Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sophia Hebron Mwakagenda (21 total)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda Waziri atuambie, kwa migodi kama ya Kiwira ambayo tayari inazalisha, je, tunapata kiasi gani kama Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nifanye masahisho kidogo, Mgodi wa Kiwira haujaanza kazi rasmi, uko katika kukamilisha detailed design na hatua za kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi. Hata hivyo, mgodi huo utakapoanza, Halmashauri zote zinazohusika zitanufaika na mambo yafuatayo. La kwanza, Halmashauri zitakuwa na uwezo wa kukusanya service levy ambayo ni asilimia 0.3. Kadhalika zitaweza kupata mrabaha ambao utaingia Serikali kuu. Pia, mradi wa Kiwira unakadiriwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 utakapoanza kufanya kazi. Kwa hiyo, wananchi wa Mbeya na Watanzania wengine wataendelea kunufaika na kupata ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika mradi huo utakuwa sasa na kipengele kinachowalazimisha wakandarasi na wamiliki wa migodi kuanza kuwashirikisha Watanzania kwa kununua bidhaa zao pamoja na huduma za jamii ili huduma za jamii zianzie maeneo yanayozunguka mgodi huo. Kwa hiyo, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge Mradi wa Kiwira utakuwa na manufaa makubwa sana kwa Taifa lakini pia kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Kwa kuwa Waziri amekiri kwamba bajeti iliyopita walitenga milioni 870, lakini ni milioni 157 tu ndiyo zimepelekwa. Je, haoni umuhimu wa kuhakikisha pesa iliyobaki inapelekwa.
Swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Rungwe imepata mafuriko na uharibifu wa barabara umekuwa mkubwa sana, naomba Wizara hii itutumie pesa za haraka kwa ajili ya emergency kwa ajili ya vijiji kama tisa zaidi ya kilometa 40; kama Kijiji cha Kyobo, Ikuti na sehemu za Lupepo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka pesa hizo haraka kwa ajili ya kusaidia barabara na madaraja yaliyoharibika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika majibu yangu ya msingi nilisema bajeti ilikuwa ya shilingi milioni 870, zilizopelekwa mpaka sasa ni shilingi milioni 157, jibu hili nimekuwa nikilitoa kila mahali katika vipindi mbalimbali. Nilisema wazi, ukiachia changamoto ya ujenzi wa barabara, lakini kuna miradi mingi kipindi kilichopita ilikuwa haiendi vizuri. Nilitolea mifano miradi ya maji na miradi mingineyo kwamba upelekaji wa pesa ulikuwa ni tatizo kubwa sana, lakini kulikuwa na sababu zake za msingi. Katika mwaka uliopita pesa nyingi sana zilienda katika matukio makubwa ambayo yalikuwa yamejitokeza kama suala la uandikishaji na uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchakato wa hivi sasa, Serikali imejielekeza zaidi katika ukusanyaji wa mapato, ndiyo maana hivi sasa hata ukiangalia kwa mara ya kwanza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imevunja rekodi katika ukusanyaji wake wa mapato. Nilisema kwamba hata miradi iliyokuwepo mwanzo imesimama, lakini hivi karibuni miradi hiyo inapelekewa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia yetu ni kwamba, katika kipindi hiki cha bajeti kilichobakia nina imani Serikali itajitahidi kupeleka fedha katika miradi yote iliyosimama nikijua wazi katika maeneo hayo mengine wakandarasi ambao ni wa ndani na wengine wa nje wanaendelea kudai. Kwa hiyo, suala hili tunaweka kipaumbele siyo kwa ajili ya maeneo hayo tu isipokuwa kwa Tanzania nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mafuriko na kuharibu miundombinu ya barabara, hili nilisema ni kweli. mwaka huu ukiangalia maeneo mbalimbali tumekuwa na changamoto ya mvua kubwa iliyonyesha. Nimetolea mfano kule Rungwe, ukienda Kyela, ukienda Kilosa na maeneo mbalimbali, yote yameathirika kwa ajili ya mvua na ndiyo maana tulipeleka utaratibu kwamba