Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ridhiwani Jakaya Kikwete (40 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia nianze kwa kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Chalinze na Halmashauri ya Chalinze kwa mafuriko makubwa yaliyowapata. Wajue tu kwamba Mbunge wao niko nao pamoja sana. Nitakwenda weekend hii ili kushirikiana nao pale panapoonekana Mbunge natakiwa nifanye kazi yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii ni nzuri na imejikita katika mambo mazuri. Mimi sina wasiwasi sana na Waheshimiwa hawa wawili katika utekelezaji wa majukumu yao. Hata hivyo, yapo maeneo ambayo yanahitaji tuzungumze ili kuweka nguvu lakini pia kuendelea kukumbushana katika mambo ya msingi ambayo nafikiri kwamba wangeweza kuyasimamia basi mambo ya Chalinze na Tanzania yangekwenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na jambo la usimamizi wa maendeleo ya miji na halmashauri zetu. Pamoja na mambo mazuri ambayo yameainishwa lakini jambo la kupanga miji ili iweze kufanana na sura ambayo kila mtu angeitaraji iwepo ni jambo la msingi sana. Kwa mfano, nimeona katika maelezo ya mipango ya kibajeti kwamba ziko Halmashauri ambazo zimeshapanga maendeleo yao na Serikali imepanga kupeleka fedha. Nataka nikumbushe kwamba katika bajeti iliyopita Halmashauri ya Chalinze ilikuwa imetengewa fedha kwa ajili ya kupanga mji wake. Kwa bahati mbaya zile fedha zilipokuja zilitumika katika kipande kidogo sana cha kufanya tathmini ya maeneo ya watu lakini pia uanzishaji wa uchoraji wa ramani ya Mji wa Chalinze. Mpaka leo fedha zile zimeshindwa kukamilika hivyo Mji wa Chalinze bado unahitaji fedha ili tuweze kuupanga vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia nataka niikumbushe Ofisi ya Mheshimiwa Waziri, TAMISEMI kwamba Halmashauri ya Chalinze ni mpya, imeanza mwaka jana. Tunawashukuru kwa mambo mazuri waliyokwishatufanyia na ofisi nzuri tulinayo lakini ipo ahadi ya Serikali ya kujenga Ofisi za Halmashauri ya Chalinze katika Makao Makuu ya Halmashauri hiyo ambayo ni Mji wa Chalinze. Mpaka leo navyozungumza fedha zile zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya matumizi hayo ili tuweze kujenga makao makuu yetu bado hazijapatikana. Kwa hiyo, ningemuomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa kufanya majumuisho au kutoa majibu au tafsiri ya mambo ambayo wameeleza Wabunge hawa basi hili jambo la Chalinze nalo liwe ni moja ya jambo ambalo akiliweka vizuri tutamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwamba upo Mfuko wa Barabara Vijiji. Chalinze kwa sura yake ilivyo ina Mamlaka ya Mji ambayo ni Chalinze na Ubena lakini pia mahitaji yetu makubwa sana au eneo kubwa sana la Halmashauri ya Chalinze bado ni vijiji. Kwa hiyo, napoona katika mpango huu ambao umepangwa kutekelezeka katika bajeti ya mwaka huu zimewekwa shilingi milioni tisa tu kwa ajili ya Mfuko wa Barabara, Wilaya ya Chalinze, binafsi naona fedha hizi ni ndogo sana haziwezi kufanya ile kazi ambayo Serikali hii inataka kuisimamia. Kubwa zaidi lazima wajue kwamba Mbunge mimi ni Mbunge nayependa kutembea, napenda sana kwenda vijijini na huko ili paweze kufikika barabara lazima zikae vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia limezungumzwa jambo la afya, niwashukuru sana kwa mipango yao mizuri ambayo wamekwishaionesha lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa fungu kubwa sana la afya maana tunajua kwamba pasipokuwa na afya mambo hayaendi. Pamoja na hayo liko tatizo kubwa limeibuka Chalinze nafikiri la wiki hii, jambo hili nafikiri nilitolee taarifa kwamba kumetokea tatizo kubwa sana la upungufu wa chanjo ya surua. Wananchi wangu wa Jimbo la Chalinze wamekwenda kwenye vituo vya afya, wamekwenda kwenye maeneo mbalimbali kwenda kutafuta chanjo hizo lakini walipokwenda hapakuwepo na chanjo hiyo. Kwa hiyo, ni vyema Wizara kama Wizara mama TAMISEMI au Wizara ya Afya ikalitolea taarifa jambo hili ili wananchi wa Chalinze wajue kwamba Serikali yao inaendelea kujali na mambo ya afya ni moja ya vipaumbele vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nishukuru sana Serikali ya CCM kwa kutupatia Hospitali ya Wilaya ya Chalinze. Hospitali hii zamani ilikuwa ni kituo cha afya pale Msoga na sasa ndiyo Hospitali yetu ya Wilaya. Kila panapokuja mazuri basi makubwa nayo hujitokeza. Hospitali ile inahitaji mabadiliko makubwa katika miundombinu ile ya kituo kile cha afya. Kwa hiyo, fedha kwa ajili ya upanuzi wa hospitali yetu ya Msoga nayo ni moja ya kitu cha msingi sana kutiliwa maanani. Ninaposimama hapa ningeomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuzungumza basi atuambie katika lile fungu aliloweka katika afya, je, fedha hizo zilizowekwa ni pamoja na upanuzi wa hospitali hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipekee kabisa nimshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla na dada yangu Mheshimiwa Ummy kwa kazi nzuri waliyoifanya pale Tumbi maana ilikuwa ni kilio kikubwa kwa watu wanaosafiri na barabara ile. Likitokea tatizo hata mtu kwa mfano akifariki mortuary hakuna Tumbi, akina mama wakipata matatizo ni shida na ndiyo hospitali tulikuwa tuinategemea kwa ajili ya rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii napozungumza hapa kazi nzuri imekwishafanyika, mortuary ile iko vizuri na wodi nzuri imekwishakamilika. Kwa hiyo, ni mambo mazuri yamefanyika na tunaendelea kuwashukuru sana viongozi wetu hawa tuliowachagua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hilo katika hotuba ya Wizara imezungumzia juu ya mradi wa maji vijijini na fedha ambazo zimekwishatengwa. Napenda tu nitoe taarifa kwamba mradi wa maji wa Chalinze umekuwa ni mradi ambao kila siku hauishi kuharibika katika miundombinu yake. Pia mahitaji ya kufikisha maji katika vijiji vyetu nalo limekuwa ni jambo moja la msingi ambalo siku zote mimi kama Mbunge wa Chama cha Mapinduzi nimekuwa nalisimamia. Naomba sana tunapotenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji vijijini basi Mheshimiwa Waziri ni vyema ukaliangalia hili nalo ili tuweze kuona watu wa Chalinze wanaendelea kupata mambo mazuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika randama yenu ya bajeti kwamba mmepanga kutumia shilingi milioni 10 kwa ajili ya miradi ya maji ya vijiji vya Chalinze, fedha hizi ni ndogo sana. Chalinze ni moja ya Majimbo makubwa sana katika Tanzania yetu na vijiji vingi sana vinahitaji maji hayo. Kwa hiyo, unapotenga fedha shilingi milioni 10 kwangu mimi hizi naziona ni fedha ambazo zitatosha kwa ajili ya uendeshaji tu na siyo mradi mzima tunaoutarajia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo Serikali imeendelea kusaidia kuweka fedha katika miradi kama ya TASAF na MKURABITA, ni jambo la msingi sana. Hata hivyo, niendelee kuwasisitiza kuendelea kukagua na kutathmini kaya zenye uhitaji wa fedha za TASAF lakini pia kupeleka fedha nyingi kwenye mradi wa MKURABITA ili vijiji vyangu sasa viweze kupimwa na hati zile za kimila ziweze kupatikana ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maendeleo ya jamii, wananchi wa Chalinze wameendelea kulilia soko lao. Katika hotuba ya bajeti iliyopita ya Wizara ya Kazi ilizungumzwa hapa kwamba patajengwa soko la kisasa ndani ya Chalinze. Cha ajabu zaidi mpaka leo hii wananchi wangu wanasubiri hawaelewi nini hatima yake. Nakumbuka ilipangwa mipango mizuri hapa pamoja na kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kiserikali kwamba wangeliangalia jambo hili lakini mpaka leo hii bado tunaendelea kusisitiza mahitaji hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Chalinze wanapounguliwa nyumba zao gari la kuzima moto halipo. Ile ni Mamlaka ya Mji na imani yangu ni kwamba mkiliangalia hili kwa vizuri basi tunaweza kuepusha vifo visivyo vya lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono asilimia mia moja hoja za Ofisi zote mbili, lakini msisitizo mkubwa ukiwepo kwamba watupe jicho la karibu sana watu wa Chalinze kwa sababu Halmashauri ni mpya na mahitaji bado yako pale pale. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa uhakika yeye na wenzake Wizarani wamethibitisha kuwa nia inapokuwepo na mengine yote yanawezekana. Hongera kwa mipango mizuri, Chalinze tunakutakia kila la kheri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri ambayo yanaendelea kutokea Chalinze, barabara inayounganisha Mkoa wa Pwani na Morogoro, inayotoka Mbwewe hadi Mziha hadi Turiani hadi Dumila imeachwa haitengenezwi. Na sasa ni takribani miaka nane toka nyumba ziwekewe alama ya “X” na hakuna lolote ambalo limeendelea. Nafikiri kwa tafsiri ya barabara ya TANROADS, barabara hii inatosha vigezo na hivyo, ni muda muafaka kuiangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliahidi kuhusu ujenzi wa kituo kikubwa cha malori na mabasi. Mwananchi mmoja wa Chalinze alisema, kama mko tayari Wizara, yeye yuko tayari kutoa eneo; ninachotambua ni kuwa hili ni jambo la kimkakati na nina imani ninyi wasaidizi wake mlitakiwa kulishughulikia. Je, jambo hili mmefikia wapi? Maana muda unakwenda na sioni hatua zikiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni takribani miaka saba toka ujenzi wa makazi ya Makao Makuu ya Wilaya ya Chalinze yaanze. Nyumba mbili zimejengwa na kwa bahati nzuri aliyefungua nyumba hizo ni Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Rais wa sasa akiwa ni Waziri wa Ardhi; sasa hali imeendelea kubaki kama kipindi kile. Je, Wakala wa Nyumba za Serikali analo eneo la heka 50 kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya watumishi watakaokuja kufanya kazi? Je, ni mkakati gani mlionao kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Makao ya Wilaya ya Chalinze yanajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mvua zinazonyesha maeneo ya Pwani hasa Bagamoyo, yameathirika sana, hususan barabara inayojengwa toka Msata kwenda Makofia, Bagamoyo, ardhi hii imesababisha kufungwa kwa barabara. Mheshimiwa Waziri tuhakikishie kuwa barabara itakapokamilika kesho au siku zijazo, hakutatokea majanga kama yanayotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka utungaji wa Sheria ya Makosa ya Kimtandao wasomi, wanasheria na wanaharakati katika kada mbalimbali wamechambua na kuonyesha mapungufu ya Sheria hiyo. Mfano, ni juu ya ukweli wa data za mteja, Sheria hii Ibara ya 32 hadi 35 zinamlazimisha mtoa huduma kutoa data za mteja wake kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi bila kibali cha mahakama. Hii kwa mujibu wa taratibu za haki, kibali cha kutoa taarifa hutolewa na mahakama, hii ni kinyume na taratibu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 3(a) ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao inampa Waziri mamlaka ya kuamua kipi ni kosa na kipi si kosa. Anapewa mamlaka ya kusimamisha na kusitisha huduma na hata pia kuondoa taarifa juu ya kitendo husika, mfano, kuondoa mijadala ambayo yeye ana maslahi nayo au ambayo anaona inagusa ofisi yake. Katika Sheria za Utoaji Haki, haki za kufanya maamuzi ni kazi ya mahakama na Hakimu ndiye mtamkaji, kumpa Waziri nafasi hii ni kufinya utaratibu wa utoaji haki. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie ana mpango gani juu ya sheria hii kandamizi kwa haki za binadamu, ukiachilia mbali matumizi mabaya yanayoendelea ambayo wewe Mheshimiwa Waziri umepewa nguvu na Ibara ya 39 ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri ambayo mmekwishaifanya katika upangaji mzuri wa mawasiliano, changamoto ya upatikanaji wa mawasiliano imekuwa ni jambo la kawaida hata baadhi ya wananchi kuamini kuwa, wao hawapaswi kuwa na simu. Hapa nawazungumzia wananchi wa Kibindu, Miono, Mkange, Msata, Chalinze na maeneo mbalimbali ya Mji wa Kiwangwa na Kata ya Talawanda. Wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne Mheshimiwa Waziri aliniahidi kuongea na watu wa Halotel/Viettel ili kumaliza taabu ya mahitaji ya mawasiliano kwa wananchi hawa waliopiga kura nyingi kuichagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa imani yao ni kubwa sana watapata suluhu ya tatizo lako. Naomba kuwasilisha.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, na mimi naunga mkono hoja hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Pamoja na kuunga mkono, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha anasimamia vizuri sekta hii ya maliasili na utalii na hata kuleta tija nzuri katika Taifa.

Mheshimiwa Spika, Waziri alipata nafasi ya kutembelea mbuga na hifadhi zetu katika Halmashauri ya Chalinze na Wilaya ya Bagamoyo. Katika ziara hiyo amejionea mengi ikiwemo migogoro baina ya wananchi na hifadhi. Lakini pamoja na maelekezo, hakuna lililofanyika hadi leo. Wananchi wameendelea kupata shida na Serikali Kuu imekuwa kimya.

Mheshimiwa Spika, ni masikitiko yangu kuwa mbuga ya hifadhi au Pori la Hifadhi la Uzigua na Wami Mbiki limekuwa sehemu nzuri kwa ajili ya mapitio ya wanyama. Lakini ujangili umekuwa shida, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali sijajua mna mipango gani kuhusu usimamizi wa WMA hii.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia juu ya uangalizi wa maeneo ya malikale. Pamoja na mipango mizuri, lakini ukweli ni kwamba Mji wa Bagamoyo ambao ndani yake kuna Caravan Serai na Mapango ya Kaole umesahaulika. Mji huu una mambo mengi ya kihistoria na majengo mengi ya kale. Kwa kifupi matarajio yangu ni Serikali kuwa na mkakati juu ya mji na historia wa Bagamoyo. Inakumbukwa katika maeneo mengi kuanzia ujio wa Wareno, Wajerumani, Waarabu na shughuli za utumwa, bandari ya kwanza Tanzania na mengineyo mengi lakini Bagamoyo mmeisahau.

Mheshimiwa Spika, Waziri atakapokuja atusaidie sisi wana wa Bagamoyo kufahamu nini kinafanyika au mpango gani uliopo juu ya Mji wa Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nianze kwa kuipongeza Serikali yangu kwa jinsi ambavyo inaendelea kufanya kazi ya kutatua matatizo ya maji katika maeneo mengi. Pamoja na hilo pia nimewasikiliza wachangiaji wengi na wengi wao nimewasikiliza vizuri sana, naomba tu nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba kinacholalamikiwa kikubwa zaidi kama umewasikiliza wachangiaji wengi ni kitu ambacho kwa lugha ya kingereza tunaweza kusema ni poor project management ambayo mnayo katika Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani miradi ya maji kwa mfano nikizungumzia mradi wa maji wa Chalinze ambao sasa una miaka zaidi ya 15 kila siku tumekuwa tunazungumzia mradi huo wa maji, Mheshimiwa Waziri nina imani kwamba sasa baada ya kumaliza kupitisha bajeti hii unaweza ukaenda ukaliangalia vizuri hili. Nina imani pia kwamba kuna vijana wazuri wa Kitanzania ambao wamesomea project management ambao tukiwapa kazi ya kusimamia project hizi wanaweza wakatufanyia kazi iliyo nzuri zaidi, lakini utaratibu ule wa kwenda kuwapa hela moja kwa moja Wakandarasi kama ambavyo umefanya pale Chalinze, ndiyo ambao umetufikisha hapa.

Mimi nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ambaye ninaamini kabisa kwa experience yako kama Engineer, msomi mzuri na ambaye uko tayari kuhakikisha kwamba maisha ya watu yanatoka katika taabu wanayoipata naomba jambo hili uliangalie vizuri sana. Nasema hivi Mheshimiwa Waziri ni kwa sababu siyo mara ya kwanza kutoa ushauri mzuri wa namna hii.

Mheshimiwa Spika,nimewahi kutoa ushauri wa namna hii miaka mitatu iliyopita, juu ya kujengwa kwa tekeo pale katika chanzo chetu Wami, lakini miaka yote Mheshimiwa Waziri imekuwa ni uamuzi ambao au ushauri ambao hamkuwahi kuufanyia kazi. Faraja yangu leo hii kwenye kitabu hiki katika moja ya jambo kubwa ambalo mnakwenda kulifanya pale Chalinze ni kwenda kutengeneza lile wazo ambalo niliwashauri na kipindi kile nilishangaa kwa nini halikufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia nimesoma vizuri kitabu chako cha hotuba ya bajeti Mheshimiwa Waziri. Uharibifu mkubwa unaofanyika katika vyanzo vyetu ni kweli lakini katika jambo ambalo sikuliona humu ndani ni nafasi ya mifugo yetu tunayokwenda kunywesha katika vyanzo vyetu na ambayo inapelekea kuharibu vyanzo hivyo. Jambo hilo hamjalizungumza humu ndani, lakini nikupe mfano mmoja wa Chalinze hasa kwa ndugu yangu kule Mheshimiwa Murrad hayupo humu ndani leo, kwamba katika eneo kubwa ambalo linasababisha matatizo ni mifugo ya wafugaji inayopelekwa katika chanzo cha Mto Wami ambayo inapelekea kuingiza matope mengi na udongo mwingi katika maji ambayo ikipeleka kule kwenye tekeo letu lililopo linapelekea panajaa matope na hata pia wakati mwingine maji yale tunashindwa kuzalisha kwa wingi kwa sababu ya uchafu huu ambao unaletwa na mifugo hiyo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo pia Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana kwa hatua kubwa ambazo mmekwishazifanya, Serikali mkishirikiana na Wizara ya Mazingira kwa jinsi ambavyo mnaendelea ku-preserve vyanzo vyetu vya maji na kuvifanya vyanzo vyetu viendelee kuwa salama. Ninaamini kama hamtoliangalia hili jambo la mifugo yetu inayofugwa na kunyweshwa kiholela katika vyanzo vyetu, hata yale mazingira mazuri ambayo mnatengeneza itakuwa nayo ni taabu tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo lingine Mheshimiwa Waziri ambalo umelizungumzia kwa ufundi mkubwa zaidi ni usimamizi wa mamlaka za maji. Mheshimiwa Waziri ni ukweli kazi kubwa mnaifanya na maji hayawezi kutoka vizuri kama usimamizi utakuwa poor, lakini nikizungumza kwa mfano wa Mradi wa Maji wa Chalinze bado tumeendelea kuwa na taabu kubwa sana katika usimamizi wa maji yale. Imefika kipindi kwamba hata unapotaka kuuliza maswali yanayohusu maendeleo ya mradi ule kumekuwa na sintofahamu kwamba huyu anaweza kukwambia hili, huyu akakwambia hili, lakini haya yote ni kwa sababu nazungumzia tu lile kwamba kutokuwa na utaratibu mzuri juu ya upashanaji wa habari, lakini pia juu ya usimamizi mzuri wa maji yetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia Mheshimiwa Waziri liko eneo kubwa ambalo nimekuwa na interest nalo sana ni katika miradi ya matokeo ya haraka.

Mheshimiwa Waziri unakumbuka ulipokuja mara ya mwisho wakati nazungumzia juu ya kusuluhisha tatizo la maji Chalinze, tulizungumza juu ya mradi wa maji yatakayotoka Ruvu kwenda Chalinze mpaka maeneo ya Mboga kwenye kiwanda kikubwa kinachozalisha products za matunda. Mheshimiwa Waziri mradi ule kwangu ni moja ya miradi ambayo naiona ni miradi ambayo inatupelekea kupata matokeo mazuri katika muda mfupi. Kitu cha ajabu zaidi katika kitabu chako hiki hakuna sehemu ambayo mradi ule umetajwa, labda sijasoma vizuri lakini kwa kuangalia kwangu katika pages zinazozungumzia miradi ya namna hiyo ya matokeo ya haraka, mradi ule haupo. Mheshimiwa Waziri naomba utakaposimama utujibu kwamba mradi ule umekufa, mmekataa kuuanzisha au ni nini kinachoendelea ili wananchi wa Chalinze wajue kama tunaendelea kunywa maji pamoja na mifugo katika malambo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja hilo, ninakupongeza sana kwa hatua kubwa unazoendelea kuzifanya hasa ile taarifa ya ukamilishaji wa uchambuzi au upembuzi yakinifu katika Mradi wa Maji wa Kidunda. Mheshimiwa Waziri mradi ule ulipofikia sasa hivi wanachohitaji ni pesa na katika kitabu chako hiki ukurasa wa 57 mmeeleza juu ya matarajio yenu ya kutafuta pesa ili mradi uweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika jambo hili naomba tu nikutie moyo na kukupa nguvu zaidi ya kwamba ukamilifu wa mradi ule ndiyo ukombozi wa watu ambao tunategemea sana mradi huu. Bwawa la Kidunda litakapokamilika faida zake kama ulivyozieleza kwenye kitabu, lakini niwaongezee kwa faida ya Watanzania wengine kwamba maji mengi tunayopoteza yanayokwenda baharini tutayapunguza. Leo hii ukienda pale kwa mfano kama ukitoka Msata unakwenda Bagamoyo, unaona katika lile Bonde la Mto Ruvu lilivyojaa maji mengi sana, maji yale mengi Mheshimiwa Waziri tunayapoteza ambapo kama tungeweza kutengeneza mabwawa makubwa kama la Kidunda, tungeweza kuwa na faida kubwa sana ya kupata maji ambayo wakulima wetu wa Bagamoyo pale wanaotegemea bonde lile wangeweza kufaidika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, pia tunategemea kupata nguvu ya umeme ambayo pia najua watu wa Chalinze na maeneo mengine ikiwemo watu wa Morogoro Vijijini tutaweza kufaidika nalo sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikupe moyo na kuendelea kukupa nguvu kwamba jambo hili lisimamie kwa sababu hapa ndiyo unakwenda kuwakomboa Waswahili au Watanzania wanaoishi katika maeneo ya Pwani hususan eneo la Chalinze, Bagamoyo na Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa sana maana leo ni siku ya kushauri tu ni eneo la Jangwani. Wengine tunaishi Dar es Salaam pia, eneo la Jangwani hasa katika Bonde la Jangwani pale ambapo kuna Mradi mkubwa wa Mabasi ya Mwendokasi, matope au mchanga umejaa mpaka umekaribia sasa kufikia level ya chini ya daraja. Ninavyofahamu kwa udogo wake, kwamba mchanga au matope yakijaa maana yake maji yatapita juu ya matope yale na ndiyo jambo ambalo limepelekea leo hii bonde lile panaponyesha mvua hata ya mililita mia moja yanapita juu ya daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mmeandika vizuri katika kitabu chenu kwamba sasa mnataka kutafauta kujenga mabomba makubwa ambayo yatasafirisha maji taka. Bonde la Jangwani sidhani kama linahitaji mabomba makubwa ya kusafirisha maji taka. Bonde la Jangwani linachohitaji ni master plan nzuri ambayo inaweza ikasaidia kutatua tatizo lile moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii ukija na hadithi ya kutengeneza mabomba unachozungumzia ni kutafuta maji yapite wapi, tatizo la Jangwani siyo maji yapite wapi, tatizo la Jangwani kwamba watu wamejenga, wameziba njia, wameharibu miundombinu na wameharibu mazingira. Kinachotakiwa ni kutengeneza master plan mpya ambayo itahakikisha kwamba maji pale yanapita vizuri kufika katika Bahari yetu ya Hindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka minne kama siyo mitano iliyopita alikuja mama yangu Mheshimiwa Profesa Anna Tibaijuka akatupa mpango mkakati juu ya jinsi gani wanataka kutengeneza Bonde la Jangwani ili liweze kuwa sehemu nzuri ya kivutio, lakini pia liweze kutumika kwa ajili ya kupitisha maji, mpango ule sijui ulifikia wapi. Taarifa nilizonazo ni kwamba ulikataliwa lakini pamoja na kukataliwa huko kuna kitu cha muhimu cha kufanya ambacho Mheshimiwa Waziri nina uhakika kabisa unajua na wewe nina hakika umetembea.

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa London wametengeneza mto wao pale ambao unaitwa River Thames ambao unapita katikati ya Jiji la London, umekuwa ni sehemu ya kivutio na sehemu nzuri, leo hii London hawana wasiwasi wa kupata mafuriko, tunashindwa nini kutengeneza

Bonde la Jangwani lile kutoka katika maeneo ya Tabata mpaka kwenye Daraja la Salender ili maji yaende baharini na maji yanayotoka baharini, na maji yanayotoka baharini hata ikiwezekana baadae huko kama nchi itakuwa imepata mambo mazuri zaidi ikiwezekana tutengeneze boats nazo ziweze kupita pale zipeleke watu mpaka huko Tabata na iwe sehemu ya kivutio pia katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la mabwawa, Mheshimiwa Waziri naomba nikukumbushe wakati Mheshimiwa Maghembe, Mbunge kwa sasa akiwa Waziri wa Wizara yako, Serikali ilibuni mradi wa kutengeneza bwawa kubwa la maji katika Kijiji chetu cha Mjenge kule Kibindu, Chalinze. Bwawa lile lilikuwa ni substitute ya mradi wa maji wa Wami – Chalinze, mradi ambao kwa mujibu wa mchoro wake ulikuwa haufiki katika eneo la Kata ya Kibindu. Mheshimiwa Waziri nimejaribu kutazama kitabu chako hiki, katika hotuba ya mwaka jana bwawa hilo limetajwa, lakini mwaka huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja naomba bwawa hili nalo lifanyiwe kazi, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia juu ya hoja iliyowekwa mbele yenu na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kazi kubwa inafanyika lakini kweli kwamba katika mambo yote ya kufanya kazi changamoto hazikosekani, hata sisi wenyewe kule majimboni tunafanya kazi nzuri lakini bado changamoto zimeendelea kuwepo. Mimi naamini kwamba tukipeana muda tukapeana mawazo yaliyo sahihi tutafika katika malengo makubwa tunayoyataka.

Mheshimiwa Waziri katika kitabu chako cha hotuba yako ya juu ya mipango yako mambo ya msingi ambayo mimi nimeyaona na ninataka niyagusie hapa, lakini katika eneo litakuwa ni kuongeza juu ya yale mambo mazuri ambayo mmeyasemea nataka nianze na jambo la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la kilimo nimeona kwamba shughuli kubwa inayofanyika ya kujenga maghala, lakini Mheshimiwa Waziri ni ukweli kabisa kwamba bado sijaona ile nia ya dhati kabisa Serikali yetu kukifanya kilimo chetu kikawa cha kibiashara. Nimeona maeneo mengi mmezungumza lakini mimi nataka nizungumzie hasa katika kilimo cha mpunga.

Mheshimiwa Waziri kama unakumbuka vizuri wakati wa hotuba ya bajeti tulichangia na kueleza kwa wazi kabisa juu ya ambavyo mabonde yetu makubwa Tanzania kwa mfano kama lile la Ruvu pale linavyoweza kuwa chanzo kizuri cha kuzalisha chakula cha kutosha lakini katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri nimeona mmezungumzia sana jambo la eneo la Kilombero kwa maana ya bonde lile la Morogoro, lakini Mheshimiwa Waziri kiukweli kabisa Tanzania inayo mabonde mengi sana ambayo kama yatatumika vizuri kilio cha watu kulia njaa kukosekana kwa chakula kitakwisha kabisa na hata itaweza kufika sehemu kwamba tuna uwezo wa ku-supply chakula kwa nchi za nje na kuuza kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.

Sasa Mheshimiwa Waziri nikuombe utakaposimama utuambie juu ya mpango mkakati mlionao wa kuendelea kutumia mabonde haya kwa ajili ya faida ya Watanzania hasa hasa mimi nazungumzia hapa Bonde la Ruvu ambalo tunalo kwa sisi wenyeji wa Pwani hasa maeneo ya Chalinze na Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo Mheshimiwa Waziri nikupongeze, nimeona katika taarifa nilizozisoma juu ya benki yetu ya kilimo jinsi ambavyo imeweza kuwasaidia AMCOS zinazolima pamba kwa kutoa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kusaidia kuweza kuvuna pamba na kuiweka katika maeneo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe sana kwamba kilimo kipo cha namna nyingi lakini pesa hizi naamini kwamba zipo na mahitaji ni makubwa sana. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri muendelee kuangalia maeneo mengineyo pia, kilimo sio pamba tu peke yake, tunacho kilimo cha korosho, kahawa, alizeti na mazao mengineyo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza hapa kama walivyotangulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia Mheshimiwa Waziri nimtoe wasiwasi ndugu yangu Mbunge wa Sumve amezungumzia juu ya pamba kukosa maeneo na kwamba pamba nyingi inasafirishwa nje. Sasa hivi pale Chalinze tunajenga kiwanda kikubwa sana ambacho kinakuja kutengeneza vitambaa na material zote zinazotokana na pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana aende akawahamasishe wananchi wake wa Sumve na maeneo yote ya wakulima wa pamba kwamba sasa pamba ile itakuwa haifiki Dar es Salaam bandarini isipokuwa itakuwa inaishia Chalinze pale kwa ajili ya kuchakatwa na kutengenezwa material ambazo zinakwenda kuwa sehemu kubwa ya kutatua tatizo kubwa la kupatikana kwa vitambaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, nizungumzie kidogo katika eneo la mifugo. Nimeona kazi kubwa na nzuri sana ambayo inafanywa na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na wizara yake kwa ujumla lakini bado tumekuwa na tatizo kubwa sana la kuchunga au kugeuza nchi nzima kuwa ni sehemu ya machungio. Mheshimiwa Waziri kiukweli kabisa nyama nzuri haiwezi kupatikana kwa ng’ombe kutembea kutoka Sumve huko Mwanza mpaka Chalinze. Ng’ombe mwenye nyama nzuri anapatikana kwa kutunzwa, kulishwa vizuri na matunzo yakawa yenye kutengeneza ubora huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nimeona hapa mmezungumza jinsi ambavyo mnataka kuhakikisha kwamba ng’ombe wetu wanakuwa wana uwezo wa kuzalisha maziwa yenye ubora zaidi. Mheshimiwa Waziri nataka nikukumbushe kama vyombo havitosimamia ile Sheria ya Usafirishaji wa Mifugo kilio hiki na matatizo haya yataendelea katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana wewe na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, namuona ndugu yangu, Mwenyekiti wangu Bwana Ulega anafanya kazi nzuri sana lakini kama hatutoweza kusimamia sheria hizi hatuwezi kupata nyama iliyo bora au maziwa yaliyo bora. Itaishia kila siku ng’ombe ambao unatarajia watoe lita 12 mpaka 14 watakuwa wanatoa lita mbili au lita moja kwa sababu ya kuchoka kwa kutembea umbali mrefu na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo nizungumzie pia jambo la afya, ni kweli kwamba fedha nyingi sana zinapelekwa katika afya. Mimi binafsi nawashukuru sana mmeendelea kutuangalia watu wa Chalinze kwa jicho la huruma zaidi, kituo changu cha afya cha Kibindu sasa kinakamilika na Lugoba kule mambo ni mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia wameeleza waliotangulia juu ya ufinyu wa watoa huduma za afya. Mimi nikuombe sana hili jambo ni jambo sensitive sana, tunaweza tukawa na majengo mazuri sana lakini kama majengo yale hayafanani na huduma zinazotolewa itakuwa ni jambo ambalo kwa kweli mwisho wa siku wananchi hawatotuelewa. Nikuombe sana tuendelee kuliangalia jambo hili na kulipa kipaumbele chake kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nikushauri Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali yangu katika eneo la bima ya afya. Sasa hivi kwa bima kubwa kabisa kwa mfano tunalipa shilingi 1,500,000, hii shilingi 1,500,000 kwa mwananchi wangu anayetoka kule Talawanda kusema kwamba akalipe kwa kweli ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana kama tutaamua kuja na mkakati wa kuwawezesha wananchi kulipa kiwango hiki cha shilingi 1,500,000 ambacho kinatakiwa kulipwa kwa mwaka kikalipwa katika installments za kila mwezi. Kwa maana sasa kwa kila mwezi mwananchi akawa analipa at least shilingi 125,000. Hili jambo wanaliweza na wananchi pia wapo tayari kufanya hivyo. Leo hii unaweza kukuta mama ana tatizo labda ana uvimbe tumboni, anatakiwa alipe shilingi 3,000,000 ili aweze kupata matibabu, lakini mtu huyu kama angeweza kulipa shilingi 1,500,000 maana yake angeweza kupata matibabu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukaja na mkakati mzuri ambao unaweza ukasaidia kupunguza matatizo na machungu kwa wananchi wanyonge ambao tuliwaahidi kwamba tutaendelea kuwaangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo limetokea jana Mheshimiwa Waziri hasa Waziri wa Afya nikupe tu taarifa kwamba Kituo chetu cha Afya cha Msata kimepata nyota nne na kimekuwa cha kwanza Mkoa wa Pwani kwa ubora. Haya ni mambo ambayo yanaendelea kufanyika katika Halmashauri ya Chalinze na sisi tunaendelea kusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee kabisa niwashukuru sana wenzangu ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba mambo haya yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la viwanda kwa kipekee kabisa nimpongeze sana Mkuu wangu wa mkoa Engineer Evarist Ndikilo kwa jinsi ambavyo anaendelea kufanya kazi kubwa ya kusimamia kuhakikisha mapinduzi ya viwanda kwa Chalinze yanakuwa ni kweli lakini kwa Mkoa wa Pwani kwa ujumla wake.

Ninachokuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha muendelee kuhakikisha kwamba yale maeneo tengefu ambayo tumeyatenga mnayapelekea fedha ili zile fidia ambazo zimeahidiwa kulipwa wananchi zilipwe, lakini pia yale maeneo ambayo tumetenga kwa ajili ya viwanda nayo pia mnaendelea kuweka msisitizo na msukumo kuhakikisha kwamba viwanda vile vinakamilika mapema iwezekanavyo na Serikali iweze kufikia malengo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la Hydro- Electric Power Rufiji; Mheshimiwa Waziri nikuhakikishie wananchi wa Chalinze wanasubiri kwa hamu kubwa sana mradi huu wa umeme. Mradi huu wa umeme unakuja kutatua kero ambayo sasa tumeanza kuipata ndani ya Chalinze, umeme hauji vizuri kwa sababu wananchi wanagawana umeme na viwanda. Viwanda vimekuwa vingi, Serikali yetu imesisitiza juu ya viwanda na sisi Chalinze tunatimiza kwa vitendo, lakini kwa kweli adha hii inayoanza leo tunaogopa isijekuwa ngumu halafu baadaye wananchi wakaja kuuliza kwamba sasa viwanda hivi mlivileta ili vitusaidie nini kama sio kuja kutuongezea tabu katika maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru na naunga mkono hoja, ahsante sana.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi napenda kuungana na wazungumzaji wa mwanzo pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu na ninyi nyote kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Siyo yeye peke yake isipokuwa na wasaidizi wake ambao wameanza kwa spidi kubwa sana. Hongereni sana Mawaziri wangu, hongereni sana viongozi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimefurahi kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kwangu mimi nikiisoma hotuba ile nzima, ndani yake naweza kusema ni semina elekezi au ni maelekezo yanayotosha kabisa kwa Mawaziri wangu hawa kuanza kufanya kazi kwa spidi kubwa kama ambavyo wameanza. Kwa sababu ndani yake kwa mfano kwenye kila eneo Mheshimiwa Rais amejitahidi kuchambua na kueleza juu ya tamaa yake ya kuona nchi inakwendaje, lakini pili jinsi gani tamaa ile inaweza ikafikiwa ili malengo yale ya kuwasaidia Watanzania walio wanyonge yaweze kufikiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuongea kidogo katika baadhi ya maeneo ambayo naamini kabisa tunao mchango au kutoa wito kwa Mawaziri wetu ili waweze kufanya kazi nzuri kuweza kumsaidia Mheshimiwa Rais. Kwa mfano, naamini katika eneo la Chalinze na Tanzania ambayo sasa wimbo wetu mkubwa ni maendeleo ya viwanda, viwanda haviwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa umeme wa uhakika. Kazi nzuri inafanywa ya kuhakikisha kwamba umeme wetu katika bwawa la Mwalimu Nyerere unakamilika na mimi binafsi yangu nitumie nafasi hii kuipongeza sana Wizara hasa kwa jinsi ambavyo wanaendelea kusimamia ujenzi wa bwawa lile lakini pia kwa ma-engineer wetu ambao hata juzi tulishuhudia wenyewe wakieleza katika vyombo vya habari kwamba hawana shida yoyote na kwamba malipo yanapatikana ndani ya muda. Kwangu mimi hii ni ishara nzuri lakini ni wito wangu kwa Wizara kuhakikisha kwamba wanasimamia ili ule muda ulioelekezwa wa mradi kukamilika uweze kukamilika mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, kwangu mimi ujenzi wa bwawa hili siyo tu kwamba unaenda kutatua kero nyingi za kimaendeleo za watu, lakini msingi mkubwa ni kwenda kuhakikisha kwamba umeme wa uhakika unapatikana ili ile sera yetu ya viwanda katika Tanzania iweze kufanikiwa. Kwa hiyo, wito wangu narudia tena kwa Waziri husika ajaribu kusimamia vizuri jambo hili ili wale wananchi wetu ambao sasa hivi wameanza kulalamika kupata matatizo ya kukatika umeme mara kwa mara, jambo hilo nalo liweze kuisha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo katika hotuba yake Mheshimiwa Rais alieleza kwa uzuri zaidi jinsi ambavyo anatamani kuona maendeleo ya utalii yanapatikana Tanzania hii. Unakumbuka katika moja ya maeneo ambayo Mheshimiwa Rais aliyagusia ni kutatua migogoro iliyopo baina ya vijiji na hifadhi zetu kwa maana ya kusaidia kuongeza idadi ya watalii kwenye maeneo yetu. Moja ya maeneo hayo ni eneo la Mbiki au Wami Mbiki lakini pia Hifadhi yetu ya Saadani.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kata ya Mkange kule Chalinze wanalalamika sana juu ya migogoro ambayo inayoendelea lakini ahadi ya Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni alieleza kwamba anatamani sana kuona migogoro hii inakwisha na katika kuhakikisha kwamba migogoro inakwisha, moja ya jambo kubwa ambalo alielekeza ni urasimishwaji wa maeneo ya vijiji hivyo ili sasa wananchi waondoke katika maeneo ya migogoro. Kwa hiyo, wito wangu kwa Mheshimiwa Waziri husika, jambo hili aendelee kuliangalia vizuri kwa sababu sisi ambao tunaamini kwamba Rais wetu ana nia njema ya kusaidia wananchi wake tusije tukamuangusha kwa sisi kushindwa kufikia malengo hayo. Mimi kama Mbunge nikiwa na viongozi wenzangu ndani ya halmashauri yetu, tutakupa ushirikiano mkubwa sana Mheshimiwa Waziri ili kuhakikisha kwamba nia ya Rais inafikiwa katika kiwango kikubwa na ikiwezekana kiwango chenye mafanikio makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa nia yake nzuri ya kutengeneza reli ya kisasa ya SGR ambayo inatoka Dar es Salaam inakwenda mpaka Kanda ya Magharibi lakini pili inafika mpaka nchi jirani. Kwangu mimi huu ni ukombozi mkubwa sana, kwanza kwa barabara zetu ambazo kwa kipindi kikubwa sana Mawaziri wamekuwa wanalalamika lakini pia wewe mwenyewe unaweza kuwa shuhuda unapotoka kipande cha Chalinze kwenda Mlandizi kimeharibika sana kwa sababu ya uzito mkubwa wa magari yanayopita pale.

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kwa kufanikiwa kukamilisha SGR hii maana yake mizigo mizito yote itaingia kwenye treni na itakwenda katika maeneo husika na hasa yale maeneo ambayo tumetengeza miradi ya kimkakati hasa ule mradi wa dry port wa pale Kwala na mwingine ule wa Kahama, maana yake ni kwamba tunakwenda kutatua tatizo kubwa ambalo linaendelea kukabili Watanzania wetu. Hivyo basi zile pesa ambazo zinatumika wakati mwingine kutengeneza barabara ambazo zinaharibika ndani ya muda ambapo hazipaswi kuharibika, kwa kweli nalo tutaliondoa tatizo hilo. Kwa hiyo, kwangu mimi ni kumpongeza pia Mheshimiwa Rais na kumuahidi kwamba tuko naye bega kwa bega kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika mapema iwezekanavyo na Watanzania waendelee kupata mafanikio ambayo yeye ameyakusudia.

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Rais alieleza juu ya nia yake nzuri ya kuona jinsi gani tunaweza tukachukua hii idadi kubwa ya mifugo tuliyonayo ambayo inatupa nafasi ya pili kwa idadi ya mifugo Tanzania kuwa ni sehemu ya uchumi kuwawezesha wananchi wetu. Katika eneo letu sisi la Chalinze lakini pia katika maeneo ya Pwani ya Tanzania, wanyama kwa maana ya mifugo, mbuzi na kondoo ni wengi sana.

Mheshimiwa Spika, naamini nia hii ya dhati ya Mheshimiwa Rais ambayo ameeleza kwenye hotuba yake ambapo analenga kuhakikisha miaka mitano itakapomilika zaidi ya machinjio tisa za kisasa zitakuwa zimejengwa, kwa kweli naamini machinjio haya yatakapokamilika tutakuwa tumesaidia sana kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji inayoendelea. Naamini wafugaji wetu wanahitaji kupewa elimu na siyo kugeuzwa maadui katika maeneo yao ili waonekane kwamba ni wakosefu. Pamoja na hilo ni muhimu pia kwa Wizara kuhakikisha kwamba wanawapelekea wafugaji hawa huduma muhimu zinazotakiwa katika maeneo yale. Kwa mfano, ujenzi wa mabwawa makubwa ili waache kusafiri na mifugo kwa umbali mrefu kwenda kutafuta huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, naomba kugusia kwenye eneo la elimu. Asubuhi hapa umeibuka mjadala mkubwa sana juu ya Bodi ya Mikopo na mikopo inayotolewa kwa vijana wetu. Nikupongeze wewe pia kwa kuliona jambo hili lakini kwa kweli sisi kama Wabunge sijui kama wenzangu wanaliona hili lakini vijana wetu wengi wanakosa fursa ya kusoma vizuri kwa sababu ya kukosa mikopo ya Bodi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shida kubwa ambayo mimi naiona binafsi ni kwamba katika maeneo mengi sana, vijana hawa wanapokuwa katika level za chini, sisi Wabunge au kupitia wahisani mbalimbali tumekuwa tunawasaidia kuwasomesha katika shule zilizo nzuri. Kwa mfano, wako vijana ambao wamesoma katika shule hizi ambazo tunasema ni private schools katika level ya form one mpaka form four lakini vijana wale baada ya kufika chuo kikuu either wazazi wale wamekosa uwezo au wale sponsor wamefariki au wale wanaowawezesha nao hawana uwezo huo, kwa hiyo, wale vijana wanajikuta kwamba wananyimwa mikopo kwa sababu ya kukosa vigezo. Wito wangu kwa Wizara iangalie historia ya mwanafunzi huyu. Kigezo kisiwe amesoma wapi, kigezo kisiwe kwamba amewezeshwa na nani, waangalie kama uwezo huo anao ili kuweza kufikia malengo mazuri aliyoyaainisha Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza sana ndugu yangu Bwana Aweso, Waziri wa Maji kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Wana wa Chalinze wanakushukuru na wanaendelea kushukuru katika kazi kubwa unayoendelea kuifanya. Wito wao mmoja tu ni kwamba zile pampu zinazojengwa pale Msoga na Chamakweza hebu hakikisheni kwamba zinakamilika mapema iwezekanavyo ili lile tatizo la maji linalowakabili wananchi wale liweze kuisha na liwe hadithi ambayo imepita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, naunga mkono hotuba zote za Mheshimiwa Rais, napenda kusema kwamba tuko pamoja naye na ajue kabisa kwamba anao vijana ambao wanamtakia mema. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya, lakini pia kwa mwanzo mzuri katika kuongoza nchi yetu katika hii Awamu ya Sita ya uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyotangulia waliomaliza kusema, naomba nitumie nafasii hii kuipongeza sana Saerikali kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wameendelea kuifanya na kazi ambayo imeanzwa na ndugu yangu Dkt. Mwigulu Nchemba na Engineer Masauni kwa kweli inatia imani kubwa sana na kwa hakika naamini tunapokwenda ni kuzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha bajeti hii ambayo kwangu naiita bajeti ya kwanza ya Uongozi huu wa Awamu ya Sita, ningependa nianze kwa kuwapongeza sana, kwa sababu yapo mbapo ambayo yamefanyika au yameelezwa kwenye bajeti ambayo mimi binafsi nataka niwashawishi Wabunge wenzangu, tuunge mkono moja kwa moja asilimia mia moja ili mambo haya yaende yakafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, lipo jambo la kuondoa ushuru katika bidhaa kwa mfano zinazotoka Zanzibar kuja Dar es Salaam. Hili jambo zuri na limekuwa ni kilio cha muda mrefu na kwa kweli sasa kimeenda kupatiwa muarobaini wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wameeleza wenzangu waliotangulia, juu ya posho sasa zinazokwenda kulipwa kwa Maafisa wetu Tawala katika maeneo yetu, kwa maana wale Maafisa Tarafa. Pamoja na hilo pia kwa ajili ya sisi wanamichezo; viwanja vya michezo kuondolewa zile tozo za nyasi bandia, kwa kweli ni jambo zuri sana. Alizungungumza juzi ndugu yangu Mheshimiwa Sanga, kwa maelezo marefu sana na sitaki kurudia huko, lakini kwa kweli ni jambo la kupongezwa na tunaishukuru sana Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nigusie malipo ya wanafayakazi kwa maana ya PAYE, kushusha kutoka 9% mpaka sasa 8%, hili ni jambo kubwa na ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutumia nafasi hii kuiomba Serikali yangu kwa sababu yapo mambo pamoja na uzuri wake, lakini pia yamekuwa ni sehemu ya mambo ambayo tunamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hapa, atuwekee sawa kidogo. Lipo jambo katika mapendekezo ya Serikali kwenye bajeti hii ya kwamba sasa Mahakama inakwenda kukusanya kodi. Hilo limeelezwa na lilielezwa kwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri, lakini mimi kwa nafasi yangu au kwa masomo niliyosoma, pia nimewahi kufanya kazi mahakamani, nikiwa kama Mwanasheria, lakini pia nikiwa mtu anayesimamia kuona kwamba haki inatokea katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi, sitaki kuamini kwanza tunakwenda kuipa kazi Mahakama ambao siyo ya kwake. Kwa sababu unapoipa kazi mahakama ya kukusanya kodi, maana yake katika mwongozo wa yale mambo ambayo Serikali inatakiwa kufanya hili sio mojawapo. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa maelezo ya majawabu ya baadhi ya mambo ambayo wachangiaji wameeleza, ningemwomba aliangalie jambo na atueleze vizuri. Ni kwa utaratibu gani mahakama inakwenda kuwa sehemu ya chombo cha kukusanya kodi; maana hatari ninayoiona hapa tusije kufika sehemu mahakama ikalazimika kuwapa watu mafaini makubwa ili mradi tu waweze kutimiza malengo au maelekezo ya Serikali ambayo wamepewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia liko jambo la kivutio chetu au alama yetu Tanzanite. Tanzanite inatambulika kama bidhaa inayotokea Tanzania. Kwa mkakati ambao umefanyika na Wizara ya Madini bado naona kwamba kuna jambo moja halijakaa vizuri, kwa sababu mpaka leo tunapozungumza bado Tanzanite inaonekana kwamba inatokea Kenya, Tanzanite inatokea India na Tanzanite na wakati mwingine inatokea Hong Kong. Sasa kama sisi wenyewe hatutochukua initiative za kuhakikisha kwamba Tanzanite hii inakuwa branded ikaonekana kwamba ni bidhaa ya Tanzania; kwa kweli tunakazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hili juzi Mheshimiwa Rais wakati anazindua Kiwanda cha Kuchenjua, kama itakuwa ndio lugha nzuri, maana nisijekuwa naongea Kikwere hapa, kama itakuwa lugha nzuri hiyo, wakati anazindua kiwanda kule Mwanza, alieleza umuhimu wa Benki Kuu kushiriki katika ununuaji wa madini haya hasa akitia msisitizo katika eneo la dhahabu. Naamini kabisa, kama Tanzanite itatengenezewa mkakati mzuri itakuwa ni sehemu kubwa ya vyanzo vya mapato kwa ajili ya kusaidia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia naomba sana nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwa mtu mwenye maono ya mbali. Mheshimiwa Rais juzi alizungumzia juu ya cryptocurrency au wengine wanasema bitcoin ambayo ndio future ya pesa za dunia hii. Tunaona nchi kama Marekani wenzetu wamefikia sehemu sasa wanatengeneza hata sarafu zao kwa kutumia dhahabu na vito vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwangu mimi kwa wito wa Wizara, wayachukue maangalizo au maono haya ya Mheshimiwa Rais, yakafanyiwe kazi ili tusije kukutwa na sisi kama vile tupo nyuma ya muda wakati dunia imetukimbia mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo pia jambo la riba alieleza hapa Mheshimiwa mzee Sanga na mimi sitaki kurudia sana lakini ni ukweli usiofichika Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wenzake ndani ya Wizara wanayo kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba jambo hili linawekwa sawa. Watanzania walio wengi wanalalamika sana, riba zimekuwa kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na riba kuwa kubwa sana, lakini ukopeshaji nao katika mabenki umepungua sana. Sasa inaweza kuwa kuna matatizo huko ndani ya mfumo wa kibenki, lakini kwangu niwaombe sana, Serikali iangalie jinsi ambavyo Benki Kuu inaendelea kusimamia mfumo wa ukusanyaji wa pesa ili mambo yake vizuri katika upande wa riba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, lakini kwa kupitia Mheshimiwa Waziri nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kushusha baadhi ya tozo katika maisha ya vijana. Vijana wengi wao walikuwa wanalalamika sana hasa wale vijana wanaoendesha bodaboda. Juzi tulikuwa tunagawa bodaboda pale Chalinze, niliwakumbusha vijana wenzangu, kwamba hakuna jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya kama kuondoa tozo au faini za bodaboda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo naomba nirudie tena hapa hasa kuongea na vijana wenzangu wa Tanzania. Kuondolewa kwa tozo au kushushwa kwa tozo hizo, si kibali cha sisi kufanya makosa ili Serikali ituadhibu. Tuwe makini sana na huo ni upendo wa dhati ambao Mheshimiwa Rais ameonesha kwetu sisi vijana na tutumie fursa hii kwa ajili kuhakikisha nchi inajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia, nataka nizungumzie jambo la TARURA. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta shilingi milioni 500 katika majimbo yetu. Jambo hili ni zuri na kwa kweli kama ni machungu, ametupunguzia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba TARURA inahitaji nguvu ya ziada. Hizi pesa zilizotolewa na Mheshimiwa Rais, uwe mwanzo wa kupanga mkakati mzuri kwa Serikali kuhakikisha kwamba inaongeza fedha nyingi katika Ofisi za TARURA ili barabara zetu ziweze kukaa vizuri. Kwa mfano, kule Chalinze, huko iko Kata ya Talawanda ambayo kama tusipokuwa makini, kata ile inakwenda kuwa kisiwa. Hakuna njia ya kuingilia wala ya kutokea. Matokeo yake tusipokuwa makini tunaweza kujikuta mwisho wa siku nchi yetu hii inakuwa na maendeleo katika maeneo ya miji lakini siyo kule kwenye vijiji ambapo yanatakiwa maendeleo yaende; na huko ndiko bidhaa kubwa zinakozalishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri, amezungumza jambo la maji, nami namshukuru sana kwa sababu Wana-Chalinze bado wanaendelea kuishukuru Serikali kwa hatua kubwa wanayoifanya. Ila namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tutakapompitishia mafungu yake hapa, pesa hizi za miradi ya maji ziende mapema ili mambo yakakae vizuri katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo hii tuna mradi kama ule unaotoka Ruvu unakwenda Mboga, bado mimi binafsi kama Mbunge mwakilishi wa wananchi sijaridhika na ile speed yake. Nafikiri kwamba zikipelekwa pesa na mambo yakawa mazuri zaidi tutaendelea kufanya vizuri. Siyo hilo tu pia hata kwenye miradi ya mabwawa na miradi ya umwagiliaji nako pia tunahitaji sana fedha zifike kwa wakati ili mambo yetu yaweze kukaa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo mwisho kwa umuhimu, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano kwa kazi nzuri anayoifanya. Amezungumza na akina mama, amezungumza na vijana leo na uelekeo wake ni maelekezo kwa Serikali na kwetu sisi viongozi tunaoongoza makundi hayo kuweza kwenda kusimamia vizuri ili nchi hii anayoiongoza iweze kwenda katika mstari ulionyooka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge
MHE. RIDHIWANI J. M. KIKWETE - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa sana Mawaziri, Wabunge wenzangu, wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana na mimi kwanza nianze kwa kushukuru kwa sababu mwanzo nilikuwa natoa salamu za jumla za Kamati, lakini sasa nimepata nafasi ya kutoa maazimio au majumuisho, naomba nikushukuru wewe binafsi kama walivyotangulia wenzangu kusema, kwa kunipa nafasi na mimi kuwa mmoja kati ya Wajumbe wa Kamati hii ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, kwa hakika sio tu kwamba, nimeendelea kujifunza kama mwanasheria, lakini pia imenipa nafasi ya kuendelea kujua Tanzania na sheria ambazo zinaendelea kuhitaji marekebisho au uangalizi wa karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia natambua kwamba michango iliyotolewa na Wabunge mbalimbali, Wabunge 14; lakini pamoja na hao pia ameongea Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera, Vijana na Walemavu ameeleza naye katika hayo mambo yake. Lakini pamoja na hilo pia, niishukuru Serikali kwa kukubali kuchukua yale yote yaliyopendekezwa na Kamati yetu na kwenda kuyafanyia kazi. Lakini kwa umuhimu zaidi niwashukuru pia wachangiaji wote, kwa michango yao mizuri iliyolenga kuboresha taarifa yetu na kuifanya taarifa hii sasa iwe taarifa ya Kibunge, iwe na sifa za kuitwa taarifa ya Kibunge, lakini pia iwe taarifa ambayo inatosha katika maudhui yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya mambo ambayo yameelezwa na mimi napenda niyasisitizie ambayo kwangu kama mtoa hoja, ni vyema nikayapazia sauti ili Serikali iweze kuyachukua katika uzito wake.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo tumelizungumza ndani ya Kamati, lakini pia kutoka kwenye michango ya wajumbe wa Bunge lako, ni juu ya huu mtazamo ambao upo wa baadhi ya watu kutunga Sheria, ambazo zimekuwa kandamizi sana. Mheshimwia Waziri na Mheshimiwa Attorney General ni ukweli kwamba haya mnaenda kuyafanyia kazi, lakini kiukweli sheria zetu bado haziendelei kufurahisha watu wengi na hivyo kwenu ninyi kuchukua na kwenda kuyafanyia kazi ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, yameibuka hoja hapa ya ile ya bajaji ya kutozwa mpaka shilingi 200,000 kwa faini, kwa ajili ya wrong parking. Mheshimiwa Waziri mhusika ningeomba utoe maelekezo kwa Halmashauri zako na ikiwezekana utaratibu mzuri uwekwe, ikiwezekana kwamba sheria hizi kabla hazijaanza kufanya kazi basi Bunge hili liweze kuzipitia. Tofauti na sasa ambazo zinafanya kazi kwanza halafu baadaye, ndio Bunge linakuja kuziangalia kama zimefuata utaratibu au hazijafuata utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia limezungumzwa jambo hapa la vijana kuwa wanaminywa katika ajira. Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Attorney General, ndugu Wabunge wenzangu, jambo la ajira limekuwa ni kilio kikubwa cha muda mrefu, kama sisi Wabunge hatutakisimamia hiki katika ile dhana ambayo, Rais wetu mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan anataka vijana wapate ajira, sio tu katika zile ajira zilizo rasmi zinazotangazwa Serikali, lakini pia katika mazingira wanayoishi hatutoweza kufanikiwa kama jambo hili halitoangaliwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini naishukuru Serikali imesema jambo hili inalichukua na kwenda kulifanyia kazi ili liweze kuwa jambo ambalo linakwenda kutatua kero hizi. Lakini hili liende sanjari na lile jambo la ile Sheria ya Filamu ambayo nayo imelalamikiwa sana na wajumbe wengi wameipazia sauti ili kuweza kuweka sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ipo sheria nyingine ambayo imeonekana kwamba ni inaweza ikasababisha shughuli za kihalmashauri zisifanyike vizuri. Hiyo sheria inatambulika kama Sheria ya Kukusanya Ushuru ambayo sisi kwenye taarifa yetu tulionesha hiyo taarifa ya Same, lakini ndugu au Msomi Mheshimiwa Tadayo akaelezea juu ya pia taarifa nyingine inayofanana na hiyo ya kule Mwanga.

Mheshimiwa Spika, niombe Serikali iliangalie jambo hili vizuri, tukifanya mchezo Halmashauri zetu zitakosa vyanzo vya mapato na kwa kukosa mapato huko kutapelekea shughuli zetu baadhi yao zikwame. Sisi leo ndani ya Chalinze kwa mfano, moja ya chanzo chetu kikubwa ni mapato yanayotokana na kokoto. Kama ukitunga Ssheria ukasahau chanzo hiki cha mapato maana yake ni kwamba Halmashauri ya Chalinze itaingia katika mgogoro mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, jambo la kufundisha wataalam wetu ili wawe waandishi wazuri hili ni jambo ambalo lazima lipangiwe mkakati ili liwe jambo endelevu lakini liweze kusaidia halmashauri zetu kuweka mikakati vizuri na waandishi wetu waweze kuwa wamejengewa weledi ulio mzuri.

Mheshimiwa Spika, nimezungumzwa jambo lingine hapa la watunzi au waandishi wa sheria kutozingatia misingi ya Katiba. Katika jambo lililo muhimu ambalo sisi pamoja na wewe Spika wetu, tuliliahidi mbele ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ulinzi wa Katiba yetu. Bila kulinda Katiba sisi ambao ndio watunzi wa sheria hizo tutakuwa ndio kituko na kichekesho cha kwanza katika nchi hii. Tusikubali Bunge lako ligeuzwe kuwa sehemu ya kuponda na kuvunja Katiba hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia kuendelea kukumbushana Wabunge wenzangu ambao pia ni Madiwani kwamba tusiache mambo yakaendelea kule kwenye Halmshauri zetu bila sisi kushirikishwa. Maana yapo mambo mengine haya tunaweza kuyamaliza kule majimboni kwetu au kwenye maeneo yetu kwa sisi kufuatilia mara kwa mara. Kitendo cha sisi kukaa huku Bungeni kisiwe kisingizio cha kupitishwa kwa mambo ndani ya halmashauri zetu bila kushirikishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia nikushukuru Mheshimiwa spika kwa maelekezo yako uliyoyatoa na hadithi uliyotupa hapa ya kweli juu ya wale vijana ambao wamejiajiri wenyewe na tabu wanayoipata, kwangu mimi hili sio tu kwamba ni maelekezo labda kwa Kamati au kwa Serikali lakini pia kwetu sisi sote kama Wabunge tujaribu kusimamia sheria hizi ili kutatua kero hizi ambazo zinakwenda kukabili vijana wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la rumbesa limezungumzwa hapa, hili jambo nadhani kwa yale maeneo au Halmashauri ambazo zina sheria hizi hebu tuziangalie tena vizuri ili tuweze kuweka mambo yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho katika michango hii, nizungumzie mchango mzuri uliochangiwa na Mbunge Ndugu Neema Lugangira juu ya Asasi zisizo Kiserikali na zile ambazo zinafanya kazi katika jamii yetu. Kamati imesikia juu ya matatizo makubwa yaliyopo katika Kanuni hizi zinazokabili NGOs na CSOs kwangu mimi kwa kuwa mamlaka ya kuita kanuni hizi unayo wewe na Kamati yako imeendelea kufanya kazi kwa maagizo yako, tukuombe kupitia Kanuni yako, kupitia Katiba inayokupa nguvu wewe, uielekeze Serikali ituletee Kanuni hizo na sisi kama Kamati tupo tayari kwa ajili ya kuziangalia ili NGOs, CSOs na Asasi nyingine ziende kufanya kazi katika utaratibu tuliokubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia niwaambie tu ndugu zagu wa NGOs na CSOs kwamba kuja kwa kanuni hizo sio kwamba tunapata tiketi ya uvunjivu wa kanuni, hapana. Kamati itaangalia vizuri na kujiridhisha juu ya yale ambayo yanalalamikiwa na baada ya kujiridhisha mapendekezo yetu yatakuja hapa katika Bunge ili ninyi Bunge muweze kuamua katika haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeniambia kwamba unanipa dakika 20; lakini dadika 20 katika maana ya kufunga hoja kwangu mimi ni nyingi sana. Ningependa kutumia nafasi hii ya mwisho; kwanza kumshukuru kabisa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya, kazi ambayo kwa hakika inaigwa katika dunia nzima. (Makofi)

Tumeshuhudia ndani ya siku zake 100 kupitia hotuba ya Waziri Mkuu aliyoisema jana pale Dar es Salaam, akieleza kwamba Mama Samia amekwisha fanya na kuendelea kukamilisha miradi zaidi ya 73 ambayo inafanywa kwa fedha za ndani na nyingine kutoka katika fedha za wahisani ambayo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia tumeshuhudia Mama Samia Suluhu Hassan katika akitimiza kwa vitendo nia yake nzuri ya kuhakikisha kwamba mazingira mazuri ya biashara yanaendelea kuimarika katika nchi yetu. Amefanya vikao zaidi ya viwili, akishirikiana na Waziri Mkuu na Makamu wetu wa Rais na Mawaziri wetu na tumeshuhudia nia yao nzuri ikianza kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia nimpongeze sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hakika ameanza vizuri sana kazi yake ya kutimiza ndoto za Watanzania. Sisi kama Kamati ya Sheria Ndogo au sisi kama Wabunge tunaendelea kumuunga mkono na niwaombe Wabunge wenzangu tuendelee kumuunga mkono mama yetu akitimiza nia nzuri ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini siyo mwisho kwa umuhimu wake, niishukuru pia familia yangu; katika kipindi cha miezi miwili/mitatu ambayo tumekaa Bungeni hapa, tumekuwa mbali na familia lakini wanangu wamekuwa wananipigia simu wakinishukuru, wakinipa moyo na kunifariji, mke wangu amekuwa anafanya hivyo na kwangu mimi imekuwa ni faraja kubwa sana hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia leo asubuhi umewatambulisha rafiki zangu wawili; nisingependa jambo hili nichukue muda sana lakini kwa upekee uniruhusu nifanye hivyo; amekuja rafikii yangu mmoja hapa anaitwa Azizi. Azizi kwa taaluma yake yeye kinyozi, ni mtu ambaye ukimuona utamuona ni mtu mdogo sana, lakini Azizi ndiye ambaye anafanya mimi na wenzangu wengine tunapendeza na kuonekana hivi tulivyo. (Makofi)

Amekuja hapa nimemualika na ni mgeni wangu, nataka mjue ndugu zangu Wabunge wenzangu kwamba kuna umuhimu wa kwamba chamber hii kama alivyozungumza Mheshimiwa Spika ikawa chamber ya kila mtu. Siyo tualike tu wale wapiga kura wetu wa Katibu, Wenyeviti, Madiwani hapana na watu wengine ambao wanafanya Maisha yetu yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo pia yupo rafiki yangu Dkt. Mwinyi; Dkt. Mwinyi amekuwa ananisaidia sana, mimi kama alivyozungumza mama yangu Waziri Jenista Mhagama mimi bado nasoma pia, nipo UDOM hapo nasoma na ile ndoto ya Mama Jenista Mhagama huenda siku moja ikawa kweli na mimi nikawa Daktari. (Makofi)

