Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Josephat Sinkamba Kandege (151 total)

STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne alipofanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana mwaka 2014 aliahidi kupatia x-ray.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya Rais hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hiyo kwa sasa haina kifaa hata kimoja katika kitengo cha mionzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2014 wakati wa ufunguzi wa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi 133,136,000 kwa ajili ya kununua mashine ya x-ray mpya ikiwa ni utekelezaji wa ahadi hiy iliyotolewa na Mheshimiwa Rais inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Wakati Rais akiwa katika kampeni aliahidi kuwa ataondoa ushuru na kodi ndogo ndogo zinazoleta usumbufu kwa wajasiriamali wadogo wadogo kama vile machinga, wachuuzi wa mboga mboga na matunda, mama lishe, waendesha bodaboda na kadhalika, lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya uamuzi wa kufuta ushuru unaotozwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi wakiwemo mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mboga mboga, ndizi na matunda. Vile vile, wafanyabiashara walio nje ya maeneo maalum ya kibiashara wenye mitaji chini ya shilingi 100,000 hawaruhusiwi kulipa ada, tozo na kodi za aina yoyote.
Mheshimiwa MWenyekiti, uamuzi huu umeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai 2017 baada ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 iliyotangaza kufuta ushuru na kodi kero kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Hatua inayoendelea sasa hivi nikuwatambua wafanyabiashara wadogo wote ili kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya. Hivyo, Serikali imetekeleza kwa vitendo ahadi hii iliyoko katika Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2015 inayolenga kuwapatia unafuu wa maisha wananchi wa hali ya chini kiuchumi ili waweze kukua na kuchangia vizuri katika uchumi wa Taifa lao. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) Aliuliza:-
Wakati Rais akiwa kwenye ziara Wilayani Rorya aliahidi ujenzi wa Daraja la Mto Mori linalounganisha Tarafa ya Suba Luoimbo na Nyancha, lakini kwenye bajeti ya mwaka 2016/ 2017 ujenzi wa daraja hilo haukuwepo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga daraja hilo ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Mori unapita katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Rorya hali inayosababisha kuwepo kwa uhitaji wa madaraja mawili ili kurahisisha usafiri katika maeneo hayo mawili. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kupitia Mfuko wa Barabara imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mto Mori kwa upande wa Tarime. Taratibu za manunuzi zinaendelea, ili kumpata mkandarasi wa kujenga daraja hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Rorya usanifu wa awali umefanyika ili kujua gharama za ujenzi wa daraja hilo ambazo zinakadiriwa kuwa shilingi milioni 300. Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imepanga kuweka kipaumbele na kutenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ili kukamilisha ujenzi huo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Msalala kwa kusaidiana na Mbunge wao wameanza ujenzi wa Vituo vya Afya Bugarama, Mega, Ngaya na Isaka na miradi hiyo ipo katika hatua nzuri.
(a) Je, Serikali imejipangaje kusaidia miradi hiyo ya ujenzi wa Vituo vya Afya?
(b) Je, Serikali imejipangaje kukamilisha maboma zaidi ya 28 ya zahanati kwenye vijiji mbalimbli Jimboni Msalala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kujibu maswali, naomba uniruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya na nguvu kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pili, naomba nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Uongozi wote wa Bunge kwa malezi na maelekezo ambayo nimepata, bila kusahau Kamati ya Bajeti, chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Hawa Ghasia kwa malezi na ushirikiano ambao nimekuwa nikiupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu kwa kuniteua kuhudumu katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Uteuzi uliopokelewa kwa mikono miwili kwa wananchi wa Kalambo na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Msalala kwa jitihada anazofanya katika kuwahamasisha wananchi wake kuibua na kuanzisha miradi mingi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Jimbo lake la Msalala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ina jumla ya vituo vya afya vitatu ambavyo ni Lunguya, Chela pamoja na Bugarama vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria. Kati ya vituo hivyo, ni vituo viwili ambavyo ni Kituo cha Afya cha Lunguya na Chela ndivyo vinavyotoa huduma za upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.
Aidha, ujenzi wa vituo vingine vitatu ambavyo ni Isaka, Ngaya na Mega upo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi ambapo lengo la Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2020 vituo hivi viwe vimekamilisha miundombinu muhimu inayohitajika kustahili kuwa vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ina jumla ya maboma 31. Miongoni mwa maboma hayo, matatu ni vituo vya afya tarajiwa ambavyo ni Isaka, Mega na Ngaya. Aidha, kwa sasa Vituo vya Mega na Ngaya maboma yamepauliwa katika jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo Boma la Kituo cha Afya cha Isaka lipo kwenye hatua za lenta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali iliweza kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya nne kwa gharama ya kiasi cha shilingi milioni 277 na saba ambazo zote zipo katika kata ambazo zilikuwa hazina huduma za afya kabisa. Zahanati hizo zipo katika Vijiji vya Nyaminje, Mbizi, Mwanase na Mwakata ambapo kukamilika kwake kumepunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mpango wa kitaifa wa kuboresha vituo vya afya kwa ajili ya kutoa huduma za dharura kwa upasuaji wa akina mama, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 400 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kujenga wodi ya wanawake, nyumba ya watumishi, jiko, jengo la kuhifadhia maiti na ukarabati wa miundombinu ya nyumba za watumishi iliyochakaa katika Kituo cha Afya cha Chela. Kituo cha Afya cha Chela tayari kina jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, maabara, kichomea taka, shimo la kutupia kondo la nyuma na mfumo wa maji safi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga kiasi cha shilingi 336,742,394 za ruzuku ya maendeleo( CDG) kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati katika vijiji saba vya Nyamigege, Gula, Ikinda, Kalole, Jomu, Buchambaga na Ndala, kati ya hayo maboma 31.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Kufuatia utoaji wa elimu ya msingi bure, shule za msingi na sekondari ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime zimekuwa na upungufu mkubwa wa madarasa na madawati hadi kufikia walimu kulazimika kufundishia chini ya mti na wanafunzi walio madarasani wanakaa kwenye sakafu kwa idadi kubwa kinyume na matakwa ya Sera ya Elimu.
Je, ni nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha shule hizo ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime zinaondokana na changamoto za miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ili kutoa elimu bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya miundombinu ya elimu nchini ni matokeo ya mwitikio mkubwa wa wananchi katika utekelezaji wa Mpango wa Elimu Bila Malipo ambao umetoa fursa kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule kupata fursa hiyo. Shule 30 za msingi katika Halmashauri ya Mji wa Tarime zinahitaji vyumba vya madarasa 625, vyumba vya madarasa vilivyopo ni 215 na upungufu ni vyumba vya madarasa 410. Aidha, madawati yanayohitajika ni 8,888; madawati yaliyopo ni 6,066 na upungufu ni madawati 2,823.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nane za sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Tarime zinahitaji kuwa na vyumba vya madarasa 133, madarasa yaliyopo ni 104 ma upungufu ni madarasa 29. Aidha, katika shule hizo kuna ziada ya madawati 421 kutokana na mwitikio mzuri wa wananchi na jitihada za Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo kupitia fedha za kuchochea Maendeleo ya Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi 119,000,000.00 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 16, matundu 19 ya vyoo na kuongeza madawati 154 katika shule za msingi. Vilevile Serikali imetenga shilingi 172,500,000 kupitia ruzuku ya maendeleo na mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 22 na matundu ya vyoo 72.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Wilaya ya Singida Mjini au kituo cha afya Sokoine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima, Mbunge kutoka Singida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanikiwa kununua vifaa tiba vyenye thamani ya Sh.102,939,700.00 kwa kutumia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Vifaa vilivyonunuliwa ni vitanda vitatu
(a) vya kujifungulia, mitungi mitano (5) ya kuhifadhia gesi, vitanda ishirini (20) vya hospitali na mashine tatu (3) za kutakasia vyombo vya hospitali. Vifaa vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine moja (1) ya kutolea dawa ya usingizi (anaestheric machine), kitanda kimoja (1) cha upasuaji (operation table) na mashine ya kutakasia vifaa tiba vyenye ujazo wa lita 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya Sh.160,866.466.01 kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwenye kituo cha afya cha Sokoine. Kati ya fedha hizo, Sh.41,451,400 zimeshalipwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD)kwa ajili ya vifaa tiba. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Hospitali ya Mkoa wa Geita inakabiliwa na kero mbalimbali kama vile ukosefu wa Madaktari Bingwa wa akinamama na watoto, dawa, vifaa tiba pamoja na uhaba wa majengo ya wodi za wazazi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutatua kero hizo katika Hospitali ya Mkoa wa Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabitha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Geita ina Daktari Bingwa mmoja wa upasuaji. Madaktari wengine watatu wako masomoni akiwemo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina Mama na Watoto. Ukosefu wa Madaktari Bingwa unasababishwa na uchache wa Madaktari ukilinganisha na uhitaji wetu. Katika kibali cha mwaka wa fedha 2017/2018 cha kuajiri watumishi 2,058 kilichokuwa na Madaktari 46, Hospitali ya Mkoa wa Geita imepangiwa jumla ya Madaktari wanne ambao wamesharipoti na wameanza kazi, naamini Madaktari hao watapunguza uhaba uliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa dawa, Mkoa wa Geita umepanga kuanzisha duka la dawa kwa kutumia mkopo wa shilingi milioni 160 kutoka NHIF. Wagonjwa watapatiwa dawa na vifaa tiba kwa gharama nafuu zaidi ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kutatua tatizo la uhaba wa miundombinu mkoa unaendelea na ujenzi wa Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. Ujenzi upo katika hatua za msingi kwa majengo manne ambayo ni jengo la upasuaji, wagonjwa wa nje, jengo la mionzi na jengo la kufulia nguo. Kazi hii inatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Mwaka 2014/2015 Serikali kupitia Agizo la Mheshimiwa Rais iliwataka wananchi kuchangia ujenzi wa maabara na wananchi waliitikia kwa kiasi kikubwa sana, hasa katika Wilaya ya Hanang:-
(a) Je, ni lini Serikali italeta vifaa vya maabara katika majengo hayo ya maabara yaliyokamilika katika Wilaya ya Hanang?
(b) Je, Serikali itasaidia vipi kukamilisha maabara ambazo kutokana na njaa wananchi hawakuweza kukamilisha ujenzi wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang ina jumla ya shule za sekondari 33 zenye mahitaji ya vyumba vya maabara 99 kwa ajili ya masomo ya sayansi. Ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule 11 umekamilika kati ya 33 hizi zilizopo.
Mheshimiwa Spika, shule 10 zilizokamilisha ujenzi wa maabara kabla ya Januri 2017 zimepatiwa vifaa vya maabara. Shule moja haikupata vifaa vya maabara kwa kuwa, ilikamilisha ujenzi baada ya Januari 2017. Aidha, Serikali kupitia Mpango wa Elimu Msingi Bila Malipo inatoa fedha ambazo sehemu yake zinatakiwa kutumika kwa ajili ya kununua vifaa na kemikali za maabara. Katika kipindi cha kuanzia Disemba 2015 mpango ulipoanza kutekelezwa, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imepokea na kutumia Sh.253,913,281/= kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara.
(b) Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, zilitengwa shilingi milioni 70 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa maabara katika Shule za Sekondari za Hanang, ikiwepo Msqaroda, Bassodesh, Gidahababieg na Simbay. Vilevile katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, zimetengwa jumla ya shilingi 233,564,900 kwa ajili ya kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa maabara ambazo hazijakamilika. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 80 zinatokana na makusanyo ya ndani ya halmashauri na shilingi 153,564,900 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa maana ya CDG.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Magu fedha za ujenzi wa ofisi za halmashauri, lakini ujenzi huo haujakamilika:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Desdery, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Magu ilianza tarehe 12 Januari, 2013 kwa kutumia Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group wa Dar-es-Salaam. Ujenzi wa Jengo hilo unatarajia kugharimu jumla ya Sh.6,765,596,533.05 hadi kukamilika kulingana na usanifu uliofanyika. Kati ya fedha hizo Sh.2,744,537,216.94 zimeshapokelewa na kutumika tangu mwaka 2013 ujenzi ulipoanza.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 600 kuendelea na ujenzi. Katika robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2017/ 2018 Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 200 ambazo zimepokelewa na halmashauri na mkandarasi anaendelea na ujenzi katika jengo hilo la halmashauri yake.
DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Zaidi ya asilimia 70 ya eneo la Jimbo la Igunga lilikuwa limefunikwa na maji ya Ziwa Victoria lakini baada ya Ziwa hilo kukauka, eneo hilo limebaki kuwa ni mbuga inayojaa maji wakati wa masika hivyo kufanya ujenzi wa barabara za vijiji kuwa wa gharama kubwa sana na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga haina uwezo wa kifedha kujenga barabara hizo.
Je, kwa nini Serikali isiandae mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara za vijijini katika Wilaya ya Igunga na Wilaya nyingine nchini zenye tatizo kama hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Jimbo la Igunga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua tatizo la udongo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini yaani TARURA imepanga kufanya utafiti wa udongo huo ili kuona kama unafaa baada ya kuongezewa kemikali (additive) badala ya kuondoa na kuleta udongo mwingine na hivyo kupunguza gharama za ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Halmashauri ili ziweze kupitika kwa kipindi chote. Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Igunga shilingi milioni 336.8 ambazo zilitumika kufanya matengenezo ya barabara kilometa 119.3, madaraja 8 na kalvati 10. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/18 Hamashauri hiyo imetengewa shilingi bilioni 1.26 ambapo hadi tarehe 30 Septemba, 2017 fedha zilizopokelewa ni shilingi milioni 241.9. Taratibu na kumpata mkandarasi zinaendelea.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Tatizo la uhaba wa watumishi wa Idara ya Afya Urambo linaathiri utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura katika kuliondoa tatizo la uhaba wa watumishi wa Idara ya Afya Wilayani Urambo?
(b) Je, Serikali inaweza kuchukua vijana wa Urambo na kuwapeleka vyuoni kusoma kwa makubaliano ya kurudi kufanya kazi Urambo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE)alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ina upungufu wa watumishi wa kada ya afya. Tatizo hili linazikabili Halmashauri nyingi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuwaajiri wataalam wa kada ya afya kipindi wanapohitimu mafunzo na kufaulu vizuri katika masomo yao. Aidha, kuanzia mwezi Novemba, 2015 Serikali ilisitisha zoezi la kuajiri ili kubaini watumishi wa umma walioajiriwa na hawakuwa na sifa stahiki na kuwatambua watumishi halali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilisha zoezi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeendelea kutoa vibali vya watumishi wa kada za afya ambapo mwezi Aprili, 2017 tulipata kibali cha kuajiri madakrati 209. Katika kibali hicho, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ilipata madaktari wawili. Vilevile mwezi Julai, 2017 tumepokea kibali cha watumsihi 2,152 ambao wamepangiwa katika Mikao na Halmashauri kwa uwiano ili kupunguza uhaba wa watumishi. Katika mgao huu Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ilipata watumishi 17. Serikali itaendelea kupanga watumishi kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kuwasomesha vijana kwa makubaliano ya kurudi kufanyakazi umeshindwa kufanikiwa kwani uzoefu unaonesha vijana wengi wamesomeshwa na kuhitimu wanakuwa wamebadili mawazo na kuamua kufanyakazi sehemu nyingine na kuacha mgogoro kati ya wasomeshaji na aliyesomeshwa. Serikali inaendelea kuboresha mazingira kama vile upatikanaji wa nyumba pamoja na huduma za kijamii ili kuwafanya watumishi wanaoajiriwa waweze kubakia katika maeneo waliyopangwa.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Ukosefu wa nyumba za walimu maeneo ya vijijini husababisha walimu kuhama maeneo hayo na hivyo kupelekea upungufu mkubwa wa walimu. Aidha, Halmashauri nyingi zikiwemo za Mkoa wa Ruvuma hazina uwezo wa kujenga nyumba za walimu kwa kutumia fedha za ndani.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi vijijini ili kuweka mazingira rafiki ya kufanyia kazi kwa walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa upo upungufu wa nyumba za walimu nchini. Nyumba zilizopo kwa ajili ya walimu wa shule za msingi ni 41,321 wakati mahitaji halisi ni nyumba 222,115 hivyo kuna upungufu wa vyumba 179,794 sawa na asilimia 81. Mkoa wa Ruvuma una upungufu wa nyumba 5,470 za walimu wa shule za msingi.
Mheshmiwa Naibu Spika, Seriakli ina mikakati mbalimbali ya kuboresha utoaji wa elimu Nchini ikiwemo kutenga fedha za ujenzi wa nyumba za walimu. Kwa mwka wa fedha 2017/18 Seriakli imetenga jumla ya shilingi bilioni
• kwa ajili ya uejzi wa nyumba 1,669 za walimu wa shule za msingi nchini. Mkoa wa Ruvuma umetengewa shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 30 za walimu wa shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuendelea kujenga nyumba za walimu kadri fedha zinavyopatikana kwa lengo la kuboresha mazingira na makazi kwa walimu. Ujenzi wa nyumba za walimu ni jukumu la wadau wote kuanzia Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, wananchi kwa ujumla, hivyo natoa wito kwa wadau wote walimu kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-
Wilaya ya Namtumbo haina huduma stahiki za Hospitali ya Wilaya wala Vituo vya Afya licha ya kuwepo kwa Sera ya kila Wilaya iwe na Hospitali ya Wilaya na kila Kata iwe na Kituo cha Afya.
(a) Je, sera hiyo kwa Wilaya ya Namtumbo itatekelezwa lini?
(b) Makadirio yaliyofanywa na TBA kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo ni shilingi bilioni19. Je, Serikali ipo tayari kutenga na kutoa kiasi hicho katika bajeti ya mwaka 2018/2019?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vitendea kazi na wataalam katika Vituo vya Afya vitano vilivyopo Namtumbo ili viweze kutoa huduma bora za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo ulianza rasmi mwaka 2010 na unatekelezwa kwa awamu tofauti ambapo mpaka sasa unaendelea. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 600 kimeshatumika kwa ajIli ya kujenga majengo ya utawala, jengo la wagonjwa wa nje yaani OPD, chumba cha kujifungulia yaani labour room, kichomea taka (incinerator), msingi na jamvi kwa chumba cha akina mama wajawazito (maternity ward) pamoja na mfumo wa maji safi na taka (water and sewage system). Kwa mwaka 2017/2018, Halmashauri imepokea shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuendeleza na kumaliza jengo la wodi ya akina mama wajawazito.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la upasuaji ili kuimarisha huduma za upasuaji katika hospitali hiyo.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Namtumbo ina jumla ya vituo vya afya saba ambapo vitano vinamilikiwa na Serikali na viwili vinamilikiwa na mashirika ya dini. Vituo vya Afya vya Serikali ni Namtumbo, Msindo, Mputa, Mkongo na Lusewa. Vituo vya Afya vya mashirika ya dini ni Namabengo na Hanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya upasuaji wa dharura kwa akinamama wajawazito inafanyika katika Kituo cha Afya Hanga. Katika Kituo cha Afya Lusewa, jengo la upasuaji lipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na vifaa vya upasuaji vipo katika mchakato wa kununuliwa lakini kuna tatizo la maji ambalo pia linashughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Namtumbo kimepokea jumla ya shilingi milioni 400 tarehe 21 Desemba, 2017 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati wa majengo ya upasuaji, wodi ya wazazi, maabara na chumba cha kuhifadhia maiti ambayo kazi yake inaendelea katika hatua za ukamilishaji na inategemea kukamilika tarehe 30 Aprili,2018. Aidha, Serikali imeagiza vifaa vya chumba cha upasuaji kwa ajili ya kutoa huduma ya upasuaji kwa akina mama wajawazito (CeMOC) kwa Vituo vya Afya vya Msindo na Mputa ili kuondoa tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni kubwa sana.
Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuliondoa tatizo hilo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu wali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya 465 ambapo waliopo ni 235 na upungufu ni 240. Upungufu huu umetokana na sababu mbalimbali ikiwemo uhamisho, vifo, kustaafu pamoja na zoezi la Kiserikali la kuondoa watumishi hewa na wale waliokuwa na vyeti fake. Hata hivyo, baada ya kukamilisha mazoezi hayo, Serikali imeanza kutoa vibali vya kuajiri kada mbalimbali ikiwemo kada ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mgao wa watumishi wa nchi nzima mwaka 2017, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilipata jumla ya watumishi 22 kati yao ni madaktari wawili. Watumishi hao wote wameripoti kwenye vitu na wanaendelea na kazi. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetenga katika bajeti na kuomba kibali cha kuajiri watumishi 121 katika sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kuajiri wataalam zaidi ili kutatua changamoto ya uchache wa watumishi katika wilaya hiyo.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Katika Mtaa wa Mongolandege, Kata ya Ukonga, kuna daraja la Mongolandege ambalo huunganisha Jimbo la Ukonga na Jimbo la Segerea. Aidha, daraja la Mto Nyebulu huunganisha Kata ya Buyuni na Kata ya Chanika Magengeni.
Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo muhimu ili kurahisisha huduma za kijamii katika maeneo yaliyotajwa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Mongolandege linatakiwa kujengwa katika Bonde la Mto Mzinga ambalo awali palijengwa makalavati kwa nguvu za wananchi. Kalavati hizo zilishindwa kufanya kazi kwa ufanisi baada ya mkondo wa mto kupanuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mwaka 2012, Manispaa ya Ilala ilijenga box culvert ili kuwezesha eneo hilo kupitika. Hata hivyo, mvua zilizonyesha kwa wingi katika kipindi hicho zilileta madhara makubwa ambapo bonde hilo lilitanuka na kalavati hiyo kusombwa na maji na kusababisha kukosekana mawasiliano katika eneo hilo. Daraja la Nyebulu linatakiwa kujengwa katika Mto Vikorongo na litakuwa na wastani wa upana wa mita 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala itatenga fedha katika mpango wa matengenezo ya barabara na madaraja kwa mwaka wa fedha 2018/2019 za kufanyia usanifu wa kina kwa ajili ya madaraja yote mawili. Aidha, baada ya usanifu huo kukamilika, gharama halisi za ujenzi wa madaraja hayo zitafahamika na kutengwa kwenye bajeti.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:-
Mji wa Kibaha ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani na yapo maombi yaliyokwishapelekwa Serikalini kuomba Mji huo upewe hadhi ya kuwa Manispaa lakini hakuna majibu kwa ombi hilo hadi sasa:-
Je, ni kwa nini mpaka sasa Serikali haijaupa hadhi Mji huo kuwa Manispaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maombi ya kuupandisha hadhi Mji wa Kibaha kuwa Manispaa kupokelewa mwezi Agosti, 2016; Ofisi ya Rais , TAMISEMI ilifanya uhakiki uliobaini kuwa Mji wa Kibaha ulikuwa na wakazi 128,488 (sensa ya Mwaka 2012), Kata 14, Mitaa 73 ambapo ni asilimia 56 tu ya wakazi ndio walikuwa wakipata huduma za maji safi na pia haukuwa na mpango kabambe wa uendelezaji wa Mji (Master plan).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali wa mwaka 2014, vigezo vya kupandisha hadhi miji kuwa manispaa unatakiwa kuwa na wakazi si chini ya 300,000, Kata si chini ya 15, Mitaa si chini ya 75, wakazi wanaopata huduma za maji wawe si chini ya asilimia 75 ya wakazi wote wa mji na uwepo mpango kabambe wa uendelezaji wa Mji (Master plan). Kutokana na vigezo hivyo kutofikiwa, ilidhihirika kuwa Mji wa kibaha haukuwa umefuzu kupandishwa hadhi kuwa Manispaa. Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani alijulishwa matokeo hayo kwa barua yenye kumb. Na. CCB.132/394/01/16 ya tarehe 12 Juni, 2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Halmashauri zina wataalam wa kusimamia na kutekeleza mipango yao na zina uwezo kisheria kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, elimu, afya, maji kilimo na ardhi pasipo kuingiliwa. Viongozi na Watendaji wa Serikali ngazi za Mkoa na Wilaya huambiwa watawajibishwa kufikia malengo mathalani, katika ujenzi wa maabara, madarasa na kutengeneza madawati:-
Je, mipaka ipi ni ya kinadharia (theoretical) na ipi inatekeleza (practical) kiutendaji na uwajibikaji kati ya viongozi wa Serikali Kuu na Halmashauri za Majiji, Miji na Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Joseph Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugatuzi wa madaraka ya kisiasa, fedha na utawala kutoka Serikali Kuu kwenda kwa wananchi kupitia Serikali za Mitaa umetokana na mahitaji ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 145 na 146. Madhumuni ya ugatuzi ni kuwapa wananchi kupitia Mabaraza yao ya Madiwani, uwezo wa kufanya maamuzi kulingana na mahitaji yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali za Mitaa zimeundwa kwa mujibu wa Sheria Na.7 (Mamlaka za Wilaya) na Sheria Na.8 (Mamlaka za Miji)kwa malengo ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi pamoja na kusimamia ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria kuweka utaratibu wa Serikali za Mitaa kujiamulia mambo yake kupitia vikao rasmi, hazijapewa uwezo wa kukataa maelekezo ya Serikali Kuu. Kwa mujibu wa Sera ya Maboresho ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1998, Serikali Kuu ina majukumu ya kutunga sera, kutoa miongozo ya namna bora ya kutekeleza sera, kuandaa mikakati ya kitaifa, kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa sera kwa kuzipatia Serikali za Mitaa rasilimali watu, rasilimali fedha na baadhi ya vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuweka viwango vya utekelezaji, kufuatilia utekelezaji ili kujiridhisha kuwa miongozo na viwango vinazingatiwa na kuchukua hatua dhidi ya utekelezaji usioridhisha inapobidi hasa inapobainika matumizi yasiyo sahihi ya fedha ikiwemo viwango duni vya miradi visivyolingana na thamani ya fedha iliyotumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali Kuu huwakilishwa na viongozi wa Mikoa na Wilaya katika kusimamia utekelezaji wa sera na miongozo, Viongozi Wakuu wa Serikali ngazi ya Mikoa na Wilaya hutekeleza majukumu yao ya kisheria ya kuziwezesha Serikali za Mitaa kutimiza majukumu yao kikamilifu ikiwemo kutekeleza maagizo halali na ushauri wa viongozi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibainika kiongozi wa Mkoa au Wilaya ameshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo kusababisha Mamlaka ya Serikali za Mtaa zisitimize vizuri majukumu yao, Mamlaka ya uteuzi huchukua hatua za kiutawala. Napenda kusisitiza kwamba Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi zikirejewa vizuri hakuna mgogoro wowote wa kimipaka wala kiutendaji utakaodhihiri.
MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Walimu wa Elimu Maalum wanapohitimu kwenye Vyuo vya Patandi na SEKOMU hawapelekwi kwenye shule za vitengo vya elimu maalum:-
(a) Je, Serikali haioni kama inapoteza rasilimali fedha na watu kwa kutoa elimu isiyo na tija kwa Walimu hao?
(b) Je, ni lini Serikali itawapanga walimu wenye elimu maalum kwenye shule na vitengo vyenye mahitaji hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo alilosema Mheshimiwa Bilago halihusiani kabisa na swali lake. Hata hivyo, nataka kumwambia kwamba kukatika kwa mkanda si kuvuliwa kwa mkanda. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa mafunzo kwa Walimu ni miongoni mwa mikakati ya kuongeza tija ya kazi na ubora wa elimu inayotolewa, si kupoteza rasilimali fedha na rasilimaliwatu. Kwa muktadha huo, Chuo wa Walimu wa Elimu Maalum Patandi hudahili Walimu kutoka kazini ambao huhitimu kwa viwango vya astashahada na stashahada. Chuo Kikuu cha Elimu Maalum SEKOMU hudahili walimu kutoka kazini na pia Walimu wapya kwa kiwango cha shahada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vyuo vyote viwili, wahitimu waliodahiliwa kutoka kazini hurudi kwenye vituo vyao vya kazi wakisubiri uhamisho kwenda kwenye shule za vitengo vya elimu maalum; na wahitimu ambao hudahiliwa kabla ya ajira huajiriwa na Serikali na kupangiwa shule zenye vitengo vya elimu maalum na wengine huajiriwa na Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2012 na 2015 Serikali iliajiri Walimu wapya 614 wa elimu maalum ambao walipangiwa kufundisha kwenye shule zenye vitengo vya elimu maalum. Hadi Desemba 2016 wapo Walimu 3,957 wa elimu maalum nchini sawa na asilimia 74.3 ya Walimu 5,324 wanaohitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha Walimu wote wenye taaluma za elimu maalum wanatumika vizuri, nazielekeza Halmashauri zote ziwahamishie Walimu wa elimu maalum kwenye shule zenye vitengo vya elimu maalum ifikapo Desemba 31, 2018. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Wananchi wa Kata ya Nkandasi wamejitahidi kujenga shule ya Sekondari ya Kata ya Milundikwa hadi kufikia kidato cha sita lakini Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeamuru shule hiyo kuhamishwa mara moja kuanzia tarehe 1 Januari, 2017 kuachia Jeshi:-
(a) Wananchi walitumia muda na rasilimali zao kukamilisha ujenzi huo na sasa wanakwenda kuanza upya: je, ni upi mchango wa Wizara kwa ujenzi mpya wa shule?
(b) Wizara ya Elimu imeafiki kuhamishwa shule hiyo ya Kata; Je, ni upi mchango wa Wizara katika uhamishaji wa shule hiyo?
(c) Je, Serikali iko tayari kufanya uthamini wa miundombinu yote ya shule na majengo, yaliyojengwa na wananchi na thamani hiyo kuitoa katika fedha taslimu kwa ujenzo wa shule mpya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deusderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Jeshi la Kujenga Taifa kuhitaji eneo lao ilipokuwa imejengwa shule ya sekondari ya Milundikwa kuanzia Januari 2017, Serikali ilihamishia shule hiyo kwenye eneo jipya la Kijiji cha Kasu A. Ushirikiano mzuri baina ya Serikali Kuu, Halmashauri, JKT, Mbunge na wananchi umewezesha ujenzi wa madarasa 13, vyoo matundu 26 na bweni moja kukamilika. Ujenzi wa maabara moja ya sayansi na bweni la pili uko katika hatua za mwisho ambapo wanafunzi 461 wakiwepo 92 wa kidato cha tano wanasoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuchangia shilingi milioni mbili na wananchi wa Kata ya Nkandasi hususan Vijiji vya Katani, Kisula, Malongwe, Milundikwa, Kasu A na Kasu B kwa kujitolea kuchimba msingi, kukusanya mawe na mchanga, kuteka maji kwa ajili ya ujenzi kwa utaratibu wa 50 kwa 50 yaani wanaume 50, wanawake 50 kila siku ya ujenzi na kufyatua tofali za kuchoma laki mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi nayo ilitoa milioni arobaini na tisa kwa ajili ya ujenzi huo na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa shilingi milioni mia mbili hamsini na tisa zilizotumika kujenga vyumba vya madarasa manne, vyoo matundu 22 na mabweni mawili ambapo ujenzi wa bweni la pili unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia ukamilishaji wa bweni la pili, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mwezi Desemba, 2017 imepeleka shilingi milioni mia moja na Jeshi la Kujenga Taifa nalo lilichangia mabati 204, miche 300 ya miti kwa ajili ya mazingira na pia imetoa Walimu 10 wanajeshi ambao wanafundisha shuleni hapo. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Serikali imependekeza shule hiyo itengewe shilingi milioni 230 ili kujenga maabara za sayansi mbili, jengo la utawala, bwalo na nyumba za Walimu endapo Bunge litaridhia.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapaleka madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni hasa ikizingatiwa kuwa hali ya hospitali hiyo kwa sasa sio nzuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupokea kibali cha ajira mwezi Julai, 2017 Serikali imepanga watumishi katika maeneo mbalimbali ili kupunguza tatizo la watumishi. Katika mgao huo Halmashauri ya Mji wa Handeni imepokea jumla ya watumishi 10 waliopangiwa vituo vya kazi Novemba, 2017. Watumishi waliopangiwa ni Daktari Daraja la II 1, Tabibu Wasaidizi wawili, Tabibu Meno mmoja, Wauguzi wawili, Afisa Muuguzi Msaidizi mmoja na Wateknolojia Wasaidizi Maabara wawili. Watumishi wote wamesharipoti na wanaendelea na kazi kama walivyopangiwa. Mgawanyo huu umefanyika ili kila eneo lipate wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na watumishi hao wapya, Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa afya inao watumishi 13 wanaofanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi ambao wanafanya kazi katika Hospitali ya Wilaya Handeni. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi wa kada za afya 182 ili kukamilisha Ikama ya Idara ya Afya ya Halmashauri ya Mji Handeni. Serikali itaendelea kupanga watumishi kadri bajeti ya mishahara itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ambazo zimeathirika kwa kiwango kikubwa kinachoathiri utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na zoezi la uhakiki wa vyeti fake zinaelekezwa kuwasilisha maombi ya ajira mbadala moja kwa moja Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuweza kutatua changamoto hiyo.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa ya Haydom inahudumia wananchi wengi lakini inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi, madaktari wakiwemo Madaktari Bingwa pamoja na ukosefu wa maji.
(a) Je, Serikali itachukua hatua gani za dharura kutatua changamoto hizo?
(b) Kwa kuwa watumishi hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu, je, ni kwa nini Serikali isiondoe kodi kwenye posho zao kama vile on-call allowance, hardship allowance na food allowance?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Haydom inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ina jumla ya watumishi 680 ambapo kati yao watumishi wa Serikali ni 156. Serikali imekuwa ikiisaidia hospitali kupitia Sera ya Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ambapo mpaka sasa imepeleka watumishi 156 wa kada mbalimbali wakiwepo madaktari 10 ambapo saba ni Madaktari Bingwa na watatu ni Madaktari wa Kawaida. Mbali na watumishi, Hospitali ya Haydom inapata ruzuku ya dawa kupitia MSD na ruzuku ya fedha za Busket Funds kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu. Hata hivyo, Serikali itaendelea kupeleka watumishi hasa madaktari na wauguzi kadri vibali vya ajira vitakavyokuwa vinapatikana.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Haydom inapata maji kutoka chanzo cha maji kilichopo umbali wa kilometa 20 katika Kijiji cha Binja, Kata ya Endamilay, Wilaya ya Mbulu. Hospitali hiyo inajitosheleza kabisa kwa maji hayo. Hata hivyo, maji haya yanapatikana kwa gharama kubwa kutokana na kukosekana kwa nishati ya umeme katika eneo husika, hivyo hospitali kulazimika kusukuma maji kwa kutumia mitambo ya dizeli (jenereta) inayotumia jumla ya lita 2,800 kwa mwezi sawa na shilingi 6,020,000/= ambayo ni sawa na shilingi 72,240,000/= kwa mwaka.
Kwa kuwa hivi sasa kupitia Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) inasambaza umeme katika maeneo mbalimbali yakiwapo ya Haydom inatarajiwa kuwa umeme huo utasaidia mradi wa maji wa Hospitali ya Haydom kupata huduma ya umeme na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji wa kutumia dizeli.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Haydom ina makundi mawili ya waajiriwa kama ifuatavyo; kundi la kwanza ni waajiriwa walioajiriwa na Hospitali ya Haydom moja kwa moja na hukatwa kodi ya mapato kama sheria inavyoelekeza; kundi la pili ni la waajiriwa waliajiriwa na Serikali lakini wanafanyakazi Hospitali ya Kilutheri Haydom, watumishi hawa wanalipwa posho ya kuitwa kazini baada ya masaa ya kazi (on-call allowance) na Hospitali ya Haydom na hii ndiyo sababu inayopelekea wakatwe kodi katika posho hiyo. Makato hayo yanatokana na Sheria ya Kodi ya Mapato (Income Tax) ya mwaka 1973.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Upembuzi yakinifu wa kutumia chanzo cha maji cha Mto Ibofwe ili kumaliza tatizo la maji katika Kata za Magulilwa, Luhota, Mseke, Ifunda, Mgama na Maboga ulifanyika kati ya mwaka 1995 – 2000 chini ya usimamizi wa Mbunge wakati huo, Mheshimiwa George Mlawa na bajeti ya utekelezaji wake kupitishwa na Bunge hili ili uwe katika kipindi cha mwaka 2000-2005/2005-2010.
Je, ni tatizo gani lililofanya mradi huo usikamilike na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka wakati Bunge lilikwishapitisha bajeti ya mradi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa kutumia chanzo cha Mto Ibofwe ulifanyiwa usanifu wa awali miaka ya 1990 lakini haukufanyiwa usanifu wa kina (detailed design) ambao ungebaini mahitaji na gharama halisi za kutengeneza mradi huo ndiyo maana haukutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwapatia huduma ya maji wananchi wa Kata za Maboga, Lumuli, Isupilo na Itengulinyi, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji unaogharimu shilingi bilioni 2.18 utakaonufaisha wakazi 6,914 katika maeneo hayo. Mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2013/2014 ulisimama utekelezaji wake mwaka 2015 kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 umetengewa shilingi milioni 800 na unatarajiwa kukamilika Desemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kati ya Julai 2016 na Desemba 2017, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imechimba visima sita katika Kata za Magulilo kisima kimoja, Luhota visima vitatu, Maboga kisima kimoja na Mgama kisima kimoja vinavyohudumia wananchi 1,600. Idadi ya visima kwenye kata hizo tangu miaka ya 1990 hadi sasa imefikia visima 41 vinavyohudumia wakazi 8,200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwaka huu 2017/2018, jumla ya shilingi 410,000,000 zimetengwa kutekeleza miradi ya maji ya Izazi - Mnadani, Migoli - Mtera, Malinzanga, Isupilo – Lumweli – Itengulinyi - Magunga na Mfyome. Mpango wa muda mrefu wa Serikali ni kufanya usanifu wa kina (detailed design) ili hatimaye tutumie chanzo cha Mto Ibofwe kumaliza kabisa matatizo ya maji kwenye maeneo hayo. Usanifu wa kina utafanyika mwaka 2018/2019 kwa gharama ya shilingi milioni 49.56 ambazo ziko kwenye mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018/2019 endapo Bunge litaridhia.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI aliuliza:-
Zahanati ya Kalenga iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa haikidhi mahitaji halisi ya wakazi wa vijiji vinavyoizunguka.
Je, ni lini Serikali itaboresha zahanati hiyo kwa kujenga vyumba vya ziada na mahitaji mengine ya msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Nuhu Mwamwindi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zahanati ya Kalenga ilijengwa zaidi ya miaka 40 iliyopita. Kutokana na ongezeko la watu, kwa sasa zahanati hii imekuwa ikitoa huduma kwa wananchi ambao wamekuwa wengi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Hata hivyo, Halmashauri haiwezi kuongeza majengo kwenye eneo la zahanati hii, kwani tayari imezungukwa na makazi ya watu, hivyo hakuna nafasi ya kuongeza majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya vijiji vilivyokuwa vinapata huduma kwenye zahanati hii, vimejengewa zahanati ambayo ni zahanati ya Mangalali iliyofunguliwa mwezi Februari, 2017. Zahanati hii imesaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika zahanati ya Kalenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, juhudi zinafanyika kwa kuhamasisha ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Jirani ya Mlanda. Ujenzi huu unafanyika kwa nguvu za wananchi na upo katika hatua za awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri katika mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 imetenga kiasi cha shilingi milioni 54 ili kufanikisha ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Mlanda. Kituo hicho kitakapokamilika, kwa kiasi kikubwa kitapunguza msongamano wa wagonjwa katika Zahanati ya Kalenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuziagiza Halmashauri zote nchini kutenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya Taasisi za Umma kama vile shule, vituo vya kutolea huduma za afya na Ofisi za Vijiji, Mitaa, Kata na kuhakikisha maeneo haya yanapimwa na kupatiwa Hati Miliki ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza siku za usoni.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:-
Je, kuvunjwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuna faida gani kwa wakazi wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, maarufu kama mashine ya Kusini, kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilivunja Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) tarehe 15 Mei, 2017 kutokana na muingiliano wa kimamlaka kati yake na Manispaa ya Dodoma ambapo licha ya kuongeza gharama za uendeshaji, ulisababisha migogoro mingi ya kiuendeshaji, ikiwemo vyanzo vya mapato na migogoro ya ardhi, hali iliyosababisha kupungua kwa kasi ya maendeleo ya mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuvunjwa CDA wananchi wamepata faida nyingi ikiwa ni pamoja na kupungua kwa gharama za uendeshaji ambazo zilibebwa na wananchi kupitia kodi, kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa kazi, kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri ambayo matumizi yake huamuliwa na Wawakilishi wa wananchi (Madiwani), kuongezeka kwa idadi ya watumishi, majengo, maabara na vitendea kazi vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hilo limewezesha kuongeza ufanisi wa Manispaa katika kuwahudumia wananchi.
Aidha, ubadilishaji wa mikataba ya upangishaji (Ground Lease Agreements) za miaka 33 iliyokuwa ikitolewa na CDA kwa kuwapatia wananchi Hatimiliki za miaka 99 umehamasisha uwekezaji katika kuendeleza kwa kasi zaidi Mji wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi kifupi cha kuanzia Mei hadi Desemba, 2017 wananchi wamebadilisha jumla ya mikataba 19,000 kati ya 65,000 iliyotolewa na CDA kuwa kwenye mfumo mpya wa Hatimiliki za miaka 99.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na faida hizo, Manispaa ya Dodoma inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo madeni na migogoro iliyorithiwa kutoka CDA. Manispaa inakabiliana na changamoto hizo kwa kuimarisha makusanyo na kuimarisha usimamizi katika sekta ya ardhi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika Jimbo la Tunduru Kusini kuna vituo vitatu vya afya ambapo Kituo cha Afya Mtina kina zaidi ya miaka 30 hakijafanyiwa ukarabati na pia hakuna wodi ya wazazi.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi ya wazazi katika kituo hicho na kufanya ukarabati ili kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa Kata za Nasya, Semeni, Nyerere, Angalia na wakazi wa Kata ya Mchesi, Vijiji vya Likumbula, Tuwemacho na Namasakata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina vituo vitano ambapo vituo vya afya viwili vipo katika Jimbo la Tunduru Kusini na vitatu katika Jimbo la Tunduru Kaskazini. Kituo cha Afya Mtina kilianzishwa mnamo mwaka 1970 na kimekuwa kikiendelea kutoa huduma za kujifungua na huduma za matibabu ya kawaida kwa kipindi chote. Kwa sasa chumba cha kupumzikia akina mama baada ya kujifungua kimetengwa ndani ya wodi ya kawaida ya wanawake. Serikali kupitia wadau wa maendeleo (Walter Reed Program) waliweza kufanya ukarabati wa jengo la tiba na matunzo (CTC) kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa msingi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Mtina unaendelea kupitia fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo la Tunduru Kusini ambapo kiasi cha shilingi milioni nne zilitolewa. Aidha, Halmashauri katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/ 2019 imetenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukarabati na kuboresha Kituo cha Afya Mtina.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Tunduru, Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Mkasale kilichopo katika Jimbo la Tunduru Kusini. Aidha, Halmashauri inajenga wodi mbili za upasuaji katika Hospitali ya Wilaya, nyumba ya mganga katika zahanati ya Naikula, ukarabati wa nyumba mbili za watumishi katika Kituo cha Afya Mchoteka na kuendeleza ujenzi wa zahanati ya Legezamwendo kupitia mapato yake ya ndani. Serikali itaendelea kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya kwa kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. AUGUSTINO M. MASELLE aliuliza:-
Ni Sera ya Taifa kuwa na Vituo vya Afya kwa kila Kata, na wananchi katika baadhi ya Kata wamejitahidi kujenga majengo kwa ajili ya vituo hadi kufikia usawa wa renta kwa nguvu zao:-
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo ya vituo vya afya vya Ikobe, Ilolangulu, Kagera na Bukandwe?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Watumishi wa Afya Wilayani Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Maselle lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutelekeza Sera ya Afya ya kuwa na kituo cha afya katika kila kata. Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ina vituo viwili vya afya ambavyo ni Kituo cha Afya Iboya na Masumbwe, vituo vingine viwili vya Nhomolwa na Kagera viko katika hatua ya ukamilishaji wa ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia uhisani wa Canada, Benki ya Dunia na Sweden imetoa kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuboresha na kujenga miundombinu ya vituo vya afya vya Masumbwe na Iboya sawa na shilingi milioni 400 kwa kila kituo ili kuboresha huduma za mama na mtoto. Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imetenga kiasi cha shilingi milioni 35 kupitia ruzuku ya Maendeleo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo katika vituo vya afya Nhomolwa na Kagera pamoja na shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la wazazi katika zahanati ya Ilolangulu. Zahanati ya Bukandwe itatengewa fedha katika bajeti ya mwaka wa 2018/2019.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeajiri wataalam wa afya 2509 ambapo kati ya hao 16 walipangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe na watumishi 13 wameripoti na kupangiwa vituo vya kazi. Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa afya kadri wanavyohitimu na kupangwa moja kwa moja kwenye vituo.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-
Matatizo ya migogoro ya ardhi na Mipango Miji ni suala nyeti sana linalohitaji kutazamwa sana katika zama hizi; na hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam lakini zoezi hilo halikufanikiwa kutokana na kukosa mkakati ulioambatana na matumizi ya ramani hizo:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ramani hizo zinapatikana kwa nchi nzima ili kusaidia kuongoza matumizi ya ardhi katika miji mingi nchini?
(b) Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema Serikali ingeuza Government Bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huo; Je, agizo hili limefikia hatua gani katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Na. 8 ya Mipango Miji ya Mwaka 2007 katika Kifungu cha 21(1) inazipa Halmashauri mamlaka ya kupanga na kuhakikisha ramani za Mipango Miji ya jumla (master plan) na ile ya kina (michoro ya mipango miji) iliyoidhinishwa na Wizara yenye dhamana na ardhi zinahifadhiwa na kusambazwa kwa wadau. Halmashauri zinaendelea kutekeleza jukumu hili kwa kutoa elimu na tafsiri sahihi ya michoro ya Mipango Miji kwa wananchi ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi shirikishi kwa lengo la kudhibiti uendelezaji holela.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kuuza bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huu, suala hili halijatekelezwa badala yake kila Halmashauri imeelekezwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ya ndani kwa kushirikiana na sekta binafsi. Utaratibu huu unatokana na Sheria ya Mipango Miji inayotoa fursa kwa wamiliki binafsi wa ardhi kuandaa mipango ya matumizi kwa mujibu wa sheria.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapelaka fedha za kutosha kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga ambao umeanzishwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kupitia fedha za ruzuku kutoka Serikalini imekamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), nyumba moja ya mtumishi pamoja na jengo la kutolea huduma za ushauri nasaha ambalo liko katika hatua ya upauaji. Jumla ya shilingi milioni 365 zilitumika kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa mchanganuo ufuatao:-
Ruzuku kutoka Serikali Kuu shilingi milioni 267; mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya shilingi milioni 86; nguvu za wananchi shilingi milioni saba na mchango wa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu shilingi milioni tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 110 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo ambapo kati ya hizo shilingi milioni 40 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi milioni 70 ni ruzuku kutoka Serikali kuu. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 zitatengwa shilingi milioni 110 kwa ajili ya kendeleza ujenzi wa hospitali hiyo ambapo shilingi milioni 50 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi milioni 60 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu. Serikali itaendeleza ujenzi wa hospitali hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha ili wananchi waweze kupata huduma.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Kwa muda mrefu wananchi wa Karagwe wamekuwa wakiahidiwa kujengewa Hospitali ya Wilaya na taratibu zote zimekuwa zikifuatwa kupitia Vikao vya Baraza la Madiwani na RCC lakini maombi haya hutupiliwa mbali na TAMISEMI.
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa hospitali hii ambayo pia ipo kwenye ahadi za Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imetenga eneo la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kupitishwa kwenye vikao vya kisheria ili kutekeleza shughuli ya ujenzi. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 imetengwa shilingi milioni 70 kutoka kwenye fedha za mapato ya ndani na shilingi milioni 60 kutoka kwenye ruzuku ya miradi ya maendeleo (CDG).
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeweka kipaumbele na kutenga shilingi milioni mia moja ili kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo endapo Bunge litaridhia maombi hayo. Chanzo cha fedha hizo ni mapato ya ndani shilingi milioni 50 na shilingi milioni 50 zitatokana na ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-
Serikali iliunda chombo kinachosimamia barabara za Vijijini na Mijini kinachoitwa TARURA:-
Je, chombo hicho kitaanza lini kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwani barabara hizi ni mbaya sana hasa wakati wa masika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, Mbunge wa Mtera, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ilianzishwa kwa Sheria za Wakala za Serikali, Sura 445 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 211 la tarehe 12 Mei, 2017. TARURA imeanza rasmi tarehe Mosi Julai, 2017, kwa ajili ya utekelezaji wa matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 108,946.2 katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA imeidhinishiwa shilingi bilioni 230.8 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 34,024. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 98.5 zimetolewa na kutumika kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 4,188.31, madaraja 35, makaravati makubwa 43 na makaravati madogo 364.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, barabara zilizojengwa katika Jimbo la Mtera zina urefu wa kilometa 93.3 kwa gharama ya Sh.356,737,115.80. Barabara hizo ni:-
Handali – Chanhumba – Igandu - Nghahalezi (kilometa nne); Nghahalezi – Miganda – Idifu - Iringa Mvumi - Mlowa barabarani (kilometa tano); na Nagulomwitikila - Huzi - Ilangali (kilometa 17) kwenda Nhinhi - Wiliko (kilometa 20); Mlowa barabarani - Makangw’a (kilometa 12); Manzase – Sasajila - Ilowelo (kilometa 21.3); Chipogolo - Loje - Igungili (kilometa 14). Wakandarasi wanaendelea kufanyakazi na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo Mei, 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019, TARURA imeomba kutengewa kiasi cha shilingi bilioni 243.3 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 23,465.05, ukarabati wa madaraja 117, mifereji ya mvua yenye urefu wa mita 67,844 na makaravati 1,881 kwa nchi nzima.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mima hadi Mkanana ni mbaya sana na inapitika kwa shida sana wakati wote; na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa haina uwezo kifedha wa kuifanyia mategenezo makubwa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia matengenezo makubwa barabara hiyo ili iweze kupitika wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mima hadi Mkanana ni barabara mlisho ya tabaka la udongo yenye urefu wa kilometa 26.5, inayounganisha barabara ya Kibakwe hadi Wotta yenye urefu wa kilometa 26 na barabara ya Gulwe hadi Seluka yenye urefu wa kilometa 64.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuifanyia matengenezo barabara hiyo ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Vijiji vya Mima na Mkanana. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 40.84 zilitumika kufanyia matengenezo ya sehemu korofi urefu wa kilometa nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2018/2019, TARURA imetenga shilingi milioni 57 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi urefu wa kilometa 6.5 na matengenezo ya kawaida urefu wa kilometa 10 ili iweze kupitika kwa wakati wote.
MHE. AGNESS M. MARWA aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la dawa katika Hospitali ya Manyamanyama iliyoko Wilayani Bunda na hii ni kutokana na hospitali hiyo kutokuwa na hati rasmi ya kuwa Hospitali ya Wilaya:-
(a) Je, ni lini Serikali itaipa Hospitali ya Manyamanyama Hati rasmi ya kuwa Hospitali ya Wilaya ili kuongeza mgao wa dawa na kupunguza shida kubwa wanayoipata wananchi?
(b) Je, ni lini Serikali itaongeza Waganga na Wauguzi katika hospitali hiyo ili kuongeza ufanisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agness Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Manyamanyama hakijakidhi vigezo vya kupewa hati ya kuwa Hospitali ya Wilaya kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na timu ya ukaguzi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto uliofanyika mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu uliobainika ni pamoja na ukosefu wa jengo la utawala; jengo la huduma za mionzi; jengo la kliniki ya macho; jengo la huduma za dharura; jengo la kufulia; ujenzi wa wodi ya upasuaji ya wanaume na wanawake; jengo la ufundi wa vifaa vya hospitali kwa maana (karakana); jengo la kuhifadhia maiti na nyumba za watumishi. Hivyo, kituo hicho kitapata hadhi ya kuwa hospitali endapo miundombinu yote inayohitajika itakamilika ili huduma za msingi zenye hadhi ya hospitali ziweze kutolewa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya watumishi wa afya katika Kituo cha Afya Manyamanyama ni 165, watumishi waliopo ni 78 na upungufu ni watumishi 87. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, kituo kimepokea watumishi watano (5) akiwemo Daktari mmoja. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi wa afya 48 ili kupunguza pengo hilo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi unaoendelea katika Vituo vya Afya Ikuti, Wilayani Rungwe na Ipinda Wilayani Kyela utakamilika ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata huduma kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Ikuti kimekarabatiwa katika awamu ya kwanza ya ukarabati wa vituo vya afya 44 ulioanza tarehe 10 Oktoba, 2017 na kukamilika tarehe 31 Januari, 2018 kwa gharama ya shilingi milioni 500 ili kuongeza huduma za upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito. Aidha, shilingi milioni 220 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba vya upasuaji na samani. Kituo hicho kinaendelea kutoa huduma zote za matibabu isipokuwa huduma za upasuaji wa dharura. Ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya Ikuti umekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni vifaatiba kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo cha afya cha Ipinda ulianza Oktoba, 2017 katika ujenzi huu jumla ya majengo mapya nane yamejengwa pamoja na ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje, uwekaji wa miundombinu ya maji safi na majitaka, kichomea taka na ujenzi wa njia zinazounganisha majengo (walk way). Jumla ya shilingi 625,899,806 zimetumika mpaka sasa katika mchanganuo ufuatao; Serikali Kuu shilingi 500,000,000, Halmashauri pamoja na wadau shilingi 90,100,975.40 na wananchi 35,798,830.60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majengo hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela imepokea vifaatiba kutoka MSD vyenye thamani ya jumla ya shilingi 73,909,900 na vilivyosalia vinatarajiwa kupatikana mnamo mwezi huu wa nne. Vilevile Halmashauri imenunua vitanda 47, magodoro na mashuka vyenye thamani ya shilingi 27,066,500 ambavyo vimefungwa na vinatumika katika majengo hayo. Kituo cha Afya Ipinda kinaendelea na ujenzi wa miundombinu kwa gharama ya shilingi milioni 500 ambao unahusisha kupanua huduma za upasuaji wa dharura na shilingi milioni 220 zimetolewa kwa ajili ya vifaatiba vya upasuaji na samani. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia vikundi vya wanawake waliopo katika Mkoa wa Rukwa katika suala la mikopo na kuwapatia elimu ya ujasiriamali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vya wanawake vinawezeshwa kupitia mfuko wa wanawake unaotokana na asilimia tano ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Sambasamba na hilo Serikali inawahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu ya ujasiliamali kwa vikundi vya wanawake ili kuwajengea uwezo, kuibua miradi yenye tija itakayosaidia kupata kipato na kurejesha mkopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 vikundi vya wanawake 55 vyenye wanachama 698 vimepatiwa mikopo ya shilingi milioni 56.87 kati ya shilingi bilioni 6.5 zilizokusanywa kutokana na mapato ya ndani katika Mkoa wa Rukwa.
Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 vikundi 33 vya wanawake vimepatiwa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 118 kati ya shilingi bilioni 4.2 ya makusanyo ya mapato ya ndani hadi machi, 2017 sawa na asilimia 2.78.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kutoa maelekezo kwa Halmashauri kuimarisha makusanyo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki iliyowekwa katika Halmashauri zote 185 na kuhakikisha kwamba fedha zinapelekwa kwenye mfuko kila zinapokusanywa.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa (ambulance) kwenye Hospitali ya Wilaya ya Handeni hasa ikizingatiwa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wengi kutoka takribani majimbo manne?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda Mbunge wa handeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji Handeni ina gari moja la wagonjwa lenye namba za usajili SM 11322 ambalo linatoa huduma kwa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni. Gari hilo kwa sasa liko katika matengenezo Mjini Tanga baada ya kupata hitilafu. Taratibu za matengenezo zinaendelea kufanyika ili liendelee kutoa huduma kwa wagonjwa. Katika hali ya dharura, Halmashauri inatumia magari ya kawaida kutoa huduma kwa wagonjwa hadi hapo gari la wagonjwa litakapotengemaa.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Vituo vya Afya Kata za Mtwango, Mninga na Makungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya afya awamu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 kipaumbele kimewekwa katika ujenzi wa Kituo cha Afya Malangali kilichoko katika Jimbo la Mufindi Kusini ambao unahusisha ujenzi wa jengo la upasuaji, nyumba ya watumishi, maabara na jengo la wazazi kwa gharama ya shilingi milioni 400 ili kukiwezesha kutoa huduma za dharura za upasuaji.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imetenga jumla ya shilingi milioni 40 kwa ajili ya umaliziaji wa Kituo cha Afya cha Mninga. Fedha hizo zinatarajiwa kufanya umaliziaji wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo itatumika kiasi cha shilingi milioni 30 na shilingi milioni 10 za kuanzia ujenzi wa nyumba ya mganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Vituo vya Afya Mtwango na Mninga umefikia hatua mbalimbali ambapo majengo ya maabara na nyumba ya mtumishi imefika hatua ya umaliziaji na vifaa vyote vya umaliziaji vimekwishafika site. Majengo ya upasuaji na akina mama yamefikia hatua ya kunyanyua kuta na vifaa vyote vya ukamilishaji vipo site, tunategemea kukamilisha kabla ya tarehe 31 Mei, kwa mujibu wa mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Kata ya Makungu hakuna ujenzi unaoendelea isipokuwa kuna kituo cha afya kinachomilikiwa na Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo. Katika kituo hicho Serikali imepeleka Watumishi ambao wanalipwa mishahara na stahili zote kutoka Serikalini na kuchangia dawa pamoja na vifaa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y RHODA E. KUNCHELA) aliuliza:-
Kuna mgogoro kati ya Manispaa na wafanyabiashara wanaomiliki vibanda katika masoko ya Buzogwe Soko Kuu na Mpanda Hoteli ambapo Manispaa inawaongezea kodi wafanyabiashara hao bila makubaliano ya pande zote mbili:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kumaliza mgogoro huo maana ni muda mrefu sasa na wafanyabiashara wamefunga vibanda vyao wakisubiri muafaka na hivyo Serikali kushindwa kukusanya kodi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashari ya Manispaa ya Mpanda imejenga vibanda vya biashara katika masoko kwa ubia baina ya Halmashauri na wafanyabiashara (wamiliki/ wajenzi). Masoko ambayo yaliongezewa ushuru wa pango ni masoko yanayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ambayo ni soko kuu la Buzogwe na Azimio.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda iliamua kufanya mabadiliko ya ushuru baada ya kubaini kuwa wamiliki/wajenzi walikuwa wakinijufaisha wenyewe kwa kuwapangisha wafanyabiashara na kuwatoza kodi kati ya Sh.100,000 hadi Sh.150,000 na kuwasilisha kodi ya Sh.15,000 tu kwa mwezi kwa Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya kodi yaliyofanyika kwa wamiliki/wajenzi ni kutoka Sh.15,000 hadi Sh.40,000 kwa mwezi. Wadau wote walishirikishwa na makubaliano yaliridhiwa katika vikao vya kisheria vya Halmashauri. Aidha, hakuna maduka yaliyofungwa, huduma zinaendelea kama kawaida na Halmashauri imeendelea kukusanya mapato.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zinaweza kufanya marekebisho ya kodi wakati wowote. Utaratibu unaotumika katika kuibua na kuongeza kodi/tozo huanzishwa, huchakatwa na kuamuliwa na kikao cha Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Halmashauri husika.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Zahanati nyingi za Vijiji vya Mkoa wa Kigoma katika wilaya zote zina upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya na baadhi ya zahanati hazina Waganga hivyo huduma zinatolewa na Manesi Wasaidizi tu:-
Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa afya wa kutosha katika maeneo hayo ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma una jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 278, hospitali sita (6), vituo vya afya 32 na zahanati 240. Kati ya vituo hivyo, vituo vya Serikali ni 224 sawa na asilimia 80%, hospitali tatu (3), vituo vya afya 23 na zahanati 198. Idadi hii inajumuisha vituo vya mashirika ya dini, kambi za wakimbizi, binafsi na taasisi za umma kama Magereza, Polisi, Jeshi na TRL.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya kwa mujibu wa ikama mpya ya mwaka 2014 katika vituo vya umma kimkoa ni 5,007, watumishi waliopo ni 1,663 sawa na asilimia 33.2 ya mahitaji na upungufu ni 3,344 sawa na asilimia 66.8. Mkoa pamoja na halmashauri zimeendelea kukabiliana na changamoto hii kwa kushawishi wadau wa sekta ya afya wakiwemo THTS, East African Public Health Lab Net, Engender Health na UNICEF kusaidia kuajiri watumishi muhimu kwa muda/mkataba, pamoja na kuweka katika bajeti kwa ajili ya kuajiri watumishi wapya.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Mkoa wa Kigoma umepatiwa watumishi wa afya 95 wakiwemo Madaktari watano (5), Matabibu 24, Wauguzi 33, Wafamasia 17 na Wataalam wa Maabara 16. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, mkoa umeomba kutengewa nafasi za ajira 1,667 kwa kada mbalimbali za afya.
MHE. SAUL H. AMON aliuliza:-
Barabara ya Pakati – Njugilo – Masukulu – Matwebe hadi mpakani ni barabara kubwa na inapita katika Kata nne ambazo ni Masoko, Bujela, Masukulu na Matwebe, barabara hii ilishapandishwa daraja na kuwa ya TANROADS:-
Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa ili kuondoa adha kwa wananchi kwa kupoteza kipato kwa mazao kuharibika njiani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Pakati – Njugilo – Masukulu hadi Mpakani mwa Wilaya ya Rungwe na Kyela yenye urefu wa kilometa 24.5 ni barabara ya wilaya. Katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa Muhtasari Na.2016/2017/ 01 cha tarehe 6/12/2016, kilipendekeza ipandishwe hadhi na kuwa barabara ya mkoa. Baada ya mapendekezo kupelekwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, barabara hiyo iliidhinishwa na kupandishwa hadhi kwa urefu wa kilometa 4.4 kutoka Njugilo hadi Masukulu katika Wilaya ya Kyela.
Mheshimiwa Spika, matengenezo ya barabara hii yanatarajia kuanza Agosti 2018, kufuatia kuwekwa kwenye Mpango wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Barabara za Vijijini kupitia ufadhili wa watu wa Marekani (USAID), chini ya programu ya Irrigation and Rural Roads Infrastructure Project – IRRIP II ambapo kwa sasa zipo kwenye hatua ya usanifu.
MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:-
Kwa juhudi zake Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale ameanzisha ujenzi wa baadhi ya majengo ya zahanati kubwa na za kisasa katika Vijiji vya Nyamikonze na Inyenze.
(a) Je, Serikali ipo tayari kusaidia kukamilisha ujenzi huo?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuifungua zahanati iliyojengwa na Mbunge katika Kijiji cha Mwamakilinga ambayo imekamilika tangu Novemba, 2014?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia mapato ya ndani ilitenga shilingi milioni 45 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati ya Kijiji cha Nyamikonze, lakini ukamilishaji haukufanyika kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Nyang’hwale kuwa kidogo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia mapato ya ndani imetenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Nyamikonze. Mpaka sasa zahanati haijaanza kufanya kazi na wananchi wa kijiji hicho wanapata huduma za afya katika zahanati ya Mwingiro iliyo karibu na kijiji hicho.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Nyang’hwale katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga shilingi milioni 90 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati katika Kijiji cha Inyenze iliyofikia hatua ya kuezekwa. Fedha hizo bado hazijapatikana kutokana na makusanyo kuwa kidogo. Mara fedha hizo zitakapopatikana utekelezaji utafanyika kama mpango unavyoelekeza. Zahanati ya Mwamakilinga iliyojengwa na Mbunge wa Jimbo hilo, ilifunguliwa na Mheshimiwa Engineer Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 29 Januari, 2018 na mpaka sasa inafanya kazi.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale alianzisha ujenzi wa majengo matatu katika Kituo cha Afya Kharumwa ambayo yote yalikuwa hatua ya lenta. Majengo hayo ni wodi ya watoto, wadi ya wazazi ambayo ndani ina chumba cha upasuaji wa dharura kwa wajawazito na jengo la kuhifadhia maiti (mortuary). Shirika la AMREF linaendelea na ukamilishaji wa jengo la wodi ya wazazi ambayo ndani ina chumba cha upasuaji wa dharura kwa wajawazito. Ujenzi huo unategemea kukamilika ifikapo tarehe 15, Mei, 2018 kwa gharama ya shilingi milioni 164.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua jitihada kubwa zilizofanywa na Mbunge wa Nyang’hwale, mwishoni mwa mwezi Desemba, 2017 Serikali ilitoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya Kituo cha Afya Kharumwa. Halmashauri imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya ukamilishaji wa wodi ya watoto na shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Kharumwa. Ujenzi huo unaaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Mei, 2018. Kiasi cha shilingi milioni 280 kilichobaki kitatumika katika ujenzi wa chumba cha upasuaji (theatre), maabara ya kisasa, nyumba ya mtumishi na wodi ya upasuaji (surgical ward) kwa wanawake na wanaume.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Serikali ilitoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Namanyere Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi hadi Ninde yenye urefu wa kilometa 40 lakini hadi sasa ujenzi wa barabara hiyo bado haujakamilika kwa muda mrefu sasa.
(a) Je, ni lini Serikali itachukua hatua kwa kufuatilia na kuchunguza matumizi ya fedha zilizotolewa na kuchukua hatua ili ujenzi wa barabara hiyo uweze kukamilika?
(b) Je, ni lini wananchi wa Ninde wataondokana na changamoto ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Namanyere - Ninde yenye urefu wa kilomita 60 katika mwaka wa fedha 2014/2015 ilitengewa shilingi milioni 350 za kufanyia matengenezo kama ifuatavyo:-
• Ujenzi wa daraja moja lenye urefu wa mita 20 kwenye Mto Lwafi kwa shilingi milioni 73.69;
• Ujenzi wa daraja moja lenye urefu wa mita 50 kwenye Mto Ninde kwa shilingi milioni 33.922 ;
• Ujenzi wa madaraja mawili yenye urefu wa mita tano kila moja kwenye msitu wa Lwafi kwa shilingi milioni 26.65; na
• Kuifungua sehemu iliyokuwa imebakia ya barabara ya urefu wa kilometa 25 kwa kufanya matengenezo kwa kiwango cha udongo na kujenga makalvati mistari 15 kwa shilingi milioni 154.735 pamoja na gharama za usimamizi jumla ya shilingi milioni 61.003.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kupambana na changamoto ya barabara kwa wananchi wa Ninde kwa kuitengea fedha za matengenezo barabara hiyo. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 shilingi milioni 44.58 zilitengwa kwa ajili ya kufanyia matengenezo ya muda maalum kwa urefu wa kilometa mbili. Aidha, mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 20 zilitengwa na kutumika kuimarisha sehemu korofi zenye urefu wa mita 500.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanyia matengenezo barabara hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha ili iweze kupitika na kuondoa tatizo la usafiri kwa wananchi wa Ninde na maeneo jirani.
MHE. MUNDE A. TAMBWE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Manispaa ya Tabora hupata huduma za afya kupitia kwenye zahanati 22 zilizopo kwenye Wilaya hii. Kwa kuwa zahanati inatoa huduma za magonjwa madogo (minor illness), wananchi wa Manispaa ya Tabora hupata huduma kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete. Hata hivyo, Hospitali ya Mkoa kwa sasa imeelemewa na wagonjwa wengi, hivyo manispaa imeona ni vyema ianzishe ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ulianza mnamo tarehe 19/10/2015 kwa kuanza na jengo la OPD kwa gharama ya shilingi milioni 150 chini ya mkandarasi HERU Construction Company Limited ambapo hadi sasa sehemu ya msingi, nguzo, ngazi na slabu vimekamilika kwa asilimia 100, mkandarasi ameshalipwa jumla ya shilingi milioni 145.7 kwa fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Manispaa ya Tabora imetenga shilingi milioni sabini kwa ajili ya ujenzi wa jengo la OPD katika hospitali hiyo. Vilevile Ofisi ya Rais, TAMISEMI itahakikisha inatoa kipaumbele kwa Manispaa ya Tabora katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mara fedha za awamu ya pili zitakapo patikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inasisitiza kuhakikisha fedha za miradi zinazopatikana zilenge katika ukamilishaji wa miradi iliyopo badala ya kuibua miradi mipya; kwa mfano fedha za Local Government Capital Development Grand (LG- CDG) milioni 483.5 kwa mwaka 2017/2018 ambazo zilitolewa maelekezo kwamba zitumike katika kukamilisha miradi iliyokwishaanzishwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Mbulu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi; upungufu huo wa watumishi umeathiri utoaji wa huduma wa Hospitali hiyo na Vituo vya Afya vya Tawi na Daudi.
• Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi katika Hospitali hiyo?
• Serikali inatekeleza mpango wa upanuzi wa Vituo vya Afya zaidi ya 200 nchini; je, Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na changamoto za watumishi, fedha na vitendea kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ni 345, watumishi waliopo ni 206 na upungufu ni watumishi 139. Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa afya kadri wanavyohitimu na kupangwa moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliajiri watumishi 2,058 wa kada za afya kwenye Mikoa na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya hao, Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilipangiwa watumishi kumi wakiwemo Madaktari wawili, Matatibu wawili; Afisa Muuguzi mmoja; Afisa Afya Mazingira mmoja na Msaidizi wa Afya, Mazingira mmoja; Mteknolojia Msaidizi mmoja na Wauguzi daraja la pili wawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeomba kibali cha kuwaajiri watumishi 91 ili kupunguza upungufu uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inaendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya 208 nchi nzima ili kuboresha huduma ya dharura kwa mama wajawazito. Ujenzi wa vituo hivyo utagharimu shilingi bilioni 132.9 hadi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi huo, vituo hivyo vimetengewa shilingi bilioni 35.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba ili kuviwezesha kutoa huduma kwa wagonjwa. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeomba kibali cha kuwaajiri watumishi wa kada ya afya wapatao 25,000 ili kuhakikisha kunakuwepo na watumishi wenye sifa stahiki kwenye hospitali, vituo vyote vya afya na zahanati.
MHE. HAWA B. MWAIFUNGA (k.n.y. MHE. TUNZA I. MALAPO) aliuliza:-
Je, ni eneo gani limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha Kubangua Korosho katika Manispaa ya Mtwara Mikindani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imetenga maeneo kwa ajili ya viwanda vya kubangua korosho kwa ajii ya wajasiliamali wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2014/2015 mpaka mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ilipanga na kupima viwanja vyenye ukubwa wa ekari 239.13 katika eneo la Mtepwezi na Mtawanya kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho na maghala. Katika viwanja hivi jumla ya ekari 28.41 imegawiwa kwa mfumo wa wakfu wa kuhudumia zao la korosho (CIDTF) na Chama cha Ushirika cha Mtwara na Masasi (MAMCU) kwa ujenzi wa viwanda vya korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ina jumla ya ekari 210.72 ambazo zipo tayari kwa ajili ya waombaji mbalimbali walio tayari kujenga viwanda hasa vya kuchakata korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Halmashauri inaendelea na utengaji wa maeneo kwa ajili ya ujasiliamali wadogo wadogo kwa mwaka 2016/2017. Halmashauri imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 7.8 kwa ajili ya wajasiliamali. Maeneo hayo yapo eneo la Chikongola, Skoya, Ufukoni A, Ufukoni Stendi na eneo la SIDO.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-
Jimbo la Segerea ni moja kati ya Majimbo ya Dar es Salaam ambalo wakazi wake ni wengi na wa kipato cha chini na sababu kubwa ikiwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara hasa madaraja na mitaro, hivyo kusababisha mafuriko ya mara kwa mara.
Je, ni lini Serikali itajenga madaraja ya Tabata Kisiwani na Kisukuru sambamba na kujenga mitaro ili kupunguza adha ya mafuriko katika Kata za Jimbo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuhudumia wananchi wa Jimbo la Segerea katika kuboresha na kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara, madaraja pamoja na mitaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua tatizo la adha ya mafuriko yanayotokana na mvua maeneo ya Tabata, Halmshauri ya Manispaa ya Ilala kupitia mradi wa DMDP imepanga kujenga mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 9.82 na vivuko katika bonde la Msimbazi – Tenge – Lwiti – Sungura na Tembomgwaza kwa gharama ya shilingi bilioni 15 ambazo zabuni za ujenzi huo zinatangazwa mwezi Mei, 2018. Hivyo, baada ya ujenzi wa mifereji hiyo na vivuko, tatizo la mafuriko kwa wananchi wa Tabata Kisiwani na Kisukuru litapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mawenzi - Tabata - Kisiwani kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ilitengewa shilingi milioni 180 za kufanyia matengenezo kwa kiwango cha Changarawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Manispaa ya Ilala imeyenga shilingi milioni 40 za kuifanyia matengenezo ya kawaida na kukarabati daraja lililopo eneo la Mwananchi.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifungua Zahanati za Solowu na Makoja ambazo zimekamilika ili kuwapunguzia adha ya kufuata huduma ya afya vijiji vya mbali akina mama, watoto, wazee na wananchi wa vijiji hivyo kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zahanati za Solowu na Makoja zimejengwa na Halmashauri kwa kushirikisha nguvu za wananchi. Ujenzi wa Zahanati ya Solowu imegharimu shilingi milioni 79.605 ambapo wananchi wamechangia shilingi milioni 10.6 na Halmashauri imechangia shilingi milioni 69; na ujenzi wa Zahanati ya Makoja imegharimu shilingi milioni ambapo wananchi wamechangia shilingi 640,000.00 na Halmashauri imechangia milioni 136.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Zahanati za Solowu na Makoja zimetengewa fedha MSD kiasi cha shilingi 640,800.00 kila moja kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa katika robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha, na tayari Halmashauri imepeleka order kwa ajili kupatiwa dawa kwa matumizi ya zahanati hizo. Dawa na vifaa hivi vitachukuliwa kutoka Bohari ya Dawa ya Serikali Dodoma mara taratibu zitakapokuwa zimekamilika. Aidha, baadhi ya vifaa na vifaa tiba mbalimbali kwa ajili ya zahanati hizi vilishanunuliwa na vimehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Chamwino na vitapelekwa kwenye zahanati hizo kabla ya mwisho wa mwezi huu Aprili, 2018. Vifaa na vifaatiba hivyo ni pamoja na vitanda vya kuzalishia, vifaa vya kutakasia, magodoro, seti za kuzalishia, vitanda vya hospitali, mizani ya kupimia uzito kwa watoto na watu wazima, vifaa tiba, vitanda vya kupimia wagonjwa, mashine za kupimia shinikizo la damu, samani kwa maana ya meza, viti na makabati pamoja na ma-shelves ya kuhifadhia dawa. Wakati huo hu halmashauri imepanga watumishi wawili wa kada ya uuguzi kwa kila zahanati ambao wataanza kutoa huduma ndani ya mwezi ujao wa mwezi Mei, 2018.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Hospitali ya Amana imepelekwa Wizarani, hivyo Wilaya ya Ilala kwa sasa haina Hospitali ya Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia Hospitali ya Kivule itumike kama Hospitali ya Wilaya ya Ilala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeandaa mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa inapata Hospitali ya Wilaya ikiwa ni pamoja na kutenga fedha jumla ya shilingi bilioni tatu katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Kivule. Kati ya hizo shilingi 2,000,000,000 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi 1,000,000,000 ni ruzuku ya Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa Hospitali ya Kivule, Serikali inaendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya vya Mzinga, Kinyerezi na upanuzi wa Kituo cha Afya Buguruni. Lengo la kuimarisha vituo hivyo ni kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya na kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika ngazi za msingi.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Ufunguzi wa Kituo cha Afya Mbwera ulifanyika tarehe 27/8/1994 na aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, wakati huo Dkt. John Samwel Malecela lakini hadi sasa kituo hicho hakina hadhi hiyo ya kuitwa Kituo cha Afya.
(a) Je, Mheshimiwa Waziri mwenyewe haoni haja ya kwenda Mbwera kuona hali halisi ya kituo hicho baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu wake kuona kama kimekamilika?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha kwani wanaotakiwa ni 39 na sasa waliopo ni wanne tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Kituo cha Afya Mbwera kilifunguliwa muda mrefu na kinakabiliwa na uchakavu wa miundombinu na uhaba mkubwa wa watumishi ikiwemo madaktari, tabibu na wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imepeleka jumla ya shilingi 560,000,000, kati ya fedha hizo shilingi 400,000,000 zimetolewa na Serikali kupitia wadau wa maendeleo wa Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Funds) na shilingi 160,000,000, zimetolewa na Serikali ya Watu wa Korea kwa lengo la kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kujenga chumba cha upasuaji, nyumba ya mtumishi, wodi ya wazazi (maternity ward), jengo la maabara, kurekebisha mfumo wa maji safi na maji taka, chumba cha kuhifadhia maiti (mortuary) na kichomea taka (incinerator).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa jengo la wodi ya wazazi na jengo la upasuaji yapo katika hatua ya msingi na ujenzi unaendelea kwa kutumia mfumo wa force account. Vilevile shilingi milioni 300 zimepelekwa bohari ya madawa (MSD) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Kituo cha Afya Mbwera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la watumishi wa afya Serikali inalitambua na mnamo mwezi Novemba, 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti ilipewa watumishi wapya 11 wa kada mbalimbali za afya. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imepanga kuajiri watumishi wapya wa kada mbalimbali za afya 199.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wilaya ya Itilima na Busega ni Wilaya mpya na hazina Hospitali za Wilaya.
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali za Wilaya kwenye Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri za Wilaya ya Itilima na Busega zilianzishwa mwaka 2015 na zina idadi ya watu 346,170 kwa Itilima na 224,527 kwa Busega. Ni kweli kwamba Halmashauri hizi bado hazina Hospitali za Wilaya na wananchi wanapata huduma kupitia zahanati 45 na vituo vya afya saba ambapo kati ya hivyo zahanati 27 na vituo vya afya vitatu vipo Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na zahanati 18 na vituo vya afya vinne vipo Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mpango wa maboresho na uimarishaji wa huduma za afya kwa kushirikiana na wadau (Canada na UNFPA), Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 1.215 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya afya. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 525 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Ikilindo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na shilingi milioni 450 ni kwa ajili ya Kituo cha Afya Nasa katika Halmashauri ya Wilaya Busega. Shilingi milioni 240 ni kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya zahanati nane ambapo kila zahanati imepatiwa shilingi milioni 30; zahanati hizo ni Gaswa, Mahembe, Migato na Nangale zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na Badugu, Nayamikoma, Ngasamo na Kikoleni zilizopo Halmashauri ya Wilaya za Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri za Wilaya ya Itilima na Busega zimetengewa shilingi bilioni 1.5 kila moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali za Wilaya.
MHE. RISALA S. KABONGO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Vwawa ambayo inatoa huduma kwa Halmashauri nne za Mbozi, Ileje, Songwe na Momba inakabiliwa na upungufu wa vifaatiba, wodi, watumishi pamoja na Madaktari Bingwa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupandisha hadhi Hospitali ya Vwawa kuwa Hospitali ya Mkoa ili iweze kutengewa bajeti ya kutosha kukabiliana na changamoto zilizopo sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Risala Said Kabongo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilituma timu ya wataalam kutoka Idara mbalimbali na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo ilifanya ukaguzi wa siku kumi kuanzia tarehe 25 Agosti, 2017 hadi 5 Septemba, 2017 katika Hospitali ya Vwawa iliyopo Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe ili kufanya tathmini kuona kama hospitali hiyo inaweza kutumika kama Hospitali ya Mkoa na hatimaye kuwasilisha matokeo ya tathmini hiyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aliridhia Hospitali ya Wilaya ya Mbozi yaani Vwawa itumike kwa muda kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe wakati Mkoa unaendelea na taratibu za kujenga Hospitali ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma katika hospitali hii, Serikali ilipeleka watumishi tisa akiwemo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina mama pamoja na kufunguliwa akaunti Bohari ya Dawa (MSD) yenye namba MB 310004 yenye kutoa mgao wa dawa ngazi ya mkoa ili kuweza kutoa huduma kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi milioni 767 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe ambapo eneo lenye ukubwa wa hekari 23 lililopo Hasamba katika Mji Mdogo wa Vwawa limeshatengwa na taratibu za kuanza ujenzi wa Hospitali hiyo kwa awamu ya kwanza zimeshaanza ikiwemo uandaaji wa michoro ya usanifu inayofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania. Inatarajiwa Wakala wa Majengo ndiye atasimamia ujenzi wa hospitali hiyo. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-
Jimbo la Segerea ni kati ya majimbo yaliyosahaulika katika miundombinu ya barabara na kupelekea mitaa mingi kuwa na madimbwi sugu na mafuriko kila mvua inaponyesha. Kadhia hii imepelekea barabara za mitaa kupitika kwa taabu na kupelekea foleni kubwa katika barabara ya Segerea mpaka barabara ya Mandela kwa kuwa ndiyo barabara pekee inayotumiwa na wananchi.
Je, ni lini jimbo hili litatengewa bajeti kwa barabara zake za mitaa kwa kiwango cha lami, changarawe na ujenzi wa mifereji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya barabara inayoendelea kutekelezwa kwa kiwango cha lami sambamba na mifereji katika Jimbo la Segerea ina thamani ya shilingi bilioni 4.6 ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imetoa shilingi bilioni 2.6 na shilingi bilioni 2.0 zimetolewa na Mfuko wa Barabara. Miradi ya barabara inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na barabara za Mnyamani kilometa 2.3 kwa shilingi bilioni 2.5; Tabata Barakuda – Chang’ombe kilometa 0.5 kwa shilingi milioni 744 na Tabata – Kimanga – Mazda kilometa 0.8 kwa shilingi bilioni 1.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Jimbo la Segerea limetengewa shilingi milioni 880 ambapo kati ya fedha hizo shilingi milioni 380 zitatengeneza kwa kiwango cha changarawe barabara za Bonyokwa – Kisukuru- Majichumvi; Tabata – Mawenzi – Kisiwani; Chang’ombe – Majichumvi; Chang’ombe - Mbuyuni, Guest Nyekundu – Jumba la Dhahabu na shilingi milioni 500 zitatumika kufanya usanifu na ujenzi wa madaraja ya Mongolandege na Nyebulu.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-
Mheshimiwa Rais katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 aliahidi kujenga kilometa 10 za barabara ya lami katika Manispaa ya Moshi.
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kusaidia Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kujenga mitaro katika barabara zake za lami ili kuzifanya zidumu muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napensa kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli, barabara zenye urefu wa kilometa 16.57 zimejengwa katika Manispaa ya Moshi kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Machi, 2018 ambapo kati ya hizo kilometa 6.06 zimejengwa kupitia fedha za Mfuko wa Barabara kwa gharama ya shilingi 2,076,497,094 na kilometa 10.51 zimejengwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Kuimarisha Miji 18 (ULGSP) kwa gharama ya shilingi 8,384,872,640.87. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri inaendelea na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 2.79 kwa kiwango cha lami kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara unaotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi 1,178,201,860.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mradi wa Kuimarisha Miji 18 (ULGSP) katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2018 Serikali imejenga mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 11.57 kwa gharama ya shilingi 1,833,520,330. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kujenga mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 9.47 na mradi huu utagharimu jumla ya shilingi 1,612,952,130 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara, ujenzi huu upo katika hatua za awali.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Jimbo la Masasi lina shule moja tu ya sekondari kwa kiwango cha Kidato cha Tano na Sita ambayo ni Sekondari ya Wasichana Masasi nayo imekuwa haitoshelezi kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaofaulu:-
(a) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi Shule za Sekondari za Mwenge Mtapika na Anna Abdallah ili ziweze kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita?
(b) Je, ni lini Serikali itaajiri Walimu katika Jimbo la Masasi ikiwa ikama ya Walimu wa Sayansi katika Shule za Sekondari tisa zilizopo ni Walimu 84 lakini waliopo ni 24 tu?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Masasi inazo shule tisa za sekondari. Kati ya hizo, ni shule moja tu ya Masasi wasichana ndiyo ya Kidato cha Tano na Sita. Katika jitihada za kutatua changamoto hiyo, Halmashauri ya Mji wa Masasi imeteua shule mbili za sekondari za Anna Abdallah na Mwenge Mtapika kwa ajili ya upanuzi na kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo bwalo la chakula, mabweni na jiko ili kuwezesha shule hiyo kuanza kuchukua wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri imewasilisha andiko la mradi wa kukamilisha miundombinu hiyo kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili ya maombi ya fedha za kukamilisha miundominu ya shule hizo. Mara baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, taratibu nyingine za kuziwezesha shule hizo kuanza kuchukua wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita zitakamilishwa.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto ya Walimu wa Sayansi, Serikali imepeleka Walimu tisa wa masomo ya sayansi katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mwaka 2017 ili kupunguza uhaba wa Walimu wa Sayansi. Serikali iko kwenye mchakato wa kuajiri Walimu 5,870 wa Shule za Sekondari na watapangwa kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Masasi.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Mwaka 2015 Serikali ilianzisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo, lakini tangu wakati huo hadi leo hii, Mamlaka hiyo haijapatiwa fedha za kujiendesha na kutoa huduma kwa wananchi:-
(a) Je, ni lini Mamlaka hiyo itatengewa bajeti ili iweze kujiendesha na kufanya kazi zake kwa ufanisi?
(b) Je, ni lini Mamlaka hiyo itapatiwa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mji huo na kujenga barabara za lami kilometa nne zilizokuwa zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni za Uchaguzi za mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mji Mdogo huanzishwa kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa, Sura ya 287, kifungu 13 - 21. Pamoja na vyanzo vya mapato vya Mamlaka ya Mji Mdogo kuainishwa katika Sheria ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kifungu cha (8), Mamlaka hizo siyo Mamlaka kamili na hufanya kazi chini ya usimamizi wa Halmashauri za Wilaya husika. Hivyo, Mamlaka ya Mji Mdogo Igunga imekuwa ikiandaa mipango na bajeti zake kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na imekuwa ikipata mgao wa fedha kama zipatavyo Halmashauri nyingine nchini kutokana na upatikanaji wa fedha.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliahidi kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 4 na katika mwaka wa fedha 2016/2017 barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 0.67 ilikarabatiwa kwa gharama ya Sh.287,068,098. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali itajenga barabara yenye urefu wa kilometa 1.164 kwa kiwango cha lami katika Mji Mdogo wa Igunga, Sh.406,664,816 zimeshapelekwa na mkandarasi amefikia 5% ya utekelezaji wa mradi. Serikali itaendelea kujenga barabara za lami Wilayani Igunga kupitia TARURA kwa kadri fedha zinavyopatikana.
MHE. NURU A. BAFADHILI (K.n.y. MHE. REHEMA J. MIGILLA) aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haitaki kujenga Hospitali ya Wilaya ya Tabora Mjini baada ya Hospitali ya Wilaya kupewa hadhi ya Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mhemishimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali Na. 96 la tarehe 18/4/2018 lilioulizwa na Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, Serikali imeanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Tabora Mjini tangu tarehe 19 Oktoba, 2015 kwa kuanza na jengo la OPD kwa gharama ya shilingi milioni 150 chini ya Mkandarasi HERU Construction Company Limited ambapo hadi sasa sehemu ya msingi, nguzo, ngazi na slabu vimekamilika kwa asilimia 100. Mkandarasi ameshalipwa jumla ya shilingi milioni 145.7 kutokana na fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Manispaa ya Tabora imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa jengo la OPD katika hospitali hiyo. Mkakati wa Serikali ni kuimarisha Vituo vya Afya 513 nchi nzima ili viweze kutoa huduma za dharura pamoja na kujenga Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kuweka kipaumbele kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa, ndiyo maana Serikali imepeleka jumla ya shilingi bilioni 2.6 Mkoa wa Tabora, kwa ajili ya ukarabati wa vituo sita vya Afya katika Wilaya za Nzega, Tabora-Uyui, Igunga, Kaliua na Urambo kupitia awamu ya kwanza na ya pili ya miradi ya afya iliyoanza kutekelezwa Septemba, 2017. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga shilingi bilioni 101 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 nchi nzima ambapo mbili kati ya hizo zipo katika Wilaya ya Uyui na Sikonge, Mkoani Tabora.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:-
Akina mama na vijana wa Jimbo la Buhigwe wanajituma sana katika kilimo na uwekezaji.
(a) Je, ni lini Serikali itawasaidia kimtaji ili waweze kujikomboa?
(b) Je, ni kiasi gani kimetolewa kuwawezesha akina mama na vijana katika miaka ya 2010 hadi 2017?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza viongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa kuwahamasisha vijana wa Mkoa wa Kigoma kuanzisha vikundi vingi vya wajasiriamali ambavyo ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya wanawake, vijana na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwasaidia wanawake na vijana kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Vijana. Mikopo hii imelenga kuwasaidia kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi hivyo kujiongezea kipato na kukuza uchumi.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe imeanza kufanya kazi Januari, 2013 hivyo taarifa zilizopo ni kuanzia mwaka huo. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ilitoa jumla ya shilingi 25,377,057 kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya wanawake na vijana. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia Mei, 2018 jumla ya shilingi 10,500,000 zimetolewa katika vikundi vya wanawake na vijana. Aidha, kupitia Mfuko wa Jimbo Mheshimiwa Mbunge alitoa shilingi 10,500,000 kwa vikundi saba vya bodaboda na kikundi kimoja cha mafundi seremala.
Mheshimiwa Spika, jumla ya shilingi 20,200,000 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:-
(a) Je, ni lini walimu wataboreshewa maslahi yao pamoja na nyumba za kuishi?
(b) Kwa juhudi za Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale ameweza kujenga madarasa mawili katika Kata ya Izunya kwa lengo la kuanzishwa shule ya sekondari tangu mwaka 2014. Je, ni kwa nini shule hiyo haijafunguliwa hadi sasa ili kuwapa moyo wafadhili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuhakikisha walimu wa nchi hii wanaboreshewa maslahi yao ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu. Katika kuboresha maslahi ya walimu, Serikali kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 2015 ilianzisha Tume ya Utumishi ya Walimu ili iweze kusimamia na kushughulikia masuala yote yahusuyo maslahi ya walimu badala ya maslahi hayo kusimamiwa na chombo zaidi ya kimoja kama ilivyokuwa awali.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Juni, 2015 hadi Desemba 2017, Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni
33.135 kwa ajili ya kulipa madeni ya walimu ambapo walimu 86,234 wamelipwa nchi nzima. Aidha, katika kuhakikisha maslahi ya walimu yanayoboreshwa na kero zao zinaondolewa, jumla ya walimu 52 wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale walilipwa jumla ya shilingi 99,685,990 za madai mbalimbali na wengine 202 walipandishwa vyeo (madaraja) katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016.
b) Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale, wananchi na uongozi wa Halmashauri ya Nyang’hwale kwa juhudi zao za kutaka kuiwezesha jamii kielimu wakiwemo wa Kata ya Izunya. Ili shule ya sekondari iweze kupewa kibali cha kufunguliwa wakati wa kuanzishwa inapaswa kwa kuanzia iwe na madarasa, kuwe na jengo la utawala, nyumba za walimu, vyoo vya walimu na wanafunzi, maktaba, viwanja vya michezo, samani pamoja na maabara kwa kuzingatia mwongozo uliowekwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa shule tarajiwa ya Izunya ina vyumba vya madarasa manne, vyoo matundu sita ya wasichana na wavulana matundu matano, jengo la utawala lenye vyoo vya walimu liko hatua za mwisho za umaliziaji na maabara zipo kwenye hatua ya jamvi. Hata hivyo, kwa kutambua jitihada za wadau mbalimbali wa elimu akiwepo Mheshimiwa Mbunge, Halmashauri imeazimia kutumia shilingi milioni 50 kutoka fedha za EP4R zilizopelekwa mwezi Februari, 2018 kwa ajili ya kukamilisha maabara zote. Ni matarajio yangu kwamba mara baada ya ujenzi wa maabara kukamilika taratibu za usajili wa shule hiyo zitakamilika. Aidha, naomba niitumie nafasi hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge, wadau wetu wa maendeleo na wananchi kwa ujumla kuunganisha nguvu zetu pamoja ili kukamilisha miundombinu inayohitajika katika shule kuweza kufunguliwa ikiwemo ya Kata ya Izunya.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-
Madarasa na Ofisi za Walimu katika shule mbalimbali katika Mkoa wa Kagera ni mabovu.
Je, Serikali inawasaidiaje wanafunzi wa Kagera kupata mahali pazuri pa kusomea kadhalika na walimu wao wapate ofisi nzuri ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera kuna mahitaji ya vyumba vya madarasa 14,275 kwa shule za msingi, vilivyopo ni 5,934 hivyo upungufu ni 8,341 sawa na asilimia 58. Aidha, mahitaji ya ofisi za walimu ni 1,780, zilizopo ni 925 na upungufu ni 855 sawa na asilimia 48. Kwa upande wa shule za sekondari kuna mahitaji ya vyumba vya madarasa 2,379, vilivyopo ni 1,582 upungufu ni 797 sawa na asilimia 34. Majengo ya Utawala mahitaji ni 212, yaliyopo ni 67 upungufu ni 145 sawa na asilimia 67.
Mheshimiwa Spika, upungufu pia umejitokeza katika miundombinu mingine mfano nyumba za walimu, vyoo na maabara. Hali hii ya upungufu wa miundombinu inatokana na mwamko mkubwa wa wazazi wa kuwaandikisha watoto shule kufuatia Mpango wa Serikali wa Elimu ya Msingi Bila Malipo ambapo idadi ya wanafunzi imeongezeka katika shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Spika, Serikali itachukua hatua na mikakati mbalimbali za kuhakikisha kuwa wanafunzi na walimu katika Mkoa wa Kagera wanapata mahali pazuri pa kusomea na kufundishia ili kuinua taaluma katika Mkoa wa Kagera. Serikali inaendelea kutoa fedha za ujenzi na ukarabati kupitia mpango wa EP4R ambapo jumla ya shilingi 1,243,600,000 zimetolewa katika Mkoa wa Kagera katika kipindi cha mwaka 2017/2018 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa, mabweni, maabara, matundu ya vyoo katika shule za Kagemu na Rugambwa zilizoko kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Nyailigamba na Profesa Joyce Lazaro Ndalichako katika Halmashauri ya Muleba, Murusagamba katika Halmashauri ya Ngara na Omurwelwe iliyoko Halmashauri ya Karagwe.
MHE. DAIMU I. MPAKATE (K.n.y HASSAN S. KAUNJE) aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mkwaya na mwekezaji Durbali:-
Je, ni lini mgogoro huo utapatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mgogoro unaowahusisha baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Lindi ambao wako kwenye Mitaa ya sokoni, Makonde na Mtere ambayo zamani ilikuwa ni sehemu ya Kijiji cha Mkwaya ambao wanasemekana kuvamia na kugawana mashamba yanayomilikuwa na Kampuni ya Indo-African Estate Limited.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu si kati ya wananchi hao na bwana Amin Durbali ambaye ni mmoja kati ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Indo-African Estate Limited bali ni kati ya wananchi na Kampuni ya Indo-Africa Estate Limited ambayo ndiyo ina hatimiliki za mashamba hayo yenye ukubwa wa ekari 3,601.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Indo-African Estate Limited ilifungua Kesi Na.17 ya mwaka 2015, ambayo hukumu yake imetolewa Februari, 2018 na kuipa Serikali ushindi. Kinachoendelea sasa ni taratibu za kufuta miliki za mashamba hayo kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999 na Kanuni zake za mwaka 2001. Baada ya kufutwa kwa miliki za mashamba hayo, Serikali itaweka utaratibu mzuri wa ugawanaji wa mashamba hayo kwa wananchi.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI aliuliza:-
Shule ya Msingi Kipela, Wilayani ya Iringa, inahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum (albinism) lakini haina miundombinu rafiki, watumishi wa kutosha, huduma za afya stahiki na umeme:-
Je, lini Serikali itarekebisha mapungufu hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Nuru Mwamwindi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kipela ina jumla ya wanafunzi 701 wakiwemo wanafunzi 93 wenye mahitaji maalum ambao wote wanakaa bweni. Shule hii ina hitaji la walimu wataalam wa elimu maalum 17 ambapo kwa sasa wapo walimu 7 na hitaji la watumishi wasio walimu 13, kwa sasa wapo 7. Vilevile shule hii ina mahitaji ya vyumba vya madarasa 16 kwa sasa vipo 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kipela ipo umbali wa kilometa 8 toka Makao Makuu ya Kata ya Mzihi ambapo ndiko kuliko na umeme wa gridi ya Taifa kwa sababu hiyo, kwa sasa shule hii inatumia umeme wa jua (solar). Aidha, shule inapata huduma za afya kwenye Zahanati ya Kanisa Katoliki iliyopo jirani na shule. Huduma hii, huchangiwa kwa malipo kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na miundombinu ya shule hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepeleka jumla ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni rafiki na la kisasa kwa ajili ya wanafunzi hao. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu itaendelea kuboresha miundombinu hiyo pamoja na shule zingine za aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ajira, Serikali ipo kwenye mchakato wa kuajiri walimu wa shule za msingi 4,785 wakiwemo walimu wa mahitaji maalum. Shule ya Msingi Kipela ni miongoni mwa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum zitakazopangiwa baadhi ya walimu hao.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Hospitali ya Mtakatifu Gaspar imekuwa Hospitali ya Rufaa tangu mwaka 2011 na inahudumia wananchi wa Mikoa ya Tabora, Singida na Mbeya. Wakati wa kampeni mwaka 2015, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kuipatia vifaa tiba, dawa na watumishi wa kutosha ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo wagonjwa:-
Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa ili kusaidia hospitali hiyo kutoa huduma za afya kwa ufanisi na kuokoa maisha ya wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika utoaji wa huduma za afya, Serikali inatoa ruzuku ya fedha kwa ajili ya kulipia mishahara ya watumishi pamoja na ruzuku ya dawa na vifaa tiba. Jumla ya watumishi 50 wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar wanalipwa mishahara na Serikali ambapo ni Daktari Bingwa mmoja (Bingwa wa Upasuaji), Daktari mmoja, Daktari Wasaidizi (AMO) wawili, Tabibu wawili, Wauguzi 43 na Mteknolojia wa Maabara mmoja.
Mheshimiwa Spika, mgao wa dawa na vifaa tiba kutoka Bohari ya Dawa (MSD) unaendelea kutolewa na Serikali katika Hospitali ya Mtakatifu Gaspar ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilitoa dawa zenye thamani ya shilingi milioni 105.67 na mwaka wa fedha wa 2017/2018 dawa zenye thamani ya shilingi milioni 114.67 zimetolewa katika hospitali hiyo. Aidha, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaandaa mwongozo wa gharama za matibabu katika hospitali ambazo siyo za Serikali ili kuzifanya hospitali hizo kutoa huduma zenye gharama nafuu.
MHE. OMARY A. BADWEL (K.n.y. MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE) aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya kutoka Mpunguzi kupitia Nagula, Mpwajungu, Ituzi hadi Ilangali itapandishwa hadhi kuwa ya Mkoa ambayo itasimamiwa na Mkoa kwa maana ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, Mbunge wa Jimbo la Mtera, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mpunguzi – Ilangali yenye urefu wa kilometa 88.3 ni barabara mjazo yenye tabaka la changarawe na udongo, ambayo inaunganisha Wilaya ya Dodoma, Bahi, Chamwino na kwa upande mwingine inaunganisha Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Iringa Vijijini. Upande wa Dodoma Jiji ina kilometa tatu, Bahi kilometa 18.3 na Chamwino kilometa 67.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ilitengeneza sehemu ya Mpunguzi hadi Nagulo kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilometa 21.3 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.032 katika mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ufadhili wa DFID. Aidha, barabara ya Mpunguzi – Ilangali katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia TARURA iliifanyia matengenezo ya sehemu korofi kwa urefu wa kilometa 17 yaliyogharimu shilingi milioni 86.2 na katika mwaka wa fedha 2018/2019, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imetenga shilingi milioni 170 za kuifanyia matengenezo ya muda maalumu kwa urefu wa kilometa 8.5 na kazi hii ipo katika hatua za manunuzi.
Mheshimiwa Spika, maombi ya kupandishwa hadhi barabara ya Mpunguzi – Ilangali kwa sasa yapo ngazi ya Mkoa. Pindi yatakapowasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na kuonekana kwamba yanakidhi vigezo vilivyowekwa na sheria, barabara hii itapandishwa hadhi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA - (K.n.y. MHE. JEROME D. BWANAUSI) aliuliza:-
Madaraja ya Mwitika – Maparawe, Mipande – Mtengula na Mbangara – Mbuyuni yalisombwa na maji wakati wa mafuriko miaka mitano iliyopita na kusababisha matatizo makubwa ya usafiri:-
Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo ili kuondoa adha ya usafiri inayowakabili wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismasi Bwanausi Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba madaraja ya Mwitika, Maparawe, Mputeni, Mtengula na Mbangala, Mbuyuni yalisombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2015/2016. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii Serikali ilifanya tathmini juu ya gharama za ujenzi wa madaraja hayo, ilibainika kuwa kiasi cha shilingi bilioni 3.5 zinahitajika kukamilisha ujenzi wa madaraja hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kiasi hicho cha fedha ni kikubwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeweka kwenye maombi maalumu, hivyo ujenzi wake utategemea kuanza pindi fedha hiyo iliyoombwa itakapopatikana. Madaraja hayo yatahudumiwa na Wakala wa Huduma za Barabara Vijijini yaani TARURA.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Nzasa – Kilungule – Buza – Temeke:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hiyo muhimu kwa wakazi wa Mbagala, Mwanagati na Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nzasa – Kilungule – Buza – Temeke ina urefu wa kilomita 7.6. Barabara hii imeongezwa kwenye mpango wa maboresho ya Jiji ya Dar es Salam kupitia mradi wa DMDP na katika awamu inayofuata itajengwa kwa kiwango cha lami. Serikali imekwishalipa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 3.25 kwa wananchi 310 ambao wanatakiwa kupisha mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya usanifu imeshakamilika na kazi zinazotekelezwa ni ujenzi wa barabara ya lami kilomita 7.6, ujenzi, wa madaraja mawili yenye urefu wa mita 60 na makalvati makubwa matano kwenye bonde la Mto Mzinga, uwekaji wa taa barabarani jumla ya taa 324 ambazo zinatumia mwanga wa jua; pia kujenga vituo tisa vya mabasi ya daladala. Gharama ya kutengeneza shughuli hii inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 22.6.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Kutokana na sera ya Serikali kujenga vituo vya afya kila kata.
Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivyo katika Kata za Maretadu, Maghangw, Endamilay, Dinamu, Geterer, Masieda na kupandisha hadhi Zahanati ya Hayderer kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imejenga vituo vya afya 210 nchi nzima kwa gharama ya shilingi bilioni 93.5 vikiwemo vituo vya afya saba vilivyoko Mkoa wa Manyara kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilipewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Dongobeshi na Halmashauri ya Miji Mbulu ilipewa shilingi bilioni moja kwa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Tlawi na Daudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutimiza azma ya kuwa na kituo cha afya kila kata hapa nchini Serikali imeweka vigezo maalum juu ya ujenzi wa vituo vya afya, lengo mahsusi ni kusogeza huduma za afya ili zipatikane ndani ya umbali wa kilometa tano kama ilivyoelekeza kwenye Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupandishwa hadhi kwa Zahanati ya Hayderer kuwa kituo cha afya miundombinu iliyopo katika zahanati hiyo haikidhi vigezo vya kuhuishwa kutoa huduma kama kituo cha afya. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeendelea kufanya uhamasishaji kwa wananchi kujitolea kujenga vituo vya afya katika kata zilizotajwa za Maretadu, Maghangw, Endamilay, Dinamu, Geterer na Masieda. Hadi sasa wananchi wa Maretadu wametenga eneo lenye ukubwa wa ekari 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi kulingana na upatikanaji wa fedha na rasilimali nyingine kama watumishi na vifaa tiba.
MHE. ORAN M. NJEZA (K.n.y. MHE. HAROON M. PIRMOHAMED) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafanyia ukarabati barabara za Mahongole – Kilambo kilometa 20, Igurusi – Utengule kilometa 22, Chimala – Kapunga kilometa 25 na Mlangali – Ukwavila kilometa 23?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haroon Mulla Pirmohamed, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 685 zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), kilometa 341 ni za kiwango cha changarawe na kilometa 344.5 ni za udongo.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 1.065 sawa na asilimia 91 ya bajeti iliyopangwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ukarabati wa Madaraja ya Mporo III, Mporo IV na Manienga. Matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha changarawe, ukarabati wa sehemu korofi zenye jumla ya kilometa 30 na matengenezo ya kawaida kwenye barabara zenye urefu wa kilometa 67.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali imetengewa kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili ya matengenezo maalum katika barabara ya Mlangali – Uturo- Ukwavila na Chimala-Kapunga kwa eneo korofi lenye jumla ya kilometa 11. Vilevile Halmashauri imetengewa shilingi milioni 12.18 kwa ajili ya matengenezo ya makalavati 21 katika barabara ya Igalako- Mwatenga - Kilambo.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-
Nkwenda I ni kata ya kibiashara yenye wakazi wengi, na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa kampeni katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 aliahidi kujenga barabara kwa kiwango cha lami.
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka kujenga kilometa kadhaa za lami ili kupunguza adha wanazopata wafanyabiashara hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliahidi kujenga barabara yenye urefu wa kilometa tano katika Wilaya ya Kyerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada za kutekeleza ahadi hii zimekwishaanza na katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imetenga shilingi milioni mia tatu hamsini kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa moja kwa kiwango cha lami Makao Makuu ya Wilaya ya Kyerwa (Rubwera). Ujenzi huu unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2018. Serikali itaendelea kujenga barabara za lami Wilaya ya Kyerwa kwa awamu ili kutimiza ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-
Halmashauri ya Mji wa Tarime imebahatika kuwa na Uwanja wa Ndege wa Magena ambao umekuwa ukitumiwa na watalii wanaokwenda Mbuga ya Serengeti, viongozi mbalimbali na hata Mgodi wa Acacia. Miundombinu ya uwanja pamoja na barabara zake ni mbovu sana.
(a) Je, ni lini Serikali itapanua uwanja huu na kurekebisha miundombinu yake ili ndege nyingi ziweze kutua kwa ajili ya watalii waendao Serengeti?
(b) Je, ni kwa nini Serikali haijajenga jengo la Uhamiaji katika uwanja huo ili kutoa urahisi wa watalii wanaotumia uwanja huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege Magena kinachomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Tarime kina urefu wa mita 1,470 na upana wa mita 120. Kiwanja hicho kimekodishwa kwa mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Coastal Aviation kwa mkataba wa kuilipa Halmashauri kiasi cha milioni 20 kila mwaka. Halmashauri imefanya ukarabati wa baadhi ya miundombinu ya kiwanja ikiwemo kujenga barabara yenye urefu wa kilometa 1.2 kutoka barabara ya Tarime – Sirari kwa kiwango cha changarawe ili kuboresha mazingira ya uwanja huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia halmashauri ya Mji wa Tarime ina mpango wa kujenga Ofisi za Uhamiaji ili kuweka utaratibu mzuri wa kuingia na kutoka kwa watalii wanaokwenda hifadhi ya taifa ya Serengeti.
MHE. DEO K. SANGA (K.n.y. MHE. BONIPHACE M. GETERE) aliuliza:-
Serikali imekuwa na mpango wa kufanya maboresho ya Vituo vya Afya nchini na Kituo cha Afya cha Ikizu ambacho kinahudumia kata zaidi ya 13, majengo yake licha ya kuwa hayatoshelezi hasa wodi ya akina mama wajawazito na watoto, lakini pia yamechakaa sana.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu maboresho ya kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Ikizu ni kati ya vituo viwili vinavyotoa huduma za upasuaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kituo kingine ni Kasahunga. Katika kukiboresha Kituo cha Afya Ikizu ili kuweza kutoa huduma bora Serikali imeendelea kufanya maboresho ya miundombinu kwa awamu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilifanya ukarabati wa wodi ya wazazi kwa gharama ya shilingi milioni 20. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 33.5 fedha za ufadhili wa AGPAHI kwa ajili ya ukarabati wa jengo la kutolea huduma na tiba na jengo la stoo. Aidha, Halmashauri imetoa kiasi cha shilingi milioni 5.98 kwa ajili ya kusimika mfumo wa kukusanya mapato na takwimu za afya ili kukiwezesha kudhibiti upotevu wa mapato. Serikali inaendelea kutenga fedha kukikarabati kituo hiki ili kuboresha miundombinu na utoaji wa huduma kwa wananchi.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, Serikali itapeleka lini gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwani ni zaidi ya miaka miwili sasa baada ya gari lililokuwepo kuungua moto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Chiwale ni moja kati ya vituo vya kutolea huduma za afya 33 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Ni kweli gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Chiwale lilichomwa moto na wananchi mwaka 2013, suala hili lilisababisha kituo hicho kukosa gari la wagonjwa kwa muda mrefu na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imefanya jitihada za kuhakikisha huduma za dharura kwa wagonjwa wanaohitaji rufaa hazikwami kwa kutoa gari lililokuwa linatumiwa na timu ya Menejimenti ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi (CHMT). Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imepewa maelekezo na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kutenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya kununua gari la wagonjwa ili kuwaondolea wananchi usumbufu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:-
Kituo cha Afya Wilaya ya Siha kimeonekana kukidhi mahitaji yote muhimu tayari kwa usajili lakini hadi sasa kituo hicho hakijapata usajili wa Hospitali ya Wilaya.
Je, ni nini kauli ya Serikali katika kupandisha hadhi kituo hicho ili kupunguza kadhia ya upatikanaji wa huduma za kiafya kwa wananchi wa Wilaya ya Siha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuanzishwa Wilaya ya Siha haikuwa hospitali ya wilaya, hivyo Kituo cha Afya Siha ndicho kilichotumika kutoa huduma za matibabu kwa ngazi ya Hospitali ya Wilaya. Mwaka 2009/2010 Wilaya ya Siha ilipata eneo ambalo lilitolewa na vyama vya ushirika viwili ambavyo vilitoa jumla ya ekari 40 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, hii ilitokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Siha na hivyo kushindwa kumudu idadi ya wagonjwa na kupelekea uhitaji wa uanzishwaji wa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na wadau wengine wa maendeleo walisaidia uanzishwaji wa ujenzi wa Hospitali ya Wilayana kufikia kuanza kutoa huduma za afya. Hospitali inapokea wagonjwa wa rufaa kutoka katika vituo 20 vya kutolea huduma za afya vikiwemo vituo binafsi, vituo vya mashirika ya dini pamoja na vituo vya Serikali. Lengo la Serikali si kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Siha kuwa Hospitali ya Wilaya, bali kuendelea kuboresha miundombinu inayoendelea kujengwa katika Hospitali ya Wilaya ili kuwa na hadhi kamili ya kupata usajili kama Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendelea kuboresha huduma Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilitoa shilingi milioni 250 ambazo zimetumika kumaliza jengo la wagonjwa wa nje ambalo ukamilishaji wake uko hatua za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuendelea kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi. Aidha, Halmashauri kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Siha imeomba wadau mbalimbali ambao wameweza kuchangia jumla ya shilingi milioni 129.38 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya akina mama ambayo iko katika hatua za umaliziaji.
MHE. ENG. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaunga mkono wananchi wa Kata ya Haneti kwa kumalizia ujenzi wa chumba cha upasuaji ambacho kilianzishwa kwa nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa pongezi kwa wananchi wa Kata ya Haneti pamoja na Mbunge wao Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga kwa juhudi kubwa za kuibua na kuanza ujenzi wa chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi hususani akina mama na watoto. Ujenzi huo umefikia hatua ya kufunika jamvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali kuboresha miradi kupitia fedha za miradi ya maendeleo na kuchagua miradi michache itakayotoa matokeo ya haraka, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilitengewa shilingi milioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya cha Haneti na shilingi 350 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mlowa Barabarani. Ujenzi huo utakamilishwa baada ya fedha hizo kupokelewa kutoka Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa majengo haya ya upasuaji yatakapokamilika kwa kiasi kikubwa yatawezesha kuboreshwa kwa huduma za akinamama wajawazito pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vitokanavyo na uzazi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa Itigi katika Jimbo la Manyoni Magharibi kusaidia kupunguza gharama kubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, pia kulipa mishahara yote ya watumishi, mgao wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), vifaa tiba na kuongeza Madaktari Bingwa:-
• Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
• Je, Serikali haioni kuwa kwa sasa ni bora kujenga hospitali ya Serikali katika Halmashauri mpya ya Itigi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika utoaji wa huduma za afya, Serikali inatoa ruzuku ya fedha kwa ajili ya kulipia mishahara ya watumishi pamoja na ruzuku ya dawa na vifaatiba. Jumla ya watumishi 50 wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar wanalipwa mishahara na Serikali ambao ni Daktari Bingwa mmoja, Daktari (MD) mmoja, Mteknolojia Maabara Mmoja, Madaktari Wasaidizi Wawili, Tabibu Wawili na Wauguzi 43.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mgao wa dawa na vifaatiba kutoka Bohari Kuu (MSD) unaendelea kutolewa na Serikali. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, kupitia MSD Serikali ilitoa dawa zenye thamani ya shilingi milioni 105.674 na mwaka wa fedha 2017/2018 hospitali ilipatiwa dawa zenye thamani ya shilingi milioni 114.671.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Itigi katika bajeti ya mwaka 2018/2019, imetengewa jumla ya shilingi milioni 600 kama ruzuku ya miradi ya maendeleo ili kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Eneo la ujenzi wa hospitali lenye ukubwa wa ekari 50 limeshatengwa katika Kijiji cha Kihanju, Kata ya Tambukareli.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y. MHE. DKT. MARY M. NAGU) aliuliza:-
Katika msimu wa mwaka 2015/2016, Wilaya ya Hanang ilikumbwa na mvua kubwa sana iliyosababisha kuharibika kwa miundombinu ikiwemo ya barabara.
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kilitengwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga na kukamilisha barabara iliyofunguliwa na Wachina inayopita katika Vijiji vya Mig’enyi, Milongoli, Gawidu hadi Ngamu na barabara inayounganisha Sechet, Wilaya ya Babati Vijijini kupitia Vijiji vya Basodesh, Basotu mpaka Mulbadaw?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zilizoharibika ziliandaliwa maombi ya fedha za dharura ambapo barabara ya Getasam – Mto Bubu ilikarabatiwa kwa shilingi milioni
438.259 katika mwaka wa fedha 2015/2016. Barabara ya Basotu – Basodesh katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilitengewa shilingi milioni 455 zilizotumika kujenga daraja moja lenye urefu wa mita 20 na kukarabati barabara hiyo urefu wa kilometa sita kwa kiwango cha changarawe.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Februari, 2018 Mfuko wa Barabara ulitoa fedha za dharura shilingi milioni 500 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Ming’enyi – Milongori. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, barabara za Endasak – Gitting – Dawar – Gawal – Gawidu zimeombewa shilingi milioni 209 za kuzifanyia matengenezo. Aidha, barabara ya Basotu – Basodesh imeombewa shilingi milioni 90 za kuwezesha ujenzi wa daraja linalounganisha Wilaya ya Hanang na Babati Vijijini.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Changamoto ya fedha za mikopo inayotolewa na Halmashauri za Wilaya kwa makundi ya wanawake na vijana nchini ni urejeshaji hafifu pamoja na kutorejeshwa kwa fedha hizo kabisa; kuna taasisi za fedha hapa nchini zinatoa mikopo kwa makundi tajwa hapo juu kwa ufanisi mkubwa na kwa uzoefu wa muda mrefu:-
Je, kwa nini Serikali isipitishe utoaji wa mikopo hiyo kwenye taasisi hizo zenye ufanisi wa muda mrefu na watalaam wa kutosha kama WEDAC ili kuepusha upotevu wa fedha za Serikali na mikopo kuwafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha Mfuko wa Wanawake na Vijana baada ya kubaini kuwa wanawake na vijana wanashindwa kupata mikopo kutoka taasisi zingine za fedha ambazo zina masharti magumu. Lengo la kuanzishwa kwa mfuko huu ni kuondoa tatizo hilo ili kuwawezesha wanawake na vijana wengi kuendesha shughuli zao za kiuchumi ili kujikwamua na umaskini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taasisi zote za fedha hufanya biashara, unapoingia ubia na taasisi yoyote ya fedha lazima kuwepo na gharama za usimamizi wa mikopo hata kama masharti yatakuwa nafuu. Gharama hizo zinabebwa kwenye riba ukiacha masharti mengine kama dhamana na kadhalika. Kwa kuzingatia lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ambapo tunawalenga wananchi wa chini kabisa ambao hata uwezo wa kugharamia gharama za uendeshaji wa mifuko hiyo kwa wengine ni vigumu, ni vema mfumo wa uendeshaji uliopo na usimamizi chini ya Halmashauri ukaendelea kutumika.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge hili nawaelekeza Wakurungezi katika Halmashauri zote, kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Vijana zinatolewa na kukopeshwa kwa vikundi hivyo kama ilivyoelekezwa katika mwongozo wa mipango na bajeti. Fedha hizo zitolewe kwa kadri mapato ya ndani yanavyokusanywa.
MHE. HAWA M. CHAKOMA (K.n.y. MHE. MARIA N. KANGOYE) aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko mengi juu ya wananchi wanyonge hususani wanawake wajane na yatima kudhulumiwa ardhi hususani maeneo ya vijijini:-
Je, ni lini Serikali itaweka mikakati ya Kiwilaya ili kuwasaidia wananchi hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndilla Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikishughulikia migogoro ya ardhi vijijini katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya Wizara. Migogoro inayopokelewa kutoka maeneo mbalimbali inahusu mirathi inayowagusa wajane na yatima katika maeneo ya vijijini, madai ya fidia ya fedha, viwanja/maeneo/mashamba, mwingiliano wa mipaka ya mashamba/viwanja, uvamizi wa wananchi katika maeneo ya taasisi za umma, taasisi kuingilia maeneo ya wananchi, migogoro baina ya wananchi na wawekezaji na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali katika kuipatia ufumbuzi migogoro ya aina hiyo ni pamoja na kuanzisha Dawati Maalum la kusikiliza na kusaidia kutatua malalamiko ya ardhi yanayowasilishwa na wananchi. Dawati hilo pamoja na mambo mengine, linabainisha siku maalum za kupokea na kusikiliza malalamiko au kero hizo. Aidha, Serikali imeimarisha utendaji wa Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji, Kata na Wilaya kwa kuelekeza kuwa uteuzi wa wajumbe wa Mabaraza hayo unakuwa wa uwiano sawia kwa kuzingatia uwepo wa uwakilishi wa wanawake.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhimiza kuandaliwa kwa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji na wilaya (land use plans) ili kudhibiti mwingiliano wa matumizi ya ardhi. Aidha, ipo mikakati ya kurasimisha makazi kwenye vijiji na miji inayoondoa migogoro ya ardhi na kuinua kipato cha wananchi kwa kuwatayarishia hatimiliki ambazo hutumika kama dhamana katika kuomba mikopo kwenye taasisi za fedha.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa barabara pembezoni mwa Ziwa Nyasa, hususan Wilaya ya Ludewa na Mkoa wa Njombe; eneo hilo lenye urefu wa kilomita 150 hutegemea usafiri wa meli ambao hauna tija kwa wananchi walio wengi:-
(a) Je, Serikali itawasaidia vipi wananchi wa maeneo hayo yenye vijiji 22 kupata barabara ya uhakika?
maeneo hayo yenye vijiji 22 kupata barabara ya uhakika?
(b) Kwa kuwa wananchi wameanza kutengeneza wenyewe barabara kwa nguvu zao. Je, Serikali inatoa tamko gani la kuunga mkono juhudi hizo za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, TARURA imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kufungua kipande cha barabara ya Mwambahesa - Makonde chenye urefu wa kilomita 3.67 na ujenzi wa daraja moja na box culvert mbili katika milima ya Mwambahesa. Tayari mkandarasi G.S. Contractor ameanza kupeleka vifaa katika eneo la mradi ili kuanza ujenzi ambao utakamilika Novemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TARURA Mkoa wa Njombe inaendelea na upembuzi yakinifu katika barabara yote yenye urefu wa jumla ya kilomita 115.51 ili kuifanyia matengenezo makubwa pamoja na ujenzi wa madaraja. Kazi hiyo ikikamilika itawezesha TARURA katika Mkoa wa Njombe kupata gharama halisi na kutenga fedha kwa ajili ya kufungua na kujenga barabara hizo pembezoni mwa Ziwa Nyasa.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika kampeni za uchaguzi tarehe 18 Novemba, 2005 aliwaahidi wananchi wa Kibiti kuwa Serikali yake itajenga barabara ya Kibiti-Kikale ili kupunguza adha kubwa ya usafiri wanayopata wananchi wa Vijiji vya Mchukwi, Rungungu, Nyamatanga na Kikale ambamo barabara hiyo inapita:-
a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
b) Je, ujenzi huo unaotarajiwa utakuwa ni wa kiwango gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibiti - Kilale ni sehemu ya barabara ya Kingwira – Ruaruke - Mtunda – Myuyu yenye urefu wa kilometa 66.2 ambapo kipande cha Kibiti - Kikale kipo kati ya barabara ya Ruaruke - Mtunda. Tangu kutolewa kwa ahadi na Mheshimiwa Rais mwaka 2005 barabara hiyo imefanyiwa matengenezo ya kilomita 56 na ukarabati wa daraja la Ruhoi lenye urefu wa mita 24 kwa gharama ya shilingi milioni 151.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, barabara hiyo imetengewa shilingi milioni 185.02 kupitia TARURA kwa ajili ya matengenezo ya kilomita 65.9 kwa kiwango cha changarawe ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka gari ya kuwahudumia wagonjwa katika kituo cha Afya cha Magunguli –Mgololo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Menrald Lutengano Kigola, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Magungulu - Mgololo kilichopo kata ya Magungulu imekwishapatikana. Gari hili lilitolewa na Mheshimiwa Rais wakati anatoa msaada wa magari ya wagonjwa kwa halmashauri mbalimbali hapa nchini mnamo mwezi Machi, 2018 na taratibu za usajili zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa kutambua uhitaji wa gari katika kituo hiki, gari hili limepelekwa kituoni moja kwa moja na kuanza kutumika huku taratibu za usajili wake zikiwa zinaendelea. Ni matumaini yetu kuwa gari hili, litasaidia kuleta wepesi kwa wananchi kufikia huduma za afya pale mahitaji yatakapo yanajitokeza.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Serikali imetumia zaidi ya shilingi milioni 350 kuimarisha barabara ya Namanyere – Ninde yenye urefu wa kilomita 67, lakini fedha hazikutosha kukamilisha barabara hiyo:-
Je, Serikali itatenga fedha zaidi kukamilisha barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Namanyere- Ninde yenye urefu wa kilomita 67, kwa mara ya kwanza iliibuliwa na mradi wa TASAF Awamu ya I mwaka 2005/2006 kwa kulima barabara hiyo kwa kutumia nguvu kazi ya wananchi. Kwa kipindi chote hadi mwaka 2014/2015, barabara haikufunguka kwa kukosa miundombinu muhimu kama vile madaraja na makalvati.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali ilitenga fedha jumla ya shilingi milioni 375.3 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ambapo fedha hizo zilitumika kwa kufyeka barabara na kuondoa miti katika barabara yote, kuilima barabara kwa urefu wa kilomita 25 kwa kiwango cha udongo, kujenga Makalvati 15 pamoja na kujenga madaraja manne. Kati ya madaraja manne yaliyojengwa, mawili yapo katika Mito ya Lwafi na Ninde, hivyo matengenezo hayo yamewezesha barabara hiyo kufunguka kwa urefu wa kilomita 25 tu.
Mheshimiwa Spika, kulingana na upatikanaji wa fedha, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanyia matengenezo barabara hiyo ambapo mwaka wa fedha 2015/2016, shilingi milioni 44.58 zilitengwa kwa ajili ya kufanya matengenezo ya muda maalum kwa urefu wa kilomita 20. Aidha, mwaka wa fedha 2016/2017, kiasi cha shilingi milioni 20 zilitumika kuimarisha sehemu korofi zenye urefu wa mita 500.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuifungua barabara hii kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana ili kusaidia wananchi wanaotumia barabara hii katika suala zima la usafiri.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU (K.n.y. MHE. MUSSA R. NTIMIZI) aliuliza:-
Barabara ya Buhekela-Miswaki-Loya-Iyumbu inaunganisha Majimbo ya Igunga, Manonga, Igagula na Singida Magharibi, pia inaunganisha Mikoa miwili ya Tabora na Singida, ina Mbuga kubwa ya Wembele ambapo wananchi wanalima mpunga na kulisha Mikoa ya Tabora, Shinyanga na Singida lakini ni mbovu sana:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuitengeneza barabara hiyo kwa umuhimu wake huo wa kiuchumi na kimawasiliano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Buhekela-Miswaki- Loya-Iyumbu inahudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), katika Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Igunga yenye kipande chenye urefu wa kilometa 102.79 ambayo ni barabara ya Igunga-Itumba-Simba na Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kwa maana ya Uyui yenye kipande chenye urefu wa kilometa 66.05 ambayo ni barabara ya Miswaki - Loya kilometa 28.68 na Loya-Nkongwa kilometa 37.37.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Igunga imepanga kufanya matengenezo ya muda maalum kilometa sita na matengenezo ya kawaida kilometa moja kwa gharama ya Sh.225,000,000. Mpaka sasa barabara zenye urefu wa kilometa sita zimeshachongwa na maandalizi ya kuziweka changarawe yanaendelea. Vilevile TARURA Halmashauri ya Igunga imepewa shilingi milioni 297 kwa ajili ya kujenga boksi kalvati tatu na kufanya matengenezo ya muda maalum kilometa 1.6.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ujenzi wa boksi kalvati tatu umefikia asilimia 30. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Igunga imetengewa Sh.165,000,000 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi kilometa 23 na ujenzi wa boksi kalvati moja.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Tabora (Uyui) imeidhinishiwa Sh.400,000,000 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya kilometa 20 kwa kiwango cha changarawe pamoja na kujenga kalvati moja. Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea Kituo cha Afya cha Palestina kilichopo Kata ya Sinza alitangaza kukipandisha hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, bado Serikali inaendelea kuipatia fedha hospitali hiyo kama Kituo cha Afya.
Je, ni lini Serikali itaitambua hospitali hiyo kama Hospitali ya Wilaya kwa kuipa fedha na vitendea kazi vinavyofanana na hadhi yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Palestina kimekuwa kinafanya kazi kama Hospitali ya Wilaya kufuatia tamko la Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne la tarehe 11 Disemba, 2012.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tamko hilo, ukaguzi ulifanyika na kubaini uhitaji wa kuongezewa eneo kwa ajili ya upanuzi wa huduma. Ifahamike wazi kuwa kituo hiki kilianzishwa ili kitoe huduma kama Kituo cha Afya, hivyo hakiwezi kuwa Hospitali ya Wilaya. Kwa kutambua umuhimu wa kituo hiki, hatua zifuatazo zimechukuliwa kutatua baadhi ya changamoto:-
(a) Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ruzuku ya ununuzi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imeongezeka hadi kufikia shilingi milioni 69 kutoka shilingi milioni 57.4 kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
(b) Madaktari Bingwa watatu wameshapelekwa katika kituo hiki kati ya watano wanaohitajika, kwa maana ya Madaktari Bingwa wa Watoto, wawili na Daktari wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi mmoja.
(c) Katika mwaka wa fedha 2018/2019, kiasi cha shilingi milioni 160 kimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la ghorofa moja ambalo lina wodi ya wanaume, wanawake na watoto.
(d) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kituo kimetengewa asilimia 25 ya fedha za Mfuko wa Pamoja wa Wafadhili (Health Sector Basket Fund) ambayo ni sawa na shilingi milioni 357.73 ya mgao wa Manispaa ya Ubungo ambayo ni shilingi bilioni 1.43. Fedha hizi ni kwa ajili ya utawala na ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako tukufu, napenda kuelekeza Halmashauri ya Ubungo kutenga eneo lisilopungua ekari 25 litakalowezesha kuwepo katika eneo moja majengo yote ya msingi ya Hospitali ya Wilaya. Aidha, Serikali itaendelea kupeleka Madaktari Bingwa na kuboresha huduma zaidi katika kituo hiki kadri bajeti itakavyokuwa ikiruhusu.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-
Wananchi wa Vijiji vya Hurumbi, Dumi na Chandimo Kata ya Serya, Ausia, Mulua na Guluma (Suruke) pamoja na Hachwi, Kutumo na Chora (Kolo) katika Jimbo la Kondoa Mjini, kijiografia wana changamoto kubwa ya huduma muhimu za afya ambapo wanalazimika kufuata huduma hizo katika zahanati za jirani au hospitali ya mjini:-
Je, ni lini Serikali itatupatia Mobile Clinic kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa wanahitaji huduma za Hospitali Tembezi (Mobile Clinic) katika kuhakikisha wanapata huduma mbalimbali za kinga na tiba kwa urahisi. Hata hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imekuwa ikitoa huduma za Hospitali Tembezi katika Halmashauri zote za Mkoa kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa kuanzia tarehe 10 – 19 Agosti, 2017 Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Chemba na Kondoa Vijijini kwa Kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa ziliendesha huduma ya kibingwa kwa Hospitali Tembezi katika Hospitali ya Kondoa. Katika zoezi hili, jumla ya Madaktari Bingwa 31 walitoa huduma mbalimbali za kibingwa kwa wagonjwa 6,873 kwa mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mji imeanzisha huduma za Hospitali Tembezi kwa watu wanaoishi na VVU kila mwezi katika Zahanati za Kingale na Kolo ili kuwapunguzia wagonjwa adha ya kufuata huduma hii katika Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa itaendelea kutoa huduma hizi mara kwa mara kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa kupata huduma za kibingwa na huduma nyingine katika maeneo yao na kuepusha kuingia gharama kufuata huduma za kiafya.
MHE.KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
Katika vikao vya Ushauri vya Mkoa wa Mwanza (RCC), moja ya kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni ujenzi wa jengo la ghorofa tatu katika Hospitali ya Mkoa linalohitaji shilingi bilioni nne na laki mbili (4.2 bilioni):-
Je, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kinachohitajika katika mwaka huu wa fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa jitihada zake za kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kuanzisha ujenzi wa jengo la ghorofa tatu katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Sekou Toure ikiwa ni jengo mahususi kwa ajili ya kutoa huduma ya Mama na Mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni mbili na hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni moja kimeshatolewa na kulipwa kwa Wakala wa Majengo Tanzania kwa maana ya TBA ambaye ndiye msimamizi Mkuu wa jengo hili. Vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia tamko la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kuagiza hospitali za Mkoa kuwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Wizara imetenga kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika hospitali za rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na hospitali ya Mkoa wa Sekou Toure.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010 Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga Kituo cha Afya katika Mji wa Nalasi na kutoa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya
Mchoteka:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nalasi?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Mchoteka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Afya - Nalasi ulianza Oktoba, 2013 kwa gharama ya shilingi milioni 80 ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa msingi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Katika mwaka wa fedha 2017/2018, kiasi cha shilingi milioni 75 zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hicho kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka kipaumbele na kutoa shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya nane katika Mkoa wa Ruvuma ambapo kati ya hivyo, vituo vya afya viwili vinajengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambavyo ni Msakale kilichogharimu shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Matemanga kilichogharimu shilingi milioni 500.
(b) Mheshimwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina gari moja ambalo linahudumia vituo vyote vya afya kikiwemo Kituo cha Afya Mchoteka. Hata hivyo, gari hiyo kwa sasa ni chakavu kwa kuwa ilinunuliwa tangu mwaka 2007. Halmashauri inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga fedha katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya ununuzi wa gari lingine la wagonjwa.
MHE. JUSTIN J. MONKO (K.n.y MHE. ALLAN J. KIULA) aliuliza:-
Wilaya ya Mkalama ina vituo vya afya vitatu ambavyo vinakabiliwa na changamoto za uhaba wa watumishi, vipimo, majengo huku idadi ya wakazi wanaohitaji huduma ikiongezeka:-
a) Je, ni lini Serikali itaongeza idadi ya watumishi wa kada zote za kitaaluma katika vituo hivyo?
b) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi zahanati kubwa ziwe Vituo vya Afya ili kuhudumia wananchi wengi zaidi kutoka Iguguno, Ilanda Msiu na Mkiko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Allan Kiula, Mbunge wa Mkalama, lenye sehemu
(a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeajiri watumishi wa afya 2,534 kwenye hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati nchini. Kati ya hao, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ilipata watumishi 12. Vilevile Serikali inakamilisha ajira za watumishi wa afya 6,018 ambao wataajiriwa katika hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati. Maeneo yenye upungufu vikiwemo Vituo vya Afya vya Mkalama vitawekwa katika kipaumbele cha kupatiwa watumishi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuboresha vituo vya afya vilivyopo ili viweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa badala ya kupandisha hadhi zahanati zilizopo. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Serikali imejenga Kituo cha Afya Kinyambuli kilichogharimu shilingi milioni 400 ili kuboresha huduma za dharura na upausuaji kwa mama wajawazito.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga theatre pamoja na vifaa vyake vya upasuaji katika Wilaya ya Namtumbo, Mji Mdogo wa Lusewa. Ahadi hii ni ya muda mrefu na wananchi wamekuwa wakiteseka kutokana na ukosefu wa huduma hiyo jambo ambalo limesababisha vifo hasa kwa akinamama wajawazito na watoto:-
a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi huo?
b) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba ya Daktari katika Kituo cha Afya cha Lusewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Lusewa ulianza mwaka 2015. Ujenzi uliendelea katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo fedha zilipelekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya kituo. Jengo la OPD limekamilika isipokuwa sakafu ya chumba cha upasuaji. Kituo hicho kitawekwa katika kipaumbele na kutengewa bajeti katika mwaka wa fedha 2019/2020 ili kukamilisha ujenzi unaoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ili kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto, Serikali imeweka kipaumbele na kutoa jumla ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya nane katika Mkoa wa Ruvuma ambapo kati ya fedha hizo, shilingi milioni 900 zimetolewa kwa vituo viwili vya afya vilivyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambavyo ni Kituo cha Afya Msakale na Matemanga. Vituo vingine vilivyopokea fedha katika Mkoa wa Ruvuma ni Kalembo (shilingi milioni 500), Mkili (shilingi 400), Namtumbo (shilingi milioni 400), Madaba (shilingi milioni 400), Mahukuru (shilingi milioni 500) na Mchangimbole (shilingi milioni 500).
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati huu wa Serikali unalenga kuimarisha huduma za dharura na upasuaji kwa mama wajawazito.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliweka kiasi cha shilingi bilioni 1.5 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kuanza kujenga hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, kutokana na ukomo wa bajeti uliowekwa, fedha hiyo iliondolewa katika bajeti:-
Je, Serikali itakuwa tayari kutenga fungu maalumu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliweka kipaumbele na kutenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe lakini kutokana na ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 bajeti hiyo haikupatikana. Hata hivyo, Serikali imetoa shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo viwili vya Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ambavyo ni Iboya kilichopokea shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Masumbwe kilichopokea shilingi milioni 400 pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, katika Mkoa wa Geita, Serikali imeweka kipaumbele na kuanza ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri ya Wilaya Nyang’hwale ambapo zimetengwa jumla ya shilingi bilioni tatu.
MHE. PHILIPO A. MULUGO aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kuipandisha hadhi Hospitali Teule ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki Dayosisi ya Mbeya iwe Hospitali Teule ya Wilaya ili wananchi wa Songwe waweze kupata huduma stahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 2 Januari, 2018, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ilisaini mkataba na Kanisa Katoliki, Jimbo la Mbeya uliopandisha hadhi ya Hospitali ya Mwambani kuwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Songwe. Kufuatia mkataba huo, Serikali imeongezea fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa hospitali hiyo kutoka shilingi milioni 27.5 kwa mwaka 2017/2018 hadi shilingi milioni 105 kwa mwaka 2018/2019. Mkataba huo utaendelea hadi Serikali itakapokamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Songwe, ambayo katika mwaka wa fedha 2018/2019 imetengewa shilingi milioni 1.5.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Serikali kupitia Mradi wa Mfuko wa Benjamin Mkapa ilidhamiria kujenga na kukamilisha huduma ya upasuaji kwenye Kituo cha Afya cha Kata ya Kala na baada ya mfuko huo kuacha shughuli zake hakuna juhudi inayoendelea.
(a) Je, kuna mpango wowote kuendeleza nia hiyo njema?
(b) Kwa kuwa kituo hicho kina upungufu mkubwa wa wataalam; je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi wakiwepo wauguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa za Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ina vituo vya afya saba, kati ya hivyo vituo vinne vinamilikiwa na taasisi za kidini na vitu vitatu vinamilikiwa na Serikali. Vituo vya afya viwili vinavyomilikiwa na Serikali vinatoa huduma za upasuaji. Kituo cha Afya Kala kinamilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga. Taasisi ya Benjamin Mkapa ilijenga chumba cha upasuaji (theatre) pamoja na kutoa baadhi ya vifaa kwa ajili ya huduma za upasuaji katika Kituo cha Afya Kala mnamo mwaka 2016/2017.
Hata hivyo, huduma hizo zimekuwa hazitolewi kutokana na changamoto mbalimbali kubwa zikiwa ni upatikanaji wa wataalam kwa ajili ya kufanya huduma za upasuaji na kukosekana kwa huduma ya umeme na mfumo wa maji kwa ajili ya kuendeshea shughuli za upasuaji. Ili kukabiliana na hali hiyo Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 17.3 katika mwaka wa fedha 2017/2018, kwa ajili ya miundombinu ya maji na umeme ambapo fedha hiyo bado haijapokelewa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na upungufu wa watumishi katika Kituo cha Afya Kala, Halmashauri ilipeleka tabibu mmoja na wauguzi wawili ili kutoa huduma katika kituo hicho mwaka 2015. Aidha, Halmashauri ilipeleka gari moja la wagonjwa lenye namba za usajili SM 4467 mwaka 2017 kutoa huduma katika kituo hicho. Serikali itaendelea kupeleka wataalam wa afya katika kituo hicho kwa kadri watakavyopatikana. Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wamiliki wa Kituo cha Afya Kala ili kushirikiana katika kutatua changamoto ya watumishi katika kituo hicho kwa kuwa watumishi watatu waliopo sasa katika kituo hicho wote wameajiriwa na Serikali.
MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y MHE. RASHID A. AKBAR) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia Hospitali ya Wilaya ya Newala watumishi pamoja na vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuhakikisha vituo vinakuwa na vifaa tiba vinavyohitajika. Hospitali zinapatiwa rasilimali watu na fedha kwa ajili ya kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi 198,671,475mpaka sasa shilingi 120,510,860 zimepokelewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali imetenga shilingi 244,066,959.92 kwa ajili ya vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Newala.
Mheshimiwa Spika, uhaba wa watumishi ni changamoto inayovikabili vituo vingi vya kutolea huduma za afya nchini. Hata hivyo Serikali inaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya kadri vibali vya ajira vinavyopatikana. Mwezi Novemba, 2017 Halmashauri ya Mji wa Newala ilipata watumishi 12 wa kada mbalimbali za afya na katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi 60 wa kada mbalimbali za afya. Serikali itaendelea kupeleka watumishi wa afya, vifaa tiba na vitendanishi ili kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Newala.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. JOSEPH M. MKUNDI) aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Nansio) inakabiliwa na msongamano wa Wagonjwa; Mwaka 2002 Halmashauri ya Wilaya ilitumia zaidi ya shilingi milioni 200 kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Nakutunguru kama njia ya kupunguza msongamano huo. Hata hivyo, ujenzi huu haujakamilika kutokana na ukosefu wa fedha:-
Je, Serikali ipo tayari kuondoa upungufu uliopo ili Kituo hicho kianze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kupitia fedha za Ruzuku ya Maendeleo kwa Serikali za Mitaa yaani (Local Government Development Grant) mwaka 2012 kwa ajili ya kuanza kwa awamu wa kituo cha Afya Nakatunguru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo hilo OPD ulikamilika mwezi Aprili, 2015 na lilizinduliwa rasmi tarehe 18 Februari, 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Mpaka sasa kituo hiki kinafanya kazi kwa kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) na huduma za Mama, Baba na Mtoto (Reproduction and Child Health (RCH).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa Fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imeidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi wa Kituo hiki. Kwa sasa Serikali ipo katika awamu ya nne ya utekelezaji wa mpango wa ukarabati wa Vituo vya Afya nchini, hivyo tutakiingiza Kituo cha Afya Nakutunguru katika awamu zijazo ili kuhahakisha kinakamilika na kutoa huduma zote ikiwemo huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Kata ya Bukene Wilayani Nzega inaundwa kwa Kijiji kimoja tu chenye wakazi zaidi ya 7,600 jambo ambalo linakwamisha uharakishaji wa huduma za maendeleo kwa wananchi. Tulishafuata taratibu zote za kuomba Kijiji cha Bukene kigawanywe ili kupata Kijiji kingine kipya:-
Je, Serikali haioni kuwa siyo sahihi kuwa na Kata inayoundwa na Kijiji kimoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kuzingatiwa wakati wa kuanzisha au kupandishwa hadhi maeneo ya utawala zimeelezwa katika Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287 na (Mamlaka za Miji) Sura 288, Toleo la 2002. Sambamba na taratibu hizo upo mwongozo uliofanyiwa marekebisho mwaka 2014 unaofafanua vigezo vya kuzingatiwa katika kuanzisha maeneo hayo ili kuepusha uanzishwaji holela wa maeneo ya utawala yasiyokuwa na sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika kuanzisha vijiji. Mapendekezo ya kugawanywa kwa Kijiji cha Bukene kilichopo katika Kata ya Bukene, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega hayajawasilishwa rasmi kwa kuzingatia taratibu zilizopo kisheria ikiwa ni pamoja na kujadiliwa na kupitishwa katika vikao vyote vya kisheria ambavyo ni Serikali ya Kijiji, Mkutano Mkuu wa Kijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kipaumbele cha Serikali kwa sasa siyo kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala bali kuimarisha maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-
Pamoja na kuhudumia wagonjwa wengi wakiwemo watokao Wilaya ya Kondoa, Chemba, Kiteto, Babati na wakati mwingine hata Hanang’, lakini Hospitali ya Mji wa Kondoa haina gari la wagonjwa (Ambulance) na uhitaji wa huduma za dharura na rufaa umeongezeka sana baada ya kukamilika kwa barabra kuu itokayo Dodoma – Babati:-
Je, ni lini Serikali itaipatia gari la wagonjwa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kwa muda mrefu hospitali ya Mji wa Kondoa imekuwa na ukosefu wa gari la wagonjwa hali ambayo imechangiwa na uchakavu wa gari lililokuwepo. Hata hiyo, Halmashauri ya Mji wa Kondoa imepata gari la wagonjwa (Ambulance) iliyotolewa tarehe 16 Machi, 2018 katika mgao wa magari yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Wananchi au taasisi zilizopewa vibali vya kupaki magari hadi saa 12 jioni katika Jiji la Dar es Salaam sasa wanatumia vibali hivyo kupaki kwa saa 24. Hali hiyo imeibua usumbufu kwa wananchi wanaotaka kupaki magari yao kuanzia saa 12 jioni:-
Je, ni lini Serikali itakomesha suala hilo ili kuwaondolea wananchi usumbufu wanaoupata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassanali Mohamedali Ibrahimu, Mbunge wa Kiembe Samaki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria Ndogo ya Maegesho ya Magari katika Tangazo la Serikali (GN) Na. 60 la mwaka 1998 na marekebisho yake (GN) Na. 41 ya mwaka 2017, maegesho ya kulipia pamoja na maegesho yaliyohifadhiwa (Reserved Parking) yanapaswa kutumika kuanzia saa 2.00 asubuhi mpaka saa 12.00 jioni, baada ya muda huo maegesho yote yanatakiwa kuwa wazi kwa ajili ya matumizi ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam kusimamia vyema utekelezaji wa sheria hii na kuhakikisha chanzo hiki cha mapato kinasimamiwa ipasavyo ili halmashauri zinufaike na chanzo hiki.
MHE. SALMA R. KIKWETE (K.n.y MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA) aliuliza:-
Kwa kuwa Serikali ina mkakati madhubuti wa kupunguza vifo vya akina mama na watoto:-
(a) Je, ni lini Zahanati ya Kiboga katika Kata ya Msongola itafunguliwa ili wananchi wapate huduma ya afya?
(b) Kwa kuwa wananchi wa Mtaa wa Mbondole katika Kata ya Msongola walitoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, je, ni lini zahanati hiyo itakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiboga na Luhanga ni mitaa miwili inayopakana ambayo hapo awali ilikuwa miongoni mwa vitongoji katika Kijiji cha Mvuti, Kata ya Msongola. Wananchi wa Mtaa wa Luhanga kwa nguvu zao wenyewe walianza ujenzi wa zahanati na Serikali ikawaunga mkono na sasa jengo la zahanati ya Luhanga lipo katika hatua za upakaji rangi, kuweka madirisha na milango. Mtaa wa Kiboga bado hauna zahanati hivyo halmashauri inatakiwa kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati. Hata hivyo, wakazi wa Kiboga wanapata huduma za afya katika Zahanati ya Mvuti ambayo ipo ndani ya kilometa tano ambayo ni matakwa ya utekelezaji wa Mpango Maalum wa Uimarishaji Afya ya Msingi 2009 - 2017.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Zahanati ya Mbondole imebaki kupigwa rangi na kuwekewa milango ili ikamilike na kuanza kutoa huduma. Halmashauri ya Wilaya ya Ilala imetenga shilingi milioni 70 katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo inaweza kukamilisha ujenzi huo.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-
Sera ya Serikali ni kuwa na Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya katika kila Kata:-
• Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko?
• Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Vituo vya Afya katika Kata za Kiziguzigu, Kasanda, Gwarama, Rugenge, Nyamutukiza na Kata nyingine ambazo hazina Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko zimeanza ambapo limetengwa eneo lenye ukubwa wa ekari 32 katika Mtaa wa Kanyamfisi karibu na yanapojengwa Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, Serikali inajenga Hospitali za Wilaya kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza zimetengwa shilingi bilioni 100.5 kuanza ujenzi wa Hospitali 67 za Wilaya. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko itapewa kipaumbele cha kujenga Hospitali ya Wilaya katika awamu inayofuata.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo tisa vya afya katika Mkoa wa Kigoma. Kati ya fedha hizo, halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imetengewa Sh.500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Gwanumpu. Maeneo yaliyobaki zikiwemo Kata za Kizuguzugu, Kasanda, Rugenge, Gwarama na Nyamtukuza yatapewa kipaumbele kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBAaliuliza:-
Je ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Bukoli?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina gari saba zinazotoa huduma kwa wagonjwa (ambulance). Gari tano zinatoa huduma katika Vituo vya Afya vya Katoro, Nzera na Chikobe ambavyo vimeanza kutoa huduma za upasuaji. Gari mbili zinatoa huduma katika vituo vya afya vinavyobaki kikiwemo Bukoli ambacho kipo katika ukarabati ili kukiwezesha kutoa huduma za upasuaji. Halmashauri inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa gari za wagonjwa kulingana na mahitaji.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI aliuliza:-

Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi ujenzi wa barabara yenye urefu kwa kilomita 12 katika Jimbo la Arumeru Magharibi na sasa imepita miaka 10 bila kutekelezwa ahadi hiyo:-

Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi hiyo hasa ikitiliwa maanani kuwa katika Jimbo la Arumeru Magharibi hakuna barabara ya lami hata nusu kilomita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gibson Blasius Ole Meiseyeki, Mbunge wa Arumeru Maghari kama ifuatayo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa ahadi ya ujenzi wa barabara ya lami kilomita 12 Arumeru Magharibi mwezi Novemba, 2012 kwenye uzinduzi wa Hospital ya Wilaya ya Oltrumeti.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishaanza utekelezaji wa ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais Msaafu ambapo kati ya mwaka wa fedha 2014/2015 hadi 2017/2018 barabara zenye urefu wa kilomita 3.55 kwa kiwango cha lami zimejengwa Arumeru Magharibi kwa gharama ya shilingi bilioni mbili. Barabara zilizojengwa ni kama ifuatavyo: Mianzini-Timbolo kilomita 0.8; Sarawani-Oldonyosapuk kilomita 0.7; Tribunal Road kilomita 2.5; na Sekei-Olglai kilomita nne (4). Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami kwa kadiri fedha zinavyopatikana.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-

