Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Abdallah Hamis Ulega (16 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kukarabati malambo ya Vijiji vya Makomariro 2, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Kihumbu, Kisangwa, Sanzete, Salama A, Salama Kati na Nyangaranga ambayo yamejaa magugu maji na mengine kina chake kimepungua?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilichimba malambo katika Vijiji vya Makomariro 2, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Kihumbu, Kisangwa, Sanzete, Salama A, Salama Kati na Nyangaranga kwa ajili ya kutatua matatizo ya ukosefu wa maji ya kunyweshea mifugo na kwa matumizi ya binadamu. Ni kweli malambo hayo kwa sasa yamejaa magugu maji na tope.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi wa vijiji husika kuyaweka malambo hayo katika mipango yao ya bajeti na kuiwasilisha Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ili yawekwe na kutengewa fedha kwenye mpango wa bajeti ya mwaka husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa malambo hayo, Halmashauri ya Bunda ilifanya tathmini ili kujua gharama halisi ya ukarabati unaohitajika kwa ajili ya kuweka kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019. Ukarabati huo utagharimu jumla ya Sh.36,825,600 kwa mchanganuo ufuatao: Lambo la Kyandege litahitaji Sh.25,618,350, Mugeta Sh.97,870,400, Sanzete Sh.36,286,000, Salama A Sh.25,926,000, Salama Kati Sh.46,315,850, Makomariro Sh.25,926,000, na Kihumbu Sh.108,883,000. Ukarabati wa malambo haya umepangwa kufanywa katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili malambo yaliyochimbwa au kukarabatiwa yaweze kuwa endelevu, Serikali inatoa ushauri kwa vijiji husika kuunda Kamati za Uendelezaji wa Malambo ambazo zitahusika na utungaji wa Sheria ndogondogo za utunzaji wa malambo hayo.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Suala la ufugaji samaki lina faida nyingi kwa wananchi kama kujiongezea kipato na kupata kitoweo lakini wananchi wa Kata za Ninde, Kala, Wampembe na Kizumbi walioko kando ya Ziwa Tanganyika hawafugi samaki kwa kukosa elimu:-
Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam kutoa elimu ya ufugaji samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa shughuli za ufugaji wa samaki zina faida nyingi kwa wananchi zikiwemo kujipatia ajira, lishe na kipato. Wilaya ya Nkasi ni moja ya Wilaya zenye mazingira na maeneo mazuri kwa ajili ya ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ina wataalam wa uvuvi saba, wawili kati ya hao wana shahada ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji na watano wana diploma zinazohusiana na masuala ya uvuvi na ufugaji wa samaki. Aidha, Kituo cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (doria) cha Kipili kilichopo katika Wilaya ya Nkasi chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kina wataalam watano. Pamoja na shughuli za usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika, watumishi hao wana jukumu la kusimamia shughuli za ufugaji wa samaki ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za ugani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza kasi ya utoaji elimu ya ufugaji wa samaki katika ukanda wa mwambao mwa Ziwa Tanganyika, Serikali kupitia Wakala wa Elimu ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) ilianzisha kituo cha FETA Kibirizi – Kigoma ambapo mwaka 2015/2016 kilidahili wanafunzi 59 na wanafunzi 29 walihitimu masomo yao na katika mwaka 2016/2017 walidahili wanafunzi 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Kituo cha Ukuzaji Viumbe kwenye Maji kilichopo Manispaa ya Kigoma kwa kushirikiana na Halmashauri zilizoko kwenye ukanda huo kimehamasisha ufugaji wa samaki na kuzalisha vifaranga vya samaki 31,404, ambapo katika mwaka 2016/2017, Wilaya ya Nkasi jumla ya wananchi 70 walipata elimu ya ufugaji wa samaki katika Vijiji vitatu vya Ninde, Msamba, Namansi ambao wameanzisha kikundi kimoja katika Kitongoji cha Chele. Katika Kata ya Kala jumla ya watu 270 kutoka Vijiji sita vya Kala, Tundu, Kilambo, King’ombe na Mlambo wamepata elimu ya ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na viongozi wenzake katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi katika kuweka vipaumbele na uhamasishaji wa ufugaji wa samaki ili wataalam waliopo waendelee kuhamasisha ufugaji wa samaki katika maeneo yaliyoainishwa na watumishi kutoka Wizarani tutahakikisha kwamba tunakwenda Nkasi kushirikiana nao katika kutoa huduma za ugani katika masuala ya ufugaji wa samaki. Aidha, vijana washauriwe kujiunga na mafunzo ya ufugaji wa samaki katika Kituo cha Wakala wa Elimu Mafunzo ya Ufundi (FETA) kilichopo Kibirizi – Kigoma na hatimaye waweze kujiajiri katika shughuli za ufugaji wa samaki kwa lengo la kujipatia ajira, lishe na kipato.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Serikali imeondoa tozo mbalimbali zilizokuwa kero kwa wananchi katika sekta ya uvuvi lakini bado kuna mkanganyiko ni tozo zipi zimefutwa na zipi zinaendelea.
