MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu swali langu linahusu suala la zao la korosho.
Mheshimiwa Spika, Serikali hivi karibuni ilifanya maamuzi mazuri ya kuhakikisha wakulima wa korosho wanaondolewa tozo na kero kubwa ambazo zilikuwa zinawasumbua kwa muda mrefu na hizo tozo tano zilitolewa maamuzi ambayo mpaka sasa hivi hajatoa tamko zuri ambalo litawafanya wananchi wale waweze kufarijika na hilo suala.
Swali langu Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama mdau wa korosho na sisi wengine ambao ni wadau wa korosho, na mikoa mingine ya Tanzania nzima ambao ni wadau wa korosho wanataka wapate tamko lako la kuhusu suala la korosho.
Je, katika msimu huu wa korosho utaweza kusimamia na kuhakikisha zile tozo tano zinafutwa ili wananchi wafarijike? Ukizingatia kwamba hali ya sasa hivi ni mbaya, mazao ya mbaazi yako majumbani, ufuta uko majumbani, kunde ziko majumbani, njugu mawe ziko majumbani, njegere ziko majumbani, choroko ziko majumbani? Mwenyezi Mungu akikujalia kusimamia na kutupa tamko lako hapa ndani ya Bunge utawafariji Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lulida, Mbunge na mdau wa korosho kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba zao hili la korosho limekuwa na matatizo mengi hasa kwenye masoko kufuatia mfumo unaotumika wa kuuzia zao hili wa Stabadhi za Mazao Ghalani. Lakini pia zao hili linaendeshwa kwa mfumo wa ushirika ambao una viongozi kutoka ngazi za vijiji, Chama Kikuu cha AMCOS na badaye kuundiwa Bodi.
Mheshimiwa Spika, zao la korosho lilikuwa na tozo zake za kisheria lakini pia wanaushirika waliongeza tozo nyingine nyingi za hovyo, na mimi ndiye niliyetamka kusimamia mazao yetu ya biashara kote nchini kuhakikisha kwamba tunafanya mapitio ya kina na kwamba tunaondoa makato ya hovyo hovyo yaliyoingizwa tu na wanaushirika kwa maslahi yao na hatimaye kupelekea wananchi wanaolima mazao haya kukata tamaa kuendelea na uzalishaji wa zao husika likiwemo zao la korosho.
Mheshimiwa Spika, Serikali baada ya kutoa tamko jukumu letu sasa ni kusimamia na tumeshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa ushirika, lakini pia hata viongozi wa taasisi yenyewe Bodi ya Korosho kuhakikisha kwamba wanasimamia maelekezo ya Serikali ya kuondoa zile tozo.
Mheshimiwa Spika, zao hili baada ya kuwa tumetoa maelekezo wajibu wa Serikali sasa ni kuhakikisha kwamba yale tuliyoyaagiza yakiwemo na yafuatayo yanaweza kukamilishwa:-
(i) Tunataka zao hili linapokusanywa na kupelekwa kwenye maghala, maghala yote ya vijijini lazima sasa yatumike kuhifadhi korosho hizo badala ya kupeleka kwenye ghala kuu ambayo yalikuwa yanatengenezewa ushuru, huku wakulima wenyewe wakiwa wameshajijengea maghala yao; na kwa hiyo kila maeneo ya Wilaya watabaini maghala ambayo yatatunza korosho hizo ili kuwapunguzia tozo ya gharama ya ghala kwenye maghala makuu.
(ii) Kumekuwa na minada inayopelekwa makao makuu ya mkoa pekee, na kuwanyima wananchi kusimamia na kuona mwenendo wa minada. Tumeagiza kuanzia sasa minada yote itafanywa kwenye ngazi ya Wilaya ili wananchi waende kushuhudia minada hiyo. (Makofi)
(iii) Kulikuwa na wanunuzi wanaoenda kwenye minada wakiwa hawana fedha. Sasa ili kujihakikishia kwamba mnunuzi ananunua na analipa lazima aweke dhamana ya kiwango cha fedha benki ambacho bodi itaamua, ili tuwe na uhakika kwamba anayekuja kuweka zabuni ya kununua zao la korosho ana fedha za kulipia; kwa sababu tumegundua watu wanakuja kutafuta zabuni hawana fedha halafu wanakimbia.
Kwa hiyo, Serikali itaendelea kusimamia haya kuhakikisha kwamba mkulima anapata fedha yake kwa kipindi kifupi sana baada ya mnada na mnunuzi awe na fedha na fedha ikishatolewa inaingizwa kwenye akaunti ya benki halafu wakulima waweze kupelekewa mahali walipo. Kwa hiyo, hiyo ndizo jitihada ambazo Serikali itahakikisha kwamba yale maelekezo yanasimamiwa na tutashuhudia kwamba yanatekelezwa vizuri. Ahsante sana. (Makofi)