Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sophia Hebron Mwakagenda (28 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kabla sijaingia kwenye kuchangia, natamani niwakumbushe Wabunge wenzangu, maana nimeona wakitoa maoni kwamba Wapinzani tulitoka nje siku ya hotuba ya Rais. Waheshimiwa Wabunge, kuna njia nyingi za kufanya advocacy. Tunafahamu fika Bunge letu ni moja ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola, tunapotoka nje, ni pale ambapo umeona hoja ulizokuwa nazo aidha zimesikilizwa au hazijasikilizwa. Hivyo kutoka nje siyo dhambi, ni dalili ya kuonesha hisia na mawazo ambayo tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuzungumzia hotuba ya Mheshimiwa Rais, amezungumza mambo mengi na hata wengine wamesema kwa sababu hatukuwepo hatuwezi kujua ni nini amezungumza. Sisi wote ni wasomi, tunasoma habari za Vasco da Gama lakini hatukuwepo na tunanakili kwenye mambo mbalimbali. Tumesoma mambo ya Hitler tunayatumia na hatukuwepo wakati wa uongozi wake. Vivyo hivyo habari hii itasomwa na sisi, itasomwa na watoto wetu wa sasa na vizazi vijavyo. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Rais ilikuwa ni nzuri kama walivyosema wengine tatizo naloliona ni utekelezaji. Nitajikita katika mambo ya uchumi aliyoyazungumzia hasa katika ukurasa ule wa 19. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika tunapozungumzia kukuza uchumi wa viwanda, nchi ambayo wasomi hatujawaandaa kuwa wabunifu, hatujawaandaa kuwaweka katika hali ya utendaji kazi, inakuwa shida.
Tunapozungumzia uchumi kilimo chetu ambacho watu wengi ni wakulima kwa asilimia kubwa, mazao wanayoyalima hatujajua ni jinsi gani ya kuwapelekea viwanda hivyo kwenye sehemu husika. Binafsi siamini kwa maana najua Magufuli ni mtu mmoja, mfumo wa Magufuli
ndiyo uliooza, atawezaje kufanya kazi peke yake? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza mengi na amezungumzia habari ya Katiba. Katiba ndiyo mama na mimi nilifikiri siku 50 za kwanza za Urais wake angeanza na Katiba.
(Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ametamka na namnukuu, anasema, Katiba ni kiporo. Unapozungumzia kiporo kinaweza kikawa kizuri au kikakuharibu, kikawa kimechacha. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Rais, Katiba ndiyo msingi wa kila kitu. Hata viwanda hivyo na huu uchumi tunaouzungumzia pasipo Katiba hiyo hatutaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado naendelea kujikitia kwenye uchumi, amezungumzia wajasiriamali wadogo, amezungumzia wanawake na vijana ambao ni kundi kubwa sana lililosahaulika. Tunawezaje kuwaunganisha wanawake hawa na viwanda endapo elimu yao ni
ndogo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, tunafahamu tuko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mheshimiwa Rais sijaona akizungumzia ni jinsi gani tutajua masoko haya ya watu wachache ambao ni wajasiriamali, wakulima wadogo, wataingiaje katika masoko hayo na kuweza kufaidika na Jumuiya hii ya Afrika Mashariki?
Mheshimiwa Naibu Spika, sijaona akizungumzia muunganiko wa vijana kujiajiri katika uzalishaji mali. Tunapokwenda kwenye viwanda, kama ni kilimo wanawezaje kujiunganisha na viwanda hivyo anavyovisema? Ndiyo maana nasema nina wasiwasi na suala hili la viwanda
analolizungumzia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii imeelezea mambo mengi yanayofurahisha kwa kuyasikia lakini nafikiria, wakulima na hivyo viwanda anavyovisema, nikizungumzia Jimbo la Rungwe Magharibi kuna wakulima wa chai. Wakulima wale wanapunjwa, wanauzia makampuni binafsi kwa bei ndogo ambayo wawekezaji hao wanafanya kwa manufaa yao na kibaya zaidi wanashirikiana na watu walio katika madaraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia viwanda, Kiwanda cha Chai cha Katumba ambacho kinaweza kutoa ajira kwa vijana wengi tumekisaidiaje kukipelekea ruzuku na kusaidia wananchi wa mji ule? Kuna viwanda vingi, Mbeya Mjini kulikuwa kuna ZZK, leo hii imekuwa ni
ghala la kuwekea pombe. Tunawezaje kusaidia vijana wetu kupata ajira? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni vyema Mheshimiwa Rais akatazama ni jinsi gani tutafufua viwanda vilivyokuwepo. Watu waliovifilisi pia wapo, tunawezaje tukarudisha vile viwanda vilivyouzwa kwa bei rahisi kwa watu ambao wamefanya maghala? Nadhani Mheshimiwa Rais angeanzia majipu ya aina hiyo kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria nyingi kandamizi kwa mfano Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, watoto wadogo tunasema wanapata mimba lakini sheria haiko sawa. Kabla hatujaenda kwenye mtazamo wa maendeleo lazima tubadilishe sheria kandamizi na nyinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria za kodi ndogo ndogo zinazowatesa wananchi tunazibadilishaje? Tunawaunganishaje wananchi kuingia katika uchumi na tukasema uchumi wetu umekua, jana tulikuwa tunaambiwa uchumi wetu umekua, kivipi? Tunawianishaje kukua
kwa uchumi mnaozungumza Serikali na maisha ya mwananchi wa kawaida, tunayazungumziaje? Tuondoe siasa tuweze kufanya kazi. Magufuli anayo kazi kwa sababu watendaji wake ni walewale, pombe mpya kwenye chupa ya zamani. Namwonea huruma na sijaelewa atafanyaje kazi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao vijana wengi ambao mpaka leo hii tumeanza kufanya marekebisho mbalimbali, kwa mfano gesi, je, Serikali imepeleka vijana hawa kusoma? Wako wachache tena wa wakubwa mnawapeleka Ulaya, kwa nini msichukue mtaalam kutoka Ulaya
akaja kufundisha watoto kwa wingi hapa Tanzania? Kwa hiyo, kuna vitu vingi tunahitaji kurekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia amezungumzia haki, ataangalia makundi ya wazee, walemavu, hakuna haki kama hakuna Katiba bora. Tunaposema haki tunamaanisha ni lazima anayestahili haki apewe. Ndugu zangu wengi wamezungumza mambo ya Zanzibar na
mengine lakini kuna haki ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), hatuoni ni jinsi gani wakisaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema haya, nafikiri kuna haja ya makusudi kabla hatujaendelea na safari hii tuanze na Katiba, tena siyo pale ilipochakachuliwa, tuanze na Katiba ya Warioba, tuanzie pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Bodi ya Ithibati, bodi hii imependekezwa kwenye kifungu cha 10(1) cha Muswada. Binafsi naona haijahusisha wadau kwa upana zaidi hasa kwa kuwaingiza wanahabari na wamiliki wa vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri wajumbe hao saba wachaguliwe na wanahabari na Waziri awapitishe. Waziri kapewa majukumu makubwa sana hata kuna maneno “Idhini ya Waziri” yaliyopo kwenye kifungu cha 14(1) na badala yake kuwepo na kifungu cha 14(3) ambacho kinasema “Waziri anaweza kuagiza bodi kurudia mchakato wa kuchagua Mkurugenzi Mkuu ikiwa kutakuwepo na uvunjifu wa kifungu 14(2).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia Wizara hii katika maeneo matatu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, uundwaji wa vikundi vya kijamii (SACCOS). Mpaka sasa ni vikundi vichache vimeweza kusajiliwa kutokana na uelewa mdogo na kutotembelewa na wahusika kwa maana ya viongozi wa ushirika kutoka katika Halmashauri zetu. Mpango huu wa kusaidia vijiji shilingi milioni 50 binafsi najua kuna vikundi havitakuwa na sifa kutokana na ugumu huo wa usajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni habari. Kama nchi tume-sign mikataba mbalimbali ya haki ya kupata na kutoa habari kwa wananchi. Masikitiko yangu ni kwamba, Serikali imezuia vyombo binafsi kuonyesha, kuandika shughuli za Bunge zinazoendelea kwa kigezo cha kuwa na Bunge TV ambayo kimsingi haionyeshi na kama inaonyesha, inaonyesha kwa upendeleo. Isitoshe kuna magazeti yamefungiwa na kama Bunge halijajua makosa yao ili vyombo vingine vijifunze. Nashukuru kuleta Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari, labda utaleta uhuru katika habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni mawasiliano. Tumekuwa na vyombo au Makampuni mengi ya Simu, lakini wasiwasi wangu ni gharama zinazotozwa kwa wananchi. Gharama zinaongezeka katika ununuaji wa vocha na wananchi wengi hawana ujuzi wa kitaalam na kupelekea mwananchi wa kawaida kulipia gharama kubwa sana bila uangalizi wa wataalam watetezi wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni uingizwaji wa simu feki unaofanywa na wafanyabiashara wachache na kujinufaisha na kuacha wananchi wanaathirika kwa ubovu wa simu hizo na hata hasara ya kuharibika baada ya muda mfupi. Nashauri TBS na wadau wanaolinda haki ya mlaji wafanye kazi yao kwa faida ya mwananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ni masoko. Tumeingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, sijaona kama tumeandaa wananchi wetu hasa wanawake kuingia katika ushindani wa soko. Pia wananchi hawana elimu ya kibiashara hasa ya utalii ukilinganisha na jirani zetu ambao ni washindani wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Rungwe Mashariki ni moja kati ya Miji inayozalisha mazao mengi ya chakula na biashara, lakini tumekuwa na tatizo la masoko na kupelekea mkulima kupata kipato kidogo na kibaya zaidi wanaofaidika ni Madalali ambao wanachukua pesa nyingi kuliko mkulima mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu; tujengewe soko kuu la mazao haya ya ndizi na chai, kwenye chai mkulima ananyonywa kwa kupangiwa bei hasa kwa kutokana na kutokuwa na ushindani katika soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbolea imekuwa tatizo kubwa hasa mawakala wengi sio waaminifu na kupandisha bei mazao kama kahawa yalikwisha kwa kukosa motisha kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, mageti ya mazao ni kikwazo kikubwa kwa wakulima wadogo kwani tozo zimekuwa kubwa sana zisizo na ulinganifu katika utozaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi katika Ziwa Nyasa unatoa samaki bora sana ambao ni kivutio cha walaji wengi. Ningependekeza Wilaya ya Kyela itengewa pesa ya kutosha juu ya utunzaji wa mazalia ya samaki na kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la maziwa; Wilaya ya Rungwe ina mazao ya maziwa kwa wingi, ni lini Wizara itasaidia upatikanaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao haya ili kuongeza thamani ya mazao haya na kupata faida katika mapato ya Halmashauri na ya mmoja mmoja katika jamii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA Wilaya ya Rungwe; Katika Wilaya ya Rungwe hatuna chuo cha ufundi na hii inatupa shida sana katika kuwaendeleza vijana wetu waliomaliza Darasa la Saba na Kidato cha Nne. Rungwe ni Wilaya yenye kutegemea kilimo sana hivyo uanzishwaji wa VETA kutasaidia vijana kujifunza elimu ya usindikaji wa mazao, ufundi wa kutumia mzao kama mahindi, migomba majani yake na kuwezesha kupatikana ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabweni Wilaya ya Rungwe, upatikanaji wa mimba za utotoni ni shida sana katika Kata za Kyimo Masukuru. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuwezesha Halmashauri ziweze kujenga mabweni ili kupunguza vishawishi, ulinzi kwa watoto wa Kata hizi. Nashauri Mkoa mpya wa Songwe upatiwe umuhimu wa kuanzisha vyuo, vikiwemo vya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Chuo cha Ualimu Mpuguso. Majengo ni chakavu kabisa idadi ya wanafunzi mabwenini siyo nzuri, miundombinu haifai, vitabu havitoshi kabisa. Pia shule ya sekondari Ndembela, Halmashauri imekuwa na deni la shule ya sekondari Ndembela takribani milioni 700 toka kanisa la Adventista Wasabato barua ya maelezo ya msaada ipo katika Wizara ya Elimu mimi nakumbusha Wizara ione umuhimu wa kulipa deni hilo na kuweka commitment kulibeba deni hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, posho na nauli za walimu. Walimu wamekuwa na madeni mengi sana Serikalini, pesa zao za likizo na nauli wafanyapo kazi nje ya kituo wengi wamekopwa na Serikali kwa muda mrefu sana. Kupandishwa madaraja pia imekuwa tatizo kwa walimu kukaa muda mrefu sana na pesa zao za uhamisho pindi wakipata uhamisho posho hizi zilipwe haraka.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii. Nafikiri sitakosea kama mwenzangu aliyetangulia.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, naomba ni-declare interest kwamba mimi nimezaliwa katika quarter za Jeshi...