(a) Je, Serikali inaweza kuainisha aina ya tozo zilizoondolewa katika sekta ya uvuvi?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa mwongozo kwa watendaji wa Halmashauri juu ya mabadiliko hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na kutekeleza Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuweka mazingira mzuri katika kuwezesha wavuvi na wawekezaji kuendesha biashara ya uvuvi kwa ufanisi.
Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 katika hotuba yake alielekeza kupitia na kuangalia tozo zote ambazo ni kero kwa wananchi ili ziondolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inaelekeza kuwezesha wavuvi wadogo kwa kuwaondolea kero mbalimbali zikiwemo tozo zisizo na tija. Ili kutekeleza maelekezo haya, wizara yangu katika Bunge la Bajeti ya mwaka 2017/2018 ilitangaza kuondoa ada na tozo mbalimbali ambazo zilionekana kuwa kero katika sekta ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada na tozo zilizoondolewa katika sekta ya uvuvi ni kama ifuatavyo:-
• ushuru wa kaa hai (waliozalishwa na kunenepeshwa) wanaouzwa kwenda nje ya nchi.
• Tozo ya cheti cha afya baada ya kukagua mazao ya uvuvi shilingi 30,000.
• Ada ya ukaguzi wa kina wa kiwanda/ghala kila robo mwaka shilingi 100,000.
• Tozo ya usafirishaji samaki yaani movement permit kuanzia kilo 101 hadi kilo 1000 shilingi 5,000; kilo 1001 hadi kilo 5000 ni shilingi 10,000; kilo 5001 hadi kilo 9999 shilingi 30,000; zaidi 10,000 na zaidi shilingi 50,000.
• Ada ya usajili wa chombo cha uvuvi chini ya mita 11 kwa wavuvi wadogo shilingi 20,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha mabadiliko ya tozo katika sekta ya uvuvi inatekelezwa na watendaji wa Halmashauri, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wizara ya TAMISEMI imeshatoa maelekezo kwa Halmashauri husika kusitisha mara moja tozo ambazo zimefutwa na Serikali. Aidha, Wizara Wizara inafanya marekebisho katika Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 ili kuendana na mabadiliko hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kupitia Halmashauri zetu kuhakikisha kuwa maagizo haya kuhusu tozo zilizoondolewa na Serikali yanatekelezwa.
MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-
Serikali kupitia Ilani ya CCM ya 2015 – 2020, ahadi namba 25(d) iliwaahidi vijana wafugaji kuwa itatoa dhamana ya mikopo kwenye asasi za fedha.
(a) Je, Serikali imeandaa mkakati gani wa kuwawezesha vijana wafugaji kuunda vyama vya ushirika ili waweze kunufaika na ahadi hiyo ya CCM?
(b) Je, Serikali inayo orodha ya vikundi vya vijana wafugaji ambao wamejiunga na vyama vya ushirika ambao wameweza kunufaika na utaratibu wowote ulioandaliwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maria Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati ulioandaliwa na Serikali katika kuwawezesha vijana wafugaji kuunda vyama vya ushirika ni pamoja na kushirikisha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvivi, Ofisi ya Rais TAMISEMI na wadau wengine katika kuhamasisha wafugaji, hususan vijana kuanzisha, kufufua na kujiunga na vyama vya ushirika vilivyopo. Uhamasishaji huo umefanyika kupitia mikutano na kampeni katika mikoa mbalimbali ikiwemo mikoa ya Tanga, Shinyanga, Mwanza, Iringa, Rukwa, Njombe, Manyara, Dodoma, Lindi na Mtwara ambapo wananchi walihamasika na kujiunga katika ushirika. Vilevile Wizara imeviunganisha vyama vya ushirika na wadau mbalimbali katika kuhamasisha ufugaji na uboreshaji wa mifugo. Baadhi ya wadau hao ni Oxfam, Care International na CARITAS.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ifuatayo ni idadi ya wafugaji waliohamashishwa kujiunga na vyama vya ushirika katika mikoa mbalimbali; Tanga jamii ya Wamasai na Wabarbaig wapatao 253; Njombe na Lindi wafugaji 265 walipatiwa elimu ya ushirika; Singida vikundi 62 vyenye wanachama 1,397 vilipatiwa elimu; Rukwa jumla ya wananchi 968 walihamasika kwa kujiunga kuanzisha vikundi vya ushirika; Dodoma kuna vikundi vipatavyo 338 ambavyo vinaundwa na rika mbalimbali; Shinyanga kuna vikundi 47, kati ya hivyo viwili vinajishughulisha na unenepeshaji wa ng’ombe na usindikaji wa ngozi. Taasisi za BRAC, Good Neighbourhood na World Vision zinatoa ufadhili wa mafunzo, ujenzi wa mabanda ya mfano, mifugo ya kuanzia kama mbegu pamoja na mashine za kuchakata ngozi kwa vikundi vya Mkoa wa Dodoma.
