Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tunza Issa Malapo (11 total)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kutoa masahihisho, Naibu Waziri wakati anajibu aliniita Malopo naitwa Malapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali iko tayari sasa kuwaambia wananchi kuwa haiko tayari kutekeleza Sera ya Elimu Bure kwa maana halisi ya Kiswahili ya neno bure isipokuwa elimu inayotolewa sasa ni ya kuchangia gharama? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nini wito wa Serikali kwa wananchi kuhusu sera hii ili kuwawezesha walimu kufanya kazi yao bila kero kutoka kwa wazazi wanaofikiri hawawajibiki kulipa pesa yoyote kwa ajili ya elimu hiyo kwa watoto wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Kwanza naomba radhi kwa kukosea jina la Mheshimiwa Mbunge ni Malapo na nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kwamba Serikali iseme haina nia ya dhati katika suala zima la elimu bure, ndugu zangu naomba niwaambie, kama sisi ni mashahidi wa kweli vijana wengi waliokuwa wanaenda sekondari walikuwa wanashindwa kulipa hizi gharama za kawaida. Hata wale waliokuwa wanaanza elimu ya msingi mnafahamu wazazi wengi sana wanashindwa kulipa zile gharama za awali ili mtoto wake aweze kujiunga na shule na ninyi wenyewe ni mashahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi juzi kupitia vyombo vya habari wazazi wanakiri kabisa kwamba suala hili limewasaidia kwa kiwango kikubwa vijana wao kwenda shule. Hata turn over katika shule zetu imekuwaje? Hata madarasa wakati mwingine shule zinahemewa kwa sababu wazazi wote ambao mwanzo walikuwa wanakwazika na gharama hizi sasa wanapata fursa ya kuwapeleka watoto wao shule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tukiri kwamba Serikali katika hili imefanya juhudi kubwa sana. Naamini jambo lolote lazima lina changamoto zake, hizi changamoto ndogo-ndogo ni kwa ajili ya kuboresha ili mradi mpango uende vizuri lakini dhana ya Serikali imekamilika na inaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sehemu ya pili, wito wa Serikali Walimu wasibughudhi wazazi, nadhani tumeshasema wazi na Waziri wangu jana alilisema wazi kwamba jambo kubwa elimu hii ni bure. Hatutarajii mwalimu awazuie watoto kwenda shule kwa kuzusha mchango wake mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tumesema tutakuwa wakali sana kwani lengo kubwa ni mtoto wa Kitanzania aweze kupata elimu ya shule ya msingi na ya sekondari mpaka form four. Lengo ni kwamba kila mwanafunzi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania apate fursa ya uongozi na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongezea majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri wa TAMISEMI kutokana na maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Malapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imefanya jitihada kubwa katika suala hili la elimu bure, lakini inasikitishwa kwamba wenzetu walihoji fedha hizi zimetoka wapi kwenye bajeti na leo fedha hii iliyotolewa kwa ajili ya kusaidia jamii maskini watoto wao waende shule wanahoji tena hiyo bure gani, ni mkanganyiko ambao haueleweki. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu, katika kila shule za msingi za kutwa tutapeleka kila mwezi shilingi 600/= kwa kila mtoto kwa ajili ya uendeshaji. Kwa shule za sekondari za kutwa tunapeleka kwa kila mwezi shilingi 3,540.57/= kwa kila mtoto kwa ajili ya uendeshaji wa shule. Kwa wale wa bweni tunapeleka shilingi 7,243.39/= kwa kila mwezi. Fedha hizi zikijumlishwa uwezekano wa kuendesha elimu upo pamoja na changamoto zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninavyozungumza kutokana na mpango huu wa elimu msingi bila malipo pale ambapo tulitegemea wajiandikishwe watoto 80 kuanza darasa la kwanza wamejiandikisha 240; pale tulipotaka wajiandikishe watoto 180 wamejiandikisha karibu 700 na hiyo ni Dar es Salaam tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako baadhi ya maeneo uwezekano tu wa kuwapokea watoto hawa ni mgumu kwa sababu wazazi maskini wameona mpango huu ni muhimu kwao na umewasaidia sana.
