Primary Questions from Hon. Fakharia Shomar Khamis (35 total)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, ni viongozi wangapi wa Kitaifa wametembelea Zanzibar kuanzia mwaka 2010 - 2015?
(b) Je, Serikali haioni kwamba viongozi wa Kitaifa kutembelea Zanzibar inaleta chachu ya upendo kwa Wananchi na kuzidi kuimarisha Muungano wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, viongozi wote wa Kitaifa, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitembelea Zanzibar.
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitembelea Zanzibar mara 20, Mheshimiwa Dkt. Gharib Mohammed Bilal ametembelea Zanzibar zaidi ya mara 30 na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, ametembelea Zanzibar zaidi ya mara 12.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na hoja kuwa, Viongozi wa Kitaifa kutembelea Zanzibar inaleta chachu ya upendo kwa wananchi na kuzidi kuimarisha Muungano wetu. Ziara za viongozi wa Kiataifa huambatana na kuangalia utekelezaji wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa, kuongea na wananchi na kutoa maagizo na maelekezo kwa viongozi wa Serikali. Aidha, ziara hizo zinatoa fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa wa Zanzibar hali ambayo pia inastawisha Muungano wetu.
MHE.FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Magari yanayobeba abiria nchini yamekuwa yakitozwa faini pindi yanapokamatwa kwa kosa la kujaza abiria zaidi ya uwezo wake badala ya kutakiwa kupunguza abiria waliozidi.
(a) Je, Serikali haioni kuwa kutoza faini na kuacha gari liendelee na safari huku likiwa limejaza ni sawa na kuhalalisha kosa?
(b) Je, Serikali haioni kuwa ikiwashusha abira waliozidi itakuwa imetoa fundisho na kupunguza ajali kwa abiria ambao hupanda gari huku wakijua limejaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabani Sura ya 168, kifungu cha 58 ni kosa kwa abiria au mtu yeyote kutokuwa na kiti cha kukaa ndani ya gari la abiria na hivyo mtu huyo atahesabika kwamba amening‟inia ndani ya gari hilo. Mabasi yanatozwa faini kwa kuzidisha abiria yakiwa kituoni na maeneo salama abiria wote waliozidi huteremshwa na kurudishiwa nauli zao na utaratibu wa kuwatafutia mabasi mengine ambayo yana nafasi. Aidha, pale ambapo mabasi haya yalizidisha abiria yakikamatwa katika maeneo ambayo si salama huachwa na kuendelea na safari kisha mawasiliano hufanyika katika vituo vya polisi vilivyopo mbele ili abiria washushwe kwenye maeneo ambayo ni salama kwa abiria.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani imekuwa ikiwashusha abiria waliozidi ndani ya basi hasa pale inapokuwa imeonekana maeneo wanayoshushwa ni salama kwa maisha na mali za abiria hao na kutafutiwa usafiri mwingine.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, ni nini maana ya kitendo cha kupiga saluti kinachofanywa na askari?
(b) Je, ni askari wa ngazi gani hupigiwa saluti?
(c) Je, ni maafisa/viongozi wa ngazi gani uraiani katika mihimili ya Serikali, Mahakama na Bunge ambao wanastahili kupigiwa saluti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, saluti ni salamu ya kijeshi ambayo hutolewa na askari kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kudumu za Utendaji wa Jeshi la Polisi (Police General Orders No. 102).
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, askari wote kuanzia cheo cha mkaguzi msaidizi na kuendelea hustahili kupigiwa saluti.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, PGO namba 200 imeainisha taratibu za saluti kwa viongozi wa Serikali na taasisi zingine kama ifuatavyo:-
Askari wa vyeo vyote wanatakiwa kupiga saluti kwa Mheshimiwa Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naJaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wanapokuwa katika maeneo ya Bunge au Majimboni mwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wengine wanaostahili kupigiwa saluti ni pamoja na Wakuu wa Mikoa na Majaji wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi. Aidha, kuanzia askari mwenye cheo cha Konstebo hadi Mkaguzi wanapaswa kuwapigia saluti Wakuu wa Wilaya na Waheshimiwa Mahakimu wote wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na matukio ya kuvamiwa kwa askari wetu wakiwa katika vituo vyao vya kazi na kujeruhiwa, kunyang„anywa silaha na wakati mwingine hata kuuawa:-
(a) Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya usalama wa askari hawa?
(b) Je, mpaka sasa Serikali imeshakamata silaha ngapi zilizoporwa kutoka kwa askari waliovamiwa wakiwa katika majukumu yao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) yote kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa usalama wa askari polisi wanapokuwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi hapa nchini kwa vitendea kazi bora na kuwajengea uwezo askari wetu kwa mafunzo ili waweze kukabiliana na matukio ya uhalifu yanayohusisha uvamizi wa vituo vya polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa kipengele cha pili, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha 19 kati ya 23 zilizoporwa kutoka kwa askari waliovamiwa wakiwa katika majukumu yao katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Septemba, 2016.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS Aliuliza:-
Biashara ya vyuma chakavu imeshamiri sana Tanzania Bara na Visiwani na imesababisha madhara ya kuharibiwa na kuibiwa kwa miundombinu yakiwemo mifuniko ya chemba na majitaka.
(a) Je, Serikali imejipangaje kupambana na wizi na uharibifu huo wa mali za Serikali na wakati walinzi wa maeneo husika wanashuhudia hayo?
(b) Je, Serikali haioni kwamba hata usalama wa raia na mali zao uko mashakani?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis kuwa biashara ya chuma chakavu imeshamiri hapa nchini na duniani kwa ujumla. Kuongezeka kwa mahitaji (demand) ya vyuma chakavu kulitumiwa na wahalifu kuharibu miundombinu iliyojengwa kwa vyuma kwa nia ya kupata chuma ili waiuze kama chuma chakavu. Maeneo yaliyoathirika sana ni mifumo ya kusafirisha umeme, reli, barabara kwa kutaja baadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hujuma hizi mamlaka husika yaani TANESCO, TANROADS na RAHCO wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Jeshi la Polisi ikiwemo kutumia walinzi wa taasisi husika kulinda rasilimali hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupata suluhu ya kudumu, Wizara yangu imekwishaandaa rasimu ya muswada wa sheria itakayoweka bayana taratibu na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa biashara ya chuma chakavu katika hatua mbalimbali za uzalishaji, ukusanyaji, usambazaji, uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa. Aidha, muswada huo umeweka bayana adhabu itakayotolewa kwa mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombinu kwa sababu ya kuchukua chuma chakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge na Watanzania kwa ujumla usalama wao na mali zao ziko salama. Aidha, nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wote kutoa taarifa pindi wawaonapo mtu anayehujumu miundombinu kwa namna yoyote ile kwa lengo la kuchukua chuma chakavu au chuma. Kwa wenye viwanda na wafanyabiashara wa vyuma chakavu jiepusheni na ununuzi wa vyuma ambavyo asili yake inatia mashaka. Kama nilivyoeleza awali, tutaharakisha sheria ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kutatua tatizo hili.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS aliuliza
(a) Je, Serikali imejipanga vipi kuzuia uvuvi haramu nchini?