MHE. ALEX R. GASHAZA Jimbo la Ngara lina mifugo mingi hususan ng’ombe na mbuzi, lakini kuna tatizo kubwa la maeneo ya kunyweshea mifugo kwa maana ya malambo/ mabwawa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Je, ni lini Serikali itaanza uchimbaji na ujenzi wa malambo/mabwawa kwa ajili ya kunyweshea mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwanza napenda kumpa pole sana rafiki yangu, Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, mpiganaji, Mbunge wa Ngara kwa maafa yaliyowapa Wanangara, lakini pia naomba kujibu swali sasa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Ngara ina mifugo mingi ambapo pia hali hii inasababishwa na mifugo kuhamia kutoka nchi jirani bila kufuata utaratibu. Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha Wilaya ya Ngara ina ng’ombe wa asili 70,000, ng’ombe wa maziwa 2,872 na mbuzi wa asili 190,000, mbuzi wa maziwa 169,000 na kondoo wa asili 14,600.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na Serikali ili kukabiliana na upungufu wa maji kwa mifugo. Serikali imekuwa ikitekeleza mkakati wa kujenga malambo ya maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mengi nchini tangu mwaka 2001/2002 kwa kupitia bajeti ya Wizara na kupitia miradi shirikishi ya kuendeleza kilimo katika Wilaya ya Ngara pia katika miradi iliyoibuliwa na jamii yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kupitia ufadhili wa TASAF Awamu ya Tatu, inatarajiwa kujenga mabirika manne ya kunyweshea mifugo katika vijiji vya Magamba, Mumuhamba, Munjebwe na Nterungwe. Aidha, mradi unajenga bwawa moja katika kijiji cha Kasulo na miradi yote ya maji ya mifugo hadi kukamilika itagharimu jumla ya shilingi 135,569,900. Ujenzi wa malambo yote umekamilika, kilichobakia ni ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo. Jumla ya watu takribani 685 watafaidika na miradi hii.
ZAINAB A. KATIMBA (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:-
Wavuvi wadogo wadogo wa Ziwa Tanganyika wana tatizo la vitendea kazi.
Je, ni lini Serikali itawapatia wavuvi hao vitendea kazi vya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako, kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kumshukuru Mheshimiwa Spika, wananchi wenzangu wa Mkuranga na kwa namna ya kipekee kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini kushika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nijibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuhamasisha wadau wa uvuvi, ikiwemo sekta binafsi na jamii ya wavuvi wenyewe kuwekeza katika matumizi ya zana bora za uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha mapato yao, baadhi ya mikakati iliyotekelezwa ni kuwawezesha wavuvi wadogo kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi kupitia halmashauri husika na pia wawekezaji wakubwa kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza boti na zana mbalimbali za uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ziwa Tanganyika, tunacho Kituo chetu cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) pale Kibirizi Kigoma, ambapo tunayo mipango kama Serikali kukiimarisha ili kiweze kuunda boti za kisasa na pia kuendelea kutoa mafunzo na elimu inayohusu sekta ya uvuvi kwa wanafunzi na jamii za wavuvi na wadau wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatekeleza Sheria ya VAT ya mwaka 2007 ambayo imetoa msamaha wa kodi ya zana za uvuvi na malighafi nyingine ikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio vyake. Vilevile katika jitihada nyingine za kuwasaidia wavuvi, Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, katika mwaka 2015/2016 ilitenga jumla ya fedha shilingi milioni mia nne ambapo jumla ya injini za boti 73 zilinunuliwa na katika hizo boti 49 zilishachukuliwa na vikundi vya wavuvi mbalimbali nchini kupitia Halmshauri zao katika mtindo wa ruzuku ambapo Serikali inachangia asilimia 40 na vikundi vya wavuvi vinachangia asilimia 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi sasa tunazo boti takribani 24 ambazo zinawasubiri wavuvi mbalimbali waliopo nchini ikiwa ni pamoja na wavuvi walioko Mpanda na Ziwa Tanganyika lote kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shime kwa Waheshimiwa Wabunge, tuhamasishe vikundi hivi vya wavuvi, mashine hizo bado tunazo, waweze kuja kupitia halmashauri zao kwa kufuata utaratibu kuzipata na kuweza kuimarisha shughuli zao za uvuvi kwa ajili ya kujipatia kipato zaidi.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Shamba la malisho lililopo katika Kata ya Shishiyu Wilayani Maswa linamilikiwa na Serikali lakini halitumiki ipasavyo:-
