Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Riziki Saidi Lulida (8 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyenijalia kunipatia afya njema inayoniwezesha kuchangia katika hoja iliyokuwepo mezani. Napenda kukishukuru Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuniona kuwa nina uwezo wa kulitumikia Taifa hili na kunipa nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum na sasa hivi nipo katika Kambi ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumshukuru Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa juhudi zake anazozifanya, Mwenyezi Mungu atamjalia na atampa haki yake iliyokuwepo mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kunipa afya njema na leo nitajaribu kuchangia katika hoja iliyokuwa mezani hasa katika upande wa uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuliingia katika uwekezaji kwa nguvu zote tukitegemea uwekezaji utatupa faraja kubwa na kuinua kipato cha nchi yetu. Tunazungumzia kipato cha 7.3%, lakini hiki ni kipato cha watu waliokuwa na uwezo wa hali ya juu. Ukienda kuangalia uhalisia huko vijijini watu ni maskini wa kupita kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Tanzania tutaweza kukusanya mapato ya trilioni 14, hii ni pesa ndogo sana. Hizi pesa kuna wafanyabiashara sasa hivi wanazo, wameingia katika soko la dunia na kuonekana wao ni matajiri wakubwa, wana uwezo wa kuwa na trilioni 26, Serikali tukiwa na trilioni 14 kwa maana moja tumezongwa, tumekamatwa na wafanyabiashara wao ndio wataitawala nchi, hii Serikali itakuwa haina uwezo wa kuweza kujitambua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia katika uwekezaji, tumeingia katika uwekezaji lakini tulisema tulikuwa na malengo, goals, strategic, commitment, transparent, implementation, monitoring and evaluation, corruption, tumekwama wapi? Tafiti zote hizi zilifanywa na tukasema sasa hivi Tanzania uchumi wetu utakuwa mkubwa mpaka nchi nyingine kama Rwanda uchumi wao unakuwa kwa kasi sisi tupo nyuma pamoja na kuwa na resources zote ambazo tunazo. Tunataka tuseme kwamba tumekwama kwanza hatupo katika usimamizi uliokuwa bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, corruption imesimama kwa hali ya juu, baadhi ya viongozi wanaosaini mikataba wanaangalia matumbo yao, siyo kuangalia nchi inafanya nini. Usimamizi na ufuatiliaji wa miradi, Sekta ya Uwekezaji imeingia katika kila sekta kwa mfano, ukienda katika madini kuna uwekezaji bado hatujafanya vizuri; ukienda katika kilimo kuna uwekezaji, bado hatujafanya vizuri; ukienda katika viwanda na biashara kuna uwekezaji, bado hatujafanya vizuri; tumekwama wapi? Tusilizungumzie pato la asilimia 7, hakuna kitu hapo ni uchumi mdogo sana kwa Mtanzania na Watanzania tunakua, tunahitaji maendeleo, watoto wapate elimu na sisi wenyewe tuwe na maisha bora, lakini maisha bora kama hatujaweza kuangalia usimamizi huu tuliokuwa nao, tutakuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na suala la utalii, utalii unaingiza kipato cha nje (in forex), lakini leo utalii unaingiza asilimia 22.7, mianya ni mikubwa katika uwekezaji. Wawekezaji ambao wapo ndani ya utalii, ndani ya mbuga zetu hawataki kuchangia hata concession fee. Tunajiuliza usimamizi uko wapi? Kama wale watu wanapata nafasi yote, TANAPA inajenga barabara, Ngorongoro inajenga barabara na mazingira yote ya kuwapelekea maendeleo wale watu, lakini hakuna pesa wanazotoa. Matokeo yake tumekwama katika usimamizi, tungepata mapato makubwa kama tungekuwa tunasimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Selous ambayo ni mbuga kubwa ya kwanza duniani, lakini haina kipato. Wawekezaji kule ni ujangili kwa kwenda mbele na hata hao watu wanaokamatwa, leo tunaona watu wanakamatwa na meno ya tembo 30,000, lakini hatujapata taarifa yoyote humu ndani ya Bunge. Mtu anakamatwa na pembe 30,000 ina maana ameua tembo 15,000 amefanywa nini, usimamizi upo wapi, mapato ya Taifa yapo wapi, tunaiacha nchi inaangamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwa na wanyamapori na misitu hakuna mapato yatakayopatikana ndani ya utalii. Utalii watu wanakuja kuangalia mazingira yetu tuliyokuwa nayo, iwe wanyama, na misitu yetu. Leo misitu inakatwa kama hatumo humu ndani, kuna Mtendaji wa Kijiji, kuna DC, kuna Mkuu wa Mkoa na watendaji wengine wanafanya nini kuhakikisha misitu inaimarishwa? Tembo atajificha wapi, faru atajificha wapi na simba atajificha wapi misitu yote inaangamia, mkaa kwa kwenda mbele, njia za panya zinaachwa, lakini viongozi wanahusika. Tunataka Serikali itupe tamko je, hali hii ya kuhakikisha utalii unakufa itaisha lini? Tunaona katika TV sasa hivi mpaka kobe, kasa wanatoka wanakwenda nje, sura pana wamekuja kuleta fujo ndani ya nchi hii, lakini tunawafanya nini sura pana? Hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika viwanda, wamechukua viwanda vyote wawekezaji vikiwemo Viwanda vya Korosho, Viwanda vya Mafuta, Viwanda vya Ngozi, lakini sijasikia viwanda vile kwa miaka 20 vikifanya kazi na Serikali ipo humu ndani, Mawaziri wapo humu ndani, watendaji wapo wanasimamia nini. Nenda Nachingwea kile kiwanda, ni ghala la kuweka mbao na majangili kuweka mapembe ndani ya vile viwanda, nani anafuatilia hivyo vitu? Nenda viwanda vya Mtama vya Korosho havifanyi kazi, Mtwara havifanyi kazi, Mbagala havifanyi kazi, halafu tunasema tunataka tupate uchumi endelevu, tutaupataje huo uchumi kama hakuna usimamizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe makini katika kusimamia, tufuatilie, tuachane na corruption. Corruption imekuwa ni donda ndugu ndani ya nchi hii. Hatujitambui, tumeachia uchumi tunaosema tuna uchumi, lakini uchumi huu ni kwa wageni, siyo Mtanzania halisia, nenda vijijini hakuna uchumi huo tunaozungumza hapa. Tusidanganye watu, tujipange katika uchumi ambao utamgusa mwananchi kijijini, siyo uchumi unawagusa watu waliopo Dar es Salaam na maghorofa. Maghorofa yale siyo ya Watanzania yale maghorofa ni ya wawekezaji ambao wanakwepa ushuru, wanakwepa kulipa kodi halafu tunajumuisha kuonekana Tanzania kuna uchumi wakati hakuna uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kuzungumzia suala la ajira na uwekezaji. Kwa vile hatusimamii humu ndani tumewahi kuuliza kwa Waziri, leo tunaona Wachina wanauza karanga Kariakoo, katika majumba ma-godown Wahindi wamejaa mle, wanatoka India kuja kufanya kazi za vibarua, je, Mtanzania atapata wapi ajira? Hakuna ajira kwa Watanzania, Watanzania hawana ajira, ina maana uchumi wa Tanzania unahamishwa kupelekwa kwa wageni. Tumejipanga kwa hilo, tunajiuliza maswali kama hayo kwa kujua, je, kama sisi Watanzania wazalendo tunajiangalia vipi. Tumeuhamisha uchumi tunaupeleka kwa wageni, lakini tumekaa hapa tunasema tunapanga mipango mipango, kila baada ya miaka mitano mipango, tunarudi nyuma katika enzi ya ujima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja katika upande wa kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo, lakini jiulize kila mwaka Tanzania kuna njaa. Hivi kweli kilimo kwanza kimemsaidia Mtanzania? Hakijamsaidia Mtanzania. Leo unampelekea Mtanzania kilo tano za mahindi, ana watoto, wajukuu, familia kubwa je, kilo tano alizopelekewa zitamsaidia nini Mtanzania yule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika mahali unajiuliza, mvua kama hivi sasa hivi ya kutosha ipo Serikali imetoa juhudi gani kuwapelekea wananchi pembejeo, Serikali imetumia juhudi gani kuwapelekea wananchi mbegu iwe za mahindi, ufuta au karanga, hakuna, lakini utasikia mwakani tunaomba msaada wa chakula. Hii inatokana na sababu kwamba, hamjazisimamia sekta ya kilimo, mnawafanya wananchi wanahangaika na hata pale anapoweza kulima, akapata mazao yake, hakuna soko kwa mkulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima ni kundi ambalo wamekuwa watu wa kutangatanga wakitafuta soko; inapofika wakati wa mazao, wanakuja wababaishaji kuja kuchukua mazao yao kwa bei ya kutupa. Mazao yale wanayapeleka nchi za kigeni kuwa kama raw material, nchi haifaidiki hata na mazao yetu. Tanzania hata mchele tunapeleka nje, tunaletewa michele mibovu, Tanzania tunatoa mbegu za alizeti, lakini tunaletewa mafuta mabovu kutoka Ulaya kwa nini. Ndiyo maana sasa hivi Tanzania tuna kasi kubwa ya kansa, tunakula mafuta mabovu, lakini je, viwanda vyetu vinafanya nini, tulikuwa na viwanda vya kusindika mbegu na kupata mafuta Mwanza…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lulida muda wako umekwisha.
