Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mbaraka Kitwana Dau (9 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie Mpango uliowasilishwa na Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia sote hapa tumeamka salama na tunaendelea na shughuli zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika namna ya kipekee kabisa niwashukuru wapiga kura wa Mafia kwa kuniwezesha kuwa Mbunge kwa kura nyingi sana na leo nimesimama kwa mara ya kwanza katika Bunge lako Tukufu nikichangia Mpango huu. Ninachotaka kuwaambia wananchi wa Mafia, imani huzaaa imani. Wamenipa imani na mimi nitawarejeshea imani. Ahadi yangu kwao, nitawapa utumishi uliotukuka uliopakwa na weledi wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wenyewe watakuwa mashahidi, wameshaanza kuona baadhi ya ahadi ambazo niliziweka kwao zimeanza kutekelezeka. Wananchi wa vijiji vya Juwani na Chole wa visiwa vidogo ambavyo hawakuwa na maji kwa muda mrefu, maji yameshaanza kutoka kule. Wananchi wa visiwa vidogo vya Bwejuu na Jibondo maji wataanza kupata baada ya wiki mbili kutoka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali makini na Serikali sikivu ya CCM kwa kuanza na sisi wananchi wa Mafia. Nimeongea na Waziri makini kabisa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi tukiomba watupatie meli ya MV Dar es Salaam ili kuondoa kero ya usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati. Kimsingi Waziri amekubaliana na hilo na naomba niwafahamishe watu wa Mafia kwamba Serikali imekubali kutuletea meli ya MV Dar es Salaam. Hivi sasa mchakato wa masuala ya kitaalam na ya kiutawala unaendelea na meli hiyo itakuwa Mafia ndani ya muda mfupi kutoka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee vilevile kuipongeza Serikali, tuliomba gati na niliongea na Waziri, Mheshimiwa Mbarawa, bahati mbaya hayupo, lakini ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani upo nakuona hapo, tuliomba gati lifanyiwe maboresho kwa kuletewa tishari kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kuwafahamisha wananchi wa Mafia na Bunge lako Tukufu kwamba tishari lile limefika Mafia juzi, taratibu za kuli-position kwenye gati lile zinaanza na usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni utaboreka zaidi.
Naomba ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani unifikishie salamu kwa Mheshimiwa Waziri, bado tuna matatizo upande wa pili wa Nyamisati, kule maboresho bado hayajafanyika. Tunatambua kwamba Mamlaka ya Bandari ilishatenga bajeti kwa ajili ya kufanya maboresho upande wa Nyamisati. Meli hii itakayokuja kama upande wa Nyamisati hakutafanyiwa maboresho itakuwa haina maana yoyote.
Kwa hiyo, nakuomba kwa namna ya kipekee ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani na nikimaliza kuchangia nitakuja hapo kwako nikuelezee in details. Maboresho ya Bandari ya Nyamisati ni muhimu sana katika kuhakikisha meli ile ya MV Dar es Salaam inafanya kazi zake baina na Kilindoni na Nyamisati bila ya matatizo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee pia nikushukuru ndugu yangu, mzee wangu Mheshimiwa Profesa Muhongo. Nilikuletea concern yetu watu wa Mafia kuhusiana na kusuasua kwa mradi wa REA. Ukachukua hatua na ninayo furaha kukufahamisha kwamba nimeongea na watu wa TANESCO na tumekubaliana kwamba mradi ule utakabidhiwa baada ya mwezi Machi, hivyo basi nakushukuru sana. Pia tulinong‟ona mimi na wewe kuhusu suala la submarine cable kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, submarine ndiyo solution …
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau, naomba sana tuendelee kutumia lugha ya Kibunge.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nilikuomba Mheshimiwa Muhongo kwamba ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme Mafia ni kuzamisha submarine cable kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni.
Kimsingi ukaniambia niendelee kukukumbusha. Mimi kwa kuwa wewe ni jirani yangu hapa kila nikifika asubuhi shikamoo yangu ya kwanza ni submarine cables…
MWENYEKITI: Kwa mujibu wa Kanuni ya 60, elekeza maongezi yako kwa Mwenyekiti.
