Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdallah Hamis Ulega (15 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge lako hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nichukue fursa hii adhimu kabisa kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Mkuranga katika Mkoa wa Pwani, naomba niwahakikishie ya kwamba kazi yao walionituma ya kuwawakilisha nitaifanya kwa weledi, uaminifu, juhudi na maarifa yangu yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizi, nami kwa kuwa sikupata fursa ya kujadili hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa hapa katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nichukue fursa hii pia kusema kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais ilimaliza kazi yote, nami binafsi baada ya pale nilifanya ziara katika Jimbo langu la Mkuranga kwa ajili ya kutoa shukrani na Wanamkuranga wana imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Wanasema Mheshimiwa Rais aendelee na kazi yake na imani yetu ya kuiona Tanzania ikielekea katika uchumi wa kati ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niendelee katika hoja hii inayohusu Mpango wa Maendeleo ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa Bungeni. Kwanza kabisa ningeenda kugusa katika eneo la viwanda. Mkakati wa Serikali yetu ni mzuri, na mimi binafsi nauunga mkono kwa asilimia 100. Hata hivyo, yapo mambo ambayo ningefikiri kwamba hatuna budi kujielekeza kuona ni namna gani tunajipanga nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la viwanda, pale Mkuranga, neema ya viwanda imeshaanza kuonekana. Tunavyo viwanda vingi sana sasa ambavyo vinajengwa kila kukicha. Sababu yake kubwa ni pamoja na kwamba Dar es Salaam imeshajaa na sasa inapumulia katika Wilaya ya Mkuranga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwetu imekuwa ni faraja kubwa sana na tungeomba jambo hili liendelee na hata Serikali iendelee kutusaidia kuhamasisha kuhakikisha kwamba wawekezaji wa viwanda mbalimbali wanaendelea kumiminika pale katika Jimbo letu hili la Mkuranga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango mkakati wa maendeleo uliopita, wakati tunaujadili utekelezaji wake, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alisema neno, kwamba katika mambo yaliyotufanya tushindwe katika uwekezaji wa viwanda hapo nyuma ni pamoja na fidia za ardhi. Fidia ya ardhi ipo kwa mujibu wa Sheria namba 4 ya mwaka 1999, lakini ninalo jambo ambalo nilikuwa nikilifikiri sana na nilikuwa nafikiri kwamba wataalam walichukue wakalijadili, waone ni namna gani tunaweza tukaboresha kitu cha namna hii. Hizi fidia za ardhi zimekuwa zikifanywa kila mara, lakini kama fidia ya ardhi inayohusu biashara, hasa ya viwanda na sisi tunataka uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati umilikiwe na Watanzania wenyewe, nafikiri tuanze kubadilisha mtazamo wetu. (Makofi)
Watanzania wamekuwa wakipewa fidia, si jambo baya, ni haki ya kisheria, lakini wakishapewa ile fidia, wanaelekea wapi. Tumeona watu wakipewa fidia Dar es Salaam, kule Kibada, Kigamboni watu wanalipwa fidia vizuri sana tu wanakwenda na sisi pale Mkuranga tutalipwa fidia, lakini baada ya hapo tunasogezwa, tunaondoka. Sasa tutasogea mpaka tutafika Rufiji, tukitoka Rufiji tutakwenda mahali pegine, ardhi ile tumepoteza na uchumi ule hatutaendelea kuumiliki. (Makofi)
Wazo langu nililokuwa nafikiri ni kwamba, ni lazima itafutwe mbinu nzuri zaidi ya kuwafanya Watanzania hawa wawe ni sehemu ya umiliki wa vile viwanda, wao mchango wao uwe ni ile ardhi yao. Tuliweke jambo hili vizuri badala ya kuja kuwapa fidia ya 1,500,000. Anaondoka Mtanzania yule wa pale Mkuranga, ameacha kiwanda kimetengenezwa pale, ile haitamsaidia. Kama ungetengenezwa mpango madhubuti na mzuri, maana yake ni kwamba eneo lake linakuwa ni mchango katika kiwanda kile atakula yeye, watoto wake, wajukuu wake na mpaka vitukuu vyake! Nadhani hii itakuwa ni namna bora zaidi ya kuwafanya Watanzania wamiliki uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo la viwanda, nimewahi kuzungumza kwamba pale sisi tunavyo viwanda vingi lakini viwanda hivi lipo tatizo la ajira, ajira zile zinazotolewa tunasema kwamba sio decent. Hazina staha! Vijana wetu wako wengi kweli wanapata vibarua mule ndani, ajira zile ndani ya saa kumi na mbili hawapumziki hata kidogo. Baada ya hapo analipwa 4,500, lakini ni ajira hatarishi kwelikweli. Naomba jambo hili wakati tunaendelea kuomba hivi viwanda tuliangalie vizuri ili tujiandae nalo lisije likatuletea matatizo hapo mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wa maji ambao umesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kwamba maji ni uhai na Mbunge mwenzangu wa Rufiji amesema vizuri sana hapa mchana huu wa leo juu ya suala la maji. Kutoka Rufiji, Mto Rufiji mpaka Mkuranga, hazizidi kilometa 100. Maji kule yamekuwa ni mengi mno yanaleta hata mafuriko! Tusaidieni tuondokane na tatizo la maji na liwe ni historia. Yatoeni maji kutoka Mto Rufiji, yafike Mkuranga, yapite Kibiti, Ikwiriri, Bungu na maeneo mengine ya Wilaya zetu hizi. Mkifanya hivi mtakuwa mmetusaidia sana. (Makofi)
Vilevile upo mkakati wa maji mkubwa pale katika Kijiji cha Kisemvule, ningeomba maji ya pale Mpera yasiondoke kwenda Dar es Salaam mpaka kwanza na sisi watu wa Mkuranga tuwe na faida nayo maji yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaendelea kuangalia namna ya kuboresha uchumi wetu, naomba nizungumzie miundombinu. Wilaya ya Mkuranga kama tulivyosema, Jimbo letu hili lipo kabisa kimkakati kwamba ni sehemu ya kupumulia katika Jiji la Dar es Salaam. Ombi langu hapa ni kuhakikisha kwamba pesa katika Mfuko wa Barabara ziongezeke. Ziongezeke ili tuweze kutengeneza miundombinu yetu. Sisi pale tuna uchumi mzuri, lakini uchumi ule umekwama kwa sababu miundombinu ya barabara katika Jimbo hilo ni mibaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenzangu wa Rufiji alisema kwamba Rufiji katika umri wake wote toka iwe Wilaya hata nusu kilometa ya lami hakuna, sisi hata robo kilometa ya lami haipo katika Wilaya yetu ya Mkuranga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja hii ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa nafasi hii niliyopata ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unaenda kuleta matumaini makubwa ya Tanzania yetu mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kwa haraka haraka kumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi kubwa na nzuri anayokwenda nayo na hasa hii ya kutumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi tunasema kwamba Mheshimiwa Rais aendelee kusonga mbele na sisi tupo pamoja naye maana katika nchi hii kama kuna watu ambao wametuangusha kwa kiasi kikubwa na kwa muda mrefu ni watumishi. Wametuangusha kwa muda mrefu na watu walikuwa wanahisi kwamba labda wao ni watu wasioguswa. Napenda kusema Mheshimiwa Rais anaendelea kuwapa hata Waheshimiwa Mawaziri wetu ujasiri wa kufanya kazi na sisi Wabunge na Watanzania kwa ujumla wake tunawaunga mkono. Lazima twende mbele zaidi ikiwezekana tuiangalie Sheria yetu ya Utumishi maana huko watu ndipo walipokuwa wanajifichia wakihisi kwamba hawana namna ya kuweza kuguswa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya, naomba sasa nielekee katika kuzungumzia Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unakwenda sambamba na uchumi wa viwanda ili kuelekea katika uchumi wa kati.
Mheshimiwa Spika, jana nimesikitika sana katika Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani rafiki yangu mwasilishaji kaka yangu Mheshimiwa David Silinde alikuwa anakatisha tamaa suala la viwanda na akafika mahali akazungumzia mpango ule wa Serikali wa kuanzisha industrial business hub pale Kurasini kwa kusema kwamba kwa kufanya vile ni kama tunakaribisha Wachina sisi tunajigeuza kwenda kuwa wachuuzi, nadhani hajaelewa vizuri jambo hili.
Mheshimiwa Spika, namwambia Waziri wa Fedha aharakishe sana ile Kurasini business hub ipatikane kwa haraka. Wachina kule kwao wanafunga vile viwanda wanakuja kufungua hapa Tanzania. Namkaribisha aanze kuona namna Wachina wanavyokimbilia hapa Tanzania kufungua viwanda pale Mkuranga, tuna viwanda vingi na vinajengwa kila siku ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa kiwanda kikubwa cha tiles kinajengwa pale Mkuranga katika Kijiji cha Mkiu. Kile kiwanda cha marumaru kitalisha East Africa nzima. Tutakapopata business hub pale Kurasini maana yake ni kwamba watu watakuwa wanajua one business stop center ipo pale Kurasini na watakwenda kupata bidhaa zinazozalishwa pale. Sisi leo pale tuna viwanda vya cement wenzangu wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa wanaomba viwanda vya cement. Tuna kiwanda cha cement cha RHINO, tuna kiwanda cha cement cha Diamond pale, tunatengeneza mpaka yeboyebo pale Mkuranga.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati njema sana bomba la gesi lipo pale na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda Mheshimiwa Mwijage kwa namna ambavyo ananipa support kubwa ya kuwaleta wawekezaji waje kuwekeza katika lile bomba la gesi ambalo lina toleo lake katika vijiji vyangu vya pale Mkuranga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niendelee kuunga mkono…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema Serikali iendelee na mpango huu wa viwanda na sisi tumejipanga vizuri sana. Katika eneo moja ambalo tumejipanga vizuri pale Mkuranga ni hilo la viwanda, tuna hekari zaidi ya elfu kumi ambazo zipo tayari kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nipongeze sana Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano ule wa kuboresha miundombinu yetu. Katika hili naomba nimwambie rafiki yangu Mheshimiwa Silinde na Kambi Rasmi ya Upinzani namna alivyopotoka tena amemtaja mpaka kipenzi chetu Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika ukurasa wa tisa eneo la barabara, eti Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuwakumbusha Watanzania kwamba aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wakati wa utekelezaji wa mpango uliopita ndiye Rais wa sasa, kwa hiyo hakuna matumaini. Nataka nimwambie matumaini ni makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza katika takwimu zake nataka nimwambie amekosea jambo moja kubwa. Waziri wa Fedha alipokuwa anasoma Mpango ule ametuelekeza kwamba mpango wa Serikali ulikuwa ni kujenga kilometa za lami 5,775 lakini mpaka tunafika Desemba 2014 zilikuwa zimeshajengwa zaidi ya kilometa 2,775. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa Waziri wa Fedha hakuweka mwaka wa 2015, kuanzia Desemba, 2014 mpaka 2015 na kufika hapa leo, Wizara ya Ujenzi katika muda huo ambao haukutajwa imejenga zaidi ya kilometa 500 za barabara za lami. Naomba nizitaje, Ndundu - Somanga kilometa 60, Tunduma - Sumbawanga kilometa zaidi ya 200, Lwanjilo - Chunya kilometa zaidi ya 36 na Iringa - Dodoma zaidi ya kilometa 259. Kwa namna ya kipekee kabisa naipongeza Serikali yangu namna tulivyojenga barabara za lami za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba niitaje barabara ya Ubungo Bus Terminal…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mpaka Mabibo na Kigogo zaidi ya Kilometa 6.4, barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege pale Jeti kwenda Vituka mpaka Devis Corner kilometa zaidi ya 10, barabara ya kutoka Ubungo Maziwa - External zaidi ya kilometa 2.25, barabara ya kutoka Kibamba - Mloganzila zaidi ya kilometa 4. Halafu watu hawa namna wasivyokuwa na shukrani tazama ukipita leo katika Jimbo la Ubungo unatoka Goba mpaka unakwenda kutokea Chuo Kikuu ni lami tupu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri wa Fedha katika Mpango huu aoanishe na Waziri wetu wa Ujenzi sasa twende katika kuijenga barabara ya kutoka Mkuranga - Kisiju ambapo eneo hilo linakwenda kuwa la viwanda. Hii ni katika kukamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuja kuwaomba kura Watanzania wale wa Mkuranga aliwaambia barabara ile itajengwa. Nina hakika kwa mwendo ambao tunakwenda nao barabara ile itajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nielekee katika maji…
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, nasikitika sana kusema kwamba muda wote huo ….
