Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Tunza Issa Malapo (5 total)

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Sera Mpya ya Elimu ya mwaka 2014 inatambua upatikanaji wa elimu ya msingi bure; lakini Serikali imeshindwa kupeleka ruzuku ya shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi wa shule za msingi za umma na shilingi 25,000/= kwa kila mwanafunzi wa shule za sekondari za umma:-
Je, Serikali inaweza kuweka mchanganuo wa jinsi gani itakavyoweza kutekeleza Sera ya Elimu ya mwaka 2014 kwa kutoa elimu bure bila kuathiri ubora wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malopo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli fedha za uendeshaji wa elimu (capitation) zikiwemo shilingi 10,000/= kwa wanafunzi wa shule ya msingi na shilingi 25,000/= kwa wanafunzi wa sekondari zilikuwa hazipelekwi kwa ukamilifu. Kwa sasa Serikali imeamua kuanzia Januri, 2016 wanafunzi wote walioandikishwa darasa la kwanza na wale walioandikishwa kidato cha kwanza pamoja na wale wanaoendelea na shule gharama zilizokuwa zinagharimiwa na wazazi au walezi kwa kulipia ada na michango mbalimbali sasa zitalipwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia Serikali imetenga shilingi bilioni 131.4 ikiwa ni fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule, chakula, mitihani na fidia ya ada. Fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja shuleni kutoka Hazina kwa wastani wa shilingi bilioni 18.77 kila mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizo zinahusisha shilingi 10,000/= kwa wanafunzi wa shule ya msingi kwa mwaka, shilingi 25,000/= kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka, shilingi 1,500/= kwa kila mwanafunzi kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya chakula, fidia ya ada ya shilingi 20,000/= kwa wanafunzi wa kutwa na shilingi 70,000/= kwa wanafunzi wa bweni kidato cha kwanza hadi cha nne kwa mwaka. Tayari Serikali imeshapeleka shilingi bilioni 18.77 kwa mwezi Januari, 2016.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Serikali inatambua umuhimu wa barabara; na barabara inayounganisha Mtwara Mjini, Nanyamba, Tandahimba, Newala hadi Masasi haipitiki vizuri wakati wote na hivyo kuwafanya wananchi waone kama wametengwa na Serikali yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ilisaini mkataba na Mkandarasi Mshauri Multi Tech Consult (pty) Ltd. kutoka Botswana akishirikiana na Unitec Civil Consultants Ltd ya hapa nchini tarehe 15 Mei, 2014 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mtwara Mjini – Nanyamba – Tandahimba – Newala na hadi Masasi yenye urefu wa kilometa 210 kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 1,280,832. Usanifu wa kina wa barabara hii ulikamilika mwezi Aprili, 2015.
Taratibu za kumpata Mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami sehemu ya Mtwara hadi Mnivata ambapo ni kilometa 50, zipo katika hatua za mwisho ambapo ujenzi utaanza mara baada ya mkataba kusainiwa. Aidha, ujenzi wa sehemu iliyobaki kati ya Mnivata na Masasi, utafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na kwa kuzingatia kwamba barabara hii imeahidiwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 hadi 2020 na wakati huo huo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne na wa Awamu ya Tano. Kwahiyo, tutaijenga.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, tunaomba utusomee tena hicho kiasi ulichosoma kwenye majibu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni shilingi 1,280.832 au shilingi bilioni 1.280.832.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Nanyamba kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida ya ukosefu wa maji safi na salama:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi hao wanapata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalumu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kufanya upanuzi wa mradi wa maji wa Kitaifa wa Makonde kutokea katika Kijiji cha Chikunda kupitia Kijiji cha Nyundo hadi Dihamba. Wakazi wapatao 49,206 waishio katika Vijiji 49 vya Halmashauri ya Nyanyamba na Vijiji saba vya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara watanufaika na mradi huo utakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na tathmini ya awali, upanuzi wa mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 11.4. Utekelezaji wa mradi huo unategemea upatikanaji wa fedha zitakazotengwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Halmashauri ya Nanyamba ina mpango wa kufanya ukarabati wa miundombinu ya bomba katika miradi ya maji iliyojengwa kwa ufadhili wa AMREF ipatayo 17 inayotumia nishati ya nguvu za jua. Ukarabati huo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 719 na unakadiriwa kuwanufaisha wakazi wapatao 15,433 waishio katika Jimbo la Nanyamba na hivyo kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Mtwara Vijijini inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya Mbembelo - Mwang‟anga na Nanyamba - Maranje. Miradi hii itanufaisha Vijiji vya Mwang‟anga, Mbembaleo, Mwamko, Maranje, Mtimbwilimbwi, Mtopwa, Mtiniko, Shaba, Mbambakofi na Mnivata vyenye wakazi wapatao 20,166. Miradi hii itakapokamilika upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Halmashauri ya Nanyamba utaongezeka kutoka asilimia 43 hadi asilimia 80.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y MHE. TUNZA I. MALAPO) aliuliza:-
Dhana ya elimu ni majumuisho ya mambo mengi sana ikiwemo matibabu ya huduma ya kwanza, gharama za umeme, maji, vyakula (kwa shule za bweni), posho za walimu (part time) pamoja na zana za kufundishia zisizohifadhika kwa muda mrefu; na nyingi kati ya gharama hizo zilikuwa zinatatuliwa mashuleni na Wakuu wa Shule kwa kutumia ada na michango waliyokuwa wanatoza wanafunzi.
Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha ufanikishwaji wa dhana hii ya elimu bure bila kuanzisha migogoro mipya kati ya wakuu wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya utoaji wa elimu bila malipo inatokana na Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inayoelekeza utaratibu wa ugharamiaji wa elimu ya awali kuwa ya lazima kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu msingi bila malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi. Hata hivyo, elimu bila malipo haiondoi dhamira ya uzalendo kwa jamii ya kushiriki kwa hiari kuchangia kwa hali na mali katika kuleta maendeleo ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kupeleka shilingi bilioni 18.777 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia mpango huu. Fedha hizo zinatumika kugharamia mitihani ya Taifa, chakula cha wanafunzi wa bweni, ada ya mwanafunzi kwa shule za kutwa na bweni na fedha za uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga ili kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu bila malipo ambao umeshaanza kwa shule zote za umma nchini hausababishi migogoro kati ya wakuu wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi. Ili kuhakikisha hilo halitokei Serikali imetoa miongozo mbalimbali katika mikoa yote inayofafanua kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Je, gharama ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni shilingi ngapi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara na Songo Songo Mkoani Lindi hadi Dar es Salaam ulianza kutekelezwa mwezi Juni, 2013 na kukamilika mwezi Oktoba, 2015. Ujenzi wa mradi huu ulihusisha ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asilia yaani Madimba (Mtwara) pamoja na Songo Songo (Lindi) kwa gharama ya dola za Marekani milioni 349.51 na pia ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo – Lindi hadi Dar es Salaam kwa gharama ya dola za Marekani milioni 875.72.
Mheshimiwa Spika, jumla ya gharama zote za mradi huu hadi kukamilika ni dola za Marekani milioni 1,225.23.
Mheshimiwa Spika, bomba lina uwezo wa kusafirisha gesi asilia futi za ujazo milioni 784 kwa siku na linaweza kufikia futi za ujazo milioni 1,002 kwa siku. Kwa sasa gesi inayosafirishwa ni futi za ujazo milioni 68.5 kwa siku.