Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Fatma Hassan Toufiq (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama katika hili Bunge Tukufu kuzungumzia kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge hili, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Dodoma kwa kunichagua na kunifanya niwe Mbunge wao. Sambamba na hilo niwashukuru pia wanaume wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwaruhusu wake zao na watoto wao kuweza kuja kunichagua kwa hiyo, nawashukuru sana wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kwa unyenyekevu mkubwa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri aliyoitoa. Nalipongeza pia Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuzungumzia kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 73 ambao ulikuwa unazungumzia suala la Ustawishaji Makao Makuu. Naamini sote tunafahamu kwamba suala la Ustawishaji wa Makao Makuu lilianzishwa mwaka 1973 lakini kwa masikitiko makubwa sana mpaka leo hii hakuna sheria ambayo inazungumzia uwepo wa Makao Makuu Dodoma. Kukosekana kwa sheria hiyo imechelewesha sana kuhamia Makao Makuu Dodoma. Pamoja na taarifa nzuri ambayo imetolewa kwamba kuna baadhi ya mambo yamepangwa katika Ustawishaji Makao Makuu, lakini kumbe ipo sababu ya msingi kabisa ya kutungwa sheria ambayo itaharakisha Makao Makuu yawe Dodoma na Ofisi ziweze kuhamia Dodoma, hatimaye Mji Mkuu wa Tanzania yetu uwe Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niwakumbushe tu kwamba wenzetu Nigeria walibaini kwamba wanatamani wapate Mji Mkuu mpya mwaka 1976, wakajitahidi by mwaka 1991 wakaweza kufanikiwa kuhama kutoka Lagos kwenda Abuja. Sisi tangu mwaka 1973 mpaka leo mwaka 2016 bado hatujaweza kuhamia Dodoma. Kwa kweli hili jambo inabidi zichukuliwe hatua za uhakika kuhakikisha kwamba sheria hii inatugwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa sheria ya kutambua kwamba Dodoma ni Makao Makuu utasaidia sana kwa sababu kuna muingiliano mkubwa sana wa utendaji kati ya Manispaa pamoja na hii Mamlaka ya Makao Makuu. Kwa hiyo, naamini kwamba ukiwekwa mkazo wa uhakika kutungwa kwa hii sheria utasaidia kabisa kutofautisha kazi kati ya Manispaa pamoja na hii Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kwamba uwepo wa sheria ile utasaidia kuharakisha kuwa na uwekezaji katika Mkoa wetu wa Dodoma. Kwa kweli katika Mkoa wa Dodoma, miaka ya nyuma kulikuwa na baadhi ya viwanda kwa mfano, Kiwanda cha Coca-cola lakini tunashangaa kiliondoka vipi, kulikuwa kuna Kiwanda cha Mvinyo bahati mbaya kikafa, kulikuwa kuna Kiwanda cha Magodoro, tunaona tu Magorodo Dodoma lakini magodoro yale hayatengenezwi hapa Dodoma.