SPIKA: Mheshimiwa Ulega kuna taarifa ngoja uipokee.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Haya ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Silinde kifupi sana....
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, sijaipokea kwa sababu rafiki yangu Mheshimiwa Silinde nimemkumbusha kwamba ujenzi wa barabara uliendelea katika mwaka wa 2015, asisahau na madaraja ambalo na yeye atakwenda kupigia picha pale Kigamboni. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kwamba wenzetu hawa hata masuala ya maji hawakuyazungumzia. Tazama Serikali yetu ina mpango mzuri sana wa maji.
Mheshimiwa Spika, katika hili la maji, napenda niipongeze sana Serikali. Napenda niseme kwamba nina hakika katika miaka mitano hii ile ajenda yetu ya kumshusha mama ndoo kichwani itafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo unaelekeza kwamba katika miaka mitano iliyopita takribani asilimia zaidi ya 60 ya Watanzania walipata maji safi na salama. Katika Jiji la Dar es Salaam, watu wanabeza tazama Jiji la Dar es Salaam lilivyopata bahati kubwa sana tena kwa pesa zetu wenyewe za ndani. Maji ya kutoka Ruvu Chini yamepita Bagamoyo yamekwenda mpaka Chuo Kikuu kule cha Dar es Salaam, bomba lile limelazwa kwa pesa ya Serikali yetu. Kwa kweli napenda sana niipongeze Serikali. Pia kuna mpango wa maji wa Dar es Salaam wa Ruvu Juu ambao sasa hivi unaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale Mkuranga upo mradi mkubwa wa maji ambao utahudumia Dar es Salaam kwa maana ya maeneo ya Kigamboni, Mbagala na Kisarawe, mradi ule wa Kimbiji na Mpera. Naiomba Serikali sasa ihakikishe kwamba mradi ule unawanufaisha na watu wa Mkuranga katika vijiji vya Mkuranga, Dundani, Mwanambaya, Mwandege, Kipala Mpakani vyote viweze kupata maji yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali katika Mpango huu wa Miaka Mitano ihakikishe kwamba inatoa maji kutoka katika Mto Rufiji kwani zaidi ya asilimia 50 ya maji ya Mto Rufiji hayana matumizi yoyote. Kilometa hata 200 hazifiki kutoka Mto Rufiji kuja Dar es Salaam. Tuyatoe maji yale tuyalete Dar es Salaam, maji haya ya visima hayana hakika hata Naibu Waziri wa Maji jana alieleza hapa, Engineer Kamwelwe yeye mwenyewe amesema kwamba maji haya ya visima hayana hakika.
Mheshimiwa Spika, tutakapotoa maji kutoka Mto Rufiji yatanufaisha Wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga na yatanufaisha Dar es Salaam yote ya Kusini bila kuisahau Kisarawe. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweke mpango huu madhubuti wa kuhakikisha tunatatua kabisa kero ya maji katika Wilaya zetu na nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba nizungumzie suala la kilimo. Katika Mpango wa Maendeleo imeelezwa kwamba kutoka 2010 kurudi nyuma ilikuwa ni karibu asilimia mbili na point lakini kutoka 2010 kuja 2015 zilizidi kidogo asilimia ikaja mpaka asilimia 3.4 bado ukuaji huu ni mdogo. Pamoja na ukuaji huu kuwa mdogo bado nchi yetu imekuwa na chakula cha kutosha na mpaka tukawa na chakula cha ziada.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tuna tatizo kubwa la mabadiliko ya hali ya hewa, naiomba sana Serikali katika mpango wake wa bajeti hii tunayokwenda nao sasa ihakikishe kwamba mambo makubwa mawili, matatu yafanyike.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni kuipa nguvu zaidi Wizara yetu ya Kilimo ili tuweze kujielekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji. Hata pale kwangu Mkuranga ipo miradi ya umwagiliaji ya Changanyikeni, Yavayava na Kisere. Miradi ile yote haiendi vyema ni kutokana na ukosefu wa fedha. Ninayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka huu tunaokwenda nao tutapata pesa ya kutosha na hatimaye miradi ile inaenda kutekelezwa na kukamilika na kuwanufaisha wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, ili kuhakikisha kilimo chetu kinaenda vizuri ni pembejeo. Ni lazima tuipe pesa ya kutosha pembejeo ili kilimo chetu kiwe na tija. Kwangu naomba sana pembejeo ya sulfur. Pembejeo hii ya sulfur nashauri iuzwe kama inavyouzwa cocacola dukani. Sisi wakulima wa korosho tukikuta sulfur inauzwa kwa wingi madukani tutaridhika sana. Nataka nikuhakikishie wakulima wote wa korosho baada ya hapo tutakipa chama chetu Chama cha Mapinduzi kura zote za ndiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna matumaini mkubwa sana, tazama mfumo wetu wa stakabadhi ghalani, Waziri Mkuu juzi amekwenda kule Mtwara na Lindi ameboresha mfumo huu. Tunayo matumaini kwa kasi tunayokwenda nayo kero zote zinazotusumbua katika mfumo wa stakabadhi ghalani zitatatuliwa. Mwaka huu korosho imeuzwa zaidi ya Sh.2,500 kwa kilo katika Wilaya yangu ya Mkuranga. Watu wamepata pesa nyingi na mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja ya Mpango huu wa Maendeleo. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nikushukuru kwa nafasi hii niliyoipata ya kuchangia bajeti ya Wizara yetu hii ya Maliasili na Utalii. Pia naomba niendelee kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe na kaka yangu Naibu Waziri, Mheshimiwa Mhandisi Ramo Makani. Nataka tu niwaambie kwamba wafanye kazi na wala wasitishike na haya manenomaneno mengine ya kuwavunja moyo na sisi tunaelewa juu ya weledi na uwezo wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine hata mimi naanza kushawishika kuunga mkono wale wanaofikiria kwamba kabla hatujaingia kwenye jengo hili tuwe tunapimwa pale kama tumevuta hata marijuana hivi. Katika hali ya kawaida, kijana hata kama umepigiwa kura na kuaminiwa na wananchi ukaenda kumtukana mzee wa namna ile na kumuita majina ya hovyo, lazima utakuwa una tatizo kidogo katika akili yako, siyo wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imedhihiri hata jana, yupo mwenzetu mmoja hapa wa kutoka katika chama ninachotoka mimi amezungumza mambo ya ajabu sana hapa. Unaweza ukaona ni kwa namna gani watu hawaelewi ni nani katika nyumba hii ameingia bila ya chama kilichomleta hapa. Wote kwa umoja wetu, iwe wa upinzani, iwe wa chama kinachotawala, sisi tumezaliwa na vyama vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima sisi kama viongozi tujue wajibu wetu na hii michezo haitaki hasira. Wala usidhani kwamba wewe ukiwa na hasira sana ndiyo hoja yako itafanikiwa, la hasha! Wakati mwingine unajielekeza tu katika kukata udugu. Nataka nikuhakikishie sisi kule kwetu tunasema mkataa udugu kala hasara huyo! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme juu ya misitu na Mheshimiwa mama Mariam Kisangi amesema vizuri hapa juu ya msitu, mkaa na vitu vya namna hiyo. Nafahamu kwamba mkaa, kwanza naomba ni-declare interest, mimi ni mwana mazingira na profession yangu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni Shahada ya Sayansi ya Mazingira. Nina weledi mzuri na mkubwa sana juu ya masuala ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam nyumbani kwetu na Mkuranga yake watu wanaendelea kutumia nishati ya mkaa na Serikali tunajua kwamba inapiga vita matumizi ya mkaa. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba nguvu tunayoitumia katika kupiga vita matumizi ya nishati hii ya mkaa, tutumie nguvu hiyohiyo katika kuhakikisha tunawatafutia nishati mbadala wananchi hawa. Watu wanapata shida sana, watu hawaelewi wafanyaje, tunawaambia watumie gesi, hata elimu yenyewe ya matumizi ya gesi inafahamika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya gesi hayakuanza leo, watu walio wengi, hata wasomi wenyewe wanaogopa kutumia majiko ya gesi maana yameua watu wengi sana katika nchi hii. Wewe mwenyewe unafahamu mwaka mmoja, mwishoni mwa miaka ya tisini, hoteli ya Kibodi ya Dar es Salaam katikati ya mji iliungua moto kwa sababu ya jiko la gesi. Sasa tufanye jitihada ya kutoa elimu, kabla ya kusema kwamba watu hawa wasitumie mkaa, tumefanya jitihada gani ya kuwaelimisha, tumefanya jitihada gani ya kupeleka nishati mbadala? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti imezungumzwa hapa kodi ya vitanda nami naunga mkono hoja ya kodi hii ya vitanda ni lazima itazamwe, lasivyo yanaendelea kuwa ni yale yale ya kutokuwasidia watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa Msitu wa Mwandege pale Mkuranga, kile kimekuwa ni kichaka cha majangili. Mkuranga yenyewe imetajwa kama ni eneo ambalo si salama sana. Wewe mwenyewe unafahamu kwamba walikamatwa pale watu zaidi ya 50 na bunduki, wamezificha. Haukupita muda mrefu Benki yetu ya NMB pale Mkuranga ikavamiwa na majambazi. Hatujakaa muda mrefu Benki ya Access pale Mbagala Rangitatu ikavamiwa na majambazi. Hawa wote wanakimbilia kwenye msitu huo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumwambia Mheshimiwa Waziri, kama tunashindwa kwa kuwa hatuna pesa za kutosha za kuutunza msitu ule Dar es Salaam imejaa, ni kweli. Eneo lile ni kubwa sana linachukua vijiji zaidi ya vinne Mwandege yenyewe, vikindu, Mlamleni Luzando na kwingineko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitenge eneo lile dogo tupate eneo la kutosha pale tujenge kituo cha kisasa, watu wanaotoka Mikoa ya Kusini hawana haja ya kwenda na mabasi yao mpaka Ubungo mpaka Dar es Salaam. Waishie pale Mkuranga waingie kwenye shuttles waende Dar es Salaam hii itatusaidia tutapata pesa tutafanya msitu ule kuwa ni botanical garden. Badala ya kuuweka tu vile kuwa ni kichaka cha majangiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niseme juu ya ng‟ombe na hasa hao wanaoingia katika maeneo ya hifadhi. Juu ya wakulima na juu ya ng‟ombe imeshazungumzwa sana. Naomba niseme wazi hapo kwetu sisi ng‟ombe ni kitu kipya, hapa nasema jambo jipya kabisa. Kwanza zamani tulikuwa tunamwita mdudu, leo tumeletewa ng‟ombe wengi sana na ugomvi ni mwingi sana pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama inavyosemwa na wenzangu ni lazima tutafute suluhisho la kudumu la jambo hili, wakulima wetu hawamjui ng‟ombe na wala hawana haja ya kumjua. Eee!
