Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Selemani Said Jafo (301 total)
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Kituo cha afya Kisesa kiliombewa kibali ili kipandishwe hadhi kuwa Hospitali kamili:-
Je, ni lini Serikali itatoa kibali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, kila Wilaya inatakiwa kuwa na hospitali moja ya Wilaya na tayari hospitali hiyo ipo katika Wilaya ya Magu. Kituo cha Afya cha Kisesa kiliombewa kuboreshwa ili kiweze kutoa huduma za upasuaji mdogo kukidhi mahitaji hayo kwa wagonjwa badala ya kutegemea hospitali ya Wilaya pekee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kituo hicho kianze kutoa huduma za upasuaji, Serikali iko katika hatua za mwisho za umaliziaji wa ujenzi wa jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti pamoja na chumba cha X-ray. Aidha, tayari X-ray machine imeshapatikana, inasubiri tu kufungwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa chumba cha X-ray.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaharakisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Kata za Manolo, Shume, Sunga na Mbaru ili kuwaondolea usumbufu Wananchi wa maeneo hayo ikiwemo ushiriki hafifu kwenye shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mlalo linakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 196,258 kati yao ni asilimia 69 tu wanaopata huduma ya maji safi na salama. Aidha, kwa kutambua tatizo hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ina mradi wa maji wa Shume, Madala na Manolo. Mradi huu unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 2.96 hadi kukamilika ambapo kampuni ya Orange Contractor Ltd. kwa kushirikiana na Linda Technical Service Ltd. kutoka Mjini Lushoto na tayari mkataba umesainiwa. Hata hivyo, kazi hii inasubiri upatikanaji wa rasilimali fedha. Mradi huu unatarajia kuhudumia wananchi wapatao 33,541 katika Kata hizo. Mradi huu utakuwa na urefu wa kilomita 55, vituo 70 vya kuchotea maji pamoja na matenki matatu ya kuhifadhia maji.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Mbaru, Halmashauri kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la CHAMAVITA liliufanyia ukarabati mradi mkubwa wa maji wa Rwangi. Kwa mwaka wa fedha 2013/2014 CHAMAVITA ilitumia shilingi bilioni 96.0 kwa ajili ya kuboresha mradi huo kwa kupanua mfumo huo kutoka Kijiji cha Nkelei hadi Vijiji vya Mamboleo na Kalumele ambavyo vipo Kata ya Mbaru. Wananchi wa Vijiji hivi wanapata maji kutoka kwenye tanki la maji kwa Kwekidevu lenye ujazo wa lita 22,500.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Sunga yenye Vijiji vitano vya Sunga, Kwemtindi, Masereka, Nkukai na Mambo inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 12,122. Huduma ya maji kwa Kijiji cha Mambo inapatikana kupitia visima vifupi viwili vyenye pampu ya mkono pamoja na vituo vinne vya kuchotea maji kutoka kwenye Mradi Mdogo na Mserereko ambao hauna tanki la kuhifadhia maji. Mradi huu mdogo ulijengwa na Mwekezaji wa Mambo View Hotel kwa gharama ya shilingi milioni 5.0. Katika mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa wastani Kata ya Sunga wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama ni asilimia 16 tu.
Mheshimiwa Spika, vijiji vya Sunga, Kwemtindi, Masereka, Nkukai na Mambo katika Kata ya Sunga vitapewa kipaumbele mara tu baada ya vijiji kumi vya awamu ya kwanza ya programu ya maji kukamilika. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Mlalo na maeneo mengine nchini kadri rasilimali fedha zinavyopatikana.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Mradi wa maji kisima kirefu katika Mji Mdogo wa Tinde umechukua muda mrefu sana kukamilika:-
Je, ni lini sasa mradi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua tatizo hilo la maji, Serikali katika mwaka fedha 2014/2015 ilitenga shilingi milioni 100 ambazo zilitumika kwa ajili ya kulipia gharama za uchimabaji wa kisima kirefu katika Mji wa Tinde, ujenzi wa vituo vinne vya kuchotea maji na ujenzi wa nyumba ya pampu. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imepeleka jumla ya shilingi milioni 200 ambazo zimepokelewa mwezi Novemba, 2015 na zitatumika kwa ajili ya ununuzi na ufugaji wa pampu na mfumo wa umeme wa jua pamoja na miundombinu yake yote. Kazi nyingine zinazofanyika ni ujenzi wa msingi wa kitako pamoja na ununuzi wa matenki ya kuhifadhia maji yenye ukubwa wa mita za ujazo 20, na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa mita 5,200. Aidha, kazi hii inafanywa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Shinyanga na inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2016.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Nyumba za kuishi walimu ni chache katika maeneo yao ya kazi na
mishahara yao pia ni midogo kuweza kumudu upangaji wa nyumba mitaani.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za walimu na
kuboresha mishahara yao?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Destery, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya nyumba za walimu wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Magu ni 1,447, zilizopo ni nyumba 284 na upungufu ni nyumba 1,183. Aidha, Shule za Sekondari zina mahitaji ya nyumba 396, zilizopo ni nyumba 53 na upungufu ni nyumba 343.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari ya Awamu ya Pili (MMES II), Halmashauri imepokea shilingi milioni 326.8 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya nyumba za walimu. Kwa upande wa Shule za Msingi, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 imetenga shilingi milioni 100 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa nyumba tano na shilingi milioni 127 zimetengwa kupitia ruzuku ya maendeleo (CDG) kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba sita za walimu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuboresha mishahara ya walimu, Serikali imekuwa ikitoa nyongeza za mishahara kila mwaka kadiri uchumi unavyoruhusu. Kwa mfano, mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2015/2016 mshahara wa mwalimu mwenye cheti yaani astashahada, uliongezeka kwa asilimia 156.28 kutoka shilingi 163,490/= hadi shilingi 419,000/= kwa mwezi. Mshahara wa mwalimu mwenye stashahada uliongezeka kwa asilimia 160.2 kutoka shilingi 203,690/= hadi shilingi 500,030/=; na kwa mwalimu mwenye shahada kwa asilimia 121.05 kutoka shilingi 323,900/= hadi shilingi 716,000/= kwa mwezi. Serikali imekuwa ikiboresha mishahara hiyo kwa kuzingatia umuhimu wa kazi wanayofanya walimu. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuboresha mishahara ya walimu na watumishi wengine kwa kadiri hali ya kifedha inavyoruhusu.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Wilaya ya Morogoro ina Halmashauri mbili; Makao Makuu ya Wilaya yapo mjini na huduma zote kuu za Kiwilaya kama vile hospitali, polisi, mahakama na kadhalika zinapatikana Morogoro Mjini, hivyo kuwalazimu wananchi wa Morogoro Vijijini kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 150 kufuata huduma hizo:-
(a) Je, ni lini Serikali itaifanya Halmashauri ya Morogoro Vijijini kuwa Wilaya kamili na kuhamishia Makao Makuu ya Wilaya katika Kijiji cha Mvuha na kuwaondolea adha wananchi?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha taasisi za fedha kama vile benki kufungua matawi na huduma ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ili kuweza kuvutia kampuni mbalimbali ya kibiashara na wawekezaji na kuinua maisha ya wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Morogoro ina Halmashauri mbili. Makao Makuu ya Wilaya yapo Mjini na huduma zote za Kiwilaya kama vile hospitali, polisi, mahakama na kadhalika zinapatikana Morogoro Mjini na kuwalazimu wananchi wa Morogoro Vijijini kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa 150 kufuata huduma hizo.
(a) Wilaya ya Morogoro inaundwa na Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Uanzishwaji wa Wilaya unazingatia Sheria ya Uanzishwaji wa Mikoa na Wilaya Sura Na. 397 ya mwaka 2002 ambayo pia imeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kuzingatia.
Mheshimiwa Spika, taratibu zinazopaswa kuzingatiwa ni pamoja na maombi ya kujadiliwa kwenye Serikali za Vijiji ili kupata ridhaa ya wananchi wenyewe, maombi kujadiliwa kwenye Baraza la Madiwani, vikao vya Kamati ya Ushauri vya Wilaya yaani DCC na Kamati ya Ushauri ya Mkoa yaani RCC. Maamuzi ya vikao hivyo huwasilishwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa ajili ya uratibu na uhakiki.
Aidha, vigezo vinavyozingatiwa katika kuanzisha Wilaya mpya ni pamoja na ukubwa wa eneo usiopungua kilometa za mraba 5,000. Idadi ya watu wasiopungua kati ya 250,000 hadi 300,000, idadi ya Tarafa zisizopungua tano, idadi ya Kata zisizopungua 15 na idadi ya vijiji visivyopungua 50.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) haijapokea maombi haya ya kuifanya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuwa Wilaya ya kiutawala. Halmashauri inashauriwa kuwasilisha ombi hili na kujadiliwa katika vikao vilivyopo kwa mujibu wa sheria ili kupata ridhaa.
(b) Mheshimiwa Spika, zipo taasisi za kibenki ambazo zimeonyesha nia ya kufungua matawi katika kijiji cha Mvuha kunapotarajiwa kujengwa Makao Makuu ya Wilaya zikewemo NMB na CRDB kwa lengo la kutoa huduma. Majadiliano yanaendela ikiwa ni pamoja na kuharakisha na kugawa viwanja katika eneo hilo.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Wilaya ya Momba ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi:-
Je, kwa nini Serikali imekuwa ikisuasua kutoa fedha ili ziweze kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Momba eneo la Chitete?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2013/2014, ilifanikiwa kupeleka fedha shilingi milioni 250; ambazo zimetumika kuanza ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya na ujenzi wa nyumba mbili za Viongozi waandamizi ambao umefikia hatua ya msingi. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 fedha zilizotengwa kwa kazi hizo hazikupelekwa. Aidha, katika mwaka 2015/2016, Serikali imetenga shilingi milioni 282.7 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa nyumba hizo na shilingi milioni 200 zimetengwa kuanza ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Serikali katika mwaka wa fedha 2014/2015, ilitoa shilingi milioni 450; kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi hizo. Katika jitihada za kuhakikisha Halmashauri inawapatia watumishi wake nyumba bora, Serikali imezielekeza Halmashauri kutumia mapato ya ndani, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi. Aidha, Halmashauri imeingia mkata wa ujenzi wa nyumba 20 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.1 na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga nyumba na Ofisi za Viongozi katika Wilaya mpya kwa kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Kata ya Katumba inakabiliwa na tatizo kubwa la maji linalosababisha akina mama wengi kwenda umbali mrefu kutafuta maji:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufikisha maji katika kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Katumba ilikuwa ni kambi ya wakimbizi chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) hadi mwaka 2014/2015. Huduma za kijamii zikiwemo maji zilikuwa zinatolewa na UNHCR. Ili kutatua tatizo la maji katika kata hii, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa kushirikiana na UNHCR imepanga kutekeleza mradi wa maji wa Nduwi Stesheni ili kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi.
Aidha, Halmashauri katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imepanga kutenga shilingi milioni 345 ambazo zitatumika kwa ajili ya upanuzi wa mradi huo utakaonufaisha vijiji vya Nduwi Stesheni, Mnyaki A, Mnyaki B, Katumba na Sokoine ambavyo viko katika Kata ya Katumba.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Mkoa wa Katavi ni moja kati ya mikoa iliyoanzishwa hivi karibuni ili kusogeza karibu na wananchi huduma muhimu za Serikali lakini mkoa huo hauna Hospitali ya Mkoa na Serikali ilishaamua kujenga hospitali hiyo na Serikali ya Mkoa ilishatenga eneo kwa ajili ya ujenzi.
(a) Je, ni lini utekelezaji wa mradi huo utaanza?
(b) Jiografia ya Mkoa wa Katavi ni pembezoni mwa nchi; je, hiyo inaweza kuwa sababu ya kusuasua kwa mradi huo na kupita takribani miaka minne sasa toka Serikali ifanye uamuzi huo lakini hakuna hata dalili chanya kuelekea kukamilika kwa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimia Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya ujenzi ya Hospitali ya Mkoa wa Katavi yanaendelea ambapo tayari eneo lenye ukubwa wa ekari 243 limepatikana na fidia ya shilingi milioni 468 imeshalipwa kwa wananchi waliopisha maeneo yao kuruhusu ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Mkoa umetenga shilingi bilioni moja ambazo zitatumika kuandaa michoro na kuanza ujenzi. Mkoa unasubiri kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili Mshauri Mwelekezi aweze kuanza kuandaa michoro yaani master plan na kuendelea na hatua nyingine za ujenzi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuwa na Hospitali ya Rufaa kwa kila mkoa. Hivyo, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mipya itakayojengwa Hospitali ya Mkoa ili kusogeza huduma za afya kwa ajili ya wananchi.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora inakabiliwa na kero mbalimbali kama vile ukosefu wa madaktari bingwa wa watoto, akina mama, mifupa, na kadhalika; ukosefu wa vifaa muhimu kama vile ECG machine, CT-Scan, MRI machine, ukosefu wa huduma za ICU pamoja na kwamba lipo jengo zuri lakini halina vifaa vya huduma za dharura:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutatua kero hizi zinazokabili hospitali hii kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua changamoto ya Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Serikali imewapeleka masomoni Madaktari Bingwa wawili akiwemo Daktari wa Upasuaji na Daktari wa Watoto. Aidha, Mkoa katika bajeti ya mwaka 2015/2016 imeomba kibali cha kuajiri Madaktari Bingwa wanne ili kuboresha utoaji wa huduma ya afya. Kwa sasa hospitali hiyo inatumia Madaktari Bingwa watano kutoka China wanaojitolea ambao wamebobea katika maeneo ya tiba, upasuaji, huduma za uzazi, watoto na huduma ya masikio, pua na koo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vifaa, Serikali imepanga kusimika vifaa vya kuangalia mwenendo wa afya ya wagonjwa (patient monitor), vifaa vya uchunguzi wa tiba vikiwemo ECG, CTG, Pulse Oxymeter na Oxygen Concentrator katika hospitali zote za ngazi ya mkoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Mpango huu unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha 2015/2016 na unahisaniwa na Uholanzi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Aidha, Serikali ina mpango wa kuweka huduma ya MRI kwenye Hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa ambapo kwa mwaka 2015/2016, huduma hii itasimikwa katika Hospitali ya Kanda ya Bugando ambayo inahudumia pia wakazi wa Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Mkoa wa Tabora umeingia makubaliano na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), ili kuweza kukopeshwa vifaa muhimu, hususan kwa ajili ya huduma za dharura (ICU).
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Sera Mpya ya Elimu ya mwaka 2014 inatambua upatikanaji wa elimu ya msingi bure; lakini Serikali imeshindwa kupeleka ruzuku ya shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi wa shule za msingi za umma na shilingi 25,000/= kwa kila mwanafunzi wa shule za sekondari za umma:-
Je, Serikali inaweza kuweka mchanganuo wa jinsi gani itakavyoweza kutekeleza Sera ya Elimu ya mwaka 2014 kwa kutoa elimu bure bila kuathiri ubora wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malopo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli fedha za uendeshaji wa elimu (capitation) zikiwemo shilingi 10,000/= kwa wanafunzi wa shule ya msingi na shilingi 25,000/= kwa wanafunzi wa sekondari zilikuwa hazipelekwi kwa ukamilifu. Kwa sasa Serikali imeamua kuanzia Januri, 2016 wanafunzi wote walioandikishwa darasa la kwanza na wale walioandikishwa kidato cha kwanza pamoja na wale wanaoendelea na shule gharama zilizokuwa zinagharimiwa na wazazi au walezi kwa kulipia ada na michango mbalimbali sasa zitalipwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia Serikali imetenga shilingi bilioni 131.4 ikiwa ni fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule, chakula, mitihani na fidia ya ada. Fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja shuleni kutoka Hazina kwa wastani wa shilingi bilioni 18.77 kila mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizo zinahusisha shilingi 10,000/= kwa wanafunzi wa shule ya msingi kwa mwaka, shilingi 25,000/= kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka, shilingi 1,500/= kwa kila mwanafunzi kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya chakula, fidia ya ada ya shilingi 20,000/= kwa wanafunzi wa kutwa na shilingi 70,000/= kwa wanafunzi wa bweni kidato cha kwanza hadi cha nne kwa mwaka. Tayari Serikali imeshapeleka shilingi bilioni 18.77 kwa mwezi Januari, 2016.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Serikali katika awamu zote imekuwa ikiweka kipaumbele katika sekta ya Kilimo na Mifugo kwa umuhimu wake kwa maendeleo ya wananchi katika nchi yetu, lakini Wilaya ya Kilwa kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchi yetu, imekuwa na migogoro inayotishia amani kati ya wakulima na wafugaji katika baadhi ya Vijiji vikiwemo vya Ngea, Kinjumbi, Somanga, Njianne, Namandungutungu na Matandu, kutokana na wafugaji kupitisha, kulisha, kunywesha na kuharibu mazingira katika mashamba ya wakulima na Hifadhi ya Misitu ya Vijiji kama Msitu wa Likonde, Mitarute na Bwawa la Maliwe katika Kijiji cha Ngea, ambacho hakipo katika mpango wa kupokea wafugaji:-
Je, Serikali inatoa wito gani kwa wafugaji wanaoruhusu mifugo yao kuwatia hasara na njaa wakulima na kuharibu mazingira ya baadhi, ili kuepusha uvunjifu wa amani ambao unaweza kutokea wakati wowote kuanzia sasa?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Wilaya ya Kilwa imekuwepo migogoro ya wafugaji na wakulima, hususan katika Vijiji vya Ngea, Kinjumbi, Somanga, Njianne na Namandungutungu. Ufuatiliaji umebaini kuwa sababu kubwa ya migogoro hii ni baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima na baadhi ya wakulima kuingia katika maeneo ya wafugaji. Hivyo, migogoro hiyo inatokea panapokuwepo mwingiliano baina ya makundi haya ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 14 vya Wilaya ya Kilwa ambao uliainisha maeneo kwa ajili ya kilimo, ufugaji, biashara, makazi na uwekezaji. Licha ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kuandaliwa bado kumekuwa na tabia ya kutofuata sheria ya Ardhi Na. 13 na Na. 14 zote za mwaka 1999 na hivyo kusababisha mwingiliano usio wa lazima.
Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji kuwa kubwa, ninawaagiza Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, wote kuhakikisha kwamba suala hili linakuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa na utatuzi wake ufanyike kwa njia shirikishi. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wale wote wanaokiuka Sheria, vikiwemo vitendo vya rushwa, hali ambayo imesababisha migogoro hii kuendelea kuwepo.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la maji katika Jimbo la Busanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kutatua tatizo la maji katika Jimbo la Busanda, Serikali katika Bajeti ya Mwaka 2015/2016, imefanikiwa kupeleka shilingi bilioni 1.144 ambazo zinatumika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji katika Vijiji vya Luhuha, Nyakagomba, Chankolongo, Kabugozo, Chikobe, Chigunga, Inyala na Katoro, ambayo inaendelea kutekelezwa. Miradi hii ikikamilika itachangia kwa kiwango kikubwa kutatua tatizo la maji linalowakabili wananchi wa Jimbo la Busanda.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Busanda na Maeneo mengine nchini kwa kadiri rasilimali fedha zinavyopatikana.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Hospitali ya Kibena inakabiliwa na uchakavu pamoja na upungufu wa madawa:-
Je, Serikali itakarabati hospitali hiyo pamaja na tatizo la upungufu wa dawa?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Wiliam Mgaya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ukarabati wa majengo yote ya Hospitali ya Kibena unakadiriwa kugharimu shilingi milioni 805.5 katika bajeti ya mwaka 2014/2015. Serikali imefanikiwa kupeleka shilingi milioni 22 ambazo zimetumika kukarabati chumba cha kuhifadhia maiti na kazi hiyo imekamilika.
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza ukarabati huo Serikali katika bajeti ya mwaka 2015/2016 imepanga kutumia shilingi milioni 260, kwa ajili ya ujenzi wa uzio na ukarabati wa chumba cha X-Ray. Hospitali ya Kibena ina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa 134,801 lakini idadi halisi ya wagonjwa wanaohudumiwa hospitalini hapo ni 471,613, wakiwemo wagonjwa kutoka Mikoa na Wilaya ya jirani. Serikali katika bajeti ya mwaka 2015/2016, imefanikiwa kupeleka shilingi milioni 77.78, kati ya shilingi milioni 106 zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Mpango wa Serikali uliopo ni kuipandisha Hospitali ya Kibena kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ili dawa zitakazopatikana ziweze kuendana na mahitaji halisi.
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA (K.n.y. MHE. OMARY T. MGUMBA) aliuliza:-
Vijana ndio nguvu kazi kubwa katika Taifa letu na Serikali haina uwezo wa kutoa ajira kwa vijana wote kwa sasa:-
(a) Je, Serikali itawawezesha kifedha vijana wa vijiji vyote 64 vya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki katika makundi ili waweze kujiajiri wenyewe na kupunguza tatizo la ajira na umasikini wa vijana na akina mama?
(b) Je, ni lini Serikali itaanzisha kituo maalum cha kuwawezesha vijana kupata sehemu ya kujifunzia kwa vitendo shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kupata taarifa mbalimbali za maendeleo?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgumba Tebweta Omary, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, vijana katika Halmashauri ya Morogoro Kusini Mashariki, wamekuwa wakiwezeshwa kiuchumi kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo kila Halmashauri hupaswa kutenga 5% ya mapato yake yandani kila mwaka wa fedha kwa ajili ya vijana. Katika bajeti ya mwaka 2014/2015 Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ilifanikiwa kutenga shilingi 10,300,000/= kwa vikundi vya vijana 19 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2015/2016 vikundi vya vijana vimetengewa Shilingi milioni 87,500,000 ili kuviwezesha kiuchumi na kujiajiri.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro imejenga Vituo viwili vya Mafunzo (Agricultural Resource Centres) katika Kata za Ngerengere na Mvuha kwa madhumuni ya kutoa elimu na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwajengea vijana dhana ya uthubutu katika kufanya shughuli za kiuchumi.
Halmashauri imetoa mafunzo ya ufyatuaji wa matofali ya interlock kwa vikundi vya vijana katika Kata nne za Kinohe, Kisemu, Ngerengere na Mvuha, ambapo jumla ya vijana 40 wamewezeshwa kupata elimu hiyo ya ujasiriamali. Mpango huu ni endelevu na Halmashauri inakusudia kutenga fedha katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kufyatulia tofali ili ziwezeshe kuwanufaisha vijana wengi zaidi kiuchumi na kuboresha maisha na makazi ya wananchi wa Wilaya hiyo.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Busokelo hasa katika Kata za Kandete, Isange, Lutebe Lwangwa, Mpata, Kabula, Mpombo, Lufilyo Kambasegela, Ntaba, Lupata, Itete, na Kisegese wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji safi na salama; na kuna maeneo mengi ambayo mabomba uyamepita lakini maji hayatoki kutokana na kukosekana kwa matenki ya maj:-
(a) Je, ni lini Serikali itatatua kero hiyo ya maji kwa kujenga matenki ya maji kwenye Kata hizo?
(b) Mji wa Lwangwa ni Makao Makuu ya Halmashauri mpya ya Busokelo na kuna ongezeko kubwa la watu ukilinganisha na miundombinu ya maji iliyopo; je, Serikali ina mpango gani wa kujenga miundombinu mipya ya uzalilshaji wa maji kwenye eneo hilo jipya la mipango miji?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ilipokea shilingi milioni 907 ambazo zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ya Mpanda katika Kata ya Lupata na miradi wa maji Kasyabone na Kisegese katika Kata ya Kisegese. Miradi hii inahusisha ujenzi wa matanki yenye ujazo wa mita za ukubwa 90 kwa Kata ya Lupata na matanki wawili ya mita za ukubwa 45 kila moja katika Kata ya Kisegese. Katika bajeti ya mwaka 1015/2016 Serikali imefanikiwa kupeleka shilingi milioni 171.94 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Kanyelele Kata ya Kabula, Ilamba katika Kata ya Kambasegela na kijiji cha Mpata katika Kata ya Mpata.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Lwangwa tayari Halmashauri imekamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mradi wa maji kutoka chanzo cha maji Mano Sekondari. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 Serikali imetenga shilingi milioni 280 ili kuanza utekelezaji wa mradi huu.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Wakati wa Kampeni za Urais mwaka 2015 wananchi wa Momba walipewa ahadi ya kutatuliwa kero ya ushuru wa mazao na mifugo kwenye vizuizi na minada:-
(a) Je, mpaka sasa Serikali imefikia hatua gani katika kushughulikia kero hii?
(b) Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mwenendo mbovu wa ukusanyaji wa ushuru huo?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru wa mazao hutozwa kwa mujibu wa sheria ya fedha za Serikali za Mitaa Sura Na. 290 kwenye eneo ambalo zao hilo huzalishwa na kuuzwa. Kwa mujibu wa sheria hii ushuru unatozwa kwa mnunuzi wa mazao kutoka kwa mkulima asilimia tatu hadi asilimia tano ya bei ya gharama (farm gate price). Aidha, kwa upande wa ushuru wa Mifugo, ushuru huu hutozwa mnadani au sokoni baada ya mifugo kununuliwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasisitiza na kuwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utaratibu wa utozaji na ulipaji wa kodi katika ushuru husikia.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo sugu nchini kwa baadhi ya vituo vya afya na zahanati kuwa na watumishi wasio na sifa za utabibu:-
Je, Serikali inatumia vigezo gani kuwapeleka watumishi wasio na sifa katika zahanati na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ambao unatumika kuajiri watumishi wa kada za afya ni kuwapanga moja kwa moja kwenye vituo vya kazi kadiri wanavyohitimu na ufaulu wa masomo yao. Aidha, ili kuhakikisha watumishi wasio na sifa hawaajiriwi, Serikali imekuwa ikafanya zoezi la uhakiki wa vyeti vyao kabla ya kusaini mikataba ya ajira. Hivyo, endapo Mheshimiwa Mbunge anazo taarifa za kuwepo kwa watumishi wa afya wasio na sifa atusaidie kupata taarifa hizo ili tuweze kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto kubwa ya upungufu wa watumishi wa afya, zipo baadhi ya zahanati na vituo vya afya ambavyo vina watumishi wenye sifa tofauti na muundo. Serikali kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) inaendelea kushughulikia changamoto hii ambapo tayari mikoa tisa yenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi imetambuliwa na kupatiwa kipaumbele cha kuwaajiri watumishi wa afya. Vilevile Serikali imepanga kuangalia maeneo yenye mlundikano wa watumishi ili kuweka uwiano wa watumishi baina ya zahanati na vituo vya afya vilivyopo mijini na vijijini.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Katika Jimbo la Ulyankulu, Kata za Milambo, Igombemkulu na Kamindo bado hazijafanya uchaguzi:-
Je, ni lini Kata hizo zitafanya uchaguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia Tangazo la Serikali Na. 295 la Tarehe 23 Julai, 2015 ilitangaza jumla ya Kata 3,946 kwamba ndizo zitakazoshiriki uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzania Bara katika uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba, 2015. Kata za Kamindo, Igombemkulu na Milambo hazikujumuishwa katika orodha hiyo kwa kuwa ni maeneo mapya yaliyowasilishwa na Serikali baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa imekamilisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2015.
Vilevile zoezi la utoaji uraia (naturalization) na utangamanisho (intergration) kwa baadhi ya wakimbizi bado linaendelea katika maeneo hayo. Zoezi hilo litakapokamilika taratibu za kisheria zilizopo zitazingatiwa kabla ya kufanya uchaguzi katika maeneo husika.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Zahanati ya Kitunda inahudumia wananchi wa Kata za Kitunda, Kivule, Kipunguni, Msongola na baadhi ya wananchi toka Chamazi na Tambani katika Mkoa wa Pwani.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuifanya zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya ili kiweze kumudu mahitaji makubwa ya wananchi wa maeneo yaliyotajwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Kitunda iliyopo Kata ya Kitunda haina eneo la kutosha kukidhi ongezeko la miundombinu inayohitajika kuwa kituo cha afya jambo ambalo litalazimu Serikali kuwaondoa wananchi na kulipa fidia. Ili kuboresha huduma za afya katika Kata ya Kitunda, Kivule, Kipunguni na Msongola na maeneo jirani, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Kivule.
Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 zimetengwa shilingi milioni 900 na tayari ujenzi uko katika hatua ya msingi. Vilevile katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni moja ili kuendelea na ujenzi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa hospitali, Serikali imepanga kujenga zahanati mpya na kuimarisha zilizopo. Kutokana na juhudi za kufanikisha jambo hilo muhimu Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 600 katika mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Lubakaya, Mbondole na Luhanga pamoja na nyumba za watumishi zilizopo katika Kata ya Msongola.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 659.13 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na nyumba za watumishi katika Kata mpya ya Mzinga na Kipunguni B katika Kata ya Kipunguni.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Serikali iliahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Mgololo lakini hadi sasa gari hilo halijapelekwa:-
Je, ni lini gari hilo litapelekwa ili liweze kusaidia Vijiji vya Idete, Itika, Holo, Isaula, Rugema, Makungu, Rugolofu na Kitasengwa?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ina gari moja linalotumika kuhudumia wagonjwa. Hata hivyo, gari hilo ni chakavu kiasi cha kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila Halmashauri inapaswa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri imeomba shilingi milioni 543.0 kwa ajili ya kununua magari matatu (ambulance) ambapo kati ya hayo gari moja litapelekwa katika Kituo cha Afya Mgololo na mengine katika Vituo vya Afya vya Sadani na Kasanga ili yasaidie kuwafikisha wagonjwa wenye dharura kwenye vituo vya kutolea huduma kwa haraka.
MHE.DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Kata ya Mamba, Majimoto, Chamalema na Mwamapuli zitapatiwa maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua tatizo la maji katika Kata ya Mamba, Serikali imetenga shilingi milioni 24.2 katika bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu katika Kijiji cha Ntaswa ambacho hakina maji, kati ya vijiji nane vilivyopo. Aidha, kwenye Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji Awamu ya Pili, zimetengwa shilingi milioni 650 ili kupanua mradi mserereko kutoka Kilida hadi Ntaswa na Kisansa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji ambavyo havijapata huduma ya maji katika Kata ya Majimoto ni Luchima na Ikulwe ambavyo vimetengewa shilingi milioni 48.4 katika bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa ajili ya kuchimba visima virefu katika kila kijiji. Vijiji vilivyobaki vinapata maji kupitia mradi uliogharimu shilingi milioni 526,8 na umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, zimetengwa milioni 48.4 kwa ajili ya kuchimba visima viwili katika Vijiji vya Chamalendi na Mkwajuni, vilivyopo Kata ya Chamalendi ili kutatua tatizo la maji kwa wananchi maeneo hayo. Katika Kata ya Mwamapuli Vijiji vyenye matatizo ya maji ni Mwamapuli Ukigwaminzi na Lunguya ambavyo vimetengewa shilingi milioni 77.4 ambapo vitachimbwa visima virefu vitatu vya maji.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA (K.n.y. MHE. ALBERT O. NTABALIBA) aliuliza:-
Mwaka 2011/2012 tuliweka Mkataba kati ya Halmashauri ya Buhigwe na Hospitali ya Heri Mission, Biharu Hospitali na Mulera Dispensary juu ya kutoa huduma ya matibabu kwa wazee, watoto na akinamama bure na Serikali imetoa fedha hizo na wananchi wamenufaika na huduma hizo lakini tangu Disemba, 2015 hadi sasa fedha hazitolewi tena:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali imeacha kutoa fedha ilizokuwa ikitoa?
(b) Je, ni lini sasa fedha hizo zitaanza tena kutolewa ili huduma hizo ziendelee?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Ntabaliba Obama, Mbunge wa Buhigwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe inatakiwa kuchangia 15% ya fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya katika Hospitali Teule ya Heri Mission, Kituo cha Afya Biharu na Zahanati ya Mulera. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, robo ya kwanza na ya pili hadi Disemba, 2015 tayari zimepelekwa shilingi milioni 27.5 katika Hospitali Teule ya Heri Mission, shilingi milioni 8.0 zimepelekwa katika Kituo cha Afya cha Biharu na shilingi milioni 8.0 zimepelekwa Zahanati ya Mulera. Fedha ambazo hazijapelekwa ni za robo tatu (Januari – Machi, 2016) na robo ya nne (Aprili – Juni, 2016) kutokana na kutopokelewa kwa fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya kutoka Hazina.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, fedha ambazo hazijapelekwa katika vituo hivyo vya kutolea huduma za afya ni za robo ya tatu na robo ya nne ambazo zitapelekwa baada ya Halmashauri kupokea fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Busket Fund) kutoka Hazina. Napenda kutoa wito kwa Halmashauri kuimarisha usimamizi kwa kushirikiana na wamiliki binafsi wa hospitali ili makundi yanayotakiwa kutibiwa bure waweze kupata huduma hiyo.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU (K.n.y. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:-
Hospitali ya Geita imefanywa kuwa Hospitali ya Mkoa tangu tarehe 8 Januari, 2016:-
Je, ni lini DMO aliyekuwa akiongoza Hospitali hiyo atahamia katika hospitali iliyopendekezwa na kikao cha RCC kuwa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, licha ya kupandisha hadhi ya Hospitali ya Wilaya ya Geita kuwa Hospitali ya Mkoa lakini bado inaendelea kuwa ya Wilaya hadi tarehe 1 Julai, 2017 itakapokabidhiwa rasmi. Hivyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita (DMO) bado anaendelea kuwa msimamizi wa hospitali hii hadi kipindi hicho itakapohamia rasmi ngazi ya Mkoa na kusimamiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Spika, halmashauri inaendelea na taratibu za kupendekeza kituo cha afya ambacho kitapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya katika kipindi cha mpito wakati taratibu za kujenga Hospitali ya Wilaya zinafanyika. Natoa wito kwa halmashauri kuwasilisha pendekezo hilo mapema katika vikao vya kisheria ili liweze kujadiliwa na hatimaye kuwasilishwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupata ridhaa.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Miongoni mwa changamoto zinazokwamisha kuleta tija katika ukusanyaji wa kodi kwenye Halmashauri zetu ni pamoja na ubutu wa Sheria Ndogo Ndogo (By laws):-
Je, ni lini sheria hizo zitarekebishwa ili zilete tija katika ukusanyaji kodi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria Ndogo katika Halmashauri zinatungwa chini ya Sura Namba 290 ya Sheria za Fedha za Serikali za Mitaa ambayo imewekwa sharti la faini isiyozidi shilingi 50,000/= na kifungo kisichozidi miezi mitatu au miezi sita au vyote kwa pamoja kutegemea na aina ya kosa ambalo mtu amefanya. Hivyo, kukosa umadhubuti kwa sheria ndogo hizi ni kutokana na masharti yaliyomo katika Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa inayotumika kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) imeandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura Namba 290 ambayo yatawasilishwa hapa Bungeni ili Bunge lako liweze kuijadili na kuridhia. Lengo letu siyo kuwaumiza wananchi, bali kuongeza umadhubuti wa Sheria za Serikali za Mitaa na hatimaye kuzipa makali Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kukuza mapato ya Halmashauri.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Suala la madai ya walimu nchini limekuwa ni tatizo sugu hususan kwa walimu wa shule za msingi na sekondari. Je, Serikali imechukua hatua gani ili kumaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kulipa madeni yasiyo ya mishahara na mishahara kwa walimu walioko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kila yanapojitokeza na kuhakikiwa. Aidha, mwezi Oktoba, 2015 Serikali ililipa madeni ya walimu yanayofikia shilingi bilioni 20.125 na mwezi Februari, 2016 imelipa jumla ya shilingi bilioni 1.17 ya madeni ya walimu nchini. Katika fedha za madai ya walimu zilizolipwa Oktoba, 2015 Mkoa wa Arusha ulipelekewa jumla ya shilingi milioni 504.6 ambapo kati ya hizo Halmashauri ya Wilaya ya Meru ilipokea jumla ya shilingi milioni 27.6 ambazo zilitumika kuwalipa walimu 716.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea kukusanya madeni mapya ya walimu ambapo hadi tarehe 19 Aprili, 2016 madeni yasiyo ya mishahara yanafikia kiasi cha shilingi bilioni 17.5 kwa shule za msingi na sekondari wakati madeni ya mishahara yakifikia shilingi bilioni 49.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, madeni haya yatafanyiwa uhakiki na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kisha kuwasilishwa Hazina ili yalipwe.
MHE. EMMANUEL P. JOHN aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaongeza gari la wagonjwa na mafuta ili kufanya huduma za kliniki katika maeneo hayo pamoja na huduma nyingine kuwaokoa kina mama na watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Papian John, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto inayo magari mawili ambayo yamekuwa yakitumika kubeba wagonjwa waliopewa rufaa ya matibabu. Magari haya pia hutumika katika huduma ya mkoba za kliniki za Afya ya Uzazi na Mtoto (RCH) kwa lengo la kuwaokoa akina mama na watoto. Katika Mpango wa Bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri haikuweka kipaumbele cha ununuzi wa gari la wagonjwa kutokana na ukomo wa bajeti. Tunaishauri Halmashauri iendelee kutumia magari mawili yaliyopo huku ikijipanga kuweka kipaumbele cha ununuzi wa gari kwa mwaka wa fedha 2017/2018
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bajeti ya mwaka 2015/2016, Halmashauri hiyo ilitengewa shilingi 43,283,040 kwa ajili ya mafuta ya gari na hadi sasa fedha zote zimeshapelekwa. Changamoto ya kijiografia ndiyo inaonekana kuwa tatizo linalosababisha bajeti iliyotengwa kutokidhi mahitaji.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wilaya ya Itilima ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuwezesha kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Itilima eneo la Itilima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORAalijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa ujenzi wa nyumba za watumishi na viongozi katika Wilaya mpya ya Itilima umeshaanza na uko katika hatua ya ujenzi wa nguzo za jamvi. Fedha zilizopokelewa kwa kazi hiyo ni shilingi milioni 100 kati ya shilingi 500 zilizotengwa mwaka 2014/2015. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa tena shilingi milioni 500 ili kuendelea na ujenzi wa nyumba na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imesaini Mkataba na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba saba za watumishi kwa gharama ya shilingi milioni 450 na fedha hizo zipo. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 47 zimetumika kuwalipia fidia wananchi waliohamishwa kupisha ujenzi huo. Vilevile katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 500 ili kuendelea na ujenzi wa nyumba na ofisi ya Halmashauri.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Mafuriko yanayotokea Mtwara Mjini kila mwaka hasa katika Kata ya Shangani, Cuono, Magomeni na Ufukoni yanasababishwa namiundombinu mibovu ambayo imejengwa chini ya kiwango katika maeneo mengi ya Mji wa Mtwara:-
(a) Je, Serikali iko tayari sasa kujenga upya mitaro, madaraja pamoja na miundombinu mingine ili maji yaweze kusafiri kuelekea baharini wakati wa masika?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya Mikindani - Lwelu ufukweni mwa bahari kwa kiwango cha lami ikizingatiwa kuwa barabara hiyo iko ndani ya Manispaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 imetenga Dola za Kimarekani 540,000 kupitia mradi wa Tanzania Strategic Cities Project (TSCP) kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu na ujenzi wa mradi wa barabara ambao utahusisha ujenzi wa mitaro na madaraja ambao utahusisha uboreshaji wa miundombinu iliyoharibika na mvua. Utekelezaji wake upo katika kukamilisha hadidu rejea ili utaratibu wa manunuzi ya kupata Mkandarasi Mshauri ziweze kufikika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza matengenezo ya barabara ya Mikindani- Mchuchu- Lwelu kwa kiwango cha lami, ambapo katika mwaka wa fedha 2013/14 kilometa moja ilitengenezwa kwa kiwango cha lami. Aidha, ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote, Serikali katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga shilingi 89,000,000 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo. Azma ya Serikali ni kuijenga barabara hiyo yote ya kilometa 11 zilizobaki kwa kiwango cha lami kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa wana majukumu mengi ikiwemo kuhakikisha amani na usalama katika maeneo yao:-
Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa posho ya mwezi ya Wenyeviti hawa ili kutoa motisha kwa kazi yao?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa katika kusimamia shughuli za Maendeleo Nchini. Katika kuzingatia uzito huo wa majukumu, Serikali imeweka utaratibu wa kila Halmashauri kurejesha katika Vijiji na Mitaa asilimia 20 ya mapato ya ndani ambapo sehemu ya fedha hizo zinatakiwa kulipa posho ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kuwa baadhi ya Halmashauri hazipeleki fedha hizo katika Vijiji na Mitaa na hivyo kuwanyima haki Viongozi hao kulipwa posho zao. Changamoto kubwa ya Halmashauri ilikuwa ni makusanyo yasiyoridhisha ya mapato ya ndani ambayo yalisababisha kushindwa kulipa posho hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia sasa Serikali inaimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ambapo imethibitika kuongeza makusanyo kwa zaidi ya asilimia mia moja. Kwa njia hiyo, Halmashauri zitakuwa na uwezo wa kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa ambao sote tunatambua mchango wao mkubwa katika Taifa hili wa kuhamasisha shuguli za maendeleo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI, itaendelea kusimamia suala la makusanyo ya mapato ya ndani kwa nguvu zake zote ili kujenga uwezo wa Halmashauri kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Serikali imeamua kutoa elimu ya kompyuta kwenye shule za sekondari nchini lakini vifaa vya kufundishia havitoshelezi na hata Walimu ni wachache katika maeneo mengi ikiwemo Mkoa wa Rukwa, ambapo ni shule mbili pekee za Mazwi na Kizwite Sekondari ambazo zimeshaanzishwa:-
Je, Serikali ina mpango mkakati upi wa kufanikisha ufundishaji wa somo hilo kwa tija?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa elimu ya kompyuta mashuleni umeanza kufanyika kwa baadhi ya shule zenye mazingira yanayowezesha somo hilo kufundishwa. Changamoto zilizopo ni uhaba wa Walimu, ukosefu wa umeme hususani maeneo ya vijijini na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Serikali inakabaliana na changamoto hizo kwa kupeleka umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), pamoja na kuhakikisha somo la Kompyuta linafundishwa katika Vyuo vya Ualimu ili kuwaandaa walimu watakaofundisha somo hilo mashuleni. Kuhusu upatikanaji wa vifaa mashuleni Serikali inashirikiana na Kampuni ya Microsoft ambayo imeonesha nia ya kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa muda mrefu wa Serikali ni kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji mashuleni hususani masomo ya sayansi. Kwa msaada wa Kampuni ya Microsoft imeanza utekelezaji wa mpango huu kwa shule 50 katika Mikoa 25. Kwa Mkoa wa Rukwa shule zilizochaguliwa ni shule ya Sekondari ya Kizwite na Mazwi. Shule hizi mbili kila Mkoa ni vituo vya mafunzo kwa Walimu ili kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa kutumia TEHAMA. Kituo cha Mazwi kinaanza kufanya kazi kuanzia Julai, 2016 ambapo kitapewa vifaa vyote muhimu vitavyohitajika katika mafunzo hayo.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Afya ni uhai na ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata afya bora katika Wilaya ya Hanang:-
(a) Je, ni lini Serikali itaziba upungufu wa watumishi wa afya katika Wilaya ya Hanang ambao wamefikia watumishi 202 hadi sasa?
(b) Je, ni lini Serikali itafungua duka la MSD na kuboresha vifaa tiba kwenye vituo vya afya katika Wilaya ya Hanang?
(c) Je, ni lini Serikali itajenga wodi zaidi za akina mama na watoto katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini iliyopo Hanang ili kupunguza msongamano katika Wodi hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang ina upungufu wa watumishi wa afya 456. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Halmashauri imeidhinishwa kibali cha kuajiri watumishi 64 ambao wataajiriwa muda wowote katika Halmashauri hiyo. Vilevile katika mwaka wa fedha 2016/2017 wameomba watumishi wengine 59 wa kada mbalimbali za afya.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka kipaumbele kwa kufungua maduka ya dawa kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa kutokana na upungufu na ufinyu wa bajeti. Maduka hayo ya Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) yatafunguliwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Mkoa wa Manyara na Halmashauri zake inaendelea kuhudumiwa na Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) iliyoko Mkoa wa Kilimanjaro.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, wodi moja ya wazazi iliyoko katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang haikidhi mahitaji kutokana na idadi kubwa ya wazazi wanaofika Hospitalini hapo kujifungua. Kwa mwezi wodi hiyo inapokea takribani wazazi 200 wengine kutoka Wilaya jirani. Serikali kwa kushirikiana na Shirika la EngeredHealth inaendelea na ujenzi wa wodi mpya moja ambao utakamilika kwa mwaka huu wa 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kulaza akina mama wajawazito 16 kwa wakati mmoja. Vilevile katika mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri imetenga shilingi milioni 70 kupitia ruzuku ya maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi ambapo fedha hizo bado hazijapokelewa.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka x-ray na CT-Scan kwenye Hospitali ya Sekou Toure Mkoani Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure ina mashine mbili za x-ray ambazo zilinunuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwaka 2002. X-Ray hizo zinafanya kazi pamoja na kuwepo kwa matengenezo ya mara kwa mara kutokana na uchakavu wake. Aidha, hospitali hiyo haina mashine ya CT-Scan na kwamba huduma hiyo inapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza mradi wa kusimika vifaa vya kuangalia mwenendo wa afya za wagonjwa na vifaa vya uchunguzi vikiwemo CT-Scan katika Hospitali za Rufaa za Mikoa utakaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi. Mpango huu utakapokamilika utasaidia Hospitali nyingi za Mikoa za Rufaa kuwa na vifaa muhimu kwa ajili ya huduma ya afya.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Wilaya ya Ukerewe inajumuisha visiwa 38 na kati ya hivyo, visiwa 15 hutumika kwa makazi ya kudumu lakini huduma za kijamiii hasa afya siyo nzuri:-
(a) Je, Serikali inachukua hatua zipi za makusudi za kunusuru maisha ya watu hasa akinamama wajawazito na watoto wanaokufa kutokana na ukosefu wa huduma bora za afya katika visiwa hivyo?