kila Halmashauri ianishe uharibifu wa miundombinu mara baada ya mvua ile kunyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu letu kubwa ni kuangalia sasa kile ambacho tunaweza kusaidia kwa kipindi cha sasa. Kwa hiyo, baada ya uharibifu huo, Serikali itachukua jukumu la kusaidia siyo maeneo ya Rungwe peke yake, isipokuwa maeneo mbalimbali ambayo yameathirika na nafahamu hata maeneo ya Morogoro hali ilikuwa mbaya sana na maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la Muheza liko sawa na sisi watu wa Rungwe Magharibi, katika Hospitali ya Makandana tuna shida ya watumishi wa afya, vile vile na usafiri kwa ajili ya wagonjwa hususan wanawake. Je, ni lini Serikali itawatazama wananchi hawa kuweza kutuletea wataalam ikiwa pamoja na gari jipya la wagonjwa kama mlivyofanya kwa watu wa Muheza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anavyosema Mheshimiwa Mbunge, siku ya Jumatatu nilikuwa katika Hospitali ya Makandana pale katika Wilaya ya Rungwe, nilitembelea Hospitali na nilibaini miongoni mwa changamoto mbalimbali katika Hospitali ile na kwa pamoja tukaangalia jinsi gani tutafanya kama Serikali kuweza kutatua changamoto zile. Ndiyo maana hata katika maagizo yangu niliwaeleza kwamba hospitali ile licha kwanza suala la madawa lakini suala la gari la wagonjwa na hata suala la ukusanyaji wa mapato katika hospitali ile haliko sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuta pale wanatumia mifumo ya analog, kutumia risiti ambayo kwa kiasi kikubwa inapoteza fedha nyingi za Serikali, ndiyo maana nimeagiza mwisho wa mwezi huu lazima wahakikishe wanatumia mifumo ya electronic. Kwa hivyo, haiwezekani hospitali kubwa kama ile wanakusanya sh. 3,000,000 kwa mwezi wakati kituo cha afya cha Kaloleni kinakusanya sh. 40,000,000 kwa mwezi!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunalifanyia kazi kwa upana wake. Kuhusu suala zima la miundombinu tumetembelea miundombinu, nina hakika maelekezo tuliyopeana siku ya Jumatatu tutaendelea vizuri na mwisho wa siku tutapata gari la wagonjwa ili hospitali yetu iwe katika mazingira mazuri na wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma bora ya afya.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Sophia Mwakagenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nataka kujua commitment ya Serikali juu ya benki hii ya wanawake ni lini itaiongezea ruzuku ili hiyo riba ambayo imekuwa ni kubwa iweze kuwa ndogo kuweza kusaidia kuwakopesha wanawake hasa wa vijijini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, commitment ya Serikali inajionesha wazi kwa Serikali kutenga bajeti ya shilingi bilioni moja kwenye mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuiwezesha benki hii kufungua dirisha maalum kwa ajili ya mikopo kwa wanawake. Hiyo ndio commitment yetu tunasubiri utekelezaji tu.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri katika suala, hili ninapenda kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vifaa hivyo anavyovizungumzia ambavyo vinasambazwa katika maeneo yetu ya zahanati, kwa Wilaya yetu ya Sumbawanga, Wilaya ya Nkasi, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini pamoja na Kalambo vifaa hivi havipo. Kama vinasambazwa vinasambazwa lini? Na je, Serikali itachukua mpango upi mkakati wa kuweza kufuatilia na kuhakikisha kwamba vifaa hivi vimesambazwa katika maeneo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba Mkoa wa Rukwa ni Mkoa uliopo pembezoni; ni Mkoa ambao hauna Hospitali za Wilaya. Hata juzi Mheshimiwa Malocha alizungumzia suala la Hospitali ya Wilaya, kwa maana ya kituo cha Rahela kipasishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado Mkoa wa Rukwa hauna Hospitali ya Wilaya, kwa hiyo ndio maana hospitali yetu ya Rufaa ya Rukwa inakuwa na msongamano wa wagonjwa wengi katika eneo lile.