Mheshimiwa Mwenyekiti, issue ya misitu tena katika mazingira naomba nimwambie jambo moja Mheshimiwa Waziri kwamba hili jambo liwe ni two way traffic. Mpaka hivi sasa sisi tunatumia nguvu nyingi sana juu ya kulinda hifadhi zetu lakini bado hatujajifunza. Nilipokuwa Mkuu wa Wilaya kule Kilwa ninao mfano mzuri sana wa Kijiji cha Nanjilinji, tulikuwa na jambo kule la hifadhi ya misitu ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Nanjilinji kimefanikiwa sana katika uhifadhi wa jamii wa misitu yake. Leo mtu akikuona umeshika fito hawezi kukuelewa, lazima atakuchukulia hatua yeye mwenyewe pasipo kwenda na askari wa games wala jambo la namna gani. Kwa hivyo, hebu tuiangalie sera yetu vizuri hapa, namna ambavyo tunaweza tukawashirikisha jamii tukawasaidia ili wao wenyewe wawe walinzi wa rasilimali hizi badala ya kutumia maguvu mengi sana ambayo wakati mwingine wala hayana tija na yanatupotezea pesa zetu nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji nawahakikishia watani zangu Wasukuma na wengineo watoe mifugo ile; kule South Africa, Limpopo kwenye hifadhi ile maarufu kabisa ya Great Kruger pametokea tatizo. Ng‟ombe wote wamepata matatizo ya magonjwa ya miguu na midomo na ule ugonjwa sasa umeshaanza kutokea kwa wanadamu na umeshaingia mpaka Zimbabwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya jitiada hao ng‟ombe watakufa na watu nao watakufa na mazingira yetu yataharibika. Kwa hivyo, ni lazima watu kukubaliana na jambo hili, ni kinyume cha utaratibu kabisa kufanya jambo la namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize na utalii. Nafasi ya Tanzania katika utalii ni nzuri, tunahitaji kufanya jitihada zaidi ili kuhakikisha kwamba utalii wetu uweze kuwa na faida hasa ya kuondoa umaskini. Juzi hapa China tarehe 21 umemalizika Mkutano wa World Tourism Organization, ulifanyikia Beijing pale, moja ya jambo kubwa kabisa lililokubaliwa katika mkutano ule ni kuhakikisha kwamba utalii uondoe…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Awali ya yote napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa nilipo leo nikiwa na afya njema. Nianze mchango wangu kwa kutamka kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, naomba kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Napenda kutumia nafasi hii kumuahidi Mheshimiwa Rais kwamba nitafanya kazi yangu kwa uadilifu na uaminifu mkubwa sana ili kuhakikisha kwamba Tanzania sekta hizi za mifugo na uvuvi zinachangia kikamilifu katika kuinua pato la mfugaji na mvuvi na kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kipato cha kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda nichukue fursa hii nimshukuru tena Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa uongozi wao mahiri na makini kabisa ambao unaipeleka nchi yetu katika uelekeo wake ule ule wa amani, utulivu na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kumshukuru Waziri wangu Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa kwa kunishirikisha kwa karibu sana katika majukumu ya kuongoza Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru sana wewe mwenyewe, Naibu Spika, Wenyeviti wote wa Bunge, Wabunge wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano wao kwa ujumla wanaonipa katika utendaji wangu wa kazi za ndani na nje ya Bunge letu tukufu. Nawaahidi ushirikiano na nasema ahsanteni sana kwa ushirikiano mnaonipa kila mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia vilevile nichukue fursa hii niwashukuru watendaji wetu katika Wizara, Katibu Mkuu Dkt. Mary Mashingo anayeshughulika na mifugo, vilevile Katibu Mkuu Dkt. Yohana Budeba anayeshughulika na uvuvi na Wakuu wa Idara zote na taasisi zote zilizoko katika wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu katika Jimbo la Mkuranga na nataka niwahakikishie kwamba mimi kijana wao niko makini na timamu kabisa kuendelea kuitumikia kazi hii ya Ubunge wa Jimbo la Mkuranga bila ya kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, naomba uniruhusu pia nimshukuru mke wangu na familia yangu kwa namna ambavyo wamekuwa wakinipa ushirikiano wa hali na mali wakati wote wa kutumikia kazi hizi za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, naomba sasa uniruhusu niweze kujibu hoja ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia mjadala wa bajeti yetu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote, sisi katika Wizara tumeyachukua mawazo, maoni na maelekezo yao mbalimbali waliyotupatia. Nataka niwahakikishie kwamba vitu vyote hivi walivyotushauri tutavifanyia kazi ili kuweza kupata uendelevu wa sekta zetu hizi za mifugo na uvuvi kwa manufaa mapana sana ya nchi yetu ya Tanzania. Mimi nitazungumza kwa uchache lakini baadae Mheshimiwa Waziri wangu atakuja kueleza kwa upana zaidi ili kuweza kujibu hoja zote bila mashaka yoyote yale.

Mheshimiwa Spika, la kwanza ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni namna ambavyo sisi kama Serikali tulivyojipanga kuhusiana na sekta hii inayochipukia ya ufugaji wa samaki. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge sisi tunaelewa namna ambavyo Wabunge wengi wamekuwa wakivutiwa na suala hili la ufugaji wa samaki kwa maana ya aquaculture. Mpango mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba Watanzania walio wengi wanaingia katika ufugaji wa samaki kwa sababu ufugaji wa samaki umekuwa ni wenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Spika, namna gani Wizara tumejipanga? Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sheria na kanuni zetu wakati fulani unaweza ukaziona kwamba, mathalani samaki ambao wanafugwa katika mabwawa yetu hawaruhusiwi kuchakatwa na hata kuuzwa nje. Hivi ni vitu ambavyo vimesababisha wakati mwingine sekta zetu zisisonge mbele kwa sababu zinakuwa si sekta shindani, watu hawavutiki kwenda kuwekeza pesa zao katika aquaculture.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie baada ya mazungumzo ya muda mrefu chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Waziri Luhaga Joelson Mpina, tumekubaliana kufanya mapinduzi katika eneo hili la aquaculture. Moja, hatuoni sababu ya kwa nini samaki wanaozalishwa katika mabwawa yetu wasiuzwe kibiashara. Kwa hiyo, nataka niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tunakwenda kulifanyia marekebisho. Tuchakate samaki wetu wanaotoka katika mabwawa (ponds) lakini turuhusu pia vilevile hata wauzwe ili tuweze kuvutia uwekezaji zaidi kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi tumeona juu ya kodi na tozo mbalimbali ambazo zinafanya sekta hii isiweze kuvutia hasa katika eneo la uingizaji wa vifaa mbalimbali. Tumekuwa tukiendelea na mashauriano na wenzetu wa Wizara ya Fedha, tunaamini kwamba watalifanyia consideration ambayo itakwenda kuwasaidia Watanzania wavutike katika kuwekeza kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumejiwekeza zaidi katika kwenda kuviimarisha vituo vyetu, tunavyo vituo nchi nzima vinavyofanya kazi hii ya aquaculture. Vituo vyote hivi tumejielekeza katika kwenda kuviimarisha ili kuzalisha vifaranga vya kutosha, tuvigawe kwa wananchi lakini vilevile kuhakikisha tunapata chakula bora kwa ajili ya ufugaji wa samaki. Maana tatizo kubwa lililopo katika eneo hili ni upatikanaji wa chakula kizuri na upatikanaji wa vifaranga. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba vyote hivi tunaenda kuvitatua.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa na Wabunge wengi ni eneo la nyavu, je, hizi nyavu mbona zimekuwa na mjadala mkubwa sana, ni nini tatizo? Pia vilevile imezungumzwa ya kwamba sisi tumetoa monopoly ya kiwanda kimoja tu katika nchi ambacho ndiyo kinaingiza nyavu kwa wavuvi, lakini Waheshimiwa Wabunge wakafika hatua ya kusema tumezuia uingizaji wa nyavu.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako tukufu hili, Wizara yetu haijazuia hata kidogo uingizaji wa nyavu nchini isipokuwa lazima tukubaliane kazi tuliyoifanya ya kuondoa zile nyavu ambazo zinasemwa na sheria kwamba ni nyavu haramu ni kubwa mno. Ukitazama anayeathirika ni yule mvuvi wa chini kule, tulipokwenda kuzichoma na kuziteketeza kwa mujibu wa sheria, waathirika wakubwa ni wale wavuvi wetu wa kule chini. Mara zote Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiuliza kwa nini Serikali inajielekeza zaidi kwenda kushughulika na wavuvi wale wa kule chini hawashughuliki na wazalishaji na wasambazaji.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maoni hayo ya Waheshimiwa Wabunge ndiyo maana sisi hatukukubali kwanza moja kwa moja kufungua mipaka yetu kuziingiza nyavu zile. Tulisema ni lazima turatibu zoezi hili ili tusiende kurudia makosa yale yale kila siku ya kwenda kumchomea mvuvi wetu, mvuvi mnyonge kwa sababu sisi tunaamini sekta hii ya mifugo na uvuvi haiwezi kuwepo bila ya kuwepo kwa hawa wavuvi wetu. Kwa hiyo, nataka niwahakikishieni baada ya kukubaliana na kufanya tathmini hii tutakuwa tuko tayari hata kufungua.

Mheshimiwa Spika, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba nyavu hizi nyingi zinazalishwa katika nchi jirani mojawapo ambayo haina hata ziwa lenyewe. Sisi hapa hiki kiwanda kinachosemwa cha hapo Arusha tumekipa kweli leseni baada ya kutuomba. Mimi mwenyewe kama Naibu Waziri nimekipitia kiwanda hiki, kina marobota ya nyavu za kuvulia dagaa mengi sana hayana mnunuzi. Tumeelewa concern ya Wabunge ya kwamba inawezekana wale mabwana nyavu zao hazina ubora. Tumekubaliana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wanaohusika na masuala ya ubora tuweze kwenda kuhakikisha kwamba nyavu zile zinakwenda kuzalishwa zenye ubora zaidi.

Waheshimiwa Wabunge tunaomba mtuamini ya kwamba jambo hili tunalizingatia ili kusudi sekta yetu ya uvuvi na wavuvi wetu wasiweze kuweza kwenda kuharibikiwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna contradictions za sheria ambazo zimejadiliwa hapa na baadhi ya wavuvi wenzangu kwamba sasa inakuwaje juu ya hizi nyavu za dagaa lakini wakati huo huo zinakwenda na zinakamatwa tena. Unafahamu wavuvi nao vilevile ni binadamu na ni wajanja, kule Kanda ya Ziwa kuna uvuvi maarufu unaitwa gizagiza. Zilezile nyavu za dagaa kwa mujibu wa sheria na utaratibu wetu zile huenda kuvua kwa kutumia karabai, lakini watu wamezigeuza, hawatumii tena karabai wamefungia zile karabai zao, usiku wanakwenda kuvua bila ya zile karabai. Wanapokwenda kuvua bila ya zile karabai ndiyo wanaita gizagiza.