(b) Je, ni lini Maabara katika kituo cha afya Bwisya katika Kisiwa cha Ukara itakamilika na kupewa wataalam ili kutoa huduma ya upasuaji kunusuru maisha ya wananchi wa kisiwa hicho na visiwa vya jirani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya utoaji wa huduma za afya Ukerewe zinatokana na jiografia ya eneo lenyewe kuwa linazungukwa na maji. Kwa kutambua hali hiyo, Serikali imejenga Hospitali ya Wilaya katika kisiwa cha Nansio, vituo vya afya viwili na zahanati 17. Hata hivyo, Serikali inatambua bado zipo changamoto ambazo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi kupitia bajeti za Halmashauri kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa wananchi wa kisiwa hiki hupelekewa huduma za afya kwa njia ya mkoba pamoja na kliniki ambazo huratibiwa na Madaktari pamoja na Wauguzi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto, Serikali imejenga jengo la upasuaji katika kituo cha afya cha Bwisya. Tayari kituo hicho kimepatiwa Daktari Msaidizi na Mtaalam wa dawa za usingizi ili kuanza huduma za upasuaji. Changamoto inayoendelea kushughulikiwa ni upatikanaji wa vifaa na nishati ya umeme na maji ambapo mpaka sasa shughuli za kuweka umeme katika kituo hiki zinaendelea.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Ileje iliwahi kuwa katika Wilaya zilizoongoza kwa ufaulu wa wanafunzi, lakini miaka ya hivi karibuni ufaulu umeshuka na hii ni kutokana na miundombinu mibovu ya mazingira ya kufundishia:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa inaboresha miundombinu yote muhimu kwa utoaji wa elimu?
(b) Je, Serikali iko tayari kujaza pengo la Walimu liliko hivi sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha miundombinu ya shule, Halmashauri ya Wilaya ya Ileje katika mwaka wa fedha 2015/2016, ilitengewa shilingi milioni 798.0 ambazo zilipokelewa kwa ajili ya ukarabati, ujenzi na umaliziaji wa miundombinu ya shule nne za Msomba, Luswisi, Itale na Bupigu. Vile vile, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imetengewa shilingi milioni 130.8 ili kuendelea na uboreshaji wa mindombinu ya shule ya sekondari ya Ngulilo. Aidha, kupitia mapato yake ya ndani Halmashauri imetenga shilingi milioni 60.0 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za Walimu, ukarabati wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa matundu ya vyoo na matengenezo ya madawati. Jitihada hizi zinakusudia kuinua kiwango cha elimu inayotolewa kwa wanafunzi katika Wilaya ya Ileje.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya Walimu wa shule za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ni 819, waliopo sasa ni Walimu 567 na upungufu ni 252. Kwa upande wa shule za sekondari mahitaji ya Walimu wa sayansi na hisabati ni 156, waliopo ni 61 na upungufu ni 95. Hata hivyo, Wilaya ina zaidi ya Walimu wa masomo ya sanaa 105. Ili kuziba pengo la Walimu katika Halmashauri hiyo, Serikali imepanga kuajiri Walimu 35,411 waliohitimu kuanzia mwaka 2013/2014 na miaka ya nyuma ambapo sehemu ya Walimu hao watapangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Sumbawanga ina Wilaya mbili ambazo ni Sumbawanga Mjini na Sumbawanga Vijijini:-
Je, kwa nini ina Mkuu wa Wilaya mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa Halmashauri mbili unatokana na Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sura 287 (Mamlaka za Wilaya) na Sura 288 (Mamlaka ya Miji) ambapo lengo ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Sheria hizi zinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kuanzisha Halmashauri katika Wilaya moja zenye hadhi ya Wilaya, Mji, Manispaa na Jiji. Aidha, Wilaya ni sehemu ya Serikali Kuu ambayo uanzishwaji wake unazingatia Sheria ya Uanzishwaji wa Maeneo Mapya kwa maana ya Mikoa na Wilaya, Sura 297 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili Wilaya mpya iweze kuanzishwa vipo vigezo na taratibu mbalimbali ambazo vinapaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na mapendekezo hayo kujadiliwa katika Mikutano ya Vijiji, Baraza la Madiwani, Kamati za Ushauri za Wilaya na Mikoa. Hivyo, endapo halmashauri hizo mbili zikikidhi vigezo na kuwa na Wilaya kiutawala na hivyo kuwa na Mkuu wa Wilaya, nashauri mapendekezo hayo yapitishwe katika vikao vya kisheria ili yaweze kujadiliwa na hatimaye yawasilishwe kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa hatua zaidi kwa mujibu wa sheria.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Serikali imeweka utaratibu wa kuzitaka Halmashauri zote za Wilaya kutenga asilimia tano ya mapato ili kuwawezesha wanawake na vijana kupata mikopo:-
Je, ni akinamama wangapi au vikundi vya wanawake vingapi vimenufaika na mikopo hiyo katika Halmashauri za Wilaya ya Mufindi, Kilolo, Iringa Mjini na Iringa Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake, Halmashauri za Mkoa wa Iringa zimewezesha vikundi vya wanawake 430 na vikundi vya vijana 47 kupata mikopo.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi iliwezesha vikundi vya wanawake 331, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo vikundi vitatu, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vikundi 73 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa vikundi 23.
Kwa upande wa vikundi vya vijana; Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi vikundi 13, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo vikundi sita, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vikundi 28 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa hakukuwa na kikundi hata kimoja.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kupitia mfumo wa electronic ili kuongeza mapato yanayokusudiwa kufanya mifuko hiyo kutengewa fedha zaidi. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 sharti la kupitisha makisio ya bajeti ya kila Halmashauri ilikuwa ni kuonesha kiwango kilichotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Napenda kulihakikishia Bunge lako kuwa tutaendelea kusimamia kwa karibu suala hili na kuchukua hatua yoyote itakayobainika kuhujumu mpango huu wa kuwawezesha wananchi.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Moja ya matukio makubwa ya kihistoria katika nchi yetu ni vita ya Majimaji iliyopiganwa kati ya mwaka 1905 – 1907 kati ya Watanganyika na Wajerumani. Pamoja na kufahamu kwamba vita hivyo vilienea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, lakini vilianza katika Kijiji cha Nandete, Wilaya ya Kilwa; Serikali inaonesha jitihada mbalimbali ya kuienzi historia hiyo, ikiwa ni pamoja na kujenga mnara katika Kijiji hicho:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara ya kutoka Njianne hadi Nandete kwa kiwango cha lami ili kulifanya eneo hilo la kihistoria kufikiwa kwa urahisi na kuliongezea umaarufu kwa kutembelewa na watalii hususani wa kutoka Ujerumani jambo ambalo litaiongezea mapato Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na Taifa kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kujenga barabara ya lami kwenda eneo hili la kihistoria ni la msingi, lakini kwa sasa wakati Serikali inajenga barabara kuu zote nchini kwa kiwango cha lami hasa zikiunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya fedha kwa ajili ya matengenezo ili kuifanya ipitike wakati wote.
Kupitia Wakala wa barabara Mkoa wa Lindi, katika mwaka wa fedha 2015/2016, zilitengwa shilingi milioni 58.8 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilomita 43 na matengenezo ya muda maalum kwa kiwango cha changarawe urefu wa kilomita sita, kwa jumla ya gharama ya shilingi milioni 192.3. Matengenezo ya barabara hii yameanza chini ya Mkandarasi Ungando Contractors Company wa Kibiti – Rufiji. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, barabara hii iko katika mpango wa kufanyiwa matengenezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilomita 10 zinazohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, katika mwaka 2015/2016, zimetengwa shilingi milioni 70 ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum kwa urefu wa kilomita nane. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, zimetengwa shilingi milioni 967.6 ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika Wilaya ya Kilwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya wazazi (maternal ward) kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwa kuwa wazazi hujifungulia kwenye chumba kilichomo ndani ya jengo ambalo pia hutumika kulaza wagonjwa wa kiume na kike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMESEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Afya Chiwale hakina wodi ya wazazi na hali hiyo niliishuhudia mwenyewe nilipofanya ziara kituoni hapo mnamo tarehe 9 Januari, 2016 ili kujionea hali ya utoaji wa huduma kituoni hapo. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Halmashauri imetenga shilingi milioni 80 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya, Chiwale. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 20 zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi milioni 60 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu ambazo bado hazijapelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuharakisha utekelezaji wa mpango huo, Halmashauri imeshauriwa kutumia fursa ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) ili kupata mkopo utakaowezesha kujenga jengo kila maabara na wodi ya kisasa ya wazazi kutokana na ukosefu wa miundombinu hiyo muhimu katika kituo hicho.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:-
Kwa mila zetu za Kiafrika imezoeleka kuwa huduma ya ukunga kwa akinamama wajawazito wakati wa kujifungua hutolewa na wataalam wanawake:-
Je, Serikali haioni kuwa kwa kuweka Wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati za Serikali nchini ni kuwadhalilisha akinamama wajawazito wanaojifungua katika zahanati hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakunga wote nchini wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mkunga ana wajibu wa kutoa huduma ya kumsimamia mama mjamzito wakati wa uchungu, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Wakunga wote wa kike na wa kiume wanaruhusiwa kutoa huduma ya ukunga baada ya kufuzu mafunzo yao na kupata leseni ya kutoa huduma hizo kutoka katika Baraza la Uuguzi na Ukunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, japo Sheria ya Uuguzi na Ukunga inampa mtaalam aliyefuzu masomo hayo kutoa huduma lakini kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya wanajamii kutokana na mila na desturi zinazotawala jamii husika. Kutokana na hali hiyo, Serikali itaendelea kuajiri wataalam wengi ili pale penye changamoto iweze kupatiwa ufumbuzi bila kuwakwaza wanajamii husika.
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Sera ya Serikali ni kuzitaka Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Akina Mama kwa mujibu wa sheria ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu; lakini Halmashauri nyingi ikiwemo Morogoro Vijijini haitoi mikopo hiyo kwa makundi hayo kama ilivyokusudiwa:-
Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuzibana na kuziamuru Halmashauri zote ikiwemo ya Morogoro Vijijini kutenga asilimia tano ya fedha za mapato ya ndani kwa vijana na asilimia tano kwa ajili ya akina mama ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu na kutimiza lengo lililokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro imewezesha vikundi 39 vya wanawake na vijana vyenye wanachama 295 ambavyo vimepata mikopo ya shilingi milioni 23.8 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, zimetengwa shilingi milioni 175, kwa ajili ya wanawake na vijana kutokana na mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili kujenga uwezo wa kutenga fedha zaidi.
Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, sharti la kupitisha makisio ya bajeti ya kila Halmashauri lilikuwa ni kuonesha asilimia kumi zilizotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake. Kutokana na mapato ya ndani Halmashauri zote zimeagizwa kuhakikisha fedha hizo zilizopelekwa kwenye vikundi husika ikijumuisha walemavu na kusimamia marejesho yake ili vikundi vingine viweze kunufaika.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Kirando katika Wilaya ya Nkasi kinatoa huduma kwa vijiji zaidi ya ishirini katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na katika kituo hicho wodi za watoto na akina mama zimekuwa ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya watoto na akina mama wanaohudumiwa katika kituo hicho.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi hizo ili kuondoa kero kwa akina mama na watoto wanaohudumiwa katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha wodi ya akina mama na watoto katika kituo cha afya cha Kirando, tathmini ya awali imefanyika na kubaini kuwa zinahitajika shilingi milioni 250 ili kukamilisha ujenzi huo. Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo Serikali itaweka katika mpango na bajeti wa Halmashauri ili kuanza ujenzi wa wodi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umbali wa kituo hicho kutoka Makao Makuu, Serikali imepeleka gari la wagonjwa ili kuboresha huduma za Rufaa kwa akina mama na watoto. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri imeweka kipaumbele katika ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Kabwe ili kiweze kuhudumia wananchi wa Korongwe na Kabwe ambao wanahudumiwa na kituo cha afya cha Kirando.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Tunduru inayohudumia majimbo mawili ina tatizo la gari kubebea wagonjwa ambapo gari lililopo ni moja na linaharibika mara kwa mara.
Je, ni lini Serikali itapeleka gari jipya katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imetenga shilingi milioni 141 kutokana na mapato ya ndani ili kununua gari la wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Tunduru. Vilevile katika mwaka huo zimeombewa shilingi milioni 300 kupitia maombi maalum ili kununua magari mawili kwa ajili ya vituo vya afya, ili kuboresha mfumo wa rufaa kwa wagonjwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha magari hayo yanapatikana kwa ajili ya huduma za afya.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu ilijengwa na mradi wa GGM kusaidia kundi kubwa la wasichana wasome Wilayani Geita, shule hii ina hosteli za kutosha na nyumba za walimu.
Je, ni kwa nini shule hiyo imebaki kuwa shule ya kutwa wakati mazingira yake yanafaa kuwa sekondari ya bweni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kanyasu Constantine John, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Wasichana Nyankumbu ilijengwa chini ya mradi wa Geita Gold Mining na kupata usajili Na. S. 1942 mwaka 2006 ikiwa ni shule ya kutwa kwa kidato cha kwanza hadi cha nne. Aidha, mwaka 2012 iliongezewa kidato cha tano na sita. Hivyo shule hiyo imesajiliwa kuwa ya kutwa kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na bweni kwa kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu zinazotumika ili kuisajili shule kuwa ya bweni, ni Halmashauri yenyewe kupeleka maombi Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ili kupata kibali.
Aidha, kabla ya kupata usajili huo, Kamishna wa Elimu atatuma timu ya wataalam katika shule husika kwa ajili ya kuhakiki uwepo wa miundombinu inayohitajika ili shule iweze kusajiliwa kuwa ya bweni.
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH) aliuliza:-
Baadhi ya miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri imekuwa ikisuasua kutokana na uchache wa fedha pamoja na kuingia mikataba na wakandarasi wasiokuwa na uwezo wa kutosha na kusababisha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati:-
Je, Serikali imejipanga vipi kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wa vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Programu ya Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Serikali ilipanga kutekeleza miradi ya maji 1,870 katika Halmashauri mbalimbali nchini. Miradi iliyotekelezwa na kukamilika ni 1,110 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri zilitengewa shilingi bilioni 129.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji. Hadi sasa fedha zilizopelekwa kwenye Halmashauri ni shilingi bilioni 97.6 sawa na asilimia 75.5 ya fedha zilizotengwa.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya upelekaji wa fedha za miradi ya maji katika Halmashauri, imechangiwa kwanza na kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato kwa mwaka na pili baadhi ya wahisani kuchelewa kutoa fedha walizoahidi. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 290 ambazo zitatumika kulipa madeni ya wakandarasi na kukamilisha miradi viporo.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha makusanyo ya fedha ili fedha zilizotengwa ziende katika utekelezaji wa miradi iliyopangwa.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Mbogwe mwaka 2012 watumishi iliyokuwa Wilaya ya Bukombe walihamishiwa Wilayani Mbogwe lakini hawajalipwa stahiki zao za posho ya kujikimu pamoja na zile za usumbufu.
Je, ni lini watumishi hao watalipwa stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, idadi ya watumishi waliohamishwa kutoka Wilaya ya Bukombe kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ni 73 ambao wanadai posho ya kujikimu na usumbufu ya shilingi milioni 164.14. Kati ya madai hayo fedha ambazo zimeshalipwa kwa watumishi ni shilingi milioni 15.15 kwa watumishi 18. Hivyo, kiasi ambacho watumishi bado wanadia shilingi 148. 99.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri imeomba fedha hizo katika Wizara ya Fedha na Mipango ili kulipa deni hilo kwa watumisi 55 waliobaki. Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea kufuatilia Hazina fedha hizo ili ziweze kupatikana na kulipwa kwa watumishi wanaodai.
MHE. BONNAH M. KALUWA aliuliza:-
Katika Jimbo la Segerea kuna zahanati kumi lakini hakuna zahanati moja iliyopandishwa hadhi kuwa kituo kikubwa cha afya chenye uwezo wa kulaza wagonjwa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipandisha hadhi Zahanati ya Tabata „A‟ kuwa Kituo cha Afya kwa sababu ina miundombinu yote inayofaa kwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali naomba nifanye correction ya data, kulikuwa kuna typing error hiyo mwaka 2015/2016 isomeke 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Kaluwa, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, zahanati ya Tabata „A‟ haina eneo la kutosha kukidhi upanuzi wa miundombinu unaohitajika na hivyo inakosa sifa ya kupandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya. Ili zahanati iweze kupandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya inatakiwa kuwa na wodi ya wanaume na wanawake zenye vitanda 24 kila moja, jengo la upasuaji, jengo la wagonjwa wa nje (OPD), huduma za mama na mtoto, chumba cha kuhifadhia maiti na kichomea taka incinerator.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zahanati ya Segerea ina eneo la kutosha, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imetenga shilingi milioni 75. katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ili kujenga wodi zinazotakiwa ikiwa ni maandalizi ya kuipandisha hadhi Kituo cha Afya. Taratibu za kupandisha hadhi zahanati kuwa Kituo cha Afya zinaanza katika Halmashauri yenyewe kupitia vikao vyake, hatimaye maombi hayo yatawasilishwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kuipatia kibali.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Kituo cha Afya Chunya kilipandishwa hadhi kuwa hospitali ya Wilaya mwaka 2008 lakini kuna tatizo la ukosefu wa chumba cha kuhifadhia maiti:-
Je, ni lini Serikali italitatua tatizo hilo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Chunya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeanza mchakato wa ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Wilaya ya Chunya ambacho kinatarajiwa kugharimu shilingi milioni 230 hadi kukamilika. Ujenzi wa jengo utagharimu shilingi milioni 60 na majokofu yatagharimu shilingi milioni 160. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti yaani mortuary.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa sasa kipo chumba maalumu ambacho kimetengwa kikiwa na uwezo wa kuhifadhia maiti mbili tu. Chumba hicho hakitoshelezi huduma hiyo hali ambayo inawalazimu wananchi kufuata huduma ya aina hiyo katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ina tatizo kubwa la msongamano katika wodi ya akina mama ambao wamekuwa wakilala zaidi ya wawili kwenye kitanda kimoja;
(a) Je, ni lini Serikali itaongeza wodi ya wazazi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro?
(b) Je, kwa nini Serikali isiboreshe baadhi ya zahanati kama Mafiga Sabasaba ili kuwa na uwezo wa kupokea kina mama wajawazito kujifungua na kupunguza msongamano katika hospitali ya rufaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Azizi Abood Mbunge wa Morogoro Mjini lenye sehemu a na b kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, msongamano wa wagonjwa katika wodi ya wazazi ya hospitali ya Mkoa unatokana na kukosekana kwa hospitali ya Wilaya ya Morogoro. Ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali imepanga kuanza ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Morogoro katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 2.5 ili kuanza ujenzi wa jengo la utawala na jengo la wagonjwa wa nje (OPD).
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuimarisha kituo cha afya cha Mafiga ambacho tayari kimeanza kutoa huduma za mama wajawazito. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga jengo la upasuaji na wodi. Vilevile, zimetengwa shilingi milioni 71 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya upanuzi wa wodi ya wazazi katika zahanati ya kihonda. Hivyo, mpango wa Serikali ni kuimarisha huduma za wazazi katika zahanati na vituo vya afya ili kupunguza msongamano katika hospitali ya rufaa ya Morogoro.
MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Halmashauri ya Mji wa Nzega haina shule hata moja ya kidato cha tano na sita na hivyo kuwafanya wanafunzi wengi kulazimika kwenda kusoma nje ya Mji wa Nzega; lakini Mbunge kwa jitihada zake amejenga vyumba viwili pamoja na bweni katika shule ya sekondari Bulende kwa ajili ya kidato cha tano na sita.
(a) Je, Serikali ipo tayari kuanzisha masomo kwa kidato cha tano kuanzia mwaka huu wa 2016;
(b) Je, ni lini Serikali itajenga vyumba vya madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Chief Itinginya ili angalau kuwe na shule mbili za kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Sekondari ya Bulende, na sasa anaendelea na ujenzi na hosteli, Mheshimiwa hongera sana kwa kazi hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha shule ya Sekondari ya Bulende inapata sifa ya kuwa ya kidato cha tano, Serikali imetenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Ili shule iweze kusajiliwa kuwa ya kidato cha tano na sita inapaswa kuwa na miundombinu ya kutosha kama vyumba vya madarasa, mabweni, samani, bwalo la chakula, vyoo pamoja na uwepo wa walimu wa masomo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri inapaswa kuwasilisha maombi ya usajili wa shule katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi ambao watatuma wataalam kukagua miundombinu ya shule kabla ya kutoa kibali. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha miundombinu ya kutosha inajengwa kwa kushirikisha nguvu za wananchi katika shule ya Sekondari ya Chief Itinginya ili kukidhi na kusajili kuwa ya kidato cha tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri imepanga kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya Chief Itinginya.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-
Jimbo la Mchinga na Mtama linaunda Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na ukubwa wa Halmashauri hii ni kikwazo cha kuwafikia wananchi kwa urahisi katika kuwapelekea huduma za jamii.
Je, kwa nini Serikali isiigawe Halmashauri hii ili kuwa na Halmashauri mbili yaani Mchinga na Mtama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishwaji wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa unazingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 145 na Ibara 146 na Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Wilaya, Sura Namba 287 kifungu cha 5 ambazo kwa pamoja zinampa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuwa na Madaraka ya kuanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kusudio la kugawanya Halmashauri ni lazima likidhi vigezo vinavyowekwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na kujadiliwa kwenye vikao vya kisheria, ikiwemo Mkutano Mkuu wa Vijiji, Kamati za Maendeleo za Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na baadae huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatambua kuwa suala la kugawa Wilaya ya Lindi liko katika majadiliano kupitia vikao vya Halmashauri; hatua hizo zitakapokamilika Serikali itatuma wataalam kwa ajili ya kuhakiki vigezo vinavozingatiwa kabla ya kugawa Halmashauri husika.
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:-
Jimbo la Pangani linakabiliwa na tatizo sugu la maji hususan katika Kata za Mkalamo, Masaika, Mikunguni, Mkaja, Mwera na Bushiri.
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili ambalo limesababisha kuzorotesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Nchini tangu mwaka 2006/2007. Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani imekamilisha miradi ya ujenzi wa miradi mitano katika vijiji sita vya Madanga, Jaira, Bweni, Kwakibuyu, Mzambarauni na Kigurusimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 kiasi cha fedha shilingi milioni 531.1 zimetengwa kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani ambapo kiasi cha shilingi milioni 55 zimeshapelekwa. Aidha, Serikali ilitekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Mkalamo, Kata ya Mkalamo, Stahabu, Mtango, Mikinguni, Mikocheni na Sange Kata ya Mkwaja, Mwera katika Kata ya Mwera, Kipumbwi Kata ya Kipumbwi na Msaraza Kata ya Bushiri na Masaika Kata ya Masaika kupitia Awamu ya Pili ya
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inayotarajiwa kuanza Julai 2016. Aidha, fedha zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ni shilingi milioni 668.2.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Jimbo la Lindi Mjini lina eneo la Bahari ya Hindi lenye urefu wa kilometa 112, lakini eneo hilo halina mchango wowote wa maana kwenye pato la Taifa na Manispaa ya Lindi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza eneo la bahari katika Manispaa ya Lindi?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendeleza eneo la ukanda wa bahari ya Hindi katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Serikali imeendelea na maandalizi ya mpango wa upimaji wa muda mrefu yaani master plan wa wilaya nzima ambao utaainisha matumizi mbalimbali ya ardhi, yakiwemo uwekezaji, makazi na matumizi mengine. Tayari kibali cha kuandaa mpango huo kimeshatolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Halmashauri. Kwa sasa mkataba wa kazi hiyo, uko kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya uhakiki yaani vetting ili taratibu za kupata mzabuni ziendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huo utahusisha uboreshaji wa makazi holela yaani resettlement scheme katika eneo la Mnazi Mingoyo, Mpilipili na Rahaleo ili kuwa na mji wa kisasa katika Manispaa ya Lindi. Kazi zote hizo zinatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni moja hadi kukamilika kwake. Mpango huo utakapokamilika utasaidia Serikali kupata mapato kutokana na aina ya uwekezaji utakaofanyika katika ukanda huo wa bahari ndani ya Manispaa ya Lindi.
MHE. DKT. RAPHAEL M.CHEGENI (K.n.y. MHE. STANSLAUS H. NYONGO) aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Maswa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia wananchi wa Mkoa wa Simiyu:-
Je, ni lini hospitali hiyo itapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ya Wilaya ya Maswa inatoa huduma za afya kwa wagonjwa wa Wilaya ya Maswa na miundombinu yake haitoshelezi kuwa hospitali ya mkoa. Mkoa wa Simiyu umeandaa makubaliano (memorundum of understanding) ya kuifanya Hospitali ya Wilaya ya Bariadi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu kwa muda ambapo inatarajiwa kuanza kutoa huduma zenye hadhi hiyo kuanzia tarehe 1/7/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, mkoa umeshaanza kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa kufuata vigezo vinavyostahili ambapo hadi sasa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD) limeanza kujengwa. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni 1.4 ili kuendelea na ujenzi huo.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyere imetimiza vigezo vyote vya kuwa Halmashauri ya Mji.
Je, ni lini Serikali itaipa hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji Mamlaka hiyo ya Mji mdogo wa Namanyere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya kupandishwa hadhi Mamlaka ya Mji mdogo Namanyere kuwa Halmashauri ya Mji yameshapelekwa katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI baada ya kukamilika kwa vikao vya kisheria. Baada ya hatua hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itakwenda kuhakiki vigezo vinavyozingatiwa katika uanzishwaji wa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati tunakamilisha taratibu za kisheria zinazotakiwa na kufanya uhakiki kabla ya maamuzi ya kuanzisha Halmashauri ya Mji kufikiwa.
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-
Moja kati ya vikwazo vya utekelezaji wa Ilani ya CCM ni kutotolewa kwa fedha kwa ukamilifu na kwa wakati:-
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kilikasimiwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa mwaka wa fedha 2015/2016?
(b) Je, Serikali imetoa kiasi gani cha fedha za Miradi ya Maendeleo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Msalala hadi kufikia Desemba, 2015?
(c) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha fedha za maendeleo zinapatikana kwa wakati na kupelekwa kwenye miradi husika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Masalala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, kiasi cha shilingi bilioni 4.1 kilitengwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Desemba, 2015 Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Aidha, wahisani wametoa jumla ya shilingi bilioni 1.6 nje ya fedha zilizoidhinishwa katika bajeti ya Halmashauri hiyo kwa ajili ya miradi ya TASAF, SEDP na AGPHAI na kufanya fedha zote zilizopokelewa hadi Desemba, 2015 kufikia bilioni 3.1.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za miradi ya maendeleo zinapelekwa katika Halmashauri zote kulingana na makusanyo yanayofanyika. Mkakati uliowekwa na Serikali ni kuimarisha makusanyo ya mapato ya Serikali na kudhibiti upotevu wa mapato katika vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha fedha zinapelekwa kama zilivyopangwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Wajasiriamali katika Mkoa wa Dar es Salaam hususan Machinga na Mama Lishe wamekuwa wakisumbuliwa sana na Mgambo wa Jiji hali inayowafanya kushindwa kujitafutia riziki ya kila siku:-
Je, Serikali inawasaidiaje Wajasiriamali hao wadogo wodogo ambao hujipatia riziki zao kupitia biashara ndogo ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inathamini sana mchango wa wafanyabiashara wadogo katika kukuza ajira na kipato. Hata hivyo, wafanyabiashara wadogo wote wanatakiwa kuendesha biashara zao katika maeneo yaliotengwa rasmi kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale wanaokiuka utaratibu huu, Halmashauri hulazimika kuwatumia Mgambo kwa ajili ya kuwaondoa wafanyabiashara hao na kuwaelekeza kwenda katika maeneo yaliotengwa rasmi. Aidha, katika kutekeleza wajibu huo, mgambo wanatakiwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara, Serikali inatekeleza mpango wa kurasimisha biashara katika mfumo usiokuwa rasmi ili kuzitambua, kuzisajili na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri zote kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili biashara hizo zifanyike katika maeneo rasmi ambayo itakuwa rahisi kuwatambua na kuwahudumia.
Aidha, wafanyabiashara wadogo wanashauriwa kuunganisha mitaji yao midogo na kuunda kampuni ndogo za biashara ili waweze kukopesheka katika Taasisi za fedha na hivyo kuongeza tija katika biashara hizo.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
Shule nyingi katika Wilaya ya Ilemela hususani shule za msingi zina upungufu mkubwa wa madawati:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayekaa chini wakati wa masomo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka karakana kwa kila shule ya msingi katika Wilaya ya Ilemela na kutumia vijana wazawa kutengeneza madawati ili kuepuka tatizo hili sugu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa madawati kwa shule za msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni madawati 13,080. Ili kukabiliana na upungufu huo Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/2016, imetenga jumla ya shilingi 228.5 kwa ajili ya upatikanaji wa madawati. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 25.69 zinatokana na Mfuko wa Kuchochea Maendeleo katika Jimbo la CDCF.
Naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa uamuzi wake wa kuelekeza fedha hizo katika upatikanaji wa madawati. Aidha, natumia fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa wote kuhakikisha agizo la Serikali la kumaliza tatizo la madawati ifikapo tarehe 30 Juni, 2016 liwe limekamilika kikamilifu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya shule yanahitaji utulivu na usalama wa watoto katika kujisomea bila kuwa na bughudha, hivyo hatushauri karakana hizo kuanzishwa katika maeneo ya shule za msingi badala yake Halmashauri zinashauriwa kuimarisha karakana za Halmashauri chini ya Mhandisi wa Halmashauri ili kujenga uwezo wa kutengeneza madawati kwa gharama nafuu. Mfano mzuri ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ambao wametumia karakana ya Halmashauri kutengeneza madawati yote yanayohitajika. Natumia fursa hii kuwahamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali katika fani ya useremala ili waweze kukopesheka na kushiriki katika shughuli za utengenezaji wa madawati na shughuli nyingine katika Halmashauri.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Hospitali ya Mji wa Mafinga inahudumia wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na pia Wilaya jirani za Mbarali na Iringa Vijjini lakini pia iko kandokando ya barabara kuu, hivyo kukabiliwa na mzigo mzito wa kuhudumia majeruhi wa ajali zinazotokea kwenye barabara hiyo kama ile ya Mafinga:-
Je, Serikali iko tayari kuiongezea hospitali hiyo fedha na watumishi mara mbili zaidi ya kiwango inachopata sasa iweze kuwa na uwezo wa kutosha kukabiliana na mzigo wa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiipatia hospitali hii fedha kwa ajili ya kuendesha huduma ambako kwa mwaka wa fedha 2016/2017, fedha zilizotengwa ni shilingi milioni 90 kwa ajili ya maendeleo na shilingi milioni 90 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za uboreshaji huduma za afya, Serikali imesisitiza umuhimu wa kila Halmashauri kuboresha makusanyo ya ndani kupitia mifumo ya afya ya jamii yaani CHF/TIKA na fedha za makusanyo mengine kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma katika hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watumishi, Hospitali ya Wilaya ya Mafinga ina jumla ya watumishi 209, upungufu ikiwa ni watumishi 95 sawa na asilimia 31.3. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imeidhinishiwa kuajiri watumishi 18 na itaendelea kuongeza idadi hiyo kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya hospitali hiyo.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Kumekuwa na wimbi kubwa la wanafunzi wa shule za Serikali za msingi na sekondari wanaofeli kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi katika darasa moja dhidi ya mwalimu mmoja kwa wanafunzi huku wakifundishwa kuanzia saa moja na nusu hadi saa kumi na nusu jioni, na kufanya walimu wakose muda wa kutosha wa kusimamia kazi za wanafunzi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na changamoto hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha elimu nchini kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, Serikali imeendelea kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitenga shilingi bilioni 67.83 ambazo zimepokelewa na zimetumika ka ajili ya ukarabati, ujenzi na umaliziaji wa vyumba vya madarasa, vyoo vya walimu na wanafunzi, ujenzi wa nyumba sita (multiple unit houses) na uwekaji wa umeme (grid house solar) katika shule za sekondari 528 nchini kote. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na juhudi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kuajiri walimu wapya 35,411 kwa shule za msingi na sekondari ili kuongeza idadi ya walimu hivyo kupunguza mzigo mkubwa uliopo kwa walimu kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya elimu hapa nchini.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA (K.n.y MHE. STANSLAUS S. MABULA) aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana inahudumia zaidi ya wakazi 300,000 wakiwemo wanaotoka Wilaya za jirani lakini haina vifaa tiba kama vile x-ray, ultrasound na kadhalika huku ikiwepo ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2013 lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.
Je, ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa na kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba vya kutosha ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaopoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa mashine ya x-ray katika utoaji wa huduma za afya, Halmashauri ya Jiji la Mwanza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 133.14 kwa ajili ya ununuzi na kufunga mashine ya x-ray katika Hospitali ya Nyamagana. Aidha, ultrasound ipo katika hospitali hiyo na inafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri pia katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 33.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo mbalimbali vya afya vinavyotoa huduma za afya ndani ya Wilaya ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Aidha Halmashauri imetenga shilingi milioni 10.5 kwa ajili ya matengenezo ya vifaa vya hospitali.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya Mnanila – Kasulu yenye urefu wa kilometa 42 kwa lami.
(a) Je, lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
(b) Zile kilometa nne ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba zingeanza kujengwa kwa kiwango cha lami katika Makao Makuu ya Wilaya ya Buhigwe utaanza lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Ntabaliba Obama, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mnanila – Kasulu yenye urefu wa kilometa 48 ni barabara ya mkoa chini ya Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na inaunganisha Wilaya tatu za Kasulu, Buhigwe, Kigoma na nchi jirani ya Burundi. Barabara hii ni sehemu ya barabara ya Kibondo – Kasulu – Manyovu yenye urefu wa kilometa 250 ambayo kazi ya usanifu wa kina inaendelea ikiwa ni hatua muhimu katika ujenzi kwa kiwango cha lami. Utekelezaji utafanyika kupitia wahisani wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) chini ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Baada ya kukamilika kwa usanifu, taratibu za ujenzi kwa kiwango cha lami zitafuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa kipande cha barabara kilometa mbili katika makao makuu ya Wilaya ya Buhigwe, Halmashauri imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu ambao utasaidia kujua gharama za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Kukamilika kwa hatua hiyo, kutawezesha Serikali kuweka katika mpango na kutenga bajeti ili kuanza ujenzi.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu ulianzishwa kisheria na Makao Makuu yake kuwa kwenye Mji Mdogo wa Bariadi badala ya Mji wa Maswa:-
(a) Je, ni vigezo gani vilitumika kuamua Makao Makuu ya Mkoa na shughuli zake yawe Bariadi badala ya Maswa ambako kuna majengo ya kutosha ya Serikali; badala yake Serikali inaingia kwenye matumizi makubwa ya kupanga ofisi toka nyumba za watu binafsi huko Bariadi?
(b) Je, Serikali inaweza kufikiria kubadilisha maamuzi haya kwa manufaa ya Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, maamuzi ya Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu kuwa Bariadi Mjini siyo Maswa yalipitishwa na wananchi wenyewe kupitia vikao vya kisheria ambavyo ni Mkutano Mkuu wa Vijiji, Kamati za Maendeleo ya Kata, Mabaraza ya Madiwani, Kamati za ushauri za Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC). Uamuzi wa mwisho ulifanyika katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa tarehe 10 Mei, 2010 ambapo Wajumbe wote waliridhia pendekezo la Bariadi Mjini kuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu. Hivyo, kigezo kikubwa kilichotumika kuamua Makao Makuu kilikuwa ni maamuzi ya pamoja kupitia vikao halali vilivyoshirikisha wadau kutoka Wilaya zote, wakiwemo kutoka sekta binafsi.
(b) Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu ya (a) ya jibu hili, maamuzi hayo yalifanywa na vikao halali vya kisheria, ikiwahusisha Wajumbe wa vikao hivyo, hivyo kitendo cha Serikali kubadilisha maamuzi hayo itakuwa ni kuwanyang‟anya madaraka wananchi yaliyowekwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 145.
MHE. LUCY T. MAYENGA (K.n.y. MHE. SALOME W. MAKAMBA) aliuliza:-
Tatizo la kukatika umeme mara kwa mara katika Jimbo la Kahama Mjini linaathiri sana uzalishaji viwandani hasa ukizingatia Serikali imepiga marufuku kwa baadhi ya viwanda kama vile vya kukoboa mpunga na kusaga mahindi kutofanya kazi usiku:-
Je, Serikali ipo tayari kuruhusu viwanda Wilayani Kahama kufanya kazi masaa 24 ili kufidia uzalishaji unaokuwa haufanyiki kipindi umeme unapokuwa umekatika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa hakuna zuio lolote la Halmashauri ya Mji wa Kahama kwamba mashine za kukoboa mpunga na mahindi zisifanye kazi wakati wa usiku au saa 24. Changamoto iliyopo ni kwamba viwanda hivyo vinatumia umeme wa jenereta ambao hautoshelezi kuendesha mashine wakati wote, hivyo kumekuwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara. Halmashauri imewasiliana na Meneja wa TANESCO Kahama na tayari tatizo hilo limeanza kushughulikiwa ili kupata umeme wa uhakika kutoka gridi ya Taifa ambapo tayari kituo cha usambazaji kimeanza kujengwa Kahama.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri inahamasisha wawekezaji wa viwanda vidogo, vikiwemo vya kukoboa mpunga, mahindi na mazao mengine ili kupanua wigo wa mapato kupitia ushuru wa huduma (service levy) na ajira kwa vijana, hivyo hakuna sababu yoyote kwa Serikali kuzuia wawekezaji katika viwanda vidogo na vikubwa. Azma ya Serikali ni kupanua uwekezaji wa viwanda kadri iwezekanavyo kwa kuzingatia fursa zilizopo. Tunachofanya ni kuboresha mazingira yatakayosaidia uwekezaji huo ufanyike kwa faida, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha umeme wa uhakika unakuwepo.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Wakulima wengi wa Wilaya ya Chemba wamefukuzwa katika mashamba yao Wilayani Kiteto licha ya kufuata taratibu na kudaiwa kuwa eneo hilo ni hifadhi.
Je, Serikali ipo tayari kufuta uamuzi uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara wa kuwazuia wakulima hawa ili kuondoa mgogoro huu wa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tamko lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara liliwahusu wakulima waliokuwa wavamizi katika eneo la Hifadhi ya Wanyamapori Makame kutoka Wilaya ya Kiteto, Babati, Chemba, Kondoa na Mkoa wa Iringa, waliokuwepo wakiendesha shughuli za kilimo katika hifadhi kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika, uamuzi huo ulitolewa kufuatia Azimio la kikao cha pamoja cha Kamati ya Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Kiteto na Chemba kilichokaa tarehe 12 Novemba, 2015. Kikao hicho kiliwashirikisha viongozi wa Vijiji vitano vinavyounda Mamlaka ya Hifadhi (WMA) ambavyo ni Ngobolo, Katikati, Ndedo, Ikshubo na Makame, pamoja na wawakilishi wa wakulima 10 kutoka kila Wilaya.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria hairuhusiwi shughuli yoyote ya kibinadamu, iwe kilimo, ufugaji au makazi kuendeshwa katika hifadhi. Naomba kutoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria za nchi ili kuepuka migogoro katika jamii. Aidha, Serikali za vijiji zinakumbushwa kusimamia vizuri sheria ya ardhi namba tano ya mwaka 1999 ambayo imeweka utaratibu wa kufuata kwa mtu atakayehitaji kupata ardhi kwa matumizi mbalimbali. Lengo ni kuzuia migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima ambayo kwa sehemu kubwa inatokana na kutozingatia Sheria ya Ardhi.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Utekelezaji wa maagizo ya Serikali Kuu kwa Halmashauri imekuwa ni changamoto na mzigo mkubwa kwa Halmashauri hizo hususan Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambapo maagizo mengi hayamo kwenye Mpango wa Bajeti na hivyo utekelezaji unakuwa mgumu.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha maagizo hayo yanatengewa bajeti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikitoa maagizo ya kiutendaji katika Halmashauri zetu nchini na si kwa Halmashauri ya Kibaha pekee ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa inatatua changamoto ambazo Halmashauri zinaikabili kwa kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya maagizo hayo ya hutolewa na Serikali huhitaji fedha. Maagizo hayo huingizwa kwenye mipango na bajeti ya Halmashauri yanapotolewa kabla ya bajeti kupitishwa, hata hivyo baadhi ya maagizo na maelekezo hutolewa na Serikali katikati ya mwaka wa bajeti, maagizo na maelekezo ya Serikali ambayo hukosa kabisa fedha katika mwaka husika huingizwa katika bajeti za Halmashauri ya mwaka wa fedha unaofuata kwa ajili ya utekelezaji au Halmashauri hufuata utaratibu wa kurekebisha bajeti.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuzihimiza Halmashauri zote nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuendelea kutenga fedha katika mpango na bajeti yao ili ziweze kutatua changamoto zinazowakabili.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. WILLIAM D. NKURUA) aliuliza:-
Wilaya ya Nanyumbu ilianzishwa mwaka 2005 lakini mpaka sasa haina Hospitali ya Wilaya hivyo kuwalazimu wananchi kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Masasi lakini pia kumekuwa na jitihada za kuomba kukipandisha hadhi Kituo cha Mangaka kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nanyumbu lakini mpaka sasa hakuna mafanikio yoyote.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi kituo hicho ili kuwa Hospitali ya Wilaya na kunusuru afya za wananchi wa Nanyumbu hasa akina mama wajawazito kwa kulazimika kupelekwa Wilaya jirani ya Masasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa William Dua Nkurua, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha Wilaya ya Nanyumbu inakuwa na Hospitali ya Wilaya, tayari Serikali imetoa kibali na kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Mangaka kuwa Hospitali ya Wilaya baada ya kukidhi vigezo na taratibu zilizowekwa. Kibali hicho kimetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia barua ya tarehe 27 Februari, 2016.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya cha Makambako kuwa Hospitali lakini tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa vifaa tiba na kufanya watu wengi kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula.
Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa hivyo ili watu wasipate taabu ya kwenda kutibiwa Kibena, Njombe au Ilembula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupandisha hadhi Kituo cha Afya Makambako kuwa Hospitali, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya umeme chumba cha upasuaji, kitanda cha kufanyia upasuaji na seti tatu za vifaa vya upasuaji akina mama wajawazito na seti mbili za upasuaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo, tukiri kwamba bado upo upungufu wa vifaa kama vile X-ray, Ultrasound, ECG machine na mashine ya dawa za usingizi, pulse oxymeters, monitors, seti ya mashine ya kufulia nguo na vifaa vya meno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 20.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kupitia vyanzo vya mapato ya ndani. Aidha, Halmashauri imepanga kukopa shilingi milioni 154.2 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza: -
Chaguzi za Madiwani zilifanyika katika kambi ya wakimbizi Katumba wa 2015:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha chaguzi za Serikali za Vijiji na Mtaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Katumba, Vijiji ambavyo havijafanya uchaguzi wa Vviongozi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2014 ni 14 na vitongoji 51. Uchaguzi ulishindwa kufanyika kwa sababu Kata hiyo ilikuwa ni kambi ya wakimbizi ambao walikuwa hawajapata uraia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kuwapa uraia wananchi wa maeneo hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo inaendelea na maandalizi ya kufanya uchaguzi mdogo katika vijiji na vitongoji hivyo na tayari katika bajeti ijayo ya mwaka 2016/2017 zimetengwa sh. 3,300,000 ili kuwezesha zoezi hilo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ni sehemu ya ghala la chakula la Taifa katika mikoa mitano (5) inayolima chakula kwa wingi nchini Tanzania; lakini kikwazo kikubwa ni usafirishaji wa mazao kufikia masoko ya nje ya Wilaya; Halmashauri imeomba ongezeko la bajeti ya barabara kufikia shilingi bilioni 7,969,000 ili kuweza kukarabati barabara zote muhimu na kuwezesha wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi na hatimaye kuongeza kipato cha Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe:-
Je, Serikali ipo tayari kukubali ombi la Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe la kuongeza fedha katika bajeti ya 2016/2017?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe iliandaa makisio ya bajeti ya shilingi bilioni 7.9 kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Hata hivyo, kutokana na ukomo wa bajeti, fedha zilizoidhinishwa ni shilingi milioni 920 ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara na ujenzi wa madaraja. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri hiyo ilitengewa shilingi milioni 870 na tayari Serikali imepeleka shilingi milioni 157.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Barabara katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ni shilingi bilioni 247.5 ambazo endapo zingegawanywa sawa kwa kila Halmashauri zote 181 zilizopo, kila Halmashauri ingeweza kupata bajeti ya shilingi bilioni 1.3 tu. Hivyo, mara zote mahitaji yamekuwa ni makubwa kuliko uwezo wa rasilimali fedha kukidhi mahitaji hayo, ndiyo maana tunaweka vipaumbele ili kutekeleza mambo machache kwanza kulingana na uwezo uliopo kibajeti. Serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya barabara kadri uwezo utakavyowezekana.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Halmashauri ya Kavuu ni mpya na mapato yake yako chini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa inawapatia wananchi mawasiliano ya barabara japo kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mtandao wa barabara za changarawe katika Halmashauri mpya ya Mpingwe ni kilomita 37.7, sawa na asilimia 19 ikilinganishwa na kilomita 202.5 kwa Wilaya nzima. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imepanga kufanya matengenezo ya kilometa 42 kwa kiwango cha changarawe ambapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo ni shilingi milioni 246.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017, ni kufanya matengenezo ya kilometa nyingine 49.8 kwa kiwango cha changarawe pamoja na matengenezo ya sehemu korofi na matengenezo ya kawaida katika barabara za Halmashauri. Jumla ya shilingi milioni 324 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-
Mkoa wa Lindi umekuwa na shule chache za Kidato cha Tano na cha Sita, matokeo yake vijana wanaofaulu Kidato cha Nne kuingia Kidato cha Tano hupangiwa shule za mbali:-
Je, ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kufanya Shule ya Sekondari Mchinga kuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi Kidato cha Kwanza hadi cha Sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhitaji mkubwa wa Shule za Sekondari Kidato cha Tano na Sita katika Wilaya ya Lindi, tayari Halmashauri ya Wilaya ya Lindi imependekeza Shule ya Sekondari ya Mchinga kuwa ya Kidato cha Tano na Sita. Hata hivyo shule hiyo ina upungufu ukosefu wa mabweni, matundu ya vyoo, jiko na bwalo la chakula. Halmashauri imeelekezwa kuweka vipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya kurekebisha upungufu wa miundombinu ili shule hiyo iweze kupata sifa ya kusajiliwa na kuwa ya Kidato cha Tano na Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya upungufu huo kurekebishwa na kukamilika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, itatuma wataalam kwa ajili ya kukagua vigezo vilivyozingatiwa ili shule iweze kupandishwa hadhi kuwa ya Kidato cha Tano na Sita na endapo itaridhika itatoa kibali. Aidha, Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita ni za Kitaifa na kwa mantiki hiyo, zinapokea wanafunzi waliohitimu na kufaulu Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne kutoka nchi nzima.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiahidi kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na Zahanati kwa kila Kijiji na Kituo cha Afya kila Kata na Hospitali kwa kila Wilaya ili kuwaondolea kero wananchi wanaosafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya na wengine kupoteza maisha wakiwa njiani:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza mpango huo wa kuwa na Zahanati kwa kila Kijiji, Kituo cha Afya kwa kila Kata na Hospitali kwa kila Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Zahanati kwa kila kijiji, Vituo vya Afya kila Kata na Hospitali kila Wilaya, unafanyika kwa ushirikiano kati ya wananchi na Halmashauri kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD).
