Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Josephat Sinkamba Kandege (34 total)

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo.
Kwa kuwa, katika swali la msingi suala zima linaloongelewa ni juu ya elimu na faida inayotokana na faida na ulipaji wa kodi. Kwa kuwa tumekuwa mashuhuda katika baadhi ya miradi ambayo inatekelezwa tukipata fedha kutoka kwa wafadhili nikitolea mfano wa barabara iliyojengwa kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga unakuta kuna vibao ambavyo vimeandikwa kwamba pesa hii imetokana na walipa kodi wa Marekani.
Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kwa ile miradi ambayo inakamilishwa kwa pesa ya ndani, vikawekwa vibao ili kuhamasisha ulipaji wa kodi kwamba miradi hii inatokana na ulipaji kodi ya Watanzania?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazo zuri na tutalichukua na tutalifanyia kazi. Hili ni jambo jema nafikiri.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza naomba nishukuru majibu ambayo yametolewa na Naibu Waziri na naipongeza Serikali kwa utendaji mahiri wa kazi ambazo zinakuwa zinaletwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, kwa kuwa, umuhimu wa barabara kwa suala zima la kiuchumi halina mbadala; na kwa kuwa, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa imeachwa nyuma kwa maana ya ukosefu wa barabara kwa kiwango cha lami, na kwa kuwa, umuhimu wa barabara kwa junction ya kuanzia Kangesa, kwenda Liapona, Kazila, unapita Mwaze pale anapotoka Muadhama Polycarp Pengo, hadi kwenda kufika Kijiji cha Mozi ambapo ndiyo customs, ni ya muhimu sana na iko chini ya TANROADS. Je, Serikali iko tayari kuiingiza katika mpango wa kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa katika bajeti ya 2016/2017 barabara hii haijaingizwa kwa ujenzi wa kiwango cha lami: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari nimkabidhi barua ya maombi maalum ili iingizwe katika mpango wa kuanza usanifu kwa 2017/2018?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kandege Serikali yake ya Awamu ya Tano ina Ilani ya uchaguzi na ahadi ambazo zimetolewa na viongozi wa Kitaifa. Naomba atupe fursa kwanza tuanze kukamilisha zile barabara ambazo tumeanza kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na hii barabara ambayo niliielezea kwa kirefu ambayo ipo katika Jimbo lake. Naomba sana hii sasa tuangalie huko mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, niko tayari, naomba niletewe hiyo barua maalum ili tukaijadili Wizarani na baadaye tuangalie kama tunaweza tukaiingiza katika miaka inayokaribia karibu tunaingia kipindi kingine, kama tunaweza kuikamilisha kufanya feasibility study na detailed design ili kuiandaa sasa ije ijengwe kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki cha miaka 10 ya Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni matarajio yangu makubwa kwamba, Serikali inakuwa na majibu ambayo hayabadiliki kutokana na muda. Swali kama hili nimeliuliza na Serikali ikakiri umuhimu wa barabara hii kwa sababu inaondoa takribani kilometa 100 na wakatutaka tutume ombi maalum. Je, ni lini Serikali itajenga kipande hiki ili barabara hii iendelee kutumika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipofika Kalambo kuja kuomba kura tarehe 25/8 akiambatana na Mheshimiwa Lukuvi, alimtaka Mkurugenzi atangaze haraka kabisa ujenzi wa kivuko cha Mto Kalambo kwa sababu ya umuhimu wake. Je, ni lini kandarasi hii itatangazwa ili kivuko hicho kiweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali huwa haibadilishi majibu yake na kwa jibu hili, tulimwambia awali kwamba alete ombi maalum, akileta swali jibu lake ambalo kwa kawaida linaletwa na wataalam wanaozingatia maombi na majadiliano yaliyoko mkoani na wilayani yatakuja kama yanavyokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ombi likiletwa maalum na kuna utaratibu wa kuleta ombi maalum, linaanzia wilayani, mkoani hadi TANROAD Taifa na hatimaye Serikali ndiyo huwa inaamua. Tukileta maombi kwa kuuliza maswali, tutajibiwa na wataalam kutegemea na taratibu ambazo zimepitia katika mikoa na wilaya hadi wakati huo. Naomba sana Mheshimiwa Kandege kama ambavyo tulimjibu katika jibu letu la awali, alete ombi maalum na Serikali italifikiria kwa utaratibu ule unaotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, naomba tuonane na Mheshimiwa ofisini, tutakuwa na wataalam tuweze kulijadili na hatimaye tumpe majibu sahihi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumepata ahadi zote za Mheshimiwa Rais na tumeziratibu vizuri na sasa tunazifanyia kazi na tutazitekeleza awamu kwa awamu (phase by phase). Ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili kama ifuatavyo:-
(a) Mpaka sasa Wizara imeweza kutoa leseni ngapi za utafiti wa madini katika Wilaya ya Kalambo?