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenijalia kuwepo leo na kuweza kuchangia katika hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu amjalie Maalim Seif Sharif Hamad kipenzi cha Watanzania hasa Wazanzibar ambao walijitahidi kumpatia kura za ndiyo lakini Mwenyezi Mungu anasema walatazidu-dhwalimiina ila hasara. Imetendeka hasara kubwa na dhuluma kubwa lakini mwenye kuwa na kiburi duniani hapa ni Mwenyezi Mungu peke yake alaysallah bi-ahkami-l-haqimiina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nataka nizungumzie suala la ajira. Uchumi wa Tanzania umechukuliwa na wageni, wageni wameuchukua uchumi wetu kwa kupitia ajira za Tanzania. Sasa hivi ukiingia katika viwanda vyetu ambavyo viko katika Manispaa wafanyakazi walioko mle ndani wengi ni wageni na wametengeneza maukuta mtu yeyote hata mfanyakazi anayetoka Wizara ya Kazi hawezi kuingia mle. Maana yake ni kuwa uchumi ukipelekwa kwa wageni Watanzania watabakia kuwa ni maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano, Dangote ameanzisha kiwanda Mtwara lakini mpaka sasa hivi wamegundulika wafanyakazi 360 kutoka nje ambao hawana vibali. Kwa maana hiyo, wananchi au Watanzania ambao wanahitaji kupata kazi pale hawana nafasi lakini nafasi hizo zimechukuliwa hasa na sura pana. Tujiulize, hawa sura pana ndani ya nchi hii wamekuwa kama panya ndani ya ghala, wanakula karanga wanatubakishia maganda na nitaitolea ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri zetu hasa za Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambazo tunalima korosho sasa hivi sura pana wanakwenda kununua mazao ndani ya vijiji. Huu ni uhuru ambao hauna mipaka. Kule vijijini wanakokwenda wanafanya kazi nyingi sana. Kwanza, wanasema wananunua korosho, ufuta lakini kazi kubwa wanayoifanya kule ni uwindaji haramu. Sasa hivi tunaona misitu imekwisha, tembo wamekwisha, tujiulize wako hapa kutusaidia au wamekuja kutuharibia uchumi wa nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napata kigugumizi sana, tunaona watu wanawasifia, jamani hatujioni kama tunateketea? Tuko katika uchumi mgumu tunahakikisha kila kinachopatikana kinakwenda kwa wageni. Tufike mahali tujiulize tutakaa lini tujitambue, tuache uzembe ili tuangalie hawa sura pana wapo kutusaidia au wamekuja hapa kutumalizia uchumi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia suala la zao ya korosho katika Mikoa ya Kusini. Tuna export levy zinapatikana zaidi ya bilioni 30, hizi pesa hazijulikani zinakwenda wapi. Tulitegemea hizi pesa zikafanye kazi ya kutengeneza madawati, kununua dawa, ni ulaji ambao hauna mipaka ndani ya mikoa hiyo. Naomba tusimamie hela za export levy tuzijue zinakwenda wapi maana zimeliwa kwa miaka mingi mpaka sasa hivi haijulikani kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mkoa wa Mtwara wana export levy, katika hela hizo 60% zinakwenda kwa Mkuu wa Mkoa anazitumia kwa kitu gani? Hakuna madawati, dawa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lulida nilikupa dakika tano na zimekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RIZIKI S.LULIDA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nakushukuru na namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kupata afya njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nashukuru kwa hoja iliyowekwa mezani, ni nzuri, lakini namwonea huruma sana shangazi yangu Mheshimiwa Mwijage kuwa atapambana na kazi kubwa sana katika suala la viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na-declare Interest, mimi ni Mjumbe katika Kamati ya Uwekezaji. Nimeangalia Uwekezaji na Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma na Taasisi zake kama ni mwiba unaoitafuna nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeingia katika uwekezaji tukikurupuka, mikataba mibovu, usimamizi mbovu, corruption ndiyo imesimama. Leo tuna Taasisi zaidi ya 200 katika uwekezaji, lakini mpaka sasa hivi ni mashirika machache sana ambayo yanaweza yakatoa faida katika nchi hii. Taasisi hizo naweza nikazitaja ambazo angalau zimeonesha zinaweza zikatupeleka mbele katika dira ya maendeleo ya uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni TANAPA. Inapeleka ruzuku katika pato la Taifa; Ngorogoro inatoa Ruzuku katika pato la Taifa; National Housing Corporation inatoa ruzuku katika pato la Taifa na NSSF. Sasa tujiulize, Taasisi nyingine zinategemea ruzuku kutoka Serikalini, kulikuwa na haja gani ya kubinafsisha wakati bado wanakula fedha ya Serikali na zinaingia katika mashirika yao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuangalia Taasisi nyingi tulizokuwa nazo, hazina Bodi. Bodi ni dira, sasa kama Shirika halina Bodi unategemea nani ataendesha usukani wa Shirika lile? Nani atasimamia matumizi katika shirika lile? Kwa nini tumekaa na mashirika kwa muda mrefu yakiwa hayana Bodi? Nataka nipate majibu katika Taasisi zote kwa nini hazina Bodi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeangalia Taasisi nyingi hazina Business Plan, uliingiaje katika mkataba wa ubinafisishaji na uwekezaji hakuna Business Plan? Matokeo yake unakuta mashirika ambayo hayahusiki na ujenzi wa majumba, sasa hivi wanakimbilia kujenga majengo. Sasa National Housing ipo, NSSF ipo, kwa nini unajenga nyumba sasa hivi? Ni kutokuwa na mwelekeo wa Business Plan yake; sivyo inavyokwenda! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaingia katika suala la Mashirika mbalimbali ambayo tumeangalia. Katika kuyaangalia kwa kweli unapata huruma! Mashirika mengi yana uwezo mdogo wa Watendaji, inaonekana hawana capacity ya kuliongoza Shirika. Kwa nini umempa taasisi mtu ambaye hana uwezo? Matokeo yake, yale mashirika haya-perform. Kama hamjafanya kazi ya kuangalia nani ana-perform, nani ha-perform ina maana tutaendelea kuwa na business as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nilizungumzie Shirika la TANESCO. Shirika la TANESCO wameingia wawekezaji wakubwa, mmojawapo IPTL, Songas, Symbion, wako pale kulila lile shirika. Tufikie mahali tujiulize, nani aliweka ule mkataba mbovu mpaka kufikia hili shirika lisiweze ku-perfom? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa kila mwaka; mkataba wa Songas unasikitisha, anasema, mimi nimechukua mkopo, hivyo sitarudisha mkopo ule niliochukuwa Tanzania mpaka kwanza TANESCO anilipe. Bei anayotoa na ya kununulia ni vitu viwili tofauti. Anatoa Dola 13, huyu analipa Dola 21; jamani ni mkataba gani huu? Mnampa mkataba huu mpaka 2020/2025 toka alipoanzia, hana ruhusa ya kuguswa. Jamani, Watanzania tunajipenda hatujipendi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna huruma na nchi yetu au hatuna huruma na nchi yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja katika Bodi ya Sukari. Bodi ya Sukari imekaa pale tu kama bodi lakini haina meno, kazi inafanywa na Wizara. Wizara ndiyo wanatoa vibali vibovu vyote vya sukari. Sukari inaandikwa inakwenda nje ya nchi, kumbe inauzwa Tanzania hapa hapa, sukari inaletwa kama malighafi, siyo malighafi, iko katika viwanda. Wanachofanya, inatembea karatasi, sukari ikishateremshwa karatasi inapita katika vituo vyote kama Lorry hii imepita na sukari mpaka inafika Tunduma, lakini sukari iko bado mjini hapa! Kwa faida ya nani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiulize na sisi Watendaji ambao Watanzania wote wamekosa uzalendo, ndiyo maana wenzetu Kenya wanatupita au Rwanda wanatupita; uzalendo wa Watendaji ni mdogo sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja katika upande wa viwanda. Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani tulikuwa na Viwanda vya Korosho 13, vile viwanda vyote vimefungwa. Matokeo yake, kama Mkoa wa Lindi, hatuna ajira kwa viwanda hivyo. Hata kiwanda kimoja Lindi hamna! Unategemea wale Wamachinga watakwenda wapi? Wakija Dar es Salaam wanafukuzwa! Lindi viwanda mmevifunga, wanakwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ile korosho sasa, ule ndiyo mwiba, amepewa sura pana ananunua korosho vijijini sasa hivi! Wanapewa kununua ufuta vijijini! Hivi jamani panya umemwingiza kwenye ghala, unategemea nini? Ufuta sasa hivi hauna bei maalum, ufuta umelimwa vya kutosha, lakini sasa hivi unaambiwa sh. 1,300/= ukienda hapa sh. 2,000/=. Matokeo yake hata soko la ufuta hakuna! Tunategemea kuletewa mafuta mabovu kutoka nje! Hivi jamani mnaziona cancer zilizojaa Tanzania? Magonjwa ya figo mnayaona yalivyojaa Tanzania? Tunakula mafuta machafu, ufuta wetu tunaupeleka nje ya nchi. Tujiulize, tuna vision? Tuna mission? Are we responsible? We are not responsible. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefikia mahali tuko business as usual. Naomba tuambiwe, ule ufuta ambao umezalishwa, maana yake sasa hivi Tanzania ni nchi ya pili kuuza ufuta duniani, lakini tunaagiza mafuta kutoka nje; kwa sababu gani tunakula mafuta mabovu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini mnatuendeleza mpaka leo tunakula mafuta machafu wakati tuna ufuta, karanga, pamba na alizeti; ni kwa sababu gani mnatufanyia mambo kama haya? Mko serious? Hamko serious, mmekaa kuangalia corruption, nitapata bei kiasi gani, nitapata fedha kiasi gani, basi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, masikitiko yangu makubwa, naangalia vijana ambao wanayumba yumba. Hizi korosho zinapelekwa nje kama raw material, tunapeleka ajira nje! Wanafanya makusudi kuhakikisha Mtanzania hapati ajira katika nchi hii. Wakiwa na viwanda vyao, Mtanzania hana nafasi! Ufuta wetu ambao ni bora, korosho zetu zilizokuwa bora, pamba tunapeleka nje ili kutoa ajira nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka majibu, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kumalizia aniambie, ajira ya vijana kwa viwanda mlivyofunga itapatikana lini? Tujiwekee time frame kwa vile viwanda vilivyofungwa vya Mtwara, Masasi, Nachingwea, Lindi na Kibaha vitafunguliwa lini ili tuone kweli makucha yapo? Kama havijafunguliwa, mwakani nitauliza tena swali hili hili! Vijana wanazurura, wanahangaika!
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikwenda Nachingwea, tulikuwa katika msafara wa viongozi, maghala yale ndani mna mbao mpaka juu. Jiulize, yeye amepewa kiwanda kwa ajili ya korosho, zile mbao zinafanya kazi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanda vya Urafiki; tumekwenda Urafiki vile viwanda ndani kumejaa ma-pampers na vitu vingine. Je, tuna vision na biashara zetu? Business Plan zetu zinasema nini? Yule wa Kiwanda cha Urafiki alikuwa atengeneze nguo, amejaza na viwanda; amechukuliwa hatua gani? Tunataka tujue, hatua gani amechukuliwa? Kama hatujajua amechukuliwa hatua gani, itakuwa ni watu ambao wanaachwa. Anakamatwa na pembe, mnaambiwa, bwana, hajui Kiswahili, ndiyo maana yake tunavyofanya sasa hivi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vyetu havina thamani, vimekuwa maghala, watu wanaweka vitu vingine; hivyo kilichowekwa pale siyo. Tunataka tujue Action Plan, Business Plan zetu zinakwendaje? Tupo kwa kujenga au tupo kuwaachia wageni na uwekezaji wao uwe wa kutubomoa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nawashukuruni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijalia na mimi kuchangia katika hoja iliyopo mezani. Katika falsafa ya uchumi wanazungumza hivi, we need to plan for future and not for wait and see attitude. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Ruvuma ndiyo mikoa ambayo iliachwa nyuma katika maendeleo, hasa katika suala la miundombinu, lakini Mwenyezi Mungu hii mikoa ameipa neema kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na Mkoa wa Lindi. Tumeingia katika uwekezaji mkubwa wa viwanda vya LNG na kutoa nafasi kubwa kwa wawekezaji kwenda kuwekeza katika Mkoa wa Lindi. Cha kusikitisha, kwa nini ninasema we don’t plan for future we are planning for wait and see attitude, kiwanja cha ndege kiko karibu na uwekezaji wa viwanda, hakimo ndani ya kitabu hiki. Sasa unajiuliza, mwekezaji anahitaji kutoka Dar es Salaam kwenda Kikwetu, uwanja ambao ni mkubwa, wa pili katika Afrika, ule uwanja ulikuwa unatumika, ndege zikitoka Ulaya zinateremka Kikwetu, zikitoka Kikwetu zinakwenda South Africa, angalieni ndani ya Encyclopedia Britannica inakupa taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ule uwanja umetupwa kwa miaka yote 50, halafu mnakwenda kuwekeza maeneo hayo. Hapa mmetufunika tu, tutakwenda kurekebisha uwanja wa ndege wa Kikwetu, sijui wa Lindi, wa Kilwa, tumejipanga? Hatujajipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuingia katika uwekezaji mkubwa wa gesi na tumeambiwa Tanzania tumepata trilioni tano gesi, lakini hatuna uwekezaji katika eneo lile, hata uwanja wa ndege haupo. Wanataka kutumia viwanda Bandari ya Lindi haipo, Bandari ya Kilwa haipo, Airport ya Kilwa haipo, tunawekeza nini hapo? Hizi ni bla bla.