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu kubwa ya miradi hii huibuliwa na kutekelezwa na wananchi wenyewe na Halmashauri huchangia nguvu kidogo ili kukamilisha miradi hiyo. Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi, inaendelea na ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali kila Wilaya. Ujenzi huo unafanyika chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi yaani MMAM, ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kwa mwaka 2016 hadi 6,935 katika mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 31.9. Aidha, utekelezaji wa program hii unaendelea, ambapo katika mwaka 2016/2017 Halmashauri zimetengewa shilingi bilioni 182.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipaumbele kimetolewa katika kukamilisha miradi viporo, badala ya kuanzisha miradi mipya. Ofisi ya Rais TAMISEMI, inafanya tathmini ya utekelezaji wa MMAM ili kujua idadi ya vijiji ambavyo havina Zahanati. Kata ambazo hazina Vituo vya Afya na Wilaya ambazo hazina Hospitali. Lengo la tathmini hiyo ni kuhakikisha maeneo haya yanapewa kipaumbele na kutengewa bajeti ili kuongeza huduma za afya karibu na wananchi.
Kituo cha afya cha Chamwino Ikulu kinahudumia zaidi ya Kata 20 za Wilaya ya Chamwino na wanawake na watoto wa kata hizo wanategemea sana huduma za kituo hicho, lakini hakina vifaa tiba muhimu kama vile ultra sound:-
Je, ni lini Serikali itanunua ultra sound kwa ajili ya kituo hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kituo cha afya cha Chamwino hakina ultra sound kwa ajili ya huduma za mama na wajawazito na watoto. Kifaa hicho kinagharimu shilingi milioni 72.0 ambazo hazijawekwa kwenye bajeti ya Halmashauri kutokana na ukomo wa bajeti. Hata hivyo Halmashauri imewasilisha maombi ya mkopo wa shilingi milioni 72 katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kupata fedha zitakazowezesha kifaa hicho kununuliwa, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, wagonjwa wanao hitaji huduma hiyo kwa sasa, wanapewa Rufaa kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo huduma hiyo inapatikana.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Mji Mdogo wa Mbalizi uliomo kwenye Halmashauri ya Mbeya ni kati ya miji inayokua kwa kasi sana lakini inakosa miundombinu muhimu na uhaba na maji pia.
(a) Je, ni lini Mji huo utapewa hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji?
(b) Je, ni lini Serikali itatatua tatizo kubwa la maji kwenye Mji huo?
(c)Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye kata zilizo ndani ya Mji wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa Halmashauri za Miji nchini unazingatia Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 288 (Mamlaka za Miji) ambayo imeainisha taratibu na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa. Hivyo, nashauri pendekezo hili lijadiliwe kwanza katika vikao vya Kamati za Maendelo ya Kata, Baraza la Madiwani na Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Endapo vikao hivyo vitaridhia, Ofisi ya Rais - TAMISEMI haitasita kuyafanyia kazi mapendekezo hayo ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa Mbalizi unapata maji kutoka chanzo cha Ilunga chenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 3,024 za maji kwa siku pamoja na visima kumi vya maji ambavyo vina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 6,300 kwa siku. Mji wa Mbalizi umeingizwa katika Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri inakusudia kuunganisha Mji huo na Mamlaka ya Maji Mkoa wa Mbeya ili kupata maji yatakayotosheleza mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mji wa Mbalizi wanapata huduma za afya kupitia Hospitali Teule ya Mbalizi pamoja na Hospitali ya Jeshi la Wananchi ambako Halmashauri imeendelea kutoa mchango wa dawa na watumishi. Hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017, kipaumbele kimewekwa katika kukamilisha ujenzi wa zahanati nane ndani ya Halmashauri zilizoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Zahanati za Nyang‟hanga, Salongwe, Nsola, Bundilya, Nyamahanga, Nyashingwe, Chabula, Ikengele, Isangijo, Langi na Lutale ziko kwenye hatua za ukamilishaji.
Je, ni lini Serikali itazikamilisha zahanati hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga Mbunge wa Magu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 Halmashauri ya Wilaya ya Magu imetengewa shilingi milioni 160 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati kumi na tano ambazo ziko katika hatua mbalimbali. Vilevile katika mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 212.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakamilisha majengo hayo ili huduma zianze kutolewa. Kama nilivyoeleza hapa Bungeni mara kadhaa, hivi sasa tunakamilisha tathmini ya ujenzi wa miundombinu ya zahanati na vituo vya afya ili kuandaa mpango wa haraka utakaosaidia kukamilisha ujenzi wa majengo hayo muhimu kwa nchi nzima.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
(a) Je, Serikali itakubali kujenga Hospitali ya Wilaya ya Busokelo hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wametoa eneo tayari na wako tayari kushirikiana na Serikali?
(b) Je, kama Serikali inakubali, ni lini kazi hiyo itaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni sera ya Serikali kuhakikisha tunajenga hospitali kila Wilaya, ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Utekelezaji umefanyika kupitia mpango wa Halmashauri kwa kushirikisha nguvu za wananchi, hivyo napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Hospitali ya Wilaya inajengwa katika Halmashauri mpya ya Busokelo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa hospitali hiyo umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo zimetengwa shilingi bilioni 2.0 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD).
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisja ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu, jana tulipata ajali mbaya lakini kwa uwezo wake na mapenzi yake alitunusuru. Shukrani zote zinamstahiki yeye kwa sababu ndiye muweza wa kila jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga unaendelea ambapo kazi zilizofanyika ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje yaani OPD, ujenzi wa wodi 2 za kulaza wagonjwa ambazo zipo katika hatua ya “renta”, ujenzi wa nyumba moja ya watumishi ambayo ipo katika hatua ya ukamilishaji, ujenzi wa jengo la vyumba vya madaktari yaani Doctors Consultation Rooms ambalo limeshapauliwa na uwekaji wa miundombinu ya maji na umeme katika jengo la OPD. Kazi zote hizo zimegharimu jumla ya shilingi 368,000,000.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imeidhinishiwa shilingi 40,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa wodi mbili za kulaza wagonjwa, umaliziaji wa nyumba moja ya mtumishi pamoja na jengo la vyumba vya madaktari. Halmashauri imetakiwa kuhakikisha inaipa kipaumbele Hospitali hiyo kwa kutenga bajeti kila mwaka ili kukamilisha miundombinu iliyobaki.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Toka imetangazwa kuwa elimu ni bure walimu wengi wanaofundisha elimu ya awali (chekechea) wameondoka katika shule walizokuwa wanafundisha na kuanzisha vituo vyao sababu ni kutolipwa.
Je, Serikali haioni hili ni tatizo kwa wanafunzi hao ambao wanahitaji msingi mzuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA TAMISEMI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa viti Maalum kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, walimu walioondoka katika shule walikuwa wanalipwa kupitia michango ya wazazi ambao wengi wao hawakuwa na sifa ya kufundisha wanafunzi wa elimu ya awali kwa maana ya kuhitimu Daraja la IIIA.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa, walimu wote wanaopangwa kufundisha shule za msingi mongoni mwao wapo ambao wanapangwa kufundisha darasa la elimu ya awali kwa sababu ya mafunzo wanayopata vyuoni yakijumuisha mbinu za ufundishaji wa elimu ya awai. Vyuo vyote vya ualimu wa shule ya msingi vinatoa mafunzo ya ualimu ngazi ya stashahada ya elimu ya awali. Hadi mwaka 2016 wapo walimu wa daraja la kwanza, IIIA wapatao 191,772 ambao kati yao walimu wenye ujuzi wa kufundisha madarasa ya elimu ya wali ni 10,994.
MHE. FREEMAN A. MBOWE Aliuliza:-
Ongezeko la ukubwa wa Serikali na watumishi wake inatokana na kuongezeka mara kwa mara kwa mitaa, vijiji, kata, tarafa, majimbo ya uchaguzi, wilaya na mikoa na hivyo kuongeza ukubwa wa bajeti ya Serikali kwenye mishahara, matumizi mengine (OC) na kusababisha kupungua kwa ongezeko la bajeti ya maendeleo na hata wakati mwingine upatikanaji wake.
(a) Je, ni Vitongoji, Vijiji, Mitaa, Kata, Tarafa, Majimbo, Wilaya na Mikoa mingapi imeongezeka mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2000 hadi 2015?
(b) Je, ongezeko hili limesababisha vipi ukuaji wa idadi ya watumishi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na mishahara imepanda vipi mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2000 hadi 2015 na ongezeko hilo ni asilimia ngapi ya bajeti ya Serikali?
(c) Je, Serikali haioni sasa umuhimu mkubwa wa kusitisha ukuaji wake ili kuelekeza fedha zinazogharamia utawala kwenda moja kwa moja kwenye bajeti za maendeleo ya wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Jimbo la Hai, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala ikiwemo Mikoa, Wilaya, Majimbo, Tarafa, Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji unazingatia matakwa ya Katiba ya mwaka 1977 Ibara ya 2(2) pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 287 na 288 ambazo zimempa Waziri mwenye dhamana wa Serikali za Mitaa madaraka na kuweka utaratibu wa kugawa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 mpaka 2015 Mikoa imeongezeka kutoka 21 hadi 26, Wilaya kutoka 114 mpaka 139, Tarafa kutoka 521 hadi 558, Halmashauri kutoka 133 hadi 185, Kata kutoka 3,833
mpaka 4,420, Vijiji kutoka 10,376 hadi 12,545, Mitaa kutoka 1,975 mpaka 4,037, Vitongoji kutoka 57,137 mpaka 64,677. Aidha Majimbo ya Uchaguzi yameongezeka kutoka 239 hadi 268.
Kati ya mwaka 2000 hadi 2015 idadi ya watumishi wa Serikali imeongezeka kutoka wastani wa watumishi 222,792 hadi wastani wa watumishi 405,314. Ongezeko hilo la watumishi limesababisha bajeti ya mishahara kuongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 668.6 hadi shilingi trilioni 3.05.
Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuongeza huduma karibu na wananchi, hivyo Serikali itaendelea kuzingatia matakwa ya Katiba na sheria zilizopo katika kugawa eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mikoa na maeneo mengine ya utawala. Hata hivyo kigezo cha uwezo wa nchi kiuchumi kitaendelewa kuzingatiwa katika utekelezaji wa azma hii.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Barabara inayounganisha vijiji vya Msanga na Kawawa ni muhimu sana kiuchumi kwa kata ya Msanga na Wilaya ya Chamwino na pia kuna mazao mengi ya uhakika kutoka Kawawa na vitongoji vyake, lakini barabara hiyo ni korofi sana kwa sababu ya mbuga iliyoko kati ya vijiji hivyo viwili na zaidi, daraja kubwa lililopo limevunjika kabisa kiasi kwamba halipitiki kabisa wakati wa mvua na wakati wa kiangazi hupitika kwa taabu sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha barabara hiyo na kulijenga daraja husika ili kuboresha mawasiliano ya vijiji hivi viwili na masuala ya usafirishaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Jimbo la Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 imetenga shilingi milioni 46.3 kwa ajili ya kujenga kivuko (box culvert), kuichonga barabara kwa urefu wa kilometa tano na kuiwekea changarawe sehemu korofi yenye urefu wa kilometa nne. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, barabara hii imeombewa shilingi milioni 130 kwa ajili ya ukarabati ili kuifanya ipitike wakati wote.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ruzuku katika Hospitali ya Haydom ambayo pia ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambayo inatumiwa na Mikoa ya Singida, Simiyu, Arusha pamoja na Jimbo la Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Haydom kwa sasa inatumika kama Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kupitia Tangazo la Serikali namba 828 la tarehe 12 Novemba, 2010. Serikali imeweka utaratibu wa kuipatia hospitali hii ruzuku ya Serikali kwa ajili ya dawa na vifaa tiba kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya, pamoja na kulipa mishahara ya baadhi ya watumishi wanaotoa huduma katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 134.04 kwa ajili ya dawa na uendeshaji wa shughuli za hospitali, kati ya fedha hizo, zilizopokelewa ni shilingi milioni 111.5. Vilevile hospitali hii imetengewa shilingi milioni 570.6 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya kulipa mishahara kwa watumishi wa Serikali wanaofanya kazi katika hospitali hiyo. Kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mkataba wa utoaji huduma ya afya, lengo likiwa ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo ambayo inahudumia Mkoa wa Manyara pamoja na Mikoa jirani.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Kushusha madaraka kwa wananchi (D by D) ni jambo muhimu sana katika masuala muhimu yakiwemo elimu, afya na kilimo na kadhalika.
Je, Serikali haioni kuwa ni mapema mno kushusha elimu ya kidato cha tano na sita kwenda TAMISEMI kabla ya kurekebisha changamoto za elimu za awali, msingi na sekondari hadi kidato cha nne?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugatuaji wa madaraka (Decentralisation by Devolution) ni suala la Kikatiba kwa kuzingatia Ibara ya 145 na Ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ambayo inatambua uwepo na madhumuni ya Serikali za Mitaa kuwa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Utekelezaji wake unafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura Namba 287 ambayo inazungumzia suala la Mamlaka za Wilaya na Sura Namba 288 - Mamlaka za Miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa kugatua elimu ya msingi na sekondari kwenda katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ulikuwa ni kupeleka madaraka kwa wananchi ili kuwapa fursa ya kushiriki katika kusimamia na kuziendeleza shule hizo. Uendelezaji wa walimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa umewezesha kubaini changamoto mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka ikiwa ni pamoja na miundombinu na masuala ya kiutumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifahamike pia kwamba uendeshwaji wa shule kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita hauwezi kutenganishwa kwa sababu sehemu kubwa ya shule hizo zina kidato cha kwanza hadi cha sita, lakini pia wananfunzi wanaofaulu kidato cha nne wanajiunga na kidato cha tano hapohapo shuleni au shule nyingine. Aidha, kwa kuzingatia matakwa ya Kikatiba na juhudi kubwa ya Serikali katika kuboresha elimu ni wazi kwamba suala la kidato cha tano na kidato cha sita kusimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni muafaka sana. Kinachotakiwa ni kuunga mkono juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika ukusanyaji wa kodi ili kujenga uwezo wa kutatua changamoto za kibajeti zilizopo.
Idadi ya Shule za Awali Nchi
Elimu bora ni uti wa mgongo wa maendeleo ya jamii yoyote ile na ni msingi bora wa elimu kwa watoto unaoanzia toka shule za awali na za msingi:-
(a) Je, kuna shule ngapi za awali kati ya mahitaji halisi?
(b) Je, ni nini mipango ya haraka kuhakikisha shule za awali zinakuwepo katika shule zote za msingi za Serikali nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselim Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji halisi ya madarasa ya awali ni 16,014 ambayo ni sawa na idadi ya shule za msingi zilizopo nchini kwa sasa. Shule zenye madarasa ya awali ni 14,946 ambazo ni sawa na asilimia 93.33 ya mahitaji. Hivyo, shule za msingi 1,068 hazina madarasa ya awali.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vyumba vya madarasa ya awali unafanywa na Halmashauri kwa kushirikisha na nguvu za wananchi kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo yaani O and OD (Opportunity and Obstacle to Development). Azma ya Serikali ni kuhakikisha inajenga na kukamilisha vyumba vya madarasa vya awali kwa shule zote 1,068 zenye upungufu huo. Hivyo nitoe wito kwa Halmashauri zenye mapungufu haya kuangalia upya vipaumbele vyake na kutenga bajeti ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Serikali ilifanya tathmini na kuona umuhimu wa kujenga daraja kwenye Kata ya Ruhembe kwa shilingi milioni mia sita lakini mpaka sasa shilingi milioni 100 tu zimepelekwa kwenye Halmashauri ya Kilosa.
Je, ni lini kiasi cha shilingi milioni 500 kilichobakia kitapelekwa ili kukamilisha daraja hilo na kuwasaidia wananchi wa Ruhembe wanaozunguka umbali mrefu ili kupata mahitaji yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zilizoidhinishwa na Serikali katika bajeti ya mwaka 2014/2015, kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Ruhembe zilikuwa ni shilingi milioni 300 fedha zilizopokelewa hadi Juni, 2015 zilikuwa shilingi milioni 100 ambazo zilitumika kwa ajili ya usanifu wa ujenzi wa daraja hilo. Mkandarasi aliyeomba fedha hizo anahitaji shilingi milioni 600 na hivyo kusababisha mradi huo kutotekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, zimetengwa shilingi milioni 700 ambazo zitatumika kujenga daraja hilo na kuchonga njia inayounganisha daraja hilo.
Hitaji la Shule za Kidato cha Tano na Sita Jimbo la Masasi
Jimbo la Masasi lina shule moja tu ya sekondari kwa kiwango cha kidato cha tano na sita, ambayo ni Sekondari ya Wasichana Masasi, ambayo imekuwa haitoshelezi kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaofaulu:-
(a) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi shule za sekondari za Mwenge Mtapika na Sekondari ya Anna Abdallah ili ziweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita?
(b) Je, ni lini Serikali itaajiri walimu katika Jimbo la Masasi ikiwa Ikama ya walimu wa sayansi katika shule za sekondari tisa zilizopo ni walimu 84 lakini waliopo ni 24 tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashidi Mohamed Chuachau, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuwa na shule za sekondari ya kidato cha tano na sita kila tarafa. Halmashauri ya Mji wa Masasi imeteua shule mbili za sekondari, ambazo ni Anna Abdallah na Mwenge Mtapila ili ziweze kuboreshwa na kuwa za kidato cha tano na cha sita. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri imetenga shilingi milioni 140 ili kuanza upanuzi wa miundombinu ya majengo ya shule hizo ikiwemo bwalo la chakula, jiko na huduma za maji na umeme. Aidha, Halmashauri imewasilisha andiko katika Mamlaka ya Elimu Tanzania yaani TEA kwa ajili ya maombi ya fedha shilingi milioni 125 za kukamilisha ukarabati wa miundombinu hiyo ya shule.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi katika Halmashauri ya Mji wa Masasi ni walimu 60. Serikali imeendelea kuwapangia vituo walimu wa masomo ya sayansi kadri wanavyohitimu na kufaulu mafunzo yao katika vyuo ili kukabiliana na upungufu huo. Mkakati tulionao kama Serikali ni kuongeza udahili wa walimu wa masomo ya sayansi katika vyuo ili kukidhi mahitaji kwa nchi nzima. Halmashauri ya Mji wa Masasi itapangiwa walimu wa sayansi na kila mara tutakapo kuwa tunaajiri walimu hao ili kupunguza pengo lililopo hivi sasa.
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-
Zaidi ya asilimia 30 ya wakazi wa mijini hupata chakula chao cha asubuhi, mchana na jioni kwa mama lishe, lakini mama lishe hao wananyanyaswa sana na askari wa mgambo wa majiji na miji kote nchini.
Je, kwa nini Serikali isiandae mazingira mazuri na masafi ya kufanyia kazi zao na wao wakatozwa ushuru mdogo kuliko hali ya kuendelea kuwanyanyasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, mama yangu huyu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafanyabisahara wadogo walioko katika sekta isiyo rasmi katika kukuza kipato na ajira. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Halmashauri zote zimeagizwa kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo mama lishe karibu na maeneo walipo wateja wao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu askari mgambo wanaonyanyasa mama lishe, jambo hili halikubaliki pia ni kinyume cha Sheria ya Polisi Wasaidizi ya mwaka 1969 inayowazuia kuwapiga, kuchukua au kuharibu bidhaa au mali za wananchi. Askari mgambo kama ilivyo kwa watumishi wengine wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na bila manyanyaso wala dhuluma wakati wa kuwaondoa wafanyabisahara katika maeneo yasiyoruhusiwa. Mheshimiwa Spika, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa askari mgambo yoyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa mama lishe na wafanyabisahara wengine wadogo, kwa sababu vitendo hivyo ni kinyume cha sheria. Aidha, napenda kutoa wito kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wote kufanya biashara zao katika maeneo yaliyotengwa rasmi na Halmashauri na kuacha kufanya bisahara hizo katika maeneo yasiyoruhusiwa.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-
Ili kuboresha elimu Serikali inashirikiana na Mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF ambao wanatoa misaada kwa sekta ya elimu:-
(a) Je, kwa mwaka 2014/2015 msaada wa UNICEF kwa Halmashauri ya Mbeya ulilenga mahitaji gani ya kuboresha elimu?
(b) Je, ni kiasi gani na asilimia ngapi ya msaada huo ulitumika katika miradi ya maendeleo ya elimu?
(c) Je, ni kiasi gani na asilimia ngapi ya msaada huo ulitumika katika matumizi ya kawaida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilitoa msaada kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya uliolenga katika uendeshaji wa shughuli za elimu ya msingi, hususan kutoa mafunzo kwa walimu, wanafunzi, wazazi na walezi, kamati ya bodi za shule, wenyeviti wa vitongoji na vijiji, kuhusu malezi na haki za msingi za watoto kwa kupata elimu bora. Kwa kuzingatia makubaliano hayo yaliyopo kati ya UNICEF na Serikali fedha hizo ni kwa ajili ya kujengea uwezo (capacity building) na hazitumiki kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule.
(b) Mheshimiwa Spika, hadi Juni, 2015 Halmashauri ilipokea shilingi milioni 308.6 sawa na asilimia 64.8 ya shilingi milioni 475.9 zilizopangwa kutolewa na UNICEF kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
(c) Mheshimiwa Spika, fedha zote zilizopokelewa sawa na asilimia 100 zilitumika kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Mji mdogo wa Wilaya ya Muheza ulianzishwa mwaka 2007 na ulihusisha
Kata tatu za Muheza Mjini, Mbaramo, Majengo na Masuguru; na tangu wakati
huo, umekuwa ukihudumia wananchi wake na taratibu za mapendekezo ya
kuidhinisha uanzishwaji wa Halmashauri ya Mji wa Muheza tangu tarehe
10/01/2016.
Je, ni kwa nini Serikali imechelewa kuiidhinisha Muheza kuwa Halmashauri
ya Mji huku ikijua kuna ongezeko kubwa la watu na Kata zimeongezeka hadi
kufikia sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab,
Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mapendekezo ya kupandisha hadhi
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Muheza, kuwa Halmashauri ya Mji wa Muheza,
yalifanyika na kupitishwa katika vikao vyote vya kisheria, vikiwemo Baraza la
Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa. Maombi haya tayari
yamepokelewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI baada ya kupitishwa na RCC. Hatua
itakayofuata ni kwenda kufanya uhakiki wa vigezo vinavyozingatiwa katika
kuanzisha Halmashauri za Miji nchini.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. FREEMAN A. MBOWE) aliuliza:-
Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa huwapa wananchi fursa ya kuchagua kiongozi na chama wanachotaka sambamba na Ilani za Vyama husika katika kila ngazi ya uchaguzi kuanzia ya Mtaa/Kijiji, Kata, Jimbo na Taifa:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali ya CCM hupuuza ukweli huu na kulazimisha Ilani ya Chama chao kutekelezwa nchi nzima kila ngazi bila kujali matakwa ya wananchi kupitia uchaguzi?
(b) Je, katika mazingira ya Manispaa au Halmashauri za Wilaya palipo na uongozi wa Chama tofauti na CCM ni ipi mipaka ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa kutoa amri au maelekezo ya kiutendaji?
(c) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka kuweka utaratibu wa kisheria na kikanuni ili kuondokana na mfumo huu kandamizi ambao ni urithi na ukiritimba wa mfumo wa chama kimoja cha siasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Hai, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inabainisha wazi kuwa nchi yetu inafuata mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa. Mfumo huo popote pale duniani hukipa Chama Tawala fursa na haki ya kuelekeza kutokana na ridhaa ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana hii ya vyama vingi inatumika pia katika mazingira ya Manispaa na Halmashauri. Vivyo hivyo, mipaka ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoa amri au maelekezo ya kiutendaji katika maeneo yao ya utawala, iko kwa mujibu wa Ibara ya 61(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na vifungu vya 5 (1)-(3) na 14(1)-(3) vya Sheria ya Utawala wa Mikoa, Sura ya 97. Hivyo, Serikali inaamini kuwa utaratibu huu umezingatia demokrasia na kwa sasa hakuna umuhimu wa kuweka mfumo mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali haioni ukiritimba wowote katika mfumo uliopo, hivyo sheria na mifumo iliyopo itaendelea kufanya kazi.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui yapo Isikizya eneo ambalo halina miundombinu, nyumba za kuishi na huduma rafiki kwa wafanyakazi. Shirika la Nyumba la Taifa limejenga nyumba Isikizya na lilipendekeza kuuza nyumba hizo kwa Halmashauri ya Uyui na kumaliza malipo ndani ya miaka mitatu lakini Halmashauri haina uwezo wa kumaliza malipo ndani ya miaka mitatu. Hivyo wafanyakazi wa Halmashauri wanaendelea kuishi katika nyumba za kupanga Mjini Tabora:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchangia ununuzi wa Nyumba za Shirika la Nyumba (NHC) ili wafanyakazi wa Halmashauri ya Uyui wahamie Isikizya?
(b) Shirika la Nyumba ni wadau wa maendeleo ya makazi na kwa kuwa Serikali ina nia ya kusaidia uanzishwaji wa Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui, je, kwa nini Serikali isishawishi Shirika la Nyumba kuongeza muda wa kuuza nyumba zake kutoka miaka mitatu hadi kumi ili kuwezesha Halmashauri kulipa polepole?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri ya Wilaya ya Tabora/Uyui ilitenga shilingi milioni 174.6 kwa ajili ya ununuzi wa nyumba tatu za watumishi ambazo zimejengwa na Shirika la Nyumba la NHC ili watumishi wa Halmashauri hiyo wahamie Isikizya yalipo Makao Makuu ya Halmashauri. Vilevile katika mwaka wa fedha 2016/2017, zimetengwa shilingi milioni 150 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa nyumba zaidi za watumishi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kifungu 14 (1) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepewa mamlaka ya kukopa katika taasisi mbalimbali za ndani au kuingia mikataba ya
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
8
manunuzi baada ya kupata kibali cha Waziri mwenye dhamana. Hata hivyo, katika kufanya hivyo Halmashauri zinapaswa kuzingatia uwezo uliopo katika kurejesha mkopo husika. Hivyo, Halmashauri inashauriwa kununua nyumba za NHC kwa kuzingatia uwezo uliopo katika bajeti iliyotengwa kwa mwaka 2016/2017.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Sera ya Serikali ya kujenga zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata haijatekelezwa vyema katika Jimbo la Masasi ambapo hakuna kata yenye kituo cha afya cha Serikali na zahanati zilizopo ni saba tu:-
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya katika kata 14 za Jimbo la Masasi?
(b) Je, Serikali inaweza kukiri kuwa kuna haja ya kuzipandisha hadhi Zahanati za Chisegu, Mumbaka na Mwenge Mtapika ili ziwe na vituo vya afya na hatimaye kuipunguzia mzigo Hospitali ya Mkomaindo pamoja na kusogeza huduma kwa jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa zahanati kila kijiji, vituo vya afya kila kata na hospitali kila wilaya unafanywa na Halmashauri kwa kushirikisha nguvu za wananchi kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD - Opportunity and Obstacle to Development). Kazi hii inafanyika kwa awamu katika Halmashauri zote, kulingana na bajeti iliyotengwa kila mwaka. Halmashauri ya Wilaya ya Masasi katika mwaka wa fedha 2015/2016 imeweka kipaumbele katika ujenzi wa zahanati ya Namatunu, Makarango, Mtaa wa Silabu ambao unaendelea. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 70 kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, inafanya tathmini ya miradi ya zahanati na vituo vya afya ambavyo havijakamilika pamoja ili kubaini vijiji na hata ambazo hazina miundombinu hiyo ili kujua gharama halisi zinazohitajika kumaliza miradi hiyo au kuanza ujenzi mpya.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kupandisha zahanati kuwa vituo vya afya, Halmashauri imeshauriwa kuanzisha mchakato huo kupitia vikao na kuwasilisha mapendekezo hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupata kibali.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Malambo ya Kijiji cha Mikomahiro, Salamakati, Salama „A‟, Sanzati, Mgeta, Kihumu/Hunyari na Nyang‟aranga yamekuwa hayatumiki ipasavyo kutokana na magugu maji na hivyo kujaa matope:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha malambo haya ili yatoe huduma nzuri kwa watumiaji?
(b) Malambo haya yalichimbwa miaka ya nyuma na watumiaji kwa sasa wameongezeka; je, Serikali ina mpango wa kuyapanua malambo hayo ili kukidhi mahitaji ya watumiaji kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa malambo umewekwa katika Mpango wa Miaka Mitatu wa Halmashauri kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo tathmini iliyofanyika imebaini kuwa zinahitajika shilingi milioni 90 kwa kazi ya kuondoa magugu maji na matope. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kipaumbele kimewekwa katika ujenzi wa masoko mawili na mnada wa Mgeta kwa gharama za shilingi milioni 60. Aidha, malambo mengine matano ya kunyweshea mifugo yatajengwa katika Vijiji vya Hunyari, Manchimweru, Kyandege, Salama Kati na Kaloleni ambayo yatagharimu shilingi milioni 200 hadi kukamilika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, mpango wa Serikali ni kukarabati malambo sita na kujenga mengine matano ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Aidha, mabirika ya kunyweshea mifugo yatajengwa katika Vijiji vya Hunyari, Kihumbu, Igundu, Salama Kati, Kaloleni, Mekomariro II, Manchimweru, Kyandege Nyang‟aranga, ambapo tathmini ilionesha zinahitajika shilingi 110 kukamilisha kazi hiyo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y MHE. ROSE K. SUKUM) aliuliza:-
Serikali ina utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya shule za bweni nchini. Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 31/08/2013 hadi tarehe10/02/2014 Halmashauri ya Hanang ilipokea kutoka Serikali Kuu kiasi cha shilingi 508,779,500 kwa ajili ya chakula cha shule za bweni. Taarifa zinaonesha kwa fedha zilizotumika kununua chakula ni shilingi 225,585,000 kwa takwimu hizo bakaa ni shilingi 283,194,500 kwa mujibu wa Mkaguzi, bakaa hiyo haionekani kwenye account yoyote benki.
(a) Je, fedha hizo zinarudishwa Hazina bila ya kuwa na uwepo wa nyaraka zozote toka Halmashauri kuonesha muamala unavyofanya kazi?
(b) Je, kama fedha hizo hazikurudishwa Hazina nani anaweza kuidhinisha matumizi bila ya mpango wake kupitishwa na Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri?
(c) Je, kama fedha zimetumika bila kupangiwa na Kamati halali, ni kwa nini wahusika bado wanaendelea kuwa ofisini bila ya kufunguliwa mashtaka ya wizi wa kuaminika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Kamil Sukum, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 Halmashauri ya Wilaya ya Hanang iliidhinishiwa shilingi 225,585,000 kwenye ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi kwa shule za bweni za Katesh, Balangdalalu, Bassodesh na Gendabi. Fedha zilizotolewa zilikuwa ni shilingi 508,779,500 zikiwa ni ziada ya shilingi 283,194,500. Fedha hizo hazikurejeshwa Hazina badala yake zilibadilishwa matumizi na kutumika kwa ajili ya vifaa vya shule na ukarabati wa shule hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizo zilizoombewa kibali cha kubadili matumizi ili zitumike kununua vifaa vya shule na ukarabati wa mabweni. Hata hivyo ni kweli maombi hayo hayakujadiliwa katika Kamati ya Fedha na Mipango na kwa mantiki hiyo utekelezaji wa jambo hilo ulikiuka misingi na utaratibu wa uendeshaji wa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na makosa hayo Mkurugenzi wa Halmashauri amesimamishwa kazi pamoja na Watumishi wengine wanne wakiwepo Afisa Mipango Wilaya, Mweka Hazina Wilaya na Wahasibu wawili ili kupisha uchunguzi. Aidha, Baraza la Madiwani limeelekeza fedha hizo zirejeshwe kupitia mapato ya ndani na tayari shilingi milioni 130 zimepelekwa kwenye akaunti ya vijiji vya Gendabi, Bassodesh, Katesh na Balangdalalu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Asilimia kumi ya bajeti ya Halmashauri nchini hutengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia fedha hizo zitolewe kwa kila Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyojibu hoja hii mara kadhaa hapa Bungeni, Serikali imejipanga kuhakikisha asilimia kumi ya fedha za vijana na wanawake zinatengwa na zinapelekwa kwa njia ya mikopo. Usimamizi wa suala hili uliwekewa mkazo katika mwongozo wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo Halmashauri zote zimetenga shilingi bilioni 56.8 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake kutokana na mapato ya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ili kuhakikisha fedha hizo zinatengwa na kupelekwa kwa vijana na wanawake. Maamuzi ya kutenga fedha hizi ni kadri ya makusanyo kila robo mwaka yanafanywa na Halmashauri kupitia Kamati ya Fedha na Mipango na Baraza la Madiwani.
Hivyo, naomba kutoa wito kwenu Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika kusimamia suala hili ambalo liko kwenye Halmashauri zetu ili kila tunapofanya maamuzi ya kugawa rasilimali fedha kutokana na mapato ya ndani, tuweke kipaumbele katika kutenga fedha hizo.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y. MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA) aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Ndembela Wilayani Rungwe awali ilijengwa kwa nguvu za wananchi na baadaye Kanisa la Waadventista Wasabato liliingia kama wabia na kuiendeleza na hatimaye kuiendesha shule hiyo ikiwa na majengo yaliyokamilika. Baada ya wananchi kuihitaji shule yao, Kanisa limekubali kuirejesha kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa fidia ya Sh.947,862,000/= Halmashauri imeomba Wizara ya Elimu isaidie kulipa fidia hiyo:-
Je, ni lini Serikali itasaidia kurejesha shule hiyo mikononi mwa wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, thamani halisi ya majengo ya Shule ya Sekondari Ndembela ni shilingi milioni 762 baada ya tathmini. Mwaka 2013, Kanisa la Waadventista Wasabato na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe walikubaliana mbele ya Mahakama kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ilipe fidia ya shilingi milioni 762 ikiwa ni thamani halisi ya maendelezo yaliyofanyika ili shule iweze kurejeshwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imeidhinishiwa shilingi milioni 190 kwa ajili ya kulipa sehemu ya deni hilo. Aidha, Halmashauri imewasilisha maombi maalum ya shilingi milioni 947.8 katika Mamlaka ya Elimu Tanzania yaani TEA kwa ajili ya kulipa fidia na ukarabati wa miundombinu ya shule.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. YOSEPHER F. KOMBA) aliuliza:-
Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza ilianzishwa miaka ya 1980 kwa ushirikiano kati ya Kanisa la Anglikana na Serikali imekuwa ikihudumia wagonjwa wengi ndani na nje ya Wilaya ya Muheza, hivyo kuzidiwa na uwezo wa kuhudumia na vifaa tiba:-
(a) Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali Teule gari la kubeba wagonjwa ili kuboresha huduma na kuokoa maisha ya Watanzania?
(b) Je, nini mkakati wa Serikali katika kumaliza changamoto ya Wahudumu wa Afya katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yosepher Ferdinand Komba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mipango na bajeti Halmashauri ina mpango wa kununua gari la wagonjwa aina ya Land Cruiser Hard Top kwa ajili ya Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza katika mwaka wa 2017/2018 lenye thamani ya shilingi milioni 200. Kwa sasa huduma za usafiri wa dharura (Rufaa) kwa wagonjwa zinatolewa kwa kutumia magari ya kawaida yaliyopo kwenye Halmashauri.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua changamoto ya Watumishi Hospitalini hapo, Halmashauri katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imeidhinishiwa kibali cha watumishi 133 wa kada mbalimbali za afya. Watumishi hawa watakapoajiriwa, baadhi yao watapangwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza ili kupunguza tatizo lililopo la uhaba wa watumishi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imepanga kuwaendeleza watumishi 24 ili wapate sifa na ujuzi unaotakiwa katika utoaji wa huduma za afya katika Hospitali hiyo.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE (K.n.y. MHE. SAUL H. AMON) aliuliza :-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya maji Mji Mdogo wa Tukuyu kwani hali ya maji ni mbaya sana na miundombinu iliyopo ni ya zamani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Rungwe Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tukuyu wenye wakazi wapatao 61,975 unapata maji kwa asilimia 40 ukilinganisha na mahitaji halisi. Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka katika chanzo cha Masoko wenye gharama za shilingi bilioni 4.7. Kazi zitakazotarajiwa kufanyika ni ujenzi wa vyanzo viwili vya Mbaka na Kigange kwa ajili ya kupeleka maji katika Mji wa Tukuyu pamoja na vijiji 15, ujenzi wa matanki manne (4), ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 13.6 na ujenzi wa vituo vya maji 125. Hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 1.7.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika Bajeti ya mwaka 2015/2016, imetumia shilingi milioni 144, kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya mradi wa maji kutoka katika chanzo cha mto Maswila ili kukidhi mahitaji ya maji kwa wakazi wa Mji wa Tukuyu. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi milioni 295.3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji katika Mji wa Tukuyu.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Bajeti ya mpango wa barabara inayopelekwa katika Halmashauri zetu ni ndogo na haikidhi mahitaji:-
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuongeza bajeti hiyo ili Halmashauri nchini ziweze kununua vifaa vya kutengenezea barabara zao za ndani ili kuondoa kero isiyokuwa ya lazima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za matengenezo ya barabara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hutengwa kulingana na Sheria ya Mfuko wa Barabara ikiwa ni asilimia 30 ya fedha za mfuko. Fedha za Mfuko zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 23.8 mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 249.8 mwaka 2016/2017. Hata hivyo, kulingana na mtandao wa barabara unaohudumiwa na mamlaka za Serikali za Mitaa, unaofikia kilomita 108,946 fedha hizo ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za Mfuko wa barabara zinahitajika kutumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara pekee. Aidha, Halmashauri zinaruhusiwa kukopa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo katika taasisi za kifedha na kurejesha mikopo hiyo kupitia makusanyo yake ya ndani. Hata hivyo, Halmashauri itatakiwa kwanza kupata kibali kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho la kudumu la matengenezo ya barabara zinazohudumiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kuanzisha wakala ambao utafanya kazi kama vile TANROADS inavyofanya. Tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaanda rasimu ya nyaraka muhimu ambazo zitaanzisha wakala huo
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Je, Shirika la UNHCR lina mpango wowote kwa usimamizi wa Serikali wa kujenga angalau wodi tatu za kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo ipo katika mazungumzo na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kuomba msaada wa kujengewa wodi ya wanawake katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Maombi hayo yaliwasilishwa na Halmashauri kupitia barua ya tarehe 30 Machi, 2016 yenye Kumb. Na. HW/A/D.30/22/Vol.1/23 na mazungumzo yanaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo imetenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa wodi moja katika hospitali hiyo ya Wilaya ya Kibondo.
MHE. ANTONY C. KOMU (K.n.y. MHE. RAPHAEL J. MICHAEL) aliuliza:-
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ilianza mchakato wa kuifanya Jiji tangu mwaka 2012 baada ya kupata baraka za Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro (RCC) na Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Moshi (DCC) na sasa mchakato huo umekamilika katika hatua zote za kikanuni.
Je, ni lini Serikali itatangaza Manispaa ya Moshi kuwa Jiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika vikao vyote vya kisheria vimekaa na kuridhia pendekezo la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Jiji. Hapo awali, maombi hayo yaliwasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya maamuzi. Hata hivyo, maombi hayo yaliyejeshwa ili yafanyiwe marekebisho kutokana na upungufu uliobainika kulingana na vigezo na taratibu zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa timu ya uhakiki kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ipo katika uhakiki wa maombi ya maeneo mapya ya utawala yakiwemo maeneo kutoka Manispaa ya Moshi ili kuhakiki vigezo vilivyozingatiwa katika kuanzisha maeneo hayo. Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo nchi nzima, Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa atashauriwa ipasavyo kuhusu maombi haya.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA (K.n.y. MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA) aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba in shule 39 za sekondari za kata na kati ya hizo, shule 31 hazina walimu wa vipindi muhimu na nyingine zina walimu wa ziada wasio na kazi; mfano shule 12 hazina walimu wa hesabu kabisa, shule tisa baiolojia, shule nane kemia, shule 18 walimu wa fizikia na shule 10 hazina kabisa walimu wa uraia.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na tatizo hilo na kuliondoa ili kuokoa kizazi cha vijana watakaoishi katika karne ya 21 bila kusoma masomo ya sayansi?
(b) Je, kuhusu walimu wa ziada takribani 213 wasiohitajika kwenye sekondari kwa sasa hivi, Serikali itaruhusu Halmashauri iwapange kufundisha kwenye shule za msingi ambapo kuna upungufu mkubwa kuliko kuingia gharama kuwahamisha na kuwarejesha tena wakihitajika kwa sababu shule za sekondari zinaendelea kupanuka?
(c) Je, Serikali itasaidiaje Halmashauri ya Muleba kutengeneza programu maalum ya mafunzo kwa walimu wa ziada kujifunza kufundisha masomo mengine ambayo walimu wake hawatoshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, Mbunge wa Muleba Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kuwapanga walimu wa sayansi moja kwa moja katika shule badala ya Halmashauri kama ilivyokuwa hapo awali ili kuleta uwiano sawa mashuleni. Vilevile Serikali imeandaa mkakati wa kuwaajiri wahitimu wa Shahada za Sayansi ambazo sio za Ualimu baada ya kuwapa mafunzo ya muda mfupi kuhusu mbinu za ufundishaji na maadili ya ualimu. Tayari kibali kimeombwa katika Ofisi ya Rais - Utumishi kwa ajili ya utekelezaji.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya tathmini ya mahitaji ya Walimu wa masomo ya sanaa kwa kila Halmashauri ili kubaini maeneo yenye ziada na yenye upungufu ili kusawazisha ikama. Mpango wa Serikali uliopo ni kuwahamisha Walimu wa ziada wa masomo ya sanaa kwenda kufundisha katika shule za msingi ndani ya Halmashauri husika. Kabla ya kuanza utekelezaji wa mabadiliko haya, Serikali itatoa waraka maalum kwenda katika Halmashauri zote.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, katika utaratibu wa mafunzo ya walimu, Halmashauri moja haiwezi kuwa na mfumo wa pekee wa wa kuandaa walimu kwa sababu ni vigumu kudhibiti ubora wa mafunzo hayo kwa walimu. Pamoja na nia nzuri, lakini ni vigumu kwa walimu hao wa ziada ambao ni wa masomo ya sanaa, mfano ni wa Kiswahili, Kiingereza au Uraia kupewa mafunzo maalum kufundisha masomo ya Hisabati, Kemia au Fizikia kwa sababu wengi hawana kabisa msingi wa uelewa wa masomo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kuongeza udahili wa walimu wa sayansi katika vituo vya ualimu kadiri iwezekanavyo ili kukidhi mahitaji. Mpango wa muda mfupi ni kuwatumia wahitimu wa shahada za masomo ya sayansi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi kama ilivyoelezwa katika sehemu (a) ya jibu langu. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) aliuliza:-
Kumekuwa na hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na
mgambo na askari polisi wanapotekeleza maagizo ya Serikali dhidi ya wafanyabiashara wadogo wadogo hususan mama lishe, bodaboda pamoja na machinga. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge
wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mgambo wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria
ya polisi wasaidizi ya mwaka 1969 kwa kuzingatia sheria hiyo, Halmashauri
zimeruhusiwa kuajiri askari ngambo kwa ajili ya kusaidia usimamizi wa Sheria
Ndogondogo za Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, askari mgambo anayefanya kazi katika
Halmashauri anawajibika kuzingatia sheria za nchi pamoja na sheria ndogo
ndogo zilizotungwa na Halmashauri. Jukumu lao kubwa ni kulinda mali za
umma, kulinda usalama wa wananchi pamoja na kutekeleza maelekezo
yatakayotolewa na Halmashauri kwa wakati wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgambo hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria
kuchukua au kuharibu mali za wananchi. Kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria
za Serikali, na Serikali haitasita kuchuakua hatua kwa vitendo hivyo. Aidha,
naomba kutumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri zote kutenga maeneo
maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili biashara hizo zifanyike katika
maeneo yaliyotengwa rasmi na kuacha kufanya shughuli hizo katika hifadhi za
barabara na maeneo mengine yasiyoruhusiwa.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya M. Kikwete aliahidi kujenga barabara za Mji wa Maswa zenye urefu wa kilometa tatu ndani ya Halmashauri ya Mji Mdogo wa Maswa.
Je, ni lini barabara hizo zitaanzwa kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne kuhusu ujenzi wa barabara kilometa tatu kwa kiwango cha lami imeanza kutekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambapo katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 20 kwa ajili ya kazi ya usanifu wa kina (detailed design).
