Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Silvestry Fransis Koka (29 total)

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Serikali kwa nia njema ilirejesha sehemu ya shamba la Mitamba lililopo Kata ya Pangani, Kibaha Mjini kwa wananchi ambao walikuwa wanaishi katika maeneo hayo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuendelea kurejesha maeneo mengine ya shamba hilo ambayo bado yanakaliwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali lake namba 66 naomba kutoa maelezo yafuatayo:-
Shamba la Mitamba Pangani linamilikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Wizara ilipata shamba hili kwa kulipia fidia kwa wamiliki wa asili, ukubwa wa shamba lililokuwa limemilikiwa ni ekari 4000. Hata hivyo, katika kipindi kifupi baada ya wananchi kulipwa fidia, shamba hilo lilivamiwa na wananchi kutoka sehemu mbalimbali na kuanzisha Mtaa wa Kidimu. Katika kutatua mgogoro huo wa uvamizi mwaka 2004, wamiliki Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Uongozi wa Serikali wa Mtaa huo ziliafikiana kuweka mipaka ya muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa 2007 Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilipima shamba hilo kwa kuzingatia mipaka ya makubaliano yaliyoafikiwa mwaka 2004. Baada ya upimaji kulizalishwa kiwanja Namba 34 chenye ukubwa wa hekta 1037.81 na eneo lililokuwa limevamiwa lilikuwa na ukubwa wa hekta 2963, lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ili lipangiwe na kupimwa kwa ajili ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na upimaji kufanyika bado kuna mgogoro kati ya wamiliki wa shamba na wananchi wanaodai kutolipwa fidia wakati wa utwaaji wa shamba hilo waliokuwa ndani ya shamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vipindi tofauti Wizara yangu kwa kushirikiana na wamiliki Ofisi ya Mkoa wa Pwani, Ofisi za Wakuu wa Wilaya za Kibaha Mji na Wilaya na wananchi wanaoishi kwenye shamba hilo, tumekuwa tukikutana mara kwa mara kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo. Mfano, tarehe 4/3/2016, Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Mji wa Kibaha na Mkurugenzi wa Upimaji na ramani ukiongozwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Kanda ya Mashariki, ilikutana uwandani kwa lengo la kuhakiki mipaka na nyaraka za walalamikaji walio ndani ya shamba. Kwa sasa tunasubiri taarifa ya utekelezaji ambayo bado wataalam wanaendelea kufanyia kazi na mara itakapokamilika tutakuwa na ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na tabia ya wananchi kuvamia maeneo ya Serikali na Taasisi zake, ili kuepuka hali hii tunaomba Waheshimiwa Wabunge na Viongozi mbalimbali kila mmoja kwa nafasi yake kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuacha mazoea yaliyojengeka ya kuvamia maeneo ya Serikali na Taasisi zake na maeneo mengine.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Upanuzi wa hospitali ya Mkoa ya Pwani ijulikanayo kama Hospitali ya Tumbi umesimama kwa takribani miaka mitatu, sasa nondo na zege la msingi na nguzo zinaoza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ili kuondoa hasara na kuleta tija katika huduma ya afya Kibaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto zinazoikabili hospitali ya rufaa ya Tumbi – Kibaha ambazo zimesababishwa kwa sehemu kubwa na ufinyu wa majengo ya kutolea huduma na uchache wa vifaa tiba. Hadi sasa Serikali imetumia shilingi bilioni 5.98 kwa ajili ya upanuzi wa hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kuendeleza upanuzi wa hospitali ya Tumbi Kibaha ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Barabara ya TAMCO hadi Mapinga katika Mji wa Kibaha, Mkoani Pwani imekuwa kwenye maandalizi ya kujengwa kwa kiwango cha lami kwa takriban miaka kumi (10) sasa:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa lami.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya TAMCO hadi Mapinga yenye urefu wa kilometa 23 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania kupitia Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa Pwani. Ili kujenga kwa kiwango cha lami, barabara ya TAMCO hadi Mapinga kupitia Vikawe kuunganisha na barabara ya Bagamoyo, Serikali imefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizo, hadi sasa tayari ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa moja kuanzia njia panda ya TAMCO umekamilika kwa kuwa eneo hili halikuwa na tatizo la ulipaji wa fidia. Eneo lote lililobaki katika barabara hii linahitaji kulipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara hiyo. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kulipa fidia kabla ya kuendelea na ujenzi wa barabara sehemu iliyobaki yenye urefu wa kilometa 22.
MHE.SILVESTRY F. KOKA aliuza:-
Kazi kubwa ya ujenzi wa Mradi wa Bomba la Maji kutoka Ruvu Juu kupitia Kibaha Mkoani Pwani hadi Kimara Jijini Dar es Salaam, imeshafanyika.
Je, ni lini mradi huo kwa upande wa Kibaha Mjini utakamilika na wananchi waweze kupata maji ya uhakika?
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji
na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutumia mkopo
wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India, imetekeleza mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ulazaji wa bomba kuu la kutoka Mlandizi hadi Kimara na ujenzi wa tanki jipya la Kibamba. Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu uliogharimu Dola za Marekani milioni 39.7 umeongeza uwezo wa mtambo wa kuzalisha maji kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na Ujenzi wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara kumeongeza uwezo wa kuzalisha maji ya kutosha na hivyo maeneo yenye mtandao wa mabomba ya usambazaji ya Mlandizi, Kibaha na Kiluvya pamoja na maeneo ya Kibamba, Mlonganzila, Mbezi kwa Yusufu, Mbezi mwisho, Kimara, Kilungule, Mavurunza, Baruti, Kibo, Kibangu, Tabata, Segerea, Kinyerezi, Vingunguti, Kipawa, Airport na Karakata yameanza kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, DAWASCO wako katika kampeni ya siku 90 ya kuunganisha wateja wote wanaohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu chini. Kwa upande wa Kibaha, DAWASCO wamepanga kuwaunganishia maji wateja wapya elfu 30. Ombi langu kwa wananchi, wapeleke maombi ya kuunganishiwa maji katika Ofisi za DAWASCO iliyoko katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara yangu itaendelea kutenga fedha kwenye programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Awamu ya Pili, ili kupanua mtandao wa mabomba ya kusambaza maji na kuweza kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Mradi wa umeme wa 400KV wa kutoka Kinyerezi hadi Arusha ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na Taifa letu; kuanzia mwaka 2015 wananchi wa maeneo ya Kibaha Mjini ambako mradi huu unapita wamechukuliwa maeneo yao na yalifanyiwa uthamini kwa ajili ya wananchi kulipwa fidia:-