TAARIFA
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.......
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, uko sahihi kwa sababu na wewe umelizungumzia. Naomba ulinde muda wangu. Naendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, nimezaliwa kambini, Jeshi ninalolijua nikikua lilikuwa ni Jeshi makini kwa maana ya kipato. Wazazi wetu walituzaa wengi kwa kuwa walikuwa wakiishi maisha mazuri, walikuwa wakipata mishahara mizuri, tulikuwa tukipata ration kwa wakati na vitu kama hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jioni ya leo naomba nichangie. Tukiangalie bajeti iliyopita, ndugu zetu pesa za maendeleo walichangiwa shilingi bilioni 220 kama sikosei, lakini Serikali iliwapatia shilingi bilioni 40 au 41. Mimi najiuliza, watawezaje kuishi maisha mazuri tuliyoishi zamani kama Bunge imepanga na imepitisha hiyo bajeti na haijaweza kufika kwenye Jeshi waweze kufanya mambo ya maendeleo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia mambo ya maendeleo, tunazungumzia makazi. Wanajeshi wanahitaji nyumba nzuri za kuishi. Ni kweli tumeona, tumetembelea miradi, kuna nyumba zipo zinajengwa, lakini hazitoshelezi. Ninashauri Bunge linapopitisha bajeti tuhakikishe zile pesa zinakwenda kutimiza ahadi tuliyoahidi, wataenda kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Wananchi kama tunavyolisifia, ni Jeshi linalohitaji kuilinda nchi yetu, mipaka ya nchi, lakini pia tunafahamu umuhimu wa chombo hiki; kama tunashindwa kuipatia pesa kwa sababu zozote zile, tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe Wabunge. Shilingi milioni au shilingi bilioni 41, ni miradi gani wafanye, ni miradi gani waache?
Mheshimiwa Naibu Spika, siasa ni nzuri, lakini tusifanye siasa kwenye vyombo vya ulinzi. Tunapozungumzia bajeti; na hii naizungumzia kwa Wizara nzima, nikimaanisha Polisi, Magereza na Jeshi wenyewe. Pesa wanazopata tuhakikishe zikipitishwa kwenye Bunge hili zikafanye kazi sawasawa na tulivyoahidi. Walipata pesa nusu karibu shilingi bilioni 600 hazikwenda kutenda kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafika mahali na wengine wameshasema, hawa ni binadamu, wanaweza wakaingia tamaa kwa sababu wakiishi vibaya hawawezi kusimamia uadilifu waliokuwa nao. Ni kweli tutawasifia, lakini ipo siku wanaweza wakaenda pembeni kwa sababu hatujawajali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba Mkuu wa Majeshi leo yupo. Wanawake walioko Jeshini, najua kwamba kuwa mwanamke siyo kwamba huwezi kufanya vizuri. Ninaamini wapo wanawake wenye vyeo, ila ninatamani na ninamwomba ikibidi wanawake waongezwe vyeo, siku moja tuwe na CDF mwanamke na sisi Tanzania tuonekane tumesonga mbele. Ninaamini vyeo kuanzia chini vipo, naomba mchakato wa kuwapandisha vyeo ufanyike sawa sawa na utashi wa kazi wanazofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi letu ni mahiri na wenzangu waliotangulia wamezungumzia habari ya Zanzibar. Sitazungumzia huko ila nina swali la kiufahamu; siku za hivi karibuni nimeona viongozi wa kisiasa waliokuwa ni wastaafu wa Jeshi wakiapa kwa kuvaa nguo za Jeshi. Naomba nielezwe ni utaratibu wao au ni kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa mdogo, niliona Mheshimiwa Rais Nyerere wakati wa vita vya Idd Amini akiwa amevaa kombati na nguo za mgambo. Nafahamu kuwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa Luteni; mpaka anastaafu sijawahi kumwona amevaa nguo za Jeshi. Sijui nimeshau kama ni Kanali au hivyo! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamishwe, inawezekana sifahamu, siku za karibuni Mheshimiwa Rais wetu amevaa nguo za Jeshi. Najua yeye ni Amiri Jeshi Mkuu, hilo nalifahamu, lakini sikuona begani kama amewekwa cheo chochote.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekezwe, utaratibu ukoje? Najua ni Amiri Jeshi Mkuu, lakini begani sikuona cheo chochote. Je, ni sahihi?
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba, vitu vingi ni ufahamu; ni suala la kuelekezwa. Inawezekana ilitakiwa ifanywe na Marais waliopita, lakini hawakutaka, lakini kama ni utaratibu, tuelekezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, Wizara hii inahitaji sana pesa na hasa maeneo ya viwanda. Tunafahamu kwamba Awamu ya Tano mnazungumzia viwanda na jeshi hili lina viwanda; naomba bajeti hii, iongeze pesa kwenye maeneo ya viwanda vya Jeshi. Tukiiongezea pesa tunaomba Serikali badala ya kuagiza vitu vya Kichina, tununue kutoka kwenye Jeshi. Wale wanaopata ten percent wakati huu wasiweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwa kumalizia, Jeshi hili linafanya biashara, mbalimbali na ukusanyaji wa maduhuli. Ushauri wangu, maduhuli haya kwa miaka hii miwili tungeweza kuwaachia iweze kuwasaidia bajeti zao. Nasema hivyo, ninajua Serikali haina hela. Bajeti imeshuka, tukiwaachia maduhuli kwa miaka hii miwili waweze kufanya kazi zao vizuri, itatusaidia kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopitisha bajeti, hatupitishi kishabiki, tunapitisha tukimaanisha ujenzi wa Taifa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, maduhuli ya Jeshi yabaki kwenye Jeshi kwa miaka miwili. Ikipita miaka miwili, tutaendelea na utaratibu mwingine, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, ninaipinga bajeti hii kwa asilimia mia moja kabla sijachangia. (Makofi)
Kwanza kabisa naomba nitoe masikitiko yangu kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mchana huu kusitisha wanakijiiji wa Mpuguso wasiendelee kujenga zahanati ya nguvu ya wananchi. Ikumbukwe kwamba Waziri wa Afya alipita na akaona wanakijiji akawaeleza waendelee kujenga kwa sababu aligundua kuna ufisadi unaofanywa na watu wa Halmashauri ya Rungwe Magharibi.
Ndugu zangu, binafsi ninaona Taifa kama linayumba, linayumba kwa sababu ya kutetea vyama na Wabunge tuko mahali hapa kutetea haki za wananchi, vyama tumeviacha milango lakini masikitiko yangu ni kwamba imekuwa hali ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika Waziri Mkuu hayupo, nilitaka kumwambia wanaopiga makofi wengi wapo zaidi ya miaka kumi katika jengo hili, walipitisha bajeti zilizopipita, wengine waliandika risala za Rais aliyepita, leo hii wanajinasibu kusema uongozi uliopita ulikuwa haufai, kana kwamba uongozi uliopo sasa umetoka mbinguni na wao ni moja ya viongozi waliokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalendo unaumbwa kwenye nafsi na uoga ni dhambi. Ukiwa kiongozi mwoga huitendei haki nafsi yako binafsi, huitendei haki kizazi kinachokuja na ni aibu kwa Taifa unaloliongoza. Leo hii tunazungumzia maendeleo, ni maendeleo gani yanaweza kufanyika pasipo utawala bora? Kama Mkuu wa Mkoa, kwa matakwa yake binafsi na utashi wa chama chake anaweza kuzuia zahanati inayotaka kusaidia wanawake wanaojifungua kwa shida, wapate sehemu murua ya kujifungulia anazuia kwa mantiki ipi na kasi ipi mnayoizungumzia ya hapa kazi tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku tutapita, walikuwepo watu walipita, na wengine mko humu mlikuwa Mawaziri leo mko pembeni. Nchi hii ni yetu sote, nchi hii tulizaliwa hapa, tuko hapa; mnazungumzia habari ya tv, mimi ni mtoto wa uswahilini, leo niko kwenye Bunge hili sikuwepo Bunge lililopita lakini nilichaguliwa, jambo la msingi tumesaini mikataba ya nchi mbalimbali ya haki za binadamu ndiyo maana tunadai tv, siyo kuonesha sura zetu, kama ni sura zinafaamika kwa waliotuoa, wanaotupenda, ndugu zetu, sura zetu wanatufahamu. Tunachosema ni haki ya msingi tunapozungumzia utawala bora ni haki ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Ndugu zangu TAMISEMI, walimu wanadai madeni, tumewakopa walimu, walimu hawajalipwa mishahara, wengine fedha za likizo kwa muda mrefu, tumewakopa. Bajeti iliyo mbele yetu haioneshi kama inaenda kulipa madeni, na walimu wako wengi katika Taifa hili. Unataka kutengeneza Taifa la viwanda, usipomtengeneza mwalimu ni nani ataingia katika hivyo viwanda? Walimu hawana nyumba, mmeeleza idadi ya nyumba mlizojenga lakini nyumba ni peanut, ni nyumba chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe serious, tusifanye sanaa kwenye maisha ya watu, tusifanye sayansi kwenye maisha ya watu. Mimi nakubaliana kwamba kama nchi iliharibika, nilitegemea Serikali ya Awamu ya Tano itangaze janga la Taifa kwamba tumeingia hatuna fedha, mafisadi wamekula fedha, tunaanza sifuri tujifunge mkanda, ningewaelewa, kuliko kujidanganya kwamba tuna fedha wakati tuna madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wametukatia fedha za msaada ndugu zangu, Mwalimu Nyerere aliwaaminisha wananchi wakati wa vita vya Kagera, wananchi walimwelewa, wengine walitoa mali zao kusaidia Taifa. Namshauri Mheshimiwa Rais Magufuli kutangaza hali ya hatari, tangaza hali ya hatari kwamba Taifa halina fedha. Tuweke vipaumbele vichache, vitakavyotekelezeka, wananchi watatuheshimu, kuliko kusema tuna fedha nyingi TRA inakusanya fedha nyingi wakati mnajua ni madeni. Mtu unayemdai akikulipa mwisho wa siku analipa nini siyo ameshalipa? Tutabaki kwenye sifuri.