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja suala la mawasiliano. Huamini ukifika Airport ya Kikwetu hakuna mawasiliano. Wanapoweka Kiwanda cha Likong‟o hakuna mawasiliano, huyo mwekezaji anakuja kufanya kazi gani pale? Bila kuwa na mtandao anafanya kazi gani? Wanakwenda kisasa, wanakwenda kidijitali sisi tunakwenda kianalogia, tumefika katika uwekezaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli. Katika maisha yangu sijapata kusikia tatizo lililofanyika reli kutoka Mtwara ikang‟olewa, waling‟oa kwa sababu gani? Kwa nini wasingeiacha? Leo tunataka kuwekeza katika mazao ambayo yatatoka Nachingwea, Liwale, Ruangwa yanapelekwa Bandari ya Mtwara, reli hamna. Wananchi wanaingia katika kutumia gharama kubwa ya kukodi magari kupeleka ufuta wao ukanunuliwe Mtwara wakati reli ilikuwepo Nachingwea. Hapa sijaiona reli ya Nachingwea inarudishwaje pale ili kuwarahisishia wananchi waweze kuingia katika hali bora ya maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia suala la barabara katika mikoa ya kusini. Katika ilani na ahadi zilizotolewa na Rais kuwa barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale mpaka Nachingwea itapatikana lami. Leo mtu anakwenda Liwale, sasa hivi mvua zimekwisha ndiyo mtu wa Liwale anaweza kwenda Liwale; lakini inambidi atoke Dar es Salaam mpaka Lindi, Lindi mpaka Masasi, Masasi – Nachingwea ndipo anakwenda Liwale. Jamani hata huruma hatuwaonei hawa watu? Wakisema hawako Tanzania wako Tanganyika mtakubaliana nao watu wa Liwale wako Tanganyika. Hawawezi kwenda Liwale, nauli ya kwenda Liwale utafikiri anatoka hapa anakwenda Kampala wakati anakwenda sehemu ya karibu tu hapa. Na ahadi zimetolewa za uwongo kwa muda mrefu. Tufike mahali tuachane na uwongo twende na ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waziri mwenye mamlaka aniambie ni lini barabara ya Liwale itajengwa kwa lami? Tumechoka na ahadi za uongo ambazo hazikamiliki. Kama ni maisha bora ya Watanzania hata mtu wa Liwale anahitaji maisha bora, hata wananchi wa Nachingwea wanataka maisha bora, hata mwananchi wa Ruangwa anataka maisha bora. Tunataka barabara za lami zifike katika maeneo, Mkoa wa Lindi wote hauna barabara za lami, haiwekezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaingia katika suala la mazao, anatoaje mazao kutoka vijijini kwenda barabara kubwa, hakuna barabara. Nimejaribu kuleta maswali wakasema watatoa pesa hakuna pesa iliyofika mpaka sasa hivi. Nangalu – Chikonji waliniambia tutatoa milioni 700 hakuna pesa. Mchinga – Kijiweni hakuna pesa iliyopelekwa, Mkwajuni Mipingo hakuna pesa iliyopelekwa kule, tunaingiaje katika uwekezaji hakuna hata mazingira bora ya barabara na mawasiliano hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunataka kuwekeza kilwa na ndilo eneo la pili limeonekana bora katika uwekezaji, hakuna usafiri bora unaozunguka katika maeneo ya Kilwa. Kwenda Njinjo, kwenda Kandawale, kwenda Mitole, utafikiri eneo lile halijapata uhuru katika miaka 50. Watu wako katika mazingira magumu, kuna ubaguzi mkubwa unafanyika katika kugawa miradi. Kuna mikoa inapata upendeleo, Mkoa wa Lindi kila siku wa mwisho, lakini Mungu ameleta ruzuku ya neema, hii neema mnaifanya nini? Neema hii haitamsaidia mtu wa Lindi, itatusaidia Tanzania nzima, tufike mahali tutathmini tulijipanga kwa future au tumejipanga for wait and see attitude? Haikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri mwenye dhamana aniambie katika uwekezaji alioupeleka Lindi anataka kutupatia kitu gani Lindi, amejipanga vipi kuhusu mawasiliano, kuhusu uchukuzi, amejipanga vipi kuhusu barabara, nitawaelewa kama kweli mnataka maendeleo, lakini bila hivyo sijaona kama kuna juhudi za kikamilifu za kupeleka maendeleo Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Lindi ni Mkoa ambao sasa hivi unaona neema, lakini unaona mipango iliyopangwa ya hovyo hovyo, tunahitaji mabadiliko ya kweli na ya dhamira ya kumkomboa mwananchi wa Lindi na Tanzania kwa Ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja suala la maendeleo ya barabara, nilileta maswali hapa wakasema fedha tayari zimeshapelekwa Lindi naomba Waziri mwenye dhamana aniambie ni fedha gani zimepelekwa Lindi vijijini kwa ajili ya zile barabara? Sasa hivi Ufuta huko vijijini unashindwa kuja mjini, barabara hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Nangaru leo wamekaa na ufuta vijijini wanatafuta barabara, hawana! Sasa tutafutieni njia maana yake tumejaribu kuongea imekuwa kama tumemfungia kengele mbuzi , tunaomba majibu yenye dhati, ni lini daraja la Mchinga, kijiji cha muda mrefu, Makao Makuu ya Jimbo hakuna daraja la kutoka Mchinga kwenda Kibiweni, Mheshimiwa Rais mwenyewe Magufuli alifika Lindi akasema nitajenga hili daraja la Mchinga na mimi ni mlezi wa hapa, naomba Waziri mwenye dhamana alimalize daraja la Mchinga na watu wa Mchinga waneemeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru na mimi kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Mimi ni-declare interest kwamba ni mdau wa maliasili. Kwanza nimezaliwa Selous, lakini ya pili ni Mwenyekiti wa Kupambana na Ujangili, say no to poaching. Bahati nzuri Kamati yangu tulizunguka Tanzania nzima, tukaona mazingira ambayo tumeyaona lakini nataka na mimi nitoe kama ushauri kama utaweza kusikilizwa, lakini tuangalie suala la uhifadhi na environment ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata bahati kuhudhuria mikutano mbalimbali ya climate change. Tanzania sasa hivi tunakwenda kwenye gold, tumetoka katika green tunakwenda kwenye gold, maana yake Tanzania inakwenda kwenye jangwa. Sasa tujiulize tunaangalia maslahi ya nchi au tunaangalia maslahi binafsi ya kwamba mimi niwe Mbunge, ili fujo ya nchi kuingia katika disaster ya kuwa katika gold na hali ya nchi kuwa katika ukame. Wabunge sisi tujiulize na tujipe nafasi ninachokizungumza nchi yangu inakwenda wapi? Tunakwenda katika jangwa! Tulikuwa na Profesa mmoja akatuambia mnaiona Tanzania? Tanzania inakwenda katika jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nchi