MHE. MBARAKA K. DAU: Submarine cable itakuwa ndiyo salamu yangu ya kwanza ya asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nianze sasa kuchangia Mpango. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Ashatu wameleta Mpango mzuri sana. Mimi naamini madaktari hawa wawili watatuvusha, tuwape ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye ugharamiaji (financing) wa Mpango huu. Mpango uliopita ulipata matatizo makubwa sana kutokana na ukosefu wa fedha. Naamini kwa ari na kasi iliyoanza nayo Serikali ya Awamu ya Tano ambapo ukusanyaji wa mapato umekuwa mkubwa sana sambamba na kubana matumizi ya Serikali, financing ya Mpango huu wa sasa haitakuwa tatizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, concern yangu ipo kwenye sehemu ya pili ya financing ya Mpango huu ambayo ni sekta binafsi. Sekta binafsi wanakuja kuwekeza lazima sisi wenyewe tuweke mazingira wezeshi kama mlivyosema katika Mpango wenu, kwamba ili watu waje kuwekeza hapa lazima mazingira yawe mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, ninachotaka kusema ni kwamba tuwe waangalifu na hawa wawekezaji wanaokuja. Nitatolea mfano kule Mafia na Mzee wangu Mheshimiwa Lukuvi naomba unisikilize vizuri sana hapa, tuna Kisiwa kinaitwa Shungimbili. Mafia imezungukwa na visiwa vingi tu lakini kimoja kinaitwa Shungimbili. Kisiwa hiki cha Shungimbili kimebinafsishwa au sijui niseme kimeuzwa au sijui niseme kimekodishwa bila ya Serikali ya Wilaya kuwa na habari. Namuuliza Mkurugenzi anasema hana taarifa, namuuliza DC wangu anasema hana taarifa, naomba sana…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na usalama na leo tumekutana hapa tukiwa na afya njema ili kuweza kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Mtukufu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyoiendesha nchi yetu mpaka sasa, kwa ukusanyaji mzuri na uongozi mzuri katika kipindi kifupi alichokua madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu pia nizielekeze kwa ndugu yangu, Komredi, Mheshimiwa Waziri Mwigulu pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Olenasha, kwa kazi nzuri na hotuba nzuri waliyoiwasilisha leo asubuhi hapa. Combination yao ni nzuri sana na tunawategemea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niendelee kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo langu la Mafia kwa kunichagua na kuendelea kuniamini niweze kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kwa kusisitiza hili, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba ile x-ray machine na ultrasound machine ambazo niliziahidi katika kampeni yangu, zimeshatoka bandarini na zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii, zitakuwa Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nukta hii, namshukuru sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kuweza kutusaidia kupata vibali muhimu vya TFDA na leo x-ray machine na ultra sound, tayari zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia Taasisi ya MIDEF ambayo ndiyo iliyo-donate mashine hizi kwa Jimbo la Mafia. Na mimi mwenyewe pia nijipongeze kwa ushindi mkubwa nilioupata kwenye uchaguzi na kwenye kesi iliyofunguliwa na mgombea wa chama cha CUF. Nimeshinda, akakata rufaa na nimeshinda tena. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo.