Nakushukuru na ninaamini kabisa maneno yako hayawezi kuanguka na amekuwa msaada mkubwa sana Dkt. Mwinyi akinisaidia kuhakikisha kwamba na mimi natimiza ndoto za kuwa Daktari siku moja, lakini kuwa katika jamii ya vijana ambao ni wasomi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa maana siasa tuna mwisho kabisa, tuna mwisho kwa umuhimu kwa umuhimu wake; mwisho kabisa niendelee kukushukuru wewe kwa kunipa ruksa hii. Umenipa nafasi kubwa ya kuhudumia katika Kamati hii na mimi binafsi yangu namshukuru tena Mwenyekiti wangu Dkt. Rweikiza kwa nafasi kubwa aliyonipa ya kuja kusoma mbele yako, lakini pia ruksa hii inatupa nafasi na sisi ya kutokuwa na woga tunaposimama mbele yako. Maana hapa panatisha, lakini kwa kipekee nikushukuru wewe pamoja na Wabunge wenzangu tuendelee kupeana ushirikiano. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo hayawezi kuwa maendeleo bila ya kuwa na maji safi na salama. Katika Jimbo langu la Chalinze kwa kipindi kirefu tumekuwa tunashughulika na mradi wa maji tumejitahidi kuhakikisha kwamba mradi ule sasa umefika katika awamu ya pili awamu ambayo imekamilika, lakini tunapoelekea katika awamu ya tatu nimeona kwamba ndani ya Mpango wa Maendeleo kitabu kizuri kabisa kilichowekwa na Dkt. Mpango kinaonesha kwamba wametenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha mradi wa maji wa Chalinze unafanyika. Ninachowaomba Mheshimiwa Waziri wa Maji atakapofika hapa atuambie juu ya jinsi gani amejipanga kwa kuhakikisha kwamba fedha za mradi ule zinafika haraka ili ujenzi wa awamu ya tatu upate kuanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia tunatambua maendeleo hayawezi kuwa maendeleo bila kuwa na viwanda lakini viwanda hivyo lazima vitegemee kilimo ikiwa ni kama sehemu ya kupatikana kwa malighafi hizo. Wamesema hapa wenzangu wanaotokea Tabora kwamba leo hii Tabora ndiyo wakulima wazuri wa tumbaku, lakini kiwanda kinachotegemewa kiko Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nafikiri muda umefika wa Serikali yetu kuwekeza nguvu zaidi katika kuhakikisha kwamba viwanda vinajengwa karibu na malighafi hizo ili hii taabu ya kupatikana malighafi ambayo zinasafirishwa muda mrefu isiwepo tena. Hata hivyo, siyo hilo tu ili kuhakikisha kwamba malighafi zinafika vizuri viwandani miundombinu ya barabara zetu na reli ni muhimu sana ikawekwa vizuri. (Makofi)
Niungane na wenzangu wanaozungumzia umuhimu wa kujenga reli ya Kati lakini pamoja na hilo pia reli inayokwenda Tanga ambayo inapita katika mashamba ya mkonge, lakini reli pia ya TAZARA inayopita katika maeneo makubwa yenye kilimo katika Nyanda za Juu Kusini nazo ni muhimu sana zikawekewa umuhimu katika kipindi hiki cha bajeti hii inayofuatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo katika ukurasa wa 31 imezungumziwa kuhusu jambo zima la elimu na afya. Ni kweli Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba inaweka mambo mazuri katika upande wa afya hasa za wananchi wetu wa hali ya chini sana. Niwapongeze sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu na rafiki yangu Dkt. Hamis Kigwangalla kwa kazi kubwa ambayo wamekwishaanza kuifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango yao mizuri ya kuhakikisha kwamba afya zinaendelea kuimarika katika maeneo ya vijiji vyetu na kata zetu, lakini uko umuhimu wa pekee wa kutambua pia kwamba ziko shughuli ambayo zimekwishaanza kufanyika, mimi nazungumzia zaidi katika Jimbo la Chalinze ambapo karibu vijiji vyote vina zahanati, lakini pia Kata Nane kati ya 15 zilizopo katika Jimbo la Chalinze zina vituo vya afya.
Sasa ninachoomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa kueleza ni vema akatuambia mpango gani walionao kuhakikisha kwamba vituo vyetu vya afya hivi ambavyo tumevianzishwa vinaendelea kuwa bora zaidi hasa kile cha kiwango ambacho tumenunua vifaa vyote lakini mkakati wa kukamilisha ile pale tunasubiri sana kauli toka kwao kama Wizara husika kwa maana nyingine tunazungumzia lugha ya kuja kukagua kwa hatua za mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo tunatambua umuhimu wa elimu ikiwa ni moja ya vitu ambavyo ni muhimu sana vikaangaliwa. Katika maeneo yetu sisi tunayotoka majengo yetu mengi miundombinu yake ni chakavu sana, ikumbukwe kwamba Bagamoyo ni moja ya Wilaya kongwe kabisa Tanzania ambapo shule zimeanza kujengwa siku nyingi na majengo yake yamekuwa chakavu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokuja kuleta bajeti zetu za Halmashauri hasa katika eneo la elimu katika kuimarisha miundombinu yetu, tunaomba sana Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu mpate kuliangalia hili kwa jicho la karibu zaidi ili tuweze kupata fedha za kuweza kuimarisha elimu hii na vijana wetu wapate kuishi katika mazingira mazuri. Bila kufanya hivyo tunaweza kujikuta tunaibukia katika matatizo ya kwenda kuzika vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa taarifa tu na nitoe pole sana kwa ndugu zangu wanaoishi katika Kata ya Kibindu au Kijiji cha Kibindu shule yetu imeanguka kule yote na vijana wetu zaidi ya 1,100 wako nje mpaka sasa hivi tunapoongea. Pia kwa kipekee kabisa niwapongeze wananchi wa Kibindu kwa hatua zao kubwa walizoanza za kuhakikisha kwamba wanajenga madarasa na mimi Mbunge wao nitakaporudi ahadi yangu ya kupeleka mifuko 1,500 iko pale pale ili kuhakikisha kwamba shule ile tunaijenga na wananchi wangu waanze kusoma hasa vijana wetu ambao ndiyo tunategemea kesho waje kuturithi mikoba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nizungumzie jambo zima la uchumi, wananchi wa Jimbo la Chalinze wengi wao ni wakulima na wako baadhi yao ni wafugaji. Tunapozungumzia ufugaji tunategemea sana uwepo wa machinjio yetu pale Ruvu yakamilike mapema sana. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alipata nafasi ya kuja pale, tulimsimulia juu ya ufisadi mkubwa unaofanyika pale lakini pia tukamwambia juu ya mambo ambayo yanaendelea na sisi pale wananchi wa Jimbo la Chalinze ni wakarimu kabisa hasa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka hifadhi ile au ranch yetu ya NARCO pale Ruvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie juu ya hatua gani wamefikia baada ya mkutano mzuri tuliofanya pamoja na yeye na wananchi wa Kijiji cha Vigwaza, wananchi wa Kijiji cha Mkenge na wananchi wa vijiji vingine ambao vilio vyao kupitia Mbunge wao nilivisema siku hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo natambua pia upo umuhimu wa kumulikwa na umeme, nishati hii ni muhimu sana, wakati wa enzi za Mheshimiwa Waziri Profesa alifanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba umeme unapelekwa katika vijiji vya Jimbo la Chalinze. Mimi binafsi yangu kwa niaba ya wananchi wa Chalinze nimshukuru, lakini pamoja na hilo mahitaji ya kujengwa na kuwekwa transfoma kubwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa Kata ya Mbwewe, Kata ya Kimange, Kata ya Miono, Kata ya Msata na Kata nyinginezo zenye mahitaji kama haya hasa Kiwangwa ni mambo ambayo ni ya msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba anapokuja hapa Mheshimiwa Waziri anayehusika na masuala ya nishati atuambie juu ya mikakati ambayo wamejipanga nayo kuhakikisha kwamba wanamalizia ile kazi ambayo walikwisha ianza katika eneo la Jimbo la Chalinze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua pamoja na hayo pia iko kazi nzuri ambayo tulianza katika awamu iliyopita ya ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. Nataka niliseme hili kwa sababu kumekuwa na kauli za sintofahamu zinazotoka kwa upande wa Serikali ambazo zimekuwa zinaripotiwa katika magazeti. Unaweza kuwa shuhuda katika gazeti moja miezi kama miwili iliyopita iliripoti kwamba ujenzi wa bandari ile hautokuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nilipata nafasi ya kuzungumza na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri akanihakikishia kwamba ujenzi wa bandari ile upo na nifurahi kwamba nimeiona katika kitabu cha maendeleo. Hata hivyo, wananchi wangu wa Jimbo la Chalinze na Wilaya ya Bagamoyo hawana raha na wakati mwingine hata wakituangalia sisi viongozi wao wanakuwa wanapata mashaka juu ya kauli zetu hasa kwa kuamini kwamba tunakitetea Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa naye awahakikishie wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo kwamba bandari ya Bagamoyo itajengwa kwa sababu bandari hii ni bandari muhimu na ni bandari ambayo imewekwa pale kimkakati. (Makofi)
Serikali ya Tanzania imekwisha fanya kazi yake ya kutathmini na kuwalipa fidia wananchi wa maeneo ya Pande-Mlingotini na Kata ya Zinga. Sasa iliyobakia ni kazi ya wawekezaji wa China na Oman kuja kuweka hela kwa ajili ya kuanzisha uchimbaji na ujenzi wa bandari hiyo. Nitahitaji sana kusikia kauli ya Serikali ili wananchi wetu wa Wilaya ya Bagamoyo wapate amani ya mioyo yao wakiamini kwamba maendeleo makubwa na mazuri yanakuja katika eneo lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo nimalize kabisa kwa kuendelea tena kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Chalinze, maana sisi kwetu Chalinze ni kazi tu na kwetu sisi tunafanya kazi kwa ushirikiano, wananchi wanafanya kazi na sisi tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja. Pamoja na kuongeza juhudi kubwa ambazo Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Watendaji wa Wizara wamekuwa wanafanya, lakini ni ukweli usio na kificho kuwa changamoto zimeendelea kuandama Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu kwenye Bunge la Kumi, niligusia juu ya mahitaji ya kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ili kuwe na tija ya upatikanaji wa chakula cha kutosha, lakini hadi leo ninapowasilisha andiko hili, bado migogoro imeendelea kushamiri. Mheshimiwa Waziri umeshuhudia athari inayotokana na kutokuwepo kwa Sheria zinazobana, kugeuzwa kwa mashamba kuwa sehemu za machungio. Ni vyema Mheshimiwa Waziri atakapokuja, atueleze juu ya mkakati mzima alionao katika kuhakikisha kabla ya Januari, 2017, migogoro imekwisha kama siyo kupungua kwa asilimia kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya sukari imeendelea kuwa kubwa na speed ya upandaji wake naufananisha na kuongezeka kwa migogoro ya wakulima na wafugaji. Katika Awamu ya Nne, kuna mradi mkubwa wa miwa ulioanzishwa Wilaya ya Bagamoyo. Mradi huu ambao una maslahi makubwa sana na Watanzania hususan ni watu wanaotumia sukari, umepelekea watu kuwa na matumaini ya kufufua upya maisha bora kwa wananchi, lakini pia huenda hili tatizo la sukari likamalizika.
Mheshimiwa Naibu Spika, linaloshangaza, hadi leo fedha za Benki toka ADB na IFAD zilikwishatengwa kwa muda mrefu zikisubiri kauli ya Serikali juu ya mradi huu. Namwomba Waziri au Serikali itakapokuja kufanya majumuisho, itoe kauli juu ya lini kauli hii itatoka na je, hawaoni kuwa kwa kuchelewa kutoa kauli ni kuhujumu Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015?
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna maendeleo pasi kuwa na teknolojia inayoendana na tija kubwa ya kimatokeo. Kilimo cha leo kinategemea matrekta na zana bora za kisasa ili kuleta tija ya kilimo hicho. Nakupongeza wewe Mheshimiwa Waziri na wataalam kwa kuonesha kupitia hotuba utayari wenu wa kuvusha kilimo chetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba matrekta 2,000 ni machache sana; ili kupata tija ni vyema tukaongeza matrekta ili tija nzuri ya kilimo ipatikane. Kwa asilimia kubwa kilimo kinategemea maji. Viko vipindi mbalimbali katika majira ya mwaka ambapo mvua ziko za kutosha, ila linaloshangaza wengi, ni ujuzi mdogo wa kuhifadhi maji hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara itengeneze program za kufundisha watu kufanya uhifadhi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na pia kuanzisha utaratibu maalum wa kufundishia Maafisa Ugani ili waweze kuwa wenye msaada mkubwa zaidi.
Katika Jedwali Na. 3, ukurasa wa 29 kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameonesha ukuaji mkubwa wa mazao ya mafuta. Linalonishangaza hapa ni kwamba, mazao yote yaliyoainishwa, ni mazao ambayo hayana vyombo vinavyoongoza na hata wakati mwingine kujiuliza hizi takwimu zimetoka wapi? Mheshimiwa Waziri aweke wazi jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao hayo yaliyoainishwa yanaweza kuwa siyo sahihi kwa upande wa taarifa. Chalinze na maeneo mbalimbali wanaofanya biashara hizi wamekuwa wanafanya kwa utaratibu wanaojipangia wenyewe na hata kupelekea Serikali kupoteza fedha nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri sasa ni muda muafaka kuwe na vyombo maalum kwa uratibu wa mazao haya ili tija ipatikane. Kama katika hali ya sasa tunapata namna hii, basi utaratibu ukiwekwa, tutapata mara tano ya hapa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru wewe kwa kuniona na kunipa nafasi hii niweze kuchangia Hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa msomi, Mheshimiwa Muhongo ambaye kwa kweli, binafsi yangu kwa aliyonifanyia kipande cha Chalinze, sina shaka kusema Mungu azidi kumzidishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu iliyopita katika vijiji 67 vya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze tumefanikiwa kupata umeme karibu vijiji vyote kupitia mpango wa REA isipokuwa vijiji 15 ambavyo vimebakia, ambavyo nina imani kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusimama hapa na kueleza juu ya mkakati wake wa kuimarisha umeme vijijijini, basi Chalinze nina hakika kabisa ataviangalia hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaoishi vijiji vya mbali kama kule Kwa Ruombo, Kibindu, Lugoba, Mkange, wanaonisikiliza wote katika Jimbo la Chalinze kule Pela, Msoga, Tonga na maeneo mengine mbalimbali hakika kabisa watakuwa wameyasikia haya. Kwa kweli Profesa najua kwamba, ramani ya eneo lile siyo mgeni nalo, basi atafanya mambo yale ambayo ametufanyia katika miaka mitano iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo, jambo la msingi nataka nimkumbushe Waziri na najua kwamba analifahamu, lakini sio mbaya nikatumia nafasi hii kumkumbusha. Pale Chalinze wakati wanaweka transformer, ile inaitwa power transformer, kwa ajili ya kuongeza nguvu za uzalishaji wa umeme Chalinze na maeneo yake walitufungia transformer yenye MVA 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu na takwimu za wasomi wa elimu ya umeme katika Jimbo letu la Chalinze wakiongozwa na ndugu yangu Mkuu wa TANESCO pale Chalinze inaonesha kwamba, matumizi ya sasa ya Jimbo la Chalinze ni almost karibu MVA 10, kwa hiyo, maana yake tunayo nafasi nyingine iliyobakia ya MVA 35 ambayo Mheshimiwa Profesa Muhongo akiiangalia vizuri hii anachotakiwa kufanya ni kuweka tu nyaya pale na wananchi wa Chalinze wale wapate umeme wa uhakika zaidi; hatuna tunalomdai zaidi ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nataka nizungumzie pia tatizo kubwa ambalo nililizungumza katika Bunge lililopita juu ya tatizo lililoibuka katika Kijiji cha Kinzagu na Makombe juu ya hati alizopewa mwekezaji. Sisi tulilalamika sana, lakini tukaambiwa kwamba, kuna utaratibu Wizara inaweza ikatoa hati ya mtu kwenda kufanya uchimbaji wa madini katika vijiji hata kama hao wataalam wa Wizara hawajafika kijijini hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie ukweli na Bunge lako lisikie na Watanzania waamini hili ninalolisema. Hati iliyotolewa, aliyopewa mwekezaji katika Kijiji cha Kinzagu na Makombe imeacha kipande ambacho nafikiri kina ukubwa, labda wa jumba hili la Bunge! Kijiji chote kipo ndani ya ardhi ya mwekezaji! Wale watu wamezaliwa pale, wameishi pale, wamekulia pale na waliokufa wamezikwa pale! Leo hii wanapowaambia kijiji kizima kiondoke, nini maana ya mimi kuwa Mbunge pale kama sio kutetea watu wangu ambao wamenipigia kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Profesa Muhongo, hata kama sheria hizo zipo nataka atambue kwamba, sheria hizo kwa watu wa Chalinze ni bad law na kwamba, tutazipigania kuhakikisha kwamba hizo sheria zinaondolewa, lakini muhimu yeye mwenyewe atakapokuja kufanya majumuisho, akatuambia ni mpango gani walionao katika hili. Kidogo nimepata nafasi ya kusoma sheria, natambua kwamba, hata kama mtu amepewa hati hiyo wanakijiji wanayo haki ya kukataa huyo mtu asipewe access ya kufanya uchimbaji wake na mwendelezo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine hapa tunazungumzia maendeleo, ninachokiona Serikali yangu inajaribu kunigombanisha nao pia, kwa sababu, mimi kama mwakilishi wa wananchi sitokubali! Nasema tena, sitokubali kuona watu wangu wa Kijiji cha Kinzagu na Makombe wanaondolewa ili kupisha bepari ambaye anataka kuja kuwekeza katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nizungumzie pia, matatizo ambayo wanayo wananchi wa eneo la Kata ya Mandela. Niliwahi kusema hapa na leo narudia tena, tulimwomba Mheshimiwa Waziri aangalie sana kuna Kijiji kinaitwa Ondogo ni kijiji ambacho wanaishi watu wanaotegemea maisha yao katika ukulima. Kama unavyojua ukulima sio shughuli ambayo inafanyika muda wote, ni shughuli ambayo inafanyika, jua likizama watu wanarudi nyumbani.
Pale nataka nikuhakikishie Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais aliyemfanya yeye leo hii akawa Waziri alichaguliwa kwa asilimia 100 katika Kijiji cha Ondogo; Bwana John Pombe Magufuli alichaguliwa kwa nini, ni baada ya mimi na viongozi wenzangu wa chama, kwenda pale kuchapa maneno na kuwahakikishia wananchi wale kile kilio chao cha transformer tu ya KV 20 itapatikana na wale wananchi watapata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba, hapa nilipo nimeshapewa taarifa kwamba, kama hiyo transformer haitakuja pale, 2020 nikatafute sehemu nyingine za kuombea kura kwa sababu, pale sitopata hata moja. Kwa maana hiyo ya kwamba, sitopata hata moja, maana yake Mheshimiwa Rais pia naye hatopata hata moja! Mimi natokea Chama cha Mapinduzi, naomba ku-declare interest kukipigania chama changu ni wajibu wangu na nina imani katika jambo hilo. Nataka pia Mheshimiwa Waziri aangalie sana pale ambapo tulipata asilimia mia moja ya kura zote ili baadaye tusije kupata sifuri ya kura zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Muhongo kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, lakini pia kwa juhudi kubwa ambazo Wizara yake inafanya. Tunao mradi pale, mkubwa, wa Bwala la Kidunda ambao katika bwawa hilo pia, tunatarajia kwamba, ipo sehemu ambayo itatoa umeme na umeme huo utafaidisha Vijiji vya Magindu, Kijiji cha Chalinze, kwa maana ya Bwilingu, lakini pia na maeneo mengine ya Mikoroshini na Kata ya Pera pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachomwomba Mheshimiwa Waziri, yeye na Wizara ya Maji wanapokwenda kusimamia, kuhakikisha kwamba jambo hili wanalifanyia kazi, basi ningeomba jambo la umeme kwa wananchi wangu wa Chalinze nao pia muwaangalie kupitia mlango huo, kama ambavyo mipango thabiti ya Chama cha Mapinduzi tumeipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Naomba kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri na kumtakia kila la heri katika safari yake ya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba nzuri ya Waziri wetu wa Maliasili na Utalii, ambayo hakika kwangu imetoa fumbo au imetoa jibu la mambo ambayo nilikuwa nahitaji kuyasikia. Mheshimiwa Waziri kwanza nikupongeze na kukuunga mkono katika hotuba yako hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote naomba kumwambia ndugu yangu Msigwa nimemsikia hapa amezungumza juu ya jambo la Green Miles. Ninachokifahamu Mheshimiwa Msigwa, hukumu imeshatolewa juu ya kesi ile ya Green Miles. Bahati mbaya sana hawa ambao wewe unaowasema ni dhaifu, hawana sifa, mahakama imeamua kuwapa kitalu. Mheshimiwa Waziri atakuja kuyazungumza vizuri, lakini nilitaka nitoe taarifa hii mapema ili upate kuifahamu halafu Mheshimiwa Waziri aje kututhibitishia kama niliyoyasikia mimi ndivyo yalivyo au yana walakini katika lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, niungane na ndugu yangu Mheshimiwa Msigwa aliposema kwamba nchi hii ni ya kwetu wote na tunapaswa kuzungumzia interest za nchi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Tanzania, mwezi Oktoba mwaka jana, walichagua Chama cha Mapinduzi, tuzungumzie maslahi ya nchi hii. Huo ndiyo wajibu wetu wa kwanza kama Wabunge tunaotokea ndani ya Chama cha Mapinduzi, kuzungumza juu ya interest za nchi yetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Msigwa anachofanya ni kutukumbusha juu ya wajibu yetu na sisi tunakushukuru kwa sababu ndiyo wajibu wetu kuendelea kukumbushana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu kwa kipindi kirefu sana imekuwa katika migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji, pamoja na hilo migogoro ya uhifadhi na vijiji vyetu nayo imekuwa ni moja ya donda ndugu. Mimi nimewahi kuzungumza katika Bunge lililokwisha, Bunge la Kumi juu ya matatizo makubwa yaliyopo baina ya watu wa kijiji cha Matipwili, Gongo, Mkange, Manda na Hifadhi ya Saadani. Ziko hatua ambazo zilikwishafanyika kipindi kile cha Mheshimiwa Nyalandu, alikwenda kule akakutana na Wananchi wale, wakafanya mikutano, lakini Mheshimiwa Waziri Maghembe, ambaye hii ndiyo bajeti yako ya kwanza ninaamini kwamba kuna vitu unabidi uvisikie kutoka kwetu Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba yale waliyokubaliana Mheshimiwa Nyalandu na wananchi wangu, mpaka sasa hivi imeendelea kuwa ni kizunguzungu na hakuna majibu sahihi yaliyokwishapatikana. Kwa hiyo, ninachokuomba Mheshimiwa Waziri, unapokuja kujumuisha au kuhitimisha hotuba yako, ni vema jambo hili pia nalo ukalizungumza ili wananchi wangu wa vijiji vilivyotajwa, waweze kusikia kauli yako wewe Waziri mpya wa Wizara hii, ukitoa majibu yaliyo sahihi na jinsi gani tunaweza kukamilisha mchakato ambao ulianzishwa na wenzako waliotangulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nimewasikia watu wengi wakizungumza juu ya matatizo ya ng‟ombe katika hifadhi zetu. Mheshimiwa Waziri, nataka nikwambie mimi ninayo Hifadhi ya Wamimbiki, na yoyote yule anayetaka kusimamia hapa kutetea ng‟ombe wakae ndani ya hifadhi huyo ni adui wangu wa kwanza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwambieni ndugu zangu, haiwezi kugeuzwa nchi yetu ikawa yote ni sehemu ya kuchunga ng‟ombe, haiwezekani, lazima tuweke mipaka na lazima tu- identify maeneo ambayo ng‟ombe wanatakiwa kwenda kuchungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Halmashauri ya Chalinze, wananchi wa Tanzania, wananchi wa Bagamoyo, kwa kipindi kikubwa sana wamekuwa wanategemea sana Hifadhi ya Wamimbiki kwa ajili ya kupata fedha za kigeni, lakini pia kwa shughuli za kitalii zilizokuwa zinafanyika katika maeneo yale. Sisi wengine Wamimbiki tunatembea na mguu kuingia kule. Tumekuwa tunashuhudia wanyama wakati tuko wadogo, leo hii Mheshimiwa Waziri, wanyama wale hawapo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu hata hatuelewi wametokea wapi, wamekaa ndani ya hifadhi ya Wamimbiki, baya zaidi ambalo linafanyika hatulipendi, inakatwa miti, watu wanatengeneza makazi ndani yake, na matokeo yake ni kwamba miezi mitatu iliyopita ndugu zangu tumeshuhudia tembo katika Mji wa Chalinze - Bwiringu. Tumeshuhudia tembo katika Mji wa Chalinze, kwa nini wamekwenda Chalinze, ni kwa sababu hawana njia zingine za kupita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupeni taarifa kwa sababu sisi wengine kule Chalinze ni kwetu, hatujaenda kutafuta vyeo. Tembo wanapotoka Mozambique, wanakuja kupitia kwa Selous na wakifika maeneo ya Mikumi wanagawanyika katika makundi mawili, lipo kundi ambalo linakwenda Kaskazini mpaka Hifadhi ya Manyara na liko kundi ambalo linakwenda Mashariki mwa Tanzania, ambalo linakwenda mpaka Hifadhi ya Saadani. Kinachoshangaza, kwa shughuli zinazofanyika pale, na shughuli ambazo zinaonekana kwamba Wizara haichukulii kimkakati jambo hili, wale tembo sasa hawana sehemu ya kwenda. Matokeo yake tembo hawa wanatafuta njia nyingine za kufika Saadani, ndiyo matokeo yake wanafika kwenye nyumba za watu na inakuwa ni taabu katika maisha yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili jambo liko serious, hatutakiwi kulifanyia mchezo, kama ambavyo leo hii wako baadhi ya wenzetu kwa mfano, Biharamulo kule, imefika sehemu kwamba wanaomba lile pori sasa ligawanywe ili watu wapate kuhifadhi ng‟ombe, badala ya kufanya shughuli za hifadhi asilia. Kama ambavyo leo hii mbuga ya Serengeti inataka nayo kupotea kwa kuwa ng‟ombe wamejaa wengi au kule katika pori la Kigosi na pori tengefu la Loliondo. Mheshimiwa jambo hilo kwa Halmashauri ya Chalinze hatuko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima leo hii, utuambie ni mkakati gani ambao kama Wizara mnao na mmejipangaje kuhakikisha kwamba mnaondoa mifugo hiyo katika eneo lile ili sasa mambo mazuri ya uhifadhi wa hizi asili uendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, Mheshimiwa Waziri tunalo tatizo lingine pia katika Uzigua forest; Uzigua forest imekuwa ni kilio cha muda mrefu na mwisho wa siku hapa mzee tunaweza tukageuzwa majina yetu yakawa ni Uzigua forest hapa, Mheshimiwa Waziri hili nalo naomba ulitolee jibu. Wananchi wamekuwa wanauliza juu ya mipaka ya hiyo Uzigua forest, lakini hifadhi yetu hii imeendelea kukua, inaonekana tofauti na ambavyo hifadhi nyingine zinaendelea kuwepo. Lakini majibu yamekuwa ni yale yale kwamba tutakuja halafu hatuna jibu la moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Mheshimiwa Waziri, na hili jambo nafikiri ni jambo la Serikali yote ilisikie. Kumekuwa na tatizo moja la ECO-Energy. ECO-Energy walipewa maeneo na vijiji vyetu, lakini cha kushangaza zaidi baada ya kutangaza juzi kwamba mradi ule hautokuwepo, kipande cha hifadhi ambacho kilikuwa katika miliki ya vijiji vyetu vile, hifadhi ile kinarudishwa katika eneo la TANAPA, Saadani.
Mheshimiwa Waziri naomba tu nikupe angalizo, wananchi wangu wa Halmashauri ya Chalinze, walitoa maeneo yale kwa ajili ya kupata faida nayo. Faida yao kubwa ilikuwa kwamba ECO-Energy walime miwa, lakini wao wawe ni outgrowers. Leo hii maeneo yao yale meamua Serikalini kuyachukuwa na kuyafanya yawe sehemu ya TANAPA. Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie, katika jambo hili hatutokubalina na mimi nitakamata shilingi yako kama hakutakuwa na jibu ambalo linatuambia kwamba ardhi hii itarudishwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Serikali mnaweza mkaamua lolote, lakini katika jambo hili la ardhi ya wanavijiji wangu, kama hatujafika na sisi kulalamika, kama alivyolalamika juzi Mheshimiwa Mbowe pale na ardhi ile ya Kilimanjaro, ningeomba jambo hili mlitolee majibu mazuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya Operesheni Tokomeza, wenzangu wamezungumza kwamba ardhi ile ya Operesheni Tokomeza imechukuwa bunduki za watu, imechukua magobole ya wazee wangu pale katika vijiji vyetu vinavyozunguka hifadhi zetu, lakini baada ya kumalizika operesheni ile hatuoni silaha zile zikirudishwa kwa wananchi wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, uje kutoa jibu katika jambo hili. Mwenzako Mheshimiwa Nyalandu hapa alikuwa kila siku anatumbia kwamba itatoka kesho mpaka anaondoka hakuna jambo lolote. Nataka wewe katika Serikali hii, uje kutuambia inakuwaje juu ya yale mambo ambayo tulikuwa tunaongea kila siku juu ya silaha hizi za jadi walizokuwa wanatumia wazee wangu pamoja na magobole na mambo mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nieleze pia kama walivyosema wenzangu juu ya jazba zilizotawala humu ndani!
Waheshimiwa Wabunge, hatupaswi kuwa na jazba! kazi yetu Wabunge ni kushauri, tutumie nafasi hiyo kushauri. Maana leo hii tunaposikia kauli kwamba hii CCM gani, mimi nikiwa kama Mjumbe wa NEC, naomba ni- declare interest, nakwazika...
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii nzuri ya Wizara ya Maji ambayo ninaamini maji ni uhai maana yake uhai wa Wana-Chalinze unaanzia kwenye hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru maana nasema usiposhukuru kwa kidogo huwezi kushukuru kwa kikubwa utakachopewa. Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wametufanyia makubwa sana katika Jimbo la Chalinze, Mradi wa Maji wa Chalinze pamoja na kukwama kwake kwa mara kwa mara kunakotokana na tatizo la mazingira yetu kuharibika mara kwa mara inapofika hasa kipindi cha mvua, lakini siku zote wamekuwa pamoja na sisi kuhakikisha kwamba wanakabiliana na changamoto hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni bomba lilikatika pale karibu na kijiji cha Chalinze Mzee, Mheshimiwa Waziri alitutafutia kiasi cha shilingi milioni 90 kurekebisha miundombinu ile ndani ya muda wa siku mbili, tatu. Kwa kweli binafsi ndiyo maana ninasema kwamba nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri. Siyo hilo tu, hata pale Kihangaiko ilipotokea uwezo wake wa ku-react mapema zaidi na haraka kwa kweli binafsi yangu unanipa nafasi ya kuunga mkono hoja yake hata kama mambo yaliyopo humu ndani wengine wanaona kwamba hayatotekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kuchangia katika eneo la utekelezaji wa Mradi wa Maji Awamu ya Tatu wa Chalinze. Pamoja na mambo mazuri yaliyoandikwa katika kitabu pia pamoja na mazuri ambayo yamekwishaanza kutokea pale Chalinze, nina jambo moja la kushauri Mheshimiwa Waziri na hili jambo naomba sana utakapo kuja kutoa majibu yako ni vema ushauri wangu huu ukauweka kama kipaumbele sana kuliko yanayoendelea kufanyika sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua fedha zimekwishatolewa zaidi ya shilingi bilioni 21 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa awamu ya tatu, ambao umetengewa dola milioni 41 ambazo zinatarajiwa kutumika katika kipindi hiki, lakini lipo tatizo ambalo naliona kwamba ujenzi wa awamu ya tatu umeanza katika kujenga matanki kwa ajili ya kuhifadhia maji. Tatizo kubwa tulilonalo Chalinze ni kwamba kila inapofika kipindi cha mvua Mheshimiwa Waziri unafahamu vizuri chanzo kinaharibika, matope yanajaa katika chanzo matokeo yake watu wa Chalinze hawapati maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri busara kubwa ziadi ungeielekeza kwenye kujenga lile tanki kubwa la kuhifadhia maji pale kwenye chanzo ili hata kama ikitokea hali hiyo baadaye yale maji yatakayokuwa yamehifadhiwa pale, ambayo kwa estimation zilizoandikwa humu ndani tanki litakuwa na uwezo wa kubeba lita zisizopungua milioni 11 maana yake ni kwamba watu wa Chalinze wanaweza wakanywa lita hizo milioni 11 wakati wanasubiri mambo yakae vizuri katika chanzo kile. Unapoamua kujenga matanki, halafu maji yakachafuka tena Mheshimiwa Waziri nataka nikuambie watu wangu wa Chalinze wataendelea kupata taabu wanayoendelea kuipata sasa na hivyo utakuwa hujawawezesha katika kutatua tatizo lao linalowakabili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo katika kitabu chako cha bajeti Mheshimiwa Waziri umezungumza juu ya usalama wa maji yetu. Mimi ninakushukuru sana kwa sababu kama maji hayatokuwa salama maana yake hata wanywaji wenyewe hali yetu nayo itakuwa ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo unapozungumza usalama wa maji pia huwezi kuepuka kuzungumzia usalama wa miundombinu yake. Kwa sababu yapo mambo yanayotokea katika maendeleo ya kibinadamu ambayo yanaharibu miundombinu na hata wakati mwingine hayo maji safi na salama tunayotarajia kuyapata hatuyapati katika muda. Kwa mfano, Chalinze Mjini katika kijiji cha Chalinze Mzee upo mradi uliokuwa unafanyika wa ujenzi wa nyumba, mtu amepima viwanja vyake vizuri lakini walipopewa kibali cha kuanza kukata viwanja yule mkandarasi aliyekwenda kutengeneza pale alivunja bomba.
Mheshimiwa Waziri unakumbuka ilikulazimu mwenyewe uje pale ili uone jinsi uharibifu ule ulivyofanyika. Sasa kama itakuwa kazi yetu tunatengeneza usalama tu wa maji, hatuangalii usalama wa miundombinu itakuwa kila siku unakuja Chalinze kama siyo kila siku unakwenda na maeneo mengine huko Geita na maeneo mengine ukihangaika. Sheria ziwekwe kwamba mtu anapopewa haki za kuendeleza maeneo basi pia haki hizo ziendelee na kulinda miundombinu ya maji yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, kipekee kabisa nizungumze katika Mradi wa Wami-Chalinze kulikuwa na extension ya maji inayotoka Wami inayotakiwa kufika hadi Mkata kwa upande wa Handeni Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua katika bajeti hii haijapangwa, hivyo ningeomba sana mnapojaribu kuangalia uendelezaji wa mradi huu ni vema pia jambo hili mkaliangalia kwa sababu watu wa Mkata kwa upande wa kupata maji ni rahisi sana kuchukua maji kutoka Chalinze kuliko kuchukua kutokea kwenye Mji wa Handeni Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali muangalie juu ya mradi wa maji wa Ruvu, mmetengeneza mradi wa maji mzuri wenzetu wa Dar es Salaam wanaendelea kufaidi na maji hayo lakini kibaya zaidi ni kwamba wananchi wa Ruvu kwa maana ya Mlandizi pale hawana maji. Ni aibu sana lakini ni jambo ambalo Wizara inatakiwa iliangalie. Natambua kwamba yapo marekebisho yanayofanyika sasa kwa ajili ya kuhakikisha mradi wetu huu wa Ruvu unaendelea kuwa efficient zaidi kwa ajili ya wananchi wa Miji ya Dar es Salaam, Kibaha na maeneo mengine. Lakini pia kuangalia sasa upatikanaji wa maji katika Mji wa Mlandizi na viunga vyake ni jambo la msingi sana ili watu hawa waliochagua Chama cha Mapinduzi waendelee kufaidika na uwepo wako Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Pia katika Mradi huo wa Ruvu lipo bomba linalotoka pale kwenye chanzo chetu cha Ruvu linafika mpaka kwenye Ruvu Ranch kwa maana ya pale kwenye mradi wetu ule wa Ruvu. Mheshimiwa Waziri lakini mradi ule ukiutazama kwa sura yake umezungukwa na vijiji vinavyotengeneza Kata ya Vigwaza, vijiji hivi mpaka leo bado vinalalamika kwamba havina maji na vimeendelea kupata maji kutoka Chalinze katika mwendo wa kusuasua. Nashauri kwamba sasa bomba hili tuweze kuwekea zile wanasema „T‟ ili maji yaweze kufika katika vijiji kama vya Kidogonzelo, Vigwaza yenyewe, Milo, huko kote watu waweze kufaidika na mradi huu ili mambo ya kuendelea kukithamini Chama cha Mapinduzi iendelee kufanyika. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, mwisho siyo kwa umuhimu sana ni maji Rufiji. Mheshimiwa Waziri natambua katika kitabu chako cha orodha hii ya miradi hujatuonyesha juu ya mradi huu, natambua kwamba mradi huu unaweza kuwa haupo katika kipindi hiki, lakini wananchi wanaoishi katika vijiji kama vya Ikwiriri, Utete, Mkuranga, Kisarawe na Temeke kwa maana ya upande wa Dar es Salaam wanategemea sana mradi huu ukiweza ku-mature ili mambo yao ya maji yaendelee kuwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika mji kama wa Temeke watu wanakosa maji wakati mwingine kwa sababu maji yao mengi wanategemea kutoka Ruvu na wakati mwingine mradi huu unapozidiwa basi matatizo yanakuwa makubwa sana. Naomba sana Mheshimwia Waziri utakapokuja kujibu at least useme neno juu ya mradi huu ambao ndiyo utakuwa suluhu ya maisha ya watu wa Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na maeneo ya Dar es Salaam kwa ajli ya kupata mahitaji yao makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo wapo wenzetu ambao wanafanya ujenzi wa bwawa la Kidunda. Mheshimwia Waziri ninakushukuru kwa kuonesha kwamba ndani ya bwawa la Kidunda upo mradi wa umeme ambao utafika mpaka Chalinze, pia kama ipo fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya kufikisha umeme Chalinze kwa nini sasa tusianze kufikiria badala ya maji yote kuelekezwa Dar es Saalam basi maji haya yapelekwe Chalinze ili wananchi hwapate nao kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, distance ya kutoka Kidunda panapochimbwa lile bwawa lenyewe mpaka Chalinze Mjini hapazidi kilometa 32 lakini kutoka Kidunda pale mpaka Dar es Salaam tunatarajia kwamba zitafika kilometa zaidi ya 68. Mheshimiwa Waziri ni vizuri ukaangalia kwamba miradi hii iwe inafaidisha pia watu wako, tunakushukuru kwa umeme lakini pia tunaendelea kukushukuru kwa kazi kubwa unayoendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho la kuzungumza japo kuwa nilisema kwamba siyo la mwisho kwa umuhimu lile la Kidunda ni jambo la upatikanaji wa fedha..
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba fedha zifike haraka. Naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kunipa nafasi leo hii ya kuzungumza. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kwa kuapishwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kipindi kirefu sana amekuwa anahangaika na masuala yanayohusu watoto, hasa yatima, wasio na uwezo na akina mama. Nina uhakika kabisa kwa kupata nafasi ya kuwa Mbunge, Mheshimiwa Rais amefanya jambo jema sana kwa makundi haya na sasa watapata mtetezi wa kweli ambaye anayaishi yale atakayokuwa anayaongea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, namwombea pia kwa Mwenyezi Mungu Rais wetu apewe afya njema sana aendelee kuhudumia Taifa hili ambalo linamhitaji sana kipindi hiki kuliko muda mwingine wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, pia namwombea heri mzee wangu, Mzee Chrisant Majiyatanga Mzindakaya ambaye anaugua pale Dar es Salaam, Mwenyezi Mungu ampe afya njema na apone mapema ili aendelee kuwa mshauri katika maisha yetu sisi vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, napenda sana pia niwape pole wananchi wenzangu wa Jimbo la Chalinze na Halmashauri ya Chalinze hasa kwa tatizo kubwa lililotupata ndani ya siku mbili au tatu, kutokana na mvua kubwa ambazo zinanyesha sasa katika maeneo yetu.
Tumeshuhudia barabara zikikatika, tumeshuhudia magari yakisimamishwa, safari zinasimama lakini baya zaidi ni uharibifu mkubwa wa miundombinu na nyumba zetu ambao umetokea katika Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa tu taarifa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba hapa ninaposimama leo hii kuzungumza, zaidi ya kaya 150 hazina mahali pa kulala wala hazijui zitakula nini kutokana na tatizo kubwa la mafuriko lililokumba eneo letu lile. Ninachomwomba yeye pamoja na Serikali ni kuangalia njia za haraka zitakazofanyika hasa katika kile chakula cha msaada ili wananchi wangu wa Halmashauri yetu ya Chalinze wapate chakula kwanza wakati tunajipanga kuona mambo mengine tunayafanya vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia kipekee kabisa, naomba sana wananchi wenzangu wa Jimbo la Chalinze kwamba Mbunge wao niko pamoja nao sana na katika kipindi hiki kigumu mimi baada ya kumaliza kuchangia leo hii, nitarudi tena kukaa nao na kushauriana nao. Pia tumeomba tukutane kama Madiwani kupitia Kamati yetu ya Fedha ili tuweze kuona tunaweza kuchanga kipi au kutoa kipi katika Halmashauri yetu ili kukabiliana na hali hiyo ngumu
ambayo wananchi wenzangu wanaikabili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa nirudi katika mchango wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na nitapenda nianze na eneo la maji na viwanda. Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunatambua kwamba Serikali yetu imeweka msisitizo mkubwa sana katika kuhakikisha kwamba viwanda vinajengwa katika eneo hili la Tanzania na katika kipindi hiki kifupi tumeshuhudia mabadiliko makubwa sana katika ujenzi wa viwanda. Waziri Mkuu mwenyewe anaweza kuwa shahidi na Serikali inaweza kuwa shahidi juu ya jinsi wananchi wa Jimbo la Chalinze au wananchi wa Halmashauri ya Chalinze walivyotoa maeneo yao kwa ajili ya kujenga viwanda. Viwanda takriban sita vikubwa vimekwishaanza ujenzi ndani ya Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na viwanda hivyo vinavyojengwa, tatizo kubwa sana lililokuwepo ni upatikanaji wa maji. Tulizungumza na hata juzi alipokuja Waziri Mkuu kufanya ziara katika Halmashauri yetu, aliona juu ya shida kubwa ambayo wananchi wanavyokabiliana na maji lakini pili alipata taarifa ya kina juu ya viwanda vile ambavyo vinaweza vikashindwa kuanza kutokana na matatizo ya maji. Tumezungumza mengi, lakini kubwa zaidi tulimwomba Waziri Mkuu kupitia Wizara ya Maji atoe kibali kwa wale wawekezaji wanaojenga kiwanda kikubwa cha tiles pale Pingo ili waweze kupata access ya kutumia maji ya Ruvu na siyo maji
ya Wami ili waweze kujenga kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa maji Ruvu mpaka kwenye kiwanda pale Pingo ni kilometa zisizopungua 16; lakini kutoa maji Wami mpaka Pingo ni kilometa zaidi ya 26. Tunachoangalia hapa ni upatikanaji rahisi wa maji hayo na ninashukuru kwamba Waziri Mkuu alinikubalia. Nimeona niseme hapa leo kwa sababu hii ni mikakati ambayo ikiingizwa kwenye bajeti itakaa vizuri. Tunachosubiri kutoka kwake ni kusikia neno kwamba kibali kile kimetoka na kwamba ujenzi wa miundombinu hiyo umeanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hili tu, maji haya yatasaidia pia hata wananchi wa Mji wa Chalinze kwa namna moja au nyingine kwa sababu makubaliano yetu siyo tu maji yaende kwenye kiwanda, lakini pia yaende mpaka pale Chalinze Mjini ili kupunguza tatizo la maji tunalokabiliana nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia, kiwanda kikubwa kingine kinachojengwa kule Mboga cha kuchakata matunda nacho kinahitaji maji. Tumezungumza na Mheshimiwa Waziri Mwijage, tunamshukuru kwa jinsi alivyo tayari kukabiliana na changamoto hiyo, lakini pia kinachohitajika zaidi ni ule Mradi wa Maji wa Wami ukamilike mapema ili maji yapate kupelekwa pale na wananchi wa Chalinze wapate kazi, wananchi wa Tanzania wapate matunda kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi hiki cha miaka mitano hii inayoanza mwaka 2015 mpaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nije katika jambo la vita ya dawa ya kulevya. Katika vita ya dawa za kulevya tunashuhudia mamlaka mbili zenye nguvu tofauti zikifanya kazi moja. Mimi ni mwanasheria, katika utafiti wangu au ujuzi wangu wa sheria, haiwezekani kazi moja ikafanywa na vyombo viwili na ndiyo maana katika mgawanyiko wa kazi hizi, mambo yanagawanyika kutokana na mihimili na kutokana na ofisi. Leo hii tunashuhudia, wako watu wanaitwa na Bwana Siro lakini pia wako watu wanaoitwa na Bwana Sianga. Matokeo yake sasa haieleweki, kumekuwa na double standards katika treatment ya watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba kwa kuwa natambua Sheria ya Dawa za Kulevya inayompa nguvu Bwana Sianga ya kuita, kukamata na kufanya inspection, hiyo sheria pia inaingiliwa na Jeshi la Polisi. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atakaposimama hapa awaeleze
ni jinsi gani vyombo hivi viwili vinaweza vikatenganisha utendaji ili kutoharibu mlolongo mzima wa upelelezi na upatikanaji wa watuhumiwa hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja kule kwetu na akaenda katika mbuga yetu ya Saadani, ameona jinsi mambo yanavyokwenda na ameona hali ilivyo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati anakuja kufanya majumuisho ya hotuba yake azungumzie vizuri juu ya jinsi gani tunaweza ku-promote utalii katika mbuga yetu ya Saadani, lakini pia azungumzie ni jinsi gani Serikai imeweza kukabiliana na vile vilio vya wananchi wanaozunguka mbuga yetu ya Saadani juu ya matatizo ya migogoro ya mipaka iliyopo baina ya mbuga yetu na makazi au vijiji vilivyo jirani hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilio vimekuwa vikubwa sana, vimefika kwenye Ofisi ya Mbunge, lakini pia vimefika kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Mkuu mwenyewe ameshuhudia watu wakigaragara kumzuia asitoke katika mbuga ya Saadani kwa sababu ya taabu kubwa wanayoipata hasa wenzetu hawa wanaosimamia mbuga wanapoamua kuchukua sheria katika mikono yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia, niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua kubwa anazozifanya. Sisi tulikutana naye, niliongea naye na baada ya kuzungumza naye, siku tatu baadaye akaja Waziri Mkuu kuzungumza juu ya kero ambazo zinawakabili
wananchi wa Chalinze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba yangu na kwa niaba ya wananchi wa Chalinze, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi alivyomwepesi kukabiliana na changamoto. Katika wepesi huo, naomba niishauri Serikali malalamiko mengine ambayo yanahitaji majawabu kama siyo majibu ya haraka ili kuondoa hizi sintofahamu walizonazo wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, hakuna sababu ya mtu kama Mheshimiwa Waziri Mwigulu kuendelea kukaa kimya wakati wananchi wanalalamika juu ya hali ya kiusalama katika maisha yao. Mimi binafsi naishauri Serikali yangu kwamba unapojibu jambo lolote lile unatoa hali ya wasiwasi na wananchi wanapata… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami uniruhusu pia niwashukuru sana wenzangu kwa kunipa pole pale nilipofiwa. Pamoja na hilo nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na hata leo naendelea kufunga katika kutimiza ibada ambayo anaisimamia yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianzie pale ambapo ameishia mjomba wangu kutoka Morogoro katika jambo la Ofisi ya CAG. Ni kweli yamesemwa mengi juu ya CAG kwamba zile fedha kwa ajili ya ukaguzi zinachelewa na ushauri mzuri umetolewa, lakini nataka nizungumzie sana kwenye hili suala la Internal Auditors.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Internal Auditors hawawezi kufanya kazi bila maelekezo ya Ofisi ya Mkurugenzi, tukumbuke kwamba huyu anaenda kukaguliwa ndio huyo huyo ambaye anatoa hiyo ruksa kwa ajili ya kukagua hizo fedha. Nataka niseme, kama utaratibu huu utaendelea haya anayoyasema Mheshimiwa Mbunge hapa kwamba unakwenda kuomba OC kwa ajili ya kufanya ukaguzi unaambiwa OC hakuna basi ndivyo ambavyo itakuwa inafanyika kila muda ambapo tunataka ukaguzi ufanyike, lakini kwa nini wanafanya hivyo? Maeneo mengi yanafanyika kwa sababu ofisi za Wakurugenzi na Watendaji wengine wamekuwa wabadhirifu na kwamba wanatumia mgongo wa kutokupatikana kwa OC ili kuficha makosa yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachopenda kupendekeza kwa Serikali yangu, sasa Ofisi ya Internal Auditor iondolewe katika Halmashauri zetu, ziwe moja kwa moja zina mahusiano na Ofisi ya CAG Makao Makuu ili kiasi kwamba wanapokwenda kukagua vitabu basi wawe wanakagua kwa mujibu wa taratibu na authority ambayo wanakuwa nayo kutoka kwenye Ofisi Kuu ya CAG, lakini kuendelea kuziacha hizi ndani ya Halmashauri ni kuendelea kutwanga maji ndani ya kinu na hatuwezi kupata unga tunaoutarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nishukuru sana kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Serikali yangu katika kuhakikisha kwamba inaendelea kuweka fedha nyingi katika maeneo ya kilimo. Nimesoma kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri juu ya jitihada kubwa zilizofanyika kupitia Benki ya Kilimo na jinsi ambavyo wameweza kuwafikia watu wengi. Pamoja na hilo, ushauri kwa Serikali yangu ni kuendelea kuangalia maeneo ya kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika mwaka uliopita tumeshuhudia katika taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kwamba katika mazao ambayo yameiletea fedha nyingi nchi yetu ni pamoja na zao la korosho, pia zao la pamba. Kwangu katika kitabu hiki niliposoma hasa katika eneo la jinsi ambavyo Serikali imeenda kusaidia wakulima, katika kuwapa elimu, fedha katika vikundi mbalimbali kwa ajili ya kujiendeleza, maeneo hayo mawili makubwa sijayaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze juu ya mkakati wake alionao sasa wa kuangalia jinsi gani anawezesha maeneo haya au wakulima hawa waweze kufaidika. Kwa mfano tumeona wenzetu Morogoro hasa katika eneo lile la kilimo cha mpunga kule Kilombero wameweza kufaidika na mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia akumbuke tunalo Bonde kubwa sana la Ruvu ambalo lina accommodate chakula ambacho kinauzwa katika eneo kubwa la Dar es Salaam. Hata hivyo, leo hii tulivyo pale, wakulima wale na vikundi vile vya wakulima havina jinsi wanavyoweza kutunisha mifugo yao. Ninachomwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuelezea kwenye eneo la kilimo basi pia aeleze na matumaini mapya ya wakulima hasa wa Bonde la Ruvu na Bonde la Wami jinsi gani wanaweza wakafaidika na fursa hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nimkumbushe Mheshimiwa Waziri jambo moja zuri. Mwaka 2009 Wananchi wa Kijiji cha Msata, Kata ya Msata, walitoa eneo lao wakawapa Chuo cha Usimamizi wa Fedha – IFM, mambo ya ajabu yakaanzia hapo. Mwaka 2013 baada ya makelele mengi sana Chuo cha Usimamizi wa Fedha wakalipa fedha kwa ajili ya uendelezaji wa eneo lile, lakini toka mwaka 2013 mpaka leo, hakuna jambo lolote lililofanyika katika eneo lile! Mji wa Msata umeendelea kukua na wananchi ambao walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kufanya maendeleo wakipata support na chuo kile, wakaanza kukata tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiona kama Mbunge wao ndani ya Kitabu cha Hotuba ni maneno ya kwamba, sasa ndio mnajipanga katika mpango mkakati wa kuanza kuchora ramani ya eneo lile. Mheshimiwa Waziri binafsi nikwambie kuchoshwa kwa wananchi wangu kusubiri hicho, lakini pia kuchoshwa kwa Chama cha Mapinduzi kwa ahadi ambazo zinaonekana kwamba, hazitekelezeki. Ninachomwomba Mheshimiwa Waziri kabla wananachi wale wa Msata hawajakikataa Chama chake kilichompa nafasi yeye kuwa Waziri wa Fedha, hebu aje na majibu mazuri ya kimkakati juu ya jinsi gani amejiandaa kuweka fedha kujenga majengo yale na maendeleo ya wananchi kuendelea kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu Mheshimiwa Waziri, ni ushauri juu ya mwenendo wa fedha katika Serikali yangu. Mheshimiwa Waziri tumeona katika lugha zinazosemwa kwa yeye na Serikali yangu, mara nyingi lugha inapozungumzwa ya maendeleo ni lugha ya kodi. Wameeleza wengi waliotangulia kwamba, watu sasa wamefikia sehemu wanafunga biashara wanapowaona Maafisa wa TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo mimi kwa usomi wangu mdogo natambua kwamba, ziko means nyingi sana za kuweza kujipatia fedha, mojawapo kuna vitu vinaitwa Municipal Bond, kuna vitu vinaitwa Infrastructure Bond, leo hii tunahangaikaje kuwaminya Watanzania maskini na wanaendelea kuumia wakati tunazo njia ambazo yeye kama msomi wa mipango anazijua vizuri na anaweza kuzisimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hatuoni sababu kwa nini miradi mikubwa kwa mfano kama hii ya Bwawa la Kidunda ambayo nategemea kwamba, ndio litatuletea maji na nguvu ya umeme katika maeneo yetu ya Dar-es-Salaam, Mkoa wa Pwani na maeneo mengine ya Tanzania, tunaendelea kukusanya hela kupitia nguvu za wanyonge wakati tunaweza kutengeneza taratibu ambazo zinaweza zikatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, katika maeneo mengi panapotokea matatizo ya kiuchumi Benki za Kimaendeleo zimekuwa ndio kimbilio. Tumeshuhudia wakifanya hivyo Wajerumani, tumeshudia wakifanya hivyo Wajapani, lakini tumeshuhudia pia nchi mbalimbali ikiwemo Marekani jinsi ambavyo wameweza kupitia vyanzo mbalimbali na kuweza kukusanya pesa na kuweza kusaidia miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo njia ambayo kiuchumi au kifedha wanaita reveragies, ambazo benki inaweza ika-raise hela mara tano ya kile kiwango ambacho kinatakiwa ili kusaidia kunyanyua kiwango cha pesa kuweza ku-finance miradi mikubwa. Mheshimiwa Waziri ni kwa nini mpaka leo hii Wizara yake imeendelea kumshauri Rais wangu, imeendelea kuwaumiza Watanzania kupitia mianya ya kodi wakati tunazo njia kupitia reveragies ambazo zinaweza zikawasaidia kupata hela nyingi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama atuambie Watanzania, amejipangaje kuweza kusaidia kunyanyua fedha kwa ajili ya kusaidia miradi mikubwa ya Serikali, lakini pia kupunguza huu ugumu na machungu kwa wananchi wetu. Maana tunatambua tunayo Benki kama TIB, tunayo Benki kama TADB, hizi zote kama zitawezeshwa kupitia fursa hizi za ku-raise hela ambazo zinaweza zikasadia kupunguza makali kwa wananchi wetu nina hakika kabisa yale malengo mazuri tuliyoahidi katika ilani tutaweza kuyafanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo Mheshimiwa Waziri nimpongeze tena yeye anavyoendelea kukamilisha na kusimamia shughuli mbalimbali za Wizara, malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa katika kuangalia kwamba, huku Serikalini wanajidai, wanatamba kwamba, uchumi unaendelea vizuri wakati maendeleo katika mifuko ya wananchi yameendelea kuwa mabaya zaidi. Mheshimiwa Waziri namwomba sana tafsiri ya maendeleo, tafsiri ya uchumi, tafsiri ya maisha yaliyo bora kwa Watanzania ni maendeleo yanayofanana na hali halisi ya maisha wanayoishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono sana mipango hii, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri atambue kwamba, huko mtaani maisha ya wananchi ni magumu na malalamiko ni mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kuniona. Kutokana na muda nianze moja kwa moja na ku-declare interest kwamba mimi ni mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo. Katika mijadala yetu ndani ya Kamati, ndiyo maana nimekaa upande huu ili niwaone vizuri Mawaziri kwa hili jambo ninalotaka kulisema ni kwamba Mawaziri wangu na Idara ya Uandishi wa Sheria Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe kuna tatizo. Sheria nyingi zinakuja haziko tayari na reference zinazofanyika siyo sahihi. Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta reference ya Sheria ya Mifugo lakini ukirudi kwenye Sheria Mama unaona ni Sheria Inayozuia Vyombo Vinavyokwenda Mwendokasi. Sasa hili si jambo zuri na wewe ni mwalimu wangu na mimi nakuheshimu sana. Hili jambo napenda kidogo tuwe makini, kwa sababu sheria hizi zinaweza kuwa katika karatasi lakini unapokwenda kuzifanyia kazi ndipo matatizo yanapoanza. Sasa tungependa jambo hili nalo tuliweke vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nieleze masikitiko yangu niliposikia wakati Mheshimiwa Adadi anatoa ripoti yake kwamba nchi yetu haina Sera ya Ulinzi. Hili ni jambo la kusikitisha. Nchi yetu ni moja ya nchi ambayo inasifika sana kwa maana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko mstari wa mbele, tuna jeshi ambalo limekuwa credited kwamba ni moja ya majeshi 10 bora duniani sasa.
Kama tena jeshi letu zuri, lenye sifa, lakini sera ya ulinzi haipo tayari, tunaweza tukaingia katika matatizo makubwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana katika jambo hili, mara kwa mara tumekuwa tunalalmika sisi Wabunge hasa mimi binafsi nikieleza juu ya matatizo yanayotokea katika eneo la Kibindu, Mvomero, Kwekonje na Kimange kwamba watu wanauana lakini majeshi yetu hayachukui hatua. Tusije kufikia sehemu tukaamini kwamba kumbe kwa sababu ya kukosekana kwa sera zinazotoa uelekeo wa jinsi ya kujipanga vizuri juu ya ulinzi ndiyo maana wananchi wangu wa Halmashauri na Jimbo la Chalinze wanaendelea kufa kwa sababu hakuna hatua zozote ambazo zinachukuliwa. Naomba sana jambo hili Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ilifanyie kazi ili sera hii ije mapema iwezekanavyo ili tuweze kupanga nchi yetu vizuri kwa faida ya leo, kesho na kesho kutwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyeiti, pamoja na hilo napenda nizungumzie suala la madeni kwenye vyombo vyetu. Nimesoma kwenye taarifa na nimesikiliza Mheshimiwa Adadi akiwa anatoa taarifa yake, vyombo vyetu vinadaiwa sana. Hebu sasa Serikali tujipange tumalize madeni haya kwa sababu itafika sehemu vyombo vyetu vitakuwa havikopesheki wala kupatiwa vifaa vya kisasa kwa sababu ya uzito wa kulipwa kwa madeni hayo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Mkuchika, Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Maadili kwa taarifa yake nzuri ambayo imeeleza jinsi walivyojadili masuala mbalimbali yaliyoifikia Kamati. Hata hivyo, jambo moja ambalo napenda niwaeleze wenzangu na hasa Mwenyekiti wetu ni kwamba mimi walionifundisha maisha walinifundisha kujiheshimu kwanza kabla wenzako hawajakuheshimu. Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya hivyo ama tusipokuwa na philosophy ya namna hiyo kila siku kazi yetu itakuwa ni kupigishana makelele kama ambavyo unaona leo hii Wabunge wanasema ya kwao, huko Serikali inasema ya kwake, kunaonekana kama kuna mgogoro baina ya makundi haya mawili jambo ambalo linahatarisha hata usalama wa Taifa letu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uliniambia unanipa dakika tano nisingependa kuzama sana kwenye mambo mengine niwaachie wenzangu nao waendelee kuchangia. Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kukushukuru wewe kwa jinsi unavyoongoza Bunge vizuri, lakini pia kwa jinsi unavyotoa matumaini ya kuendelea kulinda nyumba yako hii kwa adabu na heshima kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 nilipata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze. Katika kampeni zangu, katika matembezi yangu ya ndani ya jimbo kwa maana ya ziara, wanachi wa Jimbo la Chalinze walikuwa wanalalamika sana juu ya uwepo wa ajira. Kwa maana walikuwa wanahitaji sana ziweze kupatikana fursa ambazo zinaweza zikawaajiri. Katika Jimbo la Chalinze kwa kuwa wewe mtani wangu unasimama simama sana Kiwangwa unajua tunazo raw material za kutosha, lakini viwanda hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii miaka miwili baadaye, ninaposimama hapa, furaha kubwa niliyonayo ni kwamba baada ya miezi isiyopungua mitatu kuanzia leo tutawaalikeni Wabunge ninyi wote akiwepo Mheshimiwa Rais wetu kuja kufungua kiwanda kikubwa cha kuchakata matunda katika Halmashauri ya Chalinze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimeanza kusema hivyo? Kwa sababu tunatambua kwamba sera yetu ya kuwa na Tanzania ya viwanda, ndugu zangu Wabunge wenzangu haiwezi kufanikiwa kwa kumwangalia Bwana Mwijage anavyofanya kazi. Nataka niwaambieni ukweli kabisa, Bwana Mwijage, Mheshimiwa Waziri yeye ni sehemu ya kusukuma mambo hayo; kama ninyi Wabunge hamtokuwa wajanja kutumia mazingira yenu, kutumia mazingira ya maeneo tuliyonayo na kuyageuza yawe fursa, ili Serikali ije kutusaidia kuhakikisha kwamba mambo yake tunayoyataka sisi na wananchi wetu yanafanikiwa; hii sera ya viwanda itakuwa ni sera ambayo hatuiishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Chalinze kwetu sisi tuna fursa kubwa sana, mojawapo ni kuwa na logistic center, lakini logistic center ambayo siyo tu kwamba itakuwa inakuja ni kama sehemu ya kufanyia biashara ya kubadilishana vitu, pia sehemu ambayo watu watakuwa wanapitishia mizigo, na fursa mbalimbali. Wanachalinze wametenga maeneo, Mheshimiwa Waziri Mwijage akishirikiana na watalaam wake katika Wizara yake nimshukuru sana, ametupa ushirikaino mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba yale mawazo ambayo siku zote tumekuwa tunayalilia wanachalinze yanafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninaposimama hapa logistic center ya Chalinze inawezekana. Kiwanda kikubwa cha tiles kimeshafunguliwa na sasa ujenzi unaendelea vizuri, lakini sio hilo tu kama nilivyosema kwamba sehemu kubwa ya kufanya biashara kwa kingereza sijui wanaitaje maana yake kwa Kikwere tunasema makutano ya biashara. Logistic center ndio mnavyoita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mama Nagu ameongea logistic center kwa Kimbulu wanavyoita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanaweza kufanikiwa kwa sababu Serikali yetu inatuunga mkono katika hilo na mimi binafsi bila hata ya aibu niishukuru sana Serikali, kwa sababu kilio cha Wanachalinze kinaweza kupatiwa jibu. Mheshimiwa Lukuvi nimshukuru pia maana kulikuwa na figisu pia pale la upatikanaji wa ardhi, lakini pia kodi kubwa za ardhi. lakini ule utaratibu wa kurasimisha ardhi, toka kwenye mamlaka ya kijiji ili sasa itoke iende kuwa sehemu tengefu kwa ajili ya viwanda nalo pia linawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu ninao ushuhuda huo. Pamoja na hayo pia ziko changamoto ambazo Serikali yetu ni lazima iziangalie tunapokwenda kutimiza yale malengo ambayo tumejipangia ya kuwa na Serikali ya viwanda au kuwa na Tanzania ya viwanda. Kwa mfano moja ya tatizo kubwa ambalo Wabunge wengi wamelalamikia hapa ni jambo zima la upatikanaji wa nguvu ya nishati, kwa maana ya umeme. Tumeshuhudia kwa mfano wenzetu hasa kule kwa wajomba zangu Lindi na Mtwara wanalalamika kwamba umeme unatoka kwa siku masaa manne manne, wanasema kila baada ya dakika 20 kama sio dakika 80 umeme unakatika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tanzania tunayoitaka ya viwanda, moja ya jambo kubwa ambalo lazima tujihakikishie hapa na kama hili hatutakuwa na hakika nalo hii sera ya viwanda itakuwa ni hadithi isiyokuwa na mwisho, au hadithi isiyokuwa na majibu kama umeme wa kutosha wa uhakika hautopatikana katika Tanzania. Mheshimiwa Waziri Muhongo alitueleza kwamba katika upande wa gesi, bado michakato ya kuendelea kusambaza gesi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia wametuambia kwamba gesi itakuja hadi huku Dodoma, lakini pamoja na hayo yale maeneo ambayo yamekwishaanza shughuli za viwanda, ni lazima yapewe kipaumbele ili kuhakikisha kwamba sera ile inatimia kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mheshimiwa Hawa Ghasia Mbunge wa kule Mtwara ameeleza hapa, juu ya jinsi ambavyo mahitaji ya gesi na umeme yanatakiwa kule Mtwara. Pia Mheshimiwa Mwijage wewe mwenyewe umekuja umeona, kiwanda kile mzee, cha kilometa moja, kiwanda ambacho kitakuwa na line of processing mbili, kama hakuna umeme pale itakuwa ni kazi bure na ndoto zako ambazo kila siku umekaa unapiga kelele mpaka wengine ndugu zako akina Nkamia hapa hawaamini, kwa sababu wanaona ni kama hadithi hivi hazitofanikiwa. Kaa vizuri na Mheshimiwa Waziri Muhongo, zungumzeni jambo la sera ya umeme, zungumzeni tuone mambo siyo kwamba yanasemwasemwa tu lakini tuone mambo ambayo yanakwenda sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mnazungumzia kuweka treni ya umeme, Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie mimi mwenyewe ni mshabiki sana wa kupanda vitu hivyo lakini nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri, treni ya umeme hiyo mnayoizungumza na consumption ya umeme ambayo inatakiwa kwa ajili ya kuendesha chombo hicho na kukatikakatika kwa umeme kunakotokea kila siku sina hakika sana kama tunaweza tukafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba ajira zinapatikana katika maeneo hayo. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kipaumbele cha kwanza katika ajira hizo, mnapokaa na hao wawekezaji waambieni wawape kipaumbele cha kwanza wale wakazi wa maeneo yale. Kwa sababu haiwezekani ikajengwa kiwanda kikubwa kama kile pale Chalinze halafu ajira tukasikia wanatoka vijana Dar es Salaam sijui wapi hili jambo haliwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nitumie nafasi nyingine pia kumwomba sana Mheshimiwa Waziri hebu hii sera ya viwanda isimamie vizuri brother, kwa sababu kama mambo yakienda vizuri katika viwanda, nina uhakika kuna nyanja nyingi sana ambazo zitakuwa zimekaa vizuri. Kwa mfano viwanda vinahitaji maji, sijajua kwa maji haya yanayosuasua ambayo mpaka leo wana Chalinze bado hawajaelewa tutafikia lini ule mtandao wa maji ukaweza kusaidia watu wote sina uhakika sana Mheshimiwa Waziri kama tutafanikiwa pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo mashirikiano baina yako wewe, baina ya Wizara nyingine ambazo ni wadau katika lile ni lazima tuyaimarishe ili tuweze kwenda sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS. MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nami ninaomba awali ya yote naomba nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya njema. Kwa kipekee kabisa nikushukuru wewe kwa jinsi ambavyo unaongoza Bunge letu hili, lakini kwa kweli pamoja na wote wanaokusaidia ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, na Wenyeviti wetu, kwa hakika tunaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie heri ili mambo yaendelee kuwa mazuri kama yalivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo niruhusu nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kama ambavyo nilimshukuru siku ya kwanza niliposimama baada ya kupata uteuzi wa kuja kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Ninaendelea tena kumshukuru yeye kwa kuniamini pia naendelea kumwahidi kwamba nitachapa kazi kwa maarifa yangu yote na vipawa vyangu vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niruhusu nimpongeze na kumshukuru sana Comrade wangu Waziri wangu Mheshimiwa George Simbachawene, Mbunge, kwa ushirikiano mzuri anaonipa mimi na wenzangu wote ndani ya wizara lakini kwa hakika uongozi wake, miongozo yake na michango yake kwa kweli inatufanya sisi ndani ya wizara kwenda katika direction nzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa kipekee kabisa niruhusu niwashukuru sana Makatibu wangu Wakuu wawili na Naibu Katibu Mkuu mmoja; hapa nakusudia kuzungumzia Ndugu Maendeka wa Katibu Mkuu Ikulu na Ndugu Juma Mkomi Katibu Mkuu Utumishi wa Umma na Ndugu Xavier Daudi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara yetu. Kwa hakika ushirikiano wao umekuwa ni nguzo ya mafanikio katika Wizara yetu.

