Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lucy Fidelis Owenya (9 total)

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ni afya, michezo ni furaha, michezo huondoa mawazo na kadhalika, lakini hapa nchini hakuna viwanja vya michezo. Serikali ya Awamu ya Tano ilisisitiza sana suala la michezo. Je, mmejipangaje kuwapatia wananchi sehemu za kufanyia mazoezi? Kwa mfano katika Manispaa ya Moshi kila mwezi wa tatu tuna mashindano ya kimataifa yajulikanayo kama Kilimanjaro Marathon. Mbio hizi kwa sasa hivi zina washiriki zaidi ya milioni 10 kutoka mataifa mbalimbali lakini tumekuwa tukitumia uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi (MUCOBS) ambacho kwa sasa kinalemewa na wingi wa washiriki wa mbio hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Manispaa ya Moshi tunao uwanja mkubwa wa King George Memorial Stadium ambao kwa sasa unatumika kama soko la kuuzia mitumba. Moshi kuna sehemu nyingi za masoko mfano Pasua, Majengo, Manyema na kadhalika ambako soko hili linaweza kuhamishiwa huko na uwanja wa King George Memorial Stadium ukatumika kwa ajili ya michezo, ukizingatia uwanja ule una michezo tofauti zaidi ya saba. Ni tegemeo langu Serikali itatoa tamko kuhusu kiwanja hiki ili tuweze kudumisha michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwepo Maafisa Utamaduni lakini bado hawajaweza kutumika ipasavyo katika kukuza utamaduni wetu. Kwa mfano, cultural tourism haijapata msukumo wa kutosha kutoka kwa maafisa hawa. Urithi wetu unaelekea kupotea kwa mfano, ngoma za asili, vyakula vya asili, michezo ya asili, mavazi ya asili hata lugha za asili. Hii ni changamoto kubwa kwa Maafisa Utamaduni hasa ukizingatia tishio la utandawazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kuwa Maafisa Utamaduni wawezeshwe kwa kupewa rasilimali za kutosha ikiwa ni pamoja na vitendea kazi ili waweze kuwafikia walengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, mchakato wa Vazi la Taifa umefikia wapi na mpaka sasa hivi ni kiasi gani cha fedha kilichotumika?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shirika la Nyumba (NHC), Shirika hili lilianzishwa kwa nia njema ya kusaidia wananchi kujenga nyumba za bei nafuu lakini kwa sasa hivi Shirika hili limekuwa ni la kibiashara zaidi. Hivi huko vijijini hata mijini wananchi wa kipato cha chini wawezaje kumiliki nyumba hata ya milioni 30? Ni vizuri NHC wakijenga nyumba wazipangishe kwa bei nafuu na zile kodi zikishalipwa kwa kipindi cha kutosha kulipia deni la ujenzi ndipo mmiliki apewe offer ya kununua nyumba hiyo kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi zinazotozwa na NHC kwa sasa ni za juu sana na baadhi ya nyumba za biashara hazijakarabatiwa lakini kodi zipo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua ni master plan ipi inayotumika katika Jiji letu la Dar es Salaam? Wananchi wanajenga kama wanavyotaka, lakini ikumbukwe mifumo ya maji taka ni ile ile iliyojengwa enzi ya mkoloni, wakati huo wakazi waliokuwepo walikuwa ni wachache. Sasa hivi Jiji la Dar es Salaam lina wakazi zaidi ya milioni tano wanatumiaje mitandao ile ile ya kupitisha maji machafu? Je, ni kwa kiasi gani Wizara zinashirikiana ili kutatua tatizo hili? Je, Serikali haioni kwa Jiji la Dar es Salaam haiwezi ni wakati muafaka sasa kusitisha ujenzi wa maghorofa makubwa mpaka pawepo na master plan ili mji ujipange? Hakuna hata viwanja vya wazi, viwanja vya michezo nyumba zinasongamana hata emergency ikitokea katikati ya mji siyo rahisi fire brigade kuweza kupita na kuokoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi za majengo. Kodi hizi ni kubwa sana kwa wananchi wa kawaida kuzilipa, nikiungana na Kambi ya Upinzani, kodi hizi zilikuwa zinakusanywa na Halmashauri na hii ilisaidia sana kuweza kuleta maendeleo katika Halmashauri husika. Ni sababu zipi zilipelekea Serikali kuamua kodi hizo zikusanywe na kupeleka Hazina?