Primary Questions from Hon. Fatma Hassan Toufiq (26 total)
MHE. FATUMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Ujenzi wa Maternity Complex katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ulianza tangu mwaka 2009 ambapo majengo hayo yana uwezo wa kuweka vitanda 180, lakini hadi leo jengo hilo halijakamilika kutokana na Serikali kuamua kuimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto kwa kuzingatia vipaumbele vya Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa kutekeleza Matokeo Makubwa Sasa kwa kuiangalia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa jicho la pekee kwa kuipatia fedha ili jengo hilo likamilike haraka ili kuwaondolea adha kubwa wanayopata akinamama wakati wa uzazi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imelipa kipaumbele suala la kupunguza vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na uzazi kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi salama katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Wizara ilifanya tathmini na kubaini mikoa ambayo ina idadi kubwa ya vifo vya akinamama na watoto vinavyotokana na uzazi na kuanza kutekeleza Mradi wa Kuharakisha Kupunguza Kasi ya Vifo vya Akinamama Wajawazito Vinavyotokana na Uzazi (Strenthening Maternal Mortality Reduction Program (SMMRP). Mikoa hiyo ni Mtwara, Tabora na Mara. Serikali imefanya jitihada kubwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi salama katika mikoa hiyo kwa kujenga na kukarabati vyumba vya upasuaji, majengo ya huduma za afya ya mama na mtoto na nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mkoa wa Dodoma, Serikali kupitia Ofisi ya Rais (TAMISEMI), inakamilisha ujenzi wa Martenity Complex katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Kazi hii iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mifumo ya maji yaani plumbing system, kupaka rangi kuta na kazi ndogo za nje ya jengo hilo yaani external works na ununuzi wa samani. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, itashirikiana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani kupata huduma bora za uzazi salama.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Baadhi ya sheria ikiwemo Sheria ya Mirathi ya Kimila, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 pamoja na Sheria ya Hali za Watu zimekuwa na mapungufu makubwa na hivyo kuhitaji kutazamwa upya ili kufanyiwa marekebisho:-
Je, Serikali ina nia gani ya dhati ya kuwasadia wanawake na watoto wa kike kwa kuzifanyia marekebisho sheria hizo kandamizi na za kibaguzi hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa na ya kikanda juu ya masuala ya kuondoa ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina nia ya dhati kabisa ya kizifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa na zile zinazosimamia mirathi na urithi. Katika kutekeleza nia hiyo, mwaka 2008 Wizara iliandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wenye mapendekezo ya kufanya marekebisho katika Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na mapendekezo ya kutunga Sheria mpya ya Mirathi na Urithi. Baraza la Mawaziri ililiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kuandaa Waraka Maalumu wa Serikali (White Paper) kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi wengi iwezekanavyo kuhusu sheria hizo mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia agizo hilo, Wizara iliandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu kukusanya maoni ya wananchi juu ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kutungwa kwa Sheria mpya ya Mirathi na Urithi. Waraka huo ulifikishwa katika Baraza la Mawaziri mwezi Machi, 2010. Pamoja na kubainisha hoja ambazo wananchi wangetakiwa kuzitolea maoni, Waraka huo pia uliainisha utaratibu wa kukusanya maoni ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Disemba, 2010 kabla ya Waraka huo haujajadiliwa na Baraza la Mawaziri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliridhia kuanza kwa mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na aliahidi kuunda Tume itakayokuwa na majukumu ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya Mabadiliko ya Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza azma ya Rais, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ambayo ilisainiwa na Rais tarehe 29 Novemba, 2011. Sheria hii ndiyo iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mchakato wa kuandaa Waraka Maalumu wa Serikali (White Paper) kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na mapendekezo ya kutungwa Sheria mpya ya Mirathi na Urithi ulisitishwa kwa muda. Serikali ilikuwa na matarajio kuwa wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba huenda wananchi vilevile wangetoa maoni yanayohusu Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi na Urithi.
Baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake imebainika kwamba maoni ya wananchi hayakujielekeza kwenye maudhui ya Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi na Urithi kama ilivyotarajiwa. Hivyo basi, Wizara ya Katiba na Sheria imeamua kuendeleza juhudi zake za awali kwa kukamilisha taratibu kuhusu kupata maoni ya wananchi juu ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kutungwa kwa Sheria mpya ya Mirathi na Urithi.
Suala la Makao Makuu ya Serikali kuhamia Dodoma kwa muda mrefu limekuwa na kigugumizi na Ofisi za Wizara nyingi bado hazijahamia Dodoma, kutokana na kutokuwepo Sheria inayotamka kuwa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi.
Je, ni lini Sheria hiyo itatungwa ili kuwezesha mchakato huo wa kuhamia Dodoma?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeishaanza mchakato wa kutunga Sheria ya Makao Makuu ya Nchi. Tayari Waraka wa Baraza la Mawaziri wa kutunga Sheria hiyo umekamilika, na sasa unasubiri kupangiwa tarehe ya kujadiliwa katika kikao cha wataalam cha Makatibu Wakuu (IMTC) na kisha kuwasilishwa ngazi ya Baraza la Mawaziri kwa uamuzi na hatimaye kuandaliwa Muswada wa Sheria, utakaowekwa Bungeni kujadiliwa na kupitishwa na Bunge kuwa sheria.
MHE. FATMA HASSAN TOUFIQ aliuliza:-
Sheria ya Kutambua Haki ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid) ambayo pia inawatambua wasaidizi wa kisheria (paralegals) mchakato wake umeanza tangu mwaka 2010 kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi zisizo za Kiserikali, lakini sheria hii imekuwa ni ya muda mrefu na sasa ni zaidi ya miaka sita bado haijatajwa wala kuletwa Bungeni.
Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha sheria hii inatungwa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha hatua zote za awali za kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria katika Bunge lako Tukufu. Muswada huo unalenga kuweka utaratibu wa kisheria wa kuratibu huduma ya msaada wa kisheria nchini na kuwatambua Wasaidizi wa Kisheria waliokidhi vigezo mahususi vya ujuzi katika utoaji huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali baada ya kutungwa kwa sheria hii ni kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inapatikana nchi nzima hususani kwa wananchi walio vijijini na ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za Mawakili ambao wengi wao wanaishi na kufanya shughuli za mijini tu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Tatizo la ukeketaji katika jamii nyingi nchini bado ni kubwa na sasa ukeketaji huo unafanywa kwa usiri mkubwa hasa baada ya jamii hizo kugundua kuwa ipo sheria dhidi ya ukeketaji.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufuatilia ukatili huu wanaofanyiwa watoto wachanga na kuhatarisha maisha yao?
(b)Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru watoto wachanga dhidi ya ukatili huu wa ukeketaji unaofanywa na baadhi ya jamii nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, (a) Serikali katika kufuatilia ukatili wa watoto wachanga imekuwa na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamona na kuwa na vikundi vya uelimishaji kupitia mangariba, kuanzisha madawati zaidi ya 417 ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi, kuanzisha mtandao wa huduma ya mawasiliano ya kusaidia watoto namba 116 (child helpline) pamoja na uanzishwaji wa timu za ulinzi wa mtoto katika Halmashauri mbalimbali ili kukabili tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuongeza msukumo zadi katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuachana na mila zilizopitwa na wakati pamoja na ufuatiliaji kupitia wauguzi toka mtoto alipozaliwa hadi anapotoka hospitalini.
Mheshimiwa Spika, (b), Serikali inaendelea na mkakati wa kutoa elimu ya uzazi salama kwa wakunga wa jadi, akina mama na wauguzi katika zahanati na vituo vya afya kubaini na kutoa taarifa kuhusu mtoto aliyekeketwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mzazi huyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, mikataba ya kimataifa na ya kanda kuhusu haki na ustawi wa mtoto na Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009; na pia kutekeleza Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012, kifungu cha 169(1)(a) pamoja na Mpango wa Taifa wa Mwitikio na Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto wa mwaka 2013 hadi 2016.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeandaa mpango kazi wa Taifa wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaoanza mwaka 2017 hadi mwaka 2022 utakaozinduliwa Novemba, 2016, ambapo masuala ya ukatili hasa utokomezaji wa mila na desturi zinazopelekea ukeketaji zitashughulikiwa ipasavyo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Baadhi ya nchi za Afrika kama Uganda na Zimbabwe zimejenga viwanda vyao kwa ajili ya kutengeneza dawa za kupunguza makali ya VVU (Generic za HIV) na hivyo kupunguza gharama za kusaidiwa dawa hizo ambazo zinabadilishwa kila baada ya miaka kadhaa na hivyo
kutengeneza usugu kwa baadhi ya magonjwa.
