Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hamoud Abuu Jumaa (5 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichuke fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama kwenye Bunge lako Tukufu kwa mara nyingine, lakini pia niwashukuru wananchi wangu kwa sababu ndio ninasimama kwa mara ya kwanza, kwa kunirejesha tena bungeni kwa kipindi cha pili.
Vilevile nichukue fursa hii kukupongeza wewe kwa kazi kubwa ambayo unayoifanya hapa bungeni, waswahili wanasema; kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi; lakini wanasema raha tele, taabu ya nini? Lakini pia wanasema kwa nini uminyane na ukuta wakati malango upo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nichukue fursa hii na mimi niipongeze Serikali kwa maana ya Waziri, Naibu Waziri na wataalam wake wote kwa kuandaa bajeti nzuri yenye lengo kubwa la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2016 na hii imeonesha ushahidi hata katika kutenga bajeti ya maendeleo kwa mara ya kwanza tumetenga bajeti takribani asilimia 40. Hii yote inaonesha dalili njema ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Naamini fedha hizi zikienda vizuri na tukisimamia vizuri sisi Wabunge tunaweza tukafanya mambo makubwa zaidi, na hatimaye tukaleta maendeleo makubwa; na baadaye katika uchaguzi wa mwaka 2020/2025 tukapata kura nyingi na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi upo uwezekano mkubwa wa kuendelea kushika dola. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ningependa kuchangia katika suala zima la mabasi ya mwendokasi, lakini vile vile niipongeze Serikali kwa kuanzisha mpango huu wa mabasi ya mwendokasi japo kuwa ziko changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza na sisi wote mashahidi, lakini niseme tu jambo hili zuri na nichukue fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu na wote mashahidi tumeona amekwenda kupanda basi lile, Makamu wa Rais, Rais Mstaafu, ni jambo jema na ndio maana wanatamani na watu wengine waweze kwenda kupanda mabasi. Ziko changamoto mbalimbali, sisi wote mashahidi tunaona, kuna watu mbalimbali ambao wanavunja sheria, magari yanaigia katika njia ile ambayo hayaruhusiwi. Sasa ushauri wangu tuangalie Serikali ni jinsi gani ya kutunga sheria nyingine kali zaidi ili kusiingie tena na uharibu ambao mradi huu umeingia gharama kubwa na tumetumia pesa nyingi sana katika kuutekeleza mradi huu.
Lipo jambo lingine ninaloshauri, maana ya mabasi ya kwenda kasi, tungetafuta utaratibu, kwa mfano tungeanzisha basi lingine au mawili, matatu basi moja linatoka Kimara, linakwenda mpaka Posta, na lingine linatoka Posta mpaka Kimara. Pale Italy ipo moja treni inaitwa rapido ni treni ambayo inakwenda kwa spidi, sasa tukianzisha mabasi haya ya kwenda kasi mawili ili watu waweze kwenda kwa haraka zaidi, hata tukiongeza gharama kidogo itasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tusiishie hapo, mabasi yale sasa hivi yamesaidi kwa kiasi kikubwa kupunguza foleni Dar es Salaam na sisi wote mashahidi. Tungeanzisha kujenga hata yard pale moja ya kuegesha magari, kuna watu wanatoka maeneo mbalimbali, inawezekana wakaja pale wakaegesha magari yao, na baadaye wakapanda mabasi wakaenda Posta, mjini wakafanya shghuli zao na baadae wakarudi katika shughuli hizi za kawaida. Ili twende vizuri zaidi, Serikali ilikuwa na mpango wa kujenga barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Chalinze na baadaye kuelekea Morogoro. Naishauri mpango huu ufanywe haraka ziaidi tukijenga barabara ya njia sita itatusaidia sana kupunguza foleni. Kwa sababu leo ukitokea Dodoma, Morogoro na kuelekea Dar es Salaam ukifika Kibaha hapo katikati kuna kuwa na foleni kubwa. Kwa hiyo, tukijenga barabara ya njia sita itapunguza kwa kiasi kikubwa foleni za magari ili tuende vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala limezungumziwa sana na wenzangu suala la zima la CAG. CAG ameomba karibuni takribani shilingi bilioni 88 lakini pesa aliyopewa takribani shilingi bilioni 44; pesa hizi ndogo sana, nashauri na wenzangu wengi wamelizungumzia kwa kasi kubwa, naomba tu Serikali iangalie ni jinsi gani ya kuongeza fedha hizi kwa CAG ili tuweze kufanya kazi vizuri. Kwa sababu huyu ndio mwangalizi wetu akipata fedha ndogo hizi atashindwa kufanyakazi yake vizuri, kwa hiyo, naomba aweze kupata pesa hizo ziweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namba tu ni-declare interest mimi na Mheshimiwa Zungu wavaaji wazuri sana wa mitumba, sasa katika eneo hili naona mmeongeza kodi kubwa ya mitumba…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuweza kunifikisha mahali hapa na mimi leo hii niweze kuchangia hoja hii muhimu iliyopo mbele yetu. Napenda vilevile kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuandaa hotuba nzuri ya bajeti yenye mlengo chanya kwa mafanikio, maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii inatupa mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge, hakika ni mwelekeo mzuri na wa kupongezwa sana, kwani imezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015. Nichukue
nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kufanya ziara maeneo mbalimbali na nimshukuru pia kwa kufanya ziara jimboni kwangu Kibaha Vijijini, ziara zake zimekuwa na tija kubwa sana kwa maendelo ya wananchi, na kufungua fursa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia fursa hii kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kwa maendeleo ya Taifa letu, hatua ya kuhamia Dodoma na kuwa Mji Mkuu wa nchi yetu ni hatua nzuri na ya kuthubutu, kwani maamuzi yalishafanywa hapo awali na ilikuwa bado
