Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mgeni Jadi Kadika (11 total)

MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Kwa muda mrefu walemavu wa ngozi (albino) wamekuwa wakiishi kwa hofu katika nchi yao kutokana na kuuawa na kukatwa viungo vyao kwa imani za kishirikina ikiwemo kwa ajili ya kushinda uchaguzi au kujipatia mali:-
Je, Serikali ina mpango wa kuwalinda na kuwahakikishia usalama wa maisha yao watu hao wenye ulemavu wa ngozi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyowahi kujibiwa katika swali la msingi namba 99 na swali namba 60 katika mikutano tofauti ya Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu usalama wa ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, Serikali kupitia Jeshi la Polisi na wadau wengine imekuwa ikichukua hatua za maksudi kukomesha mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kuwasaka na kuwakamata watuhumiwa pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya pia juhudi za kuanzisha vituo vya kuwahudumia watu wenye ulemavu wa ngozi ambavyo vimesaidia kuimarisha ulinzi. Pia Jeshi la Polisi kwa kutumia falsafa ya Polisi Jamii inatoa elimu kwa umma juu ya madhara ya vitendo vya ukatili na mauaji na kujerui yanayofanywa na baadhi ya watu kwa msukumo wa imani potofu ya ushirikina. Aidha, Jeshi la Polisi limekuwa likifanya operesheni maalum za mara kwa mara zikiwamo za kukamata waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi ambazo ni kichocheo kikubwa cha ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Jeshi la Polisi ikishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama za Vijiji, Kata, Wilaya na Mikoa imeanzisha vikosi kazi hususan kwenye Mikoa na Wilaya zilizojitokeza kukithiri kwa matukio haya ili kuratibu na kusimamia kwa karibu ulinzi wa ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi. Vikosikazi hivyo hufanya kazi kwa kukusanya taarifa za kiintelejensia na kuzifanyia kazi.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Ugonjwa wa myoma ni moja kati ya matatizo makubwa yanayoathiri akinamama kuzuia uzazi na kusababisha kansa ya kizazi pamoja na kupoteza maisha:-
Je, ni kwa kiasi gani Serikali imefanikiwa katika kuwasaidia akinamama wanaoteseka na matatizo hayo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, myoma au kwa jina la kitaalam unajulikana kama uterine fibroid au leiomyoma ama kwa Kilatini leiomyomata uteri, ni uvimbe unaoota kwenye misuli ya tumbo la uzazi la mwanamke. Chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijulikani ila kila myoma huanza kwa ukuaji hovyo wa seli moja ambayo hutoa protini kwa wingi. Tafiti pia zimeonesha kwamba ugonjwa wa myoma ama fibroid hutokana na mabadiliko ya vinasaba kwenye seli za myoma ambazo hubadilisha ukuaji wa seli hizo. Aidha, mazingira pia huchangia ukuaji wa myoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ni kuwa, myoma ni uvimbe ambao siyo saratani na narudia, myoma ni uvimbe ambao siyo saratani na hauna tabia ya kubadilika kuwa saratani. Myoma ikiwa kubwa sana huweza kuonesha dalili kama vile kuvimba tumbo, kuvuja damu kwa wingi na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu. Uvujaji wa damu kwa wingi huweza kupelekea mama kupoteza maisha.
kabla ya kushika ujauzito, wakati wakiwa wajawazito au wakati wa kujifungua. Serikali kupitia Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, huwahamasisha akinamama kupima afya zao kabla ya kushika ujauzito, wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wanaogundulika na matatizo haya hufanyiwa upasuaji, aidha wa kutoa uvimbe au kutoa kizazi kama uvimbe huo umekuwa mkubwa na unaambatana na matatizo mengine kama ya kuvuja sana damu. Wataalam huamua kuondoa uvimbe peke yake au kuondoa uvimbe na kizazi. Hata hivyo, siku hizi kuna dawa ambazo Daktari anaweza kumpatia mama kabla ya uvimbe kuwa mkubwa na dawa hiyo kusaidia kupunguza uvimbe. Aidha, kama uvimbe umekaa sehemu ambayo haufai kutolewa wenyewe na mama amekwishamaliza kuzaa, basi hushauriwa kutoa mfuko wote wa kizazi (uterus).
