Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa (28 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya na kutuwezesha kukusanyika katika Bunge hili la Kumi na Moja la Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili la Kumi na Moja, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Bagamoyo kwa kunipa fursa nyingine ya kuwaongoza kama Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo. Niwaahidi tu kwamba nitawatumikia kwa juhudi zangu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kuipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa hoja hii ambayo imewasilishwa ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa mwaka 2016/2017. Niipongeze Serikali kwa kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa viwanda kama mkakati maalum wa kuendeleza ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa nchi yetu. Huu ni mkakati sahihi ambao unajipanga moja kwa moja kupiga vita umaskini katika nchi yetu na mkakati ambao utawezesha kuzalisha ajira nyingi na kuwaondoshea kadhia vijana wetu wa kiume na wa kike ambao wanahitimu katika vyuo vyetu mbalimbali na shule mbalimbali, wanaingia katika soko la ajira na kukosa ajira. Niwapongeze kwa hilo, huu ni mkakati sahihi ambao tukienda kwa kasi hii kwa miaka mitano bila shaka nchi yetu itakuwa katika hali nyingine kabisa na kujenga maisha bora kwa kila Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa viwanda huu utatumia malighafi za ndani za kilimo, mifugo, misitu na uvuvi lakini viwanda pia vitazalisha bidhaa kadha wa kadha ambazo tunazihitaji kwa ajili ya matumizi ya wananchi wetu. Pia zitazalisha ajira kama nilivyosema hapo awali lakini pia viwanda hivi vitawezesha kulipa ushuru na kodi mbalimbali ambazo ni fedha nyingi zitakazowezesha Serikali yetu kuwa na mapato makubwa zaidi na kuiwezesha Serikali kuweza kumudu huduma za jamii katika nchi yetu. Sina namna bali kuunga mkono na kupongeza juhudi hii katika Mpango huu wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuikumbusha Serikali yangu kupitia Wizara ya Fedha na Mpango kwamba wakati tunaweka mkazo huu wa ujenzi wa viwanda, tufahamu kwamba viwanda hivi hivi vinajengwa ardhini. Kwa hiyo, jambo muhimu sana katika Mpango huu ni kuhakikisha kwamba Serikali inamiliki ardhi ili iweze kujenga viwanda hivi. Maeneo yote yale ambayo tunahitaji kujenga viwanda katika mwaka huu unaofuata wa fedha Serikali ijitahidi kuhakikisha kwamba ardhi ile imemilikiwa na Serikali ili mkakati mzima wa ujenzi wa viwanda usije ukaingia katika matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu Bagamoyo tuna mpango maalum wa uwekezaji ama SEZ ambao unajumuisha ujenzi wa viwanda na Bandari ya Mbegani. Katika eneo hili, Serikali tayari imeshatambua eneo la ujenzi wa viwanda hivyo au eneo la uwekezaji. Mwaka 2008 uthamini wa ardhi umefanywa na jumla ya shilingi bilioni 60 zinahitajika kulipwa fidia, lakini hivi sasa mwaka 2016 katika shilingi bilioni 60 zile bado wananchi wanadai shilingi bilioni 47 kwa maana asilimia kubwa ya wananchi bado hawajalipwa fidia. Huu ni mwaka tisa wananchi hawajalipwa fidia lakini mwaka wa tisa pia tumepoteza fursa kadhaa za uwekezaji wa viwanda kwa vile wawekezaji hawatoweza kuweka viwanda ardhi haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka tisa ambayo tumepoteza ushuru na kodi mbalimbali lakini miaka tisa pia ambayo tulipoteza fursa za ajira mbalimbali kama viwanda vingekuwa vimejengwa. Kwa hiyo, naomba niikumbushe Serikali yangu katika mkakati huu na Mpango huu wa maendeleo kuweka mkazo wa kumaliza ulipaji wa fidia kwa wananchi wa Bagamoyo ambao wamekuwa tayari kutoa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na ujenzi wa bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo wezeshi la ujenzi wa viwanda ni ujenzi wa bandari. Nashukuru Serikali katika Mpango huu wa Maendeleo ukurasa wa 28 umeonyesha kwamba Serikali itajipanga kujenga bandari mpya ya Mwambani Tanga na Mbegani Bagamoyo. Hii ni fursa kubwa ya kiuchumi, bandari ni fursa pekee za kiuchumi ambazo mataifa mengine yametumia vizuri kama Singapore na nchi zingine na kuwawezesha kujenga uchumi mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niihamasishe Serikali yangu kwamba katika Mpango huu tusichukue muda mrefu na hasa pale ambapo mkataba wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo umeshasainiwa kati ya nchi yetu na nchi rafiki ya China na Oman. Wenzetu hawa hawatapenda kupoteza muda. Kwa hiyo, tujipange vizuri sana katika mwaka wa fedha unaofuata kuhakikisha kwamba maandalizi ya ujenzi wa bandari ya Bagamoyo yanakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali kwamba viwanda hivi na bandari hizi zinajengwa katika ardhi, wananchi katika Jimbo langu la Bagamoyo eneo ambalo litajengwa bandari, wananchi wa Pande na Mlingotini wako tayari hivi kuhama ili kupisha ujenzi wa bandari hiyo. Haikuwa rahisi sana wao kukubali lakini kwa sababu ya maendeleo ya Taifa letu wamekubali wahame kwa ajili ya kupisha ujenzi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari eneo limetengwa shamba la Kidagoni ambalo awali lilikuwa shamba la NAFCO lakini sasa lina mwekezaji binafsi. EPZ tayari imelianisha shamba hilo kwa ajili ya kuingizwa kwenye mradi wa uwekezaji. Tatizo ni kwamba ardhi hiyo inalazimika iweze kulipiwa fidia ili wananchi hawa waondoke katika maeneo ya ujenzi wa bandari wakabidhiwe eneo lingine na wao wako tayari kuhama hata leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kilio chao kikubwa ni kwamba wana ndugu zao, jamaa na marafiki ambao wanaondoka duniani, hawapendi kuwazika pale Pande na Mlingotini kwa vile ardhi hii sasa hivi itachukuliwa kwa ajili ya bandari lakini hawana namna ya kwenda Kidagoni kabla Serikali haijalipa fidia ya Kidagoni ili wakabidhiwe eneo hilo. Naiomba Serikali yangu Tukufu ijitahidi haraka na kuweka msisitizo wa kuhakikisha kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja mapema iwezekanavyo shamba lile liwe limelipiwa fidia na wananchi wa Pande na Mlingotini waweze kuhamia katika eneo hilo na ujenzi wa bandari usiweze kuchelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la uwezeshaji kwa uchumi wa viwanda ni nishati. Nimefurahi kwamba katika Mpango huu wa Maendeleo, nishati imeainishwa vizuri na msisitizo mkubwa umewekwa katika usambazaji wa nishati katika nchi yetu kuwezesha viwanda na wananchi kuweza kubadili hali ya maisha yao kupitia nishati na hasa nishati ya kutumia gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kimoja ambacho napenda kuikumbusha Serikali katika ukurasa ule wa 25 umeonyesha kwamba kutakuwa na mkakati wa kujenga miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam, nilichokishangaa Mkoa wa Pwani haukutajwa na Mkoa wa Pwani kuna ugunduzi wa gesi mpya Mkuranga na Bagamoyo. Gesi hii imegunduliwa na uchumi wa gesi ni uchumi mkubwa utatuwezesha kuongeza rasilimali, kuongeza fedha katika Serikali yetu na kutuwezesha sisi kuweza kupiga hatua kubwa za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali inajumuisha katika Mpango huu mradi wa uendelezaji wa gesi Bagamoyo, Mkuranga na maeneo mengine ya Pwani lakini pia uelimishaji wa wananchi katika Mkoa wetu wa Pwani ili waweze kushiriki vizuri katika uchumi wa gesi katika nchi yetu. Tuepukane na fujo ambazo tulizipata huko awali ambazo zilitokana pia na wananchi kutokuwa na elimu. Tuhakikishe kwamba Mpango huu unajumuisha maendeleo ya gesi katika maeneo yetu Bagamoyo, Mkuranga na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani ili tuweze kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umeisha, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri na kwa kazi nzuri. Pia, nawapongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Katibu Mkuu, viongozi na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa utendaji mzuri na maandalizi mazuri ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kushukuru mema mengi tunayofanyiwa na Serikali yetu, Jimbo langu la Bagamoyo linakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinahitaji ufumbuzi:-
(i) Kuhusu kuwalipa fidia wananchi wa Zinga, Kerege na Kiromo wanaopisha mradi wa EPZ. Mazingira wezeshi ya uwekezaji ni pamoja na kuwalipa wananchi fidia ya ardhi na mali zao kupisha wawekezaji. Ni miaka tisa sasa wananchi hao bado wanasubiri kulipwa fidia zao. Serikali yetu Tukufu iwalipe fidia wananchi hawa mapema iwezekanavyo.
(ii) Ukosefu wa ajira kwa vijana wengi Jimboni Bagamoyo. Naiomba Serikali kujielekeza zaidi katika kuongeza fursa za mikopo na elimu ya ufundi na ujasiriamali kwa vijana katika JImbo la Bagamoyo. Serikali iharakishe mchakato wa ujenzi wa Chuo cha VETA, Wilaya ya Bagamoyo. Kwa mustakabali wa Taifa, naunga mkono uamuzi wa kukabidhi Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kwa Wizara ya Elimu kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi.
(iii) Azma ya Serikali kupanua na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ni jambo jema sana. Naiomba Serikali yetu Tukufu itutengee Bagamoyo fedha za kutosha kutuwezesha kupanua miradi ya umwagiliaji hususan kujenga miundombinu katika miradi ya umwagiliaji ya JICA - Bagamoyo na Chauru na Kidogozero kule Chalinze. Serikali itutengee pia ruzuku kwa ajili ya pembejeo, msimu huu wa kilimo pembejeo zimekuwa tatizo sana.
(iv) Mtandao wa barabara zinazopitika vijijini ni nyenzo kubwa kwa ajili ya maendeleo ya uchumi na afya kwa wananchi wetu. Kasi ya ujenzi na ukarabati barabara za Bagamoyo Vijijini ni ndogo sana.
Barabara nyingi za Bagamoyo Vijijini ni mbovu na zinawagharimu wananchi kiuchumi na maisha yao. Barabara katika Kata za Fukayosi, Yombo, Kiromo, Zinga na Mapinga na barabara ya Mjini Bagamoyo ni mbovu sana. Serikali iongeze mafungu katika barabara na iangalie uwezekano wa kuunda Wakala wa Barabara Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii una fursa kubwa ya kuchangia pato la Taifa letu na utalii wa Tanzania ni wa namna mbalimbali ikiwemo utalii wa fukwe za bahari, utalii wa wanyamapori, utalii wa utamaduni, kihistoria na malikale. Bagamoyo ina fursa kubwa ya utalii wa kihistoria na malikale. Serikali ituwezeshe kuhifadhi magofu ambayo yanazidi kumalizika mwaka hadi mwaka. Serikali itenge mafungu kwa ajili ya kazi hii. Pia, Wilaya iwezeshwe kufundisha vijana katika fani za kumhudumia mtalii mfano, kuongoza watalii na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ambayo imesheheni mipango na mikakati mizuri, kwa ukombozi wa Watanzania. Nawapongeza pia Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara kwa maandalizi mazuri ya Bajeti. Ni mategemeo yetu kuwa utekelezaji wa Bajeti utakuwa wa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mipango mizuri ya Wizara inatutia moyo. Katika Jimbo langu la Bagamoyo, Kilimo Ufugaji na Uvuvi, ndizo sekta zinazoishikilia Bagamoyo, isipokuwa tuna changamoto kadhaa ambazo tunategemea kupitia bajeti hii tutapata ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ECO-energy Bagamoyo ni changamoto. Sasa ni miaka 10 tangu mradi umeasisiwa, hadi leo hakuna mashamba, hakuna miwa, hakuna sukari, hakuna ethanol, hakuna umeme. Wawekezaji hawaoneshi dalili ya kuanza na jambo hili limeleta mzozo kwa wananchi. Wapo wananchi wa Gama ambao wanadai eneo lao kuporwa na ECO-energy, lakini miaka 10 sasa ufumbuzi haujapatikana. Waziri akifanya majumuisho, atueleze nini mpango wa Serikali kumaliza mgogoro huo wa wananchi wa Kitongoji cha Gama na lini Mradi utaanza kwa uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Wizara wa kukazia kilimo cha umwagiliaji ni mpango sahihi sana. Bagamoyo tuna maeneo makubwa ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Tuna changamoto ya mafungu madogo kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji; Mradi wa umwagiliaji wa BIDP wenye eneo zaidi ya hekta 3,000, lakini ni sehemu ndogo sana ndiyo ina miundombinu ya umwagiliaji. Serikali itenge mafungu ya kutosha, kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili kuwezesha zana za kilimo na pembejeo. Kilimo kina fursa ya kutoa ajira nyingi kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la wakulima na wafugaji bado halijapata ufumbuzi katika Jimbo la Bagamoyo. Wakulima wanapata tabu sana, kwa kuharibikiwa mazao yao na wafugaji, wakulima wamejaribu kila njia lakini mafanikio hayapo. Waziri atueleze, ana mikakati gani ya kumaliza matatizo haya ya wakulima wa Bagamoyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatiwa moyo na mikakati ya Wizara kuhusu kuendeleza uvuvi nchini, ila nimjulishe Waziri kuwa uvuvi wa Bagamoyo hauna mabadiliko yanayoonekana, kwa miaka 54 ya uhuru wetu, bado mvuvi wa Bagamoyo anatumia ngalawa yenye tanga na nyenzo hafifu sana.
Mheshimiwa Waziri afahamu kuwa uvuvi una fursa ya kutengeneza ajira nyingi za vijana, wanawake na wajasiriamali. Wizara ijikite katika kuongeza elimu ya uvuvi, ujasiriamali na uwezeshaji katika Sekta ya Uvuvi katika Jimbo la Bagamoyo, Wilaya ya Bagamoyo na maeneo yote ya uvuvi nchini.
Mheshimia Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili la bajeti, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Napenda nichukue fursa hii pia kumpa pongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa hoja yake, lakini pia na kwa utendaji mzuri wa kazi katika Wizara yake. Nina imani kwamba chini ya uongozi wake, nchi hii itaingia kwenye uchumi wa kati, uchumi ambao utaongozwa na ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema kwamba mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga nchi ya uchumi wa kati, ikiasisiwa na ujenzi wa viwanda, ni mwelekeo mzuri sana, kwa sababu huu ndiyo ukombozi. Vijana wetu wengi wa kiume na wa kike wanapata madhila makubwa sana kwa kukosa fursa za ajira na fursa za kujiajiri zinazotokana na nyenzo zile ambazo zipo kama kuna fursa za ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa na viwanda vingi, maana yake ajira zitakuwa nyingi na fursa za kujiajiri pia zitakuwa nyingi zaidi. Kwa hiyo, hii itatupa heshima kubwa sana kwa vijana wetu wanaochipukia hivi sasa, lakini pia kulijengea Taifa uwezo wa mapato makubwa zaidi na kuwaondolea wananchi wetu umaskini. Tunaunga mkono jambo hili, tunawatakia heri Serikali yetu ya Awamu ya Tano waweze kufanikiwa katika jambo hili kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitangulie kusema kwamba naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia na nategemea kwamba tutapata mafanikio katika ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika mradi wa EPZ. Mradi huu ni wa Kitaifa na kule kwenye Jimbo langu, Bagamoyo tunao mradi huu, ni mradi ambao tunautarajia kwamba kwa sababu ya eneo kubwa ambalo limetwaliwa kwa ajili ya kujenga viwanda vya uchakataji wa bidhaa kwa ajili ya kusafirisha nje; tutapata ajira nyingi na nchi yetu itapata mafanikio kuelekea kwenye uchumi wa kati. Ni jambo kubwa!
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo linawatesa sana wananchi wa Bagamoyo ni kwamba tangu mwaka 2008 walifanya tathmini ya ardhi hii ili iwe free kuweza kutumika kwa ajili ya kujenga viwanda. Mpaka hii leo, miaka tisa baadaye, bado wananchi wale wanadai fidia ya ardhi ambayo wameitoa na mali zao. Hili ni jambo zito sana, kwa sababu hakuna kiwanda ambacho kitaweza kujengwa kama wananchi hawa hawajapewa fidia yao na ardhi ile iwe free ili mwekezaji anapokuja, apate ardhi ambayo haina tatizo lolote; ni ardhi ambayo iko tayari kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka tisa hii ya ukosefu wa fidia, imewafanya wananchi wawe na hasira; wana hasira na Mbunge wao, wana hasira na Madiwani na wana hasira na Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi. Wananchi hawa hamna namna ambayo naweza sasa hivi kama Mbunge kusimama na kuwaambia kwamba tuendelee kusubiri zaidi. Miaka tisa hii ni miaka ambayo tumepotea fursa nyingi ambazo tungeweza kuzipata wakati huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2008 fidia ilikuwa imetathminiwa kwamba ni shilingi bilioni 60; hivi leo ninaposimama hapa miaka tisa baadaye bado wananchi wanadai shilingi bilioni 47.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine Mheshimiwa Waziri amesema ni zaidi ya hapo, lakini siyo zaidi ya hapo kwasababu ameichanganya na fidia ya Bandari. Tunasema hii ni fidia ya EPZ, shilingi bilioni 60 mwaka 2008, bado wanadai bilioni 47 hivi sasa, kwa maana ulipaji umekuwa mdogo sana. Hatuwezi kupata uwekezaji wa viwanda kabla hii ardhi haijawa free na haiwezi ikawa free kabla hatujawalipa fidia hawa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2012/2013, Bunge hili Tukufu lilipitisha bajeti ya shilingi bilioni 52 kwa ajili ya kulipa fidia na zikawa ring fenced lakini hazikutoka. Mwaka wa fedha wa 2013/2014, tukapitisha shilingi bilioni tisa zikatoka shilingi bilioni sita; mwaka 2014/2015, sifuri; mwaka 2015/2016 sifuri; hii bajeti sasa hivi 2016/2017 nayo pia sifuri. Sasa Mheshimiwa Waziri anapojipanga kujenga viwanda na eneo liko pale, hajaweza kulitwaa lile eneo kwa sababu tu hajalipa fidia, tutafikaje kwenye viwanda kama hatutaweza kuwalipa wananchi hawa? Wananchi hawa wanapokuwa na hasira, mimi kama Mbunge nafahamu ni kwa namna gani wana hasira kwa sababu hawajalipwa fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri namtegemea sana, namwamini kwa juhudi zake, nina imani kwamba hili jambo atalitafutia dawa hivi karibuni. Aliniambia wakati fulani atakopa, lakini sasa hivi siyo wakati wa kusema tutakopa, kwa sababu jambo la viwanda kwetu na kwa Awamu ya Tano ni priority. Ni jambo kubwa kwamba tutakopa, haiwezi ikawa sasa hivi ni mpango. Sasa hivi kama tulivyotenga bajeti, mwaka 2012/2013 na 2013/2014 bajeti ndogo, ndiyo hivyo ambavyo Serikali inabidi ioneshe msukumo mkubwa sana ili tuweze kuvuka hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine napenda kusema kwamba, tathmini imefanywa mwaka 2008, huu ni mwaka 2016, miaka tisa baadaye. Thamani ya ardhi mwaka 2008 sio thamani ya ardhi mwaka 2016. Sasa hivi ardhi ya ekari moja ya shilingi milioni tatu na nusu Bagamoyo huwezi kuipata mahali. Mwananchi ananiuliza mimi, Mheshimiwa Mbunge hivi milioni tatu naenda kununua kiwanja mahali gani tena kwa ekari moja? Namwomba Mheshimiwa Waziri waangalie upya uthamini mpya kama vile Sheria ya Ardhi inavyoelekeza. Uthamini ufanywe upya, muda umepita sana ili kuhakikisha kwamba wananchi hawa tunawatendea haki na sisi tunapata mambo yaliyokuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu wa viwanda lazima uunganishwe na ujenzi wa bandari na uunganishwe pia na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, kwa sababu viwanda bila bandari na miundombinu ya usafirishaji kama barabara, reli na kadhalika itakuwa ni jambo ambalo haliwezi likawa na mafanikio.
Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu ya Awamu ya Tano ijihakikishie kwamba barabara zile za ahadi, Bagamoyo - Mlandizi mpaka Vikumbulu kwa ajili ya kuunganisha viwanda na barabara ya Morogoro ijengwe na kumalizika; lakini barabara pia ya Saadani - Pangani mpaka Tanga nayo ijengwe ikamilishwe ili kuweza kuunganisha viwanda na kaskazini mwa Tanzania na hatimaye nchi jirani ya Kenya; na zaidi ya hapo, pia ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge na kuunganisha reli ya kati na viwanda hivi Bagamoyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia mradi wa Kiwanda cha Sukari Bagamoyo ama wengine tunakiita Bagamoyo Eco-energy. Kiwanda cha Sukari Bagamoyo kimeasisiwa muda mrefu. Mimi nimepata Ubunge mwaka 2006 tayari tulikuwa tunaongelea Kiwanda cha Sukari Bagamoyo. Kina uwezo mkubwa! Kina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 kwa mwaka, lakini pia kina uwezo wa kuzalisha umeme Megawatt 100,000 kwa mwaka pia ethanol kwa meter cubes 12,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, sukari ni jambo la kimkakati, shida kubwa tunayoipata sasa hivi ni kwamba ni aibu kwa nchi, ni pale ambapo wananchi wana uhaba wa chakula. Sukari tunaitumia kwenye vyakula vyetu, tangu chai asubuhi na katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama soda na vitu vingine, ukitaja ni vingi tu. Ndiyo maana sasa hivi tupo kwenye mtikisiko na Mheshimiwa Rais ana kazi kubwa sana ya kuhangaika na watu wanaohodhi sukari katika magodauni.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri amwondolee adha hii Mheshimiwa Rais ya kugombana na watu wanaotaka kuhodhi sukari kwenye magodauni yao. Asimamie kiwanda hiki ambacho kina uwezo wa kupunguza uhaba wa sukari kwa asilimia 50. Tunataka sukari tani 600,000, tuna-produce sasa hivi tani 300,000; tuna tofauti ya tani 300,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda hiki peke yake kina uwezo wa tani 150,000. Kwa nini Mheshimiwa Rais ahangaike? Ana mambo makubwa zaidi kuliko kuzungumzia sukari sasa hivi, kugombana na hawa watu. Tengeneza sukari ili waendelee kuhodhi, viwanda viweze kuwapa tu sukari nyingi na zitoe ajira nyingi. Hana haja ya kuhangaika, maana ana mambo makubwa zaidi ya muhimu ya kuongelea zaidi ya kuongelea mambo ya sukari. Huu siyo wakati wa kuzungumzia sukari tena! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mradi huu tumeanza kuuzungumzia mwaka 2006 huu ni mwaka wa 11. Miaka 11 ya kusubiri ili Serikali yetu iweze ku-support ujenzi wa kiwanda hiki kikubwa cha sukari; ardhi tumetoa jumla ya hekta 7,800 kwa maana ni ekari 19,500. Ni ardhi kubwa, nzuri inapakana na mto Wami. Ni ardhi ambayo inafaa kwa umwagiliaji. Serikali lazima iite huu ni mradi wa mkakati. Kuna miradi mingine ya mkakati lakini huwezi kufananisha na mradi huu wa mkakati. Huu unahusu chakula cha binadamu, chakula cha Mtanzania, kumwondoa katika aibu ya uhaba wa chakula ndani ya nchi yake; anaangaliwaje Mtanzania tunavyoambiwa kwamba hatuna sukari katika nchi yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unahitaji kila support ili fursa hizi za miaka tisa iliyopita tangu shamba dogo la mfano lilipoasisiwa mwaka 2008 na kiwanda kutegemewa kuanza kujengwa miaka michache baadaye, miaka tisa sasa tumepoteza fursa chungu nzima za uwekezaji. Waliokuwa wanataka kuwekeza kwenye sukari, kwa sababu ya kutokupata support ya kutosha kwenye mradi huu, hawakuweza kujenga viwanda, labda wamekwenda kujenga kiwanda cha sukari sehemu nyingine, sisi tunaendelea kupata tabu ya sukari hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumekosa fursa nyingi sana za ajira; kiwanda hiki kimepangwa kitoe ajira direct 2,300. Ajira za out growers ama wakulima wa kimkataba kati ya 1,500 hadi 2,000, lakini ajira zinazoendana na ujenzi wa kuwepo kwa kiwanda hiki ni ajira 16,000. Maana yake tumepoteza fursa ya ajira 20,000 kwa vijana wetu wa kike na wa kiume kwa kipindi chote hiki cha miaka tisa ambayo hatujaipa msukumo wa kiwanda hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia kwenye hotuba yake ukurasa wa 18, mradi wa mkakati hamna! Nimeisoma tangu mwanzo mpaka mwisho, nimeona Liganga, Mchuchuma na kadhalika. Tunahitaji umeme, lakini kwanza tumboni kabla hata hatujafika huko; sikatai lakini huu ndiyo mradi ambao ningeuona ni mradi wa mkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia kwenye kitabu cha maendeleo cha bajeti, hakuna kitu chochote kwa ajili ya mradi huu. Namwomba Mheshimiwa Waziri akumbuke kwamba, vijana wanazihitaji hizi ajira 20,000 ambazo zinatolewa kama fursa ya kuwepo kiwanda hiki. Watanzania wanataka sukari, Watanzania wanataka umeme…
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika nikushukuru kunipa fursa hii ya kuchangia katika hoja iliyokuwa mbele yetu, na nitangulie kwa kuunga mkono hoja. Naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ya bajeti pamoja na utekelezaji mzuri wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mkakati wa ujenzi wa viwanda ili Tanzania iweze kufikia hadhi ya nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Hili ni jambo jema sana ni jambo lenye tija kwa uchumi wa nchi yetu Tanzania lakini ni ukombozi kwa mamilioni ya vijana wa Tanzania wa kike na wakiume.