Kwa upande wa Jimbo la Mafia, uchumi wa Jimbo la Mafia umebebwa na uvuvi na utalii. Kwa masikitiko makubwa sana kuna taasisi ya Serikali maarufu kama Marine Park, badala ya kuwa msaada kwa wananchi wa Mafia imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Mafia. Taasisi hii ya Marine Park, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, naomba sana na utakapohitimisha nitahitaji kusikia kauli kutoka kwako kuhusiana na Marine Park.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wanatudhulumu watu wa Mafia kwenye mgao unaotokana na mapato ya watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 wanachukua Marine Park na asilimia 30 ambapo 10 zinakwenda kwenye Halmashauri na asilimia 20 inakwenda kwa vijiji husika ambavyo watalii wale wanakwenda. Mgao huu siyo sawa ukizingatia maeneo mengine kama Hifadhi ya Wanyamapori ambapo wananchi wa maeneo husika wanapata asilimia 60 na Serikali Kuu inapata asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapokuja kwenye Marine Park, wamekuwa wakitudhulumu wananchi wa Mafia. Tumelisema sana hili! Kila ukiongea nao wanakwambia kwamba hii ni sheria, hii ongea na watu wa Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda sana wakati unahitimisha hotuba yako Mheshimiwa, ndugu yangu rafiki yangu Komredi Mwigulu ulitolee maelezo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea suala la Marine Park, watu wa Marine Park wametoka katika kazi yao ya msingi ya uhifadhi na hivi sasa wamekuwa madalali, wanauza ardhi. Visiwa vitatu vya Mafia vidogo vidogo sasa vimeshauzwa na Marine Park. Visiwa hivyo ni Nyororo, Mbarakuni pamoja na Kisiwa cha Shungimbili. Huu mchakato wa kuuza pengine siyo tatizo kubwa sana, tatizo kubwa sana kwa nini hawataki kufuata taratibu? Huwezi ukauza ardhi au kuibinafsisha bila kuwashirikisha wananchi husika wa vijiji vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, kwa masikitiko makubwa sana, watu wa Marine Park wamevibinafsisha visiwa hivi kwa kutengeneza mihtasari fake kuthibisha kwamba wananchi wameshirikishwa. Ukweli ni kwamba wananchi hawajashirikishwa na nyaraka walizo-forge ninazo hapa, nitakuletea kwako hapo ili uzione na uweze kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mgao usio sawia wa maduhuli yanayotokana na watalii, vilevile pesa zinazotolewa pale kwa mujibu wa maelezo yao wenyewe Marine Park wanasema kwamba Marine Park ya Mafia ndiyo inaendesha Marine Park zote Tanzania. Mapato yanayotoka kule, sehemu kubwa yanaendesha Marine Park nyingine za nchi yote. Kisiwa kama Mafia kidogo chenye uchumi mdogo kwenda kukitwisha mzigo wa kuendesha Marine Park zote zilizopo Tanzania, kwa kweli hili siyo sawa. Hata huu mgao wa asilimia 70 wanautoa baada ya kutoa gharama zote, kwa maana ya gharama za uendeshaji. Hii tunaiona pia siyo sawa. Namwomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, hili nalo aliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tukirudi kwenye suala la uhifadhi wenyewe, Marine Park kazi yao ya uhifadhi yenyewe imewashinda ukianzia Moa, Pwani ya Tanzania mpaka Msimbati kule, mabomu yanapigwa usiku na mchana. Pale Dar es Salaam kuanzia Magogoni pale Ikulu kwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli mpaka Pemba Mnazi, mchana na usiku ni mabomu yanapigwa kama nchi iko kwenye vita. Tunashangaa uhifadhi gani wanaoufanya hawa wa Marine Park. Mheshimiwa Waziri Marine Park ni jipu na ninaomba sana ulitumbue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, mkononi mwangu hapa ninao waraka uliotolewa na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kilimo na Mifugo wakati ule Mheshimiwa John Pombe Magufuli, waraka wa tarehe 12 Agosti, 2008, ukitoa ruhusa kwa wavuvi ambao wamezuiwa wasitumie mitungi ya gesi migongoni mwao wanapokwenda kuvua katika kina kikubwa cha maji. Kina cha mita 50 mtu hawezi kuzamia kwa kuziba pua, ni lazima aende na mtungi wa gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Marine Park wanawakataza wananchi na wanaendelea kuwakamata. Hivi ninavyozungumza, wapigakura wangu zaidi ya 20 wameswekwa rumande kwa sababu wamevua kwa ya kutumia mitungi ya gesi. Mitungi ya gesi Mheshimiwa Waziri, haiharibu mazingira, inamsaidia mvuvi aweze kwenda kina kikubwa zaidi kwenda kutoa nyavu zake zilizonasa. Haina uhusiano wowote na uharibifu wa mazingira, hata ndugu yangu Makamba anaweza akathibitisha hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo cha mwani, Marine Park...