Kwa hiyo, naamini kabisa kama ukiwekwa mkazo na naamini katika Bunge hili tutahakikisha sheria hii inatungwa basi uwekezaji utaweza kupata tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ili kupunguza mwingiliano wa kazi kati ya Manispaa pamoja na CDA, ikiwezekana kiundwe chombo kimoja tu ambacho kitasimamia ustawi na upimaji wa mipango miji katika Mkoa wa Dodoma kwa sababu Manispaa wanafanya shughuli hizohizo ambazo zinafanywa na CDA. Kama sheria itaweka chombo kimoja ambacho kitasaidia sasa kufanya mambo yote ya mipango miji, naamini kabisa itasaidia ustawishaji na hatimaye Makao Makuu yanaweza yakaja Dodoma lakini kubwa zaidi ni suala la sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie pia suala la miundombinu. Katika Mkoa wetu wa Dodoma pamoja na kwamba mji umepangwa vizuri lakini kuna maeneo tofauti tofauti kwa mfano maeneo ya Area C, Nkuhungu, Medeli na maeneo mengine mapya ambayo yameanza kujengwa, zile barabara za ndani za mitaa hazipo, mvua zikinyesha kwa kweli kunakuwa na adha kubwa sana kwa wananchi. Kuna maeneo ambapo mashimo ni makubwa sana, kuna maeneo mifereji iliyopo sio mifereji ambayo inaweza ikasaidia kupitisha maji, kwa hiyo inaleta madhara makubwa sana. Kwa kuwa Waziri Mkuu yupo hapa na analisikia sheria hii ikitiliwa mkazo naamini kabisa mambo mengi yanaweza yakafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulisisitiza ni kuhusu sewage system katika huu Mkoa wa Dodoma. Kuna maeneo ni kweli imejengwa sewage system, lakini maeneo mapya ambayo Ustawishaji Makao Makuu wameyaweka sewage system bado sio nzuri. Kwa hiyo, tunaomba na jambo hilo lifikiriwe kwa ajili ya afya ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nililokuwa nataka nilizungumzie ni kuhusu uwanja wetu wa ndege katika eneo la Msalato. Ninaamini kabisa kwamba uwanja huu uko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini bado sijaona hatua za haraka au zinazoenyesha kwamba uwanja huu unaweza kujengwa haraka. Kwa sababu uwanja huu kwa kweli utakuwa una tija sana kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma lakini pia na wananchi wengine wote wa Tanzania kwa ujumla. Kwa hiyo, nimeona na hilo nalo nilizungumzie ili uwanja huo nao uweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kwamba katika Mkoa wa Dodoma kuna eneo karibu kama kilometa nane kutoka pale Chuo cha Mipango bado halijawekwa lami. Kwa kweli imekuwa ni kero sana kwa wananchi na wamekuwa wakiilalamikia sana Serikali kwa kuona ukimya uliopo kwa sababu limekuwa la muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kabisa katika bajeti hii nalo litatiliwa mkazo ili kusudi eneo lile liweze kuwekewa lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu suala la maafa na majanga na hasa kwenye janga la moto. Tumekuwa tukisikia matukio mbalimbali kuhusu janga la moto lakini bado nchi yetu haina vifaa vya kutosha kwa ajili ya kukabiliana na janga hili. Kwa hiyo, niombe Serikali waone ni utaratibu gani tunaoweza kuufanya walau wa kuweza kupata magari na vifaa vya uokozi wa moto katika kila Wilaya ili kusudi inapotokea dharura yoyote ya moto waweze kupata fursa ya kuweza kuzima huo moto kwa sababu wananchi wengi sana wamekuwa wakipata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi wameyazungumza wenzangu kuhusu masuala ya afya, maliasili na kadhalika lakini naomba tu nizungumzie kidogo kuhusu suala la Bima ya Afya au CHF. Wenzangu wamelizungumza na mimi naomba nitoe msisitizo, hebu Serikali ione kwa sababu hii asilimia 27 ya wachangiaji ni asilimia ndogo sana, bado tuna sababu ya msingi sana ya kuhamasisha wananchi ili kusudi waweze kujiunga na huu Mfuko wa CHF kwa sababu una tija sana kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kushangaza