Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hamida Mohamedi Abdallah (27 total)

MHE.HAMIDA M. ABDALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, kwa majibu yake yenye matumaini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mikoa hii ya Lindi tuna majina mengi sana, tunaitwa Mikoa ambayo imesahaulika, Mikoa iliyokuwa pembezoni, Mikoa ya Kusini. Tunapata hofu sana tunapokosa matangazo na matangazo kusikika katika eneo la mjini tu, wakati Wilaya ya Nachingwea ina kata 34, na wanahitaji kupata matangazo. Ningependa Mheshimiwa Waziri atuthibitishie wananchi wa Wilaya ya Nachingwea ni lini atapata fedha ili kwenda kujenga mtambo huu?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimthibitishie tu kwamba tumeweka kipaumbele kwenye Mikoa ambayo iko pembezoni ambayo kwa kweli usikivu wa vituo vyetu vya Taifa umekuwa mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nimefanya ziara kwenye Mikoa 13 ya pembezoni lakini kwa Mkoa wa Lindi ambapo mimi natoka na Waziri Mkuu anatoka, na sisi ni waathirika wa tatizo hili, nataka nikuhakikishie kwamba imefanyika tathimini na hivi tunavyoongea juzi Katibu Mkuu wa Wizara yangu ametoka huko pamoja na Mkurugenzi wa TBC wakiangalia namna tunaweza tukaanza hiyo kasi ya uboreshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tu nikumbushe kwamba juzi Waheshimiwa Wabunge wamepitisha bajeti ya Wizara yangu na moja ya eneo ambalo tunawekeza kwa nguvu kubwa ni kuhakikisha tunaongeza usikivu. Wakati wa bajeti tulieleza hapa kwamba zaidi ya Wilaya 81 usikivu wa redio yetu hausikiki, kwa hiyo katika mipango yetu tutakwenda awamu kwa awamu na kipaumbele tutatoa kwa ile Mikoa ya mipakani na Mikoa inayoitwa ya pembezoni.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu wakati wa kampeni zake ilikuwa ni ahadi yake ya kujenga kivuko cha kutoka Lindi kwenda Kitunda na alisema baada ya wiki moja Mkurugenzi wa vivuko atakuja Lindi na kweli alikuja, akaja kuangalia eneo. Sasa baada ya kumaliza katika shughuli hiyo ya kwanza tulikuwa hatufahamu kinachoendelea ni kipi, lakini namshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri yenye matumaini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Rais alituahidi kwamba, katika maeneo yote kuanzia Tanga, Dar es Salaam kuja Lindi mpaka Mtwara kutakuwa na uwezekano wa kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kwa sababu wananchi hawa ni wavuvi wa samaki, kujenga kiwanda cha samaki ili kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo haya.
Je, Serikali imejipangaje katika kuhakikisha maeneo haya yanakuwa na kiwanda cha samaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea shukurani kutoka kwa Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum. Namshukuru sana na kwa kweli nafurahia sana Wabunge wengi wanatambua juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza ahadi, ana dhamira ya dhati na kila alipoahidi anajitahidi kutafuta fedha ili kuweza kuteleza ile ahadi yake. Sisi kwa kweli tulioko katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tunajivunia kwa kupewa dhamana hii ya kuwajengea Watanzania miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sehemu ya viwanda; maadam alitoa ahadi, nimhakikishie ahadi hiyo itatimia. Kama ambavyo amemsikia Mheshimiwa Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wakati akihitimisha hotuba yake ya bajeti, aliongelea kwa mapana kwamba, karibu kila mahali kuna aina ya viwanda ambavyo anavikusudia kuviboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile, katika maeneo ya Pwani, wavuvi nao watafikiriwa katika kuhakikisha kwamba, tunapata viwanda na viwanda hivyo vinahamasishwa kutoka sekta binafsi waweze kuwekeza na sisi tutawawekea mazingira mazuri ili hatimaye watujengee viwanda na kuchangia katika kuibadilisha nchi hii kuwa nchi ya viwanda itakapofika mwaka 2025.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuna dharura kubwa iliyojitokeza katika Manispaa ya Lindi; na juzi niliizungumzia hapa ndani ya Bunge lako tukufu; lakini taarifa ambazo anapewa Mheshimiwa Naibu Waziri wetu, siyo sahihi kwa sababu dharura hii ni kubwa sana na wananchi wa Lindi wanahangaika, hawana sehemu nyingine ya kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba Kisima cha Mitwero pampu imekufa na chanzo cha Mambulu kimejaa matope kiasi kwamba hakiwezi kutoa maji, wananchi leo wanahangaika na wananunua dumu moja shilingi 1,000/=. Hili ni tatizo kubwa sana! Namwomba Mheshimiwa Waziri wetu atuambie, atatusaidiaje ili kutatua hii kero ya maji wananchi waweze kuondokana nayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pale Mji wa Lindi kumekuwa na matatizo kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu ya maji ya muda mrefu, ndiyo maana Serikali imebuni na inaendelea kujenga mradi wa kumaliza tatizo hilo. Tatizo la maji kwa Mji wa Lindi litakwisha ikifika mwezi wa Kumi, huu mradi ambao unaendelea utakuwa umekamilika.