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sera ya kuwekeza kwenye viwanda, nashauri tujikite zaidi kwenye viwanda vidogo vidogo vyenye kuongeza thamani ya mazao yetu badala ya viwanda vya kuzalisha bidhaa kamili kama hatuna “comparative advantage” ya bidhaa za aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali itafute mwekezaji wa Kiwanda cha kusindika samaki katika Kisiwa cha Mafia sambamba na kupata meli za uvuvi zenye zana za kisasa zenye uwezo wa kuvua katika bahari ya kina kirefu. Mafia ipo karibu na mkondo wenye kina kirefu kunapopatikana samaki wengi na wakubwa wa aina mbalimbali kama Jodari (Tuna) nguva (King fish) samsuri (Marley) na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa viwanda vya sukari umekuwa mdogo na hautoshelezi kulisha soko la nchi nzima. Ipo hoja na haja ya kuvutia mwekezaji kuwekeza katika bonde la Mto Rufiji ili kuondokana na tatizo la kuagiza sukari kila mwaka. Naishauri Serikali pia katika kipindi hiki kuelekea kujitosheleza kama uzalishaji wa ndani wa sukari, Serikali itoe vibali kwa kuagiza sukari kwa viwanda vyenyewe, mfano, Mtibwa, Kagera na kahalika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kuwa hapa wote tukiwa salama na afya na kuweza kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa nimshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ndugu yangu Mheshimiwa Makame Mbarawa na Naibu wake rafiki yangu Mheshimiwa Ngonyani kwa hotuba nzuri sana ambayo kwa kiasi kikubwa sana imejikita katika kuondoa matatizo na kero mbalimbali za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye uchangiaji. Kuna dhana hii ambayo ilikuwa ikizungumzwa sana ya maeneo ya pembezoni, maeneo yaliyosahaulika. Kwa bahati mbaya sana, kila inapojadiliwa maeneo ya pembezoni na yaliyosahaulika kisiwa cha Mafia kinasahaulika. Wananchi wa Kisiwa cha Mafia wana kila aina ya sababu na sifa zote za kuitwa watu ambao ni wa maeneo ya pembezoni na waliosahaulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo mtu akisafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza kuanzia saa 12 asubuhi akifika saa 3 au 4 lakini mwingine akaondoka na boti Dar es Salaam pale akielekea Mafia basi yule wa Mwanza atafika wa Mafia hajafika. Nayasema haya kwa sababu adha ya kusafiri kwa boti kutoka Dar es Salaam mpaka unafika Mafia inaweza ikachukua siku moja mpaka mbili na ndiyo maana kwa makusudi kabisa tukaamua wananchi wa Mafia wanapotaka kusafiri wanakwenda Kusini kidogo kwa kutumia barabara ya Kilwa mpaka maeneo ya Mkuranga, wengine wanakata kushoto wanakwenda Kisiju. Sasa matatizo yanaanza pale, barabara ya Kisiju - Mkuranga kilometa kama 46 ni ya vumbi, ni mbaya sana na imekuwa ikipigiwa kelele sana lakini bado haijashughulikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bandari ya Kisiju ni kama economic hub ya Kisiwa cha Mafia kwani mazao yote ya nazi na yanayotokana na bahari yanapitia bandari ya Kisiju lakini tatizo la uharibifu wa barabara ile ya Mkuranga – Kisiju ni kubwa. Nimeangalia kwenye Kitabu cha Mheshimiwa, nikakisoma mara mbili mpaka tatu sikuiona barabara ya Mkuranga - Kisiju ambayo ni kilometa 46. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha basi alitolee maelezo suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namna ya pili ambayo abiria wengi wanaitumia kufika kisiwa cha Mafia ni kwenda mpaka Bungu, Rufiji wanakata kushoto wanakwenda mpaka kwenye bandari ya Nyamisati. Baina ya Bungu na Nyamisati ni kama kilometa 41, pale napo pia barabara ni kama hakuna. Ina mashimo na kipindi kama hiki cha mvua inakuwa kama imekatika. Wananchi wa Mafia wanaposafiri na boti kutoka Kilindoni wakafika Nyamisati wana kazi nyingine pale ya kudandia magari mbalimbali na wengine bodaboda ili wafike Bungu na hatimaye kuja Dar es Salaam. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha ulielezee hilo pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Kisiwani Kwenyewe Mafia, kuna barabara kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi kilometa 55. Mkononi kwangu hapa nina Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo tuliyoinadi kwa wananchi, ndani ya Ilani hii inasema wazi kabisa, Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo tutajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi (Bweni). Hata hivyo, nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuiona barabara hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana atakapokuja ku-wind up alitolee maelezo na hilo nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mafia kuna barabara inaitwa Airport Access Road kilometa 14 inatoka Kilindoni inakwenda mpaka Utende ambayo imetengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa masikitiko makubwa sana, barabara ile haijakabidhiwa huu unafika mwaka mmoja toka imekamilika. Naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri, itakapofika wakati mkandarasi anataka kuikabidhi barabara ile Serikali msikubali kuipokea kwani ina mashimo mwanzo mpaka mwisho na mpaka leo haijazinduliwa. Barabara ina matatizo, kuna jokes zinaendelea kule Mafia wanasema kama gari ikipata pancha ukipiga jeki badala ya ile gari kwenda juu basi jeki ndiyo inatitia chini kama vile umepiga jeki kwenye matope. Kubwa zaidi wenyewe wanaiita barabara ya Big G maana yake ina mashimo mashimo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nizungumzie kuhusu Bandari ya Nyamisati ambayo na yenyewe pia imo katika kitabu hiki cha Ilani ya CCM. Jana kwa bahati nilipata fursa ya kuongea na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) akanithibitishia kwamba bandari ile itajengwa lakini pesa zilizotengwa zilikuwa ni kidogo na walipoenda kufungua zabuni wakakuta ame-quote shilingi bilioni nane na wao Mamlaka ya Bandari hawana uwezo wa kulipia fedha hizo. Akanihakikishia Mkurugenzi Mkuu kwamba wamenunua dredger (mashine la kuchimbia na kuongeza kina kwenye bandari), kwa hiyo wamesema kazi hiyo wataifanya wao wenyewe.