Je, ni lini fidia hii italipwa kwa wananchi walioathirika na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi hadi Arusha. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilometa 600, pamoja na kilometa 40 kutoka Kibaha hadi Zinga na kilometa 60 kutoka Segera hadi Kange (Tanga).
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu pia unahusisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika maeneo ya Chalinze, Segera, Kange, pamoja na Zinga (Bagamoyo).
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 kazi ya uthamini wa mali za wananchi kutoka Kibaha hadi Chalinze ilifanyika kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi. Taratibu za kulipa fidia zimekamilika na jumla ya shilingi bilioni 21.56 zitahitajika kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi 855. Maeneo yatakayofidiwa ni pamoja na Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Bagamoyo pamoja na Kisarawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, malipo ya fidia yataanza mara tu uhakiki utakapokamilika.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Mji wa Kibaha ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani na yapo maombi yaliyokwishapelekwa Serikalini kuomba Mji huo upewe hadhi ya kuwa Manispaa lakini hakuna majibu kwa ombi hilo hadi sasa:-
Je, ni kwa nini mpaka sasa Serikali haijaupa hadhi Mji huo kuwa Manispaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maombi ya kuupandisha hadhi Mji wa Kibaha kuwa Manispaa kupokelewa mwezi Agosti, 2016; Ofisi ya Rais , TAMISEMI ilifanya uhakiki uliobaini kuwa Mji wa Kibaha ulikuwa na wakazi 128,488 (sensa ya Mwaka 2012), Kata 14, Mitaa 73 ambapo ni asilimia 56 tu ya wakazi ndio walikuwa wakipata huduma za maji safi na pia haukuwa na mpango kabambe wa uendelezaji wa Mji (Master plan).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali wa mwaka 2014, vigezo vya kupandisha hadhi miji kuwa manispaa unatakiwa kuwa na wakazi si chini ya 300,000, Kata si chini ya 15, Mitaa si chini ya 75, wakazi wanaopata huduma za maji wawe si chini ya asilimia 75 ya wakazi wote wa mji na uwepo mpango kabambe wa uendelezaji wa Mji (Master plan). Kutokana na vigezo hivyo kutofikiwa, ilidhihirika kuwa Mji wa kibaha haukuwa umefuzu kupandishwa hadhi kuwa Manispaa. Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani alijulishwa matokeo hayo kwa barua yenye kumb. Na. CCB.132/394/01/16 ya tarehe 12 Juni, 2017.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Mradi wa umeme wa 400KV kutoka Kinyerezi hadi Arusha umepita maeneo mengi ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na Jimbo la Kibaha Mjini, uthamini wa mali za waathirika ulishafanyika toka mwaka 2015.
Je, Serikali itawalipa lini wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshiiwa Mwenyekityi, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Kinyerezi hadi Arusha. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 400 yenye urefu wa kilometa 664 pamoja na kilometa 40 kutoka Kibaha hadi Zinga na kilometa 60 kutoka Segera hadi Kange - Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu pia unahusisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Chalinze, Segera, Kange, Tanga na Zinga Bagamoyo. Mradi huu utejengwa kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 kazi ya uthamini wa mali za wananchi kutoka Kibaha hadi Chalinze ilifanyika ili waweze kulipwa fidia na kupisha ujenzi wa mradi. Kazi inayofanyika kwa sasa ni kukamilisha taratibu za maandalizi ya malipo kwa wananchi waliohakikiwa kwa ajili ya malipo ya fidia. Zaidi ya shilingi bilioni 21.56 zimetengwa na Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi katika maeneo ya Kisarawe, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wataanza kulipwa fidia baada ya uhakiki wa madai ya fidia hiyo kukamilika. (Makofi)
MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha bidhaa za nyama nchini pamoja na mazao mengine yatokanayo na mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugona Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatekeleza mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya mifugo ambao unelanga katika kupunguza umasikini na kuboresha mazingira rafiki na endelevu katika uzalishaji wa mifugo yenye tija kwa kuzalisha mitamba milioni moja kwa mwaka kutokana na makundi ya ng’ombe wa asili kwa kufanya uhimilishaji, kuimarisha upatikanaji wa uhakika wa maji, malisho na vyakula bora vya mifugo, kuhamaisha matumizi ya teknolijia za ufugaji wa kisasa, kuboresha afya, masoko, biashara na uongezaji wa thamani wa mazao ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara inatekeleza mkakati wa kudhibiti magonjwa ya mifugo na matumizi ya dawa, chanjo na viwatilifu vya mifugo nchini ambapo inatarajiwa kupunguza vifo vya mifugo kwa zaidi ya asilimia 80 pamoja na kuwa na mifugo bora kwa ajili ya masoko ya ndani na nje kwa ajili ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mkakati huu unatarajiwa kuwa na matokeo yafuatayo; kuongezeka kwa ukuaji wa sekta ya mifugo kutoka asilimia 2.8 hadi asilimia 5.2; kuongezeka kwa mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 9; kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo kama vile kuongeza idadi ya ng’ombe wa maziwa 789,000 ambao tulionao hii leo hadi kufikia ng’ombe wa maziwa milioni tatu; kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita bilioni 2.4 hadi kufikia lita bilioni 3.8 kwa mwaka; kuongeza uzalishaji wa nyama kutoka tani 679,992 hadi tani 882,100; kuongeza uzalishaji wa ngozi kutoka futi za mraba milioni 89 hadi kufikia futi za mraba milioni 98.9 na kuongeza uzalishaji wa mayai bilioni 3.2 hadi bilioni 6.4. Pia mkakati unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za ugani, kuongeza uzalishaji wa chanjo za mifugo zinazozalishwa hapa nchini, kupongeza usindikaji wa mazao na mifugo pamoja na kuongeza usambazaji wa teknolojia za ufugaji bora ili kufikia wafugaji wengi zaidi.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Barabara ya TAMCO – Mapinga kupitia Kata ya Pangani ilichukuliwa na TANROADS takribani miaka nane (8) iliyopita:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kujenga barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imekamilisha maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya TAMCO – Mapinga yenye urefu wa kilometa 23 kwa kufanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, pamoja na uthamini wa mali ambao ulikamilika Febrauri, 2014. Baada ya usanifu wa kina kukamilika, Serikali imeanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2013/2014 kilomita moja ilijengwa kwa kiwango cha lami na katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.234 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia TANROADS imekamilisha taratibu za ununuzi wa kumpata Mkandarasi na inaendelea na maandalizi ya kusaini mkataba. Vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na mradi huu.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Mradi wa Umeme mkubwa wa msongo wa KVA 400 toka Kinyerezi kupitia Pwani, Morogoro, Singida na Arusha umechukua maeneo ya wananchi kwa muda mrefu bila kuwalipa fidia:-

