Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maryam Salum Msabaha (11 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami nipate kuchangia Mpango wa Taifa wa Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu, muumba mbingu na ardhi kwa kunipa kauli na pumzi ya bure ninayopumua kwa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mara yangu ya kwanza kusimama kuchangia. Nakishukuru sana chama changu na viongozi wangu wa Kitaifa kwa kunirejesha tena huku ndani kwa awamu ya pili. Mwenyezi Mungu awabariki sana na awape umri katika maisha yao na utendaji wao wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu nitajikita sana kwenye masuala ya ulinzi na usalama. Tunapeleka vijana kwenye makambi ya Jeshi, kwa mfano JKT, vijana wanaenda kupata mafunzo mbalimbali ya kijeshi, lakini imekuwa katika kundi hili wanachukuliwa vijana wachache sana na vijana wengine wanakuwa hawana ajira. Sasa naomba huu Mpango uelekezwe kwenye Wizara ya Ulinzi na Usalama waangalie ni namna gani ya kuboresha na kuwajengea vijana wote kwenye makambi ya JKT kuhakikisha kunapatikana viwanda vya ujasiriamali kwa ajili ya hawa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia haya makambi, pia kuna baadhi ya makambi mengine ambayo yamepakana na bahari, mengine yamepakana na maziwa. Pia hawa vijana wanaohitimu mnaweza mkawajengea na mkawapa angalau uvuvi wa bahari, wakaenda zao kujiajiri wenyewe. Sasa mnavyowarudisha vijana hawa mitaani, vijana hawa wamekuwa wanakuja mitaani hawana kazi, ndio hawa mnakuja tena kuwarubuni kwa mambo mengine na ndio wanaokuwa majambazi sugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnajikuta mnawatumia kwenye vikundi ambavyo havieleweki! Mnawatumia sana kwenye mambo ya siasa! Sasa nawasihi ndugu zangu Chama Tawala, mhakikishe mbegu mnayoipanda, ndiyo mtakayoivuna.
Leo hii mmesahau vikosi vya ulinzi na usalama mnawawezesha kipindi cha uchaguzi. Mkishawawezesha, basi, lakini leo hii vikosi hivi wengi hawana sehemu za kukaa, wanakaa uraiani. Angalieni ni namna gani Mpango huu kuhakikisha vikosi vya ulinzi na usalama vinapata makazi bora ya kuishi na vinaboreshewa mishahara yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia yanayoendelea sasa hivi huko Zanzibar, kila kiongozi atakumbukwa kwa matendo yake. Kiongozi na uongozi ni dhamana kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Leo hii sisi kama watu waliotokea Zanzibar tutamkumbuka sana Rais Amani kwa mambo yake aliyoyafanya mazuri kutuunganisha na tukaja tukapiga kura ya umoja wa Kitaifa na tukasikilizana na tukazikana na tukawa tunafahamiana. (Makofi)
Leo hamtaki kusikia la mwadhini wala mchota maji kanisani, mnakwenda tu. Tukumbuke amani tuliyokuwa nayo ni tunu ya Taifa, lakini amani hii tunaichezea, ni kama vile shilingi ikishadondoka chooni, kwenda kuiondosha shilingi ile unapata taabu sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeona kimya; ukimya wa Wazanzibari, lakini siyo ukimya. Siasa ya Zanzibar uliza waliopita Zanzibar. Tulikuwa Wabunge wengi sana ndani ya Bunge hili waliotokea Zanzibar, wengi hawakuweza kurejea. Hawakuweza kurejea! Wabunge walioweza kurejea kama akina Mheshimiwa Masauni watajua ni kwa nini hawakurejea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamwona Dkt. Mwinyi anakuwa mtulivu na mwenye hekima na busara, tunapomwambia fuatilia jambo fulani, anafuatilia. Ndiyo maana mnamkuta kila siku anarudi kwenye kiti chake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wasizibe masikio yao, wayazibue. Naomba viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano, Rais Kikwete alianza sana mambo mazuri ndani ya Zanzibar, lakini sijui ni shetani gani aliyekuja akaingia katikati akatupa mkono Wazanzibari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuhakikishe kunakuwa na Serikali ya umoja wa Kitaifa ambayo ina maridhiano bila kupigana, bila bughudha. Miaka mitano siyo mingi, mtarudia tena uchaguzi na wananchi wa Zanzibar watataka kumpa wanayemtarajia. Niondoke hapo, hilo somo litakuwa limeeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kanda zote za Pwani, tuseme mpaka kule kwetu; ukishika Zanzibar na Pemba, bado kuna umaskini, kuna watu ambao hawawezi kujenga nyumba za kisasa. Tuangalie kama mji wa Bagamoyo ni mji wa kitalii, lakini Mji wa Bagamoyo mpaka sasa hivi umesahaulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani kuendeleza mji wa Bagamoyo ili uweze kuwa ni mji wa Kimataifa kwa utalii na kuhakikisha majengo yote ya Bagamoyo yanaboreshwa? Magofu yote yale ya utalii na yale ya zamani yaboreshwe ili kutangaza mji wa Bagamoyo upate kuwa mji wa kitalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, hata Hospitali ya Bagamoyo, bado hospitali ile mashuka hayakidhi haja; wagonjwa ni wengi na jengo lile ni chakavu. Kwa hiyo, naomba muupe Mji wa Bagamoyo kipaumbele kutokana na kwamba ni mji wa kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe ni namna gani tunatangaza Mji wa Bagamoyo, kwa sababu ukitoka Bagamoyo kuna majumba ya Mji Mkongwe ambayo na Bagamoyo yapo; ni majumba ambayo yanakuwa ni kivutio sana kwa utalii. Majumba haya sasa mengine yamekuwa chakavu na mengine hata katika kujengwa ramani zile zinabomolewa, zinajengwa ramani nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusimamie Mji wa Bagamoyo utangazwe katika sekta ya kitalii na majumba ya makumbusho pia yajengwe na vitu vya kale vyote vienziwe ili tupate watalii wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Suala la Elimu; elimu ya Tanzania bado haijaboreshwa, ni tofauti na nchi jirani. Elimu ya Tanzania inasikitisha sana, ni lazima Tanzania tuwe na elimu bora ili wananchi waweze kukabiliana na changamoto za maisha. Ni vizuri Watanzania wapate elimu bora ili kujenga Taifa la watalaam wa sayansi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijijini hawana elimu bora, shule zipo mbali na makazi ya wananchi, hii inapelekea wanafunzi wa kike kupata mimba za utotoni kwani wanapoenda shule wanakutana na vishawishi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wa kike wanapata taabu sana, wanapokuwa wameingia katika hedhi; kwani shule wanazosoma hazina vyoo vizuri. Vyoo ni vibovu na pengine shule nzima hakuna, kuna vyoo viwili, kimoja wavulana na kimoja wasichana. Ni vizuri Serikali ijenge shule bora na nzuri na wanafunzi watakuwa na bidii ya kusoma na tunaweza kupata wasomi wazuri wenye vipaji mbalimbali, ambavyo vitakuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tupitishe Sheria Bungeni, Wananfunzi wa kike, wanapopata mimba wakiwa shuleni wapewe fursa nyingine, wanapozaa warudi tena kusoma shule au Serikali iwajengee shule maalum kama walivyofanya Zanzibar na hao wanaowapa mimba wanafunzi wachukuliwe hatua kali za Kisheria. Je, ni lini Serikali itahakikisha inarudisha shuleni wananfunzi wa kike waliopata mimba katika umri mdogo? Na ni lini Serikali itajenga shule bora vijijini wanafunzi wa kike wasipate taabu wanavyoingia kwenye hedhi pia vyoo bora iwajengee?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Elimu ya Watu Wazima, baadhi ya wananchi wa Tanzania, ambao ni watu wazima hawajui kusoma na kuandika. Ni vizuri Serikali ikarudisha elimu hii ya watu wazima na ikafika mpaka vijijini. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakaratibu ni wananchi wangapi hawajui kusoma na kuandika na wakawekewa muda maalum wa kusoma. Vilevile, wapewe semina elekezi kuhusu elimu na faida ya elimu kwani katika tawala wa Rais ziliopita akiwepo muasisi wa nchi hii Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, elimu hii ya watu wazima ilikuwepo na watu wazima nao walikuwa wakisoma jioni. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha elimu hii ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika inarudishwa na kuboreshwa hasa vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Vyuo Vikuu ni vizuri Serikali yetu ijenge Vyuo Vikuu vingi hapa nchini ili wanafunzi wanaohitaji kusoma Vyuo Vikuu wasiende kusoma nje ya nchi kwani baadhi ya wanafunzi wakienda kusoma nje ya nchi wanakuwa wanashawishika na kuamua kufanya kazi katika nchi jirani kwani wanakuwa wana vipaji vizuri. Wanafunzi wa vyuo Vikuu wakopeshwe mikopo na hiyo mikopo isikopeshwe kwa upendeleo. Vilevile, ni vizuri Serikali iwekeze katika elimu na wanafunzi wataka kuwa na juhudi ya kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, Chuo Kikuu Huria kwa tawi la Zanzibar liboreshwe, naona kama limesahulika. Wanafunzi wa elimu ya juu kwa upande wa Zanzibar, wapewe mikopo kwa wakati muafaka kwani wanafunzi wa elimu ya juu kwa upande wa Zanzibar wakitaka mikopo ni lazima wafuate Bara. Hii itasaidia kuondoa kero za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Walimu, walimu ni watu ambao wamesahulika! Walimu ambao wako pembezoni bado hawajawa na miundombinu mizuri ya kufundishia, wanafundisha katika mazingira magumu. Makazi wanayokaa hayaridhishi, maji ni taabu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kuwa na elimu bora ni lazima tuwawezeshe walimu kwani wakiwa wanalalamika watakuwa hawawezi kufundisha wanafunzi vizuri. Lazima mishahara yao wapate kwa wakati muafaka kwani walimu wanaoishi vijijini mishahara yao ni mpaka waifuate mjini na mshahara wenyewe ni mdogo, haukidhi mahitaji na mwalimu anakuwa hafundishi na anaanzisha kufanya biashara ndogondogo ili kujikimu na maisha kama kuuza karanga, ubuyu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi jirani za wenzetu, walimu wanathaminiwa na wanaheshimika lakini hapa Tanzania hatuwajali walimu na hatuoni umuhimu wao. Walimu ni nguzo muhimu ya maendeleo, Je, ni lini Serikali itahakikisha walimu wanapewa kipaumbele na kulipwa stahiki zao kwa wakati muafaka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la shule za binafsi, baadhi ya shule za binafsi mazingira yake siyo mazuri! Sehemu wanazolala wanafunzi haziridhishi zina kunguni na kadhalika. Vyakula wanavyokula siyo vizuri kwa afya zao. Naomba Serikali iwe inakagua shule hizi mara kwa mara na zile ambazo hazipo kwenye kiwango zifungwe au kutozwa faini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la majengo ya kale (Miji Mikongwe); Tanzania tunaongeza pato la nchi kwa utalii kwa sababu tuna vivutio vingi lakini Serikali yetu inashindwa kukarabati baadhi ya vivutio kama magofu ya kale yaliyopo Bagamoyo, Kilwa na kadhalika. Ni lazima Serikali ikarabati magofu haya ili tuweze kuongeza mapato ya nchi katika sekta hii ya utalii ili wananchi waweze kunufaika kwa kupata ajira.
Mheshimwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali itenge bajeti ya kutosha kukarabati magofu haya ya kale. Mji wa Bagamoyo ni kivutio kikubwa sana kwa watalii. Maeneo ya Bagamoyo na Zanzibar yametaka kufanana ramani ya Mji Mkongwe Bagamoyo imeanza kupotea kwa sababu wananchi wanauza maeneo hayo na wafanyabiashara wananunua maeneo haya na kujenga majengo mapya na kuondosha vivutio vya watalii. Serikali isipodhibiti hali hii ya uharibifu wa vivutio vya utalii tunaweza kupoteza vivutio vya utalii kwa miaka ya mbele na kukosa watalii katika Mji wa Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vituo vilivyokuwa vikipitisha watumwa (bandari) zimesahauliwa na bandari hizi ni vivutio kwa watalii. Baadhi ya watalii wanapofika Zanzibar ni lazima waende na Bagamoyo kwani Bagamoyo ni kivutio kikubwa kwa watalii. Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti majumba ya Mji Mkongwe wa Bagamoyo ambapo wananchi wamekuwa wakibomoa na kujenga majengo mapya na kupoteza ramani ya Mji Mkongwe. Je, ni lini Serikali itatenga bajeti ya kutosha katika sekta hii ya utalii na kukarabati maeneo ya Mji Mkongwe ili tuzidi kuongeza Pato la Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la hoteli za kitalii; Tanzania tuna hoteli nyingi za kitalii lakini Watanzania wamekuwa wanapata shida wanapoenda kuomba kazi katika hoteli kwani wanaopewa kipaumbele ni wageni kutoka nchi jirani na siyo Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya wawekezaji wanaowekeza katika sekta ya hoteli wanapokuwa wamekodi hoteli wakishindwa kulipa kodi wanabadilisha majina ya hoteli hizo au hao wawekezaji wanawakodisha watu wengine na kubadilisha majina ya hoteli kwa kukwepa kulipa kodi. Wawekezaji wakija kuwekeza katika sekta ya hoteli ni lazima Watanzania wapewe kipaumbele kwani kuna vijana wengi hawana ajira na wana uwezo wa kufanya kazi hotelini.
Je, Serikali imejipangaje kudhibiti ukwepaji wa kodi katika sekta hii ya hoteli za kitalii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Balozi zetu kutangaza utalii; nchi za wenzetu wamekuwa wakitumia Balozi zao kutangaza utalii. Kwa sababu sisi tuna vivutio vingi kuliko hizo nchi za wenzetu kama tusipotangaza utalii wetu ipasavyo hatutoweza kupata watalii wa kutosha. Kwa mfano ukitoka na ndege Uingereza ukifika Kenya watalii wengi wanashuka kiwanja cha ndege cha Kenya. Kwa maana hiyo Kenya wametuzidi kwa kutangaza utalii. Je, ni lini Serikali itatenga bajeti ya kutosha kufanya matangazo ya vivutio vyetu vya utalii nje ya nchi?
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu Muumba mbingu na ardhi kwa kuzidi kunitetea, kunipa pumzi, kunipa uhai na kusimama katika Bunge hili Tukufu na kutoa hoja yangu katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Ninaipongeza hotuba ya Waziri Kivuli, kaka yangu Mheshimiwa Mwinyi yale mazuri yachukue yafanyie kazi ili tuboreshe Wizara yetu ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa isonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, Mheshimiwa Waziri ulitamka juzi ukasema Jeshi liko stand by, nataka niwaambie Jeshi liko stand by na Serikali iwe stand by kwa kupeleka bajeti ya Wizara kwa wakati ili wapate kutatua matatizo yanayowazunguka wanajeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali iwe stand by kwa kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinapatiwa makazi bora na vinapatiwa stahiki zote zinazotakiwa ndani ya Serikali. Tumehakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinakaa katika mazingira magumu, asilimia kubwa ya vyombo vya ulinzi na usalama havina makazi. Tangu Bunge lililopita, Bunge la mwaka 2010, nimekuwa mdau mkubwa sana wa Jeshi nikilalamika kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama, hasa hivi vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vipo mipakani, vimekuwa vikikutana na changamoto kubwa sana. Tuhakikishe sasa hawa mnawapa stahiki zinazostahili, wapate kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Spika, pia hapa pamezungumzwa sana kuhusu mambo ya wastaafu wa Jeshi, na mimi nitachangia kidogo kwa sababu baadhi ya wenzangu wamechangia.
Mheshimiwa Spika, leo hii tumeona kuna wastaafu ambao wamepigania nchi hii, wamekwenda Uganda. Tukaangalia, kwa mfano, tuliona wale wastaafu ambao walikwenda kupigana Uganda, wale wazee wengine wakarudi hawana viungo, wengine hawana mikono, leo hii wengine walishakufa, wengine wana ulemavu, wako Mgulani. Hawa wazee hebu kawaangalieni wamewakosa nini? Muwapelekee angalau sabuni, msiwatumie wakati wana viungo vyao wakishakuwa hawana viungo vyao mnakwenda kuwatafutia mahali mnawaweka kama scrapper. Niombe kwa kweli kazi ya Jeshi ni ngumu sana na Jeshi wanafanya kazi katika mazingira magumu na mwanajeshi hawezi kulalamika.
Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe ni shahidi. Tumefanya ziara katika Kambi za Jeshi Zanzibar, umeona mazingira ya Zanzibar yalivyo. Ukiangalia miundombinu ya Zanzibar, leo nenda kwenye zile mess za Jeshi zile utofautishe na hizi za polisi, zina tofauti kubwa sana. Sasa hivi mwanajeshi anauziwa kitu kwa bei kubwa sana katika mess zao zile za Jeshi. Mlisema kwa kipindi cha zamani walikuwa wakipata angalau vifaa kama vya ujenzi vinashuka bei, chakula kinashuka bei, leo nenda Jeshini pale uende kama mess ya Jeshi pale, nenda mwenyewe tumefanya ziara pale na nikakuambia, uangalie vitu vinavyouzwa ghali pale, hakina tofauti na kitu ambacho unanunua dukani. Sasa huyu mwanajeshi ataponea wapi! Ukiangalia yeye ndiyo mnamwambia akae stand by, hii stand by nawaambia siyo nzuri sana. Stand by mhakikishe nao mnawapa stand by zao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, uzalendo saa nyingine unaweza ukawa tena uzalendo mtu anashindwa uzalendo. Mhakikishe wanapata nao hizo stand by lakini siyo wawe stand by kwa Chama cha Mapinduzi kwa kule Zanzibar na huku Tanzania Bara. Kwa kweli hii stand by baadaye itakuja kuwageuka nawaambia kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ukiangalia hawa wasaafu kwa kweli wengi wanapiga ramli wamekuwa waganga wa kienyeji sasa hivi. Mnawapa shilingi 20,000, unayempa shilingi 20,000 au shilingi 50,000 ukiangalia ni mtu ambaye ametumikia Jeshi na unajua ukishakaa katika kazi hii ya ulinzi na usalama, ukirudi uraiani huna rafiki kila mtu anakuona adui na ndiyo maana nasema mhakikishe wakiwa katika kazi hizi muwape hata angalau mikopo wajenge nyumba za kisasa waishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo kuna rafiki yangu mmoja ni mwendawazimu, alipigana vita Marekani pale DC, lakini Serikali yake inamlipa mshahara, anakula vizuri, vile vitu ambavyo hawezi kutumia jamaa zake wanachukua wanakula. Ukienda kwake anaishi kama mfalme lakini ni mwendawazimu. Ninyi kwa nini watu ambao wana akili zao wengine hawana viungo, hawana nini mnashindwa kuwapa pesa lakini mnaweka pesa zikifika karibia na uchaguzi mnawaambia kaeni stand by. Niwaambie wanajeshi wote msikubali kukaa stand by, mtakaa stand by pale mtakapopata stahiki zenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukirudi nyumba za wakufunzi hawa ambazo ziko kambi za JKT, nyumba nyingi siku za mvua nendeni mzunguke, zinavuja, wanavujiwa. Mnakuta nyumba ipo lakini yale majengo ni ya zamani, sasa kitu gani hamtaki kuwajengea hawa wakufunzi wa JKT nyumba nzuri ili watoto wale wanaokwenda kwa mujibu wa sheria wapate kufundishwa vizuri na mwalimu. Lakini mwalimu anafundisha wanafunzi saa ya kulala mvua ikinyesha anasimama, baadaye uchaguzi ukifika kaeni stand by, hiyo ni sawa? Hakuna kukaa stand by hapo. Wote msikae stand by.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vijana hawa ambao JKT tunawapeleka kwa mujibu wa sheria na katika hotuba yako nimeona umegusia pia Wabunge waende. Kwa kweli Wabunge waende kwa sababu hili Bunge wameingia vijana wengine ni mateja wa unga wamo humu, wengine wanavuta bangi, wengine wanavua mama zao nguo, mama zao wengine walishakufa, wanakuja humu Bungeni wanawatukana mpaka wazazi wao. (Makofi/Kicheko)
Kwa hiyo, niombe kabisa na Mheshimiwa Rais Magufuli vijana wote Wabunge ambao hawana nidhamu, hawana standard ya kuzungumza katika Bunge hili waende JKT. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, Wabunge wote vijana ambao hawana nidhamu ya kuzungumza katika Bunge hili na waende na wale ambao hawajapitia, kwa nini watu wanakwenda kwa mujibu wa sheria, form six wanakwenda, na Wabunge wote JKT wakirudi wawe na discipline ya kuzungumza ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa vijana wengine wanaokwenda kwa mujibu wa sheria mkishawachuja wale vijana, ninaomba kwanza muangalie namna gani ya kuboresha vile viwanda vya VETA mle ndani ili wale vijana wengine watakaopata ajira na wengine wabaki pale.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU...
Mheshimiwa Maryam endelea, dakika zako nimezitunza.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana najua utanilindia tu muda wangu.
Neno teja pia liko kwenye kamusi ya Kiswahili, kaangalie, mengine kama nini pia na wewe utoe semina elekezi kwenye Wizara ambayo upo na Mheshimiwa Jenista Mhagama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nakwenda kwenye suala la vijana ambao wamechukuliwa kwa mujibu wa sheria na wengine kwa kujitolea ambao wanapelekwa JKT, kuna wengine wanachukuliwa wanapata ajira, wengine hawapati ajira. Ninaomba Serikali ihakikishe viwanda vyote ndani ya kambi kuwe na VETA vijengwe viwanda ambavyo vijana wale watajiajiri, najua kuna mashamba ya kulima hata zile nguo wawe wanashona wenyewe ili tupunguze hizi changamoto kwa sababu wale vijana wakingia uraiani wanakuwa nao hawana kazi halafu wanaingia tena kwenye mambo ya uhalifu. Hilo naomba mlifanyie kazi ili vijana wale wapate kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, pia zinapotokea nafasi kama nafsi zile za ulinzi, nafasi za ndani ya Serikali, wale vijana wapewe kipaumbele kwa sababu ni vijana ambao mmeshawafundisha namna ya kutumia silaha, kila kitu walishasomea sasa mkiwaacha kama hivi watashawishika baadaye wanaweza kwenda hata kujiunga na Boko Haram. Kwa hiyo, huo ndiyo ushauri wangu natoa kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri suala lingine ninazungumzia ni kuhusu hii migogoro ya ardhi. Hii migogoro ya ardhi pia imezungumzwa sana na Mheshimiwa Halima Mdee pia pale kazungumza, utaona sana kwa upande wa Zanzibar kulivyokuwa na migogoro, kambi zote kwa sababu Mheshimiwa pia umekuwa msikivu na umzezunguka. Hizi beacon kuna ambazo zimewekwa tangu mwaka 1962, sasa zile beacons zimeshapotea.
Kwa hiyo pia uangalie namna gani kutatua hi migogoro kwa wakati na pesa zipelekwe. Hakuna kuwa standby mpaka pesa zipelekwe.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia pumzi na kauli, na mimi kusimama katika Bunge hili tena kwa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Michezo, Vijana na Utamaduni. Namshukuru sana Mungu kwa kuzidi kunipa pumzi na leo nitamtanguliza Mungu, nipo kwenye swaumu, nitakayoyasema, basi yawe mustakabali katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Michezo, naomba kwa dhati ya moyo wangu kabisa, yale mazuri yaliyozungumzwa na Kambi ya Upinzani kupitia Waziri Kivuli uyachukue uyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika sana ndani ya moyo wangu na ndani ya nafsi yangu na moyo ukanisuta na nafsi ikanisuta kama mwanamke; na katika mwanamke ambaye nimelelewa katika maadili ya kiislamu, nikalelewa na wamama ambao walinitangulia katika siasa, wamama wa Kizanzibar; akiwemo sasa hivi ni Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu na Mama Amina Salum Ally na wakifuatia wengine, hata dada yangu Saada ambaye nilifanya naye kazi katika Wizara ya Fedha kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika kwa nini? Leo hii dada yangu Mheshimiwa Malembeka, huwezi kumdhalilisha mwanamke mwenzako kiasi kama hicho na wewe ni mwanamke. Tumekaa ndani ya Bunge hili, wanawake katika Bunge la Mama Anna Makinda tulipata maadili kutoka kwa Mheshimiwa Mama Anna Abdallah, kwa Mheshimiwa Jenista Muhagama; walitupokea kama model katika Bunge hili na tukafuata nyayo zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina wasiwasi kabisa dada yangu, huna maadili ya Kizanzibari. Angalia Mawaziri wote waliotoka Zanzibar, mfano kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, angalia maadili aliyonayo ya Kizanzibari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kwa kaka yangu Waziri wa Ujenzi, angalia maadili aliyokuwa nayo, angalia maadili ya Wizara mbalimbali zilizoongozwa na Wazanzibar katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na hata wengine sasa hivi wamefika nyadhifa za juu, ni Makamu wa Rais hawajahi kutukana matusi kama unayoyatoa ya kumdhalilisha mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba kwa dhati kabisa Mheshimiwa Mama Sitta na akina Mheshimiwa Jenista na Mheshimiwa Ummy Mwalimu umekaa kwenye mambo ya jinsia, uangalie namna gani angalau sauti zile ziwe za upole, tusidhalilishane wanawake kwa wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, narudi kwenye hoja. Tatizo langu…
