Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tunza Issa Malapo (9 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu na Chama changu makini CHADEMA kwa kunipa nafasi hii. Pia napenda kuwapa pole wananchi wa Mtwara Mjini kwa kadhia ya mvua waliyoipata siku ya jana, lakini hii yote imesababishwa na miundombinu mibovu iliyowekwa na Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia mpango huu nitajikita katika mambo mbalimbali. Mtwara imewekwa katika eneo la uwekezaji kwa maana ya viwanda, lakini tatizo kubwa la Mtwara ni maji ya kutosha kuhudumia viwanda. Mtwara Mjini kuna mradi unaotakiwa utoke Mto Ruvuma kuja Mtwara Mjini kuleta maji. Huu mradi umepitia process zote, kilichobaki ni kuwekeana saini kati ya Serikali ya China kupitia Exim Bank ya China na Wizara ya Fedha ya Tanzania, lakini huu mradi ulitakiwa uanze tangu mwezi wa Saba mwaka 2015 lakini mpaka leo haujaanza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri unayehusika, tunaomba mlifuatilie jambo hili ili tuweze kupata maji ya uhakika yatakayotosheleza kwa ajili ya kuhudumia hivyo viwanda vyetu.
Hatuwezi kuhudumia viwanda mfano, Dangote maji anayoyahitaji na maji yanayopatikana sasa hivi, akipewa yeye, maana yake sisi wananchi wa Mtwara Mjini hatuwezi kupata maji ya kutosha. Lakini suala la maji Mtwara Mjini, Serikali hailipi Idara ya Maji. Kinachotokea ni nini? Watu wa Idara ya Maji wameambiwa wajitegemee, wanajitegemea vipi wakati Serikali pale Manispaa ya Mtwara Mjini inadaiwa Shilingi milioni 581? Pesa zinakwenda, mpaka Mkuu wa Mkoa nyumbani wake anadaiwa Shilingi milioni moja na ushee. Kwa hiyo, tunachokisema, Serikali wapeni pesa Idara ya Maji waweze kujiendesha ili hata hivyo viwanda vinavyokuja viweze kufanya kazi. Maji ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitaongelea elimu. Nasikitika sana, kila yanapotokea matokeo yawe ya Darasa la Saba, yawe ya Form Two, yawe ya Form Four na kwingine kote Mtwara lazima iingie kwenye kumi za mwisho. Hii ni aibu na ni fedheha kwetu, hatupendi. Nataka niwaambie, shule tatu katika mtihani wa Form Two zilizofanya vibaya, matokeo yaliyotoka juzi juzi zimetokea Mtwara. Mbili kati ya hizo, zimetoka Tandahimba ambako kuna shida kubwa ya maji; na watoto wanaohangaika wanafeli ni watoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Mtwara ya Viwanda wakati elimu yetu iko chini. Ndugu zangu tusifanye mambo yale yale kila siku, tusifanye kazi kwa mazoea. Mimi ni Mwalimu wa Walimu, naelewa vizuri. Nimekuwa nikifanya kazi na wanafunzi katika Shule. Mwanafunzi hawezi kusoma kwa kumtolea ada ya Sh. 20,000/= mwanafunzi ili aweze kusoma vizuri, anahitaji apate vitabu, anahitaji akae pazuri, anahitaji ashibe, anahitaji apate maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wetu wa kike wa Mtwara, mnawalalamikia wanaolewa mapema, amefika Form Two maji yalikuwa yamhangaisha, amefeli, kinachofuata ni nini?
MHE. TUNZA I. MALAPO: Kwa hiyo, Serikali tunaomba muweke kipaumbele kwenye upatikanaji wa maji. Huu mradi wa Mto Ruvuma utahudumia vijiji 26; miongoni mwao vipo Mtwara Vijiijini na huko Mtwara Vijijini kuna shule ya mwisho imetokea huko kama sijakosea. (Makofi)
inatumiwa Bandari ya Dar es Salaam, wakati sisi tuna eneo kubwa. Kwa kuja kuwekeza kule na kui-upgrade hii bandari tunaamini vijana wenzangu kama mimi watapata ajira za kutosha na kuondokana na umaskini ambao unawatala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho maana naona muda umeisha, nataka kusema, Chama cha Mapinduzi kilitengeneza majipu kwa miaka 55, sasa wameanza kuyatumbua hatujui watatumia miaka mingapi! Kwa hiyo, ninachosema, wala msiwaaminishe wananchi kwamba mnafanya kazi kubwa, hayo majipu mliyatengeneza wenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naomba suala la maji lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nauliza jambo moja, naomba ufafanuzi mtakapokuja kujumuisha. Suala la umeme; mimi najua mafuta yanakotoka bei inakuwa ndogo kuliko kwingine. Sisi Mtwara tunanunua mafuta bei kubwa. Kwanini umeme wote tunalipa sawa wakati unazalishwa kule kwetu? Tunalipa sawa na sehemu nyingine! Pia hilo naomba ufafanuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la elimu, mimi natambua kila Wizara ina Kitengo cha Sheria; na Wizara ya Elimu bila shaka itakuwa na Kitengo cha Sheria. Sasa kama Sheria za Elimu zimepitwa na wakati, zinaruhusu matamko ya Mawaziri yanayorudisha elimu yetu nyuma, Kitengo cha Sheria Wizarani wakae wachambue wasiwape Mawaziri mamlaka yanayodidimiza elimu yetu.
Mama yangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, hapa katika kuzungumza, wanazungumzia Shule za Sekondari na Shule za Msingi. Nataka nikukumbushe kwamba kuna Vyuo vya Ualimu, ndiyo huko nilikotokea mimi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu yenye matatizo katika tasnia ya Ualimu ni pamoja na Vyuo vya Ualimu. Watu wa Vyuo vya Ualimu naomba ukawasikilize. Sasa hivi wameingiziwa, kuna NACTE, kuna Wizara, kuna TSD, hawaelewi, wanayumbayumba. Nenda ukawasikilize, ujue matatizo yao, wanashindwa kufanya kazi. Nimetoka huko, mpaka nachaguliwa kuwa Mbunge, nilikuwa nafundisha Chuo cha Ualimu Mtwara kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea barabara. Sijui watu Mtwara tufanye nini ili mtusikie kuhusu barabara ya kutoka Mtwara Mjini, inapita Nanyamba, inapita Tandahimba, Newala Mjini mpaka Masasi. Tufanye nini ili mtusikie? Tunaomba mtujengee barabara. Korosho zinatokea huko kwa asilimia kubwa.
Mhesimiwa Mwenyekiti, vile vile Bandari yetu ya Mtwara kwanini hamtaki kui-upgrade? Kwa saabu ukisoma huu Mpango, asilimia kumi tu ndiyo inaonekana Bandari ya Mtwara na hizo nyingine, lakini asilimia kubwa
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. TUNZA I. MALAPO:Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika Wizara hii ya Elimu, mimi nitajikita zaidi kwenye vyuo vya ualimu kwa sababu nina experience huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vya ualimu wamebadilisha mtaala kwa mfano chuo ambacho kilikuwa kinafundisha diploma ya ualimu wa ngazi ya sekondari unakuta sasa hivi kimepangiwa diploma katika ngazi ya elimu ya awali. Mtaala huo umebadilishwa sijui kwa vigezo vipi, sijui kwa tafiti zipi sasa mbaya zaidi mtaala umebadilishwa, wakufunzi hawajui nini wanachotakiwa kufundisha, mtu anapewa kozi pale mwezi mmoja ama miwili unatafuta material hujui uanzie wapi, hakuna kitabu, hakuna rejea na kama rejea zipo zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza lakini wale watoto tunatakiwa tufundishe kwa lugha ya kiswahili; shida sio kutafsiri lakini ipi ni tafsiri sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukichezea elimu utafikiri ni kitu ambacho hakina msingi. Sera ya Elimu inasema elimu bure, Sera ya mwaka 2014 tumekubali elimu bure maana yake ni nini? Serikali inajinasibu wanafunzi wengi wanasajiliwa shuleni, shule za msingi lakini nataka niwaambie jambo la kusikitisha Mheshimiwa Ndalichako pita kwenye vyuo vya ualimu, nenda kaangalie capacity ya chuo ni wanafunzi 450 unakuta waliosajiliwa ni wanachuo 50; maana yake ni nini? Baada ya muda wanafunzi wale wa shule za msingi wataongezeka kuwa wengi lakini walimu hakuna, tunatengeneza kitu gani? Tusifanye vitu kwa siasa wakati tunaongezea wanafunzi pia tuhakikishe walimu idadi yao inaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongea kwa ushahidi nenda Chuo cha Ualimu Mtwara Kawaida kaangalie capacity ya chuo na kaangalie wanafunzi misuse of resources.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaitwa Wizara ya Elimu, Teknolojia na huko inaendelea. Jambo la kusikitisha sana tunapoenda kwenye vyuo vya ualimu mtandao wa internet hakuna wa uhakika, maana yake mwalimu huyo hana vitabu vya uhakika, mtandao wa internet hakuna na kulikuwepo na programu inaitwa ICT implementation in teacher education.
Mheshimiwa Waziri unapokuja kuhitimisha naomba nipate ufafanuzi programu ile imefikia wapi, ukienda kwenye vyuo vya ualimu utakuta kuna kompyuta nyingi ni mbovu, mtandao wa internet hakuna kabisa, naongea kwa ushahidi, walimu wale mnataka wafanye kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia elimu hatuwezi kumuacha mwalimu. Wakufunzi wa vyuo vya ualimu na vyuo vya ualimu kwa ujumla wake vimeingia kwenye mfumo wa NACTE ingawa mimi sijui na sioni utekelezaji wake,
lakini mfumo ule wa NACTE una stahiki zake lakini mpaka leo tunapoongea baadhi ya wakufunzi wa vyuo vya ualimu wanalipwa kwa stahiki za Wizara ya Elimu, wanafanya kazi mpaka muda wa ziada kwa sababu ule mfumo una mambo yake, mwisho wa siku mtu analipwa kama bado anahudumiwa na Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka ufafanuzi wale watu wapo katika mlengo gani, kama mmeamua kuwapeleka NACTE wapelekeni NACTE na stahiki zao zote na kama mnaamua wabakie Wizara ya Elimu basi wabakie na stahiki zao zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza vyuo vya ualimu ni vichache siji tatizo ni nini, mnashindwa kukaa mkajua mahitaji ya wakufunzi mnashindwa kuboresha miundombinu, ukienda kwenye Chuo cha Ualimu Mtwara Kawaida nakiongelea kwa experience, mabwenini kule hali ni mbaya, unamfundisha nini mwalimu? Hali ni mbaya, miundombinu mibovu, madarasa yapo hayaeleweki yaani ule utanashati wa mwalimu unapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze kwenye vyuo vyote vya ualimu kulikuwa na shule za mazoezi, shule ya msingi ya mazoezi na shule ya sekondari ya mazoezi, lakini zile shule zote sasa hivi zimerudi TAMISEMI. Sasa naomba kupata ufafanuzi kila kitu ambacho kilifanya muanzishe shule shule za mazoezi ambazo sisi tuliokuwa tunafundisha kule tuliona umuhimu wake kwa nini sasa hivi shule hizo zimerudishwa kupelekwa TAMISEMI?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ule umuhimu umepotea ama kuna kuna kitu gani hapo kilichopo katikati? Tunaomba ufafanuzi kwa sababu mwenyewe nimesoma shule ya mazoezi ya msingi na katika miongoni mwa shule ambazo zilikuwa zinafanya vizuri ni shule za mazoezi na pia wale wanachuo wa ualimu walikuwa wanaenda kufanya practice kwenye shule za mazoezi. Lakini sasa hivi, ukitaka kuitumia ile shule ni lazima uende ukaombe kibali TAMISEMI na vitu kama hivyo, kwa hiyo kuna mzunguko mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo. Mheshimiwa Waziri juzi nimekuona ukiitumbua TCU, mimi nasema umechelewa sana kwasababu malalamiko yalikuwa mengi ya muda mrefu. Watoto wa maskini ambao wana stahiki ya kupata mikopo hawapati, watu wanapeana mikopo kwa kujuana, tunaomba hilo suala ulifuatilie na wale wote waliohusika wawajibike na wale ambao walishindwa kusoma kwa sababu ya mikopo na sifa wanazo tunaomba wasome kwa sababu ni haki yao ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenzangu asubuhi hapa ametoka kuongea, kuna vyuo vinafundisha masomo ya sayansi lakini havina maabara, Vyuo vya Ualimu. Tunategemea tunazalisha watu wa namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mwalimu leo unamfundisha kwa alternative to practical, unataka akifika shuleni umejenga maabara kwa kuwakimbiza wazazi, kwa michango mbalimbali, unataka akafundishe real practical, is it possible? If it is not possible we should be more serious ili elimu yetu tuione inapaa.
Mimi kila siku nasema masomo ya sayansi sio magumu ila mfumo wa elimu ya Tanzania ndio unapelekea masomo ya sayansi yawe magumu, masomo ya sayansi is very simple, ukipata mazingira wezeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaeongea hapa nimesoma PCB na nimefaulu kwani hao wanaofeli wamekosa kitu gani? Ni mfumo mbovu, mazingira mabovu, tunatakiwa tuone namna ya kuweka miundombinu yetu vizuri ili watoto wetu wasome kila mtu ana uwezo wa kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti …
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua Serikali imejipangaje katika mambo yafuatayo kwa Wizara hii:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya Ualimu baada ya kupelekwa NACTE vimekuwa vikikosa wananfunzi wa kutosha kulingana na capacity ya Chuo na ukilinganisha na idadi kubwa ya wananfunzi wanaosajiliwa katika shule za msingi kutokana na Sera ya Elimu Bure. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha nchi yetu inakuwa na walimu wa kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya Ualimu vimeingia NACTE, lakini stahiki za Wakufunzi bado hazijabadilishwa kuendana na mfumo wa NACTE. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wakufunzi nao wanapata stahiki zao vizuri bila ubabaishaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Je, Serikali imejipangaje kuzuia ombwe kubwa la Walimu kuacha kazi na kutafuta kazi nyingine hivyo kupelekea ukosefu wa Walimu hasa katika shule za Vijijini mfano, katika Mkoa wa Mtwara, ambao mimi ninauwakilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vyuo vingi vya Ualimu vinafundisha masomo ya sayansi, lakini havina maabara. Hivyo, kufanya ufundishaji na ujifunzaji uwe mgumu na kadhalika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maabara hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi kuwakopesha wanachuo, ambao wanasoma katika vyuo vya ualimu masomo ya sayansi, lakini haijafanya hivyo, ni kwa nini na kuna mpango gani uliowekwa kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezeka kwani inawanyima haki wanachuo hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vingi vya Ualimu havina mtandao wa internet wa uhakika. Je, Serikali inalijua hilo na imejipangaje kuhakikisha mtandao unapatikana ili kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji unaenda vizuri ukizingatia hakuna vitabu vya kutosha katika vyuo hivyo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya napenda kuzungumzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula. Hospitali ile imepandishwa kuwa ya Rufaa ya Mkoa lakini jambo la kusikitisha sana tena naomba mnisikilize na Mheshimiwa Kigwangalla nilikufuata nikakuuliza lakini haukunipa majibu. Hatuna mtaalam wa x-ray wa uhakika, vijana wetu wanapopata matatizo ya kuvunjika miguu na kadhalika, ni kama sawa mtu anaendelezwa kwenda kutiwa kilema, kwa sababu karibu watu wengi wanaofungwa mikopa (P.O.P) pale wanaopata tiba za mifupa hakika tiba zile siyo za uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha zaidi inabidi watoke kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa waende Ndanda ama Nyangao bila Rufaa kwa sababu zile ki-rank ni ndogo kuliko hii ya Rufaa ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtuangalie, mmeipandisha hadhi sawa tunashukuru, lakini tukienda kwenye wodi ya wazazi vitanda ni vichache mno, mtu ametoka kwenye uchungu wa kujifungua anaambiwa alale kitandani watu watatu. Nina uhakika ninachokizungumza, nilikaa pale wiki mbili namuuguza wifi yangu hali iko hivyo, haijalishi huyu mtu kajifungua kwa operation, ama kajifungua kawaida. Kwa hiyo, tunaposema hali ni mbaya ninamaanisha hali ni mbaya kwa sababu ni kitu ambacho nakijua nanime- experience. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu duka la MSD la Kanda ya Kusini linaenda kujengwa Ruangwa kwenye Jimbo la Waziri Mkuu, sina shida na hilo. Shida yangu kubwa iko wapi, kama kweli mnakujua Ruangwa, Ruangwa ni ndani barabara ile ya kilometa 45 kutoka Nanganga kwenda Ruangwa ni ya vumbi na kipindi cha masika hakufikiki. Barabara ile na Jimbo la Ruangwa lipo ndani haliunganiki zaidi na Wilaya zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini duka hili lisikae Masasi ambako ni centre mtu wa Tunduru analikuta, mtu wa Mtwara analikuta, mtu wa Lindi na anayetoka Newala analikuta, kwa nini lisikae pale mkaamua kwenda kulipeleka kule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kama mnaona kabisa ni lazima liende likakae Jimboni kwa Waziri Mkuu, mtengeneze zile kilometa 45 za barabara ili kusudi watu wanapoenda kuchukua madawa wasihangaike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa za watu wenye ulemavu wa ngozi. Siku ya maadhimisho ya wanawake nilienda shule ya msingi Masasi ambayo inatoa elimu jumuishi. Nimewakuta watoto pale takribani 39 wenye ulemavu wa ngozi, wana ari ya kujifunza lakini yale mafuta hawapati.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba muwafikirie watoto wale ili nao wapate haki yao ya elimu. Pia kuna watoto wenye uoni hafifu na ambao hawaoni kabisa lakini vifaa vya kujifunzia vya kutosha hakuna, hivyo wanashindwa kupata haki yao ya elimu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya nafikiri mna jukumu la kuhakikisha watoto wale wanapata haki yao ya elimu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mangaka ambayo inahudumia Nanyumbu. Hospitali ile imepandishwa hadhi kuwa ya Wilaya lakini haina x-ray. Kwa hiyo, naomba katika mpango wako Mheshimiwa Waziri, basi ufanye kila linalowezekana ili x-ray ile ipatikane iweze kuwahudumia watu wa Nanyumbu na majirani zao. Tunasema afya kwanza ili twende kwenye mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri ukurasa wa 76 amezungumzia suala la kuhakikisha wodi za watoto wachanga zinaanzishwa katika hospitali zote za rufaa. Namuomba Mheshimiwa Waziri suala hili lisiwe kwenye makaratasi na maneno… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami pia naungana na Wabunge wenzangu wa UKAWA kuona kitu kinachofanywa kulizuia Bunge hili lisioneshwe live si sahihi. Kwa sababu sisi ni wawakilishi wa wananchi, tumetumwa na wananchi kuja hapa kuwatetea, kuwasimamia na wanatamani watuone. Sijui hata huyo aliyeanzisha huu mjadala Bunge lisioneshwe live alichukua maoni kutoka wapi. Ama aliamka asubuhi kwa matakwa yake binafsi akaamua Bunge lisionehswe live. Mjue kabisa hamuwatendei haki wananchi, kodi zao mnachukua lakini hamtaki kuwatendea haki. Wananchi wanajua si kwamba ni wajinga kama mnavyowafikiria, kwa hiyo, hilo mkae kabisa mnalijua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kuchangia…
TAARIFA...
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili.
TAARIFA...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malapo, naomba uendelee.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niende moja kwa moja kuchangia kwenye TAMISEMI na naanza na elimu. Kwa masikitiko makubwa sana, kama kila siku ninavyozidi kusema mimi ni Mwalimu lakini tunapozungumzia suala la elimu, tunakuja humu ndani tunajitutumua kusema kwamba tumedahili wanafunzi wengi, tumedahili lakini output yake itakuwaje? Hilo ni swali la msingi la kujiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kitu cha kusikitisha, Mkoa wa Mtwara, wakati mnazungumzia Walimu hawana nyumba, lakini nataka kuwaambia katika ripoti ya Mkuu wa Mkoa ametuambia shuleni kuna upungufu wa viti elfu moja mia mbili kwenda juu. Kwa hiyo, Mwalimu huyo amelala sehemu mbaya, akienda shuleni pia hana sehemu ya kukaa. Tunavyolalamikia watoto wanakaa chini pia kuna Walimu wanakaa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, afya. Tukienda kwenye suala la afya kwa Mkoa wa Mtwara ni majanga. Natoa mfano mkubwa wa kusikitisha, ukienda Mtwara Vijijini kwenye Kituo cha Afya cha Nanguruwe mganga wa pale anatamani afunge kile kituo kwa ukosefu wa maji. Maji hayo pesa yake ilishatolewa shilingi milioni tano kurekebisha hitilafu iliyotokea ila kuna wajanja wachache wamekula. Kwa bahati mbaya hata ukienda kwa Mkurugenzi, sijui anamwogopa nani, hataki kutoa ushirikiano wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie suala la Kituo cha Afya Nanguruwe kwa sababu kituo kile kinahudumia watu wengi lakini mazingira yake ni mabovu, hakuna matundu ya vyoo ya kutosha, hakuna dawa, hakuna maji, wananchi wa pale kila siku wanalia. Naomba akifuatilie kituo kile ili tujue mwisho wake ni nini, watu wa pale wapate haki yao ya msingi kwa sababu na wao ni Watanzania wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye asilimia kumi kwa ajili ya akina mama na vijana, hili suala tunaomba lipewe kipaumbele. Ukienda Mtwara kwa tafiti zilizofanywa inaonesha asilimia 54 ya nyumba zinalelewa na akinamama kwa sababu labda waume zao wamefariki au matatizo ya ndoa yalitokea, kwa hiyo, wanahitaji wawezeshwe. Nami nasimama hapa kwa uhakika kabisa kusema kwamba wanawake na vijana wa Mtwara ni watu ambao wako tayari kutafuta maendeleo wanachokosa ni kuwezeshwa tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Wenyeviti pamoja na Madiwani. Unamlipa posho Mwenyekiti wa Mtaa Sh. 20,000 kwa mwezi tena si guarantee, kuna mwezi anapata, kuna mwezi hapati. Hata hivyo, tukumbuke kukitokea matatizo yoyote katika mtaa, Mwenyekiti ndiye wa kwanza kufuatwa na wananchi wake kwenda kulalamikiwa, tujiulize Sh. 20,000 anafanyia kitu gani? Diwani kwenye kata ana majukumu mengi mazito, posho mnayompa inamsaidia?
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiweke tungekuwa ni sisi, wewe Mheshimiwa Waziri sasa ndiyo ungekuwa Diwani unalipwa ile posho wanayolipwa ungeweza kuendesha maisha yako? Hii inaweza kuwapelekea wale watu kufanya mambo ya kupokea ama kutamani kupokea rushwa kwa sababu ni binadamu, wanahitaji kuishi vizuri. Naomba tuwaangalie kwa sababu Udiwani ndiyo kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye suala la masoko ambapo katika Halmashauri ya Mtwara Mikindani ni chanzo pia kikubwa cha mapato. Kwa masikitiko makubwa nimetembea kwenye masoko manne ya pale hakuna soko hata moja lenye choo cha uhakika. Wananchi pale wanatozwa ushuru, wafanyabiashara wale wanatozwa ushuru, wanalipa kila siku lakini hatuna choo cha uhakika kwenye soko lolote, naongea kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, tuna vizimba vya takataka vimejengwa kwa masikitiko makubwa, sijui hata huyo injinia alikuwa anafikiria nini, kuna kizimba kipo mtaa wa Magomeni, chini yake limepita bomba la maji kubwa na maji yanamwagika pale, takataka zinaoza, funza wanatoka, wananchi wapo karibu lakini tunaambiwa Injinia wa Manispaa amekuja kujenga pale wakati anajua chini limepita bomba. Tunaomba vitu hivi mfuatilie kwa sababu sisi kila tukisema inaonekana tunaongea kisiasa, hatuongei kisiasa, tunawaongelea wananchi wale wanaoendelea kupata shida kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia suala la maji katika Mkoa wangu wa Mtwara. Ukienda Jimbo la Nanyamba kuna shida kubwa ya maji. Sisi kule tunasema watu wanatumia maji ya kuokota. Ukisikia maji ya kuokota maana yake mtu anakuwa amechimba kisima cha chini halafu anaelekeza mifereji, yale maji ya mvua yanayotiririka barabarani yanaingia kwenye kisima. Mwisho wa siku huyu mwananchi anakuja kunywa yale maji, tutaepukaje kipindupindu, tutaepukaje magonjwa ya matumbo yanayosababisha dada zetu wasishike ujauzito kwa sababu vizazi vinaharibiwa? Hali hii hatuitaki na tunaomba irekebishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu ya muda, nataka niulize, Serikali ya Magufuli inafanya vizuri, kwa nini inaogopa kuwa transparency? Kwa nini haitaki kuonekana kama kweli inafanya vizuri, maana yake ina shida. Kama ingekuwa inajiamini Bunge lingeonekana live. Ninachosema, Serikali ya Magufuli haijiamini na ndiyo maana haitaki wananchi waone kinachoendelea. Hilo Bunge analosema linaoneshwa saa nne mimi jana nimeangalia, hakuna kitu, sasa mtu hapa anakuja kutuambia linaoneshwa, tuwe serious.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka niwakumbushe kidogo hili suala la vitabu kuonekana vina makosa humu Bungeni siyo jambo geni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Susan Lyimo alisema hapa kwamba hivi vitabu vina makosa na Mheshimiwa Simbachawene alitoka kule kuja kuangalia na akajibu kwa mbwembwe na kejeli kwamba anachokisema Mheshimiwa Susan Lyimo siyo kweli. Sasa Mwenyezi Mungu kila siku yupo na wanadamu, nashukuru tu kwamba tumeona, kila mtu ameona ama amesikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu, naomba uchukue hatua stahiki, tumepoteza pesa, lakini pia tumewapoteza watoto kwa maana wamepewa knowledge ambayo siyo sahihi. Wakati sijaingia Bungeni nilikuwa namsikia sana Mheshimiwa Mbatia anazungumzia mambo ya mtaala na vitabu vina mapungufu, lakini tumechukua hatua gani naona kila siku hali inazidi kuwa mbaya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Elimu nafikiri una jukumu kubwa la kuangalia na inawezekana kwenye somo la Sayansi labda alipelekwa mwalimu wa historia maana hivyo vitu vipo, watu wanaangalia zaidi mshiko (kipato) kuliko kuangalia maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Vyuo vya Ualimu mwaka jana nililizungumzia na leo ninalizungumzia. Mradi wa ICT implementation katika Teachers Education; server zote sasa hivi kwenye Vyuo vya Ualimu ambako mradi ule umepita hazifanyi kazi, lakini ukifungua kitabu cha hotuba ya Waziri anazungumza zaidi mfano, hata pale ukurasa wa 27 anazungumza suala la kuhakikisha TEHAMA inafundishwa, kuhakikisha walimu wanaandaliwa na TEHAMA na vitu kama hivyo. Nikuhakikishie tuma watu wako ama nenda mwenyewe kwenye Vyuo vya Ualimu vingi kama siyo vyote hakuna computer na kama zipo ni mbovu na pia server hazifanyi kazi na wala hawapewi GB wala kitu gani, tunategemea hiyo TEHAMA itaendaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 158,674; lakini kwenye bajeti mwaka ujao wa fedha tumetenga kujenga vyumba vya madarasa 2000 tu kama pesa itapatikana. Kwa maana hiyo, kwa mahitaji haya 158,674 kila mwaka tukijenga vyumba vya madarasa 2000 maana yake tutatumia miaka 79 ili tuweze kukamilisha. Nafikiri inatakiwa kuwe na mkakati wa makusudi, madawati tunajua yalipatikana yaliyo mengi mengine yapo nje yanalowa mvua yanaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshauri Waziri ili kusudi tuboreshe elimu yetu na watoto wetu wakae katika vyumba vya madarasa kunahitaji pia mkakati wa makusudi. Wakati wa kuhitimisha Mheshimiwa Waziri naomba anijibu maswali yangu haya rahisi, tunaposema quality education Tanzania tunamaanisha nini? Pia napenda kujua falsafa yetu ya elimu sasa hivi ni nini? Bado ni ile elimu ya ujamaa na kujitegemea ama kuna kitu kingine? Kama ndivyo basi tujue mitaala ambayo tunaitumia kweli inawafanya watoto wetu kwenda kwenye kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Wakaguzi ama sasa hivi wanaitwa Wadhibiti Ubora. Mheshimiwa Waziri nikuombe kile kitengo kipo chini yako, Wizarani kwako, naomba ukipe kipaumbele kwa umuhimu wake, kwa sababu bila ukaguzi kwenye elimu ni sawa na hakuna. Maana yake hawa Wadhibiti Ubora wa elimu ndiyo CAG kwenye elimu, ndiyo wanaangalia kila kitu na kujua kuna matatizo gani. Inawezekana hata hili suala la vitabu leo tusingekuwa tunaliongelea hapa kama wangekuwa wanafanya kazi zao vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia naomba tu niwaulize hawa Mawaziri wa Maji, hivi ni kwa nini ninyi hampewi hela? Kuna tatizo gani? Labda wakitueleza tutatoka hapo tukajua tuwasaidie vipi, kwa sababu tunajua sekta ya maji ni sekta muhimu, lakini ukienda kwenye pesa walizopewa za maendeleo ni asilimia 19.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakaa hapa tunajadili, tunafanya nini, lakini mwisho wa siku utekelezaji finyu, kwa hiyo, wakati wanakuja kujibu watueleze kwa nini Wizara ya Maji haipewi pesa za kutosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo ni lazima nichangie tu. Kuhusu Mfuko wa Maji, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba, pesa ziongezwe kwa ile tozo kutoka shilingi 50/= kwa lita mpaka shilingi 100/=, lakini katika kuongeza huko naomba ile pesa ikiongezwa ikafanye jambo lililokusudiwa. Sisi lengo letu watu wa vijijini wapate maji, angalau ile pesa asilimia 70 ikatumike vijijini ili kuwawezesha akinamama wa vijijini wapate maji; isiwe kwamba ile pesa ichukuliwe ikafanye mambo mengine kama administration na vitu kama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma. Mimi Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha hii hoja naomba aje na majibu. Kila siku wanatwambia mkandarasi yuko site anafanya hivi, anafanya hivi. Tunataka tupate jibu la uhakika, pesa ya kufanya huu mradi ipo ama haipo? Swali la kwanza. Hata hivyo, pale unapopita mradi wamewaambia watu wasiendeleze, lakini mpaka leo hakuna fidia yoyote waliyolipwa? Watu wale mnawaachaachaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Serikali ya China na Serikali ya Tanzania kwenye mradi huu tunaomba sisi watu wa Mtwara tupate maelezo ya kina kwa sababu mradi huu ukikamilika, kama kweli tunasema tunaitaka Mtwara ya Viwanda maji haya yatatusaidia kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani; pale maji yapo ya kutosha, tatizo miundombinu. Miundombinu ya tangu mwaka 47 wakati watu wanavaa kaptula badala ya suruali ndiyo hiyo hiyo iko mpaka sasa hivi, haitoshelezi. Huwezi kuamini watu wa Mtwara Mjini kuna watu wengine ukienda mitaa ya Komoro wanachota maji, kule kwetu tunaita ya kuokota; unasubiri mvua inyeshe unachimba kisima unachota, hiyo ndiyo Manispaa ya Mtwara Mjini. Sasa nafikiri kuna haja ya makusudi kabisa Mheshimiwa Waziri wa Maji atueleze mikakati thabiti ya kuitekeleza ili kusudi tuepukane na matatizo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Mkoa wa Mtwara kwa matokeo ya elimu kila siku ni karibu unashika nafasi za chini; kwa mfano mwaka jana shule tisa katika 10 za mwisho zimetoka Mkoa wa Mtwara kwenye mtihani wa form two; na waathirika wakubwa ni watoto wa kike. Wanaathirika kwa sababu, pamoja na mambo mengine maji hakuna, wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa cha kusikitisha Mheshimiwa Rais ametoa amri ya Kata Umeme. Kweli umeme umekatwa, umekatwa mpaka kwenye vyanzo vya maji, ukienda kwenye Mradi wa Makonde umeme umekatwa, wananchi wamehangaika maji hakuna.