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kulipa fidia hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovolts 400 kutoa Kinyerezi - Dar es salaam na Rufiji - Pwani kupitia Chalinze hadi Dodoma. Malengo ya mradi huo ni kuongeza upatikanaji wa umeme katika ukanda wa Mashariki, Kati na kaskazini mwa nchi kutoka kwenye mitambo ya kuzalisha umeme (Kinyerezi) na mradi wa Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ya upimaji njia na kutathmini mali za wananchi watakaopisha mradi kutoka Kibaha hadi Chalinze ilikamilika Mwezi Desemba, 2017 na kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali Mwezi Novemba, 2018. Serikali kupitia TANESCO Mwezi Januari, 2019 itatangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mtaalam mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa Kilovoti 400 kutoka Rufiji hadi Chalinze na kuhuisha upembuzi yakinifu wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi hadi Chalinze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya shilingi bilioni 21 na milioni 600 zinatakiwa kulipwa kama fidia kwa wananchi katika maeneo ya Halmashauri za Kisarawe, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Chalinze na eneo la Kiluvya na taratibu zote za uandaaji taarifa na majedwali ya malipo ya fidia zimekamilika. Serikali inatarajia kutenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 34 kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi wa maeneo hayo baada ya kukamilika kazi ya kuhuisha upembuzi yakinifu ikiwa ni pamoja na gharama za mradi wa kipande cha Kinyerezi Chalinze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wananchi waendelee kuvuta subira wakati Serikali inaendelea kukamilisha taratibu za malipo yao ya fidia. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Serikali inajenga njia ya barabara nane kutoka Ubungo hadi Kibaha:-