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kipekee naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na nikiwa kama mdau wa utalii na Mjumbe wa Kamati ya Maliasili na Utalii niweze kuchangia yangu machache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii unachangia 17.5% kwenye pato la Taifa, lakini tunaweza tukafanya vizuri zaidi kama tutakuwa na mikakati ya kutosha kwanza kwa kuutangaza vya kutosha na pili kuhakikisha kwamba tunagundua utalii mpya. Nimefurahi Mheshimiwa Waziri amesema atatangaza sehemu za utalii Mwanza na kila mahali, lakini naomba nimshauri tu hata hapa Dodoma kuna utalii mzuri tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama naweza nikashauri kuna mawe mpaka Singida. Dodoma tunaweza tukatangaza utalii wa Stone Mountain kama ilivyo Table Mountain South Africa, watu wanaenda kwenye Table Mountain wanatembelea mashamba ya zabibu. Kwa hiyo, wanaweza wakapita hapa kama destination ya a day tour, wakifika hapa watatembelea hiyo Stone Mountain, watatembelea zabibu, wanaweza wakatembelea Chuo Kikuu na attraction ya Bunge as well. Kwa hiyo, watu wa Dodoma nao wanaweza wakapata mapato kutokana na utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaweza tukawa na watalii throughout the year kuanzia Januari mpaka Disemba lakini ningemwomba Mheshimiwa Waziri wajaribu kuwa na rates za peak season na low season. Kwenye hoteli tayari tuna peak na low season na wakati huu mwezi Machi mpaka wa Julai pia airlines zina low season. Kwa hiyo, ningeshauri Wizara muangalie ni namna gani mnaweza mkapunguza ile park fee ili tuweze kuendana na utalii kama nchi nyingine zinavyofanya; kunakuwa na low season na high season. Kwa hiyo, ningeshauri wafanye hivyo ili tuweze kuongeza watalii zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania Tourist Board imetengewa 4.1 billion. Kwenye hii 4.1 billion wametoa 1.4 kwa ajili ya mishahara, ina maana wanabaki na 2.6 billion. Mheshimiwa Waziri amesema wataenda kutangaza CNN, BBC na matangazo mengine wataweka kwenye majarida na kadhalika. Hata hivyo, kwenye Hotuba ya Upinzani wamesema mwaka 2013/2014, walifanya maonesho kule Sunderland - UK na wanadaiwa karibu shilingi bilioni tano. Sasa sielewi kama hii 2.6 billion inaenda kulipa deni au lile deni linalipwa na nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia vifungu vyote vya randama ya Maliasili na Utalii sijaona hili deni wanalipaje. Mheshimiwa Waziri hebu alete bajeti ambayo ina uhalisia, watakuja kumtumbua hapa, watasema hafanyi kazi lakini pesa hapewi. Kwa hiyo, nafikiri ni vizuri aandikie bajeti yenye uhalisia, aseme madeni ni haya na anahitaji pesa kiasi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo Mlima Kilimanjaro. National Parks zimeingiza shilingi bilioni 185, out of shilingi 185, Kilimanjaro National Park imeingiza shilingi bilioni 60, hizi ni fedha nyingi sana. Najua KINAPA wanajaribu kujenga madarasa na kadhalika lakini bado Halmashauri zinazouzunguka Mlima Kilimanjaro hazifaidiki na mapato yanayotokana na Mlima Kilimanjaro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwenye migodi wanapata 0.3% ya pesa zinazotokana na mgodi, kwa nini isifanyike hivyo kwa Kilimanjaro? Shilingi bilioni 60 ukitoa 0.3% ni hela nyingi sana ambazo zingepewa Halmashauri wakaweza kufanya maendeleo yao wenyewe, wakatengeneza zahanati na madarasa. Mheshimiwa Waziri hata Mwanga ipo katika hizi Halmashauri ambazo zinafaidika na mapato ya Mlima Kilimanjaro, kwa hiyo, nategemea atalichukulia hili on a serious note. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mlima Kilimanjaro ni lazima Wizara ishirikiane na Wizara ya Mazingira, Mlima Kilimanjaro unaharibika. Wamejaribu kukusanya takataka kutoka Mlima Kilimanjaro lakini bado hazijakwisha. Kwa sababu wataalam wako hapa kule Mti Mkubwa kupitia Lemosho na kule Barafu, vyoo viko vitatu na vya shimo ambapo ma-porter, ma-guide na wageni, zaidi ya watu 300 wanatumia vyoo hivyo. Tumekuwa tukiongea hapa ndani ya Bunge hili kuna vyoo ambavyo vilitoka Ujerumani kwa ajili ya majaribio sijui mpaka sasa hivi vyoo vile vimeishia wapi? Naomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kujumuisha atueleze vile vyoo mpaka sasa hivi vimeishia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hilo linaenda sambamba na maji. Barafu, Mweka na Millenium Towers, hakuna maji. Kwa nini sasa KINAPA wasichukue maji kutoka Karanga waka-pump yakaja pale juu ili watalii waweze kuyatumia badala ya sasa hivi wanaenda kuzoa maji mbali na kuyaleta pale. Sasa hivi kule crater watu wana camp crater lakini Mheshimiwa Waziri crater hamna choo, watu wanalala kule halafu ndiyo wanapanda juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watalii wanakuja zaidi ya mara 10 wanakuta mambo ni yaleyale business as usual. Kwa hiyo, naomba waangalie ni jinsi gani wataweza kutengeneza kule crater kuwe pasafi, ni pachafu sana.
Kwa hiyo, waangalie ni jinsi gani wataweza kutengeneza kule juu ili hawa tour leaders wanaorudi waweze kutuletea watalii kwa wingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Southern Circuit. Southern Circuit tunashindwa kuiuza kwa sababu miundombinu si mizuri. Tumekuwa tukizungumza mara nyingi, sasa Wizara hii na Wizara ya Miundombinu iangalie ni jinsi gani inaweza kutengeneza miundombinu ya kwenda Southern Circuit. Wawekezaji wanakuja wanataka wakajenge hoteli lakini wageni watafikaje huko, hoteli ni ghali sana. Kuna ndege moja inayoenda huko inaitwa Coastal Air lakini price yake ni sawa na mtu anayetoka hapa kwenda Europe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazungu wengi wanaokuja Tanzania wana-save for years. Unakuta mtu ame-save almost five, six years ili aweze kuja Tanzania. Tukumbuke wageni wengi wanakuja kwa credit card, akifika hapa anajaribu kuangalia ni kwa jinsi gani anaweza ku-save aizungukie Tanzania yetu ilivyo nzuri lakini unakuta mara nyingi wanaishia kwenye Nothern Circuit kwa sababu ni cheaper, kuna hoteli nyingi lakini wanashindwa kwenda Southern Circuit kwa sababu ni too expensive.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali muangalie ni kwa jinsi gani mnaweza kushirikiana na Wizara ya Miundombinu ili muweze kutengeneza hizo barabara ili wawekezaji waweze kuja kujenga hoteli kule na tuweze kuiuza kama tunavyoiuza Nothern Circuit. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo huyu mjusi aliyeko huko Ujerumani. Kambi ya Upinzani imezungumza vizuri sana, ni fedha nyingi zinazopatikana kule Ujerumani. Euro 25 kwa watu 550 unaongelea karibu shilingi bilioni nne, sasa hivi sisi hatuhitaji hizo shilingi bilioni nne kweli?