Kwa hiyo, kuubezabeza hapa ni kwenda kinyume kabisa na wananchi ambao wanaona mpango huu umewasaidia na kwa hakika kusema kweli unalisaidia Taifa. Tupingane katika mengine lakini kwenye jambo zuri tutiane moyo kama Watanzania. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie ni lini ujenzi huo utaanza? Kwa sababu barabara hii imekuwa ikizungumzwa kwa muda mrefu. (Makofi)
Swali la pili; issue hapo ni ku-sign mkataba ama ni pesa? Kwasababu tumekaa kwenye kikao cha RCC ingawa Meneja wa TANROADS Mkoa alishindwa kusema wazi, lakini kinachoonekana pesa hakuna. Kwahiyo, issue ya msingi naomba kujua; ni kwamba mkataba haujasainiwa ama pesa zinazofanya mkataba usainiwe hazipo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Tunza Issa Malapo, kwa niaba ya Wabunge wote wa Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu walikuwa na kikao cha RCC na walikataa kuijadili barabara hii wakataka ije ijadiliwe hapa Bungeni. Naomba nikuhakikishie, hamna sababu ya kuijadili hapa Bungeni. Barabara hii imetengewa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2016/2017 barabara hii imetengewa fedha tutakayohakikisha hizo kilometa 50 zinajengwa. Tunachosubiri ni taratibu za mkandarasi ku-sign mkataba kukamilishwa. Fedha zimetengwa!
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
(a) Naomba anieleze ni tatizo gani linalofanya Mji huu usipate maji ya kutosha na ya uhakika wakati vyanzo vya maji vipo?
(b) Pia ni lini wananchi hawa walioteseka kwa muda mrefu hasa wanawake watapata maji safi na salama? Nataka time frame, ni lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni matatizo gani yanafanya wananchi hawa wasipate maji. Ni kweli kabisa kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge ni shahidi, katika Mikoa na Wilaya ambayo nilitembelea ni pamoja na Wilaya ya Nanyamba. Maeneo yale yana vyanzo vikubwa vya maji vya Mitema na Mkunya. Tatizo ni kwamba huko nyuma tulikotoka upatikanaji wa fedha ulikuwa kidogo siyo mzuri na kwa sababu tumekuwa tunaishi kwa kutegemea wafadhili vile vile. Hilo ndilo ambalo limefanya miradi ile isiweze kukamilika na kutoa maji yale yanayotakiwa kwa matumizi ya wananchi wa Nanyamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza ni lini. Sasa hivi tumeingia kwenye program ya pili ya maendeleo ya maji ambayo tunatarajia Serikali inatenga fedha na tunaanza kutenga fedha kuanzia mwaka ujao wa fedha, pia wafadhili wametuahidi na kuna juhudi kubwa ambayo inafanywa na Serikali kupitia Waziri wa Fedha, lakini na Mwanasheria wa Serikali pia ambapo tunaongea na wafadhili waweze kutupatia pesa ili tuweze kukamilisha hii miradi ya Mito ya Mitema na Nanyamba ambayo itahakikisha kwamba vyanzo vya Mitema na Mkunya ili tuweze kuhakikisha maji yanapatikana kwa hizi Wilaya za Nanyamba pamoja na Tandahimba.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa vile Waziri amekiri kwamba, miradi mingi ya umwagiliaji ilikuwa na matatizo sasa je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu wakandarasi na wote waliohusika kufanya ubadhirifu wa pesa hizo nyingi, hasa ukizingatia kuna mradi wa umwagiliaji kule Kitele, Jimbo la Mtwara Vijijini mkoani Mtwara, ambalo kwa kweli wananchi walijitolea eneo lao, lakini mradi umejengwa chini ya kiwango, mifereji ina nyufa
na ule mradi haujaanza kutumika. Nini kauli ya Serikli kuhusu miradi hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Naibu Spika, kama nilivyosema hii miradi tunaifanyia mapitio, lakini pale itakapoonekana mkandarasi au kuna mtu yeyote amefanya ubadhirifu, Serikali itachukua hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, naomba asiwe na wasiwasi, lakini lengo kubwa hasa la Serikali ni kuhakikisha kwamba miradi hii tunaikamilisha ifanye kazi iliyokusudiwa kwa wananchi.