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:-
Tatizo la fistula limekuwa likiwakumba wanawake wengi sana hapa nchini hususan maeneo ya vijijini hali inayowasababishia kuathirika kiakili na kimwili:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza tatizo hili hapa nchini?
(b) Kwa sasa ni hospitali moja tu ya CCBRT hapa nchini inayotoa matibabu ya tatizo na iko Dar es Salaam tu; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma hii katika mikoa mbalimbali au kanda ili wanawake wengi waweze kupata huduma hiyo?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la fistula linatokana na Mwanamke mjamzito kupata uchungu pingamizi kwa muda mrefu. Tatizo hili linaweza kuepukwa iwapo tutakuwa na huduma bora kwa wajawazito ili kuepuka uchungu pingamizi wa muda mrefu. Ili kuboresha huduma kwa wajawazito, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuelimisha jamii kupitia wahudumu wa afya katika jamii na vyombo vya habari kuhusu umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Pili, kupandisha hadhi baadhi ya vituo vya afya ili viweze kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto.
Tatu kuwajengea uwezo watoa huduma ya afya ili waweze kumfuatilia mjamzito wakati wa uchungu wa uzazi na ikibidi aingilie kati kabla kufikia uchungu pingamizi na pia kuboresha mfumo wa rufaa ikiwemo magari ya kubebea wagonjwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, huduma kwa wagonjwa wa fistula inatolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda za Bugando - Mwanza; KCMC -Moshi; na Mbeya Rufaa. Hospitali nyingine ni pamoja na CCBRT - Dar es Salaam; Peramiho - Ruvuma; Seliani - Arusha; na St. Gasper - Itigi. Jitihada zinaendelea kuwezesha Hospitali za Rufaa za Mikoa ziweze kutoa huduma ya matibabu ya fistula.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Serikali inajitahidi kujenga na kuimarisha madaraja ili kuondoa kero na kupunguza maafa; Daraja la Mto Wami lililopo barabara ya Tanga ni jembamba sana kiasi kwamba magari mawili hayawezi kupishana kwa wakati mmoja:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kulipanua daraja hilo la Mto Wami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa Daraja la Wami katika barabara ya Chalinze – Segera ni kiungo muhimu kati ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania. Daraja lililopo sasa ambalo ni jembamba lilijengwa miaka mingi, hivyo halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwenye barabara hiyo kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa daraja hili katika kukuza uchumi wa nchi, Serikali kupitia TANROADS imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hili. Zabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja jipya la Mto Wami zitaitishwa mwezi Februari, mwaka 2017. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Vijana wengi walioathirika na dawa za kulevya wanaleta kero kubwa ndani ya jamii, kutengwa na wazazi wao na kukosa msaada wa kifedha pale wanapoamua kuacha na kujiunga na kituo cha tiba.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa matibabu bure kwa vijana hao ili warudi katika hali zao za kawaida na hatimaye kuendelea na ujenzi wa Taifa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kuwa nchi yetu imeendelea kuwa na wimbi kubwa la ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya katika sehemu mbalimbali hapa Tanzania, na hii hupunguza nguvu kazi ya Taifa na kudidimiza uchumi wa nchi yetu. Matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana yanaongezeka hapa nchini hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza na Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto imeendelea kutoa huduma kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini bila malipo katika vituo mbalimbali vya umma vinavyotoa huduma hizo. Hivi karibuni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefungua vituo katika Hospitali ya Muhimbili, Mwananyamala na Temeke kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambavyo vimeshahudumia waathirika takribani 3,000 kwa kuwapa tiba ya methadone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani ilianza Mradi wa Utafiti wa Matumizi ya Dawa ya Methadone Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2011, na kuonyesha mafanikio makubwa na kufuatia kufunguliwa kwa vituo vya kutolea huduma za methodone katika Hospitali za Rufaa za Temeke na Mwananyamala. Upanuzi wa huduma hizi unaendelea kwa mikoa ya Mwanza na Mbeya ambayo itaanza kutoa huduma hizo hivi karibuni na mikoa mingine itafuata. Arusha, Tanga na Pwani wako katika hatua za awali za kuanza kutoa huduma hizo.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Mafuta ya ngozi kwa watu wenye Ualbino huingizwa kama mafuta ya kawaida na kutozwa kodi na kufanya watu hao kushindwa kumudu kuyanunua:-