(b) Je, ni meli ngapi zilizokamatwa kwa sababu za uvuvi haramu kuanzia mwaka 2010 – 2015?
(c) Je, ni watu wangapi wametiwa hatiani na hukumu zao zikoje?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamisi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na wavuvi haramu, Wizara imeanzisha na kuimarisha vituo 25 vya doria kwenye maziwa makubwa, mwambao wa Bahari ya Hindi na mipaka ya nchi. Vituo hivyo vipo katika maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Kigoma, Musoma, Kagera, Mwanza, Mtwara, Mafia, Kilwa, Horohoro, Kipili, Kasanga, Sota, Sirari, Kasumulo, Mbamba Bay, Tunduma, Kabanga, Kanyigo, Rusumo, Ikola, Geita, Buhingu, Namanga na Murusagamba. Kuwepo kwa vituo hivyo kumeongeza uwezo wa kukabiliana na uvuvi na biashara haramu kupitia operesheni mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi za Serikali, tatizo la uvuvi haramu na biashara ya magendo kwenye mialo, masoko na mipaka ya nchi bado ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia, imeanzisha Kikosi
Kazi cha Kitaifa Mult Agency Task Team ambacho kinafanya kazi ya kudhibiti uhalifu wa mazingira ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu hususan matumizi ya mabomu katika shughuli za uvuvi. Wajumbe wa Kikosi kazi hiki ni kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Katiba na Sheria; Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Baraza la Taifa la Mazingira. Wajumbe kutoka Taasisi nyingine wataongezeka kadri itakavyoonekana inafaa. Kikosi kazi hiki kipo chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani. Aidha, Wizara imeendelea kufanya maboresho ya Sera, Sheria na Kanuni za uvuvi ili kuimarisha usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa kwenye maji ya ndani na ya Kitaifa (Inner and territorial waters) uvuvi unaofanyika ni wa kutumia mitumbwi, boti, mashua, jahazi na ngalawa na siyo meli. Kuanzia mwaka 2010 – 2015 jumla ya vyombo 2,795, injini za mitumbwi 118, magari 297 na pikipiki 33 vilikamatwa kwa sababu za uvuvi haramu na utoroshwaji haramu kwenye maji hayo. Aidha, katika Bahari Kuu kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 haijawahi kukamatwa meli ya uvuvi. Meli ya Uvuvi Tawariq1 ilikamatwa mwaka 2009.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi tajwa jumla
ya watuhumiwa 3,792 walikamatwa na kesi 243 zilifunguliwa mahakamani. Aidha, jumla ya shilingi 158,559,323 zilikusanywa ikiwa ni faini kutokana na makosa mbalimbali na watuhumiwa 11 wamefungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu, nawaomba Waheshimiwa Wabunge ambao ni wajumbe katika Halmashauri waendelee kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu madhara ya uvuvi haramu na kuhimiza Halmashauri zao zidhibiti uvuvi haramu kwenye maeneo yao. Pia, jamii za wavuvi na wadau wote washirikishwe katika kusimamia rasilimali za uvuvi na matumizi endelevu kwa ajili ya kuwapatia wananchi ajira, chakula na uchumi wao na Taifa kwa ujumla. Ni njia hii Taifa linaweza kudhibiti uvuvi haramu hapa chini.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Mara nyingi kumekuwa na taarifa juu ya watu wanaokamatwa na dawa za kulevya kwenye maeneo mbalimbali nchini, lakini hatuambiwi nini kinafanyika:-
Je, baada ya watu hao kukamatwa, ni nini huwa kinaendelea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali katika kudhibiti dawa za kulevya za mashambani na viwandani. Hatua hizo zinalenga kudhibiti kilimo cha bangi, uingizaji, usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya za viwandani kote nchini kwa kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia Oktoba, 2015 mpaka Mei, 2017 Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watumiaji mbalimbali ambapo watuhumiwa takribani 14,748 kesi zao zinaendelea mahakamani; watuhumiwa zaidi ya 2,000 walipatikana na hatia wakati watuhumiwa wanaozidi 600 waliachiwa huru na mahakama; na watuhumiwa wanaozidi 13,000 kesi zao ziko katika hatua mbalimbali za upelelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu natoa wito kwa wananchi na wageni kuacha kujihusisha na biashara hii haramu kwa kuwa, hakuna atakayebaki salama kwenye mapambano haya. Serikali kupitia vyombo vyake itaendelea kuwasaka wahusika wote ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Baadhi ya wafanyakazi wamejiunga na Mfuko wa NSSF na hukatwa sehemu ya mishahara yao kwa ajili ya kuwekeza ili iwasaidie baada ya kustaafu.
Je, mpaka sasa ni wafanyakazi wangapi wamejiunga na Mfuko huo?
Je, ni wafanyakazi wangapi wamestaafu kazi na kulipwa fedha zao na Mfuko huo?
Je, ni nani analipwa faida inayopatikana kwa fedha za Mfuko huo kutoka benki zinakowekwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na – kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lina jumla ya wanachama wapatao 946,533 ambao ni wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali ambao wamejiunga na Mfuko huu kufikia mwezi Juni, 2017.
• Mheshimiwa Spika, hadi kufika mwezi Juni, 2017, NSSF ina jumla ya wafanyakazi 14,946 ambao wamestaafu na wanaendelea kupata pensheni kutoka Mfuko huu.
• Mheshimiwa Spika, mapato yanayopatikana katika uwekezaji wa michango ya wanachama unaofanywa maeneo mbalimbali kama ilivyoanishwa katika miongozo ya uwekezaji hutumika kuwalipa wanachama mafao kama vile pensheni ya uzeeni, pensheni ya urithi, pensheni ya ulemavu, mafao ya kuumia kazini, mafao ya uzazi na matibabu kupitia Mfuko wa Bima wa SHIB. Aidha, Shirika hutumia sehemu ya mapato haya kulipia gharama za uendeshaji wa Mfuko.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Tatizo la kupotea kwa watoto katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa. Aidha, taarifa za kupotea kwa watoto hao zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari:-
(a) Je, ni sababu zipi zinazochangia kuongezeka kwa tatizo hilo siku hadi siku?