Mheshimiwa Waziri naomba wakati utakapokuja ku-wind up uniambie na uwaambie wananchi wa Mafia ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya Bandari ya Nyamisati kazi ambayo wataifanya wenyewe Mamlaka ya Bandari? Vinginevyo kwa mara ya kwanza mimi sijawahi kutoa shilingi hapa lakini leo kama nisiposikia habari ya Bandari ya Nyamisati kiasi gani kimetengwa na mimi nitaingia kwenye record hapa ya kuzuia shilingi au pengine hata noti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mafia. Sasa hivi tuna kilometa 1.5 ili ndege kubwa ziweze kutua tunahitaji runway yenye angalau kilometa 2.5 ili watalii waweze kuja moja kwa moja katika Kisiwa cha Mafia. Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri iliyobaki pale ni kilometa moja tu, naomba sana mtupatie hiyo kilometa moja ili watalii waweze kuja Mafia na tuweze kunufaika na biashara ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MV Dar es Salaam…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, shukurani kwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wa Wizara kwa hotuba nzuri yenye kuleta matuamini kwa Watanzania. Mradi wa umeme wa REA kwa Kisiwa cha Mafia umebakiza vijiji na maeneo 10 kukamilika, navyo ni vijiji vya Gonge, Jojo, Mariam, Bani, Jibondu, Juani, Chole, Dongo na Maeneo ya Tumbuju, Bwejuu na Tongani. Ombi langu kwa Wizara ni vijiji na maeneo husika viingizwe kwenye mradi wa REA Phase III.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uzalishaji wa umeme kwa sababu umeme Mafia unatokana na chanzo cha mafuta yanayoendesha majenereta yaliyopo. Kutokana na gharama kubwa ya ununuzi wa mafuta na matatizo ya usafiri wa mafuta hayo kwa njia ya bahari, ombi letu wananchi wa Mafia ni kwamba, Serikali sasa iunganishe na umeme wa SONGAS kupitia kupitishwa kwa submarine cable kutokea Nyamisati kwenda Kilindini takriban kilomita 50 ili kuondokana na adha ya kusafirisha mafuta mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utafiti wa mafuta na gesi, katika Kisiwa cha Mafia ni jambo linalofanywa mara kwa mara. Kwa habati mbaya sana wananchi wa Mafia wamekuwa hawapewi taarifa tunaomba Wizara na Waziri wakati atakapokuwa anajibu awaeleze wananchi wa Mafia kama mafuta au gesi vimegundulika Mafia au hapana ili kuondoa hali ya sintofahamu kwa wananchi wa Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kwenye ugunduzi wa gesi hasa maeneo ya kina kirefu cha bahari yaani off share maeneo ya Kusini mwa Tanzania. Mpakani mwa Wilaya ya Kilwa na Mafia, katikati ya bahari kuna visima viwili ambavyo kimpaka kimo katika Wilaya ya Mafia, lakini kutokana na matatizo ya usafiri shughuli za uchimbaji na utafiti zimekuwa zikifanyika kutokea Wilaya ya Kilwa.
Swali je, wananchi wa Mafia wananufaika vipi na visima hivi ambavyo kimipaka vipo Mafia lakini shughuli za uchimbaji zinafanyika Kilwa?
Suala lingine ni bomba jipya la gesi kutoka Kusini kuja Dar es Salaam, ujenzi umekamilika kwa asilimia 100. Swali, je, ni lini bomba litaanza kusafirisha gesi kutoka Kusini kwa matumizi ya kibiashara? Swali lingine, ni lini umeme ghafi utachakatwa na kuweza kutumika kwa matumizi ya majumbani?