utekelzaji tu. Yatupasa kuunga mkono jitihada hizi na kuishauri Serikali kwa namna yoyote katika uboreshaji wa mkakati huu ambao tayari umeshaanza kwa Wizara mbalimbali kuhamia Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kila mpango huja na changamoto zake, vivyo hivyo katika mpango huu wa kuhamisha Makao Makuu ya nchi yetu kuja Dodoma unachangamoto mbalimbali, changamoto hizi ni pamoja na mipango miji, barabara na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam na miji mingine leo hii tunaona kwa namna gani tulichelewa katika kupanga miji yetu na leo hii miji haijapangika, tumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo ni wajibu wetu kuzichukua kama fursa na kuja nazo Dodoma na kuziboresha hivyo kuepuka makosa yaliyofanyika katika miji mingine hususan mji wetu wa Dar es Salaam hayana budi kutokutokea katika Mji wetu wa Dodoma. Mipango Miji ipangwe vizuri, kutengwe maeneo ya viwanda, makazi ya watu, ibada, vituo vya mafuta, shule, hospitali, viwanja vya michezo na kadhalika, pia barabara zitengwe maeneo makubwa na ya kutosha ili kuepuka bomoa bomoa za kila mara ambazo tumekuwa
tukizishuhudia katika miji mbalimbali, mji wa Dodoma uwe ni mji wa mfano na wa kihistoria, mitaro ya kupitisha maji (drainage system) iboreshwe kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa mpango wa kutoa elimu bure wenye tija kubwa kwa wananchi wetu ili kila mtoto wa Kitanzania aweze kupata elimu. Uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma
umekua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na hapo awali ingawa bado zinahitajika juhudi zaidi kufanywa na Serikali ili hii dhana ya uwajibikaji iwe endelevu na yenye tija zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado tuna changamoto ya upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi. Napenda kuishauri Serikali yangu sikivu kuzichukua changamoto hizi kama fursa kwa kuboresha maeneo hayo kwa maendeleo ya wananchi wetu na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kugusia suala zima la ukuaji wa uchumi nchini. Serikali imeainisha ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2016/2017 unaonesha uchumi wetu unazidi kuimarika. Kwa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifika 7.0% mwaka 2016, pongezi kwa Serikali ila kuna changamoto nyingi sana katika ukuaji wa uchumi kwa ujumla na ukilinganisha na uchumi wa mtu mmoja mmoja, wananchi wengi ambao vipato vyao ni vidogo na maskini wamekuwa wakiendelea kulalamika hali ngumu ya maisha, mifumuko ya bei za bidhaa muhimu kama chakula na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ikiwaumiza sana wananchi na hivyo kutokuona umuhimu wa hizi takwimu za ukuaji ama nafuu ya maisha. Naomba kuishauri Serikali kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kukabiliana na changamoto hizi wanazokumbana nazo, Serikali iweze kusimamia vyema mifumuko ya bei isiyokuwa na tija na yenye kumuumiza mwananchi wa kawaida. Serikali isimamie kikamilifu bei za mazao ya wakulima ambao ndio nguvu kazi kubwa hapa nchini, wauze mazao yao kwa faida ya bila vipingamizi vyovyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo ni Serikali ilipoamua kusimamia bei la zao la korosho na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa wakulima kuuza mazao yao kwa faida nzuri. Hivyo naiomba Serikali ifanye pia katika mazao mengine nchi nzima ili wakulima wetu ambao kitakwimu
ndio wengi waweze kufaidika na kilimo, waondokane na umaskini na kuona faida hizi za ukuaji wa uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishazungumza sana na kuchangia humu Bungeni kwa umakini mkubwa na kuishauri Serikali kuwa viwanda ndio msingi mkubwa wa ukuaji wa uchumi na kumaliza kama si kupunguza tatizo la ajira. Naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kuja na kipaumbele hiki cha Tanzania ya viwanda. Na mimi nasema Tanzania ya viwanda inawezekana kwa kuungana sote na kuunga mkono jitihada hizi kwa manufaa ya nchi yetu ili tuondokane na changamoto nyingi tunazokabiliana nazo za ajira kwa vijana wetu ni lazima tuwekeze katika viwanda kwani malighafi mbalimbali tunazo hapa hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi tajiri kiuchumi duniani ni maamuzi ya uwekezaji wao katika viwanda kwa muda mrefu. Mkoa wetu wa Pwani una viwanda takriban 89, viwanda hivyo viko katika maeneo mbalimbali ya mkoa lakini mpango kazi wetu ni kuzidi kutafuta wawekezaji ili waje kuwekeza katika mkoa wetu hususan Kibaha vijijini kwani tuna maeneo makubwa yametengwa kwa ajili ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto mbalimbali katika sekta ya viwanda hususan katika utoaji wa vibali vya mazingira. Nashauri vibali hivyo vya mazingira viwe vinatolewa kwa eneo zima ili kuepuka usumbufu wa mtu mmoja mmoja kufanya maombi ya vibali hivyo. Kibaha
Vijijini kama nilivyosema hapo awali tuna maeneo ya kutosha ambayo tayari yameshatengwa kwa shughuli husika. Niliishauri Serikali humu humu Bungeni kuhusu suala la bandari kavu iliyopo Kwala, bandari hii iwe maalum kuegesha magari yote (used), kwa maana kuziondoa yard za kuuzia magari (used) ambazo zimezagaa kila kona ya Jijini Dar es Salaam na hivyo kuwepo sehemu maalum ya mtu akitaka magari (used) anajua wapi pa kwenda hili limefanyika katika nchi nyingi sana zilizoendelea kama Dubai na kadhalika, huwezi kukuta kila kona ya mji kuna yard ya kuuzia magari. Hizi yard zimekuwa zikiharibu mandhari ya miji yetu na uchafuzi wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo pia la bandari kavu kuwepo na upatikanaji wa spare tofauti tofauti za magari pamoja na mashine mbalimbali. Hiyo itapelekea kuondokana na maeneo ya mijini kutapakaa maduka ya spare hovyo kama ilivyo hivi sasa mtaa wa Shaurimoyo.
