MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi sasa hivi, eneo la Selous pamoja na Mbuga ya Tendeguru kuvamiwa na wafugaji. Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi, alikwenda akawakuta wafugaji wako ndani ya mbuga, wakichoma mikaa katika Misitu ya Tendeguru na kumaliza Miti ya Mipingo lakini kusababisha sasa hivi taharuki, Wafugaji kutoka katika misitu, kwenda kuvamia mashamba ya watu. Sasa hivi Mkoa wa Lindi tuko katika taharuki kubwa ya mapigano ya wafugaji na wananchi.
Je, Mheshimiwa Waziri aliyepo pale anatoa tamko gani leo hapa kwa vile aliyaona haya lakini utekelezaji wake haukukamilika mpaka hivi sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha swali langu. Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sisi kama Serikali tumeshajipanga, kwa maana ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, tukae pamoja kwa sababu suala hili ni suala la wananchi wetu na hao wananchi nao wanayo haki ya kuishi kama Watanzania. Tunachokifanya sasa hivi tunasimamia sheria upande mmoja lakini upande wa pili wanaegesha tu wanasubiria kuingia tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi kama Serikali tukae pamoja, tuone namna iliyo bora ya kuwahudumia hawa wafugaji ili changamoto hii sasa isiendelee kujitokeza. Kwa sababu sasa hivi sisi tumepewa dhamana.