za Uarabuni wanapanda miti na kuhakikisha wanautoa udongo India, kuhakikisha Arabuni kama Dubai inakuwa katika green na mvua wanapata sasa hivi. Lakini Tanzania mito mingi mikubwa sasa hivi inakauka na inapotea kabisa. Nataka nimshukuru na niwapongeze watu wa Ngorongoro, niwapongeze watu wa TANAPA na Wamasai waliopo ndani ya Ngorongoro, wale ni wahifadhi wazuri na wanasimamia ndiyo maana mpaka leo Ngorongoro Conservation inaonekana kama Ngorongoro Conservation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana TANAPA na uhifadhi wake, na kutoa tozo kubwa kwa ajili ya Serikali mwaka huu wametoa shilingi bilioni 10. Niko katika kamati ya uwekezaji, mashirika ambayo yameweza kujitegemea ni Ngorongoro, TANAPA, National Housing na TRA basi, mashirika mengine yote yako katika hali ya kufa. Sasa tujiulize tunataka uhifadhi au tunataka tuhakikishe uhifadhi hamna, mvua hamna tutaishije Tanzania hii? Hata mito haitakuwepo. Leo wewe ni mfugaji unaingia ndani ya Pori la Serengeti kuna simba, kuna tembo mgongoni una bunduki, nipe tafsiri yake ni nini hapo? Sielewi kabisa hiyo picha inayoniambia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu pili tuhakikishe haya mapori ni michoro ambayo ilikuwepo tangu enzi ya mkoloni, walijua tuwaweke maeneo ya uhifadhi hawa Waafrika watamaliza misitu yote watahakikisha hifadhi hakuna hata mvua itakuwa haipatikani. Na ndiyo maana kuna demarcation kuna, kuna ma-beacon ambayo yameweka mle ndani kuhakikisha hizi alama zinaendelea kudumu lakini kwa uhifadhi waliamua kuhakikisha wamewagawia, mwisho tunajiuliza je, tugawe hifadhi zote watu wachukue wamalize wafugaji halafu hii nchi ikae katika ukame? (Makofi)
Nataka nitoe tafsiri ya hili, wafugaji walipelekwa Mkoa wa Lindi walitoka Ihefu, Ihefu ilikauka kabisa TANESCO hata mvua ilikuwa hamna, maji hamna nchi ikaingia katika giza. Lile giza limepelekwa Lindi, shamba la bibi Lindi nenda leo Selous hakuna simba, nenda leo Selous hakuna ndovu wamehakikisha wafugaji wameingia mpaka ndani ya Selous.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tujiulize tunaangalia maslahi ya nchi au tunaangalia mimi nichaguliwe kuwa Mbunge halafu baadaye niendelee kuwa Mbunge nchi iingie katika disaster haikubaliki. Ninakuomba Waziri mwenye dhamana toa semina Wabunge wajitambua kama uhifadhi ni kitu kizuri ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwaka 2008 nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Maliasili Mwenyekiti wangu alikuwa Job Ndugai. Ni wewe ndiwe uliyeanzisha CNN, ndipo Tanzania ikaanza kukua katika utalii. Ni wewe ndiye ulileta fixed rate watu wakaambiwa ni lazima watu wenye mahoteli walipe baada ya kuona wewe unataka kuupaisha uchumi na wao kazi yao ni kuuhujumu uchumi walikuondoa kwa kuhakikisha uchumi ulio ndani ya maliasili unaporomoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuombea kwa Mwenyezi Mungu akulinde, akupe afya njema uiongoze nchi kama anavyoiongoza Waziri wa Ardhi na wewe nataka nikupe fimbo hiyo ufanye kazi hiyo, kazi kwa kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimezaliwa Selous, nimezaliwa Selous mimi ni Mngindo kwa asili ninatoka ndani ya Liwale. Selous ndiyo mbuga kubwa ya kwanza katika Afrika na ninaweza kusema ni duniani haijatangazwa, kuna corridor kubwa ya tembo ambao wanatoka Mozambique wanakuja Tanzania wakiingia Tanzania wanaingia Namtumbo, wanaingia Masasi, wanaingia Nachingwea, wanaingia Liwale, wanaingia Kilwa wanakwenda mpaka Mahenge wanavuka wanakwenda mpaka Tarangire. (Makofi)
Sasa ushoroba huu wanafaidika nini na watu wa Kusini? Ninaomba madawati yaliyopangwa ya TANAPA yawapeleke watu wa Lindi, Mtwara na Ruvuma wafaidike nayo. Huyu sungura asigawiwe kwa upande mmoja, hii siyo haki. Tulidai haki ya gesi mkasema gesi ni ya Watanzania kwa nini madawati mnagawa kwa mafungu? Nataka nihakikishiwe, Mheshimiwa Waziri pamoja na kukupenda sana kama haujapeleka allocation Lindi sitakubaliana, kama hujapeleka allocation Ruvuma sijakubaliana na wewe na kama hujapeleka allocation Mtwara kwa kweli sikubaliani nawe na ninaomba sheria hii irudishwe hapa tuifute ili angalau Tanzania nzima wafaidike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi unaongoza kuwa na rasilimali kubwa, tumepiga kelele ya mjusi ambaye yuko Ujerumani kila mwaka wanapata dola bilioni tatu Tanzania hata senti tano hatuipati. Hapa wanatufanyia dhihaka mjusi, mjusi, lakini ni haki ya mjusi. Maeneo yale tupate shule, tupate barabara lakini mpaka leo watu wa Ujerumani wanafaidika na yule mjusi, sisi tunapata nini? Nataka Mheshimiwa Waziri wa dhamana aniambie tozo linalopatikana kutokana na yule mjusi linakwenda Mipingo Tendeguru, sisi tusibakie kama boga linasuka mikeka wenye tunalala chini, hatukubali kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilwa iko katika urithi wa dunia na katika urithi wa dunia Kilwa ni namba 21 duniani hata hizo Ngorongoro, TANAPA ziko nyuma lakini kwa vile iko Kusini mpaka leo imeachwa katika urithi wa dunia. Hautuzwi, hakuna mapato, hakuna kinachoangaliwa kule Kilwa zaidi ya tumepaacha hakuna ndege zinazokwenda kule, watu wanakwenda kinyemela nyemela hakuna mapato yanayopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la utalii. Mtalii akija Tanzania anakuja na package, anaingia TANAPA, anaingia Ngorongoro, anakwenda Zanzibar. Masikitiko yangu makubwa Zanzibar hakieleweki hela zinakwenda wapi? Imefikia mahali kuwa tozo zinazopatikana Zanzibar ni hela za watu wajanja, inafikia kujiuliza Zanzibar kuna nini? Utalii wa Sychelles umewafanya mkawa matajiri, Zanzibar watu wanaendela kuwa maskini kwa vile hawasimamii rasilimali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Zanzibar wameshindwa kusimamia utalii tupo tayari kusimamia utalii wa Zanzibar na utaruka. Kama huku TANAPA wanaweza kukusanya shilingi bilioni 100, Ngorongoro shilingi bilioni mia moja na Zanzibar iko wapi hela ya utalii aibu kubwa sana. Ifike mahali ujiulize kuna fanyika nini mpaka Zanzibar ikaonekana hata utalii wa maana, pesa inayongia kama concession fee Zanzibar hakuna? Kule kuna ujanja na ulaji ambao hauna mwenyewe na kazi yao kutoa vitenge, wakiwapa vitenge wamemalizika tuuangalie utalii wa Zanzibar kwa jicho la huruma watu hawa waweze kusaidiwa.