sana Watanzania wenzangu hatuko makini sana kuchangia masuala mbalimbali ya kimaendeleo. Watu wako makini sana kuchangia harusi na sherehe mbalimbali, lakini kwenye suala afya inaonekana watu hawana mwamko. Nitoe shime kwamba na sisi viongozi tulifanyie kazi suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Wizara ya Elimu kudahili Walimu tarajali 5,690 katika vyuo vya UDOM, Kleruu na Monduli. Pamoja na kudahili wanafunzi hao inaonyesha kuna upungufu wa Walimu 22,000 wa sayansi bado tuna hitaji kubwa sana la kudahili Walimu zaidi. Wizara ingefikiria kufanya programu maalum walau miaka nane (8) ili kuzalisha Walimu wa Sayansi nchini kwa wingi kwa kuwapeleka vyuo mbalimbali.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
181
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kujenga maabara katika kila sekondari za kata. Naipongeza pia Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweka bajeti ya kununua vifaa kwa ajili ya maabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, inaonekana pia kuna upungufu wa Walimu wa lugha hasa Kiingereza. Je, kwa nini Wizara isirejee utaratibu wa miaka ya themanini hadi miaka ya tisini ambapo Walimu walikuwa wanasoma kwa michepuo? Kwa mfano:-
(i) Marangu – Kiingereza
(ii) Korogwe – Kiswahili
(iii) Mkwawa – Sayansi
(iv) Monduli – Kilimo
(v) Mandaka/Monduli - Kilimo
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa michepuo ulidahili wanachuo kutokana na ufaulu wao. Je, kwa nini Wizara isirejee mtindo huu ili kupata Walimu waliosomea masoma hayo? Wizara iangalie wapi tulikosea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri kuna mradi wa Education and Skills for Productive Jobs Programme (ESPT). Mradi una nia ya kukuza stadi za kazi na ujuzi. Sekta zilizopo ni sita (6) nazo ni za kukuza uchumi, kilimo, uchumi, utalii, uchukuzi, ujenzi, nishati na TEHAMA. Nashauri fani ya ushonaji na upishi nazo ziongezwe. Wizara inaweza kuona fani hii si hitaji lakini fani ya ushonaji/upishi ni fani ambazo zimeinua wananchi wengi katika ujasiliamali. Inabidi wanafunzi waanze kufundishwa fani hizi tangu msingi ili kuwaandaa wakifika VETA waweze kupata ujuzi mzuri zaidi na itasaidia vijana wengi kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu maalum wengi wameizungumzia. Nashauri Wizara ifanye utaratibu wa kufanya sensa ya watoto wenye ulemavu kwani watoto wengi wenye ulemavu wanafichwa. Katika ukurasa wa 97, kiambatanisho (6) kinaonesha idadi ya wanachuo wenye ulemavu wanaodahiliwa katika vyuo ni kidogo sana. Tunataka kujenga Taifa lenye uchumi wa kati ni budi Serikali ikaona umuhimu wa kudahili wanachuo wengi zaidi wenye ulemavu ili nao waweze kupata fursa nyingi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sula la maslahi ya Walimu TSD ambayo sasa ni TSC inabidi ipewe nguvu ya kufanya kazi. Ni vema Wizara ya Elimu na TAMISEMI kuona jinsi ya kuipatia fedha za kutosha ili Walimu waweze kuhudumiwa vizuri zaidi. Kwa kuwa TSC inasimamia Walimu wa shule ya msingi/sekondari katika masuala ya nidhamu, maadili, kupandisha vyeo, kuthibitisha Walimu kazini na kutoa vibali vya kustaafu, vikao vya kisheria (statutory meetings) havifanyiki kutokana na ukosefu wa fedha. Inabidi Wizara ya Elimu na TAMISEMI waiangalie TSC kwa jicho la pekee ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri kwa ajili ya ustawi wa Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wadhibiti Ubora wa shule za msingi/sekondari, ukurasa wa 18. Naipongeza Serikali kwa kusomesha Wadhibiti Ubora 1,435 ambao wamepata mafunzo ya stadi za KKK ili kutoa msaada kwa Walimu wanaofundisha KKK. Pamoja na kuwepo kwa Wadhibiti hao ni vema Wizara ikaweka utaratibu maalum wa kuwapeleka