Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Selemani Said Jafo (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika leo hii ambapo tunahitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa imani yake kubwa kwangu kwa kunipa nafasi ya kuhudumu katika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Napenda pia kutoa shukrani zangu kwa Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi bora. Shukrani za pekee ziende kwa Waziri wangu Mheshimiwa George Simbachawene ambaye alikuwa akinipa maelekezo ya mara kwa mara katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nachukua fursa hii kuwapongeza viongozi wote wa Bunge wakiongozwa na Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri uliowezesha Bunge hili Tukufu kujadili bajeti hii. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa uchambuzi wa kina ambao umesaidia sana kuboresha bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa kunipa fursa tena kwa nafasi hii kwa mara nyingine ya pili kuhudumu katika Bunge hili. Ndugu zangu wananchi wangu, nawapenda sana, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa umuhimu sana nipende kuishukuru familia yangu, wake zangu pamoja na watoto. Shukrani kubwa zaidi ziende kwa mama yangu mzazi aliyenizaa na kunilea vizuri pamoja na baba yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi sasa naomba nijielekeze katika kujibu baadhi ya hoja zilizochangiwa na Waheshimiwa Wabunge kwa njia ya maandishi na kwa kuzungumza. Majina ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia watatajwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI atakapokuwa akijibu hoja mbalimbali za Wabunge. Kutokana na muda, hoja ambazo hazitajibiwa hapa tutaziwasilisha kwa maandishi ili Waheshimiwa Wabunge wote waweze kuzipitia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi walichangia katika maeneo yafuatayo:-
(i) Usimamizi wa mapato katika Serikali za Mitaa;
(ii) Maeneo mapya ya utawala;
(iii) Migogoro ya ardhi;
(iv) Usimamizi wa watumishi katika mamlaka ya Serikali za Mitaa; na
(v) Kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji na mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukianza katika hoja zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ambazo kwa kiwango kikubwa zimeungwa mkono na Wajumbe wengi katika Bunge hili, lilikuwa suala zima la Halmashauri kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana. Ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Halmashauri zote zimeelekezwa kupitia mwongozo wa bajeti kutenga 10% kwa ajili ya mkopo wa vikundi vya wanawake na vijana. Aidha, katika uchambuzi wa bajeti agizo hili limezingatiwa na Halmashauri zote zimetenga 10% ya mapato ya ndani. Wakuu wa Mikoa wanaelekezwa kusimamia utekelezaji wa jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza hapa, sisi Wabunge wote ni Wajumbe wa Kamati za Fedha na Mabaraza ya Madiwani. Kwa sababu mwongozo wa bajeti umeshaeleza na Halmashauri zote zimeshatenga 10% katika bajeti zao za mapato ya ndani na ndiyo criteria iliyotumika kupitisha bajeti ya kila Halmashauri yake, tuna jukumu la kuhakikisha suala hili linatekelezwa. Kwa sababu hii 10% ni own source kwa maana kwamba ni mapato ya ndani yanayokusanywa katika Halmashauri husika, ina maana pesa zile zinaishia katika Halmashauri na kwamba Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani ndilo linafanya maamuzi hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia yangu ni kusema kwamba kila Mbunge akitoka hapa atahakikisha kitachokusanywa kinagawanywa kwa wananchi ili mradi vijana na akina mama waweze kupata mikopo hiyo. Nisisitize pia tutakapofanya hivyo lazima tuangalie ni jinsi gani tunawagusa walemavu ili mradi nao waweze kushiriki katika shughuli za ujasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kulikuwa na hoja ya ukusanyaji wa ushuru wa minara ya simu na mabango ambapo suala hili limekuwa ni changamoto kubwa. Ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba ushuru wa minara ya simu na mabango hutozwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali ya Mitaa, Sura Na. 290. Kuhusu malipo ya vijiji na watu binafsi, malipo haya hulipwa kwa mmiliki wa eneo ambalo minara huwekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, malipo haya hayahusiani na malipo ya ushuru ambayo Halmashauri inatakiwa iyapate. Hivi sasa Serikali inakusudia kuwasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Serikali za Mitaa ili kuweka mfumo mzuri wa malipo, ushuru wa minara na mabango kwa watu binafsi katika Serikali ya Vijiji ili mradi uwe sawasawa kwamba kila Halmashauri iweze kunufaika na mchakato huo tunavyoenda katika ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa suala zima la matumizi ya mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri. Jambo hili tumelielezea katika vipindi mbalimbali na Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele kulisimamia hili na kutoa maagizo. Katika bajeti ya mwaka huu tunasema itakapofika muda ulioagizwa katika hotuba ya mwaka wa fedha 2016/2017 tuliyoisoma hapa ambayo inajiainisha katika ukurasa namba 13 na 16, kwamba kuanzia Julai 1, 2016 kila Halmashauri zote zinatakiwa kukusanya mapato yake yote kwa mifumo ya kielektroniki. Baada ya mifumo hii kuanza hakuna Halmashauri itaruhusiwa kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge, sisi ni Wajumbe katika Mabaraza yetu, kila mtu akachukue nafasi yake kuhakikisha kwamba katika Halmashauri yake anakwenda kuweka misingi imara ili mwaka wa fedha 2016/2017 twende katika mfumo thabiti wa kuweza kukusanya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tumetoa maelezo sehemu tofauti kwamba tulipotumia mifumo hii mabadiliko ya ukusanyaji wa mapato yamekuwa makubwa sana. Sehemu ambayo walikuwa wanakusanya shilingi 200,000 mpaka shilingi 300,000 kwa siku, mara baada ya kuweka mfumo huu watu wanakusanya zaidi ya shilingi 3,000,000 mpaka shilingi 4,000,000. Ni jukumu la kila Mbunge kuhakikisha sasa anaenda kusimamia eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Ofisi ya Rais - TAMISEMI, tunatoa onyo kwa watendaji ambao wataenda ku-temper na mifumo hii. Naomba niwaeleze, watendaji wote ambao watathubutu kwa njia moja au nyingine kwenda kuhujumu mifumo hii, tutahakikisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaenda kuwashughulikia kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala zima la Halmashauri irejeshewe 70% ya kodi ya ardhi badala ya 30%. Majibu ya hoja hii ni kwamba utaratibu wa kugawanywa kodi ya ardhi ya asilimia 30 kwa Halmashauri na asilimia 70 kwa Wizara ya Ardhi umewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya sheria hii yanayopendekezwa pamoja na wazo la kuwezesha Halmashauri kubaki na mgao unaostahili kabla ya kuwasilisha Wizarani, mchakato huu sasa unaenda ambapo marekebisho haya ya sheria yatakapokamilika, jambo hili tutaliangalia sote kwa pamoja kuona ni jinsi gani tuliweke ili mradi Halmashauri ziweze kukidhi kupata mapato halisi katika suala zima la Kodi ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna hoja imejitokeza sana kuhusu suala zima la Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) juu ya uhamishaji wa Mfuko wa CHF. Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia na Mwenyekiti wa Kamati alilielezea hili katika taarifa yake. Kwa hiyo, ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoko sasa, imeweka utaratibu wa hiari kwa kila kaya kujiunga katika Mfuko huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa Wizara ya Afya inaandaa Muswada wa Sheria ya kufanya Mfuko wa Afya ya Jamii kuwa lazima. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Viongozi katika ngazi zote, wataendelea na jitahada mbalimbali za kuwaelimisha wananchi ili kuhakikisha kwamba wale wadau mbalimbali kama waendesha bodaboda, mamalishe, watu wa pikipiki, wafanyabiashara wadogo, basi wote mwisho wa siku waweze kujiunga katika Mfuko huu kwa ajili ya kuimarisha afya ya Taifa letu na wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lililojitokeza ni kwamba, Serikali itoe fedha za Halmashauri ili kulipa madeni ya Wazabuni na Wakandarasi, kuondoa usumbufu kwa Halmashauri kutoka kwa wadeni wao. Hoja hii imejadiliwa na Wabunge wengi. Kama nilivyosema, Waziri wangu wa Nchi akifika hapa atakuja kutoa ufafanuzi mbalimbali kwa Wabunge wote waliochangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya hoja hii ni kwamba Serikali inatambua madeni ya Wazabuni yaliyopo, waliotoa huduma mbalimbali katika Serikali kuu, Halmashauri na Taasisi zetu. Serikali itahakikisha kwamba madeni hayo yataendelea kulipwa kwa kadri fedha zitakavyopatikana. Aidha, Halmashauri zinaelekezwa kutoanzisha madeni mengine mapya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine iliyojitokeza kuhusu suala zima la ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Hii ilikuwa moja, lakini nilivyofuatilia nimeona ni watu wengi wamekuja na hoja hii kuhusu maeneo yao. Kwa hiyo, nijibu kwamba tuna Halmashauri zipatazo 44 ambazo ujenzi unaendelea na tumetenga kati ya Shilingi milioni 500 mpaka Shilingi milioni 850. Naomba nizitaje Halmashauri hizo kwa faida ya Bunge hili kwa sababu kila mtu atataka kujua katika eneo lake ni eneo gani limeguswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ambazo zimetengewa mgao huo kati ya Shilingi milioni 500 mpaka Shilingi milioni 850 ni Kalambo DC, Kyela DC, Bumbuli DC, Kaliua DC, Nkalama DC, Ikungi DC, Ushetu DC, Nyasa DC, Ilemela MC, Masasi DC, Gairo DC, Busokelo DC, Momba DC, Uvinza DC, Kakonko DC, Buhigwe DC, Mbogwe DC, Nyang’hwale DC, Njombe TC, Wanging’ombe DC, Makambako TC, Mlele DC, Msimbo DC, Mpanda DC, Simanjiro DC, Kiteto DC, Mkinga DC, Kilinda DC, Mpangani DC, Magu DC, Mtwara DC, Chamwino DC, Mafia DC, Kibaha DC, Msalala DC, Kahama TC, Butiama DC, Tarime DC, Chemba DC, Kibaha TC, Geita TC, Busega DC, Itirima DC na Bariadi TC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna Halmashauri mpya ambazo zimeanzishwa zipatazo 20 na ambazo zimetengewa Shilingi bilioni 2,140 ambazo ni Busocha DC, Bunda TC, Chalinze DC, Handeni DC, Ifakara TC, Itigi DC, Kasulu TC, Kibiti DC, Kondoa TC, Madaba DC, Mafinga TC, Malinyi DC, Mbinga TC, Mbulu TC, Mpindwa TC, Nanyamba TC, Newala TC, Nzega TC, Songwe DC na Tunduma TC. Hizi zimetengewa Shilingi bilioni 2,140 ambayo inaenda kuanza ujenzi katika harakati hizo. Nimeamua kuzitaja hizi kwa sababu kila Mbunge hapa alikuwa anazungumza suala zima la ujenzi wa Halmashauri mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maeneo ambayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa nafasi niliyopata kidogo naomba niendelee kufafanua. Vile vile kuna suala zima la Chemba ambapo Mheshimiwa Felister Bura alikuwa anazungumzia kuhusu ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Chemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi wa majibu yetu unasema, Halmashauri ya Chemba imetenga eneo la ekari nane kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, zimetengwa Shilingi milioni 20 kwa ajili ya kupima eneo ili maandalizi ya awali ya ujenzi wa hospitali hiyo yaanze.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala kwamba mradi wa umwagiliaji wa Gawaye, Manispaa ya Dodoma na Mradi wa Maji, Bahi ukamilishwe. Katika ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeendelea kukamilisha ujenzi wa mfumo wa umwagiliaji katika Kijiji cha Gawaye kwa gharama ya Shilingi milioni 631.68. Kazi hii ya uwekaji mifumo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2016, ambapo jumla ya eneo la ukubwa la ekari 97 umekamilika kati ya ekari 100. Inatarajiwa kuwekewa mifumo hiyo ya umwagiliaji na kuwezesha wananchi kulima zao la zabibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile watu wamechangia katika eneo la elimu hasa katika suala la elimu bure. Kulikuwa na mawazo ambayo wengine wanasema suala la elimu bure halikuleta tija. Kikubwa zaidi naomba niwashukuru Wabunge wote. Karibu asilimia 99, kila Mbunge aliyesimama hapa alikuwa ana-appreciate suala zima la elimu bure. (Makofi)