Hatua hii ikikamilika watu watajua wakitaka magari yaliyotumika yote ama spare zote basi wanakwenda Kwala Kibaha Vijijini na kufanya manunuzi. Itasaidia kuwa na sehemu moja tu ambayo utapata hitaji lako ama gari au spare.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili, Serikali tayari imeshaonyesha nia kwa kutenga maeneo kama ilivyo jimboni kwangu. Kilichobaki ni utolewaji wa elimu na uhamasishaji kwa sekta binafsi kuziona fursa hizi na kuzifanyia kazi. Hatua hii ikishakamilika Serikali itapata fursa ya kuanzisha njia ya treni kutoka Dar es Salaam mpaka Kibaha kuwarahisishia wananchi watakaokuwa wakienda bandari kavu hiyo. Serikali kupata fedha za uendeshaji, vilevile Mkoa wa Pwani hivi sasa umekuwa na watu wengi sana. Kupatikana kwa usafiri wa treni hiyo kutawasaidia watu wengi sana kutatua changamoto ya usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio changu cha muda mrefu ni miundombinu ya barabara na mambo mengine mengi, ila kuna hii barabara ya Makofia, Mlandizi na Mzenga ina miaka sita sasa tunazungumzia ujenzi wa barabara hii. Wananchi wamekuwa wakipata shida sana katika shughuli zao za kila siku kutokana na hii barabara, shughuli zao za kiuchumi zimekuwa zikizorota. Naiomba Serikali hii sikivu sasa katika bajeti hii wakamilishe ujenzi wa barabara hii. Wananchi wale na wao waone faraja na kuanza kutumia barabara nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii tunaomba fedha zitengwe na barabara hiyo iweze kukamilika. Hata hivyo, niipongeze Serikali kwa jitihada kubwa zinazoendelea kuzifanya kwa kuleta miradi mikubwa ya barabara za juu makutano ya TAZARA, daraja jipya la Salender, ujenzi wa barabara Dar es Salaam – Chalinze kiwango cha express way bila kusahau ujenzi wa barabara za juu (interchange) kwenye makutano ya barabara ya Ubungo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni hatua muhimu za kimaendeleo katika kukabiliana na changamoto ya msongamano wa magari. Vilevile Mji wa Mlandizi kutokana na kukua kwa kasi, kuna uhitaji wa makutano ya barabara ili kurahisisha watumiaji na kuufanya uwe wa kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa jitihada kubwa inazochukua katika kulinda na kufuatilia sekta nzima ya madini. Hatujachelewa bado na jitihada zilizoanzishwa na Mheshimiwa Rais ni mwanga tosha kwa sasa. Kazi imeanza na kama kulikuwa na upotevu wowote wa madini yetu au ukwepaji wa kodi sasa kila kitu kitakuwa wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuunda Tume Maalum ya kufuatilia suala zima katika sekta ya madini. Kama tutaitumia vizuri, basi Taifa litanufaika sana na kupata maendeleo katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Madini ni kitu ambacho hakipatikani kila sehemu au nchi madini ni bidhaa adimu sana, hivyo tukifanya maamuzi katika utulivu wenye tija basi hatua stahiki zichujuliwe na hizo
changamoto tuzichukue kama fursa na kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusimamie madini yetu yote kwa uadilifu mkubwa, zaidi madini ambayo hayapatikani sehemu yoyote duniani zaidi ya hapa kwetu tuyape thamani na kuyasimamia kwa faida ya Taifa letu ili pato la kodi liweze kuongezeka na kuleta maendeleo kwa wananchi. Vivyo hivyo, tuwawezeshe wachimbaji wadogo wadogo kwa kuwatolea kodi kwa vifaa watavyoagiza ili kuwapa motisha katika kazi zao za uchimbaji. Tuwathamini wazawa ambao ni wachimbaji wadogo kwani wametengeneza ajira hivyo kutokuwapa kipaumbele wao na kuwapa wageni tunawakatisha tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wafugaji na wakulima imeendelea kuibuka maeneo mbalimbali nchini na chanzo cha migogoro hiyo ni ardhi ambayo imekuwa ikigombaniwa. Naipongeza Serikali kwa jitihada zake katika kutatua na kupambana na migogoro hiyo, ila naishauri
Serikali kupitia watumishi wake, maafisa mifugo kuanza kutoa elimu kwa wafugaji kufanya ufugaji wa kisasa ambao hauhitaji kuwa na kundi kubwa la ng’ombe ambao baadaye madhara yake mfugaji anashindwa kuwa na chakula cha kujitosheleza na hivyo kupelekea migogoro kuibuka, kutoa elimu kwa wafugaji kulima nyasi zao wenyewe na kuzihifadhi vizuri ili kipindi cha kiangazi waweze kuzitumia nyasi hizo. Kufanya hivyo kutapunguza sana hii migogoro na kurudisha hali ya kuaminiana na kupendana baina ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sasa umepita tangu kuomba kuwekewa kivuko cha kuvukia watu na usafiri, Ruvu Station, Soga, Mpiji, Kwala, Magindu, kukosekana kwa vivuko hivyo kunapeleka wananchi kuwa katika hali ya hatari sana kwani maeneo hayo hayana alama