Barabara ya Hedaru – Vunta – Myamba Wilaya ya Same ni korofi sana na kusababisha usafiri wa barabara ya Tarafa ya Mamba/Vunta kuwa mgumu:-

Je, Serikali inawasaidiaje Wananchi wa Tarafa ya Mamba/Vunta ili waweze kuendelea kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Hedaru – Vunta – Myamba yenye urefu wa Kilometa 42.2 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA), Wilaya ya Same. Barabara hiyo ipo Ukanda wa Milimani na uhalibifu wake hunatokana na changamoto ya maji ya mvua yanayosababisha maporomoko ya udongo na kuchimbika kwa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, barabara hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi Milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua na vivuko viwili. Uwekaji wa Miundombinu hiyo utapunguza uharibifu unaotokana na maji ya mvua. Kazi hizo zinaendelea kutekelezwa. Kwenye Mpango wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2019/2020, Serikali imeweka kipaumbele na kutenga jumla ya shilingi milioni 87.72 kwa ajili ya kuiwekea changarawe kwenye sehemu korofi.
MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:-

Hospitali ya Wilaya ya Tarime imeelemewa na Wagonjwa kwa sababu inapokea Wagonjwa wengi kutoka Wilaya ya Tarime na Rorya, pamoja na uchache wa Vituo vya Afya, Zahanati na Vifaa katika maeneo mengi ya Wilaya hizo.

Je, ni kwa nini Serikali isipandishe hadhi Hospitali hiyo na kuwa Hospitali ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Wegesa Heche Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi 367,985 wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wanapata huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime iliyoko Tarime Mjini pamoja na Vituo vya Afya vinane ambavyo vitano vinamilikiwa na Serikali na vitatu vinamilikiwa na Watu Binafsi na Zahanati 23 za Serikali zikiwa 16 na 7 Watu binafsi. Vilevile, Hospitali hiyo inahudumia wilaya za jirani ambazo ni Rorya, Musoma na Bunda na wagonjwa kutoka nchi jirani ya Kenya na kusababisha msongamano wa wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina mpango wa kupandisha hadhi Hospitali ya Wilaya ya Tarime kuwa Hospitali ya Mkoa kwa kuwa Mkoa wa Mara una Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara iliyoko Musoma Mjini. Ili kutatua changamoto ya utoaji wa huduma za Afya katika Mkoa wa Mara, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali tatu za halmashauri katika Halmashauri za Wilaya ya Bunda, Rorya na Musoma.

Tayari fedha zote zimepelekwa kwenye Halmashauri husika kwa ajili ya kuanza ujenzi. Vilevile, Serikali inaendelea na Ukarabati na ujenzi wa Vituo sita vya Afya katika Mkoa wa Mara vinavyogharimu jumla ya shilingi bilioni 2.4. Ujenzi wa Hospitali tatu za halmashauri na Vituo sita vya Afya utaimarisha huduma katika ngazi ya msingi na kupunguza msongamano wa Wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:-

Barabara ya Surungaji inayoanzia Chikuyu - Chibumagwa - Majiri – Ikasi (Kilomita 76.2) ni barabara muhimu sana inayohudumia wakazi wa bonde la ufa katika Jimbo la Manyoni Mashariki kwa kusafirisha chumvi, samaki, ufuta na alizeti:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii pamoja na daraja katika Mto Nkonjigwe.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Edward Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Chikuyu- Chibumagwa –Majiri-Ikasi yenye urefu wa Kilomita 76.2 inahudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Katika kilomita 76.2 ni kilomita 32 tu zinazopitika majira yote ya mwaka (kilomita 14.8 ni za changarawe na kilomita 18.8 ni za udongo), kilomita 4.2 ambazo ni kutoka majirimpaka Ikasi hupitika wakati wa kiangazi pekee.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Chibumagwa-Majiri- Ikasi ilitengewa kiasi cha Sh.29,500,000.00 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo jumla ya kilomita tisa zilifanyiwa matengeneza (sehemu korofi kilomita saba na ya kawaida kilomita mbili) kuanzia Chikuyu-Chibumagwa na kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha Sh.11,600,000.00 kimetumika kujenga makalavati (line culvert)mbili katika eneo la Mpandagani kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/20 TARURA inatarajia kufanya usanifu wa Daraja la Mto Nkonjigwe lenye urefu wa mita 35 na kina cha mita sita lililopo barabara ya Chikuyu-Chibumagwa-Majiri-Ikasi. Fedha za ujenzi zitatengwa kwenye bajeti baada ya usanifu ili tuweze kujuwa gharama halisi.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-

Vigezo vilivyotumika kuchagua Vituo vya Afya 100 kupatiwa shilingi milioni 700 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara na upasuaji wa akina mama wanaojifungua kwa maana ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya maabara na upasuaji na shilingi milioni3 00 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa toka MSD ni vigezo ambavyo pia vipo katika Vituo vya Afya Duthumi, Tawa, Mvula na Mtamba katika Jimbo la Morogoo Kusini.

Je, ni lini Seikali itawatendea haki wananchi wa Morogoro Kusini kwa kuwatengea fedha ili kukamilisha miundombinu ya upasuaji angalau kituo kimoja Kata ya Duthumi, Tawala Mvuha na Mtamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Kuboresha Vituo vya Afya nchini ambapo hadi sasa Vituo vya Afya 350 vimepatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vilivyotumika kuchagua vituo hivyo vinavyokarabatiwa na kujengwa ni uhitaji mkubwa wa huduma za dharura na upasuaji kwa mama wajawazito, sababu za kijiografia na umbali mrefu ambao wananchi wanatembea kupata huduma za dharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitoa kiasi cha shilingi million 500 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Duthumi kilichopo katika Jimbo la Morogoro Kusini. Vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilion1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro inayojengwa katika Makao Makuu ya Halmashauri eneo la Mvuha.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. KEMILEMBE J. LWOTA) aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumalizia ujenzi wa maboma ya Zahanati yaliyoanzishwa kwa juhudi za wananchi pamoja na kuyawekea vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kemilembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 Serikali ilifanya tathmini kubaini idadi ya maboma nchi nzima ambayo ni Vituo vya Afya, Zahanati na nyumba za watumishi na kubaini kuwa kuna maboma 1,845 ambayo yanahitaji jumla ya shilingi bilioni 934 ili kukamilishwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliona ni vigumu kukamilisha maboma hayo kwa pamoja kutokana na upatikanaji wa fedha. Hivyo, ikabuni mkakati wa kujenga na kukarabati Vituo vya Afya 350 nchini vilivyochaguliwa kwa kutumia vigezo ambavyo ni uhitaji mkubwa wa huduma za dharura na upasuaji wa akina mama wajawazito, sababu za kijiografia na umbali mrefu ambao wananchi wanatembea kupata huduma za dharura.

Mheshimiwa Spika, vilevile, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019, jumla ya maboma 207, Vituo vya Afya sita, Zahanati 191 na nyumba kumi yalikamilishwa kwa fedha kutoka Mradi wa Mfuko wa Pamoja wa Afya na Mapato ya Ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuzielekeza Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwenye makusanyo yake ya ndani na kuendelea kushirikisha wananchi na wadau wengine wa maendeleo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi na ukarabati wa maboma hayo.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Ilemba katika Halmashauri ya Sumbawanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya saba kwa gharama ya shilingi bilioni 3.3 ikiwemo Kituo cha Afya Milepa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Vilevile Serikali imeweka kipaumbele cha kujenga hospitali tatu za Halmashauri katika Halmashauri tatu za Wilaya ambazo ni Sumbawanga, Nkasi na Kalambo kwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 kila moja na fedha hizo zimepelekwa kwenye Halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ina vituo vya kutolea huduma za afya saba, viwili vikiwa binafsi na vitano vya Serikali vinavyohudumia watu takribani 369,471. Ujenzi wa Kituo cha Afya Ilemba ulianza mwaka 2011 kwa kujenga Jengo la OPD na nyumba mbili za watumishi kwa kushirikisha wananchi. Mpaka sasa majengo hayo yamefikia hatua ya upauaji na kiasi cha Sh.82,805,611 ambapo ruzuku kutoka Serikali Kuu ni Sh.54,116,121 na nguvu za wananchi Sh.28,789,490 imetumika. Halmashauri inaelekezwa kuzingatia na kuweka kipaumbele kwenye bajeti kuhusu ukamilishaji wa mradi huo kabla ya kuanzisha miradi mipya.
MHE. GODFREY W. MGIMWA aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Kalenga katika kata na vijiji mbalimbali wamejitolea kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa zahanati na vituo vya afya lakini hakuna wauguzi na baadhi ya vifaa tiba. Je, Serikali inaisaidiaje Halmashauri kuhusu tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey Mgimwa, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti,ili kutatua changamoto ya watumishi wa umma katika sekta ya afya, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada za afya kadri wanavyohitimu katika vyuo vya afya pamoja na hali ya bajeti inavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Julai 2018/2019 Serikali imeajiri watumishi 8,447 wa kada mbalimbali za afya. Kati ya hao Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ilipangiwa watumishi 68 ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoko katika Jimbo la Kalenga vilipata watumishi 40. Serikali inaendelea kutoa kipaumbele cha ajira kwa watumishi wa kada za afya ili kukabiliana na upungufu uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la vifaatiba, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa inapokea fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo sehemu ya fedha hizo zinatumika kununulia vifaa tiba. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ilitumia shilingi 21,554,700 kwa ajili ya kununulia vifaa tiba ambavyo vilipelekwa katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoko katika Jimbo la Kalenga. Vilevile Halmashauri inakusanya fedha za Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ambazo kipaumbele cha matumizi kinapaswa kuwa ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Wilaya ya Kyerwa ina Vituo vitatu vya Afya, lakini kituo kimoja ndicho kina uhakika wa kutoa huduma, vilevile kuna uhaba wa watumishi ambao wanafanya kazi kwenye mazingira magumu pamoja na ukosefu wa nyumba za watumishi:-

Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na nyumba za watumishi ili kutekeleza Ilani ya CCM na kuondoa adha wanayoipata akina mama, watoto na wananchi wengine kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Seba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ina jumla ya Vituo vya Huduma za Afya 32 vinavyohudumua watu takribani 394,375. Kati ya vituo hivyo, kuna Vituo vya Afya vitatu, vyote vikiwa vya Serikali, Zahanati ziko 28; 23 za Serikali na tano ni za watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ni miongoni mwa Halmashauri 67 nchini zilizopatiwa shilingi bilioni 1.5 kila moja kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Mpaka sasa hatua za awali za ujenzi zinaendelea na ujenzi wa awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Juni 30, 2019. Vilevile Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Vituo vya Afya Murongo na Kamuli katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ambapo mpaka sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 98.
MHE. LATHIFA H. CHANDE aliuliza:-

Wananchi wa Mkoa wa Lindi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya hali duni ya huduma za afya kwa kuwa na uchache wa Wauguzi, Madaktari wa kawaida na wa akina mama na uhaba wa vifaa na dawa, lakini pia Vituo vya Afya na Zahanati hazitoshi:-

(a) Je, ni lini Serikali itaongeza Wauguzi, vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale?

(b) Hospitali ya Ruangwa kwa kipindi kirefu imekuwa haina huduma ya X-Ray hali inayowalazimu wananchi wa Wilaya ya Ruangwa kufuata huduma hiyo Lindi: Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hilo?

(c) Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa nyumba za Wauguzi na Mganga Mkuu katika Zahanati ya Mtawango katika Kata ya Mtawango, Liwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Lathifa Hasan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, Lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliajiri watumishi wa kada mbalimbali za Afya 6,180. Kati ya hao, 89 walipangwa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imepokea jumla ya shilingi milioni 345.5 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Aidha, upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vyote 242 vya kutolea huduma za afya Mkoani Lindi kuanzia Januari hadi Desemba, 2018 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Liwale ulikuwa ni kwa zaidi ya asilimia 91.9.

(b) Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa ilifungiwa mashine ya X-Ray mwaka 2015 ambapo mpaka Desemba, 2018 Wagonjwa 7,250 wamehudumiwa. Ni kweli kuna wakati mashine hii ilipata hitilafu na ikashindwa kufanya kazi, lakini hitilafu hiyo ilirekebishwa na mashine ya X-Ray inaendelea kutoa huduma. Mpango wa Serikali ni kuipatia hospitali hii X-Ray ya kisasa.