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo itawezesha kujulikana kwa gharama za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Hivyo, Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina na bajeti kutengwa kwa kazi hiyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha ahadi hii inatekelezwa pamoja na ahadi nyingine zilizotolewa na viongozi kwa manufaa ya wananchi wetu.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. MENDRAD L. KIGOLA) aliuliza:-
Mradi wa maji katika Kata ya Mtwango umechukua muda mrefu bila kukamilika na wananchi wanaendelea kupata shida ya maji:-
Je, ni lini mradi huo utakamilika na kukabidhiwa kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa maji katika Kata ya Mtwango ulianza rasmi mwezi Juni, 2015. Mradi huo katika bajeti ya mwaka 2015/2016 ulitengewa shilingi milioni 488.8 ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia 60%.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukamilisha mradi huo katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imetengewa shilingi milioni 643.5 kwa ajili ya kazi zilizobaki, ili mradi huo uanze kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Kamati za Fedha za Mipango za Halmashauri za Wilaya ni Kamati muhimu sana kwa Wabunge wote kushiriki bila kujali ni wa Viti Maalum au wa Jimbo kwa sababu zinashughulika na masuala ya fedha, bajeti na mipango ya miradi ya maendeleo; na kwa muda mrefu sasa Wabunge wa Viti Maalum wamekuwa wakiomba kuondolewa kwa sheria kandamizi na ya kibaguzi ya kuwazuia kushiriki katika Kamati hizo:-
(a) Je, Serikali iko tayari kusikiliza kilio cha Wabunge wa Viti Maalum ili kuwaruhusu kushiriki kwenye Kamati hizo?
(b) Je, Serikali iko tayari kufuta sheria hiyo kandamizi na yenye ubaguzi ambayo haina tija na hasa ikizingatiwa kuwa ilitungwa mwaka 1998 wakati ambao Ubunge wa Viti Maalum bado haujaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Halmashauri wametajwa katika kifungu cha 75(6) cha Sheria, Sura 287 ya Mamlaka za Serikali za Wilaya na kifungu cha 47(4) cha Sheria Sura 288 ya Mamlaka za Miji. Kwa mujibu wa sheria hizo mbili, Wajumbe wa Kamati hawatazidi theluthi moja (1/3) ya Madiwani wote isipokuwa Kamati ya Fedha na Mipango ambayo Wajumbe wake ni wale wanaoingia kwa nyadhifa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango umefafanuliwa katika Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa kila Halmashauri ambapo Wajumbe wake ni Mwenyekiti au Meya wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Naibu Meya wa Halmashauri, Mbunge au Wabunge wa Majimbo wanaowakilisha majimbo katika eneo la Halmashauri, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri na Wajumbe wengine wasiozidi wawili watakaopendekezwa na Mwenyekiti/Meya kisha kupigiwa kura na Baraza la Halmashauri mmoja kati yao awe mwanaume au mwanamke. Hivyo, ili Wabunge wa Viti Maalum waweze kushiriki kwenye Kamati za Fedha tutahitaji kubadili sheria kwanza ili pendekezo hilo liweze kutekelezeka.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika sehemu (a) ya jibu hili, Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango wataendelea kuwa ni wale waliotajwa katika Sheria na Kanuni za Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi hapo sheria itakapofanyiwa marekebisho kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Kutoka Kijiji cha Mutelewele kwenda Makambako ni kilometa tano wakati kwenda Halmashauri ya Wanging‘ombe ni kilometa 65; kutoka Kata ya Soja kuja Makambako Mjini ni kilometa 25 na kwenda Halmashauri yao ya Wanging‘ombe ni kilometa 88 na kutoka Kijiji cha Nyigo kuja Makambako ni kilometa 8 wakati kwenda Halmashauri ya Mufindi ni kilometa 88 na huduma zote zikiwemo matibabu wanazipata Makambako; kutoka Kijiji cha Igongolo ni umbali wa kilometa 6 kwenda Makambako wakati kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni kilometa 54.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kugawa mipaka upya ili wananchi wapate huduma karibu na Halmashauri yao ili iendane na kauli mbiu ya kusogeza huduma karibu na wananchi?
(b) Je, ni lini sasa Serikali itapima upya mipaka hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, Vijiji vya Mutewele na Saja viko katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging‘ombe na Kijiji cha Nyigo kiko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa vijiji hivyo kijiografia viko karibu na Halmashauri ya Mji wa Makambako kwa maana ya huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia njema ya Mheshimiwa Mbunge ya kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi vipo vigezo na taratibu zinazozingatiwa katika kusajili au kubadili mipaka ya vijiji. Mapendekezo haya yanapaswa kujadiliwa kwanza katika Mikutano Mikuu ya Vijiji, Kamati za Maendeleo ya Kata, Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri zote, Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC) na Kamati za Ushauri za Mikoa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mabadiliko ya mipaka hiyo yataathiri mipaka ya utawala ya Mikoa ya Iringa na Njombe ambapo lazima wadau wa pande zote wakubaliane kuhusu maamuzi hayo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, napendekeza haya yapitishwe kwanza kwenye vikao vilivyotajwa na endapo vitaridhiwa, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itayafanyia kazi mapendekezo hayo sambamba na maombi yaliyowasilishwa kutoka maeneo mengine.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikwishaanza kujenga vituo vya afya katika vijiji vya Mima na Mbori na ujenzi huo umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya Mima ulianza mwaka 2008/2009 ambapo mpaka sasa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 60. Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) liko katika hatua ya umaliziaji. Kazi ambazo hazijakamilika ni uwekaji wa dari, samani pamoja na vifaa tiba. Ili kumaliza kazi hiyo zimetengwa shilingi milioni 15 katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Aidha, imejengwa nyumba ya watumishi ambayo imekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 48.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya Mbori ulianza katika mwaka wa fedha 2011/2012 ambapo mpaka sasa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 82. Kazi zilizofanyika ni upauaji, upakaji rangi nje na ndani, uwekaji wa madirisha ya vioo pamoja na kupiga dari. Kazi zilizobaki ni pamoja na ufungaji wa umeme, ufungaji wa milango ya ndani 16, ufungaji wa taa na uwekaji wa mfumo wa maji safi na taka. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, kituo hiki kilitengewa shilingi milioni 15 ili kumalizia kazi zilizobaki na shilingi milioni 35 zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 ili kujenga nyumba ya watumishi (two in one).
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Wilaya ya Nyang’hwale ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ili kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuwezesha kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya eneo la Karumwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Halmashauri mpya ya Nyang’hwale ilipokea shilingi milioni 450 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi katka Makao Makuu ya Wilaya iliyoko Karumwa. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 177.7 zimetumika kumlipa Mtaalam Mshauri ambaye ni BJ Amili Limited kwa ajili ya kuandaa michoro, upembuzi yakinifu na usanifu wa eneo lote zinalojengwa ofisi. Kiasi kilichobaki kinajumuishwa katika fedha zilizoombwa mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri hiyo imetengewa shilingi milioni 850 kwa ajili ya kuendela na ujenzi majengo ya Makao Makuu ya Halmashauri katika eneo la Karumwa. Azma ya Serikali ni kuhakikisha ofisi na nyumba za watumishi zinajenwa katika Wilaya na Mikoa mipya kwa awamu ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. SUSANNE P. MASELLE) aliuliza:-
Mwaka 2007 Serikali ilipima viwanja vya Luchelele Wilayani Nyamagana, Mwanza na iliendelea na mpango huo ambapo mwaka 2012 ilifanya tathmini na uhakiki kwa ajili ya kulipa fidia lakini hadi leo wananchi hao hawajawahi kulipwa fidia zao.
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi hao wa Luchelele kuhusu hatma yao hasa ikizingatiwa kuwa Waziri wa Ardhi alitoa ahadi mwaka 2015 kuwa atalitatua tatizo hili ndani ya mwezi mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Luchelele lilipimwa mwaka 2008 likiwa na ukubwa wa hekta 873.38 ambapo viwanja vilivyopimwa ni 3,583. Katika zoezi hilo wapo wananchi waliokuwa ni wamiliki wa asili wa eneo hilo wapatao 683 ambao kwa makubaliano maalum yaliyofanyika tarehe 27/01/2013 chini ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, wamemilikishwa viwanja badala ya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaodai fidia katika eneo la Luchelele ni wale ambao walikutwa katika maeneo yao lakini baada ya upimaji, maeneo hayo ni kwa ajili ya Taasisi au barabara na idadi yao ni 671. Wananachi hao wanadai fidia ya shilingi bilioni sita. Kauli ya Serikali ni kwamba wananchi hao watalipwa fidia na tayari Halmashauri imeomba mkopo kutoka Benki ya CRDB ambao wamekubali kutoa mkopo huo ili wananchi hao waweze kulipwa fidia
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-
Katika miaka ya 1990, Wilaya ya Iringa Vijijini kulikuwa na mradi wa usambazaji wa maji kwa kutumia chanzo cha maji ya Mto Mtitu ili kuondokana na adha ya maji inayowakumba wananchi wa Iringa Vijijini; juhudi za kufanya upembuzi yakinifu zilifanyika ili kuweza kusambaza maji kwa gravity kwenye vijiji vyote vya Kata za Maguliwa, Luhota, Mseke, Ifunda, Mgama na Maboga:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha mradi huu ili kuweza kuondoa tatizo la maji kwa wananchi wa Kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, imepanga kufanya usanifu wa kina wa mradi mkubwa wa maji ambao utahusisha vijiji vya Kata za Ngawila, Luhota, Mseke, Ifunda, Mgama na Lugonga. Lengo ni kubaini uwezo wa chanzo cha Mto Mtitu katika kuhudumia maeneo hayo yote. Kazi hiyo imepangwa kufanyika katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo zimetengwa Shilingi milioni 49.5. Mradi huo utakapokamilika, jumla ya vijiji 17 vyenye wakazi wapatao 36,397 vitanufaika.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kuwepo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nchini kumekuwa kukileta migongano katika utekelezaji wa sera na shughuli mbalimbali za maendeleo nchini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuupitia upya mfumo wa ugatuaji wa madaraka (D by D) ili kuweza kuuboresha na kupunguza migongano mbalimbali ya kiutendaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa wapo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 61(1) mpaka (5) na majukumu yake yamefafanuliwa vizuri katika Ibara ya 61(4) kwamba atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (Decentralization by Devolution) pia inatokana na Ibara ya 145 na 146. Madhumuni yake ni kupeleka madaraka kwa wananchi yakiwemo madaraka ya kisiasa, kifedha, kiutawala ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ni wasimamizi wa sera, sheria, kanuni na miongozo katika Mikoa na Wilaya wanayoongoza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Viongozi hao kisheria hawaruhusiwi kuingilia (interference) maamuzi na utendaji wa Serikali za Mitaa endapo hakuna sheria au taratibu zilizokiukwa kimaamuzi. Hata hivyo, wamepewa mamlaka na sheria kuingilia kati (interventions) endapo maamuzi yatakayofanywa na Serikali za Mitaa yatakiuka sera, sheria na miongozo iliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa yamebadilika kutoka kwenye dhana ya utoaji amri na upokeaji amri au mdhibiti na mdhibitiwa, kuwa ya mashauriano, majadiliano na maelewano. Vilevile, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeendelea kufanya vikao vya pamoja na Wizara za Kisekta ili kuwa na uelewa wa pamoja wa dhana ya ugatuaji na mantiki yake katika kusogeza karibu huduma kwa wananchi.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Wilaya ya Mbinga imebahatika kupata mradi wa kujenga barabara ya lami toka Kijiji cha Longa hadi Kijiji cha Litoha kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya na mradi huo umeshaanza kutekelezwa:-
(a) Je, ujenzi wa mradi huo unategemewa kukamilika lini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia wananchi waliotoa mashamba na nyumba zao kupisha ujenzi wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Alexander Mtonda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa ujenzi wa barabara awamu ya kwanza kutoka Longa hadi Bagamoyo ulianza tarehe 1/10/2015 na unategemewa kukamilika tarehe 30/6/2016. Hata hivyo, kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Wilaya ya Mbinga, Mkandarasi alishindwa kufanya kazi kama ilivyokuwa imepangwa hali iliyolazimu kuongeza muda hadi tarehe 30/9/2016. Sehemu ya pili inaanzia Kijiji cha Bagamoyo hadi Kijiji cha Lutoho chini ya Mkandarasi GS Contractors Limited ambaye mkataba wake ulianza tarehe 1/5/2016 na unategemewa kumalizika tarehe 30/1/2017.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, sharti lilitolewa na Umoja wa Ulaya ili waweze kujengewa barabara ya lami kutoka Longa hadi Bagamoyo lilikuwa ni kutokuwepo kwa fidia. Halmashauri kwa maana ya Madiwani walifanya uhamasishaji wa kutoa elimu kwa wananchi ili kukubali mradi huo na wote waliridhia ndiyo maana barabara hiyo imeanza kujengwa. Serikali inawapongeza viongozi wa Halmashauri na wananchi kwa ujumla kwa kukubali kuupokea mradi huo kwa ustawi wa uchumi wa maendeleo ambayo ni uzalishaji mkubwa wa kahawa.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Upanuzi wa hospitali ya Mkoa ya Pwani ijulikanayo kama Hospitali ya Tumbi umesimama kwa takribani miaka mitatu, sasa nondo na zege la msingi na nguzo zinaoza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ili kuondoa hasara na kuleta tija katika huduma ya afya Kibaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto zinazoikabili hospitali ya rufaa ya Tumbi – Kibaha ambazo zimesababishwa kwa sehemu kubwa na ufinyu wa majengo ya kutolea huduma na uchache wa vifaa tiba. Hadi sasa Serikali imetumia shilingi bilioni 5.98 kwa ajili ya upanuzi wa hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kuendeleza upanuzi wa hospitali ya Tumbi Kibaha ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y MHE. TUNZA I. MALAPO) aliuliza:-
Dhana ya elimu ni majumuisho ya mambo mengi sana ikiwemo matibabu ya huduma ya kwanza, gharama za umeme, maji, vyakula (kwa shule za bweni), posho za walimu (part time) pamoja na zana za kufundishia zisizohifadhika kwa muda mrefu; na nyingi kati ya gharama hizo zilikuwa zinatatuliwa mashuleni na Wakuu wa Shule kwa kutumia ada na michango waliyokuwa wanatoza wanafunzi.
Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha ufanikishwaji wa dhana hii ya elimu bure bila kuanzisha migogoro mipya kati ya wakuu wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya utoaji wa elimu bila malipo inatokana na Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inayoelekeza utaratibu wa ugharamiaji wa elimu ya awali kuwa ya lazima kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu msingi bila malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi. Hata hivyo, elimu bila malipo haiondoi dhamira ya uzalendo kwa jamii ya kushiriki kwa hiari kuchangia kwa hali na mali katika kuleta maendeleo ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kupeleka shilingi bilioni 18.777 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia mpango huu. Fedha hizo zinatumika kugharamia mitihani ya Taifa, chakula cha wanafunzi wa bweni, ada ya mwanafunzi kwa shule za kutwa na bweni na fedha za uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga ili kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu bila malipo ambao umeshaanza kwa shule zote za umma nchini hausababishi migogoro kati ya wakuu wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi. Ili kuhakikisha hilo halitokei Serikali imetoa miongozo mbalimbali katika mikoa yote inayofafanua kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
MHE. HUSSEIN M. BASHE (K.n.y MHE SELEMANI J. ZEDI) aliuliza:-
Ujenzi wa vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya vya Bukene na Itobo umekamilika na kwamba vifaa vyote kwa ajili ya kutoa huduma ya upasuaji vimeshafunguliwa ikiwa ni pamoja na vifaa vya kuhifadhia damu na mashine za kufulia. Je, ni jambo gani linazuia huduma za upasuaji kuanza katika vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vituo vya afya vya Itobo na Bukene vimepata vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya upasuaji ambavyo vimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachokwamisha shughuli za upasuaji kuendelea katika kituo cha afya cha Itobo ni kukosekana kwa Mtaalam wa usingizi baada ya aliyekuwepo kusimamishwa kazi kwa tuhuma za rushwa. Mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri umepanga kumhamisha Mtaalam huyo kutoka sehemu nyingine ili huduma za upasuaji ziweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kituo cha Bukene mbali na mtaalam wa usingizi, kinachokwamisha ni ukosefu wa maji ya uhakika na tayari Halmashauri inafanya marekebisho hayo. Halmashauri imetakiwa kuhakikisha upungufu huo unaondolewa mapema ili huduma hizo muhimu zianze kutolewa na kuwaondolea adha wagonjwa kufuata huduma hiyo Nzega Mjini.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA (K.n.y MHE. RAPHAEL J. MICHAEL) aliuliza:-
Hospitali ya Mawenzi ambayo ni ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uchakavu wa miundombinu yake, samani, mlundikano mkubwa wa wagonjwa kwa sababu Manispaa ya Moshi haina Hospitali ya Wilaya, upungufu wa Madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya:-
(a) Je, ni lini hospitali hiyo itafanyiwa ukarabati ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuiongezea watumishi niliowataja?
(b) Je, ni lini Serikali itakubali ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi la kujenga Hospitali ya Wilaya?
(c) Je, Serikali itasaidiaje Hospitali ya Mawenzi iweze kupata mkopo kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili iweze kuboresha miundombinu yake?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mkoa umejiwekea utaratibu wa kufanya ukarabati wa Hospitali ya Mkoa kupitia fedha za uchangiaji wa gharama za matibabu. Hadi sasa zimeshatumika Sh. 14,700,000/= kwa ajili ya ukarabati wa mfumo wa maji, jengo la wagonjwa wa nje pamoja na jengo la Madaktari waliopo mafunzoni (intern doctors). Mkakati uliowekwa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili kujenga uwezo wa kuihudumia hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la watumishi, hospitali hiyo imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya 79, katika mwaka wa fedha 2015/2016 na watumishi 65 wamepangwa kuajiriwa katika mwaka ujao wa 2016/2017 ili kukabiliana na upungufu huo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wilaya ya Moshi imeingia ubia wa utoaji huduma na Hospitali ya Mtakatifu Joseph (DDH) ambayo itatumika kama Hospitali ya Wilaya. Ili kuendelea kuboresha huduma za afya, Halmashauri imeamua kukiboresha Kituo cha Afya cha Msaranga ili kukiongezea uwezo wa kutoa huduma zenye hadhi ya hospitali.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ya Mawenzi unafanyika, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.35 katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, kuhusu suala la mkopo kutoka TIB, Mkoa unashauriwa kukamilisha mazungumzo yanayoendelea na yatakapowasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutatoa ushirikiano baada ya kuridhishwa kama mkopo huo umekidhi vigezo vinavyozingatiwa katika tathmini ya mikopo ya aina hii.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wanawake katika Mkoa wa Simiyu wamehamasika sana kujiunga kwenye vikundi ili kukusanya nguvu za kiuchumi kwa lengo la kujiendeleza kiuchumi zaidi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wanawake hawa mafunzo ya kimtaji ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiwawezesha kiuchumi wanawake kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao kila Halmashauri inatakiwa kutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Mkoa wa Simiyu ulitoa mikopo kwa wanawake na vijana yenye thamani ya shilingi milioni 116.5 ambapo kati ya hizo wanawake walikopeshwa shilingi milioni 75.7 kwa vikundi vipatavyo 74. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Mkoa wa Simiyu umetenga shilingi milioni 978.08 kwa ajili ya vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zote zimeelekezwa kulipa madeni ya fedha ambazo hazikupelekwa kwenye Mifuko ya Vijana na Wanawake kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Hazina iliweka kigezo kwa kila Halmashauri kuonesha fedha zilizotengwa kwa ajili ya vijana na wanawake kabla ya kupitisha bajeti yake na Halmashauri zote zimetenga fedha hizo jumla ya shilingi bilioni 56.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mafunzo, Halmashauri kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii zimeendelea kutoa elimu ya masuala ya biashara na ujasiriamali kwa vikundi vya wanawake na vijana kabla na baada ya kupata mikopo ili kuhakikisha kwamba mikopo inayotolewa inatumika na kusimamiwa ipasavyo. Katika utekelezaji wa jukumu hili, Serikali inashirikiana na sekta binafsi zikiwemo asasi za kiraia.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Halmashauri ya Itilima ni mpya iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria, lakini mpaka sasa hivi haijapata fedha za kutosha kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia Halmashauri hiyo fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016 Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ilikuwa imepokea shilingi bilioni 5.04 kati ya shilingi bilioni 8.2 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwa ni asilimia 61.5 ya bajeti yote ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri hiyo imetengewa shilingi bilioni 10.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo sawa na ongezeko la asilimia 26.8 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016. Upelekaji wa fedha katika Halmashauri za Serikali za Mitaa hufanywa kwa kuzingatia hali ya makusanyo ya Serikali kila mwezi. Hivyo, naomba kutoa wito kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuweka mkazo katika kuimarisha makusanyo ya kodi na ushuru mbalimbali ili kujenga uwezo wa Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Ukosefu wa nyumba za walimu katika maeneo ya vijijini unasababisha Walimu kuhama maeneo hayo na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa Walimu, pia Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kujenga nyumba za Walimu za kutosha kwa kutumia fedha zao za ndani.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga nyumba za Walimu wa shule za msingi vijijini hasa ikizingatia kuwa vijijini hakuna nyumba ambazo Walimu wanaweza kupanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi Mbunge wa Jimbo la Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa nyumba za Walimu kupitia bajeti zilizotengwa katika kila mwaka. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 1,157 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 11.1 zimetengwa kujenga nyumba 661 kwa shule za sekondari nchini. Aidha, kupitia mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II), Serikali imepanga kujenga nyumba za Walimu 183 katika shule za sekondari kwenye Halmashauri mbalimbali zenye uwezo wa kuchukua familia sita kwa kila nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetengewa shilingi milioni 486.3 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu kwa shule za msingi na sekondari.
MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y. MHE ANTONY C. KOMU) aliuliza:-
Tarehe 13/8/2012 Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ilitangaza zabuni Tenda Na. LGA/046/2011/2012/RWSSP/1 katika gazeti la Mwananchi. Tenda hiyo ilihusu mradi wa mfumo wa kusambaza maji na ungehusisha Vijiji vya Mande na Tella katika Kata ya Oldmoshi Magharibi. Hadi sasa mradi huo haujaanza pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa Diwani na Kamati za Maji za Vijiji vya Tella na Mande hawakufanikiwa kupata majibu juu ya mradi tajwa.
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga mradi huo muhimu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antony Calist Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ilitangaza zabuni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa mitatu ya maji yaani Korini, Bori na Tella-Mande ambapo Kampuni ya Jandu Plumbers Limited ya Arusha ilipata Zabuni hiyo. Kulingana na upatikanaji wa fedha, kipaumbele kiliwekwa kuanzia utekelezaji wa mradi wa Korini na Bori ambayo imekamilika. Mradi wa Korini umegharimu shilingi bilioni 1.2 na umekamilika mwaka 2014 na mradi wa Bori umekamilika mwezi Juni, 2016 na kuzinduliwa na mbio na Mwenge.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa Tella na Mande umepangwa kuaanza mwaka 2016/2017 baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa miwili ya Korini na Bori. Mradi huo umetengewa shilingi milioni 759.4 kwa ajili ya kuimarisha chanzo cha Masokeni pamoja na miundombinu mingine ya kusambaza maji kuwafikia wananchi.
MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:-
Mji wa Sirari unakua kwa kasi kubwa sana kutokana na kuwa na mapato mengi yatokanayo na ushuru wa forodha na bandari kavu. Hata hivyo Mji huo una tatizo la ujenzi holela kutokana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kukosa fedha za kupanga mji na kulipa fidia stahiki kwa wananchi wanaotakiwa kuhamishwa:-
Je, Serikali itatoa lini fedha za fidia ili kazi ya ujenzi wa Mpango wa Mji huo ifanyike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Wegesa Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Sirari ni miongoni mwa Miji midogo inayokua kwa kasi nchini Tanzania kutokana na fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Kenya pamoja na uwepo wa bandari kavu katika eneo hilo la mpakani. Mji wa Sirari umetangazwa kuwa eneo la mpango yaani Planning Area kwa tangazo la Serikali Na. 176 la tarehe 9 Agosti, 1996.
Mheshimiwa Naibu Spika, upimaji wa makazi wa Sirari unafanyika kwa njia shirikishi ambapo wananchi wenyewe kwa kushirikiana na wataalam wataamua kuhusu upimaji wa mji huo yaani informal settlement upgrading. Hivyo, hakuna fedha zilizotengwa kulipa fidia kwa sababu hakuna wananchi watakaohamishwa katika zoezi hili ili kuboresha Mji. Wakazi wachache ambao watapisha maeneo ya umma kama barabara na huduma za jamii kwa makubaliano yao watapatiwa viwanja mbadala katika maeneo ya Lemangwe, Ng’ereng’ere na Gwitiri ambako vitapimwa viwanja 2,644.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Igoma – Kishiri – Kanindo kupitia Kata za Lwanhima na Bulongwa.
Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Igoma – Kishiri – Kanindo ina urefu wa kilometa 15 ikiwa ni mzunguko kupitia Kata za Igoma, Lwanhima na Buhongwa katika Jiji la Mwanza. Ili kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali katika bajeti ijayo ya mwaka 2017/2018 ikiwa ni hatua muhimu katika kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo itawezesha Serikali kujua gharama za mradi na kutenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Vijiji vya Iyoma, Kisokwe, Idilo, Lukole, Lupeta, Bumila, Makutupa, Mkanana, Igoji Kaskazini (Isalaza), Nana, Kisisi, Ngalamilo, Godegoge, Mzogole, Mugoma, Kiegea, Kazania, Igoji Kusini, Chamanda, Simai, Makawila, Iwondo, Lupeta, Gulwe, Majami, Mwenzele na Mlembule katika Wilaya ya Mpwapwa vina matatizo makubwa sana ya maji na hivyo kusababisha wananchi wa vijiji hivyo kutembea umbali wa zaidi ya kilometa tano hadi kumi kutafuta maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima vya maji katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.58 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Kazi zitakazofanyika ni uchimbaji wa visima pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya maji iliyopo. Vijiji vilivyopo katika mpango ni Iyoma, Mzase, Mima, Bumila, Lukole, Kingiti, Kibakwe, Mbori, Mbuga, Iguluwi, Chogola, Kidenge, Iramba, Mlunduzi na Seluka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zinazoendelea kwa sasa katika uboreshaji wa huduma ya maji ni utafiti wa maji ardhini na uchimbaji visima virefu katika vijiji vya Mima, Mzase, Bumila na Iyoma. Uchimbaji wa visima virefu katika kijiji vya Mima na Mzase umekamilika. Kazi ya kuchimba visima virefu katika kijiji vya Bumila na Iyoma unaendelea na utakamilika mapema Novemba, 2016.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Kituo cha afya kilichopo Laela kinategemewa na Kata za Lusaka, Kasanzama, Laela, Mnokola, Miangalua na Kaoze; kutokana na kupanuka kwa kasi kwa mji huo na ongezeko la watu wanaohudumiwa katika kituo hicho, kimesababisha upungufu wa dawa, wataalamu na vifaa tiba.
(a) Je, ni lini Serikali itakipa kituo hicho hadhi ya Hospitali ya Wilaya?
(b) Je, ni lini kituo hicho kitapatiwa gari la wagonjwa?
(c) Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam wa kutosha, vifaa tiba na dawa za kutosha katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Kituo cha Afya Laela hakina miundombinu inayokidhi sifa za kuwa hospitali, kazi inayofanyika kwa sasa ni upanuzi wa miundombinu ya kituo hicho ambapo tayari jengo la upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito limekamilika pamoja na wodi ya mama wajawazito na wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji. Aidha, mpango wa muda mrefu katika eneo hilo ni kujenga Hospitali ya Wilaya kukidhi mahitaji ya matibabu kwa wagonjwa wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za rufaa kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika kituo hicho kwa sasa zinatolewa kupitia magari ya kawaida ya Halmashauri kutokana na ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa. Ni matarajio ya Wizara kwamba Halmashauri itaweka kipaumbele katika kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi wa gari la wagonjwa.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa watumishi katika Kituo cha Afya Laela ni tisa kati ya 45 wanaohitajika. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imepewa kibali cha kuajiri watumishi wapya wapatao 42 ambapo baadhi yao watapelekwa kituoni hapo. Kuhusu dawa na vifaa tiba, kituo kimetengewa bajeti ya shilingi bilioni 9.3 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza maji katika Kata za Kasamwa, Shiloleli, Bulela, Nyarugusu, Bukeli na maeneo mengine ya Wilaya ya Geita na Mkoa wa Geita kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Geita kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imepanga kutumia shilingi milioni 593.14 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji katika Kata za Kasamwa, Shiloleli, Bulela, Nyarugusu na Bukolina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kutumia chemchemi ya Mawemeru katika Kata ya Nyarugusu; uchimbaji wa visima virefu katika Kata ya Bulela na Shiloleli na kuboresha miundombinu ya maji iliyopo katika kata ya Kasamwa na Kanyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa mzima wa Geita Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ambazo zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Fedha hizo zitatumika kujenga miradi ya maji 22 ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
MHE. JUMA H. AWESO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Pangani ina uhitaji wa X-Ray ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi ambao hutembea mwendo mrefu kufuata huduma hiyo Tanga Mjini:-
Je, ni lini Serikali itapeleka X-Ray katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani imeomba mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 70 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya ununuzi wa X-Ray mpya katika Mwaka wa Fedha 2016/2017. X-Ray iliyopo ni chakavu kiasi cha kuhitaji matengenezo kila baada ya miezi mitatu kupitia wakala wake wa Philips. Kwa sasa wagonjwa wanapata huduma ya X-Ray kupitia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri imefanya mawasiliano na NHIF kwa ajili ya kupata mkopo huo na mazungumzo yanaendelea. Aidha, Halmashauri zinashauriwa kuweka kipaumbele katika kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa X-Ray kutokana na umuhimu wake kwa afya za wananchi.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Bukoba Vijijini kuna Shule za Sekondari za Serikali na za Wananchi zipatazo 29 ambazo zinaishia Kidato cha nne na moja kati ya hizo ina Kidato cha tano na sita hali, inayosababisha wahitimu wengi wanaomaliza Kidato cha nne wakiwa na sifa za kuingia Kidato cha tano kukosa nafasi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga madarasa na miundombinu inayofaa kwa Kidato cha tano na sita kwenye baadhi ya shule zilizopo ili kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba inaendelea na upanuzi wa miundombinu ya shule mbili za Lubale na Lyamahoro ili ziweze kuwa na sifa na vigezo kuwa Shule za Kidato cha tano na sita ifikapo Juni, 2017. Serikali imepanga kutumia fedha za Performance for Results (P4R) kukamilisha miundombinu katika shule hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na angalau shule moja ya kidato cha tano na sita. Vileile kila Tarafa iwe na shule moja ya kidato cha tano na sita. Shule hizi ni za Kitaifa ambazo huchukua wanafunzi waliohitimu na kufaulu kidato cha nne katika mikoa yote.
MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-
Majibu ya Serikali ya Swali Na.1 la tarehe 6 Septemba, 2016 yanapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli aliyoitoa wakati akiwa kwenye kampeni katika Jimbo la Solwa:-
(a) Je, kwa nini Serikali inapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa ahadi zote za Mheshimiwa Rais unafanyika kupitia mpango wa bajeti iliyotengwa kila mwaka. Hivyo, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali haipingani na agizo la Mheshimiwa Rais na kwamba Hospitali hiyo itajengwa kama agizo lilivyotolewa. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kuhakikisha ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika jibu la msingi la Swali Na.1 la tarehe 9 Septemba, 2016, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakamilisha ujenzi wa Hospitali ile, ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 40 kutokana na ukomo wa bajeti kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kutekeleza ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais ndani ya kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani, ambapo tunatarajia kuongeza nguvu ya kibajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Mwanza alipiga marufuku na kuziagiza mamlaka zinazohusika kuacha kuwasumbua wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama Wamachinga:-
Je, Serikali inatekeleza agizo hilo kwa kiwango gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mantiki ya agizo la Mheshimiwa Rais akiwa Mwanza ilikuwa ni kutowahamisha wafanyabiashara wadogo katika maeneo walipo endapo hakuna maeneo mbadala yaliyotengwa kwa ajili ya biashara zao. Mikoa na Halmashauri zimeendelea kutimiza malengo ya kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wadogo kwa kutenga maeneo rasmi ya kufanyia biashara na kuboresha yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yaliyotengwa rasmi kwa wafanyabiashara wadogo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara ni Likonde, Mbae na Mjimwema. Vilevile, Halmashauri inaboresha Soko la Skoya ambalo halitumiki kwa muda mrefu kutokana na kujaa maji wakati wa mvua. Kazi zinazofanyika ni kurekebisha mitaro ya kupitisha maji ili eneo hilo liweze kutumika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo kutokana na umuhimu wao katika kukuza kipato na ajira. Aidha, wafanyabiashara wadogo wanatakiwa kuzingatia sheria na kuhakikisha wanaendesha biashara katika maeneo yaliyotengwa rasmi ili kuepuka usumbufu.
MHE. DEOGRATIUS F. NGALAWA aliuliza:-
Pamoja na kwamba Jimbo la Ludewa lina vyanzo vingi vya maji, lakini kuna matatizo makubwa sana ya maji na wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kusaidia tatizo hili lakini Serikali na Halmashauri zimekuwa hazitoi ushirikiano kwa kurudi nyuma katika kuchangia sehemu yao kwa kigezo cha kutokuwa na fedha. Mfano vijiji vya Maholongwa, Mlangali, Mavanga, Manda, Nkomang’ombe na Lwela.
(a) Je, Serikali iko tayari kuweka kipaumbele katika kusaidia pale inapohitajika kuchangia?
(b) Je, nini kauli ya Serikali katika kushughulikia tatizo la maji Jimboni Ludewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deogratius Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa njia shirikishi yaani Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi kupitia mpango wa fursa na vikwazo kwa maendeleo. Kwa utaratibu huo mafanikio makubwa yamepatikana katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imeweka kipaumbele na kutenga shilingi milioni 861 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji katika Kijiji cha Lugarawa, ukarabati wa miradi ya maji Lifua/Manda na Kijiji cha Ludewa K. Vilevile Serikali inashirikiana na taasisi isiyo ya Kiserikali ya Lusala Development Association kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji katika vijiji vya Mlangali, Mavanga na Nkomang’ombe utakaogharimu shilingi milioni 250 ambapo mchango wa Serikali ni shilingi milioni 50.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapongeza mchango mkubwa wa wadau mbalimbali kushirikiana na wadau wa maendeleo katika sekta za maji zikiwemo taasisi za dini. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo na kuhakikisha bajeti inatengwa kila mwaka kwa ajili ya kutatua tatizo la maji kwa wananchi wa Ludewa na maeneo mengine hapa nchi.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Mbinga inatoa huduma kwa Halmashauri Nne yaani Mbinga Mjini, Mbinga Vijijini, Nyasa na baadhi ya Kata za Songea Vijijini, hali inayopelekea Hospitali hiyo kuwa na upungufu wa vitendeakazi, wodi na vyumba vya kulaza wagonjwa pamoja na ukosefu wa Madaktari Bingwa:-
Je, ni lini Serikali itaboresha Hospitali hiyo ili iweze kutoa huduma inayotarajiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sixtus Raphael Mapunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua tatizo la vitendea kazi, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma za afya. Serikali kupitia wadau ambao ni wattereed imefanikisha upatikanaji wa gari la wagonjwa lenye namba DFP 5795 ambalo linatumika kuhudumia wagonjwa wanaohitaji rufaa. Wadau hao pia wamesaidia upatikanaji wa mashine muhimu za kupima CD4 na maradhi ya kifua kikuu pamoja na kuwezesha ukarabati wa jengo la maabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa wodi ya watoto na ufinyu wa wodi ya wazazi. Aidha, majengo ya wodi ya upasuaji, wodi ya wanaume, wodi ya daraja la kwanza na kliniki ya meno ni chakavu. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Madaktari (Medical doctors) katika hospitali ni nane, waliopo ni wawili na upungufu ni madaktari sita. Aidha, Madaktari wasaidizi wanaohitajika ni 16, waliopo ni sita na upungufu ni Madaktari 10. Halmashauri imepata kibali cha kuajiri Madaktari wanne katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016. Madaktari watatu waliokuwa masomoni wanatarajiwa kuripoti kazini mwaka huu 2016.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Sera ya Elimu inasema mlinganyo wa vyoo kwa wanafunzi wa kike uwe choo kimoja kwa wasichana 20 na choo kimoja kwa wavulana 25:-
Je, utekelezaji wa Sera hiyo kwenye eneo hili ukoje?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ya sasa kuna uwiano wa choo kimoja kwa wanafunzi wa kike katika shule za msingi ni 52 na wavulana ni 54. Kwa upande wa shule za sekondari uwiano ni wanafunzi 23 kwa choo kimoja kwa wasichana na wavulana ni 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 12.9 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 8,791 kwa shule za msingi na matundu 1,942 kwa shule za sekondari. Kazi hiyo inafanywa na Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo. Azma ya Serikali ni kuhakikisha miundombinu ya vyoo inajengwa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia mashuleni.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatambua mchango mzuri wa wasimamizi wa Rasilimali Fedha, Wahasibu Viongozi (Chief Accountants) walioko kwenye Wizara na Idara za Serikali kwa kuwapandisha kwenye ngazi ya Ukurungenzi ili waweze kuleta tija zaidi kwa ushirika wao katika maamuzi ya Menejimenti ya Wizara/Idara zao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, cheo cha Mhasibu Mkuu au Chief Accountant ni cheo cha madaraka/uongozi na kwa mtumishi anayeteuliwa kushika wadhifa huu anakuwa na hadhi sawa na Mkuu wa Idara au Mkurugenzi katika Wizara au Idara ya Serikali inayojitegemea au wakala na Wahasibu Wakuu ni sehemu ya Menejimenti ya Wizara, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika maamuzi ya Wizara na Idara zao kama ambavyo wako Wakuu wengine wa Idara au Wakurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwapatia mafunzo ya awali watumishi na viongozi wa umma kabla ya uteuzi wa madaraka yoyote katika utumishi wa umma ili waweze kuuelewa utumishi wa umma na kufahamu misingi, sheria, kanuni na taratibu za utendaji kazi katika utumishi wa umma. Mafunzo ya aina hii yamekuwa yakitolewa na Taasisi ya Uongozi, Chuo cha Utumishi wa Umma pamoja na wakala wa mafunzo kwa njia ya mtandao au (TAGLA).
MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali inakusidia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya kilometa 10 ndani ya Mji wa Nzega kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliahidi wakati wa kampeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kilometa 10 za barabara kwa kiwango cha lami zimeshaanza, ambapo kazi zilizofanyika ni upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, kuandaa michoro na makisio ya kazi za ujenzi wa kilometa 10. Mtandao huo wa barabara utajengwa katika Kata ya Nzega Mjini Mashariki, sawa na kilometa tano na Nzega Mjini Magharibi kilometa tano zilizobaki.
Mheshimiwa Spika, gharama za kutekeleza mradi huo ni shilingi bilioni 5.2 ambazo zitahusisha ujenzi wa mitaro ya barabara na makalavati ikiwemo mitaro mikubwa katika eneo la Samora, ujenzi matabaka ya barabara ya changarawe na ujenzi wa mtabaka mawili ya lami nyepesi.
Mheshimiwa Spika, makisio ya gharama hizo yatazingatiwa katika bajeti ya Halmashauri kwa mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuanza utekelezaji kwa awamu.
MHE. KANALI (MST.) MASOUD ALI KHAMIS (K.n.y MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Serikali imeanzisha mabasi yaendayo kwa kasi katika Jiji la Dar es Salaam lakini madereva wengi wamekuwa wakiendesha magari hayo kwa kasi kubwa; kiasi cha kuhatirisha maisha ya watu waendao kwa miguu.
(a) Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua madereva ambao hawafuati Sheria za Barabarani?
(b) Je, ni muda gani magari hayo ya DART yamepangiwa kuanza kazi na kuda wa kumaliza kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Muheshimiwa Ibrahim Hassanali Mohammedali Mbunge wa Kiembesamaki, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, (a), madereva wa DART wanapaswa kuzingatia Sheria ya Usalama Barabarani kama ilivyo kwa dereva yeyote. Tangu mabasi yaanze kutoa huduma madereva 20 wamepewa onyo kwa makosa ya usalama barabarani na wawili wamefukuzwa kazi. Aidha, madereva 40 wamekatwa mishahara kwa makosa mnalimbali kwa kukiuka sheria za barabarani.
Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti mwenendo wa mabasi, mabasi yamefungwa vifaa maalumu katika magari ili kutoa ishara kwa dereva anapozidisha mwendo ambao ni kilomita 50 kwa saa. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kuwajengea uwezo madereva kupitia semina zinazoendeshwa na wataalam kutoka NIT na VETA na Askari wa Usalama Barabarani ili kuwakumbusha taratibu na maadili ya kazi ya udereva.
Mheshimiwa Spika, (b), kwa kuzingatia mazingira ya Jiji la Dar es Salaam kuhusu huduma za usafiri, mkataba baina ya DART na mtoa huduma ambaye ni UDART umeainisha kwamba huduma ya mabasi yaendayo haraka itaanza saa 11.00 alfajiri hadi saa 06.00 usiku.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Wananchi wa Wilaya ya Morogoro Vijijini kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma nzuri za matibabu katika hospitali ya Wilaya kama vile X-Ray, MRI, TSCAN dawa za kutosha, Madaktari Bingwa na Wauguzi kwa sababu tu Wilaya na Halmashauri yake zimechelewa kuhamia Mvuha suala ambalo Ofisi ya Rais, TAMISEMI inalishughulikia:-
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kuanza kujenga Hospitali ya Wilaya Mvuha mahali ambapo ndipo patakapojengwa Makao Makuu ya Wilaya?
(b) Je, Serikali kwa sasa iko tayari kukiteua Kituo cha Afya cha Lukange ambacho ni bora sana kimejengwa na Kanisa Katoliki na kukikabidhi kitoe huduma kwa wananchi kama Hospitali Teule ya Wilaya ya Morogoro Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, tayari Halmashauri imetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika eneo la Mvuha yatakapohamia Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Halmashauri inashauriwa kuweka katika vipaumbele vyake na kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakubaliana na wazo la kukifanya Kituo cha Afya Lukange kuwa Hospitali Teule ya Wilaya kwa kipindi cha mpito. Hata hivyo, suala hili linahitaji makubaliano baina ya Serikali na mmiliki wa kituo ambaye ni Kanisa Katoliki. Hivyo, tunashauri vikao vya maamuzi vya ngazi husika vya Mkoa na Wilaya, vikiona inafaa vianze mchakato huo mapema. Vikao hivyo, vikikaa na kuridhia pendekezo hilo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto haitasita kuteua kituo hicho kuwa Hospitali Teule ya Wilaya.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inakabiliwa na Matatizo mbalimbali kama vile uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa, uhaba wa vitanda hasa kwenye wodi za akinamama, uhaba wa dawa na kadhalika:-
Je, ni lini Serikali itayashughulikia matatizo hayo ili kuboresha huduma zinazotolewa hospitalini hapo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, inayo magari mawili ya kubebea wagonjwa ambayo ni STK 8368 na STK 7079. Gari namba STK 7079 lilipata ajali, lakini limeshafanyiwa matengenezo kupitia TEMESA Mkoa wa Mwanza ili liendelee kutoa huduma kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali hiyo ina jumla ya vitanda 240 kati ya 420 vinavyohitajika. Kwa siku inalaza wagonjwa wanaofikia 169 katika wodi tatu za wazazi zilizopo. Mkoa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, wamepanga kujenga wodi (Postnatal Ward) ambayo itawezesha kuongeza idadi ya vitanda 20 kukidhi mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya dawa katika hospitali imeongezeka kutoka shilingi milioni 710 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 hadi shilingi bilioni1.8 kwa mwaka wa 2016/2017 sawa na ongezeko la asilimia 61. Mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ya huduma kwa njia ya kielektroniki ili kuongeza uwezo wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zote nchini.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Licha ya kwamba chanzo cha maji yanayotumika katika Manispaa ya Mpanda kipo katika Kijiji cha Ikolongo, Kata ya Mtapenda na Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, lakini wananchi wa maeneo haya hawapati maji:-
(a) Je, kwa nini Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017 isitenge fedha ya miradi ya maji ili wananchi wa viiji jirani vya Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ambazo ni Kapalala, Itenka, Machimboni, Sitalike, Kanoge na Katumba wapate maji?
(b) Kwa kuwa Mto Ugalla ni chanzo kizuri cha maji: Je, Serikali itaondoa lini kero ya maji katika Kata ya Ugalla na jirani ya Litapunga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, imetenga shilingi milioni 757.4 kwa ajili ya miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo. Miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja na upanuzi wa mradi wa Nduwi Station katika Kata ya Ntumba, kujenga mradi wa maji katika Kijiji cha Katisunga, kujenga mradi wa maji katika Kijiji cha Songambele, Kata ya Kapalala pamoja na uchimbaji wa visima virefu sita.
(b) Mheshimiwa Spika, kulingana na tathmini iliyofanywa na Mkoa kupitia Mamlaka ya Maji, Mkoa wa Katavi mwezi Desemba, 2015, chanzo cha Mto Ugalla kimeonekana kuwa siyo cha uhakika kutokana na kupungua kwa maji wakati wa kiangazi. Serikali ina mpango wa kutumia Ziwa Tanganyika ambacho ni chanzo cha uhakika kwa ajili ya kupeleka maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo na Mpanda.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto ina hospitali moja ya Wilaya ndani ya Halmashauri mbili na Majimbo matatu, hospitali hii inategemewa na watu zaidi ya 500,000.
Je, ni lini Serikali itaifanyia upanuzi hospitali hiyo hasa wodi ya akina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omar Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imepanga kufanya upanuzi wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo zimetengwa shilingi milioni 50 kwa awamu ya kwanza. Fedha hizo zitatumika kujenga jengo ambalo litakuwa kwa huduma za mama na mtoto, zikiwemo wodi za wajawazito. Hadi kukamilika jengo hilo linatarajiwa kugharimu shilingi milioni 350.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuimarisha vituo vya afya vilivyopo ili viweze kuwa na uwezo wa kufanya upasuaji mdogo wa dharura hasa kwa mama wajawazito ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya.
MHE. OMARI A. KIGODA Aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Handeni inahudumia wagonjwa kutoka Kilindi, Mziha, Wegero na Handeni yenyewe.
Je, ni lini Serikali itaipatia vifaa tiba na wauguzi wa kutosha hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mahitaji ya vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Serikali imetenga shilingi milioni 181.9 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Fedha zote zimeshapokelewa na zimetumika kununulia vifaa tiba vinavyohitajika kusaidia utoaji wa huduma vikiwemo BP machine, vifaa vya kupimia kiwango cha damu, vifaa vya kujifungulia na kupima upumuaji wa watoto, pamoja na kulipia gharama za manunuzi ya jokofu katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Halmashauri imeomba mkopo kutoka Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) ili kununua ultra-sound yenye thamani ya shilingi milioni 75. Halmashauri imeahidi kurejesha fedha zote kupitia makusanyo ya Tele kwa Tele ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi katika Hospitali hiyo ni 359, watumishi waliopo ni 170 na upungufu ni watumishi 189. Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi 118 katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo baadhi ya watumishi hao watapelekwa katika Hospitali ya Wilaya. Kati ya watumishi hao walioombwa, watumishi 49 ni wauguzi, watumishi 25 ni madaktari na kada nyingine ni watumishi 44.
MHE. JULIANA D. SHONZA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya elimu vijijini kama nyumba za walimu pamoja na kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu wanayoidai Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaboresha miundombinu ya shule nchini kupitia mipango na bajeti ya Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 1,157 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 11.14 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 661 kwa shule za sekondari. Aidha, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II), Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba 146 kati ya nyumba 183 ambazo kila nyumba wataishi watumishi sita (walimu). Ujenzi wa nyumba hizo umegharimu shilingi bilioni 21.9. Nyumba 37 zinaendelea kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.5 na zitakamilika tarehe 30 Aprili, 2017.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulipa madeni ya walimu kadri yanavyojitokeza na kuhakikiwa. Katika mwezi Oktoba, 2015 Serikali ililipa madeni ya shilingi bilioni 20.12 kwa walimu 44,700 na shilingi bilioni 1.107 zililipwa mwezi Februari, 2016 kwa walimu 3,221. Hivi sasa walimu wanadai Serikali madeni yanayofikia shilingi bilioni 26.04 kwa ajili ya walimu waliopo kazini 33,620 na walimu wastaafu 2,134. Deni hilo limewasilishwa Hazina kwa ajili ya taratibu za mwisho za kulipwa kwa walimu wanaodai.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Wilaya ya Simanjiro haina Hospitali ya Wilaya na hivyo kusababisha mateso kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo hususan wanawake ambao wanakosa huduma za kujifungua lakini pia kutokana na uchache wa vituo vya afya na zahanati.
(a) Je, ni lini Serikali itavipa hadhi vituo vya afya vya Mererani na Orkesment ili kupunguza tatizo?
(b) Wilaya ya Simanjiro ina gari moja tu la wagonjwa; je, ni lini Serikali itapeleka gari lingine kwenye Kituo cha Afya Mererani ili kuokoa maisha ya akina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, maombi ya kupandisha hadhi Kituo cha Afya Orkesment kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuwa Hospitali Teule ya Wilaya tayari yamewasilishwa katika Wiazara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwezi Oktoba, 2016 kwa uamuzi, baada ya kujadiliwa na kukubalika katika vikao ngazi ya Halmashauri na Mkoa. Kibali kikipatikana Serikali itaingia mkataba rasmi wa utoaji huduma na mmiliki wa kituo hicho ili kuainisha majukumu ya kila mdau. Aidha, Halmashauri imepokea shilingi milioni 80.0 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya cha Urban Orkesment kinachomilikiwa na Serikali. Taratibu za kumpa Mkandarasi zinaendelea.
(b) Mheshimiwa Spika, Halmashauri imetenga gari moja ambalo linatumika kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa wenye rufaa. Gari hilo hutoa huduma kwa wagonjwa katika vituo vyote kikiwemo Mererani pale inapotokea dharura.
Hata hivyo, gari hilo ni chakavu kiasi cha kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara. Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imeshauriwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti katika mwaka 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi wa gari la kuhudumia wagonjwa.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB (K.n.y. MHE. IBRAHIMU HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Wenye maduka waliopewa kibali cha kuegesha magari yao kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni wameonekana wakihodhi nafasi hiyo kwa saa 24:-
(a) Je, ni lini watu wenye tabia hiyo watachukuliwa hatua za kisheria?
(b) Katika Jiji la Dar es Salaam wakati wa usiku inakuwa kama mji huo hauna sheria kwa sababu wenye magari huegesha magari hovyo na kusababisha adha kwa watu wengine. Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua watu wa aina hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Hassanali Mohammedali, Mbunge wa Kiembe Samaki, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo ya Maegesho ya Magari GN. Na. 60 ya mwaka 1998 kifungu cha 6(1) kinaipa mamlaka ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Saalam kudhibiti na kusimamia maeneo ya maegesho ya magari yaliyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ili kuondoa kero, usumbufu na msongamano katika mitaa na barabara za umma. Kwa mujibu wa sheria hiyo, maegesho yote ya magari ya kulipia na maegesho yaliyohifadhiwa yanatumika kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni. Baada ya muda huo maeneo hayo huwa huru kwa matumizi ya umma. Pale inapobainika mtu kuhodhi maeneo hayo baada ya saa 12.00 jioni, Halmashauri ya Jiji huchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya ukaguzi na udhibiti wa maeneo ya maegesho imetolewa kwa Mawakala katika Jiji la Dar es Salaam. Napenda kutoa wito kwa wamiliki wote wa magari kuacha kuegesha magari bila utaratibu hasa wakati wa usiku na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kukiuka taratibu za maegesho ya magari katika Jiji la Dar es Salaam kwa sababu kufanya hivyo ni kusababisha msongamano na kero kubwa kwa wengine.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Halmashauri ya Nsimbo imekuwa ikipokea wahamiaji toka mikoa mbalimbali ambao ni wakulima na wafugaji na kusababisha kukosa maeneo yenye rutuba.
Je, ni lini Serikali itaongeza maeneo ya vijiji vilivyotangazwa mwaka 1974?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyote vilivyoanzishwa mwaka 1974 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, vinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Katavi na Msitu wa Hifadhi wa Msaginya, Mulele Hills na Mpanda North East. Misitu hii pamoja na Mbuga ya Katavi iko chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi za Taifa zipo kwa mujibu wa Sheria kwa maslahi mapana ya Taifa zima na hairuhusiwi kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo hayo yaliyohifadhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, endapo kuna hoja ya kuongeza eneo la kijiji kwa kumega eneo la hifadhi, kijiji kinatakiwa kwanza kuanza mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kuainisha takwimu za msingi za idadi ya watu, idadi ya kaya, ukubwa wa eneo lililopo na mahitaji ya ardhi ya ziada.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyenye mahitaji ya ardhi kutoka kwenye hifadhi vinatakiwa kujadili suala hili katika Mikutano Mikuu ya Vijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Kamati ya Ushauri ya Mkoa na hatimaye maombi hayo kuwasilishwa Wizara yenye dhamana na kuwasilishwa kwa maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa wito kwa viongozi wa Vijiji, Wilaya na Mkoa, kuweka utaratibu wa kudhibiti wahamiaji haramu katika maeneo ya mipakani wakiwemo wafugaji wanaoingiza mifugo katika Hifadhi za Taifa.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU aliuliza:-
Walimu wamekuwa wakiidai Serikali stahiki zao mbalimbali na tatizo hili la kutowalipa kwa muda muafaka limekuwa likijirudia rudia:-
(a) Je, walimu wanadai stahiki zipi na kwa kiasi gani?
(b) Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo na kulimaliza kabisa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya walimu yasiyo ya mishahara ni shilingi bilioni 26 hadi kufikia Desemba, 2016. Deni hili limeshahakikiwa na kuwasilishwa hazina kwa taratibu za mwisho ili liweze kulipwa.
Aidha, madeni yanayotokana na mishahara ni shilingi bilioni 18.1. Uhakiki wa deni la shilingi bilioni 10 umekamilika na linasubiri kulipwa kupitia akaunti ya mtumishi anayedai. Deni linalobaki la shilingi bilioni 8.06 linaendelea kuhakikiwa ili liweze kulipwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kudhibiti uzalishaji wa madeni, mamlaka za Serikali za Mitaa zimetakiwa kutohamisha walimu endapo hakuna bajeti iliyotengwa. Vilevile Serikali imeondoa kipengele kinachohitaji mwalimu akubali cheo chake kwanza ili aweze kulipwa mshahara wake mpya baada ya kupandishwa daraja jambo ambalo lilisababisha malimbikizo makubwa ya mishahara. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kukusanya madeni katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili yaweze kupatikana, kuhakikiwa na kulipwa kwa walimu wanaoidai kwa wakati.
MHE.VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-
Baada ya Serikali kutoa tamko la elimu bure wananchi wamekuwa wagumu sana kutoa michango mbalimbali ya kuboresha elimu.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kumaliza tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa na vyumba vya maabara katika shule za msingi na sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Elimu Msingi bila Malipo unazingatia uendeshaji wa shule bila ada na michango kutoka kwa wazazi au walezi. Hata hivyo, mpango huo haujaondoa dhamira na uzalendo wa jamii kuchangia shughuli za maendeleo ya nchi yao kwa hiari. Kwa uzalendo wa wananchi walioonesha hivi karibuni Serikali imefanikiwa kupiga hatua za maendeleo katika sekta mbalimbali. Mfano, katika kufanikisha utengenezaji wa madawati kwa asilimia 97.2 kwa shule za msingi na asilimia 100.3 kwa shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa rai kwa wananchi wote ambao wamekuwa wagumu katika kushiriki shughuli za maendeleo wabadilishe mwenendo wao na kuwa na uzalendo kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkakati wa kupunguza tatizo la nyumba, vyumba vya madarasa na maabara, Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga shilingi bilioni 29.3 kwa ajili yya ujenzi wa vyumba vya madarasa 3,306 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 16.3 zimetengwa kujenga vyumba vya madarasa 1,047 kwa shule za sekondari. Aidha, kupitia MMES II zimetengwa shilingi bilioni 23.6 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vyumba 1,642. Kwa upande wa maabara Serikali imetenga shilingi bilioni 18.9 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 2,135 vya maabara. Serikali itaendelea kutenga bajeti kila mwaka wa fedha na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo katika kufanikisha upatikanaji wa elimu bora hapa nchini.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Ulevi wa kupita kiasi hasa wa pombe za kienyeji umekuwa na athari kubwa za
kiafya na kiakili kwa Watanzania wenye tabia ya ulevi wa kukithiri:-
Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na tatizo hilo hasa ikizingatiwa kuwa Sheria
ya Vileo ya mwaka 1969 ni ya zamani sana kiasi kwamba inawezekana kabisa
haikidhi mabadiliko ya hali halisi ya vileo kwa wakati huu.
NAIBUWAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli. Sasa hivi kuna tabia kwenye baadhi ya Mikoa,
utakuta watoto wadogo asubuhi au wakati wa weekend wananyweshwa pombe. Jambo hili kwanza kimsingi ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu kwanza
na haki za watoto ambapo mtoto mdogo anatakiwa kuendelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuchukue huu ushauri kwa
sababu sheria hii ni ya muda mrefu sana na kutokana na maoni ya wadau
mbalimbali tutaangalia jinsi gani tutafanya turekebishe, lengo kubwa ni
kuhakikisha kwamba Taifa letu linakuwa Taifa imara kwa sababu lazima tuwalee
hawa watoto kwa kizazi kijacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuchukue ushauri.
Itakapoonekana pale ina haja, basi wadau mbalimbali wataleta maoni yao na
sisi Wabunge ni miongoni mwa wadau wa kutengeneza hizo sheria. Kwa hiyo, hili
nadhani tutalifanyia kazi vema tuweze kulifanikisha.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Ujenzi wa Maabara za Shule za Sekondari Wilaya ya Serengeti umeshakamilika kwa kiwango kikubwa lakini maabara hizo zimebaki kuwa makazi ya popo:-
Je, ni lini Serikali italeta vifaa vya maabara kama ilivyoahidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ina mahitaji ya vyumba vya maabara 63. Zilizokamilika ni 22 na zinatumika; maabara 29 zimekamilika lakini hazina vifaa na vyumba vya maabara 12 viko katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 16 kupitia mradi wa P4R kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara zote zilizokamilika nchi nzima. Vifaa hivyo vinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilianzishwa mwaka 1982, lakini mpaka leo hii haina Hospitali ya Wilaya na ina Vituo vitatu vya Afya:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kuviwezesha Vituo hivi vya Afya kutoa huduma ndogo ya upasuaji ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto pamoja na wananchi wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismail Hongoli, Mbunge wa Lupembe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi milioni 82.0 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Njombe na itaanza kwa jengo la wagonjwa wa nje, yaani OPD. Fedha hizo bado hazijatolewa kutoka HAZINA.
(b) Mheshimiwa Spika, ukarabati wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya cha Lupembe umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 21.0 kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Vile vile, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 36.0 kwa ajili ya kukarabati chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya cha Kichiwa.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kwa changarawe barabara ya Kibiti – Nyamisati. (a) Je, ni sababu zipi zilizochelewesha kukamilika kwa ahadi hiyo? (b) Je, ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za kuchelewa kwa matengenezo ya barabara ya Kibiti – Nyamisati kwa kiwango cha changarawe ni upatikanaji wa fedha. Tathmini iliyofanyika imebainisha kwamba barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 40.8 inahitaji shilingi bilioni 1.2 ili kufanyiwa matengenezo kwa kiwango cha changarawe. Hata hivyo, ili kuifanya barabara hiyo angalau iweze kupitika Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 iliitengea barabara hiyo shilingi milioni 45.79 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya kilometa 38.31 na katika mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 24 zilitumika kwa marekebisho ya sehemu korofi yenye urefu wa kilometa mbili na matengenezo ya kawaida ya kilometa 15. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matengenezo ya barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Serikali itajitahidi kutenga fedha za matengenezo kwa awamu ndani ya kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipande cha kilometa 32.8 kilichobaki baada ya hapo awali kufanyika matengenezo ya kilometa nane kwa kiwango cha changarawe kutoka Kibiti mpaka Ruaruke yaliyofanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani.
MHE. QAMBALO W. QULWI (K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO) aliuliza:- Wilaya ya Karatu inapakana na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro ambapo watalii wengi hutembelea hifadhi na kufanya Wilaya hii kupata fursa ya kujengwa hoteli za kitalii, pamoja na hoteli hizo kujengwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya, Halmashauri hiyo hainufaiki na uwekezaji huo. (a) Je, Halmashauri hiyo hairuhusiwi kutoza hotel levy? (b) Je, nini mkakati wa Serikali kuitangaza Wilaya hii kutokana na uwekezaji wa hoteli nyingi, nzuri na za kisasa zilizopo katika Wilaya hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Hoteli Halmashauri hairuhusiwi kukusanya kodi katika hoteli za kitalii, hata hivyo Halmashauri zinaruhusiwa kwa mujibu wa kifungu cha 26(3) cha sheria hiyo kukusanya ushuru wa hoteli katika nyumba za kulala wageni (guest houses) zilizopo ndani ya Halmashauri. Vilevile Halmashauri zinaruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura Na. 290 kifungu cha 6(u) kukusanya ushuru wa huduma (service levy) katika hoteli za kitalii zinazoendesha shughuli zake ndani ya Halmashauri kwa kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya mapato ghafi ya taasisi husika. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ipo katika hatua za mwisho za utengenezaji wa tovuti (website) yake ili kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kutangaza vivutio vyote vilivyopo vya kitalii hapa nchini kupitia makongamano na shughuli mbalimbali za Kitaifa yakiwemo maadhimisho ya Nanenae na Sabasaba ambayo hufanyika mara kwa mara kila mwaka ili kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kufahamu fursa za uwekezaji zilizopo huko Karatu.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Jimbo la Tabora Mjini katika maeneo ya Kata za Uyui, Misha, Itetemia, Ntalikwa, Kabila, Mtendeni, Ifucha, Itonjanda na baadhi ya vijiji vya Kata ya Tumbi vina shida sana ya upatikanaji wa maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua tatizo la maji Tabora Mjini, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao utahudumia kata na vijiji vya Tabora Mjini. Mradi huo utahudumia vijiji na miji ya Nzega, Igunga, Isikizya yaani Uyui na vijiji vyote vilivyomo ndani ya kilometa 12 kila upande kutoka linapopita bomba kuu la kupeleka maji katika miji hiyo. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 589.6 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi huu utahusisha ujenzi wa mifumo ya maji katika Kata za Uyui, Misha, Itetemia, Ntalikwa, Kabila, Mtendeni, Ifucha, Itonjanda na Tumbi. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza kati ya mwezi Aprili na Mei 2017.
MHE. ANNA R. LUPEMBE Aliuliza:-
Wilaya ya Mlele haina Hospitali ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Mlele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ni miongoni mwa vipaumbele vinavyowekwa na Halmashauri yenyewe. Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele imepanga kuboresha Kituo cha Afya cha Inyonga ili kiweze kutoa huduma zenye hadhi ya Hospitali ya Wilaya katika kipindi cha mpito kabla ya kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo hicho kwa sasa kina wodi nane zenye uwezo wa kulaza wagonjwa 98 kwa siku, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la utawala lenye ofisi sita, stoo ya dawa, chumba cha maabara, chumba maalum cha upasuaji chenye vifaa vyote, mfumo wa maji safi na majitaka katika hospitali na matundu nane ya vyoo vya nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazoendelea ni ujenzi wa jengo la upasuaji ambalo limefikia hatua ya lenta na jengo la kuhifadhia maiti (mortuary) ambalo limefikia hatua za umaliziaji. Ujenzi wa majengo hayo umeshagharimu shilingi milioni 418 na kazi inaendelea.
MHE. MARWA R. CHACHA Aliuliza:-
Wilaya ya Serengeti ina Mbuga ya Wanyama ya Serengeti inayovutia watalii wengi duniani lakini inakabiliwa na uhaba wa maji.
Je, ni lini ujenzi wa chujio na usambazaji wa maji kutoka Bwawa la Manchira kwenda Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu na vijiji vya jirani utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa chujio na usambazaji wa maji Mji Mdogo wa Mugumu utakamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Juni, 2017. Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.49 kupitia Mkandarasi M/S Pet Cooperation wa Kahama kupitia Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Mara. Utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 62.5 ambapo mkandarasi ameshalipwa shilingi milioni 933.8.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miradi ya maji inayojengwa Wilayani Sengerema katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa inakamilika haraka na kuwanufaisha wananchi wa Buchosa hasa mradi wa maji wa Lumea - Kalebezo na Nyegonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Sika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mitatu inayohudumia vijiji nane katika Halmashauri ya Buchosa inaendelea kujengwa ambayo ni mradi wa maji Lumea - Kerebezo - Nyegonge, mradi wa maji Nyakalilo - Bukokwa na mradi wa maji Luchili - Nyakasungwa hadi Igwanzozuna.
Ujenzi wa mradi wa maji Lumea - Kalebezo - Nyegonge ulianza kutekelezwa mwezi Machi 2013 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.69 kwa sasa mradi huo upo katika hatua za mwisho za majaribio ya mitambo pamoja na miundombinu na utaanza kutoa huduma ifikapo Juni, 2017.
Mradi utakapokamilika utanufaisha wakazi 16,000 wa vijiji vya Kalebezo na Nyegonge.
MHE. JEROME D. BWANAUSI Aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga madaraja ya Shaurimoyo, Nakalolo na Miesi.
Je, ni lini madaraja hayo yatajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kwa msaada wa Wakala wa Barabara (TANROADS) imekamilisha usanifu wa madaraja yanayohitajika kujengwa katika mito ya Mpindimbi - Shaurimoyo - Nakanyimbi mpaka Nakalolo. Gharama za awali za ujenzi wa madaraja hayo
zimebainika kuwa ni shilingi bilioni tatu. Kutokana na ufinyu wa bajeti ya Halmashauri, Wakala wa Barabara (TANROADS) imekubali kutenga fedha hizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni alipotembelea Wilaya ya Chemba aliahidi kuongeza fedha za ujenzi wa Jengo la Halmashauri mpya ya Wilaya:- Je, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga kiasi gani kuendeleza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Seleman Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Halmashauri ilitengewa jumla shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. Hadi Machi, 2017 fedha zote zimepokelewa na kazi inaendelea vizuri. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY (K.n.y MHE. ESTHER A. MAHAWE) aliuliza:-
Vituo vya Afya na Zahanati zilizo karibu na Hospitali za Wilaya zina changamoto ya utoaji huduma bora kwa sababu ya upungufu wa dawa na watumishi wa kada ya afya hivyo kusababisha kuhudumiwa na Hospitali za Wilaya ambazo bajeti za dawa hazikidhi:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza bajeti ya Hospitali za Wilaya zilizoko katika Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rai, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Manyara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2016/2017, Halmashauri za Mkoa wa Manyara zimetengewa bajeti ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kati ya fedha hizo, fedha zilizopokelewa hadi Machi, 2017 ni shilingi bilioni 1.07 sawa na asilimia 75%. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri za Mkoa huo zimepanga kutumia shilingi 1.58 kwa ajili ya dawa sawa
na ongezeko la asilimia 9.7 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuanza kutumia mfumo wa kupeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa moja kwa moja katika vituo vya tiba yaani Direct Facility Financing (DFF), hali itakayosaidia vituo vya kutolea huduma kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye hospitali,
vituo vya afya na zahanati. Halmashauri zitabaki na jukumu la kusimamia taratibu zote na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
MHE. KISWAGA B. DESTERY (K.n.y. MHE. LAMECK O.
AIRO) aliuliza:-
Wananchi wa Kata ya Koryo kwa kushirikiana na Mbunge wao na wananchi wa Rorya wanaoishi Mwanza, Arusha na Dar es Salaam wamejenga wodi ya akina mama na watoto pamoja na kununua jokofu lakini mapungufu yaliyopo sasa ni Jengo la upasuaji.
Je, Serikali sasa haioni ipo haja ya kusaidia jengo hilo pamoja na vifaa vyake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 mradi uliidhinishiwa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la upasuaji. Fedha zote zimepokelewa na tayari Halmashauri imeanza taratibu za kumpata mkandarasi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 25 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa jengo hilo.
MHE. PAULINE P. GEKUL (K.n.y. MHE. ANATROPIA L.
THEONEST aliluiza:-
Mkao Makuu ya Wilaya ya Kyerwa yamewekwa katika Kata ya Kyerwa.
Je, ni mchakato gani ulifanyika mpaka Kata ya Kyerwa kuwa Makao Makuu ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili eneo liwe na makao makuu ya Wilaya lazima wananchi washirikishwe kupitia mikutano mikuu ya Vijiji na Halmashauri za Vijiji, Kamati za Maendeleo za Kata, Mabaraza ya Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa kuifanya Kata ya Kyerwa kuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Kyerwa ulitolewa baada ya kupitishwa na Baraza la Madiwani katika kikao cha tarehe 30 hadi 31 Oktoba, 2012 na Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kagera katika kikao chake cha tarehe 15 Machi, 2013 hivyo uamuzi wa mwisho kuhusu eneo la Rubwera katika Kata ya Kyerwa kuwa Makao Makuu ya Wilaya Kyerwa ulizingatia mapendekezo ya vikao hivyo vya kisheria.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliluliza:-
Wilaya ya karatu ina umri wa zaidi ya mika 20 lakini bado haina Hospitali ya Wilaya jambo ambalo linawatesa wakazi wengi hasa wazee, akinamama na watoto.
Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya cha Karatu kuwa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Qulwi, Mbunge wa Karatu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kupandisha hadhi kituo cha afya kuwa hospitali yanaanza katika Halmashauri yenyewe kupitia Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa. Taratibu hizi zikikamilika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa kibali baada ya kujiridhisha kupitia timu ya ukaguzi hivyo Halmashauri unashauriwa kuanzisha mchakato wa kujadili suala hilo katika vikao vya kisheria na kuwasilisha katika mamlaka husika kwa maamuzi.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali inatambua uwepo wa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji ambao wanatekeleza majukumu yao moja kwa moja
na wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa posho viongozi hao kama inavyofanya kwa Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia kila Halmashauri imeweka utaratibu wa kuwalipa posho Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri. Katika makusanyo ya mapato kupitia vyanzo vya ndani kila Halmashauri hupeleka asilimia 20 kwenye vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba 3% hutumika kwa ajili ya maendeleo na 17% hutumika kwa ajili ya utawala ikiwemo kuwalipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa. Viwango vya kulipa posho hizo hutofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine kulingana na makusanyo ya mapato ya ndani katika vyanzo vilivyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa fedha hizo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imependekeza kulifanya suala la asilimia 20 kuwa la kisheria katika marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Maandalizi ya sheria hii yako katika hatua za mwisho na Muswada huo utawasilishwa na kujadiliwa hapa Bungeni.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Wananchi wa Mji wa Haydom wamekuwa wakiomba Haydom iwe Mamlaka ya Mji Mdogo.
Je, ni lini Serikali itaupa Mji wa Haydom hadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kuwa na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Haydom yamejadiliwa katika vikao vya awali vya Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira tarehe 25/09/2012, Baraza la Madiwani katika kikao cha tarehe 19/10/2012 na Kamati ya Huduma za Uchumi katika kikao cha tarehe 13/06/2014. Kimsingi, vikao vyote hivyo vimekubaliana na wazo la kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Haydom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri mapendekezo hayo sasa yawasilishwe katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) ili hatimaye yawasilishwe kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kupata kibali. Hivyo, taratibu hizo zikikamilika na kuonekana mamlaka hiyo imekidhi vigezo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, haitasita kuanzisha mamlaka hiyo kisheria.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Serikali ilipata mkopo kutoka Benki ya Dunia na kujenga miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Jijini Dar es Salaam. Baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika Serikali ilitoa msamaha wa baadhi ya kodi wakati wa uingizaji nchini mabasi yanayotumika kusafirisha abiria katika mradi huo. Serikali inamiliki asilimia 49 ya hisa za mradi huo na mwekezaji asilimia 51.
(a) Wakati wa kukokotoa hisa kati ya Serikali na mwekezaji, je, sehemu ya msamaha imejumlishwa katika ukokotoaji wa hisa?
(b) Je, ni nini faida na hasara za msamaha huo wa kodi upande wa Serikali?
(c) Wakati wa kulipa mkopo huo, je, ni nini wajibu wa mwekezaji katika mkopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kimsingi mwekezaji hakupata msamaha wa kodi wakati wa kuingiza mabasi nchini bali alipewa punguzo la kodi hiyo (import duty) kutoka asilimia 25 inayotozwa hadi asilimia 10. Punguzo hilo lilitolewa kwa makubaliano na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(b) Mheshimiwa Spika, punguzo la kodi hiyo limesaidia kutoa unafuu wa nauli zinazotozwa kwa abiria wanaotumia mabasi ya UDART. Endapo punguzo hilo lisingekuwepo ni dhahiri kwamba gharama hizo zingejumuishwa katika viwango vya nauli kwa watumiaji.
(c) Mheshimiwa Spika, mwekezaji anawajibika kurejesha mkopo aliochukua kwa ajili ya kununulia mabasi pamoja na kulipa kodi Serikalini kwa mujibu wa sheria za nchi. Kwa upande wake, Serikali inawajibika kulipa mkopo Benki ya Dunia ambao ulitumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi
wa DART awamu ya kwanza kwa kuzingatia makubaliano (financing agreement).
MHE. FREDY A. MWAKIBETE Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itayakubali maombi ya wananchi wa Halmashauri ya Busokelo ya kuifanya Halmashauri hiyo iwe Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali GN Namba 286 ya tarehe 9 Septemba, 2011 ikiwa ni sehemu ya Wilaya ya Rungwe kwa lengo la kusogeza karibu huduma zilizokuwa zikitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo ya kuifanya Halmashauri ya Busokelo kuwa Wilaya yaliwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) iliyokutana tarehe 4 Julai, 2013. Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Mkoa kupitia maombi hayo ili kujiridhisha kama Halmashauri hiyo inakidhi vigezo kuwa Wilaya kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekretarieti ya Mkoa ilifanya tathmini ya maombi ya wananchi wa Busokelo ya kuwa Wilaya kamili kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua nia njema na juhudi kubwa ya Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa kuzingatia taarifa ya tathmini iliyofanywa na Sekretarieti ya Mkoa, hususan katika idadi ya watu, ukubwa wa eneo pamoja na kuwepo kwa tarafa moja pekee, imesababisha kutokidhi vigezo vya uanzishwaji wa Wilaya ya kiutawala ya Busokelo.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji wananchi wa vijiji vya Jimbo la Chilonwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini, kuanzia mwaka 2012/2013 hadi mwaka 2014/2015 imetekeleza miradi ya maji kwa vijiji vya Itiso na Membe kwa jumla ya shilingi milioni 758.7 vikiwa na jumla ya vituo vya kuchotea maji 23 ambavyo vinahudumia wakazi wapatao 7,475.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri inakamilisha mradi wa maji katika kijiji cha Wilunze ambao utahudumia jumla ya watu 2,867 kwa maeneo ya Makaravati, Mbelezungu, Majengo na Chalinze Nyama kwa jumla ya shilingi milioni 347.9 katika Jimbo la Chilonwa.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imepanga kutumia shilingi bilioni 1.053 kwa ajili ya kujenga miradi ya maji ikiwa ni pamoja na vijiji vya Magungu na Segala katika Jimbo la Chilonwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Chilonwa na maeneo mengine nchini kwa kadri rasilimali fedha itakavyopatikana.
MHE.OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Ibara ya 57(b) ya Ilani ya CCM inaahidi kuweka mfumo wa kuvitambua, kuvisajili na kuviwezesha vikundi vyote vyenye mwelekeo wa ushirika na ujasiriamali nchini. Kwa kuwa kundi la waendeshaji wa vyombo vya usafiri wa abiria maarufu kama bodaboda ni kundi la kijasiriamali, na inawezekana ndilo kundi lenye mwelekeo na fursa za kiushirika ambalo ni kubwa zaidi Wilayani Biharamulo na nchini kote kwa sasa.
Je, Serikali ina mpango gani mahususi juu ya kundi hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha Ibara ya 57(b) ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inatekelezwa kikamilifu kuhusu uwezeshaji, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo imeweza kuvitambua na kuvisajili jumla ya vikundi 1,940 vya wajasiriamali vikiwemo vikundi 34 vya vijana waendesha bodaboda. Aidha, waendesha bodaboda 2,000 wametambuliwa kwa jitihada kubwa za Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri na wakawekewa utaratibu wa utoaji huduma ya usafiri wa pikipiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Biharamulo imewezesha jumla ya waendesha bodaboda 410 kupata mafunzo ya uendeshaji wa pikipiki na kupata leseni za kuendesha na kufanya biashara hiyo.
Natoa wito kwa Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhamasisha waendesha bodaboda wajiunge kwenye vikundi na SACCOS ili watambulike kisheria na kupata fursa ya mikopo inayotolewa kupitia asilimia 10 ya vijana na wanawake pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi.
MHE. PETER J. SERUKAMBA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni aliahidi kuanza ujenzi wa barabara ya Mwandiga – Chankele – Kagunga.
Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mwandiga – Chankele - Kagunga yenye urefu wa kilometa 55.76 ipo katika eneo la mwambao wa Ziwa Tanganyika. Tayari upembuzi yakinifu umefanyika na kubaini kuwa zinahitajika shilingi bilioni saba kuweza kujenga barabara hiyo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uwezo mdogo wa Halmashauri, ilikubalika kupitia Kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa wa Kigoma, iweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa (TANROADS). Maombi hayo yamewasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na ujenzi kwa ajili ya kupata kibali.
MHE. SAUMU H. SAKALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza magari yaliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kwa haraka kutokana na uhaba wa magari unaosababishwa na ubovu wa magari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saumu Heri Sakala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani
ina jumla ya magari 15 ambapo kati ya hayo magari 11 yanafanya kazi. Matengenezo ya magari ya Halmashauri yanafanyika kupitia fedha za matumizi mengineyo zinazotengwa kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri hiyo iliidhinishiwa shilingi 52,500,000 kwa ajili ya matengenezo ya magari na katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri hiyo imetengewa shilingi milioni 73. Hivyo, Halmashauri inashauriwa kuweka kipaumbele na kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatumika kutengeneza magari ili kuimarisha usimamizi wa Halmashauri.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Fedha zinazotengwa na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani; asilimia 10 ya fedha hizo zinatakiwa kwenda kwa vijana na wanawake na zinatakiwa ziwafikie walengwa kila mwaka bila kukosa.
Je, Serikali iko tayari kutoa agizo la msisitizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha hizo na wala wasichukulie kama ni hisani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinatakiwa kutekeleza agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri zilitengewa jumla ya shilingi bilioni 56.8 ambapo hadi Machi, 2017 kiasi kilichopelekwa kwenye mifuko kilikuwa ni shilingi bilioni 16.05. Halmashauri ya Jiji la Mwanza pekee imeshapeleka shilingi milioni 147.0.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuanza kutenga maeneo rafiki ya kufanyia biashara kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo, kupeleka fedha kwenye mifuko na kusimamia marejesho ili ziweze kunufaisha makundi mengine. Utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ni kipimo cha utendaji kwa Wakurugenzi wote nchini na kushindwa kutekeleza, sio vyema kabisa. Aidha, hatua zitachukuliwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
MHE. PETER J. SERUKAMBA (K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:-
Shule za Sekondari za Umma zimeendelea kufanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne na sita, ambapo kwa mwaka 2015 katika matokeo ya kidato cha nne watahiniwa waliopata daraja la nne ni 240,996 sawa na asilimia 67.91 na waliopata daraja la sifuri ni 113,489 sawa na asilimia 32.09:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika Shule za Umma za Sekondari nchini ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya madarasa, mabweni na maabara?
(b) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifuta
kazi Bodi ya Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania na kuiunda upya kutokana na kushindwa kusimamia ubora wa elimu nchini ambayo ni moja ya jukumu lake?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifufua zilizokuwa shule za vipaji maalum za Ilboru, Kilakala, Mzumbe na Kibaha zilizowahi kufanya vizuri miaka ya 1990?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II) Serikali imekamilisha uboreshaji wa Shule za Sekondari 792 kwa kukarabati miundombinu na kuweka samani; shule 264 ziliboreshwa katika awamu ya kwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 56; na shule 540 katika awamu ya pili kwa gharama ya shilingi bilioni 67.8 na zote zimekamilika. Ukamilishaji wa ujenzi wa shule hizo, umesaidia katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia katika Shule za Sekondari za Serikali.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ubora wa elimu linajumuisha mambo mengi ambayo yanahusisha kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia jambo ambalo linatekelezwa kupitia mipango na bajeti kila mwaka. Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inasimamia udhibiti wa ubora wa elimu ikishirikiana na taasisi nyingine zinazotekeleza Sera ya Elimu Tanzania. Kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha elimu nchini, hatuoni sababu ya kuvunja Bodi hiyo, badala yake tutaendelea kuiwezesha kutekeleza majukumu yake vizuri zaidi kwa kushirikiana na taasisi nyingine.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea
na ukarabati wa shule kongwe zote 89 nchini zikiwemo Ilboru, Kilakala, Mzumbe na Kibaha. Mwaka wa fedha 2013/2014 Serikali ilitoa shilingi bilioni 12.8 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule kongwe na shilingi bilioni 3.5 zilitolewa na kutumika kukarabati shule saba za ufundi za Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma, Bwiru Boys na Ifunda. Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) itakarabati shule kongwe 11 zikiwemo za vipaji maalum za Mzumbe, Ilboru, Kilakala, Tabora Boys, Tabora Girls, Pugu, Nganza, Mwenge, Same na Msalato.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa, huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya Bagamoyo zimekuwa dhaifu sana kutokana na upungufu mkubwa wa miundombinu, vitendea kazi, uhaba wa watumishi na ukosefu wa dawa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma
za afya katika Hospitali hiyo kwa kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu bora, vitendea kazi, kuiongezea watumishi na dawa za kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi 1.4 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambapo itahusisha kuboresha miundombinu ya Hospitali na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile zimetengwa shilingi 185,000,000/= kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kutokana na ruzuku ya maendeleo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya vituo vya kutolea huduma za afya, shilingi 59,790,600/= kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya upanuzi wa wodi ya wazazi, ukarabati wa kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD) na eneo la kuhudumia wagonjwa wa dharura pamoja na kumaliza ukarabati wa wodi ya wanaume. Aidha, Serikali imetoa kibali cha kuajiri Madaktari na watumishi wengine wa afya ambapo Halmashauri hiyo pia itapewa kipaumbele. (Makofi)
MHE. ROSE K. SUKUM aliuliza:-
Serikali hupeleka fedha kwenye Halmashauri baada
ya kupokea mpango kazi wa maendeleo au matumizi ya kawaida kwa Halmashauri husika. Kama ikitokea fedha zaidi zimepelekwa katika Halmashauri, maana yake kuna Halmashauri imepelekewa kidogo:-
(a) Je, kwa nini fedha za ziada zisirudishwe Hazina
na badala yake zinaombwa kutumiwa na Halmashauri ambayo haikuwa na mahitaji nazo?
(b) Je, Halmashauri ambazo zinakuwa zimepelekewa fedha kidogo zinafidiwa vipi ili kukidhi maombi ya mpango kazi wake?
(c) Je, kwa Halmashauri inayotumia fedha hizo
bila ya kusubiri maelekezo kama ilivyo pale inapokuwa ziada kuwekwa kwenye Akaunti ya Amana kama Memorandum ya Fedha ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Kifungu Na. 9(2)(e) kinavyoelekeza, endapo itabainika, wanachukuliwa hatua gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Kamili Sukum, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, upelekaji wa fedha katika Halmshauri huzingatia Mpango Kazi (Action Plan) ambao huandaliwa kwa kuzingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Fedha hizo hupelekwa na Hazina kila robo mwaka zikiwa na maelekezo ya matumizi. Uzoefu unatuonesha Halmashauri zimekuwa zikipokea pesa pungufu ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa kwa sababu upelekaji wa fedha hizo huzingatia hali ya makusanyo kwa nchi nzima. Hata hivyo, pale inapobainika kuwa fedha zilizopokelewa zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa na hakuna maelezo ya matumizi, ni wajibu wa Afisa Masuhuli kuuliza matumizi ya fedha hizo Hazina au Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kabla ya kuzitumia.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu langu, kila Halmashauri hupelekewa fedha kulingana na bajeti iliyoidhinishwa na kwa kuzingatia mpango kazi. Fedha hupelekwa katika Halmashauri kwa kuzingatia hali ya makusanyo (Cash Budget). Kwa mantiki hiyo, hakuna utaratibu wa kufidia bajeti ambayo haikutolewa kwa mwaka husika. Mwongozo wa Bajeti huzitaka mamlaka husika kuzingatia maeneo ambayo hayakupata fedha katika vipaumbele vya bajeti inayofuata ili kupata fedha.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zote zinazotumwa katika Halmashauri huambatana na maelezo ya matumizi ya fedha hizo ambayo hupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa. Pale inapotokea maelezo yamechelewa kufika, ni wajibu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika kufuatilia Hazina au Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kabla ya kuzitumia. Afisa Masuhuli atakayetumia fedha za ziada bila idhini, anakiuka sheria na taratibu za fedha na anastahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Waathirika wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamekuwa wakipoteza maisha haraka zaidi kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za matibabu.
Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi, vifaa tiba
na dawa katika kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Njombe ilitengewa bajeti ya shilingi 295,000,000 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo mpaka Machi, 2017 tayari shilingi 87,000,000 zilipelekwa na kuelekezwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya afya. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri hiyo imetengewa bajeti ya shilingi 433,000,000 sawa na ongezeko la asilimia 47. Vilevile Serikali imeongeza fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya kutoka shilingi milioni 259.4 zilizotengwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi shilingi milioni 306.2 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 18. Fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Halmashauri inatakiwa kutumia makusanyo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana pamoja na dawa katika vituo vinavyotoa huduma ya afya. Serikali itaendelea kuongeza fedha kila mwaka na kushirikiana na wananchi ili kuimarisha huduma za afya Wilayani Njombe na Tanzania kwa ujumla.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ni miongoni mwa Halmashauri mpya zilizoanzishwa mwaka 2015 na watumishi 98 walihamishiwa kutoka Halmashauri za Sengerema, Misungwi, Ilemela, Jiji la Mwanza, Kwimba na Magu lakini watumishi hawa hadi sasa hawajalipwa fedha za uhamisho:-
Je, ni lini Serikali itawalipa stahiki zao watumishi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemilembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ni miongoni mwa Halmashauri zilizoanzishwa Julai, 2015 baada ya kugawanywa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema. Watumishi 98 waliohamishwa Buchosa kutoka Halmashauri za Sengerema, Ilemela, Jiji la Mwanza, Kwimba na Magu wanadai jumla ya shilingi 354,075,500 na tayari madai ya shilingi 44,531,000 yamelipwa kwa watumishi 16. Hadi Disemba, 2016 Halmashauri imebakiwa na madeni ya uhamisho kwa watumishi 88 wenye jumla ya shilingi 292,531,000. Madeni hayo yaliyobaki yamewasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uhakiki ili yalipwe.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Wananchi wa wa Kibiti wanaishukuru Serikali kwa kupata Mji Mdogo Kibiti na kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti na viongozi.
(a) Je, kuna tatizo gani hadi leo Mamlaka ya Mji haijaanza kazi na kumpata Meya?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka Mkurugenzi wa Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya
Kibiti ni mpya na ilianzishwa rasmi Julai, 2016. Halmashauri hiyo ilipatikana baada ya kugawanywa kwa Halmashauri Mama ya Rufiji ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Sababu kubwa iliyochelewesha uundwaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibiti ni ufinyu wa bajeti. Hali hiyo imechangia Halmashauri kushindwa kuitisha uchaguzi mdogo kujaza nafasi zilizo wazi za Wenyeviti wa Vitongoji ili kuunda Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo pamoja na Mwenyekiti wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Halmashauri hiyo inajiendesha kwa kutumia mapato ya ndani ambayo yalianza kukusanywa Oktoba, 2016. Hivyo, hali ya kifedha itakapokuwa nzuri, Halmashauri itafanya uteuzi wa Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo pamoja na kukamilisha uchaguzi wa Mwenyekiti ili Wenyeviti hao waweze kumchagua Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo anayetakiwa kuchaguliwa miongoni mwa Wenyeviti hao wa vitongoji.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-
Majukumu ya Mbunge kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(3) yameainisha kwa ujumla wake bila kubagua aina ya Ubunge; lakini Sheria Namba 16 ya mwaka 2009 iliyounda Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) imeonesha ubaguzi mkubwa kwa kumtambua Mbunge wa Jimbo pekee ambaye ndiye aliyetajwa na sheria hiyo kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Mfuko huo na kuwatenga Wabunge wa Viti Maalum licha ya kwamba Wabunge wote wanatekeleza majukumu sawa ya kuwatumikia wananchi.
Je, ni lini Serikali itarekebisha sheria hii ili ijumuishe Wabunge wote ikiwemo Wabunge wa Viti Maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa mwaka 2009 kwa Sheria Namba 16 ya mwaka 2009 iliyotungwa na Bunge. Fedha za Mfuko wa Jimbo hutolewa katika Majimbo yote ya uchaguzi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyopitishwa kisheria. Vigezo vinavyotumika kugawa fedha za Mfuko wa Jimbo ni idadi ya watu asilimia 45, mgao sawa (pro-rata) kila Jimbo asilimia 25, kiwango cha umaskini asilimia 20 na ukubwa wa eneo asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Jimbo huingizwa moja kwa moja katika account ya Halmashauri na zinasimamiwa kwa taratibu za Sheria ya Fedha isipokuwa Mbunge wa Jimbo ni Mwenyekiti wa Mfuko huo. Kimsingi sheria haina ubaguzi kwa Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum kwa sababu fedha hizo za Serikali zinatumika kutekeleza miradi ya kipaumbele iliyoibuliwa na wananchi wenyewe kwenye Jimbo husika kwa kuzingatia mahitaji ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na malengo yaliyounda Sheria ya Mfuko wa Jimbo na vigezo vinavyotumika katika kupeleka fedha za Mfuko wa Jimbo, Serikali inaona sheria hiyo inajitosheleza kwa sasa kwa kuzingatia misingi ya uundwaji wake, labda Bunge ambalo ndilo lenye mamlaka ya kutunga sheria litakavyoamua vinginevyo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-
Majengo mengi yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Jimbo la Solwa kama vile vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na zahanati yako katika hatua za mwisho kukamilika.
Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kukamilisha majengo hayo ili yaweze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Solwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamejenga kwa nguvu zao vyumba vya madarasa 37, nyumba za walimu 33 na zahanati 38 ambazo zipo katika hatua mbalimbali.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 695.3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyoanza kwa nguvu za wananchi katika sekta ya elimu na afya. Hadi sasa Halmashauri imeshapokea shilingi 420,881,000 ambazo zimepelekwa katika ukamilishaji wa miundombiinu ya elimu na afya.
Vilevile Serikali imeongeza fedha za ruzuku ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 1.2 zilizotengwa katika Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi shilingi bilioni 1.7 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 42 kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi. Kulingana na muongozo wa asilimia 50 ya fedha hizo zinatakiwa kutumika katika miradi ngazi ya Halmashauri na asilimia 50 zinatakiwa kutekeleza miradi hiyo katika ngazi ya vijiji.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuhusu huduma ya mabasi yaendayo kasi pale umeme unapokatika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakala wa mabasi yaendayo haraka umejipanga vizuri kwa kuweka jenereta moja katika kila kituo kikubwa, ambalo hutumika kama chanzo cha umeme pale umeme wa TANESCO unapokatika. Vituo vikuu vilivyowekewa jenereta ni vya Kimara, Ubungo, Morocco, Kivukoni, Gerezani na katika karakana iliyopo Jangwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia kupitia DART imeweka betri za kutunza umeme (backup batteries) katika vituo vyote vidogo 27 ili zitumike kama chanzo cha umeme, pale umeme wa TANESCO unapokatika.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya Kharumwa kuwa Hospitali ya Wilaya Nyang’hwale.