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, natambua weledi wako, wewe ni mwanasheria makini, wala hubabaishwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika TBC na vyombo vya habari kwa ujumla na waandishi wa habari. Waandishi wa habari ni kioo cha jamii, waandishi wa habari na televisheni zote tumeona wakiibua mambo mbalimbali katika jamii, wakiibua watu ambao wapo vijijini; siyo TBC, siyo ITV, siyo Channel Ten; na hata Watanzania hawa wakapelekwa nje ya nchi wakapona maradhi yao yaliyokuwa yanawasumbua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeona ndani ya Serikali wakiwemo Mawaziri na Mheshimiwa Waziri ambaye nilikuwa naye kwenye Kamati moja, namna gani vyombo vya habari vilikuwa vinambeba mpaka leo hii weledi wake na kazi yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana na ninaishauri Serikali, msijenge chuki zisizokuwa na sababu kwa Watanzania na kwa wapiga kura wenu. Jambo hili ninyi mtaliona ni jepesi sana, mkalichukulia kimzaha lakini litawa-cost mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, angalia kwa makini sana namna gani Watanzania wapate habari kwa wakati muafaka na watazame Bunge linavyoendelea. Msiogope, mnaogopa kitu gani? Kwa sababu hata ninyi Mawaziri mkienda kufanya kazi katika sekta zenu, lazima muatumie waandishi wa habari. Kama mwandishi wa habari hajakutangaza, hajakuandika kwenye gazeti, kazi yako haiwezi kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna wapiga kura wenu wanatamani waone Mbunge wao kaongea nini? Waone Bunge la Bajeti linafanya kazi gani Dodoma; lakini mmeziba pamba masikioni na hii TBC mkasema sasa tena basi; lakini nakumbuka TBC ni ya walipa kodi na ndio wanaoichangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kingine zaidi nilikuwa naomba, kama hii TBC labda imekosa pesa, kwa nini hii channel ya Bunge isiangaliwe ni namna gani iboreshwe vyombo vyote vya habari virushe kupitia channel ya Bunge? Pia itaondoa sintofahamu ya TBC. Kwa hiyo, naomba mwandishi wa habari katika Tanzania hii athaminiwe na apewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa mdau sana wa waandishi wa habari. Mara yangu ya kwanza kuingia katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano nilikuwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Jamii na niliweza sana kuwatetea waandishi wa habari. Mwandishi wa habari anafanya kazi katika mazingira magumu. Leo hii waandishi wa habari wengine hawana hata bima ya afya. Kuna wengine wanakufa kwa ajili ya kuchukua habari, wanapata matukio mbalimbali, maisha yao yako hatarini kwa ajili ya kutafuta habari. Ni kwa nini mwandishi wa habari wa Tanzania anaminywa kiasi hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie ni namna gani ya kumboresha huyu mwandishi wa habari, pia wapewe maslahi yao ya kikazi. Yule mwandishi wa habari anayefanya kazi vizuri, pia muwe mnaandaa tuzo ya kuwatunza ili wawe na morali ya kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kupitia hao hao waandishi wa habari wameokoa maisha ya Watanzania, watoto wadogo na leo hii wamepona kabisa. Ni kwa nini tusiwaenzi waandishi wa habari na mkawapa habari kwa wakati muafaka bila kuminyaminya sekta hii ya habari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika lugha ya Taifa, lugha ya Kiswahili. Kiswahili ni lugha ya Taifa, tuangalie sasa hivi ni namna gani sisi Tanzania Kiswahili kinavyoporwa hapa kwetu. Sasa hivi unasikia Kenya wanatafuta ajira sehemu za Afrika ya Mashariki za walimu wa Kiswahili, lakini sasa Serikali imejipanga vipi kuhakikisha Kiswahili kinatangazwa na hata walimu wetu wa Kiswahili wanapata ajira katika Afrika Mashariki? Kwa sababu leo tunajivunia kwamba Kiswahili ni lugha ya Taifa, lakini tumekuta Kiswahili hatukitumii ipasavyo. Unakuta leo mtu anaongea Kiswahili anachanganya na Kiingereza, tunashindwa kuelewa huyu ni mswahili au ni muingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote iliyoendelea, haikuendelea kwa kuiga lugha, waliendelea kwa kusimama kwenye lugha yao. Leo ukienda China wanaongea Kichina, ukienda Korea, wanaongea Kikorea, ni kwa nini sisi tusienzi lugha yetu ya Taifa ambayo tuliachiwa na waasisi wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia uhai na uzima na mimi kusimama mbele yako kwenye Bunge lako Tukufu na kuchangia Wizara ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naipongeza hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyowasilishwa na kiongozi wetu wa Kambi ya Upinzani. Naishauri Serikali, yale yote mazuri yaliyozungumzwa kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani myachukue na myafanyie kazi kwa mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya Waziri Mkuu nitachangia ukurasa wa 11 kuhusu mambo ya Muungano. Kweli kuna mambo mengi ya Muungano, kero zimetatuliwa na nyingine mpaka leo hazijapata ufumbuzi na sio vibaya pia kuuliza ni zipi zilizopata ufumbuzi na zipi ambazo
hazijapata ufumbuzi. Nakumbuka kuna Tume ya Pamoja ilianzishwa miaka mitano ya nyuma kwa ajili ya masuala ya kifedha na Akaunti ya Pamoja kwa pande zote mbili, kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara lakini mpaka sasa hivi hii Tume sijui imeingiziwa kiasi gani cha fedha. Ukitazama hata fedha wanazozipata ni za kulipana tu mishahara, ukiangalia majengo wanayoyatumia ni ya kukodi. Nataka niulize Serikali ni kiasi gani cha fedha kimeingizwa katika Akaunti hii ya Pamoja ya masuala ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Akaunti hii ya Pamoja inashughulikia mambo mengi lakini sasa kuna kizungumkuti, hatujui kinachoingizwa. Nadhani ni vizuri wananchi kwa pande zote mbili tujue pande hii ya Zanzibar wanachangia kiasi gani na Tanzania Bara wanachangia kiasi gani ili wananchi wajue faida za Muungano na hasara za Muungano.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali zile kero za Muungano ambazo zimekuwa ni kero sugu na kama zimepatiwa ufumbuzi wa kudumu ziwe zinatolewa kwenye magazeti ya Zanzibar Leo au magazeti ya Serikali ili wananchi na vyombo vya habari mbalimbali wapate kufuatilia kero hizi
za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiondoka kwenye masuala ya Muungano bado nimo kwenye kitabu cha Waziri Mkuu kwenye ukurasa wa 10 kuhusu masuala ya siasa. Siasa ni maendeleo, tukiwa na siasa safi lazima tutakuwa na maendeleo. Tukiwa na utawala bora lazima tutakuwa na
maendeleo. Tukiwa na utawala ambao unaheshimu haki za binadamu, haki za sheria na kufuata misingi ya demokrasia ni lazima maendeleo na uchumi wa Taifa utakua kwa kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo vyama vya siasa vimezuiliwa kufanya mikutano, vyama vya siasa mtaji wao uko kwa wananchi na chama cha siasa bila kufanya mikutano, bila kutangaza sera za chama chao hamwezi kuingiza wanachama na hawawezi kujua sera za chama ni nini. Nashauri Ofisi ya Rais iangalie suala hili, Waziri Mkuu aangalie suala hili kwa mustakabali wa Taifa hili tusiingize migogoro isiyokuwa ya lazima, vyama vya siasa viruhusiwe kufanya mikutano. Vyama vya siasa vyote vyenye usajili wa kudumu vina haki ya kufanya mikutano.
Mheshimiwa Spika, tuangalie pia katika Marais wote waliopita, Zanzibar lazima kulikuwa na changamoto zake. Pia niwapongeze kwa dhati ya moyo wangu Marais waliothubutu kukaa na upande wa Zanzibar kuangalia zile changamoto na matatizo ya kisiasa na hata wakakaa wakapata muafaka.
Mheshimiwa Spika, niombe haya yaliyotokea sio mambo mazuri kwa Tanzania hii tuliyokuwa nayo. Turudi tukae mezani tuzungumze kwa kina tuangalie mustakabali wa nchi kwanza na maslahi ya wananchi kwa pande zote za Muungano ili tupate maendeleo, tupate muafaka wa
kisiasa. Tusifanye siasa za kuburuzana, chuki na ubabe. Ndiyo maana nimetangulia kusema tukiwa na siasa safi lazima tutapata maendeleo.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Rais aangalie kisiwa cha Zanzibar na Pemba kama ambavyo Marais waliotangulia wa Muungano walikaa meza moja wakaangalia mustakabali wa Zanzibar, wakaangalia mustakabali wa Pemba na Muungano ili tupate muafaka tusonge mbele tujenge Tanzania yetu, utaifa kwanza. (Makafi)
Mheshimiwa Spika, hakuna kitu kizuri kama masikilizano, hakuna kitu kizuri kama kufahamiana na mkifahamiana na mkisikilizana Mwenyezi Mungu huleta baraka, neema na kila lenye heri kwa wanaosikilizana lakini kukiwa na mfarakano mkawa hamsikilizani baraka pia inaondoka. Namshauri Mheshimiwa Rais asiogope arudi meza moja wakae na Maalim Seif, wakae na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waangalie mustakabali wa Zanzibar na Muungano unakokwenda tupate kujenga nchi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hayo kwa nini? Kuna wengi wanaogopa kumshauri Rais, lakini mimi namshauri Rais wangu namwambia rudi Zanzibar tunakupenda, wakae meza moja watafute mustakabali wa Taifa hili. Hatuwezi kwenda na siasa za chuki, hatuwezi kwenda na utawala usiokuwa na mantiki na Tanzania hii.
Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye masuala ya vyombo vya ulinzi na usalama. Suala hili ni mtambuka, nimeshangaa sana na namshauri Mheshimiwa Rais kama wengine mnaogopa kumshauri, tangu enzi ya Mwalimu Nyerere vikosi vya jeshi havijawahi kulipa umeme wala
havijawahi kuwekewa LUKU. Majeshi ni kitu muhimu katika nchi yetu, vyombo vya ulinzi ni kitu muhimu katika nchi yetu, maslahi ya vyombo vya ulinzi na usalama yatazamwe kwa jicho pana, yatazamwe kwa uangalifu, yatazamwe kwa maslahi ya nchi. Leo tusiingize migogoro isiyokuwa na sababu katika vikosi vya ulinzi na usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii nchi ni yetu sote, hakuna nchi ya CHADEMA, CCM, CUF, ACT wala ya NCCR-Mageuzi, tukae tusikilizane, tusibaguane. Leo mimi huwezi kuniambia nisiende kwa mtoto wa Ali Hassan Mwinyi kumsalimia, utakuwa umenikwaza au nisiende sijui kwa ndugu yangu Mheshimiwa Nahodha pale kumsalimia utakuwa umenikwaza, tukae tusikilizane. Tushauriane tuangalie nchi inakwenda wapi na wao watanishauri wataniambia Bi. Maryam unavyokwenda sivyo nitapokea ushauri wao kama kaka zangu, tuondoshe chuki za kisiasa, tujenge Tanzania yetu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Mungu ibariki Tanzania.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia tena kusimama katika Bunge lako hili Tukufu nikiwa na kauli thabiti na pumzi. Nitoe pole kwa walimu na wanafunzi wa Mkoa wa Arusha waliopatwa na maafa. Mwenyezi Mungu awapumzishe mahali pema peponi na wafiwa wote awape faraja, kila nafsi itaionja mauti kwa wakati na wasaa wake.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri aangalie pia hotuba ambayo imewasilishwa na Kambi ya Upinzani, siyo yote aliyowasilisha ni mabaya yapo mazuri ambayo anaweza kuyachukua akaboresha Wizara yake. Siyo useme Upinzani kila kitu ni kubeza, sisi tupo hapa kushauri na yale mazuri tuliyowashauri kwenye hotuba ya Upinzani muyachukue ili mboreshe Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la Kiswahili lugha ya Taifa. Zanzibar kuna wataalam wazuri sana wa Kiswahili lakini tumejipanga vipi katika ajira za Afrika Mashariki kuhusu lugha hii? Tunaona wenzetu Kenya hata nafasi zile za kwetu wanajitangaza. Leo hii ukiwa Marekani unakuta wenzetu wao ndiyo wanajitangaza kwenye hii fani ya Kiswahili wanakaa kule mpaka wanakuwa wakalimani, wanasomesha lakini bado Watanzania wako nyuma katika hili suala la kutangaza Kiswahili au kuchangamkia hizi ajira za soko la Walimu wa Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, nimuulize Mheshimiwa Waziri, ana mkakati gani kuhakikisha Maprofesa wa Chuo Kikuu ambao wako kwenye masuala ya lugha yetu ya Taifa ajira zinazotoka kwenye hizi nchi za Afrika Mashariki wanapata fursa? Tumemwona Mheshimiwa Rais yuko katika masuala haya ya kukuza Kiswahili na kauweka utaifa mbele hata anavyokwenda kwenye mikutano mara nyingi amekuwa akiongea Kiswahili. Hata hivyo, tuangalie hawa wakalimani ambao wanafuatana na Mheshimiwa Rais ni namna gani wanaweza kujipanga Rais akiwa anahutubia angalau waende hatua kwa hatua yale maneno ya tafsiri yafahamike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri hata wanaopata nafasi ya kuwakilisha nchi yetu ya Tanzania kwenye mikutano mbalimbali na wao watangaze Kiswahili kama lugha ya Taifa. Nasema hivi kwa nini? Hakuna nchi yoyote ambayo imeendelea duniani kwa kuiga lugha za wengine. Ukienda dukani kwa wenzetu Korea huwezi kuuziwa kitu kama hujui Kikorea, lugha yao wameiweka mbele hata Japan na China ni hivyo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasi tuangalie ni namna gani tutakuza lugha yetu ya Kiswahili siyo mtu unafika mahali unakwenda kwenye mkutano wa kimataifa unaongea Kiswahili lakini hakieleweki kama unaongea Kiswahili au Kiingereza. Tusimame tusimamie lugha yetu ya Taifa ili nasi tujitangaze na tukuze uchumi kwa kupitia lugha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la vyombo vya habari. Vyombo vya habari ni suala mtambuka. Vyombo vya habari vinatoa taarifa ya matukio mbalimbali kwa jamii.

Tumeona ni namna gani jamii imetumia vyombo hivi vya habari na wakapata msaada. Mfano kuna Watanzania hasa wa vijijini ambao walikuwa wanaugua au wako katika hali mbaya kiafya au wana maradhi sugu tumeona kalamu za waandishi wa habari zilivyotumika na Watanzania hawa wakapata msaada.

Mheshimiwa Spika, hapa tuna Wabunge wa Majimbo, Viti Maalum (Mikoa) au wa Kuteuliwa na Rais na tuna Mawaziri ambao wamepitia kwenye Majimbo wakapata uwaziri lakini utaona ni namna gani sisi wanasiasa tumeminywa katika vyombo vya habari. Napenda kujua ni kitu gani Serikali mnachoogopa katika suala hili la vyombo vya habari kwa suala la kutangaza Bunge live? Kwa sababu unavyotangaza Bunge live mimi kama mimi nimetoka Zanzibar, kuna wananchi wangu wanataka wajue leo Msabaha kaongea nini kuhusu Zanzibar lakini hawapati. Hamuoni mnajijengea mazingira ambayo ni magumu itakavyofika 2020 kwenda kuomba kura kwa sababu Watanzania wanataka wasikie wawakilishi wao waliowatuma wanasema nini Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wanakatwa kodi zao kwa ajili ya TBC, kwa hiyo wanategemea iwapatie mijadala ya Bunge la Bajeti waone Mbunge wao kasema nini Bungeni. Hata wengine tukiongea humu huwa taarifa nyingine kama hazijapendeza watu haziwezi kutoka, kila mtu ana haki katika Bunge hili na kila mtu kaletwa hapa na wananchi kuwakilisha sehemu alipotoka.

Mheshimiwa Spika, tuangalie tena suala lingine, hapa kuna wawakilishi kutoka upande wa Zanzibar, kuna Wabunge ambao wametoka kule na kuna Wawakilishi ambao wamekuja hapa kutoka Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo ni muhimu tuangalie pia sekta ya Muungano kuhusu vyombo vya habari. Katika sekta hii ya habari wale wanaokuja kuchukua habari zetu kwa upande wa pili nao wamo au habari za Zanzibar zitaishia kubaki Zanzibar na za Bara zitaishia kubaki Bara? Kwa hiyo, tuangalie namna ya kudumisha Muungano kwenye suala la habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende tena kwenye suala la michezo. Michezo ni afya lakini hata michezo ndani ya Bunge, sisi tumekuwa tukienda kuwakilisha Tanzania Afrika Mashariki. Tumeshuhudia wenzetu waliokwenda Kenya (Mombasa) kwenye mashindano ya Afrika Mashariki utajiuliza kweli Serikali ina mikakati ya kukuza michezo kwani Wabunge waliokwenda kule walitia aibu. Tuangalie tumejipanga vipi hata tunavyoshiriki katika mashindano ya Afrika Mashariki kama Wabunge na sisi tupate hadhi zetu kama Wabunge.

Mheshimiwa Spika, leo michezo haipewi kipaumbele. Tuangalie Brazil, Brazil imeendelea kutokana na michezo, kwa nini sisi Tanzania hatutaki kuipa michezo kipaumbele? Tumefanya michezo ni kama kiburudisho au kuondosha kisukari na presha kwenye mwili, hapana, michezo inaingiza pato la Taifa. Naomba tuangalie namna gani ya kukuza michezo na kutafuta vipaji, tuanze na sisi Wabunge ni mara ngapi tumekuwa tukileta makombe ndani ya Bunge hili, lakini kila tunavyokwenda mbele michezo inasahaulika.