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya kupandishwa hadhi Zahanati ya Likombe katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwa Hospitali ya Wilaya kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mrundikano wa wagonjwa hasa katika wodi ya wazazi. Je, ni lini Serikali itapanua wodi ile ili akinamama wale waweze kusitirika wakati wanatimiza haki yao ya msingi kama wanawake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, population ya Mtwara Mikindani sasa hivi imekuwa kubwa kutokana na kuingiliana na mambo ya gesi. Hata hivyo, hivi sasa tunaenda katika harakati za kufanya ukarabati wa vituo vipatavyo 142. Zoezi hili haliishi hapa; Serikali inajielekeza tena kupanua vituo vingine vipya ambako kuna population kubwa. Kituo hiki ambacho Mheshimiwa Mbunge amekizungumzia hapa tutakichukua kama sehemu ya kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kufanya commitment katika kuwahudumia wananchi. Kwa hiyo, hii tutaweka ni sehemu ya kipaumbele kuwahudumia wananchi wa Mikindani ili waweze kupata afya bora katika maeneo yao.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kutokana na ripoti ya CAG mpaka sasa hivi inaonekana ni 6% tu ya gesi inatumika, inayosafirishwa na hilo bomba na uwekezaji huu ni wa pesa nyingi. Nataka kujua Serikali imejipanga vipi kuhakikisha uwekezaji huu unaleta tija kwa Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kuna utata mkubwa katika uwekezaji huu kujua gharama halisi: Je, Serikali ipo tayari kumtaka CAG afanye special audit katika uwekezaji huu? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza bomba la kusafirisha mafuta au gesi kwa sasa kutoka Madimba (Mtwara) hadi Dar es Salaam ndiyo bomba kubwa tulilonalo kwa upande wa gesi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa sasa hivi gesi inayosafirishwa ni kati ya 6% hadi 10% ya uwezo wake na uwezo nimetaja ni milioni cubic feet 744. Sasa ni kwa nini? Bomba hilo lina upana wa inchi 36, ni kubwa; na mahitaji ya sasa ni megawati 668 tulizonazo kwa upande wa gesi, lakini miundombinu inayojengwa ndiyo mikakati sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tunajenga miradi miwili ya kusafirisha gesi Kinyerezi I na Kinyerezi II. Kinyerezi I tunafanya extension ya kuongeza megawati 185 ili katika Kinyerezi I pekee zifikie 335.
Mheshimiwa Spika, kadhalika tunajenga mradi mwingine katika Kinyerezi II ambao utaweza kutoa megawati 240. Sasa miradi hii miwili ikikamilika, mahitaji makubwa ya gesi yataongezeka. Kwa hiyo, itazidi 6% hadi 10% na tuna matarajio inaweza kufikia asilimia 20 hadi 30.
Mheshimiwa Spika, miundombinu inayojengwa kuhitaji gesi, bado ni mingi; tunahitaji umeme wa kutosha. Kwa sasa hivi umeme hautoshi. Ni matarajio yetu kwamba mara baada ya miradi mingine, tutakwenda Kinyerezi III utakaoanza mwaka 2018 utakaohitaji megawati 600. Kwa hiyo, mahitaji ya gesi bado yatakuwa ni makubwa.

Mheshimiwa Spika, lingine niseme mkakati mwingine, unapokuwa na gesi ya kutosha inakuruhusu kujenga miundombinu mingine kwa sababu una stock. Kwa hiyo, siyo hasara kuwa na gesi nyingi lakini kadhalika mikakati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba hii gesi tunasafirisha kadri iwezekanavyo ili ichangie sana katika upatikanaji wa umeme. Mkakati wa Serikali ni kutumia gesi zaidi ili kuachana na mafuta ili kuwapunguzia mzigo wananchi, hilo ni katika ufafanuzi wa swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ukaguzi, mahesabu ya Serikali hukaguliwa mara kwa mara, ni utaratibu wa kawaida. Kama ambavyo kila mwaka CAG hukagua, hata miradi hii ataendelea kuikagua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu, suala la ukaguzi wa miradi ni endelevu, CAG ataendelea kukagua ili hali halisi iendelee kufahamika.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, wamesema wanaajiri walimu wa sayansi, hisabati na kadhalika, lakini bado tatizo la walimu hao ni kubwa. Nataka kujua tu, wamefanya sensa, ni walimu wangapi wa sayansi ambao kila siku wanaacha kazi kwa sababu ya maslahi duni katika Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili ni gumu sana, kwa sababu hatuna takwimu za kila mwaka kwamba ni walimu wangapi wa sayansi na hisabati wanaacha kazi.