Na wampe Maalim Self afanye kazi
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema na niwaombee Mwenyezi Mungu vilevile awajalie Wabunge wenzangu wapate afya njema tuweze kulitumikia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanzia na mazao mchanganyiko hasa katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani. Watu wa Mikoa ya Kusini walikuwa wanategemea mazao mchanganyiko kama ufuta, korosho, kunde na mbaazi. Katika nchi hii ya Tanzania tuligawanyika katika baadhi ya mazao yanayotokana na maeneo fulani, nasikitika sana tuliwaacha wafanyabiashara wachache wanaiyumbisha nchi kwa kununua mazao kwa bei ya chini na kuwafanya wananchi kuwa maskini. Tujiulize wataendelea wao kujitangaza matajiri mpaka lini, wananchi wa Kusini na Watanzania wanaendelea kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, leo katika soko la Euro wanauza ufuta kilo moja euro tatu na wafanyabiashara hawa wanachukua ufuta Lindi, Mtwara, Pwani wanaupeleka Sri Lanka, ina maana ajira inakwenda Sri Lanka. Tunawaona hatuwaoni? Lakini tumenyamaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kutafuta soko kwa wananchi kuweza kuwakwamua leo ufuta kutoka 3,500 wananunua ufuta kwa shilingi 600 mpaka shilingi 800 na wengine upo majumbani hawana pa kuupeleka kwa ajili ya hawa wafanyabiashara wanaiyumbisha Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize kwa miaka 50 kwa nini tumeachia uchumi wetu unachezewa na kukanyagwa kanyagwa na watu wachache. Ni hali ambayo imetufanya wananchi wamedhoofika, wananchi wamekuwa maskini kwa kuwa wafanyabiashara wanajiona wanakuwa matajiri na kuwaacha wananchi wanaendelea kuwa wanyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaazi zipo majumbani kutoka shilingi 3,800 mpaka shilingi 800 hazitoki, kunde, njugu na choroko zipo majumbani wao wameukamata uchumi na uchumi huo wameukamata kwa vile wana mahali wanapoegemea, wajiulize kwa nini wanaendelea kuikandamiza nchi ya Tanzania na Watanzania wenyewe wenye ngozi nyeusi wakiwa maskini, tujiulize tunajitambua Watanzania? Hatujitambui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka kila Mtanzania humu ndani ajione kuwa yeye ni part and parcel ya kutetea wanyonge wa Tanzania. Watanzania wanadhalilika, mama lishe anakimbizwa Tanzania nzima kwa ajili ya kuambiwa atoe kodi lakini kuna ma-giant hawalipi kodi. Wanatufanya Watanzania kama sleeping giant ambapo wao hawatozwi kodi na wameamua kulindwa, Serikali kama inataka kusema kweli iwashughulikie hawa watu, haina haja ya kuwasema humu ndani mnawatambua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi, Mtwara na Pwani tulikuwa na viwanda vya korosho 13 vyote havifanyi kazi. Lindi peke yake haina ajira ya vijana hata moja kwa vile viwanda vyote vimefungwa. Je, tutawapelekaje vijana wale ambao hawana ajira watafanya kazi gani, wamelima ufuta, wamechukua mikopo benki, lakini leo ule ufuta uko majumbani. Hao vijana tunawapeleka wapi?
Tunataka tuhakikishe uchumi wetu utakwenda wapi, watoto watasomaje katika mfumo ambao unaona kabisa ni kandamizi wao wanatangaza mimi nitakuwa tajiri wa dunia, halafu hawa watu wa chini wanakwenda wapi? Ni kitu cha aibu, inabidi Watanzania tujiulize tutaendelea kuwalinda mpaka lini? Mimi na wewe wote tunataka tuangalie wananchi wanyonge wanapata haki yao, haki sawa kwa wote na asiependa haki aelimishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Serikali imesahau uwekezaji hasa katika mabenki, yameingia mabenki mengi utitiri, riba zinatofautiana lakini anayekandamizwa mwalimu, daktari, mbunge, nesi na watu ambao wanachukuwa mikopo katika mabenki. Wao wanategemea taasisi zetu kuenda kuweka fixed deposit katika mabenki yao, mikataba wanayowekeana ni kutoka asilimia nne mpaka nane lakini leo mabenki wanatutoza riba ya asilimia 18.5 na kuendelea. Je, mwalimu wa kawaida ataweza kudumu au ataweza kumudu uchumi wa namna hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize kwa nini wanaweka riba kubwa jibu halipatikani. Leo kila mwezi wanakukata kodi, unakatwa kodi katika mshahara, unakwenda benki unakatwa kodi na bado unaendelea kuweka riba kubwa mara mia tatu mpaka mara mia nne tunasema nini humu ndani kuhusu watu hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, benki ni mwiba, leo ndani ya benki tunasikia lakini hakuna anayeguswa kwa vile ndani mle hakuna Lugumi wala hamna UDA. Lakini angekuwepo UDA humu ndani mngesikia kelele Bunge zima humu ndani. Wanatuibia vya kutisha, ukiweka pesa benki ukikaa mwaka mmoja haujaigusa akaunti yako hamna pesa mle ndani ya benki, tunafanya nini na riba chafu kama hizi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata katika Qurani wamesema riba ni haramu, lakini tunaona kabisa riba ni kubwa na zinawakandamiza Watanzania hatuangalii ndio maana wanajiuliza kwa nini sasa hivi wanaanza kupata woga, wanapata woga kwa vile walizoea kufanya wizi wa kukithiri ndani ya mabenki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, benki zetu zimekuwa siyo rafiki kwa Watanzania, anakopa Mtanzania anawekewa riba kubwa ambayo anashindwa hata kuimudu, ndiyo maana leo hata akina mama lishe wakikopa pesa benki ananyang„anywa vitanda vyake, magodoro yake maana yake wao wanaweka vitu vya vidogo vidogo kutokana na uwezo wao.
Naiomba Serikali iiangalie hii riba katika mabenki ni wizi wa aina yake. Na kwa nini sasa hivi wanajaribu kukimbiakimbia kusema wanataka kufunga, huu ni uongo! Watu wa benki wamecheza michezo michafu kwa muda mrefu sasa hivi wanajaribu kusimamiwa ndiyo maana wanasema tunafunga benki, lakini hawafungi benki ni kwa ajili ya wizi waliouona ni mkubwa ambao unawakandamiza Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaingia sasa hivi katika mbunga yetu ya wanyama ya Selous Game Reserve sitaki kuangalia sehemu nyingine yoyote. Nimeizungumzia hii mbuga zaidi ya miaka kumi ndani ya Bunge hili. Selous Game Reserve ni mbunga ya kwanza kwa ukubwa duniani, lakini ndani ya Selous sasa hivi watu wanachimba madini. Tunachimba uranium, wanachimba dhahabu, wanachimba almasi sisi wenyewe tupo hapa humu ndani? Nani atatuletea ufafanuzi kuwa ndani ya Selous kunafanyika nini? Hakuna kinachojulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wameifanya Selous kama shamba la bibi, mapato ya Selous tungeweze kuhakikisha yanawasaidia Watanzania wengi na wanyonge wakafaidika hata na ajira. Lakini ndani ya Selous sasa hivi hakuna kinachoendelea zaidi ya kuchimba madini mengi yako mle ndani, kuhakikisha msitu wote unakwisha, wanyama waliokuwa ndani ya Selous wamekwisha. Je, tunakwenda wapi na uchumi wetu? Tufike mahali tujiulize Tanzania, hivi kweli tunaitakia mema nchi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wachache ambao wanaingalia Tanzania kwa huruma, watu wengi hawataki kuangalia kwa huruma na ndiyo maana mpaka leo meno ya tembo yanauzwa na tunayaacha hivi tunaangaliana. Kila siku tunaangalia meno yanaondoka, kutakuwa na tembo nchi hii, kutakuwa na utalii nchi hii? Na utalii peke yake unatuingizia 27.5 percent, lakini unaona Selous imetupwa haina ajira haina kazi wala kinachofanyika ndani ya Selous; haiwezekani hali imefikia mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kuangalia hali tete inayohusu mazao. Tufike mahali tuwaonee huruma wananchi, wakulima wanalima, mpaka leo mazao yao yamekaa ndani hawajui yatayauza wapi? Leo ufuta kutoka shilingi ngapi wamekaa nao ndani mpaka shilingi 800 hakuna soko la ufuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshindwa kutafuta soko la ufuta, tumefika mahali wananchi tumewakandamiza hata pa kupita hawajui, wamekaa wamechanganikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahali, Serikali