Mheshimiwa Spika, zamani wakati tupo shuleni michezo ilikuwa inaanza kule shuleni, unaanza kuangalia vipaji kule shule, unaanza kumkuza yule mtoto akiwa mdogo mpaka anafika kiwango cha kuwa mwanamichezo bora lakini sisi michezo tumefanya kama sehemu ya kutoa presha na kisukari kwenye miili yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itenge bajeti ya kutosha kuhusu michezo na hasa suala la Wabunge wanavyoshiriki kwenye mashindano ya Afrika Mashariki pia watengewe bajeti ya kutosha. Mheshimiwa Spika utalichukua kama wewe ndiyo kiongozi wetu wa Bunge na siyo kama tunashiriki michezo ya Afrika Mashariki tunakwenda kudhalilika mbele ya Wabunge wenzetu. Hilo naomba ulipe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yameongelewa sana mambo ya sanaa. Kwenye sanaa wanawake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili nichangie kwenye Wizara ya Ulinzi na Usalama. Kabla ya yote nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa uhai na pumzi, nimesimama tena katika Bunge lako hili, ni shukrani ya pekee nairudisha kwa Mwenyenzi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpe pole kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi kwa kutotendewa haki katika Wizara yake kwa sababu tumekuwa tukipitisha bajeti hewa, kwa sababu Wizara haitendewi haki. Hii Wizara ni Wizara nyeti, na Wizara hii mnategemea miujiza gani na hawa mnasema wasiseme, lakini wataandamana kwenye mioyo yao. Niiombe Serikali ihakikishe Wizara hii inatendewa haki kama wizara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iangalie Wizara ya Ulinzi pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa. Hili si Jeshi tu la kutuma wakati wa uchaguzi bali niseme Jeshi hili lipo kwa ajili ya kulinda mipaka ya nchi na kwamba halipo kwa ajili ya kulinda uchaguzi. Niwapongezea pia kwa weledi wao mzuri wa kulinda mipaka ya Nchi ambayo iko salama mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kukata nishati ya umeme katika Kambi za Jeshi. Mimi nashangaa sana, kwa nini Serikali isipeleke pesa kwa wakati? Kama Wizara ilikuwa inatengewa pesa kwa wakati fedha zinazotengwa hapa zinapitishwa zinapelekwa kama zilivyo pia deni hili la nishati ya umeme lingepunguzwa, lakini nasijaabu mnasema mnakata umeme mkikata umeme jueni Jeshini kuna kazi nyeti kazi nyingine haziwezi kutajwa zile kazi zitafanyika vipi au mnategemea miujiza gani? Hawa wanajeshi wawashe tochi? Kuna sehemu nyingine hawawezi kuwasha tochi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima wawe na umeme masaa ishirini na nne, lazima umeme uwake Jeshini, hakuna kusema hapa kazi Jeshini kazini umeme ni lazima uwake, Mheshimiwa Rais akate umeme sehemu zote, lakini si Jeshini. Kuna vitu nyeti vya ndani ya Serikali viko Jeshini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kufunga luku, luku mtawafungia vipi wanajeshi jamani? Tangu enzi ya Nyerere mbona akujafungwa luku hiyo luku inatoka wapi? Angalieni mkipeleka pesa haya masuala yote yataondoka, na kama kuna pesa za kurudishwa kwenye nishati zitarudishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mnasema wanajeshi wanaripoti kazini kuanzia saa 12 asubuhi anakaa mpaka jioni. Kwa mfano, anatoka Kibaha na kurudi Dar es Salaam, labda Mbagala au wapi, sasa huyu mmemfanya yeye robbot? Toeni stahiki ambazo zinapaswa kwa wanajeshi. Leo mnahamisha wanajeshi mnawapeleka vituo vingine vya kazi lakini huku nyuma wanaacha familia, mnategemea nini? kuna matukio mbalimbali yametokea wanajeshi kuua wake zao; hawawaui kwa makusudi ni hasira huko alikokwenda pesa hajapewa huku mke wake labla kafanya michepuko, ninyi ndio mnasababisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba fedha itolewe kwa wanaopata uhamisho wapewe stahiki zao waende na familia zao hakuna kutengeneza mambo mengine vifo kwa wanawake visivyokuwa na sababu na kutengeneza UKIMWI usiokuwa na sababu. Kwa hiyo, naombeni chonde chonde muangalie kwa makini, isiwe leo tunapitisha shiingi bilioni kumi na moja lakini hata shilingi bilioni moja hampeleki mnategemea nini? Yale magwanda nayo yanahitajika yafuliwe, viatu vinataka vibrashiwe (be brushed) kama mlivyosema kwamba huko barabarani traffic wakikamata nao wanataka ya brush na hawa pia wanataka brush.

Mheshimiwa Mwenyekiti tuangalie hospitali; hizi hospitali, kwa mfano Lugalo. Hospitali ya Lugalo imekuwa ni hospitali hata viongozi wengi wa kitaifa wakifa wanapelekwa kule. Lakini tuangalie changamoto zilizopo katika hospitali ya Lugalo. Naomba Serikali iziangalie hospitali hizi kwa jicho la makini, na bajeti inayopagwa tuhakikishe ina madaktari wanajeshi wanapata stahiki zao wanapata mafunzo, wanapata masomo, wapewe kila kinachopaswa kwa sababu hospitali hizi hazihudumii wanajeshi tu, zinahudumia na raia wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar unakujua na Migombani unakujua. Hospitali ile ya Jeshi ya Migombani ni ya siku nyingi kituo kile ni cha siku nyingi na kipo sehemu nyeti sana wewe mwenyewe inaijua iko karibu na Ikulu ya Migombani, lakini kituo kile kimekuwa kinapokea watu wengi mpaka majeruhi, kituo kile ni cha tangu enzi ya ukoloni. Angalieni namna gani ya kuboresha kituo kile ili kiende na sayansi na tecknolojia. Tusikae tu kituo kile ni kidogo na kiko barabarani kubwa, sehemu yenyewe ni nyeti, lakini kituo hakiko katika ubora wowote. Kwa hiyo, hilo pia naomba lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu mipaka ya Jeshi umeangalia migogoro nakushukuru, migogoro ya Zanzibar mingi umeishughulikia, lakini bado kuna migogoro umebaki wakati wa kwenda kulenga shabaha mwangalie na kule wakishalenga shabaha na vile vitu ambavyo vinavyobaki kule viondoshwe ili visiwadhuru…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwa kunipatia fursa hii niweze kutoa nami maoni yangu, nami pia ni mjumbe wa Kamati, mengi tumeshayachangia kwenye Kamati; na yale mazuri pia tuliyoishauri Wizara na Serikali pia wayachukue kwa mustakabari wa Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona haya mambo yanavyokwenda katika hii Wizara na hii Wizara haijawahi kumuacha mtu salama. Tumeona migogoro mingi ambayo imetokea kwenye hii Wizara ya Nishati na Madini, mpaka Mheshimiwa Rais akachukua jukumu la kutenganisha hizi Wizara zikawa Wizara mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna mambo mbalimbali ambayo yamefanyika kwenye Kamati hizi. Tumeona yale masuala ya makinikia, mambo ya michanga yalivyokwenda, sasa Watanzania wengi bado wanahoji pia wanataka angalau wapate taarifa kile ambacho tulikuwa tunakidai kiko wapi na ni kitu gani tulichonufaika nacho mpaka sasa hivi. Si vibaya sana tukitoa taarifa tukawaambia Watanzania kama kipindi kile tulivyokuwa tumewashirikisha namna tulivyokuwa tunaibiwa kwenye masuala ya migodi. Kwa hiyo, niiombe Serikali na Wizara itoe taarifa ili wananchi wajue ni kiasi gani tulichokipata mpaka kwa sasa hivi kwa suala lile la mchanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la wachimbaji wadogo wadogo; hawa wachimbaji wadogo wadogo huwa kuna wachimbaji ambao wanapatiwa ruzuku na Serikali. Lakini umeangalia katika suala letu la taarifa ilivyotoka umeona ni namna gani ni wachimbaji wachache sana ambao wamepata ruzuku ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri sana Serikali na Bunge lako Tukufu kuhusu hii Serikali ya wachimbaji wadogo wadogo, tuangalie humu ndani kwa kina hizi pesa zimekwenda wapi, huku tukianza kuangalia tukichimbua kwa kina kuna vitu vingi sana vimefichika huku kwa wachimbaji