Sasa ni lini Serikali itahakikisha zahanati zetu, vituo vyetu vya afya vinakuwa katika ukamilifu wake na vifaa tiba vyake ili kuondoa msongamano katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwamba vifaa vitasambazwa lini? Mpaka sasa tunavyozunguza, hatujaanza kuvisambaza vifaa hivi kwa sababu vifaa hivi 500,000 vinatokana na tamko alilolitoa Mheshimiwa Waziri wa Afya wakati wa bajeti kama mpango maalum. Bajeti imeanza kutekelezwa mwezi Julai na bado hatujapokea fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango huu mzuri ambao Waziri wa Afya ameuanzisha kwa majaribio mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa ambavyo vinapaswa kuja kwa utaratibu wa kawaida vimeendelea kupelekwa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini na hivi 500,000 ni kwa ajili tu ya kufanya majaribio ya kuona kama tukiwapa delivery packs akinamama wanaoenda kujifungua, pengine inaweza ikasaidia kupunguza changamoto mbalimbali zilizopo kwenye mfumo. Kwa hiyo, huu ni mpango mpya na maalum na bado haujaanza kutekelezwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu Vituo vya Afya na Zahanati kuweza kutoa huduma kwenye Mkoa wa Rukwa; kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge hili, ziara yangu ya kwanza ni Mkoa wa Rukwa. Mwezi uliopita kabla ya bajeti hii ya Bunge hili nilifika kwenye Mkoa wa Katavi. Baada ya Bunge hili nitafika kwenye Mkoa wa Rukwa kuona ni namna gani tunaweza tukashirikiana nao kuwawezesha kuanzisha huduma za upasuaji na huduma za maabara kwenye vituo vyote vya afya vilivyopo kwenye mkoa huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Hospitali za Wilaya, yeye kama Mbunge akishirikiana na Wabunge wa Majimbo, wanapaswa kukaa kwenye vikao vyao vya Halmashauri na kupanga mpango kabambe wa kujenga hospitali hizi na Serikali Kuu itawasaidia pale ambapo watakuwa wamekwama. Napenda watambue kwamba jukumu hili ni lao kama Halmashauri kuanzisha miradi ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya na sisi Serikali Kuu tunawajengea uwezo tu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa tatizo la Mara la vifaa tiba pamoja na gari la wagonjwa, ni kama la Rungwe. Napenda kujua commitment ya Serikali kwa Hospitali ya Makandana katika Wilaya ya Rungwe, ni lini watatuletea gari na kutuongezea vifaa tiba kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wa Wilaya ya Rungwe katika Hospitali ya Makandana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikupongeze na niwashukuru sana kwa dua zenu njema. Nakumbuka siku ile nilivyotoka kule baada ya kutoa maagizo kwamba mfumo wa kielectroniki ufanye kazi pale, baada ya muda fulani nikapata ajali, watu wakasema, watu wa huko wamekushughulikia? Nikasema hapana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana. Agizo langu nililotoa ndani ya mwezi mmoja lilitekelezeka katika hospitali ile na nilipata mrejesho kwamba makusanyo yamebadilika sana katika hospitali ile ya Makandana. Kwa hiyo, naomba niseme kwamba kweli nilitembelea pale nikakuta gari za wagonjwa hali yake sio nzuri sana. Tulibadilishana mawazo na bahati nzuri wana Mkuu wa Wilaya mzuri sana katika eneo lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nilichukue hili kwa sababu kuna vitu vingine tumeshaanza kuvizungumza kuona ni jinsi gani tutafanya kuboresha hospitali ile, tutajadili kwa pamoja ili hospitali hii iweze kupata huduma nzuri, kwa sababu kuna network nzuri ya Waheshimiwa Wabunge katika eneo hilo, mnaofanya kazi kwa pamoja kwa agenda kubwa ya hospitali yenu, basi naamini jambo hili tutalitatua kwa pamoja, kama mawazo shirikishi kuhusu tufanye nini katika mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa jibu la msingi la Mheshimiwa anasema Benki Kuu haiwezi kuingilia kutoa bei elekezi, tunawezaje kusaidia Benki ya Wanawake iweze kutoa riba ndogo kwa kupata ushauri kutoka kwenye Wizara yake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo, kwa mujibu wa sheria Benki Kuu haiwezi kutoa hiyo riba elekezi na napenda niseme kwamba riba hizi zilizopo ni kwa mujibu wa Sera ya Riba ya mwaka 1992. Kwa hiyo, lazima tuendane na sera tuliyoipitisha humu Bungeni ili kuweza kuhakikisha kwamba sekta ya fedha inafanya vizuri ndani ya uchumi wetu na kwa Benki ya Wanawake naamini Mheshimiwa Waziri wa Afya anaweza kulisimamia hili na kuweza kutoa riba ambayo ni nzuri, lakini hawezi kukiuka misingi ile iliyowekwa na Sera ya Riba ya mwaka 1992.
