Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe (73 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Mpango uliopo mezani. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mungu kwa kunijaalia afya njema. Vile vile nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee kukishukuru chama changu kwa kuniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalum ili niweze kuwatetea Watanzania. Niende moja kwa moja kwenye mchango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na suala la Utawala Bora, tunaimba amani, amani, amani na utulivu, lakini niseme ukweli ni miaka 54, hakuna amani na utulivu Tanzania. Wanawake hatuna amani wala utulivu kwa sababu tunadhalilishwa, mfano kwenye Mkoa wangu wa Njombe... (Makofi)
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wangu wa Njombe wanawake wengi wanabakwa, vilevile wafanyakazi wa kike wanaokwenda maofisini wanatakiwa kutoa rushwa za ngono. Hii ni wazi na ni dhahiri lakini sisi tumefumba macho tunasema amani. Hii ni amani kwa watu wachache, lakini kwa watu wengine hatuna amani au hawana amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna mambo mengi ambayo yanaendelea ya wanawake wajasiriamali. Wanawake wajasiriamali sasa hivi wanahangaishwa, wanakimbizwa huku na huku. Mfano, Mkoa wangu wa Njombe, wanawake wanatolewa barabarani kama vifurushi. Wanatolewa mizigo yao au bidhaa zao zinawekwa kwenye magari ya kutolea takataka, kwa kweli huu ni udhalilishwaji na huu ndiyo tunasema utawala bora, huu siyo utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bomoa bomoa, wanaodhalilishwa sasa hivi, wanaopata matatizo ni wanawake na watoto kwa sababu mali zao ziko nje na baridi, wanahangaika na baridi na watoto. Ni kweli! Kwa hivi kwa kweli tunasema bado Serikali ya sasa ijipange, ndiyo mmetuletea Mpango lakini je, utatekelezwa? Utatekelezeka?
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge utulivu tafadhali, tumsikilize.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naiomba Wizara, Wizara husika inayohusika na wanawake na kwanza niiombe Serikali, nasikitika sana kwa sababu imefuta Wizara moja inayohusika na Wanawake Jinsia na Watoto. Nasikitika kwa sababu ni chombo ambacho kingeendelea kuwatetea wanawake, Wameunganisha na Wizara kubwa, kwa nini wanatuonea wanawake? Kweli naiomba Serikali mtufikirie wanawake inatuumiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tena juu ya utawala bora tunaona kabisa malalamiko na kutoridhishwa baadhi ya watu kwa mfano watu wa Zanzibar, tunaona kuna kilio kikubwa sana lakini bado tunaimba utawala bora. Naomba hilo tulifikirie Serikali. Tuifikirie na tuone ni namna gani tunawasikiliza hao watu. Jamani Rais aliyetakiwa kutangazwa atangazwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo; asilimia kubwa ya wakulima ni wanawake na wanawake ndiyo wanaoshinda mashambani wanabebeshwa mizigo wakiwa na watoto wao, lakini ni wanawake hao hao wanaonyanyasika na Serikali haiwaangalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo wanazopatiwa ni feki, mfano Mkoa wa Njombe, safari hii wamepata ridom, dawa ile ya kupuliza ya ukungu ili viazi visipate ukungu, wamepata ridom feki ambayo imesababishia watu hawa kukosa mazao yanayotakiwa kama kipindi kingine wanavyovuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni hasara kwa hawa akinamama ningesema, maana akina mama ndiyo Taifa kubwa, ndiyo wanaolima sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pembejeo; Pembejeo zingine ni gharama sana kwa mfano, mbolea ya kupandia, watu wengi wanashindwa kupandia mbolea, wanapanda bila mbolea matokeo yake wanakuwa na mashamba makubwa, wanalima bila utaalam mwisho wa siku wanavunia kwenye kiganja. Halafu bado tunasema kwamba tunataka mapinduzi ya viwanda, tunataka kuwa na viwanda ambavyo vinategemea tena kilimo, sasa kilimo cha aina hii ni kweli tutaweza kutoka hapa tulipo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi; tunaomba wanawake kwenye huu Mpango, ioneshe wazi kwamba wanawake na wenyewe wanaweza kuwa wasemaji au waingie kwenye mpango na vilevile washirikishwe katika maamuzi ya ardhi. Pia wawe wamiliki wa ardhi. Kwa nini ardhi wamiliki akinababa peke yao na sisi akinamama tuna haki. Haki sawa kwa binadamu wote. Kwa hiyo, naomba huu Mpango tujaribu kuangalia namna gani tunawaingiza akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara; tena akinamama ndiyo waathirika wa miundombinu mibovu, kwa sababu akinamama ndiyo wanaobeba ujauzito kwa miezi tisa, wanatakiwa kwenda hospitalini kupimwa, lakini mwisho wa siku kwa sababu barabara ni mbovu wanajifungulia njiani. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mlowe, muda wako umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja ya Wizara ya Kilimo katika mambo yafuatayo kwa ajili ya Mkoa wangu wa Njombe. Katika Mkoa wa Njombe kumetokea janga la viazi kuungua kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Hivyo wananchi wamepoteza mtaji katika zao hilo la viazi na kusababisha wakulima hao kukata tamaa kulima zao hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wananchi hao kupata hasara kubwa na kupoteza fedha ambazo wengi wao walikuwa wamekopa na wanadaiwa na taasisi mbalimbali ambazo walikopa, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuona namna ya kuwasaidia wakulima hao kuwatafutia mbegu kutoka nchi ya Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ushuru wa mbao utolewe mara moja na siyo mara mbili au tatu kama ilivyo sasa. Ushuru hutozwa mbao zinapotoka porini, hutozwa mbao zinapoingia na kutoka kwenye maeneo ya halmashauri ambapo mbao zinaanikwa. Ushuru hutozwa tena zinapopita katika mageti ya barabarani zinaposafiri kwenda mikoa mingine kutoka Mkoa wa Njombe. Hivyo, naomba ushuru huo utolewe mara moja na kisha wafanyabiashara hawa wapewe risiti ambayo itaonyeshwa kwenye kila geti watakapopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mkoa wa Njombe ni kati ya mikoa mitano inayozalisha mazao ya chakula kwa wingi na kwa kuwa pembejeo ni gharama, naomba bei ya pembejeo ishuke kusudi wakulima wa Mkoa wa Njombe waweze kupata unafuu wa pembejeo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la viwanja vya michezo kwa shule za msingi katika mji wa Njombe. Shule hizo ni shule ya msingi ya Mpechi, Sabasaba na Idundilanga katika Halmashauri ya Njombe Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hizo zilikuwa na viwanja ambavyo vimechukuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM). Naomba Waziri asaidie kutatua tatizo hilo ili viwanja hivyo virudi kwenye shule hizo waweze kufanya michezo kama ilivyokuwa huko nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwalipe maslahi wanajeshi yanayoendana na gharama za maisha, kwani gharama za maisha zimepanda. Naiomba Serikali imalize migogoro ya ardhi kati ya Kambi za Jeshi na wananchi ili wananchi waweze kuishi kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ishughulikie mafao ya wanajeshi waliostaafu. Mfano, kuna wanajeshi katika Mkoa wa Njombe ambao wamestaafu, lakini hawajalipwa mafao yao. Naomba kuwasilisha.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitoe masikitiko yangu, kwa sababu nimeupitia huu Mpango lakini wanawake tumesahaulika katika Mpango huu. Wanawake ndiyo jicho la Taifa, ndiyo wachapakazi, lakini sijaona msisitizo au kipaumbele kwa wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na wanawake wajasiliamali, niki-refer Mkoa wangu wa Njombe, akina mama wajasiriamali wanahangaika sana, wanajitahidi kufanya biashara zao, wanajitahidi kuanzisha shughuli ndogo ndogo kwenye familia zao, lakini hawapati support au mwongozo ambao unaweza kuwasaidia wakasimama. Maana mwanamke akiwezeshwa na akijengewa msingi anaweza kulibadilisha Taifa, hivyo ninaomba kwenye Mpango huu akinamama vilevile waingizwe kwenye kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni juu ya miundombinu. Wabunge wengi wamechangia juu ya tatizo la miundombinu, niki-refer Mkoa wangu wa Njombe, sasa hivi mvua zinavyoendelea kunyesha, barabara zinazounganisha Mkoa na Wilaya ya Njombe hazipitiki, na huo umekuwa wimbo wa Taifa, kila kipindi zinapoandaliwa Bajeti naona watu wa Njombe wanasahaulika, na hapa kwenye Mpango sijaona Mkoa wangu wa Njombe kama angalau umefikiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la elimu bure. Elimu bure ni sera ambayo imewafurahisha watu wengi sana hasa wazazi. Lakini kuna changamoto kubwa sana kwenye hiyo sera ya elimu bure, sijaona hapa mkakati wa maandalizi ya walimu ambao watasaidia hasa kwa watoto wadogo, kwa sababu kutokana na hii elimu bure, mwaka huu watoto wengi sana wameandikishwa. Lakini maandalizi ya Walimu hakuna, vyumba vya madarasa hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri hili lingefanyika baada ya kufanya utafiti, lakini hakuna utafiti uliofanyika, matokeo yake sasa hatutakuwa na msingi kwa hao watoto wadogo, watakwenda huko mashuleni watakaa chini, watacheza cheza watarudi nyumbani, mwisho wa siku watoto hakuna watakacho kipata, na hatimaye tunaharibu msingi wa watoto kutoka kule chini, kwa sababu kule chini ndiko kwenye msingi wa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata tunapoongelea elimu ya juu lazima tuwe na msingi kule chini, kwa hivyo ninaomba mkakati uoneshwe hapa kwenye Mpango wa Miaka Mitano, kwa sababu ni miaka mitano, sasa miaka mitano maana yake hakuna kitakachofanyika kama hakijaoneshwa hapa, tunaomba Waziri wa Fedha ahakikishe anaingiza Mpango huu au mkakati huu, kwa ajili ya maandalizi ya walimu kwa ajili ya watoto wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu ada elekezi. Shule za private ndiyo zinazotupatia heshima katika nchi yetu, kwa sababu wanatafuta mbinu mbalimbali za kuhakikisha watoto wanafanya vizuri. Wanatumia mbinu mbalimbali kwa gharama kubwa, kutafuta walimu huku na huko hata kutoka nje, kuhakikisha wanaleta elimu kwa watoto wetu inayofaa na ndiyo maana shule za private ndizo zinazoongoza. Sasa tunapowaletea maelekezo juu ya ada kwamba watoe kulingana na maelekezo yetu tunawakosea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya ni tatizo kubwa kwa sababu miundombinu ya hospitali ni mibaya sana. Niki-refer Mkoani kwangu Njombe, mwezi wa pili Naibu Waziri wa Afya alitembelea Hospitali ya Kibena na akatoa maelekezo kwamba wahakikishe wanabadilisha au wanaleta mabadiliko na kurekebisha baada ya siku 90 wawe wamefanya kazi hiyo. Lakini ukienda sasa hivi pale Kibena ni majanga, hakuna hata paracetamol, hakuna x-ray, hakuna hata vipimo vile vingine kwa ajili ya maabara reagents hakuna, na miezi mitatu nafikiri tayari huu ni mwezi wa tatu sasa. Kwa hiyo niombe suala hili la afya liangaliwe kwa namna ya pekee, kwenye Mpango huu wa miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kilimo, Serikali imekuja na sera ya viwanda, lakini huwezi ukawa na viwanda kama hujaandaa mazao. Wakulima wetu wamekuwa wakipuuzwa sana. Niki-refer Mkoa wangu wa Njombe, mwaka huu wameunguliwa viazi vyao, sikuona jitihada iliyochukuliwa kuwasaidia wakulima hawa na ni kilio kikubwa sana kwa Mkoa wetu wa Njombe, sikuona Serikali inachukua jitihada ya pekee kuwasaidia wale wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima hawa wamekata tamaa, ningeomba tafadhali watu wa Njombe wafikiriwe, hasa wale wakulima wadogo wadogo, zaidi akina mama ndiyo hasa ambao wanateseka na kilimo, lakini mwaka huu wamepoteza pesa zao, na hawana tena mtaji wa kununua viazi kwa ajili ya mwakani. Niombe suala hili lichukuliwe kama inavyochukuliwa dharura sehemu nyingine au kwenye matukio mengine, mara nyingi yanapotokea mafuriko au nyumba zinaezuliwa, kuna pesa au kuna msaada wa dharula ambao huwa unatolewa kwa watu hawa, niombe hata Njombe wakulima wapate msaada kama huo kwa sababu hiyo kwao imekuwa janga.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mazingira hasa kwa Mkoa wangu wa Njombe kwa kweli yanatisha, hasa kwa upande wa takataka au karatasi plastic. Sijaona mkakati ambao unaonesha kwamba suala hili litaweza kushughulikiwa kwenye Mpango huu, imedokezwa kidogo sana, lakini mimi niombe suala hili liingizwe tena litiliwe mkazo, kwa sababu kweli takataka au makaratasi ya plastic pamoja na chupa za plastic ni majanga. Kila kona unakuta kuna chupa za plastic, siyo makaratasi tu lakini hata chupa za plastic za soda na juice zimetupwa kila kona. Hivyo ningeomba huku kwenye Mpango basi ioneshwe kwamba Serikali itachukua hatua gani kuweza kukomesha suala hili la plastic.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna tatizo kubwa la utoaji taka, kwenye mashimo ya takataka. Nili-fight na Mkoa wangu wa Njombe, takataka zinajaa, zinafurika, ukiuliza Mkurugenzi anasema gari ni moja kwa hivi inashindikana kutoa takataka hizi, hivyo basi ningeomba suala la mazingira litiliwe mkazo. Vilevile juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji, naomba vilevile lisisitizwe kwenye Mpango huu, kwa sababu ndio madhara hayo tunayoyaona sasa ambayo yanatuathiri, mabadiliko ya hali ya hewa, ni kutokana na mazingira yasiyo rafiki kwa binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ushuru, wajasiriamali wengi wanakata tamaa kwa sababu ya ushuru na kodi mbalimbali au tozo mbalimbali, kwa mfano, wajasiriamali wa Njombe, hasa pale Njombe Mjini, kwa kweli wanatia huruma. Mtu ana nyanya anatembeza kwenye sinia ameweka kantini yake ndogo hapo, lakini anatozwa hela nyingi sana, naomba hili liangaliwe kwa hawa wajasiriamali wadogo, wasaidiwe na hii ningeomba ioneshwe kwenye Mpango, ni namna gani hawa wajasiriamali watasaidiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea suala la vinyungu. Niombe Serikali ione namna ya kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Njombe ambao wanategemea vinyungu, bila vinyungu Njombe watapata umaskini. Serikali itoe mbadala wa vinyungu maana wananchi hawana sehemu nyingine ya kulima, wakilima mashamba ya nchi kavu hawapati chochote pia maji ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCIA U. M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni uwezeshaji wananchi kiuchumi:-
(i) Serikali itoe mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vya wanawake wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Makambako,Wanging’ombe, Lupembe, Makete na Ludewa. Mafunzo hayo yalenge namna ya kuanzisha na kuendesha biashara ndogo na namna ya kutunza mitaji.
(ii) Serikali ianzishe Benki za Wanawake katika mikoa yote na hasa kwa Mkoa wa Njombe kwenye Wilaya zake zote.
(iii) Wajasiriamali wadogo wa Njombe hasa Wamachinga na wauza matunda hawana maeneo maalum kwa ajili ya biashara zao, naomba Serikali iwasaidie kuwatafutia maeneo mazuri ya kufanyia biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kuhusu vijana; naomba Serikali iwafikirie vijana wa Mkoa wa Njombe kwa kuhakikisha wanapata mikopo kupitia vikundi vya vijana, fedha ambazo ziko kwenye Halmashauri. Pia wapewe mafunzo ya namna ya kuanzisha na kuendesha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusu Benki ya Maendeleo ya Kilimo; Serikali ianzishe Benki za Kilimo katika Mkoa wa Njombe kila Wilaya, yaani Makete, Wangingo’mbe, Makambako, Lupembe, Ludewa na Njombe Mjini, pia wakulima wapewe mikopo kupitia Benki hiyo ya Wakulima kwa riba nafuu
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni suala la miundombinu; barabara zote za Mkoa wa Njombe, Njombe - Ludewa, Njombe - Makete, Njombe - Lupembe, zina hali mbaya. Naomba Serikali itenge bajeti mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kutengeneza barabara hizo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ni suala la maji; katika Mkoa wa Njombe ni kubwa. Naomba Serikali itenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya Mradi wa Maji katika Vijiji vya Lugenge, Halmashauri ya Mji wa Njombe na Makambako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita ni kuhusu mazingira; Halmashauri ya Mji wa Njombe ina tatizo kubwa la mlundikano wa taka kwenye vizimba na gari ni moja. Naomba Serikali itenge bajeti kwa ajili ya kuongeza magari ya takataka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
(ii) Serikali ianzishe Benki za Wanawake katika mikoa yote na hasa kwa Mkoa wa Njombe kwenye Wilaya zake zote.
(iii) Wajasiriamali wadogo wa Njombe hasa Wamachinga na wauza matunda hawana maeneo maalum kwa ajili ya biashara zao, naomba Serikali iwasaidie kuwatafutia maeneo mazuri ya kufanyia biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kuhusu vijana; naomba Serikali iwafikirie vijana wa Mkoa wa Njombe kwa kuhakikisha wanapata mikopo kupitia vikundi vya vijana, fedha ambazo ziko kwenye Halmashauri. Pia wapewe mafunzo ya namna ya kuanzisha na kuendesha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusu Benki ya Maendeleo ya Kilimo; Serikali ianzishe Benki za Kilimo katika Mkoa wa Njombe kila Wilaya, yaani Makete, Wangingo’mbe, Makambako, Lupembe, Ludewa na Njombe Mjini, pia wakulima wapewe mikopo kupitia Benki hiyo ya Wakulima kwa riba nafuu
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni suala la miundombinu; barabara zote za Mkoa wa Njombe, Njombe - Ludewa, Njombe - Makete, Njombe - Lupembe, zina hali mbaya. Naomba Serikali itenge bajeti mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kutengeneza barabara hizo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ni suala la maji; katika Mkoa wa Njombe ni kubwa. Naomba Serikali itenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya Mradi wa Maji katika Vijiji vya Lugenge, Halmashauri ya Mji wa Njombe na Makambako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita ni kuhusu mazingira; Halmashauri ya Mji wa Njombe ina tatizo kubwa la mlundikano wa taka kwenye vizimba na gari ni moja. Naomba Serikali itenge bajeti kwa ajili ya kuongeza magari ya takataka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie katika Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Katika nchi yetu tuna rasilimali za kutosha ikiwa ni pamoja na madini, mazao, bandari, mbuga za wanyama, mifugo. Mkoa wa Njombe ni moja ya mikoa mitano inayozalisha mazao ya chakula na mazao ya biashara. Mazao ya chakula ni kama matunda, viazi, mahindi, ngano, maharage na kadhalika; mazao ya biashara ni pamoja na chai, mbao na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hadi sasa Mkoa wa Njombe hauna viwanda vinavyoeleweka. Naomba Serikali ione ni namna gani inapeleka wawekezaji watakaosaidia kuanzisha viwanda vya kripsi zinazotokana na viazi, viwanda vya mbao; viwanda vya karatasi, viwanda vya mafuta ya alizeti na viwanda vya juice.
Pia Serikali iwasaidie wajasiriamali wadogo wadogo ili kuanzisha viwanda vidogo vidogo kama vile viwanda vya vikapu, mapambo, sabuni na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kufika hapa ndani saa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwe wazi kwamba mimi nina shule, vilevile ni Mwalimu na nina Kituo cha Watoto Yatima. Hivyo vyote kwangu ni mwiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na suala la watoto yatima, tunaongelea suala la mikopo, kwangu mimi mwenye Kituo cha Watoto Yatima nimekuwa na watoto na vijana zaidi ya 451 ambapo 15 walitakiwa kwenda chuo kikuu kwa njia ya mkopo lakini hawakuweza kufanikiwa, sielewi ni vigezo vipi ambavyo vimekuwa vikitumika kwa ajili ya kupata mikopo. Hivyo naona kuna matatizo kwenye mikopo, Bodi ya Mikopo ina matatizo.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri niombe uone namna utakavyofuatilia suala hili na kuhakikisha kwamba vigezo stahiki vinatumika kwa ajili ya mikopo hiyo hasa kwa watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala la Walimu; mimi kama Mwalimu nina uchungu sana, nina uchungu na maisha wanayoishi Walimu kwa sababu mwenyewe nimekuwa katika mazingira hayo magumu. Mwalimu inafika hatua Afisa Elimu anakuchapa makofi au vibao, mfano, kule Rukwa kuna Mwalimu alichapwa na Afisa Elimu, jamani haki ziko wapi kwa Walimu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo haitoshi Walimu wanapangiwa kwenda kufanya kazi maeneo ya mbali. Mfano pale Njombe nina Walimu zaidi ya watano walipangiwa kazi Mwanza. Walimu hawa walikuwa ni wanandoa, lakini unakuta Mwalimu wa kike anapangiwa Mwanza, mume wake anapangiwa Kondoa. Hapa naona vilevile Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inakinzana na Sheria ya Ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sasa tuone namna gani tunawasaidia Walimu kwa kuweka sheria hizi mbili vizuri kwa sababu sasa hivi tunaongelea suala la UKIMWI na Mkoa wangu wa Njombe ninavyoona ndiyo unaoongoza, halafu bado tunawatenganisha Walimu hawa wanandoa, kwa kuwapeleka kukaa maeneo tofauti, tunategemea nini. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, akisaidiana na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, waone namna gani tunawasaidia Walimu hawa, wanandoa naomba wapangwe sehemu moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la mitaala; miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2005 mitaala ilikuwa imejielekeza zaidi kwenye maarifa, lakini baada ya mwaka 2005 mitaala hii ilibadilishwa na ikaja kuboreshwa mwaka 2013. Mitaala hii imekuwa angamizo kwa kweli, kwa nini imekuwa angamizo? Watoto wetu sasa hivi wanajua kusoma vizuri na kuweza kutoa maana ya vitu fulani au kujieleza lakini hawajui kufanya kazi yoyote ile. Mfano mtu mpaka yuko Chuo Kikuu hajui hata kusonga ugali, mtu yuko chuo kikuu hajui kufua nguo, sasa hiyo ni mitaala ya namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri turudi kwenye mitaala ambayo tulisoma sisi kule nyuma. Mtu kuanzia darasa la nne anajua namna ya kufanya kazi ndani ya nyumba, namna ya kuelekeza hata wadogo hata kama yeye ni mdogo anajua namna ya kuelekeza mdogo wake, anajua kufua nguo, anajua kuosha vyombo, lakini sasa hivi hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sayansi ya jamii haipo tena, nitoe tu mfano mdogo tu, tukiwa darasa la nne, mimi nikiwa darasa la nne, nilijua hata maana ya pazia, unapoweka pazia ndani ya nyumba, unapoweka kwenye dirisha ugeuzie wapi na maana yake nini, lakini hata ukimuuliza mtu aliyemaliza chuo kikuu hajui hata maana yake, hajui hata lengo la pazia ndani ya nyumba ni lipi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, tutumie njia yoyote turudi kwenye mitaala yetu ile tuliyoiacha, elimu tumeipeleka wapi? Sayansikimu tumeipeleka wapi, watoto hawajui kupika. Kwa hivyo, niombe tafadhali, Serikali ilione hili tusaidiane kuhakikisha tunarudi kule nyuma, tuwasaidie, tuokoe Taifa hili linaloangamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala linguine, sasa hivi tumeanza kwa nguvu zote na ni jambo jema, kuwahamasisha watu ambao walikopa na wengi wetu humu ndani nafikiri tulikopa, tumesoma kwa mkopo, lakini hebu tujiulize, tunapohamasisha kurudisha hiyo mikopo hao watu wote wamepata ajira! Watu wengi wako mitaani na ndiyo maana inakuwa vigumu kufuatilia kuwa na mapato makubwa yanayotokana na mikopo kwa sababu wengi hawajapata ajira, hivyo tuone ni namna gani tunawafuatilia wale wa mitaani tutumie njia ya kisasa kuweza kuwafutilia hao walioko mitaani na kuhakikisha tunakusanya pesa hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tutengeneze mazingira ya wao kuajiriwa na hata kama inawezekana basi, tutumie njia ya kuwafundisha au kuielimisha jamii namna gani iweze kuwa na njia za kujitegemea au ujasiriamali ili waweze kurudisha pesa hizi ambazo wananatakiwa warudishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la uhamisho. Sasa hivi wanahamishwa watumishi toka kona moja hadi nyingine, lakini hawapati pesa za uhamisho. Unakuta Mwalimu anapangiwa kwenda kufundisha mfano Mwanza au Tabora, anafika kule hana hela ya kujikimu, hana sehemu ya kukaa, mwisho wa siku anaanza kuombaomba, huyo ni Mwalimu na huko ni kumdhalilisha Mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, tuwasaidie watu hawa, tunapowapangia tuhakikishe basi pesa ya kujikimu tumeiandaa na mahali pa kukaa tumepaandaa na nyumba za Walimu ziandaliwe. Walimu wengi sasa hivi wamekata tamaa wanahama fani kutokana na ugumu huo wa maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge hoja ya Upinzani kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo. Ahsante sana kwa kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba niwashukuru viongozi wangu wa CHADEMA kwa kuniona. Naomba nijikite kwenye vipengele viwili. Kipengele cha kwanza utawala bora na cha pili ni TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na utawala bora. Sisi kama Wabunge ni wawakilishi wa wananchi, tupo hapa kuwawakilisha wananchi. Kama wawakilishi wa wananchi tunapaswa wananchi wetu waone nini tunakifanya humu ndani, lakini hadi sasa hivi sielewi, kama Wabunge kwa nini tumejifungia humu ndani? Sielewi kwa nini tumejifungia humu ndani na tunaogopa nini? Niwaulize Chama cha Mapinduzi kwa nini mnaogopa kutuonesha kwenye luninga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika utawala bora; watendaji walioko Serikalini wana…..