Mheshimiwa Spika, sio mwisho kwa umuhimu niruhusu nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mke wangu Mama Aziza na watoto wangu wote. Kwa hakika upendo wao na kunivumilia kwao nikiwa nachapa kazi za umma ndio jambo moja ambalo linanisukuma kwenda mbele zaidi, pia bila kuwasahau wananchi wa Jimbo la Chalinze kwa ushirikiano wao mkubwa ambao wananipa. Nataka niwahakikishie kwamba Mbunge wao nipo kazini na sijawasahau naendelea kuchapa kazi nikiendelea kuwapa heshima wana-Chalinze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba uniruhusu niingie kwenye hoja ambazo zimetajwa au zimeelezwa na Wabunge. Kwa kipekee kabisa nianze na hoja ambazo zimeelezwa na Kamati yako ya Bunge inayosimamia Wizara yetu.

Mheshimiwa Spika, katika moja ya hoja ambayo imeelezwa na kamati lakini pia na michango ya Wabunge ni hoja inayohusu eneo la TASAF. Ni hakika na ukweli kabisa maneno yote mazuri, michango yote mizuri iliyotolewa na Wabunge sisi kama Wizara kwanza nataka niwahakikishie Wabunge tunayachukua. Kwa sababu katika maelezo waliyoyatoa Waheshimiwa Wabunge yako baadhi ya maeneo ni kweli kwamba Wizara inakiri yanatakiwa yafanyike marekebisho, lakini pia yako baadhi ya maeneo wizara inakiri kwamba huenda kuna tatizo la taarifa au uaminifu wa watu wetu ambao tunawatuma kwenda kufanya kazi. Kwa hiyo nataka niwahakikishie Bunge lako, kwamba sisi kama Wizara yale maeneo yenye mapungufu tunakwenda kuyafanyia kazi pia yale maeneo ambayo yanatakiwa yaendelee kusisitizwa ni lazima tuendelee kuyafanya.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, liko eneo la utambuzi ambalo limelalamikiwa sana na mimi binafsi yangu nimshukuru sana Mheshimiwa Aida Khenani ambaye alichokoza hoja asubuhi wakati wa maswali ya msingi ndani ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo hili limekuwa na changamoto, lakini Serikali yako imekuwa kila mara inafanya utaratibu wa kuhakikisha kwamba jambo hili linabadilika au linaboreka ili kuweza kuhakikisha wafaidika wa TASAF wanapata faida ya mradi huu. Katika miaka hii ya karibuni nataka nilihakikishie Bunge lako na nitoe taarifa kwamba Serikali imekuja na utaratibu wa kuelekeza Serikali zetu za Vijiji kuhakikisha kwamba mikutano ya vijiji inawakusanya watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesikia yapo baadhi ya malalamiko juu ya siasa kuingizwa katika taratibu hizi. Nataka niwahakikishie Wabunge na hasa kwako, sisi kama Wizara tunalibeba hili jambo la mwingiliano au mgongano wa maslahi ya kisiasa na tutakwenda kulifanyia kazi ili kuondoa vilio vya Bunge lako. Pamoja na hilo pia baadhi ya Wabunge wamezungumza juu ya malipo madogo ya wafaidikaji wa TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie wananchi hawa kwamba, Serikali imefanya juhudi kubwa sana. Mwaka 2022 wakati tulipoanza mchakato wa mjadala wa kupitia tena mafanikio ya TASAF, hili jambo lilionekana na tulifanikiwa kupeleka ile pesa wanaolipwa wafaidikaji mpaka Sh.3,000, lakini ni kweli hali za maisha zimebadilika na hitajio la kuongeza linafanyika. Sasa ninapozungumza mchakato wa kujadili taarifa na kuthamini utekelezaji wa Mradi wa TASAF, awamu ya tatu, kipande cha pili unaendelea.

Mheshimiwa Spika, tutakapofanikiwa kumaliza uchambuzi huo, nataka nilihakikishie Bunge lako na Watanzania na wafaidikaji wa TASAF kwamba changamoto kama hizi ambazo zinaonekana ni moja ya jambo ambalo tunakwenda kulishughulikia na tutakuja kuleta mrejesho hapa ili wananchi na Wabunge wapate kuelewa kwamba Serikali yao ni sikivu na Mheshimiwa Rais, anaendelea kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka vilevile niwatoe wasiwasi ndugu zangu Watanzania, Mradi wa TASAF huu kwa kutegemea pesa zetu za ndani, siyo rahisi kuweza kuwafikia watu wote. Nchi yetu haiishi katika kisiwa, nchi yetu inashirikiana na nchi mbalimbali, wahisani mbalimbali ili kuhakikisha kwamba programu za maendeleo ya nchi na watu wake zinakwenda mbele. Hivyo, hawa watu wote au wadau wote tuliyowataja katika taarifa yetu ya mwanzo ni wazi kwamba wanatusaidia sana Watanzania ili tuweze kufikia miradi vizuri.

Mheshimiwa Spika, katika kufanya hilo, moja ya mafanikio makubwa tuliyoyapata ni sasa Mradi wa TASAF umeweza kufikia kaya zisizopungua 2,300 ambayo ndani yake ina wafaidikaji wasiopungua 5,200,000 ambao wao ni Watanzania wenye uhitaji ambao Serikali yao inaendelea kuwaangalia.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie kwamba, changamoto nyingine zote ikiwepo changamoto ya NIDA tutaendelea kuifanyia kazi na sisi tunaendelea na mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Idara husika inayohusika na Vitambulisho vya Taifa ili kuweza kuwafikia wananchi ilimradi waweze kufaidika na programu hii ya TASAF. Kwa wale ambao hawana vitambulisho vya NIDA, maelekezo yamekwishatolewa kwamba waende kwa sababu utambuzi wa kwanza ni katika ngazi yao ya kijiji tutawatambua na kuwaingiza katika mfumo ili waweze kuendelea kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia limezungumzwa jambo la ajira katika maeneo ya vyuo vikuu, aliyezungumza ni Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na nataka nikiri mbele ya Bunge lako kwamba, maelezo aliyotoa Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo yana ukweli kabisa, nini kimefanyika na nini kimetufikisha hapo, kwa muda nisingependa nirudi huko, lakini Serikali ilishakutana na Uongozi wa Vyuo Vikuu vya Umma wakiongozwa na Dean wao ambaye ni Vice Chancellor wa Chuo cha Ardhi kilichopo Dar es Salaam. Mazungumzo yamefanyika nimwombe Mheshimiwa Kitila Mkumbo na wenzake katika eneo la chuo kikuu watupe nafasi Serikali tupate kuangalia, nini zilikuwa sababu za kufika hapa tulipofika na nini kifanyike ili tuweze kuondoka hapa tulipofika twende mbele kwa kasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie na Bunge lako kwamba si nia ya Serikali kuchukua mamlaka ya vyuo vikuu na kuyafanya ya kwake, lakini zipo kada mbalimbali, zipo kada za administrations au eneo la kiutawala, lakini pia zipo kada za Walimu au kwa maana ya Wakufunzi wetu. Kada hizi mbili treatment zake ni tofauti ndugu Watanzania. Kada ya Administrations imeendelea kubaki chini ya utumishi, lakini pia kada ya wale wenzetu ambao ni wakufunzi imeendelea kuratibiwa katika jicho la mbali, lakini mambo yote yanaendelea kufanyika ndani ya vyuo vikuu vyenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko jambo limezungumzwa na walio wengi juu ya malipo ya madai ya malimbikizo ya mishahara. Ni kweli zipo kazi na juhudi kubwa ambazo Mheshimiwa Rais wetu anazifanya katika kipindi cha miaka miwili zaidi ya Shilingi Bilioni 2.4 zimelipwa kwa wale ambao walikuwa wanadai malimbikizo. Hata hivyo ni kweli kama walivyosema, kwenye Taarifa ya CAG inaonyesha kwamba bado ile ada ya malipo imeendelea kupanda juu. Nataka nilihakikishie Bunge lako, katika kipindi cha miaka miwili Mheshimiwa Rais, ameweza kulipa nusu ya yale ambayo anayodaiwa.