MHE. SOFIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tuliku-miss hekima zako.Kwa kuwa tatizo la wana Ngara linafanana kabisa na tatizo la watu wa Rungwe. Rungwe kuna vyanzo vingi sana vya maji, lakini tuna shida ya maji katika Vijiji vya Mpandapanda, Ikuti na sehemu nyinginezo. Je, Mheshimiwa Waziri anatusaidiaje tuweze kupata maji ukizingatia tunavyo vyanzo lakini watu bado wanahangaika kupata maji salama? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nimesimama kwa kutoa majibu ya ujumla kwa wale wengine ambao pengine watauliza swali linalofanana na la Mheshimiwa Sofia.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka huu, kama alivyosema Naibu Waziri kwamba kila Halmashauri tumepanga fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa miradi ya maji. Sasa katika Halmashauri yako, ninyi ndio mlipanga vipaumbele kwamba kwa mwaka huu mtapeleka maji kwenye Vijiji vipi?
Mheshimiwa Spika, tumetoa mwongozo kwamba kama mmeshapanga vipaumbele, tangazeni tenda ili tupate Mkandarasi aweze kufanya. Waziri wa Maji anafanya kazi ya uratibu, mtekelezaji ni Mkurugenzi wa Halmashauri ambayo wewe unatoka kule. Naomba tusaidiane kusimamia hawa Wakurugenzi kwenye Sekta ya Maji ili waweze kufanya kazi inayotakiwa wananchi wetu wapate maji.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, jibu la Mheshimiwa Waziri halijaniridhisha. Bodi ya Chai Rungwe imeweka wanunuzi wa chai wa aina mbili, wako WATCO na Mohamed Enterprises. Mohamed Enterprises amekuwa akinunua chai ya wakulima kwa bei nzuri na
WATCO ikawa inanunua chai kwa bei ya chini, lakini cha kushangaza Serikali ikaamua kumwambia Mohamed Enterprises aombe kibali upya, mpaka sasa tunaongea Mohamed Enterprises hana kibali cha kununua chai ya
wakulima na hii inapelekea wakulima kuuza kwa bei inayotaka Serikali ambayo ni ya chini.
Swali langu la kwanza, Serikali iko tayari kuvunja Bodi hiyo ili tuweze kupata watu tunaowaamini watakaotetea
wakulima wa chai wa Rungwe? (Makofi)
Swali langu la pili; Serikali iko tayari na Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kuonana na wakulima wa chai na kusikiliza kero za wakulima wa chai wanavyoteseka kwa muda mrefu? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na hilo la pili, nitakuwa tayari kuandamana naye muda wowote kuanzia sasa kwenda kusikiliza kero za wakulima wa chai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la nyongeza la kwanza, kama nilivyoeleza bei ya chai hupangwa kwenye mkutano wa wadau ambayo kawaida inakuwa ni bei ambayo tunasema ni bei dira. Maana yake ni bei ambayo hairuhusiwi mtu yeyote kumlipa mkulima chini ya hapo, lakini
Kanuni za zao la chai zinaruhusu majadiliano yafanyike kati ya mkulima na mnunuzi, maana yake wanaweza wakakubaliana bei kuwa juu ilimradi isije ikawa chini ya kile ambacho kimewekwa kama bei dira. Kwa hiyo, tofauti anayoiona Mheshimiwa Mbunge kuhusu wanachotoa WATCO na Mohamed Enterprises
inatokana na majadiliano yale ya ziada ambayo kanuni inaruhusu.
