Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Fakharia Shomar Khamis (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sina budi kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka amani na utulivu kwa muda wa miaka 52 hivi sasa Tanzania ipo katika utulivu. Lazima nitoe shukrani kwa Serikali zote mbili kuweza kukaa kwa utulivu na amani na Muungano utaendelea kudumu tena wa Serikali mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kutoa shukrani za pekee kwa Jemadari Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza kuweka amani na utulivu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na tukaweza kurejea uchaguzi kwa amani na utulivu na Wazanzibari chaguo lao likawa CCM wakamchagua Mheshimiwa Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar.
Nawaambia Wazanzibari hongereni kwa uchaguzi wenu, haya maneno ya kutupatupa yasiwashtue humu ndani ya Bunge, dua la kuku halimpati mwewe, sasa wanaokaa wakaapiza, wakasema hovyo, wakajilabu hovyo ni sawa na kujishusha tu, lakini hakuna kitakachokuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwaka 2000 wakati wa Mheshimiwa Salmini walikuwa wanawadanganya wenzi wao hawa uchaguzi utarejewa! Uchaguzi utarejewa! Iko wapi? Tukawaambia hapa Katiba inasema mpaka mwaka 2005, hayakuwa, yamekuwa mwaka 2005! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kazi kuwatia wenzenu drip mkawachoma asubuhi na jioni, wameshachoka kudanganywa! Anasimama mtu anajinasibu eti tutapeleka Mahakamani, hamkwenda Mahakamani hapo mwanzo Mheshimiwa Shein hajakamata nchi, leo mtakwenda Mahakamani nchi imeshakamatwa, siyo mnajidanganya tu? Huko ni kujidanganya, msidanganye wenzenu uchaguzi hapa mpaka mwaka 2020 kama ulivyokuwa nyuma 2000 mpaka 2005 na hii ni mwaka 2015 mpaka na mwaka 2020. Hayo mnayozungumza kama mtakwenda Mahakamani mtakwenda wapi, hiyo danganya toto, ukweli ndiyo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia masuala ya Muungano lakini lazima hawa wenzangu watani wangu niwaambie ukweli waulewe, wasidanganye wenzi wao! Uchaguzi mwaka 2015, msijisumbue tutakwenda Mahakamani! Mwaka huu mtakiona! Kitakuwa nini! Tukione nini na kuna Katiba! Kuna Katiba inazungumza na Jemadari Mkuu namshukuru, Zanzibar imetulia, ndiyo maana mnatuona tuko hapa tunapendeza! Walioweka makoti, walioweka vitenge tumekaa hapa, hakuna anayekwambia anataka kuondoka, miezi mitatu mtatuona humu tunamangamanga na shughuli zetu za Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 51, Kifungu cha 92, Gawio. Nakubaliana na maelezo yote aliyosema Mheshimiwa Waziri, sina matatizo nayo na ile aliyosema 9.9 billion ya gawio sina matatizo nayo, lakini nina ushauri kwamba 4.5 imekaa muda mrefu naona wangekaa tena Serikali hizi mbili wakakokotoa kwamba, hii 4.5 itakwenda mpaka lini? Au ndiyo makubaliano ya Serikali mbili, au ndiyo maamuzi? Naomba hili waliangalie kisha watutolee uamuzi, maana hakuna mtu anayekataa nyongeza na nyongeza huwa inakwenda kwenye fungu! Sasa na hili kama mtalikokotoa mkaliangalia na mkaona hakuna uwezekano wa kutuongezea itakuwa maa-salam, Muungano unazidi kudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira ya Muungano, ajira ya Muungano kwa maelezo yaliyoelezwa nayakubali sina matatizo. Mgawanyo wa ajira ulivyo sina matatizo, lakini tatizo langu kwa nini Zanzibar hamuweki ofisi ikawa inashughulikia ajira za Muungano? Kama tatizo lilikuwa ni jengo au ofisi, Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar ni kubwa na ofisi zipo! Mlituahidi mwaka jana kwamba mtachukua ofisi pale! Je, nini tatizo? Kumetokea nini? Au kuna jambo gani hata hadi leo jengo lipo, ofisi haijafunguliwa pale Zanzibar? Mnawafanya akina kaka na akina dada asubuhi kaenda Bara, jioni karudi kufanya interview na siku nyingine asifanikiwe na hela yake imekwenda! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais, Zanzibar. Jengo ni zuri lakini linahitaji ukarabati. Ukarabati tulikubaliana mwaka jana, Kamati ya Katiba na Sheria ilivyokwenda iliuona uozo uliokuwepo pale mkasema kwamba, tayari mtalitengeneza. Nimefuatilia halijatengenezwa, mlikwenda mkaligusagusa, lakini mmeliacha liko vile vile na usipoziba ufa utajenga ukuta! Sasa ningewaomba hii kazi na tunataka Makamu wetu wa Rais akae mahali pazuri penye usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pale tulikubaliana kwamba sehemu ya nyuma ambapo kuna jengo refu, tukasema Serikali mbili zikae zizungumze ili lile jengo lipate kuondoka au lichukuliwe au mtakavyoamua, lakini tusimpe tabu yule mwenye jengo.