masomoni Walimu kipindi cha likizo ili wapate mafunzo rejea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 10, kipengele cha 5.0, mapitio ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2015/16, katika kusimamia utekelezaji na mambo yaliyobainishwa nazungumzia kipengele (v), naomba pia Walimu wa michezo wapewe mafunzo ili waweze kuwafundisha watoto wetu michezo kwani hakuna ubishi michezo ni ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza tena Wizara ya Elimu, Waziri na timu yote. Nawatia moyo waendelee na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia bajeti hii. Sambamba na hilo naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, nimpongeze sana Waziri wa Fedha kwa hotuba yake yote aliyoitoa ya Hali ya Uchumi pamoja na hotuba ya Bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwanza kwenye pato la ukuaji wa uchumi lakini nikirejea ukurasa wa 16 wa Taarifa ya Hali ya Uchumi. Naipongeza sana Serikali kwa kuifanya nchi yetu Pato la Taifa likakua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka 2015. Nitoe masikitiko yangu kwamba kwenye eneo la kilimo ambapo asilimia 70 ya wananchi wetu ndiyo wanakitegemea imebainika kwamba uzalishaji wake umeshuka. Mwaka 2014 ilikuwa na asilimia 3.4 mwaka 2015 imeshuka kwa asilimia 2.1. Jambo hili hatutakiwi kulifumbia macho na halitakiwi tu kubakia katika vitabu. Tujiulize anguko hili limetokea kwa sababu ya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana wakulima wetu wamekata tamaa ama kwa kucheleweshewa pembejeo, pembejeo hazifiki kwa wakati lakini sambamba na hilo ni kwamba Vyama vyetu vya Msingi na Vyama vya Ushirika, vimekuwa vikidhulumu sana wakulima wetu. Kwa hiyo inawezekana kabisa Wakulima hawa wamekata tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasababau ya makusudi sana kwamba nchi yetu tufikie kipato cha kati, lakini naomba niishauri Wizara, tukitegemea mvua za masika kwa kweli hatutafika. Ipo sababu ya msingi kabisa Serikali ikaona umuhimu wa kuweka kipaumbele katika kilimo cha umwagiliaji kwa sababu tukitegemea tu mvua za msimu mwisho wa siku tutakuja kukwama, kwa sababu tunaona kuna kipindi mvua za msimu zinakuwa ni nyingi sana, kuna kipindi zinakuwa ni chache. Ningeomba niishauri Serikali iweke mkakati wa muda mrefu wa kuhifadhi maji ya mvua ili mwisho wa siku tuweze kukajikite zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni budi sasa nchi yetu ikajitahidi kupata wataalamu wengi zaidi na kujifunza kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa wenzetu ambao wameweza kufanikiwa katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano; wenzetu wa Israel wamefikia hatua nzuri, wenzetu wa Indonesia, wenzetu wa China na maeneo mengine duniani ambayo sikuyabainisha. Hebu Serikali yetu ifanye dhamira ya dhati kwa kuwapeleka wataalam wengi zaidi ili kusudi na sisi tuweze kujikita katika hili suala la kilimo cha umwagiliaji. Mwaka huu katika kilimo kumekuwa kuna shida sana hasa kwenye maeneo yale ambayo yanayolima mtama, maeneo ambayo yana uhaba wa mvua. Ni kwamba kumekuwa na ndege wengi sana ambao wamekuwa wakiharibu mazao, lakini kwa masikitiko makubwa sana, nchi yetu haina ndege ya kuweza kunyunyiza dawa. Ninaunga mkono mpango wa Serikali wa kununua ndege kwa ajili ya abiria, lakini hebu tuone kwamba je, kwa nini Serikali isifikirie zaidi kwa kununua ndege ambayo itasaidia kunyunyiza dawa kwenye yale maeneo ambayo watakuwa wanahitaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea zaidi kujikita kwenye suala la kilimo. Tumeona kwamba kwenye bajeti ya kilimo ni asilimia 4.9 ya bajeti, lakini bajeti hii bado ilikuwa haijafikia hata nusu ya lile Azimio la Maputo la mwaka 2003. Je, tujiulize, hivi