Mheshimiwa Naibu Spika, shida kubwa ya vijana wetu wa kike na wa kiume wanaoingia kwenye soko la ajira sasa hivi ni ukosefu wa kazi, ujenzi wa viwanda maana yake viwanda vingi maana yake ni ajira nyingi. Tutawapa hadhi vijana wa Kitanzania watajisikia binadamu, watajisikia kuwa na heshima na wataweza kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa kiasi kikubwa iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri katika Jimbo langu la Bagamoyo Serikali imetenga ardhi, jumla ya hekta 9,080 ama kwa kipimo cha ekari 22,700 hili ni kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika kata ya Zinga na kata ya Kiromo jumla ya vijiji vitano vitahusika na mradi huu. Tathmini imefanywa mwaka 2008 jumla ya wafidiwa 2,180 na kwa kipindi hicho thamani ya fidia ilikuwa shilingi bilioni 60, mpaka hivi sasa Serikali imelipa bilioni 26.4 kwa wafidiwa 1,155. Kwa hiyo, kuna wafidiwa 1,025 ambao bado hawajapata fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri mwaka 2008 mpaka leo mwaka 2017 ni jumla ya miaka kumi sasa. Mheshimiwa Waziri ungekuwa kule kijijini ujifanye wewe ni mzee kijijini kule Kagera mwaka 2008 shamba lako na nyumba limezuiliwa na Serikali ili liweze kufanywa mradi wa EPZ na ukazuiliwa kufanya maendelezo katika nyumba ile, ukazuiliwa kufanya maendelezo katika shamba lako, usubiri fidia kwa miaka kumi, fidia usiione. Mheshimiwa Waziri saa hizi baada ya miaka kumi hali ya nyumba yako ikoje, hali ya shamba lako ikoje, hali ya maisha yako kwa ujumla na familia yako ingekuwa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo madhira ya wananchi wa Bagamoyo ambao tangu mwaka 2008 wamezuiliwa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, wako katika hali mbaya sana. Mimi kama Mbunge nashindwa kupita hawanielewi, hakuna jambo ambalo naweza nikawaambia wakanisikiliza. Sasa hivi Mheshimiwa Waziri una fursa kubwa hii ya azma nzuri ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga viwanda, viwanda havijengwi hewani vinajegwa ardhini lazima ardhi hii iweze kulipiwa hivi sasa baada ya miaka kumi ili wananchi nao wajisikie nao wako katika nchi yao huru na wanaweza wakaendeleza maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujumuisha hoja yako unipe, ama utupe majibu mazuri na ya uhakika kwamba ni lini wananchi hawa wa Zinga, Kondo, Pande na Kiromo watalipwa fidia zao kwa sababu Mheshimiwa Waziri kwa madhira haya, wewe ni rafiki yangu na mimi nilishawahi kuwa kwenye Serikali nitaona aibu sana lakini nitakuwa sina namna nyingine bali kutangaza azma yangu ya kushikilia shilingi kama sitapata majibu ya uhakika, kwamba lini wananchi hawa watalipwa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema pia katika hotuba yake kwamba fidia hizi inategemewa zitalipwa na mwekezaji mwenyewe jambo zuri, lakini Mheshimiwa Waziri niulize, kwa nini Serikali imebadilisha utaratibu, utaratibu ambao tumejiwekea kwamba fidia za ardhi ya wananchi wetu tulikuwa tunazilipa sisi wenyewe kama Serikali, mwaka 2012/2013 kwa ajili ya mradi wa EPZ, tulitenga shilingi bilioni 50 lakini zilitoka bilioni 10.9, mwaka 2013/2014 tulitenga bilioni tisa zikatoka bilioni tatu, mwaka 2014/2015 tulitenga shilingi bilioni saba, zikatoka bilioni saba zote na huo ndiyo ulikuwa utaratibu wakati wote tunaposema kwamba mwekezaji alipie fidia ya ardhi maana yake tunapunguza vivutio kwa wawekezaji hao na mitaji inatafutwa dunia nzima, unapopata mtu ana mtaji basi huyo ni wa kumshikilia na kimojawapo ni kigezo hiki ambacho Serikali inaweza ikalipia fidia zake kama tulivyokuwa tunafanya lakini pia nimuambie Mheshiwa Waziri hata kama mwekezaji atalipa fidia katika eneo hili eneo la EPZ ni hekta 9,080 na mwekezaji yule amesema ata develop hekta 3000 peke yake, hizi hekta 6000 zingine nani atalipia? miaka 10 baadae nani atalipia?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hao wataendelea kuteseka, wananchi hawa wataendelea kuchukia Serikali yao, wananchi hao watashindwa kujiendeleza katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho atueleze vizuri kwa nini tumefanya mabadiliko haya na uhakika upi utakaotuwezesha wananchi hawa waweze kulipwa fidia zao kikamilifu na mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kuelezea kwamba mradi huu wa Special Economic Zone Bagamoyo unajumuisha pia ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Bandari mpya ya Bagamoyo, bandari yenye uwezo mkubwa zaidi kushinda bandari yoyote katika mwambao wa Afrika Mashariki na kusema kweli ni mwambao wa Afrika nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2002 ndiyo kwa mara ya kwanza mwezi Septemba tulisaini MoU ya ujenzi wa bandari, na mwaka 2013 Machi, Rais Xi Jinping wa Serikali ya China na aliyekuwa Rais wa Tanzania, walishuhudia kutiwa saini kwa framework agreement ya ujenzi wa bandari hii, mwezi Machi 2013 mpaka leo ni mwaka wa tano sasa na ni mradi ambao umeshuhudiwa kuwekewa saini na Rais Xi Jinping, tena wakati ule ana wiki chache tu baada ya kuteuliwa kuwa Rais wa Taifa kubwa lile, huo ni mradi muhimu sana kwa nchi ya China. China ni rafiki zetu, China wamekubali kutusaidia, pesa ni ya kwao na tumesaini framework agreement Machi 2013 lakini mpaka sasa hivi miaka Mitano ni muda mrefu hatupaswi kukaa muda huo wakati mtaji tumeushikilia, mtaji huu kila mmoja ndani ya Bara la Afrika na nje ya Afrika wanautafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hiki tunaongea na China Merchant Port kipindi hiki hawa wa China Merchant Port wamekamilisha maongezi na Serikali ya Sri Lanka sasa hivi wanaendesha Colombo International Container Terminal wamekamilisha maongozi na Togo, wanaendesha Lome Port Container Terminal, wamekamilisha maongezi na Nigeria wanaendesha Tincan Port Island Container Terminal na wamekamilisha miradi kadhaa mingine ambayo kwa ukosefu wa muda sitaweza kuisema, kipindi hiki tangu 2012 mpaka leo tunajadiliana nao mpaka lini?