MheShimiwa Naibu Spika, ni lazima tukiri, kuna wenzetu ambao ni maskini kabisa, hali ilikuwa ni ngumu. Leo hii ndiyo maana hata tulipoanzisha suala hili, kuna watoto ambao tumewasajili mwaka huu wana miaka 10 mpaka 11. Nini maana yake? Maana yake watoto hawa walikuwa wanakosa fursa ya kwenda shule kutokana na hali ya maisha yao. Leo hii tumekumbwa na tatizo la madawati kwa sababu idadi kubwa ya watu waliokuwa wanakosa elimu, sasa wameenda shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo la kuishukuru sana Serikali na Chama cha Mapinduzi na mtazamo wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekubali kutenga Shilingi bilioni 16.77 kila mwezi kwa ajili ya ruzuku katika eneo hili. Kwa hiyo, tunashukuru sana. Naamini kwamba jambo lolote lina changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake kwa kazi kubwa waliyoifanya; na kwa sababu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni Wizara pacha na Wizara ya Afya lakini ukienda katika Wizara ya Elimu, Wizara ya Maji unaikuta TAMISEMI inazungumzwa muda wote; na ukiangalia michango mingi sana imejilenga katika suala zima la uboreshaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea mchango wa Kamati ambao maelekezo yake kwa kiwango kikubwa na michango ya baadhi ya Waheshimiwa Wajumbe wengi sana walipendekeza ikiwezekana mambo ya afya yote yabakie katika Wizara ya Afya, ambalo hili nimeona watu walikuwa wakipendekeza kwamba itoke TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nifanye rejea kidogo katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, nawaomba Waheshimiwa Wabunge ikiwezekana turejee katika Katiba, Ibara ya 145 na Ibara ya 146 yenye kuweka utaratibu wa Serikali za Mitaa, lakini vile vile Ibara 146 ikizungumza majukumu ya Serikali za Mitaa. Hili lina umuhimu mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hapa kuna ajenda moja ya msingi ambayo tunatakiwa kama Wabunge tuiangalie kwa pamoja, tuone jinsi gani tutafanya kuweza kupata fedha za kutosha kuhakikisha tunahudumia huduma za afya. Hili ndilo jambo la msingi. Kwa sababu hata ukichukua mambo yote ukipeleka Wizara ya Afya; leo hii tunapozungumza deni hata la MSD halipo TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sugu alikuwa anazungumzia suala zima Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwamba haiko TAMISEMI. Maana yake ni nini? Ni kama Taifa, kama Serikali sasa hivi inavyojipanga ya Awamu ya Tano kutafuta fedha kwa kadiri iwezekanavyo kutoa huduma za kijamii katika jamii yetu, hilo ni jambo la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme kwamba, kama Wabunge tujiandae vya kutosha tuone jinsi gani tutaimarisha Sekta ya Afya. Tutaimarisha Sekta ya Afya katika kuhakikisha tunafanya kila liwezekanalo kutafuta fedha nyingi za kutosha kuhudumia miradi ya afya. Hili tukilifanya vizuri, maana yake ni nini? Ukizungumza kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, walioajiriwa zamani wanafahamu. Leo hii mhudumu wa afya au nurse yuko Kigoma au yuko Kibondo, umwambie siku ya kupandishwa daraja lake, maana yake ni mpaka aende Makao Makuu ya Wizara. Ndugu zangu, tutazalisha matatizo makubwa kuliko tanayoyaona hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuseme, ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, naamini