Mheshimiwa Mwenyeketi, vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri kuna mianya mingi sana ya upotezaji wa fedha, ninashauri tujikite kukusanya fedha vizuri, tuache siasa. Halmashauri zilizoshinda kwa vyama pinzani zipewe msukumo wa kuendeleza kazi na zilizoshinda kwa CCM zifanye kazi kwa faida ya wananchi. Ubabaishaji wa vitisho vya Wakuu wa Wilaya wanaoingia kwenye Halmashauri za Madiwani sijui kwa vifungu ngani na kuwatisha baadhi ya Madiwani sidhani kama ni muafaka kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mmetukejeli sana na mkasema hatutaki kuchangia tulinyamaza, tunapochangia mnatuwekea miongozo, mwisho wa siku Taifa ni letu sote, Taifa ni la Watanzania, ninyi siyo malaika na wala tusimfanye Rais kama hirizi, kila kitu Rais, Rais ni Taasisi inawategemea ninyi mkiwa waaminifu mtamsaidia Rais kutimiza ndoto zake. Leo hii Rais hata kama anafanya vizuri yuko peke yake, ninyi wengine...; potea mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wengine ni kama wapambe ninaomba mbadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Tanzania mpya tutaitengeneza sisi, Tanzania mpya haitatusaidia tukipeana vijembea au kwa mabavu, ninaomba tujitafakari kama Taifa, tutetee Taifa letu wala siyo matumbo yetu, tutetee wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya siungi hoja kwa asilimia mia moja na naendelea kusema siku moja ukweli huu utajulikana. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matatizo makubwa nchini juu ya ulipaji wa fidia kwa wananchi pale Serikali inapotoa/kuchukua ardhi kwa maendeleo na kuwa kero kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya jeshi yamekuwa na migogoro kwa jeshi kutokuwa na hati za ardhi zao na wao kusema wamevamiwa na wananchi. Nashauri majeshi yote Polisi, Magereza na JWTZ wapewe hati miliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba (NHC); nashauri mikataba yote ya nyumba iliyoingiwa na NHC na wawekezaji wengine ikaguliwe upya. Wasiwasi wangu imekabidhiwa kwa mkataba wa muda mrefu na kwa gharama kubwa mpaka Serikali itakapopata faida itakuwa ni miaka mingi.
Kuhusu maeneo ya wazi, Wizara ikague na kuwanyang‟anya wale wote waliopewa maeneo ya wazi na kuyarudisha kwa wananchi. Maeneo mengi ya michezo na kupumzika yametekwa na waporaji wachache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa ardhi. Halmashauri nyingi zimekuwa zinatoa tender kwa wadau kuweza kupima viwanja, nadhani ni kuiibia Serikali mapato yake na kuongeza gharama kwa wananchi. Ninachoomba Wizara ipewe pesa ya kutosha kuweza kusaidia huduma hii kuendelea na kufanya kazi zake kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ofisi za kanda; kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi katika mikoa hasa ya wakulima na wafugaji na maeneo ya vijijini mfano Kijiji cha Mpuguso, Wilaya ya Rungwe, wamenyang‟anywa ardhi yao ya kijiji na kujenga zahanati huku wakiwa na hukumu ya halali lakini bado wako kwenye usumbufu. Hivyo, naomba wahusika hasa ofisi ya kanda ifanye kazi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iwe makini kwa hati zinazotolewa kwa wawekezaji ambao wengi wanaingia na gear ya kuoa Watanzania ili waweze kupata ardhi. Kwa kushirikiana na Uhamiaji Wizara inaweza kuwabaini wawekezaji hao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vivutio Wilaya ya Rungwe; Wilaya ya Rungwe ina vivutio vingi sana ikiwepo Ziwa Ngozi, Mlima Rungwe, Daraja la Mungu, Kijungu na vivutio vingine vingi sana. Tatizo Wizara haijasaidia kutengeneza miundombinu ya kuwezesha watu kuja kutembelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Ngozi limeachwa chafu na kutoa tozo ndogo ambayo haiwezi kuleta maendeleo yoyote. Halmashauri zetu hazina pesa ya kuwezesha kutangaza vivutio hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu misitu; Wilaya ya Rungwe tuna misitu ya kienyeji ambayo kiuchumi haina faida kwa wananchi wa kawaida. Vyura wa Kihansi tunaomba vyura hawa warudi Tanzania na nchi ya Marekani ilipe gharama kwa kukaa nao kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina na meno ya tembo; kumekuwa na wimbi la Wachina hapa nchini wakikutwa na nyara za Serikali hasa meno ya tembo, swali langu Serikali inachuakua hatua gani ya kisheria kwa wananchi hawa, je, toka wameanza wamekamatwa wangapi na wamefungwa miaka mingapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upandaji miti na nyuki ninaomba Wizara chini ya kitengo cha upandaji miti kunisaidia miche ya kupanda kwa makundi ya vijana, katika Wilaya ya Rungwe na Mkoa wote wa Mbeya. Pia mgogoro wa wafugaji Wilayani Mbarali, je, Serikali itaumaliza lini?
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo kimepungua hadi 2.7% wakati malengo yalikuwa kikue kwa 6%. Hii inaleta wasiwasi hasa kwa wanawake ambao ni wengi katika sekta hii. Sekta hii ni muhimu sana kwani wanawake ni wadau wakubwa sana na mpango huu umejikita kwenye viwanda, hivyo kilimo kiwekewe kipaumbele cha 100% ili kiakisi na viwanda na wakati huo kitaleta tija kwa viwanda vyetu. Maskini wengi wako vijijini ambapo wengi ni wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumuko wa bei; mwaka 2011 mfumuko wa bei ulikua kwa 19.8%, mwaka 2015 ulishuka kufikia 5.6%, hii ilikuwa sawa lakini kwa sasa imefikia tena 19% na kuleta mkanganyiko kwa jamii maskini. Mfumuko wa bei una madhara mengi kwa jamii hasa wanawake. Nashauri mfumuko ubaki kwenye tarakimu moja kwa kadri inavyowezekana na ikibidi wanawake wakingwe kwa gharama yoyote. Iwepo mipango mahsusi ya kupeleka maendeleo kwa wanawake kwenye vikundi vyao mbalimbali ili kuweza kuzalisha mali kwa maendeleo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nguvu kazi ya utaalam; kuna upungufu mkubwa wa takwimu zilizochambuliwa kwa mtazamo wa kijinsia. Maeneo ya miradi mikubwa ya kiuchumi kama miradi ya Mchuchuma na Liganga ingepewa watu mahsusi na kuzingatia jinsia kutoa wataalam.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Ofisi ya Makamu wa Rais ipatiwe bajeti yake yote ili iweze kutimiza kazi zake kiukamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uchaguzi Zanzibar, Serikali ya Muungano haitaki kuiacha Zanzibar huru ifanye kazi zake kwa matakwa yake bali Tanganyika inaingilia chaguzi na hata maamuzi ya Wazanzibari hapa na pale. Inaendelea kuikandamiza CUF katika utendaji kazi za kisiasa na kero za Zanzibar bado mpaka sasa zinasuasua na sina hakika kama ziko tisa .
Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa raia toka uchaguzi wa mwaka 2015 Zanzibar haiku shwari kwani ule umoja wa Wazanzibar kwa sasa haupo baada ya kuwa na makundi mawili mahasimu wa kisiasa yaani CCM na CUF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi na wananchi waliumizwa katika marudio ya upande mmoja wa CCM na kuweka ari ya sintofahamu kwa raia baada ya Jeshi la Polisi na JKU kutanda mitaani na kutishia raia. Huu si utamaduni wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katiba mpya; ni wazi tumepoteza pesa nyingi sana kwa kuanzisha mchakato huu kwani matakwa ya wananchi hasa ilipotokea kuachwa kwa rasimu ya katiba ya Mheshimiwa Warioba ambayo CCM iliacha na kutengeneza rasimu isiyokuwa na matakwa ya wananchi. Naomba tuanzie pale wananchi walipotaka kwenye katiba ya Warioba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi za kusingiziwa; kumekuwa na mashtaka ya kubambikiwa kesi katika Serikali ya Muungano hasa kwa wafuasi wa CUF. Tunaomba Wizara hii ichukue nafasi yake ya upatanishi na kusimamia haki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa Madaraja; nashauri Serikali na Wizara hii kuweka kipaumbele cha ujenzi wa madaraja yaliyo katika mipaka ya nchi hasa Malawi kwani hakuna madaraja yatakayoweza kusaidia tukipata dharura kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usumbufu kwa magari katika mpaka. Kumekuwa na usumbufu wa foleni ndefu katika mipaka hasa magari makubwa ya usafirishaji ya transit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vya Uokoaji. Kumekuwa na uhaba wa vifaa vya uokoaji majini hasa katika boti katika ziwa Tanganyika. Tunaomba Wizara ihakikishe inaweka vifaa hivyo kwani waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ni kidogo katika Halmashauri ya Rungwe. Katika Wilaya ya Rungwe hakuna fedha za ujenzi/ukarabati wa barabara za ndani wakati Halmashauri hii ni muhimu kwa mazao ya chakula yanayozalishwa hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, TBC. Televisheni ya Taifa haifanyi matangazo kwa usawa hasa inapochukua matangazo ya kisiasa kwa uwiano sawa na vyama vingine. Pia TBC ijikite kutoa elimu ya uraia na mendeleo zaidi katika vipindi vyake badala ya kuweka vipindi vya muziki kwa muda mrefu zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee viwanja vya michezo mikoani. Katika Mkoa wetu wa Mbeya hatuna viwanja vya kutosha vya michezo vinavyoweza kusaidia watoto wetu kujifunza michezo na kukuza vipaji kama mjuavyo Mbeya na viunga vyake bado vinatoa wachezaji bora wa michezo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niongelee viwanja vya wazi. Viwanja vingi vimetaifishwa na watu wachache bila kuchukuliwa hatua za kisheria na kurudisha viwanja hivyo kwa wahusika ikiwemo Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, vazi la Taifa. Ni lini vazi la Taifa litakuwa tayari katika utekelezaji wa utumiaji huo. Kama Taifa tunahitaji utambulisho wa vazi letu.