yoyote. Kwa kuwa kikwazo kwa wananchi kufanya shughuli zao za kila siku pindi wanapotaka kuvuka ama kuvusha vitu mbalimbali. Naomba katika bajeti hii sasa tupewe kipaumbele kwa maeneo hayo kuwekewa vivuko, vilevile kuna uhitaji mkubwa sana kwa maeneo tajwa hapo kuwa na vituo vya treni ili kuwarahisishia wananchi hawa pindi kukiwa na vituo kutakuwepo na fursa mbalimbali maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano bado imekuwa kubwa hapa nchini kwetu. Jimboni kwangu Kibaha Vijijini ni wahanga wa changamoto hii kwani kuna maeneo mengi hakuna kabisa mawasiliano ya simu kwa kuwa hakuna hata kampuni moja ya simu inayopatikana maeneo hayo. Dutumi, Mpelamumbi, Miyombo, Gwata, Msua hakuna mawasiliano kabisa. Tunaomba minara ya Tigo, Vodacom na Airtel, hakika kwa wananchi wangu hii imekuwa ni kero ya muda mrefu sana. Hata hivyo, naipongeza Serikali kwa hatua yake nzuri ya
kukamilisha kituo kimoja cha kuhifadhia taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centre) na Serikali haina budi kuzihamasisha Ofisi za Serikali kutumia mfumo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu zote nilizokuwepo humu Bungeni, nimekuwa nikilisema hili la Kituo cha Afya Mlandizi kupandishwa hadhi. Sifa na vigezo tunavyo. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Awamu ya Tano walitoa ahadi ya kukipandisha hadhi kituo hiki na kuwa
hospitali. Lakini Awamu ya Nne imepita bila kituo hiki kupandishwa hadhi. Sasa tuko Awamu ya Tano, naomba ahadi hii sasa itekelezwe kwani Mheshimiwa Rais akitoa ahadi, kinachofuata ni utekelezaji kwa mamlaka husika. Hivyo, mimi na wananchi wangu tungeshukuru sana katika
bajeti hii maombi yetu ya muda mrefu na ahadi za Marais wawili zilitekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimeona bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Ni jambo jema na la kupongezwa ila rai yangu kwa Serikali na mamlaka husika kumekuwa na changamoto za upungufu wa dawa katika vituo vyetu vya afya, zaidi dawa kuchelewa kufika kwa wakati. Naamini kwa ongezeko la bajeti basi changamoto hizi hazitakuwepo tena na kuleta nafuu kwa wananchi kupata dawa kwa wakati na kuwaondolea usumbufu wa kukosa dawa pindi wanapoandikiwa dawa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama yetu ya Kibaha Vijijini ina changamoto mbalimbali ila kubwa zaidi ni jengo. Jengo lake haliko katika hali nzuri. Katika michango yangu kila mwaka humu Bungeni, mbali na jitihada zangu binafsi za kuonana na Waziri mhusika nimekuwa nikilizungumzia takriban miaka sita bila matumaini yoyote. Naomba Serikali katika bajeti hii basi ituangalie kwa jicho la huruma na sisi tupate jengo la Mahakama. Napenda pia kuikumbusha Serikali kufikisha fedha za bajeti kwa wakati katika Halmashauri zetu kwani bajeti inapita lakini fedha zinachelewa na kuzorotesha shughuli za kimaendeleo. Fedha zikifika kwa wakati na miradi ya kimaendeleo itawafikia wananchi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, napenda kugusia kidogo suala zima la vita dhidi ya dawa za kulevya. Hili ni janga kubwa kitaifa na duniani kote. Dawa za kulevya zimekuwa zikiwaathiri hasa vijana wetu, nguvu kazi ya Taifa. Ndoto za vijana hawa zimekuwa zikisitishwa na kujiingiza katika kutumia dawa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, napenda kuchukua fursa hii kuipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonyesha dhamira ya dhati kabisa ya kupambana na vita hii. Kwanza kwa kuteua watendaji wakuu watakaosimamia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Mamlaka hii ina nguvu ya kukamata, kupeleleza na kushtaki watuhumiwa wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya. Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwezo wake mkubwa na upendo alionao juu yetu sisi sote kwa kutuwezesha kuwa mahali hapa katika kutimiza majukumu yetu ya kila siku, pia kuniwezesha nami kuchangia hotuba hii ya bajeti iliyo mbele yetu ya mwaka wa fedha 2017/2018. Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara kwa ujumla wake kwa kuandaa bajeti nzuri yenye mlengo chanya, bajeti hii inaenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, mahsusi kuleta maendeleo kwa wananchi wake na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio changu cha muda mrefu ni miundombinu ya barabara na mambo mengine mengi, ila kuna hii barabara ya Makofia - Mlandizi - Mzenga, ni miaka sita (6) sasa tunazungumzia ujenzi wa barabara hii, wananchi wamekuwa wakipata shida sana katika shughuli zao za kila siku. Kutokana na hii barabara kuwa mbovu shughuli zao za kiuchumi zimekuwa zikizorota. Naiomba Serikali hii sikivu katika bajeti hii wakamilishe ujenzi wa barabara hii ili wananchi wale na wao waone faraja na kuanza kutumia barabara nzuri. Katika bajeti hii tunaomba fedha zitengwe na barabara hiyo iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niipongeze Serikali kwa jitihada kubwa inazoendelea kuzifanya kwa kuleta miradi mikubwa ya barabara za juu makutano ya TAZARA, daraja jipya la Selander, ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam - Chalinze kwa kiwango cha expressway na bila kusahau ujenzi wa barabara za juu (interchange) kwenye makutano ya barabara ya Ubungo. Hizi ni hatua muhimu za kimaendeleo katika kukabiliana na changamoto ya msongamano wa magari. Vilevile Mji wa Mlandizi kutokana na kukua kwa kasi, kuna uhitaji wa makutano ya barabara ili kurahisisha watumiaji na kuufanya uwe wa kisasa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda mrefu sasa umepita tangu kuomba kuwekewa kivuko cha kuvukia watu pamoja na vyombo vya moto, Ruvu Station, Soga, Mpiji, Kwala na Magindu. Kukosekana kwa vivuko hivyo kunapelekea wananchi kuwa katika hali ya hatari sana kwani maeneo hayo hayana alama yoyote na kuwa kikwazo kwa wananchi kufanya shughuli zao za kila siku pindi wanapotaka kuvuka ama kuvusha vitu mbalimbali. Naomba katika bajeti hii sasa tupewe kipaumbele kwa maeneo hayo kuwekewa vivuko. Vilevile kuna uhitaji mkubwa sana kwa maeneo tajwa hapo juu kuwa na vituo vya treni ili kuwarahisishia wananchi hawa, pindi kukiwa na vituo kutakuwepo na fursa mbalimbali katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano bado imekuwa kubwa hapa nchini kwetu. Jimboni kwangu Kibaha Vijijini ni wahanga wa changamoto hii kwani kuna maeneo mengi hakuna kabisa mawasiliano ya simu. Kwa kuwa hakuna hata kampuni moja ya simu inayopatikana maeneo hayo ya Dutumi, Mpelamumbi, Miyombo, Gwata na Msua. Tunaomba minara ya Tigo, Vodacom na Airtel maana hakuna mawasiliano kabisa. Hakika kwa wananchi wangu hii imekuwa ni kero ya muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naipongeza Serikali kwa hatua yake nzuri ya kukamilisha Kituo Kimoja cha Kuhifadhia Taarifa na Mifumo ya Serikali (Government Data Centre) na Serikali haina budi kuzihamasisha Ofisi zote za Serikali kutumia mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki kama nisipoipongeza Serikali kwa hatua yake iliyoichukua siku si nyingi ya kuanza mradi mkubwa kabisa wa treni ya umeme ama treni iendayo kasi kama wengi walivyozoea. Huu ni mradi mkubwa na wa kihistoria katika nchi yetu. Mradi huu utarahisisha sana usafirishaji kwenye sekta ya reli, utapunguza muda wa kusafirisha mizigo na abiria kwani treni hii itakuwa inatumia muda mfupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu na maombi kwa Wizara, naomba mradi huu usiache kuwajali vijana wetu katika kutoa ajira kwa hatua hii ya awali ya ujenzi wa reli kwa (standard gauge), kwa maeneo yote reli itakapopita basi watu wa maeneo yale wasiachwe nyuma, wachukuliwe na kupewa ajira kwa mujibu wa taratibu na sheria kama zinavyosema. Haitapendeza kuona vijana wanatoka maeneo tofauti kuja kufanya kazi katika eneo ambalo nalo lina vijana wasiokuwa na ajira. Mradi huu uwe chachu na mfano kwa miradi mingine hata na nchi jirani ziweze kuiga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari yetu hasa ya Dar es Salaam imekuwa lango kuu na tegemeo kwa nchi mbalimbali zilizotuzunguka. Naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mageuzi makubwa ya kimkakati katika kuiboresha bandari yetu hii pia na bandari nyingine zilizopo ndani ya nchi yetu. Bandari ni chanzo kizuri cha mapato kama tu kikitumiwa vizuri na kwa uadilifu mkubwa. Hivyo basi hatua hizi zilizochukuliwa ziwe endelevu ili ziendelee kuleta tija kwa Taifa letu