Mheshimiwa Spika, lingine kubwa, nataka niliambie Bunge lako, Serikali hii imechaguliwa kawa kipindi cha miaka mitano. Tumpe nafasi Mheshimiwa Rais aweze kufanya, kama ndani ya miaka miwili ameweza kulipa nusu ya madeni yanayodaiwa, iweje ashindwe katika miaka mitatu iliyobakia! Nataka niwahakikishie kuwa, tunaye Rais ambaye anawapenda na kuwajali watumishi wa umma, tunaye Rais ambaye anawapenda na kuwajali Watanzania katika hali zote. Tumpe nafasi Mheshimiwa Rais na sisi wasaidizi wake, nataka niwahakikishie kwamba madeni na malimbikizo yote wanayodai watumishi wa umma katika Tanzania tunakwenda kuyamaliza na kwenda kuyafikia yote katika maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile pamoja na hilo nataka nizungumzie juu ya uwiano wa watumishi wa umma katika vijiji na miji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA. Dakika tatu malizia muda wako, kengele mbili zilishagonga.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kupitia watalam tulionao wa TEHAMA mfumo kwa ajili ya kuchakata na kujua idadi ya watumishi katika maeneo yote ikiwemo mijini na vijijini umekamilika na unafanya kazi. Mfumo huo unatambulika kama HR Assessment, mfumo huu unawezesha siyo tu Serikali lakini pia hata Serikali za Mitaa kujua idadi ya wafanyakazi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kupitia mfumo huu, inatuwezesha sisi kuweza kupanga pia ikama za wafanyakazi katika maeneo hayo. Nataka niwahakikishie Watanzania na Bunge lako kwamba Serikali imejizatiti kimifumo kuhakikisha kwamba changamoto zote zilizopo katika maeneo haya tunazikabili na kuzitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako mengi ya kuzungumza, lakini naomba kwa ruhusa yako sasa nimkaribishe Mheshimiwa Waziri ili aweze kuendelea hapa palipobakia. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kupongeza sana juhudi zinazofanywa na Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hakika maneno haya hata kama kuna mtu anasema kwake hayajafanyika, lakini Chalinze wanaopita kwenye barabara wameshayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nimeona kwenye TV hapa wawekezaji wangu wamekuja. Ningependa nitambue uwepo wa bwana Jack Feng na ndugu yangu Beda kwa kweli, wananifanya leo hii ninaposimama hapa na ninapotazama kitabu hiki natamba na Mheshimiwa Mwijage anatamba ni kwa sababu yao. Nawashukuruni sana. Kama mnavyoona kwenye TV pale bwana Jack Feng na bwana Beda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mazuri ambayo Serikali yangu imeendelea kufanya, lakini bado zimebakia changamoto na yako maeneo ambayo mimi kwa nafasi yangu kama Mbunge ningependa nitoe ushauri maana maongezi yangu leo yamejikita sana kwenye ushauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, viwanda na maji. Kule kwangu mimi viwanda vyangu vyote ninavyotengeneza vyote vinahitaji maji. Tunapozungumzia viwanda vya vigae, mahitaji ya maji ni makubwa sana, lakini pia, nazungumzia viwanda vya mazao yanayotokana na matunda, mahitaji ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameeleza katika Hotuba yake ya Bajeti juu ya ukubwa wa viwanda hivi na vitu ambavyo vitaendelea kuchukuliwa pale. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri na huu ni ushauri wa dhati kabisa toka moyoni mwangu Wakae na Waziri wa Maji waulizane juu ya jinsi gani lile jambo linalokabili Kiwanda cha Sayona Fruits Processing pale Mboga, watakavyoweza kulimaliza. Mheshimiwa Waziri wa Maji ametoa ahadi alipokuwa anafanya majumuisho ya hotuba yake akisema kwamba jambo hilo tutaliangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua Mheshimiwa Waziri anaweza kwenda mbio sana, hebu ajaribu kukamatana na Mheshimiwa Waziri wa Maji ili tuweze kulifikisha jambo hili pazuri na ile ahadi ya kusema kwamba mwezi wa 10 Mungu akijalia Mheshimiwa Rais aje Chalinze kuja kuzindua kiwanda kile iwezekane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia, tulifanya mazungumzo na wenzetu wa TWYFORD ambao wanaonekana kwenye TV hapo; kwamba kubwa zaidi ambalo wao wanalitaka ni Serikali iwape ruksa ya kuweza kuchukua maji kutoka Mto Ruvu ili waweze kuyavuta mpaka pale kwenye kiwanda chao, lakini pia waweze kutengeneza maji ambayo watayafikisha katika maeneo mengine ya Chalinze.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua Mheshimiwa Waziri ni binadamu sana, najua kwamba katika kuwapa kibali hicho hatowasahau wananchi wa Kata za Vigwaza, Pera pamoja na Bwilingu kwa sababu maji hayo yanayohitajika yakienda kiwandani kama hayatakwenda kwa wananchi huenda tukakuta siku moja mwekezaji analalamika kwamba, maji hayaendi kwa sababu wananchi wametoboa mabomba. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili aliwekee mkakati mzuri ili tuweze kufanikisha haya mambo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo liko jambo la Bandari ya Bagamoyo. Mheshimiwa Waziri nimetazama kitabu chake chote hiki, hakuna sehemu ambayo amezungumzia Bandari ya Bagamoyo na viwanda vinavyotakiwa vijengwe katika Special Economic Zone. Si hilo tu, Mheshimiwa Waziri wakati anatoa pale ambayo mimi naiita summary ya kitabu hiki amejitahidi kuielezea Bagamoyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nimuulize swali Mheshimiwa Waziri niamini yapi, niamini aliyoyasema akiwa pale au niamini ambayo amendika kwenye kitabu hiki? Hili ni jambo ambalo Wanabagamoyo wangependa sana kulijua kwa sababu, uchumi wa maeneo ya Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla wake unategemea sana uwepo wa bandari ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si hilo tu, Mheshimiwa Waziri amezungumza kwamba mwekezaji yuko tayari kwa ajili ya kulipa lile, lakini kwa maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri nabaki na maswali ya kuuliza lini fidia hizo za wananchi wale wa Pande, Mlingotini na maeneo mengine ya Kata ya Kiromo wataweza kulipwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata kama wanataka kulipa ni jinsi gani anakuja kulipa mtu huyo? Kwa sababu fedha hizi ambazo tunazungumza hapa ni fedha za mwekezaji, lakini mwekezaji huyu anapata wapi taarifa juu ya mahitaji ya watu wale? Vile vile anaweza vipi kutambua watu wale kwa sababu niliposikiliza maneno yake naona kama kuna utaratibu wa Serikali kujitoa na kuliacha eneo lile ambalo sisi Wanatanzania tunategemea kwamba, liwe ndio sehemu ya ukombozi mkuu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Waziri amezungumza juu ya mambo mengi ambayo nchi yetu inafanya. Hata hivyo, viwanda hivi vinavyojengwa katika eneo la Chalinze in particular ni viwanda vikubwa sana, lakini mwekezaji wangu, kwa mfano Sayona ambaye anajenga kiwanda kikubwa cha matunda ambapo ndani ya kitabu chake ukurasa wa 23 ameeleza juu ya ukubwa huo, lakini pia ameeleza juu ya umuhimu wa kiwanda hicho, lakini mwekezaji huyu anahangaika mpaka leo kutafuta Strategic Investment Certificate. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajua, kwa wawekezaji ambao watahitaji bidhaa za Tanzania nzima, kwa wawekezaji ambao watatoa ajira zaidi ya watu 29,000, kwa wawekezaji ambao watachukua matunda na watatoa production ya lita zaidi ya milioni mia mbili kwa mwaka, huyu mtu ana kigezo chote cha kupewa Certificate ya Strategic Investment. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake atueleze sisi Wanachalinze na Watanzania kwamba, amejipangaje katika kuhakikisha kwamba, mwekezaji huyu anapewa hiyo Certificate ili mambo yaende vizuri katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini sio mwisho kwa umuhimu, Mheshimiwa Waziri kuna Kiwanda cha Nyama cha Ruvu, kimekufa na hakuna dalili ya kufufuka. Mheshimiwa Waziri anajua wakati kaka yangu, rafiki yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akiwa kwenye Wizara ya Kilimo, nilipata nafasi ya kwenda naye pale kwenye kiwanda akaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hilo tu, Serikali katika kuonesha kwamba, iko tayari kuhakikisha kwamba kiwanda kile kinafufuka ilinunua mashine nzuri kwa ajili ya kuja kufunga ili kiwanda kiweze kufanya kazi, lakini la kushangaza kiwanda kile na mashine zilizopo pale havifanani. Kwa hiyo, kukawa na mapendekezo ya kukipanua lakini mpaka sasa hivi hakuna juhudi zozote wala maelezo yoyote katika Kitabu cha Bajeti cha Mheshimiwa Waziri ambayo yanaeleza juu ya mkakati wake kama Waziri au kama Wizara juu ya kuhakikisha kwamba, kiwanda kile kinafufuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwambie tu Mheshimiwa Waziri, tunapolia vilio vya mifugo katika Jimbo la Chalinze, tunapolia vilio vya mifugo katika Tanzania, jibu lake ni kuwa na viwanda vya kusindika na kuchakata nyama kama hivi ambavyo vinatakiwa vifanye kazi. Mheshimiwa Waziri aisaidie nchi yake, akisaidie chama chako, tunahitaji kuweka utaratibu ulio mzuri ili mambo yaweze kwenda vizuri katika Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, maana sisi Wanasiasa tuna mwisho na mwisho kabisa! Sasa hapa mwisho kabisa, Mheshimiwa Waziri katika uwekezaji lazima kuwe na utayari wa Serikali. Utayari huo nimeuona, lakini nataka niuone kwa vitendo. Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono sana hoja ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba niendelee kama walipoanzia wenzangu kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yetu katika kuhakikisha kwamba matatizo ya maji Chalinze yanafikia mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kupata nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais, tukazungumza naye na kumweleza juu ya tatizo kubwa wanalopata wananchi wangu wa Jimbo la Chalinze. Alimwagiza Waziri Mkuu na Waziri Mkuu alikuja, alipofika katika kile chanzo chetu cha Wami, aliyoyaona, mwenyewe anayajua. Mheshimiwa Waziri alikuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu ninaposimama leo hii, nataka nimkumbushe tu Mheshimiwa Waziri kwamba katika kipindi kile ambacho tulimpa yule Mkandarasi pale, sasa zimebaki wiki mbili na nusu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anasimama, napendelea wananchi wa Chalinze wamsikie, anasemaje juu ya yule Mkandarasi na Wizara inajipangaje sasa kutoa maelekezo mapya baada ya kuonekana kwamba kazi ile inasua sua?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri jambo. Kwenye suala la maji katika Jimbo la Chalinze anajua kwamba, kuna viwanda ambavyo vinaendelea kujengwa sasa, lakini viwanda vile vinaweza kupata matatizo ya kuanza kutokana na kukosekana kwa maji. Mimi kama Mbunge nilifanya initiative za kuzungumza na wawekezaji wenzetu wa Trifod na Bwana Shubash Patel wakakubali kutoa vifaa kwa ajili ya kusaidiana na CHALIWASA chini ya Engineer wetu Christa Msomba ili kuhakikisha kwamba pale kwenye chanzo chetu wakati ninyi Serikali mnajipanga, wao wawekezaji wako tayari kuja kusaidia kuweka miundombinu vizuri. Inaonekana kwa upande wa ma-engineer au Wizarani kumekuwa na utata kidogo katika kutoa ruhusa ya wao kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, uko msemo kule kwetu Pwani wanasema, “anapokuja mgeni, basi mwenyeji ndio anapata nafuu au anapona.” Hawa wawekezaji wanataka kumsaidia kazi ya kuweza kujenga chanzo pale, wakati yeye yuko Bungeni hapa anaomba pesa kwa ajili ya kuweza kujenga miundombinu. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa jicho la karibu sana. Wananchi wa Chalinze hawahitaji siasa, wanataka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, liko jambo la mabwawa. Wananchi wa Chalinze wameahidiwa mabwawa hasa wale wanaotoka katika Kata ya Kibindu. Kuna bwawa tuliahidiwa na Mheshimiwa Waziri Profesa Maghembe kwamba atatujengea bwawa kubwa na wananchi wa Kibindu wataondoka katika taabu kubwa ya maji wanayoikabili. Kule Mjembe walitoa eneo pamoja na wananchi wa Gole, lakini mpaka leo ninapozungumza Mheshimiwa Waziri, hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kitabu cha hotuba ya bajeti hapa, nayo ameelekeza kwamba atajenga mabwawa mengi, lakini cha kusikitisha zaidi bwawa lile la Mjembe Gole limepotea hewani, silioni humu ndani na sijui tunaelekea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri Mheshimiwa Maghembe yuko humu ndani, kwa hiyo, akimwuliza anaweza kumthibitisha hilo na akampa maelekezo ni jinsi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, nitoe ushauri pia katika eneo la mabwawa. Tunaona maji mengi sana yanayopotea, tunaona maji mengi sana ambayo yanaingia baharini ambayo sisi kama Taifa tumeshindwa kuyatumia kwa ajili ya manufaa ya walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Waziri, nimeona humu ndani ametenga fedha kwa ajili ya Bwawa la Kidunda, lakini tunatambua aliwahi kusema mzee wetu mstaafu Alhaj Ali Hassani Mwinyi, Rais wetu aliyemaliza muda wake, kwamba kupanga ni kuchagua. Natambua kwamba katika bajeti hii hajapanga lolote kuhusiana na ujenzi wa mabwawa zaidi ya lile la Kidunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Waziri, yale maji yanayopita pale Ruvu kwenye Kituo chetu kinachozalisha maji kwa ajili ya wanywaji wa Dar es Salaam, yanakwenda yanamwagika baharini; nimeshuhudia juzi nikiwa kwenye ndege wakati nakuja Dodoma, maji mengi yametapakaa katika bonde lile, hata wananchi wa Bagamoyo wanashindwa kwenda mashambani. Jawabu lake ni kutengeneza bwawa lingine ambalo linaweza likazalisha maji mengi na likapeleka maji hata katika maeneo ya Miji kama ya Pangani hata kule Tanga Mjini ambapo wajomba zangu nao wanalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niongee juu ya jambo kubwa la kukatika kwa umeme. Wengi wameyasilimulia hayo, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, ndani ya Halmashauri ya Chalinze, CHALIWASA wananchi wanalipia maji, isipokuwa kuna tatizo kwa upande wa Serikali kupe...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi ningependa kuanza kuunga mkono hoja, kwa sababu kama sikuunga mkono hoja, maana yake mipango hii ambayo tunahubiri hapa haitaweza kufanikiwa.

Pamoja na hilo na mimi nichukue nafasi hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu kwa jinsi anavyofanya kazi kubwa, kazi inayoonekana, na kwamba sisi wengine tunapokwenda misikitini ni kumuombea Mungu tu, ili Mungu aendelee kumtia ujasiri, nguvu na maarifa zaidi katika kuendelea kuwapigania Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu wa leo, kubwa zaidi litakuwa ni ushauri tu, kwa sababu mambo mengi kule yanaendelea kufanyika. Nipende tu kuwaambia taarifa kwamba Wabunge watakaopenda kuungana nami, siku ya tarehe 22 Mheshimiwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli atakuwepo katika eneo la Halmashauri ya Chalinze akifungua viwanda, kuangalia barabara na maendeleo kwa ujumla wake, lakini pia atapata nafasi ya kuongea na Watanzania na kuwajulisha mambo mazuri yanayoendelea katika nchi ya Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge nawakaribisheni sana; na kwa kuwa siku hiyo itakuwa ni siku ambayo Bunge nafikili linakwenda katika break ya sikukuu, kwa hiyo, ni vema mkaja Chalinze ili mpate maneno mazuri ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo nianze katika eneo la uchumi wa viwanda. Mambo mengi yanafanyika, lakini mimi nina ushauri mmoja hasa katika eneo la biashara ya ngozi.

Mheshimiwa Waziri Mwijage anafanya kazi nzuri sana, lakini Mheshimiwa zile chapa zilizoletwa na zinazopigwa ubavuni kwenye mifugo yetu zinafanya ngozi za ng’ombe wetu zinaendelea kupoteza ubora. Na malalamiko yamekuwa mengi sana katika viwanda vya huko nje kiasi kwamba hata tunapohubiri kuweka viwanda ndani tutakabiliana na changamoto ya kwamba bidhaa tunazopeleka nje ziko chini ya kiwango kama kama kinavyotakiwa na hivyo tutakuwa tunakabiliana na changamoto ya kutonunulika kwa bidhaa zinazotoka Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu Wizara iangalie jinsi ya kuja na utaratibu mzuri hata kama ni chapa hiyo hiyo iwekwe, basi iwe chapa ambayo inakaa katika maeneo ambayo hayataweza kufanya athari kubwa katika ngozi za ng’ombe wetu na ubora ukapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia niendelee kuishukuru Serikali imefanya jambo kubwa sana katika kutoa ushuru wa mazao yanayosafirishwa. Hata hivyo, tunapozungumza kuondoa ushuru wa mazao pia tukumbuke kuongeza au kuweka mazingira mazuri ya upataikanaji wa mbolea zilizo nzuri, mbolea zilizo bora ili mazao yanayotoka yawe yenye ubora zaidi. Maana isiwe tu kwamba tunaondoa ushuru wa mazao lakini ule unaobakia nao unakuwa ni sehemu ya mzigo mkubwa kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua yako mapunguzo makubwa hasa katika tani ambazo ziko chini ya tani moja kwa yale mazao yanayotoka mashambani kwenda masokoni. Mimi najua kwamba leo hata kama mimi ninakwenda Mbeya siwezi kwenda Mbeya kuchukua tani moja ya mchele ili wananchi wangu wa Chalinze wakale mchele mzuri wa Mbeya. Kinachofanyika ni kwamba nitakwenda Mbeya nitachukua tani zaidi ya nne ili nizipeleke katika masoko niweze kufanya biashara nzuri. Tutakapofanya majumuisho ningependa mliangalie tena jambo hili la upungufu wa ushuru, ule ambao unaozidi tani moja kwa sababu si kama kweli ile nia nzuri ya kusaidia wakulima wetu mauzo ya mazao yao wanaweza kufanikisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Wizara kwa kuendelea na mkakati wake wa kumalizia na kuendelea kulipa yale mafao ambayo yalikuwa yanatakiwa yalipwe kwa wale ambao wanapisha ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Mheshimiwa Waziri nimeona katika kitabu chako na nimekusikiliza vizuri katika hotuba ya bajeti kubwa, ni kweli kwamba mmedhamilia kufanya jambo hilo. Ninachokuomba Mheshimiwa Waziri baada ya kupitisha bajeti yako jambo hili la Bandari ya Bagamoyo mlifanyie liwe kipaumbele chenu kikubwa. Kwa sababu kama hamtofanya hivyo hii mipango yote mizuri, yale mafao yalishalipwa na mambo mazuri ambayo mmeyapanga hayatoweza kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika eneo la madini. Pamoja na juhudi kubwa ambazo zimeshafanyika, na juhudi kubwa ambazo Mheshimiwa Rais wetu anaendelea kuzifanya, ikiwemo kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata malipo ambayo yamekuwa yakikosekana katika muda wote. Mimi nina jambo dogo la kuomba Serikali yangu, Serikali ifanye haraka kuleta hiyo Sheria ya madini hapa tuifanyie marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kipindi hiko kabla sijakuwa Mbunge iliundwa kamati hapa, kamati ya Mheshimiwa Bomani akiwepo kaka yangu Ezekiel Maige, walikwenda wakafanya uchambuzi na wakaja na mapendekezo, lakini sijui mapendekezo yale yamefikia wapi. Hata leo tunamuona profesa wangu, rafiki yetu Bwana Osoro naye amekuja na mapendekezo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba, tuielekeze Serikali yetu ilete mapema iwezekanavyo sheria hiyo ya madini ili tuweze kuiweka sawa na ili Watanzania wafaidike na kile ambacho tumekuwa tunahisi kwamba kinapotea siku zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko hayo ya Sheria ya Madini yaje pia kutatua tatizo kubwa lililopo sasa hivi; kwamba kila mtu ana pembe, inapofika katika suala la kutoa haki ya matumizi ya ardhi ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takribani miaka miwili nimekuwa nikipiga kelele katika Bunge hili, lakini pia nimezungumza na Mheshimiwa Waziri na maafisa wa wizarani juu ya mgogoro uliopo katika kijiji cha Kinzagu na Makombe pale Chalinze. Unakumbuka niliwahi kusema hapa kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nami niungane na Wajumbe wote au Wabunge wote kumpa salamu za pongezi sana Mheshimiwa Rais wetu Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan mama maendeleo kwa zawadi kubwa au heshima kubwa ambayo imeendelea kutupa nchi kuhakikisha kwamba nchi ya Tanzania imeweza kufahamika katika usimamizi wa miradi lakini pia kwakipekee kabisa juu ya usimamizi wa fedha za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana na kuwapongeza sana Wabunge wote waliochangia katika hoja ambayo imeletwa na Mheshimiwa Waziri wetu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo kwa jumla au kwa rekodi tulizonazo waliochangia kwa mdomo walikuwa watu 27 na waliochangia kwa maandishi ni watu wawili. Binafsi yangu kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri niwashukuru sana Wajumbe wote kwa michango yao mizuri, lakini kabla sijaanza kujibu hoja ambazo zimeelezwa nataka nikuhakikishie na Bunge lako kwamba mawazo yote yaliyotolewa, ushauri wote sisi kama Wizara tunaichukua na tutakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kwamba ardhi yetu au rasilimali ardhi yetu inakuwa salama na wananchi wetu wanaendelea kufaidi matunda ya kuwepo kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika nchi hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutoa majibu haya nitajaribu kujibu kwa jumla. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wajumbe sitatumia nafasi hii kutaja majina ya mmoja mmoja, lakini nadhani katika maelezo moja kati yenu mtakuwa mnajua kwamba hili jambo niliuliza na linatolewa majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika eneo la migogoro ya ardhi; nataka nitoe taarifa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kwamba Serikali imekuwa inafanya hatua nyingi sana za kuhakikisha kwamba migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro baina ya vijiji vyetu, lakini migogoro juu ya matumizi ya ardhi yameendelea kushughulikiwa na katika kufanya hivyo Kamati ya Mawaziri Wanane imeendelea kufanyakazi kama ambavyo imeelezwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia yamefanyika mabadiliko ya sheria, lakini yapo maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais juu ya jinsi gani migogoro hii inakwenda kutatuliwa ili kwa wananchi amani na utulivu vipate kurudi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo tumeendelea kufanya ziara za mara kwa mara; na katika kufanya hivyo migogoro mingi imetatuliwa lakini kwa kipekee kabisa nataka niwahakikishie ndugu wajumbe au Wabunge kwamba migogoro ile ambayo imetajwa katika mjadala wetu kwa mfano ule wa Efatha kule Rukwa, nataka nikuhakikishieni Waheshimiwa Wabunge kwamba kilio chenu, sauti yenu imesikika si tu ndani ya Bunge lakini hata kwa wananchi wetu katika eneo la Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Wizara yalishatolewa juu ya jinsi gani tunaweza tukautatua mgogoro ule lakini pia hatua za kimsingi juu ya utatuzi zilishafanyika lakini tunatambua kama Wizara kwamba zipo kesi ambazo zilifanyika lakini maamuzi yaliyofanyika ya mwisho ya mwaka 2018 ya kugawa maeneo kwaajili ya wananchi haya yanataka twende tukayasimamie ili yaweze kutatua mgogoro huo. Lakini pamoja na hilo nataka niwahakikishieni ndugu wajumbe mliotoa sauti yenu kwamba sisi kama Wizara tutafika baada ya Bunge hili na kubwa zaidi ni kuja kutatua kero hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia limezungumza jambo la Mbarali, nalo pia nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mtenga lakini pia dada yangu Mheshimiwa Bahati kwamba nalo tunalitambua Kamati ya Mawaziri imefika nako tutakwenda ili kwenda kukutana na wananchi tuzungumze ili tujue tunatatuaje si hilo tu pamoja na migogoro mingine yote katika eneo la nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu Wabunge nawashukuruni sana kwa mawazo wenu mazuri juu ya jinsi gani hii Wizara inaweza kuongeza makusanyo ya maduhuli, lakini pia nataka nikuhakikishieni kwamba zipo hatua za msingi ambazo Wizara imekuwa inazichukua kuhakikisha kwamba maduhuli yanakusanywa. Kwa mfano, katika hatua ambazo zimefanyika katika mwaka huu wa fedha ni pamoja na kuendelea na kazi ya kupanga na kupima kwa sababu utakapopanga na kupima maana yake tunakwenda kuzalisha hati ambazo hati zile zinaenda kututolea pesa na makusanyo yanakwenda kuhakikishiwa, lakini pamoja na hilo pia sasa tupo katika utaratibu wa kubadilisha mfumo wetu wa kidijitali ameeleza ndugu Kunambi jana juu ya umuhimu wa kuhakikisha kwamba ule mfumo ILMIS unatandazwa Tanzania nzima na ule mfumo utakapokuwa umetandazwa Tanzania nzima ndiyo tutakwenda kujihakikishia makusanyo yenye uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hilo tu pia ipo mifumo mbalimbali ambayo tunajaribu kui-harmonize pia ikiwa na mifumo mingine ya ukusanyaji wa maduhuli ikiwemo ya TRA, lakini pia kuangalia kama ipo mifumo mingine rafiki ambayo inaweza ikatusaidia katika kuhakikisha kwamba makusanyo yanahakikishiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia nataka kukuhakikishia kwamba tunaendelea kutoa elimu, si tu kwa wataalamu wetu lakini pia kwa wananchi kuelewa umuhimu wa kuwa na hati ili hati hizo zitakapokuwa zinalipiwa basi Serikali yao iendelee kukusanya maduhuli na kufikia malengo makubwa kama ambavyo tumesema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo kupitia wahisani mbalimbali fedha zimeendelea kukusanywa, lakini pia kupitia programu mbalimbali kwa mfano sasa hivi katika kipindi hiki cha Sensa ya Makazi tumeendelea pia kupima na kutambua nyumba zetu ikiwa ni moja ya hatua ya kuhakikisha kwamba tunazimbua nyumba hizo na ili tuweze kukusanya maduhuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwashukuru ndugu wajumbe au ndugu Wabunge kwa mawazo yao mazuri na msukumo walionao kuhakikisha kwamba tuna-harmonize mipaka baina ya nchi yetu na nchi marafiki. Lakini nataka nikuhakikishieni pamoja na mawazo mazuri ipo miongozo toka Umoja wa Mataifa Afrika kwamba mpaka tunafika mwaka 2027 mipaka baina ya nchi zote zinazozungukana iwe imeweka vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie na Bunge lako kwamba Serikali yako chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tunaendelea kufanyakazi kubwa ya kuhakikisha kwamba mipaka yetu inaendelea kuwa salama, lakini timu yetu ya watalaamu inaendelea kufanyakazi na watalaamu wa nchi marafiki au nchi majirani ili kuhakikisha kwamba mambo yote yanakaa vizuri na hivi karibuni ndugu Wabunge mnaweza mkawa mashahidi ujumbe wa watalaamu toka Kenya na Tanzania ulikutana kwa ajili ya kukuhakisha kwamba haya matatizo au changamoto zinazotokea katika eneo la mpaka wetu ikiwemo kule Jasini kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge nalo pia ni moja ya jambo ambalo tunaenda kulitatua. Nataka kuhakikishieni kwamba Serikali imetoa maelekezo na sisi ndani ya Wizara maelekezo hayo tumeendelea kuyasimamia na wataalamu wetu wapo site kuhakikisha kwamba jambo hili linatatulika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamezungumzia juu ya tatizo ambalo Wabunge wanalipata juu ya usalama wa mazingira yetu haya tunayofanyia kazi hasa ukizingatia eneo la Bunge ni dogo, lakini pia usalama wa maisha yetu hasa tunapovuka barabara na matumizi ya vyombo vyetu tunapotoka Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba jambo hili linakaa vizuri Ofisi yako ya Bunge iliandikia Ofisi yetu na mbele ya Bunge hili nikiri kwamba Wizara yetu imepokea barua yenu na kuifanyia kazi na hapo ninapozungumza katika viwanja 13 ambavyo vinaonekana vilivyo pembeni ya eneo la Bunge viwanja 11 vimekwishafanyiwa tathimini na value yake imekwishajulikana, lakini pia tutakapokuwa tumemaliza viwili vilivyobakia tutaleta ile taarifa kwa mamlaka husika ambaye ni Katibu wa Bunge ili sasa mchakato uweze kufanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo; katika sheria yetu Sura Namba 118 ya Utwaaji wa Ardhi na Sura Namba 113 ya Ardhi inatuelekeza kwamba unapotaka kutoa ardhi mamlaka husika lazima ihusishwe; hivyo, nataka nitoe angalizo kwetu kwamba pamoja na kwamba utaratibu unaendelea, lakini mamlaka husika ambayo kwa mujibu wa sheria na Mheshimiwa Rais basi naye lazima tumuhusishe katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nirejee angalizo alilolitoa au rai iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wakati anatoa hotuba yake juu ya kuhakikisha kwamba riba au hizo interest za maeneo au hela zinazotakiwa zilipiwe katika utoaji wa maeneo zinafanyika mapema ili kuepusha usumbufu wa kulipiana fidia na riba zingine zisizofaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nizungumzie jambo la Mabaraza ya Ardhi; nikurejeshe katika Mabadiliko Madogo ya Sheria Sura Namba 216 yaliyofanywa katika Sheria Ndogo Namba Mbili ya mwaka 2021 ambapo baadhi ya mambo makubwa yanayokwamisha utolewaji wa haki yalifanyika. Moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba wenyeviti wetu wa Mabaraza ya Ardhi sasa wanakuwa ni waajiriwa na si vibarua au watu wanaojitolea kama ilivyokuwa mwanzo na katika kufanya hivyo mafanikio yameonekana sasa; mafanikio yameonekana kwa sababu waliopo ni kwamba wanakataa rushwa kwa vitendo, lakini kwa wale wachache ambao wameendelea kupokea rushwa nataka nikuhakikishie wizara yako, Serikali yako inaendelea kutoa macho katika hao wasio waadilifu na tutaendelea kuwashughulikia kadri ambavyo tutakwenda kupata malalamiko toka kwa wananchi wetu ambao wanalalamika haki kutotendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hilo katika mabadiliko hayo ambayo yamefanyika sasa, moja ya jambo kubwa ambalo limefanyika ni kuhakikisha kwamba mamlaka yale ya kuamua juu ya kesi nayo pia yamebadilika, Mabaraza yetu ya Kata na Vijiji yamebakia na kazi ya usuluhishi tu, lakini Mabaraza kuanzia Wilaya ndiyo yanaopenda kuamua on issue of meriting, huku chini wanaamua katika mambo ya mahusiano tu, yaani katika maana kwamba kuwapatanisha wananchi na siyo kuleta mgongano ambao utakuja kutusumbua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuakikishie Bunge lako kwamba katika mwaka wa fedha uliopita Wizara yetu ya Ardhi imeweza kufungua Mabaraza mapya 20 ikiwa ni sehemu ya kuongeza mkazo wa kuhakikisha kwamba haki inawakaribia wananchi na kuwafikia na katika mwaka huu wa fedha Bunge lako litakapotupitishia mafungu yetu tunakwenda kumalizia Mabaraza 59 yaliyobakia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na wote waliotangulia kusema, kwanza, kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya iliyo njema na hata leo tupo mbele yako ukituongoza, tukiwasilisha kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wangu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Comrade Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, GBS. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu mimi binafsi nianze pia kwa kukushukuru wewe, kwanza kwa kuongoza kikao chetu vizuri. Pia kwa upekee kabisa namshukuru Mheshimiwa Spika kwa kuongoza Bunge hili vizuri, ameendelea kuwa Spika wa mfano, Spika anayetupa heshima na kwa kweli Spika wa viwango vikubwa. Nasi kwa kweli tunaendelea kumshukuru sana kwa uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, nami niungane na waliotangulia kusema kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya. Ni wazi kabisa kutokea kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia wamedhihirisha kabisa kwamba Mheshimiwa Rais wetu ni Rais wa mfano wa kuigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nirudi katika maneno mazuri yaliyosemwa na ndugu yangu Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Konde, ambaye alisema, kwa kweli akipata nafasi ya kupiga kura atamchagua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maneno haya ni maneno mazito, maneno ambayo hayapaswi kupuuzwa, na pia ni maneno ambayo yanaonesha wazi kwamba naye anakubali kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli huu ni mfano wa wazi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, nawashukuru sana wote ambao wanamsaidia ambao kwetu sisi; mimi na Mheshimiwa Waziri wangu wamekuwa ni viongozi wetu. Nikianza na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, yeye pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Mashaka Biteko, kwa kweli kazi nzuri inayofanyika ni wazi kabisa nchi yetu imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo toka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na hili linashuhudiwa kwa vitendo kutokea kwenye kazi zao, usimamizi wao na maelekezo ambayo kila siku wamekuwa wanayatoa, nasi Mawaziri wao tunatekeleza kazi hizo kwa juhudi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi katika salamu za shukurani nikamsahau Waziri wangu, ndugu yangu, Doctor…