TAARIFA...
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa kwa sababu sijasoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wangu wa Njombe watendaji hawa wanawanyanyasa sana wanawake wajasiriamali na nina ushahidi. Mfano mwaka jana Mkuu wa Wilaya ya Njombe ambaye sasa hivi kwa bahati mbaya ni marehemu, aliwakemea watu wa CHADEMA kwa sababu eti wamevaa mavazi ya CHADEMA wakiwa barabarani na aliwashtaki, hata kesi ilikuwa mahakamani. Kwa hiyo, hii inaonyesha ni namna gani Serikali inavyopendelea wana-CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu, Ibara ya 20 inasema; “Kila mtu ana haki ya kuchagua chama anachokitaka.” Lakini sijaelewa kwa nini Serikali ya CCM inawatenga UKAWA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niende moja kwa moja kwenye suala la kilimo, nikiangalia bajeti...
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Njombe wametengewa kiasi hicho kidogo, naomba unilinde Mwenyekiti muda wangu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa bajeti ya kilimo, Njombe ni kati ya Mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi, lakini ukiangalia bajeti iliyotengwa kwa ajili Mkoa wa Njombe ni fedha ndogo sana ukilinganisha na maeneo mengine ambyo pengine hata hayazalishi. Hivyo ninaomba Waziri anayehusika kuiongezea bajeti ya kilimo.
Suala lingine ni juu ya ukusanyaji wa mapato. Ukusanyaji wa mapato katika Mkoa wangu wa Njombe kwa kweli unatuchanganya kwa sababu fedha zinazokusanywa kwenye Halmshauri hazieleweki zinafanya kazi gani, wakati mwingine fedha hizo zinazokusanywa hazikusanywi inavyotakiwa. Kwa mfano, pale Njombe kuna magari mengi (mabasi) yanayotakiwa kulipa ushuru, lakini utakuta fedha zilizokusanywa ni kidogo hazilingani na yale mabasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya elimu. Walimu wengi hawana nyumba na wengine hawajapata mafao yao, lakini wameshastaafu. Hivyo naomba Waziri wa TAMISEMI kuwasaidia watu hawa wa Njombe angalau walimu waweze kupata haki zao hasa wale waliostaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo kwa Mkoa wa Njombe kwa kweli ni suala nyeti ni kuhusu miundombinu ambayo kila siku ninaongea. Mkoa wa Njombe ni kati ya Mikoa ambayo inazalisha mazao kwa wingi, ni kati ya ile Mikoa mitano ambayo inazalisha, lakini barabara zake ni mbovu. Sasa hivi watu wanashindwa kusafirisha hata mazao yao kutoka kwenye maeneo ya pembezoni, wanashindwa kuleta mijini kwa sababu barabara zimeharibika sana.
Hivyo basi niombe tena kuifikiria Njombe kwa sababu nimeangalia hapa kwenye bajeti naona fedha kwa ajili ya miundombinu ya barabara ni fedha kidogo sana. In fact katika kupitia hii bajeti karibu mafungu yote ni kidogo. Kwa hivyo, ninaomba Waziri wa TAMISEMI aliangalie hilo kurekebisha hii bajeti angalau kuwaongezea bajeti ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee juu ya suala la Mwenge. Mwenge kwa asilimia kubwa mimi kama shahidi unasaidia kueneza magojwa ya UKIMWI. Kwa sababu watu wanalala humo, wanalala wakati mwingine analala hata kwenye makuburi, wanatoa ile misalaba, hivyo naomba mwenge…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika Wizara hii ya Madini mambo yafuatayo:-
Katika Mkoa wa Njombe Vijiji vingi havina umeme, mfano, katika Halmashauri ya Njombe Mjini, Kata tatu tu ambazo ziko mjini, wakati Kata kumi ni za vijijini hata kama vijiji hivi vina hadhi ya mji. Hivyo, naiomba Serikali ione ni namna gani inasaidia hizo kata kumi ambazo hazina mradi wa REA kwa sababu zina hadhi ya mji wakati kata hizo ziko vijijini, mradi wa REA ni wa vijijini tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ukataji wa miti huharibu mazingira, ili kuzuia ukataji wa miti bei ya gesi ipungue ili watu wengi watumie gesi kuliko kutumia kuni na mkaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kuwa kuna vyanzo vingi vya kupata nishati, basi Serikali ifanye utafiti maeneo mbalimbali kwa kuzingatia rasilimali zilizopo kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kutengenezea nishati. Mfano, maeneo yenye mifugo mingi basi Serikali ione namna ya kupeleka program ya kutengeneza umeme au nishati ya gesi kutokana na kinyesi cha wanyama. Hali kadhalika maeneo yenye maji mengi au takataka nyingi kama maeneo ya mijini basi takataka hizo zitumike kutengenezea gesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Njombe hasa Njombe mjini, inazalisha takataka nyingi basi takataka hizo zitumike kwa ajili ya kutengenezea gesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ludewa ina madini mengi ikiwemo chuma, makaa ya mawe na mengine. Naomba Serikali ihakikishe inasimamia uchimbaji wa madini ambayo yatatuongezea kipato. Wawekezaji wanaofika kwenye migodi hiyo ya Liganga na Mchuchuma wahakikishe wanapeleka huduma za jamii katika maeneo hayo ya Mchuchuma na Liganga pamoja na Wilaya yote ya Ludewa. Huduma hizo kama Umeme, Maji, huduma za afya na barabara za lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Njombe na hasa Halmashauri ya Mji wa Njombe kumekuwa na changamoto nyingi sana kuhusiana na ardhi pamoja na nyumba. Changamoto ya kwanza ni upimaji wa ardhi. Maafisa Ardhi wamekuwa wakimilikisha viwanja kwa zaidi ya mteja mmoja. Maafisa wamekuwa wakipima viwanja ambavyo ni ndani ya mita 60 na mwisho wa siku wamejikuta wanawekewa alama ya “X” kwenye nyumba hizo na hatimaye kuwatia hofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekuwa wakichukuliwa ardhi bila kujadiliana na wenye maeneo husika. Mfano, Mtaa wa Kambarage na Mji Mwema, hadi sasa hivi kuna mgogoro unaoendelea kati ya mwekezaji na wananchi. Naitaka Serikali ifanye maelewano na wenye ardhi kabla ya kuchukua ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua kutoka kwa Waziri wa Ardhi; je, mashamba, majengo na rasilimali nyingine za Njodeko na Njoruma anamiliki nani? Kwa sababu mashirika hayo yalianzishwa na wananchi ili kuleta maendeleo katika Mkoa wa Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua nini kinaendelea kwenye maeneo ya utafiti Igeli na Ichenga yaliyokuwa kwa ajili ya kuwasaidia vijana? Naiomba Serikali kuona namna ya kutumia maeneo hayo kwa ajili ya vijana kujifunza na hatimaye kuwa wakulima wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali watendaji walikuwa wanakusanya kodi za majengo, asilimia 80 ilikuwa inakwenda Halmashauri na asilimia 20 ilikuwa inarudi kwenye Serikali za Mitaa. Baadaye utaratibu umebadilika, wameweka mawakala ambao wamekuwa wakikusanya asilimia 60 kwenda Halmashauri, asilimia 20 wanachukua mawakala, asilimia 20 inarudi kwenye Serikali za Mitaa. Tunapoteza mapato hayo. Nashauri Serikali kuwa kodi hizo zikusanywe na watendaji kusudi asilimia 70 iende Halmashauri, asilimia 30 irudi kwenye Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya ujenzi ndani ya mita 60, napenda kuishauri Serikali kwa Mkoa wa Njombe wawekewe utaratibu wa mita 30 badala ya 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto ya uchomaji wa misitu hovyo hasa kipindi cha miezi ya saba hadi kumi na moja. Tatizo hilo la uchomaji limekuwa kubwa sana na la kawaida katika Mkoa wa Njombe, katika maeneo ya Kifanya na maeneo mengine. Napenda kuishauri Serikali kusimamia sheria lakini pia wachukue hatua kali dhidi ya wananchi watakaobainika wanachoma moto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na changamoto ya TANAPA kufyeka mahindi, ndizi, miwa katika kijiji cha Luduga, Wilaya ya Wanging‟ombe. Nashauri Serikali itoe elimu kwa wananchi wa maeneo hayo kuhusu maeneo ya hifadhi na kuweka mipaka kati ya hifadhi na maeneo ya kulima wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wafanyakazi wa hifadhi wasinyanyase wananchi kwa kuwapiga na kuwapeleka kwenye vituo vya polisi. Wawe na
uzalendo wa kujadiliana badala ya kutumia nguvu kwa kuwafyekea mazao yao na huo sio ubinadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mchuchuma na Liganga. Suala la mradi wa madini ya Mchuchuma na Liganga limechukua muda mrefu, naiomba Serikali sasa ichukue hatua haraka ya kutatua tatizo la kulipa fidia kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya madini ambapo waliahidiwa kulipwa mwezi Juni, 2016, kiasi cha Shilingi bilioni 14. Pia Serikali ikamilishe mazungumzo kuhusu bei za umeme ambayo inasuasua. Wananchi wamehamasishwa kulima matunda na nafaka kwa kutegemea kupata soko la uhakika kwenye machimbo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Utawala Bora. Wafanyakazi/watumishi wengi wa umma wanafanya kazi kwa hofu na woga na kupoteza ubunifu kutokana na utumbuaji wa majipu ambao haufuati utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wamekata tamaa sana kutokana na kodi zisizo na utaratibu, TRA inawakamua sana wafanyabiashara hao. Wafanyabishara wadogo wananyanyaswa sana kwa kutozwa kodi nyingi na hata kuua mitaji ya wafanyabiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Miundombinu. Tunapoongelea suala la Liganga na Mchuchuma lazima suala la barabara lipewe umuhimu sana. Barabara ya Njombe Mjini – Ludewa ni ya vumbi na kipindi cha mvua inaharibika sana. Naomba barabara hii iingie kwenye mpango wa 2017/2018 kwa ajili ya maandalizi ya uchimbaji wa madini ya Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Maji; gharama za maji zinawatesa wananchi, naomba suala la maji na gharama za maji ziangaliwe, wananchi wanaletewa bili kubwa za maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi ambayo yamebadili majira ya mwaka kwa kuyachelewesha au kuyawahisha na madhara yanayotokea kutokana na mabadiliko hayo mara nyingi yanakuwa ni kuharibika kwa miundombinu na pia watu kupoteza maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali iwekeze katika sekta za kuzuia na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi. Mfano kusimamia sheria za utunzaji wa mazingira kama vile upandaji miti, kuzuia watu wanaokata miti ovyo na wanaochoma ovyo misitu na kusababisha ongezeko la ukaa. Wachukuliwe hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki. Kwa kuwa vifungashio vya plastiki vinachafua mazingira, basi naishauri Serikali ione utaratibu wa kufanya recycling ili isiathiri mazingira na isiathiri wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishati mbadala; ili kupunguza au kuondoa kabisa uharibifu wa mazingira kupitia ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa, basi Serikali waje na mkakati wa kutafuta wawekezaji wajenge kiwanda cha kuchakata gesi hapa Tanzania na kuiweka kwenye mitungi na kuisambaza nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takataka; Miji yetu inazalisha taka nyingi zikiwemo taka ngumu na taka za maji. Hakuna mfumo rasmi unaotumika ili kuhakikisha taka mbalimbali zinakusanywa ipasavyo. Naishauri Serikali kuweka mfumo rasmi wa kutupa taka hizo. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu kuna hali ya kutisha kwa sababu ya utekwaji wa watu (wananchi) lakini Serikali imenyamaza kimya, mfano kutekwa kwa Ben Saanane. Naiomba Serikali ishughulikie suala hili na hasa kumleta Ben Saanane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zetu za jinai zimesisitiza kwamba utekaji nyara kwa lengo la kuua au kuumiza mtu ni kosa kubwa la jinai. Chini ya Kifungu cha 248 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kwa mfano;
“Mtu yeyote ambaye anamteka nyara au kumtorosha mtu yeyote ili mtu huyo auawe, au aweze kutupwa ili kuwekwa katika hatari ya kuuawa, atakuwa anatenda kosa na anawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miaka kumi”
Kwa mujibu wa kifungu cha 250 cha sheria hiyo, kuteka nyara kwa lengo la kumuumiza mtekwa nyara ni kosa la jinai vilevile na adhabu yake ni kifungo jela kwa muda wa miaka kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwazuia watu wasiwe na uhuru wa mawazo ni kukiuka Katiba ya nchi Ibara ya 18(a) inayosema:-
“Kila mtu-
(a) Anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na kamatakamata ya baadhi ya Wabunge na wananchi wengine kwa sababu ya kueleza au kutoa mawazo yao ya kuikosoa Serikali. Naishauri Serikali kusikiliza mawazo hayo na kuyatendea kazi kwani ni kwa njia ya kukosolewa Serikali inaweza kuboresha utendaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ndoa za utotoni, naiomba Serikali kurekebisha Sheria ya Ndoa ili kuwatendea haki watoto wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia mikutano ya hadhara, hapa naona Serikali inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 20(1) inayosema:
“Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iruhusu mikutano ya vyama vya siasa kwani hii ni kulingana na Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Uchukuzi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara na wataalam wake, naomba nishauri kwamba viwanja vya ndege vikarabatiwe na hasa kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Njombe. Kiwanja hiki kimeharibiwa sana na watu wanaopita katikati ya kiwanja, hata magari yanapita uwanjani. Hii ni kutokana na uwanja kuwa katikati ya mji. Naiomba Serikali itengeneze uwanja huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha watu wa Njombe na kutenga fedha kwa ajili ya barabara ya Itoni – Ludewa – Njombe – Makete – Kibena – Lupembe – Madeke. Naiomba Serikali kuhakikisha kwamba fedha hiyo iliyotengwa inapelekwa ili kazi ianze kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara za vijijini katika maeneo mengi na hasa katika Mkoa wa Njombe ni mbovu, naiomba Serikali kuangalia tatizo la wananchi vijijini hasa wanawake wajawazito ambao wanapoteza maisha kwa sababu ya barabara mbovu. Naiomba Serikali itengeneze barabara za vijijini ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto wachanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akinamama wengi ni wakulima wanaojitahidi kuzalisha mazao ya chakula na biashara lakini wanashindwa kusafirisha kwa sababu barabara hazipitiki, hasa wakati wa masika. Kwa mfano wananchi wa Mamongolo, Makowo, Ng’elamo, Matola, Iwungilo. Maeneo hayo yanazalisha kwa wingi viazi, ngano pamoja na chai lakini kipindi cha kifuku hayapitiki. Naiomba Serikali itusaidie ili maeneo hayo yaweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mawasiliano. Maeneo mengi katika Mkoa wa Njombe hakuna mawasiliano ya simu. Kwa mfano, katika Wilaya ya Ludewa maeneo yote ya mwambao kama Vijiji vya Lupingu, Ibumi, Lifuma na Kilondo hayana kabisa mawasiliano, naiomba Serikali iweke minara ya simu katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wilaya ya Makete, maeneo ya Matamba, Kiteto na maeneo mengine mengi hakuna mawasiliano kabisa, naiomba Serikali kupeleka minara katika maeneo hayo. Kutokana na ukosefu wa mawasiliano husababisha akinamama kupata matatizo
makubwa ya kupata msaada wakati wa kujifungua kwa sababu wanashindwa kuwasiliana na vyombo vya usafiri ili wawahishwe hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika hoja hii ya afya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na maendeleo ya jinsia. Kwa kuwa Benki ya Wanawake iko katika maeneo machache, naiomba Wizara kuhakikisha kuwa Benki ya Wanawake inakwenda katika mikoa yote na kwa namna ya pekee naomba benki hii ianzishwe katika Mkoa wa Njombe kwenye Wilaya hata tatu za Makete, Njombe na Ludewa kwa kuwa benki hii itawanufaisha wanawake wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia, kumekuwa na matendo yaliyokithiri ya unyanyasaji wa wanawake kwa kupigwa na waume zao katika familia nyingi. Naiomba Serikali isimamie sheria hiyo. Pia kumekuwa na ukatili dhidi ya watoto na hasa watoto wa kike ambapo wamekuwa wakibakwa na hasa katika Mkoa wa Njombe. Naomba Wizara ishughulikie suala hili na kuhakikisha ukatili huo unatokomezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za ustawi wa jamii, kwa kuwa kumeendelea kuwa na wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Serikali isaidiane na wadau mbalimbali wanaojitolea kuwahudumia watoto hao kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kutoa huduma bila kuwakatisha tamaa kwa kuwatoza kodi wakati wanatoa huduma kwa watoto hao. Kwa mfano vituo vya watoto yatima visitozwe kodi yoyote. Pia wanapokuwa na vyombo vya usafiri wasitozwe mapato, pia vituo hivyo vimekuwa vikiomba leseni pamoja na kuwa vigezo vyote lakini wamekuwa hawapewi leseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba Serikali ikague vituo vyote nchini ambavyo vinakidhi vigezo wapewe leseni. Pia vituo vinavyofanya kazi vizuri basi wapewe motisha kwa kupata ruzuku. Hivyo naomba bajeti ya Wizara iongezwe ili kitengo hiki cha ustawi wa jamii kifanye kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya ya mama na mtoto; vifo vya akina mama wanaojifungua 556 kwa kila vizazi 100,000 ni idadi kubwa sana. Naiomba Wizara kufuatilia kwa ukaribu tatizo hilo na kuendelea kubaini vyanzo vya vifo hivyo na kutatua changamoto zinazogundulika kuwa ndivyo visababishi. Mfano katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Hospitali ya Kibena ambayo ni Hospitali ya Mkoa ya muda watoto wanaozaliwa njiti ni wengi lakini kutokana na kutokuwa na vifaa vya kuwatunzia watoto hao, wanapoteza maisha. Pia hawana x-ray. Naiomba Serikali itusaidie Wananjombe kuboresha Hospitali ya Kibena ili kuwaokoa wanawake wanaojifungua watoto na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la UKIMWI; watu wanaoishi na VVU wana changamoto kubwa za kupata septrin ambazo zingewasaidia sana kutopata magonjwa nyemelezi na watu hawana fedha za kununua dawa hizo. Naiomba Serikali kuwakatia bima za afya ili kunusuru maisha yao. Maana wakiwa na bima ya afya wanaweza kutibiwa bila matatizo na hivyo itasaidia kurefusha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Serikali kufuatilia suala la mila potofu zinazosababisha UKIMWI uendelee kwa kasi katika Mkoa wa Njombe. Tatizo ni kurithi wajane na mikutano ya mapangoni ambako wanajamiiana bila kujali kama ni ngono salama au laa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iboreshe maslahi ya wafanyakazi kama call allowance na posho nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, michezo mashuleni; napenda kuishauri Serikali kuhakikisha inafufua michezo na utamaduni mashuleni kama ilivyokuwa ikifanyika huko nyuma. Kwani awali kulikuwa na michezo mashuleni kama mpira, kukimbia, kurusha tufe, kuruka kamba na mambo kama hayo. Pia kulikuwa na ngoma za makabila mbalimbali na hizo zilikuwa zina mafunzo mazuri kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, TBC. Naomba kuishauri Serikali kutenga bajeti ya kutosha ili kuinusuru TBC, kwani TBC iko katika hali mbaya sana. Naomba maslahi ya wafanyakazi wa TBC yaangaliwe .