Mhesimiwa Naibu Spika, kwa hii dharura ambayo imejitokeza, kwa sababu yale mabomba yanapita chini ya maji na hatuwezi ku-control kwa sasa nguvu ya maji kwenye ile bahari, kwa hiyo, mara kwa mara yale mabomba yamekuwa yanakatika. Ninapeleka wataalam wangu wakasaidiane na wataalam walioko pale Lindi ili tumalize angalau kwa dharura wananchi wa pale waendelee kupata maji. Ufumbuzi wa kudumu ni ule wa kukamilisha mradi ambao tunaendelea kuusukuma kwa nguvu zote tuweze kuumaliza wananchi wa Lindi waweze kupata maji.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Maji, hapo ndiyo umeshawaagiza hao wataalam ama utawaagiza lini ili waende huko Lindi? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba wapo tayari wanashughulikia hilo tatizo, hivi sasa wapo huko.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, namshuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Hata hivyo, bado watu wa Kata ya Rasbura Kijiji cha Mitwero wanaendelea kulalamikia kuhusu tatizo hili ambalo lipo. Fidia ambazo wamelipwa wananchi wale ni ndogo kiasi kwamba wanashindwa kununua maeneo mengine mbadala ili waendelee kufanya shughuli zao. Je, Serikali itawasaidiaje wananchi hawa kupata maeneo mengine mbadala ili waendelee kufanya shughuli zao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba Wizara yangu ikishirikiana pia na Ofisi ya Manispaa ya kule, kuna utaratibu uliokuwa unafanywa wa kupitia upya maeneo yale ili kuweza kuona wale ambao wamelipwa fidia ndogo kulingana na thamani ya ardhi ambayo imetwaliwa wanapata stahiki zao. Ndiyo maana nimesema zoezi hili lilikuwa linafanyika upya. Mpaka wakati huu napozungumza, baadhi ya taasisi ambazo zilikuwa zimechukua maeneo hayo zimekwishawalipa watu hao fidia zao na wanaendelea na taratibu zao za kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la kusema kwamba tutawasaidiaje kupata maeneo, unapotoa ardhi yako kwa mtu au taasisi kinachotakiwa kulipwa ni ile fidia stahiki ambayo itakufanya wewe pia uweze kupata eneo lingine la kuanzisha makazi mengine au maendeleo mengine kwa kadri ambavyo utakuwa umejipanga. Kwa sababu fidia yoyote inayochukuliwa lazima iende na bei ya soko. Tatizo tulilonalo, baadhi ya wananchi wanakuwa na ule uharaka wa kutoa ardhi yao na wanapewa fidia ndogo ambayo haiwezi kuwafikisha mahali ambapo wanastahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia Bunge hili tunasema kwamba ni marufuku kwa watu kuwanyanyasa wananchi kwa kuwapa fidia ndogo ambazo hazikidhi mahitaji. Ndiyo maana vilevile tumesema kuanzia sasa hakuna ardhi itakayotwaliwa bila Wizara yangu kujiridhisha na fidia ambayo itakuwa imetathminiwa kwa wale ambao ardhi yao inakwenda kutwaliwa, ni lazima fidia ifuate bei ya soko itakayokuwepo kwa wakati huo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, majibu yenye matumani makubwa katika Mkoa wetu wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kuanzisha Mfuko huu wa UCSAF. Kwa utekelezaji wake katika Mkoa wetu wa Lindi ni kata 25 na vijiji 99 ambavyo tunavitarajia vianze kupata mawasiliano. Ningependa kujua ni kwa namna gani Serikali watapeleka msukumo kwa watoa huduma hii ya mawasiliano ili vijiji hivi 99 na kata 25 za Mkoa wa Lindi ziweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake za kufuatilia suala hili. Alikuja ofisini na alikutana na Waziri wangu na kwa kweli pamoja na Wabunge wengine wa Mkoa wa Lindi wanalifuatilia sana suala hili ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuthibitisha kwamba tutayafuatilia haya makampuni yanayotoa huduma. Kwa wale ambao hawana huduma za kutosha tutahakikisha UCSAF inaingilia ili yapatikane mawasiliano kama ambavyo tumekusudia kutoa mawasiliano kwa vijiji vyote vya Tanzania.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri samahani kidogo. Mheshimiwa kule nyuma umesimama sijaelewa. Mheshimiwa Naibu Waziri naomba umalizie.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba tutazifuatilia hizi kampuni kuhakikisha kwamba zinatimiza wajibu wake wa kupeleka mawasiliano katika vijiji husika vya Mkoa wa Lindi vyote 99 katika kata 25 pamoja na vijiji vyote Tanzania nzima.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, majibu yenye matumani makubwa katika Mkoa wetu wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kuanzisha Mfuko huu wa UCSAF. Kwa utekelezaji wake katika Mkoa wetu wa Lindi ni kata 25 na vijiji 99 ambavyo tunavitarajia vianze kupata mawasiliano. Ningependa kujua ni kwa namna gani Serikali watapeleka msukumo kwa watoa huduma hii ya mawasiliano ili vijiji hivi 99 na kata 25 za Mkoa wa Lindi ziweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake za kufuatilia suala hili. Alikuja ofisini na alikutana na Waziri wangu na kwa kweli pamoja na Wabunge wengine wa Mkoa wa Lindi wanalifuatilia sana suala hili ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuthibitisha kwamba tutayafuatilia haya makampuni yanayotoa huduma. Kwa wale ambao hawana huduma za kutosha tutahakikisha UCSAF inaingilia ili yapatikane mawasiliano kama ambavyo tumekusudia kutoa mawasiliano kwa vijiji vyote vya Tanzania.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba tutazifuatilia hizi kampuni kuhakikisha kwamba zinatimiza wajibu wake wa kupeleka mawasiliano katika vijiji husika vya Mkoa wa Lindi vyote 99 katika kata 25 pamoja na vijiji vyote Tanzania nzima.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimshukuru Mheshimiwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri yenye matumaini. Ninashukuru Serikali inatambua kwamba uwanja ule unahitaji kukarabatiwa na kuwa uwanja wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa Lindi usifananishwe na viwanjwa vingine vilivyojengwa na Halmashauri. Uwanja wa Lindi ni miongoni mwa viwanja vitatu bora vilivyojengwa na wakoloni mana yake ni kwamba tumerithi kutoka mikononi mwa wakoloni ikiwemo kiwanja cha Mkwakwani - Tanga, kiwanja cha Dar es salaam na kiwanja cha Lindi Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja ule umewahi kutumika kwa michezo ya Afrika Mashariki, kwa hiyo uwanja unahistoria ya kipekee kwamba timu za Afrika Mashariki zimechezwa katika uwanja wa Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wana-Lindi sasa tunahitaji kuona uwanja ule unabadilika na kuwa uwanja wa kisasa, tunaiomba Serikali ituambie itatusaidiaje kukarabati uwanja ule? Ninajua kwamba Halmashauri haina uwezo wa fedha wa kukarabati uwanja ule na kuwa uwanja wa kisasa, kwa hiyo ninaiomba Serikali ituambie ni namna gani itaweza ikatusaidia kukarabati uwanja na kuwa uwanja wa kisasa?
NAIBU WAZIRI, HABARI UTAMADUNI SANAA NA
MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Hamida kwa jinsi alivyokuwa mstari wa mbele kufuatilia suala la ukarabati wa uwanja huu wa mpira wa miguu wa Ilula (Lindi), kwa kweli hii imekuwa ni chachu kubwa sana katika maendeleo ya ukuaji wa soka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishauri Halmashauri ya Lindi kwamba iweke kipaumbele katika kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huu. Pili, napenda kuchukua nafasi hii kumjulisha Mheshimiwa Hamida kwamba Serikali inalitambua hili na kutokana na hilo imekuwa ikitoa ushauri kwa TFF kuzisaidia Halmashauri kufanya ukarabati wa viwanja kwa kutumia wadau mbalimbali au wafadhili wa ndani na nje ya nchi, na kwa namna hiyo basi TFF imekuwa ikiweka katika orodha kila mwaka walau viwanja katika Halmashauri mbili hadi tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumtaarifu kwamba uwanja wa Ilula upo miongoni mwa orodha ambayo imewekwa na TFF kwa ajili ya ukarabati. Niseme tu kwamba TFF watakapotaka kufanya ukarabati itabidi waweke mkataba na Halmashauri ya Lindi na mkataba huo unasharti kwamba ni lazima kipaumbele cha matumizi kiwe katika mchezo wa mpira, ahsante sana.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu haya yenye matumaini kwetu wananchi wa Mikoa hii ya Kusini, kwa sababu sasa tunaona Serikali inafanya jitihada kubwa sana katika kuharakisha maendeleo kwa Mikoa hii ya Kusini. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri ambayo tunaisubiri kwa hamu kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, napenda sasa kujua, baada ya ujenzi huu wa reli hii ya Mbamba Bay kukamilika, halafu itakapokuja katika eneo hili la Mtwara – Lindi.