Mheshimiwa Spika, vilevile ningependa kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tofauti ya bei hutokana na ukweli kwamba kunakuwa na tofauti ya ubora wa chai moja kutoka mkulima mmoja hadi mwingine, kwa hiyo mara nyingine kuna makampuni yanaamua kulipa kitu tunachoita bonus au malipo ya ziada kutokana na ubora wa chai, ndiyo maana tunaendelea kuwashauri wakulima wetu wajaribu kulima chai kwa viwango vinavyotakiwa ili kuwa na ubora ambao utawafanya wapate bei nzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuvunja Bodi ya Chai kwa sababu hiyo, katika hali kama hii inakuwa ni vigumu kusema kwamba wao wanahusika moja kwa moja, kama nilivyosema kama Mheshimiwa Mbunge haridhiki na majibu ambayo nimeyatoa niko tayari kukutana naye ili niendelee kumuelewesha zaidi, pia kuandamana naye kwenda kwa wakulima wa chai.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, Halmashauri mara nyingi tatizo la fedha ni shida kubwa sana. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutuambia ni jinsi gani atahakikisha Ofisi yake inatimiza yale malengo ya fedha iliyoahidi kwenda kwenye Halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu usimamizi, aseme
kwa kina atazisimamiaje Halmashauri zake zisifanye ufisadi kwa kuwa, imekuwa ikijirudia mara kwa mara na kutuletea matatizo katika Halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunazungumzia suala zima la fedha na fedha hizi zinatafutwa kwa gharama kubwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
Naomba nimhakikishie, nilikuwa nikifanya ziara katika Halmashauri zote na nashukuru Mungu sasa nimebakiza chini ya Halmashauri 10 kuzipitia Tanzania nzima. Ajenda yetu ya kwanza ni suala la uadilifu katika usimamizi wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia na nimetoa maelekezo katika maeneo yote kwamba Wakurugenzi na Waweka Hazina sasa lazima wanapokwenda katika Kikao cha Kamati ya Fedha ambapo Madiwani na Wabunge ni Wajumbe hapo, lazima watoe taarifa ya transactions katika Halmashauri zao, fedha zilizopokelewa na matumizi yake yalikuwaje. Siyo kupokea lile kabrasha la mapato na matumizi ambapo Mbunge au Diwani anashindwa kujua ndani kilichokuwemo. Kwa hiyo, tumetoa maelekezo haya vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge ambao sisi ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha kwamba tukiingia katika vikao vyetu, tuweze kuzisaidia Halmshauri hizi kwa sababu sisi ndio wafanya maamuzi ambao tunawawakilisha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasihi Wabunge wote kwamba kwa moyo mkunjufu na moyo wa dhati tuzisimamie Halmashauri zetu, compliance iwepo na wananchi wetu wapate huduma na maendeleo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa takribani miaka miwili iliyopita kumekuwa kuna uhitaji mkubwa sana wa mafunzo ya ujasiriamali, lakini kumekuwa kuna walimu wanaofundisha chini ya kiwango. Serikali inasema nini kuwadhibiti walimu hao kwa kupunguza bei lakini pia kufundisha katika viwango ambavyo vinaweza kusaidia walaji ambao wengi ni wanawake?