Mheshimiwa Spika, sasa niongelee kuhusu timu ya mpira wa miguu. Tumekuwa jamii na Taifa la kushindwa kila wakati kwa Wizara kutowekeza zaidi katika timu hii, lakini Wizara kutosimamia miundombinu/aina ya namna ya kupata wachezaji bora toka sehemu mbalimbali ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, mwisho niongelee suala la ufungiaji wa wanamuziki. Siku za hivi karibuni Serikali imekuwa inawafungia waimbaji wa nyimbo za bongo fleva kwa kile kinachodhaniwa hakiwafurahishi watawala. Hii inaondoa ubunifu na hali ya wasanii kuimba hisia zao kwa usahihi. Serikali itumie ofizi zake kama BASATA kuwasimamia wasanii hawa kufuata kanuni na haki za wasanii bila kubagua na kupendelea kwa kutumia hisia za kisiasa tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu utalii katika Jimbo la Rungwe. Tuna utalii katika Wilaya ya Rungwe ambao Serikali haijaweka mkazo katika uendeshaji wake na kuisaidia Serikali kuongeza mapato. Vivutio hivyo ni Daraja la Mungu na Lake Ngozi, vivutio hivi havina miundombinu ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutangaza utalii nje ya nchi. Serikali iongeze pesa katika Wizara hii ili tuweze kujitangaza na kupata wageni wengi hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Kitulo haitatunzwa na Serikali kwa kupeleka pesa kidogo hivyo nashauri pesa zitengwe za kutosha kuweza kuitunza hifadhi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu yetu, tunaomba Serikali itoe vibali kwa wazawa ili kuweza kuuza nje ya nchi miti na mazao yake na hivyo kuweza kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na hatimaye wa Taifa.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijachangia ninaunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani, nafikiri ripoti yetu iko sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoendelea nataka nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, nafahamu amefanya kazi kwenye NGO’S, hiyo peke yake inamsaidia kum-shape na kumfanya akafanya kazi vizuri ikaweza kumsaidia kidogo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia na Wabunge wenzangu wengi wamezungumzia matatizo ya mimba za utotoni. Tumepiga kelele tukijua kwamba mimba za utotoni janga la Taifa hili, kila Bunge linalopita tunazungumzia habari hii. Ndugu yetu amepeleka kesi Mahakamani ameshinda lakini Serikali imekata rufaa. Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kuweka alama katika Wizara yako tusikubali sisi kama wanawake, kwa namna yoyote, iwe ya dini, iwe ya mila, itakayopelekea watoto wakapata shida katika umri mdogo na kupewa mimba. Ninaomba tupambane na tukubaliane kabisa, hatutakubali watoto wetu wakiolewa, sasa hivi inafika mpaka miaka tisa watoto wameingizwa kwenye ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupongeza pia kwa kuanzisha kanzidata katika Wizara yako kwa upande wa mambo ya kijinsia, nafikiri hilo ni suala la kukupongeza. Bado kuna shida, tunapofanya udahili, kwenye hotuba yako ukurasa wa 81 umeelezea jinsi tutakavyofanya udahili wa wanafunzi katika Vyuo vya Udaktari, watoto wa kike ambao tumewashawishi wasome sayansi wanapokuwa vyuoni hawana pesa za kulipia mikopo japokuwa wanafanya vizuri darasani na tunajua kabisa tuna uhitaji mkubwa sana wa madaktari katika Taifa letu. Ukienda Chuo cha Kairuki kuna wasichana wameacha shule mwaka wa pili kwa kushindwa kulipa ada za masomo yao. Tunawezaje kusaidia wanawake hawa na Wizara hii kama ni Wizara husika ikawasaidia wasichana wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kukumbusha, Wizara ikahamasisha uanzishwaji wa nyumba salama (safe home), hizi nyumba salama zitasaidia wasichana wadogo, wanawake ambao wamefanyiwa ukatili wa kijinsia wakati wakishughulikiwa masuala yao, wapate sehemu sahihi ya kusubiri, wakati mambo yao yakishughulikiwa. Ninafikiri Wizara hii ni wakati muafaka sasa wa kuhamasisha. Kuna wadau binafsi wamejitokeza na wameanza, nachukua nafasi hii kumpongeza huyu Dada Janeth Mawinza wa Mwananyamala, yeye amejaribu kuwa na safe home kwa ajili ya wale akina mama wanaopigwa au wale wasichana ambao wanafanyiwa ukatili na baadaye wakaenda wakawahifadhi. Wizara lazima mtambue watu kama hawa, lakini ni wajibu wenu wa kuanzisha vituo kama hivi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la wanawake na uchumi. Hii Wizara inazungumza mambo ya wanawake na kuwatetea. Leo hii tunazungumzia Benki ya Wanawake binafsi nimefanya kazi na Benki ya Wanawake. Mwaka jana Mheshimiwa Ummy ulimwambia Meneja atoe maelezo jinsi gani anafanya kazi, sasa sikujua kama ni siasa au alikupa maelezo na wananchi haujatupa mrejesho ulifikia wapi. Benki hii ina-charge kama benki za kawaida. Inatoa riba kubwa kama benki za kawaida, jina lake ni tofauti na matumizi ya wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Mbeya benki hii ina mawakala, lakini Mikoa kama Mbeya, Mwanza, Mikoa mikubwa lazima ingekuwa na matawi makubwa na kuweza kusaidia wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wengi wamezungumza vijijini ambako kuna asilimia kubwa ya wanawake benki hii haijafika, tutaendelea kufanya siasa au tutaendelea kusaidia wanawake.

Ninaomba Mheshimiwa Ummy pamoja na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake fanyeni hima…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wanafunzi wanaopata mimba za utotoni warudishwe shuleni kwani wengi wao wanapata mimba wakiwa na umri mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo elimu ya juu; mikopo ya elimu ya juu inatolewa kwa wanafunzi wachache na wengi wenye uwezo kuachwa hasa watoto wa kike wanaochukua kozi ya Udaktari na Engineering.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi vyuo ni vichache hasa Mkoa wa Mbeya, kwani nchi yetu inajinasibu kuingia katika uchumi wa viwanda na tuna wanafunzi wengi wanaishia elimu ya msingi na elimu hii ingesaidia kuwapa elimu vijana wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Serikali ikatoa fedha kwa wakati za maendeleo kwa Jeshi letu ili liweze kutekeleza majukumu yake ya kila siku, kwani kwa kuchelewesha, tunarudisha nyuma maendeleo ya Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa kuona maduka yenye gharama nafuu yaliyokuwa yanasaidia familia hizi yamefungwa. Naomba Serikali itoe majibu, ni kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu walioajiriwa kwenye Shirika la SUMA JKT hasa kwenye ulinzi wa makampuni, wanalipwa kiasi kidogo cha mshahara kwani hii linaweza kuleta ushawishi mbaya wa vijana wetu na kuweza kuleta madhara kwa makampuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Mzinga ni muhimu kwa Taifa na Jeshi lenyewe, ila hakipati fungu la kutosha kutekeleza majukumu yake na kwa kuwa Serikali hii imetangaza mwaka wa viwanda, inabidi iwekeze sana kwenye kiwanda hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Serikali ifuatilie hati miliki za makambi yote ya Jeshi ili kuondoa sintofahamu na wananchi wanaovamia makambi hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 2000 Jeshi lilianzisha shule za sekondari nyingi na zilisaidia sana kutoa elimu bora kwa vijana wengi na hata michezo ilifanyika na kutoa wachezaji bora. Hivyo, Serikali iendeleze uwekezaji huu kwani ni muhimu kwa Taifa hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nichukue nafasi hii kuweza kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi ninayo maswali kwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha. Tunataka tujue, Jeshi lina madeni makubwa sana linayodaiwa na watu waliohudumia Jeshi. Sasa sifahamu ni lini Serikali itaweka pesa tunazozipitisha hapa Bungeni na kuhakikisha fedha hizo zinakwenda kwenye Wizara hii kuweza kutimiza majukumu yao? Leo hii mnajinasibu kwamba mnahitaji Jeshi lisiaibike, lakini wakati huo huo shilingi bilioni 200 lakini mnatoa chini ya asilimia 14. Sielewi mnaongea nini na mnafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tunafahamu Kiwanda cha Nyumbu ni sehemu ambayo Tanzania yetu ingweza kujivunia, wanatengeneza magari, lakini ukifika pale utashangaa sana mashine ni toka Nyerere yupo, alipokuwa akitegemea mkonge na sasa tuna dhahabu. Mnasema Tanzania ya viwanda, kwa nini tusiwekeze kwenye jeshi pale upande wa nyumbu tukaona hiyo dhamira ya viwanda ikitekelezwa kwa kutumia jeshi lile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale vifaa havifanyi kazi, mashine ni mbovu, lakini pesa bado ni ndogo. Ndugu zangu mimi ninaomba tuache siasa katika mambo ambayo ni ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huohuo wanajeshi hawa, amezungumza aliyepita, unawezaje kuhamisha wanajeshi ukawaleta, ni kweli wao wanatii, wakati wa kuhama unaambiwa uondoke asubuhi unaondoka, lakini ni lazima tufikirie hawa watu wana familia zao! Mheshimiwa Waziri utakapokuja kutujibu, utuambie ni lini wanalipwa, kwa sababu si kweli kwamba tunasubiri bajeti hii; kama