(b) Je, kwa nini taarifa za upatikanaji wa watoto hao hazitolewi kwenye vyombo vya habari?
(c) Je, Serikali ina mkakati gani kuondoa tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri ya Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la upoteaji wa watoto katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam. Aidha, sababu za upotevu wa watoto hawa ni pamoja na uangalifu hafifu wa watoto kutoka kwa wazazi au walezi na jamii kwa ujumla, mazingira magumu wanayoishi baadhi ya watoto, imani za kishirikina, visasi kati ya familia na kupotea kwa bahati mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kudhibiti matukio hayo kwa kutoa elimu kupitia programu ya Polisi Jamii kwa watoto mashuleni na wazazi kupitia mihadhara ya kijamii na vyombo vya habari. Jitihada hizo zimekuwa zikizaa matunda kwa kuongeza elimu ya usalama wetu kwanza miongoni mwa jamii na hivyo kuongeza umakini wa kulinda watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Disemba, 2017 kwa Mkoa wa Dar es Salaam walipotea watoto 184, ambapo watoto waliopatikana ni 176 na watoto ambao wanaendelea kutafutwa ni nane. Jeshi la Polisi linaendelea kutoa rai kwa taasisi na idara mbalimbali kama Ustawi wa Jamii kushirikiana na kuwa na programu za pamoja ili kutoa elimu ya kumlinda mtoto wa Tanzania.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Uharibifu wa mazingira nchini umeleta athari kubwa ya mabadiliko ya msimu wa kilimo, uhaba mkubwa wa maji na kukauka kwa vyanzo vya maji nchini.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi za kudhibiti uharibifu huo wa mazingira hasa katika ukataji wa miti?
(b) Je, Serikali inasema nini juu ya kupanda miti katika mashamba ya Serikali na ya watu binafsi ili kusaidia kuondoa hali hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira zinazolikabili taifa hili, Serikali imechukua hatua zifuatazo; kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaokamatwa wakikata miti bila vibali kwa mujibu wa Sheria, kutoa elimu ya mazingira kwa umma ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira hasa misitu na kuhamasisha wananchi kutumia nishati mbadala kama gesi na umeme pamoja na matumizi ya majiko banifu ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa mkakati wa Taifa wa kupanda na kutunza miti unaolenga kuhamasisha upandaji miti katika maeneo ya mashamba na viwanja vilivyo wazi, ikiwemo mashamba ya Serikali na watu binafsi ili kudhibiti hali ya uharibifu wa ardhi nchini. Katika kufanikisha mkakati huu jamii wadau mbalimbali watahusishwa katika utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati umeweka muundo wa kitaasisi wa utekelezaji unahosisha wadau wote ikiwemo Wizara za Kisekta na Idara nyingine za Serikali, asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kiraia, vijiji, shule, taasisi za dini na sekta binafsi. Kupitia mkakati huu, Serikali imepnga kupanda miti katika hekari laki 185,000 kila mwaka ambazo ni sawa na miti milioni 280. Mkakati huu utatekelezwa ipasavyo na utapunguza uharibifu wa misitu na urejeshaji wa uoto nchini.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Zipo taasisi bado zinaendelea kununua mazao kwa mkopo, jambo linalosababisha malalamiko kwa wakulima.
(a) Je, Serikali inalijua jambo hilo?
(b) Je, ni lini utaratibu huu wa kununua mazao kwa mkopo utaisha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi za Serikali zinazohusika na ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima ni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB). Hata hivyo, taasisi hizi kwa miaka mitatu ya 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018 zimeweza kununua mazao toka kwa wakulima bila kuwakopa hivyo kutopata malalamiko yoyote kutoka kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ulinunua mahindi tani 22,335,157, mwaka wa fedha 2016/2017 tani 62,099,319 na mwaka wa fedha 2017/2018 tani 26,038,643.
Aidha, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilinunua mahindi tani 3,300 kwa mwaka wa fedha 2015/2016, tani 1,971.5 mwaka wa fedha 2016/2017 na tani 2,250 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kutoka kwa wakulima. Manunuzi yote haya yalifanyika kwa fedha taslimu bila ya kuwakopa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, Serikali inaendelea kusisitiza uimarishwaji wa vyama vya Msingi vya Ushirika na Vyama Vikuu vya Ushirika ili kupitia vyama hivyo wakulima waweze kuuza mazao yao na kujihakikishia soko. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa uuzaji wa mazao katika Soko la Bidhaa za Kilimo (Tanzania Mercantile Commodity Exchange) kupitia mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani (Warehouse Receipts System) unaosimamiwa na Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi (Warehouse Receipts Regulatory Board).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali itasimamia uuzaji wa mazao ya wakulima kwa njia ya minada ili kuweka ushindani wa bei na kumwezesha mkulima kupata bei kubwa kama ilivyo katika zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hizi zitamhakikishia mkulima kuwa na soko la uhakika na hivyo kuongeza kipato chake. Aidha, Serikali inapenda kuwaomba wanunuzi binafsi wa mazao mbalimbali ya wakulima kujizuia au kuacha kabisa kuwakopa wakulima kwani vitendo ya namna hiyo huwakatisha tamaa wakulima na kusababisha kushuka kwa uzalishaji.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Tatizo la wahamiaji haramu hasa kutoka Ethiopia limeshamiri sana katika nchi yetu kwa sasa:-
(a) Je, ni wahamiaji haramu wangapi wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria?
(b) Kama wapo ambao wanaendelea na kifungo, je, ni hatua gani za kisheria ambazo zinachukuliwa baada ya kutolewa kifungoni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) yote kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji imekamata jumla ya wahamiaji haramu 13,393 katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi 2018. Miongoni mwao wahamiaji haramu 2,815 walishtakiwa, 117 walitozwa faini, 429 walifungwa, 6,316 waliondoshwa nchini, 1,353 waliachiwa huru baada ya kutoa nyaraka za uthibitisho wa ukaazi wao. Aidha, zipo kesi 2,363 zinazoendelea katika mahakama mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za kisheria ambazo huchukuliwa baada ya wahamiaji haramu kumaliza vifungo vyao gerezani ni kurudishwa nchini kwao.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la upimaji wa viwanja kwenye Manispaa mbalimbali nchini.