Je, barabara hiyo inaishia eneo gani la Mji wa Kibaha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ipo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara na madaraja nchini ikiwemo mradi wa upanuzi wa barabara kuu ya Morogoro sehemu ya Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani. Mradi huu unahusisha upanuzi wa barabara kutoka njia mbili za zamani mpaka njia nane hadi njia 12 katika baadhi ya maeneo pamoja na ujenzi wa madaraja ya Kibamba, Kiluvya, Mpiji na Mlonganzila Overpass.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali ipo katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huu kuanzia Kimara na kuishia Kibaha Maili Moja mbele ya mizani ya zamani takribani mita 150 kutoka mizani ilipo. Barabara hii inayopanuliwa ina jumla ya kilometa 19.2. Lengo la mradi huu ni kupunguza msongamano mkubwa wa magari yanayopita katika barabara hiyo ambayo yanazidi magari 50,000 kwa siku ikizingatiwa kuwa Jiji la Dar es Salaam ni kitovu cha biashara hapa nchini na kuna bandari inayotumiwa na nchi jirani za Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi Estim Construction Co. Ltd wa hapa nchini kwa gharama ya Shilingi bilioni 140.45 na kusimamiwa na Kitengo cha Usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS Engineering Consulting Unit – TECU). Utekelezaji wa mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100. Hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 48 na mradi umepangwa kukamilika mwezi Januari, 2021.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA) aliuliza:-

Shamba la uzalishaji wa Mitamba Kibaha lipo katikati ya Mji wa Kibaha na limezungukwa na makazi ya watu:-

Je, Serikali ina mpango gani juu ya matumizi ya eneo hili kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali uliopo ni kutumia shamba la mitamba lililoko katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa ajili ya uzalishaji wa chanjo za mifugo na kuendelea kuimarisha kituo cha uhalishaji cha kanda ili kuendeleza Sekta ya Mifugo. Tayari Halmashauri imepima eneo la hekta 1,037 ambalo halijavamiwa na kupatiwa hati yenye namba 395140 ya mwaka 2011. Kwa sasa eneo hilo linatumika kwa majaribio na Tanzania Veterinary Laboratory Agency (TVLA) kwa ajili ya kufanya majaribio ya kuzalisha chanjo za magonjwa ya mifugo na kuweka kituo cha kanda cha uhamilishaji na tayari mitambo ya kuzalisha kimiminika cha hewa baridi ya nitrojeni imesimikwa. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Mji wa Kibaha unakua kwa kasi hivyo mahitaji ya Watumishi yameongezeka ikiwemo Watendaji wa Mitaa, Maofisa Mifugo, Walimu pamoja na Watumishi:-

Je, ni lini Serikali itatoa kibali cha ajira na kuajiri Watumishi pungufu ili kuleta ufanisi zaidi katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa ikama ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 Halmashauri ya Mji wa Kibaha ilikuwa na uhitaji wa Watumishi 1,854 ambapo waliopo ni 1,713 na upungufu ni watumishi 140 sawa na asilimia 7.7. Hivyo, Halmashauri ya Mji wa Kibaha ni miongoni mwa Halmashauri zenye tatizo dogo la upungufu wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuajiri Watumishi wa Kada mbalimbali na kuwapanga kwenye halmashauri kwa kuzingatia mahitaji ya halmashauri kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Mwaka 2000 Serikali kupitia Mradi wa Msitu wa Nishati Ruvu ilitoa leseni ya wakulima zaidi ya 300 kutoka katika Kata za Msangani, Kongowe na Mkuza kulima kwenye hifadhi hiyo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwamilikisha wakulima hao walioendeleza kilimo kwa takribani miaka 19?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Msitu wa Hifadhi wa Ruvu Kaskazini umehifadhiwa kisheria kwa Tangazo la Serikali Na. 309 la mwaka 1957. Mwaka 1999/2000 Serikali ikishirikiana na Norwegian Agency for Development Cooperation (NORAD) ilibuni mradi wa kuinua kipato cha wananchi wanaozunguka eneo la Hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kaskazini kwa kupitia kilimo mseto ambapo mazao ya chakula pamoja na miti yalipandwa katika eneo moja. Katika kufanikisha hilo, jumla ya wakulima takribani 300 kutoka Kata za Msangani, Mwendapole, Mkuza na Kongowe walipewa eneo la ekari saba kila mmoja kufanya shughuli za kilimo kwa masharti maalum ikiwa ni pamoja na utunzaji misitu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uharibifu uliokithiri pamoja na wakulima wengi kushindwa kutimiza masharti ya leseni walizopewa, mwaka 2015, Serikali iliamua kuachana na utaratibu huo na kuamua kuanzisha mradi mkubwa wa upandaji miti katika eneo husika.

Mheshimiwa Spika, Serikali haina mpango wa kumilikisha sehemu ya msitu huo kwa mtu au taasisi yeyote. Kwa sasa, umefanyika uwekezaji mkubwa wa kupanda miti mbalimbali kibiashara. Kupitia uwekezaji huo, ajira takribani 2,000 zimezalishwa na zinaendelea kuongezeka kufuatia kuanzishwa pia viwanda vya kuchakata mazao ya misitu, hususan bidhaa za mimea ya bamboo.

Aidha, ili kukabiliana na mahitaji ya ardhi kwa wale wenye uhitaji, Serikali inatoa fursa ya kulima kwa mfumo wa kilimo mseto (taungya system), ambapo wakulima wataruhusiwa kulima mazao kwenye maeneo yanayolimwa au kuvunwa miti kwa kibali maalum.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa Wananchi wa Kibaha Mjini ambao maeneo yao yalitwaliwa kwa ajili ya mradi wa umeme wa Msongo wa KV 400 kutoka Kinyerezi hadi Arusha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa makofi hayo yanaashiria nyota njema.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa, basi nichukue nafasi fupi kuwashukuru wanachama wa Chama cha Mapinduzi lakini nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi, niwashukuru wana Jimbo la Bukoba Mjini na nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipa nafasi hii ya kutekeleza kipande hiki cha majukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvetry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kazi ya uthamini wa mali za wananchi katika mradi wa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kilovoti 400 kutoka Kinyerezi kupitia Kisarawe, Kibaha hadi Chalinze ilifanyika kati ya mwaka 2015 na 2016 ili kuwezesha pamoja na mambo mengine wananchi wanaopitiwa na mradi kulipwa fidia na kupisha ujenzi wa mradi huo. Taratibu zote za uandaaji wa taarifa na majedwali ya fidia zilikamilika mwezi Machi 2020. Fidia kwa ajili ya maeneo kati ya Kiluvya (Kisarawe) hadi Chalinze ni takriban shilingi bilioni 21.569.

Mheshimiwa Spika, aidha, malipo haya yanahusisha Halmashauri za Kisarawe, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Chalinze. Kwa sasa taratibu za kuhamisha fedha za fidia kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwenda TANESCO ili kuwalipa fidia wananchi hao zinaendelea. Fidia ya wananchi hao italipwa mara tu baada ya taratibu hizo kukamilika.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Wilaya za Ilala, Ubungo, Kisarawe, Kibaha na maeneo ya Chalinze waliopisha mradi huo kuwa na subira wakati Serikali inakamilisha taratibu za malipo ya fidia kwa wananchi hao.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. SILVESTRY F. KOKA) Aliuliza:-

Miundombinu ya maji katika Shirika la Elimu Kibaha ilijengwa miaka 50 iliyopita kwa kutumia mabomba ya Asbestos ambayo siyo rafiki kwa afya za binadamu, lakini pia ni chakavu sana:-

(a) Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya maji katika shirika hilo?

(b) Je, ni lini Serikali itakarabati majengo ya Chuo cha FDC katika Shirika hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya maji katika Shirika la Elimu Kibaha inayotokana na miundombinu mibovu na ya muda mrefu ambayo ni kutokana na uwepo wa mabomba ya maji ya kipenyo cha milimita 200 yenye urefu wa kilomita nne na kipenyo cha milimita 150 yenye urefu wa kilomita mbili yaliyojengwa kwa asbestos tangu kuanzishwa kwa Shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali ilikwishabadilisha bomba la asbestos lenye urefu wa kilomita 0.75 la kipenyo cha milimita 200 na bomba lenye urefu wa kilomita moja na kipenyo cha milimita 150 kuwa PVC. Serikali itaendelea kubadilisha mabomba hayo kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Shirika linaendelea kufanya matengenezo madogo madogo kwa kutumia mapato ya ndani pindi uharibifu unapotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa shirika hili, imekamilisha ukarabati wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.6. Vilevile katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini ya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Shirika la Elimu Kibaha ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.48 kinahitajika ili kufanya matengenezo. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati. Hata hivyo, Shirika la Elimu Kibaha lilifanya ukarabati mdogo wa madarasa na jengo la utawala kwa kutumia mapato ya ndani ambao uligharimu shilingi milioni 25.73.
MHE. SIYLVESTRY F. KOKA aliuza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kumaliza mradi wa ujenzi wa barabara ya Makofia - Mlandizi - Vikumburu kupitia Mbwawa kwa kiwango cha lami ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Siylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Makofia – Mlandizi – Vikumburu yenye urefu wa kilometa 135.97 ni barabara ya mkoa inayounganisha Wilaya ya Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uhakiki wa mali zitakazoathiriwa na mradi kwa sehemu ya Makofia – Mlandizi – Maneromango yenye urefu wa kilometa 100 umekamilika. Kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii zitaanza kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara ya Ujenzi itaendelea kuihudumia barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 1,524.07 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Jimbo la Kibaha Mjini bado lina changamoto kubwa ya maji katika maeneo ya Kata za Mbwawa na Pangani; na Mradi wa Ujenzi wa matanki ya maji unakwenda kwa kusuasua. Je, ni lini Mradi huo utakamilika ili Wananchi wa Kibaha Mjini waondokane na adha ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/21, Serikali imekamilisha utekelezaji wa mradi wa maji ambao ulihusisha ulazaji wa bomba kuu pamoja na mabomba kwa ajili ya kutawanya maji kwa wananchi yenye urefu wa kilomita 27. Wananchi wapatao 6,500 wa Kata ya Mbwawa wananufaika na huduma ya maji tangu mwezi Aprili, 2021. Kwa upande wa Kata ya Pangani usanifu kwa ajili ya ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lita millioni 6 umekamilika.

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2021/2022, jitihada za kuboresha huduma ya maji katika maeneo ya Kibaha Mjini zinaendelea na kazi ya ujenzi wa tenki kubwa utaanza na ulazaji wa bomba kuu urefu wa kilomita tano utaanza katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/ 2022. Mradi huu utanufaisha wananchi wa Kata ya Pangani, pamoja na eneo la Viwanda la Kibaha Mjini (TAMCO).
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Mradi wa kusambaza umeme katika Jimbo la Kibaha Mjini unakwenda kwa kusuasua:-

Je, ni lini Mradi huo utakamilika ili Wananchi wa Kibaha Mjini waondokane na adha ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kusambaza umeme kwa Wilaya ya Kibaha Mjini (Peri-Urban) ulianza mwezi Novemba, 2019. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yanayonufaika na mradi huu ni pamoja na Pangani, Maili Moja, Picha ya Ndege na Sofu. Gharama ya Mradi ni shilingi bilioni 18.56.
MHE. SYLVESTRY F. KOKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kinazalisha bio-larvicides za kuangamiza viluilui vya mbu kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kiwanda cha viuadudu Kibaha, Tanzania Biotech Products Limited ni mali ya Serikali kwa asilimia 100. Kiwanda hiki kinao uwezo wa kuzalisha lita milioni sita za viuadudu vya kibaolojia (bio-larvicides) kwa mwaka vinavyotumika kuua viluilui wa mbu waenezao Malaria na aina nyinginezo.

Mheshimiwa Spika, kiwanda kinaendelea kuzalisha viuadudu vya kibaolojia ambapo tangu kiwanda kilipoanza uzalishaji mwaka 2017 hadi mwezi Agosti, 2021 kimeweza kuzalisha jumla ya lita 700,286.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali kupitia Shirika letu la Maendeleo ya Taifa (NDC) ni kuhakikisha kiwanda hiki kinazalisha kwa ukamilifu wake (full installed capacity) kwa kutafuta masoko zaidi ya viuadudu ya ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
MHE. SYLVESTRY F. KOKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuijenga kwa kiwango cha lami njia nane barabara ya Dar es Salaam hadi Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa la Mheshimiwa Sylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetangaza zabuni kwa ajili ya Expression of Interest kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Kibaha – Mlandizi – Chalinze hadi Morogoro yenye urefu wa kilometa 205 kwa utaratibu wa Engineering, Procurement, Construct and Finance (EPC + F). Gharama za ujenzi wake zitatolewa na Serikali au na sekta binafsi (PPP) kwa utaratibu wa Jenga, Endesha, Rudisha (Build Operate and Transfer) ambapo sekta binafsi itajenga barabara hii kwa fedha zake na kuiendesha hadi pale itakaporejesha fedha zake kupitia tozo za magari. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE K.n.y. MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza: -

Je, ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kibaha – Chalinze hadi Morogoro umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imekamilisha upembuzi yakinifu wa awali kutathimini uwezekano wa kujenga barabara ya Kibaha – Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilomita 205 kwa utaratibu wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi. Matokeo ya utafiti huo yalionesha mradi kuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi na kifedha iwapo itajengwa barabara ya njia nne ya kulipia katika ushoroba mwingine (new corridor). Barabara ya sasa inayotumika itaendelea kutumika na watumiaji ambao hawatakuwa tayari kupita katika barabara ya kulipia.

Mheshimiwa Spika, Mtaalam Elekezi ameanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ili kumpata mwekezaji wa kufanya ujenzi wa barabara ya kiwango cha expressway yenye njia nne ambapo sehemu ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze kilometa 78.9 imekamilika na kuidhinishwa na Wizara ya Fedha na Mipango tarehe 7/3/2023. Tangazo la kuwataka wazabuni kuonesha nia ya kuwekeza katika mradi huu limetolewa tarehe 14/3/2023 na mwisho ni tarehe 18/4/2023.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya Chalinze hadi Morogoro kilomita126.1, upembuzi na usanifu wa awali unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2024, ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani kuhakikisha wazee waliopigana Vita ya Pili ya Dunia chini ya Chama cha TLC wananufaika na mali zao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwezi Julai, 2022, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliunda Kamati maalum ya kuchambua na kutoa ushauri kuhusu hatma ya Askari waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1939 – 1945 na kuhusu mali za Chama cha Tanzania Legion & Clubs (TLC).

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini hiyo ilibaini kuwa Askari waliopigana Vita Kuu ya Dunia walikuwa 737, kati yao 57 wapo hai na 680 wamekwishafariki. Tathmini ilionesha pia kuwa TCL inazo mali zenye thamani ya Shilingi 37,366,323,048.000. Hata hivyo, baadhi ya mali hizo zina madeni na zingine zipo chini ya usimamizi au umiliki wa Taasisi nyingine na hivyo kusababisha mashaka kuhusu umiliki wake. Katika hali hii, mali zilizothibitishwa kuwa ni za TLC bila utata zina thamani ya Shilingi 15,952,574,800. Tathmini ilionesha pia kuwa, maveterani walio hai wanahitaji matunzo ikiwa ni pamoja na bima ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imetoa mapendekezo ya kuuza mali zisizo na utata ambazo nimezitaja za Shilingi 15,952,574,800 na kutoa fidia kwa Maveterani wote walio hai na warithi wa walio fariki. Pia kuwapatia bima ya afya Maveterani walio hai na kuwaenzi Maveterani wote kwa kujenga mnara wa kumbukumbu wa Askari wote waliopigana Vita Kuu ya Pili. Serikali inayafanyia kazi mapendekezo haya na tathmini kuhusu mali zenye utata inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ndiyo mkakati wa Serikali wa kuwaenzi waliopigana Vita ya Pili ya Dunia na kuhakikisha wananufaika na mali zao.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaupa hadhi ya Manispaa Mji wa Kibaha ambao ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri huanzishwa au kupandishwa hadhi kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 287 na 288 pamoja na Mwongozo wa uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014 ambapo umeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuanzisha na kupandisha hadhi halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Aprili, 2023 Halmashauri ya Mji Kibaha iliwasilisha ombi la kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Manispaa. Maombi haya yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa kuzingatia vigezo vilivyopo.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza eneo la ekari 1000 za Shirika la Elimu Kibaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) aliuliza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Elimu Kibaha lina eneo lenye ukubwa wa hekta 1,358 katika Mji wa Kibaha. Eneo lenye ukubwa wa hekta 675.31 limeendelezwa kwa huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika. Aidha, eneo lenye ukubwa wa hekta 220.1 limetengwa kwa ajili ya upanuzi wa huduma za Shirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lenye ukubwa wa hekta 170.913 limetengwa kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa la kilimo cha umwagiliaji (block farming). Aidha, Shirika limetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 38.84 kwa ajili ya uwekezaji (investment hub) lililopo mkabala na barabara ya Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lililobaki lenye ukubwa wa hekta 252.837 linatumika kwa ajili ya huduma nyingine za kijamii ikiwemo Makanisa na Misikiti na lina miundombinu ya umeme, maji na limepitiwa na bomba la mafuta (TAZAMA).
MHE. SYLVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Je, ni lini Mji wa Kibaha utakuwa Manispaa ambao kwa sasa ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri huanzishwa au kupandishwa hadhi kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 287 na 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014 ambao umeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuanzisha au kupandisha hadhi Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, ni kweli mapendekezo ya kupandisha hadhi Halmashauri ya Mji Kibaha kuwa Manispaa yaliwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Mapendekezo hayo yalifanyiwa uhakiki na timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI mwaka 2016 kati ya vigezo 20 Halmashauri ya Mji wa Kibaha ilikuwa imekidhi vigezo 15 sawa na asilimia 75 tu.