juu ya hizi ruzuku zilizotolewa kwa Serikali kwa ajili ya kuwafikia wachimbaji wadogo wadogo. Umeona ni namna gani wamepata wale wachimbaji, waliopata ni watatu. Sasa tuangalie zile pesa ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo hizi fedha zimekwenda wapi? Na kama zimeishia kwenye mifuko ya watu au kama watu wamepiga deal basi naomba haya masuala yafuatiliwe kwa kina zaidi ili tuzidi kugundua huu uozo ambao uko kwenye Kamati ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu GST, hawa ni wataalam na endapo tungekuwa tumewatumia vizuri hata hawa wawekezaji wanaokuja kwa kweli wasingeweza kuvamia maeneo kabla hawajapata utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuangalie hii bajeti ambayo tunaitenga katika hii Wizara, hizi taasisi zinafikiwa au zinapelekwa kwa wakati? Sasa kama vitu kama hivi hawa GST hawawezeshwi kwa wakati, sasa tuangalie ni namna gani hii Wizara tuwawezeshe hawa GST kabla wachimbaji hawajaenda kuvamia maeneo wafanye kama utafiti kama kweli huko wanakoenda kuchimba kuna madini au wanaenda kufanya uharibifu wa mazingira. Hata kama wawekezaji wamekuja hawa wafanye kwanza utafiti wa kutosha na waangalie pale kuna madini kiasi gani ili waruhusu wawekezaji sasa nao wachimbe yale madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie wataalam ni namna gani Serikali sasa mnaweza kuwapa kipaumbele ili tuangalie tunadhibiti haya madini tunayosema tumeibiwa kwa siku nyingi yawanufaishe Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi sana kuhusiana na masuala ya REA. Niipongeze Serikali kwa haya masuala ya REA, lakini bado kijijini kuna tatizo sugu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme unapotolewa utakuta wale wafanyabiashara au mtu ana shule yake, au mtua ana uwezo, basi wanaruka vijiji vya wale watu ambao hawana uwezo. Niombe hao watu wakusanywe kwa pamoja umeme kama unapita usibague huyu ana uwezo,
huyu hana uwezo, ili wapate wote kwa wakati muhafaka hayo yanatotakiwa kwenye umeme wa REA.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuje kwenye madeni ya TANESCO. Hili Shirika limekuwa likijiendesha sana kwa hasara, kama ulivyoona tulivyotoa maoni yetu kwenye Kamati yetu. Tuangalie na hawa wadaiwa sugu wanachukuliwa hatua gani na Serikali ili wapate kulipa. Hata kama ni taasisi za Serikali basi tuhakikishe ni namna gani wanarejesha haya madeni TANESCO ili TANESCO iweze kujiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Kamati yetu tumechambua mambo mengi mazuri yaliyoongelewa humu kwenye Kamati, naomba yachukuliwe, lakini sana sana pia niende kwenye suala la barabara. Kuna barabara hizi ambazo tumekuwa tukizijenga, lakini barabara hizi tunazijenga kwa gharama kubwa halafu zinaharibika kwa muda mchache. Sasa niulize Serikali hawa wakandarasi wanaohusika na hizi barabara wanachukuliwa hatua gani endapo zile barabara zinaharibika kwa kipindi ambacho ni cha… na watoe guarantee kama hizi barabara wanazozijenga zitachukua muda gani, na zikiharibika kabla ile guarantee haijaisha basi wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuangalie suala la bandari. Tuangalie bandari hizi bandari bubu ambazo ni tatizo, kuna vitu vingi sana vinapita kwenye bandari bubu. Sasa tunazidhibiti vipi hizi bandari bubu ili tuache kupitisha, ziache kupitisha mizigo, vitu vya haramu na mambo mengine ili wale ambao wanakwepa kodi nao wadhibitiwe ili zile kodi zirudi Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar bado kuna malalamiko sana kwa wafanyabiashara ambao wanatoka Zanzibar. Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye suala hili la wafanyabiashara wa Zanzibar. Unakuta umelipia mzigo wako Zanzibar, ule mzigo ukifika tena pale bandarini unakuwa-charged ushuru. Unakuta umetoka na kiporo (mfuko) chako kidogo, labda ni kiporo cha mchele au vitu vyako vidogo vidogo umenunua unapeleka Zanzibar, kwa hiyo ukifika pale unachajiwa ushuru. Sasa tuangalie ni namna gani ili suala la Muungano kuhusu masuala ya bandari ni namna gani sasa tuliweke ili pande zote mbili zinufaike, upande wa Zanzibar wasilalamike na upande wa Tanzania Bara usilalamike. Tusiwe kule tumeshalipa kodi wakija tena huku wanalipa kodi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na pumzi na kuwa tena katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape pole viongozi wangu wote wanaopitia changamoto za kisiasa, yote ni mitihani, lakini Mwenyezi Mungu atawavusha salama. Pia nimpe pole Mheshimiwa Spika kwa neema na kwa baraka ambayo pia Mwenyezi Mungu amemjalia na kurudi Tanzania akiwa katika hali ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitajielekeza sana kwenye changamoto za Muungano. Nimepitia kitabu cha Waziri Mkuu ukurasa wa 11 bila kukosea, nimeona masuala ya Muungano Mheshimiwa Waziri Mkuu ameorodhesha sehemu chache sana. Ni kitu ambacho hata ukurasa huu ametoka page hii ya 11 ameishia hapa, hata hii page hapa hakufika akaendelea huku kwenye Serikali kuhamia Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar bado kuna changamoto kubwa ya kero za Muungano. Nilikuwa nategemea angalau tunakuja humu kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na sisi tumetokea upande wa pili na tumechaguliwa kwa ajili ya kuja kuwakilisha Zanzibar, tuambiwe ni kero ngapi za Muungano mpaka sasa hivi zilishapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuambiwe hata angalau ile Akaunti ya Pamoja tunaichangia kwa namna gani; Bara wanachangia shilingi ngapi na Zanzibar wanachangia shilingi ngapi ili wananchi wakapata ufahamu na wakajua sasa sisi huku labda hatuchukuliwi chetu kabisa au huku sisi hatutumiki, yakawekwa yale masuala yakawa wazi kabisa, kama ni kutangaza kwenye redio au magazeti ya Serikali ili wananchi wakajua huu Muungano ni wa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoungana tunatakiwa tuungane kwa maendeleo na kwa changamoto na zile sekta ambazo ni za Muungano zipewe kipaumbele. Leo tunataka tujue ni Wazanzibari wangapi ambao wameajiriwa kwenye sekta za Muungano, ni Wazanzibari wangapi ambao walikuwa wanakaimu zile nafasi na mpaka sasa hivi wamepata nyadhifa zao kamili, bado kunakuwa na kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ikija Ofisi ya Makamu wa Rais pia ile bajeti ambayo inawasilishwa na Serikali haipelekwi kwa wakati muafaka. Sasa hizi kero za Muungano zitatatuliwa wakati gani? Leo tukihoji Akaunti ya Pamoja,

Mheshimiwa Mzee Dkt. Mipango akija hapa Zanzibar inasahaulika. Tuseme sisi Wazanzibari ndio hamtutaki au hatuna haki huku kwenye hili Bunge, mtuambie kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna wimbi la vijana, hawa vijana wengi mlikuwa mnasema ni vijana wa Zanzibar wanaenda kufanya kazi nchi za Uarabuni; Oman na sehemu zingine, lakini pia mpaka vijana wa Tanzania Bara wapo ambao wanafanya kazi Uarabuni. Sasa Serikali imejipanga vipi kusaini mkataba wa kimataifa ili kutambua hawa watumishi wanaofanya kazi nje ya nchi, hasa sehemu za Uarabuni, viwandani na majumbani ili hata zile haki zao waweze kuzidai wanapopata matatizo huko nchi ambazo wanafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie Zanzibar kuhusu masuala ya biashara. Tunatumia bandari ya pamoja lakini hii bandari imekuwa kizungumkuti. Zanzibar unakuta mtu anachukua kimzigo kidogo tu analeta Tanzania Bara, kisiwa kile kinategemea biashara, kinategemea utalii, kinategemea uvuvi, sasa anavyoleta vibiashara vyake kiasi ambacho angalau naye apate kujikimu unakuta analipa kodi mara mbili.

T A A R I F A . . .