Je, ujenzi huu wa reli ya Mtwara - Lindi utaishia Lindi tu au itakuwa Mtwara – Lindi – Dar es Salaam? Napenda kujua hilo, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendeleza Mikoa ya Kusini katika masuala ya miundombinu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kutupongeza na nimwahidi kwamba reli ambayo tunaiongelea hapa ni ile ambayo ilikuwepo zamani ambapo ilikuwa inatoka Mtwara – Lindi inapita Mnazi Mmoja na ilikuwa inaishia Liwale. Hoja ya kujenga reli kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam hatujawahi kufikiria. Tumesikia na tutaendelea kulitafakari hilo suala.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ningependa sasa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, katika Mji wa Lindi Manispaa, kumetokea tatizo la dharura kubwa sana katika wiki hii. Wananchi wamekosa maji, wanahangaika na visima ambavyo vilikuwa vinatoa maji pale Kitunda kuleta mjini, visima viwili pampu zimekufa na kisima kimoja kimebomoka. Wananchi wanahangaika sana, ningependa kujua Serikali itatusaidiaje ili ku-solve tatizo hili la maji, wananchi waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli muda mrefu tumekuwa tunapata matatizo kwa wananchi wa Mji wa Lindi kupata shida ya maji kutokana na setup ya miundombinu jinsi ilivyo. Kwa sababu visima viko ng‟ambo ya pili vinazalisha maji, mabomba yanapita chini ya bahari, halafu yanaleta maji kwenye Mji wa Lindi, yakitokea mawimbi, yale mabomba yanakatika. Kwa hiyo, Mji wa Lindi unakosa maji na ndiyo maana Serikali ilikuja na mradi mkubwa ule wa Ng‟apa ambao ukikamilika sasa matatizo katika Mji wa Lindi yatakuwa yamekwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa sina taarifa, lakini kwa taarifa hii, leo baada ya saa saba nitafuatilia ili kujua tunafanya nini na nitampatia majibu Mheshimiwa Mbunge.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu haya ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini na Nishati, majibu ya jumla ambayo yanaelekeza katika maeneo yote ya uchimbaji wa madini, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika Mkoa wetu wa Lindi tunayo madini mbalimbali lakini katika eneo hili la Wilaya ya Ruangwa tuna madini ya green gannet, green tomalin, dhahabu, safaya na graphite pamoja na madini mengine, lakini maeneo haya wachimbaji waliopo ni wachimbaji wadogo wadogo ambao wanatumia zana ambazo si bora, zana hafifu.
Ningependa kujua tunayo Sera na Sheria Mpya ya Madini ya kuwatengea maeneo wachimbaji hao wadogo wadogo, sera hii imewanufaisha vipi na Sheria mpya ya Madini wachimbaji wadogo wadogo wa maeneo hayo ya Wilaya ya Ruangwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza ningependa kumuomba Mheshimiwa Waziri, yupo tayari sasa kuja katika Mkoa wetu wa Lindi maeneo ya Ruangwa kuja kuona maeneo ya machimbo haya ya madini na kuona changamaoto mbalimbali zinazowakumba wachimbaji hao wadogo wadogo na kuona namna gani Wizara yake inaweza kuwasaidia? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sio tu nipo tayari kwenda Lindi isipokuwa nipo tayari kufuatana na Mheshimiwa Hamida twende pamoja mpaka Lindi. Kwa hiyo kwa ruhusa ya Kiti chako nipo tayari na ukitupa ruhusa hata kabla ya Bunge kumalizika nipo tayari Mheshimiwa Mbunge kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Hamida Abdallah anavyoshughulikia masuala haya, tangu ameingia katika Bunge hili tumeshashirikiana naye sana na katika juhudi zake amefanikisha kutenga maeneo mawili muhimu sana katika Mkoa wa Lindi, eneo mojawapo ni Kitowelo pamoja na eneo la Maguja Nachingwea, kwa hiyo, Mheshimiwa hongera sana kwa kazi zako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mkoa wa Lindi una madini mengi sana, baadhi ya madini yanayopatikana katika Mkoa wa Lindi kama alivyoyataja Mheshimiwa Mbunge ni pamoja green tomaline, safaya pamoja na madini load garden, lakini kuna dhahabu, kuna chumvi kuna madini mengi yanayoitwa ruby ambayo ni madini ya mfano sana katika nchi yetu. Kwa mkoa wa Lindi una utajiri wa madini mengi tu pamoja na chumvi. Nichukue nafasi hii kuwahamsisha sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Lindi na maeneo mengine ili kuhamasishe wachimbaji wadogo wakachimbe madini hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera na sheria kweli kabisa zinataja kuwatengea maeneo wananchi nchi nzima. Katika Mkoa wa Lindi tumeshatenga maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga eneo la hekta 300 Kilwa Masoko kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya chumvi, tumetenga maeneo ya hekta 525 eneo la Kitowelo katika Wilaya ya Liwale na eneo la kilometa 7.2 katika eneo la Maguja Wilaya ya Nachingwea na tunakwenda sasa kutenga eneo lingine la hekta 825 katika eneo linaitwa Hoteli Tatu. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge tunaendelea kutenga maeneo kama na sera ya madini inavyoelekeza.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya yenye kuleta matumaini kwa wavuvi wetu, lakini yametuelekeza namna ambavyo Serikali inaendelea kulinda mazingira ya bahari na kuendelea kulinda viumbe vilivyopo ndani ya bahari na kuendelea kuleta tija kwa wavuvi wetu. Sasa napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ya Lindi Manispaa, Lindi Vijijini maeneo ya Kilwa, vijana sasa wameamua kujitengenezea ajira kupitia shughuli za uvuvi na tayari wamejiunga katika vikundi mbalimbali. Napenda kujua ni lini sasa Serikali itakuja kuwawezesha angalau kuwapa fiber boat na injini za boti ili vijana wale waendelee kuwa na uvuvi wa tija na kuongeza vipato vyao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, napenda sasa Serikali ituambie italeta lini mwongozo ambao utatuelekeza ni nyavu zipi zitatumika katika maziwa, mito na bahari. Unaposema kutumia nyavu ya nchi mbili, samaki wa baharini ni tofauti na samaki hao wa maziwa. Kwa mfano baharini kuna chuchungi…
