Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Susanne Peter Maselle (3 total)

MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika,Serikali inatoa kauli gani kwa Jeshi la Polisi kupitia askari wasio waadilifu wanaokamata watu hasa viongozi na wafuasi wa UKAWA na kuwaweka mahabusu kwa zaidi ya saa 24 bila kuwapeleka mahakamani wakijua kwamba wanavunja sheria kwa kuwabambikizia kesi za uchochezi na CyberCrime? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linapokamata watu huwa haliangalii itikadi zao na linapowafikisha watu mahakamani haliwaulizi kadi ya chama alichonacho, bali Jeshi la Polisi hukamata watu kufuatana na kosa alilofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa Watanzania wengine, akishakamatwa, kuna hatua ambazo zinafanyika na baada ya hapo anafikishwa mahakamani. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. SUSANNE P. MASELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Ni lini sasa Serikali itaondoa hii dhana ambayo imeanza kujengeka kwamba Serikali haiwezi kuajiri kwa sababu haina fedha na kwamba Mheshimiwa Rais ndiye amekuwa akiajiri kwa utashi wake bila kufuata sheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali inajigamba kwamba imekusanya mapato mengi na imeondoa Wafanyakazi hewa, lakini ni kwa nini haijapandisha mshahara wala kupandisha watu madaraja? Serikali iwaambie Watumishi, ni kwanini haifanyi hivyo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa napenda kusema hakuna dhana kwamba Serikali haina uwezo wa kuajri. Wote mnafahamu katika mwaka wa 2015/2016 mazoezi yaliyokuwa yakiendelea katika uhakiki, lengo letu kubwa lilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na idadi ya rasilimali watu ambayo tuna uhakika nayo, pia kujiriddhisha fedha ambayo tunalipa kama kweli ni thamani ya fedha kulingana na rasilimali ambayo ipo kazini.
Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa kufanya hivyo, tumeweza kuondoa zaidi ya watumishi hewa 19,708 ambao endapo wangeendelea kubaki katika orodha ya malipo ya mshahara, wangeisababishia Serikali hasara kila mwezi ya zaidi ya shilingi bilioni 19.8 fedha ambazo zingeweza kwenda kutumika katika miradi mingine ya maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia tu katika mwaka huu wa fedha, tayari katika bajeti yetu tuliji-commit kama Serikali kwamba tutatoa ajira katika mwaka huu wa fedha 2017/ 2018 zaidi ya ajira 52,436. Pia tumeshaanza, ukiangalia katika mwaka huu wa fedha ambao tulikuwa tunaumalizia mpaka Julai, tayari tumeshatoa zaidi ya vibali vya ajira 10,184 na zaidi ya vibali vingine 4,816 pia viko katika taratibu za kutolewa kwa ajili ya kuziba mapengo yaliyojitokeza kutokana na suala zima la vyeti vya kughushi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala zima la kupandisha mishahara pamoja na vyeo au madaraja; katika suala la mishahara, mwaka huu kilichofanyika na nimekuwa nikilisema mara nyingi, ni kweli hatujapandisha mishahara. Hatujapandisha mishahara kwa sababu bado tunaendelea kuangalia hali ilivyo, pia na hali ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, tulichokifanya kwa mwaka huu ni nyongeza ya miashahara ya mwaka ambayo ni annual increment na wakati wowote kuanzia sasa nyongeza hiyo ya mishahara ya mwaka itaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa madaraja, tayari fedha ilishatengwa. Kuna zaidi ya shilingi bilioni 660 zimeongezeka katika bajeti ya mwaka huu ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2016 iliyokuwa shilingi trilioni 6.6. Mwaka huu tumetenga zaidi ya shilingi trilioni 7.205 na hii itasaidia kulipa maadeni ya watumishi, itasaidia pia kupandisha watumishi zaidi ya 193,166 na tunaamini wakati wowote stahiki hizo watumishi wataweza kuzipata.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo maelezo ya Serikali na hakuna dhana iliyojengeka kwamba hatuwezi kuajiri wala kupandisha mishahara. (Makofi)
MHE. SUSANNE P. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, baada ya taratibu kukamilika, je, Serikali itachukua muda gani kuwapatia leseni wachimbaji hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, yamejitokeza madai kuwa zuio la mchanga pale bandarini makinikia halikuwagusa wachimbaji wakubwa tu hata wadogo pia.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wachimbaji hao wadogo wanasafisha mchanga wao hapa nchini ili kuendeleza uwekezaji na kutengeneza ajira zaidi kwa wachimbaji hawa wadogo? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itachukua muda gani, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba, taratibu za kuunda Tume ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya leseni ya uchimbaji madini, iko katika hatua za mwisho za kuundwa. Mara itakapokamilika kazi hiyo itaanza mara moja, kwa hiyo, haitachukua muda mrefu sana baada ya Tume hiyo kuwa imeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la zuio la mchanga, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Watanzania, kwamba Sheria ya Madini haijazuia usafirishaji wa michanga nje ya nchi isipokuwa zipo taratibu na sheria ambazo yule mtu anayetaka kusafirisha mchanga kama madini lazima azifuate kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tumezuia yale makontena kwa sababu yalikuwa na mgogoro ambao Serikali tuliona kuna haja ya kujiridhisha kabla ya kuruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekti, kama kuna wananchi ambao wana madini ya mchanga ambao wanataka kuyasafirisha kwenda nje ya nchi kama wengine ambavyo wanapata vibali na wao wafuate taratibu watapewa vibali. (Makofi)