Mheshimiwa mwenyekiti, ni kwa nini sasa msifanye arrangement aidha na sisi tupate percent yetu kama ikishindikana msafirisheni basi yule mjusi. Akiwekwa kwenye meli akawekwa pale Dar-es-Salaam ina maana watalii watakuja Dar-es-Salaam badala ya kwenda Ujerumani na sisi tutafaidika. Kuna vipesa vidogovidogo tunahangaikanavyo kwa ajili ya zahanati na kadhalika si vitapatikana pale! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nategemea sasa Mheshimiwa Waziri anavyokuja kutujibu atatueleza ana mkakati gani wa kuhakikisha kwamba yule dinosaur wanamsafirisha aje hapa. Katika Bunge hili yule mama wa Lindi mpaka tukamuita mama mjusi humu ndani, alikuwa anamzungumzia kweli lakini hakuna kilichofanyika mpaka leo. Ni mategemeo yangu sasa kwa wakati huu Mheshimiwa Waziri atakuja na majibu atueleze ana mikakati gani ya kuhakikisha mjusi yule anarudi Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachonisikitisha, mpaka sasa hivi hatuna Bodi ya TANAPA. Naomba Waziri anapokuja kujumuisha hapa hebu atueleze ni kitu gani au ni kwa nini wanashindwa kuunda Bodi ya TANAPA? Vitu vingi sana haviendi, tunalalamika hapa bila Bodi hawawezi kwenda kufanya chochote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aje atueleze ni lini ataunda Bodi ya TANAPA…
(MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uokoaji katika Mlima Kilimanjaro bado huduma ya uokoaji siyo nzuri. Gari halifiki kwenye high altitude na tunapoteza maisha ya watu huko mlimani, kwa nini TANAPA wasinunue helkopta ambayo inaweza kuokoa watu na wagonjwa kwenye high altitude? Hii inaweza kutumika kwenye park zote kwa ajili ya uokoaji pia kulinda majangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake waliopo half mile katika Mlima Kilimanjaro wananyanyaswa sana, wanapigwa na askari wanaolinda msituni, wanafikia hata kubakwa. Ikumbukwe kuwa wao ndiyo wanaolinda mlima, wanatumika kuzima moto unapowaka, wanasaidia watu wasikate miti na pia watu hutumia njia ili kwenda nyumbani. Kuna kijana alipigwa risasi akielekea nyumbani kutoka Kibosho anaitwa Kiwale, je, kesi yake imefikia wapi? Copy nimempa Mheshimiwa Waziri kwa reference.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Umbwe route katika Mlima Kilimanjaro, route hii ni nzuri sana lakini Umbwe cave hakuna maji wala choo, watu wanajisaidia kwenye misitu, hii ni aibu wakati wageni wanalipa kuingia kwenye hifadhi, ni kwa nini wasifuatwe walipe forest fees na park fees wakati park ni moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine Umbwe route hakuna walinzi wa msituni na ukizingatia camp hii ipo karibu kabisa na Kibosho. Umbwe kwa wana vijiji ni rahisi watalii kuvamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, route ya Old Moshi tayari Wizara ya Miundombinu imetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara kutoka Kiboriloni, Kikarara, Kidia, mpaka Tsuduni na njia hii ni fupi kufika Uhuru Peak, kuna water falls na vipepeo, sasa ni lini route hii itaanza kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na wimbi la wazungu wanaojitokeza ku-volunteers kuja kufanya kazi, lakini sasa hivi wanachokifanya wanafanya biashara ya utalii na wanawalaza wageni majumbani katika mitaa ya Moshi, Soweto Rau na kadhalika, wanatumia biashara ya mlima bila kulipa kodi, nashauri tour operaters wote kuwe ni lazima wapeleke TALA licence na tax clearance ili kuonyesha wanalipa kodi. Hii itafanya kodi nyingi kukusanywa na itakuwa ngumu kubakiza fedha nyingi Ulaya.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Pamoja na kuleta Mpango wa Maendeleo wa 2017/2018 napenda kujua ni kwa kiasi gani mpango wa 2016 uliweza kutekelezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya uchumi kwa maelezo ya Waziri inaimarika, lakini kwa uhalisia hali ni mbaya katika sekta nyingi. Mfano benki nyingi za biashara mikopo imeshuka na riba ni kubwa hata vyombo vya habari vimenukuliwa vikisema hayo. Baadhi ya benki mfano CRDB imepata hasara ya shilingi bilioni mbili na zaidi. Wafanyabiashara wanashindwa kurudisha mikopo na wengi wao hawaagizi tena bidhaa kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Serikali yenyewe kwa mwaka 2016 akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola milioni 3,870.3 na hizi zinaweza kuagiza bidhaa nje kwa miezi minne. Je, baada ya miezi minne Serikali imejipangaje? Thamani ya Tanzanian shilling inazidi kushuka na deni la Taifa linazidi kukua, hii ni hatari sana kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya viwanda; Serikali imekuwa ikiimba wimbo wa nchi itakuwa ya viwanda, je, kuanzia wakati wa kampeni hadi sasa ni viwanda vingapi vimeongezeka? Bila kuwa na umeme wa uhakika na kilimo cha kibiashara ili wazalishe, viwanda hivyo vitakuwa ni vya nini? Tulikuwa na kiwanda cha General Tyre Arusha kilichobinafsishwa na Serikali ikakichukua na imekuwa ikitoa ahadi zaidi ya miaka kumi kiwanda kitaanza kazi lakini mpaka leo hakuna uelekeo. Ikumbukwe kiwanda kile kilikuwa kinazalisha matairi bora na kutoa ajira nyingi na Serikali kupata mapato. Nilitegemea Serikali ingetueleza ina mpango gani na kiwanda kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Utalii; hii ni kati ya sekta inayochangia katika pato la Taifa kwa zaidi ya 17%, lakini kwa sasa Serikali inaelekea kwenda kuua kabisa utalii katika nchi yetu. Kitendo cha Serikali kuongeza VAT katika utalii ukizingatia tayari sekta hii ina zaidi ya kodi/leseni 31 zinazolipwa, utalii wetu umekuwa ni ghali sana. Sipingi kulipa kodi lakini tupandishe kwa taratibu. Baadhi ya nchi za Ulaya sheria zao huwezi kupandisha bei zaidi ya 10%. Hivi hawa tembo, simba, twiga na kadhalika kutoka Tanzania tumewaongezea thamani gani wawe na bei kubwa kuwaona kuliko wale waliopo nchi jirani ya Kenya ambao hawalipiwi kodi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ningetaka kujua hivi Wizara ya Fedha inapoandaa Mpango ni kwa kiasi gani wanashirikiana katika mawazo ya kupanga hii mipango na Wizara nyingine? Hivi inapoanzisha viwanda ni kwa kiasi gani wameandaa wataalam, malighafi na kadhalika?