(a) Je, Serikali ina mpango wowote wa kujenga kiwanda cha kutengeneza ARVs za watu wazima pamoja na watoto?
(b) Kwa dawa zinazoletwa hapa nchini, je, kuna ARVs za watoto?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama
ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahamasisha mashirika, taasisi, wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha dawa mbalimbali zikiwemo dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kuna kiwanda kimoja Mkoani Arusha TPI ARV Limited ambacho kimepewa leseni ya kutengeneza ARVs. Kiwanda hicho bado hakijaanza uzalishaji. Wizara inatarajia kuwa kiwanda hicho kitaanza uzalishaji wa ARVs hivi karibuni.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa za ARV zinazoingizwa nchini, kuna dawa za watoto ambazo ni pamoja na Nevirapine Syrup, Lopinavir/Ritonavir Syrup, dawa nyingine ni pamoja na mchanganyiko wa dawa za vidonge mfano Lamivudine/Atazanavir zenye nguvu ya miligaramu 30 na miligramu 60 pamoja na Lamivudine zenye nguvu ya miligramu 30 na miligramu 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote kwa ujumla kwamba nchi yetu haina tatizo la upungufu wa dawa za ARV kwa watoto.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Katika miaka ya 70 kulikuwa na Community Centres ambapo wananchi wa rika tofauti walikuwa wakikutana na kubadilishana mawazo na maeneo hayo yalikuwa ya muhimu kupata huduma za jamii kama afya ya akili, wananchi wenye msongo wa mawazo, ugonjwa wa kisukari, kifafa, pumu na shinikizo la damu:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurejesha Community Centres?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa siku hii ya leo, lakini namshukuru vilevile Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu. Niwashukuru pia wananchi wa Kigamboni kwa kuendelea kuwa na imani nami kama mtumishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali Namba 72 la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na pia namuunga mkono Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri kuhusiana na suala zima la kurejesha majumba ya maendeleo na umuhimu wake ulionekana hapo awali katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa dhumuni la kuwapatia wananchi taarifa mbalimbali, maarifa, burudani, lakini pia stadi za maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mapendekezo yaliyotolewa na Wizara yangu ya kuimarisha sekta ya maendeleo ya jamii ya mwaka 2007, pamoja na mambo mengine yaliyopendekezwa suala la kuyafufua majengo ya maendeleo na kuyarejesha katika matumizi yake ya awali lilitiliwa mkazo. Hata hivyo, Halmashauri 135 ndizo zilizokuwa na majumba ya maendeleo yaliyojengwa mwaka 1961 na mwaka 1962. Zipo Halmashauri zimerejesha matumizi ya awali ya majumba hayo, ikiwa ni pamoja na Iringa Manispaa, Dodoma Manispaa na Mpwapwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo Halmashauri ambazo zimebadilisha matumizi ya majengo haya na hayawezi yakarudishwa katika matumizi ya awali. Kwa mfano, Manispaa ya Temeke imekuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Mtwara imeendelezwa na kuwa Ofisi ya Ardhi na Maendeleo ya Jamii na Manispaa ya Ilala imeendelezwa na kuwa Ofisi za Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara yangu imekuwa ikifanya mawasiliano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI mara kwa mara, juu ya kukumbusha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kurejesha matumizi ya majengo ya maendeleo kwa lengo la kutumika kama sehemu ya kujadili masuala ya maendeleo, kupata taarifa mbalimbali, burudani na stadi za maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuwa, hili ni jukumu la kila Halmashauri, hivyo niwaombe tunapokutana katika vikao vyetu kujadili mipango mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri zetu, basi tulisisitize suala hili muhimu na lipewe uzito unaostahili ili kulitekeleza kwa vitendo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Mheshimiwa Rais amesisitiza sana kuhusu Tanzania ya Viwanda na