Primary Questions from Hon. Hamida Mohamedi Abdallah (19 total)
MHE. HASSAN E. MASALA (K.n.y. MHE. HAMIDA M. ABDALLAH) aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Lindi karibu 40% hawana ajira kutokana na ukosefu wa viwanda mkoani humo; na kwa kutambua kuwa sehemu kubwa ya uchumi wetu unategemea kilimo na Serikali ilitunga Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 1996 -2020 itakayosimamia maendeleo ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao:-
Je, Sera hiyo imesimamiwa vipi katika kuvifanya viwanda vilivyopo vya usindikaji wa mazao viendelezwe ili kuongeza thamani ya mazao yetu na kukuza uchumi na hatimaye vijana kupata ajira katika Mkoa wa Lindi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuchochea maendeleo ya viwanda nchini, Serikali iliandaa na kuanza utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda (Sustainable Industrial Policy – (SIDP) 1996 -2020) na baadaye iliandaa Mkakati Unganishi wa Kuendeleza Sekta ya Viwanda (Integrated Industrial Development Strategy 2025) ili kuimarisha utekelezaji wa Sera hiyo. Moja ya vipaumbele vya Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ililenga katika kipindi cha muda mfupi kuendeleza viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana nchini ikiwemo mazao ya kilimo ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa utekelezaji wa Sera unaanza mwaka 1996, mkoa wa Lindi ulikuwa na viwanda vitano vinavyosindika mazao ya kilimo, vikiwepo viwanda vya kubangua korosho na viwanda vingine vidogo vidogo vya samani, kukamua mafuta ya ufuta, usindikaji nafaka na kadhalika. Aidha, viwanda hivyo vilibinafsishwa na kwa bahati mbaya havijawahi kufanya kazi hadi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na utekelezaji wa Sera, ikijumuisha uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda, upatikanaji wa miundombinu muhimu kama vile maji, umeme, mawasiliano, barabara na kuimarisha mazingira ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu za sasa zinaonesha Mkoa wa Lindi una jumla ya viwanda vinavyosindika mazao pekee vipatavyo 329 vinavyoajiri watu 770 na kati ya hivyo viwanda vikubwa vinavyoajiri watu watano mpaka kumi vipo kumi. Kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina, sasa tunapitia vile Viwanda vya Korosho vilivyobinafsishwa ili viweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati unganishi wa kuendeleza Sekta ya viwanda umeibua mwambao wa Pwani kuwa kitovu cha kuendeleza viwanda na kuuza mauzo nje (Water Front Industrial and Export Frontiers). Lengo la mkakati ni pamoja na kukuza sekta ya viwanda vijijini itakayoongozwa na maendeleo ya kilimo na kutoa fursa ya ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati kwa kuchukua hatua za makusudi za kuvisaidia katika ngazi zote za maendeleo ili viweze kukua.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Mji wa Lindi imezungukwa na bahari, ambapo wananchi wa Kijiji cha Kitunda wanajishughulisha na shughuli za kilimo na kuishi huko kutumia usafiri ambao sio salama wa mitumbwi midogo midogo kutoka kijijini hapo kwenda Lindi Mjini kwa ajili ya mahitaji muhimu ya kibinadamu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kivuko kwa ajili ya kuvusha wananchi hao ambao maisha yao yapo hatarini kwa kutumia mitumbwi midogo midogo kutoka Lindi Mjini kwenda Kata ya Kitumbikwela?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyao:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuweka kivuko kati ya Lindi Mjini na Kijiji cha Kitunda. Mradi huu pia utahusisha ujenzi wa maegesho ya kivuko na barabara za maingilio. Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi huu.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Katika karne hii ya sayansi na teknolojia, mawasiliano ya simu za mkononi ni muhimu sana katika kurahisisha na kuharakisha huduma mbalimbali kwa watumiaji wakiwemo wavuvi, wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi, wasanii na kadhalika:-