ni kweli kabisa tunavyosema kwamba tunataka tufikie hatua ya kati na tunategemea mali ghafi kutoka kwa wakulima, kwa asilimia 4.9 ya bajeti yote, kweli tutafikia hilo lengo? Mimi naomba Serikali ione kwamba hili jambo inabidi tujipange upya kuhakikisha kwamba angalau bajeti ya kilimo nayo inafikia zaidi ya nusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwenye pembejeo hasa matrekta, kulikuwa na matrekta ambayo yalitolewa kwa wananchi wakakopeshwa. Labda tu mimi nipate ufahamu, yale matrekta yaliyokopeshwa, wale wananchi waliokopa, je, wamerudisha kwa utaratibu mzuri? Je, ni muendelezo gani ambao unafanyika kuwe kuna revolving kwamba wale ambao waliokopeshwa yale matrekta wanayarudisha na wananchi wengine zaidi wanafaidika kupata yale matrekta. Isiwe utaratibu kwamba watu wakiona kwa sababu matrekta haya ni ya Serikali basi mtu akichukua halipi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kufahamishwa pia, je ni wananchi wangapi ambao pia wameendelea kufaidika baada ya wale wa mwanzo kuchukua mkopo huo? (Makofi)
Naomba pia nizungumzie suala la mifugo. Inasemekana kwamba miongoni mwa nchi ambazo zina mifugo mingi Tanzania pia ni mojawapo, lakini bado sekta ya mifugo haijaleta tija sana kwenye Pato la Taifa. Kwa hiyo naomba niishauri Wizara na nimshauri Waziri kwamba hebu katika bajeti kwa ajili ya ujenzi wa majosho, majosho kwa kweli bado yako katika hali mbaya sana, pamoja na dawa kwa ajili ya mifugo kwa sababu kama kweli tunasema kwamba tunataka tuanzishe viwanda vya kusindika na viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vya nyama, sasa kama tukiwa na mifugo ambayo hali yake ni dhoofu kweli hivyo vya kusindika tutaweza kuvipata? (Makofi)
Naomba nishauri kwamba hebu tuone kwamba lazima suala la majosho liangaliwe upya lakini pia kuna baadhi ya yale mashamba ambayo yalitelekezwa kabisa, mashamba ya mifugo. Mashamba yale yamevamiwa na wananchi na mengine yameachwa zaidi ya miaka 22. Hebu tuone Serikali iwe na nia ya dhati ya kufufua mashamba yale ili kusudi sasa kama kweli tunataka kupata hivyo viwanda vya kusindika tuweze kuvipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wamezungumzia sana kuhusu suala la afya na mimi pia naomba nizungumze. Katika bajeti yetu, Wizara ya Afya imetengewa asilimia 9.2 ambayo vilevile haijafikia lile Azimio letu la Abuja, Serikali ivute soksi kuhakikisha kwamba angalau tunafikia asilimia ile ili kuboresha afya za wananchi wetu. Kwa kweli inabidi Serikali ijipange zaidi, kwani tunapozungmzia afya, kama mtu asipokuwa na afya bora maana yake elimu haitakuwa bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim M. Majaliwa, kuhusu hatuba ya Bajeti aliyoiwasilisha Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika kipindi cha mwaka mmoja wa Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mengi yamefanyika. Nampongeza sana juhudi zinazofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais kuhakikisha Serikali inahamia Dodoma. Bado napenda kukumbusha sheria ya kuhamia Dodoma haijapitishwa katika Bunge lako Tukufu. Je nini kinasababisha ucheleweshaji wa utungaji wa Sheria
hii. Pamoja na nia nzuri ya Serikali kuhakikisha Dodoma inakuwa Makao Makuu, kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali mfano Nkuhungu Centre, Kiwanja. P. 639 wanalalamika pamoja na kulipia viwanja vyao lakini wengine wamenyang’anywa kwa madai wameshindwa kuviendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaweza kuleta mgogoro mkubwa sana kati ya Serikali na wananchi, hata kama kuna baadhi ya wananchi wameshindwa kuendeleza maeneo ni vema wakapewa taarifa ili ithibitike mapema isiwe Serikali inapokea pesa ya kodi na baadhi ya wananchi