• Je, kwa nini wananchi wanalazimishwa kuuza maeneo hayo kwa Manispaa na kulipwa bei ndogo badala ya kufanya zoezi hilo kwa ubia?
• Kwa sababu maeneo hayo mengi ni mashamba, je, Serikali haioni kufanya hivyo kunasababisha Watanzania kukosa kazi maana asilimia 75 ni wakulima?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 inaelekeza kuwa eneo lolote likishatangazwa kuwa ni eneo la upangaji yaani planning area linapaswa kupangwa kwa kuzingatia Sheria ya Upangaji Mijini. Wananchi wanaokutwa kwenye maeneo hayo wanatakiwa kutambuliwa, kuelimishwa na kushirikishwa katika hatua zote za upangaji hadi umilikishaji. Pia Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, Sheria ya Upimaji wa Ardhi Namba 4 na Namba 5 za mwaka 1999 na kanuni zake za mwaka 2001 na Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake na miongozo yake, zinaelekeza Mamlaka za Upangaji kufanya upangaji na upimaji kwa kushirikisha wadau wote muhimu katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Aidha, Sheria ya Utwaaji Ardhi Namba 47 ya mwaka 1967 pamoja na mambo mengine inazingatia mamlaka za upangaji miji uhalali wa kutwaa ardhi iliyopangwa na inayohitaji kupangwa kutoka kwa wamiliki na kuwalipa fidia kwa kufuata miongozo ya ulipaji fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera na Sheria za Ardhi zinaelekeza umuhimu wa kutathmini ardhi na maendelezo ya wananchi waliokutwa nayo na kulipwa fidia sambamba na kupima na kumilikisha kwa makubaliano yatakayoridhiwa na pande zote mbili bila kuathiri sheria. Hata hivyo uzoefu unaonesha kuwa mamlaka za upangaji hupenda kutumia njia ya kulipa fidia ya Ardhi na maendelezo hali ambayo imeleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi. Serikali inazielekeza mamlaka zote za upangaji kutowalazimisha wananchi kutumia njia moja ya kulipa fidia na badala yake wananchi washirikishwe kuchagua njia wanayoona inafaa kati ya kuingia ubia au kulipwa fidia.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ambayo yametangazwa kuwa ni maeneo ya upangaji yaani planning area yanapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia Sheria ya Upangaji Mijini. Ni kweli kuwa kuna maeneo yanayotwaliwa na kuingizwa kwenye mpango ya kuendelezwa kimji ambayo ni mashamba ya wananchi. Mamlaka za Upangaji kwa kuwashirikisha wananchi wenye maeneo hayo hupanga matumizi mbalimbali yakiwemo makazi, kilimo cha mjini, viwanda vidogo vidogo, masoko, biashara kubwa na ndogo, huduma mbalimbali za kijamii kwa kutegemea maendeleo ya kimji na matakwa ya sheria. Kwa hatua hii wananchi huwa na fursa ya kupata kazi za kuwaingizia kipato kwa kupata viwango vya matumizi watakayo pendelea.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Moja kati ya matatizo makubwa yanayoikabili nchi yetu ni maradhi ya figo na idadi ya wagonjwa wa figo inazidi kuongezeka siku hadi siku:-
(a) Je, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hupokea wagonjwa wangapi kwa siku?
(b) Je, Serikali ipo tayari kutoa elimu kwa umma juu ya chanzo cha ugonjwa huo na namna ya kujikinga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 wakati wa huduma za utakasaji wa damu kwa wagonjwa wa figo zilipoanzishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kulikuwa na wagonjwa wa figo chini ya 10 waliokuwa wakihitaji huduma hii, lakini kwa sasa tuna wagonjwa 240 waliopo kwenye huduma hii. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili inatoa huduma ya utakasaji damu kila siku isipokuwa siku ya Jumapili na kuna jumla ya vitanda 42 vya kutolea huduma ambapo kwa siku wanahudumiwa wastani wa wagonjwa 80.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kiliniki ya wagonjwa wa figo ambayo inafanyika kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imekuwa ikiona wastani wa wagonjwa wapatao 60 kwa siku. Sanjari na hilo, Serikali kupitia hospitali zake za kibingwa imefanikiwa kuanzisha huduma za kupandikiza figo ambapo jumla ya wagonjwa 10 wameshapata huduma hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mgonjwa mmoja katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na upandikizaji huu utaendelea kwa wagonjwa watano kila mwezi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wakati huohuo Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiendelea kujengewa uwezo.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Chama cha Wataalam wa Magonjwa ya Figo Tanzania tunaendelea na jitihada za kutoa elimu za kujikinga na madhara ya magonjwa ya figo kwa kuzingatia kanuni za afya na kupima mapema ili kutambua na kupata matibabu kwa wakati. Elimu juu ya uelewa wa madhara yatokanayo na matumizi ya vileo, lishe isiyozingatia misingi ya afya bora na kutofanya mazoezi vinaweza kusaidia sana kuzuia magonjwa ya figo. Elimu hii imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari, ikiwemo makala kwenye magazeti, vipindi vya runinga na redio, vipeperushi, utoaji wa elimu za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na pia kwenye kampeni mbalimbali za magonjwa yasiyoambukiza.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Rushwa ni adui mkubwa wa haki. Aidha, rushwa ikishamiri husababisha athari hasi kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiteknolojia na hivyo kuchangia ongezeko la umasikini:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kulinusuru Taifa dhidi ya Rushwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba rushwa ni adui wa haki, kwani ni kikwazo katika kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi kwa haki na usawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua athari za rushwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, Serikali imeandaa kutekeleza mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa na mpango wa utekelezaji Awamu ya Tatu kwa maana ya NACSAP III ule wa mwaka 2017 hadi 2022.