Mheshimiwa Waziri nakuomba utakapokuja hapa uweze kusema kwamba ni lini bandari hii itajengwa, lini tutakamilisha maongezi na China Merchant Port?

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la bandari nalo pia lina mgogoro wa fidia, wananchi 687 walipunjwa fidia zao, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo alithibitisha hivyo na Mthamini Mkuu wa Serikali ameshafanyia tathimini tayari. Mheshimiwa Waziri ndani ya bajeti yako hakuna pesa za kuwalipa hawa wananchi, naomba utakapotoa majumuisho utuambie hawa wananchi 687 waliopunjwa fidia yao watalipwa lini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala kubwa zaidi, katika kipindi hiki cha maandalizi Serikali iliwaahidi wananchi hawa jumla ya kaya 2000, kwamba itawahamishia mahali pengine na shule yao ya msingi ya Pande itajengwa huko, zahanati yao waliyojenga kwa nguvu zao wananchi na nguvu za wahisani itahamishiwa kule, Ofisi ya Serikali ya Kijiji itahamishiwa kule, nyumba zao za ibada, makanisa na misikiti itajengwa kule ili wawe na makazi mapya. Nyumba watajenga wenyewe lakini miundombinu hii ya jamii itajengwa kule, hili jambo halijatokea mpaka hivi sasa, na wananchi hawa wanaishi kwa wasiwasi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara yako ya Viwanda ambaye wakati ule alikuwa DG wa EPZA anakumbuka safari zangu nyingi ambazo nilikuwa nimeenda kule EPZA kufuatilia jambo la makazi mapya.