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba ku-declare kwamba mimi ni mdau wa utalii na nitaanza na suala zima la hali ya utalii nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyotambua, utalii ni kati ya sekta ambayo inachangia katika pato la Taifa kwa asilimia 17.5, lakini nasikitika na naona kwamba asilimia hizi zitapungua. Mheshimiwa Waziri wakati akijibu hoja tulivyokuwa tunachangia Kamati ya Bajeti alisema ongezeko la VAT halikuathiri wageni kuja nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mdau; wageni wengi waliokuja mwaka jana; VAT tuliipitisha hapa Bungeni mwezi wa Sita na Sheria ikaanza kutumika mwezi wa Saba; watalii wanatoka nchi mbalimbali wengi walikuwa wameshaanza kusafiri kuja nchini Tanzania, kwa hiyo walikuwa wamesha-book package zao. Kwa vyovyote vile mgeni anakuja mpaka hapa Tanzania amefika unamwambia kwenye package yako na kuongezea eighteen percent hawakubali. Sasa badala yake wale local tour operators ndio waliolipia zile fedha za zaidi na badala ya kuwasaidia Watanzania mmezidi kuwaumiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa ili tuweze kupata figure halisia baada ya mwaka huu tujue ni watalii wangapi wamekuja. Kwa mfano compare Januari mwaka jana na Januari mwaka huu tuone ni watalii wangapi wamefika. Mimi nipo kwenye sekta hii na Januari mwaka huu sasa hivi mahoteli ni matupu hakuna wageni, tujiulize ni kwa nini hakuna wageni? Kule kilimanjaro huwa tuna-run Kilimanjaro marathon; Kilimanjaro marathon ni international inaleta wageni wengi sana hapa Tanzania. Baada ya kukimbia huwa wanapanda mlima, wanaenda safari na wanaenda kwenye beach tours; lakini mwaka huu wageni ni wachache, mahoteli bado hayajajaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba muangalie ni kwa nini wageni hawa hawaji tena Tanzania wanaenda nchi jirani, wanaenda Mombasa. Tuna wanafunzi huwa wanakuja Tanzania kama volunteers wale wanafunzi they are about sixteen to eighteen years old, wanakuja, wazazi wao wanajitolea, wanakuja kwa three weeks holiday; wazazi wanajitolea, wanachangisha fedha wanakuja wanasaidia kwenye kujenga mashule kupaka rangi na kadhalika, lakini hapa Tanzania tumekuwa tukiwachaji work permit ya dola mia tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke wale wanafunzi wakija wanalipa visa fee ya Dola hamsini, bado wakikaa hapa kwa wiki mbili wanapanda mlima, wanaenda safari na wanaenda mpaka Zanzibar. Sasa wazazi wao wamejitolea kuja kutusaidia Watanzania lakini wanachajiwa dola mia tano kwa kuja kujitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali mliangalie hili kwa sababu tunapoteza wageni wetu. Mwaka huu nilikuwa na wageni zaidi ya mia saba lakini wote wame-cancel wanaenda Mombasa, tutapata wageni karibu hamsini tu. Naomba Serikali iliangalie hili tujaribu kuondoa ile permit visa ya dola 500 atleast mchaji reasonable price, labda hata kama dola mia moja hivi itakuwa ni fair, lakini dola mia tano ni nyingi sana tukumbuke na wale ni wanafunzi na wale wazazi wanakuja kutusaidia sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunaamini michezo ni afya na kama Bunge la Tanzania ningefurahi sana tarehe 26 mwezi wa Pili kuwaalika Wabunge na nyie mje mkashiriki kwenye Kili Marathoni; mnaweza mkakimbia zile kilomita tano kama sapoti kwa sababu zile ni fun run mnaweza mkatembea ama mkakimbia, lakini itakuwa na sisi kama Watanzania tumeonesha moyo katika haya mashindano ya Kimataifa ambayo watu wanatoka all over the world lakini sisi kama Watanzania na kama Bunge la Tanzania bado wengi wetu hatujaweza kwenda katika mashindano yale.