(b) Kwa kuwa kuna taarifa kwamba kuna uwezekano mkubwa sana wa kupatikana mafuta hasa ndani ya Ziwa Tanganyika ambalo linafika mpaka Kalambo, je, Serikali imefanya jitihada gani za makusudi kuhakikisha kwamba utafiti huu unafanyika na kukamilika ili tuweze kupata mafuta ndani ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kwa ujumla wake?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu leseni ngapi tumetoa, eneo la Kalambo bado linafanyiwa utafiti mkubwa sana na Wakala wa Jiolojia. Mpaka sasa leseni ambazo zimeshatolewa katika eneo la Kalambo ni tano tu ambapo leseni tatu za uchimbaji ambazo zimetolewa kwa Kampuni ya Agricultural Fast Limited na leseni mbili zimetolewa kwa kampuni ya binafsi ambayo inaitwa Shamze Ahmed Limited ambazo ni za madini ya dhahabu. Hata hivyo, bado eneo hili linafanyiwa utafiti na hadi sasa kuna waombaji wengine wameomba leseni nne za uchimbaji ambao ni pamoja na Mheshimiwa Antony Chilumba ambaye ameomba leseni za utafutaji wa madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la utafutaji wa mafuta, ni kweli kabisa eneo la Ziwa Victoria, Ziwa Natron, Eyasi na mengine mpaka Wembere bado TPDC na makampuni mengine wanafanya utafiti. Kwa eneo la Ziwa Tanganyika bado hawajagundua mafuta pamoja na gesi kwa ajili ya kufanyiwa utafiti wa kina. Bado TPDC na makampuni mengine wanafanya utafiti na wako katika hatua nzuri za kuweza kubainisha kama mafuta yanapatikana au la. Namuomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, TPDC wanaendelea na ukaguzi ili kuona kama bado kuna mafuta maeneo ya Ziwa Tanganyika.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa sababu swali la msingi limeongelea kuhusiana na tatizo kubwa la umeme na Wilaya ya Kalambo ni miongoni mwa Wilaya chache ambazo zilikuwa na umeme sifuri, je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini wananchi wa Kalambo juu ya vijiji vile ambavyo havijapata umeme kupatiwa umeme kabla hatujaenda awamu ya III?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge wa Kalambo kwamba vijiji 24 vilivyobaki katika eneo la Kalambo ambavyo vilikuwa kwenye REA Awamu ya II vitakamilika ndani ya mwezi huu, siku 10 zilizobaki kwa mwezi wa Juni. Hata hivyo, vijiji ambavyo vimebaki ambavyo ni nje ya vijiji hivyo vitaendelea kupatiwa umeme katika Mradi wa REA unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika bado TANESCO inaendelea kusambaza umeme kama kawaida. Kwa hiyo, vijiji ambavyo vitakuwa bado havijapitiwa umeme kwenye vitongoji vyake kwa umeme wa underline transformer ambao utakuwa unashusha umeme kwenye vijiji na vitongoji Mheshimiwa wa Kalambo bado vitapatiwa umeme. Tunataka kufikia 2025 vijiji vyote, kama nilivyokwisha kusema, vya Watanzania vitakuwa vimepatiwa umeme pamoja na vijiji vyote vya Jimbo la Kalambo.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali ambayo kimsingi sijaridhika sana, naomba kwanza niifahamishe Serikali kwamba maporomoko ya Kalambo ni ya pili Afrika yakifuatiwa na maporomoko ya Victoria. Kwa hiyo, yana unyeti na upekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuifahamisha Serikali, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mazungumzo yalikuwa yameshaanza kati ya Halmashauri ya Kalambo na TANAPA wakijua umuhimu wa maporomoko haya. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuhakikisha kwamba anayasukuma mazungumzo haya na ili maporomoko ya Kalambo yapandishwe hadhi na kuchukuliwa na TANAPA? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa maporomoko ya Kalambo yapo mpakani mwa Tanzania na Zambia na wenzetu wa upande wa Zambia wamekuwa wakiyatumia na kuyatangaza maporomoko haya na wakinufaika pamoja na kwamba scenery nzuri iko upande wa Tanzania. Je, Serikali iko tayari kuweka mkakati mahsusi kuhakikisha kwamba maporomoko haya yanafanyiwa promotion ya pekee?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza la mazungumzo yaliyokwishafanyika awali kati ya TANAPA na Halmashauri ya Wilaya inayohusika lakini akihusianisha na umuhimu wa maporomoko haya yakiwa ni ya pili kwa ukubwa na umaarufu katika Afrika, napenda niungane naye kusema kwamba mazungumzo yakianza ni sharti yakamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe pia kuhusu kuwa maporomoko haya ni ya pili kwa ukubwa na umaarufu Afrika, Wizara inayo taarifa hiyo. Hata hivyo, nimfahamishe tu kwamba, tukisema bado yatasimamiwa chini ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) haimaanishi kwamba tunayashusha hadhi wala haimaanishi kwamba tutapunguza kasi na nguvu ya kuyatangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa nimesema kwamba suala hili ni kwa mujibu wa sheria, Hifadhi za Taifa zina tafsiri yake kama ambavyo nimesema hapo awali na kwamba misitu ama maporomoko haya ambayo yapo ndani ya msitu tuliouzungumzia kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa hivi yenyewe hayawezi kuwa Hifadhi ya Taifa kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikubaliane na Mbunge kwamba nakwenda kufanya rejea ya mazungumzo yaliyokwishafanyika kwamba nini kilizungumzwa, tuliamua nini hapo nyuma ili kutotoka nje ya mazungumzo, lakini kwa sasa hivi mpaka nitakapokwenda kuona mazungumzo hayo msimamo ni kwamba, Hifadhi za Taifa zitabaki kuwa Hifadhi za Taifa na misitu itabaki kuwa misitu na itasimamiwa kwa sheria zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kuweza kufanya promotion ya pekee, hili nakubaliana nalo moja kwa moja na namwomba Mheshimiwa Mbunge nikitoka hapa hebu tukutane, inawezekana ana maoni mazuri zaidi kuliko hiki ambacho Serikali imefanya. Nakiri kabisa siyo tu kwa maporomoko haya bali kwa ujumla wake kutangaza vivutio vya utalii ni jukumu la Serikali na kwamba tunapaswa kuboresha namna ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote ili tuweze kufanya vizuri zaidi ili vivutio vyetu viweze kufikiwa na watalii kwa wingi na kuongeza pato la Taifa.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu kuuliza maswali mawili ya
nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wakati naandika swali hili, nilitaka lijibiwe na Wizara ya Fedha na si kwamba nilikuwa nimekosea kwa kuitaka Wizara ya Fedha ijibu swali hilo.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika na Serikali wanakiri pale ambapo mwekezaji unampunguzia badala
ya kulipa asilimia 25 akalipa asilimia 10 maana yake hiyo ni pesa ambayo ingeweza kwenda kwa Watanzania, ni tax ambayo ilitakiwa kuwa imekusanywa, haikukusanywa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, isingekuwa busara nafasi hiyo inekuwa imetolewa kwa Mtanzania awae
yeyote ambaye ananunua mabasi ya aina hiyo either anapeleka Mwanza, anapeleka Sumbawanga akaweza
kupata fursa kama hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, katika utaratibu wa Serikali kujenga barabara hizi kwa awamu ya kwanza
ambayo imeshakamilika sasa tunaenda awamu ya pili na mpak aya tatu, ni wazi kwamba Serikali itaendelea kuwekeza na katika hali ya kawaida ili muweze kugawana lazima kila mmoja aoneshe rasilimali ambayo amewekeza. Je, ni busara kwamba pamoja na uwekezaji ambao utaendelea kuwekwa na Serikali, bado mwekezaji huyu aendelee kumiliki asilimia 51 na Serikali ibaki na asilimia 49?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri Mheshimiwa Jafo, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kandege kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tufahamu kwamba mradi huu kwa nature yake ni PPP ni Public Private Partnership na kwa sababu ni PPP na kusema ukweli sisi hatuna uzoefu mkubwa sana wa miradi ya PPP hapa nchini, lakini PPP hii ni PPP ambayo kusema ukweli inagusa the public direct, kwa maana ya usafiri wa wananchi wa Dar es Salaam lakini PPP hii ni PPP ambayo inawahusisha kampuni ya Kitanzania na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la misamaha ni kweli jambo limekuwa likipigiwa kelele kuhusu misamaha.
Ipo misamaha mingi imetolewa na Bunge limekuwa likisema juu ya suala la misamaha. Lakini huu ni msamaha wa aina yake, tena ni kwa eneo ambalo linaleta unafuu kwa wananchi hao hao. Sasa mimi nimuombe tu Mheshimiwa
Kandege aje tumpe details zaidi za suala hili. Pengine swali hili aliliuliza muda mrefu uliopita kwa hiyo limeshabadilika sana na tumekwenda mbali zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili ameuliza je, katika mwendelezo wa hatua zingine zinazofuata za uendelezaji wa mradi huu, umiliki wa kampuni hii binafsi na Serikali utabakia asilimia ile ile?
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema tu kwamba katika hiyo asilimia 51 na asilimia 49 ni katika mradi huu wa
awamu hii kwa sababu ni kampuni inayoundwa na Serikali kwa maana ya Simon Group na Serikali wameunda kampuni inayo-operate mabasi haya ya UDART ambayo yanafanya usafiri Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unaona Serikali katika kila hatua imo na ndiyo maana tusipokuwa makini na jambo
hili sio watu wote wanalipenda na hasa wenzetu. Kwa hiyo, ninaposema wenzetu sina maana upande wowote wa Bunge hapana, nina maana nje kwasababu wangependa PPP ya aina fulani. Nadhani mmenielewa.
Kwa hiyo, niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge, hii ni PPP nzuri ambayo kila kitu kinabaki hapa hapa ingelikuwa
ni kampni imetoka Bogota imetoka wapi, hapo ndio lakini hii ni PPP nzuri na ninaomba sana kama Jiji waliuza hizi asilimia 51 na Serikali tumeweza ku-acquire, kwanza ilikuwa zaidi ya hapo; tumeweza ku-acquire back karibu hizi 49%. Tuendelee lakini ni kwa hatua ya awamu hii tu ndiyo wameshinda hii tender ya kuendesha hii na awamu zinazofuata na zenyewe zitakuwa procured kwa utaratibu mwingine.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la moja. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri ameonesha utayari wa kutembelea vivutio mbalimbali na kimsingi hajakuwa na ziara hivi karibuni ya kutembelea Nyanda za Juu Kusini ili akajionee maporomoko ya pili Afrika ya Kalambo pamoja na Ngome ya Bismark iliyoko Kasanga. Je, katika mwezi huo Agosti aliojipanga atatembelea na Nyanda za Juu Kusini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukanda wa Kusini ni eneo ambalo sasa hivi kama Taifa tunaliangalia kuwa ni eneo la kupanua shughuli za utalii nchini kwa maana ya kufanya kwamba utalii sasa unakwenda kila eneo nchi nzima na si upande wa Kaskazini peke yake. Kwa hiyo, kwa ufupi jibu ni kwamba; kipindi hicho kitakapofika tutatembelea pia Ukanda wa Kusini ikiwa ni pamoja na maporomoko ya Kalambo.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali. Kwa kutambua na kukiri umuhimu wa mradi huu, naomba nipatiwe majibu; lini mradi huu utakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba commitment ya Serikali kwamba hiyo 2018/2019 hakika pesa itatengwa kwenye bajeti.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na swali la Mheshimiwa Mbunge kwamba lini utakamilika, mradi huu kujua ni lini utakamilika ni baada ya kukamilisha usanifu na kuingia mikataba ndipo tarehe itapangwa, kulingana na scope ya kazi itakayojitokeza ndiyo tutajua ni lini mradi utakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni commitment. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu iko commited kuhakikisha kwamba inanyanyua kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kuondokana na njaa. Na Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo inazalisha chakula kwa wingi, kwa hiyo kwa mikoa hii Serikali iko commited kuhakikisha kwamba tunaendeleza kilimo cha umwagiliaji; tutahakikisha kwamba bajeti hii tunaitenga.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika awamu iliyotangulia Wilaya ya Kalambo ilipatia umeme vijiji vichache sana kutokana na scope ya kazi iliyokuwa imetolewa. Je, Serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba vile vijiji ambavyo vilikuwa viwe kwenye REA Awamu ya Pili vinaanza kuwekewa umeme haraka iwezekanavyo, ikiwepo kijiji cha Mwazi ambacho tayari transfoma iko pale ni suala la kushusha umeme pamoja na kijiji cha Kazila? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri ni shuhuda, tulienda naye, akaenda kijiji cha Samazi na Ukanda wa Ziwa Tanganyika, miundombinu ya kule alikiri jinsi ambavyo iko haja kubwa ya kuhakikisha kwamba umeme unafika maeneo yale.
Je, yupo tayari kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinapatiwa umeme haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kandege tumetembea naye kwenye Jimbo lake, hakika wananchi wa Jimbo lako Mheshimiwa wanafarijika sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maswali yake mawili ya nyongeza, kweli katika Jimbo la Kalambo ni vijiji 12 tu vilipitiwa na vyenyewe tulipeleka kwenye vituo tu vya umeme, sasa nikuhakikishie Mheshimiwa Kandege, vijiji 89 vyote vilivyobaki, ikiwemo kijiji cha Jengeni, Nondo, Santa Maria, Legeza Mwendo na vingine vyote ninakuhakikishia kwamba vitapelekewa umeme sasa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili ninahakikisha vipi. Hatua ya kwanza kabisa tumempelekea mkandarasi, hivi sasa Mkandarasi Nakroi ameishaonana na Mheshimiwa Mbunge na ataanza sasa jitihada za kuendelea katika Jimbo lako la Kalambo. Nikuhakikishie kwamba ataanza na maeneo ambayo tayari kuna transfoma kazi iliyobaki sasa ni kuwasha na ataanza na kuwasha. Katika eneo la Santa Maria pamoja na kwamba msishindane na lenyewe itapelekwa transfoma ili umeme uanze kuwaka mara moja. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa kulikuwa na mpango ambao ulisemekana kwamba Serikali ilikuwa inanunua meli tatu Korea Kusini na sasa hivi katika majibu ambayo yanatolewa na Serikali ni kama mpango ule umekufa kabisa.
Je, Serikali ituambie ina mpango gani kuhakikisha kwamba hizo meli ambazo zilikuwa zinunuliwe kutoka Korea Kusini zinanunuliwa na kupelekwa katika maziwa yote matatu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mhimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tulikuwa na mazungumzo na Serikali ya Korea na mimi nilikaa miezi miwili iliyopita nilizungumza na Balozi wa Korea na mazungumzo hayo bado yanaendelea, lakini itategemea hasa Exim Bank ya Korea itaamua vipi ndiyo tutaendelea na utaratibu huo.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa umuhimu wa barabara ya kutoka Matai kwenda Kasesha ni sawa sawa kabisa na umuhimu wa barabara iliyouliziwa katika swali la msingi, na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana alipata nafasi ya kwenda kutembelea barabara hii na akaahidi kwamba mkandarasi angetafutwa ili ujenzi ufanyike, na kwa kuwa pesa ilitengwa katika bajeti iliyopita, jumla ya shilingi bilioni 11 na ujenzi huo haukufanyika, je, Serikali iko tayari kuwahakikishia wananchi wa Kalambo kwamba ujenzi wa barabara hii utafanyika hivi karibuni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Waziri wangu Profesa Makame Mnyaa Mbarawa alitembelea katika eneo hili, na kwa namna alivyoona mazingira ya barabara hii ya Matai hadi Kasesha alitoa ahadi kwamba hii barabara ataishughulikia. Nimhakikishie Mheshimiwa Kandege na wananchi wa Kalambo hasa wale wanaoguswa na barabara hii ya Matai hadi Kasesha, kwamba Wizara yetu tumeshapokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na kazi inafanyika ili kuhakikisha ahadi au dhamira ya Mheshimiwa Waziri inakamilika kwa kuhakikisha kwamba tunafuata taratibu za kupata fedha za kujengea barabara hii ili ipitike vizuri zaidi.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Naomba niulize swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba uwepo wa taasisi kama NRFA na Bodi ya Mazao Machanganyiko ni pamoja na ku-act kama price stabilizer.

Je, ni hatua gani ambayo Serikali imechukua ili chombo hiki kiweze kutoa pesa na uwezo mkubwa ili kinunue mazao kwa wananchi tukijua kabisa kwamba majadiliano ya kupata guarantee Serikalini imechukua muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Kandege, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wizara, tumeendelea majadiliano na hazina, lakini vilevile katika kipindi cha hivi karibuni taasisi yetu ya CPB imeweza kupata fedha kutoka katika mifuko ya hifadhi ya jamii zaidi ya bilioni saba na fedha hizo wameshaanza kurudisha kwa hiyo, wamekuwa credible na wameonesha proper business plan. Bado tunaendelea na maongezi na wenzetu wa Hazina na tutapata solution.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna maongezi na Benki ya CRDB na NMB katika ku-finance miradi ya CPB ya kununua mazao kwa kutumia collateral management system badala ya kusubiri kibali kutoka Hazina. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mazungumzo yetu yako katika hatua nzuri na tutafikia kule ambako siku zote yeye toka akiwa Kamati ya Bajeti akisukuma tutafika huko Mwenyezi Mungu akijalia hivi karibuni, Inshallah. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. pamoja na majibu mazuri na maelezo mazuri ni ukweli usiopingika kwamba, tatizo la maji katika nchi yetu ni tatizo kubwa na kama ambavyo Mheshimiwa Aida amesema kuhusiana na matumizi ya Ziwa Tanganyika. Je, sio wakati sahihi kwa Serikali kuhakikisha kwamba, Mkoa wote wa Rukwa, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Songwe unaanza kutumia chanzo cha uhakika cha Ziwa Tanganyika, ili kupata maji maeneo yote? Kwani imethibitika kabisa matumizi ya maji kutoka Ziwa Victoria yamekuwa ni ufumbuzi mkubwa katika maeneo mengi, sasa si wakati muafaka kwa hiyo mikoa niliyoitaja kutumia chanzo hicho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Kandege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu awali, tayari Wizara tuna mikakati ya kuona maziwa yote ambayo yanapatikana katika nchi yetu tunakwenda kuyatumia kikamilifu katika kutatua tatizo kubwa la maji katika mikoa inayohusika. Hivyo mikoa yote ambayo inapitiwa na ziwa hili tutakwenda kuifanyia kazi na hakuna mkoa utakaorukwa, tutagawa maji kulingana na bomba litakavyopita kadiri mradi utakavyosanifiwa, ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa sababu, iko study ambayo ilifanyika enzi za mkoloni kwamba, kuna umuhimu wa kujenga reli kuanzia Tunduma kwenda Kasanga, lakini kwenda mpaka Ziwa Nyasa kwa maana ya Kyela na study hiyo iko NDC hadi leo ninavyoongea. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufuatilia study hiyo ambayo ilifanywa na mkoloni na akaona viability ya mradi huo ili sasa ianze kutekeleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, Mheshimiwa Rais ambaye wakati ule alikuwa Makamu wa Rais, wakati amekuja kuomba kura kwa ajili ya CCM, katika mahitaji ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa ilikuwa ni pamoja na ujenzi wa kipande hicho cha reli na akasema amepokea na ambaye leo ndio ndio Rais; na kwa kuwa mahusiano yetu na Serikali ya China hayana shida hata kidogo na kwa sababu, wao ndio walitusaidia katika ujenzi wa Reli ya TAZARA. Je, Serikali haioni umuhimu uleule ili tutumie window ya uhusiano mzuri na China ili vipande hivi viweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, study aliyosema Mheshimiwa Mbunge ya mkoloni ni wazi kwamba haiwezi ikatumika kwa sasa. Kitakachofanyika inaweza kuwa tu ni kufanya review ya hiyo study kwa sababu, mazingira yamebadilika sana. Pia kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi ni kwamba, miradi hii ni miradi ambayo inahitaji fedha nyingi sana. Ikumbukwe tu kwamba, kwa sasa hivi kipaumbele cha Serikali ya Tanzania ni kujenga reli ya SGR Awamu ya Kwanza kutoka Dar-es-Salaam mpaka Mwanza ambayo nina hakika ikishakamilika tutakwenda na awamu nyingine. Kwa hiyo, kama Serikali hasa kwa kulingana na ufinyi wa bajeti, naamini hatuwezi kwenda na miradi yote miwili. Ndio maana nimesema upembuzi yakinifu utatuambia gharama ni kiasi gani, ili huo mradi uweze kuanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kandege, Mbunge wa Kalambo ameeleza pia kwamba, Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba, ujenzi huu uweze kufanyika wa reli na ilikuwa ni ahadi. Nakubaliana naye na hatusemi reli hii haihitajiki kujengwa. Tunachosema ni kwamba, tutakwenda kwa awamu na study ndio itakayotuambia gharama iliyopo, lakini pia itazingatia na vipaumbele vya Taifa, tuanze nini tumalizie na nini. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pamoja na majibu ya Serikali naomba niulize maswali madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; hii hadithi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege Sumbawanga ni hadithi ya muda mrefu na wananchi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu. Sasa naomba kupata majibu ya Serikali ni nini ambacho kinakwamisha upatikanaji wa fedha kwa sababu tumekuwa tukisubiri muda mrefu ili ujenzi huu uanze mara moja? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa sababu ujenzi wa uwanja ulioko Sumbawanga uko katikati ya Mji na kwa kuliona hilo Serikali iliamua kwa makusudi mazima kutenga eneo lingine na si kama airstrip kama ambavyo Naibu Waziri amejibu. Aliyekuwa Makamu wa Rais Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Dkt. Ghalib Bilal alifika eneo la Kalambo na kuweka jiwe la msingi ili eneo lile liendelee kulindwa. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba eneo lile halivamiwi ili itakapofika wakati wa kujenga uwanja mkubwa kusiwe na haja ya fidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotoa maelezo yangu kwenye jibu la msingi ni kwamba jambo hili linafanyiwa kazi na Mheshimiwa Kandege anafahamu taratibu za Serikali, kama jambo ni makubaliano ya kimkataba lazima yakamilike. Hata hivyo, nipokee hoja yake kama kweli kuna ucheleweshaji tutalifanyia kazi ili uwanja huu ukamilike kama ambavyo tumeahidi kwenye jibu letu hapa kwa niaba ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipokee ushauri wake wa pili kwamba eneo hili ni kweli kwamba juzi nilikuwa Mtwara, hoja mojawapo iliyopo kule ni kwamba wananchi wamesogea karibu na eneo na wahitaji kulipwa fidia ambayo ni gharama nyingine kubwa tena kwa Serikali. Eneo hili litasimamiwa, lipimwe liwekwe mipaka na vizuizi ili libaki kwa matumizi ambayo limekusudiwa na wananchi wasianze kugombana na Serikali kwa kudai fidia ambayo itaongeza gharama pia katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri yanayotia matumaini ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hizi Tarafa ambazo zimetajwa zenye Mahakama kwa maana ya majengo; Mahakama kujenga ni jambo moja na kutoa huduma ni jambo la pili: Je, Serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba Mahakimu wanakuwepo muda wote katika hizi Tarafa nne ambazo zina Mahakama tayari? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mahakama ya Wilaya ya Kalambo sasa hivi wanatumia jengo la CCM na hivyo sisi kama CCM tunaona kama wanatunyima mapato: Je, Serikali ipo tayari katika mpango wa kujenga Mahakama za Wilaya, Wilaya ya Kalambo ikapewa kipaumbele kujenga Mahakama ya kisasa yenye kulingana na hadhi ya Wilaya yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Kandege, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu masuala ya watumishi, Mahakimu. Ni mpango wa Mahakama kuendelea kuongeza idadi ya Mahakimu ili waweze kutosheleza ingawa kwa kweli bado watumishi ni tatizo kubwa katika sekta mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni la kuhama kwenye majengo ya CCM na kurudi kwenye majengo ya Mahakama. Kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi ni kwamba tunao mkakati ambao kufikia 2025/2026 nchi nzima, Makao Makuu ya Wilaya zote yatakuwa na majengo mapya ya Mahakama zetu na Makao Makuu ya Tarafa zote nchini yatakuwa yamepata hayo majengo. Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa awe mvumilivu kidogo. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba pia nishukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali yanakiri kwamba upembuzi yakinifu ulifanyika mwaka 2018 ambapo aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye ndiye Rais wa sasa naye alikuja kutoa ahadi. Swali; natakiwa kuikumbusha mara ngapi Serikali ili ujenzi uanze?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni ukweli usiopingika kwamba pale ambapo maeneo yetu na mikoa yetu inapopata fursa ya kutembelewa na viongozi wa Kitaifa kuna mambo ambayo tunanufaika ikiwa ni pamoja na ahadi za viongozi hao wa kitaifa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba hawa viongozi wa kitaifa wanapangiwa ziara ili kutembelea mikoa yote ili na sisi tuweze kufaidika katika ahadi ambazo wanatoa viongozi hao?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tunakubaliana na mawazo yake Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli Serikali imeshafanya kazi ya awali ya kuandaa detail design na imeshakamilika; na kama ambavyo nimemjibu katika swali langu la msingi hapa, nilimwambia kwamba sasa hivi kazi ambayo tunaifanya Serikali ni kutafuta fedha tu ili daraja hilo lianze kujengwa, hicho kivuko ambacho tumekitaja hapo. Kwa hiyo nimwambie tu kwamba hahitaji kuikumbusha Serikali mara kwa mara kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali makini inakumbuka kila ahadi ambayo tumeitoa. Kwa hiyo na kwenye hili nimwondoe shaka kabisa kwamba fedha itakapopatikana tutakamilisha ujenzi huo, na ninaamini ndani ya kipindi hiki cha miaka 5 ya Mheshimiwa Rais wetu tutalitekeleza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili linalohusu ziara za viongozi, ninaamini hapa anazungumzia Mawaziri, Naibu Mawaziri, na hususan Ofisi yetu ya Rais TAMISEMI. Nimuahidi tu kwamba nitafika katika eneo lake na tutafanya ziara ya pamoja kwenda kujionea shughuli za kimaendeleo zinazofanyika eneo lile ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi naomba nikiri majibu ya Serikali ni majibu mazuri sana ya kutia matumaini kwa wananchi wa Kalambo. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Tumaini la kuanza kujenga barabara hii limechukua muda mrefu na barabara hii itapita maeneo ambayo wananchi wanahitaji kupata fidia.

Swali la kwanza je, Serikali itakuwa tayari kuhakikisha kwamba kwa sababu imechukua muda mrefu unafanyika tathmini ili wananchi waweze kulipwa haki zao kwa mujibu wa kipindi cha leo?