Mheshimiwa Naibu Spika, natanguliza shukurani na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba hizi mbili alizozileta Waziri wa Fedha na Mipango, Hali ya Uchumi na Bajeti ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na salama, leo tumekutana hapa kujadili mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana Dkt. Phillip Mpango, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kutuletea bajeti ambayo nimeiita ni bajeti ya kihistoria. Haijapata kutokea katika historia ya nchi yetu Bajeti ya Maendeleo ikawa asilimia 40 ya bajeti yote ya Taifa. Kwa kweli pongezi nyingi sana zimwendee Mtukufu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa dhamira hii ya dhati ya kuwaondoa wananchi wa Tanzania katika lindi la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata faraja kubwa sana, nilikuwa najaribu kufanya tathmini ndogo hapa, nikagundua miundombinu peke yake imetengewa asilimia 25.4, elimu asilimia 22 na bajeti ya afya ni asilimia 9.2. Hapa kwenye bajeti ya Wizara ya Afya, Abuja Declaration inatutaka tutenge bajeti ya asilimia15. Wanasema Rome haikujengwa siku moja, kidogo kidogo ndani ya bajeti mbili, tatu zijazo tunamwomba sana Dkt. Mpango Azimio hili la Abuja la asilimia 15 katika bajeti ya Wizara ya Afya lifikiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze moja kwa moja kwenye kuchangia bajeti. Ushiriki wa sekta binafsi na sekta ya umma katika miradi ya pamoja kimekuwa ni kilio cha siku nyingi sana, tumelizungumza sana hili na ninayo furaha na nahisi faraja kubwa sana, kupitia kwenye bajeti hii nimeuona ushiriki huu wa sekta binafsi na sekta ya umma kwa maana ya PPP, tatizo langu ni dogo tu!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha basi atuletee na mchanganuo, kwa sababu tumeona tu humu miradi, mimi naiona kama ni blanket imewekwa humu, miradi kama ya barabara ile ya Chalinze – Dar es Salaam express way, mradi wa Reli ya Kati, miradi hii ya umeme ya phase III kule Kinyerezi ipo tu kwa ujumla ujumla!
Mheshimiwa Naibu Spika, tungeomba sana hebu watupatie break down na frame work, timeline kwamba miradi hii tunafanya labda tutaanza na mradi wa reli ya kati standard gauge, labda tarehe fulani mpaka itakapofikia mwaka wa fedha miaka miwili, mitatu, mbele mradi huu utakuwa umekwisha; labda mradi wa bandari ya Bagamoyo utaanza tarehe fulani mwaka wa fedha fulani na utakwisha hivi, ili tupate kwa ujumla wake haya mambo yanakwendaje; lakini kutujazia tu miradi ya jumla bila ya kutupa timeline inatusumbua sana, kwa sababu tunajenga matumaini, lakini ndani yake hatujui miradi hii itakuja lini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye suala la utalii. Nilizungumza hapa kwenye Wizara ya Maliasili na Utaii ilipoleta bajeti yake na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri namwona pale na namwomba Mheshimiwa Waziri anitegee sikio. Takwimu zinatuambia kwa miaka miwili kati ya mwaka wa fedha uliopita na mwingine wa nyuma yake, utalii wetu umeshuka kwa karibu watalii laki moja, sasa sitaki kujielekeza kwenye sababu gani zimepelekea watalii kupungua. Nataka nijielekeze kwenye namna ambavyo tunaweza tukatangaza utalii wetu ili tupate watalii wengi na kuhakikisha kwamba tunapata mapato katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumza utalii mara nyingi tunajikita kwenye vitu viwili tu, Mlima Kilimanjaro na Mbuga, wakati Tanzania na Naibu Waziri wakati anajibu swali hapa juzi alisema wazi kwamba Tanzania ni ya pili duniani kwa vivutio vya kitalii, sasa hivi vivutio vingine vitatangazwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Kisiwa cha Mafia na nilizungumza hapa wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwamba kule Mafia tuna samaki anaitwa ‗Papa Potwe‘, huyu samaki ni samaki wa ajabu, anatabia kama za dolphin, ni samaki rafiki, watalii wanapenda sana kuja kuogelea naye. Je, ni wangapi wanajua habari za samaki huyu ‗Papa Potwe‘?