iangalie kwa makini mabenki na wakulima wanaokopa katika mabenki wanadhurumika vibaya mno. Mabenki yanaweka riba kubwa na ndiyo maana sasa hivi wanajidai ooh tumefilisika, hawajafilisika hawa, wanabadilisha majina tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia hii nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kunipatia afya njema. Ukimuona mtu mzima analia basi ujue amepatwa huyo mtu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka ni-declare interest kama mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC au Uwekezaji. Kwa kweli, kama ingekuwa Wabunge wote wanapata taarifa za mikataba mibovu ambayo imeingiwa na mashirika mbalimbali basi, humu ndani tusingekuwa pamoja tungekuwa tumepata msiba mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitu ambacho nimejifunza katika kukaa katika Kamati ya Uwekezaji, kwanza ni mikataba mibovu ambayo imeifanya nchi isiweze kwenda. La pili, tumeshindwa kusimamia Sheria ya Uwekezaji. Tatu, kulindana kulikopitiliza, matokeo yake wanapewa watu nafasi ambao hawawezi kuzifanyia kazi, iwe Mwenyekiti wa Bodi au awe Mkurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na ninakotoka, Mkoa wa Lindi na Mtwara. Mkoa wa Lindi na Mtwara tulikuwa na viwanda vya korosho vinane na wawekezaji au ubinafsishaji wakapewa vile viwanda kwa bei ya kutupa. Tangu walipopewa viwanda vile wamevifungia mpaka leo, je, Serikali ipo, haipo? Serikali ina macho, haina macho? Lakini wamelifumbia macho na kuacha viwanda vile vikifungwa mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamewapa wawekezaji, wale wawekezaji wamevifunga vile viwanda, wametoa mashine na kuzipeleka Mozambique ambako wamefungua viwanda vingine na kuwaacha watu wa Mtwara na Lindi wakiwa hawana ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza watu wale wale wamepewa kazi ya kupeleka korosho nje as a raw material, tujiulize tunajitambua? Kama kweli tunakwenda katika uwekezaji wa viwanda kwa mfumo huu hatutoki, maana mnawajua nani anasafirisha korosho nje, anapeleka ajira nje, anapeleka kila kitu nje, viwanda amevifungia kwa sababu ya nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri mwenye dhamana atuambie kwa nini viwanda hivi vimefungwa zaidi ya miaka kumi wananchi hawana ajira na korosho inapelekwa nje ajira inapelekwa nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haikubaliki ni aibu. Lazima tujitambue na tufunguke, kwa hiki tunachofanyiwa ni aibu. Hata kama utasema tunataka kuwekeza kama mikataba mibovu itakwenda hivi, hakuna uwekezaji hapa. Ina maana tunataka kutoa mfumo wa kukandamiza taasisi zetu kuhakikisha watu wa nje wanakuja kuwekeza hapa na kuleta pollution. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda Amerika ya Kusini; uwekezaji umepelekwa mkubwa sana Amerika ya Kusini; sasa hivi Amerika ya Kusini ni eneo ambalo lina pollution ya hali ya juu. Na Tanzania kwa mikataba mibovu tutakayoendelea nayo nina imani baada ya miaka mitano nchi hii itakuwa polluted yote; na mazingira yote mnayoyaona haya yatakwisha. Tujitambue na tusimamie kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na viwanda vya nguo zaidi ya kumi MUTEX, MWATEX, Urafiki, Sungura Textile, Tabora Textile na Riziki Textile, lakini viwanda vile vyote vimefungwa. Na katika kufungwa bahati nzuri Kamati ilitembelea EPZA, tukaenda kuangalia kiwanda ambacho kinatengeneza nguo za jeans, tukawauliza je mnapata wapi nyuzi? Wametujibu kuanzia sindano, uzi na kila kitu tunapata kutoka China. Tujiulize kweli tuko serious na uwekezaji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona ndugu yangu Mwijage wamekupa mzigo mzito kwa vile uliokuwa nao chini hawako serious kukusaidia, utakuwa unakimbia peke yako wataalam wako huku pembeni hawako serious na wewe kabisa. Haiwezekani tumefunga viwanda vya kusokota nyuzi, leo nyuzi zinatoka China, maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka uchumi endelevu, pana uchumi hapo? Wanawaajiri watu kwa miezi mitatu mitatu, Mtanzania huyo atapata faida gani hapa? Ina maana unamchukua miezi mitatu unamuachisha, miezi mitatu unamuachisha, hii nchi haiwezi kwenda katika mifumo ya namna hiyo ya mikataba mibovu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na viwanda vya kukamua mafuta; tulikuwa na Tanbond inatoka Tanzania, Super gee inatoka Tanzania, pride Tanzania na Mara ghee Tanzania; leo viwanda vyote mmefunga. Na wamevifunga tunaagizia blue band kutoka nchi za nje, are we serious? Halafu unapotaka kutuambia sisi tunakwenda katika mfumo wa viwanda vyote tumevifunga tunategemea vya nje hivi vina kasoro gani hata vimefungwa? Nenda Urafiki ni ma-godown, nenda Mtwara ni ma-godown, je, maendeleo haya mnayoyafanya mnayadumaza kwa makusudi halafu mnasema sasa hivi tunataka ulimwengu wa maendeleo ya viwanda, tutafika katika mfumo huo? Hatufiki, mikataba mibovu imefikia mahali ambapo sijui dawa yake ni nini, ni msiba kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelewa na Shirika la Madini Tanzania (STAMICO), walikuwa na maeneo yao ya madini Tanzania nzima viwanda vya chumvi Lindi, Mtwara na Kigoma. Vile viwanda vyote vimefungwa na walipewa maeneo mengine kama ya uwekezaji ya Mererani. Mererani ina vitalu 29, STAMICO amepewa vitalu viwili tu. Mle ndani watu ni fujo tu na ndiyo maana unaona leo Tanzania tuna Tanzanite lakini inapelekwa nje ni kwa ajili tumesababisha njia za panya. Tunashindwa nini kuwauliza wale watu kwa nini wale watu wote wasishirikiane na STAMICO ili akaweze kupeleka uchumi, lakini imeshindikana yote ni kwa ajili ya mikataba mibovu. Tufike mahali tujiulize tunatakaje maendeleo ya uwekezaji na mikataba mibovu? Hii nchi imekuwa kaputi kabisa kwa ajili ya mitaba mibovu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa mradi wa uwekezaji na TANZAMOB ambao wamepewa na STAMICO; yule mwekezaji ni tapeli wa kutupa, ameanza kuchimba madini kwa muda toka mwaka 2011 anasema hajapata faida. Tujiulize, kwa nini hajapata faida na kwa nini anaendelea kuchimba? Miradi yote unayoiona Tanzania haina time frame, anafanya mtu biashara kwa miaka yotote anayotaka yeye. Sasa je, utasemaje tunaenda katika ulimwengu wa viwanda, ulimwengu wa uwekezaji tukiwa katika mfumo mbovu? Aibu. Tujiulize kweli nchi hii tunataka kuikwamua? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea National Housing, mwekezaji Kawe alinunua majengo ya Kawe na heka 300 kwa milioni sita, milioni sita Watanzania nawaambia. Kawe ameinunua kwa milioni sita akalipa milioni mbili na laki tano, hakufanya chochote leo ameambiwa ana share na National Housing. Meneja wa National Housing anahangaika kutafuta fund yule anachukua hela ya bure na mapato ya bure, tutafika? Kwa mfumo huu tutafika? Kwa nyumba za bei rahisi mtazipata wapi? Huwezi kuzipata Tanzania anatozwa mpaka tozo la vifaa vya kuingiza kutoka nje kwa ajili ya ujenzi wa nyumba halafu unasema zile nyumba za bei rahisi, Mtanzania wa kawaida hawezi kukaa katika nyumba ya National Housing kwa vile mmeweka mikataba mibovu ya kumfanya National Housing asiendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelewa na TANAPA. Kuna wawekezaji wako ndani ya Shirika la TANAPA ambao ni watu wa mahoteli, wake watu ni majambazi sugu ambao hawataki kulipa concession fee, halafu wanachokifanya ni kukimbilia mahakamani wakicheza na mahakama kuhakikisha TANAPA haipati tozo, mahakama iko chini ya nani? Matokeo yake sasa hivi tumeshashinda lakini bado wale watu hawataki kuona Waziri ambaye anafanya kazi wanasema tutamtoa kwa vile anatudhalilisha. Uchumi wa nchi umeshikiliwa na watu wachache ambao wamehakikisha nchi hii haiendi. Tunawajua, tunawafahamu na tunawafumbia macho.