Mheshimiwa Spika, wasanii; naomba kuishauri Serikali kuheshimu kazi za wasanii na kuwasaidia katika kupitisha kazi zao bila kuchukua hatua ndefu za uandaaji wa kazi zao.

Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA); Taasisi hiyo ndio inayoandaa wakuzaji wa sanaa, wasanii, waendeshaji na wasimamizi wa shughuli za sanaa, lakini bajeti inayotengewa ni ndogo na haiendi kwa wakati. Naomba Serikali ipeleke bajeti inayoidhinishwa na Bunge na ipelekwe kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, usalama wa waandishi wa habari. Waandishi wa habari wanaishi katika hali ya wasiwasi, naiomba Serikali ione namna ya kuwalinda waandishi wa habari.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
HE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja hii ya Wizara ya Elimu. Nami niungane na Watanzania wenzangu kuwapatia pole wazazi wa Arusha kwa kufiwa na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miradi ya Wizara ya Elimu hususani fedha za miradi kutopelekwa kwa wakati. Nikiwa mwanakamati wakati tulipotembelea miradi tuligundua kwamba fedha haziendi kwenye miradi au kama zinakwenda basi zinakwenda kwa kuchelewa. Kwa mfano, mradi wa Chuo Kikuu cha Sokoine, mwaka jana walitengewa shilingi bilioni nne lakini mpaka Machi fedha hizi hazikwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo walitengewa shilingi bilioni
9.4 hadi Machi fedha hizi zilikuwa hazijaenda. Niwaombe Waziri wa Elimu na Naibu wake fedha hizi zitakapotengwa safari hii mhakikishe zinakwenda kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee campus ya Mloganzila. Campus hii kwa kweli ni mfano, imekamilika mwaka jana na hii ina vifaa vyote vya kisasa lakini hakuna watumishi. Niombe Serikali kuhakikisha watumishi wanapatikana kwa ajili ya campus hii kwa sababu ni aibu kwetu sisi Watanzania kuwa na campus kama hii halafu haina wafanyakazi, hii inaonesha kwamba hatukuwa tumejipanga. Kwa hiyo, niiombe Serikali ipeleke watumishi katika campus hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee suala la watoto wa kike kurudi shuleni au kutorudi shuleni baada ya kupata ujauzito. Mimi kama mama na kwa yeyote ambaye ana uchungu wa mtoto au uchungu wa kuzaa, nafikiri jukumu la huyu mtu au la mzazi huyu ni kutetea kwamba mtoto wa kike akipata ujauzito kwa sababu anapata ujauzito huu kwa kurubuniwa si kwa kutaka na kwa mazingira magumu na wengi wanakuwa hawana fedha, hiyo ndiyo inayowasababishia kupata ujauzito. Kwa maana hiyo, naiomba Serikali watoto hawa warudi shuleni mara baada ya kujifungua.

TAARIFA...

HE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naikataa taarifa hii kwa sababu akina baba ndiyo mnaosababisha matatizo haya ya watoto wetu kupata ujauzito.

TAARIFA...

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naipokea taarifa hiyo. Kwa asilimia kubwa hata kama sheria imekwishawekwa watu hawachukuliwi hatua yoyote, wanaopata matatizo ni watoto wetu wa kike, ndiyo wanaoathirika. Kwa hiyo, niiombe Serikali kulifikiria suala hilo kwa sababu imekuwa ina kigugumizi kulipitisha jambo hili. Niiombe tafadhali Mheshimiwa Waziri atusikilize safari hii walipokee suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la shule za private. Mimi pia na- declare interest kwamba, nina shule ya private, tena shule hii ni ya watoto yatima. Kwa kweli watu wa shule za private wanapata matatizo mengi sana. Tatizo la kwanza ni kodi nyingi halafu wanafuatiliwa sana wakati watu wa private wanakuwa wana vigezo vyote tofauti na shule za Serikali. Wana Walimu wazuri ambao wamegharamiwa kwa hela nyingi na wanalipwa vizuri, wana vifaa vyote vya shule, wananunua vitabu vyote vya kutosha kwa ajili ya wanafunzi lakini bado Serikali inawabana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepania kuwa na Tanzania ya viwanda, naiomba Serikali ianzishe au itafute wawekezaji kwa ajili ya Mkoa wa Njombe. Njombe ni katika mikoa inayozalisha kwa wingi chakula kama vile mahindi, ngano, alizeti na matunda. Hivyo, naiomba Serikali itafute wawekezaji kwa ajili ya kiwanda cha kusindika matunda, unga wa mahindi na unga wa ngano Mkoani Njombe. Pia naiomba Serikali ianzishe au itafute wawekezaji kwa ajili ya viwanda vya karatasi, lami, kiwi na toothpicks.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kuwa Mkoa wa Njombe unazalisha viazi kwa wingi, naiomba Serikali itafute wawekezaji kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza bidhaa zinazotokana na viazi kama crisps, katika Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wafanyabiashara wananyanyasika sana na TRA kutokana na kuwa na tozo nyingi, naiomba Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wafanyabiashara wasikatishwe tamaa kwa kukimbizwa na tozo nyingi na hasa kwa wafanyabiashara wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wadogo wadogo (wajasiliamali) wa Njombe watafutiwe eneo rafiki kwa ajili ya kufanyia biashara zao. Napendekeza eneo hilo liandaliwe maeneo ya stendi mpya iliyopo Mji Mwema.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uti wa mgongo, bila kilimo hatuwezi kufikia lengo letu la Tanzania ya Viwanda. Ukiangalia bajeti ya kilimo kama kweli kilimo ni uti wa mgongo bajeti ni ndogo sana, asilimia 4.9 ambayo inakwenda kuwasaidia Watanzania ambao ndiyo asimilia kubwa ya wakulima, asilimia 70. Bajeti hii ni ndogo naiomba Serikali iongeze bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushindani wa soko usio wa haki. Kuna ushindani wa soko usio wa haki. Kwa mfano, Mkoa wa Njombe wanazalisha viazi kwa wingi, viazi hivi hawaruhusiwi kuweka zaidi ya kilo mia moja wakati Wakenya wanaweka zaidi ya kilo mia moja na wanauza soko moja. Naiomba Serikali iliangalie suala hili kwa sababu Watanzania wanapata hasara, viazi vyao havitoki, Wakenya wanaweka vingi na viazi vyao vinatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama za upimaji wa udongo. Katika Mkoa wa Njombe wakulima wanachukua udongo ule kupeleka Mbeya kwa ajili ya kupima na udongo huu unapimwa kwa unit moja kwa Sh.75,000/=, kila shamba linatakiwa liwe na unit nane, kwa hivyo shamba moja linagharimiwa kwa shilingi laki sita na elfu saba. Kwa kweli wakulima hawataweza kuendelea na suala hili la upimaji wa udongo kwa sababu ya gharama hizo. Naiomba Serikali iwapunguzie au iwasaidie wakulima wa Njombe udongo huu upimwe kule kule Njombe badala ya kusafirishwa kwenda Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tozo. Ninaishukuru Serikali kwamba katika hotuba ya Waziri umeeleza kuondoa tozo mbalimbali, ninashauri kwamba tozo hizi zingeorodheshwa zote, halafu tuone ni tozo zipi zinatoka na tozo zipi zinabaki. Kwa sababu ukiangalia kwa mfano, wakulima ambao wana vyama vyao vya ushirika wametolewa ile tozo ya Sh.500/= isiwepo, nafikiri ni vema kuondoa zile tozo kubwa zinazotozwa na Serikali kuliko kuziondoa zile tozo ambazo ni za wakulima wadogowadogo, kwa sababu zile zitawasaidia kwenye vyama vyao vya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaiomba Serikali iliangalie suala hilo tena kwa sababu ni kweli tozo hii imetolewa kulingana na hotuba yako lakini bado wakulima wadogo ambao wana vyama vyao vya ushirika watapata hasara, kwa sababu hawatapata kitu chochote cha kuendeshea vyama vyao vya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbegu za viazi. Mwaka jana kulikuwa na tatizo katika Mkoa wa Njombe wa kuunguliwa viazi kutokana na hali ya hewa, hawakupata kabisa viazi na Serikali iliahidi kuwasaidia na wakawa wamesaidiwa kiasi fulani cha mbegu. Zile mbegu walizosaidiwa kwa kweli hazifai na siyo nzuri, hivyo wakulima hao wamepata hasara vile viazi haviuziki kwa sababu zile mbegu siyo kama mbegu ambazo walizoea kuzitumia miaka yote. Naiomba Serikali iwasaidie wakulima hawa kama inawezekana kufika Njombe na kuona ni namna gani wanaweza kuwasaidia wapate mbegu ambazo ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Kilimo mpaka sasa hivi siielewi ni namna gani inawaisaidia wakulima. Mwaka jana tulipata maelezo mazuri tene ilikuwa semina nzuri sana ya Wabunge wote tulielekezwa kwamba benki hii itakwenda katika mikoa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa hivi katika Mkoa wangu wa Njombe wakulima wanalalamika na wanahangaika sana kwa sababu benki hiyo ingeweza kuwasaidia sana wakulima kupata mikopo na kuweza kuboresha kilimo chao ili waweze kupata maao kwa wingi na iwasaidie angalau kupanda kwa uchumi wao na Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe ni kati ya Mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi, tatizo kubwa ninaloliona ni kwamba hawana maghala ya kutosha. Kuna ghala moja Makambako. Naishauri Serikali kuhakikisha maeneo kama haya na hasa Nyanda za Juu Kusini na kila Mkoa unakuwa na ghala za kutosha kwa sababu vyakula wanavyozalisha vinaishia kuoza au kutawanya ovyo kwa sababu hawana ghala. Ghala zingesaidia sana angalau kuhifadhi chakula na kusaidia nchi nzima

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo; nashukuru kwamba Serikali imetamka sasa pembejeo na hasa mbolea zitawekwa madukani, ninachoomba na kusisitiza ni utekelezaji. Mbolea iwekwe madukani pamoja na pembejeo zingine ziwekwe madukani ili kusudi wananchi hawa waweze kununua kwa urahisi na kwa wakati wowote hasa kwa Mkoa wa Njombe karibu mwaka mzima wanalima. Kwa hivyo, kama watakuwa na mbolea hizi madukani maana yake watazalisha kwa wingi na muda wote hawatakuwa na shida na bei za pembejeo hizi zitakuwa zimeshuka kwa sababu zitakuwa madukani. Kwa hivyo, niiombe sana Serikali na nisisitize utekelezaji wa suala hili ambalo Serikali yenyewe imeahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mifugo, wafugaji na wakulima. Kuna maeneo yanayopakana na Mbeya ambalo ni eneo la Wilaya ya Makete, kuna tatizo la wakulima na wafugaji, wakulima wanalima vyakula vyao lakini wafugaji wanapeleka mifugo yao wanalisha mashambani. Naiomba Serikali kwa sababu nafikiri ni maeneo mengi ambapo tatizo hili lipo, suala hili lishughulikiwe kwa sababu linawakatisha tamaa sana hasa wakulima, kwa kuwa wanalima kwa bidii halafu ng’ombe wanakuja wanakula, kwa hivyo tunawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naiomba Serikali isaidie kutatua mgogoro huu wa wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iongeze tozo ya sh.50/= kwenye mafuta ili isaidie masuala ya maji, asilimia 70 iende vijijini na asilimia 30 mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, bili za maji ni kubwa sana hasa katika Mkoa wa Njombe na hasa katika Halmashauri ya Njombe Mjini. Naomba Serikali ifuatilie suala hili la bili lifungwe, maana wananchi wanalalamika sana kwa sababu ya bili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Njombe ni tajiri wa mito, lakini wananchi wanahangaika sana maji hayatoki; hata Njombe Mjini maji hayatoki, lakini watu wanaendelea kulipa bili kubwa. Maeneo ambayo maji hayatoki ni Mtaa wa Mpechi, Joshoni, Idunditanga, Sido, Ramadhani, Kibena na maeneo mengine. Naiomba Serikali iwasaidie wananchi hawa kwa kuwaboreshea miundombinu ya maji ili maji yaweze kutoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vingi vya Mkoa wa Njombe havina maji. Katika Wilaya ya Wanging’ombe kulikuwa na maji huko nyuma, lakini kwa sasa mabomba haya hayatoi maji, yameshaharibika; akinamama wanapata shida, wanakwenda umbali mrefu kutafuta maji. Naomba miradi hiyo ya maji ifike vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashairiki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ishughulikie suala la Watanzania wanaonyanyaswa katika nchi za nje hasa huko Uarabuni. Kuna mabinti wengi wanateswa na hata wengine wanauawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi hawana uelewa wa Wizara, hivyo kukosa fursa. Hivyo naiomba Wizara kutoa elimu kwa wananchi wa Tanzania kazi ya Wizara hii. Pia majengo mengi ya Balozi ni chakavu, naiomba Serikali ikarabati majengo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la diaspora bado halina nguvu, ninaiomba Serikali ilichukulie kwa umuhimu kwani inachangia katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwa kuwapa fursa mbalimbali za uchumi kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa bajeti ya Wizara huchelewa, naiomba Wizara kuhakikisha bajeti inatolewa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wengi nchini ni wajasiriamali, mfano akina mama wana viwanda vidogo vidogo kama vile vya kushona vikapu, kutengeneza vinyago, vyungu na vitu vingine, ninaiomba Wizara iwakumbuke akina mama ili waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi na waweze kukuza uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe kipaumbele katika kulipa michango ya nchi yetu kwenye Taasisi za Kimataifa ili kuepusha kukwamisha uendeshaji wa taasisi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kuwapongeza Waziri na Naibu wake pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri mnayoifanya.