Mkakati huu unalenga kuzuia na kupambana na rushwa katika Sekta za uchumi za kimkakati zenye mazingira shawishi ya rushwa ambazo ni manunuzi ya Umma, ukusanyaji wa mapato, uvunaji na matumizi ya maliasili, madini, nishati, mafuta na gesi, utawala, vyombo vya utoaji wa haki na shughuli za Vyama vya Siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa malengo ya mkakati huu ni kuimarisha na kuboresha mifumo ya utawala ya vyombo vya utoaji wa haki, kuimarisha elimu ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa na kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za Umma na vilevile za binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba wala rushwa na wahujumu uchumi wanachukuliwa hatua za kisheria, Sheria ya Uhujumu Uchumi ile Sura ya 200 imefanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 ya Mwaka 2016 kwa kurekebisha vifungu kadhaa kwa kupanua wigo na kuongeza makosa ya uhujumu uchumi pamoja na kuanzisha Division ya Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi katika muundo wa Mahakama Kuu na Mahakama hii imeshaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapambano dhidi ya rushwa yameonesha mafanikio ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kitengo cha urejeshaji mali chini ya TAKUKURU kwa ajili ya urejeshaji mali zilizopatikana kwa njia za rushwa kwa maana ya Asset Tracing and Recovery Unit. Kupitia kitengo hiki, Serikali imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 127.9 na kutaifisha au kuzuia akaunti za fedha zenye shilingi bilioni 4.5. Kesi 1,340 zimefunguliwa Mahakamani na Serikali imeshinda kesi 685.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, miradi ya maendeleo 899 yenye thamani ya shilingi 1,642,522,950,825.10 ilifuatiliwa ambapo miradi ipatayo 111 yenye thamani ya shilingi bilioni 23,256,624,083.40 iligundulika kuwa na kasoro au kufanyiwa ubadhirifu. Hivyo, uchunguzi unafanyika na upo katika hatua tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Moja kati ya majukumu ya kuimarisha Muungano ni pamoja na kuhakikisha kuwa kero zote za Muungano zinatatuliwa; na vikao vingi vimekaa na kujadili kero hizo:-
Je, ni kero ngapi tayari zimetatuliwa na zipi ambazo hadi sasa zimeshindikana kupatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambazo zimekwishapatiwa ufumbuzi ni 11 kati ya 15 zilizowasilishwa na kutafutiwa ufumbuzi. Changamoto nne zilizobaki zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi na hakuna changamoto iliyoshindikana kupatiwa ufumbuzi. Dhamira ya Serikali zetu zote mbili ni kumaliza changamoto zote zinazoukabili Muungano wetu ili uendelee kuwa nguzo pekee ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Sera ya Wazee imeelekeza kuwapatia wazee matibabu bure lakini utekelezaji wake haueleweki na pia una urasimu mkubwa.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa uhakika wa kuwaondolea kero na shida hizo wanazozipata wazee katika suala zima la matibabu yao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sera ya Afya ya Mwaka 2007 iliweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba wazee wanapata huduma bora za afya. Katika kutekeleza uamuzi huo Serikali ilitoa tamko la makundi maalum wakiwemo wazee wasio na uwezo kupatiwa huduma za afya bila malipo. Hata hivyo, changamoto iliyopo katia utekelezaji wa Sera hii ni ufinyu wa bajeti ikilinganishwa na mahitaji ya kuwapatia huduma za afya makundi hayo bila wao kuchangia gharama za huduma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya Mkakati wa Ugharamiaji wa Huduma za Afya ambao lengo lake ni kuibua vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya kugharamia huduma za afya (Health Care Financing).
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa vyanzo vilivyopendekezwa katika Mkakati huo ni uanzishwaji wa Bima ya Afya Moja (Single National Health Insurance) ambapo uchangiaji katika bima hiyo utakuwa ni wa lazima kwa wote walio na uwezo wa kuchangia.
Kulingana na tatifi zilizofanywa, njia hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza rasilimali fedha katika sekta ya afya na kuweza kugharamia makundi maalum yanayohitaji msamaha wa kulipia huduma za afya. Serikali inatarajia kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wote mwezi Septemba, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwataka watoa huduma kutenga madirisha maalum kwa ajili ya kwuahudumia wazee na halmashauri ziwatambue na kuwapa kadi za wazee kwa ajili ya matibabu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la Watoto wa Mitaani Jijini Dar es Salaam hali ambayo inakosesha Watoto hao haki zao za msingi kama elimu na malezi bora?
Je, Serikali imechukua hatua gani kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kufiwa na wazazi, migogoro ya familia, kutengana kwa wazazi, vitendo vya unyanyasaji na ukatili na umasikini katika ngazi ya kaya, vimesababisha ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya utafiti ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani iliyofanywa mwezi Mei mwaka 2018, inayohusisha mikoa sita nchini ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Arusha na Iringa, jumla ya watoto wapatao 6,393 wakiwemo wa kiume 4,865 na wa kike 1,528 wanaoishi na kufanya kazi mitaani, walitambuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2018 hadi mwezi Machi, 2019 jumla ya watoto 2,702 walipatiwa huduma mbalimbali katika mikoa ifuatayo: Arusha, watoto 330; Dar es Salaam 475, Dodoma 337, Iringa 313, Mwanza 770 na Mbeya 447. Huduma zilizotolewa ni pamoja na huduma za, chakula, afya, malazi, kurudishwa shuleni, stadi za ufundi, stadi za maisha, kuunganishwa na familia pamoja na msaada wa kisaikolojia na kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau, itaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa malezi na ulinzi wa watoto wakiwemo walio katika mazingira hatarishi. Pia itaendelea kuwajengea uwezo wazazi na walezi kwenye eneo la stadi za malezi na ulinzi wa watoto. Aidha, Serikali itaendelea kufanya tafiti ili kubaini kiini cha tatizo na kupanga mipango mahsusi ya kupambana na kutokomeza tatizo la watoto wa mitaani nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba jukumu la matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto linatekelezwa ipasavyo.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Kwa kuwa Muungano wetu ni Tunu na tunahitaji kuwatunza hata wazee wetu wanne walioshiriki kuchanganya mchanga wa Muungano wetu baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar:-
(a) Je, Serikali inawaangalia vipi wazee wetu hao wanne kwa kuwapa ahsante baada ya utu uzima kuwafikia?
(b) Wakati wa sherehe za Muungano, wazee hao hufikishwa kwenye sherehe; je, huko ndiko kuonesha Serikali inawatunza?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua michango ya watu mbalimbali walioshiriki katika ukombozi na Nchi yetu na ujenzi wa Taifa ikiwa ni pamoja wazee wetu walioshiriki katika tukio la kuchanganya udongo tarehe 26 Aprili, 1964. Kundi hili ni moja kati ya makundi mengi yaliyotoa mchango wa hali na mali katika kulijenga Taifa hili ikiwemo wastaafu na walioshiriki katika vita vya Kagera. Hata hivyo, kwa sasa hakuna sheria mahsusi ya ahsante au malipo kwa watu waliofanya mambo makubwa yanayojenga historia ya nchi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwashirikisha wazee hawa katika maadhimisho ya sherehe za Muungano ni sehemu ya kutambua mchango wao na kukumbuka tukio muhimu la uchanganyaji wa udongo wa Tanganyika na Zanzibar. Ushiriki wao huwezeshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais. Aidha, pamoja na wazee hawa, yapo makundi mengine ya wazee ambao kwa namna moja au nyingine walitoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa ambao pia hualikwa kushiriki katika maadhimisho hayo mfano Viongozi Wastaafu na Wanasiasa Wakongwe.