kila Mbunge alishiriki katika bajeti ya Halmashauri yake na kila Mbunge aliainisha vipaumbele vyake vya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na kila Mbunge aliweka kipaumbele chake cha ununuzi wa gari la wagonjwa, halikadhalika Hospitali ya Wilaya, lakini bajeti ni mchakato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaanza katika ngazi za Vijiji, unakuja katika ODC, inakuja katika Halmashauri, inaenda katika Wizara, lakini mara nyingi sana tunazungumza ukomo wa bajeti. Ukomo huu wa bajeti tusipoweka nguvu za kutosha za ukusanyaji wa kodi, maana yake hapo tutakwama. Kwa hiyo, nataka niwashawishi Waheshimiwa Wabunge, kwamba katika ile ajenda ya kufikiria kwanza saa nyingine tuiondoe yote, ina maana kwanza tunakuwa tumevunja Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara 145 na Ibara 146. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata watumishi tunaowahudumia ambao wako vijijini itakuwa ni changamoto kubwa, itakuwa ni mzigo mkubwa sana, tutakuja kumlaumu hapa Waziri wa Afya kwamba kuna watumishi wako, wako kule Kibondo, Mtwara au wapi, hawajapanda madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utaratibu utakuwa mzuri, kama fedha zitakuwa zinapatikana vizuri, naamini tuta-empower Mabaraza yetu ya Madiwani, yatafanya maamuzi sahihi zaidi katika kuweka vipaumbele vya kuhakikisha Sekta ya Afya inakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwashawishi Waheshimiwa Wabunge hapa, haya mambo kwa sababu naamini Wizara ya Afya kama ni regulator, yeye anasimamia sera na anasimamia hospitali za Serikali, halikadhalika katika sekta binafsi, jambo hili tukiliweka vizuri hasa katika kutafuta rasilimali fedha halafu kuzisukuma chini katika Halmashauri na kwa sababu kuna mfumo uliokamilika kwa…
Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kuleta Azimio hili hapa Bungeni, kwa sababu najua jambo hili ni jambo lenye manufaa makubwa sana kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa Kiongozi mwenye dhamana katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Azimio hili kwetu tunalipokea kwa mikono miwili, nikijua wazi kwamba vijana wetu wanaosoma shule za msingi na sekondari, hivi sasa tunapojielekeza katika suala zima la michezo mashuleni, sasa Azimio hili linatupa nafasi nzuri sana ya kuwaandaa vijana wetu katika michezo bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia kuhusu vijana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na timu yake. Juzi tuliwashuhudia vijana wetu wa Serengeti Boys kule India wakifanya maajabu makubwa sana. Mheshimiwa Naibu Waziri, ikikupendeza sana vijana wale inapaswa tuwalete hapa Bungeni tuwatie moyo, walifanya kazi kubwa kwa kushiriki michezo ile, katika michezo yote hakuna mchezo waliofungwa, walifanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana vilevile nilishuhudia katika vyombo vya habari, timu yetu ya Azam ya Vijana, walipokuwa wakishirikisha timu za Uganda, Kenya na hapa Tanzania, katika timu yao ni kwamba michezo yote wameweza kufanikisha, wameshinda michezo yote na kupata kombe lile, imeleta heshima kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ina jukumu la michezo ya UMISETA ambayo inaendelea hivi sasa, naomba tulipokee Azimio hili kwa moyo mkunjufu, nikijua kwamba katika michezo yetu hii, sisi kama Serikali tunaoasisi michezo mashuleni, vijana wetu hawa tukiwaandaa vizuri katika Azimio hili sasa, maana yake tutaweza kupata vijana bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siku za usoni tujue vijana hawa ndiyo tunatakiwa sasa tuwalee vizuri katika suala zima la taaluma, huko baadaye tukapate Madaktari na Professors. Kama tusipokuwa na usimamizi mzuri katika eneo hili maana yake vijana leo hii wanaposhiriki michezo wataweza kutumia madawa haya, mwisho wa siku wanapofika sasa katika kutumia akili yao katika taaluma inawezekana tukawa na vijana wengi ambao watashindwa kufanya vizuri kimasomo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nampongeza sana, Azimio hili limekuja katika muda muafaka. Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba nimhakikishie wazi, kwa sababu tuna mtandao mpana wa vijana katika shule zote, tutahakikisha tunashirikiana na Wizara ya Habari na Michezo kuhakikisha kwamba jambo hili linatelekezwa vizuri katika shule zetu zote ili vijana wetu wanapokwenda kushiriki katika michezo, kwanza iwe ni ajenda ya kudumu katika michezo yote; kwamba wafahamu utumiaji wa dawa hizi siyo sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kwamba, kutoa maelekezo ya kutosha kwamba wao wawe Mabalozi wazuri kuhakikisha kwamba tunalea kizazi cha vijana ambao watakuwa wazuri wa kuelewa jambo hili la utumiaji wa madawa ya kuongeza nguvu katika michezo siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, langu lilikuwa ni commitment katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwamba tutashirikiana vema kuhakikisha kwamba Serikali yetu inakuwa ni Serikali ya mfano, kwa suala la utumiaji wa dawa katika kuongeza nguvu katika michezo halitoruhusiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia zote mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwa upande wangu kwanza, nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha leo hii tunajadili hoja muhimu sana za Kamati, lakini kubwa zaidi nipende kuzipongeza Kamati zote mbili.
Kamati hizi mbili zote zilizowasilisha hotuba zake hapa zimetuonesha kwamba, ni jukumu gani tunatakiwa tulifanye katika kipindi hiki cha sasa baada ya kupata ripoti hizi zilizofanyika mwaka 2014 na 2015. Tukiwa mwaka 2016 sasa, kama Wabunge na kwa ujumla kama Serikali tujue tutafanyaje ili wananchi waweze kupata huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze katika Kamati ya LAAC. Naomba nimpongeze Mwenyekiti na timu yao yote ambayo katika njia moja au nyingine, wao wanatusimamia zaidi kwa karibu katika ofisi yetu. Naomba nikiri wazi kwamba, maelekezo waliyoyatoa kwetu sisi na kaka yangu Boniface Simbachawene tumepata viongozi ambao wanatushauri ili kazi yetu iweze kufanyika vizuri katika kipindi cha sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja mbalimbali lakini zote zina mashiko. Hoja ya kwanza ilikuwa ni suala zima la Sheria ya Manunuzi na kweli ukifuatilia ripoti ya Mkaguzi na hali kadhalika Kamati ilivyofanya uchambuzi mbalimbali ilibainika kwamba kuna changamoto kubwa sana na kutoa maelekezo nini tukifanye. Katika hili, ofisi yetu imeshaanza kuyafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza tumetoa maelekezo katika Halmashauri zote; kwa vile tuna watendaji katika ngazi mbalimbali wengine wakiwa wapya, wahakikishe katika utiifu wa utendaji wa kazi zao, jambo la kwanza wanazingatia Sheria ya Manunuzi ili kuleta tija katika Halmashauri zetu. Hata hivyo, ukifuatilia ile ripoti imeonesha maeneo mbalimbali ambayo watu walifanya mambo ya hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie na nilijulishe Bunge lako kwamba, katika eneo hili tumechukua hatua mbalimbali. Katika Halmashauri mbalimbali baadhi ya Wakurugenzi wamepoteza nafasi zao, lakini baadhi ya Wakuu wa Idara waliobainika, wameweza kuchukuliwa hatua mbalimbali na hivi sasa wengine wamepelekwa mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili katika ofisi yetu hatutavumilia kabisa, wale wote ambao wameonekana ni kikwazo ambao kwa njia moja au nyingine wamehujumu fedha za Serikali na sisi tukiwa tumepewa dhamana katika eneo hilo; naomba tulihakikishie Bunge lako kwamba, ofisi yetu imejipanga hivi sasa tutafanya marekebisho makubwa sana na ndiyo maana nimesema kwamba, Kamati imeibua jambo hili ambalo ni jema, ni maelekezo na sisi tunakwenda kulifanyia kazi.