Pamoja na kazi hii nzuri mnayoifanya naomba nielezee matatizo yaliyoko hasa katika Mkoa wangu wa Njombe nikianza na migogoro ya wananchi na watu wa TANAPA. Kwa mfano, nikiangalia maeneo ya Wanging’ombe, Kijiji cha Ruduga kuna tatizo la wananchi na watu wa TANAPA, mara kadhaa wamekuwa wakiwasumbua sana na kuna kipindi waliwakatia mazao yao.

Kwa hiyo, nimuombe Waziri kufika maeneo yale kutusaidia kutatua tatizo hili kwa sababu limekuwa ni tatizo la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa sasa wametishiwa kwamba watatakiwa kuhama kwenye kile Kijiji cha Mpanga. Sasa wanakaa kwa wasiwasi wana hofu kubwa kwamba watahama na wana shida kwa sababu ya hofu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la migogoro katika Wilaya ya Makete. Katika Wilaya ya Makete kumekuwa na migogoro kati ya Hifadhi ya Kitulo na wananchi wa kijiji cha Misiwa. Watu wa hifadhi wameweka beacons kwenye mashamba ya wananchi wa maeneo yale ya Kitulo, wanasema kwamba wanapanua hifadhi. Hivyo, nimuombe Waziri kutusaidia suala hili angalau hawa wananchi kuwaondoa hofu maana yake nao sasa hivi wanashindwa kufanya uzalishaji kwa sababu wanaona wanaendelea kuingiliwa, mwisho wa siku hata mashamba yote yatachukuliwa, ninawaomba sana mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niongelee suala la migogoro Makete na Wanging’ombe. Kuna tatizo la mipaka kati ya Wanging’ombe na Makete, vilevile kuna tatizo kati ya shamba la Ludodolelo, kuna mwekezaji ambaye yuko katika shamba la Ludodolelo ambaye anawasumbua sana wananchi, sasa wanavutana kati ya wananchi na yule mwekezaji. Kwa hiyo, niwaombe Serikali mtusaidie mfike maeneo yale kusudi tuweze kutatua tatizo hili. Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Mradi wa Umeme wa Makaa ya Mawe Mchuchuma; Serikali imekuwa na kigugumizi cha kuanza utekelezaji wa mradi wa Mchuchuma. Naomba Serikali sasa ianze mara moja kutekeleza Mradi wa Mchuchuma na Liganga kwa sababu ahadi zimekuwa kwa muda mrefu lakini hakuna utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madini na gesi, naiomba Serikali ihakikishe inakusanya mapato kwenye madini kama kodi za wawekezaji kwani tuna migodi mingi lakini hatukusanyi mapato mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kodi, vyanzo vyote vya mapato vimechukuliwa na Serikali Kuu. Halmashauri zinashindwa kujiendesha kwa sababu hazirudishwi kwenye Halmashauri. Hii inakatisha tamaa kwani watendaji wetu wanashindwa kabisa kuendesha Halmashauri; Halmashauri zinakufa. Naiomba Serikali irudishe vyanzo hivyo vya mapato kwenye Halmashauri zetu ili utendaji wake uwe bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima. Tunapanga kwenda kwenye Tanzania ya viwanda, hatuwezi kwenda kwenye Tanzania hiyo kama hatujaboresha kilimo. Bado Watanzania tunalima kwa mikono, pembejeo ni gharama, bei ya vyakula ni chini. Tunawezaje kuingia kwenye ushindani wa masoko? Kwa vyovyote vile hakuna soko tena. Matokeo yake hatuwezi kuondoa umaskini katika nchi hii. Naiomba Serikali ione namna gani itaboresha kilimo na kuwasaidia wakulima. Naiomba Serikali ipunguze bei za pembejeo na pembejeo zifike mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wananyanyasika sana, wanabanwa kila upande, wanatozwa kodi kubwa ambayo hailingani na mitaji yao, hasa wafanyabiashara wadogo. Wafanyabiashara wengi wamefunga biashara zao kwa sababu ya usumbufu mkubwa wanaoupata hapa nchini. Naiomba Serikali iangalie namna ya kuwatoza kodi wafanyabiashara hawa bila kuwanyanyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja hii ya uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa mitaji; Mashirika mengi na Taasisi za Umma hazina mitaji ya kutosha. Mfano Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). Benki hii ingekuwa na mtaji wa kutosha ingepelekwa katika Mikoa yote ya Tanzania na ingeweza kuwainua Watanzania walio wengi, maana wakulima wengine kuliko wafanyakazi na wafanyabiashara, lakini Serikali haijachukua jitihada ya kutosha kuisaidia benki hiyo kwa kuipa mtaji wa kuweza kuendesha benki hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, benki ilianza na mtaji wa shilingi bilioni 60 ingawa mtaji ulioidhinishwa ni shilingi bilioni 800. Kiasi hicho ni pungufu kwa asilimia 92.5. Serikali inaishia kuahidi lakini haitekelezi. Naiomba Serikali kutimiza ahadi yake ya kupeleka pesa yote ambayo iliidhinishwa kwa ajili ya uendeshaji wa Benki ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kutolipa madeni yake kwa wakati; Mashirika mengi yanashindwa kujiendesha na kukamilisha miradi yake kwa ufanisi kutokana na Serikali kukopa lakini inachelewa kulipa madeni hayo. Naishauri Serikali kulipa madeni yake kila inapokopa. Hii inasikitisha kuona Serikali ndiyo inayodidimiza uchumi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikikopa fedha zake kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Matokeo yake imedhoofisha mifuko hiyo, mfano PSPF. Naiomba Serikali ijirekebishe namna nyingine Serikali itadidimiza uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Kwanza, naipongeza Kamati kwa ufuatiliaji wa miradi mbalimbali na kwa ripoti nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, bei za gesi ziko juu sana mpaka wananchi wanashindwa kununua gesi hiyo. Naomba Serikali ione ni namna gani bei zinapungua na kuwawezesha kununua kwa bei nafuu. Kwa namna nyingine watu wataendelea kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo kwa ajili ya kutengeneza mkaa na kutumia kuni kwa ajili ya kupikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO); nashukuru Serikali inajitahidi kupeleka umeme hadi vijijini, lakini kuna tatizo limezuka la kukatika umeme kila mara. Mfano, Mjini Njombe na baadhi ya maeneo hapa Dodoma hasa eneo la Kisasa umeme unakatika mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ione namna gani inarekebisha miundombinu ya umeme ili usikatike mara kwa mara, iimarishe miundombinu kama transformer na nguzo na waya wa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC); bei za mafuta zinapanda kila kukicha hii inatokana na kuwa tunategemea kutoka nje maana sisi hatuna matanki kwa ajili ya kuhifadhi mafuta hayo. Naiomba Serikali iweke matanki yake kwa ajili ya kuhifadhi mafuta haya ili bei ishuke.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina madeni TANESCO; hii inasababisha uendeshaji unakuwa mgumu na Shirika limekuwa likijiendesha kwa hasara. Serikali iwachukulie hatua watu wenye madeni sugu lakini pia Serikali yenyewe ilipe madeni yake

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na migogoro ya ardhi katika maeneo mengi kwa sababu hayajapimwa na wanapotokea Wawekezaji huyachukua maeneo makubwa na wananchi wanabaki hawana ardhi. Pia Wawekezaji wengi wanachukua maeneo makubwa lakini hawajayaendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; Kanisa la KKKT katika Halmashauri ya Njombe Mjini ambao wamemilikishwa eneo la hekta 120 wanashindwa kuliendeleza. Naiomba Serikali ichukue maeneo ambayo hayajaendelezwa na yarudishwe kwa wananchi

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA, Shirika hili linawasumbua sana wananchi, mipaka iliyowekwa wameongeza na kuingia kwenye maeneo ya wananchi na kusababisha migongano kati ya wananchi na TANAPA. Niombe Serikali kuwaacha wananchi kwenye mipaka yao iliyowekwa zamani. Mfano, Wilaya ya Wanging’ombe, Kata ya Luduga kuna migogoro hiyo ya mipaka Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali kuongeza bajeti ya Wizara ya Ardhi ili kuweza kupima ardhi na kupanga matumizi yanayofaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutoa bei elekezi kwa wakulima wakati pembejeo zinauzwa kwa bei ya juu mfano, mbolea ya DAP Sh.60,000/= na Urea ni Sh.50,000/= siyo sahihi kabisa. Wananchi wamehamasishwa kulima mazao mbalimbali lakini bei za mazao hayo iko chini sana. Mahindi yanauzwa hadi Sh.3,000/= mpaka Sh.5,000/= kwa debe. Kwa kweli hii inasikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ione ni namna gani itawatafutia soko la uhakika la mahindi na mbaazi na kushusha bei ya pembejeo.

Mheshimiwa Spika, kilimo ni uti wa mgongo na asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima, lakini Wizara hii haipewi bajeti ya kutosha itakayosaidia kuleta pembejeo za kutosha na kwa wakati. Naiomba sana Serikali itenge bajeti ya kutosha na kuitoa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, naiomba Serikali ione ni namna gani inatenga maeneo ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ng’ombe wanazagaa ovyo ovyo kwenye maeneo ya wakulima, watu wamekuwa wakiuana. Naishauri Serikali ifanye haraka kutenga maeneo, mfano nimeshuhudia wakulima na wafugaji wanapigana pale Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu uwasilishaji wa Sheria Ndogo Bungeni; kwa kuwa kuna sheria ndogo ndogo ambazo zina dosari, naishauri Serikali kuleta hapa Bungeni na kufanya marekebisho hapa Bungeni kwa mfano; Sheria ya Vyombo vya Usafiri ambayo inatumika kwa vyombo vyote vya usafiri kuanzia bodaboda hadi magari makubwa. Kama ni kulipa faini wote wanalipa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Sheria ya Ndoa inayoruhusu watoto chini ya miaka 18 kuolewa ibadilishwe na kuweka umri wa kuolewa uwe miaka 18 na siyo chini yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Serikali ilete marekebisho ya Sheria ya Ardhi ambayo itawaruhusu wanawake kumiliki ardhi kuliko ilivyo sasa kwamba ni wanaume tu wanamiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya UKIMWI imepitwa na wakati, sera hii ya UKIMWI imepitwa na wakati kwani sera ya mwaka 2001 naishauri Serikali ihuishe sera hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya masuala ya UKIMWI ni ndogo nasikitika kuona Serikali inatenga fedha kidogo wakati ugonjwa huu ni janga la kitaifa. Hii inaonyesha kuwa Serikali haina mpango na kuona ugonjwa huu unatokomezwa. Naishauri Serikali kuhakikisha inatenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huu mbaya. Pia fedha zikitengwa zipelekwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya madawa ya kulevya; naishauri Serikali itenge pesa kwa ajili ya kujenga sober house ili kuwanusuru vijana wetu ambao wanashindwa kwenda kwenye private sober houses ambako wanatoza shilingi laki 400,000 kwa mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo dume unachangia sana katika ongezeko la ugonjwa wa UKIMWI. Hii inatokana na akinamama kutokuwa na uhuru na miili yao. Mfano, baba mlevi anatumia nguvu au analazimisha mama kufanya tendo la ndoa. Naomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, lakini pia kupitia taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iandae program maalum mashuleni kuanzia shule za misingi, sekondari ya vyuo zinazohusika na masuala ya UKIMWI. Fedha zinazopelekwa kwenye mkoa kwa ajili ya semina au mafunzo halmashauri moja ili zitumike kwa ajili ya kununua dawa za magonjwa nyemelezi na virutubisho.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika hoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Walimu; tatizo la upungufu wa Walimu hasa katika shule za msingi ni kubwa sana. Njombe Mjini inakosa Walimu 454. Nchi hii inaenda kuua elimu kwa sababu hatuwezi kuwa na elimu bora kama hatuna Walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia walimu hawa walipandishwa madaraja wakawekewa pesa za kupandishwa madaraja haya, lakini baada ya mwezi mmoja wakasitishiwa pesa hizo. Naiomba Serikali ipeleke Walimu wa kutosha mashuleni lakini pia Walimu wapandishwe madaraja yao na wapandishiwe pesa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo mabaya ya mitihani; matokeo ya mitihani ni mabaya sana hasa shule za Serikali. Shule zinazoongoza kuanzia ya kwanza hadi ya 10 ni shule za binafsi. Hata hivyo, shule za binafsi zinakandamizwa sana kana kwamba siyo Watanzania. Naomba Serikali itambue kuwa shule binafsi zinalipatia sifa na heshima Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itende haki kwa shule za private na za Serikali kwa sababu uendeshaji wa shule binafsi ni mgumu sana, kwa kweli ni huduma tu. Mbaya zaidi kwa wale wanaohudumia watoto yatima na wanaoishi mazingira hatarishi lakini wanasoma katika shule hizo, lakini Serikali inawatoza michango mingi kama ya ukaguzi Sh.5,000 kila mtoto, Sh.15,000 ya Mitihani ya Taifa na Sh.1,000 kila mtoto kwa ajili ya michezo. Naiomba Serikali ione ni namna gani inawasaidia hasa shule za watoto yatima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya elimu ya juu ni kitendawili; vijana wengi wenye vigezo vya kupata mikopo wanaachwa. Naiomba Serikali kufanya tafiti kwa umakini namna ya kuwatambua vijana hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; naomba watumishi wa afya waajiriwe wa kutosha na hasa kwenye vituo vya afya. Pia majengo ambayo yamejengwa na wananchi kama Vituo vya Afya na Zahanati, basi Serikali isaidie kumalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Naibu Naibu Spika, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao; inasikitisha sana kushuhudia matukio yanayohatarisha maisha ya raia na mali zao na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa wananchi. Mathalani, kumekuwa na kupotea kwa wananchi wengi katika maeneo mbalimbali kama vile kupotea kwa Ben Saanane na wengine. Naiomba Serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha inadhibiti matukio haya.

Mheshimiwa Naibu Naibu Spika, ulinzi na usalama wa Wabunge; kwa kweli inasikitisha sana kwa kuwa Wabunge hawana ulinzi wowote na hata maeneo wanayoishi hayana ulinzi wowote. Naomba Serikali ijifunze kutoka nchi nyingine namna Wabunge wanavyolindwa wao na mali zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inasikitisha kuona Wabunge wanajilinda wenyewe na hii imehatarisha maisha ya Wabunge na hata kupelekea Wabunge hao kuvamiwa na kupigwa risasi mfano, Mheshimiwa Tundu Lissu, aliyepigwa risasi 38 hapo mwaka jana. Naiomba Serikali kuleta marekebisho ya Sheria ili kiingie kipengele cha kuweka walinzi kwa ajili ya Wabunge, siyo hapa Bungeni tu bali hata maeneo wanayoishi Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Naibu Spika, kukamatwa Wabunge kwenye maeneo ya Bunge, kumekuwa na kamata kamata Wabunge kwenye maeneo ya Bunge. Huu ni udhalilishaji wa Wabunge, maana ya kinga za Bunge ni nini? Naiomba Serikali ilete marekebisho ya sheria kuheshimu maeneo ya Bunge ambapo Wabunge wana kinga pia askari wawe na heshima kwa Wabunge na hasa wawapo kwenye Majimbo yao, maana askari wanawadhalilisha Wabunge. Mfano, mnamo tarehe 16 Novemba, 2017, Mbunge wa Viti Maalum alidhalilishwa na askari kule Kilolo Kata ya Kimala.

Mheshimiwa Naibu Naibu Spika, mrundikano wa mahabusu na wafungwa; katika magereza mengi hapa nchini kuna mrundikano wa mahabusu ambao wakati mwingine hawana kesi yoyote, bali wanajaza magereza, mfano, Gereza la Njombe Mjini kuna mrundikano wa mahabusu, naomba kuishauri Serikali mahabusu ambao hawana kesi, kesi zao ziharakishwe kusikilizwa ili kuondokana na mrundikano wa wafungwa.