Hata hivyo, Serikali yetu ni sikivu sana na moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha inawaenzi watu wake wote ambao wamechangia kwa namna moja au nyingine kuifanya Tanzania ya leo na pia kuendelea kulinda historia kwa ajili ya faida ya kizazi kilichopo na kijacho.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Askari wa Jeshi la Polisi Zanzibar (Ziwani) wanakabiliwa na matatizo makubwa ya makazi kama vile miundombinu ya maji, nyumba chakavu, uhaba wa vyoo na kuharibika kwa uzio uliokuwepo katika eneo hilo unaohatarisha usalama wao:-
(a) Je, kuna mpango gani wa kufanyia matengenezo nyumba na vyoo kwa wakati huu?
(b) Je, Uzio wa boma hilo la Ziwani utafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linakabiliwa na tatizo la uchakavu wa miundombinu kama majengo ya ofisi na nyumba za kuishi Askari kutokana na kuwa ya muda mrefu. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikifanya ukarabati wa miundombinu hiyo kwa awamu ili kuboresha huduma kwa wananchi Mheshimiwa Spika Mipango ya ukarabati ya miundombinu hiyo kwa awamu ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, mipango ya ukarabati wa miundombinu katika Kambi hiyo imeanza kwa kuandaa makadirio ya ukarabati kwa kuzingatia vipaumbele hasa kwa nyumba ambazo zimechakaa na ambazo zinaweza kukarabatika, mahitaji na gharama za majengo husika.
Mheshimiwa Spika, uzio wa Kambi ya Polisi - Ziwani ni wa fensi ya waya ambayo imezunguka eneo kubwa na waya huu katika baadhi ya maeneo ambao umechoka na kuchakaa kabisa. Aidha, upo mpango wa kujenga fensi ya matofali mara tu pale fedha zitakapokuwa zimepatikana.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Je, Serikali inatoa elimu gani kwa vijana waliopo mashuleni/vyuoni ili kujikinga na tatizo sugu la utumiaji wa dawa za kulevya nchini.
WAZIRI MKUU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga na imekuwa ikitoa elimu kwa vijana waliopo Mashuleni na vyuoni ili kujikinga na tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Ikumbukwe, mwaka 2017, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alianzisha rasmi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo licha ya kupambana na biashara hiyo, Mamlaka hii imejikita katika suala zima la utoaji wa elimu juu ya tatizo hilo kwa Umma wakiwemo vijana waliomo mashuleni na vyuoni kama moja ya vipaumbele vyake muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa, mamlaka imeweza kutoa elimu mashuleni na kutengeneza mwongozo wa uendeshaji wa vilabu vya kupinga matumizi ya dawa za kulevya mashuleni na wakati mwingine kutumia Vilabu vya UKIMWI mashuleni kuzungumzia pia suala la tatizo la Dawa za Kulevya. Sambamba na hilo, Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanafanya utaratibu wa kuingiza suala la dawa za kulevya katika mitaala ya kufundishia wanafunzi wa mashuleni na vyuoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, elimu imekuwa ikitolewa na Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Taasisi za Serikali, Asasi za kiraia pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kupitia vyombo vya habari kama vile Televisheni, Redio, Magazeti na mitandao ya kijamii pamoja na matamasha. Aidha, Mamlaka imekuwa ikitumia hafla maalum za kitaifa kama vile siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya Duniani, Mbio za Mwenge wa Uhuru, Sikukuu ya Sabasaba, Sikukuu ya Nanenane pamoja na siku ya UKIMWI Duniani ili kutoa elimu kwa Umma.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la uhakika la matunda ndani na nje ya nchi pamoja na kuanzisha viwanda vya kusindika matunda ili kufanya kilimo cha matunda kuwa chenye tija?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mpango wa utafutaji masoko ya ndani na nje kwa mazao na bidhaa mbalimbali, ikiwemo masoko ya matunda ni jukumu endelevu. Utekelezaji wa jukumu hilo huhusisha taasisi zetu kama TanTrade, Balozi za Tanzania nje ya nchi, Bodi za mazao, Soko la Bidhaa za Mazao na sekta binafsi. Lengo la kutumia balozi zetu nje ni kupata taarifa za kina kuhusu mahitaji ya masoko ya mazao na bidhaa za Tanzania katika nchi husika.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Serikali katika kutafuta masoko unahusisha uhamasishaji wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kupitia taasisi zetu za uwekezaji TIC, EPZA, Balozi zetu nje pamoja na Serikali ngazi za Wilaya na Mikoa. Uhamasishaji huo unaenda sambamba na kutoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kupitia sheria za uwekezaji pamoja na zile za Uendelezaji Maeneo Maalum ya Uwekezaji yaani EPZ na SEZ. Aidha, Serikali kupitia Taasisi za SIDO, NDC na EPZA inaendelea kutoa ushauri wa namna ya kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya aina mbalimbali ikiwemo vya kusindika matunda na kuvilea ili viweze kukua na kuweza kuwa soko kwa matunda yetu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Juhudi za Serikali ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda na ambapo juhudi hizo zimezaa matunda ambapo kwa sasa kuna viwanda viwili vikubwa vya kusindika matunda katika Wilaya ya Bagamoyo ikiwa ni vya Elven Agri Co. Ltd na Sayona Fruits Co. Ltd vyenye uwezo wa kusindika tani 28 za matunda kwa siku na kuajiri jumla ya wafanyakazi 755.
Mheshimiwa Spika, viwanda hivyo hutoa soko la uhakika la matunda kwa wakulima mbalimbali hapa nchini. Aidha, ili kuwa na uhakika wa malighafi za kutosha kwa mwaka mzima, tunashauri Mheshimiwa Mbunge kuendelea kushirikiana na Serikali kuhamasisha uzalishaji wa aina mbalimbali za matunda yatakayotumika katika viwanda hivyo ili viwanda hivyo viweze kupata malighafi za uhakika kwa kipindi kirefu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, Serikali imejipanga vipi kupambana na tishio la uvuvi haramu nchini?