Je, ni lini Serikali itaboresha ujenzi wa minara ya huduma ya mawasiliano ya simu katika Vijiji vya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa mawasiliano ya simu za mikononi ni muhimu katika kurahisisha na kuharakisha maendeleo na ndiyo maana Serikali imeweka sera madhubuti za kuhakikisha wananchi katika maeneo yote ya nchi wanapata huduma hiyo. Kwa kutambua hilo, Serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili kutekeleza sera hiyo kwa kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya nchi yenye uhitaji wa huduma husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imetenga jumla ya dola za Marekani 2,186,061 kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika jumla ya kata 25 za Mkoa wa Lindi zilizokuwa ama na huduma duni au kutokuwa na huduma kabisa za mawasiliano ya simu za mikononi. Kati ya Kata hizo, Kata ya Kiegi Wilaya ya Nachingwea imeshapata mawasiliano ya simu za mkononi kupita kampuni ya TTCL wakati kata nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote itaendelea kuyaainisha maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla wa kadri ya uhitaji na upatikanaji wa fedha katika kufanikisha malengo ya uanzishwaji wa Mfuko ambayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila mwananchi wa Tanzania bila kujali mahali alipo anapata huduma za mawasiliano ili kurahisisha na kuhakikisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kimaendeleo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Uwanja wa mpira wa miguu Lindi ulijengwa tangu mwaka 1957 wakati wa ukoloni wa Gavana Sir Edward Twining na mpaka leo haujafanyiwa maboresho.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuukarabati na kuwa wa kisasa ukizingatiwa kwamba uwanja huo ulikuwa ukitumika kwa ajili ya michezo ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge Viti Maalum. kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli uwanja wa mpira wa miguu wa Lindi (Ilula) ni mkongwe ulijengwa wakati wa ukoloni wa Mwingereza na unahitaji ukarabati ili kuufanya kuwa wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Maendeleo ya Michezo inahimiza kila taasisi yenye kiwanja au viwanja vya michezo kuvitunza viwanja hivyo ili viweze kudumu. Uwanja huu upo chini ya Halmashauri ya Lindi kama ilivyo kwa viwanja vingine vingi vilivyoko chini ya Halmashauri hapa nchini. Wizara yangu inashauri Halmashauri ya Lindi kuangalia uwezekano wa kuufanyia ukarabati uwanja huo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali pamoja na wananchi wa Lindi wakiongozwa na Waheshimiwa Wabunge.
Aidha, Wizara yangu itakuwa tayari kutoa ushauri wa kitaalamu ili kusaidia kukarabati uwanja huo na kuufanya kuwa wa kisasa na kutumiwa na wanamichezo wengi zaidi wa Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Katika miaka ya 1950 Lindi kulikuwa na reli inayotoka Nachingwea kupitia Mtama, Mnazi Mmoja, Mingoyo hadi Bandari ya Mtwara na ilikuwa ikisafirisha korosho, mbao, magogo na watu. Kwa sasa Lindi kuna viwanda vingi na vingine vinatarajiwa kujengwa, barabara ya Kibiti – Lindi ambayo hupitisha mizigo mizito huenda ikaharibika mapema, hivyo reli ni muhimu sana.
Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuifufua reli ya Kusini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara inaunganishwa kwa reli ili kutumia Bandari kubwa ya Mtwara katika kusafirisha mizigo mbalimbali, Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu wa reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay ambapo inatarajiwa reli hiyo ijengwe kwa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP). Baada ya kukamilika kwa reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay utaratibu wa kuunganisha Lindi na Mtwara kwenye reli utafuata.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kumwajiri Mshauri wa Uwekezaji (Transaction Advisor) atakayekuwa na jukumu la kuunadi mradi kwa ajili ya wawekezaji mbalimbali na hatimaye kujenga reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay na matawi ya kwenda Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya urefu wa kilometa 1,000. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Mji wa Ruangwa Mkoani Lindi una madini mengi lakini wachimbaji walio wengi wa madini hayo ni wachimbaji wadogo wadogo ambao hawana zana za kisasa za kuchimba madini.