pesa ni za bajeti iliyopita lazima utuambie wanalipwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapinga UKIMWI kama Taifa, leo mwanaume mwanajeshi yuko Dodoma, familia yake iko Dar es Salaam, hajui anarudije kwa sababu kazi zao zinaenda kwa order, usipompatia hela unataka nini? Mke wake kule atatafuta mtu, atatafuta mbadala na yeye huku atatafuta mbadala. Kwa hiyo, ninaomba walipwe sawa sawa na stahiki yao wanayotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshini kulikuwa kuna maduka ambayo yana punguzo la bei, lakini tunaambiwa kwamba yale maduka yamefungwa. Wanajeshi hawa hawana muda wa kufanya biashara, wanahitaji kupata incentives, kumuwekea duka lenye bei nafuu ni kumtia moyo wa utendaji kazi. Sasa sijajua hizo bajeti na jinsi ya kufunga mikanda kama kunafika hadi kwenye Jeshi, tukifika hapo nchi inaangamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kauli zinasemwa na Waheshimiwa Wabunge wengine, sitaki kuwataja umekataza, tunapozungumzia haki sisi sio Wazambia, sisi ni Watanzania, ni wazawa, tunazungumzia mustakabali wa Taifa hili bila kupendelea. Si sawa kutuona sisi ni magaidi tunapozungumzia na kusema tunawachonganisha wanajeshi na wananchi, kwani wanajeshi hawajui kama wao wanakosa haki zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haki ya kuzungumza pasipo kupendelea; na msijifiche kwenye kichaka cha kwamba sisi ni wapinzani, tunayo haki, tunalipwa mshahara sawa na ninyi na lazima tulalamike na lazima msimamie haki na muifanye kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi linajitahidi sana kutetea Taifa letu, lakini ijapokuwa hii inahusika na miundombinu pia, kwenye mipaka yetu madaraja ni mabovu. Leo hii tukipata shida kama nchi mimi nakwambia hivyo vifaru ambavyo wanavyo kwa kupitisha hawana. Sasa hapa Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi uonane na Waziri wa Miundombinu uone ni jinsi gani utaweka mipakani madaraja. Kule kwetu Kyela madaraja ni mabovu, Malawi wameonesha chokochoko kuja kwetu, je, wakifanya kweli, tunapita wapi? Ninaomba unapokuja kuhitimisha ujaribu kuliweka hili wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wanafanya kazi ya ulinzi kwenye SUMA JKT, mishahara wanayopata ni midogo. Sote tunajua kuna makampuni ya ulinzi yanalipa hadi shilingi 500,000 wafanyakazi wao, vijana hawa wanapata chini ya shilingi 200,000, mimi nafikiri si sawa. Ninaomba Mheshimiwa Waziri kwa bajeti inayokuja ufikirie jinsi gani vijana wale wataongezewa mshahara. Na ninaomba pia na ninashauri kama ikiwezekana makampuni binafsi mengine yapunguzwe, ili tuongeze idadi ya vijana kwenye JKT na kuchukua tender, ikiwezekana zote kwenye Serikali, lakini pia hata makampuni binafsi tulazimishe wachukue SUMA JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi pamoja…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwanza kuhusu wakulima wa chai Rungwe. Kumekuwa na migogoro mingi sana kati ya wakulima wa chai Mkoa wa Mbeya, Wilaya ya Rungwe na wadau wa chai akiwemo Mohamed Enterprises na WATCO kwani bei ya chai ni ndogo sana na baadhi ya wakulima kujiondoa katika uuzaji wa chai katika viwanda vya Katumba na Busokelo kwa madai ya maslahi madogo na wakati huo huo Bodi kuzuia kuuza kwa chai na kampuni ya Mohamed Enterprises na kuzuia uhuru wa kibiashara ambapo mwisho wa siku mkulima ndiyo hunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili mazao kuuzwa kwa ujazo wa lumbesa. Naomba Wizara iweke mkazo na msisitizo wa kusaidia wakulima wanapouza mazao kulazimishwa kujaza mazao katika mfumo wa lumbesa kwani wakulima hupata hasara kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba niongelee kuhusu pembejeo zisizo bora. Kumekuwa na malalamiko ya pembejeo zisizo na kiwango na kupelekea makusanyo duni na kuwapa hasara wakulima wetu hasa wa Mkoa wa Mbeya. Serikali ina mkakati gani wa kusaidia wakulima hawa na pia kuchukua hatua kwa wahalifu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, niongelee kuhusu bei ndogo za mazao. Wizara inasaidiaje wakulima wauze mazao yao kwa bei ya faida ambayo itasaidia kulipa gharama za kilimo walichowekeza na kudhibiti madalali wanaopata pesa nyingi kuliko wakulima wenyewe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, Kituo cha Kilimo Uyole. Kituo hiki ni muhimu sana kwa wakulima wa Nyanda za Juu Kusini kwani utaalam wao unahitajika lakini cha kushangaza pesa inayotengwa kwa shughuli za maendeleo haziwafikii kwa wakati na hata wakati mwingine kutofika kabisa na kukwamisha shughuli za kitafiti na kiutendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita ni kuhusu wakulima na wafugaji. Tunaomba ufumbuzi wa kudumu juu ya wakulima na wafugaji utafutwe ili kupunguza/kuondoa ugomvi kati ya jamii hizi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kuweza kuchangia Wizara hii ya Kilimo. Nimesimama kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya, kila mtu hapa anafahamu Mkoa wa Mbeya ni mkoa ambao unaweza ukalisha nchi hii vizuri lakini bado nashangaa kwa nini Serikali haitaki kuwekeza zaidi katika mkoa huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda hasa kwa kuchambua Mkoa wa Mbeya nitazungumzia Wilaya ya Kyela. Wilaya ya Kyela ina mambo mengi ambayo yanaweza kulisaidia Taifa hili. Tunafahamu Ziwa Nyasa linatoa samaki wa aina nyingi ambapo kama tukiwekeza katika lile ziwa tunaweza tukasafirisha samaki katika nchi yetu wenyewe lakini katika soko la Afrika Mashariki. Tunafahamu Kyela kunapatikana cocoa, Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hotuba yake atuambie ni nguvu gani amewekeza katika zao la cocoa. Tunajua cocoa inanunulika sana katika soko la dunia lakini mwananchi wa Kyela amefaidikaje na zao hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye mpunga, Wabunge mnafahamu kuna mahali mpaka tunadanganywa mpunga wa Kyela, kwa nini tusiwekeze katika mpunga huu kama unapendwa na una soko zuri kuweza kusaidia wale wakulima wadogo wadogo ambao pia wengi wao ni wanawake tukaweza tukapata zao hilo na faida yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua hii Benki ya Kilimo kwa nini isiende kusaidia wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Wananchi wanapolima tatizo kubwa tunaona ni mitaji, twende mahali tuachane na kilimo cha jembe, tunahitaji kilimo cha kibiashara ili kuweza kumkwamua mwananchi katika kujiendeleza maisha yake ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Benki ya Kilimo, najua ipo Dar es Salaam sijui kama ina matawi, kama ina matawi hayafanyi kazi, ukienda huko kwetu Rugwe, Kyela, Mbarali hakuna mwananchi anayeijua na wala hata kupata maelezo ya benki hii ikaweza kuwasaidia hawa wananchi. Naomba Wizara ichukue juhudi za makusudi kusaidia wanawake na wananchi wa Mkoa wa Mbeya waweze kujua maana ya kuwa na Benki ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia pembejeo. Pembejeo imekuwa ni tatizo kubwa sana katika Mkoa wa Mbeya. Kwanza haziji kwa wakati, pili nyingi ni feki, hata hatujaelewa Serikali imechukua hatua gani kwa wale walioleta pembejeo zisizofaa. Naomba kwa bajeti ya mwaka huu pembejeo zifike kwa wakati na zilizo bora kwa sababu hata Wabunge wenzangu wamelalamika mazao hayatoki mengi ni kwa sababu mbegu hizi si bora na hata hizi mbolea zinazokuja si sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara isimamie na ituambie inafanyaje na kama inaweza ikabadilisha mtindo ambao unatumika sasa wa ugawaji wa pembejeo kwa sababu wachache wananufaika na wakulima wanaingia kwenye nafasi ambayo haziwafikii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la chai, nimezungumza mara nyingi katika Bunge lako Tukufu nikilalamika juu ya wakulima wa chai wadogo wanavyolalamika chai isivyowasaidia wao kama wakulima. Ni watu wachache sana wananufaika na zao la chai, mwananchi wa kawaida chai bado iko chini wakati chai inauzwa bei nzuri soko la dunia lakini sisi wenyewe Tanzania tunahitaji kunywa chai kwa nini chai isimnufaishe mkulima wa Mkoa wa Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia mazao, Mbeya ina mazao mengi sana. Sisi sote tunafahamu unapotaka kupata karoti unapata Mbeya, unapata viazi lakini linakuja tatizo kwenye soko, bei ya mkulima ni ndogo anayefaidika ni mtu wa katikati ambaye ni dalali. Tunawezaje kusaidia wakulima wakauza mazao yao kwa bei ambayo ni nzuri. Mwananchi wa kawaida anahangaika kulima mwisho wa siku anauza gunia la viazi Sh.25,000, Sh.20,000 au Sh.30,000 lakini ukija Dar es Salam gunia hilo hilo linauzwa kwa Sh.150,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inamsaidiaje mwananchi huyu aweze kuuza kwa bei kubwa na tunajua kabisa mpaka sasa kuna watu wanatoka Kenya wanakuja huku kwenye masoko yetu na mashamba yetu bado wananunua kwa bei ndogo. Tunahitaji wateja waje lakini Serikali inawabanaje wanunue kwa bei inayomnufaisha mkulima wa kawaida?