Je, Serikali Kuu haioni haja ya kulirejesha shamba hilo kwa Halmashauri ya Wilaya ili lipangiwe matumizi mengine?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha kupumzishia mifugo (holding ground) cha Shishiyu kina ukubwa wa hekta 4,144 na ni kati ya vituo 28 vilivyotengwa nchi nzima kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 kwa ajili ya kukusanya na kupumzisha mifugo inayotoka minada mbalimbali kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa kabla ya kusafirisha mifugo hiyo kwenda katika viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama au kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, uwepo wa vituo vya kupumzishia mifugo ni hitaji la Kimataifa katika biashara ya mifugo. Zipo sheria mbalimbali za Kimataifa zinazolazimisha uwepo wa maeneo haya, yanayolenga utoaji huduma unaozingatia viwango ambazo zinasimamiwa na Shirika la Afya ya Wanyama ulimwenguni - OIE na makubaliano ya Kimataifa ya afya ya wanyama na mimea (Sanitary and Phytosanitary (SPS) chini ya Shirika la biashara la Kimataifa (WTO).
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili pia hutumika kama kituo cha karantini kwa ajili ya kuchunguza magonjwa, hususan yale ya milipuko yanapojitokeza hasa kutokana na Kanda ya Ziwa kuwa na mifugo mingi na baadhi ya mikoa katika Kanda hii inapakana na nchi jirani hivyo ni rahisi ka magonjwa ya wanyama ya milipuko kujitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kuna mwingiliano mkubwa wa wanyama wafugwao na wanyama pori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori Tengefu la Maswa kutokana na umuhimu wa kituo hiki kwa ajili ya biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi. Hivyo, siyo vema kubadilisha matumizi na madhumuni ya kuanzishwa kwa kituo hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo hili litaendelea kubaki chini ya usimamizi wa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili eneo hili liweze kutumiwa na wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa kuongeza thamani (value chain) ya mifugo na mazao yake.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
(a) Ranchi ya NARCO Mbarali ilianzishwa kwa ajili ya mifugo; Je, ni kwa nini eneo hilo sasa linatumika kwa kilimo?
(b) Migogoro ya wakulima na wafugaji Mbarali imekuwa ni mingi; je, kwa nini Serikali isitoe eneo la Ranchi ya NARCO Mbarali ili litumike kwa ajili ya malisho ya mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ranchi ya NARCO iliyopo Mbarali inajulikana kwa jina la Ranchi ya Usangu na ina ukubwa wa hekta 43,727 ambazo zimegawanywa katika vitalu 16 vyenye ukubwa wa hekta kati ya 2,000 na 3,000. Kutokana na maelekezo ya Wakala wa Baraza la Mawaziri Namba (2) wa mwaka 2002, vitalu vya Ranchi ya Usangu vimekodishwa kwa mkataba maalum kwa wawekezaji wa Kitanzania kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wa kisasa na kibiashara ili kuwa na ufugaji wenye tija. Kwa sasa vitalu vya wawekezaji hao vina jumla ya ng’ombe 2,722, mbuzi 1,145 na kondoo 500.
Mheshimiwa Spika, shughuli za uendelezaji mifugo zinaendana na kilimo cha malisho ya mifugo na mazao mengine ambayo mabaki yake hutumika kwa kulishia mifugo. Shughuli za uendeshaji wa nyanda za malisho ni kipengele muhimu kulingana na mkataba wa uwekezaji. Aidha, unenepeshaji wa mifugo hufanyika ndani ya vitalu vya wawekezaji ili kuvuna mifugo kwa muda mfupi na hivyo mabaki ya mazao hutumika kulisha mifugo kama sileji na hei.