Mheshimiwa Waziri utakapofanya majumuisho tafadhali chonde chonde uwaambie wananchi wa Bagamoyo hao wanaopisha bandari lini watapata makazi yao mapya ili waondoke pale na nchi yetu iweze kujenga bandari mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa muda ulionipa na naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali kabisa, nitangulie kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ya bajeti ambayo imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama katika nchi yetu unaendelea kuwekewa mkazo na msisitizo ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaendelea na shughuli zao za maendeleo bila kubughudhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kuyapongeza majeshi yetu ya Polisi na Magereza kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Wanalitumikia Taifa kwa juhudi kubwa ambayo imetuwezesha sisi kuweza kufanya kazi za kila siku bila ya matatizo makubwa. Nakiri matunda ya kazi zao tunayaona, yamejionesha katika hali nyingi. Kubwa ni hali ya amani na utulivu katika nchi yetu ambayo imetuwezesha kufanya kazi vizuri. Pia udhibiti wa wimbi la ujambazi katika nchi. Ujambazi hakuna katika nchi yetu hivi kama tulivyokuwa tunaathirika huko nyuma, ambapo imepunguza hofu kubwa sana, imepunguza hofu kwa wananchi wetu na kuwawezesha kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hasa kwa Jeshi la Traffic, wamejitahidi sana kutusaidia katika Majiji yetu makuu hususan Dar es Salaam, kuhakikisha kwamba msongamano wa magari nyakati za kwenda na kutoka kazini msongamano huu umekuwa nafuu sana. Tunapoteza muda mwingi sana katika kwenda kazini na kurudi kazini, lakini kwa juhudi zao ambazo tunaziona wazi wazi hivi sasa kazi kubwa ambayo wananchi wanaifanya ni kutekeleza wajibu wao ndani ya sehemu zao za kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza hali kadhalika linafanya kazi kama hiyo ya kutekeleza wajibu wao. Magereza pamoja na upungufu kadhaa ambao wanao lakini wanajitahidi kuhakikisha kwamba wananchi wenzetu wale ambao wamekabidhiwa mikononi mwao wanawalea vizuri na kuwaweka katika hali ya mafunzo mpaka kipindi wanapotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri kwamba kuna upungufu kadhaa ambao naiomba Serikali ijitahidi sana kuhakikisha kwamba upungufu huu unaondolewa. Suala kubwa la uchakavu wa Vituo vya Polisi ni suala ambalo linaathiri Jeshi letu, kuwanyima nafasi ya kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi. Vituo vingi ni chakavu, hakuna ofisi za kufanyia kazi vizuri na hata zile ambazo zipo, pamoja na udogo wake, lakini Polisi wanafikia hata kunyeshewa na mvua katika ofisi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri alenge juhudi zake kuhakikisha kwamba vituo hivi vinakarabatiwa kwa haraka iwezekanavyo na pia kuweza kujenga vituo vingi zaidi. Nikitoa mfano wa kule kwetu Bagamoyo, Kituo kile tumekikarabati kwa harambee, kilikuwa kinavuja sana wakati wa mvua hata Ofisi ya OCD inabidi asogeze meza huku na kule wakati wa mvua; na hivi sasa baada ya harambee hizi ndipo kinaweza kufanya kazi vizuri. Najua hali kama hiyo inawaathiri wananchi wengi na Askari wengi katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, naomba Serikali yetu Tukufu iweze kuliangalia jambo hili na kuondoa kadhia hii nzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika miundombinu hii ya Vituo vyetu vya Polisi ni suala kubwa la uhaba na uchakavu wa nyumba za Polisi. Hili ni jambo zito sana. Polisi hawana makazi mazuri. Nashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri umekuja na mpango wa ujenzi wa nyumba mpya 4100 na kidogo, lakini hizi hazitatosha kwa sababu uhaba tulionao ni mkubwa zaidi. Tunahitaji mpango mkubwa zaidi wa kuhakikisha kwamba Polisi wana mahali pazuri pa kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Bagamoyo tuna Askari 171, lakini chini ya robo ya Askari hawa wana nyumba za kuishi za Polisi. Wale ambao wana nyumba za kuishi za Polisi hizo chache, usiombe kuingia katika nyumba zile, kwa sababu ukiingia utatoka katika hali ya masikitiko na unyonge. Askari wetu hawa ambao wanatuwezesha sisi kuweza kufanya kazi vizuri na kulitumikia Taifa letu hili vizuri, wana haki ya kupata mazingira bora zaidi ili waweze kutumikia vizuri zaidi na sisi tupate ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wao wanapanga uraiani, sasa unapopangisha uraiani unakaa na wananchi hao hao ambao kesho unataka uwadhibiti, anapokudai kodi na kesho huyo huyo anayekupangisha nyumba ndiye amefanya makosa, sijui yeye kama Askari anafanya kitu gani! Haya ni madhila makubwa ambayo Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana Serikali ikajikita vizuri sana katika kuhakikisha kwamba nyumba; jambo kubwa sana, zito, muhimu katika familia yoyote ya baba mama na watoto; Askari wetu wapate nyumba ambazo ni nzuri zenye hadhi ya kazi yao na ambayo itawawezesha wao kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho ningependa kusikia mpango ambao Serikali inauleta kuhusu ukarabati mkubwa zaidi na ujenzi mpya wa nyumba; ujenzi, ametutajia zile nyumba 4,000 lakini je, katika zile zilizopo ukarabati huu ataufanya kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuyataja yale ambayo yanawasibu sana na wakati mwingine kuzorotesha uwezo wa Polisi kufanya kazi. Uhaba mkubwa wa mafuta na vipuri kwa Jeshi la Polisi ni jambo ambalo halina kificho. Hawawezi kufanya kazi vizuri kama magari yao hayana mafuta; kwanza magari ni machache halafu mafuta hakuna. Wakati mwingine inabidi kuombeleza; hata safari hii nimewapiga jeki kidogo Polisi katika Jimbo langu kwa kuwapelekea pesa za kununulia mafuta. Sasa haiwezekani ikawa mafuta ni ya harambee wakati ulinzi ni jambo la muhimu sana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yetu Tukufu ihakikishe kwamba jambo hili inalisimamia kwa umakini. Mafungu ya mafuta yawe mazuri, vipuri vipatikane, vitendea kazi kama magari yawe angalau ya kutosha kuwawezesha Polisi wetu wafanye kazi inayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii pia kuzungumzia hayo hayo kama nilivyozungumzia Jeshi letu la Polisi kwa Jeshi la Magereza, nao wako katika hali ngumu. Ofisi mbovu, hawana ofisi nzuri, miundombinu ya Magereza siyo mizuri, kwa maana ya mabweni ni haba, kuna mlundikano mkubwa wa wafungwa na mahabusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa Serikali ikajikita kuhakikisha kwamba inafanya ujenzi mkubwa sana katika miundombinu ya Jeshi letu la Magereza ili nao waweze kufanya kazi vizuri. Pamoja na vitendea kazi lakini pia pamoja na sare. Siyo jambo ambalo linafahamika sana lakini jambo hili limeanza kunyemelea Jeshi letu la Magereza. Hata sare nayo imeanza kuwa pungufu ambayo itawakatisha moyo sana Wanajeshi wetu hawa. Ni muhimu sana Serikali ikajikita kuhakikisha kwamba hili haliwatii unyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri ililenga kufanya Magereza yetu ni Vituo vya Uzalishaji Kilimo, lakini Magereza yetu hayana vitendea kazi vya kilimo. Gereza kubwa kama la Kigongoni lenye zaidi ya ekari 6,000 katika Jimbo la Bagamoyo halina trekta hata moja, halina lori, gari ya Mkuu wa Gereza ni mbovu. Sasa ardhi ile ni nzuri kwa kilimo inayofaa kwa mpunga, safari hii Mkuu wa Kikosi ameweza kulima ekari 50 tu katika ekari 6,000. Kwa hiyo tuweze kufanya kweli…
MHE. DKT. SHUKURU KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda umekwisha, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii ya Waziri wa Nishati na Madini.
Awali ya yote niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anaifanya yeye pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa Wizara kwa juhudi kubwa ambayo wameionyesha kulitumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yangu kwa kusimamia vizuri Mradi huu wa Umeme Vijijini. Mradi huu ni ukombozi wa wananchi na katika vijiji vile ambavyo umeme umefika wananchi wamepata maana nyingine kabisa ya maisha. Wanafurahia maisha yao, wameanzisha miradi ya uzalishaji, wameanzisha biashara, huduma za elimu na za afya zimeboreka, kwa kila namna mradi huu ndiyo ukombozi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti ya wa umeme vijijini mwaka huu kwa asilimia 50. Hii ni hatua kubwa, hatua adhimu na nina imani kwamba Mheshimiwa Waziri akiendelea kusimamia hivi basi ndani ya miaka hii mitano Serikali ya Awamu ya Tano itamudu kufikisha umeme katika vijiji vyote vilivyobaki 10,000 katika nchi yetu na kwa maana hiyo nchi yetu itakuwa katika hali nyingine kabisa ambayo tunasema kwamba tutakuwa tumejipanga kwa ajili ya kufika mwaka 2025 kama nchi inayoelekea uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuombea Waziri na Wizara na Serikali yetu Tukufu ili wamudu kulitekeleza ndani ya miaka mitano kusibaki kijiji ndani ya nchi yetu ambacho hakina umeme. Najua kwamba hilo litaambatana pia na uzalishaji mkubwa zaidi.
Nimuunge mkono Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu ambaye amesisitiza mradi wa Stigler’s Gorge ambao una uwezo mkubwa, tumeuzungumzia kwa muda mrefu, Marehemu Baba wa Taifa aliufikiria katika Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili haikuwezekana pia, ya Tatu, nina imani Awamu hii ya Tano chini ya uongozi wako Waziri mradi huu utawezekana ili ndoto ya kufikisha umeme katika vijiji vyote Tanzania ndani ya miaka mitano hii iwezekane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika REA Awamu ya Pili Jimbo la Bagamoyo lilipata miradi kumi tu, vijiji kumi ndiyo ambavyo vilipata umeme wa REA lakini kinachonisikitisha au kinachotupa tatizo katika Jimbo la Bagamoyo ni kwamba katika miradi hiyo kumi, minne mpaka hivi sasa haijamalizika na mmoja umefutwa. Sasa miradi minne ambayo ilitegemewa ilipofika Juni mwaka jana 2015 iwe imemalizika mpaka hivi sasa haijamalizika, wananchi wana hasira, hawaelewi, hakuna ambacho wanaweza wakasikiliza kutoka kwa Mbunge, wanashindwa kuelewa kwamba wao wanaishi katika nchi gani kama siyo hii hii nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kijiji cha Buma nguzo zimesimamishwa lakini nyaya hazijafungwa. Kwa hivyo kunguru nao wanatembea pale wanafanya ndiyo viotea wanakaa kule, wananiuliza Mbunge, sasa hawa kunguru tutawafanya nini, tuwafuge majumbani kwetu au iweje? Katika kijiji cha Kondo hivi karibuni nguzo zimeenda.
Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa sauti yako ya wiki iliyopita ambayo imefanya kijiji cha Kondo sasa hivi mkandarasi yule ndiyo anajitahidi ameweka juhudi kubwa ya kuweza kufikiza umeme. Lakini kabla ya hapo kila tulilolisema lilikuwa haliwezekani. Kijiji cha Kondo na mradi wenyewe haujaanza mpaka hivi sasa. REA wamejichanganya kwamba Kondo kuna bandari ambayo haijengwi Kondo, bandari inajengwa Pande na inajengwa Mlingotini. kijiji ambacho kimefutwa kwa ajili ya mradi wa bandari ni kijiji cha Pande na wao siyo kwa utashi wao isipokuwa ni mradi wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Kondo Mheshimiwa Waziri naomba utumie juhudi yako yote kuweza kuhakikisha kwamba mkandarasi huyu anaanza kufanyaazi mapema iwezekanavyo. Kijiji cha nne ni Matimbwa ambacho sehemu ya umeme imekamilika lakini kuna nguzo 20 ambazo bado hazijafungwa nyanya. Nguzo hizi bahati mbaya ni eneo hilo ndilo ambalo tuna zahanati mpya ya kijiji cha Matimbo. Wenzetu NGO ya Korea imejitolea kutujengea zahanati nzuri ya kisasa katika kijiji kile cha Matimbwa, wanatushangaa kwamba nguzo ziko pale zimesimama, sehemu nyingine umeme unawaka lakini pale hapawaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba REA ihakikishe kwamba mkandarasi huyu anamsimamiwa vizuri ili kijiji hiki nacho cha Matimbwa mradi wake ukamilike. Pande imefutwa sawa kwa sababu mnatengemea kujenga bandari pale, lakini mradi huu ulishakabidhiwa kwa mkandarasi, imani yangu ni kwamba basi mradi huu ungehamishiwa katika kijiji kingine. Nimezungumza REA bado hatujapata mafanikio, nina imani kwamba kwa juhudi zako Mheshimiwa Waziri bila shaka REA watapata maelekezo ya kuweza kusaidia kuhamisha mradi ule kuupeleka katika kijiji kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimwa Waziri naomba atakaposimama kufanya majumuisho basi ututhibitishie wana Bagamoyo kwamba miradi hii michache itapewa kipaumbele kuweza kumalizwa ndani ya mwaka huu wa 2016. Ni miradi michache tumeipata basi nayo iweze kukamilishwa wananchi waweze kupata huduma hii adhimu ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile hatukufaidika kiasi hicho katika REA Awamu ya Pili, mategemeo yangu sasa baada ya mimi kama Mheshimiwa Mbunge pamoja na Madiwani kuwasilisha REA miradi 29 katika Jimbo hili la Bagamoyo kwa ajili ya REA III, nina imani kwamba safari hii tutaonewa huruma na miradi hii yote 29 ambayo tumeiwasilisha itaweza kuingizwa katika utekelezaji katika Awamu hii ya Tatu ya Umeme Vijijini. Mheshimwa Waziri najua kwamba kwenye REA II kulikuwa na tofauti kubwa sana kati ya Majimbo na Majimbo, Wilaya na Wilaya, bila shaka Wilaya zile ambazo hazikuweza kufaidika sana katika REA II basi safari hii utaziangalia kwa jicho la huruma ili nazo ziweze kupiga hatua nzuri zaidi na kuweza kuwakaribia Wilaya zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na umeme vijijini ni jambo moja, lakini umeme wa uhakika nalo ni jambo muhimu sana. Katika Mji wa Bagamoyo na Kata za jirani kama vile Magomeni na Kiromo kumekuzuka tabia kubwa sana ya ukatikaji wa umeme mara kwa mara. Hukai siku mbili umeme umekatika mara kidogo umeme umekatika. Mheshimiwa Waziri nadhani jambo hili linafanya wananchi nao wanakosa faida zile ambazo walikuwa wakizitegemea wazipate kutokana na uwepo wa umeme, naomba Mheshimiwa Waziri Shirika la TANESCO waliangalie jambo hili kwa umakini, kama ni vipuri, kama ni mitambo ambayo imechakaa iwe transfoma au viunganishi vingine, mitambo hii iweze kushughulikiwa kwa umakini, ukarabati na ukarafati uwe mila na desturi ya Shirika letu la TANESCO ili wananchi waweze kupata huduma bora katika upatikanaji huo wa umeme usiwe unakatika mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie jambo moja la mwisho na hili ni kuhusu nishati ya gesi. Katika Wilaya yetu ya Bagamoyo watafiti wameendelea kufanya kazi kutafuta gesi, wakitarajia kupata gesi katika Jimbo langu Bagamoyo, Kata ya Fukayosi wamefanya kazi sana pale na katika Jimbo la Chalinze Kata ya Vigwaza wamefanya kazi sana pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa fununu kwamba kuna gesi lakini hatujapata taarifa rasmi naomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri. Pia nawapongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Kamati na viongozi mbalimbali na watumishi wa Wizara kwa maandalizi mazuri ya bajeti. Naipongeza Serikali kwa kuwa na mradi huu adhimu wa umeme vijijini. Faida nyingi zimepatikana na uchumi wetu umeboreshwa na mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika REA II, Jimbo la Bagamoyo lilipata miradi 10 tu na miradi hii ilitegemewa kukamilishwa Juni 2015. Ingawa miradi hiyo ni michache lakini utekelezaji wake umesuasua sana na uko nyuma ya ratiba, hadi leo miradi minne (4) kati ya hiyo 10 haijakamilika kama ifuatavyo:-
(i) Kijiji cha Buma, nyaya hazijafungwa katika nguzo;
(ii) Kijiji cha Kongo, hivi karibuni tu ndiyo nyaya zimepelekwa;
(iii) Kijiji cha Kondo, mradi haujaanza;
(iv) Kijiji cha Matimbwa, nguzo 20 hazijafungwa nyaya. Zahanati mpya ya Kijiji ilijengwa kwa ufadhili wa NGO ya Korea ipo katika eneo hili ambalo halijafikiwa na umeme; na
(v) Kijiji cha Pande, mradi umehamishwa kwa sababu wananchi wanapisha ujenzi wa bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri atuthibitishie kuwa miradi hii itapewa kipaumbele kumalizika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu REA III, katika Jimbo la Bagamoyo tumewasilisha miradi 29 tu. Ni matumaini yetu kuwa utekelezaji REA III Bagamoyo utakuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo linaathiri maendeleo ya uchumi na ya kijamii kwa wana Bagamoyo ni kukatika kwa umeme mara nyingi Bagamoyo Mjini na katika Kata za Magomeni na Dunda. Serikali isimamie upatikanaji wa umeme kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ugunduzi wa gesi asilia Bagamoyo na Chalinze, tumeshuhudia utafutaji ukifanywa na fununu za kupatikana gesi Bagamoyo na Chalinze. Tatizo ni kuwa hakuna taarifa za kugundulika gesi katika majimbo tajwa. Waziri atujulishe kama kweli gesi imegunduliwa Bagamoyo na Chalinze.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DKT. SHUKURU KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya
kuchangia katika hoja ya Kamati hizi mbili, Miundombinu na Nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipa pongezi sana Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kuthubutu kutenga fedha jumla ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati
kwa standard gauge. Ni jambo kubwa, jambo la uthubutu na hilo ndilo ambalo limewezesha
wahisani kuweza kuunga mkono juhudi hizo na sasa hivi ujenzi karibu utaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zote duniani ambazo zina mtandao mzuri wa reli, zenye
uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena kubwa na nyingi zimeunganisha usafiri huo wa reli
pamoja na bandari kwa maana ili tunapojenga reli yenye uwezo mkubwa, inayoweza kuhudumia shehena kubwa ya makontena na shehena mchanganyiko maana yake lazima
uwe na bandari kubwa ambayo inaweza kupokea mzigo huo na kuweza kuingiza kwenye reli.
Mwaka 2009 TPA wamefanyastadi na wakaibua mpango wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane mkono na maoni ya Kamati ukurasa wa 41 ambapo
wameitaka Serikali iharakishe ujenzi wa reli hii ya kati, lakini uharakishaji wa ujenzi huu wa reli ya
kati lazima uungane sasa na uharakishaji wa ujenzi wa Bandari kubwa ya Bagamoyo ambayo
itakuwa na uwezo sasa wa kuzalisha shehena hiyo ambayo inahitajika kwa miundombinu
mikubwa hii. Bila kufanya hivyo tutakuwa tumetwanga maji katika kinu. Hatuwezi kupata
mafanikio yale ambayo tulikuwa tunayatarajia kwa uchumi wetu ambao unakua na ambao
tunategemea tufike katika uchumi wa kati mwaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu wa Bandari ni muhimu tuupe kipaumbele na katika
kuupa Kipaumbele maana yake kwanza tumalize kadhia ile ya fidia kwa wale wananchi
ambao wanapisha ujenzi wa Bandari hii. Hivi sasa nisemapo baadhi ya wananchi wachache
bado hawajalipwa fidia zao. Nadhani ni muhimu zaidi wakati tunaamua kujenga Bandari
tuhakikishe kwamba hakuna mwananchi ambae hajalipwa fidia lakini wapo wananchi wale
ambao walipunjwa na Mkuu wa Wilaya au Kamati ya Mkuu wa Wilaya ilibainisha kwamba
wananchi 687 walipunjwa fidia katika mradi huu wa ujenzi wa bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wanahakikiwa. Naiomba Serikali iweze kutenga fedha
mapema ili mara uhakiki utakapomalizika hawa ambao walibainishwa kwamba wamepunjwa,
basi waweze kulipwa fedha zao kwa wakati na waweze kupisha ujenzi wa bandari. (Makofi)
Mhehimiwa Naibu Spika, pamoja na suala hili la fidia lakini kuna suala kubwa zaidi ya
kwamba ujenzi wa Bandari hii kubwa, unamaanisha kwamba tutaondosha katika ramani ya
Tanzania kijiji kinachoitwa Pande.
Mheshimiwa Naibu Spika, kijiji chote cha pande na Vitongoji viwili vya kijiji cha Mlingotini
vitaondoka kabisa katika ramani kwa maana vitamezwa na bandari hii, sasa hivi hao ndiyo
wapo katika mchakato wa kulipwa fidia. Sasa hawa wapewe maeneo ya kuhamia, kaya zaidi
ya 2,200 hawawezi wakaambiwa tu tokeni bila ya kuwa na sehemu ya kwenda. Muda
umeniishia naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja ya Waziri wa Fedha na niungane na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kukupongeza sana kwa kazi nzuri unayoifanya, tunakutakia kila la heri na mafanikio, najua kiti kizito, lakini kimepata mwenyewe, hongera sana na tunakutakia kila la heri.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha kwa hotuba na bajeti nzuri na ni mategemeo yangu kwamba chini ya uongozi wake tutapata utekelezaji unaofanana na hotuba yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukamilisha mradi wa mabasi yaendayo kwa kasi na kuuzindua vizuri na kuwapa wananchi fursa ya kuweza kuuzindua mradi huo kwa siku kadhaa bila ya malipo yoyote. Kwa kweli mradi huu ni mradi mkombozi, utakaowawezesha wananchi wetu kupiga hatua za maendeleo, unawaondoshea adha ya usafiri, lakini mradi huu pia unawapunguzia muda mwingi ambao walikuwa wanaupoteza kwa ajili ya kusafiri na badala yake muda huo sasa watautumia kwa ajili ya kuzalisha mali na bila shaka tutapiga hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo kwa sababu ya uwezo huu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, wakati inaendelea katika kusimamia mradi huu ihakikishe kwamba inashughulikia changamoto zilizobaki ili mradi huu uwe na mafanikio zaidi. Serikali iweze kununua mabasi yale 140 mengine ambayo yanahitajika zaidi katika mradi huu, lakini pia kukamilisha jengo la kuwawezesha watumishi wale waweze kufanya kazi vizuri na mradi uweze kuwa na mafanikio. Mradi ni mzuri na uwekezaji huu ni wa mfano katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia pia katika kuipa pongeze Serikali katika kuthubutu, uthubutu wenyewe ni katika ujenzi wa reli ya kati kwa ngazi ya standard gauge, huu ni uthubutu mkubwa. Gharama ni kubwa sana lakini Serikali imeamua kuwekeza pale karibu trilioni moja katika gharama ya dola bilioni saba ili ionyeshe nia thabiti ya kutaka kujenga Reli ya Kati. Serikali ya Awamu ya Tano katika hili inaandika historia kwa sababu jambo hili litasukuma maendeleo ya nchi yetu kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya kati hivi sasa ina takribani miaka 100 sasa, kwa hiyo vizazi vingi vijavyo vitakuja kuikumbuka Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi huu adhimu wa ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge. Reli hii ya Kati kwa mawazo ya awamu iliyopita ni reli yenye uwezo mkubwa, treni yake ni ya kilometa mbili yenye uwezo wa kuendesha speed 120 kwa treni ya abiria na speed ya kilometa 80 kwa saa kwa treni ya mizigo na wagon ambazo zinabeba makontena mawili mawili, ni kontena moja juu ya lingine, kwa hiyo huu ni uwekezaji mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye dola bilioni saba za uwekezaji ambazo zimetajwa hapa ambazo sawasawa na takribani shilingi bilioni 15, bila shaka tutahitaji wabia wenye nguvu, wenye uwezo ili waweze kushirikiana na Serikali yetu. Ile shilingi trilioni moja ambayo imewekwa pale ya shilingi katika shilingi trilioni 15 haiwezi ikajenga treni hii, kwa hiyo naiomba Serikali yetu iweke mkazo mkubwa kwa kupata wawekezaji wenye nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009, Serikali tatu; Rwanda, Burundi na Tanzania, iliiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kuwakusanya wawekezaji kwa ajili ya treni hii na mkutano ule mkubwa ulifanywa Tunis. Lakini mwaka 2009 mpaka sasa hivi 2016 ni miaka saba baadaye, hatujaweza kuijenga hii reli, kwa hiyo nina imani kwamba Serikali hii itachukua jambo hili kwa uzito zaidi ili ihakikishe wawekezaji waliojitokeza Tunis mwaka 2009 au wengine waweze kufanya kazi hii wakishirikiana na Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kusema kwamba reli kubwa kama hii mwenzake ni bandari kubwa. Kwa maana hiyo ningesema kwamba ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambao tayari imetengwa jumla ya ekari 2000, sasa usemwe kwa herufi kubwa na uanze ujenzi huo ili uendane sambamba na uwekezaji mkubwa wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Bila kufanya hivyo uwekezaji huu wa reli hautakuwa na tija, tuna jukumu sisi la kutoa fursa kwa nchi zisizokuwa na bahari ili ziweze kuendesha uchumi wao kwa kutumia bahari hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Rwanda, Burundi, Kongo Mashariki nao wote watategemea sana matumizi ya bandari katika nchi yetu kwa kutumia njia hii ya reli ya standard gauge. Sasa nikisema kwamba ni wakati huu sasa ambapo tufanye juhudi kubwa, Serikali ijipambanue kuhakikisha kwamba ujenzi wa bandari unaanza mara moja na zile changamoto zote ambazo zipo ambazo zingeweza kuzuia ujenzi wa Bandari hii ya Bagamoyo mapema basi ziweze kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imesaini MoU kwa ajili ya ujenzi wa bandari mwezi Septemba, 2012, lakini ikasaini pia framework agreement kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mwezi Machi, 2013. Baadaye ikasaini implementation agreement ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mwezi Desemba, 2013, na hatimaye nchi tatu; Tanzania, China na Oman zimesaini mkataba wa ujenzi wa bandari hii na kuzindua ama kuweka jiwe la msingi mwezi Oktoba, 2015 na aliyeongoza uzinduzi ule ni Mheshimiwa Rais Mstaafu. Oktoba, 2015 mpaka hivi sasa ni miezi tisa, nchi za Uchina na Oman ni nchi ambazo ziko serious kabisa katika ujenzi wa bandari hii, na wenzetu wana uwezo wa kifedha na uwezo wa kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuitumie fursa hii mapema. Miezi tisa hamna kitu ambacho ardhi hatujaigusa maana yake ni kwamba ujenzi wetu wa bandari unaweza ukaingia katika kitendawili. Muda ndiyo huu lazima tufanye kazi ya uhakika ili kuhakikisha kwamba bandari ya Bagamoyo inajengwa kwa wakati iweze kuungana na reli ya kati ya kiwango cha standard gauge kuhakikisha kwamba reli pamoja na bandari inatugeuza sisi sasa kuwa Singapore ya Africa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Pande na Mlingotini walipwe fidia zao kwa wakati walipwe ahadi zao walizopewa na Serikali za makazi mapya pamoja na kujengewa nyumba zao, bila ya kufanya hivyo tutashindwa kuanza kujenga bandari hii kwa wakati. Wananchi …
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda umeisha naunga mkono hoja na nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja ya Mawaziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo inayoifanya katika sekta mbalimbali. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi mzuri na kuhakikisha kwamba Taifa letu linasonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchukua fursa hii kuchangia hoja katika suala la elimu. Kwanza katika Sekta ya Elimu niungane na Waheshimiwa Wabunge ambao wameipongeza Serikali kwa kutekeleza mpango wa elimu bila malipo. Huu ni uthubutu mkubwa ambao umehitaji ujasiri kuweza kuutekeleza. Ni mpango ambao umewahusisha wananchi wetu wengi. Watoto wa kiume na wa kike wa Taifa letu hili jumla yao wanazidi milioni 10; milioni kama tisa katika shule za msingi na milioni mbili katika shule za sekondari, wote wakisoma bila ya malipo. Jambo hili limewafanya wanafunzi wa tabaka mbalimbali kuweza kushiriki katika elimu, lakini ni jambo ambalo limewapa imani na uhuru wananchi wetu wasio na uwezo wa kuwapeleka watoto wao katika shule na kuwafanya watoto wao waendelee na masomo yao ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo ni la ukombozi, elimu ni msingi wa maendeleo ya Taifa letu. Hatuwezi kufika mwaka 2025 kama Taifa la uchumi wa kati bila wananchi wetu kuwa wameelimika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia hii thabiti ya Serikali na juhudi hii ya Serikali katika kuelimisha Taifa hili, tunaiona pia katika bajeti. Inatenga bajeti nzuri kwa Sekta ya Elimu ambayo inaendana na mahitaji katika shule zetu. Hata hivyo, tunajua kwamba changamoto katika shule zetu za msingi na sekondari ni kubwa mno, kwa hivyo bajeti hii ambayo tunaijadili hivi sasa tunaihitaji mno iweze kufika katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ni katika wasilisho la bajeti ndani ya Halmashauri zetu. Katika Halmashauri ya Bagamoyo hili limekuwa changamoto moja kubwa sana na ili tufanikiwe katika elimu tafsiri ya bajeti lazima itekelezwe katika utekelezaji wa bajeti yenyewe ndani ya Halmashauri. Kwa mfano Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 imetengewa pesa maalum kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu, jumla ya Shilingi milioni 200 lakini hivi sasa tunaingia quarter ya nne bado hatujapokea .
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuna fedha za MMES kwa ajili ujenzi wa nyumba za Walimu na kwa ajili ya usambazaji wa umeme katika shule za sekondari, jumla ni Sh. 466,000,000,000. Pesa hizo hivi tunavyoongea quarter ya nne bado hela hizi hazijaingia katika Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile fedha za LGCD, jumla Sh. 147,000,000 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule. Fedha hizi Sh. 147,000,000 mpaka tunamaliza quarter ya tatu tumepata asilimia 49. Kwa ujumla bajeti ya miradi ya elimu kwa mwaka huu wa fedha kwa
Halmashauri ya Bagamoyo jumla ya Sh. 814,000,000 tumepokea Sh. 72,000,000 ambayo ni chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa bila Serikali kusimamia utekelezaji wa bajeti katika Halmashauri zetu kwenye sekta ya elimu hatutoweza kufanikiwa katika elimu. Tutaizungumzia elimu na tutawapa matumaini wananchi wetu lakini mwisho wa siku pesa haikutoka hakuna kitu tutaweza kumudu. Sasa hivi tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 291 katika Halmashauri yetu, ni fedha nyingi sana, lakini kama
tungeweza kupata pesa hizi za mwaka huu wa fedha maana yake hatua kwa hatua tungeweza kuanza kupunguza shida hii ya vyumba vya madarasa na miundombinu mingine muhimu ya kuwezesha elimu bora iweze kupatikana kwa watoto wa kike na kiume wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yetu tutakapoingia katika bajeti hii ya mwaka 2017/2018, ihakikishe kwamba tunapomaliza mwezi wa Sita bajeti hii utekelezaji wake uwe kwa wakati na ukamilifu kufuatana na mafungu yale ambayo tumeyapanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuzungumzia kuhusu huduma ya afya. Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ni hospitali ya zamani sana, tangu tumepata uhuru tulikuwa na hospitali hii. Miundombinu yake ni chakavu, tuna upungufu mwingi; tunahitaji wodi za kulala wanaume, wodi za kulala wanawake, chumba cha kujifungulia na vifaa vya tiba, tuna upungufu pia mkubwa wa dawa katika hospitali ya Bagamoyo. Hata hivyo, hospitali hii inatoa huduma kwa wananchi wengi, Halmashauri ya Wilaya nzima ya Bagamoyo inaitegemea hospitali hii. Kwa maana kila mtu anapotoka kwenye zahanati, kata mbalimbali na vijiji mbalimbali tegemeo lake ni hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri yetu ya Bagamoyo haina uwezo wa kuijenga upya au kuikarabati au kuijengea miundombinu inayohitajika katika hospitali ili iweze kutoa huduma inayofanana na mahitaji ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Naisihi Serikali, katika bajeti hii ihakikishe kwamba inatupa uwezo Halmashauri ya Bagamoyo ili tuweze kuipandisha kufikia ngazi au huduma ambao inafanana na mahitaji ya wananchi wa Wilaya hii ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya miundombinu na upatikanaji wa madawa ipo pia katika zahanati zetu. Naishukuru Serikali kwa hatua ambazo imeweza kuzichukua katika mpango wa RBF, lakini naomba iongeze juhudi katika suala hili la afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, awali nampongeza Waziri kwa hotuba nzuri ya Bajeti yenye mwelekeo wa kuipeleka nchi yetu katika ngazi nyingine. Nawapongeza pia Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watumishi wote wa Wizara kwa kujituma, hali inayopelekea utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuendelea na mkakati wa ujenzi wa Bandari ya Mbegani Bagamoyo kama inavyooneshwa katika hotuba ya Waziri ukurasa 90. Jambo ambalo naliomba kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo ni kuwa, Serikali ijitahidi kumaliza malipo ya fidia kwa wanaopisha Mradi wa Bandari, pia kuwalipa fidia sahihi wale ambao wamegundulika kupunjwa fidia zao. Hiki ni kilio kikubwa kwa wananchi wanaopisha ujenzi wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kaya zipatazo 2,000 katika Kijiji cha Pande na Mlingotini zitahamishwa kupisha mradi wa Bandari. Kijiji chote cha Pande katika Kata ya Zinga kinafutwa kwenye ramani ya nchi pamoja na sehemu ya Kijiji cha Mlingotini. Kaya hizi kupitia wafidiwa waliahidiwa eneo la kuhamia katika shamba la Kidogoni Bagamoyo ambalo lilitengwa na Mamlaka ya EPZA tangu 2008.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makao hayo mapya ndiko kungehamishiwa miundombinu yao ya jamii ikiwemo Shule ya Msingi Pande, Zahanati ya Pande, Ofisi ya Kijiji Pande, Misikiti na Kanisa. Naomba Waziri aharakishe upatikanaji wa eneo la makazi mapya ya wananchi hawa wanaopisha mradi na pia Serikali iwajengee katika makazi mapya miundombinu yao ya huduma za jamii zikiwemo shule, zahanati na kadhalika ambavyo vitavunjwa kupisha mradi. Ni zoezi gumu kaya 2,000 kujitafutia zenyewe mahali pa kuishi. Kwa vile ilikuwa ni ahadi ya Serikali, naomba Mheshimiwa Waziri alisimamie jambo hili muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaofidiwa kwa ajili ya bandari jumla yao ni 2,211. Ukitoa taasisi na wananchi wasioishi Kijiji cha Pande na Mlingotini, kaya zinazohamishwa ni karibu 2,000. Kijiji kizima cha pande kinavunjwa na sehemu ya kijiji cha Mlingotini. Hizi ni kaya nyingi. Mwaka 2013 wananchi hawa waliahidiwa eneo la makazi mpya lililotengwa na EPZA, shamba la Kidagoni. Ila kwa sasa hakuna dalili ya utekelezaji wa ahadi hii na wananchi wamepatwa na wasiwasi mkubwa! Naomba Mheshimiwa Waziri atuambie: Je, kaya hizi 2,000 zinazopisha mradi, zitapatiwa eneo la makazi mapya? Lini? Kwa Bajeti ipi? Naomba Mheshimiwa Waziri atupe jibu lenye matumaini ili kaya hizi zisije kuishi kuwa ombaomba mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya fidia ya shilingi bilioni 57,670/= imelipwa shilingi bilioni 45. Balance ya fidia ya wanaopisha bandari haionekani katika vitabu vya bajeti. Je, fidia hii italipwa? Pia kuna wananchi 687 waliothibitika kupunjwa fidia zao na uhakiki umefanywa na Mthamini Mkuu. Wananchi hao wanategemea malipo halali ya fidia zao, lakini fedha hizo sizioni. Mheshimiwa Waziri atueleze kama wananchi hao watalipwa mapunjo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Bandari Bagamoyo ni mradi mkubwa na wenye manufaa makubwa kwa nchi yetu. Bandari hii ndiyo itakayoipa maana reli ya standard gauge inayojengwa. Hesabu za kiuchumi za reli mpya zitakuwa tofauti sana, reli hiyo ikiunganishwa na Bandari ya Bagamoyo. Naiomba Serikali yangu itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Bagamoyo badala ya kuwaachia wawekezaji peke yao. Katika mradi mkubwa kama huu, Serikali iwekeze fedha zake ili iweze kuwa mshiriki kikamilifu katika mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kazi nzuri ya ujenzi wa miundombinu ya maendeleo ya nchi yetu. Katika ukurasa wa 90 wa hotuba ya Waziri ametaja maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Hili ni jambo zuri sana, bandari kubwa yenye uwezo wa kuhudumia shehena nyingi kwa nchi yetu na nchi jirani, ni nyenzo kubwa ya maendeleo ya uchumi wa nchi ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu, kauli hii ya ujenzi wa bandari haina bajeti. Maandalizi haya ya ujenzi wa bandari yatafanywa vipi? Waziri atueleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri yenye mwelekeo wa kuboresha afya ya Watanzania. Pia nawapongeza Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara kwa kujituma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado utoaji huduma ya afya katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ni changamoto kubwa. Hospitali hii ni ya zamani sana tangu uhuru, miundombinu ya hospitali ni chakavu sana na haitoshi. Hospitali inahitaji wodi za wanawake, wodi za wanaume, chumba cha kujifungulia, wodi ya wazazi, OPD na miundombinu mingine. OPD kwa mfano, ni chakavu sana, inahitaji ujenzi mpya. Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo haina uwezo wa kugharamia ujenzi na ukarabati mkubwa unaohitajika. Namwomba Mheshimiwa Waziri aiwezeshe Halmashauri kwa bajeti maalum ili kuiboresha hospitali hii iweze kutoa huduma bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha upungufu wa miundombinu, hospitali ya Wilaya pia ina upungufu wa vifaa tiba na madawa. Nashauri Wizara itusimamie katika matatizo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba ya bajeti nzuri na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mkakati wa ujenzi wa viwanda ili Tanzania ifikie hadhi ya nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025. Ni jambo la tija sana kwa uchumi wa nchi yetu na ukombozi kwa suala la ukosefu wa ajira kwa vijana na wananchi wetu. Serikali imezuia eneo la SEZ Bagamoyo jumla hekta 9,080. Mwaka 2008. Serikali ilitathmini eneo lenye ukubwa wa hekta 5,742 katika Vijiji vitano vya Zinga, Kondo, Pande, Mlingotini na Kiromo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafidiwa walioainishwa ni 2,180 na fidia ya wakati huo ilikuwa ni shilingi bilioni 60. Mpaka hii leo hekta 2,399 zimetwaliwa, wafidiwa 1,155 wamelipwa jumla ya shilingi bilioni 26.4. Wananchi 1,025 hawajalipwa mpaka leo; miaka 10 sasa tangu mwaka 2008! Wananchi hawa wanadai jumla ya shilingi bilioni 51 (pamoja na interest).