Kutokana na jengo kuweko pale refu, usalama wa Ofisi ya Makamu, usalama wa nyumba anayokaa Makamu haupo, kwa sababu jengo refu, yule akikaa juu anaona wote mle ndani! Sasa usalama uko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hamjatuambia kwenye hiki kitabu mmefikia hatua gani? Kama kweli hii kazi mliifanya na vikao vilikaa, lazima mngeleta mrejesho! Ningeomba na hili kujua kipi kinachoendelea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na njia ya dharura ambayo kuna njia main road ya kuingilia ambayo ndiyo mnayotokea, lakini tukasema nyuma kuna geti lingine, kujengwe barabara ya dharura ambayo anaweza Mheshimiwa Makamu akaitumia. Tulikubaliana mkasema itakuweko njia ya dharura kwa usalama wa Mheshimiwa Makamu! Hiyo njia hadi leo haijajengwa na sitegemei kama mtaijenga kwa sababu hata kwenye hiki kitabu hamjaelezea! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nizungumzie vitu ambavyo vitaweza kudumisha Muungano. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliahirisha sherehe za Muungano siyo kwamba kaziahirisha, aliboresha maendeleo akasema zile fedha zipelekwe Mwanza kwa ajili ya maendeleo, sasa kwa ajili zile fedha zilikuwa ni za Muungano na Muungano ni wa nchi mbili, hili gawio ilibidi tulipate na sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. FAKHARIA S. KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa na imetoa mwelekeo kwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Nimezungumza kwa kusema fumbo hilo; tunalizungumzia Jeshi. Jeshi wajibu wake ni kwenda Zanzibar na kuwepo Bara. Sasa kupelekwa Jeshi Zanzibar imekuwa hoja kubwa hapa ndani, kwa nini Jeshi limekwenda Zanzibar?
Mheshimiwa Waziri ukurasa wake wa 20 alizungumza hivi, nanukuu: “Kukamatwa kwa mabomu ya kutengenezwa kwa mkono katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.” Sasa kwanini majeshi yasiende? Atakayeyategua mabomu haya ni nani kama siyo Jeshi? Sasa haya mabomu kayatengeneza nani? Wakasema ni wananchi wa Zanzibar. Sasa ikiwa ni kweli jambo hilo limefanyika Zanzibar, wa kufanya shughuli hiyo ni majeshi; wa kuangalia ulinzi huo ni majeshi na mabomu yamelipuliwa Zanzibar. Tatizo liko wapi? Anayetaka kusema na aseme tu ili afurahishe roho yake na maamuzi yake, lakini ukweli ndiyo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia kuhusu mgao wa nafasi za ajira Zanzibar. Nakubali wanajeshi wanaajiriwa Zanzibar, lakini utaratibu unaotumiwa Mheshimiwa Waziri angalieni. Mnapeleka nafasi katika Mikoa, watu wanatafutwa katika mikoa, wanaajiriwa. Kwa nini msiende JKU kama mnavyokwenda JKT? Kwanza kule mtapata vijana tayari wameshapata elimu ya jeshi, wakakamavu, wameshajua nini wanakwenda kutenda; lakini kuchukua Mkoani, hamumjui mtu yupo vipi, lakini kwa sababu vipi aajiriwe! Nafikiri hilo mliangalie tena na mlipange tena. Bora vijana wetu wakimaliza, waende JKU wapate elimu ya ukakamavu na inakuwa rahisi kwenu kujua wapo vipi, afya yake ni vipi na uwezo wake uko vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuja katika ukarabati wa ujenzi wa majengo ya jeshi Zanzibar. Kambi za Zanzibar zipo kwenye hali mbaya. Ukiangalia Mtoni, Mwanyanya, Mazizini na nyingine zote hazipo kwenye hali nzuri na sielewi toka zilipojengwa lini zimekarabatiwa. Nimeona katika kitabu chako ukurasa wa 37 umeelezea kwamba kuna nyumba kama 4,744; siyo mbaya hiyo kazi mtakayoifanya; na mmesema tayari kwa Pemba. Kama zipo nyumba 320 siyo mbaya; lakini kwa Unguja hali ndiyo mbaya. Kwa Unguja majeshi yetu pale ndiyo Zanzibar City. Sasa tunataka kama mlivyojenga nyumba 320 na Zanzibar tujue nyumba zetu mtazijenga lini? (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, malipo ya wanajeshi wastaafu yanakuwa yana matatizo; matatizo yake ni nini? Inabidi lazima mwanajeshi aende Bara kutoka Zanzibar kufuatilia. Kwani Zanzibar hamwezi kuweka kituo kukawa na kituo kama Bara? Mwanajeshi kastaafu Zanzibar, anakwenda pale anahudumiwa, anapata malipo yake Zanzibar baada ya kuondoka. Maana akifika Bara kwanza humjui mtu, wala humwelewi mtu, hujui unaanzia wapi! Wakati mwingine huyo mwanajeshi hajapata nafasi hata ya kwenda huko. Mwenyewe yupo Zanzibar tu! Sasa mnampeleka Bara akafuate kiinua mgongo, akahangaike! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, asaidie Wizara kama inaweza kujigawa na Zanzibar wakawepo wafanyakazi na wakaweza kufanya kazi hiyo vizuri na kwa wepesi bila matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kuhusu uvamizi wa ujenzi wa nyumba karibu na kambi za Zanzibar. Kambi za Zanzibar zimevamiwa, zipo katikati ya mji. Kambi hizo kwa kweli ukiangalia Mtoni, Mazizini, Mwanyanya na nyingine kadhalika, pale linalofanywa ndani ya kambi wananchi wa pale wanajua, kinachotokea wananchi wa pale wanajua na inatakiwa ndani ya kambi kuwe kuna siri. Huwezi kuyajua mambo ya kambini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine inawezekana ikatokea madhara itakuwa rahisi kwa wale wananchi kupigwa. Itabidi wananchi wanaokaa karibu na kambi wapate elimu wajue jinsi ya kujihami, maana ukishakaa kambini na wewe ni sawa sawa na mwanajeshi, litakalotokea na wewe umo. Sasa mngechukua wakati wenu mkatoa elimu kwa watu waliokuwepo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza sina budi kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, na viongozi wote wa Wizara hii, kwanza kwa hotuba nzuri waliotusomea imeifunika hotuba ya Kambi ya Upinzani, ndio maana mkawaona wamekuja na jazba kubwa mpaka mwisho mtu anakunywa maji, ili kutafuta sauti akwamue, aifunike speech ya Mheshimiwa Waziri, lakini ameshindwa na vilevile nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani wamezungumza kwamba Mheshimiwa Rais anajifungia Ikulu, anashindwa kutoka nje. Nawaambia Mheshimiwa Dkt. Magufuli ndiye Rais bora duniani na ambaye ameweza kutekeleza sera zake, kwa Watanzania na hivi sasa ana sifika Tanzania nzima na nje ya nchi kwa sababu ya uwezo wake, na hapo anapokuwepo Ikulu si kwamba anakaa anafanya kazi, anatafakari nini cha kuwafanyia Watanzania kuwaondoshea madhila, lakini mimi ninajua wenzetu ninyi kazi yenu ni kupinga tu kila kilichokuwa kizuri kazi yenu ninyi kupinga, kila kinachotendeka kikiwa kimekaa sawa imekuwa sawasawa na mke mwenza, amelisifia kaburi la mke mwenzie, hili kaburi la nani zuri limependeza, alipambwa na mke mwenzie, ndio maana nikaona limekaa upande, ndio upinzani huo, wakati ameshalisifia anakuja analiponda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mabalozi. Mabalozi wetu wanafanya kazi nzuri, hata wao wanapokwenda nchi za nje, wanahemea kwa Mabalozi. Sasa leo imekuwaje maana yake baniani mbaya kiatu chake dawa, jamani hebu tuwe makini katika masuala yetu tunapozungumza. Maana yake wakati mwingine mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, tusiwe kwa sababu kuna upinzani, ndio upinge kila kitu mengine mshukuru kwa sababu yanawafaeni na ninyi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na suala lingine, kuna siku alisimama Mbunge akazungumza kwamba Zanzibar utalii wao kama hauna uendelezo wala hauna faida nao upo upo tu. Namwambia huyo Mheshimiwa kwamba Zanzibar hivi sasa bajeti yake anatumia pesa za ndani, hategemei za nje na kinachofanya hivyo ni kwa sababu utalii unaenda vizuri, karafuu anauza vizuri na ndio maana ikaweza kujitosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utamkuta mtu anakurupuka anakuambia, Seif ndio atakuwa Rais atauweza uchumi, unajidanganya. Seif alitia mpira kwapani na Bwana Jecha alimpa uhuru mkubwa tu wa kugombea na alimuambia tarehe 20 Machi, 2016 uchaguzi kashindwa. Katia mpira kwapani, ninawaambieni msilolijua ni sawa na usiku wa kiza, tulieni Mheshimiwa Shein akamate madaraka aendelee nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa uchaguzi mwaka 2020, mwaka 2020 kama hamkuja