katika Mkoa wa Dodoma kulikuwa na Kiwanda cha Kutengeneza Mvinyo (DOWICO) ambacho kilikuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima wa zabibu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua kiwanda hicho ili kufanya wakulima wapate tija kwa kuuza zabibu zao kiwandani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU - K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mhehsimiwa Fatma Hassan Taufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Dodoma Wine Company Limited (DOWICO) cha hapa Mjini Dodoma kinamilikiwa na Bw. Thakker Singh aliyeuziwa kwa njia ya ufilisi mwaka 1993. Kwa sasa kiwanda hiki kimefungwa tofauti na matarajio ya wakati kinabinafsishwa. Mpango wa Serikali ni kukifufua kiwanda hiki na vingine vilivyofungwa, pia kuendeleza vilivyopo na kujenga viwanda vipya hasa vinavyotumia malighafi za ndani na kuajiri watu wengi kama Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021 unavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kufuata Mpango huo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina tunashauriana na wawekezaji mbalimbali namna ya kuvifufua viwanda vilivyofungwa na ikibidi kuwapa wawekezaji wengine ili wavifufue na kuviendeleza viwanda hivyo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba, Mwekezaji wa Kiwanda cha DOWICO ameingia mkataba na mmiliki wa Kiwanda cha SETAWICO kilichopo Hombolo kwa makubaliano ya kukifufua na kazi hii imeanza kwa kufanya ukarabati. Ni matumaini ya Serikali kuwa kazi ya ukarabati na usimikaji wa baadhi ya mashine utafanyika na kukamilika mapema.
Wizara yangu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tunaendelea kufuatilia ukarabati wa kiwanda hiki kwa karibu ili kuhakikisha uzalishaji unaanza na kukiwezesha kuchangia katika uchumi wa Taifa hasa kutoa ajira kwa vijana na kuwa soko la zabibu ya wakulima hapa mkoani Dodoma.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Imebainika kuwa baadhi ya Madereva wa bodaboda wamekuwa wakifanya ukatili kwa kufanya ubakaji, ulawiti na kuwapa baadhi ya wanafunzi mimba:-
a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti hali hii hasa kwa wale bodaboda wanaowahadaa baadhi ya wanafunzi wa kike?
b) Je, ni wanafunzi wangapi walioripotiwa kupewa mimba na waendesha bodaboda katika kipindi cha miaka mitatu (3) iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa kuna wanaume wanaojihusisha na vitendo vya ubakaji, ulawiti na kuwapa mimba baadhi ya wanafunzi. Baadhi ya Madereva wa bodaboda wameripotiwa kujihusisha na vitendo hivyo viovu, vitendo hivyo hutokana na tabia mbaya, vishawishi na changamoto za mazingira kama vile umbali kutoka nyumbani kwenda mashuleni kwa wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na vitendo hivyo mwaka 2016 Serikali ilifanya Marekebisho ya Sheria ya Elimu Na. 25 ya Mwaka 1978 ambapo mtu atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi akihukumiwa hufungwa miaka 30. Aidha, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16 inabainisha Hukumu ya kifungo cha maisha kwa mtu atakayetenda kosa la kubaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sheria hizo Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti vitendo hivyo kwa kutoa huduma za ushauri na unasihi ambapo shule zimeelekezwa kuwa na Walimu washauri wa kike na kiume. Hivyo, mwongozo wa ushauri na unasihi shuleni na vyuoni umeandaliwa. Vilevile Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea na ujenzi wa mabweni, hostel na shule katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi hupewa mimba na wanaume mbalimbali, wanaweza kuwa ni wakulima, wafugaji, wafanyakazi au wafanyabiashara wakiwemo Madereva bodaboda. Hata hivyo takwimu za wanafunzi waliyopata mimba hazikokotolewi kwa kuanisha makundi ya wanaume waliowapa ujauzito. Hivyo ni vigumu kupata idadi ya wanafunzi waliyopewa mimba na madereva wa bodaboda.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Baadhi ya wanawake wameathirika na vipodozi vikiwemo kucha na kope kubandika.