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna dagaa, lakini unaposema tutumie nyavu ya nchi mbili maana yake samaki wale huwezi kuwapata. Napenda Serikali iseme ni lini itatuletea mwongozo wa namna nyavu zitakavyotumika zile za bahari, maziwa pamoja na mito?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza sana kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa masuala yanayohusua wananchi na hasa wavuvi wa kule Lindi. Anauliza lini Serikali itawawezesha vijana, nataka nimhakikishie tu kwamba Serikali iko tayari, tunapokea maombi hasa yanayohusu vifaa kwa maana ya injini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari wiki iliyopita tumeshapokea maombi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge wa Lindi anayeitwa Mheshimiwa Hamidu Bobali akiomba mashine kwa vikundi viwili. Kwa hivyo, nafahamu Mheshimiwa Hamida ni Mbunge makini na yeye namkaribisha ofisini kutuletea hayo maombi na mashine zipo kwa ajili ya kuweza kuwasaidia vijana na vikundi vya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni lini Serikali itaweka mwongozo wa matumizi ya nyavu katika maeneo mbalimbali. Tunafikiria mwaka huu kuleta maboresho ya sheria lakini kwa maelezo zaidi na kwa uelewa mpana zaidi wa sekta hii ya uvuvi Wizara yetu imeandaa semina kwa Wabunge wote ambayo itakwenda kujibu masuala yanayohusu tasnia nzima ya uvuvi siku ya Jumapili na tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge muweze kushiriki kikamilifu katika semina hii. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru kwa majibu hayo ambayo yamejibiwa sasa hivi lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Madiwani wanafanya kazi sawa na Wabunge. Kwa nini Serikali isiwalipe mishahara kama ambavyo Wabunge wanapewa mishahara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kwa nini Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, sasa hivi Serikali haijaona umuhimu wa kuwalipa posho ambayo wanastahili kupata maana wanalipwa posho ndogo sana. Serikali ingeona umuhimu kwa sababu wao wanasimamia kazi za miradi ya maendeleo katika mitaa. Kwa hiyo, ningeomba sasa Serikali ifanye maamuzi ya kuwaongezea posho ili waweze kukidhi mahitaji yao. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) : Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza, ni kweli kwamba Madiwani wamekuwa na mtazamo huo wa kuomba kwamba kuwe na malipo hayo ya mshahara, Serikali iliyapokea na hata wakati Rais alivyohudhuria kikao cha ALAT mwaka jana alipokea maombi yao. Mimi nasema tu kwamba majibu yaliyotolewa pale ndiyo sahihi na hadi hapo Serikali itakapotoa maelekezo mengine lakini kwa sasa hivi tutaendelea na utaratibu ambao tunao.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusu Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Vitongoji na Mitaa kwamba posho ni ndogo sana, msisitizo ambao tunautoa sisi kila Halmashauri ifanye mapitio (review) ya vyanzo vyake vya ndani pamoja na mbinu zao za makusanyo, wakusanye kiwango cha kutosha cha mapato ya ndani na wahakikishe kwanza, hata hiyo ndogo maana maeneo mengine mengi tuna malalamiko kwamba hawalipi, hata hiyo ndogo basi inalipwa baada ya hapo sasa ndiyo tutaona tunaendaje huko mbele. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, alifanya ziara Mkoa wetu wa Lindi kuja kumaliza mgogoro wa mpaka wa Kikulyungu Wilaya ya Liwale lakini na mpaka wa Selous na Wilaya ya Kilwa. Kwa bahati mbaya sana kwa dharura iliyojitokeza Mheshimiwa Naibu Waziri alishindwa kukamilisha ile kazi. Sasa ningependa kujua ni lini Serikali itakuja sasa kumaliza ule mgogoro ili wananchi wa Kikulyungu na wananchi wa Wilaya ya Kilwa waendelee kufanya shughuli zao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya kujibu naomba niseme kweli kwamba nilikuwa nimeenda kwenye lile eneo hasa katika Wilaya ya Liwale kwa ajili ya kushughulikia ule mgogoro ambao upo katika Kijiji cha Kikulyungu. Bahati mbaya siku ile wakati tunajipanga kuelekea kule ndiyo siku ambapo Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alipata ajali kwa hiyo nikalazimika kuahirisha ile safari ndiyo maana sikuweza kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Maafisa mbalimbali wa kutoka Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili walienda katika eneo husika walikaa na wananchi wakatoa elimu na wananchi wakawapokea na wakawa sasa kwamba wako tayari sasa kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kubaini mpaka uliopo na kuondoa huo mgogoro ambao umedumu kwa miaka mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kusema kwamba, sasa tuko tayari wakati wowote tena tutarudi kuhakikisha kwamba sasa tunashirikiana na wananchi katika kuonesha mipaka ya eneo hilo husika na Mheshimiwa Mbunge utashirikishwa kikamilifu katika hilo suala.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri katika Bunge lililopita aliniahidi kuja Lindi kutembelea maeneo haya na kwa kweli alikuja na aliambatana na viongozi wa Mkoa na Wilaya katika kutembelea na kujionea maeneo haya ya mgogoro wa ardhi. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, mwaka 1974 mpaka huu ulikuwa Mto Matandu lakini mwaka 2010 katika marejeo ya mpaka, mpaka huu ulikuwa katika Bwawa la Kihurumila, Kijiji cha Kikulyungu. Napenda kujua ni kwa nini Serikali iliamua kuhamisha mpaka huu kutoka katika Mto Matandu na ukafika katika Bwawa hili la Kihurumila?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili napenda kujua sasa baada ya ziara yake na kujionea mwenyewe, nini sasa Serikali itafanya katika kumaliza mgogoro huu wa mipaka kati ya Serikali kupitia Selous na Serikali ya Wilaya ya Kilwa lakini na mpaka wa Wilaya ya Liwale na Selous?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Wabunge wote kwa maombi makubwa ambayo mmekuwa mkiyatoa kwa sababu siku ambapo tulikuwa tutatue hili tatizo ndiyo siku ambayo Mheshimiwa Waziri alipata ajali na hivyo ikalazimika kwamba tukatishe ile ziara na tuende kumhudumia Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Mheshimiwa Waziri jana ametolewa hospitalini na sasa yupo nyumbani, kwa hiyo, tunawashukuru sana kwa maombi yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, kweli kwa muda mrefu amekuwa akilifuatilia tatizo hili na sisi kama Serikali ndiyo maana tuliamua kwamba hili tatizo sasa lifike mahali lifikie mwisho. Naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, si kweli kwamba Serikali ilisogeza mpaka ilitokana tu na tafsiri. Tafsiri ya mpaka iliyoandikwa kwenye GN ya mwaka 1974 ndiyo wataalam walipotafsiri wakaona mpaka unapita wapi. Hata hivyo mwaka 2010 wananchi hawakuridhika ndiyo maana tukaamua kwamba kwa sasa hivi tufanye tena upya kwa kutumia wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kutokana na hiyo ziara na maagizo ambayo tulikuwa tumeshayatoa tumeamua kwamba Kamati rasmi kutoka Wizara ya Ardhi iko tayari inapitia mpaka wa Ruangwa na Kilwa ili kurekebisha ile mipaka na baada ya hapo tarehe 18 Septemba wataenda katika Kijiji cha Kikulyungu ambapo wataangalia mpaka wa Kijiji cha Kikulyungu pamoja na mpaka wa Selous. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba baada ya hapo tatizo hili litakuwa limekwisha kwa sababu wananchi wameahidi kushirikiana vizuri kabisa na hiyo Kamati. Naomba tu ushirikiano na Mheshimiwa Mbunge awe na subira.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu haya ambayo ameyatoa japokuwa hayaoneshi dhamira ya dhati ya kutaka kumaliza mgogoro huo. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu sana, lakini kwa majibu ya Serikali hayakuonesha hapa ni lini watakutana na viongozi wa Mkoa ili kumaliza huu mgogoro. Kwa sababu umesema tu watakaa lakini haisemi ni lini. Kwa sababu huu mgogoro ni wa muda mrefu kwa hiyo, ningeomba Serikali ituambie ni lini watadhamiria kumaliza huu mgogoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, kuna mgogoro pia kwenye Serikali ya Wilaya ya Kilwa na Wizara kuhusiana na mpaka huu wa Selous. Kwa hiyo, nayo Mheshimiwa Waziri ningependa aniambie ni lini mgogoro huu watamaliza ili kuepukana na vurugu ambazo zinaweza zikatokea katika kugombania mipaka hii katika maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hi kumpongeza sana kwa sababu amekuwa ni mdau mzuri sana wa mambo ya utalii katika eneo la kusini, kwa kweli tutaendelea kushirikiana naye. Sasa kuhusu lini tutakutana naomba nimhakikishie tu kwamba kati ya mwezi wa saba na wa tisa kabla ya Bunge la mwezi tisa tutafanya jitihada za kuhakikisha kwamba tunakutana na viongozi wa Lindi na tutashughulikia migogoro yote inayohusiana na hilo Pori la Akiba la Selous.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu haya ya Serikali. Swali la kwanza, maeneo haya ni yale ambayo walikaa wakoloni wa mataifa haya makubwa ambayo leo hii wanasaidia. Je, Serikali imesaidia kwa namna gani katika kuendeleza miundombinu ya Kilwa Kisiwani na Msongo Mnara ili kuendeleza utalii wa maeneo haya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili la nyongeza, napenda kujua Serikali inasaidiaje katika kuhakikisha Kilwa Kisiwani na Msongo Mnara tunaendeleza utalii, maana hali ya kule ni mbaya sana, miundombinu ni mibovu, watalii sasa wanapungua kwa sababu hakuna hoteli, hakuna vifaa vya kuwawezesha watalii kuvuka kwenda Kilwa Kisiwani na Kilwa Msongo kuona haya magofu ya ukoloni? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Hamida Abdallah, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kutambua mchango wake ambao amekuwa akiutoa katika hii sekta ya utalii kule Lindi. Kwa kweli amekuwa akifanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika lile eneo mimi mwenyewe nimefika Machi na nimeona jinsi miundombinu ambavyo iko kwenye hali mbaya. Hiyo inasababisha watalii wengi washindwe kufika katika lile eneo. Hivi sasa tumeandaa mkakati maalum kwa ajili ya kuboresha ile miundombinu katika vile Visiwa vya Kilwa pamoja na Songo Mnara ili kuhakikisha ile miundombinu inapitika wakati wowote; iwe ni kipindi cha masika au kipindi cha kiangazi, kusudi watalii waweze kufika.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya changamoto kubwa ambayo iko pale ni pamoja na kutafuta boti ya kisasa itakayokuwa inawavusha watalii kuwapeleka kule katika Kisiwa. Sasa hili tunashirikiana na Wizara ya Uchukuzi ili tuone namna ambavyo tunaweza tukapata boti nzuri ya kuweza kusaidia katika shughuli hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu namna ya kuimarisha utalii katika eneo lile, mpango mkubwa ambao tunao kama Wizara ni pamoja na kuunganisha na Pori la Akiba la Selous. Tunataka iwe ni circuit moja, watalii wanapokwenda kutembelea Selous katika upande ule, basi tuunganishe na hii circuit ya Kilwa Kisiwani pamoja na Songo Mnara kusudi vyote kwa pamoja iwe package moja. Hiyo tunaamini itasaidia sana katika kuimarisha utalii katika lile eneo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini napenda kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kimekuwa ni chanzo kizuri cha mapato katika maeneo ya majiji, manispaa na maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, kumekuwa na kero kubwa sana kwa sababu ya kutosimamiwa vizuri kwa sheria hii. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri amewatangazia Wakurugenzi wa Halmashauri pia wangepelekewa maagizo haya kwa maandishi ili sheria hii iweze kusimamiwa na kupunguza kero ambayo ipo sasa hivi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nijibu na nipokee ushauri wa kutoka kwa Mheshimiwa Hamida na nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo yake anasema kwamba chanzo hiki pamoja na kwamba ni cha uhakika lakini kimekuwa kero na mimi naomba niungane naye. Katika maeneo mengi unakuta kwamba mtumiaji anapo-park inakuwa kama ni suala la kuviziana, kwamba je, huyu atakosea ili adhabu iweze kutolewa. Naomba niwaagize Wakurugenzi wote kusimamia sheria hii lakini pia alama za parking ziwe ni zile ambazo zinaonekana kwa kila mtu ambaye anatumia gari ili anapo-park isije ikaonekana kwamba ni wrong parking.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu ambayo ameyatoa lakini sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru wafadhili ambao walijitokeza katika kuja kuendeleza Mji wa Kilwa kwa shughuli mbalimbali ambazo zimetolewa. Hata hivyo urithi wa sasa upo mbioni kutoweka kwa sababu yale yaliyofanyika kama Wizara imeshindwa kuyasimamia katika kuendeleza utalii Kilwa. Kuna shida ya miundombinu ya kutoka Kilwa Mjini kwenda Kilwa Kisiwani,kwa maana ya usafiri wa boti; kumekuwa na boti ile ya kizamani ambayo haina usalama zaidi. Ningependa Serikali sasa kuweka miundombinu sawa ili kuufanya Mji wa Kilwa uweze kuendelea katika upande huo wa utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Kilwa bado kuna maeneo ya Kilwa Kivinje kuna magofu pale ambayo waliishi wakoloni lakini bado hayajaendelezwa kwa ajili ya utalii katika Mji wa Kilwa. Sasa ningeomba kuiuliza Serikali wanatumia njia gani kutangaza kwanza utalii Kilwa lakini ni kwa namna gani wizara hii sasa itakuja Kilwa kuona magofu ambayo wameshindwa kuyaendeleza kwa muda mrefu ili kufanya utalii wa Kilwa kuendelea. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza kwa nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah kwa juhudi kubwa ambayo amekuwa akiifanya kuulizia namna gani wizara inaendeleza utalii katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ujumla na amekuwa akitusumbua sana ofisini ili kuweza kufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba eneo hili miundombinu imekuwa ni mibaya kutokana na eneo hili kushindwa kujiendesha kutokana na mapato madogo ambayo yamekuwa yakipatikana kutokana na watalii wachache wanaokwenda maeneo hayo. Kwa hiyo, wizara katika kulitafutia ufumbuzi suala hili, imeyagawa maeneo yote ya malikale ambayo yametambuliwa ambayo ni maeneo 18 kwa taasisi zake nne. Eneo hili la Kilwa tumewapa TAWA; TAWA watachukua eneo hili wataliingiza katika packageyao ya utalii na kwa sababu hiyo watalazimika kulikarabati na kutengeneza miundombinu ili liweze kutumika vizuri na watu waweze kupata huduma zote ambazo Mheshimiwa Mbunge amesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kweli kwamba pamekuwa na tatizo la watalii wachache katika maeneo haya na sababu kubwa ni kwamba maeneo haya yamekuwa hayatangazwi. Sasa ili kukabiliana na suala hili, tumeyaingiza mambo haya yote kwenye taasisi na TAWA watakapokuwa wamechukua rasmi watayaingiza katika package zao za utalii ambazo zitakuwa pia zinajumuisha mbuga za wanyama na kwa hali hiyo suala hili la kuongeza mapato na kuongeza usimamizi wa vituo hivi utakuwa umelipa. Naomba nikushukuru.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini ningependa kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni kiongozi wa kwanza wa ngazi ya Mtaa, lakini ukiangalia kazi kubwa anayoifanya katika kusimamia majukumu mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwanganisha wananchi kwenye Mtaa wake pamoja na kusimamia ulinzi na usalama kwenye Mtaa wake, kiwango cha posho wanazopewa na Halmashauri ni kidogo…

SPIKA: Sasa swali.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, napenda kujua, ni lini sasa Serikali itaongeza kiwango hiki cha posho wanayopata ya shilingi 10,000/= kulingana na kazi ambayo wanaifanya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza, napenda kujua kwamba Waheshimiwa Madiwani sasa wanadhaminiwa kukopeshwa mikopo kutoka kwenye vyombo vya fedha: Ni lini sasa Serikali itasimamia kuhakikisha kwamba Wenyeviti nao wanakopeshwa katika vyombo vya fedha? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anazungumzia kiwango cha posho kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Kama ambavyo nimejibu kwenye swali langu la msingi ni kwamba ni kweli kwamba Wenyeviti hawa wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa wanafanya kazi kubwa na Serikali inawadhamini.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, mapato ambayo wanapewa ya asilimia 20 ni makusanyo katika Halmashauri husika. Hivi viwango vya shilingi 10,000/=, shilingi 20,000/=, shilingi 50,000/= mpaka shilingi 100,000/= vinategemeana pia na uwezo wa Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote, kadri tunavyokuwa tunabuni vyanzo mbalimbali kwenye Halmashauri zetu, zikipata uwezo mkubwa Wenyeviti hawa watapata posho kulingana na mapato ya ndani kulingana na Sura ya 290 ya fedha za Serikali za Mitaa kama nilivyotaja.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anauliza ni lini Wenyeviti wataanza kupata mikopo? Yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge amesema hiki kiwango ni kidogo na wakati mwingine ni kweli kwamba Wenyeviti wa Mitaa wanaendelea kudai. Kwa hiyo, namna ya kurejesha ukikopeshwa fedha benki inakuwa na ugumu wake, inaonekana mapato pia hayana uhakika. Halmashauri wanaweza wakapata kiasi kidogo, wakapata kidogo. Wakati mwingine kulingana na msimu wakapata fedha nyingi, wakapata nyingi kidogo. Sasa mabenki yatakuwa ni ngumu sana kuweza kuwawezesha.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuja na mpango wa kuwezesha Halmashauri kuwa na miradi ya kimkakati, Halmashauri ikiwa na uwezo mkubwa wa kutosha kuanzisha kama masoko, stendi na vitu vingine vile vikubwa itawawezesha Halmashauri kuwa na uwezo, kuwa na kipato cha uhakika na Wenyeviti wetu watakopeshwa na watasimamiwa na Halmashauri na Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yao ya kazi. Ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimshukuru Waziri kwa majibu ya Serikali ambayo ameyatoa, lakini naiomba Serikali kwamba MV Kitunda ni kivuko ambacho kinawasaidia sana wananchi wa Lindi kuvusha magari na bidhaa mbalimbali na shughuli za kiuchumi zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninavyoongea kivuko kimesimama kwa muda wa wiki moja changamoto iliyopo injini Na.2 kwenye selecta valve kuna shida. Naiomba Serikali kusaidia kwa haraka kupatikana kwa valve hii ili kivuko kiendelee kufanya kazi na wananchi waendelee kutumia kivuko hicho.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua umuhimu wa kivuko hiki cha MV Kitunda na kutokana na umuhimu wake tayari Wizara kupitia TEMESA imeshapeleka boti na hata hivi kutokana kwa kweli na ufuatiliaji wa karibu sana wa Mheshimiwa Hamida, Mbunge wa Lindi Mjini, tumepeleka boti kwa ajili ya kusaidia changamoto ambazo zinajitokeza.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba, kama tulivyoahidi kivuko hiki kitatengenezwa, lakini wakati kiko matengenezo boti hilo litaendelea kubaki hapo kwa ajili ya kusaidiana na boti la Halmashauri ya Lindi ili kuhakikisha kwamba eneo hilo halisimami kufanya kazi kati ya Lindi na Kitunda. Ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, kwa kutuwezesha fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mapenzi yake mema, lakini naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Lindi Mjini tuna kata 20 lakini kata 13 ziko katikati ya Mji, lakini ukiangalia wananchi wale, katika kata 13 zaidi ya watu 70,000 wanakosa mahali pa kukimbilia kwa maana ya kituo cha afya. Sasa ninaomba kuiuliza Serikali watatusaidiaje kuhakikisha kwamba tunapata Kituo cha Afya Lindi Mjini kuwasaidia wakazi wa kata 13 waishio Lindi Mjini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili katika Kata ya Kitumbikwela upande wa pili wa bahari pana kituo cha afya lakini bado hakijakamilika, wanawake wanapata changamoto wakati wa kujifungua na wanapolazimika kufanyiwa upasuaji, kivuko wakati mwingine kinakuwa kina changamoto.

