Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Saumu Heri Sakala (2 total)

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita katika mchango wangu moja kwa moja katika suala la mazingira. Mazingira yaliyoimarika ni suala muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu na dunia kwa ujumla na ndiyo maana leo kila pembe ya dunia kama siyo nchi huunda vikundi ama asasi mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira. Sasa basi nikija katika nchi yetu uharibifu wa mazingira unazidi kuwa mkubwa kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote ni kwa sababu, kwanza, elimu ya mazingira kwa wananchi ni duni mno haiwafikii wananchi kwa ukamilifu unaotakiwa. Nitolee mfano Wilaya ya Kondoa na Chemba ambapo kule napo uharibifu ni mkubwa kutokana na ukosefu wa elimu watu
wanakata miti ovyo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kuni, mkaa na hata maandalizi ya mashamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linasababisha uhaba wa mvua na ukosefu wa maji tena kwa kiasi kikubwa mno, lakini mpaka leo hii watu walio wengi wa Kondoa na Chemba hawaelewi ni kwa nini wanakosa maji. Wenyewe wanasema ni “wenye ardhi ndiyo hawataki na maji yao.” Sasa ukiwauliza hao wenye ardhi ni akina nani na wako wapi wanakujibu, hata wao wanasikia tu kuna wenye ardhi. Unaweza kuona ni kwa kiasi gani elimu inahitajika katika maeneo mengi ili kunusuru mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine linalochangia uharibifu wa mazingira ni pamoja na kukosa nishati mbalimbali katika kupika hasa ukizingatia familia nyingi katika nchi yetu bado uwezo wao ni wa kutumia kuni na mkaa hivyo mazingira yetu bado yataendelea kuharibiwa sana kama bado elimu na nishati mbadala havitatolewa kwa makini na ukamilifu. Tunasikia kuna mkaa wa mabaki ya vyakula lakini bado elimu hiyo wananchi hawawezi kabisa na hata vifaa vya kutengeneza mkaa huo pia havipatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Wizara hii badala ya kujikita kwenye kutembelea mazingira na kutoa miti ya kupanda ni vyema ingejikita katika kutafuta elimu itakayosambazwa katika shule za msingi na sekondari ambako huko watatoa elimu juu ya nishati mbadala, kupeleka vifaa, kufundisha masuala ya majiko banifu ambayo majiko hayo hupatikana mjini tu. Hivyo wakipatikana walimu hawa wa kufundisha juu ya utunzaji majiko banifu na utumiaji wa mikaa inayopatikana kutokana na mabaki ya vyakula tutapata faida mara mbili; kwanza, itaongeza ajira kwa vijana na tutakuwa tumepiga hatua katika utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho ni juu ya elimu sahihi kuhusu mazingira. Ufike wakati sasa elimu ya mazingira itolewe katika kuanzia ngazi ya Kaya hadi Taifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii mimi niweze uchangia katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Wizara ambayo binafsi naiona ni muhimu sana na imebeba kauli mbiu ya Rais ya Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kweli kabisa tusipoimarisha Wizara hii, Tanzania ya viwanda inakwenda ku-fail. Kilimo ndicho ambacho kimeibeba nchi yetu. Tangu enzi za Ukoloni tumekuwa tukisikia kwamba kilimo ni uti wa mgongo na mpaka sasa bado tunaendelea kuamini hivyo. Kilimo kimekumbwa na changamoto nyingi sana kiasi ambacho hata hiyo kauli ya kwamba kilimo ni uti wa mgongo ni kama vile inachezewa haileti maana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwa kusema kuwa kilimo kama ambavyo nimesema kimezungukwa na changamoto nyingi sana hasa ukizingatia wakulima walioko vijijini ambao ndiyo wanabeba kauli hii ya kwamba kilimo ni uti wa mgongo bado wanalima kwa asili, kwa mazoea, tangu enzi za mababu wamekuwa wakirithi. Shamba ni lile lile ambalo mimi nalijua bibi yangu alikuwa akilima na ndiyo hilo hilo sasa hivi mama yangu analima na ndiyo hilo hilo najua mimi nitalima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalima sina mbolea, mbolea imezungukwa na urasimu mwingi tena mkubwa sana na hata nikiipata mbolea nyingi zinakuwa ni fake wakulima tunaathirika sana. Pia wakulima sisi tunalima kwa kutegemea mvua kitu ambacho sasa hivi kimepitwa na wakati. Mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa Tanzania, mvua siyo za kutegemea tena tunatakiwa twende kwenye kilimo cha kisasa, lakini Serikali imekaa kimya hakuna elimu ya kutosha inayopelekwa vijijini kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Hakuna miundombinu inayopelekwa vijijini kwa ajili ya kilimo cha umwangiliaji tunategemea kilimo hili kitatubeba vipi? Kwa kweli Serikali kama kweli imedhamiria kumbeba Rais na kauli yake mbiu ya Tanzania ya viwanda ni lazima ihakikishe kilimo kinawekewa mazingira ambayo yatakuwa ni wezeshi kwa wakulima hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano Wabunge wa Mkoa wa Tanga hapa wamesimama hapa wakasema tulikuwa na zao la nazi katika Mkoa Tanga katika Wilaya ya Pangani na Wilaya ya Muheza, sasa hivi zao lile limekufa lakini wote tunafahamu zao la nazi jinsi lilivyo na faida katika nchi yetu. Licha tu ya kuuza nchi jirani Kenya na sehemu nyingine lakini pia ilikuwa ndiyo kitu ambacho kilikuwa kinatusaidia sisi katika kupika, kupaka, urembo na vitu vingine. Pia nazi sisi tunajengea, ni mbao kule kwetu Pangani, lakini zao hili limekufa na hakuna mtu ambaye anajali. Haya yote ni mazingira ambayo yanasababisha kilimo kiweze kurudi nyuma. Kwa hiyo, mimi nawasihi sana muangalie hali halisi ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata viwanda navyo vya mazao yetu ambayo yanapatikana kwa kudra ya Mwenyenzi Mungu. Nasema hivyo kwa sababu tunalima kwa kutengemea mvua, siku mvua ikiwa nzuri maana yake ndiyo mazao yanapatikana sasa yakipatikana tunayapeleka wapi hata hilo soko nalo pia siku hizi hakuna. Hakuna soko la kuaminika, hakuna barabara za kuaminika ili mkulima aweze kutoa mazao yake pale na kuyafikisha sehemu inayohusika, naomba tuangalie sana sehemu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga tunalima matunda katika Wilaya ya Muheza, tuna matunda mengi sana pale, tuna machungwa sijui uende wapi usisikie chungwa la Muheza, nina imani hata huko Kusini kuna chugwa la Muheza pia, lakini Mkoa wa Tanga hatuna kiwanda cha kuchakata matunda yale. Wananchi wale wanalima machungwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Sakala.