya kibiashara wenye mitaji chini ya shilingi 100,000 hawatatozwa ada, kodi na tozo zozote. Kodi nyingine zilizofutwa ni ushuru wa huduma (service levy) kwenye nyumba za kulala wageni, ada za vibali vinavyotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zilikuwa zinatozwa na TFDA, OSHA, Fire na Bodi ya Nyama na ada ya makanyagio.
Serikali pia imepunguza ushuru wa mazao kutoka asilimia tano haid asilimia mbili kwa mazao ya chakula na asilimia tatu kwa mazao ya biashara. Aidha, mazao yanayosafirishwa kutoka wilaya moja hadi nyingine yasiyozidi tani moja hayatatozwa ushuru wa mazao.
MHE. EDWARD F. MWALONGO - (K.n.y. MHE. DEO K. SANGA) aliuliza:-
Mji wa Makambako unakabiliwa na tatizo kubwa la maji kutokana na ongezeko la watu na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kuanza kwa ujenzi wa mradi wa maji na kazi ya usanifu wa mradi huo imeshafanyika:-
Je, ni lini sasa ujenzi wa mradi huo wa maji utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Mkambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP I) imekamisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Makambako. Kazi zitakazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa Tagamenda, uchimbaji wa visima virefu vya Idofi na chemichemi ya Bwawani, ujenzi wa bomba kuu na mfumo wa usambazaji wa maji na matanki makubwa ya kuhifadhi maji. Mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 155,253.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepata fedha za kutekeleza mradi huo kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India wa Dola za Marekani milioni 500 zitakazotumika kutekeleza miradi ya maji katika Miji mbalimbali ukiwemo Mji wa Makambako. Tayari Serikali imesaini Mkataba wa Kifedha na Serikali ya India na ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019.