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya kuamini na kuzikubali bandari kavu ila bandari kavu kama tukizipa kipaumbele zitakuwa na msaada mkubwa sana. Hapa nazungumzia bandari kavu za pembezoni mwa miji kama Jimboni kwangu Kibaha Vijijini tumetenga maeneo maalum kwa ajili ya bandari kavu na kama mpango huu ukifanikiwa ina maana utapunguza msongamano ambao uko mjini. Mfano niliwahi kuishauri Serikali humu humu Bungeni kuhusu suala la bandari kavu iliyopo Kwala, bandari hii iwe maalum kwa kuegesha magari yote (used), kwa maana kuziondoa yard za kuuzia magari (used) ambazo zimezagaa kila kona Jijini Dar es Salaam na hivyo kuwepo sehemu maalum ya mtu akitaka magari (used) anajua wapi pa kwenda. Hili limefanyika katika nchi nyingi sana zilizoendelea kama Dubai na kadhalika huwezi kukuta kila kona ya mji kuna yard ya kuuzia magari. Hizi yard zimekuwa zikiharibu mandhari ya miji yetu na uchafuzi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo pia la bandari kavu kuwepo na upatikanaji wa spea tofauti tofauti za magari pamoja na mashine mbalimbali. Hiyo itapelekea kuondokana na maeneo ya mijini kutapakaa hovyo maduka ya spea kama ilivyo hivi sasa katika Mtaa wa Shauri Moyo. Hatua hii ikikamilika watu watajua wakitaka magari yaliyotumika yote ama spea zote basi wanakwenda Kwala Kibaha Vijijini na kufanya manunuzi. Itasaidia kuwa na sehemu moja tu ambayo utapata hitaji lako ama gari au spea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili Serikali tayari imeshaonesha nia kwa kutenga maeneo kama ilivyo jimboni kwangu, kilichobaki ni utolewaji wa elimu na uhamasishaji kwa sekta binafsi kuziona fursa hizi na kuzifanyia kazi. Hatua hii ikishakamilika, Serikali itapata fursa ya kuanzisha njia ya treni kutoka Dar es Salaam mpaka Kibaha ili kuwarahisishia wananchi watakaokuwa wakienda katika bandari kavu hiyo na Serikali kupata fedha za uendeshaji. Vilevile Mkoa wa Pwani hivi sasa umekuwa na watu wengi sana, kupatikana kwa usafiri wa treni hiyo kutawasaidia watu wengi sana na kutatua changamoto ya usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya teknolojia yamekuwa yakikua siku hadi siku na Taifa hatuwezi kukwepa ukuaji huo. Ndio maana takwimu za watumiaji wa mawasiliano zimezidi kukua siku hadi siku. Serikali imejaribu sana na inaendelea kujitahidi kuimarisha miundombinu yake na kuwasisitiza wadau wa mawasiliano pia kuzidi kuongeza jitihada mahsusi kwa ajili ya kuleta tija. Leo tunaona Serikali imezitaka kampuni zote za simu za mikono kutoa hisa kwa wananchi na wao kuwa ni wamojawapo wa wamiliki wa haya makampuni lakini bado kuna changamoto katika hili kwani uhamasishaji wa kununua hisa hizo umebaki kwa makampuni yenyewe na si Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali nayo kutilia mkazo juu ya kuhamasisha wananchi ili kuleta nguvu na imani kubwa kwa wananchi wetu. Vilevile naishauri Serikali kuzidi kuchukua hatua stahiki kwa wale wote wanaokiuka sheria na taratibu zilizowekwa kisheria ili kuzifanya sekta hizi kufanya kazi zake kwa kufuata taratibu, sheria na misingi iliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini si kwa umuhimu, naipongeza Serikali kwa juhudi ilizozifanya na inazoendelea kuzifanya kwa shirika letu la ndege. Shirika hili lina historia yake kubwa sana lakini hapa miaka ya karibuni historia hii ilitaka kufutika lakini sasa tuna ndege zetu na nyingine zimeagizwa zinakuja muda wowote. Hatua hii ni ya kujivunia sana na ya kihistoria. Ushirikiano na makubaliano waliyokubaliana kati ya nchi mbili za Ethiopia na Tanzania katika nyaja mbalimbali hususani ya ushirikiano wa mashirika yetu haya ya ndege ni hatua nzuri ukizingatia wenzetu shirika lao ni kubwa na lina historia ndefu. Hatua hizi zote si za kubezwa kwani zitasaidia kuliimarisha shirika letu la ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue fursa hii ya kipekee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwepo mahali hapa. Vilevile ninamshukuru Mungu kwa kunipa nguvu na nafasi hii na mimi nichangie hotuba hii ya bajeti ya mwaka 2017/2018 ambayo inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Mawaziri pamoja na wataalam wao kwa kuandaa bajeti nzuri yenye kukidhi mahitaji na kutatua kero zilizopo katika sekta nzima ya afya. Bajeti hii inatekeleza Ilani ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi. Katika misingi hiyo ilani yetu imezungumzia utekelezaji wa sekta ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa juhudi zake za dhati kabisa katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kila eneo la nchi yetu, pia kuhakikisha maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto yanazingatiwa kwa mujibu wa sheria zetu na taratibu zilizopo. Kwenye kila jambo lolote la kimaendeleo halikosi changamoto na changamoto hizo yatupasa Serikali kuzichukua kama fursa katika kuhakikisha zinatatuliwa na kuboresha huduma kwa manufaa ya wananchi wetu. Bado tumekuwa na matatizo ya upungufu wa wahudumu wa afya katika zahanati zetu hasa maeneo ya vijijini. Mapungufu haya yamekuwa yakileta kero kwa wananchi wetu kwa kukosa huduma kwa wakati. Kumekuwa pia na upungufu wa madaktari ilhali tunao madaktari wengi waliomaliza vyuo na kufaulu vizuri lakini hawana kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali iajiri watumishi hawa kwa wingi ili waende katika maeneo mbalimbali kuhudumia wananchi. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwapa ajira madaktari takribani 250 ingawa Wizara hii imesema haina fedha za kuwalipa mishahara, lakini Rais kafanya uthubutu ili wataalam hawa waende kuwahudumia


wananchi. Naishauri Wizara kuchukua hatua madhubuti na kutafuta vyanzo vya fedha ili iweze kuajiri wataalam wa afya wengine. Kufanya hivyo kutasaidia sana kumaliza tatizo hili la muda mrefu la upungufu wa wataalam hawa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawasawa na hilo, Wizara iweke mkakati wa kujenga nyumba za wataalam wa afya hasa vijijini, mfano katika Jimbo langu la Kibaha Vijijini tuna changamoto kubwa sana ya uhaba wa nyumba za watumishi wa afya na imekuwa kawaida kwa watumishi hawa wakipangiwa kuja katika maeneo ya kwetu, hufika kuripoti na punde wakigundua mazingira siyo rafiki, kwa maana hakuna nyumba basi huondoka kwa kusema wanaenda kuhamisha vitu watarudi, lakini hawatokei tena. Hali hii inarudisha nyuma juhudi tunazochukua kama viongozi katika kujitolea huku Serikali ikilalamika kila siku haina fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya vijijini ndiyo kumeonekana kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa nyumba, nafikiri watumishi hawa wanastahili kabisa kukaa sehemu nzuri, Wizara lazima iwe na mkakati wa kujenga nyumba za watumishi hawa wa afya ili kwao iwe motisha na kutoa huduma kwa mazingira yaliyo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ninaishauri Serikali ihakikishe inaongeza kujenga vituo vya afya ili kuepusha wananchi kutembea umbali mrefu kufuata vituo hivyo vya afya, kwani vimekuwa vikisababisha vifo vya watoto wakati wa kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Jimboni kwangu Kibaha Vijijini tumetenga kabisa maeneo ya kujenga vituo hivi, hivyo katika bajeti hii naomba Wizara kupitia Serikali kumaliza changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la watoto kuzagaa mitaani nimelisema sana humu Bungeni katika nyakati tofauti na changamoto hii bado ipo. Wizara hii ndiyo wahusika wakuu wa kuchukua hatua na kuhakikisha watoto wote wanakuwa katika vituo maalum siyo kuzagaa mitaani


kuomba omba. Hata hivyo naishauri Serikali kuwachukulia hatua baadhi ya wazazi wa watoto hawa ambao wao ndio wamekuwa wakiwatuma kwenda kuomba na wao wazazi kukaa pembeni. Ni jambo la aibu sana kwa nchi yetu kwani mambo haya yameshapitwa na wakati katika dunia ya leo.

Napenda kugusia pia suala la wazee, natambua uwepo wa vituo vya wazee maeneo mbalimbali hapa nchini, vituo hivi vimekuwa havitengewi bajeti ya kutosha na Serikali na zaidi vituo hivi vimekuwa vikitegemea misaada kutoka kwa jamii. Nafikiri ni wakati sasa Serikali ikachukua hatua kwa kutenga fedha mahsusi kwa ajili ya vituo vyote vya kulelea watoto na wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu zote nilizokuwepo humu Bungeni, nimekuwa nikilisemea hili la Kituo cha Afya Mlandizi kupandishwa hadhi, sifa na vigezo tunavyo, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Awamu hii ya Tano walitoa ahadi ya kukipandisha hadhi kituo hiki na kuwa hospitali, lakini Awamu ya Nne imepita bila kituo hiki kupandishwa hadhi, sasa tuko Awamu ya Tano naomba ahadi hii itekelezwe, kwani Mheshimiwa Rais akitoa ahadi kinachofuata ni utekelezaji kwa mamlaka husika. Hivyo mimi na wananchi wangu tunashukuru sana katika bajeti hii maombi yetu ya muda mrefu na ahadi za Marais wawili zikitekelezwa.

Mimi kama Mbunge najitahidi sana kujitoa kwa hali na mali katika kuhakikisha majengo na vifaa mbalimbali vinapatikana katika vituo vyetu vya afya, kama sasa kuna ujenzi wa ukuta kwa maana uzio katika kituo cha afya Mlandizi na hizi ni juhudi zangu kama Mbunge, hivyo Serikali ikituunga mkono katika mambo mazuri kama haya basi na sisi viongozi pamoja na wananchi tunafarijika sana na kupata moyo wa kuzidi kujitolea.