MBUNGE FULANI: He, amekuwa Doctor?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetaja madaktari hapa nimeona, nikampa naye Mheshimiwa Dkt. George Boniface Simbachawene. Mwenyezi Mungu atamjalia atafika huko. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri mimi binafsi kwa niaba ya wenzangu wote ndani ya Wizara. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie nafasi hii kabla sijaingia kwenye michango hii mizuri ya Waheshimiwa Wabunge, kumshukuru sana, kwanza kwa uongozi wake, na pia mazingira mazuri ambayo anatengeneza ndani ya Ofisi yetu. Amefanya Ofisi imetulia, anatoa ushirikiano mkubwa, maelekezo yake, maangalizo yake, kwa kweli ni Waziri wa mfano na Mwenyezi Mungu amjalie katika safari yake ya uongozi, basi ampandishe madaraja. Mwenyezi Mungu ampe na mengineyo ndani ya nyumba yake ili tuweze kuyaona na sisi tulio chini yake tuendelee kufaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wa leo, tumepata bahati ya Waheshimiwa Wabunge 23 kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara yetu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Michango yote imejikita katika maeneo ya kimsingi kabisa ambayo yameelekezwa kuwa ndiyo kazi yetu ya msingi kabisa sisi ndani ya Ofisi ya Rais, inayosimamia Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, nataka kuanza kwa kulikumbusha Bunge lako kwamba, msingi mkubwa wa ofisi yetu ni usimamizi wa sheria, sera na taratibu ili kuweza kuisadia nchi katika kuhakikisha kwamba Utawala Bora na Utumishi wa Umma unaendelea kustawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, yote yaliyozungumzwa hapa kwa mfano kwenye upande wa Utawala Bora, Waheshimiwa Wabunge wameeleza juu ya mambo ya msingi ambayo wao wanayaona kwamba yana changamoto kwa upande wao; siyo huko tu, pia hata katika eneo la Utumishi wa Umma, nalo pia wameeleza mambo ya msingi ambayo wanaona kwamba yana changamoto kwa upande wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, pia katika michango yao wametumia nafasi hiyo kuishauri Serikali juu ya maeneo ya kimsingi ambayo wanadhani yakifanyiwa kazi, yakiwekwa vizuri au yakiangaliwa kisera na kisheria mambo yatakuwa mazuri zaidi kuliko ilivyokuwa jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niendelee kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba, sisi ndani ya Serikali tukiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Waziri wetu, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, kazi ya kuendelea kuangalia sera, sheria na taratibu kuendelea kuongoza nchi yetu, tumeshaanza kuifanya na tunaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo ambayo kutokea kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge, imejidhihirisha wazi kwamba tunayo kazi ndani ya Wizara yetu ya kuendelea kutoa elimu kwa Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu yapo mambo yanafanyika ndani ya Wizara na kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge ni wazi kabisa yanaonekana mawasiliano kutoka kwenye Wizara yetu kuja kwa Waheshimiwa Wabunge kwa maana ya wananchi, bado yamekuwa ni hafifu. Katika mchango wangu au katika uchambuzi wangu nitayagusia maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nianze kwa hoja ambazo zimeelezwa na Waheshimiwa Wabunge hasa katika eneo hili la TASAF. Katika hoja ambayo imeelezwa na Waheshimiwa Wabunge iliyochangiwa ni kwamba, Serikali iharakishe upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ili kuwawezesha wananchi wenye sifa za kunufaika na mradi wa TASAF kupata fursa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba, TASAF imeingia kwenye mkataba wa makubalino (MOU) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kufanya mazoezi maalum ya kusajili na utoaji wa Namba za Vitambulisho vya Taifa kwa wanufaika wa mradi huo. Mpaka sasa wanufaika wa TASAF 680,816, wameshasajiliwa na kupokea ruzuku zao kwa njia ya elektroniki, kigezo kikubwa kikiwa ni kupatikana kwa hivyo vitambulisho vya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge Omar Ali Omar yeye ameeleza na amesikitika sana juu ya utaratibu ambao unaonekana kwamba kuna baadhi ya watu wapo juu ya sheria, miongozo na taratibu zinazosimamia miradi miradi ya TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naliambia Bunge lako kwamba, kama malalamiko hayo yapo, namwomba Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwa ujumla waendelee kutuletea ili tuyashughulikie. Isitoshe katika hilo, miongozo inayosimamia mradi wa TASAF inaelekeza wazi njia ya ku-deal na malalamiko ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kama inatokea kuna tatizo katika ngazi ya shehia, basi kwanza malalamiko yanatakiwa yapelekwe katika Kamati ya Uchambuzi kwamba, sijafanyiwa haki na ninahitaji kufanyiwa haki hiyo, lakini kama ataona pale katika shehia ambapo ndiyo matatizo yametokea labda wale watu wamekusanyana kwa pamoja dhidi yake, basi utaratibu unaelekeza kwamba, malalamiko yapelekwe katika ngazi ya wilaya, hasa kwa Wakurugenzi ili waweze kusimamia na kuchambua vizuri malalamiko hayo. Pale watakapoona kweli mtu huyu ana haki, lakini hakupendekezwa katika mradi, basi uamuzi wa kumrudisha ili awe sehemu ya wafaidika utafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, endapo mtu huyu ataona pia Mkurugenzi katika ngazi ya wilaya hajafanya haki, basi utaratibu wa kukata rufaa kwenda Makao Makuu inabidi ufanyike ili mfaidika huyu aweze kupata haki anayostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba, utaratibu huo unafanyika na uko wazi. Naomba yeye aendelee na kama ataona mambo yanakwenda hovyo, basi Ofisi ya Waziri na Ofisi ya Naibu Waziri zipo wazi, tuletee tuyashughulikie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia 4R alizosema Mheshimiwa Rais, moja ya kazi kubwa ni kuhakikisha kwamba sisi wasaidizi wake tunawafikia mara moja wananchi wetu na tunakutana na changamoto wanazokabiliana nazo ili kuweza kuzitatua. Katika kufanya hilo, nataka kulieleza Bunge lako kwamba, tumepokea malalamiko 52,376 na baada ya kudodosa kaya hizo, tumeridhika kwamba kaya 7,412 zinajitosheleza katika vigezo na zimerudishwa katika mpango, lakini kaya 44,964 ambazo hazijajitosheleza katika vigezo, zimetolewa baada ya rufaa zao kushindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine ni Serikali ihahakikishe matokeo ya rufaa za waombaji wa kujiunga na mradi wa TASAF yanatolewa mara moja. Ushauri umepokelewa na kuzingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulieleza Bunge lako kuwa Serikali inaendelea kufanyia kazi rufaa zilizopokelewa kama ambavyo nimeeleza na ambapo sasa tunapozungumza kaya zile ambazo nimezitaja 7,412 ambazo zimeleta rufaa zake na kusikilizwa, zimeshajulishwa. Hapa tunapozungumza, watu wapatao 1,300,000 kutoka kwenye kaya hizo wanaendelea kufaidika na mradi huu wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia wapo baadhi ya wajumbe ambao walizungumza na kuitaka Serikali iendelee kuimarisha misingi ya utawala bora pamoja na kuboresha mifumo ya utendaji kazi katika utumishi wa umma, sambamba na kuboresha mishahara na maslahi ya watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninataka nizungumzie eneo la watumishi na mishahara. Serikali imepokea ushauri huo na inaendelea kusimamia misingi ya utawala bora kwa kuzingatia uwajibikaji, uwazi na ushirikishwaji. Katika kuboresha mifumo ya utendaji kazi, Serikali imejenga mifumo ya kielektroniki katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia utendaji katika utumishi wa umma, ukiwemo Mfumo wa PEPMIS na PIPMIS ambao unawezesha kupima utumishi na ufanisi wa kazi wa watumishi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa sasa mambo yote yanayohusu utumishi wa umma yanapimwa kwa kupitia vigezo ambavyo vimeainishwa na PEPMIS na PIPMIS. Kupitia Mfumo wa PEPMIS na PIPMIS wafanyakazi wanaweza kuorodhesha majukumu yao na vigezo vya kuwapima watumishi hawa vinatumika kwa kupitia vigezo vilivyowekwa katika utaratibu huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wajumbe wengi wamezungumzia jambo la msawazo wa watumishi wa umma, hasa katika maeneo ambayo yanaonekana kwamba kuna shida kubwa ya watumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa maneno mazuri ambayo yameelezwa na Naibu Waziri, Mheshimiwa Katambi wakati anatoa mchango wake kuhusiana na hoja iliyowekwa Mezani. Nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali katika utaratibu wa kusimamia utendaji kazi, imebuni mfumo unaoitwa HR Assessment. Mfumo huu unaiwezesha Serikali kujua idadi ya watumishi katika maeneo yao, ni wapi ambapo kuna upungufu mkubwa na ni wapi pana uhitaji mkubwa ili kuwezesha mipango na misawazo ya utumishi wa umma kuweza kukaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kueleza jambo hili, nataka nirudi katika maneno au hoja iliyoelezwa na Mheshimiwa Yahaya Massare, Mheshimiwa Francis Isack Mtinga na Mheshimiwa Lujuo Mohamed Monni ambao wamezungumza hasa katika eneo la hitaji la walimu na upungufu mkubwa wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako kuwa, pamoja na changamoto hiyo, Serikali kupitia Mfumo wa HR Assessment inaendelea kupanga na kukamilisha zoezi la tathmini ya rasilimali watu ili kubaini upungufu au ziada ya walimu na watumishi wa kada mbalimbali katika Halmashauri zetu. Katika kufanya hivyo, Wilaya ya Mkalama na Wilaya ya Iramba zimetengenezwa nafasi za ajira mpya 86 na 70 za msawazo wa kada ya ualimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, pia nalikumbusha Bunge lako kwamba, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ilitarajia kuajiri walimu 10,505 ili kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu, lakini katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga jumla ya nafasi za ajira mpya 10,590 za kada ya ualimu ili kuendelea kujaza nafasi katika maeneo yenye upungufu wa watumishi wa kada hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwa upande wa Wilaya ya Mkalama na Iramba katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2021/2022 hadi sasa, walitengewa nafasi za ajira mpya 192 na 175 za mtawala wa kada ya ualimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi ameeleza masikitiko yake, hasa katika eneo la malimbikizo ya mishahara ya watumishi na kwamba bado kuna maeneo hawajalipwa malimbikizo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kulikumbusha Bunge lako juu ya kazi kubwa ambayo inafanywa na Serikali, hasa baada ya muundo mpya wa mfumo wa taarifa ambao unaitwa HCMIS. Mfumo huu unaiwezesha Serikali siyo tu kupata taarifa za watumishi, lakini pia katika kupanga vizuri mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, pia napenda kulieleza Bunge lako kwamba, mfumo huu kwa namna moja au nyingine umewezesha watumishi kutokuwa na malimbikizo ya madai kutokana na kupandishwa vyeo kutokana na mabadiliko ya miundo kwa sababu sasa, kupitia mfumo huu mfanyakazi au mtumishi wa umma anapopanda daraja pale pale mabadiliko ya mishahara na taarifa zake, ikiwemo posho zake anazostahili nayo pia yanabadilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kueleza mbele ya Bunge lako kwamba, kwa mwaka 2021/2022 hadi 2023/2024 Serikali imelipa zaidi ya shilingi bilioni 193.15 kwa watumishi 118,584 wenye madai. Aidha, Serikali inaendelea na uhakiki wa madeni yaliyowasilishwa kwa waajiri kwa ajili ya malipo. Hadi sasa madai ya malimbikizo ya watumishi 21,660 yenye jumla ya shilingi bilioni 45 yamehakikiwa na yanasubiri kulipwa na Serikali kulingana na uwezo wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Joseph Kakunda amehimiza na kuikumbusha Serikali kufuatilia uzingatiaji wa maadili ya watumishi wa umma sehemu za kazi. Kwanza nalihakikishia Bunge lako kwamba mawazo mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge tunayabeba na kwenda kuyafanyia kazi, lakini katika kufanya jambo hilo, Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya maadili kwa watendaji na watumishi wa umma ili kuwakumbusha wajibu wao wa kazi pamoja na kutekeleza mipango na malengo ya Serikali. Mpaka sasa tunapozungumza jumla ya watumishi 24,922 wamepatiwa mafunzo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya taasisi 92 zimefanyiwa ufuatiliaji na kubaini maeneo yenye upungufu katika kuzingatia maadili na kuchukua hatua stahiki. Jibu hili ninalotoa hapa ni sanjari na mazungumzo au kumbusho lililotolewa na Waheshimiwa Wabunge kwamba, Tume yetu ya Watumishi wa Umma siyo tu isubiri kesi na kufuatilia mienendo, pia iende katika taasisi na Idara za Serikali ili kuweza kujua ni nini ambacho kinatokea hasa katika stahiki na haki za watumishi hao?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, pia Mheshimiwa Kakunda ameeleza kuwa kuna wakati uanzishwaji wa OPRAS ulipigiwa debe sana, lakini hajui kiutendaji OPRAS hiyo imepimwa vipi na ni lini imefanyiwa tathmini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kulieleza Bunge lako kuwa, kwanza Mfumo wa OPRAS kwa sasa haupo. Sasa hivi mfumo unaotumika kupima utendaji kazi unaitwa PEPMIS na matokeo ya mtendaji mmoja mmoja wa PEPMIS ndiyo unaitwa PIPMIS kwa maana ya taarifa ya taasisi au ofisi ambayo inasimamia watumishi wa umma. Mfumo huu umeanza kutumika katika kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma katika mwaka wa fedha 2023/2024, baada ya Serikali kutoa waraka na kufuta mfumo ule wa zamani wa OPRAS.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango mwingine umeelezwa na Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage, ambaye ametaka mtumishi anapobadili kada asianze katika cheo kipya au mshahara wake uweze kusomeka kama ulivyokuwa zamani, na kwamba, watumishi wa umma ambao wamejiendeleza kielimu ndiyo ambao wanakabiliana sana na changamoto hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie mfano mmoja, hasa watu ambao wamesomea shahada ya kilimo. Kwa mtumishi wa umma ambaye ana Stashahada ya Kilimo ambayo ndiyo imemfanya aajiriwe katika kazi, pale anapokwenda kujiendeleza na kutunukiwa Shahada ya Kilimo kwa maana kwamba sasa ametoka katika stashahada, ameingia katika shahada, mara nyingi miundo ya kazi nayo hubadilika, kwa sababu, sasa huyu anakuwa ni Bwana Kilimo, lakini yule mwenye stashahada ya kazi kwa mujibu wa vyeo vya kimuundo anakuwa ni Afisa Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa wawili wote wana vyeo tofauti, lakini anapofika kwenye ngazi ya juu kabisa katika ngazi ya cheti, kwa maana ya mtu mwenye stashahada, maana yake ni mshahara wake unaweza kuwa juu ya mshahara ambao akiwa na shahada anaenda kuanzanao.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulieleza Bunge lako kwamba, inapotokea mtu ana mshahara mkubwa katika nafasi ya cheo anachoomba kubadilishwa, basi maombi kwa ajili ya kumwezesha kuondoka na mshahara wake ule ulio juu, yanafanyika kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi. Kibali kinapotolewa, utaratibu wa kumhamisha mtu huyo na mshahara wake unafanyika ili aweze ku-enjoy uwepo wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba, taratibu zipo wazi. Tunachoomba ni watumishi wa umma mfuate taratibu ili mambo yaende vizuri katika stahiki zenu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hoja nzuri zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, lakini wapo baadhi yao ambao wametaka kujua juu ya mifumo mipya ya Sekretarieti ya Ajira inavyofanya kazi katika eneo zima la usaili wa vijana wetu. Mheshimiwa Francis Mtinga ameeleza kwamba, utaratibu uliopo unafanya baadhi ya vijana wasafiri umbali mrefu, kwa mfano, wapo ambao wanatoka Kigoma, Mwanza, Bagamoyo, Lindi na Mtwara kuja kufanya usaili katika Mji wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelekezo yaliyotolewa na Kiti chako ya kutaka Sekretarieti ya Ajira iangalie tena utaratibu wa jinsi ambavyo watumishi wapya wa umma wanapatikana, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri George Boniface Simbachawene, naomba kuliarifu Bunge lako kwamba, tumeanza usajili kwa njia ya kidijitali ambapo sasa online aptitude test imeanza kufanya kazi na mara ya kwanza ilipotumika usaili ulifanyika Tanzania nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako kwamba, katika siku ulipofanyika usaili kwa mara ya kwanza kupitia utaratibu huu mpya, hatukupata lalamiko lolote. Baada ya utaratibu huu kuonekana umefanikiwa, malengo ya Serikali ni kuhakikisha taratibu nyingine za usaili wa vijana wetu katika kada zote unaingia katika utaratibu huu wa online aptitude test system ili waweze kupata nafasi ya kufanya usaili katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba, kwa wale vijana wanaotokea Singida, kwa utaratibu huu mpya maana yake ni watafanya usaili Singida. Hivyo ndivyo itakavyokuwa pia kwa watu wote wanaotokea katika kona zote za Tanzania, ikiwemo wale wenzetu wanaotokea upande wa Visiwani au Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, pia Mheshimiwa Mbunge Dkt. Alice Kaijage amezungumzia eneo la Sekretarieti ya Ajira, anapenda aone uwezekano wa kutoa kipaumbele kwa waombaji kazi waliohitimu vyuo muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uendeshaji wa michakato ya ajira katika utumishi wa umma unazingatia Sera ya Menejimenti ya Ajira ya Mwaka 2008, Sheria ya Utumishi wa Ajira Sura ya 298, na Kanuni ya Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira ya Mwaka 2021. Aidha, kanuni ya 18 (2), (c) inampa kipaumbele msailiwa mwenye umri mkubwa kupangiwa kazi pale inapoonekana amepata alama za ufaulu. Kwa hiyo, nalihakikishia Bunge lako kwamba, utaratibu huu unaendelea, lakini najua kwamba hapa kinachozungumzwa hasa ni watu ambao wamemaliza shule muda mrefu na hawajapata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kulikumbusha Bunge lako kwamba, ndani ya vikao vya Bunge hili tumekubaliana kwamba, ajira zote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa sheria, zitatolewa kwa njia ya ushindani. Kwa hiyo, sisi ndani ya Sekretarieti ya Ajira au ndani ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma tunachokifanya ni kusimamia sheria, sera na taratibu tulizokubaliana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge, mijadala juu ya hao wenzetu ambao wamemaliza shule muda mrefu na hawajapata nafasi za kuajiriwa inaendelea kujadiliwa ndani ya ofisi yenu. Katika kufanya hivyo, chini ya uongozi wa Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, ninaamini kabisa kwamba majibu yatakapokuwa tayari tutayaleta mbele ya Bunge na huenda yakachagiza kubadilishwa kwa sera, sheria na mambo mengine. Haya yote yanayozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge tunayachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ninazungumza juu ya ujenzi wa mifumo. Mheshimiwa Yahaya Massare amekuwa na tamaa ya kutaka kujua sana na ninadhani hili ni kwa Bunge lako lote, kwamba mifumo imekuwa inalalamikiwa kwamba haisomani. Hili limekuwa ni changamoto kubwa sana lakini pia Bunge lako limezungumza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie wewe na Bunge lako kwamba juhudi kubwa sana zimeendelea kufanyika ndani ya Serikali. Moja ya eneo kubwa ambalo limefanyiwa kazi ni kutengenezwa kwa mfumo wa kubadilishana taarifa ambao unaitwa Government Enterprise Bus au kwa lugha ya ki-TEHAMA inaitwa GovESB. Hadi sasa taasisi 122 ambazo zinatumia mifumo 132 zimeweza kuunganishwa na zinabadilishana taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuthibitisha hili, nataka nitoe mfano wa Mfumo wa Haki Jinai ambapo wenzetu wa Jeshi la Polisi, Mahakama, Ofisi ya DPP na wenzetu wa TAKUKURU, mifumo yao inabadilishana taarifa kwa sasa. Sasa hivi likifunguliwa jalada katika ofisi, labda katika Jeshi la Polisi, basi jalada lile likiwekwa tu ndani ya utaratibu, Ofisi ya DPP itapata taarifa, wenzetu wa TAKUKURU watapata taarifa, pia Mahakama nayo itapata taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, pia mfumo huo umewezeshwa na mfumo mwingine wa malipo wa Serikali ambao unaitwa GePG ambapo mfumo huo umeunganishwa na mifumo yote ya watoa huduma wa simu. Ikiwemo hawa wenzetu wa Vodacom, Tigo, Halotel, TTCL na wengine wote ili kuwezesha mifumo yote kusomana. Leo hii mimi ninayetumia simu fulani ya kampuni fulani, nikitaka kufanya malipo kwa simu ya kampuni nyingine kupitia Mfumo wa GePG, malipo yanawezekana na mambo yanakwenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niendelee tena kuishukuru Serikali yangu. Pili, namshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wote wakiongozwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais, kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika ya kuwahudumia Watanzania; kuwahudumia watu wote ambao wana mahitaji bila kusahau kaya masikini zinazohudumiwa na TASAF ambapo Serikali imeendelea kuongeza pesa kila siku kuhakikisha kwamba tunawaondoa Watanzania katika umaskini, huku ikibuniwa miradi ya mfano wa kipekee kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2024
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kwanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kufanya majumuisho ya mjadala katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Hifadhi ya Jamii Mwaka 2024 [Social Security Laws (Amendments) Act, 2024].

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza, nami naomba radhi kidogo mbele ya Bunge lako kwa kuchanganya madesa hapa, kwa kumpa nafasi Mheshimiwa Almas Maige ambayo hakuwa nayo wala hakustahili. Namwomba radhi sana Mheshimiwa Riziki Lulida, pia naliomba radhi Bunge lako maana Mheshimiwa Almasi Maige huyu nimekutana naye kabla sijaanza kuhutubia hapa, nahisi kuna jambo la Kinyamwezi kalifanya. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Maige namtambua kama Mjumbe na nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni ya Mheshimiwa Riziki Lulida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mchana wa leo, jumla ya Wajumbe saba kwa maana ya Wabunge wamepata nafasi ya kuchangia, bahati mbaya sikupata michango ya maandishi, lakini waliochangia wote nimewasikia. Yapo baadhi ya maeneo ambayo wametoa maoni yao, pia yapo baadhi ya maeneo wametuelekeza nini cha kufanya. Nataka nitumie nafasi hii kuwashukuru sana kwa kuunga mkono hoja ambayo tumeileta hapa leo.

Mheshimiwa Spika, nataka kwa kipekee kabisa niwashukuru sana Wabunge kwa michango yao mizuri. Kwa niaba ya Wizara na kwa niaba ya Serikali nakiri tumepokea maoni yao mazuri ambayo yanalenga kuboresha Muswada wetu pia kuweka sheria zikae vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni ushahidi kwamba suala la sheria hii tuliyoileta Mezani kwako ambayo ina lengo la kuboresha, kurekebisha na kuweka umadhubuti sheria ya kusimamia Mifuko ya Hifadhi, imegusa jamii yetu na hivyo jamii kupitia Bunge lako imeendelea kutetewa na kusimamiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa hoja, nataka nieleze katika maeneo machache. Kwanza nataka nianze katika ushauri wa mwisho ambao umetolewa na Mheshimiwa Prof. Muhongo. Kwa kweli ushauri wake ni mzuri hasa katika eneo hili la kwamba kwa kuwa wanachama hawa wanachangia Mifuko na sisi tunakwenda kutumia fedha hizo kwa ajili ya uwekezaji na shughuli nyingine, ni vyema tukaangalia katika mazingira hayo ili wanufaika nao wale wanachama waendelee kunufaika.

Mheshimiwa Spika, nataka nichukue hili jambo, tutakwenda kuliangalia pamoja na wenzangu na kulifanyia valuation nzuri ili tutakapoleta jambo hapa mbele ya Bunge lako, basi liwe jambo ambalo limeandaliwa vizuri na siyo jambo ambalo litakwenda kutikisa mifuko yetu.

Mheshimiwa Spika, pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba pensheni hizi zinaangaliwa thamani yake kwa ustahimilivu wa uwezo wa pensheni hizo kulipika. Hapa nakusudia kuzungumzia actuarial evaluation ambazo zinafanyika mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba haya tunakwenda kuyaangalia mara kwa mara kuweza kujua ustahimilivu wa Mifuko yetu na uwezo wa kuweza kulipa hayo yote ambayo ameyasema, hasa hapa nakusudia sana alipozungumzia jambo ambalo hata mimi mwenyewe linanigusa kwa sababu wako baadhi ya watu walionifundisha Chuo Kikuu na pensheni zao, kwa kweli ni ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo ndiyo athari za sheria na sisi tuliopo ambao tumepewa majukumu haya, kazi yetu ni kuangalia na kwa sababu tunatambua michango yao, basi nadhani tunalo jukumu la kuangalia ili tuweze kuwasaidia walimu wetu waliotufanya leo hii napata hata nguvu ya kusimama mbele yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kutumia nafasi hii pia kuwatoa wasiwasi. Nimesikia michango ya Wajumbe wako na hasa katika eneo hili, nataka nimhakikishie ndugu yangu Mheshimiwa Getere ambaye amezungumzia sana jambo lile linalohusu wale Watendaji Kata ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa hawafurahii sana pensheni zao wanazolipwa. Nataka nimkumbushe na nimrudishe katika Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, tatizo lile ulilonalo wewe na mimi ninalo hapa la sheria hizi kuzitaja kwa Kiswahili wakati ziko kwa Kiingereza. Hata hivyo, hapa nakusudia kuizungumzia Sheria ya PSSSF section ya 20 inatoa Mamlaka kwa Mkurugenzi Mkuu pale ambapo ataridhika kwa ushahidi kwamba huyu Mtumishi wa Umma amefanya kazi na mishahara yake ilikuwa inakatwa hizo pensheni zake kupelekwa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, basi kama ikithibitika kwamba hilo jambo limefanyika, Mtumishi huyu atakuwa katika nafasi ya kulipwa pensheni zake.

Mheshimiwa Spika, tumeeleza katika sheria kwamba sasa hivi katika sheria tunachokihitaji ni ushahidi kwamba huyu mtu alikuwa anafanya kazi na alikuwa anapata makato. Kama huyu anayetakiwa kulipa alikuwa halipi, hilo linakuwa ni kesi baina yake na taasisi husika na siyo kwa yule mwanachama au mwananchi wetu ambaye amehudumia nchi yake kwa jasho kubwa, wakati mwingine kuvuja damu halafu mwisho wa siku anakuja kukosa ile thamani ya jasho ambalo amevuja kwa ajili ya nchi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie, Serikali kupitia sheria tuliyoiweka leo hapa, imeeleza wazi kwamba maisha ya mwanachama wetu ni msingi mkubwa wa mabadiliko ya sheria hii.

Mheshimiwa Spika, pia nataka niwahakikishie Wajumbe wengine wakiwemo Mheshimiwa Ali King ambaye alizungumza kwa sauti kubwa sana, akieleza wasiwasi wake juu ya kanuni ambazo zitatengenezwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Ali King, mimi ni Mbunge, pia kama alivyo yeye, mimi naongoza watu, pia ninao wazee, ninao vijana lakini pia ninao watarajiwa na mimi mwenyewe pia ni sehemu ya watarajiwa wa pensheni hizo.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kwenda kutengeneza sheria ambayo itakwenda kuvunja na kufinya haki za watu. Tutatengeneza sheria ambayo inakwenda kuangalia maslahi mapana ya watu, lakini sheria ambayo inakwenda kuangalia maslahi makubwa ya wale ambao wanavuja jasho kwa ajili ya mama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sheria hii ambayo tumeleta mbele yako inathibitisha kwa lugha nyingine kwamba inakwenda kusimamia haki za watu. Tumeeleza kupitia sheria kwamba sheria hii moja ya jambo kubwa ambalo tunaenda kuongeza ni kwanza, muda wa wanachama kulipwa. Kwa mfano, wameeleza Wajumbe wengi na mimi nataka niweke nukta katika jambo hilo, lakini pia kuliwekea msisitizo kwamba kama alivyozungumza Mheshimiwa Katani kwamba sheria hii sasa hivi inafungua wigo siyo tena kubanwa kwamba ndani ya miezi 12 lazima ulete taarifa ili uweze kulipwa na WCF.

Mheshimiwa Spika, tunatambua katika changamoto za utendaji kazi, ziko baadhi ya mazingira ambayo yanamfanya huyu Mtumishi wa Umma anayehudumia umma wake kushindwa kupeleka taarifa mapema. Kwa mfano, kwa wenzetu ambao wanafanya huduma ya ulinzi wakati mwingine anaweza akavamiwa, akapigwa akaumia vibaya. Huduma yake kuhudumiwa inaweza ikachukua zaidi ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, pia wako wengine ambao wanafariki. Jeshi la Polisi linaweza likaamua kwamba wale ambao wamefanya ujambazi huo na kuua wakamatwe. Sasa hatuwezi kusubiri wajane na wanufaika wasubiri kesi ile ambayo inaunguruma zaidi ya miaka minne iishe ndiyo wao wafaidi kwa jasho la mzazi wao au kwa jasho la mlezi wao. Sheria hii kwa kutambua mchango wa mtu huyu, inakwenda kutoa lee way ya kuhakikisha kwamba yule mtumishi aliyeumia akiwa kazini anaenda kuangaliwa na kufaidi matunda hayo hayo ya utumishi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niendelee kuwatoa wasiwasi. Sheria hii pia inakwenda kuondoa baadhi ya watumishi ambao kwa namna moja au nyingine wangeweza kugongana kimaslahi na utekelezaji wa Sheria hii. Kwa mfano, yako baadhi ya mambo ambayo yanatokea kwa mfano katika maeneo ya kazi, unahitaji mtu wa OSHA yeye aje kufanya assessment lakini mtu akiumia hapo hapo wanataka taarifa ya OSHA pia ije kumsadia yule mwajiriwa. S

Mheshimiwa Spika, sheria hii imeondoa watu hao, sasa inaeleza juu ya nani ambaye anatakiwa kwenda kusimamia juu ya kuhakikisha kwamba mtu huyu anapata haki. Pia, kuhakikisha kwamba siyo haki tu inapatikana lakini haki hiyo ionekane ikitokea.

Mheshimiwa Spika, sheria hii inaenda kuheshimu pia Mamlaka ya vyombo vingine. Wajumbe wako wa Kamati walizungumza juu ya kuhakikisha kwamba majeshi kama Polisi siyo linaingia moja kwa moja katika utekelezaji wa jambo hili, lakini pia liingie kupitia utaratibu mwingine. Bahati nzuri nchi yetu katika kuhakikisha kwamba hiyo haki inatokea, imeweka pia chombo kama Mahakama ambacho kama mtu atahitaji msaada wa Mahakama ili aweze kuwatumia Jeshi la Polisi, basi atapata Order ya Mahakama ili aweze kwenda kufanya shughuli hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tumekubaliana na hilo kwa sababu tunatambua kwamba moja ya msingi mkubwa wa Serikali hii ya Awamu ya Sita ni kuheshimu utawala wa kisheria na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan analifanya hili kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria hii inaelekeza kuhakikisha kwamba haki ya wananchi au wanachama inapatikana hasa kwa wale ambao wamepata kazi au wana ajira zaidi ya moja.

Mheshimiwa Spika, wako watu ambao wanafanya kazi zaidi ya moja. Unakuta mtu anafanya kazi labda Hospitali ya Aga Khan au akitoka hapo anakwenda kufanya kazi Hospitali ya Benjamini Mkapa. Sasa katika mazingira haya tumempa nafasi huyu mwanachama aweze kuchagua mchango upi uende? Kama akitaka yote ili uonekane mchango ni mkubwa uweze kutafsirika katika pensheni yake, nayo pia tumempa nafasi hiyo.

Mheshimiwa Spika, sheria hii inampa nafasi ya mwananchi kuweza kupata fungu analolitaka. Kwa maana nyingine maana yake hata kama akihama nalo pia sheria hii inamtaka yule mwajiri wa kwanza aweze kutunza zile taarifa zake na kule anapohamia taarifa ziende ili kuhakikisha mwanachama huyu hapotezi kumbukumbu za michango yake katika Mifuko yetu ya Hifadhi.

Mheshimiwa Spika, pia nataka niwahakikishie kwamba Serikali yenu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejizatiti kuhakikisha kwamba wanachama ninyi mnapewa kile ambacho mnastahili. Sheria inawataka wanachama wapewe michango yao ndani ya muda uliotajwa lakini pia michango hiyo iendane na ile haki yao inayotaka.

Mheshimiwa Spika, ya kusema yako mengi, lakini nataka nirudie tena kukushukuru wewe kwa kutupa nafasi ya kuleta hoja yetu hapa. Pia kwa ujumla nieleze tena maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni ushahidi kwamba suala la marekebisho ya sheria kwa lengo la kuboresha utekelezaji madhubuti wa sheria zilizopo linamhusu kila mmoja wetu katika Bunge hili na ni jambo endelevu. Ndiyo maana mara kwa mara Serikali yenu imekuwa inaleta Miswada hii ili kuifanyia marekebisho, kuboresha masharti ya sheria zetu na kuzifanya ziendelee na wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena naomba kutoa hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mungu na kumtakia rehema, kiongozi wa umma, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wasaidizi wao ukiwemo wewe Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wasaidizi wenu kwa kazi nzuri mnayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika. Pamoja na juhudi nzuri na kubwa ambazo zimekwishafanyika kama ujenzi wa Hospitali ya Mloganzila, upatikanaji wa vifaa na dawa, magari ya kubeba wagonjwa na dawa, lakini ukweli changamoto hasa kwa sisi wenye majimbo ya vijiji tumeendelea kupata taabu na changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri yetu ya Chalinze, hitaji la wauguzi na waganga kwa ajili ya kutoa huduma za kitabibu imeendelea kuwa changamoto. Mfano, katika Kituo cha Afya Kibindu kuna daktari mmoja tu; yeye asikilize mgonjwa, achome sindano, agawe dawa na hata pia atoe ushauri nasaha. Hapo sizungumzii wakati anatibu mgonjwa wa malaria au surua akaja mama mjamzito anayehitaji kujifungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi kubwa, bado tunahitaji kubwa la waganga hasa katika vituo vya afya Kibindu, Miono, Msata, Lugoba, Vigwaza, Ubena na maeneo mengine yanayofanana na shida hii ya Halmashauri yetu ya Chalinze.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi kubwa zinazofanyika na zinazofanywa na Halmashauri yetu ya Chalinze ya kujenga nyumba za waganga, natumia nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutupatia fedha kiasi cha fedha halali shilingi milioni 750 kwa ujenzi wa vituo vya afya Lugoba na Kibindu. Licha ya juhudi hizo, ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Chalinze umeendelea kusuasua. Juhudi za Serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Chalinze kumalizia zinazofanyika.

Mfano pesa kiasi milioni 50 zimetengwa, lakini ukweli nguvu hii inahitaji mkono wa Serikali kumalizia mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa hospitali hii kutapunguza rufaa zinazokwenda Kibaha na Bagamoyo hivyo kupunguza wingi au Lundo la wagonjwa katika hospitali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tumeshuhudia zoezi lililoendelea pale Dar es Salaam ambalo kwa ukweli kabisa kumekuwa na uvunjifu mkubwa wa maadili na sheria ambazo zimesababisha hata heshima za watu kuvunjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine zoezi hili limeibua changamoto ya kuonesha kuwa kuna walakini katika taasisi zetu za kiutendaji. Hapa nakusudia Taasisi au Idara ya Ustawi wa Jamii. Taasisi hii ilikuwa wapi kufanya haya? Je, mfumo gani wanatumia kufanya kazi? Je, kwa nini hawatoi elimu kwa wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Chalinze, miaka 13 iliyopita tulikubaliana kujenga shule za sekondari za kata. Katika makubaliano hayo, ujenzi wa mabweni kwa ajili ya kuwalaza vijana wetu wa kike na wa kiume ulikubaliwa. Matatizo makubwa hasa kwa watoto wa kike wanaoishi kwenye mabweni yamekuwapo kipindi wanapoingia kwenye siku zao za hedhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ombi kwa Serikali, kutokana na hali ngumu za maisha za wazazi wetu na hali ya malezi, niombe Serikali ikubali kuondoa kodi kwenye taulo hizi ili kuwezesha lengo la milenia la kumuelimisha mtoto wa kike kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Chalinze kijiografia ni jimbo pana sana na hata wakati mwingine huchukua umbali mrefu sana toka point moja ya Halmashauri kwenda point nyingine. Umbali huo umekuwa ni kero hasa kutokana na mapungufu ya magari ya kubebea wagonjwa kuwatoa zahanati au nyumbani/vijijini hadi kwenye hospitali au kituo cha afya. Pamoja na hili hakuna gari la chanjo la Wilaya. Tunaomba gari la wagonjwa kwa Kituo cha Afya Lugoba na Kwaruhombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, ombi la Halmashauri kuhusu kuongezewa waganga ili kupambana na mapungufu yaliyopo sasa limeendelea kuwapo. Kwa sasa watumishi waliopo ni asilimia 30 ya mahitaji halisi. Kwa taarifa hadi sasa zipo zahanati ambazo zinaongozwa na wahudumu wa afya na hili limesababisha kushindikana kufunguliwa kwa zahanati mpya zilizojengwa huko Magulumatari, Talawanda na Buyuni Vigwaza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja tukafanye kazi sasa kutatua kero za afya Tanzania na hasa Chalinze.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kupata japo dakika chache kuzungumza juu ya mchango uliotolewa hapa na Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Sheria Ndogo, Mheshimiwa Mtemi Chenge. Kwa hakika nampongeza sana hasa kwa jinsi anavyotuongoza sisi, lakini pia yeye amekuwa mwenye msaada mkubwa kwa sisi wanasheria kuendelea kutusaidia kuelewa nini maana ya sheria katika uhalisia wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu waliotangulia wameeleza mengi na kwenye taarifa yetu ya Kamati tumeeleza mengi. Nataka nijikite katika mambo makuu mawili kama siyo matatu kama muda utaniruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa ni mahitaji ya kuwa na rasilimali watu ya kutosha katika Ofisi ya Attorney General. Haya yote yanayolalamikiwa hapa kama umesikiliza vizuri wengi wao wamejikita sana katika hoja kubwa ya uandishi wa sheria. Yapo maeneo mengi, tukitaka kuyaelezea hapa unaweza ukachukua muda wote uliobakia.