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Mimi nitachangia katika suala zima la UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zinaonesha kwamba UKIMWI bado maambukizi yapo nami ninaona kama ni janga la Taifa. Watu zaidi ya milioni 1.4 sasa hivi wameambukizwa HIV na watu 54,000 wana maambukizi mapya na watu 36,000 wamekufa na AIDS, asilimia 53 wanatumia dawa za ARV. Takwimu hizi zinatisha, lakini kitu kinachonisikitisha, Mfuko wa UKIMWI bado haujatoa fedha za kutosha. Zamani tuliona kwamba waliweza kutoa matangazo, kuweka vibao kwa ajili ya kutoa elimu kwa ajili ya UKIMWI, lakini sasa hivi matangazo yale hayapo na tumeona mara nyingi nimekuwa nikizungumzia suala zima la maambukizi ya UKIMWI kutokana na wanawake wanavyoenda saluni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake huwa wanakwenda saluni kutengeneza kucha na wakitengeneza kucha wana-share vile vyombo, zile nail cutters kwa ajili ya kusafishia kucha. Ni hatari sana sababu vyombo vile havisafishwi ni chuma na huwa saa nyingine mtu anaweza akajitoboa na kuambukiza yule ambaye alikuwa ameenda saluni kutengeneza kucha. Sijui ni kwa jinsi gani mpaka leo hii Wizara imeweza kuwapelekea wale wenye saluni elimu hii ili waweze kutumia vifaa vya kinga, maana saa nyingine wanafanya hata scrub, anaweza akam-scrub yule mtu lakini yule mtu ukute ana kidonda au yule anayefanya ile scrubing na yeye ana kidonda, kwa namna moja au nyingine anamuambukiza yule ambaye alikuwa anamfanyia hiyo scrubing.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hizi treatment centre, unakuta watu wenye UKIMWI wanaenda sehemu moja kwenye kitengo ambacho wanakwenda kupata ushauri nasaha pamoja na kupewa dawa, lakini wamekuwa wanapata unyanyapaa na unyanyapaa bado unaendelea. Mimi ningeshauri, ni kwa jinsi gani Serikali inaweza ikajumlisha magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu na hawa wenye magonjwa ya UKIMWI wakakaa pamoja, wakapewa zile treatment, wakapewa dawa na hii itawafanya wale wagonjwa wenye UKIMWI kuwa na ari zaidi ya kuweza kwenda kupimwa na wale ambao wana magonjwa ya kisukari na magonjwa ya shinikizo la damu wataweza kukubali kupimwa kwa urahisi kwa sababu watajisikia kwamba hawanyanyapaliwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo hii inaenda sambamba na dawa za kulevya na viroba. Hivi ni vitu ambavyo vinapunguza sana nguvu kazi katika nchi yetu, vijana wengi sana wameathirika, tunajaribu kujenga shule lakini sijui hawa watoto watakaokwenda kwenye hizo shule ni nani kama hatutalichukulia janga hili kama janga la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha vijana zaidi ya 550,000 wameathirika na dawa za kulevya . Kati ya hao 550,000 ni 50,000 ni kwa ajili ya kujidunga zile sindano na tunajua kabisa wakijidunga sindano wanaweza wakapata maambukizi ya UKIMWI. Mimi nafikiri Serikali ingewachukulia hawa mateja kama wagonjwa badala ya kuwakamata na kwenda kuwafunga lock up. Hawa ni watu ambao wanahitaji kutibiwa kwa sababu ni wagonjwa na mara nyingi hawa mateja badala ya kuwapeleka hospitali za watu wenye magonjwa ya akili, mimi nashauri mtengeneze centres za kuwapeleka hawa vijana kwa sababau vijana hawa siyo vichaa, unakuta tu wamekuwa mazombi fulani wala hawamdhuru mtu lakini ukienda kuwachanganya na wale wagonjwa wenye matatizo ya akili wale wanakuwa hyper wanaweza wakawapiga, wanachukua vyuma wanapiga watu, lakini hawa wanahitaji kwamba wawekwe mahali vizuri, wapewe dawa, wapewe elimu ili waweze kuondokana na dawa za kulevya .