Mheshimiwa Naibu Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uchunguzi wa kina kabla ya kutoa adhabu kwa Wabunge; kumekuwa na adhabu mara kwa mara kwa Wabunge na hasa Wabunge wa Upinzani, nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini? Nimegundua kuwa Wapinzani wanapoona mambo fulani yanakwenda isivyotegemewa au bila haki kutendeka ndio maana inawafanya kupata hasira na kuropoka au kutenda vitendo kinyume na maadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba kuishauri Serikali kuchunguza ni kwa nini mambo haya yanatokea. Serikali ikitenda haki na usawa na ikiwasikiliza hasa yale wanayoshauri kwa manufaa ya Taifa, watu hawataweza kutenda matendo kinyume na maadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda wa adhabu; naomba Wabunge waliopata adhabu mwaka jana walipata adhabu ya muda mrefu mno. Naomba adhabu zipunguzwe maana Wabunge wanakosa uwakilishi kwenye majimbo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, upendeleo; katika kupeleka watu kwenye maadili wanapelekwa wa upande mmoja, ni wale wa kutoka Upinzani tu. Mara nyingi nimesikia maneno ya kuudhi kutoka upande wa Chama Tawala hawachukuliwa hatua yoyote. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LUCIA U. M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niachangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu. Kumekuwa na ongezeko kubwa la usajili wa watoto wengi wa darasa la kwanza, lakini hakuna ongezeko la Walimu, madarasa na madawati. Naomba kuishauri Serikali kuajiri Walimu wa kufundisha, hasa madarasa ya awali, darasa la kwanza na la pili, ambapo Walimu wanaofundisha madarasa hayo ni wachache na shule nyingine hakuna kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naishauri Serikali kuwapa moyo wananchi ambao wamejitolea kujenga madarasa, lakini wanakatishwa tamaa na viongozi wanaposhindwa kuwasaidia wanapokuwa wamejenga majengo hayo hadi kufikia kiwango fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kusimamishwa wazazi kuchangia, kumejitokeza tatizo kubwa la kupunguza mitihani ya mwaka mfano, katika Mkoa wa Njombe kila mwaka ratiba ya mitihani ya mock hutolewa mapema mwanzoni mwa mwaka, lakini safari hii haikutolewa ratiba hiyo. Hadi mwezi huu Aprili hakuna taarifa yoyote ya mitihani ya mock. Naomba suala hili lifuatiliwe ili watoto wetu waweze kujipima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji ni kubwa sana nchi nzima. Kuna maeneo ya vyanzo vizuri vya maji na mito ya kutosha, lakini bado maeneo hayo yana matatizo makubwa ya maji. Mfano, Mkoa wa Njombe kuna vyanzo vya maji vya kutosha, pia mito ya kutosha, lakini bado kuna tatizo kubwa la maji, hasa maeneo ya Makambako, Wanging’ombe, Njombe Mjini. Naishauri Serikali kuwa na mawasiliano ya karibu na wananchi wa maeneo husika ili waweze kuweka mikakati ya kuibua njia za kupeleka maji katika maeneo yao. Pia, wawawezeshe kwa kuwapelekea wataalam na vifaa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna tatizo kubwa la uchakavu wa mabomba ambayo yanapasuka kila siku. Mfano, hapa Dodoma maeneo ya Kisasa, mabomba yanapasuka kila siku na kusababisha upotevu wa maji. Naomba mabomba hayo yabadilishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi na usalama; kumekuwa na matukio yanayohatarisha maisha ya raia. Kwanza kumekuwa na mauaji maeneo mengi ya nchi yetu, watu wamekuwa wakiuawa na kuwekwa kwenye mifuko na kutupwa baharini. Naiomba Serikali ichukue hatua haraka ya kukomesha mauaji hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na TARURA, kwa kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya TARURA ni ndogo na barabara za vijijini na mitaa ni nyingi na zinahitaji matengenezo makubwa, naomba Serikali itafute vyanzo vingine vya mapato kwa ajili ya TARURA kwa ajili ya kuboresha barabara vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za vijiji na mitaa katika Mkoa wa Njombe ni mbaya, hazipitiki. Naiomba Serikali kuhakikisha fedha hizo za TARURA zinatengeneze barabara hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutengeneza barabara za Itoni - Ludewa, Njombe – Makete na Kibena – Lupembe – Madeke ni ndogo. Naiomba Serikali iongeze fedha hizo lakini pia fedha hizo zitolewe kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Njombe ni kibovu. Kiwanja ni pori ambalo linasababisha vibaka na majambazi katika viwanja hivyo. Pia wafanyakazi wa viwanja vya ndege wanapokea rushwa kwa wananchi ili kuweza kukatisha kwenye viwanja hivyo ambapo bado uhalifu ni mkubwa. Naiomba Serikali itengeneze kiwanja hicho haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uvunaji maji, mwaka huu kuna mvua kubwa zinanyesha nchi nzima, lakini hakuna juhudi zozote za Serikali kuandaa mabwawa ya kutunza maji haya kwa ajili ya kutumia wakati wa kiangazi. Naiomba Serikali iweke mkakati wa makusudi wa kutengeneza mabwawa makubwa yatakayotumika kwa ajili ya kuhifadhi maji hayo ambayo yatatusaidia kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya michezo mashuleni, viwanja vingi vya michezo nchini hasa viwanja vya shule vimechukuliwa na taasisi mbalimbali wakiwemo wanachama wa CCM, matokeo yake shule zinahangaika hakuna sehemu ya kuchezea watoto wa shule. Naomba Serikali ihakikishe viwanja hivyo vinarudishwa kwenye shule ili wanafunzi wetu waweze kuvifurahia. Kwa mfano, uwanja wa sabasaba ulioko Njombe uliochukuliwa na CCM, uko kwenye eneo la shule ya msingi ya Sabasaba na Mpechi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo mashuleni watoto wetu wa shule za msingi na sekondari wamelemaa, awali kulikuwa na michezo hata mchakamchaka lakini hivyo vyote vimefutwa, naomba Serikali irudishe mchakamchaka mashuleni na itiliwe mkazo somo la michezo na mazoezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maadili katika nchi yetu yameporomoka, naomba somo la maadili lifundishwe mashuleni kuanzia shule za msingi hadi vyuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iwasaidie wasanii kuboresha kazi yao badala ya kuwaadhibu kwa kuwafungia. Tutoe maelekezo vizuri badala ya kutumia nguvu, pia tusiache wasanii kuonesha sanaa zao kama nyimbo kwa muda mrefu halafu baadaye tunawafungia wakati tayari watu wamekwisha sikia nyimbo hizo, tuwasaidie wasanii wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu michango iliyokithiri kwa shule za private. Shule za msingi na sekondari za private wanatozwa michango mingi mno. Shule za private za msingi zinatozwa shilingi 1,000 kila mtoto kwa ajili ya ukaguzi wa shule; shilingi 1,000 kila mtoto kwa ajili ya michezo; shilingi 3,500 kwa kila mtihani wa mock wa kila mtoto; shilingi 15,000 kila mtoto kwa mitihani ya kitaifa. Hata shule zinazosaidia watoto nao wanatozwa michango hiyo. Naiomba Serikali ipunguze utitiri huu wa michango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kukariri masomo. Watoto wengi wanaokwenda kusoma kwenye shule za private wanabadilika na kuwa na matokeo mazuri kutokana na utaratibu wa kukariri. Hivyo watoto wengi wanakazana
kusoma kwa sababu wanaogopa wasiposoma kwa bidii watarudia. Hivyo wanakazana sana. Naiomba Serikali irudishe utaratibu wa kukariri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watoto ambao wana vigezo vya kupata mikopo lakini hawapati mikopo hiyo. Naiomba Serikali iangalie wanafunzi wenye vigezo wapewe mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mmomonyoko wa maadili katika nchi yetu, naiomba Serikali kuingiza kwenye mitaala suala zima la maadili. Kwa kuwa wanafunzi wa kike wanapata ujauzito kutokana na kuishi mbali na makazi yao, lakini pia wanafunzi wengi wa kike wanapanga mitaani, naiomba Serikali ihakikishe inaongeza hosteli kwa ajili ya watoto wetu wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iingize masomo ya ujasiriamali kwenye mitaala ili baadae watoto wetu wajue namna ya kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika hoja hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa viwanda katika Mkoa wa Njombe, kwa vile Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati wa Tanzania ya viwanda, naiomba iandae mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Njombe ili wawekeze katika viwanda. Tatizo kubwa ni kwamba inawabana sana wafanyabiashara kwa taratibu ngumu zinazosababisha watu waone vigumu kuanzisha viwanda. Pia zile hatua za uanzishwaji wa viwanda ni ngumu na ni ndefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa jokofu la kuhifadhia matunda (maparachichi), Mkoa wa Njombe unazalisha matunda ya parachichi kwa wingi lakini hakuna jokofu la barafu kwa ajili ya kuhifadhi matunda hayo. Naiomba Serikali itusaidie kutafuta fedha ya kununulia jokofu hilo au kupata mwekezaji mkubwa anayeweza kutufadhili jokofu hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa soko la mahindi; wakulima wa nchi nzima wanahamasika kulima mahindi kwa wingi lakini tatizo kubwa hakuna soko, mfano wakulima wa Mkoa wa Njombe walipata mahindi kwa wingi lakini mahindi hayo yanaoza. Naiomba Serikali ifungue mipaka ili wananchi wa Mkoa wa Njombe wauze mahindi yao nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja hii ya maji na umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miundombinu mibovu ya maji katika Halmashauri zetu. Katika Halmashauri zetu, miundombinu ya maji ni mibovu sana ndiyo maana kuna upotevu wa maji. Kwa mfano, katika Ripoti ya CAG ya mwaka 2016/2017 inaonesha upotevu wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 huko Babati peke yake. Tuone ni namna gani tunapata hasara ya upotevu wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hapa Dodoma peke yake, karibu kila siku mabomba yanapasuka. Hii inatokana na kuweka mabomba yenye kiwango cha chini. Namwomba Mheshimiwa Waziri kufuatilia suala hili na kuhakikisha upotevu huu wa maji unadhibitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije suala la bili za maji. Kuna watu wanaletewa bili za maji mpaka shilingi milioni mbili kwa mwezi, kwa kweli ni janga. Tumekuwa tukilalamika kila siku tukaambiwa hizo bili zitarekebishwa, lakini tatizo linaendelea. (Makofi)

Naomba kuuliza kwa Mheshimiwa Waziri, ni tatizo gani linalosababisha hizi bili ziendelee kupanda siku hadi siku. naiomba Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri, suala hili la bili za maji lishughulikiwe haraka iwezekanavyo kwa sababu wananchi wetu wanaumia. Hata sisi Waheshimiwa Wabunge wengi kati yetu tunapata bili hizo kubwa na ukienda kuwaonesha wanasema tunarekebisha, lakini hawarekebishi. Sasa kama inatokea hivi kwetu sisi Wabunge, je, wananchi wa kawaida inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la mikataba mibovu ya maji. Karibu nchi nzima kuna tatizo la mikataba mibovu na kusuasua kwa miradi ya maji. Nitoe mfano wa mikataba mibovu ya maji ambayo baada ya muda mfupi inavunjwa. Mfano, Mkoa wangu wa Njombe kuna mradi wa Lugenge, Utalingolo na Ihalula. Mradi huu ni wa mwaka 2013. Yule mkandarasi aliyewekwa kukamilisha mradi huu, mkataba ule ulivunjwa baada ya miezi mitatu na baada ya kuvunja ule mkataba yule mkandarasi alishitaki na baada ya kushitaki alishinda kesi yake. Hata baada ya kushinda hadi leo hii hajalipwa pesa zake, alitakiwa alipwe shilingi milioni hamsini hajalipwa na mradi huu hadi leo hakuna kinachoendelea na mabomba yamelala tu hapo. Naomba suala hili Mheshimiwa Waziri alifuatilie haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine vilevile wa Lwangu umetekelezwa na mkandarasi na hela zile za mwanzo zimepotea. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri afuatilie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ukosefu wa maji. Ukosefu wa maji ni janga la nchi hii. Ukiangalia maeneo mengi yana vyanzo vya maji, yana maji ya kutosha, lakini bado kunakuwa na tatizo la maji. Kwa mfano, Njombe inazungukwa na mito ya maji, lakini nenda pale Njombe Mjini unakuta watu wanapata maji mara moja kwa wiki.

Mheshimiwa Waziri ni tatizo gani? Ninaomba tafadhali fuatilia suala hili kuhakikisha hiyo miradi ambayo mmeahidi, basi itekelezwe kwa wakati. Tumekuwa tukiahidiwa sasa muda mrefu lakini hakuna utekelezaji. Siyo hiyo tu, kuna Wilaya ya Ludewa, vijiji vya Mkomang’ombe wananchi wale kwa kweli wanatia huruma. Wamekuwa wakiahidiwa kupatiwa maji… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi wa amani, Askari wetu hasa Wanajeshi wanaotumwa kwenda nchi za nje kusaidia kulinda, wamekuwa wakipoteza maisha yao huko nje, wanarudi maiti na familia zao zinapata shida. Naiomba Serikali iwafikirie wajane na familia za wanajeshi hao wanaofariki kwenye mapambano ili wapate pensheni hadi wanapofariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira. Kuna vijana wapatao 2,000 waliahidiwa kupata ajira kwenye Jeshi lakini hadi sasa vijana hao hawajaajiriwa. Naiomba Serikali iwapatie kipaumbele vijana wetu walioahidiwa kupata ajira wapate ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi mipakani; kumekuwa na tatizo la ulinzi mipakani watu wamekuwa wakiuawa lakini Serikali inasema kuna usalama. Naiomba Serikali ichukue hatua za haraka kudhibiti vifo hivyo. Wanajeshi wetu wapewe vifaa vya kutosha ili wafanye kazi nzuri huko mipakani kulinda mipaka ili kupunguza vifo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanajeshi kutumika kwenye siasa. Wanajeshi wamekuwa wakitumika kwenye siasa. Mfano, Wanajeshi kutumika kwenye kupokea Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya ugaidi. Kuna matukio mengi yanayoashiria ugaidi, watu wamekuwa wakiuawa, wakipotea wakati Majeshi yetu yapo. Naiomba Serikali idhibiti mauaji hayo na upotevu huo kupitia Wanajeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu SUMAJKT; niwapongeze kwa kazi nzuri ya ujenzi wa shule ya sekondari huko Bukoba. Wametumia ubunifu kutumia fedha ndogo iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari hiyo. Naomba Wanajeshi hao waongezewe bajeti ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania. Ripoti ya CAG ya mwaka 2016/ 2017 inaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha fedha kinawekwa amana ya kudumu. Kwa mwaka 2016/2017, inaonyesha kwamba fedha zilizowekwa amana ni shilingi bilioni 54.7. Badala ya kutoa mikopo kwa wakulima fedha inakwenda kuwekwa kwenye amana na shughuli kubwa ya benki hiyo ilikuwa ni kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/2017, benki hiyo imetoa shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya watumishi. Kwa hiyo, kiasi kidogo ambacho kilitolewa mkopo kwa ajili ya sekta ya kilimo, shilingi bilioni 2.2 tu. Vilevile benki hiyo imekuwa maeneo ya mjini tu na hasa Dar es Salaam. Waziri atueleze ni kwa nini benki hiyo haiendi mikoani na hatimaye wilayani na vijijini? Naomba kuishauri Serikali ifanye haraka sana kuhakikisha benki hiyo inafika huko chini kwa wakulima. Kwa sababu Dar es Salaam hakuna wakulima kule, wakulima wako huko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kuchangia ni upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Mwaka jana tualiahidiwa hapa Bungeni kwamba mbolea zitafika kwa wakati na kwa bei nafuu lakini cha kushangaza wakulima wetu wamepata shida sana, kuanzia mwaka jana Oktoba walipoanza kufanya shughuli za kilimo mbolea ikachelewa na Januari hapakuwepo mbolea ya kukuzia. Kama kweli tunataka kwenda kwenye Tanzania ya viwanda, tunaendaje kama hatutekelezi yale ambayo tunawaahidi wananchi wetu? Mheshimiwa Waziri kwa kweli inasikitisha wananchi wetu mwaka huu wamekata tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala la ukosefu wa soko. Wananchi wetu pamoja changamoto walizo nazo wamehamasika, wamelima kwa wingi lakini hakuna soko, mazao yote hakuna soko. Katika Mkoa wangu wa Njombe tunalima kwa wingi mahindi, viazi na matunda lakini hivyo vyote havina soko. Kwa mfano, mwaka 2016/ 2017 tumezalisha mahindi tani 571,000 na matumizi yanatakiwa tani 172,000 hivyo kuwa na ziada tani 399,000. Inasikitisha, baada ya kuzalisha kwa wingi namna hiyo wananchi hawa walitakiwa wapate faraja, wapate fedha za kuweza kusomeshea watoto wao lakini wakazuiliwa wasipeleke mahindi haya nje. Kwa kweli inasikitisha, inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atueleze wananchi hawa watafanya nini na mahindi hayo? Maana sasa hivi tunaingia kwenye msimu mwingine, mahindi sasa hivi yamestawi nchi nzima, je, tutafanyaje na mahindi hayo? Naomba tuone ni namna gani tunawahurumia hawa wananchi ambao wanatumia gharama kubwa kununua pembejeo lakini mwisho wa siku wanakuja kuuza debe moja Sh.3,000 au Sh.2,000 kwa kweli inasikitisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuhusu uchapaji chapa wa ng’ombe. Uchapaji chapa ng’ombe unaharibu ngozi ya ng’ombe, hivyo itasababisha hasara ya ngozi ya ng’ombe. Naishauri Serikali waweke nembo kwenye masikio ya ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, uchomaji nyavu moto unasababisha hasara kubwa kwa wavuvi. Naishauri Serikali badala ya kuchoma nyavu hizo, zingepelekwa VETA kwa ajili ya kuunganisha ili wapate nyavu inayotakiwa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kamata kamata ya watu wanaoshikwa na samaki. Hii kamata kamata ya wanawake wanaokuwa na samaki hata wachache siyo haki. Naiomba Serikali waache kuwanyanyasa wanawake hao na badala yake waone ni namna gani watawadhibiti wavuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, pia bado kuna tatizo kubwa la mifugo kuzunguka zunguka mijini. Naiomba Serikali iondoe mifugo mijini na iwatafutie wafugaji maeneo ya vijijini ambako kuna nyasi za kutosha. Pia naomba Serikali itoe elimu kwa wafugaji, wafuge kwa kutumia utaratibu wa zero grazing.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu bajeti ya maendeleo. Inasikitisha kuona kwamba pamoja na Wizara kutengewa bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2016/2017 lakini kwa bahati mbaya fedha hiyo haikwenda kwa ajili ya maendeleo. Naiomba Serikali ihakikishe inafuatilia fedha yote tunayoidhinisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu migogoro ya mipaka, kumekuwa na migogoro ya mipaka kati ya TANAPA na wananchi wa Kijiji cha Luduga katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe. Pia huko Kituro, Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe wananchi wamekuwa wakisumbuliwa na TANAPA, kutokana na kuweka beacon kwenye maeneo yao ambayo hapo awali hayakuwa kwenye eneo la hifadhi lakini Serikali imeongoza. Hii imesababisha kuwavurugu wananchi wanaoishi maeneo ya mipaka ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali isitishe zoezi hili la kuweka mipaka hadi wawashirikishe wananchi katika maamuzi ya Serikali yanayohusu kuongezeka kwa maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, kutopeleka fedha kwa wakati naomba kujua ni kwa nini fedha hazipelekwi kwa wakati. Lakini pia kutopelekwa fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge, lakini kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tozo nyingi kwenye sekta ya utalii, matokeo yake kumesababisha kupunguza watalii wanaokuja nchini kwetu. Naiomba Serikali ipunguze tozo zisizo za muhimu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kurejesha Wafungwa Nchini; naomba Wizara ishughulikie kurudisha Watanzania waliofungwa huko nje, kama vile Msumbiji, warejeshwe nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wanajeshi Wanaofariki Kwenye Mapambano; kuna Wanajeshi wanaokwenda kusaidia nchi nyingine kwa ajili ya ulinzi kama vile Congo na sehemu nyingine, wanapofariki kwenye mapambano hayo familia zao zinasahaulika. Naiomba Serikali ihakikishe familia za Wanajeshi hao zinapata huduma stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Unyanyasaji wa Mabinti Wanaokwenda Kufanya Kazi za Majumbani Nje; naiomba Serikali ifuatilie wale wote wanaowasafirisha mabinti kwenda nje kufanya kazi za ndani, wachukuliwe hatua kwa sababu mabinti hao wanateseka sana na wengine wanakufa na hawapati masaada wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Upungufu wa Maafisa Kwenye Balozi; Maafisa kwenye Balozi zetu hawatoshi. Naiomba Serikali ijitahidi kupeleka maafisa katika balozi zetu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Viwanja Visivyoendelezwa. Kuna viwanja ambavyo havijaendelezwa basi viendelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu kutoza kodi kabla ya kufungua biashara; TRA imekuwa ikikadiria kodi za wananchi wanaotaka kufungua biashara kabla ya kuanza biashara bila kujua kama biashara hiyo itaingiza fedha kiasi gani, matokeo yake wafanyakabishara wanaendesha biashara kwa hasara. Mfano, kuna Mbunge amefungua biashara yake baada ya kukadiriwa kiasi cha mtaji wake shilingi 3,000,000, wakamkadiria kulipa shilingi 22,000 kwa miezi mitatu, ambapo jumla yake kwa mwaka atalipa shilingi 834,000, hadi sasa Mbunge huyo kwa siku anaingiza shilingi 5,000 hadi shilingi 20,000. Maana yake anakusanya fedha zote kwa ajili ya TRA tu. Naomba Serikali ifuatilie TRA, ni kwa nini wanaanza kuwatoza wafanyabiashara kabla ya kuwapa muda wa matazamio ya biashara zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mashine za EFD; tatizo la EFD ni kubwa, hadi sasa kuna mfanyabiashara na hasa wanaoanza biashara wamelipia mashine za EFD shilingi 650,000 lakini hadi sasa hawajapata mashine hizo kwani wameambiwa mtandao uko chini. Hivyo, wametumia risiti za mikono ambapo wateja wanagoma kupokea risiti za mkono. Ninaomba Serikali ishughulikie suala hili haraka iwezekanavyo kwani Serikali yenyewe inapoteza mapato yake.