Tunapozungumzia kilimo tunahitaji kuwekeza kwenye kilimo kweli kweli wala si katika maneno. Tunapozungumzia mpunga, tumezungumzia mpunga wa Kyela ulivyo mzuri lakini tuna Mbarali, Mbarali kuna shamba kubwa sana la mpunga lakini je Serikali imewasaidiaje wale wakulima wa Mbarali, imesaidiaje wale wakulima….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Malengo ya Milenia (MDGs) hatukuweza kufikia malengo, tulifanikiwa maeneo matatu tu na hata hivyo UNESCO ilitupatia tuzo katika uandikishaji wa watoto, kwa hilo napongeza japo hatukuweza kuwa na elimu bora kwa watoto wetu japo waliandikishwa kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwa sasa tuna SDGs ambayo malengo yake ni mengi zaidi ya MDSs. Je, katika Mpango huu Serikali imejipangaje kuhakikisha inaingiza katika Mpango huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yoyote makini, lazima iwe na vipaumbele vichache visivyoweza kushindwa katika utekelezaji, Tanzania kwa sasa ina vipaumbele gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje kuwa na maendeleo na mipango bila kilimo. Viwanda bila kilimo ni uti wa mgongo ni vema tukazingatia kilimo maana viwanda vinategemea malighafi za kilimo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kama Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, sikitiko langu ni sawasawa na Wajumbe waliopita. Tatizo la bajeti, Bunge tunapitisha lakini mwisho wa siku pesa haziendi kwa wakati kwenye kasma ambayo sisi tumeipelekea. Sasa Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujibu hoja yako jioni, ninaomba utuambie safari hii utafanya nini kuhakikisha fedha hizo zinafika kwa wakati hasa zikasaidie kazi za Balozini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunazungumzia uchumi wa kidiplomasia. Sisi kama Kambi, Mbunge wetu ameelezea vizuri sana ni jinsi gani inabidi tujikite kwenye uchumi wa kidiplomasia. Na mimi nazidi kusisitiza kwamba bila kuwa na uchumi wa kidiplomasia hatuwezi kufanya vizuri kwenye zama hizi za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunafahamu biashara nyingi sana zinaendelea, lakini kundi kubwa la wanawake ambao ndio wajasiriamali wakubwa, sijaona kama Wizara imefanya juhudi za makusudi kuweza kutambulisha fursa hizo za kijasiriamali kwa wanawake wa Tanzania kwa ujumla wake. Kuna maonesho mbalimbali yanafanyika, likiwemo Jua Kali na mengineyo, sijaona kama Wizara imetangaza hata kwa kutumia Televisheni ya Taifa kuwaeleza wanawake wa Tanzania kuzijua hizo fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni ya muhimu sana. Tunajua kwamba Mabalozi wanalipwa mishahara kule waliko. Wanatumia juhudi gani kuitangaza Tanzania hasa katika maeneo ya kiutalii pamoja na mambo mengine ambayo watu wetu wanaweza wakanufaika na hizo nchi. Nadhani ifike wakati tupeleke wataalam na kama wapo, wapewe onyo kali wasipofanya kazi zao na wajibu wao wa kuitangaza nchi katika hizo nchi wanazokaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tuna tatizo katika Wizara hii. Balozi mmoja, kwa mfano Balozi wa Msumbiji, anasimamia na Balozi nyingine zinazomzunguka. Ni kweli tunabana bajeti, lakini mwisho wa siku ufanisi unakuwa mdogo kwa sababu hakuna pesa zinazokwenda mahali pale. Kwa hiyo, nashauri bado ninafikiri tuna wasomi wengi katika Taifa hili, ninaomba wapewe nafasi za Ubalozi katika hizo nchi badala ya kutegemea Balozi mmoja kusimamia Balozi zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie Chuo cha Diplomasia, Kurasini. Chuo kile ni cha muhimu sana na wote tunajua kwa nini kilianzishwa. Hivi tunavyoongea kile chuo wenzetu wa Msumbiji walijitoa, lakini pia hatuna pesa ya kukiendeleza kile chuo. Mapato yanayotumwa kwenye kile chuo ni madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakapokuja tunaomba atuambie, tunasimamiaje chuo kile ili kiendelee kutoa Wanadiplomasia makini katika Taifa letu la Tanzania? Tunataka kujua kwa nini wenzetu wa Msumbiji walijitoa na wengineo? Basi watuachie tubadilishe matumizi ya chuo kile kiweze kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki na lile jengo letu la AICC pale Arusha. Nataka kujua linasaidiaje? Kwa sababu ninaamini pesa zinazopelekwa bado ni ndogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ukuaji na uingiaji wa watalii ulikuwa asilimia 12.9 mwaka 2015/2016; mwaka 2016/2017 mwaka wa kwanza wa Awamu ya Tano kasi imeshuka mpaka asilimia 3.5 tu. Hifadhi ya Ruaha inayopakana na wananchi maeneo ya Mbarali wapo katika wakati mgumu wa kufukuzwa kwenye makazi yao na mpaka sasa hakuna hata waliopata fidia yoyote mpaka sasa hawana cha kufanya.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ukataji wa miti kilometa za mraba 1,430 sawa na zaidi ya ukubwa mkoa mzima wa Dar es Salaam huu mradi si wa Watanzania kwa maana ya kuwasaidia. Tunaomba Serikali ichunguze na kuamua kwa faida ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Guanzhuo ni mji wa kibiashara lakini hatuna Balozi Mdogo na timu ya kutangaza biashara hasa watalii kuja nchini kwetu kwani Kenya ina timu inayofanya matangazo ya nchi yao. Hakuna pesa za kutangaza utalii kwa nchi yetu na kutegemea makampuni binafsi ambayo hata wao hawaweki mkazo juu ya utalii huu. Vifaa vya kutendea kazi kwa wafanyakazi mbugani kama magari, tochi, bunduki hata boti sehemu zenye kuhitaji mabomu. Tunaomba Serikali iongeze bidii katika kuwezesha fedha za utendaji.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Rungwe kuna vivutio vingi sana lakini hakuna uwekezaji wa kutosha ili kuvuta watalii maeneo hayo ni Daraja la Mungu, Lake Ngozi na Kijungu. Haya maeneo ni ya muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Rungwe tunaomba Serikali iwekeze maeneo hayo.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pia kuwa mmoja wa wachangiaji wa bajeti hii. Binafsi naunga mkono bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani iliyozuiliwa kusomwa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake kama tulivyosema bajeti hii ni ya kufikirika na sidhani kama itatekelezeka. Kwanza kabisa Deni la Taifa. Wizara hii ndiyo msimamizi mkuu wa Deni la Taifa na mali za nchi. Toka awamu hii imeingia madarakani Deni la Taifa limeongezeka kwa kasi kubwa sana na yeye kama kiongozi anayehusika haoni kama analiletea Taifa hili changamoto inayotusubiri hapo mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwezi ameji-commit na Wizara yake kulipa Deni la Taifa shilingi bilioni 883. Ameji- commit na ana wajibu wa kulipa mishahara ya watumishi karibu shilingi bilioni 617 na kuendelea. Wakati huohuo kuna OC shilingi bilioni 254. Mapato, tukiachia mnavyo-forge maana mmeeleza mapato ni mengi wakati uhalisia si kweli. Matumizi ni 1.7 lakini mapato ni 1.2, hizi nyingine anapata wapi? Kwa hiyo, namsisitiza kwa faida ya Watanzania na hasa wanawake ninaowawakilisha namwomba awe realistic, asiweke figure za kufurahisha viongozi au baraza lake, ahakikishe anaweka figure ambazo zitawasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, naona niache habari ya Deni la Taifa kwa sababu ni cancer ya Taifa. Nataka niingie kwenye habari ya kilimo. Toka tunapata uhuru tulikuwa tunasema kilimo ni uti wa mgongo na kilimo kinachukua zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, bajeti ya 2016/2017

T A A R I F A . . .

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, mama ni yake wa kambo, kwa hiyo, naelewa anachofanya. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kusema ni kwamba 2016/2017 tuliweka bajeti ya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya bajeti ya kilimo lakini ni shilingi bilioni 3 tu ndiyo zilitoka. Kama unazungumzia kilimo ni uti wa mgongo na sisi kama Bunge tulipitisha hizo pesa tukijua hata kama hazitoshi zinaweza zikasaidia lakini ikatoka shilingi bilioni 3 peke yake. Mwaka huu tunaoumaliza sasa tulitenga shilingi bilioni 150 lakini mpaka leo zimetoka shilingi bilioni 27 peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ndiyo kila kitu na wewe mwenyewe umetoka kwa wakulima unafahamu, kama pesa haijatoka na sisi Bunge tumepitisha, sioni umuhimu wa kuwepo mahali hapa unless tunafanya siasa. Bunge kama chombo muhimu kimesema pesa kadhaa itoke Wizara haijatoa na wanajinasibu wanakusanya pesa nyingi, sielewi wanasimamia mpango gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutoa pesa ndogo kwenye kilimo bado kilimo kinaingiza kwenye pato la Taifa takribani asilimia 30 ya pato la Taifa. Kwa nini kama Watanzania tusione umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye kilimo pamoja na viwanda tunavyovizungumzia tukaweza kupata pesa nyingi isiyokuwa na matatizo. Leo hii tuna Vyuo vya Kilimo, kwa mfano, SUA na Uyole huu ni mwaka wa tatu hawajapata pesa za utafiti. Unawezaje kuwa na kilimo safi hufanyi utafiti?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza kilimo, tunazungumzia mbegu bora, jana kuna mmoja ametoka kuuliza swali juu ya mbegu za alizeti, mkulima kwa gharama yake anapanda mbegu lakini mbegu haioti. Watafiti hawawezi kusema lolote kwa sababu hawajapewa pesa kwa ajili ya utafiti. Leo hii kuna mbegu za mahindi zinapandwa, hakuna chochote kinafanyika kwa sababu hizo mbegu si mbegu bora lakini hatuwezi kuwalaumu watafiti wetu kwa sababu hawana fedha ya utafiti. Tukienda kwenye mambo hayo hayo ya kilimo, katikati ya kilimo kuna mitamba ile inayotakiwa kufanyiwa utafiti hawajapata pesa. Pale SUA Arusha hawajapata pesa kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya kilimo ambacho kimebeba idadi kubwa sana ya Watanzania na mimi ninayewakilisha Mkoa wa Mbeya asilimia kubwa wewe ni shahidi, wanawake ndiyo wanaoingia kwenye kilimo. Kwa gharama zao wenyewe wanaamua kulima, hawana Maafisa Ugani, wako wachache, hawana maelekezo yoyote mwisho wa siku wameshalima lakini masoko pia hamna. Tumeingia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki wenzetu wamejipanga kwa nini na sisi tusiige, kwa kweli masoko ni shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi nikisimama hapa nazungumzia suala la chai. Mpaka sasa hatuna viwanda vidogo vidogo vya kusaidia wakulima hawa. Hatuna mkakati wa mbolea au kuwasaidia kwa namna yoyote kama Taifa lakini bajeti inayotengwa ni ndogo na hata hiyo ndogo inayotengwa Wizara haitoi pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii bajeti sijajua walifikiria nini au kuna kitu gani wanakifanya? Hali ya hewa huwezi kuitegemea kwenye kilimo. Tanzania tunaishi kwa kutegemea Mungu anasema nini kwa ajili ya kutuletea mvua. Hatujajipanga kwenye umwagiliaji, hatujajipanga kuhifadhi maji ya mvua, tunasubiri Mungu atoe na asipotoa hatuna kilimo. Naomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango tulitazame suala hili kwa upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niende kwenye eneo la wafanyakazi. Sasa hivi imeletwa sheria ya ufutwaji wa Tume ya Mipango. Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango alikuwepo toka awamu iliyopita kwenye Idara hiyo, Marais karibu wanne wamepita hakuna aliyethubutu kufuta hii Idara lakini wanafanya hivyo kwa sababu wanataka wawe huru na kufanya wanavyotaka. Hawataki kuwa na chombo cha kuwasimamia, wanachota hela Bombardier, Chato, hawataki usimamizi. Kwa sababu tukiwa na hii Idara sisi tutaiuliza lakini wanaiondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mfuko mmoja wa mapato ya Serikali wanataka ubadilishwe sijajua wanawaza nini. Hatuwezi kumlazimisha maana ameshika mpinina sisi tumeshika makali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki wa wafanyakazi umekuwa kwa muda mrefu, kuna sehemu umemalizika lakini kuna watu walipandishwa madaraja miaka miwili iliyopita hawakulipwa mishahara yao. Umefika wakati wa kulipa mishahara yao sawasawa na madaraja waliyopanda