Je, ni lini Serikali itaongeza majengo kwa ajili ya wodi
za wagonjwa na wodi za wazazi katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA SERIKALI ZA MIKOA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri ya Wilaya ya Ngang’wale ilitengewa ruzuku ya maendeleo isiyokuwa na masharti (LGDG) kiasi cha 533,822,000 kwa ajili ya ujenzi wa miradi, ikiwemo sekta ya afya. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 186.6 zimeshapokelewa. Fedha hizo zinapaswa kutekeleza miradi ambayo ni kipaumbele cha halmshauri kilichowekwa na wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeongeza ruzuku ya maendeleo hadi shilingi bilioni 1.038 sawa na ongezeko la asilimia 95. Vipaumbele vya matumizi ya fedha hizo ikiwemo ujenzi wa wodi, vitapangwa na halmashauri zenyewe kwa kuzingatia fursa na vikwazo vilivyopo.
MHE. JOHN J. MNYIKA (k.n.y MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali iliahidi kuhamisha Kituo cha Mabasi cha Ubungo na kukipeleka eneo la Mbezi katika Jimbo la Kibamba lakini mpaka sasa jambo hilo halijatelekezwa.
(a) Je, Serikali imefikia hatua gani ktaika kutekeleza ahadi hiyo?
(b) Je, mradi wa kuhamisha Kituo cha Mabasi unatarajiwa kutumia kiasi gani cha fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hadi sasa tayari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Serikali za Mitaa (LAPF) umeanzisha kampuni ya ubia ya Mzizima Properties Limited ambayo itahusikana usimamizi na uendeshaji wa shughuli za kituo za kila siku. Kazi inayoendelea ni kutafuta Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kuthibitisha usanifu wa mwisho wa kina wa mradi ili kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi.
Mheshimiwa Spika, gharama za ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi cha Mbezi Luis zinakadiriwa kuwa shilingi bilioni 28.71 zitakazotolewa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Jiji na LAPF. Gharama halisi zitajulikana baada ya usanifu wa kina (detailed design) utakapofanywa na Mtaalam Mshauri.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI (K.n.y. MHE. SELEMANI J. ZEDI) aliuliza:-
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Tabora (RCC) mwaka 2014 ilikubali ombi la wananchi wa Wilaya ya Nzega la kutaka kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Bukene hasa ikizingatiwa kuwa Jimbo la Bukene lina vigezo vyote vinavyohitajika kwa uanzishwaji wa Wilaya na ombi hili lilipelekwa TAMISEMI ili kufanyiwa kazi.
Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa maamuzi ya RCC ya kuomba uanzishwaji wa Wilaya mpya ya Bukene?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Tabora uliwasilisha maombi ya kuanzishwa kwa Wilaya ya Bukene baada ya kupitishwa na Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika tarehe 29 Mei, 2015. Kikao hicho kilijadili pendekezo la kuanzisha Mkoa mpya wa Ngega sambamba na kuanzisha Wilaya mpya ya Bukene. Aidha, tarehe 26 Februari, 2016 Katibu Tawala Mkoa wa Tabora aliandikiwa barua yenye Kumb. Na. BD. 310/365/31 ya tarehe 26/02/2016 ili kufanyia kazi mapungufu yaliyobainishwa katika maombi hayo. Tayari mkoa umefanyia kazi upungufu huo na kuwasilisha taarifa kwa barua ya tarehe 11 Aprili, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi wa kina unafanyika sambamba na maombi ya maeneo mengine. Aidha, timu ya wataalam imefanya zoezi kubwa la uhakiki wa vigezo na taratibu (physical verification) kwa maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kumshauri Mheshimiwa Rais kuhusu mapendekezo hayo kwa kuzingatia Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
MHE. SALOME W. MAKAMBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais aliyoitoa wakati wa kampeni kwa wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini ya kujenga kwa kiwango cha lami kilometa 10 za barabara za mitaa ya Mji wa Kahama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Wcyliffe Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kwanza ya utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kuzitambua barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Mji wa Kahama ambayo imekamilika. Ujenzi huo utahusisha barabara ya Mama Farida yenye urefu wa kilometa 1.305; barabara ya Phantom -Majengo yenye urefu wa kilometa 5.214; barabara ya Malunga Mashineni - Mwamvua yenye urefu wa kilometa 1.852, barabara ya Nyihogo - Namanga yenye urefu wa kilometa 0.6, barabara ya Florida - Stendi ndogo yenye urefu wa kilometa 0.829 na barabara ya Royal ya Zamani - Stendi Ndogo yenye urefu wa kilometa 0.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara hizo utafanyika kwa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018, zimetengwa shilingi 603,604,733 kwa ajili ya kujenga barabara yenye urefu wa kilometa moja kwa kiwango cha lami. Vilevile, kupitia fedha za Mfuko wa Barabara, zimetengwa shilingi 320,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa barabara za lami zenye urefu wa mita 800 katika Mji wa Kahama.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Vifo vya mama na mtoto vinachangiwa na huduma hafifu ikiwemo ukosefu wa usafiri hasa gari la kubebea wagonjwa (ambulance).
Je, ni lini Serikali itatoa gari la wagonjwa kwa Jimbo la Nsimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ina jumla ya vituo vya afya vitatu. Kituo cha Afya cha Katumba, Kituo cha Afya cha Kanoge na Kituo cha Afya cha Mtisi vinavyohudumiwa na gari moja la wagonjwa. Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ina upungufu wa magari mawili. Kwa kuzingatia changamoto hiyo, Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 220 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi wa gari la wagonjwa ili kuharakisha huduma za rufaa na kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Kumekuwa na mpango kabambe wa Mfuko wa Afya wa Bima (CHF) ambao ni “Papo kwa Papo na Tele kwa Tele”’ na Watanzania waliopo Serengeti wamekuwa wakichangia huduma hiyo lakini kila waendapo kwenye matibabu hupewa cheti badala ya dawa.
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la ukosefu wa dawa kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mala Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa dawa unategemea upatikanaji wa fedha kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja ambapo Halmashauri hiyo imeshapokea fedha zote kiasi cha shilingi milioni 826.4 zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 843 kwa ajili ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo. Kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Halmashauri zinakusanya mapato yatokanayo na uchangiaji kwa kuzingatia sheria ndogo za Halmashauri ambapo kipaumbele ni upatikanaji wa dawa. Natumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kuhamasisha wananchi kuchangia mfuko.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Mwaka 2012/2013 Serikali ilichukua ardhi ya wananchi wa Mtwara Mjini eneo la Mji Mwema na Tangira. Aidha, Serikali imewazuia wananchi hao kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo hayo. Serikali iliahidi kuwalipa wananchi hao fidia lakini hadi sasa fidia hiyo haijalipwa.
Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maaftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia stahiki itaanza kulipwa kwa wananchi 2,020 kuanzia mwezi Juni, 2017 hadi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018. Taasisi ya UTT - PID kwa kushirikiana na Halmashauri inatarajia kutumia shilingi 7,523,000,000 kwa ajili ya malipo ya fidia kabla ya kuanza kwa kazi ya upimaji wa viwanja. Ofisi ya Rais - TAMISEMI ilitoa kibali cha kuendelea na utekelezaji wa mradi kupitia barua yenye Kumb. Na. GB. 203/234/01/117 ya tarehe 02/09/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ulipaji wa fidia haukuanza mapema kutokana na kampuni husika ya UTT -PID kutokuwa na Bodi. Bodi imeshaundwa na makubaliano ya pamoja yamefanyika katika kikao cha tarehe 02/05/2017 baina ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, UTT – PID na Halmashauri.
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Wananchi wa Songea Mjini wamekuwa wakiitumia Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kama Hospitali yao ya Wilaya hivyo kufanya kuwepo na mgongano wa kiutendaji kati ya Mamlaka ya Mkoa inayoitambua Hospitali hiyo kama Rufaa ya ngazi ya Mkoa na Mamlaka ya Wilaya. Tarehe 10 Januari, 2016, Mheshimiwa Waziri wa Afya alifika kuona hali halisi na juhudi za wananchi wa Songea Mjini za kujenga Kituo cha Afya Mji Mwema ambacho kimefikia hatua kubwa, hivyo wakamwomba Waziri kituo hicho kipandishwe hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya, Songea Mjini.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuiacha Hospitali ya Mkoa ifanye kazi ya Rufaa Kimkoa?
(b) Je, Serikali haioni haja ya kupunguza msongamano katika hospitali hiyo kwa kuanzisha Hospitali ya Wilaya Songea Mjini?
(c) Je, ni lini basi Serikali itakipa hadhi Kituo cha Afya cha Mji Mwema, Songea Mjini ya kuwa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma inatakiwa kutoa huduma za rufaa kama inavyofanyika kwa Hospitali zote za Mikoa nchini. Hata hivyo, mahali ambapo hakuna Hospitali ya Wilaya, wagonjwa hawazuiliwi kwenda katika Hospitali ya Mkoa kwa ajili ya matibabu. Mpango uliopo ni kuimarisha Zahanati na Vituo vya Afya ndani ya Halmashauri ili viweze kutoa huduma kwa wagonjwa wengi ili kupunguza msongamano katika Hospitali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakusudia kuboresha Kituo cha Afya cha Mji Mwema ili kiweze kutoa huduma bora za matibabu kwa lengo la kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mkoa kwa sasa. Serikali itatoa kipaumbele kwa mpango wowote wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea juu ya uanzishwaji wa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Mji Mwema kimeshaombewa kibali kuwa Hospitali. Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeshakagua kituo na kuelekeza yafanyike maboresho ya miundombinu inayohitajika ili kiweze kukidhi vigezo vya kuwa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, imepanga kukutana tarehe 17 Mei, 2017 ili kujadili utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya Afya.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE (K.n.y. MHE. BERNADETA K. MUSHASHU) aliuliza:-
Wazabuni wanaotoa huduma shuleni wanaidai Serikali fedha nyingi kwa huduma walizotoa miaka iliyopita.
(a) Je, Serikali inadaiwa fedha kiasi gani na kwa miaka ipi na wazabuni hao?
(b) Je, ni lini madai hayo yatalipwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa wapo wazabuni mbalimbali ambao wanaidai Serikali baada ya kutoa huduma Serikalini. Wapo wazabuni waliotoa huduma za vyakula katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum za msingi na shule za bweni za sekondari na wazabuni waliochapisha na kusambaza vitabu shuleni. Kiasi cha shilingi bilioni 54.86 zinadaiwa na wazabuni waliotoa huduma ya chakula, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 9.907 ni za wazabuni waliotoa huduma ya uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya shule za msingi. Hivyo jumla ya deni ni shilingi bilioni 64.767.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa madeni haya ni yale yaliyojitokeza kabla ya Serikali kuanza kutekeleza elimu msingi bila malipo. Kwa kutambua umuhimu wa kuwalipa wazabuni hawa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 13.239 hadi kufikia Mei, 2016. Wazabuni wengi ambao madeni yao hayajalipwa hadi sasa wataendelea kulipwa kwa awamu kwa kadri ya uwezo wa Serikali na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba wazabuni hawa wawe na uvumilivu kama ambavyo wamekuwa wakifanya wakati Serikali ikiendelea kulipa madeni haya ikiwa ni pamoja na madeni mengine ya ndani.
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-
Kwa sasa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo Jijini Dar es Salaam kimezidiwa uwezo wa kutoa huduma kwa ufanisi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vituo vingine kikanda ili kuboresha huduma za usafiri wa mabasi yanayoingia na kutoka mikoani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ipo katika mipango ya kuanzisha vituo vingine mbadala vya mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani baada ya kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo kuzidiwa uwezo wa kutoa huduma kwa ufanisi kama ifuatavyo:-
(a) Kituo cha mabasi Mbezi Luis, chenye eneo la mita za mraba 68,000 kitahudumia mabasi yatokayo katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Rukwa, Iringa, Ruvuma na Njombe); Kanda ya Ziwa (Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara, Geita na Simiyu); Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Manyara); Kanda ya Magharibi (Tabora, Kigoma na Katavi) na nchi za jirani za Malawi, DRC, Burundi, Rwanda, Zimbabwe na Zambia.
(b) Kituo cha mabasi cha Boko Dawasa chenye eneo la mita za mraba 63,121 kitahudumia mabasi yatokayo mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Mashariki (Arusha, Kilimanjaro na Tanga) na nchi za jirani za Kenya na Uganda.
(c) Kituo cha mabasi cha Kanda ya Kusini, kitatafutiwa eneo sehemu ya Kongowe kwa ajili ya kuhudumia mabasi yatokayo Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:-
Pamoja na lengo la Serikali kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi na kuzuia magonjwa ya mlipuko, Manispaa ya Mpanda ina changamoto ya ukosefu wa vifaa kama magari ya taka.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Manispaa ya Mpanda ina maroli mawili kati ya manne yanayohitajika kwa ajili ya kuzolea taka ngumu. Kutokana na changamoto hiyo, uongozi wa Manispaa umejiwekea mikakati ifuatayo:-
(i) Manispaa ya Mpanda imebinafsisha (outsource) shughuli ya uzoaji na udhibiti wa taka kwa mzabuni anayelipwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, mMzabuni huyu ana magari mawili na hivyo kufanya jumla ya magari kuwa manne.
(ii) Manispaa ya Mpanda imeanzisha mpango shirikishi jamii wenye jumla ya vikundi vya uzoaji na udhibiti wa taka ngumu katika mitaa 17, vimejengwa vizimba vitano kwa ajili ya kuhifadhia taka na vitakabidhiwa mikokoteni 17 tarehe 21/06/2017 siku ya uzinduzi.
(iii) Kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi wananchi wote hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya makazi, biashara na maeneo mbalimbali ya kufanyia kazi.
(iv) Kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi usafi wa kina hufanyika ambapo wananchi pamoja na viongozi mbalimbali hushiriki kufanya usafi katika maeneo yao.
(v) Siku hiyo ya Ijumaa kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi watumishi wa Manispaa hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya Ofisi ya Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhamasisha usafi nchini ili kuepuka mlipuko wa magonjwa na kuongeza unadhifu wa miji yetu.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhamira ya dhati ya kuboresha maslahi ya Watumishi hususan Walimu kwa kutoa nyaraka mbalimbali ikiwemo Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa tarehe 20/10/2014 unaohusu mishahara na Posho ya Madaraka kwa Viongozi wa elimu (Responsibility Allowance):-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutekeleza waraka huo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) ili kuleta ufanisi wa kazi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 tangu tarehe 1 Julai, 2016 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Walimu Wakuu wanalipwa sh.200,000/= kila mwezi na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wanalipwa sh.250,000/= kila mwezi. Kwa mwezi mmoja, Serikali inatumia takriban shilingi bilioni 5.01 kwa ajili ya kulipa Posho za Madaraka kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya kufundishia ilijumuishwa katika Mshahara wa Walimu ili kuboresha maslahi ya Walimu wanapostaafu. Hata hivyo, Serikali hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inafanya mapitio ya kazi kwa watumishi wote nchini ili kuboresha maslahi kwa kuzingatia uzito wa kazi.
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini mradi wa maji wa Chankolongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilianza kutekeleza mradi mpya wa maji wa Chankolongo mwaka 2014/2014 ukiwa ni mojawapo ya miradi ya vijiji 10 kwa kufanya usanifu upya na kusaini mikataba ya ujenzi mwezi Machi, 2014 wenye thamani ya shilingi bilioni 4.39 baada ya mradi wa awali wa Nyakagomba kushindikana hadi kuchakaa kwa miundombinu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi unalenga kutumia chanzo cha Ziwa victoria na utahudumia vijiji vinne vya Chankolongo, Chikobe, Chigunga na Kabugozo vyenye wakazi wapatao 24,724. Kazi yote ina mikataba sita iliyoandaliwa na kusimamiwa na COWI (T) Consulting Engineers and Planners kwa kushirikiana na Association with Environmental Consult Limited. kama Mtaalam Mshauri. Malipo yaliofanyika hdi ssa ni kiasi cha shilingi bilioni 1.99 ambayo ni sawa na asilimia 45.3 ya gharama ya mradi, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulikumbwa na changamoto kutokana na uwezo mdogo wa mkandasi (Fare Tanzania Limited) aliyekuwa akijenga choteo na kusambaza mabomba. Hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imesukuma utekelezaji wa mradi huu ambapo mkandarasi (Fare Tanzania Limited) ameingia makubaliano (sub contract) na kampuni nyingine iitwayo Katoma Motor Factors Limited ambayo inaleta mabomba yote ya mradi pamoja na pampu ndani ya mwezi huu wa Julai 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ya sasa mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba, 2017.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Kumekuwa na mrundikano wa wagonjwa kwenye Hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana:-
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya mpya katika Mkoa wa Dar es Salaam.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni, Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 10 katika Kata ya Somangila kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali kubwa ya Wilaya ya Kigamboni. Ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kufanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali ya Morocco. Kwa sasa Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Morocco ili kuanza ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kuboresha Zahanati na vituo vya afya vilivyopo ambapo katika bajeti ya mwaka 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 557.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.
MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:-
Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji; hata hivyo Wenyeviti hao wamekuwa wakifanya kazi kwa kujitolea bila kulipwa posho za kujikimu na Serikali imekuwa ikiahidi kuangalia uwezekano wa kuwalipa posho za kujikimu viongozi hao:-
Je, ni lini sasa Serikali itaacha kuendelea kuahidi juu ya malipo hayo na kuanza utekelezaji kwa kuanza kuwalipa viongozi hao posho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Ahmed Badwel, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inathamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na viongozi wa vijiji na mitaa katika kusimamia shughuli za maendeleo katika ngazi ya msingi ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka utaratibu ambapo posho za viongozi wa Serikali za vijiji na vitongoji zinalipwa na Halmashauri kupitia asilimia 20 iliyotengwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na kurejeshwa kwenye vijiji. Napenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge tushirikiane katika kuzisimamia Halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinatengwa na kulipwa posho stahiki. Hata hivyo, kutokana na baadhi ya halmashauri kushindwa kutekeleza suala hili kikamilifu, suala la kutenga asilimia 20 litawekwa katika sheria kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ambayo inatarajiwa kuletwa Bungeni ili kurekebisha kasoro zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kuendelea kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ili kujenga uwezo mkubwa zaidi wa kulipa posho hizo.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Wilaya ya Serengeti ni kitovu cha utalii na ni Wilaya inayopata watalii wengi lakini haina Hospitali ya Wilaya na hivyo kuleta usumbufu kwa wageni pamoja na wakazi wa Serengeti:- Je, ni lini Hospitali ya Wilaya itakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Halmashauri
ya Wilaya ya Serengeti haina hospitali ya Wilaya, hivyo wananchi hutumia Hospitali Teule ya Nyerere yaani DDH ambayo inamilikiwa na Kanisa la Mennonite Tanzania. Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti ulianza mwaka 2009 katika Kijiji cha Kibeyo ambao unafanyika kwa awamu. Katika awamu ya kwanza, jumla ya shilingi bilioni 5.4 zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya kuandaa michoro, kuanza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, pamoja na jengo la upasuaji (operating theater). Fedha hizo zinatarajiwa kupatikana kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo ruzuku kutoka Serikali Kuu, Mfuko wa Maendeleo wa Halmashauri, Benki ya Maendeleo ya Afrika, pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri (own source).
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa uandaaji wa michoro pamoja na jengo la upasuaji lenye vifaa vyote (operating theater) vimekamilika na kukabidhiwa kwa Halmashauri tayari kwa matumizi. Aidha, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeweka mpango wa kupeleka fedha ili jengo la wagonjwa wa nje (OPD) liweze kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali mbalimbali za Wilaya hapa nchini ili kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mji mdogo wa Lamadi kwa muda mrefu umeidhinishwa kuwa Halmashauri ya Mji Mdogo:- Je, lini sasa utekelezaji wake utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mwaka 2016 Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipokea maombi ya kupandisha hadhi Mji wa Lamadi kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lamadi. Mwezi Agosti, 2016, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilifanya uhakiki wa vigezo na taratibu zilizopo kwa mujibu wa sheria zoezi ambalo lilifanyika sambamba na maeneo mengine hapa nchini. Tathmini imeonesha kwamba kuna mambo ya msingi yanayotakiwa kukamilishwa yakiwemo kuwa na mpango wa uendelezaji wa mji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna miji midogo mingi inayochipua, Serikali inaendelea na mazungumzo na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) ambalo limeonesha nia ya kusaidia utekelezaji wa mpango huo ambao utawezesha kupima na kuweka miundombinu ya barabara na maji katika miji inayochipua ikiwemo Lamadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pindi baadhi ya vigezo vikikamilika, Serikali haitasita kuupandisha hadhi Mji Mdogo wa Lamadi kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lamadi.
MHE. DOTO M. BITEKO aliuliza:-
Wilaya ya Bukombe ina mahitaji ya walimu wa shule za msingi 1,425; waliopo ni walimu 982 na upungufu ni walimu 443:- Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa shule za msingi wa kutosha kuondoa upungufu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko, Mbunge wa Bukombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua upungufu wa walimu uliopo nchini ambapo mahitaji ya walimu wa shule za msingi ni walimu 235,632; waliopo ni walimu 188,481 na upungufu ni walimu 47,151.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imejipanga kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo walimu wa shule za msingi ili kupunguza pengo lililopo. Aidha, Serikali inakamilisha mpango wa kuwahamishia shule za msingi walimu wa ziada wa masomo ya sanaa wanaofundisha shule za sekondari. Utaratibu huu utasaidia shule za msingi kupata walimu wa kutosha ili kuboresha taaluma.
MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza:-
Hospitali ya Vwawa Wilayani Mbozi inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa vitanda vya kulalia wajawazito pamoja na vile vya kujifungulia, pia wodi ya akinamama ni ndogo huku ukizingatia kuwa hospitali hiyo inahudumia Wilaya ya Mbozi na Momba:-
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya akinamama kubwa yenye vifaa vya kutosha ili wanawake hawa waondokane na adha ya kulala wawili wawili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi yaani Vwawa ni hospitali iliyopandishwa hadhi kutoka Kituo cha Afya kuanzia mwaka 2001. Kwa sasa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wengi kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Wilaya za Momba, Mbozi na Ileje. Ili kuboresha huduma ya uzazi katika hospitali hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018, imepanga kutumia jumla ya shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa wodi ya wazazi baada ya kujifungua (post natal ward) ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja na kuondoa msongamano uliopo hivi sasa.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhana ya ugatuaji madaraka kwa wananchi ili kuharakisha maendeleo, hususan katika sekta za afya na elimu:-
Je, Serikali inasema nini kuhusu mfumo huo kutokuwa na tija endelevu katika sekta hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dhana ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi (Decentralisation by Devolution) inatokana na Ibara ya 145 na Ibara 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Madhumuni ya kupeleka madaraka kwa umma yakiwemo madaraka ya kisiasa, kifedha na kiutawala ni kusogeza madaraka ya kufanya maamuzi kwa wananchi ili kuboresha, kuimarisha utoaji wa huduma kulingana na matakwa yao ya kuboresha maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kupata mafanikio katika sekta ya afya na elimu kwa kuwashirikisha wananchi katika kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi na Sekondari (MMEM na MMES) na Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM). Kupitia utekelezaji wa hiyo fursa ya elimu ya msingi na sekondari zimeweza kuongezeka kutokana na ujenzi wa miundombinu ya elimu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Vilevile huduma za afya zimeimarishwa kwa kuratibiwa kwa karibu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ugatuaji wa madaraka kwa wananchi bado ni dhana muhimu kwa nchi yetu kwani ndio mfumo unaotoa fursa kwa wananchi kuweza kushiriki katika maamuzi na utekelezaji wa vipaumbele vyao katika mchakato mzima wa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Kwa muda wa zaidi ya miaka miwili, Hospitali ya Wilaya ya Kibondo haina mganga wa meno licha ya hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wengi kwa sasa ikiwemo wakimbizi kutoka nchini jirani ya Burundi:-
Je, ni lini Serikali itapeleka mtaalam wa meno katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Injinia Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishapeleka mtaalam wa meno (Daktari Msaidizi wa Meno) tangu tarehe 12/4/2016. Kwa sasa yupo katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo na anaendelea kutoa huduma kwa wagonjwa.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Kumekuwa na wimbi la mabweni na hata shule kuungua moto, hususan Tanzania Bara. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulikuwa na wimbi la shule kuungua moto na mwaka 2016 pekee kuanzia mwezi Januari hadi Disemba nchi ilikuwa na janga kubwa la kuunguliwa na shule za sekondari 29, zikiwemo mbili zisizo za Serikali na shule za msingi mbili ikiwemo moja isiyo ya Serikali.
Matukio hayo yalitokea mfululizo na hata shule nyingine kukumbwa na tatizo hilo zaidi ya mara moja. Mbaya zaidi, katika mwezi wa Agosti, 2016 kasi ya matukio ya shule kuungua moto iliongezeka ambapo kati ya tarehe Mosi hadi 12 Agosti, 2016 jumla ya shule za sekondari za Serikali tano ziliungua. Tumeshukuru Mungu mwaka 2017 matukio haya ya moto hayajatokea tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa hakuna uhakika wa chanzo halisi cha matukio haya moto yanayojitokeza. Hata hivyo, inadhaniwa kuwa chanzo cha moto hususan katika shule kongwe ni hitilafu ya umeme iliyotokana na uchakavu wa miundombinu na hujuma kutoka kwa watu na vikundi visivyo na nia njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, majanga ya moto katika shule zetu yanaweza kudhibitiwa ikiwa wote kwa pamoja tutashirikiana kutambua na kudhibiti viashiria na vyanzo ambavyo huleta majanga hayo. Serikali imetoa maelekezo kwa Mikoa, Halmashauri na wadau wengine wa elimu ili kudhibiti majanga ya moto mashuleni ikiwa ni pamoja na uundwaji wa Kamati za kukabiliana na majanga katika ngazi ya Halmashauri na katika ngazi za shule husika kwa kushirikisha wadau muhimu wa elimu katika ngazi mbalimbali.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali katika Wilaya mpya ya Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe imeanza maandalizi ya awali ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa kutenga eneo la ekari 60 katika kijiji cha Igwachanya ambalo limetolewa na wananchi bila kuhitaji fidia. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 35 kwa ajili ya kupima eneo hilo na kuliweka mipaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 24 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya maandalizi ya awali ili kuanza ujenzi. Serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri katika kusukuma vipaumbele vilivyoainishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe sambamba na kutafuta fedha ili kufanikisha huduma ya afya kwa wananchi wa Wanging’ombe.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-
Serikali inapaswa kuharakisha upimaji wa ardhi na utoaji wa hati za viwanja katika Jimbo la Kibamba ili kuepusha makazi holela.
(a) Je, ni maeneo gani ambayo hayajapimwa na lini yatapimwa?
(b) Je, kuna mpango gani wa kupunguza gharama na muda wa upimaji na utoaji wa hati ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma tajwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Kibamba, maeneo ambayo bado hayajapimwa yapo katika kata za Manzese, Mabibo na baadhi ya sehemu katika Kata za Ubungo, Mburahati, Kimara, Saranga, Goba, Mbezi, Kibamba, Kwembe na Makuburi. Tayari upimaji unaendelea katika Kata ya Kimara ambapo viwanja 3,196 vimepimwa. Taratibu zinakamilishwa ili kuwapimia wananchi 186 waliolipia gharama katika kata ya Kibamba ambao unahusisha upimaji wa maeneo ya huduma za umma 123 katika Manispaa ya Ubungo. Aidha, upimaji umepangwa kufanyika katika Kata za Mbezi, Msigani, Goba na Kwembe kupitia kampuni binafsi zilizoidhinishwa na Serikali ili kuharakisha zoezi hilo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, viwango vya gharama
za upimaji vinavyotumika sasa vipo kwa mujibu wa sheria ambavyo vilipangwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali na kwa kuzingatia matumizi ya zana za kisasa za upimaji ikiwemo mifumo ya kijiografia na kompyuta (Geographical Information System). Matumizi ya mifumo hiyo imerahisisha zaidi upimaji ambapo ramani za hati (deed plan) katika Manispaa ya Ubungo zimeongezeka na kufikia hati 1,000 kwa mwezi.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Serikali ilitoa Waraka Na.3 wa mwaka 2014 kuhusu Posho ya Madaraka kwa viongozi wa elimu wakiwemo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo na Waratibu Elimu Kata lakini tangu waraka huo utolewe yapata karibu miaka miwili sasa posho hiyo haijaanza kulipwa.
Je, ni lini Serikali itaanza kulipa posho hiyo ya viongozi wa elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Viongozi kuanzia Julai, 2016. Walimu Wakuu wanalipwa kiwango cha shilingi 200,000 kila mwezi na Wakuu wa Shule na Warataibu wa Elimu Kata wanalipwa Posho ya Madaraka kwa kiwango cha shilingi 250,000 kwa mwezi. Kuanzia Julai, 2016 hadi Aprili, 2017, Serikali imelipa posho hiyo jumla ya shilingi bilioni 1.87. Posho hiyo inalipwa kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa elimu katika ngazi ya shule nchini.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:-
Je, nini mkakati na sera ya Serikali kwa wafanyakazi hususani walimu wanaojiendeleza katika kuwapandisha madaraja na kuwaongezea mishahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za 2009, watumishi wa umma hupandishwa vyeo kwa kuzingatia sifa na ufanisi na utendaji kazi. Mwalimu anapohitimu mafunzo yake anastahili kubadilishiwa muundo wake wa utumishi mfano, Mwalimu Daraja la III - Stashahada kwenda Daraja la II ngazi ya Shahada. Kupanda daraja kwa mtumishi kunategemea utendaji kazi utakaothibitishwa na matokeo katika Mfumo wa Wazi wa Upimaji Utendaji Kazi wa mtumishi husika yaani OPRAS system. Watumishi wote wanatakiwa kujaza fomu hizo na kupimwa utendaji wao wa kazi kama wanastahili kupandishwa daraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kama ilivyoelezwa na Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, walimu wakiwemo watumishi wengine wenye sifa watapandishwa madaraja katika mwaka wa fedha 2017/ 2018 baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa watumishi.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-
Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani, Wabunge na Rais huchaguliwa na watu wanaoishi katika eneo la mipaka yake na wote hawa wanafanya kazi ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
Je, Serikali imeridhika na malipo wanayopata Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji katika kusimamia shughuli za maendeleo. Majukumu yanayotekelezwa na viongozi hao ni utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ambapo mipango yote na usimamizi yanafanywa katika ngazi za msingi za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya Waheshimiwa Madiwani kadri uchumi wa nchi unavyoruhusu. Kwa mfano posho ya Madiwani ilipandishwa mwaka 2015 kutoka shilingi 120,000 hadi shilingi 350,000 kwa mwezi. Kwa vipindi tofauti hususani Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipokutana na Waheshimiwa Madiwani katika mkutano wa ALAT hoja hii imekuwa ikijitokeza. Hata hivyo Serikali inalifanyia kazi jambo hili kulingana na mwenendo wa Kifedha wa nchi na jambo hili litakapokamilika utekelezaji wake utafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa hulipwa posho kutokana na asilimia 20 ya makusanyo ya ndani inayopaswa kurejeshwa kwenye ngazi ya msingi katika kata na vijiji. Kila Halmashauri imetakiwa kuhakikisha fedha hizo zinapalekwa kwenye vijiji kwa ajili ya shughuli za utawala ikiwemo kulipa posho na shughuli za maendeleo. Aidha, Halmashauri zimetakiwa kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ili kujenga uwezo wa kulipa posho hizo kupitia makusanyo yanayofanyika.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ni mpya na haina Hospitali ya Wilaya.
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ili wananchi wa Wilaya hiyo waweze kupata huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa jumla ya ekari 30 zimepatikana kwa gharama ya shilingi milioni 30 ili kupata eneo la ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 159.6 kutoka mapato ya ndani na shilingi milioni arobaini na tano kutokana na ruzuku ya maendeleo (CDG) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 371.16 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 169.9 zinatokana na mapato ya ndani na shilingi milioni 201.2 ni fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu (CDG).
MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:-
Kuna vyanzo vingine mbadala ya maji katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kama vile Mto Mbezi, Mto Ruvu na chanzo cha maji katika Kijiji cha Bamba Kiloka.
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi, kati na muda mrefu wa kutatua changamoto ya maji safi na salama katika vijiji vya Mkuyuni, Madam, Luholole, Kibuko, Mwalazi, Kibuko na Mfumbwe katika kupanua na kuongeza uwezo wa tanki la Mto Mbezi ili liweze kukidhi mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Fulwe unaogharimu shilingi bilioni 2.2; Gwata unaogharimu shilingi milioni 440.6; Chanyumbu unaogharimu shilingi milioni 785.7; Mkulazi unaogharimu shilingi milioni 216.7; Kibwaya unaogharimu shilingi milioni 627.2 na Kiziwa unaogharimu shilingi milioni 785.8. Aidha, halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 368.5 kwa ajili kufanya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika kijiji cha Mkuyuni na Kivuma ambao unatumia chanzo cha maji cha Mto Mbezi.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda wa kati, Halmashauri imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya maji ya mtiririko (gravity water schemes) ambao utahudumia vijiji vya Mwalazi, Luholole, Kibuko na Madam, Lubungo na Maseyu.
Mheshimiwa Spika, mpango wa maji wa muda mrefu utahusisha ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 19 vikiwemo vijiji kumi vya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Miradi hiyo itagharamu shilingi bilioni 8.62 kuanzia mwaka 2017 mpaka 2021.
MHE. ELIBARIKI E. KINGU aliluliza:-
Wilaya ya Ikungi hasa Jimbo la Singida Magharibi inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vituo vya afya na zahanati. Aidha, umbali mrefu wa kutafuta matibabu umekuwa ukisababisha adha na taabu kwa wananchi wa kata za Lyandu, Igelansomi na vijiji vya Mduguya, Kaangeni, Chengu na Mayahu.
Je, Serikali ipo tayari kushirikiana na wananchi katika kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya na vituo vya afya vilivyoanzishwa kwa ushirikiano wa wananchi na Mbunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Emmanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza miradi ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa kushirikisha nguvu za wananchi kupitia mpango wa fursa na vikwazo yaani O & OD. Serikali inampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi na wananchi wake kwa kuanza ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.
Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono juhudi hizo, Serikali imetoa ruzuku ya maendeleo kwa Halmashauri hiyo, kiasi cha shilingi milioni 110 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika Wilaya ya Ikungi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.49 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda ilikuwa ya bweni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, lakini sasa imekuwa ya kidato cha tano na sita tu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuirejesha shule hiyo kama ilivyokuwa awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda ilisajiliwa kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita pekee ili kukidhi malengo ya kuwa na shule za kutosha za Kitaifa katika Mkoa wa Katavi. Shule hii ni miongoni mwa shule saba za sekondari zenye kidato cha tano na sita kati ya shule 38 za sekondari zilizopo Mkoani Katavi. Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa shule za sekondari za kutwa za kidato cha kwanza hadi cha nne, Serikali imeona umuhimu wa kuongeza shule ya kidato cha tano na sita ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mpanda.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Tarafa inakuwa na sekondari ya kidato cha tano na sita. Serikali inatambua nia njema ya Mheshimiwa Mbunge kwa watoto wa eneo hilo. Hata hivyo, kama kuna ulazima wa kufanya hivyo, inahitajika maombi yafanyike kupitia taratibu husika za usajili wa shule. Serikali inaendelea kuboresha shule za kata zilizoko Mkoani Katavi ili kupunguza msongamano na kutoa elimu bora.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazo Mahakama Kuu mbili, ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar.
(a) Je, ni Mahakama ipi ipo juu ya nyingine?
(b) Je, kuna utaratibu gani wa ushirikiano katika kusimamia kesi au mashauri ambayo yanaanzia upande mmojawapo wa Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Mgogoni, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 108 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, kwa mujibu wa Muundo wa Mahakama katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna Mahakama ya Zanzibar iliyotamkwa katika Ibara 114 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 93 ya Katiba ya Zanzibar. Mahakama zote tajwa zina hadhi sawa katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, upo ushirikiano katika masuala ya utekelezaji wa amri za Mahakama katika suala linaloanzia upande mmoja wa Muungano ambalo limeshughulikiwa na kufikia mwisho. Ingawa kama ilivyoelezwa hapo juu, kila Mahakama ina hadhi sawa na nyingine na hivyo shauri lililoanza kusikilizwa upande mmoja, haliwezi kuhamishiwa upande wa pili ili kukamilisha usikilizwaji wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, shauri likianza kusikilizwa, linapaswa kusikilizwa na kuhitimishwa na Mahakama Kuu ya upande husika wa Muungano.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Serikali iliahidi kutoa shilingi milioni 60 kwa ajili ya mradi wa maji wa Sakare ulioko Tarafa ya Bungu na mpaka sasa imetoa shilingi milioni 20 tu; Je, ni lini fedha iliyobaki itatolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Sakare unahudumia jumla ya vijiji saba kutoka kwenye Tarafa ya Bungu vyenye wakazi wapatao 18,460. Ili kutekeleza ahadi iliyotolewa katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeidhinisha shilingi milioni 81.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Sakare. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi wa vijiji saba katika Tarafa ya Bungu waweze kupata maji safi na salama.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-
Mheshimiwa Rais alipokuwa anaomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015 aliahidi kuwa Serikali itakarabati mabwawa matatu ya josho, mto Mbu na Olkuro:-
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ili wananchi wa Esilalei waweze kupata maji kwa ajili ya mifugo yao?
(b) Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Sepeko na Lepurko maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS- TAMISEMI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius K. Laizer, Mbunge wa Monduli, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017, imekamilisha usanifu kwa ajili ya ukarabati wa mabwawa ya Joshoni na Olkuro na kubaini kuwa shilingi bilioni 1.45 zinahitajika kwa kazi hiyo. Mahitaji hayo yatazingatiwa katika mpango wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea
na utekelezaji wa miradi ya maji katika Vijiji vya Lendikinya Kata ya Sepeko ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 868.07. Kazi imefikia asilimia 35 na itakamilika mwezi Octoba, 2017 kwa kuzingatia mkataba. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeidhinisha shilingi milioni 639.5 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Nanja ambacho kipo Kata ya Lepurko ambao utahudumia pia shule ya Sekondari ya Nanja, Kata ya Sepeko.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Halmashauri za Wilaya ya Nkasi na Sumbawanga Mjini hazina Hospitali ya Wilaya; wanawake na watoto wanapata shida ya matibabu wakati wa kujifungua na huduma za watoto.
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali katika Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa umeanza taratibu za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika eneo la Milanzi. Hospitali ya Mkoa inayotumika sasa itabaki kuwa Hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga wanapata huduma za afya katika Hospitali Teule ya Dkt. Atman inayomilikiwa na Kanisa ambayo imeingia mkataba na Serikali wa utoaji huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Taratibu za kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo zinakamilishwa. Kwa sasa wagonjwa wanapata huduma katika Hospitali Teule iliyopo pamoja na vituo vya afya na zahanati. Serikali itajitahidi kutafuta fedha na kushirikiana na wananchi wa Nkasi ili kufanikisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. JAMES F. MBATIA) aliuliza:-
LEKIDIA imeweza kushirikiana na wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki na kufanikiwa kukarabati barabara za kata hiyo zenye urefu wa kilometa 17 kwa gharama ya shilingi milioni nane, lengo kuu ni ujenzi wa barabara inayoanzia Uchira hadi Kolaria yenye urefu wa takribani kilometa 12 kwa kiwango cha lami; na LEKIDIA wamefanikiwa kufanya harambee na kupata shilingi milioni 130 ambapo shilingi milioni 60 zimetumika kununua mapipa 300 ya lami na kubakiwa na shilingi milioni 70.
Je, Serikali itashirikianaje na LEKIDIA kutekeleza mradi huo kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Uchira -Kisomachi - Kolaria yenye urefu wa kilometa 12 ilijengwa kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 300 kutoka katika Mfuko wa Barabara katika mwaka wa fedha 2013/2014. Barabara hiyo imeendelea kufanyiwa matengenezo ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 zilitumika shilingi milioni 74.2 ili kuifanya ipitike wakati wote. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 31 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa nane na matengenezo ya sehemu korofi kilometa mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapongeza juhudi kubwa inayofanywa na LEKIDIA. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) itafanya tathmini ya barabara zote nchini pamoja na barabara ya Uchira hadi Kolaria ili kuona namna bora ya kuziboresha barabara hizo kwa kiwango kinachohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa barabara ili kuhakikisha barabara hiyo inafanyiwa matengenezo kurahisisha usafiri na usafirishaji.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna vituo vitatu vya afya. Kituo cha Afya Mtina kina zaidi ya miaka 30 hakijafanyiwa ukarabati na pia hakuna wodi ya wazazi.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika kituo hicho na kufanya ukarabati ili kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa vijiji vya Nasya, Semeni, Nyerere, Angalia na wakazi wa kata ya Mchesi na Lukumbule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na nguvu za wananchi imekamilisha ujenzi wa zahanati sita za Njengi, Mwenge, Tuwemacho, Nasumba, Semeni na Kazamoyo ambazo zimeanza kutoa huduma.
Aidha, nampongeza Mbunge wa Jimbo kwa kuweka kipaumbele na kutumia shilingi milioni 6.2 kwa ajili ya ukarabati wa chumba cha kujifungulia na chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya Mtina.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaweka kipaumbele na kuhakikisha fedha zinatengwa kupitia Halmashauri katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha afya Mtina kinakamilika. Ahsante.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa walimu madai yao ya kusimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015 na mtihani wa kidato cha pili mwaka 2016?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, walimu waliosimamia mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2015 wanadai jumla ya shilingi bilioni 1.6 na walimu waliosimamia mitihani ya kidato cha pili mwaka 2016 wanadai jumla ya shilingi bilioni 3.2. Hivyo, jumla ya madai kwa mitihani yote miwili ni shilingi bilioni 4.89.
Mheshimiwa Spika, madeni hayo yamewasilishwa Hazina kwa ajili ya uhakiki ili walimu hao wapewe madai yao.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Fedha zinazokusanywa za asilimia 0.3 ya service levy zimeshindwa kusaidia Halmashauri nchini kwa uwiano unaolingana.
Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka fedha hizo kukusanywa na TAMISEMI ili kila Halmashauri iweze kupata mgao unaolingana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, service levy ni chanzo kinachokusanywa na Halmashauri kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kifungu cha 6(1) na 7(1). Ushuru huo unatozwa kutoka kwa makampuni, matawi ya makampuni na mfanyabiashara yeyote mwenye leseni ambaye anafanya shughuli zake katika Halmashauri husika. Hivyo, Halmashauri ndiyo yenye mamlaka ya kukusanya ushuru huo kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kazi yake ni kuandaa sera, sheria, kanuni na miongozo na kusimamia utekelezaji wake kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuboresha utaratibu unaotumika kukusanya ushuru huo kwenye Halmashauri kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ili kuondoa utata uliokuwepo ambapo makampuni yalikuwa hayalipi ushuru huo kwa kuzingatia kuwa unalipwa Makao Makuu ya Kampuni.
Mheshimiwa Spika, Bunge litapata fursa ya kujadili marekebisho hayo ambayo yanakusudia kuziwezesha Halmashauri kukusanya ushuru wa huduma kwa kiwango cha kuridhisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. DAVID E. SILINDE) aliuliza:-
Katika Tarafa ya Kamsamba kuna Shule ya Sekondari ya Wazazi inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM ni muda mrefu sasa shule hiyo haitumiki na haina mwanafunzi hata mmoja na hivyo kufanya majengo yake kuharibika.
Je, kwa nini Serikali ya Awamu ya Tano isirudishe shule hiyo kwa wananchi ili waweze kuitumikia au kubadili matumizi na kuwa Chuo cha Ufundi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ernest David Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Kamsamba, iliyoko katika Tarafa ya Kamsamba, Wilaya ya Momba ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM haitumiki na haina wanafunzi. Shule hii ni ya kutwa kwa wavulana na wasichana, kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 225 iwapo miundombinu yake yote itakamilika na kutumika.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri itafanya mazungumzo na mmiliki wa shule ili kuona uwezekano wa kurejesha majengo hayo Serikalini ili shule ianze kupokea wanafunzi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY aliuliza:-
Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilipeleka maombi maalum ya fedha za ujenzi wa daraja la Gunyoda na wakati huo kutokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Mbulu kupata Wilaya mbili, daraja la Gunyoda limebaki kuwa kiungo muhimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mbulu vijijini.
Serikali Kuu ilitoa kiasi cha Sh.100,000,000/= ambazo Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Mbulu kwa maagizo ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne fedha hizo zilielekezwa kwenye ujenzi wa maabara za sayansi katika Halmashauri zote nchini na kuacha daraja hilo bila kujengwa kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu haina uwezo wa kulijenga kwa fedha za ndani:
(i) Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi wa daraja hilo ambalo ni kikwazo kikubwa kwa huduma za kijamii katika Halmashauri zote mbili?
(ii) Kwa kuwa mabadiliko ya Tabianchi yamesababisha uwepo wa makorongo makubwa ambayo yako katika Kata za Gonyoda, Silaloda, Gedamara, Bargish, Dandi, Marangw’ na Ayamaami jambo linalosababisha jamii kukosa huduma za jamii, afya na utawala. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta fedha za dharura ili kusaidia janga hilo katika Halmashauri mbalimbali ikiwemo Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Mbulu linalopita kwenye Korongo la Gunyoda lenye urefu wa mita 70.4 na kina cha mita tano lilifanyiwa usanifu wa awali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na kubaini kwamba zinahitajika shilingi milioni mia nane na hamsini kulijenga. Hadi sasa ni muda mrefu umepita, hivyo Serikali kupitia Wataalam wa Halmashauri itafanya usanifu wa kina kujua gharama halisi za kuingiza katika mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuanza ujenzi.
(ii) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwkaa wa fedha 2017/2018 Serikali inaanza utekelezaji wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambao utatekelezwa kwenye halmashauri 15 ili kuandaa mpango wa kuzingatia athari za tabianchi. Serikali itashirikiana kikamilifu na halmashauri ili kuhakikisha fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya matengenezo ya dharura. Natoa wito kwetu sote kwa pamoja tushirikiane kikamilifu katika kutunza mazingira.