Sasa wakati ule wanapokuwa hawatumii karabai wanampata sangara mchanga, wanapata sato na mazao mengine ya uvuvi, ukitumia karabai haupati matatizo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya ufinyu wa muda, naomba niende katika upigaji chapa. Waheshimiwa Wabunge wengi sana wameeleza juu ya upigaji chapa na tena babu yangu Mzee Ndassa pale ameenda na kuniambia mimi kwamba tena wewe Ulega mwenyewe hata hii shughuli ya ufugaji hujawahi kuifanya.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishieni Waheshimiwa Wabunge mawazo na ushauri wenu wote mlioutoa katika kulinda sekta ya ngozi kwenye eneo hili la upigaji chapa tumeyachukua na sasa timu yetu inafanya tathmini. Kwa sababu hili eneo ni endelevu kwa maana ya kwamba upigaji chapa si kitu cha kusema kwamba kinaisha leo au kesho, ni kitu ambacho kipo kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kile ambacho ninyi mmekiomba ni kuhakikisha kwamba tunaboresha, tumeyachukua yale mawazo kwamba tusichome tena ng’ombe badala yake tuwavalishe hereni ama tutafute mbinu nyingine zozote ambazo zitakwenda kuifanya ngozi yetu na mifugo yetu iendelee kuwa na thamani. Mimi nataka niwahakikishieni kwamba jambo mlilotushauri ni jema na tumelichukua na tunakwenda kulifanyia kazi mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa pia vilevile hoja na jirani yangu Mheshimiwa Dau iliyohusu MPRU kwa maana ya hifadhi ya bahari. Nataka nimhakikishie kwamba kama nilivyokuwa nikijibu kila mara kwamba hifadhi ya bahari ipo kwa mujibu wa sheria lakini yeye concern yake ni juu ya mapato na amezungumzia kwamba kwa nini tusichukue MPRU kwa maana ya Hifadhi wachukue asilimia 50 na Halmashauri wachukue asilimia 50. Kwa sasa hivi asilimia 30 zinakwenda katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa maana ya 10 zinakwenda katika Halmashauri yenyewe na 20 inakwenda katika vijiji ambavyo vimezungukwa na ile hifadhi ya bahari. Ushauri wake wote aliotupatia wa kwamba tunataka twende katika usawa tunauchukua. Haya ni mambo ambayo tuna uwezo wa kuyazungumza, tukakaa kwa pamoja, tukashauriana na kuona ni namna gani bora zaidi ya kuweza kuwasaidia watu wetu.

Mheshimiwa Spika, mwisho nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wengi waliozungumzia ufugaji wa kuku kwamba Wizara yetu inao mradi mkubwa sana wa kuhamasisha ufugaji wa kuku. Kwa hivi sasa tumeshazifikia halmashauri 20 katika nchi nzima. Tunagawa bure kabisa mbegu ambazo ni za Kitanzania zenye kuhimili matatizo na ugonjwa kama vile ugonjwa wa mdondo na mengineo.

Kwa kusema ukweli tutahakikisha kwamba tunafikia Halmasharuri zote nchini. Mradi huu umefadhiliwa na wenzetu wa Bill & Melinda Gates ambapo tunahakikisha mpaka kufika mwaka 2019, Halmashauri zetu nyingi ziwe zimepata mradi huu wa ufugaji wa kuku. Nia na madhumuni yetu ni kuhakikisha tunainua kipato cha wafugaji wetu lakini pia tuwe na uhakika wa chakula vilevile.

Mheshimiwa Spika, yapo magonjwa ya mifugo vilevile yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Nataka niwahakikishie kwamba sisi katika Wizara tumeweka mkakati madhubuti kabisa wa kupambana na magonjwa ya mifugo. Tumeweka magonjwa ya kipaumbele, yapo magonjwa kama kumi ambayo tumeona kwamba haya tuyafanye kuwa magonjwa ya kipaumbele katika ng’ombe kwa mfano ugonjwa wa kuangusha mimba na magonjwa ya miguu na midomo na katika kuku magonjwa kama vile ya mdondo, yote tumeyapa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi maabara yetu ya pale Temeke Veterinary tuna chanjo takribani nne. Tunaamini kabla ya mwaka huu haujaisha tutakuwa tumeipata chanjo ya ugonjwa unaowasumbua ng’ombe wetu wengi sana, chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu. Mpaka mwisho wa mwaka huu tunahakikisha kwamba tumeipata chanjo ile. Baada ya hapo ni lazima niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba kama tunataka kweli kabisa sekta yetu ya mifugo isonge mbele ni lazima upigaji wa chanjo yaani uchanjaji wa mifugo yetu uwe wa lazima ili kuweza kuifanya sekta hii iweze kukua vizuri na hatimaye tuweze kushindana katika masoko ya kimataifa, tuuze nyama yetu na watu waikubali nyama yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Waheshimiwa Wabunge tutakapofika katika hatua za namna hii nanyi muendelee kutuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, naomba tena nichukue fursa hii kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia moa moja kabisa. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge yale yote ambayo leo mmetuambia katika Bunge hili na kututaka tuweze kurekebisha ili hali iweze kuwa nzuri zaidi katika sekta zetu hizi za mifugo na uvuvi, tumeyachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi. Ninaamini kwamba baada ya muda mfupi mtakuja hapa kutushangilia kwa namna ambavyo tumefanya vyema katika kazi mliyotutuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, naipongeze sana Serikali kwa jitihada zake za uchumi wa viwanda kwenye nchi yetu. Pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri na kwa namna ya pekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hoja moja kwa moja. Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze ni namna gani iliyo rahisi kabisa viwanda vinaweza kupata malighafi ya gesi kwa ajili ya uzalishaji wa umeme? Mfano, Kiwanda tarajiwa cha marumaru (tiles) cha Goodwill Ceramic Tiles kinahitaji gesi na wawekezaji hawa wapo tayari kabisa kujenga bomba kwa gharama yao wao wenyewe (Mkopo kwa TPDC): Je, Wizara itasaidiaje kuharakisha jambo la namna hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji hawa pia wa Goodwill Ceramic pia wameomba bei ya gesi iweze kuwa stable (imara). Naiomba Wizara ya Viwanda isaidie pia katika kuhakikisha inashirikiana na Wizara ya Nishati na Madini kuharakisha jambo hili pia. Mwisho, naipongeza tena Serikali kwa jitihada hizi na kusisitiza kuwa jitihada hizi ziendelee kwa manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yoyote na mimi nianze kwa kuipongeza Serikali na kuunga mkono hoja hii. Lakini kutokana na ufinyu wa muda naomba nizungumze mambo makubwa matatu halafu nitajielekeza katika ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yenyewe ni kama ifuatavyo, na ningeomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wayachukue mambo haya
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kariakoo ni sehemu yetu ya biashara tunayoweza kuiita ni sehemu ya biashara ya kimataifa. Hivi sasa Kariakoo inahudumia zaidi ya nchi tano za Kiafika ikiwa na sisi wenyewe wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tulikuwa na tatizo bandarini, lakini hapa karibuni kwa takribani wiki mbili, tatu, mwezi tatizo la upatikanaji wa mizigo kwa ajili ya soko letu hili la Kariakoo, kwa maana eneo la Kariakoo limejitokeza kutokana na agizo lile la kwako Mheshimiwa Waziri la TBS. Nomba nikueleze kuwa jambo hili siyo baya, lakini nataka hili jambo la TBS uweze kuliweka vizuri na elimu kwa wafanyabiashara wale iende sawasawa.
Mheshimiwa Waziri, wafanyabiashara wa Kariakoo wengine ni wafanyabiashara wadogo wadogo ambao ni wanakusanya mitaji yao wanaunganisha katika kontena moja. Mmoja tu anapokosa kukutana na SGS, wakala wetu shida kubwa inatokea pale bandarini. Nataka nikuambia storage ya wafanyabiashara wale wa Kariakoo hivi sasa imekuwa kubwa sana na mitaji yao inakatika.
Nakuomba sana jambo hili uliingilie uone ni namna gani ya kuweza kuwasaidia ili waweze kuendesha maisha yao na hatimaye biashara iendelee kuweza ku-propel katika eneo hili la biashara la Kariakoo.
Mheshimiwa mwenyekiti, naomba nizungumzie BRT, nimeiona katika Mpango wa Maendeleo wa Mwaka huu wa 2017/2018. Naomba nisisitize ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Mkuranga, alisema kwamba BRT itakwenda mpaka Mkuranga, itavuka pale maeneo ya Mbagala. Naomba iende kwa sababu tunalo eneo zuri la Serikali, linaweza kutusaidia kwa kazi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana yuko msemaji mmoja hapa alisema hakuna viwanda vipya. Nikuombe Mheshimiwa Waziri uwachukue baadhi ya Wabunge walete kule Mkuranga wakione kiwanda cha Good Will Ceramics kipya ambacho zaidi ya shilingi bilioni 200 zimewekwa pale na tunategemea zaidi ya wafanyakazi 4,500; watu wa Mtwara, Lindi wanajua kiwanda kile cha kilometa moja kinachojengwa pale Mkuranga, naomba jitihada hizo zifanyike zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba pia ulitangaze eneo la Mkiu kuwa ni eneo rasmi la viwanda. Tunazo ekari nyingi pale hazihitaji compensation, walete. Na naomba uwabadilishe mindset Waheshimiwa Wabunge hawa, mambo ya kuwaza kiwanda kikubwa sana kama kile cha Mkiu Mkuranga waachane nayo. Viwanda vidogo vidogo vya dola 5,000, 10,000, ardhi tunayo pale, waje wawekeze katika kubangua korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie na maneno yafuatayo ya ahadi ya Mheshimiwa Rais. Wakati Mheshimiwa Rais anachukua nchi hii mwezi Novemba, 2015 aliahidi kupambana na rushwa, aliahidi kufanya kazi kubwa ya kuzuia matumizi yasiyokuwa mazuri ya pesa za umma pamoja na kushughulika na watu wasiokwepa kodi. Mheshimiwa Rais alipokuja Mkuranga alieleza wazi hana tatizo na wafanyabiashara akitumia uwanja ule wa Bakhresa. Watu leo humu ndani wanazungumza kwamba Serikali hii haina urafiki na wafanyabiashara.
Mheshimiwa Rais aliwaeleza wazi mfanyabiashara anayelipa kodi huyo atakuwa ni rafiki yake, lakini mfanyabiashara asiyelipa kodi hana urafiki naye. Nataka niwaambieni IMF wametoa ripoti Jumatatu, timu ile inaongozwa na mtaalam mmoja anayeitwa Mauricio Villafuerte. Huyu bwana ameeleza wazi, ameeleza namna nzuri ambayo tunakwenda nayo, lakini wametushauri pia juu ya kujaribu kurahisisha kidogo juu ya mzunguko wetu wa fedha na mengineyo, lakini wametupongeza na wamefikia hatua nzuri ya kuwaambia Watanzania kwamba hata madeni ya nje na mengineyo sasa tuko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka nimalizie na maneno ya Mwenyezi Mungu katika kitabu kitakatifu cha Qurani. Mwenyezi Mungu subhana wa ta’ala anasema katika Qurani tukufu kama ifuatavyo; “Na wale wanaojitahidi kwa ajili yetu tutawaongoza njia zetu. Nasema fanyeni kazi basi ataona Mwenyezi Mungu vitendo vyenu na Mtume wake na waumini wataviona vitendo vyenu. Enyi wanangu wala msikate tamaa na rehema za Mwenyezi Mungu, hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu waliokosa imani.”