mnawaambia waandike barua kwa wakati mliosema kwa maana miaka ile mingine inapita bila wao kupewa haki yao, huu ni dhuluma na hii ni dhambi mnaipanda kwenye Taifa hili. Jasho la mtu likipotea, kuna wakati hata tunapeleka watoto wetu shule hawafaulu mitihani kumbe ni pesa ya laana. Umempeleka mtoto shule unalipa ada kumbe ile ada uliyolipa kuna watu wanalalamika mahali fulani. Namuonya Mhesimiwa Dkt. Mpango naomba atetee hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye viwanda, nitazungumzia upande wa Kiwanda cha Ngozi. Hatuna kiwanda cha ngozi na ng’ombe wanagongwa alama tayari hiyo ngozi yao haina thamani. Ng’ombe wanatembea kilometa nyingi, hiyo ngozi haina thamani. Nashauri kuwawekea wafugaji maeneo mazuri ya kulima na kutunza mifugo hiyo ili tupate thamani ya ngozi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda anavyovizungumza Mheshimiwa Mwijage, cherehani tatu anaita ni kiwanda, huku ni kuwachezea Watanzania. Namshauri kaka yangu asifanye vitu kisiasa. Mnapokuwa kwenye cabinet, Mheshimiwa Mwijage nakuamini, shauri hali halisi. Mimi nimegawa vyerehani zaidi ya 400, anataka kuniambia mimi ni mfadhili wa viwanda? Hiyo si sawa. We need the real project, hatuhitaji kufanya vitu kisiasa, kuwanufaisha Watanzania. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya ni tatizo hasa kwa magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii. Kabla ya yote, nataka nimpongeze Mwenyekiti wetu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na viongozi wa CHADEMA ambao kwa sasa wako katika kadhia ya kuripoti Polisi kila Ijumaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nizungumzie suala la Zimamoto. Zimamoto mwaka 2016/2017, Bunge lilitenga pesa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kununua magari mawili ya Zimamoto, lakini pesa hizo hazikuweza kutoka sawasawa na Bunge lilivyopitisha. Tender Board ilikaa wakazungumza na Wizara ya Fedha pesa ziweze kutoka, zilitoka shilingi milioni 117 peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia viwanda, viwanda na moto ni vitu vinaenda pamoja. Kama hutaweza kutenga pesa kwa ajili ya magari ya Zimamoto unakuwa hujafanya sawasawa katika utekelezaji wa kuleta maendeleo. Mwaka 2017/2018 Serikali ilitenga shilingi bilioni 3.5, haikutoka hata senti tano kwa ajili ya watu wa Zimamoto. Jeshi hili ninavyoliona ni kama Jeshi ambalo limesahaulika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu kabisa kwamba Jeshi hili hata ukiangalia mavazi yao, ni chakavu kuliko majeshi mengine. Sasa sijajua tunawaweka katika ma-grade kwa sababu gani? Kwa hiyo, naomba Serikali na namwomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kujibu hoja, tunataka kujua hizi pesa tunazopitisha kama Bunge, halafu hazitumiki na wala hazitoki, Wizara ya Fedha haitoi pesa. Kama Bunge limepitisha, kwa nini Wizara haitoi? Namwomba Mheshimiwa Waziri aje atoe majibu anapokuja kuhitimisha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia jengo la Mchicha. Unajua Zimamoto mpaka sasa hivi wanapanga na kuna jengo tayari Serikali imeshaweka pesa pale, jengo halijakwisha, limechakaa na safari hii hakuna hata senti tano iliyotengwa kwa ajili ya jengo lile. Sijajua tunawaza nini na tunafikiria nini kwa ile pesa tuliyoizamisha pale Mchicha, mpaka leo hiyo pesa hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi kuna wakati niliwahi kuongea na IGP nikamwambia kwamba Jeshi linafanya kwa professionalism. Unapokuwa na jeshi lazima na intelijensia inafanya kazi yake kwa makini kwa kufuata weledi wa kile walichosomea. Leo hii Jeshi la Polisi linafanya kazi na mitandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binti mdogo anaitwa Mange Kimambi anaanzisha maandamano mtandaoni, leo wanalitoa Jeshi sehemu za siri kulileta barabarani. Sidhani kama wako sahihi. Wakitokea Mange Kimambi 10, wanataka kuniambia watashinda wakifanya mazoezi barabarani? Sidhani kama wako sahihi. Mheshimiwa IGP, nafikiri inabidi kujitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri Mwigulu alipokuwa Singida sikumbuki ilikuwa hafla gani, alizungumzia kuhusu waandamanaji na akasema waandamanaji watakapoandamana inaweza ikatokea kupigwa risasi. Sasa sijajua kwamba anaota au sijajua kama yeye ni Mfalme Njozi, sijafahamu. Ninachojua, Polisi kazi yake ni kulinda raia. Maandamano mimi naona wanazungumzia kama ni dhambi au kitu kibaya. Jeshi la Polisi kazi yake kufanya intelijensia. Elimu waliyosomea ipo kwa ajili ya kuzuia mabaya, wala haipo kwa ajili ya kutetea kwa kutumia vitu vya kufikirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa Waziri, Mheshimiwa Mwigulu, yeye ni kiongozi wa wote. Hisia zake za kichama ajitahidi kuzidhibiti zisiweze kumtoa kwenye reli. Naomba afanye kwa weledi, ataacha alama katika jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapolalamika, Polisi wanaposema wamefanya utafiti na kugundua kuwa kutatokea hali mbaya, sijaelewa huwa inaangalia upande mmoja, au ni pande zote. Kiongozi wa Chama cha Upinzani, kiongozi wa Jimbo kwa maana ya Mbunge, anaandika barua ya kufanya Mkutano ambao huo wameuruhusu, lakini Polisi inatoa majibu ndani ya masaa mawili kabla ya Mkutano kusema kwamba tumegundua amani haitakuwapo. Kwa kweli nashindwa kuelewa. Mikutano hii akifanya Polepole intelijensia haioni ubaya, lakini akifanya mtu wa CHADEMA Mheshimiwa Heche, intelijensia inaona ubaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, nataka kuwaambia, siku zote ubaya wa kidogo kidogo huwa unajenga chuki ndani ya watu. Mheshimiwa Bwege mchana wa leo amezungumza na mkamshutumu kwamba anaongea kwa hisia, lakini kumbukeni mabaya huwa hayatokei isipokuwa yamefanywa kidogo kidogo mwisho wa siku yakawa makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili ni la wote na wala siyo favour sisi kuwepo hapa. Ni haki yetu na wajibu wetu na kwa sababu walikubali vyama vingi, wakubali kumeza vidonge vya vyama vingi. Polisi watuachie CCM tukae nayo pembeni sisi wenyewe tufanye nao siasa, wao wakae pembeni. Kwetu sisi CCM ni wepesi kama karatasi wakikaa pembeni; lakini wakitulazimisha na sisi ni binadamu, tutatafuta njia mbadala ili kuhakikisha tunafikia wapi tufike kwenye malengo tunayoyataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Uhamiaji, dada yangu kiongozi wa Uhamiaji anafanya kazi vizuri, lakini bado kuna maeneo madogo madogo hasa kwenye biashara ya kujenga nyumba za Uhamiaji, asimamie vizuri pesa za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye Jeshi la Magereza, wako vizuri, wanafanya vizuri. Tatizo lao Magereza pia ni kama la Zimamoto kutokuwa na vifaa vya kutosha ikiwemo nyumba za kuishi, lakini uniform ni kilio kikubwa sana kwa wafanyakazi hao. Magari kwa Magereza ni shida. Ukienda mikoani, wanahitaji kupeleka wafungwa kwenye kesi, hawana magari. Sasa sijajua tunategemea nini? Kesi zitaendaje? Watafanyaje kama hatutaliwezesha jeshi hili kufanya kazi zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba uhalifu umeongezeka kama wanavyosema, lakini Magereza mengi yana vyumba vidogo. Magereza mengi hayana vyumba vya mahabusu vya wanawake. Wanawake kwa mfano ukienda Gereza la Kyela, hakuna sehemu ya kuweka wanawake, wanaenda kulala Tukuyu. Ni mwendo mrefu sana na wakati huo huo hawana gari la kuchukua hao watuhumiwa na kuweza kuwapeleka Tukuyu na Kyela. Naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja atuambie amejipanga vipi kuondoa changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nafikiria sisi kama Bunge hatujajipanga sawasawa kuisimamia Serikali. Ni mara nyingi tumepitisha bajeti lakini bajeti hizi hazitoki. Bajeti hizi, pesa hazitoki, ni hadithi. Watu wetu wanakuja hapa Dodoma, tunakaa nao, tunawasikiliza kwenye Kamati, tunakubaliana. Ikifika kwenye utekelezaji, hiyo imekuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako Tukufu linapopitisha bajeti, tunataka tukija kwenye mwaka mwingine wa fedha hizo pesa zifanye kazi na ziwasaidie watu wetu kufanya kazi zao na waweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono Kambi Rasmi ya Upinzani, najua hatujaleta maoni yetu, lakini bado tunaamini kwamba maoni yetu yangali yanaishi hata yale ya mwaka 2017 yanaweza kuendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nashukuru. Ahsanteni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SOPHIA. H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa nitazungumzia utawala bora kama wenzangu walivyosema. CAG mara nyingi alikuwa akitoa ripoti na ripoti zake nyingi sana zimeeleza ubadhirifu wa mali uliofanywa na Serikali ya CCM. Ninachotaka kushangaa kuna msemaji aliyepita amezungumzia habari ya Chama cha CHADEMA lakini nikaona huyu mwenzangu labda hajasoma kitabu chote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wa Chama cha Mapinduzi wamechukua pesa za watu ambao walitakiwa walipwe pension kwa cheque number 156424 wakazitumia vibaya. Mpaka CAG anakagua hesabu mwezi wa Pili hizo pesa hazijarudishwa. Anazungumzia tujitoe boriti kwenye jicho letu, huwezi kuwa nyoka ukazaa mjusi. Ili uweze kuwa safi pia lazima uzae mtoto safi, makosa ni ya CCM, si ya CHADEMA.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia utawala bora wewe kama kweli ni chama tawala na uko vizuri na unafanya kazi sawasawa na ilani ya chama chako kwa nini unatumia nguvu ya kuzuia upinzani ambao tayari ulipita kihalali na uliusaini na ukakubalika? Huwezi kuwa mzazi, watoto wawili wanagombana mmoja umemshika mkono halafu unajiita wewe ni mshindi, hiyo siyo kweli. Tupewe uwanja sawa, twende viwanjani na sisi tukazungumze, tuone zile kule milioni sita feki mlizotupa kama hatujawapiga 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye Wizara sasa, maana na mimi nilikuwa najibu ndugu aliyezungumza. Soko la Kariakoo lilijengwa kwa makusudi ya kusaidia wakulima na kuuza vifaa na pembejeo kwa ajili ya wananchi. Najua ni miaka mingi imepita soko lile kuwa pale, lakini tuna Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayozalisha mazao mengi; huu ni wakati sasa mngejenga masoko hayo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, Mkoa wa Mbeya ni mkoa ambao uko katikati, una mazao mengi sana, tunashauri mtupatie masoko ya kimataifa yanayoweza kusaidia wanawake ambao wanalima kwa nguvu zao zote waweze kupata masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejiunga na Afrika Mashariki lakini cha kushangaza wenzetu wa Kenya, Waganda wanakuja hadi vijijini kununua maparachichi bila utaratibu unaokubalika. Tukiwa na masoko haya tunaweza tukafanya kazi nzuri na tukasaidia uchumi wa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nazungumzia habari ya masoko hayo hayo. Leo hii Mheshimiwa Jafo, Tunduma wamefunga masoko; sijaelewa wanaposema ninyi mnatetea wanyonge, mmepoteza hela ngapi kwa siku ya leo kufunga soko la Tunduma? Sijajua ni kwa nini tunawaachia Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa waamue mambo bila kutumia utaratibu na professionalism?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri kama kiongozi wa Wizara hiyo, tunaomba Soko la Tunduma lifunguliwe. Tunadaiwa madeni mengi, kwa sababu mwishowe wafanyabiashara wamesema wanatupeleka mahakamani; ni nani atalipa pesa hizo? Halmashauri hii wameifungia Madiwani, kazi haziendi kisa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya. Hapa ndipo ninapoushangaa huu utawala bora Mzee Mkuchika. Naomba ninyi wazee ambao bado mpo na mpo kwenye system shaurini Serikali ifanye kazi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija upande wa mikopo, ilitengwa bilioni sitini na moja kwa ajili ya wanawake na vijana, lakini bilioni kumi na tano ndizo zilizotumika. Idadi ya wanawake ni wengi lakini pesa zilizotoka ni kidogo. Tunaomba waachilie vyanzo vya mapato kwenye halmashauri ili tuweze kukusanya pesa nyingi na kusaidia wanawake na vjiana kwa ajili ya ahadi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ugawaji wa mikopo hii unakwenda kiitikadi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nianze na suala la upelekaji fedha Wizarani kwa ajili ya miradi. Kutotoa pesa za mradi kwa wakati ni changamoto kubwa sana kwa asilimia tano kwenye miradi mbalimbali na kupelekea kuzorotesha miradi ya maendeleo. Nikichukulia Wizara ya Mambo ya Ndani kazi nyingi zimeishia njiani na kupelekea kupoteza fedha nyingi zilizokwishatumika katika miradi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu fedha shilingi trilioni 1.5; mnamo mwaka huu kulitoka report ya mkanganyiko ya mwaka 2016/2017 kuna hoja ya shilingi bilioni 203.9 ya Serikali Kuu ya Tanzania kwamba ulikusanya kwa niaba ya SMZ, hii si kweli kwani SMZ mwaka 2016/2017 bajeti yao ilikuwa shilingi bilioni 841 na kati ya hizo shilingi bilioni 452 ni vyanzo vya ndani na nje na shilingi bilioni 58.9 katika mapato ya ndani, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 366.0; makusanyo ya ZRB na TRA na mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 23.6. Shilingi trilioni 1.5 ni karibu mara mbili ya bajeti yote ya Zanzibar. Naomba kujua zipo wapi?