Mheshimiwa Spika, tukiwa hapa Bungeni Serikali ilitamka hapa ndani Bungeni kwamba road license imefutwa badala yake fedha imeingizwa kwenye mafuta. Kuna wananchi ambao hadi sasa magari yao yameshikiliwa na TRA. Mfano, kuna mwananchi mmoja pale Njombe ambapo gari yake inaendelea kushikiliwa pale TRA kwa kudaiwa road license ya huko nyuma. Naomba Serikali ifuatilie suala hili na kuona kwamba magari hayo yanaachiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya usalama katika nchi yetu ni tete. Watu wengi wamekuwa wakitekwa na kuuawa na hata wengine wanauawa na Polisi kama vile Suguta Chacha, mdogo wake Mbunge mwenzetu, ameuawa na Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hali hii inaharibu kabisa hali ya amani na utulivu. Naiomba Serikali mchukue mkakati wa makusudi kuhakikisha mnakomesha hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Wabunge, hasa Wabunge wa Upinzani, wamekuwa wakizuiwa kufanya mikutano. Polisi wamekuwa wakiwaandikia barua ya kuwazuia wasifanye mikutano. Hii siyo sahihi kabisa. Huko ni kukiuka Katiba ya nchi yetu. Naiomba Serikali ichukue hatua ya makusudi kuhakikisha inatenda haki kwa watu wetu na hasa kuwaruhusu Waheshimiwa Wabunge wafanye mikutano kama Katiba inavyodai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wa barabarani wanafanya kazi ya TRA, wanasumbua sana madereva. Madereva wananyanyasika, kulipa faini kila Kituo cha Polisi, pia kama hawana pesa za rushwa wananyang’anywa kadi za gari na leseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwasaidie vijana wetu wanaoendesha bajaji, bodaboda na magari madogo ya mizigo; wanatozwa pesa bila sababu. Naomba Serikali isimamie Polisi wa Usalama Barabarani wasiwapige viboko madereva. Huo kwa kweli ni uonevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iache kutumia Polisi kwa kuwadhalilisha Wabunge wa Upinzani kwa kuwakamata kamata ovyo, hata kuwapiga makofi, mfano, Mheshimiwa Susan Kiwanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja ya Ofisiya Rais, Utumish na Utawala Bora kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie katika utawala bora; kumekuwa na tatizo la Wakuu wa Wilaya kuwanyanyasa Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Mfano; Mkuu wa Wilaya ya Njombe amekuwa anaingilia vikao vya Madiwani na kutoa amri zisizo na tija kinyume na kanuni. Naomba wakuu hao wapewe maelekezo wasivuruge Baraza la Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Utumishi; watumishi kutopewa maslahi stahiki; kuna watumishi ambao wamepandishwa madaraja lakini mishahara yao imebaki ile ile, mfano Wlimu. Naomba Serikali iwapandishe madaraja, lakini pia wapandishwe mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Waziri wa TAMISEMI kwa moyo wake wa kujituma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu Bure/Bila Malipo; kumekuwa na mkanganyiko mkubwa katika utekelezaji wa matamko ya viongozi wa juu wa Serikali. Matamko hayo yamekuwa yakitolewa bila kufanyiwa utafiti; matamko hayo yamekuwa yakiathiri wananchi. Mfano, Rais alipotamka kuwa wanafunzi wasitozwe kitu chochote, wazazi walikwenda shuleni na kudai fedha zao za michango na vyakula ili kurudishiwa. Hivyo, naiomba Serikali ihakikishe inapotamka ifanye utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wa sekondari kwenda kufundisha shule za msingi; kumekuwa na changamoto kubwa kwa kuhamisha Walimu wa sekondari kwenda kufundisha shule za msingi. Kwanza walimu hawa waliandaliwa kwa ajili ya kufundisha wanafunzi wakubwa na siyo watoto wadogo. Hivyo, inakuwa vigumu sana watoto hawa wadogo kuwaelewa Walimu hawa wa sekondari na hii itasababisha watoto kufeli. Naiomba Serikali iajiri Walimu wanaolingana na ufundishwaji wa shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vya mapato vya halmashauri kuchukuliwa na Serikali Kuu; Serikali Kuu imechukua vyanzo muhimu vya halmashauri. Kwa mfano, ardhi ndiyo rasilimali pekee ambayo kila halmashauri inamiliki; ardhi ndicho chanzo cha mapato cha uhakika kwa kila halmashauri ya nchi hii. Halmashauri zinatakiwa kuchukua asilimia 30 ya kodi ya ardhi, lakini Serikali imechukua kodi hiyo na fedha hizo hazirudishwi na zikirudishwa zinarudi kwa kuchelewa. Naiomba Serikali kurudisha baadhi ya vyanzo vya mapato katika halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo; wananchi wamehamasika wamelima mazao ya mahindi, matunda, nazi na mazao mengine. Wamejitoa kununua mbolea, dawa za wadudu na kutunza mazao yao kwa gharama kubwa na hatimaye wamevuna kwa wingi lakini hakuna soko. Kwa mfano, wananchi wa Ludewa katika Mkoa wa Njombe wanategemea sana zao la mahindi ambalo limekuwa likichukuliwa na watu NFRA, lakini mwaka huu hawajachukua mahindi hayo. Naiomba Serikali itafute soko kwa ajili ya wananchi wetu kwa kufungua mipaka ili mazao hayo yauzwe nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji; miradi ya maji katika halmashauri nyingi inasuasua; mfano, katika Halmashauri ya Mji wa Njombe kuna Miradi ya Maji ya Lugenge na Hagafilo, inasuasua. Naiomba Serikali ifuatilie miradi hiyo na kubaini tatizo linaloikwamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bili za maji zimekuwa ni tatizo kubwa; zinaletwa bili kubwa wakati maji yanayotumika ni kidogo. Pia kumekuwa na uchakavu wa mabomba, mfano maeneo ya Kisasa mabomba yanapasuka ovyo. Naiomba Serikali ifuatilie suala hili la uchakavu wa miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu kuruhusu Taasisi binafsi katika Upimaji Ardhi. Kutokana na uhaba wa fedha katika Wizara kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Wizara hususan upimaji wa ardhi, naiomba Serikali iruhusu Taasisi binafsi katika kufanya shughuli za upimaji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa watu binafsi wanatoa huduma kwa wananchi wengi lakini changamoto kubwa ni VAT ambayo wanatozwa na hii hupelekea gharama za upimaji kuwa kubwa, naiomba Serikali iondoe VAT kwenye kampuni hizo za upimaji kusudi gharama za upimaji wa ardhi kwa wananchi zipungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa gharama za upangaji wa ardhi ni kubwa na wakati huo huo mtu analipia jengo; na kwa kuwa wananchi wanalipia kodi mara tatu, yaani kiwanja, nyumba na vifaa, naiomba Serikali ibakize kodi mbili tu. Yaani kodi ya kiwanja na kodi ya vifaa vya nyumba ambavyo vinakuwa vimelipiwa na mtu akishajenga jengo. Basi alipie jengo tu na siyo kulipia tena kiwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kanisa la K.K.K.T Njombe Mjini limemilikishwa eneo kubwa hekta 120, katika Kijiji cha Magode na limeachwa bila kuendelezwa na kusababisha mivutano kati ya Kanisa na wananchi wa Magoda; naiomba Serikali ichukue eneo hilo na kuwagawia wananchi wanaohangaika na wamechukuliwa maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madini Mchuchuma, ni muda mrefu sasa mradi huu wa makaa ya mawe huko Mchuchuma Serikali imekuwa ikiahidi kuanza lakini bado haujaanza. Nataka kujua ni kwa nini ahadi hizi za Serikali hazitekelezeki miaka nenda rudi. Naomba Waziri atakapotoa majumuisho atueleze kwa uhakika ni lini mradi huo wa uchimbaji wa makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa maeneo ya Mchuchuma na Liganga wameondolewa lakini bado hawajalipwa fidia zao. Naomba Waziri atueleze kwa uhakikia ni lini wananchi hao watalipwa fidia zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaosafirisha kokoto, matofali na mchanga wanasumbuliwa sana na kodi nyingi wakati vifaa hivyo ni vya kuwasaidia wananchi ili wajenge nyumba bora lakini wanabanwa sana na watu wa madini. Naomba kodi zisizo na tija zipunguzwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wachimbaji wadogo wapewe leseni ili waweze kujipatia kipato halali, hasa wachimbaji wadogo wadogo wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wachimbaji wadogo wadogo hawana mitaji, Serikali itoe ruzuku kwa wachimbaji hawa ili wachimbe kwa tija na kuweza kuleta maendeleo ya nchi hii, tofauti na wachimbaji wakubwa wanaonufaisha nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika hoja hii ya mpango. Awali ya yote, namshukuru Mungu ambaye ametujalia uhai nami siku hii ya leo kusimama hapa na kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Halima Mdee kwa uwasilishaji mzuri na kwa taarifa nzuri aliyoitoa. Naomba Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango ayachukue mawazo ya Upinzani, ni mazuri sana, ayafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kuchangia hoja hii kwa kuanza na sekta ya kilimo. Katika hotuba hii, ukurasa wa 29, imeeleza kwamba kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo umeongezeka kwa asilimia 7.1 mwaka 2017 ukilinganisha na ile ya 2016 ya 5.6. Suala la kilimo ni changamoto kwa wananchi wetu. Mwaka huu wakulima wengi wamekata tamaa kulima na hasa wa zao la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wananchi wetu wamejitahidi wamelima sana na wakapata mazao mengi sana ya mahindi, lakini kihoja kilichopo, sasa hivi wamefungia mahindi yao, yako ndani ya nyumba, panya wanakula, kwa sababu debe moja la mahindi ni Sh.2,500. Huu ni mfano wa eneo moja tu ambako natoka Mkoa wa Njombe. Wananchi wanafika mahali wanashindwa mbolea wanunuaje kwa sababu akiuza mahindi hata debe sita au kumi na kitu bado hawezi kununua hata chakula cha nyumbani. Hata akiuza maroba matano hawezi kununua mbolea au hata sukari kwa hela hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sielewi tutawasaidiaje wananchi hawa. Pendekezo langu, kwa sababu bei ya zao la mahindi na mazao mengine kama mbaazi zimeshuka, basi na bei za pembejeo zishuke kusudi hawa wananchi wapate morali kuweza kulima tena mazao yao na mwakani waweze kuuza kama mtakuwa mmefanya utaratibu wa kuwawezesha kuuza mazao yao kwa bei zinazotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye hotuba ya Upinzani, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ya Kilimo iliidhinishiwa fedha za maendeleo shilingi bilioni 100, lakini hadi Machi 2017 fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 2.2. Halikadhalika mwaka 2017/2018, Wizara iliidhinishiwa fedha za maendeleo shilingi bilioni 150.2 lakini hadi mwezi Machi zilikuwa zinatolewa tu shilingi bilioni 16.5. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii tunawezaje kuendelea na mpango huu kama kile ambacho tumepanga mwaka jana na mwaka juzi tumeshindwa kukitekeleza? Naiomba Wizara kufuata haya Waheshimiwa Wabunge tunayoyapendekeza. Tunapoidhinisha bajeti, maana yake ile bajeti itolewe, isiwe tunaidhinisha kwenye makaratasi halafu ukija kwenye hali halisi kiasi kinachotolewa sicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la maji. Suala la maji nalo ni changamoto kubwa sana katika nchi nzima. Hata leo hii ukizunguka mkoa mmoja hadi mwingine, unaona kwa jinsi gani watu wanavyohangaika na suala la maji. Hata maeneo ambayo yana vyanzo vya maji vya kutosha kama vile Mkoa wa Njombe, bado pale Njombe Mjini hakuna maji. Hilo ni eneo ambalo lina vyanzo vya maji, sembuse maeneo ambayo hayana hata vyanzo vya maji vya kutosha! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aone ni namna gani zinatengwa fedha za kutosha na kutafuta vyanzo vingine vya kuweza kukidhi haja na hitaji hili la wananchi. Kwa sababu kwanza fedha zinazotengwa ni kidogo sana hivyo wananchi hawa wanashindwa kupata mahitaji ambayo yangetakiwa wayapate. Naomba Mheshimiwa Mpango atenge pesa iende kwenye Wizara husika ya Maji ili iweze kutekeleza miradi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, kuna suala la wataalam wanaokwenda kwenye utekelezaji wa hiyo miradi. Katika Halmashauri nyingi wanapelekwa wataalam ambao wanaenda kuharibu ile miradi, wakishaharibu wanapelekwa sehemu nyingine, baada ya hapo sasa Halmashauri zinaanza kubanwa kwamba mbona miradi haikutekelezeka vizuri. Mfano mzuri ni Njombe, naweza nikatoa hata mfano wa Mradi wa Utengule Ngaranga. Mradi ule umetekelezwa chini ya kiwango. Mabomba hayafai, viungio vinakatika, hadi sasa hivi mradi umekamilika lakini maji hayatoki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye taarifa ya Waziri anasema kwamba miradi ya maji vijijini iliyotekelezwa ni 1,595 na imeshakamilika. Naomba kujua, hii miradi anayosema imetekelezwa, je, imefuatiliwa na kuona inafanya kazi? Nachoomba, tunapoandika taarifa hizi, tuhakikishe tumetembelea na kuona kweli miradi inafanya kazi, ndiyo tuweze kuiingiza hapa kwenye taarifa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la viwanda. Kwenye taarifa ya Waziri, ukurasa wa 31 amesema viwanda vipya ni zaidi ya 3,306. Naomba kujua, hivyo viwanda ni vya aina gani? Hivyo ni viwanda ambavyo vilikuwa toka kipindi cha Nyerere au?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika hoja hii, kama ifuatavyo. Kwanza, ni matumizi ya mifuko ya plasitiki. Baada ya katazo la mifuko ya plasitiki, naomba Serikali itoe njia mbadala ya mifuko hii ya plasitiki. Serikali itoe maelekezo ya vifaa vitakavyotumika badala ya plasitiki. Mfano, vitengenezwe vifungashio kwa kutumia karatasi za kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa kuna ukataji mkubwa sana wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Niombe Serikali ipunguze bei ya gesi ili wananchi waweze kutumia gesi badala ya kuni na mkaa ambao unasababisha uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya Muungano, naomba wananchi waendelee kupata elimu juu ya Muungano huu. Hata wanafunzi wafundishwe masuala ya Muungano ili kuendelea kuenzi juhudi za waasisi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hadi sasa Tanzania haina Tume Huru ya Uchaguzi, naiomba Serikali kuunda Tume Huru ya Uchaguzi ili kutenda haki na kudumisha demokrasia ya kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Katiba ya sasa ina upungufu mwingi, mfano muundo mzima wa kupata uongozi unaondoa uhalali wa Katiba hiyo. Hivyo, naiomba Serikali iendeleze mchakato wa kupata Katiba mpya maana kipengele kilichobaki ni kupiga kura kwa Katiba hiyo mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kutokutenda haki kwa Mahakama zetu nchini. Mahakimu wengi wamekuwa wakifuata maelekezo ya Serikali katika kutoa haki badala ya kusimama kama mhimili unaojitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo: vyombo vya habari siyo huru kabisa, haiwezi kufanya kazi yake ipasavyo. Matokeo yake Serikali haiwezi kujisahihisha na kupata maendeleo, haiwezi kujua ni wapi imekosea. Naiomba Serikali iangalie upya Sheria hiyo ya Vyombo vya Habari, kuvibaini ili visifanye kazi zake inavyostahili.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii iangalie ni namna gani inatoa elimu kwa wananchi juu ya kudumisha maadili mema. Hata walimu mashuleni, pia wazazi wafundishe maadili kwa watoto wao maana kuna mmomonyoko mkubwa sana wa maadili kwa watoto na vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya mila na desturi katika makabila mbalimbali ni nzuri. Hivyo, nashauri makabila wahamasishwe kudumisha mila na desturi ambazo ni nzuri. Mfano, heshima kwa wakubwa kwa kuwapokea wakubwa mizigo au kuwaachia viti maeneo ya mikusanyiko.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ifanye tathimini juu kutoangalia Bunge, kwa sababu watu wengi wanalalamika, hawaelewi nini kinaendelea Bungeni na kwamba hawaelewi kama wawakilishi wao wanawawakilisha vyema au la.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo. Makatazo ya vikao vya ndani. Jeshi la Polisi limeendelea kukataza vikao vya ndani vya Vyama vya Upinzani hasa kwa kipindi hiki ambapo wanafanya changuzi za ndani ya chama. Mfano, kikao cha ndani cha wanawake huko Geita tarehe 8 Machi, 2019 Jeshi la Polisi lilizuia kikao cha ndani cha BAWACHA na kulazimisha wanawake hao wa CHADEMA kuungana viwanjani na wanawake wa CCM ambao walikuwa kiwanjani, hii siyo sawa na siyo halali. Naomba Serikali itende haki iache wananchi wafanye vikao vyao vya ndani bila bughudha. Vyama vyote viko kwa mujibu wa Katiba ya nchi, halafu utekelezaji unakuwa kinyume chake.

