Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rose Kamili Sukum (1 total)

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ambayo kwa kweli hayatekelezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili lilipitisha Mpango wa Miaka Mitano 2011/2012 hadi 2015/2016 na swali langu ndiko lilikoelekea, lakini kitu cha kushangaza ni kwamba, tuliamua kwamba Bunge hili shilingi bilioni 100 ziwe zinatengwa na zinatolewa kila mwaka kwa ajili ya benki hiyo kama mtaji ambapo ni shilingi bilioni 60 tu zilizotolewa katika benki hiyo kwa miaka mitano. Je, shilingi bilioni 440 ambazo hazikutolewa na Serikali hii, ziko wapi? Tunataka kujua, kama hamna huo mtaji, hiyo Benki ya Mikopo itafanyaje kazi kwa Watanzania ambao ni wakulima 98%? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nasikitika sana kuwadanganya Watanzania. Hii benki imeundwa kwa ajili ya kuinua uchumi wa wakulima wadogo wadogo. Wako wakulima zaidi ya 98% nchini. Leo tangu benki imeanzishwa imekwenda Iringa tu na kuwapa vikundi vinane tu shilingi bilioni moja: Je, kati ya zile shilingi bilioni 60, nyingine zilikwenda wapi kama ni shilingi bilioni moja tu zilitolewa kwa hao wakulima ambao ni wachache? Je, asilimia..
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kesho tunatarajia kwamba tutafanya negotiation na African Development Bank kwa ajili ya mkopo nafuu wa UA milioni 50 lakini pia UA milioni 25 ambao tunatarajia kwamba utakuwa ni mkopo nafuu ambao Serikali ita-own land TADB kwa ajili ya kuboresha mtaji wa benki hiyo iweze kuendelea kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya fedha zote hizo zile 50 za kwanza ni takriban shilingi bilioni 150 na hizi nyingine ni takriban shilingi bilioni 75. Kwa hiyo, Serikali inafanya jitihada ya dhati kabisa kuongeza mtaji wa TADB.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; niseme tu kwamba, Benki hii imetoa mikopo kwa vikundi mbalimbali zaidi ya hivyo ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amevieleza, Mheshimiwa Rose Sukum naweza nikakupatia orodha ya vijiji ambavyo vimepatiwa jumla ya bilioni 5.9 kwa Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga hadi hivi sasa na naweza nikatoa hii taarifa ya mikopo iliyotolewa hadi kufikia tarehe 31 Oktoba.