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, somo la ujasiriamali ni somo ambalo linaweza likafundishwa katika ngazi mbalimbali kama ambavyo wengi tunafahamu, ujasiriamali upo katika sura mbalimbali. Kuna ule ambao unakuwa informal ndio wajasiriamali hawa wadogo wadogo wanaanza, lakini kuna ule ambao unakuwa katika ngazi kubwa zaidi. Kwa hiyo kunaile kupata mafunzo ya awali na kupata mafunzo makubwa zaidi. Jambo kubwa ambalo ningependa leo Waheshimiwa Wabunge mlifahamu ni kwamba katika suala zima la ujasiriamali wengi tunafikiria ni ile kufanya biashara, kuuzauza labda vitu au maduka na vitu kama hivyo. Lakini ujasiriamali tunachotamani hasa watu wakifahamu, ni ile namna gani mtu anafanya shughuli zake kwa njia tofauti ili kuongeza thamani, kiasi kwamba hata Waheshimiwa Wabunge kufanya Ubunge pia ni ujasiriamali wa aina yake. Kwa hiyo, naomba tulizingatie katika sura hiyo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa nchi za Uturuki, Ujerumani na Italy wanakunywa sana chai ya Tanzania. Je, ni lini Serikali itapeleka Kiwanda katika Wilaya ya Rungwe kwa ajili ya wakulima wa chai ili waweze kuuza chai yao ambayo ni nyingi ikaweza kusaidia katika hizo nchi nyingine?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilonalo ni nguvu ya soko. Mheshimiwa Sophia tumeshazungumza kwenda kwenye maonesho ya Kimataifa kwenda kutafuta hayo masoko. Leta hizo order zako kusudi demand pool iwashawishi watu wachakate chai. Kuna watu wana chai hawana soko, sasa wewe nimeshakuruhusu uende kwenye maonesho. Nenda basi ulete hizo order. (Kicheko/Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Natambua katika Mkoa wa Mbeya tayari REA Awamu ya Tatu imeishazinduliwa, lakini kuna changamoto kubwa sana katika Wilaya ya Rungwe katika vijiji vya Lupoto, Katabe na Ibungu mpaka sasa hawajapata umeme na hatujajua ni lini watapata. Naomba majibu ya Serikali tuweze kujua ni lini Wilaya hizi zitapata umeme wa REA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nakushukuru ulivyouliza, hapa tunapoongea katika kijiji cha Lugota wakandarasi wanaendelea na kazi, kwa hiyo wanaendelea kupata umeme, lakini vijiji vya jirani pia tutavitembelea ambavyo bado lakini vijiji vyote ulivyotaja kwenye eneo lako vitapata umeme wa REA na umeanza mwezi wa tatu na kwako wewe utakamilika mwakani mwezi wa saba.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Swali la kwanza, kwa kuwa jibu la msingi la Serikali inakiri kwamba shamba hili lilipata hati kuanzia mwaka 1978 mpaka mwaka 1981.
Je, ni kwa nini Serikali haikuwa na hati ambayo leo hii mwekezaji huyu amekuwa akiwaonea wananchi wa vijiji hivyo tajwa alivyovitaja Mheshimiwa Waziri?
Swali la pili, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali akiwemo na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali binafsi siwaamini katika utekelezaji wao wa kazi zao. Je, Mheshimwa Waziri huoni umuhimu wa mimi na wewe kuongozana na kwenda kuwasikilisha wananchi na wanakijiji wa Nyelegete waliokataa kusikiliza mahusiano yao, mimi na wewe tukaenda kwa pamoja. Ni lini na utakuwa tayari tukaongozana kwenda kusimamia hili?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema ni kwa nini Serikali haikuwa na hati. Si kweli kwamba Serikali haikuwa na hati kama anavyosema, maeneo yote yanayomilikiwa na Serikali yanafahamika toka awali, na wanakijiji wanaozunguka eneo lile walitambua kwamba lile lilikuwa ni eneo la Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kumuuzia mmiliki mwingine tofauti na Serikali ili aweze kuishi vizuri na wanakijiji wanaomzunguka ni lazima ule uhakiki wa mipaka ufanyike kwa kuhusisha pande zote ambazo zinahusika katika mgogoro huo, kwa sababu huwezi ukampa tu wakati huo huo na wananchi pia nao walikuwa wanalitazama shamba lile.