Naomba nizungumze kwa uchache zaidi, kwa mfano ukifungua ukurasa wa 7 na wa 17 kuna tatizo kubwa sana la uandishi unaojichanganya. Waandishi wetu wa sheria wanapenda kufanya reference ya vitu ambavyo havifanani na hizo sheria zenyewe, wameeleza hapa waliotangulia. Kwa mfano mmoja kwamba kuna mtu ameandika ana-refer Sheria ya Traffic ambayo ukiangalia sheria yenyewe kinachotambulishwa sicho ambacho kimeelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, majedwali mbalimbali ambayo wameyaweka kwa mfano katika ukurasa wa kwanza kwenye ile Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Gesi (Oil and Gas) unaona kabisa kwamba Waziri wa Fedha anapewa mamlaka ambayo mamlaka yale kwa utaratibu wake yalivyo hayatambuliki katika sheria inayoelezea juu ya usimamizi wa makusanyo ya mapato yanayotokana na oil and gas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunachosema ni kwamba hapa hakuna mtu anayetaka kupambana na Serikali au kuivuta Serikali, lakini basi waandishi wetu mnapofanya nukuu hizo muwe makini katika kitu gani ambacho mnaki-refer, isije kuwa baadaye mkaonekana kama vile kwamba ni watu makanjanja ambao hamjui hata mnalolitenda. Ndani ya ukurasa wa 10 katika Sheria Ndogo ya Mining Local Content nayo pia kosa hilo linajitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi sana ya kueleza, lakini siyo hilo tu pia iko shida nyingine ya kutotekeleza kwa yale ambayo tumekuwa kila siku tunaeleza. Siyo mara ya kwanza Kamati inaleta mbele yako mapendekezo juu ya kazi ambayo imekwishafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unakumbuka katika taarifa yetu iliyotolewa miezi sita iliyopita tulieleza juu ya watu wetu kutokuwa makini juu ya uchapishaji wa sheria hizi ndogo. Kama unakumbuka vizuri tulieleza hapa iko sheria ambayo inaeleza kwamba watu wa Kahama katika barabara zao au katika nyumba zao mbele waweke pavement blocks.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulieleza kwa masikitiko makubwa kwamba ziko sheria ambazo zimetungwa Dar es Salaam, wakafanya copy and paste wakazipeleka katika maeneo mengine, lakini matatizo hayo yanaonekana yanaendelea kujitokeza na bado shida imekuwa kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sheria ya Electronic and Postal Communication Act iko lugha ambayo imeelezwa mle ndani ambayo watu wengi hata kwenye kamati tuliijadili sana juu ya kitu kinachoitwa sim swap, lakini unavyoona mpaka leo hii mambo bado yameendelea kuwa vilevile. Tunachokiomba ni kwamba Wizara au Serikali ichukulie mawazo yale kama ni mawazo sahihi na kama kuna maeneo ambayo wanatakiwa kuyaweka sawa basi ni vyema tukaelezana katika mikutano ya Kamati inapokutana na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo, yako mambo mengine ambayo nayaona ni kwamba kwa tafsiri yangu ni mambo ya kutozingatia weledi tu, yako mambo ambayo yanaweza yakarekebishwa hata ndani ya ofisi. Ameeleza hapa Mheshimiwa Halima Mdee, lakini pia wameeleza waliotangulia hasa juu ya uandishi mbovu wa kutojua kupangilia vipengele na vifungu vya kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi yangu naiomba sana Serikali iendelee kuamini kwamba wanao muda wa kutulia na kujipanga vizuri na wakatengeneza kitu ambacho kitakapokuja kwetu sisi tuwe na sehemu ndogo ya kuongezea nyama na siyo kufikia sehemu ya kuonesha kabisa kwamba hakuna kitu kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza mwanzo, mengi yameelezwa na wenzangu, lakini pia katika hotuba yetu ya Kamati tumejaribu kuchambua kwa undani zaidi na kueleza yale ambayo tumeweza kuyafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitumie nafasi hii kupongeza tena Kamati yetu, lakini pia kuendelea kuwatia moyo Serikali waendelee kuchukua yale ambayo Kamati inafanyia kazi kwa sababu sisi Kamati inafanya kazi kwa niaba ya Bunge na unaposema kwa niaba ya Bunge tunamaanisha kwa niaba ya wananchi wote wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja tuliyotoa, lakini pia naendelea kuunga mkono hoja zote zinazotolewa. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Rais katika Wizara hizi mbili kama zilivyotajwa. Nataka niende moja kwa moja kwenye masuala makubwa yanayohusu eneo langu la utawala, nalo si lingine, ni Halmashauri ya Chalinze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha bajeti iliyopita, Serikali ikishirikiana na halmashauri imeweza kufanya mambo mengi makubwa, ikiwemo kusaidia kuimarisha maeneo ya afya, maeneo ya elimu na maendeleo ya vijiji vyetu kwa ujumla wake. Pamoja na jitihada hizo bado yapo mapengo ambayo leo hii ninaposimama hapa nataka nimkumbushe hasa Mheshimiwa Waziri Jafo; kwa sababu kwenye eneo huko la Ofisi ya Rais upande mwingine sina mengi; lakini eneo la TAMISEMI ndiko nina mengi mengi kidogo; nataka nimkumbushe juu ya mapengo machache ambayo naamini tukishirikiana kwa kasi ambayo ameendelea kufanya kazi, tutaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na eneo la afya. Kwanza nianze kushukuru maana tunaelekezwa kwamba usiposhukuru kwa kidogo huwezi kushukuru kwa kikubwa. Katika kipindi cha bajeti iliyopita ndani ya Halmashauri yangu ya Chalinze nimeweza kuletewa zaidi ya shilingi milioni mia saba kwa ajili ya maendeleo ya afya. Katika shughuli hizo tumeweza kufanya mambo makubwa sana kwa mfano kwenye zahanati yetu kule Kibindu, mambo yanakwenda vizuri, naishukuru sana Serikali yangu. Vile vile pale Lugoba nako pia mambo ni mazuri sana na naendelea kuishukuru Serikali yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo, upande wa watumishi imekuwa sasa ni kizungumkuti kikubwa sana. Tumeweza kufanikiwa na kama tunavyoendelea kufanikiwa kujenga miundombinu mizuri lakini kuna upungufu wa Wauguzi na Wakunga imekuwa ni shida kubwa sana. Vifo vya akinamama na watoto vimeendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kwa sasa hivi tumevipunguza sana, lakini kwa kweli kukosekana kwa watu hawa ambao ni viungo vizuri sana katika kutimiza eneo zima au lengo zima la Serikali kwa upande wa afya mambo yameendelea kuwa si mazuri sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama aseme neno kidogo ili watu wa Chalinze waweze kufurahi juu ya mikakati mizuri ambayo Serikali imepanga katika kuhakikisha kwamba anatupatia wauguzi na waganga ili mambo ya afya yaweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia mahitaji makubwa ya sasa ni mahitaji ya gari za kupakia wagonjwa. Kama anavyojua Mheshimiwa Waziri alipokuja kwa mara ya mwisho tulimwonesha tulikuwa na magari mengi lakini Mungu naye ana yake. Magari yetu mawili ambayo tulikuwa tunayategema yamepata ajali na sasa hivi imekuwa ni tabu kweli kweli, hasa inapofika wakati wa kuwasafirisha wagonjwa kutoka katika vituo vya afya kwenda katika hospitali kubwa za rufaa; kama ambavyo anazifahamu, kule Tumbi, Bagamoyo na nyingine ambazo zinakwenda Msoga pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika eneo la elimu kilio kinafanana kidogo na kilio cha afya. Jitihada kubwa tumeendelea kuzifanya katika kuhakikisha kwamba madarasa, tunaendelea kujenga nyumba za Walimu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba upungufu wa Walimu pia umeendelea kutusumbua. Kwa mfano, kama anakumbuka vizuri katika ile zoezi letu la kukagua vyeti feki tumepata shida sana kwa sababu baadhi ya Walimu walionekana kupungukiwa na sifa na kuondolewa, lakini sasa hivi kwa jinsi ambavyo tunakwenda nina imani kabisa kwamba kama katika bajeti yake mzee atatuangalia vizuri, basi mambo kule nako yataendelea kuwa mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ya bajeti sikumbuki ukurasa wa ngapi lakini upo ukurasa anaozungumzia mradi wa uendelezaji wa miji kimkakati. Katika eneo hili sihitaji kusema mengi sana. Geographical position ya Chalinze inajieleza, wala sihitaji kueleza kwamba kuna maji, kuna kitu gani. Sielewi wanapozungumzia mikakati ya uendelezaji wa miji kimkakati, maana hapa ni strategical development ambayo tunaizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji kama wa Chalinze ambao sasa hivi umeendelea kupanuka na idadi ya watu imeendelea kuwa kubwa, viwanda vimeendelea kushamiri na maendeleo ya mmoja mmoja yameendelea kuwa makubwa; mipango miji, mahitaji ya kijamii kuanzia kwenye upande wa mahitaji ya masoko, afya, elimu na miundombinu yameendelea kuwa ni mahitaji ya muhimu sana kwa mji ule. Hata hivyo, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri niliposoma ametaja maeneo mengine lakini Chalinze sijaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tu kujua ni mkakati gani alionao Mheshimiwa Waziri katika miji kama hii ambayo kwangu mimi naona kama ndiyo sehemu ya kupumulia kwa Mji mkubwa kama wa Dar es Salaam kwa sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo, lipo jambo ambalo pia limekuwa kizungumkuti na nafikiri kwa namna moja ama nyingine tumelizungumza sana katika vikao vya maendeleo ya Mkoa, hili jambo la TARURA. Ni kweli TARURA imeanza kufanya kazi na matunda katika baadhi ya maeneo tumeyaona. Hata hivyo, sisi ndani ya halmashauri ambako ndiko tunakoibua miradi ile mara nyingi tunapokuja kutekelezewa miradi ile na TARURA hatuoni ile tija ya yale ambayo tumeyakusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja; iko barabara inayotoka kwa Ruombo mpaka Kijiji kinachoitwa Kwa Mduma. Barabara hii umbali wake unakaribia kufika kilometa 12, lakini ilipopelekwa katika TARURA, ilipokamilika zilizokuwa zimetengenezwa ni kilometa nane tu. Sasa tunaomba tujue, hii mipango ya TARURA inakaakaa vipi? Wanajipangaje na je, ni lini tunaweza tukafikia malengo tajwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia tunatambua uchache wa fedha katika eneo hili. Kwa hiyo nafikiri siku nyingine tukikaa na TARURA wetu hawa, tukaenda kwa pamoja, tujadiliane nao juu ya vipaumbele ambavyo wananchi wanavitaka halafu wao watuambie. Sisi tunaposema barabara ya kutoka kwa Ruombo kwenda kwa Mduma maana yake tunaelewa umuhimu wa barabara ile. Sasa mtu akija akitengeneza barabara ile ya kilometa nane halafu yale malengo ambayo tunayakusudia sisi kama Halmashauri hayafikiwi nina uhakika kabisa hata malengo hayo ya Serikali Kuu pia hayatafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo pia, niendelee kuipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inayoendelea kufanya katika kuhakikisha kwamba tunahakikisha halmashauri zetu zinapata mapato ya kutosha. Mheshimiwa Waziri katika hatua hizi ningeomba sana tuendelee kuangalia vyanzo vipya tena, tuendelee kuhamasisha halmashauri zetu ziendelee kupata maendeleo katika kutatua au kuamsha vyanzo vilivyo vipya. Wameeleza waliotangulia hapa kwamba katika fedha ambazo zimepelekwa ndani ya Halmashauri zetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba ya Kamati hizi mbili; Kamati ya Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Sheria Ndogo katika kuweka mambo sawa juu ya sheria zetu na mambo yanayoendelea ndani ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi kabisa, naomba niruhusu nianze kwa kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili, Mheshimiwa Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo na Mheshimiwa Mchwengerwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Hakika kazi zao zinaonekana na binafsi napenda kuwaambia kuwa waendelee kupambana hivyo hivyo kwa sababu sheria inataka wasimamizi wazuri kama wao na wanafanya kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nishukuru na kupongeza sana sana Kamati ya Katiba na Sheria kwa jinsi ilivyoendesha mchakato wa usimamizi wa utungaji kama si urekebishaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Hakika mchakato ule ulikuwa mgumu kutokana na makundi mengi kuwa na interest katika jambo lile. Kwa kweli jinsi mchakato ulivyoendeshwa vyama na wadau walivyoweza kushirikishwa mpaka mwisho tumekuja kupata marekebisho yaliyotokana na lile pendekezo la Serikali, kwa hakika ni jambo zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwaambia wanasiasa wenzangu kwamba siku zote tusitegemee kupata kitu kilichokamilika kwa asilimia mia moja isipokuwa kwa hii hii asilimia 90 tuliyoipata tushukuru na pale kwenye upungufu basi twende katika taratibu za vyombo vya sheria ili kuweza kupata kilicho haki yetu au kile ambacho tunakiona kimekosewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, niendelee kuzungumza na Mheshimiwa Waziri wa Sheria, mara zote tunapokutana kwenye Kamati ya Sheria Ndogo kilio chetu sisi kama Wanakamati kimekuwa ni dosari zinazojitokeza katika utungaji wa sheria. Makosa ya kiufundi katika uandishi, makosa ya kutotambua au kutoangalia sheria mama inasema nini, makosa ya kiuandishi kwa maana ya copy and paste na kusahau mamlaka, ni mambo ambayo yamekuwa yakiendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa mawazo na maoni yetu katika mchango wetu kikao kilichopita kwamba Wizara yenu Profesa wangu, Mheshimiwa Kabudi ijikite zaidi kuangalia jinsi gani inatengeneza waandishi wazuri ambao watakuwa na weledi wa kutosha ili siku nyingine tutakapokuja tuwe na kazi ya kuelezea mazuri au upungufu wa kisheria na si ya kimuundo kama ambavyo tumekuwa tunafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Kamati yetu hatuna wataalamu wa kutunga sheria, hivyo Waziri kupitia ofisi yake anaweza kutusaidia kufanya kazi hii ya kuweka vizuri miundo ya kuangalia vizuri dosari zinazojitokeza ili tuendelee kuwa wenye kufanya kazi ndogo ambayo imetuleta Bungeni. Bungeni hapa hatukuletwa kwa ajili ya kuangalia miundo tumeletwa kwa ajili ya kutunga sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, niendelee kuishukuru Serikali katika kufanya kazi yake kubwa imeendelea kukamilisha miundombinu ya Mahakama. Pamoja na kazi nzuri ambayo imeendelea kufanywa hakuwezi kuwa na Mahakama kusipokuwa na nyumba na nyumba hiyo lazima watu wakutane ili haki ziweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zama hizo haki zilikuwa zinatolewa chini ya miti lakini katika dunia ya sasa Mahakama zetu zinahitaji majengo mazuri, teknolojia za kisasa pamoja na kuwa na miundombinu rafiki zaidi ili kusaidia ile shughuli ya kutoa haki iweze kufanyika. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo ameendelea kulisimamia jambo hili lakini pia nimeona kupitia hotuba ya Kamati na taatifa mbalimbali za Wizara kwamba kuna Mahakama za Mwazo zaidi ya tano ambazo zimeshakamilika ikiwemo ile Mahakama ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya watu wa Bagamoyo nitumie nafasi hii kukushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu watu wetu wakati mwingine walikuwa wakitamani wakae nje ya Mahakama kwa sababu ya kuogopa kuangukiwa na dari za majengo ya Mahakama hizo. Pamoja na hilo, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo ameendelea kutoa mchango mkubwa sana katika tasnia ya sheria lakini pia kuonesha kwamba ni Profesa wa Sheria na kuendelea kusaidiana nao kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Kamati yetu imeweza kuangalia na kutoa mapendekezo mbalimbali ya jinsi sheria zinavyoweza kukaa vizuri. Hata hivyo, bado upo upungufu ambao unaendelea kuonekana hasa katika sheria, kwa mfano, ile ya Baraza la Sanaa ambayo mapendekezo yake tumeyatoa na kupitia Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe tulimpa taarifa. Binafsi nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe kwa sababu alishafika mbele ya Kamati yetu na kueleza hatua ambazo zimeshachukuliwa na kwa kweli sisi kama Kamati tumeridhika. Namwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kusimamia tasnia na wasanii wetu ili waendelee kunufaika naye. Pamoja na hilo, yapo mapungufu ambayo tumeendelea kuyaeleza kama ya kiuandishi na kimuundo ambayo yanatakiwa yawekwe sawa ili sheria ile iweze kuchukua nafasi ya utelelezaji na tusije tukapata mikwamo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limeelezwa jambo lingine juu ya kodi zetu kuwa si rafiki. Katika kitabu cha hotuba ya Wizara ya Sheria imeelezwa kwamba ipo baadhi ya migongano inayotokana na sheria ambazo zipo katika maeneo mengi, hasa katika sheria za vijijini kama zilivyoelezwa na Mheshimiwa Getere hapa, leo hii kuna baadhi ya vijiji ikionekana mtu amejenga nyumba ya bati basi kuna ushuru mkubwa kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimkumbushe tu Mheshimiwa Waziri katika utaratibu ambao tumeshajipangia ni kwamba nchi hii kakuna mtu ambaye atatozwa kodi mara mbili. Ipo kodi tunayolipa tunapokwenda kununua mabati na cement, je, iweje leo hii tufike sehemu ya kulipa kodi nyingine ambazo ziko kinyume na utaratibu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini si mwisho kwa umuhimu, ziko baadhi ya sheria ambazo zinahitaji sana marekebisho. Katika kitabu chetu cha hotuba ya Kamati ya Sheria Ndogo zimeelezwa na jinsi ambavyo zimeendelea kuonekana zinakinzana na sheria mama lakini pia zinakinzana na sheria nyingine zilizopo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nami nianze kwanza kwa kumpongeza sana mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; pia kipekee kabisa, niendelee kumpongeza, hasa kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa Siku ya Wafanyakazi. Kwa hakika sisi ambao tumeajiri watu wawili, watatu, imetupa matumaini makubwa sana juu ya mwenendo wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachowaomba sana Waheshimiwa Mawaziri na watumishi wa Serikali, wafanye kazi nzuri na iliyotukuka ili ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu tunayempenda sana ya kuwawekea mafao mazuri watumishi wetu itakapofika tarehe 10, mwezi wa Tano mwakani iweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, niongeze pia kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, ndugu yangu, Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa hakika Wanachalinze kwa kipekee kabisa tunaendelea kumshukuru na kumpongeza kwa sababu matokeo chanya au matokeo mazuri ya miradi ya maji kwa kuondoa kero za maji Chalinze yanaonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hakika nataka nikupe taarifa kwamba leo tunaposimama hapa Halmashauri au Wilaya ya Chalinze imeendelea kukushukuru wewe na kukuombea Mungu kwa sababu maji yanatoka vizuri sana katika maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba yangu leo inajikita katika kukumbusha, siyo kulalamika kama ilivyokuwa zamani, kwa sababu mambo mazuri yameendelea kufanyika katika eneo letu lile. Mheshimiwa Waziri, katika eneo la Halmashauri ya Chalinze ipo miradi ambayo imeanza, lakini kwa maelezo au maoni yangu, naona bado kidogo speed haijaniridhisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, upo mradi wa mabwawa makubwa ya maji kwa ajili ya kunusuru hali ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Kibindu. Mheshimiwa Waziri, ninachokiona ni kwamba mradi ule bado umeendelea kuwa unakwenda taratibu sana. Natambua kwamba watu wa RUWASA ambao wako chini yako wamefanya kazi ya feasibility study na hata maombi ya bajeti yalishaletwa kwako. Ninachomwomba Mheshimiwa Waziri, baada ya kukupitishia mafungu haya, basi jambo hili liwe moja katika vipaumbele vya kwanza kabisa kwenda kuvitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, pamoja na hilo, ipo miradi midogo mingine inayoendelea katika maeneo mbalimbali, ukiwemo mradi ambao juzi juzi Kamati inayoongozwa na ndugu yangu, Mheshimiwa Humphrey Polepole, ilikuja kuona Kata ya Ubena pale, mradi ambao uko katika Kijiji cha Tukamisasa na unaoenda katika maeneo ya Makao Makuu ya Kata ya Ubena, nao bado unaendelea kusuasua. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, uiangalie miradi midogo kama hii ambayo inakwenda kutatua kero za watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo natambua pia katika mafungu ya Mheshimiwa Waziri, yako mafungu kwa ajili ya kurekebisha malambo yetu ambayo yanaendelea kujaa michanga katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Chalinze. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri hili nalo liwe kipaumbele kwako ili wananchi wa Chalinze kama walivyo maeneo mengine, waendelee kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Waziri ameeleza juu ya msaada mzuri na muhimu sana unaotoka katika Serikali ya India ambao wametenga zaidi ya shilingi bilioni 13 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maji nchini. Hata hivyo namkumbusha Mheshimiwa Waziri, katika Awamu ya Pili ya Mradi wa Maji wa CHALIWASA, unaotoka Wami kwenda Chalinze, iko component ya ujenzi wa matanki makubwa ya maji ambayo mpaka leo bado yameendelea kusimama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipita katika maeneo kama ya Kibiki, Pera na Mazizi katika Kata ya Msata unaweza kushuhudia mwenyewe kwamba yako mahitaji makubwa ya ukamilishaji wa matanki haya. Haya ninayoyataja ni baadhi ya matanki kati ya matanki mengi ambayo yanatakiwa kujengwa katika Halmashauri ya Chalinze. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tunapokwenda kupitisha bajeti yake hii, hebu ujenzi wa matanki haya uishe mara moja kwa sababu haiwezekani kuwa kilio cha Wanachalinze kila siku ni kuwa na maji ya uhakika na wakati maji yao yanaweza kupatikana kwa ujenzi wa matanki haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo anaendelea kuangalia ustawi wa maji katika eneo la Tanzania yetu kwa kujua kabisa Tanzania inaendelea kufarijika naye mtoto wa Kitanzania anayeamua kupigania maisha ya watu kupitia eneo la maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, naomba nimsisitizie Mheshimiwa Waziri juu ya jambo ambalo tumekuwa tunalizungumza sana mara kwa mara. Serikali ilibuni Mradi wa Maji wa Bwawa la Kidunda, bwawa ambalo kwa namna moja au nyingine linaunganisha Mkoa wa Morogoro na Halmashauri ya Chalinze kwa maana ya Mkoa wa Pwani. Ujenzi wa bwawa hili ndiyo utatuzi wa maji katika eneo la Pwani, Dar es Salaam na mikoa ya jirani kama ambavyo mradi utakuwa umeelekezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, anajua mradi huu utakapokamilika mradi wetu wa maji wa Ruvu Chini na Ruvu Juu, hautakuwa na ukakasi wa kwamba ipo siku maji yatakauka, kwa sababu mradi huu wa maji utakapokamilika unatarajiwa kuchukua maji yasiyopungua lita milioni 200 kama sikosei. Ukamilishaji wake maana yake utasaidia, hata kama pakitokea kiangazi cha namna gani, maana yake maji yakikauka katika Ruvu yatakuwa yanafunguliwa na kupelekwa Ruvu na wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wataendelea kufaidika na huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nmwomba sana Mheshimiwa Waziri, wanapokaa na kubuni miradi ya maji hasa kwa maeneo yenye watu wengi kama Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, hili ni eneo muhimu sana, na pia ukiangalia Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa miradi midogo na mizuri ambayo anaendelea kuisimamia. Pia naomba, kwa wajomba zangu na shemeji zangu kule Same, ule mradi wao ni muhimu sana. Nimeona jinsi ambavyo ulivurugika kwa mara ya kwanza. Mimi sio engineer lakini ukiusoma mradi ule, unajua tokea kwenye design ya mradi ule kulikuwa na matatizo. Sasa naamini kabisa, katika kipindi cha miaka sita Mheshimiwa Waziri alichokaa katika Wizara hiyo, ameweza sasa siyo tu kuwa mwanasiasa, pia amekuwa engineer wa maji kwa maana ya kwamba sasa hata tukizungumza gravitational force kwa ajili ya kupitisha maji tunamaanisha kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namtakia kila la heri ndugu yangu, Mheshimiwa Waziri, nawombea sana katika utekelezaji wa majukumu yake na mwisho nimtie moyo kabisa, asiwe na wasiwasi, ndugu zake tupo, tutaendelea kumwombea Mungu na kumsimamia kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami ningependa sana kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika mjadala huu wa Sheria Ndogo juu ya mabadiliko au mapungufu ambayo tumeyaona katika uchambuzi tulioufanya ndani ya Kamati yetu. Leo sitakuwa na mengi sana ya kusema isipokuwa ni kukumbushana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya msingi ambayo yamekuwa mara kwa mara tunapoleta taarifa zetu hapa yamekuwa yanatokea. Jambo la kwanza ambalo kwangu mimi ninaona ni la kwanza kwa umuhimu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo nyingi zinazoandikwa zimeendelea kuwa sheria zinazokinzana na hali halisi kwa maana ya utekelezaji wa majukumu yake. Kwa mfano, ipo sheria ambayo ndani ya taarifa yetu inaonekana inahusu Sheria ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sheria ile yameelezwa masharti ambayo mvuvi au mfanyabiashara wa samaki anatakiwa kuyatimiza ili aweze kupata vibali kwa ajili ya kufanya biashara hiyo, lakini kwangu mimi na wenzangu ndani ya uchambuzi wetu tumelitazama jambo hili katika upanda wake hasa katika lile hitaji la kumfanya huyu anayeomba kibali kwa ajili ya kufanya biashara hiyo aweze kuwa na vitambulisho muhimu ikiwemo kile cheti kinachoonesha uthibitisho wa yeye kuwa amezaliwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sheria zetu za nchi sasa hivi ni wazi zimeweka kwamba mwananchi ili aweze kuthibitishwa mojawapo lazima awe na kitambulisho cha uraia, lakini bado sheria hii inataka kuangalia zaidi ya kile kitambulisho chake cha uraia, kwa maana ya kuthibitisha kama ambavyo wenzetu nchi nyingine wanafanya, tukitolea mfano kwa mfano Japan kule ambapo mtoto au mimba tu inapotungwa tayari mzazi anapewa kitabu na kijiji kinamsajili kwa maana ya kwamba sasa kuna kiumbe kipya tunamtarajia katika maeneo hayo. Sheria ambayo katika Tanzania haipo na wala haizungumzwi hivyo, masharti yenyewe yalivyowekwa ni magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande mwingine imeelezwa hapa sheria hii inamnyima haki yule mvuvi wa kawaida aliopo pale Kigoma aweze kufanya biashara hii. Kwa sababu inamtaka mvuvi huyo aweze kufungua kampuni, lakini kwa kufungua kampuni maana yake pia anatakiwa awe na tin number. Sasa Bunge lako linajua hali za wavuvi wetu, lakini pia ni moto wa Serikali yetu kuona jinsi gani inawasaidia wale wanyonge wa Tanzania ili waweze kujikomboa katika hali ya umaskini walionayo. Sasa leo hii mtu mwenye mifuko yake miwili ya samaki naye pia anatakiwa awe na hivyo vibali jambo ambalo kwa kweli kama kamati tuliona haliendani na hali halisi ya maeneo yetu haya ambayo tunaishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu pia lipo jambo la sheria zetu hizi kusahau msingi wa uandishi au utungaji wa sheria zetu yaani drafting principles. Mara kwa mara tunaposimama Bungeni hapa tunaendelea kukumbusha Serikali, wakati mwingine sheria hizi si jambo la dharura ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa maana ya kwamba wanatakiwa wakae chini, watunge sheria wakiwa wametulia, wakague katika principles kama zimetimia, lakini kila siku zinapokuja sheria kumekuwa na mapungufu hayo kwa hiyo kwangu la msingi zaidi narudi tena kuikumbusha Serikali, utaratibu wetu ulivyo upo wazi, sheria hizi wanaanza wao wenyewe katika Ofisi za Attorney General huko kuzitengeneza siamini kwamba sheria hizi labda zinaandikwa na mtu mmoja na kwamba zinafika hapa iwe sisi kazi yetu badala ya kusimamia maendeleo ya nchi iwe kazi yetu kuangalia na kugundua makosa yakiwemo yale ambayo yanatakiwa ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu yawe yanaangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia yapo matatizo mengine ambayo sheria hizi zinakosewa sana na katika jambo kubwa ambalo kwa wanasheria tunasema hizi ni fundamental error katika uandishi au tafsiri ya sheria ya kukosea kuweka vifungu vinavyohusika au vifungu halisi katika sheria. Kwa mfano, yapo baadhi ya majedwali yanaonekana katika uandishi huu, mtu kwa mfano jedwali la kwanza la sheria linanukuu kipengele au kanuni ya tatu ya sheria wakati Kanuni halisi ya jedwali hilo labda ni kanuni ya nne. Kwa hiyo imekuwa mara kwa mara jambo hilo linatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sheria kwa mfano nikizungumzia kwa sheria hii ya samaki maana yake kwa yeye ambaye anataka kwenda kutafuta hivyo vibali maana yake akienda akitumia sheria hii ni wazi anakuwa yuko nje ya utaratibu na anaweza akajikuta sheria yenyewe pia haiwezi kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo mwisho kwa umuhimu naomba niikumbushe tena Serikali lakini hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuendelea kukumbuka kwamba nchi hii katika sheria zake zinaanzia kwenye Katiba ambayo ndiyo Sheria Mama na ndiyo mwongozo wake, lakini siyo Katiba peke yake, lakini pia kwa Sheria Ndogo zinaanzia kwenye Sheria Mama ambayo inampa mamlaka yule ambaye anakwenda kutunga Sheria Ndogo hizi, lakini mara nyingi sana kumetokea matatizo ya kwamba waandishi wetu wanasahau kwenye uandishi mamlaka hayo au kutambua mamlaka hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu kutambua mamlaka pia tumeona katika baadhi ya sheria, zikiwemo sheria zile zinazozungumzia masuala ya mazingira kwamba unakwenda unakuta sheria ambayo inapewa references haifanani kabisa na sheria ambayo imeletwa mbele yetu kama Kamati yako ya Sheria ya Bunge. Kwa hiyo, kwangu nilianza kusema kwamba leo nasimama kuendelea kuikumbusha Serikali yapo mambo ya msingi ambayo ni lazima yaendelee kuangaliwa katika utunzi wa Sheria Ndogo hizi na katika mambo hayo ya msingi zaidi ni kuendelea kukumbuka wapi mamlaka imetolewa, lakini pia zile principles za drafting za sheria zetu pia kuangalia kwamba sheria zenyewe zinaendana na hali halisi ya maisha ya Watanzania ambao wanakwenda kuathirika kwa namna moja au nyingine na sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja ya Kamati. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi niungane na wenzangu kukupongeza. Pamoja na hayo yote pia niendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya yako na unavyoendelea kutuongoza.

Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja nzuri iliyowekwa mezani hapa na Kamati yetu, kwa sababu ukiangalia hoja zao zote wametoa mawazo mazuri. Mawazo ambayo yanaendelea kutuimarisha sisi kama Wizara ya Ardhi, lakini pia kuishauri Serikali juu ya nini kifanyike. Yapo maeneo ambayo nataka nichangie kidogo ili kuweka zile taarifa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza limezungumzwa hoja ya kukwama kwa miradi mikubwa minne ya Shirika la Nyumba. Pale katika Mkoa wa Dar es Salaam wakimaanisha Plot No. 300 ya Regent, Plot No. 711 na nyingineyo ikiwemo ya Morocco Square.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika moja ya mawazo mazuri yaliyotolewa na Kamati ni kwa…

Mheshimiwa Spika, nisamehe kidogo unajua tumeshazoea. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Hakuna neno Naibu Spika ni msaidizi wangu kwa hiyo usiwe na wasiwasi. (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wewe ndio mkuu wa Mhimili basi watu wote wako chini yako.

Mheshimiwa Spika, nataka nieleze kwamba Serikali imefanya juhudi kubwa sana kuhakikisha kwamba, miradi ile inakwamuka kutoka pale ilipokwama ili sasa iweze kukaa vizuri. Katika hatua ambazo tumefanya ndani ya Wizara ilikuwa ni kuomba Serikali itupe ruhusa, ya kuchukua fedha au kupata fedha kutoka ndani ya vyanzo vyetu. Ikiwepo almost karibu Shilingi bilioni 700 ili twende tukafanye utaratibu huo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan akaelekeza Kamati, inayosimamia madeni iangalie vizuri juu ya yale ambayo sisi tumeyaomba. Katika kuchakata kwake ikaturuhusu tukope, Shilingi bilioni 44.7 ili tuweze kumalizia miradi hiyo. Katika fedha hizo ambazo zilielekezwa Shilingi bilioni 19 ilikuwa ni kwa ajili ya mradi uliopo katika Plot No. 300 na iliyobakia iende kumalizia Morocco Square.

Mheshimiwa Spika, juu ya lile eneo la Kawe maelekezo yako wazi kwamba, tukae na mbia katika ule Mradi wa Kawe ili tuweze kuzungumza naye na baada ya kumaliza kuzungumza naye, basi makubaliano tutakayokubaliana nayo tuone tunakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa mpaka sasa baada ya mikutano mitatu ni kwamba mbia wetu anakwenda kuwasiliana na wenzake ndani ya Bodi yao, ili yatakayokuwa yamekubaliwa basi tuje kuzungumza kwa pamoja ili tuweze kwenda vizuri. Kwa faida ya kikao hiki eneo ambalo limejengwa yale maghorofa unayoona Kawe pale, ni eneo ambalo miliki yake iko chini ya National Housing. Kwa hiyo, mazungumzo yanayofanyika ikiwezekana ni kutoa kile kipande, cha lile eneo ili sasa tuweze kupewa nafasi sisi wenyewe. Tuweze kujenga majengo yale ili majengo yakae vizuri na Watanzania, wapangishe na yanayouzwa yauzwe ili sasa tuweze kupata faida ya mradi ule.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia ndani yake limezungumzwa na ushauri mzuri umetolewa na Kamati, juu ya Serikali kutochangia fedha katika miradi ya upimaji, upangaji na umilikishaji. Nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba, neno hili halina ukweli wowote. Serikali imekwishatoa fedha na maelekezo yametolewa juu ya kuhakikisha kwamba, miradi hii inakwenda kupangwa vizuri. Katika kufanya jambo hilo fedha Shilingi bilioni 50 zimetolewa na zimekwenda kwenye Halmashauri zaidi ya 44 ili Serikali au Halmashauri zetu zikapime vizuri maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa furaha kubwa zaidi katika bajeti inayokuja Serikali inapanga kutumia zaidi ya Dola milioni 150, ambayo ni sawa na Shilingi bilioni 400 kwenda kuwasaidia zaidi kuendelea kupanga nchi yetu. Pia kuendelea ku-finance hii miradi ya upimaji, upangaji na umilikishaji.

Mheshimiwa Spika, yako mengi ambayo Serikali inaendelea kufanya, lakini nataka niwahakikishie kwamba mifumo, iko tayari kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za ardhi nasi ndani ya WIzara tunaendelea kutoa elimu pale ambapo tunapata nafasi. Sera zile ambazo zimepitwa na wakati, zimeendelea kupelekwa katika vikao husika ili ziweze kuhusishwa. Halafu baada ya hapo Serikali au wadau mbalimbali, tuendelee kuhimiza katika mipango mizuri ya usimamizi wa ardhi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami nianze kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa na Kamati yetu na pia hoja zote mbili kwa maana iliyoletwa na Kamati ya USEMI na ile ya Utawala na Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli yamezungumzwa mengi sana nami binafsi yangu nataka kuchangia katika baadhi ya maeneo. Serikali ilikuwa inaongeza Bajeti mara kwa mara, na katika maeneo mengi sana tunashuhudia mabadiliko makubwa sana ya kimaendeleo hasa katika maeneo yanayohusu huduma za wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo, pia yako maeneo ambayo kwa kweli tunaweza kusema kwa namna moja au nyingine ongezeko hili la bajeti limeleta mchango ambao uko chanya kabisa kwa maana ya kusaidia wananchi wetu kama ambavyo imeelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, pia nataka niishukuru Kamati kwa kuweza kuangalia mambo ya msingi kabisa ambayo sisi kama Wizara kwa upande wetu yanatupatia nafasi ya kwenda kuboresha zaidi majukumu yetu, na kwa namna moja au nyingine kuendelea kuyafanyia kazi yale ambayo yanaonekana kuwa ni upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu mimi nataka niseme tu kwa niaba ya Serikali naunga mkono sana mawazo yote mazuri yalitolewa na watu wote waliochangia, lakini na mimi nataka niongezee kidogo katika maeneo hayo, kwa mfano katika hili eneo ambalo Kamati imeeleza kwamba walemavu ni kama wamesahaulika

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nilihakikishie Bunge lako, lakini pia kuwaambia umma wa Watanzania pamoja na Bunge lako kwamba, Serikali imeendelea kuwaangalia watu wenye mahitaji maalum katika maana ya ajira, lakini pia katika kuzingatia wanapewa kipaumbele kikubwa, hasa nafikiri katika upendeleo hasa katika eneo hili la utoaji wa ajira. Kupitia Gazeti la Serikali lenye kumbukumbu namba 326 ambalo lilieleza juu ya mabadiliko ya Kanuni ya 17 ya usaili wa katika eneo la watu wenye ulemavu ni kwa kweli, upendeleo mkubwa sana umefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikiri mbele ya Bunge lako kwamba, bado changamoto zipo katika baadhi ya maeneo, lakini kiukweli katika kipindi cha miaka mitatu zaidi ya watu wenye ulemavu 190 wameajiriwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo wanaume 108 na wanawake 82, wote wakiwa ni sehemu ya wafaidikaji. Lakini pamoja na hilo pia, nataka niunge mkono juu ya hoja iliyoelezwa na kamati yetu kuhusiana na malimbikizo ya madeni ya watumishi. Kwa kweli, kibinadamu haipendezi, inauma na ni wajibu wetu kama Serikali, ni wajibu wetu kama Bunge kuendelea kuwasemea watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nipongeze juhudi mbalimbali ambazo zimeendelea kufanywa na Serikali yetu, hasa baada ya kutambulisha mfumo wa mishahara na taarifa za kitumishi ambao kwa lugha ya kitaalamu unaitwa HCMIS ambao mfumo huu umesaidia sana kupunguza madeni, lakini pia na malimbikizo mbalimbali ambayo watumishi wetu walikuwa wanadai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hadi kufikia Disemba, 2023 Serikali imefanikiwa kulipa bilioni 210.67 ikiwa ni sehemu ya madai makubwa ya watumishi zaidi ya 125,147 ambao wamekuwa wanaidai Serikali. nataka nikuhakikishie katika fedha hizo ambazo zimelipwa, ndani ya makundi hayo, Serikali imelipa bilioni 157 kwa watumishi ambao walikuwa wanadai katika malimbikizo ya upandishwaji wa vyeo na kubadilishwa muundo wao wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mengi mazuri yamefanyika katika Serikali na ninataka Bunge lako niendelee kulishawishi kuamini kwamba, Serikali bado inaendelea kufanya mambo mazuri na hayo yanaweza kutafsirika katika eneo kama la bajeti ilivyoongezeka, hasa katika Ofisi yetu ya Rais, Utumishi ambapo asilimia 17 bajeti imeongezeka ambayo tafsiri yake imetafsiriwa katika eneo la kazi na ikiwemo mojawapo kwenye uundaji wa miundo au mifumo ya kiserikali, kuwezesha utoaji huduma nzuri kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu pia nataka niongee katika eneo moja ambalo limechangiwa na Wabunge wengi, hasa wakiongozwa na Mheshimiwa Janejelly Ntate ambaye alizungumzia hasa juu ya maslahi ya watumishi, hasa wanawake ambao wakipata likizo zao wamekuwa wanapunjwa, lakini wakati mwingine wanapata matatizo makubwa wanapoomba likizo hasa baada ya wenzetu kujifungua watoto njiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleza asubuhi juu ya utayari wa Serikali kukutana na wadau katika mabadiliko makubwa tunayokuja kuyafanya kwenye sheria zetu za utumishi, kuweza kuingiza kundi hili maalum ambalo linakwenda kutatua vilio vya walio wengi, akinamama zetu. Tunaamini katika nchi hii ambayo tuliamua kumpa Rais wa kwanza mwanamke, Dkt. Samia Suluhu Hassan awe kiongozi wetu kwa kuleta maendeleo, hatuwezi kuwaacha nyuma hawa ambao wanazaa watoto njiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuona unavyoshika kengele yako, maana yake muda wangu umetosha. Hoja nyingine zote kama zilivyotolewa na Kamati tunachukua, tutakwenda kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya. Pili, nampongeza msaidizi wake Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wote waliopo katika ofisi yake wakiongozwa na dada yetu shupavu, Malkia wa Nchi ya Ruvuma, Mama yetu Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na ndugu yangu, rafiki yangu, Mheshimiwa Deo Ndejembi. Kwa kweli, kazi nzuri inafanyika na sisi tunaendelea kuwaombea kwa Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu michango nane imeelekezwa katika Wizara yetu na hasa katika eneo la utumishi na pia katika eneo la Mfuko wa Kunusuru Umaskini (TASAF). Katika hii michango nane, saba ilielekezwa moja kwa moja katika eneo la utumishi, lakini mmoja ambao ulichangiwa na dada yangu Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, uliekezwa katika eneo la TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, naomba nianze kwa kuwashukuru sana wale wote ambao walitoa ushauri na sisi, kama Serikali, tumeuchukua ushauri wao na tutakwenda kuufanyia kazi. Katika watu waliotoa ushauri nawatambua wanne, akiwemo mjomba wetu Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate na wengine waliopata nafasi ya kuchangia Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge Neema Lugangira alitaka kujua Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kwamba, inaendelea kutambua na kuwasajili watu wanaoishi katika kaya maskini wanaostahili kunufaika na Mradi wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulihakikishia Bunge kwamba, Serikali imeendelea kufanya hivyo. Nataka nilikumbushe Bunge kwamba, katika Awamu ya Kwanza ya Utekelezaji wa Mradi wa TASAF utambuzi ulifanyika katika wilaya tatu ambazo ndiyo zilitekeleza mradi huu. Baada ya mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza, Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa utambuzi na sasa Wabunge wanaweza kushuhudia kwamba, katika awamu ya kwanza tuliweza kutambua watu kwa 70% ya makazi yao. Sasa hivi mradi huu umefikia 100% ambapo vijiji vyote, mitaa yote na shehia zote zimeingizwa ndani ya mradi na mambo yanakwenda vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya hali ya walengwa waliodumu kwenye mpango huu katika kipindi cha kwanza imefanyika kwa lengo la kuwabaini walengwa ambao wameimarika kiuchumi na kuwafanyia graduation, ikiwa ni katika utaratibu wa kuwaondoa ili wengine ambao wanatakiwa waingie nao tuwaingize katika kutimiza lengo la mapambano ya kuondoa umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia, nataka nitambue mchango mzuri wa Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara ambaye, ushauri wake umelenga katika kuboresha mishahara ya watumishi wa vyuo vikuu ili kuendana na majukumu yao. Nalihakikishia Bunge lako pamoja na wananchi wanaotusikiliza kwamba, Serikali imeendelea kuboresha mishahara ya walimu wa vyuo vikuu pamoja na watumishi wengine kwa kadri ya uwezo wa Serikali kibajeti unavyoruhusu. Katika kufanya hivyo, taratibu za kimsingi na miongozo ya kiutumishi imeendelea kuwa ndio kiongozi mkuu katika kufanya uhakiki wa mambo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge Athuman Almas Maige naye ameomba Serikali iendelee kuboresha Sheria za Kazi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kufanyia kazi. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na kazi nzuri ambayo imeendelea kufanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi ya kuendelea kuangalia mifumo na taratibu za Sheria ya Kazi, ili kuendana na taratibu za sasa, sisi kama Ofisi ya Rais, Utumishi tumeendelea nayo. Tunaangalia na kupitia miongozo na Sheria mbalimbali zilizopo za utumishi wa umma ili ziendane na matakwa ya Sheria ya Kazi na kuondoa vilio ambavyo vimekuwepo mara kwa mara kwa watumishi wetu hasa linapofika suala la kupandishwa madaraja na kuweka vizuri mambo ya mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Mbunge Nicholaus Ngassa ambaye ametumia nafasi yake kuishauri Serikali iangalie mifumo mizuri ya uhamisho wa watumishi ili kuweka vipindi vizuri vya kushughulikia masuala ya utumishi. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kipindi maalum cha miaka mitatu kama kilivyowekwa kwa ajili ya watumishi wetu kimeendelea kuangaliwa, lakini Sheria hiyo ya miaka mitatu haimbani mwajiri kumhamisha mfanyakazi endapo mazingira yaliyopo yanakwamisha utendaji wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kushughulikia masuala ya kiutumishi kwa kupitia njia mbalimbali za kimtandao. Kwa sasa matatizo yote ya kiutumishi yamewekewa siku 30 yaweze kushughulikiwa na kukamilika ili kuondoa kero za watumishi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru mchango mzuri uliotolewa na Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga ambaye ameikumbusha Serikali iendelee kuboresha maslahi ya watumishi wake, hasa katika Sekta ya Umma na Binafsi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Hasunga kwamba, hii Serikali ni pana, lakini Ofisi ya Rais inayosimamia Sekta ya Umma imeendelea kuangalia maslahi ya watumishi na kuyawekea msisitizo mkubwa. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara hadi kufikia 23%. Watumishi wote waliongezewa mishahara kwa viwango tofauti kadri bajeti ilivyoruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuweka kumbukumbu sawasawa, mwezi Julai, 2022, Serikali ilihuisha Waraka wa Posho ya Kujikimu kwa Safari za Kazi za Ndani na Waraka wa Posho za Kufanya Kazi kwa Muda wa Ziada. Mpaka sasa tunapozungumza, kwa upande wa Taasisi za Umma, Serikali imeendelea kuidhinisha mipango ya motisha ili kuwawezesha Watumishi wa Umma katika Taasisi za Umma kuweza kujikimu vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Anastazia Wambura ametaka kuona Serikali inaweka mikakati ya kupunguza uhaba wa walimu nchini, ili kuendana na mitaala mipya ya elimu. Serikali imeendelea kufanya zoezi hilo na katika kutatua changamoto hiyo watumishi katika Sekta ya Umma wameendelea kuajiriwa na pia tumeendelea kuboresha mishahara yao ili iwe kama motivation kwa watumishi wetu wote Serikalini. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imeajiri walimu 10,505 ili kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalihakikishia Bunge lako kwamba, kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika kazi hii itakuwa imekamilika. Katika mwaka ujao wa fedha ambapo bajeti yake tutaiwasilisha mbele yako hivi karibuni wiki hii, Serikali imetenga nafasi 10,590 za ajira mpya kwa ajili ya Kada ya Elimu ambayo nina hakika kwa asilimia kubwa inakwenda kutatua kero zilizo katika eneo hili hasa ya walimu, lakini pia katika maeneo mengine ndani ya ya halmashauri mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na michango mizuri iliyosemwa, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge, hasa waliochangia katika eneo hilo la utumishi kwamba, Serikali itaendelea kuangalia masuala ya kiutumishi na pia Mheshimiwa Rais ameeleza nia yake ya dhati wakati alipokuwa analihutubia Bunge. Katika kipindi hiki cha miaka mitano Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba, maslahi ya Watumishi wa Umma yanaendelea kufanyiwa kazi katika kuyaboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya ambayo yalielezwa au yaliombwa na Waheshimiwa Wabunge, tuyatolee maelezo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja kwenye Muswada na mimi kama Mwanasheria naomba niitendee haki professional yangu kwa kutoa masahihisho ambayo ningefikiri Mheshimiwa Waziri akiyachukua yatatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nianze na section six (6). Mheshimiwa Waziri section six (6) inatambua vyombo vya habari vilivyopo katika mtazamo wangu hasa nikitazama katika Sheria ya Mawasiliano inatambua uwepo wa community radios, lakini cha ajabu sana, Muswada huu hautambui hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeomba Mheshimiwa Waziri wakati anajumuisha atueleze kama community radio ni sehemu ya public on the media au ni private on the media kwa sababu hizi sizielewi. Pia nitoe angalizo zaidi, kwa kuwa sheria hii inakwenda kubadilisha sheria zote ambazo zinahusiana na maeneo ya redio na mahusiano katika printing medias, ningeomba sana nitakapomaliza jambo hili, basi pia tugeuke katika Sheria ya Mawasiliano ili kuweka uwiano ulio sawa, kwa sababu yatakapoanza mambo ya kesi tunaweza tukapata shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo section seven (7) kwenye obligation za media houses. Kwa mujibu wa dhana nzima ya utengenezwaji wa sheria hii inaonesha kwamba inataka kuleta kitu kinachoitwa transparency and responsibilities. Hata hivyo, nikiangalia katika vitu vyote hivi, sioni eneo lolote ambalo linagusia accountability and transparencies hasa katika upande wa management of funds. Kwa hiyo, ningeomba tutakapokuja kurekebisha jambo hili basi Mheshimiwa Waziri aliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije Part III ya Muswada wetu, katika Part III section 11 inaeleza muundo wa bodi, lakini kilichonishangaza mimi section 14 and 15 inaelezea kwamba kutakuwa na mtu anaitwa Director General wa Bodi hiyo, ambaye pia atakuwa ndiyo Chief Executive Officer. Cha ajabu zaidi, yeye si Mjumbe katika Bodi hiyo, sasa mnakuwaje na bodi ambayo Katibu wake si Mjumbe na yeye Mtendaji Mkuu wa kila kitu katika hiyo. Kwa hiyo, pamoja na hayo mazuri, Mheshimiwa Waziri angeliangalia hili jambo na atakapokuja atueleze kidogo tuone limewekwaje vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo section 29 nakwenda haraka haraka Mheshimiwa Waziri naomba anisikile vizuri. Section 29 ni suala tu la language shake. Kuna kitu hapa ninavyotazama kwa kingereza changu cha Kikwere, naona kuna kitu kinatakiwa kiongezwe pale. Sentensi inasema: “There shall be a secretary to the Council who shall be appointed by the Council through competitive recruitment.” Kiingereza nafikiri kuna neno linakosekana pale ambalo ningekuomba uongeze neno process ili sentensi ile ikae vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo section 31 inazungumzia jambo la kumwondoa Katibu. Tunaposema kwamba Katibu anaweza kuondolewa on any other ground that may justify removal, kwa kweli binafsi yangu kuna watu wanafukuzwa kwa sababu tu wana sura mbaya. Sasa katika misingi ya haki za binadamu Mheshimiwa Waziri haiko sawa, nafikiri ni vyema sheria ikaeleza sababu zinazoweza kumtoa mtu.
Mheshimiwa Mwenyekit, hata ukiangalia kwenye sheria nyingine hata unapotaka kumwondoa Judge, unapotaka kumwondoa Wakili, unapotaka kumwondoa Daktari, unapotaka kumwondoa mtu yeyote yule, hakuna sehemu inayosema any other ground that may justify removal. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu unaweza kuweka wakati mwingine hata kwamba; watu wakafika sehemu ya kikabila au ya kidini ikawa pia ni sababu tosha ya kumwondoa mtu. Pamoja na hayo pia, nataka niongee jambo moja la kisheria zaidi, katika maelezo inaonesha wazi kwamba hii sheria yetu inalenga kuelekeza pia mahakama iweze kutunga sheria juu ya masuala ya defamation. Mheshimiwa Waziri, naomba nimkumbushe jambo moja mahakama ina taratibu zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa adabu kubwa sana na kwa niaba ya watu wa Chalinze naomba kuunga mkono hoja, asante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba nzuri na mijadala mizuri ambayo inaendelea sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mwanasheria ningeomba nijikite moja kwa moja katika kuzungumzia sheria na sio mipasho kama wenzangu wengine waliotangulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya Pili ya Muswada wetu inazungumzia sheria ya vyombo vyetu vinavyoruka, lakini Sheria hii inampa mamlaka yule Mkurugenzi Mkuu wa viwanja vya ndege nafikiri kama tafsiri yake itakuwa sahihi, kuweza kukamata ndege, kuomba reflection na hata pia kuita ndege kama ikiwa inataka kuondoka katika kile ambacho kisheria kinatamkwa kwamba kufikiria kwamba kuna tatizo katika ndege hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ni Mwanasheria na napenda sana haki na haki ili itokee msingi mkubwa zaidi ni kufuata utaratibu wa kufanya maamuzi katika utaratibu wa Kimahakama. Katika lugha fupi tunasema katika judicial proceedings, sasa mtu mmoja kukaa ofisini na kufikiria kwamba ile ndege ina tatizo fulani aka-order hiyo ndege iwekwe chini au isiondoke, binafsi yangu sioni kama liko sawa. Isipokuwa kwa kuwa Mwanasheria Mkuu anajua nia madhubuti ya kutengeneza jambo hili, ningemwomba atakapokuja kutoa majumuisho basi atueleze nia ya Serikali juu ya jambo hili kabla hatujaamua kupiga kura na kupitisha au kukataa kipengele hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi niseme kwamba kipengele hiki kitatuweka kwenye matatizo. Kuna ndege kubwa ambazo hizo tunazijua hasa zile za nje zinataka ziende kufanya connection kwa maana ya transit huko nje. Ukiziweka hapa zinaweza zikachukua muda mrefu na baadaye tuka discourage hata usafiri wa watu wanokwenda nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia kipengele kidogo kipya cha 19A ambacho kimeongezwa, binafsi yangu sijakielewa. Ningemwomba Mheshimiwa AG atoe maelezo ya kutosha katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia niwapongeze kwa kuweka vizuri utaratibu wa kukusanya fedha za wale ambao wamekopeshwa katika waliokwenda kusoma elimu ya juu. Pia niungane na wenzangu wa mwanzo kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba kipengele cha kuwaambia wanafunzi walipe baada tu ya kumaliza masomo yao kwa kweli hiki hakijakaa vizuri na sababu kubwa kwangu ni hii ifuatayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu matatizo ya kupatikana kwa ajira kwetu bado yameendelea kuwa ni mtihani mkubwa na pia wanafunzi hawa wanapomaliza mpaka wajipange waweze kupata uwezo wa kuanza kulipa nao wakati mwingine imekuwa ni mtihani mkubwa sana. Ningeomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu, pia aangalie kama Serikali uwezo wa kufungua milango mizuri ya ajira ili vijana hawa wapate kurudisha fedha mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niipongeze sana Serikali kwa kuleta Sheria ya mabadiliko katika Public Service Act. Waheshimiwa Wabunge mnaweza kukumbuka, katika Bunge lililopita, kumekuwa na shida kubwa sana na hata kulalamika sana kwa baadhi ya Wabunge nikiwa mimi mmojawapo juu ya marupurupu wanayojilipa hawa ambao wanajiita wafanyakazi na wanachama wa Bodi mbalimbali zile ambazo Serikali Kuu haina mkono mrefu ndani yake. Tumeshuhudia malalamiko hayo wafanyakazi wengi na bodi nyingi zikienda kufanyia Hong Kong, Marekani na maeneo mengineyo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tija ya safari zao ikiwa hatuzioni, binafsi yangu niipongeze Serikali kwa sababu sasa ule mwiba au mwarobaini wa ugonjwa ule unaletwa sasa. Niipongeze Serikali kwa kuona kwamba kuna kila sababu ya kuendelea kusimamia mambo hayo. Sheria yetu katika mabadiliko madogo ya kipengele cha 8(3) ambayo inampa mamlaka Katibu Mkuu Utumishi ya kuoanisha na kuainisha mishahara, posho na marupurupu mbalimbali wanayojilipa hao wenzetu kwenye bodi huko na hata wakati mwingine ilipokuja kuambiwa kwamba Wabunge sio member wa board wengi tulilialia kwa sababu tunajua kwamba sasa mzee ulaji nao umekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo pia kupitia Sheria hii niipongeze Serikali kwamba, sasa inaweka uhusiano mzuri au uwiano mzuri juu ya mshahara, maana kuna bodi nyingine zilikuwa zinajipangia tu mishahara halafu unasikia tu huko kwamba “bwana Mkurugenzi wa Bodi fulani analipwa mabilioni ya fedha halafu kazi ambayo anafanya wakati mwingine haionekani” japokuwa kuna wengine najua watahuzunika kwa kipengele hiki. Binafsi niseme naunga mkono sana hoja kwenye kipande hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuendelee kuangalia maeneo mbalimbali na hasa tuzingatie zaidi yale maeneo ambayo mkono wetu au mkono wa Serikali usije kujikuta unaingia katika kukabiliana na interest nyingine. Mfano, katika eneo kama la Mahakama ambao wana chombo chao ni eneo ambalo kidogo ingebidi Serikali iangalie vizuri na kuona utaratibu utakapokuja basi tusiingie kwenye migogoro isiyo ya lazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia nizungumze kidogo katika jambo zima la mamlaka ya leseni. Niipongeze Serikali kwa kuleta sheria hii pia ninayo maneno machache ya kusema juu ya utaratibu wa kugawiwa kwa leseni. Nimeona pamoja na utaratibu ambao umewekwa pia liko jambo ambalo sasa ni jipya limeingizwa jambo la utoaji wa adhabu.
Mheshimiwa Menyekiti, ningemba sana Serikali inapokuja kutoa majumuisho hapa ione sababu ya kutenganisha juu ya nafsi hizi tatu katika utaratibu mzima wa uendeshaji wa vyombo vya moto. Natambua yako magari, wako wenye magari na wako watu wanaitwa madereva.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuhukumu gari kwa kosa alilofanya dereva si jambo zuri. Natambua kwamba, katika marekebisho yake Mheshimiwa AG ametenganisha jambo hilo, lakini bado adhabu kuondolewa kwenye magari ni jambo la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na mwisho sio kwa umuhimu sana, nizungumzie jambo la mazingira, Management of Environment Act, kwa kipindi kirefu sana hasa mimi ninayetokea Chalinze, nimekuwa nalalamika sana juu ya uharibu wa mazingira hasa katika eneo letu la Wami Mbiki. Mazingira yameharibika sana, kiasi kwamba imefikia sehemu sasa hivi hata wanyama wakali kama tembo wanafikia sehemu ya kuingia kwenye Mji wa Chalinze, kwa sababu tu mazingira katika maana ya njia zao, watu wameanza kujenga nyumba, pia ng‟ombe wengi waliojaa katika hifadhi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikusudii kusema kwamba ng‟ombe hawa hawafai, lakini nataka niwaeleze ndugu zangu, ukweli kwamba mifugo hii ya ng‟ombe imekuwa inaharibu sana mazingira. Leo hii, tunapozungumza hapa Bonde la Mto Rufiji, linataka kupotea, bonde la Mto Wami linataka kupotea, maeneo mengine mengi sana ya mabonde yetu na mito yetu nayo pia yanapotea. Nakumbushwa hapa kwamba kuna Mto unaitwa Mbwemkuru nao pia unapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana huyu Mheshimiwa Waziri wa Mazingira anapokuja, pamoja na kutuambia mambo mazuri haya, naomba ndugu yangu Mheshimiwa January Makamba atambue kwamba kilio cha uharibu wa mazingira kinagusa kila mtu. Mazingira yetu kama hatukuyaweka vizuri leo, kesho ndio kilio chetu kitakuwa kikubwa sana. Ningemwomba sana, pamoja na sheria hii ya management ya mazingira, basi atakapokuwa anatengeneza zile sheria ndogo aangalie juu ya uhifadhi wa mabonde yetu haya ili kwenda kuweka uoto wetu wa asili vizuri, maji yetu yapate kupatikana vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana naingalia Chalinze yangu na mradi mkubwa wa maji ambao tunatengeneza pale naweza kufika ndani ya miaka mitano tukabakiwa na mitambo mitupu halafu maji yakawa hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja ya Serikali lakini pia nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na Mawaziri wengine wanapokuja…
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Usuluhishi wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nikushukuru kwa kupata nafasi ya kueleza machache katika mchango wangu juu ya hii hoja tunayojadili sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba kwanza nianze kwa kuwatoa wasiwasi wenzangu. Aliwahi kusema konkara mmoja wa Eastern Europe anaitwa Bwana Ganji Skan alipokuwa anaingia katika Mji mmoja unaitwa Antanapolicy aliwaambia wananchi kwamba “The only time you can say you are late is when you‟re on death bed”. Kwa hiyo nataka niwaambie wenzangu kwamba hatujachelewa, na nafasi yetu tuliyonayo kama Wabunge ni kutunga sheria; na nafasi yetu pia kama Bunge ni kuishauri Serikali juu ya mambo ambayo ni ya msingi na tunaona kwamba yanatakiwa yawekwe katika sera na sheria ili nchi yetu iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba sana kwa wenzangu, hasa dada Salome nimemsikia anaongea kwa nguvu, na ndugu yangu Catherine ni ukweli mnaweza kuwa na uchungu lakini hamjachelewa nafasi ni yenu mseme na Serikali yenu ipo; Serikali sikivu inayoweza kuwasikiliza na ikafanya yale ambayo kwa maslahi ya Watanzania wanayataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasimama leo kurekebisha sheria ambayo inatoa mamlaka makubwa kwa nchi yetu kuweza kufanya mambo ambayo wananchi wetu wamekuwa wanayalilia. Ni ukweli usiofichika kwamba sheria hii baada ya kuisoma kwa muda mrefu na kujadiliana na Serikali ni wazi kabisa kwamba sheria hii inalenga kulinda maslahi mapana ya wananchi wetu. Kwa mfano, ndani ya vifungu vya sheria viko vifungu ambavyo vinatoa nafasi kwa mtu ambaye hakushirikishwa katika makubaliano au mijadala hiyo naye akapewa nafasi ya kuingia na kuwa sehemu ya majadiliano. Hii ni nafasi ambayo inawapa watu wanyonge nafasi ya kuweza kuingia katika mijadala na kulinda rasilimali zao, hususan katika rasilimali zaa ardhi. Kwa mfano tulipokuwa tunajadiliana tuliainisha wazi kwamba inakuwaje kwa mtu ambaye hakushiriki mjadala ule halafu baadaye mali inayokuja kuuzwa ni mali ambayo yeye anaishi juu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii ambayo tunaitunga leo inakwenda kutoa nafasi ya mnyonge huyu kuweza kujadiliana na kuweza kuonanafasi yake na pia kujua hii hatma ya maisha yake. Pamoja na hilo sheria inaanzisha kituo cha usuluhishi wa mijadala hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, wameeleza waliotangulia hapa kwamba sheria hii ipo tokea mwaka 1938; lakini ni ukweli kwamba vitu hivi havikuwepo. Leo hii tunapata nafasi ya kutunga chombo ambacho kinakuja kusimamia mijadala ya usuluhishi wa migogoro ya sheria za kimataifa. Ni opportunity pekee ambayo nchi yetu inapewa kupitia proposal hii au bill hii ambayo imeletwa na Serikali yetu hapa ili kuweza kutunga chombo au kuanzisha chombo ambacho kitahakikisha kwamba rasilimali zetu au mustakabali mzima wa usuluhishi unaoenda kuangaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia ni ukweli kwamba yapo mapungufu ambayo yameelezwa kama taarifa ya Kamati ilivyojieleza. Mimi kwangu ni kumweleza tu Mheshimiwa Waziri wangu wa sheria ayaangalie na kuyachukua mapungufu hayo ili aweze kutengeneza kitu ambacho kitakuwa na faida ya kweli kwa watu. Kwa mfano liko eneo ambalo linaeleza mara kwa mara role ya mahama zetu katika kuingilia makubaliano hayo. Mimi ninaamini kwamba Sheria ya Arbitration inalenga zaidi katika kuwawezesha watu wenyewe walioingia katika mikataba kuweza kuamua hatma yao. Sasa unapokuwa unairuhusu mahakama iwe na role kubwa ya kushiriki katika makubaliano binafsi ipo wakati unaweza ukajiuta ile dhana nzima ya sheria ya masuluhisho inaweza kukwama kwa sababu ya nafasi ambayo mahakama inayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, katika mijadala yetu umekuwa msikivu na umekuwa unatusikiliza sana na yako baadhi ya maeneo ambayo tumekubaliana; hebu ipe nafasi ile center iweze kushughulika na mambo kabla haujaamua kwenda kuishirikisha mahakama yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo katika mjadala wetu tuliona mambo makubwa ambayo tunafikiri yanalenga kufungua milango ya kiuwekezaji nchini kwetu. Sheria hii kwa upande mmoja au mwingine inafungua mlango mmoja na kufunga mlango mwingine kama si kuwa inaweza kukwamisha nia ya dhati ya wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaamini nafasi nzuri imefunguka hii na muda tunao wa kufanya marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja zote mbili; iliyotolewa na Kamati lakini pia ile iliyotolewa na Serikali kwa sababu ukizisoma unaona zote zinakwenda katika uelekeo mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa, natambua kwamba sheria iliyoletwa mbele yako mbele ya Bunge hili, ni mwendelezo au ni hatua katika utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa kimkataba baina ya nchi zetu mbili na washirika wengine tarehe 26 Mei, 2017 na kufuatiwa na mkataba mwingine au sehemu ya Addendum hizo iliyosainiwa tarehe 20 Mei, 2021 kule nchini Uganda na baadaye mkataba uliosainiwa Dar es Salaam na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni na Mama yetu Samia Suluhu Hassan pale Ikulu Dar es Salaam mapema wiki tatu zilizopita. Mimi naanza kwa kuunga mkono hoja lakini kuunga mkono hoja inaweza ikawa ni neno la Kiswahili kizuri lakini kwa lugha ya kisomi au lugha ya Kibunge nadhani ni vyema nikatumia nafasi hii kueleza ni kwa nini naunga mkono hoja hii. Yapo mambo ya msingi yaliyonisukuma kusimama mbele ya Bunge lako sio tu kuunga mkono lakini pia kuwashawishi Wabunge wenzangu tukubali kwa pamoja kuunga mkono hoja zilizowekwa mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, ukisoma vizuri sheria iliyoletwa, kwanza ni sheria ambayo inakwenda kutafsiri makubaliano hayo. Kwa hiyo, kama tutafanya utaratibu wowote ule, Wabunge wenzangu naomba niwakumbushe kwamba vipengele vya kisheria vilivyowekwa ni vinakwenda kutafsiri makubaliano hayo. Hakuna kitu kipya ambacho sisi kama Wabunge tunaweza tukasema kwamba hiki labda kuna mtu amekichomeka au amekitohoa katika maeneo yake bila kuangalia masharti ya kimkataba. Hili la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni ukweli kwamba sheria hii inakwenda kuangalia jinsi gani mkataba huu unakwenda kuwa implemented au kuhakikishiwa utekelezaji wake bila ya kuwa na kigugumizi chochote. Kwa mfano, katika sheria zetu za halmashauri ambazo zimeelezwa katika mchango uliotolewa na Kamati lakini pia na hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Attorney General, sheria zetu za sasa ukizingalia kama zilivyo na ukaamua kuzisimamia maana yake utakwenda kupata shida mbele katika utekelezaji. Mapendekezo yaliyoletwa yanaondoa kigugumizi hicho na kutoa nafasi kwa Baraza la Mawaziri, ikiwa linasimama kwa niaba ya Serikali yake, ikiwa linasimama kwa niaba yetu sisi kufanya maamuzi yaliyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwakumbushe kwamba hili si jambo linalofanyika kwa mara ya kwanza. Kama mnakumbuka vizuri tulikuwa na mikataba ya madini na kama mnavyofahamu nchi yetu ina maeneo mbalimbali yanayotoa madini. Wenzetu wa Geita kule wanazo sehemu wanazochimba madini, wenzetu wa Kahama kwa maana Shinyanga wanazo sehemu wanazochimba madini, wenzetu wa Mara kwa maana ya North Mara wanazo sehemu wanazochimba madini, kama Serikali hii isingefanya kama ambavyo inataka kufanya katika mkataba huu ikaziachia halmashauri husika au mikoa husika itunge sheria ili kuangalia jinsi gani mirabaha inapatikana katika maeneo yao, huenda mikataba ile isingefanyika kama ambavyo imefanyika sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Serikali zetu zilizopita zimefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba sheria zinasimamiwa na mirabaha ya wananchi inapatikana. Hili ndilo ambalo linaenda kufanyika katika upande huu wa kusimamia halmashauri zetu ili mambo yakae vizuri na halmashauri ziendee kupata kipato kinachotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni upande wa usimamizi wa rasilimali. Katika upande wa usimamizi wa rasilimali imeelezwa katika sheria ilivyo; kilichofanyika katika mapendekezo ya sheria hizi zinazotajwa ni kuhakikisha kwamba sasa katika maeneo ambayo bomba hili linapita, Serikali inakwenda kuangalia kwa niaba yetu jinsi gani rasilimali zetu zinaenda kusimamiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma kipengele cha sheria siyo kwamba kinakwenda kubadilisha hayo ambayo yamesemwa isipokuwa kinatoa nafasi kwetu kuendelea kuona Serikali yetu ni kwa jinsi gani inaweza kusimamia mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Wabunge wenzangu na wananchi wenzangu wa Tanzania, tuiamini Serikali yetu chini ya Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais kwamba itakwenda kutufanyia haki na Baraza letu la Mawaziri litakwenda kusimamia yale ambayo yamekusudiwa kimkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia lipo jambo ambalo lilijadiliwa sana kwenye Kamati. Hili jambo kwa namna moja au nyingine baadhi ya Wabunge wamekuwa wakituuliza ni jinsi gani sheria hii au mkataba huu unakwenda kusimamia mali za Serikali yetu bila ya kuathiri mambo ya kimkataba? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwatoeni wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba katika sheria ya mashauri ya Serikali inazungumza wazi kwamba yapo mambo ambayo huwezi kuyafanya bila sheria kuwa imekuruhusu kuyafanya. Mojawapo ni ukamataji wa mali za Serikali. Ila katika mkataba huu kinachozungumzwa, siyo mali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzani, ni zile mali ambazo zitaingizwa katika kile chombo au lile shirika linaloanzishwa ambalo kwa mujibu wa mkataba huu ni lile Shirika la EACOP ambalo linakwenda kusimamia mradi mzima wa mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishieni Watanzania wenzangu na Wabunge wenzangu kwamba tukubali kupitisha mkataba huu au sheria hii ili kuhakikisha sasa Serikali yetu au Serikali wanachama katika jambo hili la mafuta ya bomba linalotoka Hoima kwenda mpaka Chongoleani kule Tanga linakwenda kusimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa umuhimu wake, naomba sana Wabunge wenzangu na Wajumbe wenzangu waamini kwamba sheria hizi kama zilivyowekwa zinakwenda kuwahakikishia Watanzania mustakabali mzuri kama ambavyo wenzangu waliotangulia wamesema hasa katika eneo la ajira na ustawi mzuri wa maisha na maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 2) Act, 2022
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kuunga mkono hoja. Kipekee kabisa niipongeze sana Kamati ya Bunge ya Sheria kwa mchango wake mzuri waliotoa lakini pia michango iliyotolewa na Wajumbe wote waliopata nafasi ya kuchangia hoja hii iliyowekwa mbele yetu ya marekebisho ya Sheria ya Miscellaneous Amendment No. 2 ya Mwaka 2022, ambayo ndani yake inabadilisha au inafanya marekebisho katika sheria zetu tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi niwapongeze sana Wajumbe lakini kwa kipekee kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Attorney General kwa yeye mwenyewe kuona kwamba kuna umuhimu wa kuleta sheria hii sasa hivi lakini kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, kwa sababu sheria hizi zinaenda kuipa sura nzuri nchi yetu katika uwanda wa mahusiano ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Sheria hii ya Zuio la Usafirishaji wa Binadamu inatupa heshima kubwa sana nchi yetu kwa sababu, dunia imekumbwa na tatizo kubwa sana la biashara isiyokatika ya kuuza watu nje lakini katika vigezo mbalimbali. Sheria hii inafanya marekebisho katika kipengele cha Nne, kipengele cha tano, kipengele cha Sita, kipengele cha Saba na kipengele cha Nane. Pia kipengele Namba 13 na kuongeza sasa badala ya faini na kuiachia Mahakama kuamua vipengele vya vifungo ikiwa ni sehemu kwa lugha ya kisheria au kwa lugha ya Kiingereza wanasema ni mandatory sections. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vipengele hivi kwa kweli vilikuwa vinaleta ukakasi mkubwa sana kwa sababu, wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wanafanya biashara hii mpaka inaonekana kwamba ni biashara sahihi kufanyika, lakini kwa kuleta vipengele hivi Bunge lako nataka niwashawishi Wabunge wenzangu kwamba tupitishe sheria hii kwa sababu sasa inaenda kutoa mwarobaini wa wale ambao walikuwa wanafanya biashara hii wakiamini kabisa kwamba wao ni watu wenye haki ya kuuza watu wengine duniani.

Mheshimiwa Spika, kwa kipekee kabisa ninaipongeza Serikali na mimi ninaunga mkono sana hoja hii ya kubadilisha au kuongeza baadhi ya vipengele katika Sheria yetu hii ya Madawa ya Kulevya.

Mheshimiwa Spika, madawa ya kulevya yameumiza vijana wengi sana yameharibu rasilimali ya nchi lakini pia yamepoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa letu. Kwa kuongeza vipengele hivi ambavyo vimeletwa sasa ambavyo vinatoa ushahidi wa dhati juu ya nia ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kupambana na kuhakikisha kwamba nguvu kazi ya Taifa hili inaendelea kuhifadhiwa ni jambo kubwa la msingi ambalo linapaswa kuongelewa kwa lugha kubwa lakini kupazwa sauti ya juu zaidi.

Mheshimiwa Spika, nataka niwatoe wasiwasi baadhi ya wazungumzaji ambao walichangia katika hoja hii, ambao walionesha kwamba wanao wasiwasi kwamba viko baadhi ya vipengele vya kisheria ambavyo vinakwenda kuondoa mamlaka katika baadhi ya mamlaka zao. Kwa mfano, ndugu yangu Mheshimiwa Mpina amezungumza juu ya kwamba uundwaji wa sheria hii au marekebisho ya sheria hii yanakwenda kuinyima haki Jeshi la Polisi katika nguvu yake ya kuendelea kushikilia wafungwa au wale watu wanaoshutumiwa kutenda baadhi ya makosa.

Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Mpina kwamba sheria hii inayowekwa inakwenda kuipa Mamlaka ya Madawa ya Kulevya siyo kwamba sheria hii inainyima Jeshi letu la Polisi hapana, Jeshi la Polisi inayo mamlaka yake na kitengo cha madawa ya kulevya nayo pia kina mamlaka yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu jinsi gani wale watuhumiwa wanaenda kukaa nataka nimrudishe katika Sheria ya National Prosecution Act ambayo inatoa mamlaka kwa DPP ya kuangalia juu ya uendeshaji wa jela zote au cell zote na jinsi gani wale wafungwa wanaopelekwa katika maeneo hayo wanaangaliwa katika utaratibu ambao unasomwa pamoja na sheria nyingine zikiwemo zile zinazozingatia haki za binaadamu. Kwa hiyo, nataka nilihakikishie Bunge lako lakini pia kuwahakikishia Umma kwamba sheria hii si kwamba inawanyima Polisi mamlaka yao lakini inakwenda kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na hivyo wawe na hakika kabisa kwamba taratibu na sheria zitasimamiwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia, sheria hii inakwenda kuweka utaratibu wa jinsi gani Jeshi letu hili au kitengo hiki cha madawa ya kulevya kinakwenda kusimamia utaratibu kuanzia kwenye investigation, kukamata mpaka kupeleka watu katika maeneo husika. Kwa hiyo, nilitaka nizungumze hili pamoja na kuunga mkono mchango mzuri uliotolewa na Waziri wetu wa nchi juu ya kwamba sheria hii inakwenda kuweka taratibu nzuri ambazo zinakwenda kuhakikisha kwamba ulinzi wa ushahidi nao pia unaangaliwa, hivyo wasiwe na wasiwasi Watunga Sheria kwamba kuna tatizo litaenda kujitokeza katika hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa mchango wanguhuo mfupi, naunga mkono hoja na nnawaomba Wabunge wenzangu tupitishe sheria hizi kwa nguvu moja.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa Mwaka 2023.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, niungane na wote waliochangia katika hotuba hii nzuri ya sheria zetu hizi mbili. Pia nitumie nafasi hii kuungana na wenzangu kukutakia kila la kheri katika nafasi unayogombea na sisi tunakuombea sana kheri na Mwenyezi Mungu Insha Allah atakusaidia, utafikia yale malengo makubwa ya ndoto zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya, lakini pia kuendelea kumshukuru yeye kutuamini mimi na bosi wangu Mheshimiwa Simbachawene kwa majukumu haya ambayo tunaendelea kuyatekeleza. Pamoja na hilo pia niishukuru Kamati yako nzuri na kwa kweli nataka nikwambie au nikuhakikishie wewe na Bunge lako, sisi kama Serikali kama ambavyo wenyewe wamejielezea hapa na ndiyo ukweli wenyewe kwamba hoja zote zilizotolewa na Kamati yako tumezichukua na tunawashukuru pia kwa yale maeneo machache ambayo na sisi tulitoa hoja zetu nao pia wamezichukua lakini hii ndiyo Serikali ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuiongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika muda mchache nilionao huu, naomba nijielekeze moja kwa moja katika maeneo machache sana na yale makubwa zaidi nimemwachia Mheshimiwa Waziri atakuja kudadavua zaidi.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, nataka nizungumze katika Tume ya Mipango. Tume yetu ya Mipango mnaweza kuwa mashuhuda kama alivyoeleza Profesa Kitila kwamba imekuwa inabadilika mara kwa mara tokea mwaka 1962 ilipoundwa. Wameelezea Wajumbe wengine sitaki kurudia, lakini Tme inayoundwa sasa tofauti na Tume iliyokuwepo zamani. Tume ya zamani ilikuwa inaendeshwa kwa matamko yanaitwa Hati Idhini au kwa lugha ya Kiingereza wanaita instruments lakini hii ya sasa imekuja na sura ya kisheria na hii kwa kweli inaenda kutoa nguvu zaidi na hasa kama alivyoeleza Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati kwamba hii pia inakwenda kutoa na ulinzi wa mawazo mazuri na jinsi ambavyo Tume itaendeshwa na kwamba hakuna kitakachobadilika isipokuwa kwa idhini yako au ya Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii kuendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha kwamba Nyerere wetu, Mwalimu Julius Nyerere mwanzilishi au founder anaendelea kuishi katika mioyo yetu kwa sababu hii yote ilikuwa ni ndoto yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia naendelea kuwashukuru sana wenzetu wote waliochangia katika hotuba ya bajeti kuhusiana na mabadiliko ya Sheria yetu ya Usalama wa Taifa. Nataka kuwatoa wasiwasi baadhi ya Watanzania ambao wana wasiwasi katika hili. Ndugu zangu, sheria hii imekuja kutuhakikishia usalama mkubwa kwetu. Imeongeza majukumu, lakini imeongeza responsibility kwa chombo, lakini pia imetoa nguvu kwa chombo na imeenda kutuhakikishia kwamba sasa chombo kinakwenda kupewa majukumu makubwa zaidi ikiwemo kwenda kulinda mpaka rasilimali zile ambazo zimeendelea kuanzishwa na kuendelea kusimamiwa katika maeneo yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, pia nitumie nafasi hii kuunga mkono hoja na pia kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Yatokanayo na Urekebu wa Sheria wa Mwaka 2023 .
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, niungane na wote waliochangia katika hotuba hii nzuri ya sheria zetu hizi mbili. Pia nitumie nafasi hii kuungana na wenzangu kukutakia kila la kheri katika nafasi unayogombea na sisi tunakuombea sana kheri na Mwenyezi Mungu Insha Allah atakusaidia, utafikia yale malengo makubwa ya ndoto zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya, lakini pia kuendelea kumshukuru yeye kutuamini mimi na bosi wangu Mheshimiwa Simbachawene kwa majukumu haya ambayo tunaendelea kuyatekeleza. Pamoja na hilo pia niishukuru Kamati yako nzuri na kwa kweli nataka nikwambie au nikuhakikishie wewe na Bunge lako, sisi kama Serikali kama ambavyo wenyewe wamejielezea hapa na ndiyo ukweli wenyewe kwamba hoja zote zilizotolewa na Kamati yako tumezichukua na tunawashukuru pia kwa yale maeneo machache ambayo na sisi tulitoa hoja zetu nao pia wamezichukua lakini hii ndiyo Serikali ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuiongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika muda mchache nilionao huu, naomba nijielekeze moja kwa moja katika maeneo machache sana na yale makubwa zaidi nimemwachia Mheshimiwa Waziri atakuja kudadavua zaidi.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, nataka nizungumze katika Tume ya Mipango. Tume yetu ya Mipango mnaweza kuwa mashuhuda kama alivyoeleza Profesa Kitila kwamba imekuwa inabadilika mara kwa mara tokea mwaka 1962 ilipoundwa. Wameelezea Wajumbe wengine sitaki kurudia, lakini Tme inayoundwa sasa tofauti na Tume iliyokuwepo zamani. Tume ya zamani ilikuwa inaendeshwa kwa matamko yanaitwa Hati Idhini au kwa lugha ya Kiingereza wanaita instruments lakini hii ya sasa imekuja na sura ya kisheria na hii kwa kweli inaenda kutoa nguvu zaidi na hasa kama alivyoeleza Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati kwamba hii pia inakwenda kutoa na ulinzi wa mawazo mazuri na jinsi ambavyo Tume itaendeshwa na kwamba hakuna kitakachobadilika isipokuwa kwa idhini yako au ya Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii kuendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha kwamba Nyerere wetu, Mwalimu Julius Nyerere mwanzilishi au founder anaendelea kuishi katika mioyo yetu kwa sababu hii yote ilikuwa ni ndoto yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia naendelea kuwashukuru sana wenzetu wote waliochangia katika hotuba ya bajeti kuhusiana na mabadiliko ya Sheria yetu ya Usalama wa Taifa. Nataka kuwatoa wasiwasi baadhi ya Watanzania ambao wana wasiwasi katika hili. Ndugu zangu, sheria hii imekuja kutuhakikishia usalama mkubwa kwetu. Imeongeza majukumu, lakini imeongeza responsibility kwa chombo, lakini pia imetoa nguvu kwa chombo na imeenda kutuhakikishia kwamba sasa chombo kinakwenda kupewa majukumu makubwa zaidi ikiwemo kwenda kulinda mpaka rasilimali zile ambazo zimeendelea kuanzishwa na kuendelea kusimamiwa katika maeneo yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, pia nitumie nafasi hii kuunga mkono hoja na pia kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)