Serikali kupitia NARCO inafanya tathmini ya vitalu hivyo na wale watakaobainika kukiuka makubaliano, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuvunja mikataba ya ukodishaji ili kuwapatia wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuwekeza kulingana na mikataba.
(b) Mheshimiwa Spika, kutokana na mkataba wa uwekezaji, Ranchi hiyo haiwezi kugawiwa kwa wananchi, kwa kuwa kuruhusu maeneo ya Ranchi kutumiwa na mifugo kwa ajili ya malisho itakuwa ni ukiukwaji wa sheria ya mkataba kati ya wawekezaji na NARCO. Aidha, kuruhusu uingizaji wa mifugo ndani ya Ranchi kutasababisha maambukizi ya magonjwa kwa mifugo ya wawekezaji.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Sekta ya uvuvi bado haijatumika kikamilifu kulipatia Taifa pato na kuwaondoa Watanzania hususani wavuvi katika dimbwi la umaskini.
(a) Je, ni lini Serikali itaweka jitihada za kusaidia wavuvi hasa wale wanaojihusisha na uvuvi wa Bahari Kuu?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wavuvi wadogo wadogo ili waweze kuvua katika Bahari Kuu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya Uvuvi nchini kwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kuendeleza wavuvi nchini ili waweze kupata ajira, lishe, kipato na kuchangia katika Pato la Taifa. Kwa mwaka 2016 sekta ya Uvuvi imechangia asilimia 2.0 katika Pato la Taifa na imekua kwa asilimia 4.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kuwasaidia wavuvi wadogo hususani wale wanaojihusisha na uvuvi wa Bahari Kuu Serikali imeanza kuweka vifaa maalum vya kuvutia samaki (Fish Aggregating Devices - FADs) ili kuwasaidia wavuvi kupata samaki wengi na kutumia muda mfupi katika uvuvi. Hadi sasa jumla ya FADs 77 za mfano zimewekwa katika maeneo mbalimbali. Vilevile Serikali imetoa mafunzo kwa wavuvi wadogo ili waweze kuvua katika Bahari Kuu ambapo hadi sasa jumla ya wavuvi 150 wakiwemo 83 wa Ukanda wa Pwani ya Bahari wa Hindi.
• Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima wakiwemo wavuvi na wafugaji ili waweze kununua zana bora za uvuvi. Aidha, Serikali imeanzisha Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB). Mikopo hiyo inatolewa kupitia vyama vya ushirika ambayo pamoja na majukumu mengine inatoa pia mikopo ya masharti nafuu kwa watu wanaojishughulisha na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. Ili kuweza kukidhi masharti ya kupata mikopo hiyo, Serikali inaendelea kuwahamasisha wavuvi kujiunga katika Vyama vya Ushirika vya Msingi wa Wavuvi ili kuwa na nguvu ya pamoja na kuweza kukopesheka.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA (K.n.y MHE. HASNA S. K. MWILIMA) aliuliza:-
Shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika ni uvuvi lakini nyavu zimekuwa zikikamatwa na kuchomwa moto.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wavuvi hao nyenzo au vifaa vya kisasa vya uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi ili kuwawezesha wavuvi wakiwemo wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika kufanya uvuvi endelevu na wenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeondoa kodi kwenye zana na malighafi za uvuvi zikiwemo engine za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio kupitia Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2007. Aidha, kupitia Umoja wa Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (The East African Community Common External Tariff) engine za uvuvi na malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake kwa maana ya fishing gear accessories 10% na outboard engine 0%) zimepewa punguzo la kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi wakiwemo wavuvi ili waweze kununua zana bora za uvuvi. Hivyo wavuvi wahamasishwe kujiunga katika Vyama vya Ushirika ili kuwawezesha kupata mikopo hiyo.
Vilevile Serikali inatekeleza mpango wa kutoa ruzuku ya zana za uvuvi, ambapo wavuvi wenyewe huchangia 60% na 40% iliyobaki ya gharama huchangiawa na Serikali. Hadi sasa engine 73 zimenunuliwa kupitia mpango huu, nakati ya hizo engine 49 zimelipiwa na kuchukuliwa na vikundi vya wavuvi vilivyokidhi vigezo vikiwemo vitatu kutoka katika Wilaya ya Kalambo na kimoja kutoka katika Wilaya ya Sumbawanga.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Sekta ya Uvuvi ni moja ya maeneo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayaona kuwa yanaweza kukuza uchumi kwa kuongeza Pato la Taifa, kupunguza umaskini na tatizo la ajira.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo Wilayani Kilwa kwa kuwapatia zana za kisasa za uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha wavuvi wadogowadogo wakiwemo wa Wilaya ya Kilwa kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu ili kufanya uvuvi endelevu na wenye tija. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuondoa kodi kwa zana na malighafi za uvuvi zikiwemo engine za kupachika, nyuzi za kushonea, nyavu na vifungashio kupitia Sheria ya VAT ya mwaka 2007.