Mheshimiwa Spika, lazima kufanya ule uhakiki wa mipaka ili kumfanya huyu mwekezaji ambaye yupo aweze kutambua mipaka yake vizuri. Kwa vyovyote unavyouza kwa mtu lazima umkabidhi eneo lako na kuhusisha kwamba ni wapi ambapo mipaka yako inaishia. Kwa hiyo, suala hilo nadhani linaeleweka kwa staili hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema habari ya kwenda Mbarali, nakumbuka mwezi Machi nilikwenda katika Mkoa wa Mbeya na Mbarali nilifika na suala hili lilizungumzwa, lakini kama bado halijatatuliwa na mgogoro bado upo, nadhani tutaangalia ratiba itakavyokuwa imekaa ili tuweze kuongozana na kusikiliza wale wananchi jinsi wanavyolalamika lakini najua chini ya mikono salama ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi masuala hayo yatatatuliwa. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa SIDO ndio wanaohusika kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo lakini imeonekana wanachaji pesa kubwa sana hasa mafunzo ya vifungashio. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie ni jinsi gani SIDO itapunguza bei na kusaidia hao wajasiriamali wadogo waweze kufanikiwa katika biashara zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kimsingi bei iliyokuwa inakuwa-charged ilikuwa inategemeana na gharama halisi za upatikanaji wa vifungashio hivyo. Jambo ambalo tunaweza tukafanya ni kuendelea kuangalia uwezekano wa kuipatia SIDO ruzuku ya kutosha lakini pia kuwakaribisha watu binafsi katika kutengeneza vifungashio hivyo kwa kadri itakavyowezekana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kutokana na jibu la msingi alilojibu Mheshimiwa Waziri ni kwamba ranchi ile imepewa wawekezaji wazawa, ni kweli; lakini wao wazawa wanawakodisha wananchi kulima na si kama vile mkataba unavyosema. Hiyo ni moja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkataba ni mkataba unaweza ukavunjwa kama unakiukwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuvunja huo mkataba na kuwapatia wananchi wafugaji wa Mbarali waweze kufuga kwani hawana nafasi za kufuga kutokana na maeneo tengefu kuzuiwa na Serikali? Naomba Serikali iwapatie wananchi waweze kufuga mifugo yao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni juu ya wawekezaji wanavunja mkataba kwa kuwakodisha wananchi. Jambo hili tumelisikia na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeweka mkakati kwanza kabisa tunathaminisha Ranchi zetu zote katika Taifa letu kwa kuangalia ile mikataba yote ambayo tuliwakodisha wawekezaji ambao hawakukidhi mahitaji yetu sawa na mikataba; tutavunja kwa kutangaza upya na kuwakaribisha wafugaji wote wenye uwezo wa kuweza kufuga kulingana na matakwa ya mkataba.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Mwakagenda anauliza kama tutawapa wananchi. Lengo letu sisi ni kuona kwamba ranchi hizi zinatumika kwa malengo mahususi; mosi ya kuhakikisha pia hata ranchi hizi zitusaidie katika kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima; lakini mbili, ranchi hizi ambazo zimetapakaa nzima, ziwe ni sababu kubwa ya kuongeza kipato katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, huu mkakati utakapokamilika na tutakapokuja nao; tunaomba Wabunge wote nchi nzima watupe ushirikiano ili tuweze kufanikisha ajenda hii ya kusukuma mbele tasnia ya ufugaji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri bado kuna shida katika ujenzi unaoendelea pale Ipinda, nilikuwa nataka kujua Serikali imefuatilia gharama ya pesa ilizotoa na uhalisia wa majengo yanayojengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ujenzi wa zahanati ni kitu kingine, lakini utendaji wa wafanyakazi ikiwemo madaktari ni shida hasa Zahanati ya Ikuti Rungwe na hapo Ipinda hakuna watendaji wa kazi. Ni lini Serikali itatoa wafanyakazi ikiwemo madaktari na hasa Madaktari Bingwa wa wanawake kusaidia wanawake wa Wilaya ya zahanati ya Ipinda lakini pia Zahanati ya Ikuti Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo:-
Katika swali lake la kwanza anauliza iwapo Serikali imefuatalia kujua gharama iliyotumika na majengo ambayo yamejengwa. Majengo ambayo yanajengwa ni kwa mujibu wa ramani ambayo imetolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na ni na suala ambalo matarajio yangu makubwa na Mheshimiwa Mbunge akiwa ni sehemu ya wananchi wa Halmashauri ile ni vizuri akatuambia ni sehemu ipi ambayo anadhani kwamba haridhiki, lakini mpaka sasa hivi ninavyoongea hata Mbunge wa Jimbo hajaleta malalamiko yoyote kwamba labda kuna ubadhilifu katika ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaongelea juu ya suala zima la upatikanaji wa wataalam, suala la kujenga majengo jambo moja na suala la wataalam jambo la pili, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni nia ya Serikali kuhakikisha pale tunapomaliza ujenzi na wataalam wapatikane kwa mujibu wa Ikama na jinsi mahitaji yanavyopatikana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sambamba na ufutwaji wa kodi wa vifaa vya watu wenye ulemavu, je, ni lini Serikali itawagawia bure walemavu kwenye kaya maskini vifaa vya uhafifu hauoni kwa watu wenye ulemavu wa macho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kadri vinavyokuwa vinapatikana, kwa hiyo, hili ambalo ameliuliza dada yangu Sophia nimhakikishie tu kwamba Serikali itaendelea kutoa vifaa hivi. Hata hapa, muda mfupi uliopita kama wiki mbili/ tatu/mwezi mmoja uliopita tumekuwa na hilo zoezi la kugawa vifaa hivi saidizi. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya hivyo kupitia bajeti zake lakini pia kupitia wadau mbalimbali wanajitokeza kusaidia kundi hili la watu wenye ulemavu (Makofi).