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napokea taarifa ya kaka yangu na Wazanzibari tutasimama pale ambapo tunasimama tunakuwa kitu kimoja tunaitetea Zanzibar, Zanzibar ina Serikali yake, Zanzibar ina Baraza la Mawaziri, Zanzibar ina Baraza la Wawakilishi na sisi tumetumwa na wananchi kuja kutetea Zanzibar ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, haki za Wazanzibari tunataka zipelekwe kwa wakati muafaka. Ahsante kwa kunipa taarifa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe na niiombe Serikali ya Muungano iangalie wafanyabiashara wa Zanzibar isiwe inawatoza kodi mara mbilimbili. Kama kodi ilishalipwa nao kama wanakuja huku wapate haki sawa kama wanavyopata haki sawa huku Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie kwenye taasisi kama hii miradi ya TASAF ambayo inatolewa Zanzibar, ni kaya ngapi maskini ambazo zimenufaika au hizi pesa zinaishia tu kwenye mifuko ya watu wachache ambao wana uwezo. Hiyo pia tunatakiwa tupate taarifa ya kina na wale wananchi nao wapate taarifa ya kina kama zile fedha kweli zinawafikia walengwa au ndio zinaishia kwenye mikono ya watu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Marais waliopita walithubutu kuiweka Zanzibar vizuri kulikuwa na zile kero wakazipelekapeleka mambo yakaenda. Nimshauri Mheshimiwa Rais na tumwombe naye afuate nyayo za Marais waliopita, aangalie Zanzibar. Kwa sababu hata kama mkikopa nje ni lazima mnaishirikisha Zanzibar, sasa Zanzibar nayo inanufaika vipi na hii mikopo ambayo inakopwa nje? Tuangalie kabisa masuala haya, ambalo ni fungu la Zanzibar lirudi Zanzibar, ambalo ni fungu la Tanzania Bara lirudi Tanzania Bara, hapo tutakwenda sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ajira kwa vijana. Vijana wengi wameingia kwenye matatizo, sasa hivi vijana wanasoma hawana ajira. Serikali imejipanga vipi kuwasomesha vijana ili waweze kujiajiri wenyewe? Kwa sababu tunaona vijana wengi wanaranda na vyeti mpaka vinapauka kwenye mifuko lakini suala la ajira hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kujua Serikali ina mpango gani hasa kwenye sekta ya kilimo vijana wanapata namna ya kujiajiri, wanapata elimu na mitaji. Tumesikia kuna pesa ambazo zilikuwa zinatakiwa zitolewe, shilingi milioni 50; hizi shilingi milioni 50 vijana wa Kitanzania ambao hawana ajira watanufaika vipi na hizi pesa angalau wajiajiri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wana vipaji, Serikali inatumia vipi hivi vipaji vya hawa vijana ili wapate kujiajiri? Tumesikia Tanzania ya Viwanda, kama huyu kijana hujamuandaa bado tutakuwa na vijana wengi maskani na wengi wataishia kwenye mambo ya uhalifu. Tuangalie ni namna gani ya kuwaandaa hawa vijana waende kwenye Tanzania ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye suala la vyama vya siasa. Siasa si ugomvi, siasa siyo uhasama, sisi sote ni wanasiasa na sisi wanasiasa wote ni ndugu. Leo mimi niko CHADEMA, kuna mwingine yuko CUF, kuna mwingine yuko CCM, lakini vyama vya siasa visitutenganishe. Tuangalie ni namna gani kila mwanasiasa anapata fursa sawa katika Serikali hii, hasa kwenye suala la mikutano na kutangaza vyama vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama chama cha siasa mitaji yetu ipo kwa wananchi, hawa wananchi tutawatumia vipi kama sisi sera za vyama tumekatazwa kuzitangaza. Hawa wapigakura wetu wataelewa vipi kama sisi chama fulani sera yetu ni hii na sera ya chama hiki ni hii. Kwa hiyo, vyama vyote vitendewe haki, viruhusiwe kufanya mikutano bila kubagua chama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Watendaji wa Serikali maana baadhi yao wanashindwa kufanya kazi zao wanamsingizia Mheshimiwa Rais…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuimarisha elimu na ushiriki wa wazazi na jamii. Wazazi na jamii kwa ujumla ni wadau muhimu sana katika kusimamia suala la upatikanaji wa elimu bora. Ni vizuri tuwape fursa ya kutoa michango yao ya kimawazo.

Vilevile wazazi na jamii wanatakiwa waelewe majukumu yao kwa ufasaha juu ya mchango wao kwenye elimu, kwa mfano kuchangia chakula shuleni, ujenzi na kadhaliaka. Wanafunzi wana haki zao za msingi wanapokuwa shuleni ikiwa ni pamoja na haki ya kulindwa, haki ya kupata elimu bora, kutobaguliwa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naiomba Serikali ijenge mabweni katika shule. Hii itasaidia wanafunzi wa kike kutobakwa njiani wanapokuwa wanaenda shule. Wakati umefika Tanzania kuwa na bodi maalum ya kusimamia sera za elimu. Kuna baadhi ya wazazi wanawashawishi watoto wao wasifanye vizuri kwenye mitihani ili wa-fail wapate kuolewa au wanakuwa hawana uwezo wa kuwasomesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iongeze bajeti ili kuboresha elimu. Pia Serikali ihakikishe kwamba wanafunzi wanapata chakula bora shuleni. Hii inawapa vishawishi watoto kwenda shule na kuwa na akili kwa sababu wanakula chakula bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ijenge madarasa ya kutosha; lakini pia katika shule zetu kuna upungufu wa vyoo vya wanafunzi na baadhi ya shule kukosa walimu wa kike. Je, ni lini Serikali itaboresha na kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora katika Shule za Umma ambazo ndizo zinazowahudumia wanafunzi wengi katika Taifa hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule za pembezoni wanaishi katika mazingira magumu. Hawana miundombinu, hawana makazi mazuri kwa ajili ya kuishi na miundombinu ambayo siyo rafiki kwao. Kwa sasa fani ya ualimu siyo wito ni ajira kama ajira nyingine. Ni vizuri kuajiri walimu wenye sifa ya ualimu wenye weledi. Siyo ualimu kwa ajili ya mshahara. Vilevile kuna upungufu wa ofisi za walimu. Baadhi ya walimu kukosekana mafunzo shuleni (kazini) lakini pia kutopandishwa madaraja; walimu kutolipwa kwa wakati, stahiki zao, (walimu wanaohamishwa, kustaafu, pesa ya usafiri).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mikopo ya elimu ya juu (vyuo vikuu); Serikali inapaswa kutekeleza kwa vitendo mkataba wa utoaji nafasi sawa ya elimu kwa wote. Serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa elimu inakuwa 6% ya pato la ndani. Tanzania haijaweze kufikia lengo hilo kwa miaka mitatu mfululizo ambapo bajeti yetu ya elimu ni 17%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba bajeti iongezeke ili kumudu gharama za udhamini wa wanafunzi wote nchini wenye sifa ya kudahiliwa katika vyuo vikuu. Kwa kuwa elimu ni haki ya msingi ya kikatiba ni vyema Serikali iache sera ya kibaguzi ya kuhusisha wazazi kuchangia elimu ya juu ambayo mpaka sasa imekuza tabaka la wasionacho na wenye nacho kwa ubashiri unaofanywa na Bodi ya Mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utambuzi wa wanafunzi wenye sifa ya kupata mikopo, kwa mfano; takwimu za mwaka 2015/2016 ni wanafunzi 21,500 ambayo ni asilimia 24 tu kati ya wanafunzi wote 88,000 wenye uhitaji wa mikopo walidhaminiwa mikopo. Wanafunzi asilimia 76 hawakudhaminiwa mikopo. Serikali inapaswa kutekeleza kwa vitendo utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu bila ubaguzi wowote, kwani kila mtu ana haki ya kupata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile robo tatu ya wanafunzi wahitaji wanakosa mikopo na siyo kwa sababu hawana sifa ni kwa sababu ya usiri uliopo Bodi ya Mikopo. Naiomba Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kuweka utaratibu endelevu wa kukusanya fedha za mikopo kwa wanufaika waliodhaminiwa mikopo ili kuongeza wigo wa kuwadhamini wanafunzi wa vyuo vikuu nchini na siyo kukusanya fedha kwa nguvu na kinyume cha sheria kama ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepandisha makato kutoka asilimia nane hadi 15 ili kuharakisha makusanyo ya mikopo kinyume na utaratibu na sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kodi kwenye shule binafsi, Serikali ipunguze kodi kwenye shule za private kwa sababu shule hizi zinasaidia Serikali. Vilevile shule hizi za private zifanyiwe ukaguzi mara kwa mara kwani kuna baadhi ya shule zinakiuka maadili (hazipo kwenye viwango) na Serikali ihakikishe wanafunzi wa shule za private wanapewa mlo ulio kamili, kwani wazazi wanakuwa wanalipa ada nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu ya watu wazima bado ni tatizo. Watanzania wengi ambao wanaishi pembezoni hawana elimu. Waelimishwe kuhusu suala la elimu na faida zake. Watu wazima wakipatiwa elimu itasaidia kupunguza umaskini na ujinga katika nchi yetu. Ni vizuri Serikali irudishe mfumo kama wa zamani. Jioni watu wazima wapatiwe elimu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma wanafunzi wakitoka shule jioni wanaenda kusoma watu wazima.