Vilevile kupitia Chapisho la Pamoja la kodi la Afrika Mashariki engine za uvuvi na malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake zimepewa punguzo la kodi ili kuwawezesha wavuvi kumudu bei za vifaa hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Programu ya Kutoa Ruzuku kwa Wavuvi, Serikali katika Awamu ya Kwanza ilinunua engine 73 na hadi sasa engine 49 zimelipiwa na kuchukuliwa na vikundi vya wavuvi vilivyokidhi vigezo vikiwemo vikundi 27 kutoka Ukanda wa Pwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kuomba Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuhamasisha wavuvi kujiunga kwenye Vyama vya Ushirika vya Msingi ili waweze kunufaika na fursa hii kama wavuvi wengine katika ukanda huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo ambayo pamoja na masuala mengine inaweza kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wavuvi ili kuboresha shughuli zao za kimaendeleo. Kutokana na kuwepo kwa benki hii na taasisi nyingine za kifedha, Serikali inaendelea kuhamasisha wavuvi kote nchini kujiunga katika Vyama vya Ushirika wa Wavuvi ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana za kisasa za uvuvi.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Kwenye bahari na maziwa yetu kuna samaki wa aina mbalimbali kama vile dagaa, furu, uduvi au dagaa mchele na wengine ambao ni wadogo sana.
(a) Je, ni nyavu zenye ukubwa wa size gani zinahitajika kwa ajili ya uvuvi wa aina hizo ndogo ndogo za samaki?
(b) Je, Serikali inafanya utaratibu gani wa kuwapatia wavuvi wa nyavu ndogo ndogo za samaki nyavu zinazohitajika kwa uvuvi huo?
(c) Je, elimu ya kutosha kwa nyavu husika imefanyika kwa kiwango gani hasa kwa wavuvi wanozunguka Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi lenye sehemu (a), (b) na
(c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kila samaki hunaswa kwa kutumia wavu wa aina yake bila kuathiri samaki wengine. Kwa mfano kulingana na kanuni za uvuvi nyavu za kuvulia dagaa baharini zinapaswa kuwa na macho au matundu yenye ukubwa wa milimita 10 na kwa upande wa dagaa wanaovuliwa ziwani ukubwa wa macho au matundu ya milimita nane. Aidha, dagaa huvuliwa nyakati za usiku kwa kutumia mwanga wa taa za karabai.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuwawezesha wavuvi kupata dhana za uvuvi kwa gharama nafuu ikiwa ni pamoja na kuwaondelea kodi katika dhana na malighafi za uvuvi zikiwemo nyuzi za kushonea nyavu vifungashio na injini za kupachika. Aidha, Serikali inaendelea kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi, vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua dhana na vyombo bora vya uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia programu ya utoajiwa ruzuku kwa wavuvi Serikali katika awamu ya kwanza ilinunua engine 73 ambapo hadi sasa engine 49 zimelipiwa na kuchukuliwa vikiwemo vikundi 13 kutoka ukanda wa Ziwa Victoria. Vile vile Serikali imeweka mazingira ya kupata mikopo kwa ajili ya kununua dhana bora za uvuvi kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwatumia Maafisa wa Idara ya Uvuvi na BMUs imekuwa ikitoa elimu ya kutosha kuhusiana na matumizi endelevu ya nyavu za uvuvi kwa wavuvi wanaozunguka Ziwa Victoria na katika maeneo mengine nchini. Aidha, viongozi wa mikoa na Wilaya wamekuwa wakiongelea suala hili katika hotuba zao wanapofanya ziara za kuwatembelea wavuvi katika maeneo yao.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kupiga marufuku uingizwaji wa nyama kutoka nchi za nje ili kuruhusu ukuaji wa viwanda vya nyama nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika baada ya Ethiopia. Aidha kumekuwepo na uingizaji wa nyama ya ng’ombe, nguruwe na kondoo kwa wastani wa tani 2,000 kwa mwaka kuanzia mwaka 2013 hadi 2015. Hata hivyo kiasi hicho kimepungua kuanzia mwaka 2016 tani 1,182.79 na mwaka 2017/2018 tani 1,225 kutokana na kuwepo kwa machinjio na viwanda 23 vyenye uwezo wa kuzalisha tani 44,820.6 za nyama na bidhaa zake kwa mwaka zenye ubora linganifu na nyama inayotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2016/2017 jumla ya nyama tani 2,608.93 yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 5,679,217.28 iliuzwa katika nchi za Oman, China, Hong Kong, Dubai na Vietnam. Vilevile idadi ya machinjio nchini kwa sasa ni 1,632 na yana uwezo wa kuchinja nyama kiasi cha tani 625,992 kwa mwaka.