(c) Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ujenzi wa Zahanati pamoja na nyumba za Watumishi Mtawango ulikuwa ni mradi unaofadhiliwa na TASAF katika mwaka wa fedha 2015/2016 kujenga nyumba mbili kwa moja (two in one), ambapo fedha zilizopangwa na kutumika ni shilingi milioni 27. Hata hivyo, fedha hizo hazikutosheleza kumalizia ujenzi wa nyumba. Hivyo, Halmashauri imepanga kutenga shilingi milioni 10 katika bajeti ya mapato ya ndani ya mwaka 2019/ 2020 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Muuguzi na Mganga katika Zahanati ya Mtawango.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-

Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Mkoa wa Shinyanga aliahidi ujenzi wa Vituo viwili vya Afya katika Jimbo la Solwa:-

Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inayoelekeza kuwa na Kituo cha Afya kila Kata sambamba na utekelezaji wa ahadi mbalimbali za viongozi wa Kitaifa. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yenye Jimbo la Solwa ilipewa kipaumbele na kutengewa shilingi milioni 900.0 kwa ajili ujenzi na ukarabati wa Kituo cha afya Tinde, kilichogharimu shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Samuye kilichogharimu shilingi milioni 500. Vituo hivyo vimekamilika na vimeanza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni miongoni mwa Halmashauri 67 zilizoidhinishiwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Fedha zote zimepokelewa na ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Ahmed Ally Salum Mbunge wa Solwa kuwa ahadi za viongozi zitaendelea kutekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:-

Katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo Dodoma wapo watoto ambao hutoa huduma ya kubeba mizigo na kupewa ujira mdogo. Kutokana na kufanya kazi hizo ni wazi wanakosa haki za msingi kama elimu na malezi bora.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huduma za ulinzi wa mtoto zinatekelezwa kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2021/ 2022. Tathmini imebaini kuwa watoto wengi wanaojihusisha na kazi za kubeba mizigo masokoni ni matokeo ya umasikini uliokithiri kwa baadhi ya kaya, kuondokewa na wazazi wao kwa maambukizi ya UKIMWI, migogoro ya ndoa na ukatili dhidi ya watoto.

Mheshimiwa Spika, mkakati unaotekelezwa na Serikali ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za msingi za mtoto kupata elimu na malezi bora. Aidha, utoaji wa elimu bila malipo umetoa fursa kwa watoto wengi wenye umri wa kwenda shule kuandikishwa kuanza elimu ya awali kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi. Vilevile, mradi wa TASAF umewezesha kuzitambua kaya za watoto walio katika mazingira hatarishi na kuzisaidia kiuchumi ili ziweze kumudu mahitaji ya kaya zao kwa kuwapatia watoto mahitaji ya msingi ikiwemo elimu na afya.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea na kuwatunza watoto ikiwemo kuwapa fursa ya elimu. Aidha, jamii inao wajibu wa kushirkiana na wazazi kuwatunza na kuwalinda watoto ambao ni Taifa la kesho kwa kutowatumikisha katika kazi ambazo haziendani na umri wao. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa vitendo vyovyote vya unyanyasaji wa watoto vinavyokiuka Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-

Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Songwe yapo Mbozi na hakuna barabara ya kuunganisha Wilaya mpya ya Songwe kufika mkoani hadi upitie Mbeya:-

Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza barabara ya mkato toka Songwe kupitia Kata ya Magamba kwenda Mbozi Makao Makuu ya Mkoa ili kuwarahisishia usafiri wananchi wa Wilaya ya Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishaona haja ya kutengeneza barabara ya mkato kutoka Wilaya ya Songwe kwenda Wilaya ya Mbozi kupitia Kata ya Magamba. Barabara iliyopendekezwa inaitwa Galula – Itindi – Magamba yenye urefu wa kilometa 32.

Mheshimiwa Spika, barabara hii imeshaanza kutengenezwa kupitia TARURA ambayo katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 imetengwa shilingi milioni 65 kwa ajili ya kujenga daraja lenye urefu wa mita tisa katika Kijiji cha Itindi na mpaka sasa Mkandarasi anaendelea na kazi. Vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, barabara hii imeombewa kiasi cha shilingi milioni 63 kwa ajili ya kufanya matengenezo sehemu korofi kwa urefu wa kilometa saba.

Mheshimiwa Spika, TARURA Wilaya ya Songwe inaendelea kufanya usanifu wa kina ili kujua mahitaji na gharama halisi za kufanyia matengenezo makubwa. Mara kazi hiyo itakapokamilika Serikali itatafuta fedha kuhakikisha inajenga barabara hiyo na kufanya ipitike majira yote ya mwaka.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-

Jimbo la Mikumi lina uhaba mkubwa wa Vituo vya Afya na hata pale ambapo kuna Kituo, basi dawa na Wataalamu ni tatizo:-

Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo hilo sugu la uhaba wa Vituo vya Afya na dawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ina jumla ya vituo vya afya vitano. Kati ya vituo hivyo viwili vipo katika Jimbo la Mikumi ambavyo ni Kituo cha Afya Kidodi na Ulaya. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Kituo cha Afya cha Kidodi kilipatiwa jumla ya shilingi milioni 400 za ukarabati na kwa sasa kinatoa huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito. Vilevile Kituo cha Afya Kidodi kimepatiwa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 95 ili kukiwezesha kuanza kutoa huduma. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 zahanati ya Mikumi ilipewa jumla ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuongeza majengo ili iweze kukidhi vigezo vya kupandishwa hadhi kwa Kituo cha Afya na mpaka sasa kazi ya ujenzi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wa Kata ya Malolo inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya Malolo kwa kutumia mapato ya ndani ambapo ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo la upasuaji na wodi ya wazazi yapo katika hatua ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 1.07 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi. Vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi Februari, 2019 Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imepokea shilingi milini 849 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na 2017/2018 Serikali iliajiri jumla ya wataalam wa afya 8,238 ambapo Halmashauri ya Kilosa ilipata jumla ya wataalam 42 wa kada mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kujenga vituo vya afya kote nchini pamoja na kuajiri wataalam wa afya kulinga na upatikanaji wa rasilimali fedha.
MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-

Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya vituo vya Afya Mkoani Mwanza kukosa vyumba vya upasuaji:-

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kwa kucheleweshwa kufanyiwa upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndilla Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mwanza una jumla vya vituo vya kutolea huduma za Afya vya Serikali 272 ikiwepo Hospitali sita, Vituo vya Afya 35 na Zahanati 231. Kwa sasa huduma ya upasuaji wa dharura kwa akina mama inatolewa kwenye Hospitali zote sita na Vituo 10 vya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza vifo vinavyotokana na uchelewashwaji wa akina mama wakati wa kujifungua kwa kutokufanyiwa upasuaji, mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Vituo vya Afya 14 Mkoani Mwanza ambavyo kwa sasa viko katika hatua ya ukamilishaji na hivyo kuna Vituo 11 vya Afya ambavyo vilikuwa havitoi huduma za upasuaji, vitaanza kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali ilipeleka kiasi cha shilingi bilioni tatu Mkoani Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya za Ilemela na Buchosa ambazo zitatoa huduma ya upasuaji wa dharura kwa akina mama, hivyo kutanua wigo na kuboresha huduma za upasuaji Mkoani Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kujenga vituo vya kutolea huduma za afya na kuongeza wataalam ili kumaliza tatizo la vifo vya akina mama vinavyotokana na uchelewashaji wa huduma ya upasuaji wakati wa kujifungua.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE (K.n.y. MHE. SELEMANI S. BUNGARA) aliuliza:-

Hospitali ya Wilaya ya Kilwa haina Jokofu la kuhifadhi maiti na pia majengo yake mengi ni chakavu:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kununua jokofu jipya sambamba na kukarabati majengo ya hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE.MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Saidi Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti Hospitali ya Wilaya ya Kilwa (Kinyonga)ni miongoni mwa Hospitali Kongwe za Wilaya hapa nchini na imekuwepo tangu mwaka 1965. Kwa kutambua umuhimu wa Hospitali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekua ikifanya ukarabati na upanuzi wa majengo mbalimbali ya kutolea huduma kama ifuatavyo:-

Mwaka wa Fedha 1996/1997, ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya hospitali ulifanyika pamoja na ujenzi wa kliniki ya Mama na Mtoto; Mwaka 2010 ulifanyika ujenzi wa Jengo la Huduma za UKIMWI (CTC); Mwaka 2012 ulifanyika ujenzi wa jengo la wazazi; na Mwaka 2017 ulifanyika ujenzi wa jengo la mama ngojea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Kilwa ina jokofu moja la kuhifadhia maiti lililonunuliwa mwaka 1996. Hata hivyo, jokofu hilo lina uwezo wa kuhifadhi mwili mmoja tu. Serikali inaendelea nautaratibu wa kukamilisha hatua za kuanza ujenzi wa jengo jipya la kuhifadhia maiti kwenye hospitali hiyo sambamba na ununuzi wa jokofu jipya la kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kukarabati miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha utakavyokuwa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Mafuriko yaliyotokea Mlalo mwaka 1993 yalisababisha uharibifu mkubwa kwa barabara inayounganisha Tarafa za Umba na Mtae:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kukarabati barabara hiyo muhimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara inayounganisha Tarafa za Umba na Mtae yenye urefu wa kilometa 12.7 inajulikana kama barabara ya Mtae – Mtii – Mnazi. TARURA Wilaya ya Lushoto imekamilisha usanifu na tathmini ya kuifanyia matengenezo makubwa, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kinahitajika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia matengenezo hayo kwa kuwa inatambua umuhimu wa barabara hii.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Segerea – Sheli kwenda Kipawa kupitia Seminari itaanza kutengenezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Segerea – Sheli – Kipawa kupitia seminari yenye urefu wa kilometa 2.93 inasimamiwa na TARURA Manispaa ya Ilala, imesajiliwa kwa jina la Majumba Sita, Sitakishari. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, barabara hiyo imechongwa kwa grader ili kuiwezesha kupitika. Hata hivyo, barabara hii inakatisha katika mto Msimbazi ambapo hakuna daraja. Daraja linalohitajika kujengwa ni kubwa na usanifu wake ulishafanyika.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo inatokana na mto kutanuka, hivyo inahitajika kufanyiwa study ya kina na mapitio ya usanifu wa awali ili kupata mahitaji halisi ya ujenzi wa daraja kutokana na changamoto hiyo. Mara baada ya kukamilika kwa mapitio ya usanifu na tathmini ya gharama Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kujenga daraja na kuifanyia matengenezo makubwa barabara hii. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia TARURA imeitengea barabara hii jumla ya shilingi milioni 43 kwa ajili ya matengenezo ya maeneo korofi.
MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:-

Mtambo wa kuchoma takataka za hospitali na dawa zilizokwisha muda wake upo katika Kijiji cha Dundani Wilayani Mkuranga. Uchomaji unapofanyika moshi mzito huingia kwenye nyumba na maeneo ya wananchi wanaoishi karibu na mtambo huo na kuhatarisha afya zao:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kunusuru afya na maisha ya wananchi wanaoishi karibu na mtambo huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upo mtambo wa kuchomea taka na dawa zilizokwisha muda wake uliojengwa na mwekezaji katika Kijiji cha Dundani, Wilaya ya Mkuranga. Hapo awali mtambo huo ulikuwa na kasoro za ujenzi ambapo Serikali ilimwagiza mwekezaji kuzirekebisha kwa ilani ya tarehe 18, Oktoba, 2017 yenye kumbu. Na. NEMC/HQ/EA/05/0702/VOL1/7 sambamba na kusimamisha shughuli za mtambo mpaka kasoro zitakapokuwa zimerekebishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho hayo yamefanyika na baada ya mamlaka zote, ikiwemo Serikali ya Kijiji cha Dundani kujiridhisha kwamba hakuna tena moshi unaoathiri mazingira, mtambo huo umeruhusiwa kuendelea na kazi na mpaka sasa hakuna taarifa yoyote iliyofika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Mkuranga kulalamikia shughuli za mtambo huo.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Hospitali ya Wilaya ya Lushoto ni ya muda mrefu na hata ujenzi wa majengo yake ni wa kizamani ambao hauendani na utoaji huduma na Serikali ina utaratibu wa kukarabati na kuongeza majengo katika Hospitali za Wilaya:-

Je, ni lini Hospitali ya Wilaya ya Lushoto itakarabatiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa Hospitali Kongwe za Wilaya nchini na imekuwepo tangu mwaka 1967. Tangu kuanzishwa kwake, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleleo imefanya ukarabati na upanuzi wa majengo kama ifuatavyo:-

(i) Mwaka wa fedha 2006/2007, ujenzi wa jengo la mapokezi, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la famasi, jengo la maabara na jengo la upasuaji kupitia mradi wa KfW;

(ii) Kwa mwaka wa fedha 2008/2009, ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti kwa maana ya mortuary na uwekaji wa vigae (tiles) katika wodi zote;

(iii) Kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ujenzi wa jengo kwa ajili ya ndugu wa wagonjwa kusubiria yaani waiting bay;

(iv) Kwa mwaka wa fedha 2014/2015, ukarabati mkubwa wa jengo la upasuaji;

(v) Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ukarabati wa jengo la mapokezi, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la famasi, jengo la maabara, jengo la wodi ya watoto na ujenzi wa jengo la dawa za ziada la Halmashauri kwa maana ya buffer store;

(vi) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ujenzi wa kichomea taka (Incinerator) na shimo la kutupia kondo la nyuma la uzazi kwa maana ya placenta pit;

(vii) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ukarabati wa jengo la CTC linalovuja unaendelea kupitia ufadhili wa AMREF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kukarabati miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kadri upatikanaji wa fedha utakavyokuwa unaruhusu.
MHE. JOSEPH L. HAULE (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-

Hospitali na Vituo vya Afya vinatakiwa kukidhi viwango vya utoaji huduma kwa wagonjwa; lakini hospitali na Vituo vya Afya vingi havina viwango vya utoaji huduma.

Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuhakikisha Vituo vya Afya na hospitali vinakidhi viwango vya utoaji huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye maeneo mbalimbali ya vituo vya kutolea huduma za afya ili kukidhi viwango vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha viwango vya utoaji huduma za afya nchini, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018 na 2018/2019, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 285.17 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 67, ujenzi na ukarabati wa Hospitali za Wilaya tisa (9), Vituo vya Afya 304 na Zahanati 39. Vilevile, Serikali imejenga na kukarabati nyumba za watumishi wa afya nchini 301. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga shilingi bilioni 23.9 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri mpya 27 na ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya 52.


Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 8,444 wa kada mbalimbali za afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya afya, kuajiri wataalamu, kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba ili kuhakikisha vituo vya kutolea huduma vinakidhi viwango vinavyohitajika.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilitoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 67 za Halmashauri. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga shilingi bilioni 23.9 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 52 na Hospitali 27 za Wilaya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ni miongoni mwa Hospitali hizo 27 na imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta fedha za on call allowance kwa madaktari wanaofanya zamu hasa katika hospitali za Wilaya na vituo vya afya ambavyo mapato yake ni madogo kwani sasa ni zaidi ya miaka miwili fedha hiyo haijaletwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hapo awali Serikali iliweka utaratibu wa kulipa fedha za on call allowance kupitia Hazina, ambapo halmashauri ziliwasilisha orodha za madaktari na wataalamu wote wanaostahili kulipwa fedha za on call allowance. Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo hupeleka madai hayo Wizara ya Fedha na Mpipango. Hata hivyo utaratibu huo ulipelekea baadhi ya wataalam wasiyo waaminifu kutoa taarifa ambazo siyo sahihi na hivyo kusababisha madeni makubwa kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na hali ya kuwa na madeni makubwa yasiyo na uhalisia, halmashauri zilielekezwa utaratibu wa kuweka fedha za on call allowance kwenye mipango na bajeti zao ili kuweza kulipa stahiki hizi. Pamoja na kuweka fedha za on call allowance kwenye mipango na bajeti, ilibainika kuwa zipo halmashauri zenye uwezo mdogo wa kimapato hivyo maelekezo yaliyotolewa hospitali na vituo vya afya kutenga asilimia 15 kutoka kwenye mapato yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya kwa ajili ya kulipa motisha kwa wataalam ikiwa ni pamoja na on call allowance.
MHE. MARIAM N. KISANGI (K.n.y. MHE. BONNAH M. KALUWA) aliuliza:-

Barabara ya Segerea Sheli kupitia Seminari, Stakishari Polisi kwenda kutokea Majumba Sita ni suluhisho la Msongamano wa magari yanayopita barabara ya Segerea - Tabata kutokea barabara ya Mandela, lakini kwa sasa barabara hiyo haipitiki kwa kuwa daraja la Seminari liliondoshwa na maji ya mvua mwaka 2013.

Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kujenga daraja la Seminari ili kuondoa tatizo hilo na kurahisisha huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bonnah Moses Kaluwa, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja la Seminari Segerea liko katika barabara ya Majumba Sita Stakishari yenye urefu wa kilomita 2.93. Hapo awali usanifu wa kujenga daraja hili ulishafanyika. Hata hivyo, ipo changamoto inayotokana na mto kutanuka, hivyo inahitajika kufanyika stadi ya kina na mapitio ya usanifu wa awali ili kupata mahitaji halisi ya ujenzi wa daraja kutokana na changamoto hiyo. Mara baada ya kukamilika kwa mapitio ya usanifu na tathmini ya gharama, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kujenga daraja hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 TARURA imepanga kufanya usanifu wa kina wa daraja hilo ili kujua gharama halisi kwa maana ya cost estimates zinazohitaji kulijenga. Namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati Serikali inachukua hatua hizo muhimu kwa ajili ya kutatua tatizo la kukosekana kwa daraja hilo.
MHE. ESTER A. MAHAWE Aliuliza:-

Halmashauri ya Mbulu haina Hospitali ya Wilaya hivyo wananchi wa Kata za Gidhim, Yayeda, Ampatumat hutembea umbali mrefu kufuata huduma katika kituo cha Afya Dongobeshi.

(a) Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Kituo cha Afya Dongobesh ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Mbulu Vijijini na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Hydom?

(b) Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya, dawa na vifaa tiba katika kituo hicho cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Ester Mahawe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwe Mwenyekiti, Kituo cha Afya Dongobeshi kilianzishwa mnamo mwaka 1974 kipo kata ya Dongobeshi, kinahudumia jumla ya wakazi takribani 30,000 wa Tarafa ya Dongobeshi na wakazi wa maeneo jirani wakiwemo wananchi wa Kata za Gidhim, Yaeda na Amputamat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kituo hiki, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha kwa lengo la kuboresha miundombinu pamoja na huduma za afya zitolewazo kwenye kituo hiki. Mwezi Machi, 2018 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ambayo ujenzi wake umekamilika hivi karibuni. Majengo hayo ni wodi ya Mama na Mtoto (Maternity and Pediatric Ward), jengo la upasuaji, jengo la maabara, nyumba moja ya mtumishi na jengo la kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuongeza idadi ya watumishi katika Kituo cha Afya cha Dongobeshi. Mwaka wa fedha 2017/2018 watumishi sita wapya wameajiriwa na kufanya kituo kuwa na jumla ya watumishi 37. Aidha, Serikali imetuma fedha bohari Kuu ya Dawa (MSD) jumla ya shilingi milioni 320 zikiwa ni kwa ajili ya kunua vifaa tiba, hadi sasa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 37 vimepelekwa kituoni hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa fedha 2018/2019, jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu inayojengwa katika Tarafa ya Dongobesh. Kukamilika kwa hospitali hii kutaondoa msongamano kwenye Hospitali ya Hydom. Kwa kuwa, Hospitali ya Wilaya inajengwa katika eneo la Dongobesh hakuna sababu ya Kituo cha Afya kilichopo sasa kupandishwa hadhi kuwa hospitali.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa Wilaya ya Kilindi haina Hospitali ya Wilaya lakini wanayo Hospitali ya Rufaa inayomilikiwa na Kanisa la KKKT, lakini watumishi wote na huduma zote za Hospitali hiyo zinagharamiwa na Halmashauri ya Wilaya (DED) na wao KKKT ni wamiliki wa majengo:-

Je, Serikali haioni imefika wakati wa kufanya makubaliano ya kununua Hospitali hiyo ili kupunguza gharama kwa Serikali ya kujenga Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2010 Serikali kupitia Halmashauri ya Kilindi iliingia mkataba na Kanisa la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa lengo la kutumia majengo yanayomilikiwa na kanisa hilo kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kilindi. Hospitali hiyo Teule ya Wilaya (DDH) ya Kilindi inahudumia wananchi wapatao 264,000. Serikali inatumia utaratibu huo ikiwa ni ushirikiano na Taasisi binafsi yakiwemo Mashirika ya Dini pale ambapo hakuna Hospitali ya Wilaya ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hospitali hiyo, Serikali inalipa mishahara ya baadhi ya watumishi walioajiriwa na Serikali na kupeleka fedha kwa ajili ya uendeshaji wa hospitali ambazo zinatumika kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, hospitali hiyo iliidhinishiwa shilingi 153,646,500/= kutoka Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo ni asilimia 25 ya fedha zote za Mfuko wa Afya kwa Hospitali ya Wilaya. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/2020, hospitali hiyo imetengewa jumla ya shiligni 153,646,500/= kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mpango wa kununua Hospitali ya Wilaya ya Kilindi inayomilikiwa na KKKT. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na Hospitali ya Halmashauri ya Serikali. Pale ambapo bado Serikali haijajenga, itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kama inavyofanyika sasa.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-

Barabara zinazotoka Kidiwa hadi Tandali, Daraja la Mgeta hadi Likuyu, Visomolo hadi Lusungi na Langali SACCOS hadi Shule ya Sekondari Langali Tarafa ya Mgeta Wilayani Mvomero zimejengwa kwa nguvu za wananchi, lakini bado hazipitiki kutokana na vikwazo vya miundombinu na madaraja:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hizo ili kuondoa adha wanazopata wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine T. Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kidiwa – Tandali – Maguruwe yenye urefu wa kilometa 13.8 imefanyiwa upembuzi yakinifu na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kubaini zinahitajika shilingi bilioni 2.81 kwa ajili ya matengenezo makubwa (Rehabilitation Works) kwa kiwango cha zege katika sehemu za maeneo ya milimani na ujenzi wa miundombinu ya madaraja. Serikali inaendelea na mpango wa kutafuta fedha kwa kizingatia uwingi wa fedha zinazohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 34.6 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum (Periodical Maintenance) kwenye barabara za kibaoni – Lukuyu na barabara ya Visomoro – Bumu – Mwalazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja (vented drift) katika Mto Songa.
MHE. SUSAN L. KIWANGA (K.n.y MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-

Kituo cha Afya Ujiji kinahudumia zaidi ya wakazi 20,000 lakini kituo hicho hakina mashine ya ultrasound.

Je, ni lini Serikali itapeleka mashine ya ultrasound katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Sungura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji imeidhinisha kiasi cha Shilingi 15,475,254.28 kupitia Mradi wa Malipo kwa Ufanisi (Result Based Financing) kwa ajili ya ukarabati wa chumba kitakachotumika kwa huduma za mionzi na shilingi 45,000,000.00 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa ultrasound. Fedha hizo zimepelekwa MSD kwa ajili ya taratibu za ununuzi wa kifaa hicho. Kwa sasa huduma ya Ultrasound inapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Maweni na Hospitali Teule ya Manispaa ya Baptist.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-

Hospitali ya Handeni inahudumia karibu Majimbo manne lakini ina upungufu wa vifaa ambao unasababisha wagonjwa wengi kupewa rufaa:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza vifaa ili watu wengi wapate huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayofaa katika Hospitali ya Mji Handeni kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 na 2017/2018 Serikali imeongeza vifaa tiba muhimu ambavyo ni; ultra sound, urine chemistry analyzer, gene expert machine na cryotherapy machine. Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya vifaa tiba kila mwaka na katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 fedha zitakazotumika kununua vifaa tiba katika Hospitali ya Handeni ni shilingi milioni 96 ikiwa ni ongezeko la shilingi milioni 20 ikilinganishwa na bajeti ya vifaa tiba kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kuondoa msongamano kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni, Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020 imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Handeni. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Vituo vya Afya vya Kabuku na Mkata vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 300 ili kuviwezesha vituo hivyo kutoa huduma bora. Serikali inazielekeza halmashauri kuendelea kutenga fedha kwenye bajeti zake kwa ajili ya ununuzi na ukarabati wa vifaa tiba.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya cha Kiagata kwani Wananchi wote wa Wilaya ya Butiama wanategemea Kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA Z A MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyeiti, katika mwaka wa fedha 2017/2028 Serikali iliidhinisha na kutoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha miundmbinu ya Kituo cha Afya cha Kiagati. Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba ya mtumishi, wodi ya wazazi, jengo la maabara, jengo la mionzi, jengo la kuhifadhia maiti na kichomea taka. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kupitia mapato yake ya ndani imetumia kiasi cha shilingi milioni 37.5 kwaajili ya kukamilisha miundombinu iliyosalia pamnoja na kununua Jokofu la kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, KItuo hicho cha afya kwa sasa kinatoa huduma za upasuaji wa dharura, huduma za ultrasound, huduma za Mama na Mtoto na kulaza wagonjwa.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-

Wastani wa akinamama wanaojifungua kwa siku ni 18 - 20 katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi; licha ya idadi kubwa ya akinamama wanaojifungua, kuna ufinyu wa majengo mbalimbali ikiwepo na wodi ya akinamama:-

(a) Je, ni lini Serikali itashughulikia ujenzi wa wodi ya akina mama katika hospitali hii?

(b) Hospitali ya Wilaya ya Mbozi inatumika kama Hospitali ya Mkoa wa Songwe na haina maji safi na salama. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya maji safi na salama katika hospitali hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imefanya tathmini na kubaini zinahitajika jumla ya shilingi milioni 37 kwa ajili ya upanuzi wa wodi ya akina mama wanaojifungua. Mradi huo umepewa kipambele katika mpango wa bajeti wa mwaka 2020/2021 ili kuanza ujenzi.

Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri imeidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 12 kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji katika hospitali ya Wilaya ya Mbozi ili kutatua changamoto ya maji katika hospitali hiyo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-

Moja kati ya maombi yaliyowasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati wa ziara yake Mkoani Ruvuma, katika Wilaya ya Songea ni zahanati za Mbangamawe na Magingo zilizoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba zitakapokamilika zipandishwe hadhi kuwa Vituo vya Afya kutokana na ukubwa wake na mahitaji kwa Wananchi:-

Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza jukumu hilo muhimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa akiwa ziarani Mkoani Ruvuma tarehe 05 Januari, 2017 katika Halmashauri ya Madaba alipokea maombi kutoka kwa wananchi ya kuiomba Serikali kuzipandisha hadhi Zahanati za Magingo na Mbangamawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini iliyofanyika imebaini kuwa ujenzi wa Zahanati zote mbili umefikia asilimia 45 kila zahanati ina jengo moja kubwa lenye vyumba 21 kwa kufuata ramani zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kabla ya mwaka 2010 kwa kuzingatia mpango wa MMAM. Vyumba 5 kati ya 21 kwa kila zahanati vimekamilika. Tathmini inaonyesha kuwa ili kukamilisha ujenzi kiasi cha shilingi milioni120 kinahitajika kwa zahanati ya Mbangamawe na milioni 100 kwa zahanati ya Magingo. Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha ili kukamilisha na kufuata taratibu zote zinazotakiwa ili kuzipandisha hadhi zahanati hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma za afya Madaba katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepatia Halmashauri ya Madaba kiasi cha shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati, ujenzi na upanuzi wa vituo vya afya vya Madaba, Mtyangimbole. Vilevile katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Madaba. Serikali inaendelea na jitihada za kujenga, kukarabati, kupanua na kuboresha miundombinu ya afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi haina Hospitali ya Wilaya na kuifanya Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi izidiwe na idadi ya wagonjwa:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili kujenga Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Moshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha taratibu za kukabidhi majengo na ardhi ya Kituo cha Afya Moshi Arusha kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ili kipanuliwe na kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Halmashauri. Baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu inayohitajika kwa hadhi ya Hospitali ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa sasa wananchi wa Manispaa ya Moshi wanapata huduma katika Hospitali Teule ya Mtakatifu Joseph ambayo inafuata miongozo ya Serikali kwa kutoa matibabu bure kwa wazee, watoto chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito.
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-

Kazi zote za Utawala na fedha katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya zinasimamiwa na Mganga Mfawidhi wa Wilaya wa eneo husika:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa elimu ya Utawala na Usimamizi wa Fedha Madaktari hao ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliajiri Wahasibu Wasaidizi 335 na kuwapanga kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuimarisha usimamizi wa fedha kwenye Vituo vya Afya kupitia mfumo wa kielektroniki wa Facility Financing, Accounting and Reporting System (FARS). Aidha, ili kukabiliana na upungufu uliopo wa wataalam hao wa utawala na usimamizi wa fedha, Waganga Wafawidhi katika Hospitali za Halmashauri, Vituo vya
Afya na Zahanati wamepatiwa mafunzo ya utawala na usimamizi wa fedha yaliyofanyika kuanzia tarehe 24 Desemba, 2018 hadi tarehe 22 Januari, 2019 katika kila Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwajengea uwezo wataalam hao kwenye masuala ya fedha na utawala katika vituo wanavyovisimamia. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imewasilisha maombi ya kibali cha kuajiri zaidi watumishi wa kada za Wahasibu Wasaidizi kwa lengo la kuimarisha utawala na usimamizi wa fedha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-

Watu wanaoishi na VVU wanapata shida sana katika kupata lishe bora na matibabu ya uhakika:-

(a) Je, Serikali imejipangaje katika kuwapa mikopo itakayowasaidia kuendesha maisha yao kupitia vikundi mbalimbali?

(b) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kutenga sehemu ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya kundi hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inatoa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa wagonjwa wote wanaoishi na VVU ili kuimarisha afya zao na kuwakinga na magonjwa nyemelezi. Aidha, kwa kuwa watu wanaoishi na VVU wanashiriki kama kawaida katika shughuli za ujenzi wa Taifa, Serikali inawanashauri waendelee kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi za kifedha ikiwemo pamoja na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na VICOBA.

Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri na kusisitiza watu wanaoishi na VVU kuitumia fursa ya mikopo inayotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi na jumuishi yatakayonufaisha makundi yote kiuchumi wakiwemo watu wanaoishi na VVU.
MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:-

Mji wa Mto wa Mbu ni mji wa kitalii na unaingiza mapato mengi ya kitalii; lakini unakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara;

(a) Je nini mkakati wa Serikali kuupatia Mji wa Mto wa Mbu angalau km 5 za lami?

(b) Je Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu mpaka Loliondo kwa kiwango cha lami ili kusaidia mradi wa kimkakati wa magadi Engaruka?

(c) Je ni lini Serikali itatimiza ahadi ya Mhe. Rais ya kuweka lami barabara ya Ngarasha mpaka Monduli Juu kwa Sokoine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini – TARURA imekamilisha usanifu wa barabara za Mji Mdogo wa Mto wa Mbu kwa kiwango cha lami zenye jumla ya urefu wa kilometa 9 ambazo ujenzi wake utagharimu jumla ya shilingi bilioni 7.32. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi ambao utafanyika kwa awamu.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mto wa Mbu – Loliondo ina urefu wa kilometa 247 na ipo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Serikali imeanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2019/20 kiasi cha Shilingi bilioni 87 kimetolewa kwa ajili ya kujenga kipande chenye urefu wa kilometa 49 na ujenzi umefikia asilimia 43. Serikali itaendelea kujenga barabara hii kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Ngarasha mpaka Monduli Juu kwa Sokoine yenye urefu wa kilometa 11.66 iko chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Wakala wa Barabara unaendelea na usanifu wa barabara hiyo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo unaotarajia kuanza pindi usanifu wa barabara hiyo utakapo kamilika.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. MARGARET S. SITTA) aliuliza:-

(a) Je, Serikali ipo tayari kuangalia bajeti ya Hospitali ya Wilaya ya Urambo ambayo inahudumia wananchi wa maeneo ya Kaliua, Ulyankulu na maeneo ya jirani ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma?

(b) Hospitali ya Wilaya ya Urambo ina majengo mawili ya ICU na maabara ambayo hayajakamilika tangu yalipoanza kujengwa 2011 kupitia utaratibu wa LGDG ya mradi wa ADB. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu ombi la wananchi wa Urambo la shilingi milioni 200 ambazo zinaweza kumaliza majengo hayo?

(c) e, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kuongeza wafanyakazi angalau Manesi 12 na Wafamasia 6 kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa Hospitalini hapo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Serikali imepanua Kituo cha Afya Ulyankulu, Kituo cha Afya Usoke na kujenga Kituo cha Afya Usoke Mlimani kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 1.2. Mpango huu utasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika vituo hivyo na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mradi wa ujenzi wa majengo ya upasuaji, ICU na maabara uliofadhiliwa na ADB haukukamilika kutokana na tatizo la kukisia chini ya kiwango gharama za ujenzi wa majengo hayo. Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa kutenga fedha kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa Fedha 2018/2019, jumla ya watumishi wapya 26 wa kada ya Wauguzi, Madaktari, Maafisa Tabibu, Mtaalam wa Mionzi na Maabara walipangwa kufanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo. Serikali itaendelea kuajiri na kuwapanga watumishi wa kada za afya kadri watakavyokuwa wakipatikana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Kati ya Kijiji cha Mbori na Kijiji cha Tambi upo mto ambao hujaa maji wakati wa mvua na kusababisha wananchi na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Tambi na Sekondari ya Matomondo kushindwa kuvuka:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja katika mto huo ili wananchi na wanafunzi waweze kuvuka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga katika mwaka wa fedha 2019/2020 kufanya usanifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja linalounganisha Vijiji vya Mbori na Tambi vilivyopo katika Wilaya ya Mpwapwa ili kurahisisha mawasiliano kati ya maeneo hayo. Kazi hiyo ya usanifu itakapokamilika itawezesha kujua gharama zinazohitajika ili kutafuta fedha za kuanza ujenzi wa daraja hilo.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-

Kituo cha Afya Kilwa Masoko kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi, upungufu wa dawa, upungufu wa vitanda, magodoro, mashuka, vifaa tiba, kipimo cha sukari, kipimo cha damu, uchakavu wa majengo na pia kituo hicho hakina gari la kubebea wagonjwa hali ambayo ni kero kubwa kwa wagonjwa wanaohamishiwa Hospitali ya Wilaya iliyo umbali wa zaidi ya kilometa 25:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto zinazokabili Kituo hicho cha Afya ili kuondoa adha kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kilwa Masoko kilipatiwa kiasi cha shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi ambapo ujenzi na ukarabati wa majengo sita ya kituo umekamilika. Aidha, baada ya ujenzi na ukarabati kukamilika, kituo kimepokea vifaa tiba mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma hususan za upasuaji ambapo hadi Oktoba, 2019 kituo kimepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 332,916,070/=. Hali ya upatikanaji wa dawa zote muhimu (Tracer medicine) katika Kituo cha Masoko ni asilimia 87.

Mheshimiwa Spika, kituo kina jumla ya watumishi 30 wa kada mbalimbali za Afya ikiwa ni upungufu wa watumishi 22. Kituo kina nafasi ya vitanda 55, vitanda vilivyopo ni 31 na mashuka 126. Idadi ya vitanda vilivyopo vinakidhi mahitaji kwani kwa sasa kituo kinapokea wagonjwa wa kulazwa angalau watano kwa siku. Kwa sasa Halmashauri ina gari maalum ambalo hutumika kubeba wagonjwa katika kipindi cha dharura.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta rasilimali fedha za kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kununua gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kilwa Masoko.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa muda mrefu imekuwa na maombi ya kupandishwa hadhi kwa Zahanati za Msarango, Longuo B na Shirimatunda kuwa Vituo vya Afya:-

Je, ni lini Zahanati hizo zitapandishwa hadhi kuwa Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Moshi ina jumla ya Zahanati 31, 12 za Serikali, tatu za Mashirika ya Dini na 16 binafsi. Vituo vya Afya viko 10. Viwili vya Serikali, kimoja cha Shirika la Dini na saba ni vya watu binafsi; na Hospitali nne zote za Mashirika ya Dini ambapo Serikali imeingia mkataba na Hospitali ya St. Joseph kuwa hospitali teule kwa maana ya CDH.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mwongozo wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) Kituo cha Afya kinapaswa kuhudumia wakazi kati ya 10,000 hadi 60,000. Zahanati inapaswa kuhudumia wakazi wasiozidi 10,000 na hospitali ina wakazi kuanzia 50,000 na kuendelea. Zahanati ya Msarango inahudumia wakazi 7,699, Longuo B wakazi 6,632 na Shirimatunda wakazi 4,485, hivyo, zinakosa sifa ya kupandishwa hadhi kuwa vituo vya afya.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inasisitiza kujenga Vituo vya Afya vipya badala ya kuhuisha Zanahati izopo ili kuendana na ubora wa miundombinu inayohitajika na pia kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya na siyo kupunguza zahanati zilizopo ili kuongeza Vituo vya Afya.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Shule ya Msingi Kambarage ni shule pekee katika Wilaya ya Liwale inayochukua watoto wenye mahitaji maalum (walemavu); lakini shule hiyo haina walimu wenye taaluma hizo na vilevile miundombinu ya shule hiyo sio rafiki kwa watoto wenye ulemavu:-

(a) Je, ni lini shule hiyo itapatiwa walimu wenye taaluma husika ili kukidhi mahitaji ya shule?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya shule hiyo ili iweze kukidhi mahitaji ya watoto hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kambarage ina wanafunzi 1,283 wavulana wakiwa 636 na wasichana 647. Shule inatoa elimu changamani ambapo wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wapo 10, wenye ulemavu wa akili kwa maana ya mtindio wa ubongo wapo watano na wenye ulemavu wa ngozi wapo watatu. Uwiano wa walimu na mwanafunzi unatofautiana kulingana na aina ya ulemavu wa wanafunzi. Ulemavu wa akili mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano, ulemavu wa kusikia mwalimu mmoja kwa wanafunzi tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kambarage ina walimu watatu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia na mwalimu mmoja kwa wenye ulemavu wa akili. Kwa uwiano huo walimu na wanafunzi ni wazi kuwa hakuna upungufu wa walimu kwa wanafunzi kwenye mahitaji maalum katika shule hiyo.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya tathimini ya miundombinu katika Shule ya Msingi Kambarage na kubaini kuwa kiasi cha shilingi milioni 50 kinahitajika kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu kwenye Shule ya Msingi Kambarage. Naielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Liwale kutenga fedha hizo kwenye bajeti zake zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kufanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu.
MHE. SUSAN L. KIWANGA Aliuliza:-

Jimbo la Mlimba lina mito mingi mikubwa inayotenganisha kata pamoja na vijiji.

Je, ni lini TARURA itajenga madaraja ya kudumu katika Kata ya Mbingu na Kijiji cha Chiwachiwa, Kata ya Igima na Kijiji cha Mpofu, Kijiji cha Ngajengwa (kwa Mtwanga), Kata ya Mchombe na Kijiji cha Igia, Kata ya Mofu na Kijiji cha Ikwambi, Kata ya Mbingu, Kata ya Utengule na Kijiji cha Ipugasa, Kata ya Kamwene na Kata ya Uchindile, Kata ya Msagati Kijiji cha Taweta na Kijiji cha Tanga, Kata ya Kalengakelu na Merela, Kata ya Mlimba - Sokoni na Kata ya Idete – Barabara ya Itikinyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kushughulikia ujenzi wa vivuko katika Halmashauri ya Kilombero hususani Jimbo la Mlimba. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilinunua na kuweka daraja la chuma katika Mto Kihansi linalounganisha Vijiji vya Chita, Idunda na Melera kwa gharama ya shilingi milioni 717.62. Kazi hiyo tayari imekamilika ikiwa ni hatua ya awali ya kuunganisha Kata za Chita na Kalengakele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2019/2020 TARURA imetenga kiasi cha shilingi milioni 127.94 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja/makalvati katika barabara za Miembeni - Vigaeni, Kichangani katika Kata za Mbingu, Namwawala - Mofu katika Kata ya Mofu, Iduindembo - Utengule katika Kata ya Utengule, Manyasini katika Kata ya Mlimba, Ngwasi - Uga katika Kata ya Kalengakelu na Uchindile.

Aidha, TARURA kwa kushirikiana na Mfuko wa Barabara (Road Fund) imeweza kutenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la mita 25 katika barabara ya Kisegese - Chiwachiwa - Lavena ambapo kwa sasa lipo katika hatua za upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha na kujenga barabara, madaraja na makalvati kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JOEL M. MWAKANYAGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuitengeza barabara inayounganisha kijiji cha Bwawani kilichopo Kata ya Manchali na Kijiji cha Ikowa kilichopo Kata ya Ikowa ili iweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshmiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-

Mheshmiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Chamwino imekuwa ikifanya matengenezo ya mara kwa mara ili kuwezesha barabara hiyo kupitika nyakati zote. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilifanyia matengezo barabra ya Chinangali II – Ikowa yenye urefu wa kilomita tatu kwa gharama ya shilingi milioni 14.15.

Mheshimiwa Spika, ili kuifikia barabara ya Chinangali II – Ikowa ni lazima kutengeneza kwanza barabara ya Mwegamile – Makoja - Ikowa na katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 114 kwa ajili ya kufanyia matengezo barabara ya Mwegamile –Makoja – Ikowa. Aidha, tathmini iliyofanywa na Wakala wa Barabra za Vijiji na Mijini (TARURA) imebainisha kuwa jumla ya shilingi milioni 668.2 zinahitajika kufanya matengenezo makubwa ambayo ndiyo itakuwa suluhisho la kudumu kwenye barabara ya Ikowa - Kiegea kwa maana ya Bwawani yenye urefu wa kilomita 12.3.

Mheshimwia Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imetengewa bajeti ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 1.2 ikiwa ni asilimia 82 ya bajeti. Baadhi ya barabara zilizotengenezwa ni barabara ya lami ya Chamwino Mjini, Haneti – Kwahemu- Gwandi na Zajilwa. Chinangali II – Chilowa na barabara ya Dabalo – Segela. Aidha, kwa mwaka fedha 2019/2020 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.366 kwa jili ya matengenezo ya barabara.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kuiwezesha TARURA kuimarisha mtandao wa barabara wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ikiwa ni pamoja na barabara inayounganisha Kijiji cha Bwawani – Ikowa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2018/2019, Serikali imeajiri watumishi 8,444 wa sekta ya afya nchini ambapo watumishi 45 walipangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepata kibali cha kuajiri watumishi 550 wa sekta ya afya na taratibu zinakamilishwa ili waweze kupangwa kwenye vituo vya kutolea huduma kote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-

Mkoa wa Rukwa una wilaya nne na hakuna Hospitali ya Wilaya:-

Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali za Wilaya katika wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imeupatia Mkoa wa Rukwa kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo ambapo kila Halmashauri imepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5. Vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, Mkoa wa Rukwa umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali za Halmashauri za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo, ambapo kila Halmashauri itapewa kiasi cha shilingi milioni 500. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 500 kimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-

Katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha sukari katika Jimbo la Rufiji, hata hivyo ardhi iliyokusudiwa kujengwa kiwanda hicho kwa sasa amepewa mwekezaji ambaye hana nia ya kujenga kiwanda hicho:-

Je, ni lini Serikali itaamua kutumia Sheria ya Ardhi Na. 113 na 114 kuichukua ardhi hiyo kutoka kwa mwekezaji na kuyapa Mashirika ya Umma ili kujenga Kiwanda cha Sukari Rufiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omar Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha sukari Wilayani Rufiji baada ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kukamilisha kazi ya kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa Wilayani Rufiji na maeneo mengine nchini. Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, kwa maana ya TIC, ilipata mwekezaji kutoka nchi ya Mauritius, Kampuni ya Rufiji Sugar Plant na Kampuni ya Agro Forest Plantations.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Rufiji Sugar Plant inategemea kuwekeza katika Vijiji vya Tawi hekta 6,600, Nyamwange hekta 1,728 ambapo Kampuni ya Agro Forest Plantation inatarajia kuwekeza katika Vijiji vya Muhoro Magharibi hekta 5,710 Muhoro Mashariki hekta 1,529 na Vijiji vya Chumbi A, B na C hekta 1,926.77. Taratibu za kupata ardhi kwenye Serikali zote za vijiji ngazi ya wilaya ilianza mwaka 1912 na kukamilika mwaka 1916. Nyaraka zote zimewasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo inaendelea na taratibu zake za kujiridhisha ili itoe hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi iliyofanywa na mwekezaji hadi sasa ni kupima mipaka ya maeneo husika, kuchukua sampuli za udongo katika vijiji vyote na kupima kiasi cha kemikali zilizopo ardhini kwa kuzingatia masharti ya kanuni za kilimo. Aidha, taratibu za uwekezaji zitaendelea baada ya kampuni hizi kupewa hatimiliki za ardhi kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati Serikali inaendelea kukamilisha taratibu hizi.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Halmashauri nyingi zina uwezo mdogo wa kujiendesha kwa kutumia mapato yake ya ndani.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha katika bajeti ili kuzisaidia Halmashauri kujenga hospitali na vituo vya afya badala ya kuziachia jukumu hilo Halmashauri pekee?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitekeleza mkakati wa ujenzi, upanuzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya kwenye Halmashauri mbalimbali nchini. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 na mwaka 2018/2019 Serikali imejenga, imekarabati na kupanua vituo 352 ikiwa hospitali tisa, vituo vya afya 304 na zahanati 39 vya kutolea huduma za afya nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 184.67.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 100.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali 67 za Halmashauri. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 10.4 kwa ajili ya ujenzi wa vituo 52 vya afya na shilingi bilioni 46.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 27 za Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha na kujenga vituo vya afya vya kutolea huduma kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. MARTHA M. MLATA) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga vizuri barabara za Kibaya - Urughu, Urughu – Mtekente na Mtekente – Ndago zilizopo Wilayani Iramba ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Moses Mlata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara za Kibaya – Urughu, Urughu – Mtekente – Kisonga na Mtoa – Kisonga – Ndago yenye urefu wa kilometa 61.46 zimekuwa zikifanyiwa matengenezo kwa nyakati tofauti ili kuhakikisha zinapitika nyakati zote.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 barabara ya Kibaya – Urughu ilifanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa urefu wa kilometa 16 kwa gharama ya shilingi milioni 40.8 na pia barabara ya Mtoa – Kisonga – Ndago ilifanyiwa matengenezo ya muda maalum kwa urefu wa kilometa sita na makalvati matatu yalijengwa. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 barabara ya Urughu – Mtekente – Kisonga ilifanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa urefu wa kilometa 12.5 kwa gharama ya shilingi milioni 53.3.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, jumla ya shilingi milioni 188.8 zimetengwa kwa ajili ya kujenga box culvert kubwa la midomo miwili katika Mto Mtekente, kazi ya ujenzi imeanza na inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2019. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020 kupitia TARURA barabara ya Urughu – Mtekente – Kisonga imetengewa kiasi cha shilingi milioni 224.3 kwa ajili ya ujenzi wa box culvert kubwa katika Mto Kisonga na barabara ya Mtoa – Kisonga – Ndago imetengewa kiasi cha shilingi milioni 18 kwa ajili ujenzi wa kufanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa urefu wa kilometa sita.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Serikali ina Mkakati gani wa kuhakikisha kuwa watumishi hewa hawapo katika payroll ya Serikali:-

Je, Serikali inadhibiti vipi mishahara ya watumishi wasiostahili kulipwa kama wastaafu, waliofariki, walioacha kazi na waliofukuzwa kazi katika Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHESHIMIWA JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2015 kumekuwepo na mkakati madhubuti wa kudhibiti uwepo wa watumishi hewa katika Mfumo wa Malipo ya Mishahara kwa Watumishi wa Umma nchini. Utekelezaji wa mkakati huo ulifanyika kuanzia mwaka 2016 kwa kuendesha zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi wote waliopo kwenye taasisi zote za Serikali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika uhakiki huo, watumishi wote ambao hawakuwa na sifa ya kulipwa mishahara waliondolewa mara moja katika Orodha ya Malipo ya Mishahara (Payroll).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti malipo ya mishahara kwa watumishi wasiostahili kulipwa kama vile wastaafu, waliofariki na waliofukuzwa kazi, Serikali imekuwa ikisitisha mara moja malipo ya mishahara ya watumishi wa aina hiyo kupitia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi (Human Capital Management Information System) na Mfumo wa Malipo ya Mishahara (Government Salary Payment Platform) pindi tu wanapokosa sifa ya kuendelea na Utumishi wa Umma. Mifumo hii inatumika katika Taasisi zote za Serikali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna udhibiti ulivyo hivi sasa na ufuatiliaji unavyofanyika, hakuna mtumishi anayeweza kulipwa mshahara bila kustahili. Aidha, naomba kutoa wito kwa Maafisa Masuuli katika Taasisi zote za Umma kuendelea kusimamia kikamilifu udhibiti wa malipo ya mishahara kupitia mifumo iliyopo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-

Kituo cha Afya kilichopo Kigoma Ujiji Manispaa kinahudumia wakazi zaidi ya elfu arobaini katika Kata kumi na moja za Manispaa lakini kina kinakabiliwa na ukosefu wa Chumba cha theatre, X-ray pamoja na Ultra Sound:-

Je, ni lini Serikali itakipatia Kituo hiki vifaa hivyo ili kusaidia wananchi hao wanaohudumiwa na Kituo hicho?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 24, hospitali mbili, vituo vya afya vinne, Zahanati 17 na Kliniki moja. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 45 za bakaa iliyopo MSD kununua mashine 1 ya Ultra sound.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020 Kituo kimetenga kiasi cha shilingi milioni 15.4 kupitia fedha za mradi wa malipo kwa ufanisi (RBF) kwa ajili ya ukarabati wa chumba kinachotumika kwa huduma za mionzi.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuitengeneza kwa kiwango cha kupitika muda wote wa mwaka barabara inayounganisha Kijiji cha Mbelezungu na Kijiji cha Majeleko vyote vikiwa ndani ya Kata ya Majeleko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mbelezungu – Majeleko yenye urefu wa kilometa 10 imeingizwa kwenye mtandao wa barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na hivyo kukidhi vigezo vya kufanyiwa matengenezo kupitia fedha za Mfuko wa Barabara. Aidha, tathmini ya barabara hiyo imefanyika na kubaini zinahitajika shilingi milioni 288.9.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuifanyia matengenezo barabara hiyo kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. SEIF K. GULAMALI) aliuliza:-

Wilaya ya Igunga ilipata ufadhili wa Benki ya Dunia wa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Simbo, Ziba, Chomachankola na Igurubi ambapo Vituo vya Afya vya Ziba, Chomachankola na Igurubi vimekamilika na vifaa tayari vipo japo majengo na vifaa katika Kituo cha Afya cha Chomachankola na Igurubi bado havijaanza kufanya kazi; Kituo cha Afya cha Simbo bado hakijakamilika na vifaa havipo na Wafadhii walishakabidhi Halmashauri bila kukamilisha ujenzi huo:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kujua nini kilichojificha juu ya Mradi huo kukabidhiwa bila kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Wilaya ya Igunga ilipata ufadhili wa Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya Simbo, Ziba, Chomachankola na Igurubi. Sababu kuu ya kushindwa kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati ilitokana na makadirio ya chini ikilinganishwa na gharama halisi za kukamilisha ujenzi. Ili kukamilisha ujenzi wa Vituo hivyo kwa kuzingatia ramani mpya, Serikali ilitoa jumla ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya Simbo na Igurubi ambapo kila kituo kilipatiwa shilingi milioni 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Simbo kimekamilisha ujenzi wa majengo ya upasuaji na nyumba ya mtumishi na sasa vifaa tiba vinaendelea kuletwa. Aidha, Kituo cha Afya Igurubi kinaendelea na ujenzi wa majengo manne ambayo ni Maabara, Jengo la Wazazi, Jengo la Kufulia na Jengo la Kuhifadhia maiti. Majengo yote haya yapo katika hatua za ukamilishaji.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Serikali ilikuwa na Mpango wa kuifanyia matengenezo makubwa barabara ya kutoka Mima kwenda Mkanana hadi Chibwegele, Mpango huo haujatekelezwa mpaka sasa.

Je, ni lini Serikali itatekeleza Mpango huo ili barabara hiyo iweze kupitika wakati wote bila matatizo kuliko ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mima hadi Mkanana yenye urefu wa kilomita 23 inaunganisha Kijiji cha Mkanana kilichopo Uwanda wa Mlimani na barabara ya Wilaya iitwayo Gulwe, Chitope inayoambaa uwanda wa chini wa safu za mlima. Barabara hii inahitaji matengenezo makubwa ya kuwekewa tabaka la zege katika sehemu yenye miamba na mlima kwa urefu wa kilomita tano, changarawe kwenye maeneo ya tambarare na ujenzi wa vivuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 99 kwa ajili ya kufanya matengenezo makubwa ya barabara ya Gulwe - Chitope yenye urefu wa kilomita 58.8 ambayo inaunganisha barabara ya Mima - Mkanana hadi Chibwegele, Makao Makuu ya Wilaya na Barabara kuu ya Iringa - Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa barabara ya Mima - Mkanana inafanyiwa matengenezo kwenye maeneo korofi kwa urefu wa kilomita tano kwa gharama ya shilingi milioni 42. TARURA imefanya tathmini ya kuikarabati barabara hiyo na kubaini kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.6 zinahitajika ili iweze kupitika katika nyakati zote. Hivyo, Serikali inaendelea kutafuta kiasi hicho cha fedha ili kuiwezesha TARURA kukamilisha kazi hiyo.