Je, Serikali haioni haja ya kuwasaidia kwa kuwapa mikopo ili waweze kununua zana za kisasa za uchimbaji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalaum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeweka vipaumbele vya kusaidia wachimbaji wadogo ili kufanya shughuli zao za uchimbaji huo kuwa wa manufaa kwao pamoja na kuongeza pato la Taifa. Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuboresha sekta ya uchimbaji madini mdogo kwa kutoa ruzuku kwa wachimbaji hao wadogo ili waweze kuboresha shughuli zao kuwa za kisasa na kuboresha uchenjuaji na shughuli nyingine za uchimbaji. Lakini vipaumbele vingine ni kuwapa ushauri wa kitaalamu, taarifa za upatikanaji wa vifaa vya uchimbaji, mafunzo kwa vitendo pamoja na masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2010 na 2013 Serikali ilitoa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 910.195 kwa kampuni nane za wachimbaji wadogo. Aidha, kati ya mwaka 2013 na 2015 Serikali ilitoa ruzuku ya shilingi bilioni
• kwa wachimbaji 115 kwa ajili ya uchimbaji wao nchi nzima pamoja na Mkoa wa Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianza kutoa ruzuku badala ya mkopo kwa wachimbaji wadogo kutokana na wachimbaji wadogo kushindwa masharti ya mikopo na hivyo kushindwa kurejesha na badala yake sasa wanapewa ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele muhimu vinavyozingatiwa katika kutoa ruzuku hiyo ni pamoja na kumiliki leseni hai na halali ya shughuli za uchimbaji, kuwa na utambulisho wa kodi na mlipa kodi (TIN) na rekodi nzuri ya kulipa mrabaha na mapato mengine ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Jiolojia Tanzania wataendelea kufanya utafiti wa maeneo yote nchini ili wachimbaji wadogo nao sasa waweze kunufaika na rasilimali hii ya Taifa.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Mwaka 1974 Tanzania iliridhia Mkataba wa Kuzuia Uchafuzi wa Bahari na Usalama wa Bahari ambao lengo mojawapo ni kuzuia uvuvi haramu wa kutumia mabomu na kutoa misaada ya vifaa vya kuzuia uchafuzi wa bahari:-
(a) Je, Serikali imeweka mikakati gani ya kuzuia uvuvi haramu wa kutumia mabomu ambao bado unaendelea?
(b) Je, Serikali inawasaidiaje wavuvi ili waachane na uvuvi haramu wa kutumia mabomu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mikakati mbalimbali ya kupambana na uvuvi haramu ukiwemo uvuvi wa kutumia mabomu, mikakati hiyo ni pamoja na:-
(a) Kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi kupitia Halmashauri, Serikali za Vijiji na Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi kwa maana ya BMUs;
(b) Kuendelea kutoa elimu kuhusu athari za uvuvi haramu kwa mazingira, jamii na uchumi;
(c) Kufanya maboresho ya sheria ili kuwa na sheria kali dhidi ya uvuvi haramu hasa uvuvi wa kutumia mabomu ama milipuko ikiwa ni pamoja na kuweka kipengele cha kuonesha uvuvi haramu ni uhujumu wa uchumi; na
(d) Kuimarisha Mashirikiano ya Kikanda na Kimataifa kwa kushirikiana na nchi mbalimbali zikiwemo nchi za SADC katika kuzuia uvuvi usioratibiwa na usioripotiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kufanya operesheni ikiwa ni pamoja na Operesheni Sangara, Jodari na operesheni za Kikosi cha Kitaifa kwa maana ya Mult Agency Task Team (Matt) cha kuzuia uharibifu wa mazingira ili kulinda rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia MATT, Serikali imefanya operesheni katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga na Dar es Salaam ambapo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kupungua kwa idadi ya milipuko kutoka asilimia 88 kwa mwezi hadi kufikia asilimia mbili mwezi Machi 2018, kukamatwa kwa vifaa vya milipuko na watuhumiwa 32 ambapo kesi 13 zimefunguliwa mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuwasaidia wavuvi kuachana na uvuvi haramu ukiwemo wa kutumia mabomu, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wavuvi wa jamii za Ukanda wa Pwani kuhusu athari za uvuvi haramu kama vile uharibifu wa mazingira, matumbawe, mazalia na makulio ya samaki, kusababisha jangwa katika bahari, kuua viumbe vingine visivyo kusudiwa, vifo, ulemavu ili waache kabisa vitendo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inaendelea kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Msingi, Vyama vya Akiba kwa maana ya SACCOS na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana na vyombo bora vya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu pamoja na nyuzi kwa ajili ya nyavu za uvuvi na vifungashio kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2011na Sheria ya Mamlaka ya Mapato (VAT) ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu. Aidha, Serikali inahamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kutengeza boti na zana bora za uvuvi ili kuwezesha wavuvi kuzipata kwa bei nafuu na kwa urahisi.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Mgogoro wa ardhi kati ya Mbuga za Wanyama Selous – Kilwa na wananchi wanaoishi karibu na mbuga hiyo umezidi kuwa mkubwa kwa sababu mipaka halali haijulikani. Kwa mfano, mwaka 1974 mpaka halali ulikuwa Mto Matandu, mwaka 2010 mpaka huo ulisogezwa kufikia Bwawa la Kihurumila katika Kijiji cha Kikulyungu:-
a) Je, Serikali iko tayari kuhakiki eneo hilo ili kuondoa mgogoro mkubwa uliopo kati ya Wanakijiji wa Kihurumila na Mbuga?