Je, ni wanawake wangapi wameathirika macho kutokana na matumizi ya kope bandia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa kucha za kubandika na kope za kubadnika siyo vipodozi. Kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura ya 219 inayosimamiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kipodozo ni kitu chochote kinachotumika kwenye mwili au sehemu ya mwili kwa njia ya kupaka, kumimina, kufukiza, kunyunyiza au kupuliza kwa ajili ya kusafisha, kuremba, kupamba, kuongeza uzuri, mvuto au kubadili muonekano. Takribani wagonjwa 700 kwa mwaka hupokelewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili…
Mheshimiwa Spika, takribani wagonjwa 700 kwa mwaka hupokelewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa na matatizo ya ngozi yanayotokana na kumeza vidonge vinavyobadili rangi ya mwili mzima pamoja na vipodozi vyenye kemikali. Imeelezwa kuwa watu hao wapo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani na magonjwa ya ngozi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Wizara kupitia TFDA haina utaratibu wa kudhibiti kope wala kucha za kubandika kwa sababu hakuna sheria inayoipa mamlaka ya kudhibiti bidhaa hizo. Hivyo basi, kutokana na hilo, Wizara kwa kupitia TFDA haina takwimu za kuonesha madhara yanayotokana na matumizi ya bidhaa hizo kwa kuwa hakuna mfumo wa kupokea taarifa za matumizi ya bidhaa husika.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Kutokana na ugumu wa maisha na mabadiliko ya mtindo wa kuishi, baadhi ya wananchi wamekata tamaa ya kuishi.
(a) Je, Serikali ina utaratibu gani wa kutoa elimu ya unasihi kwa wale wanaohitaji?
(b) Je, ni vyuo vingapi hapa nchini vinatoa wataalam wa elimu ya unasihi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto mbalimbali za maisha zinazowakabili watu na kuwasababishia msongo wa mawazo. Changamoto hizo ni pamoja na hali ya umasikini, magonjwa, migogoro ya kifamilia, kujihusisha na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na ulevi, ukatili na unyanyasaji wa kimwili, kijinsia na kisaikolojia. Aidha, Wizara inatambua umuhimu wa huduma za unasihi na msaada wa kisaikolojia na jamii katika kusaidia kuondokana na msongo wa mawazo. Kwa kuzingatia umuhimu wa huu wa huduma hiyo, Serikali huwatumia Maafisa Ustawi wa Jamii waliopo ili kutoa huduma hii.
Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya ugatuaji wa huduma za ustawi wa jamii kwenda katika Halmashauri ili kufikisha huduma za ustawi wa jamii ikiwemo unasihi karibu zaidi na wahitaji walio wengi. Katika ugatuaji huo jumla ya Maafisa Ustawi wa Jamii 731 tayari wameajiriwa katika halmashauri 185. Wizara itaendelea kuajiri Maafisa Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kadri bajeti itakavyoruhusu ili kuwa na wataalam wa kutosha katika eneo la huduma za unasihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vyuo 18 vinavyotoa elimu ya unasihi kati ya hivyo viwili ni vya umma na 16 ni vya binafsi. Taasisi ya Ustawi wa Jamii inatoa mafunzo ya fani ya ustawi wa jamii katika ngazi ya cheti, stashahada, shahada na shahada ya uzamili kwa lengo la kupata Maafisa Ustawi wa Jamii wenye utaalam wa kutoa huduma za unasihi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya wanafunzi 265 walidahiliwa katika ngazi zifuatazo; cheti 192, stashahada 216, shahada 189 na shahada ya uzamili 28. Katika mwaka wa masomo 2017/2018 jumla ya wanafunzi 607 walidahiliwa katika ngazi zifuatazo; cheti 186, stashahada 210, shahada 190 na shahada ya uzamili 21. Aidha, Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara kimeanza kutoa mafunzo ya wasaidizi wa ustawi wa jamii katika mwaka 2017/2018 ambapo jumla ya wanafunzi 225 wamedahiliwa katika ngazi za cheti 192, stashahada 216, shahada 189 na stashahada ya uzamili 28. Wanafunzi hawa baada ya kuhitimu watakuwa na jukumu la kutoa huduma za unasihi katika ngazi ya kata, vijiji na mitaa na katika vituo vya afya na zahanati.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha wanawake na watoto kuporwa mali zao na ndugu za waume zao ni kukosekana kwa wosia, jambo ambalo jamii haijaona umuhimu huo wakiamini kuwa kuandika wosia ni kujitakia kifo:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani endelevu wa kukabiliana na kadhia hii?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuielimisha jamii umuhimu wa kuandika wosia kama njia mojawapo ya kulikabili tatizo hili ambalo ni kubwa katika jamii?