Mheshimiwa Spika, Wizara imeonesha udhaifu kusimamia Deni la Taifa kwa kuwa deni limezidi kuongezeka na kuwa na athari za kitaifa; mid-year review katika mwaka 2017/2018 iliyotoka mwaka huu Februari, 2018 ni kwamba Deni la Taifa liliongezeka kwa dola 1,054.6, sawa na shilingi trilioni mbili, bilioni mia tatu na milioni mia moja ishirini. Deni limefikia trilioni hamsini na tisa, bilioni thelathini na saba. Ni shida kwa Taifa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi naomba niunge mkono Kambi Rasmi ya Upinzani maana na sisi tumetoa dira, mwelekeo na mpango ambao tunafikiri Serikali mnaweza mkaufuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nataka nizungumzie kilimo. Tunapozungumzia kilimo ambayo tukimechukua asilimia takribani 75 ya Watanzania wamejikita katika kilimo, lakini katika mpango huu ambao Mheshimiwa Mpango umeuleta hatuoni nguvu ya Serikali kusaidia wakulima wa Tanzania waweze kukuza uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambazo tumekuwa tukipanga Wizara inatoa asilimia mbili tu ya mapato kusaidia wakulima. Tunafahamu kwamba katika kilimo usipoweka pesa wewe kama Serikali na ukitegemea wafadhili wakupatie pesa kwa ajili ya kilimo na bahati mbaya sana wafadhili wenyewe mmeanza kuwakorofisha. EU iliahidi kutoa hela zaidi ya bilioni 200 kwa ajili ya kusaidia kilimo tayari tumeanza kukorofishana nao sijui tutafika wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kwa Nyanda za Juu Kusini niachilie mikoa mingine hakuna dalili zozote za kusaidia hasa katika tafiti ili uwe na kilimo bora kwanza kabisa lazima ufanye tafiti. Mwalimu Nyerere alijitahidi kuweka vyuo mbalimbali vya kilimo ikiwemo Chuo cha Uyole mpaka sasa zaidi ya miaka mitano hawajawahi kupata pesa za maendeleo kwa ajili ya chuo kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vingi vilianzishwa ili viweze kusaidia wakulima kwa mfano ZZK walikuwa wakitengeneza zana za kilimo ikawa rahisi kuwafikia wananchi kwa ngazi ya chini, leo hii kila kitu tunatoa nje, tunatoa China kwa gharama za kigeni kuweza kuwafikia wakulima mwisho wa siku pembejeo zinakuwa ni bei kubwa sana kuwafikia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu ambazo ndio zinatakiwa zizalishe chakula cha Watanzania asilimia 90 ya mbegu tunaagiza kutoka nje. Bahati mbaya sana mbegu nyingine zimekuwa sio rafiki kwa ardhi ya kitanzania ndio maana ninarudi nyuma kwamba tunahitaji kuwa na watu wanaofanya research ambao watajua mbegu hii inafaa kwa ardhi hii au zao hili linafaa mkoa fulani na watu hawa waweze kusaidia wakulima waweze kupata mazao yanayostahiki.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia connection ya Wizara tofauti ili kuweza kusaidia Wizara mama kuwa na mafanikio sisi kama watanzania tumeshindwa. Leo hii watu wanaohusika na mambo ya hali ya hewa hawawezi kufanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Kilimo kuweza kujua mwaka huu tunalima mazao kadhaa kwa kupata taarifa kutoka kwa wataalam, kila mtu anafanya kazi anavyoona yeye inafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo; maji na kilimo vinaenda sambamba, lakini wasipofanya kazi kwa pamoja Wizara ya Maji haina pesa, Wizara ya Kilimo haina watafiti, tunawezaje kufanikiwa katika kilimo na tunawezaje kuwa na maendeleo ya kiuchumi kama Watanzania na kuwafanya wakulima wanapata mazao kwa wakati sawasawa na ubora tunaoutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mashirika mbalimbali yakisaidia upatikanaji wa mbegu. Kama mnakumbuka Ukiliguru zamani walikuwa wanashughulika na mambo ya mbegu, sasa hivi watu kama wale wako wapi? CCM mlikuwa na kitu kinaitwa SUKITA kiko wapi? Vitu mbalimbali vilikuwepo zamani kwa ajili ya kusaidia wakulima hawapo, havipo na wala hakuna ubunifu wa kuanzisha vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie habari ya utawala bora na ukuaji wa uchumi. Usipokuwa na utawala bora na umoja na wananchi kutoka ngazi ya chini mpaka Taifa mnakosa nguvu na moyo wa watanzania kufanya kazi ili kuweza kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamezungumza mahali hapa kuhusu Katiba Mpya na hii ipo katika mpango ambao sisi tumekuwa tukiuzungumzia. Huwezi kuwa na maendeleo yoyote kama hamjajiwekea utaratibu wa utawala. Watu walitoa pesa (kodi) tukaweka Tume, wakazunguka nchi nzima, wakaweka utaratibu wa kuweza kuona kama Watanzania tunaishije, leo hii tumeacha na kuishia pembeni, kwa maana pesa zote zilizotengwa zimekwishakupotea ambayo ilikuwa ni kodi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba utakaporudi utueleze umepanga nini na ni kwa nini Serikali yako inakataa kuzungumzia Katiba Mpya ili twende kwenye mustakabali wa maendeleo yetu hapo baadae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi na usalama ni kitu cha muhimu sana katika Taifa letu la Tanzania. Usipokuwa na ulinzi na usalama wawekezaji wanaondoka. Tumekuwa tukisikia mambo mengi yakitokea na sisi kama wananchi na hata kama Wabunge hatujapata taarifa ya kueleza kwa nini wawekezaji wanatekwa na wanafukuzwa na kama wamekosea je, mmefanya njia gani mbadala mpya ya kuweza kuwatangazia utaratibu mpya wa kuwekeza ili watu wasiwe na mashaka na ulinzi wa Tanzania na usalama wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pasipo na usalama hakuna mtu atakuwa tayari kuja kujiunga na Watanzania. Tupo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, watu wanaona ni bora wahamishe bidhaa zao kwenda Kenya, Uganda na sehemu zingine kuliko kuja sehemu ambayo haina uhakika wa ulinzi wa maisha, mali na mitaji yao watakayowekeza. Tunaomba unapokuja kutueleza Mheshimiwa Mpango ueleze Watanzania pamoja na sisi Wabunge ni mkakati gani umejiwekea wa usalama wa wawekezaji; utatumia njia gani ya kuwalinda hata hao wachache waliobaki waendelee kutumika katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda sana kutoa ushauri, vitu vingi sana vinavyofanyika sasa ambavyo vinaharibu kabisa umoja wetu na hasa katika maandalizi ya kutetea uchumi wa Taifa letu. Mimi ninaomba usimamie TRA ambao ni wakusanyaji wa kodi kwa kweli wamekuwa kama ni askari, hawana umoja na wafanyabiashara na sasa hivi imefika mahali hata wenye mitaji ya 300,000 wanahitaji kulipa kodi, ni kweli sikatai kwamba wasilipe kodi lakini lazima zitungwe sheria ambazo zinasaidiana kuweza kuwasaidia hawa watu wajione wana wajibu wa kufanya hiyo kazi ya kukusanya kodi pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na hali ya udhalilishaji mkubwa sana kwa wafanyabiashara na kumekuwa na matamko mengi hasa Wakuu wa Wilaya kufungia makoso kwa sababu za kisiasa. Wakati mwingine tuliona pale Tunduma, muda mrefu sana masoko yamefungwa, zile pesa ambazo siku ile hazikuingia Serikali ilikosa mapato sababu ya siasa. Vivyo hivyo Mbeya soko la SIDO lilifungwa kwa muda mrefu kwa sababu za kisiasa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji