MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri Mkuu, TMA imekuwa ikijitahidi sana kutoa taarifa sahihi kuhusu uwepo wa mvua kubwa nchini kwetu na Serikali ina vyombo vyake vingi vya kujua kwamba mvua inanyesha kubwa sehemu gani. Sasa, badala ya kuacha utashi wa mzazi aseme nimpeleke mtoto wangu shule au nisimpeleke, kwa nini zile mamlaka zetu kule chini zisiwe zinatoa taarifa kwamba leo Mtwara kuna mvua kubwa, watoto wote wasiende shuleni ili kuepusha maafa ambayo yanatokea na yanawakumba watoto wetu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema kwamba, Serikali yetu imefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye mfumo wa utoaji taarifa ya hali ya hewa kila siku hapa nchini. Taarifa hizi ambazo zinatokana na mitambo na wataalam walioko kwenye sekta zinatakiwa zizingatiwe pia na mamlaka zote mpaka kule vijiji. Kwa hiyo ni jukumu la mamlaka zetu ambazo pia ni Kamati za Maafa kutoa taarifa za hali ya hewa ili kuepusha maafa hayo kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa maelekezo hapa kwa halmashauri zote nchini na mikoa kwa kupitia wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wahakikishe kuwa wanajenga utamaduni wa kutoa mawasiliano wakati wote pindi wanapopata taarifa za hali ya hewa. Kama taarifa ya hali ya hewa hiyo inaweza kuwa mbaya kwenye eneo hilo, basi ni wajibu wa Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bado narudia tena kuwasihi na kuwataka Wakuu wa Mikoa kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa hasa kipindi hiki ambacho kinaonesha kwamba mvua zitaendelea kuwa kubwa mpaka mwezi Mei, waweze kujua, je, kwenye mkoa wao hali ya hewa ikoje na waweze kutumia njia hiyo kuweza kutoa taarifa kwa wananchi wao kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza viongozi wetu walioko mikoani kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa hizi mara kwa mara na ndio wajibu wao ili kuweza kuokoa hali hii ambayo watu wengine walikuwa hawapati taarifa huku mamlaka zetu za Serikali zikiwa ziko pale.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nalichukua hili kwa ajili ya kuendelea kuliimarisha zaidi kwenye kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kuwa nyingi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika nchi yetu matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, wanawake na watu wengine wa makundi mengine umekithiri sana. Watu wanafanya na adhabu zinatolewa, lakini matukio hayo yamekuwa yakiendelea, sasa hivi hali imekuwa mbaya, watu wanalawiti mpaka wanyama. Nataka kujua Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuleta muswada Bungeni ili aidha, tuongeze adhabu, ama tubadili adhabu ili zitolewe adhabu zitakazokidhi haja ili matukio hayo yaweze kukoma kwani yamekuwa yakiathiri watoto wetu, wanawake wenzetu na watu wengine? Nakushukuru.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba matukio kadhaa ya unyanyasaji wa kijinsia yapo na Serikali inachukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaokutwa wakitenda matukio haya ya unyanyasaji wa kijinsia. Matendo haya na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kwa sasa si Serikali pekee bali pia hata jamii inatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea na kuchukua hatua kwa kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, kwa sababu matukio ya unyanyasaji wa kijinsia mengi yanatokana na ulevi wa vilevi holela ambavyo vinatumika vinavyoweza kumpotezea mtu uwezo wa kufikiri na kutafakari matendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, malezi ya watoto wetu kutoka ngazi ya chini na makuzi yao na namna ambavyo wazazi tunawajibika kulea watoto hawa. Pia, tunazo zile imani kwenye jamii zetu, watu wanaamini labda ukitenda tendo fulani unapata mafao, unapata utajiri, haya yanasukuma watu kufanya matendo ya unyanyasaji wa kijinsia. Pia kuna zile mila kandamizi za baadhi ya makabila. Haya niliyoyataja machache yanachangia sana kwenye utendaji wa matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua Mheshimiwa Mbunge, ameshauri kuchukua hatua kali zaidi kwa kuweka sheria kali na ikiwezekana sheria iletwe hapa ifanyiwe mapitio kwa ajili ya kuongeza ukali zaidi. Kwa kuwa, nimekiri kwamba tatizo lipo kwenye jamii kwa baadhi ya maeneo na hatua kali zinachukuliwa, inawezekana pia yanajirudia kwa sababu ya baadhi ya maeneo ambayo pia yana sheria, sheria zake bado si kali sana kwa sababu jambo hili ni mtambuka na linagusa Wizara nyingi na kila Wizara inaweka sheria yake katika kukinga jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napokea ushauri wa kufanya mapitio wa sheria hizi, malengo yetu ni kuhakikisha kwamba jamii inabaki kuwa salama na wale wote wanaotenda matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia wanaendelea kuchukuliwa hatua kali zaidi na tunatamani tuone jambo hili likikoma kwenye jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiase jamii yetu kuzingatia mila, desturi na tamaduni zetu ili tusiingie kwenye matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia kwa sababu kila mmoja ana haki ya kuishi, kupunguza ulevi holela ambao unaweza kusababishia watu wakalewa halafu wakatenda vitu visivyo, kwa sababu ukishalewa akili inakuwa siyo ile ya kawaida na hizi imani ambazo ziko kwenye baadhi ya makabila, mila potofu na malezi kwa mfululizo wake kama ambavyo nimesema awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nakiri kwamba, jambo hili tutaendelea kulifanyia mapitio na pale ambapo panahitaji mabadiliko ya sheria, kanuni, tutaleta Bungeni kwa ajili ya kufanya marekebisho zaidi ili tuweze kujipanga zaidi. Ahsante sana. (Makofi)