Swali la pili je, Serikali imejiandaa kuanza kulipa fidia lini ili ujenzi ukamilike maana nimeambiwa kwamba iko kwenye vetting na AG namuona hapa naamini hata chelewesha katika hilo?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kandege kama ifuatavyo. Tutawalipa wananchi wote ambao watapitiwa na barabara kwa mujibu wa sheria Na. 13 ya mwaka 2007 Serikali itafanya hivyo.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kutenga na kuanza kujenga vyuo vya ufundi ni jambo jema, lakini ipo haja ya kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinaanza kufanya kazi. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba vyuo vinapomalizika kujengwa na vifaa vya kufundishia vijana vinakuwa vinapatikana?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa sababu wananchi wa Kalambo wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu ujenzi wa chuo, je, ujenzi huu utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikamilisha au tunakamilisha ujenzi wa vyuo 25 katika wilaya 25 pamoja na vile vya mikoa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeweza kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa pamoja na samani ili vyuo hivi viweze kuanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo. Tunatarajia kama mambo yote yatakwenda sawasawa kunako Januari vyuo vile ambavyo vitakuwa vimekamilika au tunavyokamilisha hivi sasa vitaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, kwa upande wa kule Kalambo, tayari Serikali tupo katika mchakato wa kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo hicho. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi, ndani ya quarter hii ya pili tutahakikisha tunapata fedha hizi ili ujenzi wa Kalambo uweze kuanza mara moja. Nakushukuru sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa sababu miradi mingi ambayo Serikali inaiongelea ni ile ambayo ilijengwa miaka ya zamani na teknolojia ambayo imekuwa ikitumika ni ile ambayo ni ya mifereji ambayo inatumia maji mengi sana na inaharibu maji unnecessary. Kuna teknolojia mpya ambayo inatumika na tunaona katika nchi za jirani. Je, Serikali iko tayari kwenda kutumia teknolojia mpya ambayo inatumia maji kidogo lakini inakuwa na ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Kandege, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama Serikali tupo tayari kuendelea kutumia teknolojia ambayo italeta ufanisi katika kilimo cha umwagiliaji na hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na mimi mnatuona pale ni vijana ambao pia ni wa kidigitali, kwa hiyo tutahakikisha ya kwamba tunapitia kuona mifumo mbalimbali hasa yenye kuleta ufanisi ambayo naamini kabisa kama ni mfumo ambao Mheshimiwa Mbunge ameuzungumza hapa ambao utaleta tija kwa wakulima wetu sisi tuko tayari kuutumia mfumo huu na tutaelekeza pia Tume ya Umwagiliaji kuhakikisha kwamba inafanya utafiti wa kugundua teknolojia mbalimbali ili kumletea tija mkulima wetu wa Tanzania. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninaomba niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri ambayo yamesheheni taarifa za kutosha. Naomba niulize maswali madogo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba pamoja na hayo madini ambayo yametajwa kwa idadi kubwa shughuli ya uchumi kwa maana ya uchimbaji haijaanza kufanyika, na hii inawezekana ni kwa sababu hamasa na elimu haijatolewa kwa ajili ya wananchi kuweza kuchimba.

Je, Serikali iko tayari kutoa hamasa na elimu ili wananchi waanze kuchimba madini hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika taarifa ambayo imetajwa na Serikali imetajwa kwa ujumla kwa mfano Kata ya Katazi.

Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti wa kina kujua exactly deposit hiyo inapatikana wapi? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la kwanza; ni kweli uchimbaji bado haujapata kasi katika wilaya yake, lakini nimhakikishie kwamba, kama ni kutokana na uelewa mdogo Tume ya Madini wamejipanga kuzunguka nchi nzima kuhamasisha wachimbaji wadogo katika maeneo yenye madini ili waweze kujipanga waunde vikundi na tuweze kuwasaidia kwa ukaribu wafaidike na madini waliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la pili ni kweli taarifa hizi tulizozitoa hapa ni taarifa za utafiti wa awali unaofanywa na taasisi yetu ya GST, lakini utafiti wa kina ufanywe kwa kutumia vifaa vya kisasa vya uchongaji. Na kutambua umuhimu wa kuwasaidia wachimbaji wadogo Wizara ya Madini imeagiza kupitia Taasisi yake ya STAMICO mitambo mitano ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wafahamu kiwango cha madini kinachopatikana katika maeneo yao ili wanapokwenda kuanza kuzalisha wachimbe madini wakiwa na uhakika kwamba watapata tija kutokana na juhudi zao. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maharage ya soya niliyokuwa namaanisha ni maharage ambayo yanatumika kukamua mafuta ya kula, lakini katika majibu ambayo yametolewa na Serikali naamini wanamaanisha maharage ya kula kama mboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu hayo, lipo tatizo kubwa sana la upatikanaji wa mbegu za maharage ya soya ambayo yanatumika kwa ajili ya kukamua mafuta. Utakubaliana na mimi kwamba sisi kama Taifa tumepata soko kupeleka maharage haya China.

Swali langu; je, Serikali inafanya mpango gani mahususi wa kuhakikisha kwamba mbegu hizi zinapatikana kwa ajili ya wananchi wa Mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mingine yote Tanzania ili tuweze kujitosheleza katika kilimo cha mafuta? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni ukweli usiopingika kwamba kuna formular ya synergy, kwamba moja kujumlisha moja ni tatu na siyo mbili, kwa sababu soya meal inayopatikana ni chakula kizuri sana kwa ajili ya mifugo ikimaanisha ng’ombe, samaki na kuku.

Je, siyo wakati mwafaka kwa Serikali, kwa sababu Wizara ya Mifugo bado bajeti yake haijaja ikahakikisha kwamba ina-inject kiasi cha fedha ili mbegu bora zipatikane ili wakulima na wafugaji wetu wasihangaike ili wawe na uhakika wa chakula kwa ajili ya mifugo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kandege kwa ujumla wake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja kati ya changamoto kubwa tuliyonayo hivi sasa ni upatikanaji wa mbegu bora za soya na Serikali imeanza kuchukua hatua na hatua za kwanza ambazo tumezichukua ni kwa kushirikiana na Taasisi za TOSCI pamoja na ASA kuruhusu uingizaji wa mbegu kutoka nchi za karibu za Malawi na Zambia ili tuweze kufanya seed multiplication na lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunasambaza mbegu hizi kwa wakulima wengi zaidi na zipatikane kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa kunayo changamoto hiyo kubwa, lakini TOSCI na ASA wameshakaa chini na kukubaliana na uingizaji wa mbegu hizi katika hatua ya awali na lengo letu kubwa ni kufanya wananchi wengi zaidi waweze kuzipata kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli liko soko kubwa sana la mahitaji ya soya beans duniani na hasa kule nchini China, mahitaji ni zaidi ya metric tons milioni 100, na kama nchi tumejiandaa pia kulifikia soko hilo. Na katika maeneo ambayo tutayapa kipaumbele ni maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja na hivi sasa Mkurugenzi Mkuu wa ASA yuko njiani anaelekea...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kwa kifupi.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: ...anaelekea kwenda katika Mikoa ya Rukwa na Katavi kwa ajili ya kupata mashamba mengine makubwa kwa ajili ya uzalishaji mbegu ambayo yatakidhi mahitaji ya maeneo husika.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kunipa nafasi niulize swali moja kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, katika moja ya safari zake ambazo Mheshimiwa Waziri alifanya Mkoani Rukwa alifika Kalambo na akafika Ziwa Tanganyika eneo la Kasanga na alijionea jinsi ambavyo tuna utajiri mkubwa sana wa maji. Sasa katika majibu yake sijamsikia katika utafiti ambao unaendelea kama na chanzo kile cha kutoka Kasanga nacho ataki-consider ili kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, Songwe na ikiwezekana hata Mbeya maana maji ni mengi sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kauli ya Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru sana lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge. Kwa kweli nilifanya ziara na akanipa ombi maalum la kwenda kunionesha eneo lile, nikushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, tumefanya ugunduzi mkubwa sana na nimwombe sasa tuwaachie wataalam, lakini bila kuwaachia tu wataalam na sisi tuendelee kutoa mawazo yetu ni namna gani sasa rasilimali ile toshelevu tuliyonayo iende kunufaisha Kalambo na maeneo mbalimbali mengi ili katika kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji, ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ziwa Tanganyika ukianzia Kigoma mpaka Kalambo tulikuwa tukitegemea meli ya MV Liemba pamoja na MV Mwongozo, ni muda mrefu sana hatuna usafiri wa meli.