wanazo slip za Bank ambazo wamekuwa wanazilipia kodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kuwa Serikali hii ni sikivu ni vema kufuatilia kwa ukaribu jambo hili ili kupata ukweli. Pia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu hayo inatakiwa itende haki kwa wale wote waliovamia maeneo, hali kadhalika Kamati za Makazi nazo zifuatiliwe kwani kuna baadhi ya Wanakamati hao wanafanya udanganyifu wa kuuza maeneo bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Serikali suala la ukusanyaji mapato unaofanywa na TRA, lakini mamlaka inabidi itumie mbinu mbadala ili ulipaji kodi uwe hiyari na wananchi waone ulipaji kodi ni wajibu wa kila Mtanzania. Kwani mtindo unaotumika wa kutumia maaskari na mabunduki mengi inaleta hofu. Ushauri wangu elimu ya mlipa kodi au ulipaji kodi ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi katika masuala yote ya kijamii, elimu, afya, miundombinu, kilimo na ufugaji ni kwa maendeleo ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuweka dhamira ya dhati katika kuendeleza kilimo cha biashara, pamoja na kuzalisha mbegu za nafaka ni budi pia kilimo cha biashara cha mbogamboga ambacho kimeanza kuwa na tija na kikitiliwa mkazo kitasaidia kupunguza
umaskini kwani kilimo cha mbogamboga mfano matikiti maji, matango, carrots, hoho, vitunguu, nyanya na mboga zingine zinaweza kuongeza pato la Taifa, iwapo Taifa litaweka mkazo na kufanya tafiti zaidi na kuzalisha mbegu za mbogamboga. Ili zizalishwe kwa wingi, kwa bei nafuu ili ikiwezekana mazao ya mbogamboga yaweze kuzalishwa kwa wingi na hatimaye kusafirisha nchi mbalimbali duniani. Kwani uhitaji wa mazao ya mbogamboga ni mkubwa sana na una tija kwa wazalishaji mazao hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukame na njaa, pamoja na wadudu waharibifu nalo ni jambo la kuliangalia kwa jicho tofauti. Kutegemea mvua katika kilimo bado kunasababisha njaa, kwani mvua hazitoshelezi kutokana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni budi Serikali ijikita katika kilimo cha umwagiliaji na pia uvunaji maji ya mvua ili yatumike kumwagilia kipindi cha kiangazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya maeneo ikiwemo kanda ya Kati, Mikoa ya Dodoma na Singida, pia baadhi ya mikoa inayolima mazao ya mtama, mfano Shinyanga kumekuwa na tatizo la ndege waharibifu ushauri wangu Serikali ifanye utaratibu wa kupata ndege yake ili inapotokea uharibifu wa ndege iwe rahisi kutekelezwa kwa haraka kuliko kusubiri ndege ya kutoka Nairobi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa vita dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Bado mkazo utiliwe na Serikali kutoa elimu kwa jamii waone ubaya wa rushwa, pia kwa vijana kujihusisha na madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujenga uchumi na viwanda na kuimarisha viwanda vyetu bado naendelea kushauri, wananchi wa Tanzania wahamasishwe kuzalisha malighafi kwa ajili ya kuhudumia viwanda. Kwani tukiwa na viwanda halafu malighafi ikaletwa kutoka nje haitakuwa na maana. Ni budi Serikali ikaweka mkakati wa makusudi ili kuhakikisha malighafi zaidi zinazalishwa nchini ili ziweze kukidhi mahitaji ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza ujenzi wa miundombinu vijijini unaotekelezwa na kampuni ya Viettel, je, ni ofisi ngapi za Wakuu wa Wilaya zimepatiwa miundombinu ya mitandao ya Internet nauliza jambo hili kwa sababu baadhi ya Ofisi za Wakuu wa Wilaya hazina huduma