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa wamesubiri miaka 10 kulipwa fidia na wamepata madhila mengi. Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho atuambie, lini wananchi hawa watalipwa fidia zao? Kwa vile mwekezaji ameainisha eneo atakalotumia kuwa hekta 3,000 tu: Je, hekta zilizobaki zitalipwa na nani? Lini? Kwa bajeti ipi? Mtindo huu wa kumtaka mwekezaji alipe fidia ya ardhi inapunguza vivutio vya uwekezaji katika nchi yetu, Serikali irudishe utaratibu wa Serikali kulipa fidia ili kushawishi wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bandari Bagamoyo ni sehemu ya SEZ ya Bagamoyo. Ila katika mradi kuna wananchi 687 ambao wamepunjwa fidia zao. Sasa wameshahakikiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Serikali iwalipe fidia zao halali wananchi hawa. Mbona katika bajeti hii ya 2017/2018 haina kasma kwa ajili ya malipo ya fidia hii? Mheshimiwa Waziri awape jibu sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu wa ujenzi wa bandari Bagamoyo utahamisha kaya zinazofikia 2,000. Wananchi hawa waliahidiwa makazi mapya katika shamba la Kidogoni - Bagamoyo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda ni shahidi wa jambo hili, yeye alilisimamia alipokuwa DG, EPZA. Nyaraka mbalimbali za EPZA zinaonesha mpango na ahadi hiyo. Kwa vile Mwekezaji yuko tayari kulipa fidia, naiomba Serikali ifanye maongezi na mwekezaji afidie shamba la Kidogoni ili wananchi wahame eneo la bandari haraka.

Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho atueleze ni lini wananchi wanaopisha mradi wa bandari watapewa eneo la makazi yao mapya? Kuhusu mradi wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, Serikali yetu imesaini mikataba ifuatayo: MoU Septemba, 2012; Framework Agreement, Machi 2013; na Implementation Agreement, Desemba, 2013. Kutia saini Fremework Agreement kulishuhudiwa na Rais Mstaafu Mheshimiwa Kikwete na Rais wa China Mheshimiwa Xi Jingping.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni mwaka wa tano. Kwa vile CMPort Holding na mbia wako Oman wana mtaji na uzoefu; na kwa vile CMPort watalipa fidia ya ardhi, naiomba Serikali yangu Tukufu Iharakishe majadiliano na Mwekezaji huyo ili ujenzi wa bandari ya Bagamoyo uanze mapema. Tangu tumeanza majadiliano mwaka 2012, CMPort wamekamilisha mikataba ifuatavyo:-

(i) Sri Lanka, tayari wanaendesha Colombo International Container Terminal (CICT).

(ii) Nigeria, tayari CMPort inaendesha Tin-Can Island Container Teminal.

(iii) Togo, tayari, CMPort inaendesha Lome Port Container Terminal.