Mheshimiwa Mwenyekiti wale watu waliokosa imani wote wamepotea. Leo mkubwa mmoja amekuja humu ndani anahangaika, anaweweseka, nazungumzia shilingi milioni 10, kama anazitaka zile shilingi milioni 10 aje timu kubwa huku CCM asikate tamaa wamebanwa.
heshimiwa Mwenyekiti, nashukura sana naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye mjadala huu unaoendelea wa hali ya uchumi lakini pia na bajeti yetu kuu ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu subhanahu wataala, kwa kunijalia siku hii ya leo kuwa ni siku ya kipekee kwangu mimi Abdallah Hamisi Ulega na familia yangu ikiwa ni pamoja na mke wangu kipenzi Bi. Mariam Abdallah kwa kutujalia kupata mtoto, tena mtoto wa kike. Kwa kweli, nazidi kuthibitisha kwamba akinamama ni wastahamilivu, wavumilivu, ni watu wenye uwezo mkubwa sana kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mke wangu huyu mwaka wa jana alipoteza mtoto wa umri wa miezi tisa. Mwaka juzi pia alipoteza mtoto wa umri wa miezi tisa. Hakukata tamaa, hatimaye mwaka huu wakati wake umefika na mambo yamependeza. Huyu mtoto katika moja ya jina zuri nitakalompa nitampa jina la Tulia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni katika ile kuthibitisha kwamba ninyi akinamama mnaweza. Wallah nataka nikuhakikishie kwa mikasa hii aliyoipitia mke wangu kipenzi, ningekuwa mimi ningekata tamaa, lakini yeye hakukata tamaa kama vile ambavyo wewe hukati tamaa na hawa manyang‟au wanaotaka kutusumbuasumbua humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naendelea kumpa pongezi sana mke wangu kipenzi kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwa ajili yangu na kwa ajili ya nchi hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika kuchangia bajeti. Kwanza kabisa hali ya uchumi na nashukuru sana baadhi ya wasemaji wamesema juu ya hali ya uchumi na mimi nitasema kwa muhtasari sana. Ombi langu kubwa kwa Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha atakapokuja kufanya winding up hapa atueleze, maana sitaki kusema kwamba sisi watu wa Mkoa wa Pwani tumewekwa katika bahati mbaya ya kuwa matajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa tajiri ni jambo jema sana lakini nataka atuambie ni criteria gani alizotumia za kutufanya sisi kuwa ni miongoni mwa mikoa matajiri. Maana nilikuwa napitia kwamba ni vigezo gani vinaweza vikamfanya mtu akaambiwa wao ni matajiri, per capita income au huduma za kijamii? Sisi kule kwetu huduma za kijamii hali ni mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mmoja katika wasemaji waliowahi kusema siku ya jana nilipokuwa nikifanya mijadala yangu, anasema kwa kuwa ninyi mpo karibu na Dar es Salaam, hospitali za rufaa ziko karibu, nikamwambia hospitali ya rufaa si ya watu wa Mkoa wa Pwani, Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ni ya watu wa Taifa zima la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni nini hasa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwingine akaniambia ninyi mna lami inapita kila mahali katika mkoa wenu. Nikamwambia si kweli, sisi kutoka Nyamwage - Utete tuna shida kubwa, kutoka Mkuranga Mjini - Kisiju tuna shida kubwa, kutoka Bungu - Nyamisati kuna shida kubwa, kutoka Mlandizi - Makofia Bagamoyo kuna shida kubwa, kutoka Mlandizi - Mwaneromango - Mzenga – Vikumbulu - Mloka pana shida kubwa, sasa kwa nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna haja ya kuwa na wasiwasi isipokuwa tunataka tujue ugunduzi gani uliofanyika katika Mkoa wa Pwani ukawafanya watu wa Mkoa wa Pwani leo wakawa na maisha makubwa ya kuwashinda wengine katika Taifa letu? Maana sisi tuna korosho na korosho yenyewe watu wa Mtwara wanatuzidi kwa mbali, watu wa Lindi wanatuzidi kwa mbali, ni nini hasa, ni vigezo gani, atuambie waziwazi ili na sisi tuongeze jitihada zetu. Pale ambapo atapataja kwamba ninyi watu wa Mkoa wa Pwani mahali hapa mko vizuri, basi inshallah sisi tuongeze nguvu zetu na tufanye vizuri zaidi ili tuweze kuwa na maisha bora ambayo Taifa letu linataka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naomba sasa niende kwenye maji. Kama walivyosema wenzangu, naomba sana Mfuko wetu wa Maji uendelee kuongezewa nguvu. Tazama mimi katika Jimbo langu la Mkuranga uko mradi wa muda mrefu wa pale Mpera na Kimbiji, unahitaji shilingi bilioni 12 tu. Tutazipataje pesa hizi bila ya kuongeza nguvu katika Mfuko wetu wa Maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, nina shida kubwa ya maji katika Mji wa Mkuranga, hatuwezi kupata pesa ya kuweza kuusababisha mradi ule wa Mkuranga unaohitaji takriban shilingi bilioni 2.2 uanze. Tunasema tunaendelea kufanya mazungumzo na kampuni ya Strabag ya Australia kwamba hii ndiyo itakayotusaidia, wasipokubali hawa kutusaidia maana yake watu wa Mkuranga Mjini waendelee kuwa na shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwa heshima kubwa na taadhima, nguvu zetu tuzielekeze katika kuongeza Mfuko wa Maji ili tutatue kabisa tatizo la maji ambalo linawakabili hasa hawa niliowasifu pale nilipokuwa naanza kutoa hotuba yangu, akinamama. Unaposaidia tatizo la maji unawasaidia akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningeomba sana tuongeze nguvu zetu katika utalii. Naomba niseme kwamba suala la utalii kuongezewa kodi zote hizi ni tatizo kubwa. Katika takwimu inaonesha kwamba bajeti yetu ya 2015/2016 sekta ya utalii iliongoza kwa asilimia 25. Katika mwaka wa 2014/2015, inaonesha kwamba pesa za kigeni takriban shilingi trilioni 8.3 zimetoka katika utalii. Inaonekana kwamba mwaka 2015 takriban ajira milioni moja, laki mbili na tisini na nne elfu zimetokana na utalii. Leo hii utalii huu umeongezewa kodi nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi zetu za Afrika Mashariki Wakenya wameondoa kodi mbalimbali katika utalii na nia yao ni kuongeza utalii katika nchi yao, nia yao ni kuongeza idadi ya watalii, ajira na kipato chao. Tusipofanya jitihada ya kuondoa kodi hizi utalii utashuka. Tazama katika utalii kazi ambazo zimepangwa kufanywa na Watanzania peke yake ni pamoja na kukodisha magari, wakala wa safari (travel agents), kupanda milima na waongozaji watalii na zote zimewekewa kodi. Kwa hiyo, hii itasababisha kupunguza idadi ya watalii, projection yetu ya kupata idadi kubwa ya watalii itapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapiga kelele hapa ya kupata pesa za kutosha kwa ajili ya miradi yetu ya maji, afya, ambapo afya imeachwa mbali katika bajeti hii. Tutazipataje hizo pesa kama tunaongeza kodi ambazo zitawakimbiza watalii wetu? Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa positive measure aliyoifanya ya kuongeza kodi ya utalii katika vyombo vya usafiri wa anga lakini apunguze kule kwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena kumpongeza sana mke wangu na kuwapongeza akinamama wote. Naunga mkono hoja hii na ahsanteni sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika mjadala huu unaohusu Kamati yetu ya Viwanda na Biashara na Mazingira lakini nikienda sambamba na ile ya Mitaji na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nichukue fursa hii kupongeza sana Kamati yetu, imefanya kazi nzuri yenye kupendeza ambayo imeeleza mambo mbalimbali hasa hii ya Viwanda na Biashara ambayo ningependa nijielekeze kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naomba niwe shuhuda mzuri sana wa Tanzania ya viwanda. Katika Jimbo langu la Mkuranga mpaka sasa nina viwanda 56 vyenye kufanya kazi na nina viwanda 11 ambavyo wakati wowote vitakamilika. Katika hivyo 11, kimoja ni kile kipya na kikubwa kushinda vyote katika Afrika Mashariki na Kati, kiwanda cha tiles ambapo tutakuwa na uhakika sasa wa kutokuagiza tiles kutoka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa na uwezo sisi wenyewe katika nchi yetu kupata huduma hii bila kuagiza kutoka mahali kokote. Kwa fursa hii kwa kweli kabisa napenda niipongeze sana Serikali yetu kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kuwavutia wawekezaji wale na wakaja katika Jimbo letu la Mkuranga na kuwekeza pesa zao nyingi kabisa juu ya kujenga kiwanda hiki kikubwa cha tiles.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli uwepo wa viwanda umetuinulia sana uchumi wetu sisi watu wa Mkuranga na nchi kwa ujumla wake. Mwaka jana 2016/2017 mwaka huu ambao tunamalizana nao tuliweka kadirio la kupata service levy isiyopungua milioni 500 na sasa tutakuwa na uhakika wa kupata service levy isiyopungua bilioni moja katika huu mwaka wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme ukweli na hapa ndipo nilipokuwa nataka nisisitize sana, kwamba bado tunayo fursa kubwa zaidi ya kuwa na viwanda vingi zaidi, hasa hususani katika Jimbo la Mkuranga na sehemu zingine katika nchi. Kazi kubwa ambayo ningependa niiseme hapa ni kwa wenzetu wa Wizara ya Nishati na Madini, wajitahidi sana katika kuhakikisha nishati hii ya gesi, ya umeme, iweze kuwa ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimekikosa kiwanda pale Mkuranga cha kutengeneza nguo katika eneo la Dundani. Mwekezaji amekuwa yuko tayari kabisa ataajiri vijana wasiopungua 14,000 lakini sharti la kwanza anataka umeme wa uhakika. Sasa pamoja na jitihada kubwa sana za kuwavuta wawekezaji zinazofanyika na wao wanaitikia, lakini bado tunayo changamoto kubwa ya nishati. Kwa hivyo wenzetu wa nishati wajitahidi wahakikishe mipango yao ya kusambaza gesi katika viwanda vyetu iende sambamba na mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani katika viwanda hivi vyote 56 hakuna kiwanda hata kimoja leo kinachotumia gesi na hilo bomba la gesi limepita hapo hapo Mkuranga. Kwa hivyo wenzetu ni lazima watuambie; nimemsikia Naibu Waziri asubuhi anasema kuna zaidi ya bilioni tano ambazo zitaelekezwa katika kwenda kusambaza gesi majumbani katika maeneo ya Tabata na Sinza na kwingine kule Dar es Salaam, lakini hakueleza ni kiasi gani cha fedha ambacho kitatumika kwenda kutengeneza mtandao wa mabomba ya kusambaza gesi katika viwanda hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kupata huduma hii ya nishati kwa bei nzuri na hatimaye uzalishaji wa bidhaa katika viwanda vile uwe ni wa gharama nafuu na hatimaye kumsaidia Mtanzania mlaji wa zile bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vile ili aweze kupata zile bidhaa kwa bei nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu alipokuja katika kiwanda cha Bakhresa aliagiza jambo hili, aliagiza kwa sababu watu Bakhresa food industry wameomba wapate gesi kwa muda mrefu na bado hawajafanikiwa mpaka hivi sasa. Jambo ambalo linapelekea uzalishaji wa bidhaa katika viwanda mbalimbali katika maeneo yetu unakuwa ni wa gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tuwaombe wenzetu watuambie ni namna gani, viwanda viko vingi sana, vinaingia kila siku ya Mwenyezi Mungu lakini je, tumetengeneza mazingira ya namna gani ya kuweza kuvisaidia kupata huduma hii ya gesi na nishati kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana nawashauri na kuwaomba wenzetu hawa wa nishati na madini waone umuhimu wa kuiweka Mkuranga kuwa hata na substation yake ya umeme, uwezekano huo upo na wala hakuna tatizo lolote la eneo wala hakuna tatizo lolote la upatikanaji wa gesi. Gesi tap ziko pale valve namba 12 na 13 katika maeneo ya Mbezi na Mkiu zinapatikana kwa wingi kwa hivyo tunawaombeni sana mtuweke substation pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu wa viwanda ni lazima kama ilivyopendekezwa na Kamati katika ukurasa wake wa 50 juu ya elimu ya ufundi. Vijana wetu wengi sana wanakwenda kuwa vibarua katika viwanda hivi, lakini tunaomba sasa ikiwezekana na wenzetu wa elimu muone umuhimu wa maeneo kama haya ya viwanda kuyapa uwezekano wa kuwa na vyuo vya elimu, ili vijana wetu waweze kupata elimu na hatimaye waweze kwenda kuwa na uwezo wa kwenda kuajiriwa katika viwanda vile. Hivi sasa unaweza ukakuta ni asilimia ndogo sana ya vijana wa Mkuranga ambao wanafanya kazi katika viwanda hivyo. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri anayehusika pia alitazame hili jambo kama ilivyopendekezwa na Kamati yetu ya Viwanda na Biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ningeomba sana masuala haya ya ukuaji wa viwanda na sisi tumejiandaa vizuri na tayari maeneo yapo ya kutosha. Mathalani tunalo eneo pale katika Kijiji cha Dundani, zaidi ya ekari 700 na Waziri wetu wa Viwanda na Biashara amekuwa akilitaja kila mara. Sasa afanye kazi ya kuhakikisha wananchi wale zaidi ya miaka minne sasa, asiwe anakuja tu kaka yangu Mwijage kulitangaza lile eneo, awalipe fedha za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu wamezuiwa kufanya chochote katika eneo lao, sasa ni miaka minne hawawezi kuendeleza chochote, hawazalishi chochote, hawasafishi maeneo yao ni kwa sababu wamejitolea eneo lao lile liwe ni eneo la viwanda. Sasa wale wananchi wamekata tamaa, ni lazima tuone ni namna gani either hawa wa Mkuranga au ni kwingineko kokote katika nchi watu walikojitolea katika kuhakikisha kwamba Tanzania ya viwanda inapatikana, basi mambo haya yakamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana nisisitize tena kwa mara nyingine juu ya kupatikana kwa nishati ya gesi katika viwanda vyetu ili uzalishaji uwe wa gharama nafuu. Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naanza kwa msemo wa Waswahili tunaosema kwamba “Haja ya mja hunena muungwana ni vitendo.” Namshukuru sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na kila mmoja anaona kabisa. Tuseme ukweli kwamba ni lazima tukubaliane kwamba hatuwezi kufanikiwa bila ya kufunga mkanda na ku-sacrifice kwa ajili ya kizazi cha leo na cha kesho. Wazungu wanasema no pain no gain. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa, tulikuwa tukitukanwa hapa, nchi kubwa ya Tanzania tunashindwa na nchi ndogo ndogo. Leo tumenunua ndege sita na mwakani tunanunua ya saba, wapo watu wanakuja na maneno sijui terrible teen, sijui kitu gani. Hayo ni matango pori na mimi namshauri sana Mheshimiwa Waziri akiinuka hapa aseme maneno ya kitaalam awaambie Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wasiwe na wasiwasi, hatuna wasiwasi na Mheshimiwa Waziri Profesa aende akanunue ndege eti zenye wasiwasi. Nina hakika kabisa kwamba akiinuka Mheshimiwa Waziri hapa atatuwekea na kutufungia mjadala huu ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo, naomba pia niishukuru sana Serikali yangu, kwa sababu nimekuwa nikiinuka mara nyingi sana kuzungumzia barabara ya kutoka Mkuranga Mjini kwenda Kisiju - Pwani na sasa kazi imeanza. Nimeona katika hotuba ya Rais ya kwamba upo uwezekano mkubwa mwaka huu tukapata pesa za kutengeneza kilomita mbili za lami, hii ndiyo Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa kuwa barabara hii imekuwa ikitengewa pesa nyingi kila mwaka kwa ajili ya maintenance, tunanunua kokoto zinazotoka Jaribu Mpakani takribani kilomita 65 kufika Mkuranga. Tafadhali sana Mheshimiwa Waziri atazame jambo la namna hii. Waone kabisa kwamba huu mpango waliouanzisha wa lami ya kidogo kidogo waufanye kila mwaka badala ya kuingiza hela nyingi katika maintenance ambayo baada ya muda mfupi inaharibika tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaiona Mkuranga ya viwanda na Mheshimiwa Rais amekuja Mkuranga mara mbili, mwezi huu wa Tano au wa Sita atakuja mara ya Tatu kuja kufungua kile Kiwanda cha Tiles. Mvua hizi za masika zimetaka kukifanya kiwanda kile kisipate malighafi, kwa nini? Kwa sababu barabara ya Kimanzichana mpaka Mkamba, Mkamba - Mkuwili kuungana na wenzetu wa Kisarawe imekufa kwa sababu ya mvua. Naomba sasa tuliangalie jambo hili kwa umakini sana, kwa sababu kiwanda kile kinakwenda kulisha tiles za nchi nzima, hatutakuwa na sababu ya kununua tiles kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri iangalie hii ni barabara ya uchumi, watu walikuwa wakisema humu kwamba malighafi za kiwanda hicho zinatoka nje ya nchi. Nataka nikuhakikishie malighafi yote inatoka Kisarawe, Kilindi
- Tanga, Mkuranga, Kisegese, Vianzi na Mkamba. Hivyo, naomba barabara hii ifanyiwe kazi maridadi kabisa ili tuweze kuinua uchumi wa watu wetu na watu wetu waweze kuona kwamba utengamano wa viwanda na uchumi wao unakwenda sambamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kwa ufupi sana nizungumzie suala la kupandishwa hadhi za barabara. Ninazo barabara mbili ningependa zipandishwe hadhi. Barabara ya Kiguza – Hoyoyo, Hoyoyo mpaka kwenda kutokea Kitonga - Mvuti. Barabara hii upande mmoja ni trunk road ya Natioal Road - Kilwa Road na upande mwingine ni barabara ya Mkoa wa Dar es Salaam. Pande zote hizi mbili zinabeba mizigo mizito tena zina lami, lakini sisi barabara yetu ya Kiguza – Hoyoyo kupita pale Hoyoyo kwa Mama Salma pale ni barabara ya vumbi na barabara imechoka. Sasa tunabebeshaje mizigo mikubwa barabara hii na Halmashauri hazina uwezo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akiona barua ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kamanda Injinia Evarist Ndikilo aipitishe haraka barabara hii nayo pia vilevile iweze kupata kupandishwa hadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo iko barabara ya Vikindu mpaka Vianzi – Marogoro – Sangatini, upande wa Dar es Salaam kutoka Tundwi - Songani, Pemba Mnazi - Kibada - Mwasonga mpaka Kimbiji inawekwa lami. Upande wetu huku kilomita kama kumi bado ni barabara ya Halmashauri inabeba mzigo mzito. Naomba sasa kwa heshima kubwa na taadhima tuendelee kuthibitisha ya kwamba hii ni Serikali ya Hapa Kazi Tu na akiiona barua ya Engineer Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa, Kamanda kabisa basi aitie mkono wake pale Mheshimiwa Waziri, ahakikishe kwamba mambo yanakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nichukue fursa hii kuipongeza tena Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya ya kulipa madeni ya Wakandarasi. Tunaomba pia iendelee kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa ufasaha kwa maana liharakishwe na pesa zinazokwenda katika Halmashauri zetu ziharakishwe, tena nafahamu kwamba Serikali ina mpango mzuri sana wa kuanzisha Agency ya Barabara za Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu hapa wamezungumzia jambo la kwamba agency hii ikiwezekana wapewe TANROADS. Sasa sisi hatutaki kurudi nyumba, tunachosema tutakuja kumwambia Waziri wa Fedha aangalie uwezekano ikiwezekana hii Agency ya Barabara za Vijijini ipate pesa na asilimia kubwa zaidi ya ile ya thelathini. Kwa sababu uti wa mgongo wa wananchi wetu ili kuwatoa katika umaskini ni kuwatengenezea barabara zao. Watu wangu wa Mkuranga wakiboreshewa barabara zao vizuri ambacho ndiyo kipaumbele namba moja cha miundombinu, nina hakika kabisa kwamba, watainuka zaidi kiuchumi na watafanya shughuli zao wenyewe. Leo hii mananasi pale yanaharibika ni kwa sababu barabara ni mbovu za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa na taadhima naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia mjadala wa hotuba hii ya maji. Nami naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na niwapongeze sana kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya.


Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajielekeza katika kuwaombea maji wananchi wangu wa Mkuranga, uniruhusu nitumie nafasi hii ya dakika moja, mbili kuwaonesha Watanzania kwamba Chama cha Mapinduzi bado ndiyo Chama imara chenye haki ya kuendelea kuwaongoza Watanzania. Tulipokuwa katika uchaguzi wa East Africa kwenye Bunge hili, hatua ya kwanza Chama cha Mapinduzi kiliwakataa Mheshimiwa Wenje na Mheshimiwa Masha. Wenzetu wakaondoka wakaenda kuwaambia Watanzania kwamba sisi tunataka kuwachagulia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana unafiki wa Vyama vya Upinzani umedhihiri katika Bunge hili. Wale waliowaleta sisi tukawakataa, wametusaidia jana kuwakataa kwa vitendo. Makamu Mwenyekiti wao Profesa Safari wamempa namba ya viatu, namba 35, Wenje wamempa namba 34, Masha wamempa namba 44. Tunaendelea kuwaambia Watanzania kwamba Chama cha Mapinduzi ndicho chama cha kweli na ndicho chama cha kukiamini na Wapinzani hawa ni wanafiki wakubwa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo na ujumbe umefika, naomba nisema yafuatayo sasa.

UTARATIBU...

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tuwaambie sisi bado ni Walimu katika Taifa hili, wao wakijua hivi, sisi tunajua hivi, hiyo ndiyo habari. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waitara, rafiki yangu kwamba hiki ndiyo Chama cha Mapinduzi ambacho hata yeye kilimlea pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tumeendelea kuuthibitishia Umma wa Watanzania kwamba hiki ndiyo Chama cha Mapinduzi. Tutaendelea kuwafunzeni siasa, kwa sababu hiyo ndiyo kazi yetu. Kesho tutakwenda kupitisha bajeti ya Wizara ya Maji. (Kicheko/Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu ni kutaka kuona kwamba katika bajeti hii ya Wizara ya Maji tozo ya shilingi 50 inaongezeka. Mheshimiwa ukikaa hapo katika kiti tuelekeze, Kamati yetu ya Bajeti ikakae na Serikali iongeze bajeti ile ya tozo ya shilingi 50 tukawahudumie Watanzania. Watanzania wa Mkuranga Mjini wanayo maji pale katika Mlima Kurungu, kisima cha mita 600, kuna maji ya litres nyingi yanapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu mmoja pale anaitwa Manyaunyau, anawauzia Watanzania wa Mkuranga maji. Mtu mmoja amechimba yeye binafsi. Katika bajeti ya 2014/2015 zilitengwa hela hazikwenda, mwaka huu wa fedha wa 2015/2016 uliokwisha zilitengwa pesa hazikwenda. Sasa katika bajeti hii tunachotaka pesa ziende. (Makofi)Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali. Katika miradi ya visima kumi, mimi nimechimba visima kumi Mwanambaya, Mlamleni, Mkenezange, Kimanzichana, Mdimni, Ng’ole, Mbulani, Yavayava, nimechimba huko kote. Ninachosubiri sasa ni kuona miundombinu ya maji inaenea kwa wananchi wa Jimbo langu la Mkuranga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina wasiwasi kwa sababu nikimtazama jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, naamini kabisa kwamba maji yanakwenda kutatuka na Watanzania ile nia yetu tuliyowaambia ya kumshusha mama ndoo kichwani, tutaifanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri mimi ni Mbunge mpambanaji.