b) Je, Serikali iko tayari kutatua mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kilwa na Mbuga.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Pori la Akiba Selous uliwekwa kwa kuzingatia Tangazo la Serikali Na. 275 kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 12 ya mwaka 1974. Tangu wakati huo hadi sasa mpaka huo haujafanyiwa marekebisho yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Kikulyungu na Pori la Akiba la Selous unatokana na kijiji hicho kutokukubaliana na uhakiki wa mpaka wa pori hilo uliofanyika mwaka 2010 kwenye eneo la Wilaya ya Liwale kwa kuwatumia wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa, Wizara yangu ilitembelea Pori la Akiba la Selous – Kanda ya Kusini Liwale tarehe 3 na 4 Agosti, 2018 na kukutana na wananchi na viongozi wengine wa Serikali ikiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa mgogoro huo. Kupitia ziara hiyo, wananchi sasa wameridhia kazi ya uhakiki ifanyike upya na kuhakikisha kuwa watatoa ushirikiano kwa wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; wanakijiji; na Halmashauri ya Mji kuhakiki mpaka wa Pori la Akiba Selous katika eneo la Kijiji cha Kikulyungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wananchi, wawekezaji na maeneo yaliyohifadhiwa, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote katika uhakiki wa mipaka na uwekaji wa alama kwenye mapori yote nchini na kuandaa na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Mgogoro wa ardhi katika Hifadhi ya Wanyamapori Selous-Kilwa umechukua nafasi kubwa kati ya Serikali na wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo. Mpaka halali haujulikani kwani mwaka 1974 mpaka halali ulikuwa Mto Matandu na mwaka 2010 mpaka huo ulisongezwa mpaka Bwawa la Kilurumila, Kijiji cha Kikulyungu.