(iv) Djibouti, tayari CMPort inaendesha bandari ya Djibouti na Container Terminal.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zinatuacha nyuma! Mheshimiwa Waziri akija kufanya majumuisho atuambie ni lini Serikali itakamilisha Mikataba na CMPort Holding? Ni lini ujenzi wa Bandari, Bagamoyo utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM. Pia nawapongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote kwa utendaji kazi mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa 81 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ametujulisha kuwa mkataba wa Bandari ya Bagamoyo utasainiwa Juni, 2018. Naipongeza sana Serikali kwa hatua hii. Sisi wa Bagamoyo tunahamu sana Waziri atuambie lini ujenzi utaanza? Pia atujulishe lini fidia zilizobaki takribani shilingi bilioni 12 zitalipwa? Pia lini wananchi 687 wanaopisha bandari ambapo wamethibitishwa kupunjwa fidia zao watalipwa? Kukamilisha malipo ya fidia yatasaidia kuliweka eneo la bandari kuwa huru ili likabidhiwe kwa mwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makazi mapya ya wananchi wa vijiji vya Pande na Mlingotini wanaopisha mradi wa bandari, wananchi hawa waliahidiwa na Serikali kupitia EPZA kuwa watapewa makazi mbadala (barua ya EPZA ya tarehe 20.01.2014 ambayo nimekabidhi meza ya Spika) Kijiji kizima cha Pande na sehemu ya kijiji cha Mlingotini vinahamishwa. Kaya zipatazo 460 (wakazi 1,670) zitaathirika. Wananchi hawa wanapoamuliwa kuondoka wanaenda kuishi wapi? Wengi fidia zao hazitowezesha kununua ardhi au kujenga nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali itimize ahadi yake. Ahadi hii ni deni! Ikiwa Serikali itashindwa basi nashauri Serikali imuagize mwekezaji kulipia gharama za makazi mbadala kwa wananchi hawa (resettlement). Hizi ni taratibu za kawaida duniani kwa viwango vya utawala bora. Ni imani yangu mwekezaji atakubali kwa vile hata China na Oman wanawapa wananchi wao makazi mbadala kwa ujenzi wa miradi mikubwa.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Saadani - Pangani – Tanga katika ukurasa 129 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameahidi ujenzi wa barabara tajwa na kwamba kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ujenzi utaanza kwa kilometa 50 Tanga – Pangani. Naomba kumjulisha Mheshimiwa Waziri tuliopigania barabara hii ni pamoja na wananchi wa Bagamoyo na Mbunge wao! Naomba Waziri aweke wakandarasi wawili, mmoja aanze Tanga na mwingine aanze Bagamoyo kilometa 25 kila upande. Hii itaharakisha kazi na Tanga na Bagamoyo. Tulishafanya hivyo kwa miradi ya Manyoni – Tabora, Tunduma – Sumbawanga na kadhalika kipindi hicho mimi nikiwa Waziri. Naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa ahadi ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara za Bagamoyo mjini kilometa tano na atutengee fedha mwaka huu 2018/2019 kuendelea utekelezaji wa ahadi ya Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Nitangulie kwa kuunga mkono hoja na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na namshukuru Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wa wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 81 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri umetupa faraja sana sisi watu wa Bagamoyo, lakini tuseme kwa Taifa zima la Tanzania kwamba sasa majadiliano yanafikia ukomo. Mwezi Juni mwaka huu mkataba utasainiwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari kubwa ya Bagamoyo. Hii ni bandari ya ukombozi kwa dhana (vision) ya China Merchant na Serikali ya Oman kwamba hili ndilo lango kuu la uingiaji katika nchi za Afrika Mashariki, ni ukombozi kwa ajili ya uchumi wetu na 2025 bila shaka tutaweza kufika katika hali nzuri zaidi tukiwa na bandari hii kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani majadiliano yamechukua muda mrefu, sasa ni miaka sita na kwa maana hiyo naiomba Serikali yangu ijitahidi sasa katika utekelezaji wa mradi huu kwa sababu miaka sita ni kipindi kirefu. Kipindi hicho sisi tulikuwa tunafanya majadiliano lakini China Merchant wamejenga bandari Djibouti, Tin Can Island, Nigeria; Abidjan, Ivory Coast; Colombo Sri Lanka kwa hiyo, kipindi hiki tumepitwa na mambo mengi sana. Nadhani sasa niiombe Serikali yangu kufanya haraka sana katika kuhakikisha kwamba utekelezaji unaenda kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili utekelezaji huu sasa, mwekezaji aweze kuanza kazi, wananchi wangu wale 687 ambao hawajalipwa fidia walipwe fidia. Fidia ya jumla ambayo ilikuwa bilioni 57 na ikalipwa 45, ile tofauti nayo sasa ilipwe ili ardhi hii iwe free mwekezaji aweze mara moja kuanza kuweka miundombinu ya bandari katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kumaliza tatizo hilo litakuwa jambo zuri sana, lakini wananchi hawa kilio chao kikubwa zaidi ni wapi wanaenda kuishi. Wananchi hawa ambao wanapisha bandari waliahidiwa na Serikali. Naomba niweke mezani barua hii ya EPZ ambayo iliwaahidi wananchi hawa kupewa sehemu ya kuweza kwenda kujenga makazi yao na eneo lilikuwa limeshatengwa na hivi sasa mpango huo upo kwenye mtihani haieleweki kama watapewa makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni kaya 460, Kijiji kizima cha Pande kinaondoka kwa ajili ya mradi huu; kaya 460, wananchi 1,670, tunapowaambia tu ondokeni nendeni mkaishi mahali popote wataenda kuishi wapi, kuna wazee, wajawazito, walemavu na watoto wadogo; wapi wanaenda shule yao na zahanati ipo pale, hawajui mahali pa kwenda. Wakitaka kwenda Zinga, Zinga ipo kwenye mpango wa EPZ ambao nao wanatakiwa waondoke kuna kaya 2,269, wakisema waende Kondo nayo inaondoka, kuna kaya 418, wakisema waende Mlingotini, nayo inaondoka kuna kaya 694 yaani hawana sehemu ya kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taratibu nzuri za nchi yetu ni kuhakikisha kwamba faida hii ya maendeleo ya Tanzania, basi wananchi hawa wanahama wanaenda mahali ambapo wataanza kuishi vizuri, vinginevyo tutatengeneza ombaomba, watu ambao hawana mahali pa kuishi. Kati yao wengi wamepata fidia ambayo haitawawezesha kununua ardhi wala kujenga nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila mpango wa resettlement, haitawezekana wananchi hawa wakaweza kuishi katika maisha ambayo yatakuwa ya heshima bila kutengeneza ombaomba katika mradi huu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalisisitiza sana, hili wananchi wangu wanalia sana, lisipoweza kutokea maana yake tutakwenda kuwahamisha wananchi pale kwa mitutu ya bunduki na sidhani kama Mheshimiwa Rais wetu jambo hili anapenda kulifanya. Naomba sana Mheshimiwa Waziri alisimamie ili ahakikishe linafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 129 kuna habari njema ya ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Saadan – Pangani mpaka Tanga, hii ni habari njema ni ahadi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya miaka mingi. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuweka hili, lakini… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, natanguliza kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri, pia pongezi kwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji kwa utekelezaji mzuri wa Ilani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Bagamoyo wanaishukuru Serikali kwa kujengewa tenki kubwa la maji Mjini Bagamoyo, huu ni ukombozi wa huduma bora za maji safi na salama kwa wananchi wa Mji wa Bagamoyo na maeneo ya jirani. Kwa vile tenki sasa limekaribia kukamilika je, mradi wa usambazaji wa mabomba lini utaanza? Pia mradi wa usambazaji mabomba ya maji utahusu kata zipi za Jimbo la Bagamoyo? Tunaomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu ya maswali haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa CHALIWASA unahudumia vijiji vya Mwavi, Fukayosi na Makurunge katika Jimbo la Bagamoyo ila huduma ya maji kwa vijiji hivi imekuwa hairidhishi tangu mradi umeanza. Mabomba ya CHALIWASA hayatoi maji. Napendekeza Wizara ibuni mradi wa maji kutoka Mto Ruvu katika eneo la Mtoni ili kuhudumia vijiji vya Kata za Makurunge na Fukayosi kwa upande wa Jimbo la Bagamoyo. Huduma ya maji katika kata hizi ni duni sana. Mheshimiwa Waziri atujulishe mpango wa Serikali juu ya kuwapatia maji wananchi wa Makurunge na Fukayosi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa fursa hii ya kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Nitangulize kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kwa utekelezaji mzuri wa ilani, nampongeza yeye, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na watendaji kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mkakati huu wa ujenzi wa viwanda. Hili jambo ni jambo adhimu, ni jambo zuri ambalo litaweza kutupelekea sisi mwaka 2025 kufikia hadhi ya nchi ya uchumi wa kati na hili ni jambo la ukombozi pia kwa vijana wetu wa kike na kiume wa Tanzania kwa sababu katika matatizo makubwa ambayo vijana wanayapata ni tatizo la ajira, hili ni tatizo namba moja. Kila kijana awe wa chuo, awe wa shule ya msingi, awe wa sekondari na kadhalika shida yake kubwa ni ajira na viwanda ni ajira kwa hivyo tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa mkakati huu wa ujenzi wa viwanda katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga vizuri na kutenga maeneo ya EPZ na SEZ na maeneo haya ni maeneo muhimu sana yanatoa fursa moja nzuri sana, yanatoa fursa ya kujenga viwanda katika mpangilio mzuri na katika hali ambayo mazingira yanalindwa vizuri kwa maana unaweza mkaamua kwamba hapa ni viwanda vya madawa, hapa vya nguo, kule vya chuma na kule vya chaki bila muingiliano usiokuwa na mpangilio kwamba mtu anaamua huyu anaweka hapa cha tofauli na mwingine anakuja hapo hapo anaweka cha battery, mwingine anakuja hapo hapo anaweka kiwanda cha alizeti, kwa hiyo inakuwa shaghala baghala hakuna mpangilio mzuri. Naiomba Serikali yetu iweke mkazi mkubwa iweze kuhakikisha kwamba maeneo maeneo haya ya EPZ na SEZ yanafanyiwa kazi kwa umuhimu na kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1979 China iliamua kwamba itenge eneo la mfano la viwanda ikachangua SEZ ilikuwa na watu 30,000 tu pale sasa hivi ina watu zaidi ya milioni 11 na viwanda ambavyo vina mpangilio mzuri na vinatoa tija kubwa sana na huo ndiyo mfano ambao inabidi twende nao na kwa haraka. Tumechukua muda mrefu sana, tumezungumza sana lakini vitendo vimekuwa nyuma, kwa hivyo sasa ni wakati ambao Mheshimiwa Rais ameshaweka nia yake lazima tufanye sasa huu ndiyo wakati sasa wa kuweza kutekeleza jambo hili kimakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Bagamoyo Serikali imetenga eneo la EPZ, imetenga kwa awamu mbili, awamu ya kwanza jumla ya hekta 5,742 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na mpaka hivi sasa tayari imeshalipia hekta 2,399 isipokuwa kuna wananchi 1,025 ambao mpaka hivi sasa hawajalipwa fidia zao katika maeneo hayo, kwa maana ni miaka 10 sasa tangu eneo hili limetengwa na wananchi wakatathminiwa lakini hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ninaposema kwamba tufanye uharaka, basi uharaka unaanzia kupata ardhi ambayo iko free, haina tatizo na mwananchi yoyote kwamba walipwe hawa mapema iwezekanavyo ili eneo hili sasa wawekezaji waanze kulitumia kwa ajili ya kujenga viwanda ambavyo viko katika mpangilio mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, juhudi kubwa najua anaifanya lakini kwa sisi kule Bagamoyo nguvu zake tutaziona tu kwamba zimekuwa za kutosha kama pale ambapo tutakuta kwamba fidia hizi zimelipwa kwa haraka ili eneo hili liweze kuwa free na viwanda vianze kujengwa bila hivyo ujenzi wa viwanda unakuwa mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na stahiki ya fidia hii na hasa kwa sababu najua kwamba sasa hivi mwekezaji ana jukumu la kulipa fidia na kwa hiyo wawekezaji hawa wapo tayari kulipa fidia, basi niiombe Serikali ifanye haraka sana kuweza kuwapa ruhusa au kuwasukuma ili waweze kulipa fidia zao mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la EPZ, eneo la Awamu ya Pili la EPZ jumla yake ni hekta 3,338 hili eneo hili linajumuisha maeneo yenye makazi makubwa ya wananchi na limeingia kwenye EPZ bila ya wananchi kuridhia kwamba liingie kwenye EPZ. Linajumuisha Kijiji cha Zinga, Kijiji cha Mlingotini, Kijiji cha Pande na Kijiji cha Kiromo na Kijiji cha Kondo. Vijiji hivi ni vya zamanai na vimejengwa, vina wananchi wengi sana wamejenga kwa miaka mingi wako mle tayari wameshatoa eneo la zaidi ya hekta 5,000 kwa ajili ya EPZ. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaomba chonde chonde tafadhali Mheshimiwa Waziri wananchi hawa waruhusiwe kuishi katika maeneo yao haya kwa amani na usalama na hasa kwa kuzingatia kwamba wameshatoa maeneo ya kutosha kwa ajili ya EPZ eneo ambalo ni mji mzima kabisa tunaweza tukapata SEZ nyingine katika Jimbo la Bagamoyo kwa kuchukua tu eneo lile ambalo tayari limeshakubaliwa katika awamu ya kwanza. Naomba kwa heshima na taadhima Serikali ikubali kuwaaachia wananchi hawa jumla ya kaya 3,381 kwa sensa ya mwaka 2012 ama wananchi 12,797 hawa wataathirika maeneo yao ambayo tayari yameshajengwa, ni vijiji vinavyojulikana kuingizwa kwenye EPZ na kuambiwa kwamba waweze kuondoka kwa ajili ya kujenga viwanda.

Mheshimiwa Waziri utakuwa umefanya jambo zuri sana na la muhimu sana kwa wananchi hawa kama utaweza kusimamia kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanaweza kuendelea na maisha yao kwa amani na usalama katika maeneo haya bila kubughudhiwa tena kuweza kuhama kupelekwa maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la SEZ Bagamoyo kuna eneo la ujenzi wa bandari ambalo waziri anahusika moja kwa moja na analisimamia kwa uzuri na alifuatilia, ameshafanya safari mpaka China kwa ajili ya kufuatilia ujenzi wa bandari hii, lakini wananchi hawa wanaopisha ujenzi wa bandari, jumla ya kaya 460 wao wananchi hawa mpaka hivi sasa hawana eneo mbadala la kwenda kuishi na kwa bahati Serikali iliwahi kuahidi kwa maandishi kwamba watapewa eneo mbadala la kwenda kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu tukufu, namuomba Mheshimiwa Waziri chonde chonde ahakikishe wananchi hawa wa Kijiji cha Pande na sehemu ya Kijiji cha Mlingotini ambao wanapisha ujenzi wa bandari wapatiwe eneo lile la makazi mbadala ili waende wakaanze maisha mapya katika eneo hilo ama sivyo watakuwa ni watu ombaomba tu ambao tutakutana nao miaka inayofuata hawana mahali pa kuishi, wako hovyo, wanamuangalia Mbunge wanamuona hafai, hana maana kwa maana kwamba wao walikuwa wamekaa mahali pazuri, wanapopapenda lakini sasa leo imekuja bandari imewafanya wawe watu ombaomba, watu masikini wa kutupa. Naiomba Serikali chonde chonde ihakikishe kwamba suala la resettlement kwa wananchi hawa wa Pande na Mlingotini ambao tayari walikuwa wameshaahidiwa na Serikali basi waweze kupatiwa maeneo yao waweze kuanza maisha mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kwa utekelezaji mzuri wa ilani. Nawapongeza pia Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji kwa utendaji mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano kwa utekelezaji wa mkakakti wa ujenzi wa viwanda ili Tanzania ifikie hadhi ya nchi ya uchumi wa kati mwaka 2025. Huu ni ukombozi kwa vijana na wananchi kwa ujumla, vijana shida yao kubwa ni ajira na viwanda ni ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Bagamoyo Serikali imetenga eneo la viwanda kwa awamu mbili; EPZ I hekta 5,722 (= eka 14,355) na EPZ II hekta 4,338; jumla hekta 9,080.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya EPZ I, yamethaminiwa mwaka 2008 na hekta 2,399 zimeshalipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo ni kuwa wananchi 1,025 kati ya 2,180 hawajalipwa fidia zao hadi leo miaka kumi sasa. Namuomba Mheshimiwa Waziri awajulishe wananchi wa Kata za Zinga na Kiromo wanaopisha EPZ ni lini watalipwa fidia zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la EPZ II - hekta 4,338 linajumuisha maeneo yenye makazi ya wananchi katika vijiji vya Zinga, Kondo, Mlingotini na Kiromo. Vijiji hivi vina jumla ya kaya 3,381 (sensa ya zoezi) zenye watu 12,797. Maeneo haya hayajathaminiwa wala watu hawajalipwa fidia. Suala kuu ni kwamba, wananchi hawaridhii kuhamishwa maeneo yao ya makazi hasa kwa kuzingatia kuwa tayari wameshatoa hekta 5,742 kwa ajili ya EPZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu tukufu kuwaachia wananchi maeneo yao ya makazi, wananchi hawa hawana hamu wala hawana nguvu ya kuhama na hawana mahali pa kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kijiji cha Pande wanaopisha bandari mpaka sasa hawana eneo la makazi mbadala. Ni utaratibu wa kawaida duniani kwa wananchi wanaopisha miradi mikubwa ya kitaifa kupatiwa makazi mbadala. Wananchi wa Vijiji vya Pande na Mlingotini waliahidiwa na Serikali makazi mbadala. Naiomba Serikali tukufu iruhusu wananchi hao kupatiwa eneo la makazi mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na utekelezaji mzuri wa Ilani. Nawapongeza pia Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji kwa utendaji mzuri.

Mheshimiwa Spika, idadi kubwa ya wananchi wa Jimbo la Bagamoyo ni wakulima na wanaendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo. Shida kubwa wanayopata wakulima wa Bagamoyo ni wafugaji wavamizi. Wafugaji wavamizi wamevamia karibu katika Kata zote za Jimbo la Bagamoyo, wanachunga ng’ombe mpaka katika mashamba ya wakulima bila kujali. Vyombo vya ulinzi na usalama Wilayani vimeshindwa kudhibiti uvamizi huo na wananchi wanapata shida sana.

Naiomba Serikali yangu tukufu iweke utaratibu wa kudhibiti wafugaji wavamizi. Naishauri Serikali iwaboreshee miundombinu ya ufugaji wafugaji hao katika maeneo wanakotoka.