Sasa najiuliza mwananchi wa kawaida akipelekewa maji nyumbani kwake bili analipa, wale wanaenda kukata umeme kwenye chanzo ambacho maji yale wanaowadai si wananchi wa kawaida; wanadai Jeshi, wanadai Polisi, wanadai Hospitali, lakini wanaenda kukata maji ambayo wananchi wote hawapati; wanaenda kukata umeme kwenye ule mtambo ambapo unasababisha wananchi wengine huku wote wasipate maji, hata wale ambao wanalipa bili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hilo hilo la kukata maji; kwa mfano ukienda katika Manispaa ya Mtwara Mikindani watu wa maji wanadai sana madeni. Ukiangalia wanadai Jeshi, wanadai Polisi, wanadai Hospitali, lakini na wao kwa sababu hawalipwi, wanadaiwa umeme! Ikafikia stage wakakata maji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula siku nne. Niambie yule mama yule tunayemtaka akajifungue, yule mtoto anayeumwa anatibiwa katika mazingira gani? Mpaka maabara ilifungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo mimi nayaongea kwa uchungu sana kwa sababu wale watu wanateseka tatizo sio la kwao, tatizo la Serikali hii hampeleki hela za kulipia hizi huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Umwagiliaji. Naomba nipate maelezo ya kina, inavyoonekana issue ya umwagiliaji kwetu si kipaumbele. Sasa kama si kipaumbele watu wakilalamika njaa msiwazuie waacheni waseme, kwa sababu nina mfano. Kuna Skimu ya Umwagiliaji Mtwara Vijijini katika Bonde la Mto Kitere, ile skimu ilifunguliwa na mbio za mwenge mwaka 2014, lakini cha ajabu sijui walifungua kitu gani. Ndiyo maana sometimes tunasema mwenge tuuweke makumbusho! Walienda pale wametumia hela chungu nzima, wamefungua, lakini hakuna kinachofanyika. Sasa walifungua ili iweje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bonde lile likitumiwa vizuri sisi watu wa Mikoa ya Kusini naamini hatutahangaika kwenda kufuata mchele Ifakara, hatutahangaika kwenda kufuata mchele Mbeya. Mheshimiwa Waziri anakiri kabisa kwamba miradi mingi ya umwagiliaji ilifanyika kifisadi.

Sasa tunamwomba afanye jitihada za makusudi kuhakikisha miradi ile inafanya kazi na wale watu ambao walihusika katika kuhujumu miradi ile wachukuliwe hatua za kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, magonjwa mengi, karibu asilimia tisa ya wagonjwa wanaolazwa hospitali matatizo yao yanatokana na kutumia maji ambayo si safi na salama. Serikali inatumia pesa nyingi kutibu watu wetu. Kwa hiyo, ushauri wangu tuwekeze kwenye maji kwa sababu tutapunguza kutibu watu na kuwafanya watu wakose vizazi, kwa sababu haya magonjwa ya UTI na nini yanaenda kusababisha watu wengine wakose vizazi kwa sababu, vinakuwa vinapata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la uvunaji wa maji ya mvua, nafikiri wenzangu wengi wameliongea, tuweke msisitizo kabisa, tuweke mkakati maalum kama tunavyofanya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa pesa nyingi za dawa zinapotea kwa ajili ya kununulia dawa za malaria. Wakati tuko kwenye Kamati tumefika Kibaha kwenye kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu, viluilui wa mbu, lakini kusema ukweli tumekuta hakuna jitihada za makusudi za kutangaza dawa ile ili watu waweze kuitumia na kuua yale mazalia ya mbu, ili watu wasing’atwe na mbu na kupata ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namshauri Mheshimiwa Waziri watilie maanani utumiaji wa dawa hii kwa ajili ya kuua hivi vimelea, ili pesa ya kununua dawa za malaria ipungue na tufanye mambo mengine katika sekta ya afya kwa sababu, ina mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Kanda ya Kusini, wenzangu wengi wameongea na mimi naomba niongee. Sisi tumechoka, tumechoka kwa sababu kila siku tunaongea. Safari hii imetengwa bilioni moja, bilioni moja ni pesa ndogo lakini tunaomba hiyo hiyo ndogo iende. Maana hapa tunaongea ndogo, lakini hatimaye hata hii ndogo haiendi. Mmetutengea bilioni moja kwa mwaka huu wa fedha unaokuja, tunaomba hii pesa iende, ili ikaweze kujenga hospitali ile na sisi tupate huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula. Ukifika pale ni masikitiko makubwa, mvua hizi za masika zinaponyesha jengo la OPD linavuja. Vile vile theatre yetu ya Hospitali ya Mkoa wa Ligula inahitaji matengenezo makubwa. Kama mwenzangu alivyosema X- Ray mbovu, jengo lenyewe linahitaji ukarabati mkubwa. Kwa mwezi OC inakwenda shilingi milioni ishirini na tano, ni ndogo, hospitali ile inatoa huduma ya watu wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivi tunavyosema hatuna hospitali ya kanda, tunategemea hiyo hospitali ihudumie watu wengi, lakini mazingira yake ni magumu, mazingira yake ni duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda pale Machi, 2016 palikuwa na matatizo. Madaktari 13 wakahamishwa, tangu Machi, 2016 mpaka leo ninapoongea hata daktari mmoja hajaletwa. Tunatarajia hawa waliopo wafanye kazi kwa kiwango kipi? Hawa wahudumu wenyewe wa pale wana madeni, mpaka sasa hivi wanadai si chini ya milioni mia tano na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi watu wa Kusini, sisi watu wa Mkoa wa Mtwara pia tunahitaji