Je, Serikali iko tayari kuondoa kodi katika mafuta hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote, naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ulinzi na fadhili zake na rehema kwangu. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa nafasi hii ambayo ameniamini katika Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye Ualbino hutumia mafuta kinga (sunscreen lotion) ili kulainisha ngozi zao zisikauke na hutumika kwa maelekezo ya wataalam wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye Ualbino na imechukua hatua kadhaa ikiwemo kusambaza vifaa mbalimbali vinavyotumiwa na watu wenye Ualbino. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesambaza miwani ya jua 50, mafuta kinga boksi 100 na tayari Bohari Kuu ya Dawa Nchini (MSD) imejumuisha katika orodha ya madawa mafuta kinga kwa ajili ya kuzuia miale ya jua kwa watu wenye Ualbino na mafuta hayo hutolewa bila malipo katika hospitali za Serikali hapa nchini. Vilevile, Serikali inaandaa Mwongozo wa Msamaha wa Matibabu (National Health Exemption) kwa watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa napenda kuwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, kuhakikisha kuwa wanaweka katika orodha mafuta haya wakati wanapoagiza dawa nyingine kutoka MSD.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeondoa kodi kwa nyenzo za kujimudu kwa watu wenye Ualbino (Technical Aids/ Appliances) yakiwemo mafuta kinga kwa bidhaa zinazozalishwa nje na ndani ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:-
Mradi wa MIVARF ni wa Muungano na Makao Makuu yapo Arusha ambapo kazi yake kuu ni kujenga masoko, miundombinu ya barabara, kuongeza thamani na kupeleka maendeleo vijijini:-
Je, ni kwa kiasi gani mradi huu umechangia kuleta maendelezo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, MIVARF ni programu inayohusika na miundombinu ya masoko, uongezaji thamani ya mazao na huduma za kifedha vijijini. Miundombinu ya masoko ni pamoja na majengo, barabara, maghala na vituo vya kuongeza mazao thamani. Katika utekelezaji wa programu hii Zanzibar imenufaika kukarabatiwa barabara zenye urefu wa kilometa 144; Unguja kilometa 68; na Pemba kilometa 80.
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara zilizokarabatiwa zimechangia katika kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo pamoja na kushamiri kwa usafiri wa abiria yaani daladala kati ya Kibwegele, Makunduchi, Bwejuu, Vikunguni, Uwandani, Mwachealale na maeneo mengine. Gharama za ukarabati wa barabara hizo ilikuwa ni shilingi bilioni tisa na milioni mia tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unatarajia kuchangia tena shilingi bilioni nne na milioni mia sita katika kujenga masoko matatu ya ghorofa na yenye vyumba vya baridi kwa ajili ya kuhifadhia mazao. Kinyasini Unguja, Tibirizi na Konde - Pemba, pamoja na ujenzi wa kituo cha mafunzo juu ya uhifadhi na utunzaji wa mazao baada ya mavuno Pujini – Pemba. Mradi unatarajiwa kujenga masoko 16 Tanzania nzima hivyo, Zanzibar imenufaika kwa asilimia 20 ya idadi hiyo ya masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unashughulikia pia na kuhamasisha na kuimarisha shughuli za vyama vya kuweka na kukopa yaani SACCOSS ambapo kwa kipindi cha mwaka 2013 mpaka mwaka 2016 SACCOSS kwa upande wa Zanzibar zimewezeshwa kukuza mtaji kutoka shilingi bilioni
• zilizokuwepo hadi kufikia shilingi bilioni 10.5. Mikopo nayo imepanda kutoka shilingi bilioni 3.9 mwaka 2013 hadi kufikia shilingi bilioni 15 mwaka 2016. Aidha, idadi ya wanachama hai imepanda kutoka 8,000 mwaka 2013 hadi kufikia 28,000 mwaka 2016.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Imekuwa ni mazoea sasa vijana wetu wengi, hasa wa kike wanapokwenda kufanya kazi za ndani katika nchi za Uarabuni kama vile Oman, Dubai na Saudi Arabia, kunyanyaswa na kuteswa na hata wakati mwingine wanauawa.