Hata hivyo nimeona bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/ 2016 hadi shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017, ni jambo jema na la kupongezwa ila rai yangu kwa Serikali ni mamlaka husika


kumekuwa na changamoto za upungufu wa dawa katika vituo vyetu vya afya, zaidi dawa kuchelewa kufika kwa wakati. Naamini kwa ongezeko la bajeti basi changamoto hizo hazitakuwepo tena na kuleta nafuu kwa wananchi kupata dawa kwa wakati na kuwaondolea usumbufu wa kukosa dawa pindi wanapoandikiwa dawa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwepo mahali hapa nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara husika kwa mwaka 2017/2018. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa katika Wizara hii. Pia nimpongeze Waziri pamoja na wataalam wake kwa kuandaa bajeti nzuri yenye mwelekeo chanya, bajeti hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze timu yetu ya Serengeti Boys kwa kuonesha mfano wa kufanya vizuri katika mechi zake zote, hii ni alama tosha na kuikumbusha Serikali kuwa mchezo wowote unahitaji uwekezaji kuanzia chini kwa maana ya kuanzisha vituo vya michezo na kukuza vipaji. Utaratibu huu umekuwa ukifanywa na nchi mbalimbali kama Ulaya, Amerika, Asia na Afrika ingawa sisi hatukuliona jambo hili kwa miaka ya hivi karibuni ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Mheshimiwa Spika, michezo hivi sasa ni ajira ambapo imeajiri vijana wengi sana na wamekuwa wakinufaika kama akina Mbwana Samata ambaye anaiwakilisha nchi vizuri sana huko Ulaya. Hivyo, niishauri Serikali bado hatujachelewa tuwekeze katika michezo kwani kuna faida nyingi sana ambazo zitakwenda kutatua changamoto kwa mfano za ajira.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa havifuati taratibu na sheria zilizowekwa. Hata Mheshimiwa Rais aliwahi kulisema hili kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikivuka mipaka. Habari au uandishi kwa kuzungumzia hapa tunaweza kuona ni vitu vya kawaida tu lakini uandishi wa habari wa aina hasi unaweza kuliingiza Taifa katika machafuko makubwa sana. Mifano iko mingi sana ambayo vyanzo vya machafuko ni vyombo vya habari. Habari zinaenea kwa urahisi sana kuliko kitu chochote na sumu yake ni kali sana.

Mheshimiwa Spika, hivyo, tunahitaji kuwa makini sana na vyombo vyetu vya habari ambavyo habari zake ziko katika malengo hasi, habari zake si za kujenga nchi, wala za kimaendeleo, tuviangalie vyombo ambavyo vinatoa kipaumbele kwa habari binafsi ambazo hazina tija kwa Taifa. Serikali sasa kupitia Wizara ni wakati wa kuchukua hatua kali bila woga wala aibu kwa chombo chochote cha habari ama iwe redio, magazeti au televisheni ambacho kinakiuka taratibu na sheria zilizowekwa. Vinginevyo tukivionea haya na nchi ikaingia katika machafuko kutokana na vyombo vya habari basi ni sisi viongozi ndiyo tutakuwa wa kulaumiwa kwa sababu tulipewa dhamana ya kuvisimamia lakini kwa utashi wetu tukashindwa.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia utamaduni huwa tunazungumzia tamaduni ya nchi au mahali husika. Sisi kama Taifa tuna tamaduni mbalimbali lakini tamaduni hizi tumekuwa tukiziona tu katika maadhimisho mbalimbali vikundi vikikaribishwa kucheza ngoma na kadhalika lakini hakuna mkakati madhubuti uliowekwa wa kuhakikisha tamaduni zetu zinadumishwa kwa namna yoyote na kuzitangaza. Tamaduni zetu ni fursa kama tukizitumia vizuri kwa sababu wageni watakuja kuziangalia na sisi tumejaliwa kuwa na makabila zaidi ya 100, hivyo tamaduni tunazo nyingi sana. Naishauri Serikali sasa kuchukua hatua katika sekta hii pia ili kuiwezesha kukua na kuleta manufaa kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, juzi Jijini Dar es Salaam wasanii wetu wa Bongo Movie waliandamana na dhumuni lao ni kuzuia filamu za nje kutokuuzwa nchini na kuzipa kipaumbele filamu za kwao. Nina ushauri mzuri kupitia Wizara hii naamini utawafikia. Kuzuia filamu za nje sio utatuzi bali wasanii wetu wanatakiwa kuangalia ni wapi walipokosea mpaka soko lao likashuka. Bila kujua walipokosea na kujirekebisha haitakuwa suluhisho kwao kwani hata wakizuia hizo filamu za nje na zikabaki za kwao tu pia soko halitakuwa zuri.

Mheshimiwa Spika, wananchi wamekuwa wakilalamika sana kuhusu ubora wa filamu za ndani kuanzia kwa waigizaji, vifaa wanavyotumia na matukio katika filamu zao. Ninavyofahamu, filamu haiwezi kutengenezwa kwa miezi miwili halafu ikawa tayari sokoni, ni ngumu kuingia katika ushindani wa soko la filamu hata tu la Afrika Mashariki. Hatuwezi ndugu zangu ni lazima tuishi kwa kujifunza, asiyetaka kujifunza lazima atakuwa na mawazo mgando.

Mheshimiwa Spika, hivyo tuwape elimu vijana wetu wa Bongo Movie kuacha kuharakisha filamu kwa miezi miwili au mitatu kuitoa sokoni huku ubora ukiwa finyu. Hakika wakibadilika watauza kwani hapo nyuma walikuwa wakifanya vizuri katika soko hili hili la filamu. Kama nilivyosema hapo awali ni wakati wao kujiuliza ni wapi walipokosea na kujipanga.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.