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunaomba sana mtengeneze package ya vivutio vyote ili muweze kwenda kuviuza huko nje, kwa sababu Halmashauri hatuna uwezo wa kumtangaza ‗Papa Potwe‘! Ni lazima tusaidiwe na nguvu ya Serikali. Kwa hiyo naomba sana tutanue wigo katika utalii wetu katika kuutangaza na kuhakikisha kwamba tunapata mapato mengi ili kuendeleza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango, hili nililizungumza kwako kama mara moja au mara mbili hivi, masikitiko yangu makubwa kuona kwamba Kisiwa cha Mafia hakikuingizwa katika zile flagship project kwa ajili ya Mpango wa Pili wa Maendeleo, kwa maksudi kabisa! Mimi nilikuwa naiona Mafia kama ndiyo Zanzibar mpya! Tuifungue kiutalii Mafia ili watalii waje.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale tuna matatizo mengi na tunahitaji investment ndogo sana kuifungua Mafia. Barabara inayotoka Kilindoni mpaka Rasimkumbi kilometa 55 ikitengenezwa hiyo ikitiwa lami pamoja na bandari yetu na ndugu yangu Ngonyani pale ananisikia, kuhusu bandari ya Nyamisati, Mamlaka ya Bandari imetenga nafahamu kwamba bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ile, ikikamilishwa sambamba na bandari ya Kilindoni na kuongezwa kwa runway, airport ya Mafia…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Maliasili na Utalii. Mheshimiwa Waziri nianze kwa kuunga mkono hoja yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili suala la utalii ni suala ambalo lipo interconnected, tunazungumzia utalii ambao uko under utilized. Utalii ili uwe utalii, utalii ili uweze kufanya kazi sawasawa ni lazima sekta nyingine saidizi ziweze kusukuma twenda sambamba, kwa mfano, suala la miundombinu kuanzia barabara na maeneo mengine ya usafiri, hata huduma za viwanja vya ndege. Matatizo yetu ya usafiri na utalii yanaanzia pale airport ya Dar es Salaam na Kilimanjaro. Mtalii anakuja anakutana na mazingira ambayo ni very unfriendly, hawezi kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtalii anakaa anasubiri wale wanaochukua visa on arrival anakaa masaa matatu, mwingine anakaa kwenye foleni pale airport yenyewe, kuna joto, air condition hazifanyi kazi anaanza ku-experience matatizo akiwa pale kiwanja cha ndege. Sasa tunapozungumzia kukuza utalii tuangalie na aspect kama hizi tuhakikishe kwamba vituo vyetu vya airport na maeneo mengine ambayo watalii wanakuja wanaanza ku-experience mambo mazuri, pamoja na vitanda kule kwenye hoteli zetu ziwe za kutosha na miundombinu mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii dhana ya utalii tumejikita zaidi kuangalia mbuga pamoja na Mlima Kilimanjaro na vivutio kama hivyo. Lakini dhana ya utalii ni pana zaidi ya Mlima wa Kilimanjaro na mbuga. Kwa mfano, mimi natokea kisiwani Mafia, Kisiwa cha Mafia ni kisiwa tajiri sana kwa utalii, lakini mazingira ili uingie Mafia ni magumu kweli kuanzia usafiri kwa maana usafiri wa bahari na usafiri wa ndege. Lakini kubwa zaidi ni namna gani Serikali inatangaza utalii katika maeneo mbalimbali ya vivutio hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia tuna samaki anaitwa a whale shark au kwa jina lingine la Kiswahili anaitwa Potwe, samaki huyu ana tabia kama za dolphin, ni samaki friendly anaweza akaogelea na watalii, hana matatizo. Lakini dunia nzima samaki huyu anapatikana Australia na Mafia tu. Ni wangapi miongoni mwa Watanzania tunalijua hilo kwa utalii wa ndani peke yake ikilinganishwa na utalii wa nje? Kwa hiyo tunahitaji kwanza kutangaza na kuwekeza katika miundombinu ili vitu hivi vinapokuwa connected pamoja, basi utalii wetu utasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia kuna vivutio mbalimbali kama scuba diving, sport fishing na utalii wa kwenda kuangalia papa Potwe, lakini bado Serikali haijatia mkazo kuweza kutusaidia kutangaza utalii huu. Kikubwa zaidi Mheshimiwa Waziri pale kisiwani Mafia hatuna hata Afisa wa Utalii utawezaje kukuza utalii kwenye destination muhimu kama ya Mafia bila ya kuwa na Afisa wa Utalii wa Wilaya? Tumelizungumza hili sana, tumeandika barua lakini mpaka leo hatujapata Afisa wa Utalii.