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kuhakikisha kwamba inapatikana meli kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Ziwa Tanganyika tuna changamoto za meli, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuelekeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, sekta ya Uchukuzi kwamba mwaka huu wa fedha tunakwenda kusaini mikataba minne ya ujenzi wa meli tatu pamoja na chelezo kubwa katika Ziwa hili la Tanganyika kwa maana ya meli tatu, meli mbili zitakuwa Ziwa Tanganyika na chelezo na meli moja itakuwa Ziwa Victoria. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wa ukanda wa Kigoma kwamba kwa meli hii ya MV Liemba ambayo tayari tupo hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi pia itakarabatiwa.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo tunavyoongea mpaka ule unatumika lakini kwa kiasi kidogo sana na hili tatizo limetokana na upande wa pili wa Zambia ambapo wafanyakazi kama walivyo TRA Tanzania, ZRA wamekuwa hawaishi pale. Je, Serikali kwa kutumia ushirikiano uliopo na Zambia haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuongea na upande wa pili ili watumishi wa ZRA wawepo muda wote ili kusiwe na shida kwa wasafirishaji wa mizigo.

Swali la pili; ukitaka kwenda Congo ya Lubumbashi njia iliyokuwa rahisi kabisa ni kwa kupita Kasanga Port ambayo naomba niipongeze Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana. Kazi ndogo ambayo imebaki ni upande wa pili kwa maana kupitia Mlilo kule na kwa wakati huu ambao ni rahisi kabisa kutumia PPP.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kutangaza mradi huu ambao economically unaonekana kwamba viable? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mpaka wetu wa Kasesya ambao una taasisi mbalimbali, kuna taasisi za Uhamiaji, Polisi, watu wa kilimo, TRA, kwa hiyo tunafanya kazi masaa 24, lakini upande wa wenzetu Zambia haufanyi kazi masaa 24, Serikali imechukua juhudi za kuwasiliana kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na hata mwaka jana tulifanya mikutano Tarehe 14 na 15 mwezi wa Kumi, kuhakikisha mpaka huu tunauhuisha na unafanya vizuri, waliahidi Serikali ya Zambia kwamba watafanya kama ambavyo tunafanya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekti, swali la pili kuhusu PPP hususan katika Bandari yetu ya Kasanga ambayo ni kweli imegharimu zaidi ya Bilioni 4.7 na Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumekuwa tukifanya mikutano mbalimbali kuishirikisha sekta binafsi ili upande wa pili wa Congo waweze kutengeneza barabara ili bandari yetu ya Kasanga Port iwe na tija. Kwa hiyo, haya tunaendelea kuyafanya, tunataendelea pia kuwasiliana na wenzetu wa Serikali ya Congo ili kuhakikisha miundombinu upande wa kwao inafanya vizuri, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Mahakama za Mwanzo katika Tarafa za Mwimbi, Kasanga na Mwazye na Mambwe Nkoswe ni chakavu kwelikweli. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wakati ikiwa inafikiria kujenga Mahakama mpya za Mwanzo?

Swali la pili; kwa kuwa Tarafa ya Mambwe Nkoswe ambayo ni kilometa 150 kwenda Makao Makuu ya Wilaya haina kabisa hata Mahakama ya Mwanzo. Je, Serikali iko tayari kwa uharaka kuhakikisha kwamba tunajengewa Mahakama ya Mwanzo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Kandege, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu wa fedha Mahakama imetenga fedha kwa ajili ya kujenga Mahakama katika Kata hii ya Kasanga ambayo ni hitaji la Mheshimiwa Mbunge. Kwa Tarafa ambayo ameitaja katika swali la pili, naomba nimuarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Mahakama itaendelea kutenga fedha kukamilisha Mahakama za Mwanzo ambazo hazijajengwa katika maeneo ambayo kuna uhitaji, ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nipongeze majibu mazuri ya Serikali. Lakini pamoja na pongezi hiyo naomba niulize maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhitaji wa vituo vya afya kwa ajili ya kutoa huduma za afya unahitajika sana katika Wilaya ya Kalambo na Halmashauri ya Kalambo na wananchi kwa kulijua hilo wameweza kujenga zahanati nane na ziko usawa wa lintel. Zahanati hizo ni pamoja na Uyumi, Sengakalonje, Limba, just to mention. Je, Serikli haioni kwamba iko sababu ya kuhakikisha kwamba inapeleka fedha ili kumalizia juhudi kubwa zilizofanywa na wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, uhitaji wa kujenga kituo cha afya katika Kata ya Katete ni wa muhimu sana kwa kuzingatia jiografia yake; Je, Serikali haioni kwamba iko sababu ya kuhakikisha kwamba katika bajeti inayokuja maeneo haya yanapelekewa fedha ili vituo vya afya vijengwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kandege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza juu ya hizi zahanati ambazo zimejengwa kwa jitihada za wananchi wa kule Kalambo. Kwanza nitoe pongezi tena kwa wananchi wa kule Kalambo kwa jitihada zao za kujenga maboma haya ya zahanati, lakini vile vile niseme mbele ya Bunge lako tukufu kwamba ni azma ya Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ina boresha afya za Watanzania kwa kujenga zahanati na vituo vya afya, hospitali za wilaya na hospitali za mikoa na rufaa kadri ya upatikanaji wa fedha. Hivyo basi sisi kama Serikali tutaangalia zahanati hizi na kuona ni namna gani tunaweza tuka-support katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 katika umaliziaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika swali lake la pili la kujenga Kituo cha Afya cha Katete. Tutatuma timu kule Kalambo kwenda kufanya tathmini ya Kituo hiki cha Afya cha Katete, na tutaona ni namna gani tunaweza tuka-support jitihada hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa kule Kalambo wote wamezifanya, za kupata kituo cha afya hapa. Mara tu tathmini itakapokamilika basi tutaona ni namna gani tunatenga fedha katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kalambo ni miongoni mwa Wilaya ambazo hazina Mahakama za Wilaya na tayari kiwanja kilishapatikana kwa ajili ya ujenzi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya. Je, Serikali ina kauli gani kwa ajili ya kujenga Mahakama katika Wilaya ya Kalambo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Josephati Kandege Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika maelezo yangu ya utangulizi ni kwamba Serikali iko kwenye mkakati wa kujenga Mahakama za Wilaya na mradi huu utachukua kama alivyouleza AG unaishia 2025/2026. Kwa hiyo napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba anakwenda kujengewa Mahakama ndani ya kipindi hiki nilichokitaja na nitawasiliana nae kumpa uhalisia wa mwaka ambapo tunapeleka mradi wake.