Nchi hata kama mtafika mahali hapo kama hamsimamii sheria zetu, hamuangalii mikataba yetu nina imani kuwa hatutaweza kufika popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelewa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (Tanzania Airport Authority); Tanzania tuna airport 58 amepewa airport nane tu; 50 zote zipo kwa watu wachache wanafanya shughuli zao huko, madini yanapotea huko, wanyama wanapotea huko na mali zinapotea huko ni kwa ajili ya mikataba mibovu. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na mimi leo kuchangia katika hoja iliyowekwa mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna barabara isiyokuwa na kona, hivyo hata katika masuala ya siasa kona hazikosekani, lakini Mwenyezi Mungu mwisho wake atairekebisha na hali itakuwa nzuri. Nikitakie kheri Chama changu cha Wananchi (CUF) kitakwenda vizuri na Mwenyezi Mungu atatujalia kufika salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nami nichangie katika hoja iliyokuwa mezani. Kwa muda mrefu tulikuwa tunautaka huu Muswada ufike ili uweze kutusaidia na hasa katika maslahi ya nchi yetu ya Tanzania. Nataka nitoe mfano wa kwanza ambao mimi kwangu umekuwa ni mashaka makubwa, mfano ni TBC! TBCni Shirika la Utangazaji la Taifa, lakini kutokana na mazingira magumu ambayo yamekwazika katika TBC, leo ukienda Lindi na Mtwara hatuwezi kusikia TBC mpaka tunafika Vikindu. Hii yote kutokana na muda mrefu vilio vya Wabunge vya kutaka kusikilizwa na kupata taarifa, haikupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC iliingia mkataba na Star Media, mkataba huu ulikuwa usaidie kusambaza na kupata taarifa mbalimbali za habari Tanzania nzima, jambo la kushangaza hawa Star Media wameingia mkataba na Star Times bila kuishirikisha TBC. Wameingia mkataba na Star Communication bila kuishirikisha TBC. Hawa TBC hawana meno hata hawaombi taarifa kwa nini kumeingia mikataba ya hivyo, waweze kujua mapato yanayopatikana, taarifa hizo TBC hawana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalizungumzia Shirika ambalo sasa hivi linakufa kwa sababu taratibu nyingi ambazo hazikufuatwa na wao wenyewe wanakiri kuwa hata wakiwaomba hawa Star Media waliingiaje mkataba mkubwa na Star Times ili angalau na wao waweze kujijua kimeingiwa nini, hapa kuna sintofahamu. Sasa tujiulize kama Wabunge kwa muda mrefu walikuwa wanataka kujua vinavyoendelea, leo tunaikuta TBC inakufa wakati imeingia katika uwekezaji mkubwa na Star Media. Napenda nipate majibu ni nini kinatokea TBC hajui kinachoendelea ndani ya Star Times.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameingia katika suala la kuleta ving‟amuzi – Tanzania nzima tumepelekwa katika ving‟amuzi, wanasema wameendesha kwa hasara! Ningetaka kujua kwa nini wanawafanya wenzao wawe na mikataba ambayo haiwashirikishi na hata taarifa hawazijui, hii ni hatari kwa usalama wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja Tanzania Airport Authority, hili ni Shirika la Ndege linalosimamia viwanja vya ndege, nao wamekuja pale hawajui kinachoendelea! Tanzania tuna viwanja 600 katika viwanja 600, viwanja 58 tu ambavyo wao wanakuwa na authority navyo, matokeo yake hata wakiomba taarifa kwa viwanja vilivyobakia angalau usalama wa nchi uweze kujua, revenue collection zijulikane, mapato ya landing yajulikane, ni sintofahamu. Je tujiulize, kwa nini tumekaa kwa muda mrefu tukiacha vitu hivi vikiingia katika kikwazo kikubwa na kuifanya nchi iingie katika uchumi uliodorora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo Airport ambazo zipo tunaona kabisa unasikia Kenya leo wanauza Tanzanite, ndiyo wanarusha vitu kama hivyo. Tunaona leo kuna Airport ndani ya mbuga za Selous, ndiyo wanatoa pembe na wanaokota pembe katika maeneo hayo! Kutokana na taratibu hazikuwekwa za kupata taarifa hata katika Kamati za Bunge ukiomba ilikuwa hupati. Hii ni hatari katika nchi ambayo tunataka kwenda katika uchumi endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja katika Halmashauri. Wabunge wote wanafahamu kama ni Madiwani, lakini baadhi ya Wakurugenzi hawataki kutoa taarifa za miradi mbalimbali matokeo yake unakuta shule zimeharibika, madarasa yako chini ya viwango, ukienda katika upande wa afya, hospitali hazina madawa, hela zinapelekwa lakini unapoomba taarifa inakuwa ngumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano katika kijiji cha kinyope, kile kijiji kimekaa kwa muda wa miaka 50 hawana hospitali, tukatafuta njia ya kusaidia na misaada mbalimbali tukapeleka pale mpaka leo nyumba ya Daktari haijajengwa. Watu wanahangaika kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kwenda kupata matibabu. Wanawake wanahangaika kutafuta kujifungua lakini sintofahamu! Ukiuliza au wanakijiji wakisema tunataka kujua kwa nini, anakuja DC anasema mimi ndiyo Rais wa Wilaya hii, umeleta maneno ya uchochezi na uwongo nakutia ndani. Sasa je, kama DC anawatisha wananchi kwa kutafuta haki zao na utaratibu wa habari, yeye anasema mimi ndiyo Rais, nchi hii itakuwa na Marais wangapi? Lazima sheria iseme, haya mambo ya kila DC Rais, basi hata mimi nitakuwa Rais ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahali tusimamie haki, hawa watu wanaojenga kiburi kuwa mimi ndiyo Rais hawafanyi haki kwa wananchi, akiomba mtu taarifa basi taarifa hiyo atakayepeleka anatiwa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaona misitu inakwisha, wanyamapori wanakwisha, lakini mwananchi atakayekuwa na taarifa akipeleka Polisi basi yule mwananchi wanamtia ndani! Tufike mahali Serikali isimamie sheria hii kwa makini maana inaweza kuja sheria lakini isisimamiwe. Watu wamesimama na corruption.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshukuru sana hii hoja imeletwa. Sasa ushauri wangu sheria hii hata kama imekuja kama hakuna usimamizi, basi itakuwa hakuna chochote ambacho kimeletwa hapa, tunaomba makucha yafanye kazi. Ahsante sana.