Je, inapotokea kadhia hiyo, kwa nini Balozi wetu anaewakilisha nchi yetu hatoi taarifa mapema na inachukua muda mrefu kujulikana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA NCHI NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za kiarabu zimekuwa zinatoa fursa nyingi za ajira katika kada mbalimbali kwa Watanzania na Serikali inapata faraja kuona vijana wake wanapata kazi hizo zinazowawezesha kuendesha maisha yao na familia zao. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika baadhi ya maeneo wanayofanyia kazi na haya yameonekana zaidi upande wa akina dada wanaokwenda kufanya kazi za ndani nchi za kiarabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia ripoti mbalimbali kuhusu kadhia wanazopata Watanzania walioajiriwa katika nchi za kiarabu, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali kupitia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira, ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA), kwa kushirikiana na Wizara zinazoshughulikia masuala ya kazi na ajira na balozi zetu zilizopo nchi mbalimbali huko Mashariki ya Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia matakwa ya mikataba inayosainiwa na waajiriwa hao pamoja na waajiri wao na kushuhudiwa na Balozi zetu, haki za Watanzania zinalindwa ipasavyo na hutakiwa kuripoti Ubalozini pale ambapo waajiri wao wanakiuka mikataba hiyo, ikiwemo kunyanyaswa au kuteswa. Mara baada ya kupokea taarifa hizo Serikali kupitia Balozi zetu zilizopo maeneo hayo huchukua hatua za mapema kuwasiliana na muajiri pamoja na mamlaka husika katika nchi hizo katika kusimamia na kutetea maslahi ya Watanzania. Hivyo, ni muhimu Watanzania wote wakaelewa kwamba mikataba hii ina dhamira ya kuwalinda dhidi ya madhara yanayoweza kuwatokea, kama ajali na majanga mengineyo. Serikali itaendelea kudhibiti mawakala kwa lengo la kulinda maslahi ya Watanzania wanaochangamkia fursa za ajira katika nchi mbalimbali na hivyo kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kukuhakikishia kuwa, balozi zetu hufanya juhudi na kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia masuala ya vifo yanapotokea na kujulikana na kutoa taarifa mapema kadiri zinapopatikana. Inawezekana kuna nyakati baadhi ya taarifa hizi, hasa za kiuchunguzi zinachelewa kupatikana kulingana na matukio au mazingira na utaratibu wa utendaji wa nchi husika. Na endapo hilo linajitokeza, Serikali hulazimika kusubiri, lakini wakati hilo linafanyika ndugu pamoja na vyombo vinavyohusika wanapewa taarifa kuhusu kinachoendelea.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Vituo vingi vya Polisi havina miundombinu mizuri na vingine ni vibovu na vichakavu:-
Je, ni lini Serikali itakifanyia maboresho Kituo cha Polisi Konde?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa miundombinu ya Kituo cha Polisi Konde ni mibovu na imechakaa kama ilivyo katika maeneo mengine nchini. Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kufanya ukarabati wa vituo hivyo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa Kituo cha Polisi Konde, utafanyika mara fedha zitakapopatikana ili kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wetu na kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD (K.n.y MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:-