MWENYEKITI: Ahsante muda wako ulikuwa ni dakika tano tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuanza kwa kuunga mkono hoja. Pili, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri Profesa Jumanne Maghembe na Naibu wake Engineer Ramo Makani kwa hotuba nzuri na yenye kuleta matumaini kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali sikivu ya CCM kutanua wigo wa vivutio vya utalii kwa muda mrefu kumejengeka dhana kuwa utalii maana yake ni mbuga za wanyama na maeneo ya fukwe peke yake. Dhana hii si sahihi, kwani utalii una wigo mpana zaidi. Kwa mfano katika jimbo langu la Mafia (Kisiwa) kuna samaki aina ya papa mkubwa sana anaitwa Mhaleshark (Potwe) ni one of the species of shark, papa huyu ni adimu sana duniani, kwa sasa anapatikana Australia na Mafia tu dunia nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Australia ni ghrama kubwa kwa mtalii kwenda kumuona samaki huyo na moja ya sifa za whaleshark ni papa rafiki ana tabia zinazofanana na dolphin (pombuwe) mtalii anaweza kuogolea naye bila ya kupata madhara yoyote ile. Hivyo mtalii Australia anatumia gharama kubwa ikiwa ni pamoja na kukodi helikopta kwenda maeneo ya mbali sana kuogolea na papa. Lakini kwa upande wa Mafia papa huyu anaonekana umbali usiozidi mita 300 kutoka bandari kuu ya Kilindini Mafia. Ombi letu wana Mafia Serikali kupitia Bodi ya Utalii itusaidie kuutangazia ulimwengu upatikanaji na papa huyo ili kuongeza watalii wengi Mafia sambamba na maboresho ya hoteli zetu za kitalii na miundombinu ya kuingia na kutoka Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uvunaji wa mikoko katika Kisiwa cha Mafia mwekezaji Tanspesca amewekeza kiwanda cha kamba katika kijiji cha Jimbo na kupewa kibali na Wizara ya Utalii kukata baadhi ya mikoko. Tunaiomba Wizara sehemu ya mapato yatokanayo na kukatwe kwa mikoko hiyo ibaki katika Halmashauri ili kuweza kusaidia shughuli za uhifadhi katika Kisiwa cha Mafia ikiwemo kupanda mikoko mingine kufidia ile iliyokatawa.
Suala lingine ni kukosekana kwa Afisa Utalii katika Wilaya ya Mafia. Pamoja na potential kubwa ya utalii katika Wilaya ya Mafia bado mpaka sasa hatuna Afisa wa Utalii wa kuratibu shughuli za utalii kisiwani Mafia, tunaomba Wizara kulifanyia kazi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine nawashukuru Waziri na timu yake yote na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mahiga, Naibu wake na timu nzima ya Wasaidizi wao katika Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia hoja kwa kuelezea masikitiko yangu ya utoaji wa Visa katika Balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia tunataraji Serikali sasa imefika wakati tuanzishe utaratibu wa kutoa Visa online, utaratibu huu sasa wa watu kutakiwa waende wenyewe moja kwa moja ni wenye usumbufu na umepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Wizara ione umuhimu pia wa kufungua ofisi za ubalozi wa Tanzania Korea ya Kusini, kule kuna potential kubwa ya kunufaika na fursa za teknolojia na watalii kutembelea nchi yetu. Pia Balozi zetu kutumika vizuri kwa kutangaza Tanzania kiutalii na fursa nyingine za kibiashara ili nchi yetu inufaike na uwepo wa Balozi hizo badala ya utaratibu wa sasa wa kutoa Visa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia ione umuhimu wa kuongeza kasi ya kujenga au kununua majengo kwa ajili ya Balozi zetu wenyewe, baada ya miaka 55 ya uhuru badala ya kuendelea kupanga wakati nchi nyingine ndogo kama Eritrea zimejenga nyumba zao wenyewe. Umefika wakati sasa Serikali iongeze kasi ya ujenzi au ununuzi wa majengo yetu wenyewe kwenye Balozi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.