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wenzangu wote kabisa hii habari ya kukamata vijana ambao wanatumia dawa za kulevya wale ni innocent, wanatumia tu zile dawa mimi nafikiri ni vizuri mkawakamata wale wanao-supply na hawa vijana wapelekwe waende wakatibiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka naomba nizungumzie suala zima la saratani; Saratani tunajua kutokana na taarifa ni zaidi ya watu 27,000 wanafariki kwa ajili ya magonjwa ya saratani. Kuna baadhi ya saratani kama elimu ikitolewa ya kutosha yanaweza yakatibika, kama tezi dume, saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti inayotokana na ulaji mwingi wa mafuta, kuna Saratani nyingine za ngozi ambazo wanawake wanatumia vipodozi vya kujichubua wanapata ugonjwa wa kansa kutokana na vipodozi. Wizara itoe elimu, wanawake waache kutumia hivi vipodozi vya kemikali kali ili...
(Hapa kengele ililia kuashiri kwisha kwa muda wa Mzungumzaji )
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia. Utunzaji wa mazingira ni muhimu sana katika kuleta maendeleo, kuleta hewa safi, kuongeza mvua na kadhalika. Sisi wote ni mashahidi katika nchi yetu, kumekuwepo na ukame wa kupitiliza kiasi hata mazao hayawezi kulimwa, vyanzo vya maji vinakauka na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, Serikali kwa kupitia kila Kitongoji na Kijiji zile Kamati za Mazingira ziimarishwe, ziwezeshwe kama ilivyokuwa miaka 30 iliyopita. Ilikuwa ni lazima kupanda miti kila shule kuwa na vitalu vya miche, mfano Kilimanjaro ilikuwa hairuhusiwi kulima au kujenga kandokando mwa mto na mifereji iliyokuwa inatiririka maji na mito lakini sasa hivi yote imekauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuyeyuka kwa theluji ya mlima Kilimanjaro, miaka ya hivi karibuni Profesa L. Thomson kutoka University ya Ohio kule Marekani walikuja kufanya utafiti ni kwa nini theluji inapungua kwenye mlima Kilimanjaro, walibeba barafu nyingi sana (in tons) kuzipeleka Marekani. Je, Serikali mmefuatilia walibaini ni kwa nini theluji inapungua katika mlima Kilimanjaro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukisubiri sababu ni vizuri kuhimiza miti kupandwa kwa wingi ili wananchi waweze kupata maji na mvua, kwa sasa hivi Mji wa Moshi ndio wenye joto kubwa kuliko popote hapa nchini na Moshi ipo chini ya Mlima Kilimanjaro hii ni hali ya hatari sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa, ni vizuri Wizara hii na Wizara ya Nishati na Madini waangalie ni jinsi gani wanaweza kushusha bei ya gesi ya kupikia ili kila mwananchi aweze kununua gesi ya kupikia. Hii itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira, miti haitakatwa kwa sababu ya mkaa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia. Ucheleweshwaji wa kusikiliza kesi za mahabusu. Baada ya kesi zilizopo katika uchunguzi chini ya DPP zinachukua muda mrefu sana na wakati watuhumiwa wengine hawana hatia lakini wanaweza kuwa gerezani kwa zaidi ya miezi sita. Je, kesi hizi hazina kikomo cha uchunguzi? Inakuwa kama wanakomoa na kudhalilisha wengine na huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Mfuko wa Mahakama, bado mfuko huu wa fedha zinazoainishwa hazifiki kwa wakati na hata wakizipata zinakuja zimechelewa na pungufu ambayo inakuwa ni vigumu kutekeleza miradi ya maendeleo hii inajionesha mpaka Machi 2017, fedha hazikutumwa kwa wakati. Chombo hiki ni muhimu sana nashauri fedha zipelekwe kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wapo watumishi wa kutosha, kuhakikisha posho za wazee wa mabaraza zinalipwa, wazee hawa wanaacha shughuli zao wengine inabidi watumie nauli zao, hivyo, wana haki ya kupata stahili zao kwa wakati.