basi tena tunaendelea, tunapiga more waliyojionea vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nitajikita katika diplomasia ya kiuchumi. Ninajua Wizara imejipanga katika kukuza diplomasia ya kiuchumi na kwenye kitabu chenu nimeona kwamba tayari mmejikita na mnakwenda vizuri. Nilikuwa nataka kusema hivi, kwa sababu Tanzania hivi sasa inataka kujikita katika viwanda, je, Wizara imejipanga vipi kutafutia masoko ya biashara ambapo kwa sababu tutakapojiingiza kwenye viwanda, lazima tuwe na masoko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namtaka Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujumuisha, uniambie masoko ya nje tumejikita vipi ili kwa bidhaa zetu tuweze kuuza. Kwa kweli Tanzania inajikita katika mambo ya utalii, kwa sababu tunavyo vitu vinavyotufanya ili tuweze kuvutia watalii wetu. Kuna Mlima Kilimanjaro, kuna fukwe za Bahari za Zanzibar, kuna bustani ndani ya Bahari ya Hindi na hiyo wanakuja wanapoenda kuangalia, vilevile tuna mbuga za wanyama. Sasa ningekuomba na haya sasa myafanyie kazi ya kuyatangaza, msiwaachie Kenya ambao wakitoka wao ndio Tanzania wakatutangazia, wakati sisi tuna uwezo na uwezo huo najua Mheshimiwa Waziri unao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia ambalo sikuliona kwenye kitabu chake, mwaka jana tulizungumza kwamba kuna vijana Wazanzibari 13 mliwasomesha, ili baadae muwaajiri katika Wizara zenu au vitengo vyenu. Lakini kwenye kitabu chako sijaona hao vijana ambao wameajiriwa au hawakuajiriwa, umetuambia kwamba kuna watu wamestaafu, kuna watu wamemaliza muda wao, lakini hujasema vijana gani ambao tayari umewaajiri kama kutoka Tanzania Bara au Tanzania Visiwani. Sasa hivyo Mheshimiwa Waziri ningependa pia ukija unijulishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuhusu kitabu chako cha mwaka jana ukurasa wa 61; mlisema Wizara mnajikita katika kuweka vitega uchumi, kufanya wafanyakazi watakaokuwa nje ya taasisi yenu ambao watakua Ubalozi kupata sehemu zao za kukaa na ofisi zao za kukaa. Lakini sijaona kwenye kitabu chako maendeleo yake yamekuwaje kama kweli, maana ulisema mpaka mtakuwa na mapato katika sehemu za vitega uchumi, kwa kupata viwanja na majengo ambayo mengine mtaweza kukodisha. Sasa na hilo ningependa utakapokuja Mheshimiwa Waziri nipate kujua maendeleo yake yakoje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki makao makuu yake yako Zanzibar. Sasa hili lazima nitoe pongezi kwamba Zanzibar ambayo mmeipa kitengo kama mlivyosema kwamba Kamisheni ya Kiswahili Makao Makuu yake yatakuwa Zanzibar, ni katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ilianzia kuanzia mwaka 2014. Sasa hili kwangu ni pongezi na ninashukuru, na tutaendelea kuilinda, na tutaendelea kuilea kama tunavyoilinda na kuilea CCM, kwa maelezo hayo naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru kwa kupata nafasi hii adhimu katika Bunge lako Tukufu ya kuweza kuchangia hoja ya PAC na LAAC kama hivi nitakavyoelezea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Kamati na CAG wote fedha za kufanyia kazi zilikuwa ndogo, lakini tumshukuru Mwenyezi Mungu kila mmoja ilibidi atekeleze wajibu wake ili suala hili liweze kufanikiwa. Ukweli ni kwamba kulikuwa na uhaba wa fedha za kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Kulikuwa na hoja hapa ilizungumzwa kuhusu ujenzi wa Kigamboni ambapo NSSF waliingia mkataba na Azimio Housing Estate. Azimio House Estate ilikuwa watoe ekari 20,000 za ujenzi huo kulingana na makubaliano ya mkataba. Kiukweli ekari walizotoa ni 300. Makubaliano yao ilikuwa kama wangetoa ekari 20,000 ilikuwa na sawasawa na 20% ya hisa na 35% ya hisa ilikuwa ni kuchangia fedha, lakini hayo hayakuweza kutendeka na ndiyo maana ujenzi wa Kigamboni ukasuasua na kusimama kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo ya Kamati aliyoeleza Mwenyekiti nakubaliana nayo kwamba kuundwe Kamati Ndogo iweze kusimamia na kufuatilia nini kilichokwamisha, nini ilikuwa tatizo hata makubaliano hayo hayakufikiwa na mradi huo ukawa haukuendelea. Taarifa hiyo baadaye iletwe Serikalini kuangaliwa na kujadiliwa hadi suala hilo liweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuongelea Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma. Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma una matatizo, baadhi ya wastaafu wetu wanahangaika, hawalipwi na kutokana na upungufu uliojitokeza katika tathmini ya kitaalam kwa muda mrefu mfuko huo umekuwa unasuasua haufanyi kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naona mfuko huu unakwamishwa na Serikali, inatakiwa Serikali ikikopa kwenye mifuko hii iweze kulipa. Serikali imechukua fedha za mfuko huu na tumefanya kazi zetu, lakini hatulipi tutegemee hawa wastaafu wetu watapata fedha wapi na wanategemea walipwe na mfuko? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa tathmini iliyofanyika inaonesha kuanzia mwaka 1999 hadi leo wazee wetu wanahangaika. Wengine hawana watoto, wengine hawajiwezi, tunategemea hawa watapata wapi matumizi yao? Ingawa wamezungumzia kwamba wanategemea Februari watamaliza tathmini yao na waweze kuwalipa, hivi kweli mtu ataweza kukaa bila kutumia, bila kula mpaka ifike Februari? Naiomba na Serikali iweze kulipa madeni ya mashirika yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala lingine la Bandari. Udhibiti wa mapato ya bandari kidogo uko hafifu, na kwanini nasema hivyo? Kuna meli nne zilikuja bandarini lakini hakuna mapato yaliyokusanywa kutokana na meli hizo kuwepo pale. Meli ziliondoka na baada ya kuondoka, baada ya muda wa miezi 18; CAG katika kuangalia taarifa kwenye vitabu vya hesabu za bandari ile anakuta kwamba meli nne zimeingia na zimetoka, makusanyo hayakupatikana kiusahihi na meli zimeshaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie ni meli ngapi zimeingia. Hizi nne CAG ameziona, je, hizo za nyuma ambapo siku nyingine hata kwenye vitabu hazikuingizwa? Inamaana wao wenyewe Bandari wanajikosesha mapato yao kutokana na kutokuwa udhibiti katika makusanyo yake.
Mimi ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kufanya ziara bandarini, kaujua udhaifu wa bandari yetu na ndiyo maana Mheshimiwa Rais ikabidi aende akaangalie hali halisi na sote tulisikia kwenye vyombo vya habari nini Mheshimiwa Rais alichogundua na matokeo yake yalikuwa nini. Ushauri wangu, naiomba bandari iweze kudhibiti mapato yao maana tunaitegemea kimapato. Wakiweza kudhibiti mapato yao ndipo Serikali yetu itakapoweza kufanyakazi na wananchi tutafaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kuzungumzia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Taarifa ya CAG inayoishia Juni 30, 2015 ilionesha kwamba misamaha ya kodi imepungua kufikia jumla ya bilioni 1.6, sawa na asilimia 15.1 kwenye makusanyo ya TRA. Ingawa tunasema misamaha ya kodi imepungua lakini Serikali bado inapoteza mapato yake kutokana na misamaha hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano naweza kutoa. Kuna misamaha ya kodi iliyotolewa kwenye mafuta yenye thamani ya shilingi bilioni 22.3 ya Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita na Resolute. Mafuta hayo badala ya kutumiwa na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita na Resolute wao wakawapelekea wakandarasi wengine kuyatumia. Sasa msamaha umepewa wewe kisha wewe unampelekea mwenzio, hilo si tatizo? Tena tatizo sugu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningeiomba Serikali, masuala kama haya CAG akishayaona lazima tuwe tunayafuatilia. Lakini wakati mwingine ufuatiliaji unashindikana kwa sababu fedha ambayo ndiyo nyenzo hakuna.
Kamati imetaka kufuatilia ili ipate uhakika, inashindwa kwenda kutokana na nyenzo ziko hafifu. Sasa nafikiri kwa haya machache niliyoyazungumza na yote ambayo yanakwamishwa na nyenzo za kifedha naomba kuunga mkono hoja.