Kwa hiyo, ninaomba kuiuliza Serikali ni lini wataweza kutusaidia kuboresha Kituo cha Afya cha Kitumbikwela ili wanawake wajawazito waweze kuhudumiwa pale? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Hamida Mohamed kwa kuwasemea kwa dhati kabisa wananchi wa Lindi Mjini na mimi nimhakikishie kwamba Serikali hii sikivu ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan tutaendelea kushirikiana naye na kuhakikisha kwamba wananchi wa Lindi wanapata maendeleo ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vituo vya afya katika Jimbo la Lindi Mjini; ni kweli kwamba wana vituo vya afya vichache. Lakini Serikali tumeshatoa fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Mnazimmoja, lakini tumepeleka fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya kisasa ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bado tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga vituo vya afya katika kata za kimkakati ambazo hazina vituo vya afya.

Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba Serikali inafahamu changamoto hiyo na mipango inaandaliwa kuhakikisha Manispaa ya Lindi tunapata vituo vya afya.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Kitumbikwela ni kweli Kata ya Kitumbikwela ipo upande wa pili wa bahari na njia kuu ya kuvuka pale ni kwa kutumia mapantoni lakini pia na boti. Kwa hiyo, kwa kweli tunahitaji kuboresha kituo kile cha afya ndio maana tulianza ujenzi kwa awamu ya kwanza, sasa tutakwenda kujenga miundombinu iliyobakia zikiwemo wodi na majengo mengine kwa awamu ya pili ili kuhakikisha huduma zinakwenda vizuri. Ahsante. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo ya Serikali, majibu ambayo sasa yanaleta matumaini kwa maana mradi huu umekuwa wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina swali la nyongeza, lakini nina maombi kwa Serikali. Mheshimiwa Waziri Innocent Bashungwa alikuja Lindi tarehe 29 Julai, kwenye Maadhimisho ya Sherehe ya Kumpongeza Mheshimiwa Rais. Katika mambo ambayo tulimwomba ni suala zima la utekelezaji wa mradi huu wa TACTIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Lindi tuna mapokeo ya mradi wa LNG, tunahitaji sasa kuboresha miundombinu mbalimbali. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba wanatuharakishia huo mwezi Januari ambao wameuahidi katika utekelezaji wa mradi huu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa kujibu kwa ufasaha, pia na Mheshimiwa Hamida Abdallah kwa ufuatiliaji wa mradi huu ambao Waheshimiwa Wabunge kutoka miji 45 wamekuwa wakiufuatilia kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maelekezo ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwamba baada ya Serikali kusaini na benki ya dunia Juni, 16 mwaka huu 2022, Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alituelekeza kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya TACTIC unaanza mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, kwenye tier one, miji 12 kwa maana ya majiji tayari kama nilivyosema, mkataba ulisainiwa na Serikali na Benki ya Dunia Juni 16 na usanifu wa miji 12 umeshakamilika. Sasa hivi kazi ya kutangaza kwa ajili ya kupata wakandarasi itafanyika muda wowote ili kazi zianze Machi, 2023 kwa ile miji 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini tunafanya kwenye miji 15 ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema? Tunafanya kila aina ya jitihada kuhakikisha tier one na tier two zina-overlap katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Hamida Abdallah, pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwenye miji 45 msiwe na wasiwasi, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan baada ya kusaini Mkataba na Benki ya Dunia mwaka huu 2022, utekelezaji wake wa tier one, tier two na tier three viweze Kwenda kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu tuna group la TACTIC na mnafuatilia kwa karibu sana, tutakuwa tunaandaa vikao ili kuwapa mrejesho wa utekelezaji wa miradi hii utakavyokuwa unaenda. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDHALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo yenye matumaini lakini pia nishukuru Serikali kwa kutenga fedha 5.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kampasi ya Lindi. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ziara ambayo ameifanya Lindi wiki mbili zilizopita kwa kuja kukagua maeneo haya ambayo yatajengwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kampasi ya Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

(i) Kwa kuwa Kampasi hii ambayo itajengwa ya Lindi itakuwa mahususi kwa ajili ya kozi ya ufugaji wa nyuki, kilimo, uchumi na biashara, sayansi na teknolojia. Kwa nini Serikali isipanue kwa kuongeza kozi ya uvuvi pamoja na kilimo cha mwani?