Minara mingi ya simu imejengwa katika makazi ya watu na minara hiyo inatumia mionzi hatari kwa maisha ya binadamu. Je, Serikali inaliangaliaje suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa baadhi ya minara ya simu hujengwa karibu na makazi ya watu kwa lengo la kutoa mawasiliano bora. Ili kuhakikisha usalama kwa binadamu kuhusiana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na huduma za mawasiliano hususani mionzi inayotumika katika mawasiliano, Tanzania huzingatia viwango na miongozo ya udhibiti wa mionzi inayotolewa na Tume ya Kimataifa ya Kudhibiti Mionzi ijulikanayo kama International Commission on Non-Ionizing Radiation Protection (ICNIRP). Tume hii ilianzishwa na Umoja wa Mawasialiano ya Kimataifa International Telecommunication Union (ITU) ili kutafiti juu ya madhara yatokanayo na mionzi inayotokana na vifaa vya redio hususani simu za mkononi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa kuzingatia tafiti mbalimbali za kisayansi hakuna madhara yatokanayo na mionzi ya mawasiliano hata watu wanaoishi karibu na minara ya simu. Kulingana na tafiti za Tume (ICNIRP) imebainishwa kwamba hakuna athari zinazoweza kusababishwa na mionzi au masafa ya redio, kwa vile nguvu iliyomo katika masafa au mionzi inayosafirishwa hupungua kwa kiwango kikubwa sana kutoka kwenye antena (mara 1000 katika umbali wa mita moja kutoka kwenye antena) na kwa vile antenna hufungwa mita kadhaa juu ya minara, nguvu ya mionzi hiyo huwa ni ndogo sana ifikapo chini kiasi cha kuweza kuleta athari yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 inaelekeza kukuza usalama katika matumizi ya bidhaa na huduma za TEHAMA. Sawasawa na maelekezo haya ya kisera, katika kuhakikisha kuwa viwango vya mionzi vinavyotokana na minara ya mawasiliano havizidi kiwango kilichoelekezwa kimataifa. TCRA kwa kushirikiana na Tume ya Nguvu za Atomiki (Atomic Energy Commission) imekuwa ikifanya ukaguzi mara kwa mara na kubaini kwamba hadi sasa hakuna mionzi yeyote inayotokana na minara hii inayoweza kuathiri watu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:-

Katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo Dodoma wapo watoto ambao hutoa huduma ya kubeba mizigo na kupewa ujira mdogo. Kutokana na kufanya kazi hizo ni wazi wanakosa haki za msingi kama elimu na malezi bora.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huduma za ulinzi wa mtoto zinatekelezwa kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2021/ 2022. Tathmini imebaini kuwa watoto wengi wanaojihusisha na kazi za kubeba mizigo masokoni ni matokeo ya umasikini uliokithiri kwa baadhi ya kaya, kuondokewa na wazazi wao kwa maambukizi ya UKIMWI, migogoro ya ndoa na ukatili dhidi ya watoto.

Mheshimiwa Spika, mkakati unaotekelezwa na Serikali ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za msingi za mtoto kupata elimu na malezi bora. Aidha, utoaji wa elimu bila malipo umetoa fursa kwa watoto wengi wenye umri wa kwenda shule kuandikishwa kuanza elimu ya awali kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi. Vilevile, mradi wa TASAF umewezesha kuzitambua kaya za watoto walio katika mazingira hatarishi na kuzisaidia kiuchumi ili ziweze kumudu mahitaji ya kaya zao kwa kuwapatia watoto mahitaji ya msingi ikiwemo elimu na afya.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea na kuwatunza watoto ikiwemo kuwapa fursa ya elimu. Aidha, jamii inao wajibu wa kushirkiana na wazazi kuwatunza na kuwalinda watoto ambao ni Taifa la kesho kwa kutowatumikisha katika kazi ambazo haziendani na umri wao. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa vitendo vyovyote vya unyanyasaji wa watoto vinavyokiuka Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.