za Internet. Nahitimisha kwa kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa nami nichangie katika hii Miswada miwili ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba moja kwa moja nijielekeze kwenye Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya mwaka 2016, nianzie pale katika Kifungu cha pili (2) ambacho kinatoa tafsiri ya maneno yatakayotumika katika Sheria hii. Naomba ninukuu ukurasa wa 36 kwenye tafsiri ya maneno ya Chama cha Wakulima ambayo inasema kwamba maana yake ni Chama ambacho kimesajiliwa na mamlaka husika na kilichoanzishwa na watu wanaojihusisha na uzalishaji, usindikaji au biashara ya mazao maalum ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri wangu hapa kwamba kwa nini ibainishe kwamba mazao maalum ya kilimo, hapa tungeweza tukasema kwamba ni mazao ya kilimo, lakini huko kutakuwa kuna vikundi vidogo vidogo kile chama kiwe ni umbrella organization. Naona kwamba tujaribu kuliona hili na kwamba libadilishwe hapa kwa sababu kama tukisema kwamba ni mazao maalum ya kilimo ina maana kwamba itabidi yabainishwe, kama ni ufuta ubainishwe kwamba ni ufuta, kama ni alizeti au chochote basi tubainishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichangie katika Kifungu cha 18(4) naomba ninukuu, kimesema: “Endapo ugunduzi, uvumbuzi au ubunifu ni mali ya taasisi chini ya Kifungu cha (1), Taasisi inaweza, (a), (b), (c) kwamba kutoa tuzo kwa mtu yeyote aliyehusika na ugunduzi, uvumbuzi au ubunifu huu inaendelea mpaka (c).”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba badala ya kusema kwamba hii taasisi inaweza litumike neno, ilazimike, kwamba iwapo ugunduzi au uvumbuzi au ubunifu ambao uko chini ya kifungu hiki, taasisi inalazimika kutoa tuzo, kwa sababu tukisema kwamba inaweza, ina maana kwamba hapa ni optional, kwa hiyo inawezekana kabisa kwamba mhusika katika taasisi hii anaweza asiitoe ile tuzo iwapo hata kama yule mtafiti anastahiki kupewa hiyo tuzo. Kwa hiyo, huo ulikuwa ni ushauri wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba nitoe pongezi zangu kwa Kifungu cha 24(1) na (2) ambapo sheria hii imebainisha kwamba lazima Mtafiti ambaye atatoka nje ashirikiane na Mtafiti wa kutoka Tanzania, ndani ya nchi. Kwa kweli nipongeze sana jambo hili na hili nadhani lingetumika kwa baadhi ya sheria zetu za nchi hii. Hata Sheria ya Uwekezaji na sheria zingine kwamba Watanzania wangekuwa wanashiriki au ni lazima washirikiane na wawekezaji, hili naomba niipongeze sana Wizara, hii itasaidia sana kuwapa weledi watafiti wetu na hivyo wajione kwamba wanakubalika na wanaaminika katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kutoa mapendekezo ni kwamba katika Kifungu cha 35 ambacho kinazungumzia masuala ya rufaa, naona kwamba pale kifungu kidogo cha (1), (2) na (3) cha Muswada huu ambacho kinapendekeza kwamba Waziri peke yake ndiye awe na mamlaka ya kumaliza ile rufaa. Nashauri ingewezekana kwamba hata Mahakama kwa sababu Waziri ni binadamu na yeye, kwa kuwa ni binadamu inawezekana kabisa kuna vitu vingine na yeye anaweza akakosea, nashauri kwamba kwenye suala la rufaa ingekwenda zaidi kwenye Mahakama nayo ipewe mamlaka ya kutoa rufaa kwa mtu ambaye atahitaji kupata rufaa hiyo badala ya kuwa Waziri peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kupendekeza kwenye Kifungu cha 36 Kifungu (1), (2) pia nikiangalia zile herufi kuanzia (a) mpaka (m) kwamba, kwa kuwa Muswada umependekeza Kifungu kitekelezwe kupitia Kanuni zitakazotungwa na Waziri, nashauri pale kuna maneno yameandikwa katika Muswada huu Kifungu 36 kwamba Waziri anaweza kutunga Kanuni kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa masharti ya sheria hii. Naomba nishauri kwamba hapa siyo lazima Waziri aweze, hapana, nashauri iwe Waziri inabidi alazimike kutunga Kanuni hizi kwa sababu kama tukimpa option ina maana kwamba inawezekana asitunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haya machache niliyoyaona, nikaona na mimi nitoe ushauri wangu otherwise nawapongeza sana. Naunga mkono hoja.