huduma bora za afya. Tunaomba waone kwamba kule kuna watu ambao wanahitaji huduma bora. Tuna korosho tunachangia pato kubwa la Taifa hili; kwa hiyo nasi pia tunahitaji tupate huduma, si kwamba kila siku tukiingia humu tunaongea yanawekwa kwenye vitabu wanafunika, tukirudi kwenye bajeti nyingine mambo ni yaleyale, kitu kama hicho hatukipendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ile hospitali, tunaisemea hii hospitali kwa sababu kama unakuja Mkoa wa Mtwara huwezi kuacha kuongelea Hospitali ya Ligula. Ni hospitali tunayotaraji iwe na mazingira mazuri kwa ajili ya kuwahudumia watu. Tukienda kwenye wodi ya wazazi majanga, wodi ni ndogo, watu wanarundikana, hospitali mmesema ya rufaa ya mkoa, lakini inatoa huduma utasema labda ni hospitali ya wilaya. Watumishi wana madai mengi, watumishi wako asilimia 39 tu, maana unapohitaji watumishi 10 wewe unao wanne tu, tunategemea watafanya kazi katika mazingira gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema Wizara inahusika na watoto pia tunajua ina wajibu wa kulinda haki zao. Leo watoto wanadhalilishwa kwenye vyombo vya habari, wanadhalilishwa kwenye mitandao ya kijamii; mtoto ametelekezwa na mzazi wake, pata picha kama ni mwanao wewe kesho anaambiwa na wenzie shuleni; wewe baba yako alikutelekeza; hivi kweli huyo mtoto ataweza kujifunza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusifanye vitu just for kwa ajili ya show up, tuonekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto yule tunampa athari ya kisaikolojia. Mimi ni Mwalimu najua mtoto hawezi kujifunza vizuri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nataka kusema kwamba elimu ni uwezo si idadi tu ya watu ambao wanaingia shuleni. Tunatarajia watoto wanaoingia wafundishike, wawe na uwezo wa kutatua changamoto zilizopo katika mazingira yao; hapo tutapata maendeleo katika elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akija atujibu kwa ufasaha kuhusu hivyo vitabu vya darasa la nne ambavyo mpaka sasa hivi bado havijafika shuleni, watoto wetu wanajifunza kwa kutumia kitu gani? Ukifungua katika hotuba yako ukurasa wa 69 yaani tunaanza mbele kabla ya nyuma. Ukurasa wa 69.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 69 pale namba 62 roman (ii) inasema; “Mradi wa kuendeleza elimu ya ualimu imeandaa mapitio ya mitaala wa elimu ya ualimu ili kuwa na mtaala unaokidhi mahitaji ya sasa na unaoendana na mtaala wa elimu msingi ulioboreshwa.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, muone mambo ya ajabu ya Serikali ya CCM, kumbe mpaka wanapeleke mtaala shule za msingi, huku kwenye ualimu hawajawafundisha. Tunategemea walimu wale wakawafundishe wale watoto ambao mtaala ule hawaujui sasa wanaenda kufundisha kitu gani. Mheshimiwa Waziri naomba unapokuja hapa uje na majibu, haya ni maneno yako siyo ya kwangu nimekwambia ukurasa wa 69 roman (ii). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia vyuo vya ualimu; hawa watu wamesahaulika sana. Wakufunzi wa vyuo vya ualimu wamesahaulika, mimi nimetoka kule, takriban wazungumzaji wote waliozungumza hapa hawajataja vyuo vya ualimu. Wakufunzi wanadai, morale imeshuka, wana matatizo mengi katika kazi yao ya ualimu. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri una vyuo 35 tu vya ualimu nchi hii, mwenzako Mheshimiwa Jafo ana shule za msingi ngapi, ana shule za sekondari ngapi lakini wewe una vyuo vya ualimu 35, naomba uende ukawasikilize, utatue matatizo yao. Shida ya ualimu inatokea huko kwa sababu watu wamechoka, mpaka leo unamwambia amfundishe mwalimu, mtaala wenyewe maskini haujui anamfundisha kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye fedha za ruzuku. Hizi fedha zimekadiriwa tangu mwaka 2001; mwaka 2001, shilingi 10,000 kwa mtoto wa shule ya msingi, shilingi 25,000 kwa mtoto wa sekondari. Katika hiyo shilingi 10,000 shilingi 4,000 inabakia Serikali haiendi shuleni kwa ajili ya ununuzi wa vitabu. Sasa nakuuliza Mheshimiwa Waziri shilingi 6,000 inayoenda shule kumgharamia mwanafunzi kwa karne hii inatosha? Na kama haitoshi utuambie mkakati wa makusudi ambao umeuweka wa kuhakikisha kwamba hiyo fedha inaongezwa. Pendekezo langu ifike shilingi 20,000 kwa mtoto wa shule ya msingi na ifike shilingi 50,000 kwa mtoto wa shule ya sekondari. Pia uniambie katika hiyo 4,000 inayobakia Serikali Kuu imenunua vitabu kiasi gani na kwa takwimu zipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo; katika Wizara ya Elimu fedha zinazotengwa ni chache karibu zote asilimia 100 ya fedha za maendeleo mnategemea wahisani, ninyi mapato yenu ya ndani hayatengi fedha za maendeleo. Sasa nataka kukuuliza Mheshimiwa Waziri tunajua kuna miradi mingi, kwa mfano mradi wa KKK, ni mradi mzuri ambao implementation yake ingekuwa nzuri tunaamini ingesaidia, lakini mnategemea wahisani. Mtuambie nyinyi kwenye mradi huu mmeweka kiasi gani na mmefuatilia kwa kiasi gani mradi huu unaweza kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la walimu wa sayansi tumekuwa tukiliongea na tutaendelea kulio... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)