Lakini comfort niliyonayo na ambayo nataka niwape Waheshimiwa Wabunge ni kwamba malalamiko tuliyonayo ni ya walimu kutaka kuhama haraka katika shule wanazopelekwa, yaani mwalimu anaweza akapelekwa kwenye shule fulani, akikaa baada ya wiki mbili anataka ahame. Hiyo ndiyo changamoto kubwa tuliyonayo ambayo tunaishughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuacha kazi, hilo naomba sana tutoe majibu baadae.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuendeleza viwanja vingi vya michezo, ikiwemo kiwanja cha Nangwanda Sijaona katika Manispaaa ya Mtwara Mikindani.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kurudisha viwanja hivyo Halmashauri kama ilivyofanya kwenye mashamba yasiyoendelezwa ya watu binafsi? (Makofi)
Swali langu la pili, kwa kuwa michezo ni afya, michezo ni ajira, na michezo ni furaha. Kwa kuwa chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuviendeleza viwanja hivi na kuwafanya wanamichezo wetu wacheze katika mazingira duni...
Mheshimiwa Spika, naomba unisikilize. Michezo ni afya, ni furaha na ni ajira. Kwa kuwa, Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuviendeleza viwanja hivi hatuoni kwamba Chama cha Mapinduzi kina nia ya kudunisha wanamichezo wetu kwa sababu wanapata ajali mbalimbali wanapokuwa wanachezea katika viwanja hivyo? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nikuhakikishie kupitia Bunge lako tukufu kwamba, siyo kweli kwamba CCM imeshindwa kwa sababu asilimia 99 ya michezo yote nchini inaendeshwa kwenye viwanja hivyo, sasa kushindwa huko kukoje? Sasa hivi tunaanza Ligi Kuu ya Tanzania na sehemu kubwa ya michezo hiyo itachezwa kwenye viwanja hivyo hivyo.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na wewe kwamba vingi haviko kwenye hali nzuri sana na Wizara ilikuwa imeiachia Shirikisho la Soka nchini kufanya majadiliano na wenye viwanja, sasa tumeona maendeleo siyo ya kasi ya kutosha, Wizara imeamua yenyewe sasa siyo tu kwa kushirikisha Shirikisho la Soka nchini, mashirikisho yote ya michezo nchini, kukaa pamoja na wamiliki tuweze kukubaliana namna ya kuboresha hivi viwanja na kuweza kupata misaada ambayo kwa kawaida itakwenda kwa urahisi zaidi kwa taasisi ambazo zina ubia na Serikali. Tunataka watuachie ubia wawe na ubia na Serikali ili tuweze kurabati viwanja, kama ambavo FIFA ilivyoweza kukarabati Kiwanja cha Kaitaba na Kiwanja cha Nyamagana.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba mitambo ni michakavu na ni kweli ni ya muda mrefu; je, imejipangaje kununua mitambo mipya ulizingatia kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme katika mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara?
Swali la pili; ni lini Serikali itaunganisha mfumo wa gesi asilia ili uweze kutumika katika majumba ya Mkoa wa Lindi na Mtwara ukizingatia kwamba kule ndiko gesi inakozalishwa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Tunza Malapo kwa kufuatilia masuala ya umeme katika Mkoa wa Mtwara. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi; kwanza, Serikali baada ya kuona uchakavu wa mitambo hii tisa ya Kituo cha Mtwara, imenunua mitambo miwili mipya. Hivi ninavyozungumza, kazi ya ufungaji wa mitambo hii inaendelea ambayo itazalisha megawati nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua Mikoa ya Mtwara na Lindi mahitaji yanaongezeka, Serikali imekuja na mpango wa kujenga mitambo mingine ya kuzalisha umeme megawati 300 kwa kutumia gesi na mpaka sasa Kampuni ya JICA imeendelea na upembuzi yakinifu. Kama ambavyo tumesema kwenye bajeti yetu mradi huu utaanza kutekelezwa mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeliona hilo na kwamba mradi huu mkubwa wa megawati 300 utatatua matatizo yote katika Mikoa hiyo ya Kusini na pia itaupeleka umeme katika Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameeleza ni lini mpango wa kusambaza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Tunza ameulizia ni lini mpango wa kusambaza gesi asilia majumbani katika Mkoa wa Mtwara utaanza? Napenda nimthibitishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo ameona hivi karibuni tumezindua mpango wa kusambaza gesi asilia katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini Mkoa wa Dar es Salaam unakwenda sambamba na Mikoa ya Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, hii kazi itafanyika katika mwaka 2018/2019, tutasambaza gesi katika maeneo mbalimbali kwa matumizi ya majumbani kwa Mikoa hiyo. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawaili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika Manispaa ya Mtwara Mikindani tatizo kubwa ni miundombinu ya usambazaji wa maji, maji yapo, lakini miundombinu ndilo tatizo. Namuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini miundombinu ile itaboreshwa, ili kusudi zile kata za pembezoni zipate maji ya uhakika? Maana tumekuwa tukiliongea suala hili siku nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kumekuwa na kero, watumiaji wa maji katika Manispaa ya Mtwara Mikindani wanalalamika kwamba, wanabambikiwa bill na hiyo inatokana na mamlaka kushindwa kusoma bill katika nyumba zote kutokana na ufinyu wa wafanyakazi. Je, Mheshimiwa Waziri, anatambua kama kuna ufinyu wa wafanyakazi katika mamlaka na kuna jitihada gani za kuhakikisha wanapatikana wafanyakazi wa kutosha? Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtaarifa Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tumesaini mkataba wa shilingi bilioni tano kwenye Mamlaka ya Maji ya Mtwara ambayo katika huo mradi utaongeza vyanzo lakini pamoja na miundombinu ya kusambaza maji katika Mji wa Mtwara na hiyo ni hatua ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na usomaji wa bills kwenye nyumba za watu tayari sasa hivi malalamiko yaliyokuwepo baada ya muda mfupi, yatakwisha kwa sababu, sasa tunatumia teknolojia mahususi ambayo kwanza hakutakuwa na mtu kuzidishiwa bill. Ni kwamba, zile mita zitasoma unit baada ya maji kupita sio baada ya hewa kupita, kwa hiyo, suala hilo Mheshimiwa Mbunge tutalimaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo Mheshimiwa Mbunge Ilani ya Chama cha Mapinduzi tayari itatekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma ambao utaleta maji Mjini Mtwara na baada ya hapo Mji wa Mtwara hautakuwa na tatizo tena la maji, maji yatakuwa mengi, yatahudumia maji ya majumbani pamoja na maji ya viwanda. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira tu, Serikali yake ya Chama cha Mapinduzi inafanyia kazi hili na tayari baada ya muda mfupi utekelezaji wa mradi huo mkubwa utaanza.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Mwambe nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kuna taarifa kwamba mkandarasi ambaye amepewa kazi ya kukamilisha miradi hii ya REA katika Mkoa wa Mtwara, hasa Wilaya ya Masasi yenye Jimbo la Ndanda pamoja na Nanyumbu ana matatizo ya kiusajili.
Je, Serikali haioni ni wakati mwafaka wa kuachana na mkandarasi huyu na kumtafuta mwingine ambaye atakamilisha kazi hii kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, umeme ni huduma, lakini pia umeme ni biashara. Inakuaje mji mpya unapoanzishwa watu wamekaa wanahitaji huduma ya umeme lakini hawaipati kwa wakati? Serikali mnahujumu shirika hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza kwa niaba ya Mheshimiwa Cecil Mwambe na swali lake la kwanza limejielekeza kwa Mkandarasi anayefanya Mradi huu wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza ambaye kwa mujibu wa jibu langu la msingi nimemtaja, JV RADI Services.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo ya Mheshimiwa Mbunge, nataka nimthibitishie kwamba mkandarasi huyu siyo kwamba ana tatizo la usajili, ni utaratibu wa kawaida wa kuhakiki ambao upo ndani ya Serikali. Kuna jumla ya Wakandarasi sita katika Mradi huu wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza ambao uhakiki wao unaendelea kwa vyombo mbalimbali.
MheshimiwaMwenyekiti, kwa hiyo, naomba wakazi wa Mtwara wavute subira kwamba hivi karibuni tu uhakiki huo utakamilika na ataendelea na kazi. Sambamba na hilo, pamoja na uhakiki huo, huyu mkandarasi alipewa mkataba kwa mujibu wa taratibu, lakini pia ameanza kazi. Kuna vijiji kama vitatu Mtwara Vijijini amewasha umeme, anaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kwa maeneo ya miji ambayo inakua, Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba upatikanaji wa umeme au uunganishwaji wa miundombinu ya umeme unakuwa ni shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na kama ambavyo tumewasilisha bajeti yetu jana, kuna miradi mbalimbali ambayo Serikali imeona ianze kutekeleza ili kukidhi mahitaji ya umeme katika miji inayokua. Mfano, kuna mradi unaokuja peri-urban Awamu ya Kwanza utakaoanza mwaka wa fedha 2018/2019. Pia hata densification ya awamu ya pili ambayo ni kwa mikoa 11 ikiwemo Mtwara, Dodoma, Kagera, Singida, Lindi, Kilimanjaro, itaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali imeliona hilo kwa kuwa kazi ni nyingi na tumeona tuisaidie hilo liweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)