Mheshimiwa Spika, Polisi wa Barabarani wamekuwa kero kubwa sana kwa wananchi hasa kwa madereva wa hiace na kirikuu. Madereva wanasimamishwa kila kituo ambapo wapo Polisi na wanatozwa fedha. Naiomba Serikali itafute utaratibu wa kudhibiti makosa ya barabarani kwa kutumia mashine badala ya Polisi kuwa barabarani. Wafunge maeneo yote mashine za kubaini makosa mbalimbali na madereva waweze kwenda kulipa faini na kodi zingine kwenye vituo vya polisi bila shuruti.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwako bado na tatizo la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu hasa watoto wanaotoka katika familia duni ambapo hawana uwezo wa kufuatilia na hawana watu wanaoweza kuwasemea. Nina mfano wa wanafunzi ambao ni wa kike na walifaulu masomo yao ya sayansi na mmoja alikuwa ni mwenye ulemavu, lakini ameomba mkopo mfululizo kwa miaka mitatu hakufanikiwa hadi alipokuja kwangu na kuomba nimsaidie kwa sababu awali shirika langu la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na yatima lilimsaidia toka shule ya msingi hadi sekondari. Baadaye shirika likawaachia ndugu waendelee kumhudumia lakini hatimaye huyu alikatishwa tamaa na kukosa mkopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifuatailie hasa watoto yatima na wanaoishi maisha hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu kufungia Vyuo vya Dini. Kumekuwa na ufungaji wa Vyuo Vikuu kiholela. Kwa kuwa vyuo hivi vimesajiliwa na Serikali, basi wapate maelekezo na kukaguliwa mara kwa mara; na kunapokuwa na upungufu warekebishwe badala ya kuwafungia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi zisaidiwe kulipia mitihani. Kwa kuwa elimu bila malipo ni kuwa Watanzania wote, basi naomba watoto wanaosoma kwenye shule binafsi wapewe pia ruzuku kwa ajili ya mitihani na hasa kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wanaotoka katika mazingira hatarishi na yatima ambao wamesaidiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, wamefaulu kwenda VETA za Serikali, wamefukuzwa. Wanadai mashirika hayo yawalipie wakati mashirika hayo yamekuwa yakijitolea tu. Matokeo yake vijana hawa wanakatishwa tamaa na kuacha vyuo. Nina mfano halisi wa kijana ambaye amefukuzwa kule Chuo cha VETA cha Morogoro, anaitwa John Mwingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkanganyiko mkubwa sana wa mitaala ya shule za msingi. Kulitoka mtaala wa shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita na kwamba watoto wataishia darasa la sita na kujiunga na sekondari. Hadi sasa hivi wanafunzi wanaendelea kufundishwa kwa mtaala huo ambapo hata vitabu vyake havipo. Hivyo walimu wanafundisha katika mazingira magumu. Naomba Mheshimiwa Waziri atoe mwelekeo wa nini kifanyike ili kurekebisha mkanganyiko huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni tatizo la uhamisho wa walimu. kuna walimu wanakaa shule za vijijini kwa muda mrefu hadi wanazeeka huko vijijini. Wanaishi katika mazingira magumu bila hata motisha. Naomba wakikaa miaka kadhaa wahamishiwe maeneo ambayo yana unafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kupungua kwa bajeti ya elimu. Bajeti ya Wizara ya elimu pekee imepungua kutoka shilingi trilioni 1.408 kwa mkwa 2018/2019 hadi shilingi trilioni 1.357 kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Upungufu huu ni wa shilingi bilioni 51. Elimu haiwezi kuwa bora kwa mfumo huo. Naomba pesa zinazotakiwa kwenye Wizara hii ya Elimu ziende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuhusu wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii. Serikali imetoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 10,000. Wahudumu hawa wamekuwa msaada mkubwa sana kwenye ngazi ya jamii kwa kuzuia vifo vya watoto na akina mama lakini Serikali haiajiri tena wahudumu hawa. Naomba Serikali ione namna ya kuwapatia motisha na siyo mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, bima ya afya. Naomba Serikali iharakishe Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuwa matibabu ni gharama na watu wengi wanapoteza maisha kwa kukosa pesa za matibabu. Pia watu wanaotumia bima wanakosa baadhi ya dawa za magonjwa makubwa kama moyo na mengine. Hivyo, naomba bima hizo ziingize matibabu yote na siyo baadhi ya magonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, Maafisa Ustawi wa Jamii. Maafisa hawa ni muhimu sana lakini hawana bajeti ya kutosha. Mara nyingi wanatumia fedha zao za mfukoni kwa ajili ya kazi za kutembelea na kufuatilia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Hivyo, naomba Maafisa Ustawi wa Jamii wapewe bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutembelea na kufuatilia familia mbalimbali zenye matatizo pamoja na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, ada ya usajili wa dental clinics. Gharama za usajili wa clinic hizi ya Sh.1,000,000 ni kubwa. Naomba gharama hizo zipunguzwe kwani ni huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya. Pili, naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye mchango wangu nikianza na fedha za maendeleo kwenda kidogo. Nikiangalia mwaka 2015/2016, fedha za maendeleo zilizokwenda ni asilimia 28; mwaka 2016/2017 zilikwenda asilimia 25 na mwaka 2017/2018 zilikwenda asilimia 22. Ukiangalia huo mtiririko unaona kabisa Wizara hii inazidi kwenda chini na kwamba wananchi watazidi kupata matatizo siku hadi siku badala ya kwenda juu inakwenda chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kwenye ripoti ya CAG inaonesha kwamba fedha zilizokwenda kwenye Bodi ya Mabonde ya Maji ambapo zilipangiwa kwenda shilingi bilioni 49.5 kwa mwaka 2016/2017 lakini zilikwenda shilingi bilioni 6.6 tu, sawa na asilimia 13 tu. Fedha ambazo hazikwenda ni shilingi bilioni 42.9, sawa na asilimia 87. Tukiangalia mwaka uliofuata wa 2017/2018 kati ya shilingi bilioni 38.4 zilizoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zilikwenda shilingi bilioni 7.2 tu, sawa na asilimia 19 ya bajeti yote ya mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza, je, Serikali ina dhamira kweli ya kumtua mama ndoo kichwani? Kwa sababu tumekuwa tukiimba kwamba Serikali inataka kumtua mama anayetaabika ndoo lakini kwa mtiririko huu tutafika kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia upotevu wa maji, ni mkubwa sana ambao umesababisha hasara ya shilingi bilioni 47.18. Ukiangalia mikoa 15 yenye upotevu wa maji ambayo imeoneshwa kwenye ripoti ya CAG, tukianza na Mkoa wa Njombe ambao inaonesha hapa kiasi cha upotevu wa maji kisichokubalika shilingi milioni 196.2. Tukija Mwanza ni shilingi milioni 677.52 na mikoa mingine imeorodheshwa hapa ambayo jumla yake inakuja shilingi bilioni 47.18. Wakati huo huo tunaongelea juu ya uhaba wa maji. Upande mwingine tunaona upotevu wa maji upande mwingine tunaona uhaba wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweke mfumo ambao utasaidia kupunguza upotevu huu wa maji. Niishauri Serikali wale wanaokwenda kusoma mita za maji basi wawe na wajibu wa kuhakikisha wanaangalia mabomba au miundombinu ambayo inatoa maji ambayo inavujisha maji kwa sababu kuna upotevu mkubwa sana wa maji, nikianza hapa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakaa kisasa nimeshawasilisha hii hata mwaka jana kwamba kuna mabomba yana tiririsha maji na nimeenda kuripoti mara nyingi huko kwenye mamlaka ya maji DUWASA juu ya upotevu wa maji huu, lakini ukija siku inayofuata unaona maji bado yanaendelea kutiririsha, sasa kama hapa Dodoma ipo hivi hayo maeneo mengine inakuwaje? Kwa hiyo niiombe Serikali ifuatilie suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ni suala la wateja kutokuwa na mita za maji kuna wateja wengi ambao hawana mita za maji matokeo yake, unakuta bill zinakadiriwa juu na mtu anaendelea kutoa bili hizi maana hajuwi sasa nitoe mfano halisi mimi wazazi wangu walikuwa kila mwaka wanatozwa pesa nyingi sana mwaka huu nikashtuka nikasema haiwezekani hizi bili ni kubwa sana nikaenda kufuatilia, nikakuta hawana mita nikawauliza watu mamlaka ya maji kwanini hamjawawekea mita hawakuwa na chakuwaeleza, kwa hiyo niombe Wizara ifuatilie suala hili kuhakikisha wateja wote wanapata mita za maji, kusudi watu walipe hela kwa uhalali wasizidishiwe na wala isiwe chini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la uhaba wa maji kwa ujumla.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Malizia kengele ya pili hiyo.

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niombe Wizara ifuatilie suala hili kwa sababu kuna maeneo ambayo tulikuwa tukiimba kila siku hapa kwamba tunaomba maji kwa mfano kuna kijiji cha Itengelu huko Wanging’ombe huko nyuma walikuwa wanamaji mengi tu kwenye bomba mpaka mabomba toka mabomba yamekufa sasa hivi wanahangaika hawa wananchi wanachota maji machafu kwa kilometa nyingi naomba Wizara ifuatilie suala hili. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uwanja wa ndege; kwa kuwa Kiwanja cha Ndege Njombe kiko katika hali mbaya, niombe Serikali ikarabati kiwanja hicho. Serikali imekuwa ikisema iko kwenye mchakato lakini sasa ni miaka minne Wananjombe wanajibiwa kuwa kiko kwenye mchakato.

Mheshimiwa Spika, Barabara za Itoni – Ludewa (Njombe) – Njombe – Makete. Hali ya barabara zile sio nzuri, hasa kipindi hiki wakati wa mvua. Naomba wakandarasi walipwe kwa wakati ili waweze kuharakisha ujenzi wa barabara hizo.

Mheshimiwa Spika, mawasiliano ya simu; maeneo mengi ya Jimbo la Lupembe hakuna mawasiliano ya simu mfano Madeke, Kanikerere na maeneo mengine. Naomba Serikali iwasaidie wananchi kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, miradi kushirikisha Sekta Binafsi; kwa kuwa miradi mingi inasuasua kwa sababu Serikali peke yake inagharamia. Ili kuharakisha maendeleo, nashauri miradi hiyo washirikishwe sekta binafsi kwani sekta hiyo wakipewa miradi hiyo wataharakisha kumaliza miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda kuchangia kuhusu matatizo ya wafanyabiashara. Watu wengi wamefunga biashara zao kutokana na manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa watu wa TRA. Wafanyabiashara wengi kabla ya kuanza biashara anapitia hatua nyingi ambazo zote ni za tozo mbalimbali. Kabla mtu hajaanza kuuza biashara yake anaanza kutoa fedha za kodi na wakati huo makadirio ya TRA yanakuwa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali kwamba watu wanapofungua biashara wasikadiriwe tozo hadi wafanye biashara zao kwanza waone mapato wanayoyapata ndipo waanze kutozwa kodi. Ndiyo maana watu wanafungua biashara kwa kodi hiyo kubwa, mwisho wa siku wanaona ni gharama wanaamua kufunga biashara zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, SIDO. Naomba viwanda vidogovidogo viimarishwe kwani ni muhimu sana. Vimekuwa vikiwasaidia wajasiriamali wadogowadogo lakini SIDO haichukuliwi kama ni muhimu. SIDO inaweza kuajiri wanawake na vijana wengi nchini lakini hata bajeti ya kutosha haitengwi. Naitaka Serikali ilichukue suala hili la SIDO kwa umakini na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya SIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, Liganga na Mchuchuma. Sijui ni kwa nini mradi wa Liganga na Mchuchuma unasuasua wakati sisi kama Wabunge wa Mkoa wa Njombe tumehamasisha wananchi kufanya maandalizi ya mradi huo kwa kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo matunda na mbogamboga. Wananchi wamefanya bidii kulima lakini mazao yao hayana soko kwa kuwa walikuwa wanategemea mradi wa Liganga na Mchuchuma. Niitake Serikali iharakishe mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. LUCIA U. M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo zimekwenda asilimia ndogo sana, asilimia 18 tu hadi sasa na kipindi kilichobaki ni mwezi mmoja tu kuisha mwaka wa Serikali. Naitaka Serikali ipeleke bajeti iliyosalia kipindi hili kilichobakia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maslahi ya wanajeshi na polisi; kwa kuwa kazi hii ya uanajeshi au polisi ni kazi hatarishi inahitaji motosha, naomba Serikali ihakikishe inawapa motisha na kuongeza maslahi ya wanajeshi na polisi. Mavazi ya wanajeshi yatolewe pale wanapohitaji maana kazi yao inahitaji mavazi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bima ya wanajeshi, wanajeshi hawana bima za afya, naitaka Serikali iwapatie bima za afya wanajeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kauli za vitisho, kumekuwa na kauli za vitisho kwa wananchi. Wananchi wengi sasa hivi wamejengwa na woga badala ya Jeshi kuwa kimbilio. Naomba Wakuu wa Majeshi wawe na kauli zinazohamasisha utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Pembejeo. Kwa kuwa wakulima wamelima mazao, kwa nguvu zote na kwa ari lakini pembejeo ni gharama sana matokeo yake wananchi wanapanda mazao bila utaalam wa kutumia mbolea na dawa za wadudu, mazao yamekuwa kidogo. Niishauri Serikali kupunguza gharama ya pembejeo ili wananchi walime kitaalam na kuwa na mavuno yenye tija.

Mheshimiwa Spika, Ukosefu wa Masoko ya Mazao. Pamoja na kwamba wakulima wanajituma kuzalisha mazao hata kwa gharama kubwa lakini mwisho wa yote hakuna soko la mazao. Naishauri Serikali kutafuta masoko kwa mazao ya wakulima wetu. Pia Serikali itoe elimu kwa wananchi juu ya usindikaji wa mazao mbalimbali kama vile mahindi ili kuongeza thamani ya mazao yetu, hii itasaidia kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Tafiti. Kwa kuwa tuna tatizo kubwa la kukosa soko la mahindi, naomba watumike watafiti kutafiti kwenye nchi yetu na kubaini maeneo ambayo yana chakula cha kutosha na yale ambayo hayana chakula cha kutosha, na kisha kupeleka chakula hicho kutoka maeneo ambayo hayana chakula.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ufugaji wa samaki; kwa kuwa kuna umuhimu sana wa wananchi kupata lishe ya samaki ambapo samaki hawana madhara kama nyama, naiomba Serikali itoe elimu kwa wananchi namna ya kufuga samaki. Pia samaki hao watawapatia wananchi kipato.

Mheshimiwa Spika, nyavu za uvuvi kumekuwa na uchomaji wa nyavu holela kwa wavuvi. Hii siyo sawa, naomba kuishauri Serikali nyavu zinazochomwa basi zirudi kiwandani zikarekebishwe.

Mheshimiwa Spika, wataalam; kwa kuwa sekta ya ufugaji na uvuvi haina wataalam wa kutosha, naomba Serikali iajiri wataalam wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu. Awali ya yote niunge mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie mambo yafuatayo. Jambo la kwanza ni bajeti isiyotosheleza. Kumekuwa na tatizo kubwa la upelekaji wa bajeti za maendeleo karibu kila mwaka, maeneo mengine imekuwa inapelekwa pungufu au haipelekwi kabisa. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo katika mwaka wa fedha 2016/2017 pesa za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 100.25, zilikuwa zimetengwa lakini hadi kufikia mwaka 2017 zilizotolewa zilikuwa shilingi bilioni 2.2 tu sawa na asilimia 2.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeona katika mwaka 2017/2018, Wizara hii iliidhinishiwa na Bunge pesa za maendeleo shilingi bilioni 100.2 lakini hadi kufikia mwezi Machi ni shilingi bilioni 16.5 tu zilikuwa zimetolewa sawa na asilimia
11. Tukija katika mwaka wa fedha 2018/2019 fedha iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya kilimo ilikuwa shilingi bilioni 98.119 lakini fedha iliyotolewa ilikuwa ni shilingi bilioni 41 sawa na asilimia 42.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeona huu mtiririko wote wa bajeti ya miradi ya maendeleo kwa jinsi ambavyo imekuwa ikisuasua na kwamba haipelekwi kwa wakati au inapelekwa pungufu hata pungufu ya asilimia 50. Napenda kuishauri Serikali kutokana na tatizo hilo la kutoweza kupeleka bajeti za kutosha kwenye miradi ya maendeleo au kutopeleka kabisa ni vema basi Serikali ikaona namna gani tunawekeza au tunaweka mazingira wezeshi au mazuri kwa wawekezaji ili waweze kutusaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama maji, miundombinu na miradi mingine. Hii ingeisaidia sana Serikali angalau kutokuwa na mapengo makubwa kama ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee suala la miradi ya maji. Miradi ya maji imekuwa ni tatizo nchi nzima katika utekelezaji wake. Kwanza miradi mingi imekuwa ikiripotiwa imekamilika lakini kwa uhalisia haifanyi kazi na wakandarasi wamekuwa tatizo. Naishauri Serikali na Wizara ya Fedha tuone namna gani pesa zinazokuwa zimetengwa zipelekwe kwa wakandarasi kwa wakati unaotakiwa lakini wakati huo huo tuwapime hawa wakandarasi maana wakandarasi wengine siyo waadilifu kabisa. Inapogundulika kwamba hawa wakandarasi siyo waadilifu basi watolewe mara moja wasilelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la maji limekuwa ni tatizo hata maeneo yale ambayo yana vyanzo vya maji vingi tu vya kutosha. Naiomba Serikali tuone namna ya kuwapata wataalamu wanaokuwa wabunifu katika miradi mbalimbali ya maji. Nitoe mfano tu katika Mkoa wa Njombe, ule mji umezungukwa na maji lakini pale Njombe Mjini hakuna maji na tuna wataalamu, kwa nini hao wataalamu wasiwe na ubunifu na kutumia njia nyingine kuhakikisha maji yanaingia pale mjini ukiacha vijijini au ukiacha maeneo mengine ambayo yana ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la maji katika nchi yetu tumeona kipindi cha mvua kunakuwa kuna maji mengi sana na mafuriko. Hivi hatuwezi kupata wataalamu ambao wanaweza wakatuelekeza namna kuvuna haya maji na kuweza kuyatumia wakati wa ukame? Naishauri sana Serikali tuone namna gani tunaweza kuelekeza nguvu zetu kwenye vitu tulivyonavyo kwa sababu haya maji ya mvua tunakuwa nayo na hata sasa hivi kuna maeneo mvua zinanyesha sana lakini haya maji hayavunwi mwisho wa siku maeneo haya yanakujakuwa makame lakini wakati huo huo kulikuwa kuna mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni watumishi. Suala la watumishi kwa kweli ni changamoto kubwa. Naiomba Serikali ione namna gani angalau kipindi kilichobakia maana toka tumeingia mwaka 2015 hadi sasa watumishi hawajapandishiwa mishahara angalau hata ya kudanganyishia tu. Watumishi wako katika hali ngumu sana. Nikitoa mfano wa walimu hata nyumba wanazokaa zinatia huruma. Kwa mfano, sasa hivi kuna shule ambazo zinakarabatiwa vizuri sana lakini nyumba za walimu hakuna. Sasa hata kama shule zimekarabatiwa vizuri walimu wanaweza kwenda kufundisha lakini kama wao hawana nyumba nzuri bado haitasaidia. Niombe Wizara ya Fedha tuone namna gani tunawasaidia hawa watumishi hasa walimu kuwajengea nyumba kama tulivokarabati shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni madini. Naomba kuongelea suala la madini Mchuchuma na Liganga umekuwa wimbo wa taifa. Tumekuwa tukiongea juu ya Liganga na Mchuchuma, tulifikiri kufikia kipindi hiki tungekuwa tayari tumeshaanza kufaidika na mradi ule. Ule mradi ungekuwa na faida kubwa sana kwa Taifa letu, haya mambo tunayohangaika nayo sasa hivi ya pesa pengine ingekuwa ni msaada mkubwa sana mradi ule. Naiomba Serikali kwa kweli ichukue hatua ya haraka kutekeleza ule mradi wa Liganga na Mchuchuma kusudi uweze kusaidia kuinua uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni barabara. Maeneo mengi barabara zimetengenezwa lakini mengine kwa kweli ni tatizo, barabara zimeanza kutengenezwa muda mrefu lakini hadi sasa hazijaisha. Mfano katika Mkoa wa Njombe barabara inayounganisha Ludewa na Njombe Mjini maana ya Itoni –Ludewa, barabara ile kwa kweli ni tatizo, kama ingefanikiwa kwisha ingekuwa msaada mkubwa sana. Hadi sasa hivi ni asilimia 30 tu na tunaambiwa kwamba mpaka mwakani inatakiwa iwe imekamilika. Sasa najiuliza kama mpaka sasa hivi imetekelezeka asilimia 30, je, mwakani inaweza kumalizika kwa hizo asilimia 70 zilizobaki? Niiombe Serikali mtusaidie fedha kwa ajili ya kukamilishia ile barabara. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. LUCY M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Taarifa za Kamati hizi tatu.