(b) Je, ni meli ngapi zilikamatwa nchini tokea mwaka 2015 - 2020 kwa kosa la uvuvi haramu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupambana na tishio la uvuvi haramu, Serikali imeandaa Mkakati wa Ulinzi na Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi ambapo katika mpango huo ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi kupitia Halmashauri, Serikali za Vijiji na Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi utaimarishwa. Aidha, kupitia mkakati huo, Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu athari za uvuvi haramu kwa mazingira, jamii na uchumi. Vilevile Serikali itaendelea kuimarisha Mashirikiano ya Kikanda na Kimataifa kwa kushirikiana na nchi mbalimbali zikiwemo Nchi za SADC katika kuzuia uvuvi haramu usioratibiwa na kuripotiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bahari Kuu, Serikali inao mfumo wa kufuatilia mienendo ya meli zote za uvuvi. Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015-2020, meli moja ya uvuvi haramu ilikamatwa Bahari Kuu na kufunguliwa mashtaka, ambapo Mahakama iliamuru mmiliki wa meli hiyo kulipa jumla ya shilingi bilioni moja au kufungwa jela miaka 20.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
(a) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na wizi wa vyuma unaosababishwa na kushamiri kwa biashara ya chuma chakavu nchini?
(b) Je, Serikali haioni kwamba biashara ya vyuma chakavu ni hatarishi hata kwa usalama wa raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kupitia vifungu vya 133 hadi139, Serikali imeweka kanuni za udhibiti wa taka hatarishi ikihusisha ukusanyaji, usafirishaji na uhifadhi wa taka hizo. Sambamba na uwepo wa kanuni, Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali pamoja na elimu kwa jamii katika ulinzi wa miundombinu. Aidha, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na jeshi la polisi imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda ili kudhibiti suala la uhujumu wa miundombinu ya Serikali na watu binafsi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya vyuma chakavu imesaidia kuziondoa taka hizi katika mazingira na hivyo kutengeneza mazingira safi na salama kwa afya ya binadamu. Aidha, vyuma chakavu ni malighafi ya viwanda hasa viwanda vya nondo na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji ili kudhibiti hujuma ya miundombinu ya Serikali na watu binafsi. Aidha, wananchi na vyombo mbalimbali vinaombwa kushiriki kwa pamoja katika kulinda miundombinu dhidi ya watu waovu na wale watu wasio na uzalendo, ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu usalama wa Askari ambao wakati mwingine huvamiwa na kujeruhiwa pamoja na kuporwa silaha wakati wakiwa kazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge Viti Maalum kutoka Zanzibar, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari wa Jeshi la Polisi wapo imara katika kutimiza majukumu ya kazi zao za kila siku na wamepata mafunzo mbalimbali yakiwemo mafunzo ya mbinu za medani, matumizi ya silaha na mafunzo ya kujihami. Pia katika utendaji wa kazi wao hufuata utaratibu wa kujilinda na kulinda wengine, ila mazingira na maeneo ya utendaji kazi husababisha changamoto mbalimbali kutokea kama hizo za kuvamiwa na kujeruhiwa. Mara zote Jeshi la Polisi hudhibiti hali hiyo na kushughulikia kwa haraka matukio ya namna hiyo na kuimarisha amani na utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaondoa kabisa utaratibu wa kununua mazao kwa mkopo ambao unaendelea kutumiwa na baadhi ya Taasisi jambo ambalo linasababisha manung’uniko kwa Wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ni Taasisi za Serikali pekee chini ya Wizara ya Kilimo ambazo imekuwa ikizitumia kuchochea soko la mazao ya wakulima hasa mazao ya nafaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia NFRA na CPB imetumia jumla ya bilioni 119 kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka ambayo yatauzwa katika masoko ya ndani na nje.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Oktoba, 2021 NFRA imetumia jumla ya bilioni 37 kununua jumla ya tani 75,000 za mahindi na CPB imetumia jumla ya bilioni 12 kwa ajili ya tani 27,000 za mahindi na ununuzi unaendelea. Aidha, ununuzi huo umefanyika katika Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi, Shinyanga, Arusha na Dodoma.
Mheshimiwa Spika, NFRA na CPB hazitumii utaratibu wa kukopa wakulima wa nafaka kwani, zimekuwa zikinunua nafaka kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima na kufanya malipo mara baada ya mapokezi ya nafaka katika vituo vya ununuzi. Katika msimu wa 2021/2022 taasisi hizi zinaendelea na ununuzi wa nafaka kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima kwa utaratibu wa malipo ya fedha taslimu na si kwa njia ya kuwakopa wakulima.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuwawezesha Wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana ajira kulipa mikopo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu mojawapo la msingi la Serikali ni kuandaa mazingira wezeshi kuhakikisha Watanzania wanapata maarifa na ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri na kuajirika ili kukuza uchumi wa Taifa na vipato vyao. Kutokana na msingi huo, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilitunga Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Na. 9 ya Mwaka 2004 ambayo inawezesha kutoa mikopo au ruzuku kwa wanafunzi wahitaji waliokidhi vigezo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, wazazi au wadhamini wanatakiwa kuhakikisha mikopo inarejeshwa ili iweze kunufaisha Watanzania wengine wanaohitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wanufaika wa mkopo ambao baada ya kumaliza vyuo wanachukua muda mrefu kupata ajira au kujiajiri, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Miongoni mwa hatua ambazo Serikali imezichukua ni pamoja na zifuatazo: -
(i) Kutoa mafunzo ya uzoefu wa kazini (internship) kwa wahitimu wa elimu ya juu nchini kupitia waajiri wa ndani na nje ya nchi ambapo jumla ya wahitimu 6,624 wamepatiwa mafunzo ya uzoefu wa kazini na wahitimu 11,475 wamepatiwa mafunzo ya kushindania fursa za ajira katika sekta mbalimbali za kiuchumi;
(ii) Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, jumla ya Shilingi bilioni 3.3 katika Serikali hii ya Awamu ya Sita, zimetolewa katika kipindi cha miaka ya nyuma mitano kwa ajili ya kuwapatia vijana mikopo nafuu wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu.