Mheshimiwa Spika, vigezo ambavyo havikuwa vimefikiwa na Mji wa Kibaha ni pamoja na idadi ya watu, idadi ya kata na mitaa, kutokuwa na mpango kabambe wa uendelezaji mji, kutofikia asilimia zinazohitajika za wakazi waliokuwa wameunganishwa na huduma ya maji. Hivyo, Halmashauri hii haikuweza kupandishwa hadhi kwa kuwa ililazimu kukidhi vigezo vyote kwa pamaoja kwa mujibu wa Mwongozo wa Kuanzisha Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014 ili kupandishwa hadhi ya kuwa Halmashauri ya Manispaa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo za Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Serikali kwa sasa inakusudia kuimarisha maeneo yaliyopo ili yaweze kutoa huduma zilizokusudiwa ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo. Hivyo, ninashauri Halmashauri ya Kibaha, kujikita katika kuboresha zaidi huduma za wananchi.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha Mamlaka ya Maji Mkoa wa Pwani ili kuondoa changamoto ya maji maeneo mengi ya mkoa huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya huduma majisafi na salama katika Mkoa wa Pwani ni wastani wa 79.8% kwa vijijini na 90% kwa mijini ambapo huduma hiyo inatolewa kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa upande wa vijijini na kwa maeneo ya mijini huduma hiyo inatolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaridhishwa na taasisi zinazotoa huduma ya majisafi na salama katika Mkoa wa Pwani ambapo maeneo yote ya mijini yanapata huduma za maji safi kwa viwango mbalimbali. Hata hivyo, Serikali ipo tayari kufanya mabadiliko yoyote yanayolenga kuboresha eneo la utoaji huduma ya maji katika Mkoa wa Pwani pindi itakapoonekana inafaa. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwegere Wilaya ya Ubungo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa Daraja la Mto Mpiji linalounganisha Halmashauri ya Mji wa Kibaha na Kibwegere katika Wilaya ya Ubungo. TARURA kwa kushirikiana na Mhandisi Mshauri Smarcon imefanya usanifu wa kina (detailed design) wa daraja hilo lenye urefu wa mita 60. Kazi hiyo imekamilika na inakadiriwa gharama za ujenzi kuwa ni shilingi bilioni tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo, na pindi zitakapopatikana, ujenzi utaanza mara moja.
MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Je, ni lini Mradi wa Ujenzi wa Tenki la Maji la Pangani – Kibaha utaanza kwa kuwa mkataba wa ujenzi ulishasainiwa tangu mwezi Desemba, 2023?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kukamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa tank la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni sita katika Kata ya Pangani, Jimbo la Kibaha Mjini ambapo utekelezaji wake unatarajia kuanza Oktoba, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingine zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (Pump Station), sambamba na ununuzi na ufungaji wa pampu zenye uwezo wa kuzalisha maji lita 250,000 kwa saa, ujenzi wa tank la kukusanyia maji (sump well) lenye ujazo wa lita 540,000 na ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 18.7. Muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi 12 ambapo unatarajiwa kuhudumia wananchi 6,800 waishio kwenye Kata ya Pangani.