(ii) Ningependa sasa kujua kwa sababu kanda nzima ya kusini tuna uhitaji mkubwa wa chuo hiki cha usafiri na usafirishaji baharini, ni lini sasa Serikali itafanya utafiti kuhakikisha kwamba tunapata ujenzi wa chuo hiki cha usafiri na usafirishaji kwa ajili ya kuongeza ajira kwa vijana lakini kuendelea kukuza uchumi na kuwekeza wataalam kama rasilimali watu katika nchi yetu ili waendelee kukuza uchumi kupitia bahari yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu wa suala hili. Amekuwa akifika Ofisini kwetu mara kwa mara na alikuwa akiliulizia mara kwa mara lakini sasa mwarobaini au majawabu ya suala lake hili linakwenda kufikia ukingoni. Kwa hiyo, nikushukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji huo wa karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba Serikali inakwenda kujenga Kampasi hii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mkoa huo wa Lindi na tutaanza na kozi hizo na tathmini tutafanya iwapo kama tutaona uhitaji wa kuanzia hizi kozi za uvuvi pamoja na Kilimo cha Mwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Mbunge nikutoe wasi wasi baada ya kufanya market survey na need assessment na kujiridhisha kozi hizo zitakapoanzishwa zitapata wanafunzi basi tutakwenda kuzianzisha kozi hizo kwa kadri ya mahitaji yatakavyookuwa yanaruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili kuhusiana na uanzishwaji wa chuo cha usafiri, nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge kwa vile tunaenda kuanza ujenzi wa chuo hiki katika kampasi hii. Ni utaratibu wa vyuo vyote duniani, tutafanya tathmini ya kuanzisha kwanza kozi za usafirishaji katika chuo hiki au katika Kampasi hii. Badaaye katika upanuzi iwapo kama tutaona uhitaji tunaweza sasa kwenda kuanza majengo au chuo kingine katika maeneo ambayo yatakuwa yanapatikana. Ndiyo utaratatibu wa vyuo vyote duniani hata uanzishaji wa Chuo Kikuu cha Muhimbili ulianzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ardhi kilianzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata hiki baada ya kuanzisha na kuona kwamba uhitaji unazidi kupanuka tutaweza kufika katika maeneo hayo Mheshimiwa Mbunge anapendekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu ya Serikali ambayo yameonesha matumaini sasa ya kuanza mchakato wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri na Usafirishaji pale Kikwetu.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi tumetoa Hekari 125 bure kwa Ndugu zetu hawa wa NIT, lakini hekari 150 kwa Ndugu zetu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Kilimo pale Lindi Mjini, sasa ni miaka mitatu, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Je, ni lini sasa Serikali itawawezesha ndugu zetu wa NIT kuwapatia fedha kwa ajili ya kuharakisha ujenzi wa chuo hiki cha Usafiri na Usafirishaji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili tunategemea kwamba chuo cha Kilimo Kampasi ya Lindi tungependa sasa kuongeza Kitivo cha Uvuvi na masuala ya kilimo cha Mwani kutoa fursa ya ajira kwa vijana na wananchi wa maeneo hayo ya Lindi na Mtwara. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamida Abdallah Mbunge wa Lindi Mjini. Mbunge huyu ni katika Wabunge wafuatiliaji sana wa masuala ya Wavuvi

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni hili la lini watapewa fedha NIT. Nafikiri ni wakati mzuri ameuliza swali hili kwa sababu ni kipindi ambapo Serikali tupo katika kuwasilisha bajeti hapa Bungeni na kwa hivyo chuo cha NIT ni chuo cha Serikali na kipo katika hodhi ya Wizara zetu na hili litajibiwa wakati Wizara husika itakapokuwa ina wasilisha bajeti yake hapa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni juu ya jambo la Kitivo ha Kilimo kuhusianisha na course za mifugo na uvuvi. Wazo na fikra aliyoitoa Mheshimiwa Hamida ni nzuri na mimi naomba niichukue kwa niaba ya Serikali ya Serikali na kwa hivyo basi tutaipeleka kwa wenzetu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama ilivyo desturi waweze kuunganisha fani hizi nazo ziweze kutolewa pale pindi chuo kitakapokuwa tayari. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu hayo yenye kuleta matumaini. Pamoja na kwamba wamechukua hatua mbalimbali za upimaji wa eneo na kuchukua tathmini ya hati ya mazingira, ninaomba niulize swali moja la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Lindi Manispaa limejengwa mwaka 1950, kwa hiyo ni soko ambalo tumerithi kutoka kwa wakoloni, ni la muda mrefu tangu Lindi ikiwa eneo dogo na sasa hivi Lindi Manispaa ina kata 31 na makusanyo ya manispaa ni shilingi bilioni tatu kwa mwaka. Makusanyo ni madogo lakini tunatoa huduma katika kata 31.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lini Serikali itaona umuhimu mkubwa wa kutupatia fedha katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kutekeleza mradi huu wa kimkakati wa ujenzi wa soko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua shauku ya Mheshimiwa Mbunge juu ya soko hili, na amekuwa akilipambania tangu akiwa Mbunge wa Viti Maalum na mpaka sasa ni Mbunge wa Jimbo. Na ukweli ni kwamba Manispaa ya Lindi ipo katika Tier II katika miradi ambayo inaanza kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2023/24, kwa hiyo nimuondoe shaka tu na wananchi wake kwamba utekelezaji wao utafanyika kama ambavyo watu wa Tier I sasa hivi wako katika hatua za mwisho, ahsante sana.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu hayo ya Serikali yenye kuleta matumaini kwa wananchi wa Lindi Manispaa. Hata hivyo, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Lindi Manispaa tumeshatenga ekari moja na nusu kwa ajili ya ujenzi wa soko hili la samaki, vilevile tuna wavuvi 2,193 ambao wamesajiliwa na wachuuzi wadogo wadogo 470 ambao wanakosa mahali pa kufanyia shughuli zao za biashara. Naomba Serikali itupe majibu ya uhakika na ya kueleweka ya kuwapa wananchi wa Lindi Manispaa matumaini; ni lini sasa mtaanza kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa soko la Samaki?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake kwa wavuvi kwa kuwakopesha maboti, pamoja na nyavu na injini ili wavuvi hawa sasa waendeleze uvuvi wao kwa vifaa hivi vyenye uhakika na usalama wa kutosha? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza swali lake la nyongeza kuwa tayari Halmashauri ya Manispaa ya Lindi tayari wameshakupata eneo, namwomba baada ya Bunge hili twende na wataalamu pale Lindi tukahakiki hilo eneo na wataalamu na tukishajua eneo hilo lililopatikana lina ukubwa gani na linafaa kwa matumizi hayo, Wizara iko tayari kuanza ujenzi wa soko hilo mara moja.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza kuhusu zana. Tathmini tayari imeshafanyika, wataalamu wameshafanya tathmini ya zana gani zinafaa kwa maeneo hayo ya wavuvi, namwomba baada ya hili, kwa sababu tayari kila kitu kimeshafanyika, basi baada ya Bunge hili tuambatane naye kama nilivyosema hapo awali, twende kwa wavuvi hao kuhakiki ni aina gani ya zana zinazohitajika ili Serikakli ione namna ya kuanza kuwakopesha wavuvi hao hizo zana, ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nishukuru kwa majibu ya Serikali, lakini ningependa kujua katika eneo la Ngongo, sisi Manispaa tulishatoa hekari 120; nini msukumo wa Serikali kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana na kuwawezesha Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuja kujenga Chuo cha Kilimo campus ya Lindi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdalaah Mbunge wa Lindi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukuwa fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge amekuwa akilifuatilia sana jambo hili na hii si mara ya kwanza kuliulizia. Sisi kama Wizara ya Kilimo tumefanya mawasiliano na wenzetu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia jambo hili limeshaanza na ndani ya muda mfupi ujao wataendelea na taratibu za kuhakikisha kwamba mchakato huu unakamilika, ili ujenzi uanze mara moja.

Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Serikali inafanya kazi kwa pamoja na wenzetu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam wako tayari kuendelea na mchakato huu na hatua zimefikia sehemu nzuri.