T A A R I F A....

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, unilindie muda wangu. Nimesema hapa ya kwamba na sisi hicho alichokisema ndicho tunachokitaka. Hizi pesa zilizotengwa tuhakikishe zinakwenda kwa wananchi. Hizi pesa zikienda, tuna hakika azma yetu ya kumshusha mama ndoo kichwani itakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hapa ya kwamba tuongeze tozo hiyo shilingi milioni 181, ninety something millions zote zimetoka katika tozo ya mafuta. Tukiongeza tuta-double, tutawasaidia Watanzania wakiwemo wa kwa rafiki yangu Mwalimu Marwa kule Serengeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa umuhimu kabisa, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri anisaidie kunipelekea pesa zile. Ukurasa wa 163 ziko peza zinapelekwa kwenye Miji 63. Mmoja katika huo Mji uwe ni Mji wa Mkuranga. Sisi hatutaki pesa nyingi, tunataka kama shilingi milioni 800. Nami kwa kuwa ni Mbunge mpambanaji, nimeshajiongeza, nimezungumza na Ubalozi wa Kuwait, wameniambia yatoe maji kutoka mlima Kurungu yapeleke katika tenki. Jenga tenki, sisi tutakusaidia katika pesa za kufanya distribution. Unataka nini tena? Mungu akupe nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa heshima kubwa na taadhima niseme kwamba Mawaziri wetu chapeni kazi, sisi tuko pamoja na ninyi, kazi yenu mnayoifanya tunaiona na tunataka tuwahakikishie mkienda mkakaa Serikali na Kamati yetu, mkatukubalia, tukaenda kubadilisha katika Sheria ya Fedha, tukaongeza tozo ya shilingi 50, basi mambo yatanoga sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia dakika hizi mbili, tatu za mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ya kwangu ni ushauri. Kwanza napenda ni-declare interest kwamba katika fani ambazo nimezisomea ni pamoja na hii fani ya uvuvi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishauri Serikali yangu, nimshauri Mheshimiwa Rais na kwa kusema ukweli, Mheshimiwa Rais wetu nia yake ni njema sana. Nataka nimwambie kwamba kuna mapato makubwa sana kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa dunia nzima inahamia kwenye jambo linaitwa blue economy. Naomba niitolee mfano Kisiwa kidogo cha Maldives ambacho kina wavuvi 8,139, sisi tuna wavuvi wadogo wadogo 203,000. Maldives ina vyombo vilivyosajiliwa vya kufanya uvuvi ambao wao wanategemea spicies moja tu ya samaki aina ya tuna, mwenzangu Mheshimiwa Ngwali ametoka kusema hapa, tena amesema kwa kufoka kwelikweli, sisi tuna vyombo vilivyosajiliwa vya maji baridi na maji chumvi zaidi ya 59,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ikiwekeza katika uvuvi, hasa huu wa Bahari Kuu ambao hatujautumia vyema mpaka hivi leo, nataka nikuhakikishie kwamba tutapata kipato kikubwa sana na inaweza ikawa ni sababu ya kuinua uchumi wetu na ajira za watu wetu kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Mheshimiwa Rais katika mwaka mmoja huu na nusu amenunua ndege za kutosha na anaendelea kutuboreshea, tunajenga SGR, tunajenga flyovers, namwambia Mheshimiwa Dkt. Tizeba mwambie Rais wetu anunue meli ya uvuvi wa kisasa, wa kibiashara. Meli ambayo itachakata na itafanya na mambo mengine yote, utaona namna ambavyo GDP inayopatikana kutokana na uvuvi, Wabunge wote humu tutakuja kushuhudia sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni huo, najua kwa kufanya hivyo, sisi watu wa Mkuranga tutapata sasa matrekta tunayoyalilia. Maana Wilaya nzima ya Mkuranga haina trekta la Serikali hata moja, tuna matrekta 22 katika vijiji 125, yote ni ya watu na yote ni mabovu. Sasa katika uchumi wa namna hii tutapataje lakini tukienda katika blue economy, sisi tumesoma pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwalimu wangu, Mheshimiwa Dkt. Sware yule pale na wapo Walimu wangu wengine wengi kule, akina Dkt. Tamatama Rashid na wengineo, hawajatumika ipasavyo katika blue economy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, Mheshimiwa Dkt. Tizeba na kaka yangu Mheshimiwa Olenasha, mwambieni Mheshimiwa Rais tununue meli ya uvuvi hata moja tu ya Serikali, mtaona namna ambavyo uchumi wa nchi hii utakavyopanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii niliyopata.
The Finance Bill, 2016
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, nilisahau hili la dakika tano lakini nilichokuwa nataka nikizungumze ni juu ya mabadiliko ya sheria hii niliyoitaja hapo hususani kifungu cha 86 na kile kifungu kidogo cha (3) kilichoongezwa. Sheria hii inahusu matumizi ya mashine za kielektroniki. Nimesoma katika mapendekezo katika kifungu kidogo cha (3), yanamtaja mnunuzi kupewa risiti, muuzaji kutoa risiti lakini pia inataja endapo kama mnunuzi hakupewa risiti ile na muuzaji na hakuripoti jambo lile achukuliwe hatua za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nilichokuwa nataka kukizungumza kwa makini kabisa kwanza ni kushukuru kwamba Kamati imeeleza namna ambavyo Serikali imepokea mapendekezo ya kutenganisha vitu hivi vitatu, muuzaji awe na namna yake, mnunuzi awe na namna yake lakini na bidhaa yenyewe, hili jambo bado limekuwa ni pana sana. Napenda Serikali itupe ufafanuzi juu ya bidhaa kwamba mtu anayekwenda sokoni kununua bidhaa za Sh.20,000 na mtu anayekwenda kununua bidhaa za Sh.1,000,000, tuelezwe kinagaubaga juu ya watu hawa ili wananchi wetu waweze kuelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu walipoona mabadiliko haya ya sheria yameandikwa katika vyombo vya habari, huko vijijini kwetu taharuki imekuwa ni kubwa sana. Sisi tungependa tupate kujua na kuelezwa waziwazi lakini tusiishie katika kuelezwa waziwazi, Serikali kwa maana ya Wizara yetu ya Fedha na TRA ni lazima zihakikishe kwamba zinakwenda kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wetu wawe na uelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba Mtanzania mzalendo ni yule ambaye yuko tayari kulipa kodi, tena kulipa kodi bila shuruti, lakini haiwezi kuwa kulipa kodi bila shuruti bila wananchi hawa kupewa elimu. Naomba vitengo vyetu katika Wizara ya Fedha na TRA visiwe vya kuzima moto, liwe ni jambo endelevu hadi huu utamaduni wa kulipa kodi uweze kuzoeleka na watu waone kwamba ni wajibu wao na ni haki yao kulipa kodi kila wakati katika kila transaction wanayoifanya. Bila kufanya hivyo, kuwafanya Watanzania kuona kwamba ulipaji wa kodi ni utamaduni wao bado jambo hili litakuwa ni tatizo na wananchi wetu wengi watajikuta wanaingia katika mikono ya sheria wakaenda kufungwa au kulipishwa faini ambazo hawatakuwa na uwezo nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, ningeomba wenzetu wa Wizara ya Fedha na TRA waweke utaratibu wa bonus. Nimetazama katika nchi mbalimbali nimeikuta nchi ya South Korea wameweka utaratibu wa bonus ambao umeanza mwaka 2004 na umefanikiwa sana. Wale wauzaji na wanunuzi zile risiti zao wazihifadhi, waweke bonus kwa muuzaji ambaye anaonesha vizuri juu ya utoaji wa risiti na mnunuzi ambaye anaonesha vizuri juu ya risiti zake, hii itasaidia wananchi wetu kuunga mkono zoezi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami naunga mkono agenda hii. Ahsante sana.
Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua fursa hii kukushukuru sana kwa nafasi hii niliyoipata. Pia naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Mheshimiwa Mabula, Katibu Mkuu na Makamishna wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa, nimpongeze sana rafiki yangu Kamishna Mathew wa pale Dar es Salaam kwa kazi kubwa anayoifanya, halali usingizi, ni kwa sababu ya kuhakikisha migogoro inakwisha Dar es Salaam. Kamishna wangu wa Kanda ya Mashariki, kwa kweli amenisaidia sana katika mgogoro wa vijiji vinne vya Mlamleni, Luzando, Mwanambaya na Mipeko. Amefanya kazi kubwa na natumai kazi hii ataimalizia vizuri hapo mbele. Vile vile, kwa namna ya kipekee, nitambue kazi nzuri anayoifanya Kamishna wetu wa Kanda ya Kusini, kaka yangu Luanda, wote Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue fursa hii kurudia tena kusema kwamba kazi hii kubwa wanayoifanya, Mheshimiwa Waziri, tunalo sisi la kujifunza. Kwa sababu Waswahili wanasema, ukiona vyaelea ujue vimeundwa, Mheshimiwa Waziri Lukuvi, kwake yeye kwa kazi
kubwa anayoifanya na Wabunge wote humu tunamsifu, ni kwa sababu tunakwenda kila mahali, tunatatua migogoro na tunafanya vema sana. Hata kwangu Mkuranga migogoro niliyoitaja na mingine ambayo sikuitaja ameifanyia kazi kubwa sana. Namshukuru sana na Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo tatizo katika Kijiji cha Dundani na hili ni tatizo la maeneo mengi linalohusu fidia. Wananchi wanazuiwa kwa ajili ya uendelezaji wa ardhi zile kwa ajili ya uwekezaji, ni jambo jema. Tunapenda uwekezaji, lakini sasa inapofika mahali watu wanasubiri jambo kwa muda mrefu sana inafika miaka mitatu, minne, mitano, maeneo yao yanageuka kuwa mapori, hawawezi kuendeleza chochote katika maeneo yale. Hili linakuwa ni tatizo na linawakatisha tamaa sana wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri, yeye ni champion, atusaidie tutoke mahali pa namna hii. Wananchi wanaozuiwa kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu na yanageuka kuwa ni mapori, hawawezi kuvuna nazi zao, hawawezi kulima mihogo pale, hawawezi kufanya maendeleo ya namna yoyote, tuwasaidie. Kama tumeshindwa tutafute namna ya kukaa nao na tuwarejeshee maeneo yao waweze kuendelea na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nitoe ushauri ni eneo la upimaji na uendelezaji wa ardhi. Hili eneo lina potentiality kubwa sana, wazo langu ni kwamba, kwanza nawapongeza sana Wizara, wamekubali kuchukua taasisi na makampuni binafsi kuweza kushiriki katika kazi hizi na hili ni jambo jema, ni lazima tubiasharishe mawazo yetu. Hata hivyo, hapa bado liko tatizo, Wizara ya Ardhi mshirikiane vema hasa na wenzetu wa TAMISEMI, uendelevu wa ardhi kwa kutumia kampuni binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanachukua pesa zao lakini mlolongo unachukua muda mrefu sana, hasa mtu akiwa amekopa pesa yake benki kuweza kufanya marejesho haiwezi kuwa kazi nyepesi tena. Kutoka kununua ardhi mpaka kufika kuipima, mpaka kufika kuisaidia Serikali kuwauzia wananchi ili sasa papatikane ardhi iliyoendelezwa, inachukua kipindi kirefu sana. Matokeo yake inawakatisha tamaa, Mheshimiwa Waziri aMheshimiwa Mwenyekiti, amefanya kazi nzuri ya kuweka bei elekezi, maana sasa ardhi ilikuwa inafanya inflation, kila mtu anajipangia anavyoweza tu, sasa tume-control hilo jambo, ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, lazima tuwe na ushirikiano ili hii kazi ya kuipima ardhi yetu ya Tanzania kwa kutumia taasisi binafsi iweze kuwa yenye kuvutia, kazi hii ya kupima Mheshimiwa Waziri peke yake hataweza, tutarudia hapa mwaka hadi mwaka hata miaka mia moja, hatutaweza, ndiyo ile nasema lazima tubiasharishe mawazo yetu. Wizara ya Ardhi na Wizara ya TAMISEMI tushirikiane, milolongo, bureaucracy zimekuwa nyingi sana. Ushauri wangu ni huo kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia mjadala huu wa mapendekezo ya bajeti. Nami moja kwa moja napenda nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu Dkt. Mpango, lakini pia napenda nichukue fursa hii kumshukuru Naibu wake na timu nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, popo hajafahamika kama ni mnyama ama ni ndege mpaka hivi leo. Hawa wenzetu hata sitaki kuwaita ni vinyonga, naomba niwaite popo. Maana yake hawajafahamika either ni ndege ama ni wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo limewashuka! Walijigeuza kuwa ni Mawakili wa wale ambao sisi tumewatuhumu kwamba ni wezi wetu na yule mhusika mkuu amewathibitishia mchana wa leo, ameingia na amekiri mwenyewe kwa kinywa chake kwamba wako tayari kulipa pesa tunazotaka au tunazowadai. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena lile liliokuwa linaonekana kwamba ni jambo gumu la kujenga smelter katika nchi hii amelichukua na amesema wako tayari kujenga smelter katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Afrika, our home land; Afrika ina bahati mbaya, Wapinzani wa Afrika wamekuwa wakitumika na mabeberu miaka yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, UNITA wametumika na mabeberu kuiangamiza Angola miaka yote, wale pia wanatumika na mabeberu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna kila sababu ya kutamba. Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, eneo la madini ukurasa wa 32 Kifungu cha 35 (a) kinaeleza wazi wazi, “kuweka na kusimamia mfumo thabiti wa kukagua shughuli za migodi.” Ukienda ukurasa wa 34, hiyo hiyo 35(k) utaambiwa…. (Makofi)

TAARIFA . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaliyotokea mchana wa leo hayawezi kupita hivi hivi, lazima kuna watu wahangaike. Yale mambo siyo mchezo mchezo! Wale Wazungu wakimwaga mzigo hata wa trilioni 10, 20 au 50 tu hapa, haya mambo tunayoyazungumza juu ya barabara zetu, juu ya maji, juu ya shilingi milioni 50 katika vijiji, juu ya SGR, juu ya kuongeza ndege nyingine, juu ya maendeleo yote katika nchi hii, tutapaa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikwambie tu na Bunge hili pia, Word Bank wametoa ripoti na wame-predict Tanzania is going to be the third fastest growing economy katika Afrika. Itapitwa na Ethopia kwa 8.3 percent; itapitwa na Ghana kwa 7.8 percent; sisi tutakuwa 7.2. Hiyo ndiyo habari. Nataka nikwambie, ukitaka kuyaona hayo, ndiyo maana utaona watu wamekimbia siti zao leo, wametoka mbele wamehamia kule nyuma. Aibu! Eeh, habari hii ni ngumu! Hii habari ni nzito!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mpango na timu yake msumari huo umeingia! Hatari sana haya mambo! Huyu JPM sio mtu wa mchezo mchezo, watu wanaweweseka, watu wamepoteza uelekeo! Haya mambo siyo ya mchezo mchezo! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi sasa katika bajeti yetu, natoa ushauri ili yale mapato yaendelee kutuimarisha katika uchumi wetu. Dozi imeshaingia, hela za Morena zimepotea, basi tunasonga mbele. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi katika blue economy. Nasisitiza ya kwamba fisheries, kama Ilani yetu inavyoeleza, tunayo nafasi kubwa sana ya kuendelea kukuza kipato chetu kwa kutumia Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu, tununue meli tuhakikishe kwamba tunachakata na kufanya maendeleo mengine katika Bahari Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii pia kuelezea juu ya kilimo. Wapo watu hapa wamesema Serikali hii haishughuliki na kilimo wakija kwetu sisi tunaolima korosho tunaweza tukawapopoa kwa mawe. Sisi tumeambiwa msimu huu wa kilimo, korosho tutapata sulphur bure, mabomba ya kupulizia bure. Ni nani huyo anayeweza kusimama hapa; Serikali imetuondolea zaidi ya tozo tano za kilimo, wewe leo unasimama unasema mambo yasiyokuwa na kichwa wala miguu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba sasa, sisi kama Taifa tunapoteza siyo chini ya Dola milioni 110 kwa kupeleka korosho ghafi nje ya nchi. Hiyo tukibaki nayo, tunao uwezo wa kutengeneza kiwanda cha kuchakata korosho na tukaweza kuuza na tukatoa ajira za kutosha. Tuweke mkakati maalum kabisa; ule uliowekwa na Bodi ya Korosho wa kuhakikisha tunatengeneza viwanda vyetu, basi hilo tusiliache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza wakati, katika bajeti hii nimeona mambo mengi; mojawapo ya jambo nililoliona ni misamaha mbalimbali kwa viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa fursa hii. Nami moja kwa moja naomba nijielekeze kwanza kwa kuwapa pole wenzetu wa kule Bukoba kwa maafa yaliyotokea ya tetemeko la ardhi na Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi wale wote waliotangulia mbele ya haki, lakini awaponye kwa haraka zaidi wale wote ambao hivi sasa wamekuwa wakiugua maumivu mahospitalini na adha mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue fursa hii pia vile vile kuipongeza sana Serikali yetu kwa kuleta sheria hii inayohusu Taasisi zetu za Utafiti wa Kilimo na Taasisi ya Utafiti Uvuvi. Imekuja wakati muafaka katika kuwasaidia watafiti wetu kuhakikisha kwamba wanaifanya kazi yao vizuri kwa maendeleo ya Taifa letu na kwa maendeleo ya dunia yetu kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo angle mbili, tatu ambazo ningependa nizizungumzie katika sheria hizi. Nitayazungumza mambo yote mawili kwa pamoja yanayohusu uvuvi lakini pia vile vile nitayazungumza mambo yanayohusu kilimo. Kabla sijakwenda katika kuzungumzia uvuvi na kilimo, nataka nitoe ombi hasa kwa wenzangu, maana unasikia hapa, watu wanajadili Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, mwingine anaanza kuzungumzia mambo ya Polisi na UKUTA, anaacha kuzungumzia masuala yanayohusu utafiti wa uvuvi kwa kuwa hana jambo anaenda kuzungumzia jambo linalohusu nyanya zake kule Kilombero zimepondeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni wakati muafaka watu kama hawa, rafiki yangu Mheshimiwa Lijualikali, jamani mtusaidie tupate elimu ya kujua hivi vitu vya kwenda kujadili. Hili jambo linahusu utafiti! Bahati njema sana katika sayansi hakuna blah blah! Sayansi inazungumzia facts! Sasa mimi nataka nitoe elimu inayohusu facts na siyo blah blah!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikia Yalaah, ujue imempata huyo! Ehee! Kwa hiyo, usishituke, imewapata hiyo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali juu ya suala hili linalohusu utafiti, kwanza, tuhakikishe kwamba COSTECH ndiyo inayopelekewa pesa na baadaye taasisi zetu zinakwenda kushindania pesa kule COSTECH. Jambo lililokuwa la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba COSTECH wanaweka vipaumbele sawa na watu wote wanavyohitaji, maana Taasisi ziko nyingi. Inawezekana kwamba Taasisi nyingine zisipate pesa hizo kutoka COSTECH.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba ili kila taasisi iweze kupata zile pesa, wakati mwingine taasisi zetu za uvuvi na kilimo hazipati kabisa hizo pesa, kwa sababu COSTECH inakuwa kwamba, hawa watu wa uvuvi na kilimo labda hawakuingia katika ushindani wa zile pesa ambazo zinagombaniwa kule COSTECH. Kwa hiyo, ni jambo la msingi kwamba COSTECH wajitahidi kuweka utaratibu ambao utasaidia taasisi zetu zote zihakikishe zinanufaika na pesa hizi za walipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kirefu sana, taasisi zetu zimekuwa zinategemea pesa za wafadhili, ambapo maana yake ni nini? Ni kwamba Donor anayeleta pesa zile, analeta kufuatana na kile anachokitaka yeye. Anayelipia zumari, ndiye anayechagua nyimbo. Sasa ni jambo la msingi kuhakikisha tunaongeza nguvu kule COSTECH na kuipa utaratibu mzuri ili taasisi zetu hizi tunazozitungia sheria leo ziweze kunufaika na pesa za Watanzania badala ya kutegemea zile pesa za Donors tu peke yake. Tukitegemea pesa za Donors peke yake, matokeo yake ni kwamba tafiti nyingi hazitafanyika na hivyo matatizo mengi yanayotokana na kutokufanyika kwa tafiti yatajitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo, nataka nizungumzie jambo la vifaa vya uvuvi. Kwa kipindi kirefu sana tumeona kwamba yanatokea matatizo mengi katika maziwa na bahari kwa ajili ya vifaa vya uvuvi, lakini sheria haijataja juu ya kutafiti ni vifaa gani hasa vilivyokuwa bora. Tunafahamu kwamba wakati wote imekuwa ikizungumzwa size ya nyavu kwamba size hii ndiyo inayofaa zaidi, lakini tungefurahi kuona kwamba sheria inataja na hivi vifaa vya uvuvi viweze kufanyiwa utafiti ili viendane na hali halisi ya kimazingira na wakati vile vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumza ni database. Tumefanya tafiti nyingi sana, nami nawashangaa wale ambao wanasema kwamba tunatunga sheria hizi za tafiti hazitusaidii kitu. Leo nataka nikuhakikishie, bila hizi tafiti hata hii jeuri ya kusema kwamba hakuna kilichofanyika na hazina faida hizi tafiti, watu wasingekuwa nayo. Hata hivyo wanasayansi tunafahamu kwamba hizi tafiti ni muhimu na hii sheria bado ni muhimu, cha msingi ni kuhakikisha tunakuwa na database ya tafiti zetu zote tulizozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi tafiti kama hazikutusaidia leo, zitasaidia vizazi vyetu; ndiyo maana ya elimu! Elimu haishii kwamba itatusaidia leo. Watoto wetu kule mbele watakapokuwa wanakwenda kusoma, wataona kwamba sisi huko nyuma tuliwahi kufanya utafiti wa jambo kadha wa kadha na limewekwa mle katika archives au vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nililokuwa nataka nilizungumze la kuishauri Serikali, najua lipo katika mipango yetu, lakini mipango iliyopo ni ya kiuchumi juu ya bandari ya uvuvi. Uwepo wa bandari ya uvuvi utasaidia pia watafiti wetu. Unapokuwa na bandari ya uvuvi maana yake ni kwamba watafiti wetu wanapokwenda kufanya shughuli zao za utafiti wanapata mahali pa kuweza kutia nanga na hatimaye kutoa results za utafiti wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nashauri sheria itaje juu ya muda wa ufanyikaji wa tafiti. Wadau wanalalamika sana; wapo watu wanapewa nafasi ya kufanya utafiti kwa miaka tisa...
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.