Je, Serikali ipo tayari kuhakiki eneo hilo ili kutatua mgogoro uliopo kati yake na wananchi wa Kijiji cha Kihurumile?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Abdallah Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Kikulyungu ni moja ya vijiji tisa vinavyopakana na Pori la Akiba la Selous kwa Wilaya ya Liwale. Ndani ya pori hilo kuna bwawa lijulikanalo kama Kihurumila ambalo ni sehemu muhimu kwa mazalia ya samaki na wanyamapori kama vile mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka1970 wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu walikuwa wakivua samaki katika bwawa hilo baada ya kupewa vibali maalum. Hata hivyo, mwaka 1982 Serikali ilizuia shughuli za uvuvi kutokana na baadhi ya wananchi kukiuka taratibu za kuvua samaki ikiwemo matumizi ya sumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Pori la Akiba Selous umewekwa kwa kuzingatia Tangazo la Serikali Na. 275 la mwaka 1974. Tangu wakati huo hadi sasa mpaka huo haujafanyiwa marekebisho yoyote. Hata hivyo, wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu hawakubaliani na tafsiri na uhakiki wa mpaka uliofanyika licha ya vijiji vinne kukubaliana na uhakiki huo. Aidha, wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu wanadai kwamba Bwawa la Kihurumila ni sehemu ya eneo la kijiji hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilituma maafisa kuhakiki mipaka ya vijiji vitano kati ya vijiji tisa vinavyounda WMA ya Liwale vinavyopakana na Pori la Akiba la Selous. Vijiji hivyo ni Kimambi, Kikulyungu, Barikiwa, Chimbuko na Ndapata. Uhakiki huo ulishirikisha pia Maafisa kutoka Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi Tanzania, Maafisa Ardhi Wilaya ya Liwale, Taasisi isiyo ya Kiserikali ijulikanayo kama World Wide Fund for Nature (WWF) na wananchi na Viongozi wa Kata na Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Liwale. Zoezi hili lililenga kutatua mgogoro wa mpaka na kutangaza WMA ya Liwale. Hata hivyo, wananchi wa Kikulyungu waliwafanyia vurugu watalaam wa Wizara ya Ardhi walipotembelea eneo la mgogoro kwa ajili ya kutafsiri Tangazo la Serikali na kusababisha watalaam kukimbia kuokoa maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hali hiyo, Wizara imepanga kukutana na viongozi wa Mkoa wa Lindi akiwemo Mheshimiwa Mbunge kwa lengo la kutatua mgogoro huo kwa manufaa ya uhifadhi na ustawi wa wananchi.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Kilwa ni moja ya miji mikongwe katika Afrika Mashariki tangu Anno Domino (AD) 900 -1700 pamoja na miji mingine ya Lamu, Mombasa, Sofala na Zanzibar. Miji hiyo ilipewa heshima ya jina la Urithi wa Dunia (World Heritage Site). Kwa kawaida miji hiyo husaidiwa na Mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani, Japan, Ujerumani, Uingereza na Shirika la UNESCO:-
Je, Serikali ya Tanzania imefaidika nini kutoka katika Mataifa hayo yanayosaidia nchi za urithi wa dunia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohammed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yaliorodheshwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia mwaka 1981. Mwaka 2004 eneo la hifadhi la visiwa hivi liliingizwa kwenye orodha ya maeneo yenye urithi ulio hatarini kutoweka (Endangered Site). Hatua hiyo ilisababishwa na hali yake ya uhifadhi kutokidhi kiwango cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO).
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2005, Wizara kwa kushirikiana na UNESCO na nchi za Ufaransa, Norway, Japan na Marekani iliandaa miradi ya kukarabati magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na mafunzo. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na mradi wa Euro 600,000 kutoka Serikali ya Ufaransa; Mradi wa Dola za Kimarekani 201,390 kutoka Norway; mradi wa Dola 119,000 kutoka Ufaransa na UNESCO; mradi wa Dola 66,000 kutoka ILO; mradi wa Dola 100,000 kutoka World Monuments Fund; mradi wa Dola 700,000 kutoka Ubalozi wa Marekani; na mradi wa Dola 43,900 kutoka UNESCO. Kukamilika kwa ukarabati kuliwezesha magofu hayo kuondolewa kwenye orodha ya urithi uliokuwa hatarini kutoweka mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, faida nyingine zilizopatikana ni pamoja na ushauri wa kitalaam na misaada ya vifaa mbalimbali; kuendelezwa kwa miundombinu katika maeneo husika na ongezeko la kipato kwa jamii husika kupitia biashara ya utalii.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Kilwa ni moja kati ya miji mikongwe katika Afrika Mashariki tangu 900 – 1700 AD ikiwemo Lamu, Mombasa, Sofaa na Zanzibar. Miji hii ilipewa heshima ya jina la urithi wa dunia (World Heritage Sights) na husaidiwa na mataifa mbalimbali kama Marekani, Japan, Ujerumani, Uingereza na Taasisi ya UNICEF;