RITTA E. KABATI aliuliza:-
Mwaka 2000 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini:-
Je, hali ya utekelezaji wa mpango huo wa TASAF ikoje?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali na Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mwaka 2000 ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini. Mafanikio makubwa yamepatikana katika awamu zote za utekelezaji kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa awamu ya kwanza ambayo ilitekelezwa mwaka 2000 hadi mwaka 2005 iliwezesha jamii kutekeleza miradi 1,704 yenye thamani ya shilingi bilioni sabini na mbili katika halmashauri 40 za Tanzania bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Miradi hiyo iliibuliwa na wananchi na ilihusisha sekta zote muhimu za afya, elimu, maji pamoja na barabara vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa awamu ya pili, TASAF ilitekelezwa mwaka 2005 hadi mwezi Juni, 2013 ambapo miradi 12,347 yenye thamani ya shilingi bilioni 430 katika halmashauri 126 za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Miradi hii iliongeza upatikanaji wa huduma za maji, elimu, afya, pamoja na barabara vijijini na kuongeza upatikanaji wa chakula
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya tatu ilizinduliwa mwaka 2012 na utekelezaji wake ulianza mwezi Januari, 2013 na unaendelea kutekelezwa hadi mwaka 2022 katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Madhumuni ya TASAF awamu ya tatu ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato, fursa pamoja na uwezo wa kuwagharamia mahitaji muhimu. Kazi zilizofanyika katika awamu ya tatu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kaya maskini milioni 1.1 zenye jumla ya watu takribani milioni tano zimeandikishwa katika vijiji, mitaa na shehia 9,986. Hadi kufikia mwezi Agosti mwaka huu kaya hizi masikini zilishapokea ruzuku ya shilingi bilioni 521.9. Kaya hizo pia zimetekeleza miradi ya kutoa ajira za muda kwa kaya za walengwa 354,648 kutoka katika halmashauri 42 za Tanzania Bara pamoja na Tanzania Zanzibar. Hadi kufikia Agosti mwaka huu, jumla ya miradi 3,553 yenye thamani ya shilingi bilioni 51.1 kutoka katika vijiji 2,063, mitaa 329 na shehia 168 imeibuliwa na kutekelezwa. Hadi sasa miradi 2,952 imekamilika; lakini pia miradi 601 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa kukamilishwa katika mwaka huu wa fedha
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Agosti mwaka huu, miradi ya kuendeleza miundombinu ya huduma za jamii 192 yenye thamani ya shilingi bilioni nane imetekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, mpango wa kuhamasisha kaya kuweka akiba na kuwekeza unatekelezwa na umewawezesha walengwa kushiriki katika kuweka akiba katika vikundi na kutekeleza miradi ya ujasiriamali ikiwa ni mkakati endelevu wa kaya kutoka kwenye umaskini. Jumla ya vikundi 5,136 vya kuweka akiba na kuwekeza vyenye wanachama 11,907 vimeundwa katika Halmashauri sita za Tanzania Bara ambazo ni Kibaha, Bagamoyo, Chamwino, Lindi, Mtwara pamoja na Manispaa ya Lindi, Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Walimu Wilayani Biharamulo na kwingineko nchini wanalalamika kwamba jitihada zao kwenda masomoni kujiendeleza zinafuatiwa na kusitishwa kwa upandaji wa madaraja yao katika utumishi wa umma. Pale ambapo mwalimu kapanda daraja kunaenda sanjari na yeye kuwa masomoni.
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kero hii na kukatishwa tamaa kwa walimu wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawapongeza walimu wote na wataalam mbalimbali wanaojiendeleza kwa lengo la kuongeza ufanisi wao wawapo kazini. Kwa utaratibu wa sasa kupanda daraja kunaendana na matokeo ya ufanisi kazini baada ya kupimwa jinsi mtumishi alivyotekeleza malengo yake. Kwa utaratibu uliopo, mwalimu aliyejiendeleza hadi ngazi ya stashahada au shahada anapaswa kubadilishiwa muundo baada ya kuwasilisha vyeti vyake kwa mwajiri wake. Hivyo, waajiri wote wanapaswa kuzingatia taratibu za utumishi kwa kutenga bajeti kwa watumishi walio katika maeneo yao.
MHE. ORAN M. NJEZA (K. n. y MHE. HAROON M. PIRMOHAMED) aliuliza:-
Mji Mdogo wa Rujewa ni kitovu cha shughuli za biashara na Makao Makuu ya Wilaya ya Mbarali na kwa bahati mbaya barabara nyingi za mji huo hazipitiki kutokana na ubovu. Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliahidi kujenga kilometa tano za barabara kwa kiwango cha lami.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo kwa wananchi wa Mbarali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri Wilaya ya Mbarali iliidhinishiwa na kupokea shilingi milioni 793.02 kwa ajili ya matengenezo ya barabara kilomita 20, kalavati kubwa 17 na matengenezo ya madaraja matano. Serikali itafanya kila liwezekanalo ili ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais iweze kutekelezwa ndani ya miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani. Halmashauri imepanga kuweka kipaumbele na kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuanza utekelezaji wa ahadi ya kujenga kilometa tano za barabara kwa kiwango cha lami kwa usimamizi wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA).
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Zaidi ya wananchi 181 wa kijiji cha Ngadinda Halmashauri ya Madaba wanalima ndani ya Wilaya ya Namtumbo kwa sababu ya kukosa eneo katika kijiji chao. Baraza la Madiwani lilishauri sehemu ya shamba la hekta 6,000 la Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lililopo ndani ya kijiji hicho ambalo lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ili litumike kwa shughuli za kilimo na sehemu ibaki kwa ajili ya mifugo. Hivi sasa wafugaji toka maeneo mbalimbali nchini wapo katika shamba hilo lakini wakulima hawajatengewa eneo.
(a) Je, Serikali haioni kwamba kitendo hicho ni ubaguzi na kinaweza kuchochea migogoro kati ya wafugaji na wakulima?
(b) Je, ni lini Serikali itasikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Ngadinda cha kutengewa eneo la kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mwaka 2014 iliunda Tume ya kuchunguza matumizi ya shamba hilo ambalo lilikuwa linamilikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kubaini kuwa shamba hilo halitumiki vizuri kwa shughuli za ufugaji. Kwa msingi huo Tume ilipendekeza hekta 4000 wapewe wananchi wa Kijiji cha Ngadinda na eneo linalobaki la hekta 2000 libaki kwa shughuli za uwekezaji na ufugaji. Hata hivyo, baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Songea kugawanywa na kupata Halmashauri mpya ya Wilaya ya Mababa uamuzi huo haukutekelezwa. Hivyo, Halmashauri ya Madaba inatakiwa kujadili suala hili katika vikao vya Halmashauri na kufanya uamuzi kuhusu matumizi ya shamba hilo kwa kuzingatia maslahi ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika sehemu (a) ya jibula msingi, Halmashauri ndiyo yenye jukumu la kujadili na kukubaliana kuhusu matumizi ya shamba hilo lililokuwa linatumika kwa shughuli za ufugaji. Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha maslahi ya wakulima na wafugaji yanazingatiwa kuhusu matumizi ya shamba hilo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha Kata mpya ya Mkanana ambayo ina vijiji vya Mkanana na Chibwegele na vipo mlimani ambapo hakuna huduma yoyote kama vile barabara ambayo ni mbaya sana na hupitika kwa shida wakati wote.
Je, mpango huo wa kuanzisha Kata mpya umefikia wapi?
Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba kuanzishwa kwa kata hiyo kutawezesha kuwasogezea karibu huduma mbalimbali wananchi wa kata hiyo kuliko ilivyo sasa ambapo Makao Makuu yapo Kijiji cha Chitemo, umbali wa kilometa 45?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Geogre Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kwa jitihada anazozifanya kupeleka maendeleo katika Jimbo lake. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria maombi ya kugawa kata mpya yanaanzia katika Mikutano Mikuu ya Vijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa. Vikao hivyo vikikubali maombi hayo na endapo yataonekana yamekidhi vigezo, Serikali haitasita kuanzisha Kata hiyo ya Mkanana kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha maeneo mapya ya utawala zikiwemo kata, ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Hivyo, kama ilivyoelezwa katika sehemu
(a) ya jibu langu hapo juu, endapo Kata ya Mkanana itakidhi vigezo vya kuanzishwa, ili kurahisiaha upatikanaji wa huduma na kuchochea maendeleo katika kata hiyo, itafanyika.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Barabara inayounganisha Vijiji vya Msanga na Kawawa ni muhimu sana kiuchumi kwa Kata ya Msanga na Wilaya ya Chamwino na pia mazao mengi ya uhakika kutoka Kawawa na Vitongoji vyake lakini barabara hiyo ni korofi sana kwa sababu ya mbuga iliyopo kati ya vijiji hivyo viwili na daraja kubwa lililopo limevunjika kabisa kiasi kwamba halipitiki kabisa wakati wa mvua na wakati wa kiangazi hupitika kwa taabu sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha barabara hiyo na kulijenga daraja husika ili kuboresha mawasiliano ya vijiji hivyo viwili na masuala ya usafirishaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 ilitoa shilingi milioni 40 ambazo zimejenga kivuko (box culver) na kufungua mifereji ya kuitisha maji ya mvua (river draining). Aidha, mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetumia shilingi milioni 100 kuifungua barabara hiyo urefu wa kilomita 8, kujenga madaraja mbonyeo (solid drifts) matano likiwemo la mita 50 katika mto unaopitisha maji kutoka Hombolo na kuweka changarawe sehemu korofi kwa urefu wa kilomita 1. Serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ili kuhakikisha daraja hilo linatengewa fedha na kujengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 kupitia TARURA.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la maji katika Wilaya ya Musoma Vijijini hasa vijiji vya Kabulabula, Bugoji, Kangetutya na Saragana. Aidha, visima vilivyochimbwa na wanakijiji hao vinakauka wakati wa kiangazi.
Je, ni lini Serikali itahakikisha programu za maji zinapelekwa na zinatekelezwa kwa umakini katika Wilaya ya Musoma Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bita Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli visima vingi hasa vilivyochimbwa na kufungiwa pampu hukauka wakati wa kiangazi na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma katika maeneo husika. Sababu kubwa ni mabadiliko ya tabianchi hali inayosababisha maji kupatikana katika kina kirefu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali kupitia Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Maji (WSDP II) imeanza kufanya usanifu wa mradi mpya utakaotumia Ziwa Victoria kama chanzo cha maji cha uhakika. Vijiji vitakavyoingizwa katika mpango huo ni Kabulabula, Bugoji na Saragana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Serikali ilikuwa na mpango wa kuchimba mabwawa katika vijiji vya Msagali, Bumila, Makutupa, Lupeta, Inzomvu, Vibelewele, Kimagai, Chunyu na Ng’ambi ambayo yatahudumia wananchi pamoja na mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Je, Serikali imefikia hatua gani ya utekelezaji wa mpango huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TASAF III imekamilisha uchimbaji wa malambo sita katika vijiji vya Bumila, Msagali, Lupeta, Chunyu, Kazania na Nzogole kwa gharama ya shilingi 83,194,200. Wananchi 19,304 watapata huduma ya maji kupitia vyanzo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu umefanyika katika kijiji cha Chunyu kwa ajili ya kujenga bwawa kubwa ambalo litahudumia vijiji vya Msagali, Berege, Kisokwe, Chunyu na Ng’ambi. Jumla ya shilingi bilioni 17 zitahitajika kukamilisha kazi hii. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza ujenzi wa bwawa hilo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:-
Wilaya ya Itilima ni mpya na ina eneo kubwa linalovutia kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha miundombinu ya barabara ya Migato, Nkuyu, Longalombogo, Laini, Bulombeshi na Bumera ili kuvutia watu kufanya biashara za mazao katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuunganisha maeneo ya Migato, Nkuyu, Longolombogo, Laini na Bulombeshi kwa uboreshaji wa mtandao wa barabara kama ifuatavyo:-
Barabara ya Bumera - Bulombeshi na Bumera - Gaswa - Sagata - Laini ya kilometa 20, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 imefanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa kunyanyua tuta na kuweka changarawe kilometa 3 na kujenga Kalavati 9 katika barabara ya Bulombeshi – Bumera - Gaswa. Katika bajeti ya mwaka 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 99.6 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum urefu wa kilometa sita na matengenezo ya kawaida urefu wa kilometa nane katika barabara ya Bumera - Gaswa - Laini.
Barabara ya Migato - Ndoleleji - Nkuyu yenye kilometa 22.9, mwaka wa fedha 2016/2017 imefanyiwa matengenezo katika maeneo korofi kwa kiwango cha changarawe na kujenga makalvati matatu katika barabara ya Migato - Ndoleleji yenye urefu wa kilometa 6.5.
Lagangabilili - Muhuze - Migato mpaka unapofika Longolombogo yenye kilometa 40, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 barabara hiyo imefanyiwa matengenezo katika kipande cha Lagangabilili - Muhuze - Migato kilometa 11 na kujenga makalvati kumi. Katika bajeti ya 2016/2017 yamejengwa makalvati sita na kuwekwa changarawe baadhi ya maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 15. Aidha, katika bajeti ya 2017/2018, jumla ya shilingi milioni 49.18 zimetengwa kwa ajili ya kufanya matengenezo mbalimbali katika barabara hii.
MHE. MUSSA R. SIMA (K.n.y. MHE. AISHAROSE N. MATEMBE) aliuliza:-
Watumishi wa sekta ya afya hususani madaktari wanatakiwa kuishi kwenye maeneo ya kazi ili inapotokea akahitajika inakuwa rahisi kuwahi kwenda kutoa huduma kwa wagonjwa. Hata hivyo, katika Mkoa wa Singida watumishi wengi wa sekta ya afya wanaishi mbali na eneo la kazi hivyo kuwa na changamoto kubwa na wakati mwingine kusababisha vifo vya wagonjwa wakiwemo wajawazito.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha watumishi wa sekta ya afya wanakuwa na makazi kwenye maeneo jirani ikiwa ni pamoja na kuboresha nyumba chache zilizopo pamoja na kujenga zingine mpya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida una jumla ya nyumba za watumishi wa sekta ya afya 345 kati ya nyumba 1,072 zinazohitajika. Hivyo, kuna upungufu wa nyumba za watumishi wa afya 737. Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi 21 katika vituo vya afya na zahanati. Aidha, shilingi milioni 280.8 zimetengwa katika mwaka 2017/2018 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa nyumba za watumishi wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutoa ruzuku ya maendeleo (Local Government Development Grant) ambayo inatumika kumalizia maboma yaliyoanza kwa nguvu za wananchi katika sekta za afya, elimu na sekta nyingine. Kipaumbele cha matumizi ya fedha hizo kinapangwa na Halmashauri zenyewe kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD).
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Wilaya ya Mkalama ni mpya na haina vitendea kazi kama vile magari katika katika Idara ya Afya na huduma za dharura zinapatikana makao makuu huku tarafa zikiwa zimetawanyika hivyo wananchi hasa wajawazito na watoto wamekuwa wakipoteza maisha kabla ya kufika hospitali kwa kukosa usafiri.
Je, ni lini Serikali itatoa gari la wagonjwa (ambulance) tatu kwa kila tarafa ikiwemo Makao Makuu ili kunusuru vifo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ina gari moja la kuhudumia wagonjwa lenye usajili wa namba SM 4263 ambalo lipo katika Kituo cha Afya Kinyangiri. Kwa sasa Halmashauri imeandaa mpango wa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Nyamburi ambacho kimewekwa katika mpango wa kufanyiwa ukarabati mkubwa kuwezesha huduma za upasuaji kutolewa.
Aidha, Serikali imepanga kuimarisha vituo vya afya na zahanati ili ziwe na uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wengi na kupunguza rufaa kwenda katika Hospitali ya Wilaya. Ofisi ya Rais, TAMISEMI itatoa ushirikiano wake pale Halmashauri hiyo itakapoweka kipaumbele katika kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa gari la wagonjwa katika eneo hilo.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali ina mpango gani wa kuwalipa posho au mishahara Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili kurahisisha ufanisi wa shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inathamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa katika maendeleo ya Taifa. Serikali imezingatia na kuweka utaratibu wa kushirikisha viongozi hawa wanaolipwa posho maalum kwa motisha kupitia asilimia 20 ya mapato yanayorejeshwa na Halmashauri kwenye vijiji. Asilimia 17 ya fedha hizo zinatakiwa kutumika kwa shughuli za utawala, ikiwemo kulipa posho ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa na asilimia tatu kwa shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuboresha utaratibu huu kwa kuingiza katika mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ili kuweka utaratibu mzuri wa urejeshaji wa asilimia 20 kwenye vijiji na kuwanufaisha walengwa. Aidha, tumeimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri zote ili kujenga uwezo wa kutenga asilimia 20 kwenda kila kijiji.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Kijiji cha Nyakanazi, Wilaya ya Biharamulo kiko kwenye njia panda kwenda Kigoma, Kahama, Ngara na kina wakazi wapatao 15,000. Kulingana na hali hiyo, kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinaibuka na idadi ya watu inaongezeka kwa kasi; aidha, kijiji hicho pia kimebanwa na hifadhi inayopakana nacho.
Je, Serikali ipo tayari kujadiliana na Halmashauri ya Wilaya na wakazi wa Nyakanazi ili kuona uwezekano wa upanuzi wa eneo la kijiji kwa upande wa hifadhi inayopakana na kituo cha polisi kwa nia ya kufungua fursa za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa ya mwaka 2002 Sura Na. 282, shughuli za makazi, ufugaji, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu huwa haziruhusiwi isipokuwa kama Wizara yenye dhamana ya Maliasili na Utalii itaruhusu kwa kibali maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, endapo ardhi ya Nyakanazi haitoshelezi mahitaji, kijiji kinapaswa kuwasilisha maombi ya ardhi ambayo yatajadiliwa katika vikao vya Halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa ili kupata ufumbuzi. Maoni hayo yatawasilishwa Wizara ya Maliasili na Utalii na endapo Wizara hiyo yenye dhamana itaridhia upanuzi wa eneo hilo la kijiji, basi unaweza kufanyika.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE ( K.n.y MHE. JOHN P. KADUTU) aliuliza:-
Kumekuwa na maombi ya kupata Wilaya na Halmashauri ya Ulyankulu kwa muda mrefu sasa. Pia zimetolewa ahadi za kuunda Wilaya na Halmashauri tangu mwaka 2010.
(a) Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi Wilaya na Halmashauri kwani vigezo vya kuwa Wilaya/Halmashauri ni kama vile vya Jimbo ambavyo tayari vimetimia?
(b) Je, ni kikwazo gani kimesababisha kutopata Wilaya/Halmashauri mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya kuanzisha Wilaya ya Ulyankulu ya mwaka 2010 hayakufanikiwa kutokana na kutokidhi vigezo vikiwemo idadi ya watu pamoja na sehemu kubwa ya eneo hilo kuwa ni hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maombi ya mwaka 2010 hayakukidhi vigezo na kwa sasa kama Halmashuari inaona eneo hilo limekidhi vigezo hivyo, tunashauri Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kuanzisha mchakato wa kujadili mapendekezo hayo upya na kuyapitisha katika Baraza la Madiwani na Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa na hatimaye kuwasilisha Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ili yaweze kufanyiwa kazi. Serikali haitasita kuridhia pendekezo hilo endapo litakuwa limekidhi vigezo na taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa mujibu wa Sheria.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Kampuni ya Group Sogesca Lanari Estero (GSLE) iliyokuwa inajenga barabara ya Nyanguge – Musoma kati ya mwaka 1979 – 1990 iliacha majengo katika Kijiji cha Yimtwila “A” ambapo Serikali kwa kushirikiana na wananchi wakaanzisha shule ya sekondari ya kutwa.
Je, ni kwa nini Serikali isitumie fursa ya uwepo wa majengo haya kupandisha hadhi shule hiyo kuwa ya kidato cha tano na sita kwa kuwa nyumba za walimu na mabweni yanaweza kupatikana?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo yaliyokuwa kambi ya Kampuni ya Group Sogesca Lanari Estero iliyokuwa inajenga barabara ya Nyanguge kwenda Musoma kati ya mwaka 1979 hadi 1990 kwa sasa yanatumika kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Sogesca ambayo ni ya kutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanikisha uwepo wa shule ya kidato cha tano na sita Wilayani Busega, Serikali imeweka kipaumbele cha kuanzisha shule ya sekondari Mkula kuwa ya kidato cha tano na sita katika mwaka wa fedha 2016/2017. Tayari Serikali imepeleka shilingi milioni 259 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi, vyumba vya madarasa vinne, matundu ya vyoo kumi na ukarabati wa maabara. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha shule za sekondari za kidato cha tano na sita zinaanzishwa katika kila tarafa.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Mkandarasi anayejenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino anaidai Serikali shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha jengo la Halmashauri.
Je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi huyo kiasi hicho cha fedha ili ujenzi huo uweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya Mkandarasi aliyejenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mpaka sasa ni shilingi milioni 758.2 yakiwemo madai yaliyohakikiwa ya shilingi milioni 368.0 na madai ambayo hayajahakikiwa ya shilingi milioni 390.2 ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/ 2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zinapaswa zitumike kulipa deni ambalo Mkandarasi anadai kabla ya kuendelea na kazi nyingine. Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo la Halmashauri unakamilika.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA aliuliza:-
Kwa zaidi ya miaka kumi sasa Serikali imejenga jengo la ghorofa moja kwa ajili ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbinga lakini jengo hilo bado halijakamilika, ujenzi umesimama kwa muda mrefu hali inayosababisha jengo hilo kuharibika na kuanza kupoteza ubora wake. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sixtus Raphael Mapunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wilaya ya Mbinga, Serikali imetenga shilingi milioni 250 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018. Fedha hizo zitatumika kukamilika ujenzi wa tanki la maji, uwekaji wa mfumo wa maji safi na maji taka, ujenzi wa uzio, ufungaji wa mfumo wa umeme,vifaa vya kuzuia moto, upigaji rangi na kukamilisha kazi ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwasihi kwamba fedha hii itakapotolewa wahakikishe jengo hili linakamilika na kuanza kutumika mara moja.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Lupembe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni ya muda mrefu na tulishaomba na kufanya maandalizi ya kuwa na Kidato cha Tano kwa Mchepuo wa CBG.
Je, ni lini Serikali itaanzisha Kidato cha Tano katika
Shule hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Lupembe ni miongoni mwa shule mpya 22 ambazo zimeombewa kibali Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili iweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano katika mwaka 2017. Hivyo, shule hiyo itaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano baada ya kupatikana kwa kibali kilichoombwa kufuatia ukaguzi wa miundombinu ya shule iliyofanyika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y MHE. BONNAH M. KALUWA) aliuliza:-
Katika Jimbo la Segerea zipo shule kumi na moja za sekondari za Serikali ambapo wanafunzi wa shule hizo wanafaulu vizuri kwa kupata daraja la I, II na III na kuwa na sifa ya kujiunga kidato cha tano. Kwa mfano mwaka 2015 wanafunzi zaidi ya 400 walifaulu kwenda kidato cha tano, lakini katika Jimbo la Segerea hakuna hata shule moja ya kidato cha tano licha ya kuwa na maeneo ya kujenga ya kutosha katika shule za sekondari za Kinyerezi, Magoza na Ilala.
Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuanzisha shule za kidato cha tano na sita katika maeneo ya shule zilizotajwa ili kuwapunguzia wanafunzi hao adha ya usafiri wanayopata kwa kufuata shule mbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Moses Kaluwa, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ina jumla ya shule za sekondari za Serikali 49 zikiwemo shule sita kongwe. Kati ya shule hizo, saba ni za kidato cha tano na sita. Halmashauri inaendelea kuboresha miundombinu ya shule ya sekondari Juhudi ili iwe na Kidato cha tano na sita. Aidha, katika mpango wa muda mrefu Halmashauri imepanga kuanzisha shule sita za kidato cha tano na sita kuanzia mwaka 2017 hadi 2022. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha shule hizo zinakuwepo katika kila tarafa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za kidato cha tano na sita ni za kitaifa ambapo zinachukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini, ndiyo maana wanafunzi 400 kutoka Jimbo la Segerea wamechaguliwa kwenda shule mbalimbali nchini.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inawapa mamlaka ya kipolisi Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwatia nguvuni watu wa muda wa saa 48, lakini sheria hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kutoa amri za kukamata Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na hata watumishi wa umma wakiwemo madaktari.
• Je, Serikali inawachukulia hatua gani Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaotumia vibaya madaraka na sheria hiyo?
• Je, ni lini Serikali itaifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuwaondolea Wakuu wa Mikoa na Wilaya mamlaka ya kuwaweka watu ndani kwa kuwa ni kandamizi, inakiuka haki za binadamu na inatumika vibaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu
(a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kisheria ni wasimamizi wa shughuli zote za Serikali katika maeneo yao ya utawala. Hivyo, ni jukumu lao kuchukua hatua pale sheria za nchi zinapokiukwa ili kuhakikisha kunakuwepo amani na usalama kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa jumla. Hata hivyo, wapo baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao wanatumia vibaya mamlaka yao, tayari Serikali imetoa maelekezo mahususi kuzingatia mipaka yao ya kazi katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa Wakuu wa Mkoa na Wilaya wamepewa madaraka ya kuwa mlinzi wa amani na usalama (peace and security). Kifungu cha 7 na 15 vya Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura, 97 Vinawapa Mamlaka viongozi hao kumweka ndani mtu yeyote kwa muda wa saa 48 ikiwa itathibitika kuna hatari ya uvunjifu wa amani na usalama au mtu huyo ametenda kosa la jinai. Tumetoa maelekezo yanayofafanua matumizi mazuri ya sheria hii kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote pamoja na mafunzo kuhusu mipaka na majukumu ya kazi zao, hivyo kwa sasa sheria inajitosheleza, ila tutaendelea kusisitiza matumizi sahihi ya sheria husika.
MHE. JAMAL KASSIM ALI (K.n.y MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-
Serikali ilitoa mafunzo kwa walimu ambao walihitumu mwaka 2015 lakini walimu hao hawajaweza kuajiriwa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaajiri walimu hao walioachwa ingawa kiuhalisi bado kuna uhaba mkubwa wa walimu katika shule za sekondari hasa vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2017 Serikali imeajiri walimu 3,081 wa masomo ya sayansi na hisabati ambao wameshapangwa na kuripoti katika shule walizopangiwa nchi nzima. Ajira hizo zimetolewa kwa walimu waliohitimu mafunzo mwaka 2015 na mwaka 2016. Mpango wa Serikali ulikuwa ni kuajiri walimu 4,129. Hata hivyo, walimu 1,048 wa masomo hayo ya sayansi na hisabati hawakupatikana katika soko wakati wa uhakiki wa vyeti uliofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imepanga kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo walimu katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA (K.n.y. MHE. DEO K. SANGA) aliuliza:-
Serikali iliahidi kufuta Ushuru mdogo mdogo unaokusanywa na Halmashauri ili wajasiriamali wadogo wakiwemo akina mama lishe waweze kuongeza kipato kupitia shughuli zao.
Je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwa Halmashauri zetu nchini ili wasikusanye tena ushuru huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyanda Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefuta ushuru na tozo ambazo zilikuwa zinatozwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi mfano Mama Lishe, wauza mitumba wadogo wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo wadogo kama mboga mboga na ndizi na matunda isipokuwa biashara za migahawa na maduka na wale ambao wako kwenye maeneo rasmi. Vilevile wafanyabiashara wadogo walio nje ya maeneo maalum ya kibiashara wenye mitaji chini ya shilingi 100,000 hawatatozwa ada, kodi na tozo zozote. Kodi nyingine zilizofutwa ni ushuru wa huduma (service levy) kwenye nyumba za kulala wageni, ada za vibali vinavyotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zilikuwa zinatozwa na TFDA, OSHA, Fire na Bodi ya Nyama na ada ya makanyagio.
Serikali pia imepunguza ushuru wa mazao kutoka asilimia tano haid asilimia mbili kwa mazao ya chakula na asilimia tatu kwa mazao ya biashara. Aidha, mazao yanayosafirishwa kutoka wilaya moja hadi nyingine yasiyozidi tani moja hayatatozwa ushuru wa mazao.
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Sokoine Mkoani Lindi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji na ubovu wa vyoo katika wodi zake, pia watumishi wa hospitali hiyo wamekuwa na lugha na huduma duni zinazokera wateja.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto zinazoikabili hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS,TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje Mbunge wa Lindi Mjini kama kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua changamoto zinazokabili Haspitali ya Mkoa wa Lindi zikiwemo uchakavu wa miundombinu, katika mwaka wa fedha 2016/2017 iliidhinishiwa kiasi cha shilingi miioni 344 kwa ajili ya kazi ya ukarabati wa miundombinu ambapo fedha zote zimepelekwa.
Vilevile Mkoa umepanga kutumia shilingi milioni 185 kwa ajili ya kujenga kichomea taka (incinerator) ya kisasa na ukarabati wa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kazi zinazoendelea hivi sasa ni ukarabati wa wodi ya wazazi, wodi ya upasuaji wa wanaume na aidha, katika kutatua tatizo la maji Serikali inakamilisha mradi mkubwa wa maji katika eneo la Ng’apa, Manispaa ya Lindi unaotarajiwa kumaliza kabisa tatizo la maji katika Manispaa ya Lindi. Wodi ya daraja la I. Aidha, mkandarasi atakayejenga kichomea taka ameshapatikana ili kuanza kazi hiyo. Vilevile Serikali ipo katika hatua za mwisho ya kupata mkandarasi kwa ajili ya ukarabati wa wodi ya watoto, jengo la upasuaji (theatre) jengo la huduma ya afya ya kinywa na meno na jengo la huduma ya macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kukarabati wodi ya wagonjwa ya akinamama, chumba cha mionzi na jengo la utawala. Ukarabati wa miundombinu utafanyika sambamba na uboreshaji wa mfumo wa maji safi na maji taka.
MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:-
Pamoja na lengo la Serikali kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi na kuzuia magonjwa ya mlipuko, Manispaa ya Mpanda ina changamoto ya ukosefu wa vifaa kama
magari ya taka.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Manispaa ya Mpanda ina maroli mawili kati ya manne yanayohitajika kwa ajili ya kuzolea taka ngumu. Kutokana na changamoto hiyo, uongozi wa Manispaa umejiwekea mikakati ifuatayo:-
(a) Manispaa ya Mpanda imebinafsisha (outsource) shughuli ya uzoaji na udhibiti wa taka kwa mzabuni anayelipwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, mMzabuni huyu ana magari mawili na hivyo kufanya jumla ya magari kuwa manne.
(b) Manispaa ya Mpanda imeanzisha mpango shirikishi jamii wenye jumla ya vikundi vya uzoaji na udhibiti wa taka ngumu katika mitaa 17, vimejengwa vizimba vitano kwa ajili ya kuhifadhia taka na vitakabidhiwa mikokoteni 17 tarehe 21/06/2017 siku ya uzinduzi.
(c) Kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi wananchi wote hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya makazi, biashara na maeneo mbalimbali ya kufanyia kazi.
(d) Kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi usafi wa kina hufanyika ambapo wananchi pamoja na viongozi mbalimbali hushiriki kufanya usafi katika maeneo yao.
(e) Siku hiyo ya Ijumaa kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi watumishi wa Manispaa hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya Ofisi ya Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhamasisha usafi nchini ili kuepuka mlipuko wa magonjwa na kuongeza unadhifu wa miji yetu.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Madiwani ni wasimamizi wakuu wa rasilimali za halmashauri na wakati wa uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais ni mafiga matatu:-
• Je, ni lini Serikali itawaongezea posho ya mwezi Madiwani hao?
• Je, ni lini Serikali itawapa usafiri na msamaha wa kodi Madiwani katika vyombo vya usafiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 Serikali ilipandisha posho za Madiwani kwa mwezi kutoka Sh.120,000/= hadi Sh.250,000 kupitia Waraka Maalum wa tarehe 16 Agosti, 2012. Vile vile katika Mwaka wa Fedha 2014/2015 posho hiyo iliongezwa kutoka Sh.250,000/= hadi Sh.350,000/= kwa mwezi kwa Madiwani na Sh.400,000/= kwa mwezi kwa Mwenyekiti au Meya. Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya Waheshimiwa Madiwani kadri hali ya uchumi wa nchi inavyoruhusu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Waheshimiwa Madiwani kupewa vyombo vya usafiri na msamaha wa kodi, kwa sasa Serikali imeridhia Waheshimiwa Madiwani wakopeshwe na Mabenki kwa masharti nafuu kutokana na posho zao. Tayari mabenki yameanza kutoa mikopo kwa Waheshimwa Madiwani zikiwemo Benki za NMB na CRDB.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Ikongolo, TASAF ilijenga bwawa kubwa la kukinga maji ya mvua kwa madhumuni ya umwagiliaji na matumizi ya vijiji vyote vinne vya Kata ya Ikongolo, lakini bwawa hili lilivuna maji kwa mwaka mmoja tu na kisha kwa masikitiko makubwa bwawa hilo lilipasuka kingo yake moja na maji yote yakatoka:-
(a) Je, wataalam wa Serikali wamegundua ni kwa nini bwawa hilo limepasuka kingo yake kuu?
(b) Kwa vile bwawa hilo lilileta shughuli nyingi za kiuchumi kwa wananchi kwa kilimo cha umwagiliaji, je, ni lini Serikali itaanza harakati za kuziba mpasuko uliotokea katika kingo za bwawa ili wananchi waendeleze shughuli zilizosimama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora kaskazini lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kubomoka kwa tuta (Embarkment) la Bwawa karibu na sehemu ya kupumulia (spillways) katika Kijiji cha Majengo kulitokana na athari za mvua nyingi zilizonyesha msimu wa mwaka 2013/2014.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa bwawa hilo, Serikali imeidhinisha shilingi milioni ishirini kwa ajili ya ukarabati wa bwawa hilo ambao utahusisha ujenzi wa njia ya kuchepusha maji (spillways). Fedha hizo zitatokana na ruzuku ya maendeleo kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-
Serikali imeziagiza Halmashauri zote za Wilaya nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya vijana na wanawake:-
Je, Serikali imetoa kiasi gani kwa vikundi vya vijana na wanawake tangu zoezi hilo lianze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2010 – 2016 Serikali imefanikiwa kutoa shilingi bilioni 122.4 kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake ambazo zinatokana na asilimia kumi iliyotengwa kila mwaka kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imepanga kutoa shilingi bilioni 56.8 ambapo mpaka mwezi Machi 2017 zimeshapelekwa shilingi bilioni 17.3 kwenye vikundi vya wanawake na vijana. Serikali itaendelea kutenga fedha hizo kila mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeshatenga shilingi bilioni 61.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Ujenzi wa Vituo vya Afya Kata za Mninga na Mtwango bado haujakamilika, hivyo wananchi wa Kata hizo wanaendelea kupata shida ya matibabu:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa vituo hivyo ili wananchi waweze kupata huduma za matibabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Mtwango ulianza mwaka 2012, ambapo umeshagharimu Sh.22,500,000/=. Aidha, Kituo cha Afya Mninga kilianza kujengwa mwaka 2008 ambapo umegharimu Sh.41,000,000/=. Vituo hivyo vipo katika hatua ya umaliziaji wa majengo ya OPD na nyumba za watumishi ili huduma zianze kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali ilitenga Sh.32,500,000 kwa ajili ya kuendelea kuchangia ukamilishaji wa Vituo vya Afya Kata ya Mninga na Mtwango. Fedha zilizopokelewa mpaka sasa ni Sh.8,000,000/=. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018, zimetengwa Sh.65,000,000/= kwa ajili ya kuimarisha Vituo vya Kasanga na Kituo cha Afya Mbalamaziwa katika Jimbo la Mufindi Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali kuunga mkono juhudi za wananchi katika miradi ya maendeleo kwa kutenga fedha kupitia LGDG kila mwaka ili kumalizia miradi mbalimbali.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhamira ya dhati ya kuboresha maslahi ya Watumishi hususan Walimu kwa kutoa nyaraka mbalimbali ikiwemo Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa tarehe 20/10/2014 unaohusu mishahara na Posho ya Madaraka kwa Viongozi wa elimu (Responsibility Allowance):-
• Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutekeleza waraka huo?
• Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) ili kuleta ufanisi wa kazi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 tangu tarehe 1 Julai, 2016 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Walimu Wakuu wanalipwa sh.200,000/= kila mwezi na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wanalipwa sh.250,000/= kila mwezi. Kwa mwezi mmoja, Serikali inatumia takriban shilingi bilioni 5.01 kwa ajili ya kulipa Posho za Madaraka kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya kufundishia ilijumuishwa katika Mshahara wa Walimu ili kuboresha maslahi ya Walimu wanapostaafu. Hata hivyo, Serikali hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inafanya mapitio ya kazi kwa watumishi wote nchini ili kuboresha maslahi kwa kuzingatia uzito wa kazi.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K.n.y MHE. ESTHER L. MIDIMU) aliuliza:-
Barabara za Vijiji katika Wilaya ya Maswa ni mbovu kiasi kwamba sehemu nyingi za maeneo ya vijijini hayapitiki.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za kutosha za Mfuko wa Barabara ili barabara hizo zifanyiwe matengenezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Maswa inao mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,055. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri hiyo imetengewa shilingi bilioni 1.4 kutoka katika Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kufanya matengenezo ya kawaida kilometa 203.5, matengenezo ya sehemu korofi kilometa 54, matengenezo ya muda maalum kilometa 32, kujenga madaraja manne, Makalvati yenye urefu wa mita 28 na mtandao wa kupitisha maji ya mvua yenye mifereji ya mita 400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutafuta fedha ili kuimarisha mtandao wa barabara za Halmashauri hapa nchini.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE (K.n.y. MHE. HASNA S. K. MWILIMA) aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Nguruka kinahudumia Wakazi wa Kata Nne za Tarafa ya Nguruka pamoja na wananchi wa Usinge katika Wilaya ya Kaliua.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi kituo hicho kwa kuongeza miundombinu na kumalizia ukarabati wa jengo la Mama na Mtoto ambalo limeachwa bila kukarabatiwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Nguruka kinahudumia watu wapatao 108,330 wa Kata nne za Tarafa ya Nguruka na majirani Wakazi wa Tarafa Usinge Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora kama kituo cha rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona haja ya kukiboresha Kituo cha Afya cha Nguruka ili kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi ikizingatiwa kwamba Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli alitoa ahadi ya kukiboresha kituo hicho alipokuwa katika kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetenga shilingi milioni
• katika mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuongeza miundombinu ikiwemo wodi ya akinamama wajawazito na watoto, ujenzi wa uzio, ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti, mfumo wa maji taka na ukarabati wa nyumba ya watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuimarisha na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha huduma za afya hapa nchini.
MHE. GIBSON B. OLE MEISEYEKI aliuliza:-
Hivi karibuni Serikali ilianza zoezi la kubomoa nyumba kwenye vyanzo vya maji na waathirika wa operesheni hiyo sheria imewakuta na wengi wao walikuwa kwenye maeneo hayo tangu enzi za ukoloni hususani wananchi wa Kata ya Kiranyi:-
Je, Serikali inawafikiriaje wananchi hawa ambao sheria imewakuta kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gibson Blasius Ole-Meiseyeki, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Kiranyi na Olorien hutegemea kupata maji katika chanzo cha Sailoja katika Halamshauri ya Wilaya ya Arusha. Chanzo hiki kinahudumia sehemu ya Mamlaka ya Mji mdogo wa Ngaramtoni kwa ajili ya matumizi ya maji ya wakazi wa Mji huo na viunga vyake katika Jimbo la Arumeru Magharibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha imefanya utambuzi wa nyumba na mali zilizopo ndani ya chanzo cha maji cha Sailoja katika Kata ya Karanyi. Halmashauri inakusudia kukaa na watu ambao wamo ndani ya chanzo. Aidha, utambuzi wa awali umebainisha jumla ya Kaya 120 zimetambuliwa kwenye eneo la chanzo hicho cha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Halmashauri ina mpango wa kukutana na wananchi ambao wamebainika kuwa katika chanzo hicho cha maji ili kufanya mazungumzo ya pamoja ya namna ambavyo utaratibu utakavyokuwa kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo. Ofisi yangu itasimamia zoezi hili ili kuhakikisha kwamba sheria, kanuni na taratibu zinazingatiwa wakati wa kunusuru chanzo hiki.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Kutokana na wananchi wa vijijini kuwa na uelewa mdogo wa masuala ya sheria na haki zao, Watendaji wa Vijiji na wa Kata wakishirikiana na Mahakama za Mwanzo na Mabaraza ya Ardhi huwaonea na kuwadhulumu kwa kuwabambikizia kesi na kuwanyang’anya ardhi:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua za kukomesha tabia hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba yapo malalamiko dhidi ya baadhi ya Watendaji wa Kata na Vijiji ambao wamekuwa wakilalamikiwa na viongozi na wananchi kuwabambikizia kesi na kushirikiana na Mahakama za Mwanzo na Mabaraza ya Ardhi kuwaonea na kuwadhulumu ardhi wananchi hao kwa kuwanyang’anya ardhi yao. Serikali inakemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu na ambao wanakiuka maadili ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukomesha tabia hii, Serikali inaelekeza kwa viongozi na watendaji mambo yafuatayo ya kuzingatia:-
• Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wahakikishe wanasimamia uzingatiaji wa maadili ya watendaji walio chini yao.
• Watendaji wote katika ngazi zote za mamlaka za Serikali za Mitaa wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miiko na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
• Serikali haitasita kumchukulia hatua Mtendaji yeyote atakayekiuka sheria, kanuni, taratibu na maadili ya kazi yake, ikiwemo kujihusisha na tabia ya ubambikiziaji kesi wananchi na kuwanyang’anya ardhi;
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha inasimamia kikamilifu maadili ya watumishi wa umma ili kuongeza nidhamu katika utumishi wa umma na haitasita kuchukua hatua mara moja dhidi ya Mtendaji yeyote wa Kata au Kijiji atakayethibitika kutumia vibaya madaraka yake ikiwemo kubambikia kesi wananchi kwa lengo la kuwanyang’anya ardhi. Nitoe wito kwa viongozi na wananchi wote nchini kuhakikisha wanafichua utendaji na watumishi wa umma wenye tabia kama hii ili waweze uchukuliwa hatua stahiki.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:-
Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Suleiman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji katika Kijiji cha Ngomalusambo chenye jumla ya wakazi 1,672 ulianza kujengwa mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2015 kwa gharama ya shilingi 268.9. Mradi huo unategemea jenereta ya dizeli inayopampu maji kutoka kwenye kisima kwenda kwenye tenki. Mradi huu umeshindwa kutoa huduma kwa wananchi kutokana na kuibiwa betri ya pampu iliyofungwa katika mradi huo. Ili kukabiliana na changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imekamilisha ununuzi wa betri mpya na kuifunga wananchi wa Ngomalusambo wameanza kupata maji kuanzia tarehe 22 Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina mpango wa kuchimba kisima kingine katika mwaka wa Fedha 2017/2018 ili kuwezesha mradi huo ufanye kazi kwa ufanisi kutokana na kisima kilichopo sasa kupoteza uwezo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wizi wa betri uliojitokeza hapo awali, Serikali inatoa wito kwa wananchi wa Kijiji cha Ngomalusambo kulinda mradi huo kwa manufaa ya wananchi wote. Napenda kusisitiza kuwa, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa uharibifu wowote wa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya watu binafsi.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO (k.n.y MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:-
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Mheshimiwa Rais aliahidi kujenga nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Itilima katika Kijiji cha Langabidili. Je, ni lini ahadi hiyo itaanza kutekelezwa?
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Itilima ni kati ya Wilaya tano zinazounda Mkoa wa Simiyu. Wilaya hii ilianzishwa mwaka 2012 kwa GN Na. 73, na Halmashauri yake ilianzishwa mwezi Mei, 2013 kwa GN Na. 47. Wilaya ya Itilima imezaliwa kutoka katika Wilaya ya Bariadi na kuunda Mkoa wa Simiyu wenye Wilaya tano na Halmashauri sita. Watumishi wa Halmashauri wanalazika kuishi Bariadi Mjini na kusafiri umbali wa kilometa 33 kila siku kutoka Bariadi hadi Makao Makuu ya Wilaya kwa ajili ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na usumbufu na gharama za usafiri Serikali ilitoa shilingi milioni 500 kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi na kulipa fidia maeneo ya wananchi. Hadi sasa ujenzi wa nyumba nne unaendelea katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi milioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za wananchi. Aidha, Serikali imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji. Ujenzi unaendelea na unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nyingine nne za watumishi. Serikali itaendelea kutenga fedha kidogo kidogo kwa kadri zitakavyopatikana ili kuweza kukamilisha nyumba za watumishi.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Walimu Wilayani Maswa wana uhaba wa nyumba za kuishi; pamoja na juhudi za wananchi kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari lakini walimu hao bado wanahitaji kujenga nyumba zao wenyewe za
kudumu.
Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa kutoa mikopo kwa walimu hao ili wajenge nyumba zao binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ina uhitaji wa nyumba za walimu 1,358. Nyumba zilizopo ni 479 na hivyo upungufu ni nyumba 879.
Mheshimiwa Spika, kutokana na upungufu huu Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ina mpango wa kujenga nyumba 16 katika mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, kati ya nyumba hizo, nyumba nane zitajengwa kwa bajeti ya 2017/2018 (CDG) na nyumba nyingine nane zitajengwa kwa kutumia mapato ya ndani y (own source) ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kuwa tatizo la upungufu wa nyumba halitaweza kumalizwa na Serikali peke yake, Serikali inawashauri walimu wa Halmashauri ya Maswa na walimu wote nchini wanaohitaji kujenga nyumba zao binafsi kukopa fedha kutoka katika taasisi za fedha zinazokubalika Kisheria.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inatoa wito kwa walimu nchini kote kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili waweze kukopa kwa riba nafuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za binafsi. Pia Serikali inawashauri walimu kutumia mikopo ya nyumba inayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
MHE. ROSE K. SUKUM aliuliza:-
Serikali ina utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya shule za bweni nchini. Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 31/08/2013 hadi 10/02/2014 Halmashauri ya Hanang ilipokea kutoka Serikali Kuu kiasi cha shilingi 508,779,500 kwa ajili ya chakula cha shule za bweni. Taarifa zinaonesha kuwa fedha zilizotumika kununua chakula ni shilingi 225,585,000. Kwa takwimu hizo bakaa ni shilingi 283,194,500 na kwa mujibu wa mkaguzi, bakaa hiyo haionekani kwenye akaunti yoyote ya benki.