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, pamoja na majibu yasiyoridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, atakubaliana nami kwamba imekuwa ni kawaida kwa Serikali kutokuwalipa waathirika wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo Wilaya hii ya Kyela? Barabara hii toka imejengwa hakuna aliyelipwa mpaka sasa na ndiyo maana wananchi wamefungua kesi Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, imekuwa ni kawaida ya Serikali kutokulipa wananchi wengi katika Taifa hili wanapowabomolea kwa kigezo cha ujenzi wa barabara, wakati huohuo mmewawekea umeme na maji. Kama mlijua wameingia kwenye hifadhi ya barabara kwa nini mlitoa huduma hizo za kijamii? Nataka majibu ya Serikali ni kwa nini wanafanya hivyo, wananchi hawapati haki zao wakati wamekaa kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 50 katika eneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza, namuomba sana Mheshimiwa Mbunge aridhike tu kwa hatua ambayo Serikali inachukua. Kwa sababu hivi navyozungumza shilingi bilioni 1.008 zililipwa kwa wananchi ambao walikuwa wanaathirika na ujenzi wa barabara. Hao wachache waliobakia kwa sababu wamepeleka kesi Mahakamani, ni haki yao wasikilizwe na Mahakama ili waweze kupata haki zao.
Mheshimiwa Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba sisi kama viongozi tunalo jukumu kubwa sana la ku-influence wananchi wetu. Kwa hiyo, labda nikuombe tu kwa sababu hii kesi iko Mahakamani tuonane ili angalau nikupe mbinu za kushawishi wananchi hawa ili waweze kuondoa kesi yao na ikiwezekana huduma ya barabara iweze kupita kwa sababu ni muhimu sana katika ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba zimekwenda huduma kwa wananchi sehemu ambazo tunatekeleza miradi, inaweza kuwa kweli kwamba pale ambapo wakati mwingine ujenzi wa barabara haujaanza au hata kabla ya kuwa na mradi wa barabara, yaweza kuwa kulikuwa na huduma, lakini wakati sasa mradi wa ujenzi wa barabara unakuja ndipo sasa pale tunalazimika kufanya zoezi hili la kuweza kuwaondoa wananchi lakini na kuwapa haki zao kwa mujibu wa sheria.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nafikiri ukiliangalia kwa ukaribu unaweza ukagundua kwamba ni wakati gani huduma ilikwenda na wakati gani mradi huu wa barabara umekuja. Ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na shida ya walimu wa alama kwa ajili ya wanafunzi viziwi. Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha tunapata walimu zaidi kuweza kuwasaidia watu wanaotumia alama katika kujifunza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi hawa walimu ambao wanatumia alama nayo ni elimu maalum. Kwa hiyo, sisi tunalitazama kwa mapana yake yote na ndiyo maana nimesema kwamba katika hao walimu watakaoajiriwa, naamini na hao wanaotumia alama ni miongoni mwa hao wenye uhitaji maalum na watachukuliwa ili kuweza kuhudumia wanafunzi wanaohitaji walimu wenye kutumia alama.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itazuia wagombea Urais kutoa ahadi ambazo zinachukua muda mrefu kutekelezeka ikiwepo suala la zahanati na barabara? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, wagombea nafasi za Urais wanaenda kuuza sera kwa wananchi ili kwa sera hizo waweze kuchaguliwa. CCM ambao ndiyo tulichaguliwa na wananchi baada ya kuuza sera na ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais na katika kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais mkataba wake na wananchi waliompa kura ni miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shuhuda, tumekuwa tukipata fursa ya kujibu maswali juu ya maeneo mbalimbali ambayo ahadi za Mheshimiwa Rais zilishatekelezwa. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kuzuia ahadi hizo kwa sababu zimekuwa zikitekelezwa. (Makofi/Kicheko)