Mheshimiwa Spika, ufugaji samaki ni eneo ambalo lina uwezo wa kuboresha lishe na ajira kwa Watanzania. Namuomba Mheshimiwa Waziri aweke mkazo na bajeti kubwa ya kutoa elimu ya kufuga samaki nchini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya katika Sekta hii muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu. Nawapongeza pia Katibu Mkuu, viongozi na watumishi wote wa Wizara kwa bajeti nzuri na kwa kuchapa kazi. Mwenyezi Mungu aendelee kuwawezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa maboresho makubwa katika Sekta ya Afya nchi nzima. Hii ni kazi kubwa sana na ni ukombozi kwa wananchi wa Tanzania. Kufungamananisha uchumi na maendeleo ya wananchi kunaonekana katika sekta hii. Sasa naiomba Serikali yangu ilete Muswada Bungeni wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ili wananchi wafaidike na huduma bora za afya nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kulipatia Jimbo langu zaidi ya shilingi bilioni moja kujenga vituo vya afya viwili na kuvipatia vifaa tiba. Vituo hivyo ni Kerege na Matimbwa. Vituo hivi vitachangia sana kuboresha huduma ya afya Bagamoyo. Kituo cha Afya Kerege kimeanza kufanya kazi isipokuwa cha Matimbwa (Yombo) bado hakijaanza kazi. Namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kupata samani, vifaa tiba na watumishi wa ajili ya Kituo cha Afya cha Matimbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji zaidi ya 20 (kata tano) katika barabara ya Bagamoyo Msata (kilometa 64) havina huduma ya kituo cha afya. Namwomba Mheshimiwa Waziri atupangie kituo cha afya katika eneo hilo kubwa toka Bagamoyo mpaka Msata.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE.DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Nianze kwa kuunga mkono hoja. Pili napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara hii ya Fedha kwa bajeti nzuri yenye mwelekeo wa kuipeleka nchi yetu Tanzania katika hadhi ya uchumi wa kati mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa mkakati wa ujenzi wa viwanda ili nchi yetu iweze kujikomboa kutoka kuwa nchi tegemezi kwa karibu kila kitu na kuelekea katika hadhi ya uchumi wa kati nchi yenye uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza mpango wa kutenga maeneo maalum ya uwekezaji EPZ na SEZ. Uwekezaji katika maeneo haya utachochea sana maendeleo ya viwanda katika nchi yetu hususani maendeleo ya viwanda ambayo yana mpangilio mzuri na yanawezesha kulinda mazingira na kusaidia ukuaji wa miji yetu katika hali nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Bagamoyo Serikali imetenga hekta jumla ya 9,080 kwa ajili ya viwanda, eneo maalum la EPZ katika jimbo la Bagamoyo. Awamu mbili zilifanya hivyo, awamu ya kwanza jumla ya hekta 5742 na EPZ awamu ya pili jumla ya hekta 3388. Katika EPZ awamu ya kwanza ilitathiminiwa mwaka 2008, wafidiwa 2,180 kwa thamani ya shilingi bilioni 60, lakini mpaka hii leo mwaka 2018 kwa maana baada ya miaka 10 baadaye, wafidiwa 1,025 bado hawajalipwa fidia yao, jumla ya shilingi bilioni hamsini na moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba, fidia ni mazingira wezeshi ya viwanda, kwa maana unapolipa fidia ardhi ile sasa inakuwa huru ili mwekezaji aweze kuwekeza viwanda. Kabla hujafanya hivyo maana yake mazingira yale si wezeshi tena. Pia inamuwezesha mwananchi wa kawaida kuweza kujenga upya maisha yake, kumudu kukimu familia na kuweza kuhakikisha kwamba anafaidika na eneo lile ambalo ameliacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu Tukufu iwalipe fidia wananchi hawa ili ardhi ile iwe huru, pia wananchi waweze sasa kuendeleza maisha yao vizuri na wawekezaji waweze kuwekeza viwanda. Muda si rafiki, miaka imepita mingi na wananchi wa Tanzania wanakiu ya maendeleo wamechoka na umaskini, sasa tufanye kazi tu kama ambavyo Mheshimiwa Rais anasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya EPZ Bagamoyo ilihusisha maeneo ya makazi ya watu wengi, naiomba Serikali kwamba iondoshe maeneo ya makazi ya watu wengi katika mpango wa EPZ, wananchi hawalikubali hili, hawana mahali pengine pa kwenda. Tuache katika hiyo awamu ya kwanza ya hekta 5,742 iwe sehemu ya EPZ kwa ajili ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua ya kijasiri ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, hili ni jambo kubwa sana. Reli ni kichocheo cha maendeleo ya viwanda na kichocheo cha maendeleo ya uchumi katika nchi yetu. Ila reli hii ya kisasa yenye uwezo mkubwa italipwa na sehena za mizigo kutoka nchi yetu na nchi jirani ambazo zinatuzunguka kama Rwanda, Burundi, DRC-Mashariki, Zambia na Malawi, ni shehena hizi za mizigo ambazo zitalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya abiria ni nyongeza tu na ni faida ambayo itawezesha watani wangu Tabora na Mwanza kuweza kusafiri lakini siyo nauli za abiria hazitoweza kulipa. Kwa maana kwamba bila shenena ya mizigo itakuwa vigumu sana reli hii kubwa kuleta manufaa katika nchi yetu, haitoweza kujilipa. Sasa mwenzie reli yenye uwezo kama huu ni nini? Mwenzie ni bandari, bandari kubwa, yenye uwezo mkubwa wa kuweza kuleta shenena ya mzigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 Mamlaka ya Bandari iliweza kufanya study na ika-establish kwamba itahitaji kujenga bandari Bagamoyo, bandari kubwa ya kisasa, miundombinu mipya ambayo inaendana na Tanzania ya kesho. Sasa Mheshimiwa Waziri ili reli hii iwe na tija maana yake ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ni bora uanze mapema na uanze kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi na mkakati wa ujenzi wa Bandari Bagamoyo, kwa sababu Rais wa China na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete tarehe 24 Machi, 2013 walishuhudia utiaji saini wa implementation agreement kuhusu ujenzi wa Bandari Bagamoyo, leo ni miaka mitano baadaye bado tunazungumza. Katika kipindi hiki cha miaka mitano wabia wetu wa China Merchant wamekamilisha mazungumzo na wamejenga bandari katika maeneo yafuatayo; Djibouti, Abuja, Ivory Coast, Colombo-Sirlanka, wamejenga pia Tin-Can City Nigeria na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa wenzetu hawa wanawezaje kukamilisha maongezi na kuanza kujenga ndani ya miaka mitano hii wakati sisi tunaongea. Wao wana nini na sisi tuna nini? Tuna watalaam wa kutosha wa kuweza kukamilisha maongezi na kuweza kuhakikisha kwamba ujenzi unaanza mapema iwezekanavyo. Wananchi wa Tanzania wana kiu ya maendeleo na ni muhimu tuhakikishie kwamba
tunaondoa umaskini wa wananchi hawa mapema iwezekanavyo. Hatuwezi kuendelea kusubiri kila siku wakati, wakati tuna watu ambao wanaweza kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha atuambie ni lini tunaanza ujenzi wa Bandari Bagamoyo ili bandari hii iweze sasa kuungana na reli mpya ya SGR na barabara zetu kuu za usafirishaji ili kuweza kuchochea maendeleo ya uchumi katika nchi yetu, tunahitaji tuondokane na umaskini. Mwaka 2025 Tanzania kuwa na uchumi wa kati ni miaka sita tu usoni yaani muda hatuna. Muda umekwisha ama sivyo tutafika mwaka 2025 tunajitathmini ni kwamba hakuna ambacho tumeweza kukifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali kubwa kabisa namba moja kwa maendeleo ya nchi yetu ni watu wetu, wakiwemo vijana wetu wa kike na vijana wa kiume. Kuna mahitaji makubwa sana ya mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wetu wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne ambao wanakosa nafasi ya kuendelea katika elimu ijayo. Jambo ambalo linanisikitisha ni kwamba, Serikali imekuwa na mtindo wa kutokupeleka VETA fedha za SDL na hili ni jambo la kisheria. Kwa taarifa nilizonazo takribani shilingi bilioni 65 hadi mwezi Aprili mwaka huu zilikuwa hazijapelekwa katika Wizara ya Elimu kama fedha za SDL kwa ajili ya VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni fedha za malimbikizo karibu miaka mitatu, sasa VETA wanahitaji hizi hela za SDL ili waweze kupanua nafasi za mafunzo kwa ajili ya vijana wetu. Kupanua nafasi za mafunzo kwa kutujengea VETA katika Wilaya zetu, kununua vifaa vya mafunzo na kununua vifaa vingine ambavyo vinawezesha mafunzo mazuri kwa ajili ya watoto wa kitanzania yaweze kutekelezwa. Vijana hawa wawe na skills mikono mwao, waweze kuingia katika soko la ajira wakiwa na skills katika mikono yao, wawe watu ambao wataisaidia nchi hii kufika katika uchumi wa kati mwaka 2025. Naiomba Wizara ya Fedha wahakikishe kwamba hizi pesa zinapelekwa….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekjiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Nitangulize kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri hawa kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais pamoja na kulitumikia Taifa hili kwa juhudi kubwa na kwa nidhamu kubwa. Naomba pia niwapongeze Manaibu Waziri, Mheshimiwa Mwita Waitara, Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kuwasaidia Mawaziri na kumsaidia Rais katika kulitumikia Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na sekta ya afya; naomba kuchukua fursa hii kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano na kuwashukuru sana Mawaziri kwa kutuwezesha sisi Jimbo la Bagamoyo kuweza kupata vituo viwili vya afya. Vituo hivi viwili vya afya kimoja kimejengwa Kata ya Kerege, kingine kimejengwa katika Kata ya Yombo. Vituo hivi vitachangia sana kutoa huduma nzuri ya afya kwa wananchi wetu akinababa na akinamama na watoto katika kata hizi na kwa maana hiyo pia kupunguza mzigo mkubwa ambao ulikuwepo katika hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ambayo ilikuwa inazidiwa kiasi cha kwamba inashindwa kutoa huduma nzuri. Tulitengewa pesa nyingi jumla ya shilingi milioni 910 kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivi vya afya, lakini pia tumetengewa pesa jumla ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya vifaa tiba kwa vituo hivi viwili. Nashukuru sana kwa kazi hii nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, hili jambo ni kubwa sana. Tunapozungumzia kuunganisha au kujumuisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi hapa ndipo ambapo kwa kweli mwananchi anaweza akaona ukuaji wa uchumi wa nchi yake na hili ndiyo jambo kubwa la kumfanyia mwananchi wa Tanzania. Mwananchi mfanyie mambo mawili; mpe elimu na mpe afya bora. Hivi vitu viwili ndivyo vinatengeneza rasilimali kuu ya nchi yetu ambayo ni mwananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna rasilimali zaidi ya rasilimali watu katika hii nchi yetu. Kwa hiyo niishukuru sana Serikali kwa jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile cha afya katika Kata ya Kerege kimeshaanza kazi na kituo cha afya katika Kata ya Yombo kinatarajiwa kuanza kazi baada ya muda mfupi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, katika Kata yetu ya Kerege ambapo kituo kimeanza kazi, lakini bado kina upungufu. Upungufu ni katika theatre haijakamilika na vifaa tiba bado havijakamilika, kwa maana hiyo hata upasuaji bado inabidi tuendelee kuufanya kule katika hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo. Hivyo, tunaomba tusaidiwe ili upungufu huu uweze kuondoka, tuwe na jengo la OPD, theatre ikamilike ili wananchi wetu waweze kupata huduma ile ambayo inatarajiwa katika Kituo cha Afya cha Kerege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Yombo chenyewe bado hakijakamilika kwa maana kinahitaji sasa samani na vifaa tiba ili kituo hiki kiweze kufanya kazi, lakini pia hakijapangiwa watumishi bado. Kwa hivyo, tumefanya kazi nzuri ya kujenga vituo hivi na nina imani kwamba, kwa kazi nzuri ambayo tumeifanya na mwaka jana tulitangazwa kuwa ni Jimbo namna moja kwa ubora wa kituo cha afya tulichokijenga katika awamu ile. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atuunge mkono ili tukamilishe na hiki Kituo cha Afya cha Yombo ili nacho kiweze kuanza kufanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho haya yanapelekea wivu pia kwa sababu afya ni jambo muhimu sana. Katika Jimbo langu la Bagamoyo, barabara hii inayotoka Bagamoyo kwenda Msata njia nzima hii kuna zaidi ya vijiji 20, Kijiji cha Makurunge, Kidomole, Fukayosi, Mwavi, Mkenge, Kiwangwa na vijiji kadhaa ndani ya Jimbo la Chalinze vyote hivi havina huduma yoyote inayofanana na kituo cha afya. Kwa hivyo, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa heshima na taadhima niombe katika bajeti hii inayokuja angalau tupate kituo kimoja cha afya katika barabara hii ya Bagamoyo kwenda Msata ambacho kiweze kuhudumia wananchi wengi katika vijiji vingi katika eneo hili, pamoja na wasafiri kama ambavyo nakumbushwa. Barabara hii imeshaanza kuwa maarufu sana na inatumika na wananchi wengi wa Kanda ya Kaskazini. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuwe na huduma nzuri ya afya katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu TARURA; Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana na hili jambo ni nyeti, ni muhimu sana Serikali ikaliangalia kwa mapana yake. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, barabara za TARURA zina jumla ya kilomita 332 lakini ziko katika hali ngumu sana. Mwaka huu wa fedha hakuna pesa kabisa ambayo imetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya barabara za vijijini kwa maana hiyo hatuwezi kufungua barabara, hatuwezi kuzitengeneza barabara katika hali nzuri zaidi. Kipindi kama hili cha mvua barabara zimefungwa kabisa, vijiji vimefungwa, huduma za jamii kama shule, afya na kadhalika zinakuwa mtihani kupatikana. Tumetoka safari ndefu sana ya miaka mingi iliyopita wakati Wilaya zilikuwa hazijaunganishwa kwa barabara za lami, mikoa haijaunganishwa na barabara za lami, lakini hivi sasa kwa kazi kubwa ambayo zimefanywa na Serikali zilizopita na Serikali ya Awamu ya Tano mikoa yote inafikika kwa barabara za lami na karibu Wilaya zote zinafikika pia. Sasa mkazo tuupeleke kwenye barabara za vijijini huku ambako wananchi wanaishi na huku ambapo wananchi wanafanya kazi nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri Serikali yetu iangalie uwezekano hata wa kubadilisha mgao ule katika Mfuko wa Barabara ambao traditionally tulikuwa tunapeleka asilimia 70 ya TANROADS, asilimia 30 katika Halmashauri na kwa sasa TARURA ili angalau tuifanye 50 kwa 50 ili tuweze kufanyakazi nzuri zaidi ya barabara katika vijiji vyetu. Huko tutakuwa tumemkomboa mwananchi aweze kuzalisha mazao na kufanya kazi zingine zitakazotuletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo la mpango wa kunusuru kaya maskini chini ya TASAF. Mpango huu ni mkombozi sana kwa kaya maskini, ni mpango ambao unaleta tabasamu kwa kaya maskini, yaani hakuna jambo ambalo limenifurahisha katika Jimbo langu kama pale kukutana na mwananchi wa kaya maskini naye anatabasamu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekjiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii kuchangia katika hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Waziri. Nitaenda moja kwa moja katika hoja ya Bandari ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa uwekezaji umeorodheshwa na Serikali katika bajeti ya mwaka huu ambayo inamalizika 2018/2019 ikiwa ni mradi mkuu wa kielelezo ambao Serikali mlitaka kuutekeleza kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii. Mradi huu unajumuisha ujenzi wa bandari, lakini pia unajumuisha ujenzi wa viwanda. Eneo hili maalum la uwekezaji ni kichocheo kikubwa sana cha maendeleo ya nchi yetu, maendeleo ya viwanda na maendeleo ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa yale ambayo umeyasema kwa maana kwamba, umeendana kabisa na mawazo ambayo nilikuwanayo mimi kama Mbunge wa Bagamoyo. Imekuwa faraja sana kupata hao wawekezaji; China na Serikali ya Oman, marafiki zetu kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema. Lazima tutumie fursa hizi za marafiki ambao tumehangaika nao sana kwa miaka mingi ambapo sasa fursa hizi wanatumia watu wengine sisi hatuzitumii, ni muhimu sana tutumie fursa hizi.

Mheshimiwa Spika, China na Oman wamekubali kuwekeza jumla ya dola bilioni 10 ama takribani trilioni 23 za Kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa bandari na ujenzi wa viwanda. Mwanzoni wamekubali kwamba watajenga viwanda vikubwa 190 vya kuanzia. Maana yake kwa ajili ya ujenzi huu, vitatoa fursa za ajira takribani 270,000.

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa imefanyika na viongozi wetu na wataalam katika nchi hii, kwa miaka mingi iliyopita, tumeanza na mwaka 2012 ambapo MOU ilisainiwa, Machi, 2013 Framework Agreement imesainiwa; Desemba, 2013 Implementation Agreement imesainiwa; Oktoba, 2015 Tripartite MOU imesainiwa; na Septemba, 2015 jiwe la msingi la ujenzi wa bandari limewekwa na Rais Mstaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Pande na Mlingotini wamejitolea ardhi yao kwa ajili ya maendeleo haya ya ujenzi wa bandari pamoja na viwanda katika hali ngumu sana, lakini wakasema potelea mbali acha tutoe maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, nasikitika sana kwamba inavyoelekea sasa juhudi hizi zote hazikuzaa matunda. Nimesoma ukurasa wa 99, aya ya 136 ya Hotuba ya Waziri, inaelekea kwamba bandari hii sasa haipo.