(a) Je, fedha hizo zinarudishwa Hazina bila ya uwepo wa nyaraka zozote toka Halmashauri kuonesha muamala unavyofanya kazi?
(b) Je, kama fedha hizo hazikurudishwa Hazina, nani anaweza kuidhinisha matumizi bila ya mpango wake kupitishwa na Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri?
(c) Je, kama fedha zimetumika bila kupangiwa na Kamati halali, ni kwa nini wahusika bado wanaendelea kuwa ofisini bila ya kufunguliwa mashtaka ya wizi wa kuaminika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Kamil Sukum, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ ilipokea kiasi cha fedha shilingi 508,779,500 kwa ajili ya chakula cha shule za msingi nne za bweni ambazo ni Katesh, Balangdalalu, Bassodesh na Gendabi. Jumla ya shilingi milioni 225.58 zilizopangwa kwenye bajeti zilipelekwa kwenye shule za msingi za bweni kadiri fedha hivyo zilivyopokelewa kutoka Hazina. Kiasi cha shilingi milioni 283.19 zilizosalia hazikurudishwa Hazina badala yake fedha hizo zilibadilishiwa matumizi kwa kuombewa kibali cha kubadilisha matumizi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango kwa barua yenye kumb. Na. HANDC/ED/F.1/12/ VOL.IV/198 ya tarehe 10/04/2014 na kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa barua yenye kumb. Na. HAN/ED/F1/12/ VOL.IV/205 ya tarehe 01/08/2014.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri baada ya kupokea taarifa ya matumizi ya fedha, iliagiza fedha hizo zirudishwe kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza shughuli za ununuzi wa vifaa na samani kwa wanafunzi wa shule husika. Ili kutekeleza agizo hilo, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, kiasi cha shilingi 130,000,000 zilipelekwa kwenye akaunti za vijiji vya Gendabi, Bassodesh, Katesh na Balangdalalu kwa ajili ya kununulia magodoro, vitanda na ukarabati wa mabweni kwa shule za msingi za bweni zilizopo kwenye vijiji hivyo. Aidha, Halmashauri imeagizwa kurejesha fedha zilizobaki kiasi cha shilingi milioni 153.19 ndani ya mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, kutokana na matumizi ya fedha za halmashauri yasiyoridhisha, ikiwa ni pamoja na matumizi ya fedha hizo, tangu mwezi Aprili, 2016, Mkurugenzi Mtendaji amesimamishwa kazi na mamlaka yake ya nidhamu. Aidha, watumishi wengine wanne akiwemo afisa mipango wilaya, mweka hazina wilaya na wahasibu wawili wamesimamishwa kazi na Baraza la Madiwani ili kupisha uchunguzi.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO (K.n.y. MHE. LAMECK AIRO) aliuliza:-
Wilaya ya Rorya iliyoanzishwa mwaka 2007 sasa ina wakazi wapatao 400,000 na ina kata 26 na vijiji takriban 87 na ina vituo vya afya 4 lakini haina Hospitali ya Wilaya na wananchi wake hulazimika kutembea umbali wa takribani kilomita 30 kufuata huduma za afya Tarime na akina mama ambao ni asilimia 52 wanahitaji huduma ya hospitali kamili:-
Je, ni lini Wilaya ya Rorya itajengewa Hospitali ya Wilaya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya 67 hapa nchini ikiwemo Hospitali ya Rorya ambayo tumeitengea shilingi bilioni 1.5.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Serikali imefanya kazikubwa sana ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Korogwe lakini haikuunganisha nyumba za Walimu zilizopo Shuleni hapo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati nyumba hizo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Korogwe ni miongoni mwa shule 45 zilizokarabatiwa katika awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule kongwe nchini. Ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza ulihusisha vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, mabweni, maabara, ofisi za walimu, majengo ya utawala, mabwalo ya chakula na majiko, mifumo ya maji safi na taka na mifumo ya umeme.
Mheshimiwa Spika, ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza haukuhusisha nyumba za walimu kutokana na sababu za kibajeti. Awamu ya pili ya ukarabati unaoendelea inahusisha shule shule kongwe 19 ikiusisha halikadhalika nyumba za walimu kwenye shule zinazokarabatiwa. Serikali inatafuta fedha ili kukarabati nyumba za walimu ambazo hazikujumuishwa kwenye mpango wa ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Sera ya Afya ni kuwa na Kituo cha Afya kwa kila Kata na Zahanati kwa kila Kijiji; Tarafa ya Nambis katika Jimbo la Mbulu Mjini haina Kituo cha Afya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Vituo vya Afya kwenye Kata za Kainem, Murray, Nambis na Nahasey?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay,Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Tarafa ya Nambis haina Kituo cha Afya na wananchi wa Tarafa hiyo wanapata huduma kwenye Zahanati 4 za Serikali zilizoko katika Tarafa ya Nambis pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ambayo iko jirani na Kata ya Nambis.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Mji wa Mbulu, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya Daudi na Tlawi sambamba na vifaa tiba ambapo hadi Oktoba, 2019 Kituo cha Afya Daudi kimepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 203.8 na Kituo cha Afya Tlawi kimepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 203.8.
Vilevile Mkoa wa Manyara umepatiwa kiasi cha shilingi billioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri za Wilaya za Mbulu na Simanjiro. Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbulu utapunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu iliyoko Mbulu Mjini.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati Vituo vya Afya nchini kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha uliopo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-
Kuna upungufu mkubwa wa Walimu katika Shule za Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba:-
Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ina jumla ya shule za msingi za Serikali 141 zenye jumla ya wanafunzi 80,224. Halmashauri ina walimu 1,172 wa shule za msingi kati ya walimu 1,783 wanaohitajika hivyo kuwa na upungufu wa walimu 611.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kutatua changamoto ya upungufu wa walimu nchini kuanzia Mei, 2017 hadi Oktoba 2019, Serikali imeajiri walimu 15,480 wa shule za msingi, walimu 7,218 wa shule za sekondari na fundi sanifu wa maabara 297 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imepatiwa walimu 66 wa shule za msingi yaani 37 ajira mpya na 29 walihamishiwa kutoka sekondari kwenda shule za msingi. Serikali itaendelea kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari kwa kadri fedha na vibali vitakavyopatikana?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
(a) Je, ni nini sifa au vigezo vya kupata Halmashauri?
(b) Inachukua miaka mingapi kuendelea kuitwa Halmashauri ya Mji Mdogo hadi kuwa Halmashauri kamili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, Mkoani Iringa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura 287 na (Mamlaka za Miji) na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 288 zimeweka utaratibu wakuzingatiwa katika kupandisha hadhi maeneo ya utawala. Vigezo vya kuanzisha Mamlaka za Miji Midogo vimeainishwa kwenye Mwongozo wa Uanzishaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, Kipengele Na.4.2.5 (a-q) na miongoni mwa vigezo muhimu ni pamoja eneo linalopendekezwa kuwa na idadi ya watu isiopungua 50,000, kata zisizopungua 3, vitongoji visivyopungua 30 na ukubwa usiopungua kilometa za mraba 150.
Mheshimiwa Spika, vigezo vya kuanzisha Halmashauri ya Wilaya au kuipandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo kuwa Halmashauri ya Wilaya vimeanishwa kwenye Kipengele Na. 4.2.4 (a-q) kama nilivyosema awali na miongoni mwa vigezo muhimu ni pamoja na uwezo wa kujitegemea kibajeti kwa walau 20% kutokana na mapato ya ndani, eneo lenye ukubwa usiopungua kilometa za mraba 5,000, kata zisizopungua 20, vijiji visivyopungua 75 na idadi ya watu wasiopungua 250,000. Hivyo, upandishaji wa hadhi wa Mamlaka za Mji Mdogo kuwa Halmashauri unategemea vigezo vilivyoainishwa na sio muda wa Halmashauri.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Wananchi wa Mipande – Mtengula na Mwitika Maparawe wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa madaraja na Rais wa Awamu ya Tano aliwaahidi Wananchi hao kuwajengea madaraja:-
Je, ni lini ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza usanifu wa Daraja la Mwitika hadi Maparawe linalounganisha barabara yenye urefu wa kilomita 4 na daraja la Mputeni-Mtengula linalounganisha barabara yenye urefu wa kilomita 3.06. Lengo la usanifu huo ni kubaini gharama zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi wa madaraja yote mawili. Hivyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati Serikali inakamilisha kazi hiyo ya usanifu ili kuanza shughuli za ujenzi.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Viwanja vya Mwanalugali Mjini Kibaha vimeshindwa kupimwa kutokana na mgogoro uliopo kwa wenye ardhi hiyo kutolipwa fidia wakati wa upimaji mwaka 2000:-
Je, Serikali inatoa msaada gani kwa wananchi hao ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao na kuwasababishia umaskini mkubwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha uthamini na kubaini watu 62 wanadai fidia kiasi cha Sh.575,017,858. Serikali imepanga kulipa fidia hiyo kwa kutumia fedha zitatokana na mauzo ya viwanja vilitolewa kwa wananchi na taasisi tangu mwaka 2004 lakini mpaka leo bado havijalipiwa na havilipiwi kodi ya Serikali.
Aidha, Serikali inakusudia kubadili matumizi ya eneo moja la ibada ambalo wananchi wanadai fidia ili wananchi wamilikishwe maeneo yao. Vilevile, Halmashauri inakusudia kuomba kibali kwa Kamishna wa Ardhi ili kufuta baadhi ya viwanja ili viweze kuuzwa kutunisha Mfuko wa Fidia na vingine kukabidhiwa kwa wananchi wanaodai fidia ili kumaliza mgogoro uliokuwepo kwa muda mrefu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Wilaya ya Karagwe ina Sekondari moja tu ya kidato cha Tano na Sita ambayo ni Bugene Sekondari.
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Sekondari za Nyabionza na Kituntu ili ziwe shule za kidato cha Tano na Sita?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 190 katika shule Nyabionza kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na mabweni mawili. Aidha, ujenzi na ukarabati wa maabara tatu, bweni moja la wasichana, maktaba, bwalo na jiko unaendelea kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe. Vilevile Shule ya Sekondari Kituntu, imepokea jumla ya shilingi milioni 52.5 ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na bweni moja ambalo liko katika hatua ya umaliziaji. Kadhalika, halmashauri inaendelea na ujenzi wa maktaba moja, bweni moja la wavulana, madarasa mawili, bwalo la chakula na jiko kwa kutumia mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli hizi za ujenzi wa miundombinu ni maandalizi ya kuzipandisha hadhi shule hizo mara tu zitakapokamilika ambapo zitasajiliwa na kupangiwa wanafunzi wa kidato cha tano.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Katika Bajeti ya mwaka 2018/2019 Mkoa wa Katavi ulitengewa kiasi kidogo cha fedha kuliko mikoa yote.
Je, Serikali iko tayari kuongeza mgao wa fedha kwa Mkoa wa Katavi kwa kuzingatia jiografia na kilomita za mtandao wa barabara?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi Mbunge wa jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kupanga bajeti kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara kwenye Mamlaka za Serikai za Mitaa. Serikali inazingatia vigezo mbalimbali ikiwemo kigezo cha mtandao wa barabara ullisajiliwa. Mkoa wa katavi katika mwaka wa fedha 2018/2019, uliidhinishiwa shilingi 3.62 kwa kuzingatia matandao wa barabara uliopo ambao ni kilomita 1,441.3. Vigezo vingine vinavyozingatiwa na pamoja na tabaka la barabara hali ya mtandao wa barabara, idadi ya magari yanayotumia barabara na idadi ya watu wanaohudumiwa na barabara husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia bodi ya mfuko wa barabara inaendelea na zoezi la uhakiki wa mtandao wa barabara zinazosimamiwa na TARURA ili kuishauri Serikali kufanya mapitio ya mgawo wa fedha za mfuko wa barabara na kuhakikisha barabara zinazohudumiwa na TARURA zinatengewa bajeti ya kutosha kwa ajili ya matengenezo hayo.
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MENDRAD L. KIGOLA) aliuliza:-
Miundombinu ya shule nyingi za msingi katika Jimbo la Mufindi Kusini ni chakavu:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati miundombinu ya shule hizo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Sekta ya Elimu hapa Nchini ni uhaba na uchakavu wa miundombinu ya shule ikiwemo nyumba za walimu, vyumba vya madarasa pamoja na vyoo. Serikali kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Sekta ya Elimu (Education for Results – EP4R) inaweka kipaumbelea na kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo ya elimu.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/ 2019, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imepokea jumla ya shilingi milioni 223.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Shule za Msingi Kilolo na Makalala. Shule ya Msingi Kilolo ilipokea jumla ya shilingi milioni 136.6 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu, ujenzi wa madarasa manne na ujenzi wa matundu sita ya vyoo na Shule ya Msingi Makalala imepokea jumla ya shilingi miloni 86.6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo. Serikali itaendelea kutoa fedha kwa kadri ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ya msingi kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Kupitia Sera ya Serikali ya kila kata kuwa na kituo kimoja cha afya, ni kata mbili tu zimebahatika kuwa na vituo vya afya kati ya kata kumi na saba (17) za Halmashauri ya Mji wa Mbulu; vituo hivi viko kwenye Tarafa za Daudi na Endagikot:-
(a) Je, ni lini Serikali itajenga kituo kimoja cha afya Kata za Kainam au Muray kwa ajili ya kupeleka huduma ya afya katika Tarafa ya Nambis yenye kata nne na vijiji ishirini na mbili na wakazi 24,800 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012?
(b) Serikali ina sera ya kutoa huduma za afya bila malipo kwa watoto walio chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito; je, Serikali inachukua hatua gani katika vituo ambavyo bado vimeendelea kuchangisha kundi hili muhimu katika jamii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa vituo vya afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuanza na ujenzi wa Vituo vya Afya viwili na Daudi na Tlawi vilivyogharimu jumla ya shilingi bilioni moja kwa kila kituo kupata shilingi milioni 500. Hata hivyo, Serikali inatambua na imesikia kilio cha Mheshimiwa Mbunge, Serikali itafanya juhudi kwa kadri iwezekanavyo ili kuwasaidia wananchi wa kata hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi bilioni 270 ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi yakiwemo makundi yenye msamaha wa matibabu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imeidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 104 kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja, ile basket fund, ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo ni kwa ajili ya dawa na vifaatiba. Hivyo, Serikali haitarajii kuona akina mama wajawazito pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakichangishwa. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kuwatoza makundi hayo kwa kuwa ni kinyume na maelekezo ya Serikali. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Kuna baadhi ya Bar na Club ambazo zimejengwa kwenye makazi ya watu ambazo zimekuwa kero kwa jamii:-
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu Bar na Club hizo ambazo zinakiuka sheria na maadili ya jamii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba biashara nyingi, zikiwemo za uendeshaji wa bar na club zipo kwenye maeneo ya makazi ya watu. Serikali inawaelekeza wamiliki wote wa bar na club kuwa wanapaswa kuzingatia maelekezo ya Sheria ya Vileo Sura Na. 28 ya mwaka 1968, kifungu cha 14(1) katika uendeshaji wa shughuli zao. Aidha, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa vitendo vyovyote vitakavyobainika kukiuka sheria na kusababisha kero kwa wananchi wengine.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Mabweni katika shule za sekondari zilizoanzishwa Kitarafa ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kupata elimu iliyo bora Mkoani Shinyanga?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hilal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa shule za sekondari kuwa na mabweni ili kuboresha elimu. Kwa sasa mpango wa Serikali ni kuziboresha shule za sekondari zilizopo ambapo kipaumbele ni katika ujenzi wa miundombinu muhimu wa vyumba vya madarasa, vyoo mabweni na maabara ili kuboresha mazingira ya kufundishi na kujifunzia. Ukarabati wa shule hizo unahusisha miundombinu ya mabweni hasa kwa watoto wa kike ili kuweza kupata elimu iliyo bora. Hadi sasa, shule za sekondari 1241 zimejengewa mabweni kati ya shule za sekondari 3634 zinazotumia ruzuku ya Serikali Kuu, mapato ya ndani ya Halmashauri na mchango wa jamii. Serikali itaendelea kujenga mabweni na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-
Barabara ya Msambiazi - Lutindi – Kwabuluu ni muhimu kwa uchumi na maisha ya watu wa Korogwe hususan Kata za Tarafa ya Bungu, lakini barabara hii ni mbovu na korofi sana.
(a) Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini barabara hii itapandishwa kuwa ya mkoa hasa ikizingatiwa kuwa inakwenda kuunganisha Bumbuli na Lushoto?
WAZIRI WA NCHI, OFISI WA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, barabara ya Msambiazi – Lutindi – Kwabuluu ni barabara ya Mkusanyo (Collector road) yenye urefu wa kilometa 17.5. Kuanzia Mwaka wa Fedha 2017/2018 hadi 2019/2020 Serikali imeifanyia matengenezo kwa gharama ya shilingi milioni 43. Katika Mwaka wa fedha 2020/2021 Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Korogwe umeomba kutengewa shilingi milioni 50 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. TARURA Wilaya ya Korogwe inaendelea kufanya upembuzi wa kina wa mtandao wa barabara zake utakaobaini vipaumbele vya ujenzi wa mtandao wa barabara Wilayani Korogwe kwa viwango vya lami, changarawe na vumbi.
(b) Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanzishwa kwa TARURA, barabara hii iliombewa kuingizwa kwenye orodha ya barabara zinazohudumiwa na TANROADS kupitia Baraza la Madiwani ambapo baada ya kuanzishwa kwa TARURA imepewa jukumu la kuendelea kuihudumia barabara hiyo. Aidha, Serikali imeshatoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini kuhusu utaratibu wa Bodi za Barabara za Mikoa, Wabunge au Kikundi cha watu kutuma maombi ya kupandishwa hadhi barabara. Utaratibu huu umetolewa na Kamati ya Kitaifa ya Kupanga Barabara katika Hadhi Stahiki (National Roads Classification Committee- NRCC).
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa Wilaya ya Manyoni umekuwa na madhara makubwa ikiwemo kusababisha vifo vya akinamama na watoto pindi wanapotakiwa kukimbizwa kwenye hospitali za Rufani.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia Manyoni gari la Wagonjwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI WA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ina magari mawili ya wagonjwa, gari moja lipo kwenye Kituo cha Afya cha Nkonko na jingine katika Kituo cha Afya cha Kintinku. Hospitali ya Wilaya inatumia pickup na gari aina ya land cruiser hardtop. Serikali itatoa kipaumbele kwa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni pindi itakapopata magari ya wagonjwa kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Serikali inatambua vivutio kadhaa vya utalii ikiwemo Kalambo Falls Mkoani Rukwa. Hata hivyo, barabara ya kuelekea maporomoko hayo kutokea Kijiji cha Kawala hairidhishi.
(i) Je, Serikali ina mpango gani wa kuiboresha barabara hiyo itakayokuwa ikitumika na watalii?
(ii) Je, kwa nini kipande hiki chenye urefu wa kilometa 12 kuanzia barabara ya Kijiji cha Kawala kisiwekewe lami?
WAZIRI WA NCHI, OFISI WA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya matengenezo ya kilometa 6.5 za barabara ya Kalambo Falls kwa kiwango cha changarawe na kujenga makalvati kwa gharama ya shilingi milioni 160.8 ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika katika kipindi chote cha mwaka.
(b) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021 Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga kufanya usanifu wa kina wa kipande cha barabara ya kutoka Kijiji cha Kawala hadi Kalambo Falls chenye urefu wa kilometa 12 ili kubaini gharama halisi zinazohitajika kwa ajili ya kujenga kipande hicho cha barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Je Serikali inatumia sheria gani kuwahamisha wakulima kwenye maeneo ya mijini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji, Na.8 ya mwaka 2017 na Sheria ya Ardhi, Na.4 ya mwaka 1999, Serikali haihamishi wakulima kwenye maeneo ya mijini badala yake inazuia wananchi kujihusisha na shughuli za kilimo cha mazao marefu katika maeneo hayo. Aidha, mazao mafupi kama kilimo cha mazao ya mikunde yanaruhusiwa kulimwa maeneo ya mijini kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
(a) Je, kuna miongozo ya fedha mingapi inayoitaka Halmashauri kutenga fedha za ndani kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo?
(b) Je, ni halali kuwepo miongozo zaidi ya mmoja ukizingatia kuwa sasa Halmashauri hazina ruzuku?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, usimamizi wa fedha kwenye Halmashauri unafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Kifungu cha 37 na Kifungu cha 68 vinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kutoa miongozo ya usimamizi wa fedha katika Serikali za Mitaa.
(b) Mwongozo wa mgawanyo wa mapato ya ndani kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya Kawaida umezingatia uwezo wa Halmashauri kukusanya mapato ambapo Halmashauri zenye mapato makubwa zinachangia asilimia 60 ya mapato yake kwa ajii ya Miradi ya Maendeleo na Halmashauri zenye mapato kidogo zinachangia asilimia 40 ya mapato yake kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Mheshimiwa Rais amefanya marekebisho ya jina na mipaka ya iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na sasa kuna Halmashauri mpya ya Mtama inayojumuisha eneo lote la Jimbo la Mtama:-
Je, nini hatma ya eneo lililobaki la Jimbo la Mchinga ambalo hapo awali Lilikuwa ipo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Lindi kama ilivyo kwa Jimbo la Mtama?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kufuatia agizo la Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuhamishia Halmashauri ya Wilaya ya Lindi katika Jimbo la Mtama na Jimbo la Mchinga kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaendelea na uhakiki wa mipaka ili kundaa Tangazo la Serikali la kurekebisha mipaka ya Halmashauri hizo. Zoezi hilo linafanyika sambamba na maeneo mengine yaliyotangazwa na Mheshimiwa Rais ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Sekta ya Afya nchini inakabiliwa na uhaba wa Watumishi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuziba pengo hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za Sekta ya Afya nchini ambapo kuanzia Mei, 2017 hadi Julai, 2019 jumla ya watumishi 8,994 wameajiriwa na kupangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepewa kibali cha kuajiri Madaktari 610 ambao watapangwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.
MHE. ROSE K. SUKUM aliuliza:-
Kutokana na wingi wa watu na shughuli za kiuchumi zilizopo katika Kata ya Bassotu kama vile uchimbaji madini, uvuvi, kilimo, ufugaji na biashara na hivyo kuwa na hatari ya milipuko ya magonjwa:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Wodi ya Watoto, Wanawake, Wanaume na nyumba za watumishi wa Zahanati ya Bassotu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Kamili Sukumu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na Mwongozo unaosimamia utoaji wa huduma za afya, zahanati hazina Wodi ya Watoto, Wanawake na Wanaume. Hata hivyo, kutokana na umbali uliopo kati ya zahanati hiyo na Hospitali ambao ni kilometa 55, Serikali itafanya tathmini ili kuboresha miundombinu iliyopo na kuifanya Zahanati ya Bassotu kuwa na hadhi ya Kituo cha Afya.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-
(a) Je serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru na Katika Vituo vya Afya Nakapanya na Matemanga?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Vituo vya Afya na Zahanati katika Kata na Vijiji ili kuendana na Sera ya Afya na Ilani ya CCM?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wa uboreshaji wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru ambapo wodi mbili ziko katika hatua ya ukamilishaji kwa gharama ya Shilingi milioni 140. Aidha, Hospitali imewezeshwa kufungua duka la dawa na kupatiwa mashine ya Ultrasound. Serikali imetumia shilingi milioni 500 kukarabati Kituo cha Afya Matemanga na Shilingi milioni 200 kujenga wodi ya mama na mtoto na jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Nakapanya?
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa Vituo vya Afya kwa awamu na tayari imekamilisha ujenzi wa Vituo vya Afya vitatu Wilayani Tunduru kwa gharama ya shilingi biloni 1.3 na inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya Nakapanya kwa gharama ya shilingi milioni 200. Majengo mengine yaliyobaki yataendelea kupewa kipaumbele ili kufikia azima ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
MHE. MARIAM AZZAN MWINYI K.n.y. MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga tuta la kuzuia maji ya Bahari yanayoharibu mashamba ya Wananchi wa Vijiji vya Nanguli, Jundamiti, Mwambe na Kiwani katika Jimbo la Kiwani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdalla Rashid, Mbunge wa Kiwani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi kote duniani kwa sasa yapo dhahiri na athari zake zinaendelea kuonekana hapa nchini. Mojawapo ya athari hizo ni kuongezeka kwa kina cha bahari katika maeneo mbalimbali ya fukwe likiwemo Jimbo la Kiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeanza kufanya upembuzi wa awali kwenye fukwe zilizoathiriwa nchini kutokana na kujaa maji ya bahari ili hatimaye kujenga kingo za kuzuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi na mashamba ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza juhudi za wananchi na Mfuko wa TASAF katika Jimbo la Kiwani kwa kuanza kushughulikia changamoto hizi na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jimbo la Kiwani ni miongoni mwa maeneo yatakayofanyiwa upembuzi yakinifu ili kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa baadaye. Ahsante.
MHE. JULIANA D. MASABURI aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje katika kudhibiti uchafuzi unaofanyika pembezoni mwa Ziwa Victoria ambao unapunguza samaki kuzaliana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, uchafuzi wa mazingira unaofanyika pembeni mwa Ziwa Victoria unatokana na shughuli za kibinadamu zisizozingatia hifadhi ya mazingira. Shughuli hizo ni pamoja na utiririshaji wa majitaka kutoka katika maeneo ya makazi, utupaji taka ngumu kutoka majumbani na viwandani, kilimo kisicho endelevu kinachosababisha uchafuzi wa maji kutokana na kuongezeka kwa tabaki, matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na mbolea za viwandani na uchimbaji wa madini usio endelevu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa Kanuni, miongozo na mikakati ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya maziwa. Aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa tathmini ya athari za kimazingira (TAM) inafanyika kwa miradi ya maendeleo iliyopo inayotarajiwa kufanyika pembezoni mwa Ziwa Victoria ili kuhakikisha udhibiti wa vyanzo vya uchafuzi wa maji ya Ziwa Victoria inayotokana na shughuli za kibinadamu zisizohusisha miradi hiyo unazingatiwa.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa tathmini ya athari za kimazingira (TAM) inafanyika kwa miradi ya maendeleo iliyopo, inayotarajiwa kufanyika pembezoni mwa Ziwa Victoria ili kuhakikisha udhibiti wa vyanzo vya uchafuzi wa maji ya Ziwa Victoria inayotokana na shughuli za kibinadamu zisizohusisha miradi hiyo, inazingatiwa.
Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastic kwa ajili ya kubebea bidhaa ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikichangia uchafuzi pembeni mwa Ziwa Victoria.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -
Je, Programu za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), Mfuko wa Taifa wa kuendeleza Wajasiriamali (NEDF) na Mfuko wa kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali wadogo (SMF) zimewasaidiaje Vijana, Wanawake na Wajasiriamali wa upande wa Zanzibar katika kujikwamua kiuchumi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Program ya Mifuko yote hiyo iliyotajwa ya kuwaendeleza vijana, wanawake na wajasiriamali, inafanya kazi Tanzania Bara na haitekelezwi upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, mifuko hiyo ilikuwa ni Mfuko wa YDF, WF na NEDF. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awasiliane na mamlaka inayohusika na mifuko hii kwa upande wa Zanzibar ambayo ni Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuona namna ya bora kuwasaidia vijana, wanawake na wajasiriamali wa Zanzibar. Ahsante sana.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -
Je, Serikali inatumia utaratibu gani wa kugawa miradi ya maendeleo kama shule, barabara na afya inayotokana na Muungano na ina mkakati gani wa kuyapa kipaumbele maeneo ya vijijini ikiwemo Jimbo la Wingwi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -
(a) Serikali zetu zote mbili Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa utaratibu wa kugawa miradi ya maendeleo ya Muungano kama shule, barabara na afya unafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizokubaliwa na pande zote mbili za Muungano. Vipo vigezo vinavyotumika katika kutoa fedha za kugharamia miradi ya Muungano kama vile Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo na Sheria nyinginezo zinazotumika kwa pande mbili za Muungano.
(b) Sambamba na hilo, Serikali kupitia misaada ya kibajeti (general budget support) hugawa fedha hizo kwa kigezo kilichokubalika kutumika cha asilimia 4.5 kwa Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar. Aidha, fedha hizo hugawanywa kwenye miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar.
(c) Kwa upande wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania (TASAF) Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili uliozinduliwa Februari, 2020, shilingi bilioni 112.9 zimepangwa kutumika Zanzibar ikiwemo katika miradi ya kijamii ambapo kipaumbele ni kwenye maeneo yenye mahitaji zaidi.
(d) Serikali itaendelea kutekeleza vigezo na tatatibu zilizokubaliwa na pande mbili za Muungano pamoja na kuimarisha majadiliano na mashirikiano kwa lengo la kuhakikisha kuwa miradi inayokubaliwa inatatua changamoto zinazowakabili wananchi waliopo maeneo ya vijijini wakiwemo wa Jimbo la Wingwi. Ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -
Je, zimebaki changamoto ngapi za Muungano kutatuliwa baada ya kufanyika jitihada za kuzipunguza?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, changamoto au hoja Muungano zilizobaki na ambazo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi ni nne (4). Hoja hizo ni Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Usajili wa Vyombo vya Moto, Uingizaji wa sukari inayozalishwa Zanzibar katika Soko la Tanzania Bara, na Mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu.
Mheshimiwa Spika, changamoto hizo zipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na ni matumaini ya Serikali zetu mbili kuwa changamoto zote zitapatiwa ufumbuzi.
MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa kuondoa magugu maji katika Ziwa Jipe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Anania Tadayo, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi imeona changamoto ya uharibifu wa mazingira unaotokana na kuenea kwa magugu maji katika Ziwa Jipe. Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira tayari imefanya tathimini ya uharibifu uliopo na kuandaa andiko la mradi wa hifadhi ya ardhi, na vyanzo vya maji wenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni sita kwa ajili ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Jipe ambapo hadi sasa jitihada za kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia ya Serikali kuhakikisha inarejesha ikolojia ya Ziwa Jipe ili kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo pamoja na uhifadhi wa mazingira. Serikali inamhakikishia Mbunge kwamba mara fedha zitakapopatikana itatekeleza mradi huu mara moja. Ahsante sana.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMED K.n.y. MHE. KAPT. ABBAS ALI MWINYI aliuliza:-
Je, ni kero gani za Muungano bado hazijapata ufumbuzi hadi sasa; na ni jitihada gani zinafanyika ili kero zilizosalia zipate ufumbuzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Kapt. Abbas Ali Hassan, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za Muungano ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi mpaka sasa ni saba ikiwa ni pamoja na:
(i) Moja ni mgawanyo wa Mapato yatokanayo na Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu;
(ii) Usajili wa Vyombo vya Moto;
(iii) Ongozeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO;
(iv) Malalamiko ya Wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili;
(v) Kodi ya Mapato (PAYE) na kodi ya Mapato inayozuiliwa (Withholding Tax);
(vi) Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha;
(vii) Changamoto ya uingizaji wa sukari katika soko la Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuimarisha uratibu wa utatuzi wa hoja zilizobaki kati ya sekta zenye hoja za pande zote mbili za SMT na SMZ na kuwasilisha maamuzi kwenye Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja yenye jukumu la kufuatilia hatua za utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Pamoja na kutoa ushauri kwa sekta zenye hoja namna ya kuendelea kuzitatua hoja hizo. Aidha, Serikali za pande zote mbili zinashirikiana kwa karibu kuhakikisha vikao vya pamoja vilivyokubaliwa kwa ajili ya kupata ufumbuzi hoja zilizosalia vinaendelea kama utaratibu ulivyopangwa.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR aliuliza:-
Je Serikali ina mpango gani wa kupitia upya fedha za Mfuko wa Vichocheo vya Maendeleo ya Majimbo na kuziongeza fedha kwa upande wa Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Jibo la Malindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5(3) cha Sheria ya Mfuko wa Jimbo kimefafanua vigezo vinavyotumika kugawa fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kama ifuatavyo:-
(a) Mgao sawa kwa kila jimbo asilimia 25;
(b) Idadi ya watu katika jimbo asilimia 45;
(c) Kiwango cha umaskini katika Jimbo 20; na
(d) Ukubwa wa eneo katika Jimbo 10.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuangalia uwezekano wa kuboresha mgao wa fedha za Zanzibar kulingana na upatikanaji wa mgao. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuomba fedha katika mifuko ya kupunguza hewa ukaa duniani na kuwalipa wananchi wanaopanda na kutunza misitu katika Wilaya ya Kilolo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justine Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hewa ukaa ni moja ya gesijoto ambazo mrundikano wake angani husababisha mabadiliko ya tabianchi. Moja ya njia zinazotumika kupunguza hewa ukaa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ni misitu ambayo hunyonya hewa ukaa wakati mimea inapotengeneza chakula.
Mheshimiwa Spika, Mkataba huo hauna mfuko mahsusi wa kulipa miradi ya uhifadhi ya misitu inayotekelezwa katika nchi wanachama zinazoendelea kwa ajili ya kupunguza hewa ukaa. Badala yake mkataba huo umeweka utaratibu wa kibiashara ambapo makampuni kutoka nchi zilizoendelea ambazo zinawajibika chini ya mkataba huo kupunguza gesijoto hulipa miradi ya kupunguza hewa ukaa kupitia hifadhi ya misitu katika nchi zinazoendelea. Mfano wa kampuni kutoka nchi zilizoendelea ni Carbon Tanzania kutoka Uingereza ambayo hugharamia miradi ya MKUHUMI katika mikoa ya Manyara na Katavi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ongezeko kubwa la wadau wanaotaka kufanya biashaa hii, Ofisi ya Makamu wa Rais inaandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Biashara ya Hewa Ukaa utakaotumiwa na wawekezaji, taasisi, watu binafsi n a kadhalika wenye nia kufanya biashara hii hapa nchini.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa Mto Kanoni uliopo katika Manispaa ya Bukoba unasafishwa, kina kinaongezwa na kingo za mto zinajengwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshachukua hatua muhimu za kudumu za kuondoa changamoto za Mto Kanoni uliopo katika Manispaa ya Bukoba. Kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba tayari imeibua mradi wa utunzaji wa Mto Kanoni kupitia mradi wa TACTIC unaotarajia kuanza Januari, 2023 wenye thamani ya shilingi milioni 500. Lengo la mradi ni kuondoa kero kubwa ya mafuriko ambayo hutokea kila mwaka nyakati za mvua ya masika na kuathiri zaidi ya kaya 331. Mradi huu utahusisha ujenzi wa maeneo makuu mawili ambayo ni kuongeza kina na upana wa mto; na ujenzi wa kingo za mto.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa sasa Serikali imeendelea kuchukua jitihada za muda mfupi ambapo Manispaa ya Bukoba kila mwaka hutenga kiasi cha shilingi milioni sita kwa ajili ya shughuli za kusafisha, kupanua na kuongeza kina cha mto kwa kuondoa tope, uchafu na miti.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kuleta marekebisho ya Sheria baada ya Serikali kukubaliana kuondoa baadhi ya changamoto za Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge na mtumishi wa Wananchi wa Jimbo la Mwera kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Changamoto zote za Muungano zimekuwa zikitatuliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya Majadiliano na Maridhiano utaratibu ambao umekuwa na mafanikio makubwa. Aidha, katika utatuzi wa Changamoto hizo umeandaliwa utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kushughulikia Masuala hayo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu umetumika kwa mafanikio makubwa na kuhakikisha changamoto nyingi za Muungano zinatatuliwa. Hata hivyo, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge ni mzuri na Serikali inaangalia uwezekano wa kufanya vikao vya pamoja baina ya SJMT na SMZ ili changamoto zilizotatuliwa kupewa na nguvu ya kisheria, nakushukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani kuhakikisha NEMC na ZEMA zinasajiliwa kwenye Mfuko wa GCF?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mkakati uliopo ni kuhakikisha NEMC, ZEMA pamoja na taasisi nyingine zilizoomba au zitakazoomba usajili chini ya GCF zinapata usajili katika Mfuko wa GCF. Hivyo, kwa sasa Serikali inaendelea na mawasiliano, majadiliano na mazungumzo ya kuhakikisha usajili kwa taasisi mbalimbali za Serikali unakamilika.
Mheshimiwa Spika, NEMC tayari imeshaomba na kuanza mchakato wa usajili (accreditation) tangu mwaka 2021, na kwa upande wa ZEMA ilikuwa bado haijawasilisha maombi ya usajili kwenye Mfuko wa GCF. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuhakikisha taasisi zote zilizoomba usajili katika Mfuko wa GCF zinapata usajili ili kunufaika na faida za mfuko huo, ahsante sana.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -
Je, biashara ya Kaboni katika misitu ya asili na ya kupanda imechangia kiasi gani kwenye pato la Taifa tangu iingie nchini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe Mkoani Kigoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka soko huria la biashara ya kaboni ikijumuisha misitu ya asili na ya kupanda. Biashara hii ya kaboni imeanza kushamiri hapa nchini na kuonesha inaweza kuchangia kwenye pato la Taifa. Katika kipindi cha mwaka 2018 – 2022 fedha zilizopokelewa kupitia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri mbalimbali hapa nchini inafikia kiasi cha shilingi bilioni 32.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2023 tumepokea jumla ya miradi mbalimbali 35 ya biashara ya kaboni, pindi mchakato wa usajili utakapokamilika na kuanza kutekelezwa kwa miradi hii, tunategemea kupata wastani wa dola za Marekani bilioni moja, sawa na shilingi trilioni 2.4 ambazo zitachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa, ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, kuna mikakati gani kuhakikisha changamoto za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi hazileti madhara nchini na lini zitapatiwa ufumbuzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetengeneza utaratibu wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za Muungano. Serikali za (SMT) na (SMZ) zimeunda Kamati ya pamoja ya (SMT) na (SMZ) ambayo huundwa na Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano. Katika Kamati hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza changamoto nyingi za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwa Kamati ya Pamoja ya (SMT) na (SMZ) za Kushughulikia hizi kero za Muungano za mwaka 2006, hoja 25 zimepatiwa na kujadiliwa kwa lengo la kulipatia ufumbuzi. Kati ya hoja hizo, hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja ya changamoto za Muungano. Hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kuzipatia ufumbuzi na kwa kuwa Serikali zetu zote mbili za SMT na SMZ zina nia thabiti na dhahiri ya dhati ya kuhakikisha mambo yote yanayoletwa na changamoto katika utekelezaji wa masuala ya Muungano yanapatiwa ufumbuzi ni matumaini yangu ya kwamba hoja hizo zitapatiwa ufumbuzi hivi karibuni. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Je, kuna fursa na changamoto gani kwa Tanzania kushiriki kwenye biashara ya carbon.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fursa kubwa ambayo Tanzania inanufaika katika biashara ya kaboni. Fursa ya kwanza ni uhifadhi wa baioanuai na pili, ongezeko la pato la Taifa. Hivi karibuni halmashauri mbalimbali zimepokea fedha zilizotokana na biashara ya carbon kutoka katika kampuni mbalimbali ambazo zinatumika kujenga miundombinu ya kusaidia jamii katika halmashauri mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na fursa zilizopo bado kumekuwa na changamoto kadhaa katika biashara ya kaboni. Kwanza ni uelewa mdogo wa jamii katika utekelezaji wa biashara ya kabon na pili ni uwazi wa biashara ya kaboni katika soko la dunia. Pamoja na changamoto hizo, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote ili kuhamasisha uwekezaji wa miradi ya biashara ya kaboni katika sekta mbalimbali pamoja na biashara ya kaboni kwa wadau mbalimbali ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu biashara hii, ahsante.
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaenzi na kuwatunza Waasisi wa Muungano?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Haroub Suleiman, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetunga Sheria maalum Na. 18 ya Mwaka 2004 mahususi kwa ajili ya waasisi hao wa Muungano wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na sheria hiyo imetungwa kanuni ya mwaka 2005 inayoweka utaratibu wa namna ya kuwezesha waasisi wetu, ikiwemo kuhifadhi kumbukumbu zao, kazi zao na kueneza falsafa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara Maalum ya Kuwaenzi Waasisi imeundwa ikiwa chini ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Taifa, ikishughulikia na kusimamia ukusanyaji na uhifadhi wa kumbukumbu na vitu vya waasisi wa Taifa kwenye umuhimu wa kihistoria. Aidha, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa kila mwaka kumbukumbu za kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinafanyika, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -
Je, lini Serikali itafanyia kazi changamoto ya kodi na tozo kwenye fedha za Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi na tozo hutozwa kwa mujibu wa sheria pindi bidhaa au huduma zinapotolewa au kununuliwa. Aidha, bidhaa na huduma zinazotolewa hukatwa kodi ya zuio la kodi (With Holding Tax) kwa kuzingatia Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura Na. 332 chini ya kifungu cha 83 (1)(c) kwa malipo ya ada ya kwa huduma kwa ajili ya utoaji wa huduma ya kitaalamu na kifungu 83(a) malipo kwa bidhaa zinazotolewa na mkazi wa uendeshaji biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kodi hutozwa kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi inayotumika Zanzibar inayojulikana kama Sheria Zinazotolewa na Mkazi Wakati wa Undeshaji wa Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Jimbo zinaendelea kuleta tija na matokeo chanya katika kuimarisha na kukuza uchumi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla na hivyo kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haielimishi wananchi kujiepusha na madhara yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabianchi hadi pale maafa yanapotokea?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa kuelimisha wananchi kuhusu madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi ili waweze kujilinda na maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kutoa elimu kupitia njia mbalimbali hasa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu inayotolewa inalenga kukuza uelewa kwa makundi mbalimbali katika jamii hasa makundi ya wakulima, wafugaji na wavuvi kuhusu mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi endelevu zinazoweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini pia kujilinda na maafa yanayoweza kutokea kwa jamii. Ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, lini Serikali itatenganisha dhana ya ushindani na dhana ya kuwalinda watumiaji wa bidhaa na huduma nchini?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kimsingi dhana ya ushindani na kumlinda mlaji zina uhusiano mkubwa kwa sababu ushindani wenye afya katika soko ni mojawapo ya njia bora ya kumlinda mlaji. Kupitia ushindani, mteja hunufaika kwa kupata unafuu wa bei, kuongezeka kwa wigo wa upana, bidhaa bora na chaguo sahihi kwa mlaji, kukuza ubunifu wa uzalishaji wa bidhaa na kudhibiti ukiritimba katika soko.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusimamia ushindani wa haki na kuwalinda watumiaji wa bidhaa na huduma hapa nchini kwa kutumia Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003 ambayo inatarajiwa kufanyiwa marekebisho katika Mkutano huu wa Bunge kwa lengo la kuongeza tija kwa watumiaji kwa kumlinda mlaji, ahsante sana.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga vipi kuendana na kasi ya uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara, pamoja na majukumu mengine iliyonayo, ina majukumu mahsusi ya kusimamia maendeleo ya viwanda na biashara, kuendeleza miundombinu ya viwanda na kukuza mauzo ya bidhaa nje na ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kufuatia uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kama ifuatavyo: -
(i) Kuimarisha na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mahitaji ya usafirishaji wa bidhaa za mazao kwenda sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi;
(ii) Kuimarisha Kamati za Pamoja Mpakani na Asasi za Wafanyabiashara ili kurahisisha ukaguzi wa pamoja wa bidhaa na mazao;
(iii) Kutoa usaidizi kwa wafanyabiashara wadogo wanaonufaika na itifaki ya Soko la EAC, SADC na AfCFTA ili kuharakisha ufanyaji biashara mipakani; na
(iv) Kuanza maandalizi ya Mpango Kabambe wa Ujenzi wa Viwanda kwa Mwaka 2025/2026 hadi 2030/2031 wenye lengo la kuhamasisha uwekezaji nchini.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi zitasaidia kuharakisha ufanyaji wa biashara kupitia usafirishaji na kuhakikisha kwamba uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na miundombinu mingine ikiwemo Reli ya SGR italeta faida kubwa za kiuchumi na kijamii hapa nchini, ahsante sana.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-
Je, lini TBS itaweka utaratibu wa kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo wanaojihusisha na biashara ya kusindika vyakula?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), inatekeleza programu ya kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wakati (SMEs) kwa kushirikiana na SIDO pamoja na wadau mbalimbali katika dhana nzima ya viwango kwa kuhimiza uzingatiaji wa viwango katika uzalishaji wa bidhaa ili kukidhi matakwa ya ubora na ushindani katika soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha kuanzia Mwaka wa Fedha 2020/2021 hadi 2023/2024, jumla ya wajasiriamali wadogo na wadau wa sekta mbalimbali 14,354 walipatiwa mafunzo ya ubora. Aidha, kupitia programu hiyo Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga takribani milioni 350 kila mwaka kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wakati SMEs (Small and Medium Enterprise).
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -
Je, lini Kiwanda cha Mang’ula Machine Tools kitafunguliwa baada ya kufungwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa katambua umuhimu wa Kiwanda cha Mang’ula Machine Tools katika uzalishaji wa mashine na vipuri nchini, Serikali imekusudia kukifufua Kiwanda hicho na kuwezesha kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mitambo, kukarabati badhi ya majengo, uhakiki mali (stocktaking) na uthamini mali wa kiwanda (valuation) ambapo thamani ilibainika kuwa shilingi bilioni 9,571,000,000 kulingana na taarifa ya tarehe 21 Machi 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua itakayofuata ni kutafuta Mbia mwenye uwezo wa kifedha na teknolojia inayohitajika kwa ajili ya kufufua kiwanda hiki. Aidha, kutokana na mpango kazi inatarajiwa mwekezaji apatikane mwishoni mwa Mwezi Februari 2025, ukarabati wa majengo na usimikaji mitambo kukamilika mwezi Disemba, 2025 na hatimaye uzalishaji kuanza Januari, 2026, ahsante!