Je, Serikali ya Tanzania inafaidika na nini kutokan kwenye mataifa hayo yanayosaidia nchi zenye Miji ya Urithi wa Dunia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Urithi wa Dunia yanaratibiwa kimataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization – UNESCO) kupitia mkataba wa mwaka 1972 na ulinzi na uhifadhi wa urithi wa dunia. Mji wa Kilwa una magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ambayo ni miongoni mwa maeneo ya urithi wa utamaduni ambayo yalipewa hadhi ya urithi wa dunia mwaka 1981. Maeneo mengine ya urithi wa utamaduni yenye hadhi hiyo ni pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar, Michoro ya mapangoni ya Kolo – Kondoa na urithi mchanganyiko wa Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo manufaa ambayo Serikali ya Tanzania inafaidika kutoka kwa mataifa mbalimbali na nchi wahisani kwa kuwa na maeneo yenye hadhi ya urithi wa dunia. Kuwa na maeneo ya aina hii kunasaidia kuwepo kwa juhudi za pamoja za kimataifa za kuhifadhi, kulinda na kuyaendeleza maeneo haya. Manufaa haya yanaweza kugawanywa katika makundi matatu ambayo ni ushauri wa kiufundi katika masuala ya uhifadhi, misaada ya kifedha na kulitangaza eneo kiutalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya manufaa ambayo Mji wa Kilwa umepata kwa kuwa ni hadhi ya urithi wa dunia ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2002 – 2005 ulifanyika ukarabati wa msikiti mkuu na mdogo pamoja na kubwa, yalitolewa mafunzo kwa mafundi sanifu, ilinunuliwa gari na ukarabati wa boti kwa ufadhili wa Serikali ya Ufaransa wenye thamani ya Euro 660,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2005 - 2008 ulifanyika ukarabati wa Kasri ya Sultani, ununuzi wa mashine ya boti, ukarabati wa nyumba ya wageni ya Kijerumani, ujenzi wa kinga maji eneo la Gereza la Kale na ujenzi wa Birika la Maji la Songo Mnara kwa ufadhili wa UNESCO na Norway wenye thamani ya USD 201,390.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 – 2009 yalitolewa mafunzo kwa waongoza wageni, mapishi, usindikaji wa chakula pamoja na uanzishaji wa vikoba kwa wananchi, uandaaji wa kitabu cha urithi wa Kilwa kwa ufadhili wa UNESCO na Serikali ya Ufaransa wenye thamani ya USD 159,780.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 – 2014 ukarabati wa majenzi Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kwa ufadhili wa Ubalozi wa Marekani wenye thamani ya USD 700,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi hii yote unafanyika kwa kushirikisha wananchi kwa kuwapatia mafunzo ya uhifadhi na kufanya ukarabati wenyewe. Aidha, wananchi wanapatiwa mafunzo ya namna ya kutumia fursa za utalii ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uongozaji watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuishukuru UNESCOna nchi wahisani kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza maeneo haya yenye urithi wa utamaduni.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka injini mpya ya Kivuko cha MV Kitunda - Lindi Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), umetenga fedha kiasi cha Shilingi Milioni 850 kupitia vyanzo vyake vya ndani kwa ajili ya ukarabati wa Vivuko nchini kikiwemo MV Kitunda ambacho ukarabati wake utahusisha ubadilishaji wa injini pamoja na matengenezo mengine. Ukarabati huu utaanza robo ya pili ya mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Lindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi. Mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo na kuanza kutoa huduma, miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya sasa itakuwa Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.
Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za afya kwa wananchi Serikali tayari imekwishaipatia Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya kwenye eneo la Kimkakati na lenye mahitaji makubwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko kuu na stendi ya mabasi Lindi Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imejumuisha mradi wa soko kuu na stendi kwenye Mpango wa TACTIC unaojumuisha Halmashauri 45 ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ipo katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo inayohusisha Halmashauri 15 zinazotarajiwa kuanza Januari, 2023.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kusaidia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uvuvi na Usafiri Baharini Lindi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimwa Hamida Mohamed Abdhallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuongeza idadi ya vyuo vikuu kulingana na uhitaji na upatikanaji wa rasilimali fedha. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) imetenga shilingi bilioni 5.8 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mkoa wa Lindi. Kampasi hiyo itakuwa mahususi kwa ajili ya kozi za Ufugaji wa Nyuki, Kilimo-Uchumi na Biashara, Sayansi na Teknolojia ya Chakula, na Uhandisi Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tayari kinatoa kozi za Uvuvi katika Shule Kuu ya Akua na Teknolojia ya Uvuvi - Kunduchi na kozi za Sayansi ya Bahari katika Taasisi ya Sayansi ya Bahari Zanzibar, Serikali itafanya tathmini ili kuona kama kuna uhitaji wa kuongeza kozi za Uvuvi na Usafiri wa Baharini katika kampasi mpya ya Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo Kikuu cha Uvuvi na Usafirishaji baharini katika eneo la Kikwetu - Lindi ambapo tayari Ekari 150 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi haina mpango wa kujenga Chuo Kikuu cha Uvuvi katika eneo la Kikwetu Lindi Mjini. Hata hivyo, Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kwa maana ya NIT imepewa eneo lenye ukubwa wa ekari 125 lililopo Kikwetu Lindi. Eneo hilo ambalo tayari NIT imekamilisha taratibu za kumiliki, litatumika kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Lindi ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ambacho kitatoa kozi katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada katika fani mbalimbali za usafirishaji na uchukuzi ikiwemo Utengenezaji wa meli, uendeshaji wa vyombo vya majini na huduma za bandari.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/2023 kazi zitakazofanyika katika eneo hilo ni kuandaa mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi katika eneo hilo. Sambamba na maelezo hayo, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inatarajia kujenga Kitivo cha Kilimo katika Halmashauri ya Lindi Mjini ambapo tayari wameomba kupatiwa hekta 500.
Mipango ya maandalizi ya ujenzi wa chuo hicho inaendelea kwa ushirikiano kati ya Mkoa wa Lindi, Halmashauri ya Lindi Mjini na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: -
Je, lini Serikali itaipatia fedha Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ili iweze kutekeleza mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Soko Kuu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ni miongoni mwa miji 45 ambayo imepewa kipaumbele cha kupata ufadhili wa Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji, Manispaa na Majiji ambapo ujenzi wa soko ni miongoni mwa miundombinu itakayotekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha upimaji eneo la ujenzi wa soko na kupata hati yenye ukubwa wa mita za mraba 5,845 pamoja na cheti cha Hati ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) kutoka NEMC kama sehemu ya lazima katika kuanza kwa mradi huu katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga soko kubwa la Samaki Lindi Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kila kitu, pia ninaamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Hassan Suluhu kwa imani yake kubwa kwa kunipa nafasi hii nimsaidie kumuwakilisha katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi nchini, ikiwemo masoko ya samaki katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kwa kuzingatia upatikanaji wa maeneo na rasilimali fedha. Changamoto iliyopo ni upatikanaji wa maeneo katika Halmashauri zetu kwa ajili ya ujenzi wa masoko. Kwa sababu hii, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwa nafasi yake, asaidie kupatikana kwa eneo la ujenzi wa soko hilo katika Manispaa ya Lindi na mara likipatikana, Wizara yangu itafanya tathmini za awali ikiwa ni pamoja na kuandaa michoro na gharama za ujenzi. Aidha, baada ya kukamilika kwa hatua hizo, Wizara itatafuta fedha za ujenzi wa soko hilo katika vyanzo vya ndani, yaani bajeti ya Wizara au miradi kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha Kilimo katika eneo la Ngongo Mkoani Lindi ambapo tayari hekari 120 zimetengwa kwa ajili hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge Lindi Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha huduma za ugani iliamua kuanzisha Vyuo Vya Mafunzo vya Kilimo vya Serikali tangu miaka ya 1930 ili kuendeleza sekta hii hapa nchini. Mpaka sasa vimeshaanzishwa Vyuo Vya Mafunzo ya Kilimo 14 ambavyo vinatoa mafunzo ya fani mbalimbali za kilimo ngazi ya Astashahada na Stashahada kikiwepo Chuo cha MATI Mtwara kwa ajili ya Kanda ya Kusini kwa maana ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wizara inaendelea na ukarabati wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo na kuvipatia vifaa vya kufundishia. Hata hivyo, Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Mradi wa HEET ambapo katika eneo hilo la Ngongo kitajengwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kampasi ya Lindi kitakachotoa programu za kilimo.