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuandika wosia kama njia mojawapo ya kukabiliana na migogoro katika jamii inayohusiana na mgao wa mali za marehemu. Kwa kutambua hilo, mwaka 2008, Wizara yangu kupitia Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) iilianzisha huduma ya kuandika na kuhifadhi wosia ikiwa ni pamoja na kuuelimisha umma kuhusiana na huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu wakati huo, Wizara yangu kupitia Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi inaendelea kubuni na kutekeleza mikataba ya aina mbalimbali ili kuhakikisha na kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuandika na kuhifadhi wosia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukitumia njia mbalimbali kutoa elimu ya kuandika wosia ikiwa ni pamoja na mikutano ya hadhara, redio, televisheni, vipeperushi, magazeti na mitandao ya kijamii. Pamoja na jitihada hiyo, mpaka sasa tumeweza kuandika na kuhifadhi wosia 578 kati ya hizo 32 tayari zimeshatumika. Hata hivyo, idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi kubwa ya Watanzania waliopo kwa sasa. Bado kuna changamoto ya uelewa kwa wananchi wengi juu ya umuhimu wa suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulithibitishia Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu itaendelea kubuni njia mbalimbali za kuelimisha jamii kuwa umuhimu wa kuandika wosia ikiwa ni jitihada mojawapo ya kukabiliana na migogoro ya mgao wa mali za marehemu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kutumia fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote kuchangia katika juhudi zinazofanywa na Serikali za kuhamasisha wananchi kujijengea tabia na utamaduni wa kuandika na kuhifadhi wosia sehemu maalum hadi utakapohitajika. Endapo wananchi watahamasika, tutakuwa tumeondokana na migogoro isiyo ya lazima na hivyo kuruhusu maendeleo ya ustawi wa jamii. Hii ni njia muhimu ya kulinda haki za wanawake na watoto waliofiwa ndani ya familia.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Ukatili dhidi ya wanawake na watoto bado unaendelea kwa kiwango kikubwa hapa nchini:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwahudumia kwa unasihi na unasaha wahanga wa ukatili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq (Viti Maalum) kutoka Mkoa wa Dodoma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini. Kwa kuliona hilo, Serikali iliandaa mpango kazi wa kitaifa wa miaka mitano wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao unatekelezwa kwa kipindi cha 2017/2018 na utaisha mwaka 2021/2022. Mpango mkakati huu unaainisha mikakati mbali mbali ya kupambana na kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha vituo 11 vya mkono kwa mkono (One Stop Centres) ambapo huduma za ushauri nasaha, huduma za kipolisi na huduma za matibabu zinapatikana katika eneo moja kwenye mikoa ya Dare es Salaam, Pwani, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Arusha, na Simiyu kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Katika vituo hivi huduma za kipolisi, ushauri nasaha na huduma za afya zinatolewa kwenye kituo kimoja. Lengo la Serikali ni kuwa na kituo angalau kimoja kwa kila Mkoa na hii inaenda pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu katika eneo la utoaji huduma husika.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Serikali imeanza kampeni ya kusajili watoto chini ya miaka mitano ili kupata vyeti vya kuzaliwa, lakini bado Watanzania wenye umri zaidi ya miaka mitano na kuendelea hawana vyeti vya kuzaliwa:-
Je, Serikali imejipangaje kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa Watanzania wenye umri zaidi ya miaka mitano na kuendelea?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imekuwa ikitekeleza Mkakati wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu ili kuboresha hali ya usajili nchini. Mkakati huo una mipango mbalimbali ambayo imekuwa ikitekelezwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Watanzania wote wenye umri wa zaidi ya miaka mitano wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya mipango hiyo ni kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wote waliopo kwenye mfumo rasmi wa elimu na kufanya kampeni za uhamasishaji kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ya makazi.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu wa kusajili watoto waliopo katika mfumo rasmi wa elimu umefanikiwa kusajili jumla ya watoto 325,583 wenye umri wa miaka mitano hadi 17 katika jumla ya wilaya kumi na tisa ambazo ni Njombe, Ludewa, Makete, Wanging’ombe, Ilala, Kinondoni, Kigamboni, Temeke, Iringa, Kilindi, Musoma, Bariadi, Tarime, Singida, Songea, Bunda, Maswa, Kahama na Manyoni. Wakala utaendelea na utaratibu huu ili kuhakikisha wilaya zote nchini kulingana na mpango uliopo.