Pia masoko ya nyama inayozalishwa ndani ya nchi yameongezeka ambapo inauzwa katika hoteli za kitalii, maduka maalum (super markets) na migodi yote nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inafanya tathmini ya kina kuhusu biashara ya mifugo na mazao yake ili kujua kwa uhakika kiasi cha nyama kinachoingizwa nchini, masoko na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuzalisha nyama na mazao yenye ubora na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha, kuchakata na kusindika nyama na bidhaa zake zenye viwango na ubora unaokubalika. Pia, imeweka mapendekezo ya kuongeza tozo ya uingizaji wa nyama na bidhaa zake ili kuleta ushindani wa haki katika soko la ndani utakaowezesha kukua kwa viwanda vya ndani, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa uingizaji wa nyama kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba wizara inaupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kuufanyia kazi na kwa kuzingatia matokeo ya tathmini tunayoendelea hivi sasa.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunikumbusha, naomba isomeke dola za kimarekani 5,679,217.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Mnada wa Magena uliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime una miundombinu yote licha ya kufungwa na Serikali bila sababu maalum na kusababisha adha kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo pamoja na upotevu wa ushuru. Mwaka 2016 aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alitembelea mnada huo na kuagiza mnada ufunguliwe.
Je, ni kwa nini mnada huu wa Magena haujafunguliwa mpaka sasa ili kutoa fursa za ajira na kuokoa mapato yanayopotea?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, na mimi naomba uniruhusu kwanza kukukaribisha kama vile walivyokukaribisha Waheshimiwa Wabunge wenzangu katika Bunge letu tukufu.
Mheshimiwa Spika, niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mnada wa Magena ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani uliokuwa chini ya Wizara ya Kilimo na Mifugo mwaka 1995. Mnada huo ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996 ambapo ulifanya kazi kwa takriban mwaka mmoja, ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na jumla ya shilingi milioni 260 zilikusanywa kama maduhuli ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, ikiwemo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, tarehe 14 Mei, 1997 iliagiza mnada huo ufungwe na kuwapatia wafugaji mnada mbadala wa Mpakani. Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Mkoa wa Mara uliiomba Wizara ya Maendeleo ya Mifugo ya wakati huu ifute mnada wa Magena na Kirumi Check Point iteuliwe kuwa mnada wa mpakani kwa kuwa tayari kuna kizuizi cha Mto Mara.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilikubali ombi la uongozi wa Mkoa wa Mara na hivyo ikaanza kujenga mnada eneo la Kirumi sehemu ambayo kuna kizuizi cha asili cha Mto Mara na ujenzi huu umekamilika kwa asilimia 80 na unatarajiwa kufunguliwa mwaka huu wa 2017/2018. Kwa kuwa kazi ya Kituo cha Polisi inaendelea na kazi ya kuweka umeme katika eneo lile imekamilika.
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Mnada wa Kirumi yameanza kuonekana ambapo Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Mara, kuanzia mwezi Julai, 2016 hadi Februari, 2018 imekusanya jumla ya shilingi 221,270,000 kutokana na vibali na faini mbalimbali za ng’ombe 9,842, mbuzi na kondoo 4,886 kutoka Mikoa ya Rukwa, Kagera, Simiyu, Shinyanga, Mara na Mwanza waliokuwa wakisafirishwa kwenda Kenya bila ya vibali. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-
Je, ule mpango wa Serikali wa kuzalisha vifaranga na kuwapa wafugaji umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali wa kuzalisha na kusambaza vifaranga kwa wafugaji wa samaki unaendelea kutekelezwa kupitia bajeti ya kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea na mkakati wake wa kuimarisha miundombinu ya uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki katika vituo vyake vya Kingolwira (Morogoro), Mwamapuli (Tabora) na Ruhila (Ruvuma) ambapo kwa kipindi cha mwaka 2009/2010 mpaka mwaka 2017/2018 jumla ya vifaranga milioni 21 vilizalishwa na kusambazwa kwa wafugaji kwa bei ya ruzuku ya shilingi 50 kwa kifaranga aina ya sato na shilingi 100 kwa kifaranga aina ya kambale.