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Utakubaliana nami kwamba katika jibu ambalo limetolewa na Serikali, wanaongelea suala la kuajiri watumishi 7,612; na kitakachoenda kufanyika ni kugawa kwa kuzingatia quality na siyo equity. Katika swali langu la msingi nimeongelea juu ya upungufu mkubwa wa watumishi wa kada ya afya katika Halmashauri yetu. Hivi karibuni wamehama watumishi 33 na wakahamishiwa watumishi watatu tu: Je, Serikali katika mgao huu itaenda kuzingatia equity badala ya equality?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa watumishi ambao wamekuwa wakipelekwa katika maeneo yanayoonekana kama ya pembezoni wanaenda kuishi kule kama kupata confirmation na kupata ukuu wa idara na baadaye kuhama; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi wote ambao wanapangwa katika maeneo hayo wanaenda kuishi kwa kipindi chote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, baada ya kumaliza mchakato wa ajira, maana yake kitakachofuata ni kugawanya katika Halmashauri zote nchini na tutagawa kulingana na mahitaji katika maeneo husika. Kwa hiyo, hatutakuwa na ile namba kwamba tutagawa Halmashauri zote kwa usawa, Hapana, tutagawa kulingana na mahitaji. Tunatambua kabisa kwamba katika maeneo kama Kalambo kuna uhitaji mkubwa, kwa hiyo, tutawapa kulingana na hiyo idadi.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwenye suala la kuhusu kuhama watumishi baada ya kwenda katika maeneo ya pembezoni, moja, ya utaratibu ambao tumeweka sasa, mtumishi haruhusiwi kuhama siyo chini ya miaka mitatu, lazima afanye kazi katika eneo alilopangiwa na baada ya hapo, labda kuwe na sababu za msingi sana ambazo zinapelekea mtu huyo apaswe kuhama. Kwa sasa ni kwamba tunafunga na wote wanakuwa na commitment letter ya kuhakikisha wanabaki katika maeneo hayo, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, maporomoko ya Kalambo ni miongoni mwa vivutio vilivyo Kusini Nyanda za Juu na ni ukweli usiopingika kwamba maporomoko haya kuachiwa chini ya TFS ambayo siyo kazi yake ya kutangaza vivutio vya kitalii ni kukosesha Taifa hili mapato sahihi.

Je, Serikali iko tayari kuyaondoa maporomoko haya kuwa chini ya umiliki wa TFS na kupeleka katika taasisi ambayo kazi yake mahsusi ni kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii?

Swali la pili, kwa sababu kutangaza ni pamoja na uwepo wa bajeti na Wizara bado haijaleta bajeti yake. Je, watatuhakikishia kwamba kama maporomoko haya yataendelea kuwa chini ya TFS bajeti yake itaonekana ambayo iko mahsusi kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kuyapeleka haya maporomoko haya maporomoko katika taasisi ya TFS tuliona kuna mbinu nyingine ambazo zinahitaji kusimamiwa na taasisi hii ya huduma za misitu Tanzania. Kwanza, kuna misitu ndani yake lakini pia kuna uoto wa asili ambao ndani yake unatunza vyanzo vya maji, hivyo TFS ni sahihi kabisa kusimamia maporomoko haya.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zote zinatangaza masuala ya utalii. Tumeanza kujenga miundombinu ya barabara katika eneo hilo, pia tumetengeneza ngazi za kufika chini, tunatarajia pia kuanzisha masuala ya cable car katika maporomoko hayo ambayo tunatarajia kwamba tutapata watalii wengi sana ambao watakuwa wanatoka nchi jirani na ndani ya nchi.

Sambamba na hilo, tunajenga daraja ambalo litaunganisha Zambia na Tanzania, hii yote ni mikakati ambayo imepangwa ndani ya bajeti ya TFS. Kwa hiyo nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaenda kufanya mambo mazuri na Kalambo inaenda kufunguka. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa zao la michikichi limekuwa likifanya vizuri katika mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Katavi lakini pia hata kule Kyela inafanya vizuri sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba miche bora inagawiwa katika mikoa yote hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Josephat Kandege, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika mikoa aliyoitaja na yenyewe ikolojia inakubali kuzalisha michikichi na mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji wa miche ili kuweza kufikia maeneo haya yote na nichukue fursa hii pia kutoa rai kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa katika mikoa ambao umeitaja kutenga maeneo makubwa ya mashamba makubwa tumeanza kuwaleta wawekezaji wakubwa kwenye mchikichi. Kwa hiyo, nitoe rai kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha kwamba wanakuwa na maeneo ya kutosha ili wakija wawekezaji hao wawe na maeneo ya kuwapeleka na naamini kabisa kwa mkakati tulionao tutakwenda kutatua changamoto hii ya upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kalambo ni miongoni mwa Wilaya ambazo hazina Mahakama za Wilaya na tayari kiwanja kilishapatikana kwa ajili ya ujenzi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya. Je, Serikali ina kauli gani kwa ajili ya kujenga Mahakama katika Wilaya ya Kalambo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Josephati Kandege Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika maelezo yangu ya utangulizi ni kwamba Serikali iko kwenye mkakati wa kujenga Mahakama za Wilaya na mradi huu utachukua kama alivyouleza AG unaishia 2025/2026. Kwa hiyo napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba anakwenda kujengewa Mahakama ndani ya kipindi hiki nilichokitaja na nitawasiliana nae kumpa uhalisia wa mwaka ambapo tunapeleka mradi wake.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize Serikali swali moja. Usikivu wa TBC ndani ya Mkoa wa Rukwa ni wa taabu na hususani katika Wilaya ya Kalambo hakuna kabisa, najua kuna juhudi za Serikali kujenga mtambo pale Kijiji cha Mkoi. Je, ujenzi huo utaanza lini ili Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wapate usikivu wa TBC? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa amekuwa mstari wa mbele kuwatetea sana wananchi wake na anahitaji wasikilize TBC Taifa. Sisi kama Serikali tulilipokea ombi lake na tulishaliingiza kwenye bajeti. Hivyo, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati utekelezaji utakapoanza basi tunashirikisha kwa hatua zaidi, ahsante sana. (Makofi