Suala lingine ni Udhaifu Katika Usimamizi na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Ni kweli, Kamati ilibaini kulikuwa na udhaifu mkubwa sana katika maeneo mbalimbali, lakini katika eneo hili kulikuwa na marekebisho ya kimuundo kidogo baada ya kupitia hizi hoja mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ofisi yetu hivi sasa kuna Kitengo Maalum cha Ufuatiliaji ambacho kinafuatilia maeneo mbalimbali katika jitihada za kuhakikisha kwamba miradi hii iweze kutekelezeka vizuri, hasa kwa fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, jukumu lake kubwa vilevile ni kuhakikisha kwamba inatoa ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya CAG na Kamati ya LAAC. Ndiyo maana katika kipindi chote cha mijadala baadhi ya wawakilishi wa kitengo hiki walikuwepo katika mijadala hii kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa jinsi ya kufanya katika maeneo mbalimbali ili yaweze kuleta tija katika eneo letu la kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana katika suala zima la ufuatiliaji, Waziri wangu hapa alitoa maelekezo mbalimbali hata kule Kigoma na Kasulu na baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali walichukuliwa hatua za kinidhamu mara baada ya kubainika kwamba baadhi yao walishindwa kutimiza wajibu wao wa kikazi waliopewa. Katika taarifa mbalimbali hivi sasa, ukisoma racket news, ukiangalia kule Kinondoni, Kondoa, Kahama, Kigoma-Ujiji na maeneo mengine mbalimbali baadhi ya watu wamechukuliwa hatua. Hii ni kwa sababu tunatekeleza lile ambalo limeonekana kwamba lilikuwa ni changamoto kubwa sana katika ofisi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kila sababu kulinda rasilimali hizi za wananchi ili ziweze kuleta tija katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja inayohusu uzembe katika kusimamia Mifumo ya Makusanyo ya Mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika hilo na ndiyo maana tumefanya kazi kubwa sana. Wakati tunaingia pale na kaka yangu Boniface Simbachawene Halmashauri zilizokuwa zinakusanya kwa kutumia mifumo ya kielekitroniki zilikuwa chini ya asilimia 30; leo hii tumefikisha karibuni asilimia 92. Hata hivyo, tumetoa maelekezo mbalimbali katika zile Halmashauri mpya ambazo hazina network hasa za umeme na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunafikia lengo la asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini, maelekezo haya ya Kamati tuna kazi kubwa tunayoifanya katika ofisi yetu hapa na tutafika mahali pazuri na ndiyo maana leo hii Halmashauri mbalimbali zimeweza kukusanya karibuni mara mbili ya ukusanyaji wa mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikushukuru sana, na kwa vile nina ufinyu wa muda, nipende kushukuru. Kubwa zaidi ni Kamati iliyotusaidia na naomba tukiri katika Kamati hii kwamba, ofisi yetu itajitahidi kutekeleza maelekezo yote kwa mustakabali wa nchi yetu ambao tunajua ndiyo tija wanayoitarajia wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.