Mheshimiwa Spika, China Merchant wakati tunasaini MoU ya 2012 wamesaini pia MoU na nchi ya Djibout kwa ajili ya ujenzi wa bandari. Hivi sasa wameshajenga multipurpose port inayoitwa Doraleh kule Djibout. Bandari hii sasa inafanya kazi. Kama vile haitoshi mwezi Machi mwaka huu wamesaini tena na China Merchant ujenzi wa Special Economic Zone Djibout kwa mtaji wa dola bilioni tatu na nusu, takribani shilingi za Tanzania trilioni nane; kwamba, 2012 wamesaini kama sisi na wameongeza tena sasa hivi wanajenga Special Economic Zone.

Mheshimiwa Spika, kama vile haitoshi, katika kipindi hiki sisi tunaongea tangu 2012, China Merchant weamesaini na kujenga bandari Nigeria, Tin Can Ireland; wamejenga Lome, Togo; wamejenga Abidjan, Ivory Coast, wamejenga Colombo – Sri-Lanka.

Mheshimiwa Spika, kipindi hiki cha miaka hii karibu saba sisi tunafanya maongezi, nchi tano nilizozitaja zimekamilisha maongezi. Djibout imekamilisha maongezi na wamejenga bandari, Nigeria wamekamilisha maongezi na wamejenga bandari, Togo wamekamilisha maongezi, Ivory Coast wamekamilisha maongezi, Sri-Lanka wamekamilisha maongezi na wamejenga bandari isipokuwa Tanzania tumeshindwa kwa muda wote huu kukamilisha maongezi. Tuna tatizo gani? Tuna shida gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wataalam wa nchi hizi tano nilizotolea mfano ni bora zaidi wanaweza wakakamilisha maongezi isipokuwa sisi nchi yetu ya Tanzania haina wataalam wa kuweza kukamilisha maongezi.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani 2025 nchi hii kuwa nchi ya uchumi wa kati ni miaka sita ijayo. Hatuna muda tena hata kidogo wa kusubiri katika jambo hili. Mtaji wenyewe una wakati, kwa sababu sasa hivi China wanatekeleza mradi wao wa Belt and Road Initiative nao uko time bound, tukiuacha huo maana yake watakwenda kuwekeza mahali pengine. Huwezi kupata mtaji mkubwa kama huu unasubiri nchi moja tu ifanye maongezi miaka saba haikamiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, atakapokuja Mheshimiwa Waziri, kama ulivyoweka msisitizo, atuambie kwa kina. Tanzania tuna wataalam, Watanzania ni mahodari, Watanzania hatuna fani ambayo iko nyuma. Haiwezekani nchi hizi zikaweza kukamilisha, bandari zikajengwa, sisi tunaendelea kuzungumza kila siku. China wana usemi wao, maneno matupu ni hatari kwa Taifa. Na sisi tunataka kukumbatia kuzungumza tu na kuzungumza tu na kuzungumza tu kila siku, tutaliangamiza Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Viwanda na Biashara. Nichukue fursa hii kumpongeza sana yeye Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa pongezi sana kwa Serikali kwa mkakati huu wa ujenzi wa viwanda; ni mkakati mzuri, mkakati wenye tija sana na ni mkakati ambao utapelekea nchi yetu kuweza kufika katika hadhi ya nchi ya uchumi wa kati. Mkakati huu wa ujenzi wa viwanda nchini naomba nimpe pongezi sana Mheshimiwa Rais kwa kuusimamia mkakati huu kwa nguvu zake zote. Ni mkakati ambao una tija sana na ni mkakati ambao ni ukombozi kwa vijana wa kike na wakiume Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukombozi mkubwa kwa sababu katika mambo ambayo yanawaathiri vijana sana hivi sasa na tatizo hili linaendelea, ni ajira. Vijana hawana ajira; waliosoma wasiosoma, wenye vyeti vya Chuo Kikuu, nakadhalika, ajira imekuwa mtihani mkubwa. Viwanda vitatuletea ajira. Kwa hiyo, Mheshimiwa suala hili la viwanda lisimamie kwa dhamira nzuri ili ilete ukombozi kwa wananchi wetu na hususan vijana wa kiume na wa kike katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali kwamba katika ujenzi wa viwanda hivi, basi msisitizo uwe katika viwanda ambavyo vinatumia malighafi ya hapa ndani nchini kwetu. Malighafi ya hapa nchini kwetu ndiyo maana miradi kama Mchuchuma, Liganga ni miradi migumu sana kwa sababu inatumia moja kwa moja malighafi ya nchi yetu, lakini viwanda vya saruji, viwanda vya vigae, viwanda vya kuchakata minofu ya samaki, viwanda vya kuchaka muhogo na kadhalika, hivi ni viwanda muhimu sana, kwa sababu kule tunapata faida mara dufu; tunapata ajira viwandani, tunapata pia kazi katika uzalishaji wa zile malighafi ambazo zinaenda kwenye viwanda hivi. Kwa maana hiyo, tunakuza zaidi wigo ule wa ajira kwa vijana wetu wa Kitanzania ambao tunahitaji sana waweze kupata kazi hizo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vinajengwa ardhini. Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikafanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba inatoa maeneo ya kujengea viwanda mapema; na kwa maana hiyo pia kuyalipia fidia kwa wale wananchi ambao wana maeneo hayo. Nalisema hili kwa uchungu sana kwa sababu katika juhudi hii ya kutwaa maeneo, katika Jimbo la Bagamoyo kuna wananchi sasa ni miaka 11. Huu ni mwaka wa 11 wametwaliwa maeneo yao chini ya EPZ I na EPZ II na mpaka leo mwaka wa 11 hawajalipwa fidia hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1971 Mheshimiwa Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwaka aliwaita Waingereza kuja kuwaonesha maendeleo makubwa ambayo tumepiga ndani ya kipindi cha miaka kumi. Miaka kumi ni muda mrefu. Sasa huu ni mwaka wa 11, wengine wamefariki, wengine wamepata vilema, wengine yaani wamekata tamaa. Wananchi hawa ni wananchi masikini kabisa, hawana uwezo mkubwa. Kimfaacho mtu chake, wamekaa mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu, wa 10 na wa 11 hawajapata fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Bagamoyo EPZ imechukua maeneo mara mbili; EPZ I imechukua eneo jumla ya hekta 5,742, halafu tena EPZ II hekta 3,338 kwa maana ya jumla ya hekta 9,080 katika hao wafidiwa ni 2,180, mpaka leo kuna wafidiwa 1,025 ambao bado hawajalipwa, miaka 11 baadaye wafidiwa 25,000. Jumla ya fedha ni shilingi bilioni 51 tu ndizo wanazodaiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shilingi bilioni 51 zimesubiriwa kwa miaka 11. katika bajeti ya shilingi trilioni 32, shilingi bilioni 51 ni tone tu katika bahari; na wananchi hawa ndiyo kila kitu, maana yake wanategemea kila kitu. Wengine akina mama wajane wameachiwa watoto, wajukuu na kadhalika, kupata hela hii ndiyo ukombozi wa kila jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu adhimu, Tukufu iweze kuwalipa fidia wananchi hawa mapema iwezekanavyo, wamesubiri sana. Katika kusubiri kwao maana yake watakapokuwa wamelipwa tu, ardhi hii iko free sasa kuweza kutumika kwa ajili ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo mwaka 2018 katika bajeti nililiongelea, naiomba tena Serikali yangu Tukufu mwaka huu, EPZ II imehusisha maeneo yenye makazi makubwa ya wananchi jumla ya hekta 3,338; Ziha kwa Awadhi, Ziha kwa Mtoro, Mlingotini, Kondo na Kiromo, vijiji vyote hivi vina wakazi wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na tahadhima, naiomba Serikali yangu Tukufu iondoe maeneo haya ya makazi makubwa ya wananchi katika mradi wa EPZ ili wananchi hawa waendelee kuishi kwa amani na utulivu. Wameshatoa zaidi ya hekta 5,700 kwa ajili ya hii EPZ na nadhani inatosha kabisa na hawajalipwa kwa miaka 11, wala hawana mahali pa kwenda na hawana nguvu za kuhamia mahali pengine. Naiomba Serikai yangu adhimu iwaache wananchi waendelee kuishi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE.DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, muda umekuwa mfupi. Nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri. Pia nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mkakati wa ujenzi viwanda ili Tanzania ifikie hadhi ya nchi ya uchumi wa kati 2025. Huu ni mkakati wenye tija kubwa sana kwa nchi yetu. Mkakati wa viwanda ni ukombozi kwa vijana wa Tanzania, tatizo kubwa sana la vijana leo ni ajira, viwanda vitaondosha tatizo hili kubwa kwa vijana. Naiomba Serikali iweke msisitizo katika ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga katika Jimbo la Bagamoyo eneo la viwanda kwa awamu mbili, EPZ I (hekta 5,7420 na EPZ II (hekta 3,338). Jumla ni hekta 9,080. Vijiji vitano (5) vimehusika: Zinga, Kondo, Mlingotini, Pande na Kiromo. Maeneo ya EPZ I yamethaminiwa mwaka 2008 ikiwa na jumla ya wafidiwa 2,180. Cha kusikitisha ni kwamba miaka 11 leo wafidiwa 1,025 hawajalipwa fidia yao. Naiomba Serikali yangu Tukufu iwalipe fidia wananchi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, EPZ II (hekta 3,338) inajumuisha maeneo yenye makazi ya wananchi wengi, zikiwemo Zinga kwa Awadhi, Zinga kwa Mtoro, Kondo, Mlingotini na Kiromo. Vijiji hivi vina jumla ya kaya 3,381 (sensa 2012) zenye watu 12,797. Wananchi hawaridhii kuhamishwa maeneo yao. Naiomba Serikali yangu Tukufu kuwaachia wananchi maeneo yao ya makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Awali kabisa niungane na Waheshimiwa Wabunge walioongea kumpa pongezi sana Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri wameendelea kuifanya katika sekta hii. Pia nampongeza Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Nishati kuendelea kufanya kazi nzuri ya kulijenga Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa Mradi wa Stiegler’s kwa kweli mradi huu ni mradi wa maendeleo na mkombozi sana wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii yetu. Megawatts zile 2,115 zitatuchangia sana katika kuendeleza huduma ya maji, huduma ya afya, huduma za kielimu, viwanda, standard gauge, reli na kadhalika. Kwa kuzingatia lengo ni megawatts 10,000 ifikapo mwaka 2025 ni kwamba Mheshimiwa Waziri ajitahidi mapema hata kabla ya miaka mitatu kwa sababu tunahitaji bado Megawatts nyingi sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru pia kwa niaba ya Mkoa wa Pwani kama sisi wenyeji wa mradi huu kwa kweli tumeupekea kwa mikono miwili na tutajitahidi kwa kila hali kuhakikisha kwamba unafanikiwa na madhara yoyote yanaweza kujitokeza ya kimazingira bila shaka Tanzania tunao watalamu wetu wazuri ambao watajipanga kwa ajili ya kudhibiti madhara yoyote ya kimazingira.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuzungumzia ahadi zile ambazo zinatolewa kwa ajili ya kupeleka umeme vijiji na maeneo yote yanaahidiwa kupelekewa umeme vijjijini ni vizuri sana tukatekeleza ahadi hizo Waswahili wanasema ahadi ni deni. Katika Jimbo la Bagamoyo, Kijiji cha Kondo kilikuwa katika Mradi wa REA awamu ya pili mpaka Juni, 2016, mradi ulipomalizika kutekelezwa. Katika REA, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza mpakaleo hicho kijiji hakimo kabisa na wala hatujui lini kitatekelezwa. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri aliahidi hapa Bungeni kwamba miradi yote ambayo itakuwa haijatekelekezwa katika awamu ya pili, basi itapewa kipaumbele katika awamu ya tatu.

Mheshimiwa Spika, Sasa hili ni jambo ambalo kulitekeleza ni muhimu sana kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri na wananchi wakiwa wamesubiri tangu 2013, awamu ya pili ya REA mpaka leo 2019 wanasubiri, hata Mbunge akizungumza namna gani wanamwona tu kama anapiga maneno hana kitu cha kweli ambacho anaendelea kukisema. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri aendelee na ahadi yake ile ile ya first in first out. Waliokuwa kwenye awamu ya pili wapate na nisisitize katika awamu ya tatu waanze wao kutekelezewa kabla ya wengine.

Mheshimiwa Spika, naomba kushauri kwamba kwa ufanisi wa miradi hii ya umeme vijiji basi REA izingatie mapendekezo ya Wabunge ambayo yanawasilishwa kwa utaratibu ambao umewekwa kwa maana kupitia katika ofisi za TANESCO Wilaya na TANESCO mikoa. Baada ya hapo inapelekwa REA lakini wasifanye vinginvyo. Katika Jimbo vya Bagamoyo vitongoji saba katika Kata ya Dunda vimeorodhesha katika awamu tatu ya REA ambavyo vyenyewe vina umeme, hakuna mahali pa kuweka umeme na havikupendekezwa na TANESCO Wilaya wala havikupendekezwa na TANESCO Mkoa, vimekuja namna gani?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nawaomba wataalam wa REA wawe wanaangalia mapendekezo ya Wabunge na hasa yale ambayo yamepita katika taratibu zilizowekwa na hiyo ndio dira ya kutekeleza miradi hiyo isiwe wanachomekea chochote ambacho wamekipenda hata ambapo umeme upo hakuna shida yoyote wananchi wenyewe wanashangaa. Vile vitongoji ni vya Mjini Bagamoyo, hakuna nyumba ambayho haina umeme, vikawekwa mle. Kwa hiyo haina tija, badala yake tunahangaika kutoa scope mahali pamoja kupeleka sehemu nyingine katika hali nzito sana.

Mheshimiwa Spika, ningependa kumalizi kwa kusema kwamba tunapotekeleza miradi hiii katika vijiji basi msisitizo uwe, Kijiji kile ikiwezekana basi kiwekewe kwa ujumla wake badala ya kuweka vijiji kwa mfano katika Jimbo langu, Kata ya Yombo, Kijiji cha Matimbwa kimewekewa umeme, lakini siyo kijiji chote, vitongoji kadhaa havina umeme, Kongo kadhalika. Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo linafaa liangaliwe kwa umakini.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, awali nawapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara ya Nishati kwa hotuba nzuri na kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa Mradi wa Stiegler’s kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kwetu, huu ni mradi wa ukombozi. Tunahitaji umeme mwingi sana wa megawatts 2,100 za Stiegler’s zitatupaisha katika huduma za maji, afya, elimu, viwanda, reli (SGR) na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa miradi ya REA ahadi zitekelezwe. Kijiji cha Kondo, Kata ya Zinga kilikuwa katika orodha ya REA III, lakini mpaka mwisho wa mradi (Juni, 2016) mradi haukutekelezwa na katika REA IIIA Kondo haimo, lakini Mheshimiwa Waziri aliahidi miradi ambayo haikutekelezwa katika REA II itapewa kipaumbele katika REA III. Naomba Mheshimiwa Waziri aelekeze Mradi wa Kijiji cha Kondo utekelezwe haraka wananchi hao wamesubiri muda mrefu sana, tangu 2013.

Mheshimiwa Spika, kwa ufanisi wa miradi ya REA nashauri REA izingatie mapendekezo ya Wabunge yaliyowasilishwa kwa utaratibu uliowekwa yaani kupitia TANESCO (W) na TANESCO (M). Katika Jimbo la Bagamoyo, vitongoji saba (Kata ya Denda) vyenye umeme viliorodheshwa katika REA IIIA wala havikupendekezwa na Mbunge wala TANESCO (W) wala TANESCO (M). Wataalam wa REA wazingatie mawasiliano ya Wabunge ikiwezekana mapendekezo ya Wabunge ndiyo yafanyiwe kazi ilimradi yamepitia utaratibu uliowekwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.