Mhesheshimiwa Mwenyekiti, ni Mjumbe katika Kamati ya Utawala na TAMISEMI, tulijadili mambo mengi sana katika Kamati na hoja nyingi zimewasilishwa na Mwenyekiti wetu wakati anatoa Taarifa, naomba nisisitize mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni miundombinu inayoelekea kwenye Chuo cha Hombolo, barabara ya Ihumwa-Hombolo; hali ya barabara ile ni mbaya sana na ni ya muda mrefu na wakati wataalam wanatengeneza wamekuwa wakitengeneza kwa changarawe. Naiomba Serikali badala ya kutengeneza kwa changarawe basi watengeneza barabara ya lami kusudi isilete tena usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni uhaba wa watumishi; karibu sekta zote kuna kilio cha uhaba wa Watumishi. Nikitoa mfano katika hospitali ya Mkoa ya Njombe, watumishi wanaotakiwa ni 320 lakini hadi sasa waliopo ni 149. Kwa kweli inakua ngumu sana katika kutekeleza kazi sawa sawa na kama tunavyojua kwamba upande wa afya tunahangaika ili kupunguza vifo vya wakinamama lakini tunapokua na Watumishi wachache namna hii itakuwa ni vigumu sana kupunguza vifo vya wakinamama. Niiombe Serikali kwasababu tunaenelekea kwenye kipindi cha Bajeti, basi itenge Bajeti ya kutosha kusudi kuweza kuwaajiri Watumishi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Watumishi hao hao ni miaka takribani minne sasa na huu ni wa tano hawajaongezewa mishahara yao. Niiombe Serikali iwaongezee kishahara kwa sababu tunaelekea kipindi cha Bajeti sasa basi iwafikirie hao Watumishi kuongezewa mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni Utawala Bora; Utawala Bora ni pamoja na kuwapa watu au wananchi uhuru wa kutoa mawazo yao. Tumeshuhudia watu wanatoa mawazo yao lakini wanakamatwa. Mfano; kuna Mwanafunzi wiki mbili zilizopita huko UDOM alipiga picha kwenye ndoo za maji kulalamikia tatizo la maji, mwanafunzi yule alikamatwa. Niiombe Serikali itoe uhuru wa wananchi kutoa mawazo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ni suala la Utawala Bora; wananchi wana haki ya kuchangua viongozi wanaowataka lakini pia kuchaguliwa. Nimeshuhudia toka kipindi cha chaguzi ndogo za Ubunge na Udiwani na hatimaye Serikali za Mitaa. Wananchi wamelazimika kuwa na viongozi wasiowapenda ndiyo maana hadi sasa hivi ukienda maeneo mbalimbali wananchi wanawagomea wale viongozi waliowekwa, wanasema hawataki kuongozwa na hao wenyeviti. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunaabudu na tuna dini zetu. Kila mtu ana imani yake. Tuliapa hapo mbele kwamba tutasema ukweli kwamba yale tutakayoyatekeleza yatakuwa ni kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa nimeshuhudia tunafanya kinyume kabisa. Hata dhamira yangu kama Mkristo, mimi dini yangu ni Mkristo, wakati mwingine najisikia vibaya kwamba sisi Wabunge sio wakweli. Naomba tuishauri Serikali yetu, pale inapokosea tuikosoe ni pamoja na kuisisitizia Serikali kuwa na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, kwa sababu imekuwa haizingatii matakwa ya Katiba, itunge Katiba mpya, pia kuweka Tume huru itakayosaidia kutatua haya mambo ambayo yamejitokeza huko nyuma hasa kipindi hichi cha uchaguzi. Kwa sababu tunaenda kipindi cha Uchaguzi Mkuu, isije ikatokea kama ilivyotokea huko nyuma. Ninaomba sana, kila mtu atafakari, kama kweli unamwabudu Mungu wako, basi ikuguse hiyo kwamba tunahitaji kuwa na haki, tutende haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tozo nyingi; kwenye sekta hii ya utalii kuna tozo nyingi mno. Serikali ipunguze kodi hii ili iwe kama kivutio cha kupata watalii wengi ambao watatuingizia fedha za kigeni za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Migogoro Baina ya Serikali na Wananchi. Kwa kuwa kuna migogoro kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za wanyama, Serikali ijitahidi kutatua migogoro hiyo hata kama Wizara imejitahidi kupunguza kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vivutio vya Utalii – Njombe. Ninaomba Serikali ivitambue vivutio vya kiutalii katika Mkoa wa Njombe ili kuliingizia kipato taifa letu. Vivutio hivyo ni Mapango ya asilia yaliyoko katika Halmashauri ya Njombe Mjini eneo la Nyumbanitu. Eneo hilo lina kuku wa ajabu na vivutio vya kale. vilevile Mbuga za Kitulo ambapo kuna maua ya kila aina, jiwe lenye ramani ya Afrika asilia, maporomoko ya Mto Mwihe na Lupali – Njombe. Naomba Serikali ifuatilie mambo hayo na kisha kupeleka watalii.

Mheshimiwa Sika, Bajeti. Kwa kuwa sekta hii ya utalii ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa taifa letu basi Serikali ihakikishe fedha inayoidhinishwa na Bunge itolewe kwa wakati na itolewe yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. LUCIA U. M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja hii kama ifuatavyo; Mradi wa chuma wa Mchuchuma na Liganga. Nasikitika kwamba mradi wa Mchuchuma na Liganga uko kimia. Hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri haujatajwa. Mradi wa Mchuchuma na Liganga ungefanikiwa ungekuwa na manufaa makubwa sana. Kwanza ungewasaidia wananchi wa Mkoa wa Njombe kupata ajira pia pamoja na kuuza mazao yao. pia ingesaidia Serikali kujiingizia kipato chake. Lakini pia ingepnguza gharama kwa Serikali kununua chuma nje na badala yake chuma hicho kingesaidia hata ujenzi wa reli inayojengwa (Standard Gorge Railway). Naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake alieleze Bunge ni kwa nini Mradi huo unasuasua?

Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wana changangamoto nyingi. Moja ya changamoto hizo ni kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya namna ya kuwa na bima ambayo angewasaidia wanapopata majanga kama vile kufukiwa na kifusi; hivyo kwa kuwa hawana bima wakipata majanga familia zao zinabaki katika hali ya umasikini. Naiomba Serikali itoe elimu kwa wachimbaji hao ili kila mchimbaji awe na bima.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekit, naomba kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo; kwanza naomba kuwashukuru kwa jitihada ya kuhakikisha umeme unaenea vijiji vyote vya Tanzania, hususan katika Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Spika, kuna vijiji vya Matola, Mamanyolo, Kitulile, Luponde, Lugenge na vijiji vya Wilaya ya Ludewa Makete na Wanging’ombe bado havina umeme. Naomba Waziri atusaidie kuhakikisha vijiji vyote vvya Mkoa wa Njombe vinafikiwa na umeme.

Mheshimiwa Spika, pia hapa Dodoma kuna maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme kama vile Kata ya Mtumba Mtaa wa Vikonje A karibu na majengo ya VIGUTA wananchi wanaomba umeme.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Gesi Asilia. Wananchi wengi wameshapata uelewa wa kutumia nishati ya gesi. Lakini tatizo ni kwamba gesi ni gharama. Naiomba sana Serikali ishushe bai ya gesi ili kupunguza uharibifu wa mazingira unaoendelea nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia muswada huu. Kwanza niseme tu mimi niko kwenye Kamati na nishukuru Waziri wakati wa majadiliano kwenye Kamati yetu vipengele vingi wakati tunajaribu kushauri walivipokea kwa mabadiliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile niko kwenye Kamati basi nitatoa ushauri kwa ujumla kwa sababu mengi tumeshayajadili tukiwa kwenye Kamati. Kifungu cha kwanza ambacho napenda kushauri ni kifungu cha 7(2) juu ya Mwenyekiti wa Bodi. Nashauri uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi utokane na Mtanzania. Kifungu hicho kisomeke; “Bodi itakuwa na Mwenyekiti Mtanzania atakayeteuliwa na Rais mwenye uzoefu usiopungua miaka kumi ya utawala na mtaalam mbobezi katika masuala ya sayansi.” Msisitizo hapa awe Mtanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha pili ambacho napenda kushauri ni kutoka kifungu hicho hicho cha 7 ambacho kinazungumzia juu ya Wajumbe wa Bodi. Pia napenda kushauri au kusisitiza kwamba katika kifungu hicho cha 7 kuongezwe herufi (j) kwa ajili ya wawakilishi wanaotokana na taasisi za maabara lakini (h) iwe ni wawakilishi wanaotoka kwenye vyuo binafsi vya elimu ya juu. Nasema hivi kwa sababu mara nyingi watu binafsi tumekuwa tukiwaweka pembeni katika baadhi ya masuala lakini kwenye masuala mengine tunasisitiza kwamba watu binafsi au mashirika binafsi yashirikishwe. Hivyo basi, kwa kuweka kipengele hiki tutakuwa tumepata uwakilishi kutoka sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri vilevile kwenye kifungu cha 10(1) juu ya uteuzi wa Mkemia Mkuu. Kifungu hiki kinasema kwamba Mkemia Mkuu atokane na watumishi wa umma. Mimi nashauri kuwa Mkemia Mkuu atoke miongoni mwa Watanzania siyo tu atoke kwenye utumishi wa umma ili tusionyeshe ubaguzi kwa sababu kwenye sekta binafsi unaweza ukawa na mtu mzuri ambaye ana vigezo vya kuweza kufanya kazi hiyo lakini tu kwa sababu yeye yuko nje ya utumishi wa umma basi tukaamua kumuacha hata kama ana vigezo. Kwa hiyo, nashauri hilo suala tuliangalie kusudi tuweke uwiano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ambalo napenda kushauri ni kile kifungu cha 45 kinachozungumzia nia njema. Naomba hilo neno “nia njema” lisiwepo kwa sababu watu wengine wanaweza wakatumia kipengele hicho cha nia njema kwa ajili ya kufanya mambo ambayo siyo sahihi au maovu. Kwa hiyo, nashauri eneo hilo au kipengele hicho kitolewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niishie hapo kwa sababu mambo mengi yameshasemwa na wengi wameshachangia. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti hii. Awali ya yote naomba niunge mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina vitu kadhaa ambavyo nitachangia. Kitu cha kwanza ni suala la vitambulisho vya wajasiriamali. Suala la vitambulisho vya wajasiriamali limeleta mkanganyiko takribani nchi nzima. Jana huko Njombe wamesomewa barua makanisani, kwamba watu wote wanatakiwa kuwa na vitambulisho vya ujasirimali. Kwa mfano akina mama ntilie ambao wameajiri wafanyakazi kuwasaidia, kuosha vyombo na shughuli zingine ndogo ndogo wameambiwa wanatakiwa wawe na vitambulisho vya wajasiriamali. Watu wanaofanya kazi kwenye bustani wanatakiwa wawe na vitambulisho vya ujasiriamali, mafundi ujenzi wanatakiwa wawe na vitambulisho vya ujasiriamali. Ninaomba kujua, hivi kodi ya kichwa imerudi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli inasikitisha kwa sababu wananchi hawa wamechanganyikiwa. Wamenipigia simu mimi asubuhi wanaongea kwa masikitiko makubwa sana wamechanganyikiwa. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atupatie basi ufafanuzi na mwongozo kuwa ni watu gani wanaotakiwa kuwa na vitambulisho hivi vya mjasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili naomba niongelee mradi wa Liganga na Mchuchuma. Juma lililopita nilikuwa nimeuliza swali; kwa kweli wananchi wa Mkoa wa Njombe, ingawa haya madini ni ya Taifa zima lakini kwa kweli tunasikitika; kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Njombe wamejiandaa kwa muda mrefu, wametafuta maeneo karibu na mradi, wamewekeza wanajiandaa tayari mradi uanze lakini mradi hauanzi. Kuna watu walilima mazao kama mboga mboga, matunda wakidhani kwamba sasa watapata soko, lakini mradi uko kimya; na nimeangalia katika kitabu hiki sijaona mahali popote kuhusu mradi wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni fidia. Wananchi wanalia na fidia, hawajafidiwa. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie hao wananchi watalipwa lini fidia, kwa sababu hii kwa kweli inakatisha tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine naomba niongelee juu ya mashine za EFD; mashine za EFD kwa kweli ni mbovu. Nina watu kadhaa ambao wamenionesha zile mashine na zile mashine inaonekana kila inapoharibika anatakiwa kutengeneza kwa 150,000. Kwa hiyo unaweza kukuta imetengenezwa wiki hii, wiki ijayo tena inaharibika, anatakiwa atoe 150,000. Ni kwa nini Serikali isitafute kampuni ambayo inatengeneza hizi mashine imara? Nitaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja basi atuelekeze, atutolee ufafanuzi kama kuna uwezekano wa kutafuta kampuni nyingine inayoweza kutengeneza mashine imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine naomba niongelee suala la taulo za kike. Mwaka jana baada ya kupata msamaha wa kodi kwa taulo za kike kwa kweli wananchi walifurahi sana, hususan wanawake; lakini mwaka huu tena imerudi. Ninaomba Waziri atakapokuja atueleze ni namna gani hawa akina mama tutaenda kuwafariji? Kwa sababu mpaka sasahivi watu wameshachanganyikiwa tena, kwamba kwa nini hizo kodi zimerudi ilhali viwanda vya kutengeneza taulo hizo bado havipo?. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika hoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; Tanzania haiwezi kuwa Tanzania ya viwanda kama hatujaimarisha kilimo, viwanda vinavyotegemea malighafi zinazotokana na kilimo. Kilimo chetu ni bado kilimo cha mkono, tunahitaji kuwa na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipunguze kodi kwenye pembejeo ili wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa na kisicho na kikwazo chochote. Naiomba Serikali itenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuwaajiri Maafisa Ugani ambao watawasaidia wananchi kulima kilimo chenye tija ambacho kitatusaidia kupata malighafi za kutosha kwenye viwanda vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi nchini wanafanya kazi kwa kinyongo na bila ubunifu kwa sababu wana madeni yao ya muda mrefu na hasa Walimu, ndio maana elimu inazidi kushuka. Naiomba Serikali ilipe madeni hayo ili kuwamotisha watumishi pia waongezewe mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi ya mitambo ya kuchimbia visima; kutokana na uhaba wa maji nchini, naiomba Serikali iondoe kodi kwenye mitambo ya kuchimba visima ili watu wengi wachimbe visima kwani bei ya uchimbaji itashuka na hatimaye tutapunguza tatizo la maji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuongezeka kodi kwenye nywele za bandia; ni kweli tunahitaji kuongeza pato la Taifa, lakini naomba tungeangalia vile vitu vikubwa kuliko kuangalia kwenye nywele za bandia ambazo ni kama Serikali inawakandamiza wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi kukusanywa na TRA; kutokana na kushuka kwa makusanyo kwenye halmashauri zetu na hasa kodi zinazotokana na majengo, naomba Serikali irudishe makusanyo hayo yakusanywe na halmashauri lakini yawekwe moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, taulo za kike, nasikitika kwa kuondoa msamaha wa kodi kwenye taulo za kike. Serikali ifikirie upya uamuzi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Maendeleo kutokwenda kwenye miradi kwa wakati na pia kupelekwa bajeti ndogo. Katika mikoa yote pesa ya maendeleo imekwenda chini ya asilimia 50, hivyo naishauri Serikali kupeleka kwa wakati na kiasi chote kilichoidhinishwa na Bunge kipelekwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta binafsi, tatizo kubwa ninaloliona ni kwamba Serikali inachukua fedha taslimu kwenda kufanyia miradi kama vile kununua ndege. Nashauri Serikali kutumia sekta binafsi kuendesha miradi hii mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Liganga na Mchuchuma; naiomba Serikali ifikirie ni namna gani inaweza kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Kama kuna kikwazo kwa mwekezaji, basi Serikali ibadilishe mwekezaji mwingine atakayekuwa na vigezo vinavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mashine za EFD; mashine hizi ni mbovu kila zikipelekwa kwa fundi unatakiwa kulipa shilingi laki moja na nusu (150,000/=). Naiomba Serikali iangalie upya mfumo wa mashine hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ili na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani, pili, nachukua nafasi hii kuishukuru Kamati pamoja na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakivalia njuga suala hili la dawa za kulevya, lakini papo hapo nimshukuru Mheshimiwa Waziri ambaye aliyapokea mawazo yetu ya Kamati na kuyafanyia kazi, ikiwa mojawapo ni suala la viroba, Kamati ilipolizungumzia suala hili, tunashukuru lilikubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nina masuala machache ambayo naomba niongezee. Suala la kwanza ni suala la muswada huu pamoja na suala la Uteuzi wa Kamishna wa Tume ya Masuala ya kudhibiti dawa za kulevya kucheleweshwa kuteuliwa. Serikali imechelewesha kumteua Kamishna, lakini vilevile imechelewesha kuleta muswada hapa ndani, ingewahisha kuteuliwa huyu kamishna pamoja na kuingiza muswada hapa ndani kusingekuwa na tatizo la ukiukwaji wa haki za binadamu ambao ulikuwa umejitokeza hapa karibuni wa kamata kamata kule Dar es Salaam, niki- refer kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ameingia madarakani na kuanza kukamata kamata watu hovyo hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni suala la matumizi ya silaha. Sisi kama Kamati tuliona kunaweza kukawa na tatizo la matumizi ya silaha wakati wa ukamataji kwa wanaotumia na wanaosafirisha dawa za kulevya. Tulipohoji na kujadili kwenye Kamati ikaonekana kwamba wakati wa kuwakamata hawa wanaokuwa wanauza dawa za kulevya au kuingiza dawa za kulevya huwa wanakuwa na silaha, kwa hiyo, hawa wanaodhibiti watu wa dawa za kulevya wanajitahidi kuwa na silaha ili wajihami.

Naomba niishauri Serikali hawa watu wanapotumia hizo silaha watumie inapobidi au kama kuna ulazima, lakini namna nyingine naona kuna hatari na inaweza ikawa ni kichaka, wanaweza wakatumia loophole hiyo kwamba, kuna watu wanatumia dawa za kulevya, kumbe sivyo, kumbe ni kichaka tu. Kwa hiyo, niishauri Serikali namna nyingine kuwa makini na maafisa hawa kupata mafunzo maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee juu ya kemikali ambazo sasa hivi zinatumika badala ya dawa za kulevya. Baada ya kukatazwa dawa za kulevya watu sasa wamebuni njia nyingine ya kutumia kemikali nyingine ili kutengeneza dawa za kulevya. Hivyo, naishauri Serikali kujaribu kudhibiti uingizwaji wa kemikali hizo holela na hasa wale wanaotumia njia za panya, kwa hivyo, Serikali iwe makini.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la utata unaoweza kujitokeza wakati wa ukamataji wa hawa wanaoingiza na wanaotumia dawa za kulevya. Kwa sababu wakati mwingine mtu anaamua tu ana chuki na hila anaamua kumbambikiza mtu kesi kwamba yeye anauza dawa za kulevya au anasafirisha dawa za kulevya kumbe sio.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, ninaomba suala hili Serikali iliangalie, lisitumike kisiasa, kwamba kwa sababu tu ya chuki basi mtu fulani anaambiwa huyu anauza dawa za kulevya. Wafanye kwanza utafiti kabla ya kutoa hukumu au kumchukulia mtu hatua ili kuweza kubaini kama ni kweli huyu mtu anauza au anasafirisha dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nishukuru kwa kunipatia nafasi.