Mheshimiwa Mwenekiti, aidha, bei ya vifaranga kwenye mashamba ya watu na taasisi binafsi ni kati ya shilingi 150 hadi shilingi 300 kwa kifaranga kimoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019 Wizara imekamilisha ujenzi wa hatchery ya kisasa ya kituo cha Kingolwira (Morogoro) yenye vitotoleshi 20 vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga takribani milioni 15 kwa mwaka.
Aidha, ni mkakati wa Wizara kujenga hatchery kama hiyo na kufunga vitotoleshi kama hivyo kwenye vituo vya Mwamapuli (Tabora) na Ruhila (Ruvuma) kwa lengo la kuzalisha takribani vifaranga milioni 45 kwa mwaka kutoka sekta ya umma ifikapo mwaka 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika kudhibiti ubora wa vifaranga wa samaki wa kufugwa Wizara imeendelea na mkakati wake wa kuimarisha vituo vyake kwa lengo la kuhifadhi samaki wazazi bora (broodstock) watakao sambaza kwenye hatchery za sekta binafsi zinazotambuliwa na Wizara ili kuongeza uzalishaji wa vifaranga kwa mwaka kutoka vifaranga 14,120,000 (2016/2017) hadi vifaranga 60,000,000 ifikapo mwaka 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kuhamasisha Halmashauri na sekta binafsi kuanzisha vituo vya kuzalisha vifaranga bora vya samaki ambapo vituo 23 vimeanzishwa na kuzalisha takribani vifaranga milioni 20 kwa mwaka na kusambazwa kwa wafugaji. Aidha, ni lengo la Wizara kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi kutekeleza mikakati wa kuongeza uzalishaji wa samaki wa kufuga kutoka tani 10,000 tulizonazo sasa hadi tani 50,000 ifikapo mwaka 2020/2021(Makofi).
MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-
Kumekuwa na changamoto nyingi katika uvuvi wa Ziwa Victoria unaosababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa uvuvi.
Je, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha inamaliza malalamiko hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndilla Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli uvuvi wa Ziwa Victoria umekuwa na changamoto nyingi zikiwemo shughuli za uvuvi haramu uliokithiri ambapo takribani asilimia 90 ya wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi hufanya vitendo vya uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo hivyo ni pamoja na kuvua kwa kutumia nyavu zilizounganishwa (vertical integration), kutumia nyavu za utali/timba (monofilament nets), kuvua kwa makokoro na nyavu zenye macho madogo chini ya kiwango kinachokubalika kisheria cha milimita nane na kadhalika. Aidha, uchakataji na biashara ya samaki wachanga na utoroshaji wa mazao ya uvuvi yakiwemo mabondo na kayobo kwenda nchi jirani bila kuzingatia sheria ni mojawapo ya vitendo vinavyoshawishi uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na vitendo hivyo, Serikali imedhamiria kulinda rasilimali za Taifa kwa kufanya Operesheni Sangara mwaka 2018 dhidi ya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. Operesheni hii ni kweli imeleta malalamiko kwa baadhi ya wadau wa uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kushughulikia malalamiko hayo, Serikali inaendelea kuhamasisha wavuvi, wafanyabiashara, watendaji wa Serikali na wadau wengine wote kufuata sheria na kanuni za uvuvi na kufanya mapitio ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 ili kuendana na mabadiliko ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imetoa elimu na inaendelea kutoa elimu kwa wadau wote kuhusu uvuvi endelevu. Pamoja na kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia wadau katika kuendeleza Sekta ya Uvuvi nchini katika kuchangia ukuaji wa uchumi wetu na wananchi wetu kwa ujumla. Tafiti hizo zinalenga kufanyika katika samaki wa maji ya asili na ukuzaji viumbe katika maji (aquaculture).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kufanya tafiti zitakazopendekeza zana na njia sahihi za uvuvi zisizo na ahari katika uvunaji wa rasilimali za uvuvi. Pia kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi na kuandaa mwongozo wa kuvifanya vikundi hivyo kufanya kazi zake kwa ufanisi ili kutokomeza uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatarajia kufanya semina kwa Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania kwa lengo la kutoa uelewa mpana kuhusu uvuvi haramu na jitihada zinazofanywa na Wizara yetu kupambana na uvuvi haramu kupitia operesheni zinazofanyika zikiwemo Operesheni Sangara, Jodari na ile ya MATT.