(iii) Kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri ya asilimia 10, jumla ya shilingi bilioni 145.8 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu;
(iv) Kutoa mafunzo ya ujasiriamali, kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, hadi sasa programu hii imewafikia vijana 8,736 wa elimu ya juu nchini;
(v) Kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa sekta binafsi ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ametilia mkazo sana eneo hili kuhakikisha kwamba tunapokuwa na uwekezaji na private sector kwa sababu ndiyo inaandaa watu wengi zaidi, vijana waweze kupata fursa ya kuajirika, kuajiriwa na kujiajiri. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya ajali zinazosababishwa na bodaboda kwa kutoa sight mirror?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Fakharia Shomar Khamis Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sheria ya usalama barabarani Sura ya 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, Kifungu 39 (1) inayotumika Tanzania bara, na sheria ya usafiri barabarani Sura ya 7 ya mwaka 2003, Kifungu cha 22 inayotumika Zanzibar zinatamka kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kuendesha chombo cha moto barabarani ikiwemo gari na pikipiki bila kuwa na vifaa kamili ikiwemo sight mirrors kwani chombo hicho kitahesabika kuwa ni kibovu.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kuwa, mtu yeyote anayeendesha chombo cha moto zikiwemo pikipiki za biashara (bodaboda) kufuata sheria na kutotoa sight mirror kwenye pikipiki. Kitendo cha kutoa sight mirror ni kukiuka sheria na mhusika atapaswa kukamatwa na kutozwa faini ya papo kwa papo au kufikishwa mahakamani na chombo chake kuzuiwa hadi akirekebishe.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa vijana walio mashuleni juu ya kujikinga na dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa na kuzindua Mwongozo wa Utoaji Elimu Kuhusu Dawa za Kulevya nchini ambao ulizinduliwa tarehe 2 Julai, 2022 na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye kilele cha siku ya Taifa ya Kupinga Dawa za Kulevya, Jijini Dar es Salaam. Mwongozo huo tayari umeanza kutumika kuelimishia walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na asasi za kiraia zinazojihusisha na utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii wakiwemo vijana waliopo mashuleni, juu ya tatizo la dawa za kulevya nchini.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa nakala ya Sheria ya Maadili kwa Viongozi nchini ikiwemo Wabunge na Viongozi wengine ili kuepuka kukiuka Sheria hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamisi (VITI MAALUM) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika; Serikali imekuwa ikitoa nakala za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya Mwaka 1995 kwa Viongozi. Serikali hutoa nakala hizo kupitia mikutano, warsha, semina, makongamano na maonyesho mbalimbali. Kati ya mwaka 2015 hadi 2022 Jumla ya nakala 12,400 za Sheria zilichapishwa na kutolewa kwa Viongozi na wadau wengine. Aidha, nakala tepe (soft copy) ya Sheria imewekwa katika tovuti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz. Hivyo, Viongozi wa Umma wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wanashauriwa kutembelea tovuti na kupata nakala ya Sheria.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, ni vijana wangapi wa Tanzania wamepata nafasi za masomo nje ya Nchi kwa mwaka 2015-2020 na wangapi wanatoka Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nafasi za ufadhili wa masomo unaotolewa na mashirika au nchi rafiki zinazopitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, huratibiwa kwa ushirikiano baina ya pande mbili za Muungano. Idara za elimu ya juu zina jukumu la kubaini sifa za waombaji na kupendekeza wanufaika wa ufadhili kwa kuzingatia vigezo bila kujali mwombaji anatoka upande upi wa Muungano. Aidha, zipo baadhi ya nafasi za ufadhili wa masomo ambazo huratibiwa moja kwa moja na nchi au shirika linalotoa ufadhili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015 - 2020, Wizara ya Elimu, Sayani na Teknolojia kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar iliratibu ufadhili wa masomo katika nchi za Uingereza, Hangaria, China, Morocco, Misri, Algeria, Urusi, Ujerumani, Msumbiji, Thailand, Mauritius, Iran na Indonesia. Watanzania walionufaika na ufadhili huo ni 873 ambapo kati yao wanaume ni 587 na wanawake 286.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Je, lipi tamko la Serikali kwa watuhumiwa waliopo magereza ya nchi za nje wanaomiliki vitambulisho na hati za kusafiria za Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria, Sura ya 42, pasipoti hutolewa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya kusafiria nje ya nchi. Pale inapothibitika kuwa raia wa nchi za nje wanamiliki hati za kusafiria za Tanzania kinyume na matakwa ya sheria yetu ya pasipoti wanakuwa wametenda makosa na hivyo wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Mbunge kama ana taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa watuhumiwa hao azikabidhi kwa vyombo vyetu ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki, nashukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -
Je, ni vijana wangapi wamepata nafasi za masomo nje ya nchi kwa mwaka 2015 - 2020 na kati yao ni wangapi wanatoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015 - 2021, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar iliratibu ufadhili wa masomo katika Nchi za Uingereza, Hangaria, China, Morocco, Misri, Algeria, Urusi, Ujerumani, Msumbiji, Thailand, Mauritius, Iran na Indonesia. Watanzania walionufaika na ufadhili huo ni 856 ambapo kati yao wanaume ni 609 sawa na 71.1% na wanawake 247 sawa na 28.9%.
Mheshimwa Naibu Spika, nafasi za ufadhili wa masomo nje ya nchi hutolewa pasipo kujali mwombaji anatoka upande upi wa Muungano.
Mheshimwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kuwasaidia wazee waliopata ulemavu wakati wa kupigana Vita ya Kagera mwaka 1979?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa wazee walemavu wa vita ya Kagera wapatao 272 wanalipwa pensheni ya ulemavu. Baada ya vita kumalizika Serikali iliwasaidia wapiganaji wote waliopigana vita. Wengi kati ya wapiganaji hao walipewa ajira katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza. Aidha, wapo walioshindwa kuajiriwa kutokana na sababu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, wazee walemavu waliopigana vita ya Kagera wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za Jeshi na wanalipwa pensheni za ulemavu kwa mujibu wa Kanuni za Pensheni na Viinua Mgongo za mwaka 1966. Wizara inaendelea kufuatilia hali halisi za wazee waliopigana vita ili kuchukua hatua stahiki. Endapo kuna wazee na walemavu waliopigana vita ya Kagera ambao hawanufaiki na huduma zinazotolewa inashauriwa wawasilishe taarifa zao kwa ajili ya uhakiki na hatimaye waweze kunufaika na huduma hizo, nashukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Je, kwa nini Kodi ya Jengo na Kodi ya Ardhi zisiunganishwe na kuwa moja ili kumwondolea usumbufu mwananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi inaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya mifumo ya kodi, ada na tozo za huduma kwa lengo la kuondoa urasimu na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Tathmini hiyo inajumuisha mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa usimamizi wa kodi ya jengo na kodi ya ardhi kama inavyopendekezwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hiyo, Serikali inaandaa mfumo wa kielektroniki wa kutoa ankara ya pamoja kwa huduma zinazolandana ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaostahili kulipa kodi ya jengo na kodi ya ardhi. Ahsante.