Vilevile wakala umeendelea kuwafikia wananchi wasio katika mfumo rasmi wa elimu kupitia kampeni za maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na hasa kama vile maonesho ya Saba Saba na Nane Nane yanayofanyika nchini kwa kutoa elimu ya muhimu wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Usajilli, Ufilisi na Udhamini (RITA) unatarajia kuanzisha huduma ya usajili kwa njia ya mtandao ili kuwafikia wananchi wengi kwa urahisi ambapo wananchi wataweza kufanya maombi yao katika mfumo wa mtandao na baadaye kufika ofisi ya RITA iliyo karibu na hasa katika maeneo ambapo Serikali za Mitaa zipo.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Usajilli, Ufilisi na Udhamini (RITA) umejiwekea malengo ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi wapatao 15,917,602 ifikiapo mwaka 2025. Idadi hii itafanya wananchi wasio na vyeti vya kuzaliwa kupungua hadi kufika 21,508,277 ambao ni chini ya asilimia 50 ya wananchi wote ambao wamefikisha umri wa zaidi ya miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa wananchi wote ambao hawana vyeti vya kuzaliwa kufika kwenye Ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa ajili ya kusajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa ikiwa ni haki yao muhimu ya kutambuliwa. Kadhalika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuwaelimisha wananchi katika majimbo yenu juu ya umuhimu wa kusajili matukio muhimu ya binadamu ikiwa ni pamoja na kujisajili na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa. Ahsante.
MHE. FATMA H. TOUFIQ Aliuliza:-
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha kwamba asilimia saba ya Watanzania wanaishi vijijini lakini katika miaka ya hivi karibuni watu wengi hasa vijana, wanakimbilia mijini wakidai kuwa maisha ni magumu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza au kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 asilimia 70.4 ya Watanzania wanaishi vijijini. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 imeelekeza Serikali kuboresha na kukuza uchumi wa vijijini ili kuongeza tija ya uzaliashaji mali na kukuza uchumi katika maeneo hayo kwa lengo la kuongeza fursa zaidi za ajira kwa vijana. Katika kupunguza hali hii Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-
(i) Kuboresha miundombinu ya kiuchumi pamoja na huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa barabara za vijijini, ili kuwezesha wananchi waishio vijijini kusafirisha malighafi, hasa mazao, kupeleka sehemu zenye masoko, Mpango wa Umeme Vijijini kupitia REA, ujenzi wa miradi mikubwa inayotoa fursa za ajira kwa vijana kama miradi ya ujenzi wa reli, mradi wa uzalishaji umeme Stiegler’s Gorge na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za ugani.
(ii) Kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa SACCOS za vijana zilizoundwa katika Halmashauri ili kujenga mitaji yao kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mifuko mingine ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo katika mwaka 2017/2018 kiasi cha shilingi 783,280,000 kimetolewa kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
(iii) Kutekeleza programu ya ukuzaji ujuzi nchini kwa lengo la kuwapatia vijana ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, hususan vijijini. Mafunzo haya ni pamoja na mafunzo ya ufundi stadi kwa njia ya uanagenzi na urasimishaji wa ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu ambapo katika mwaka 2018/2019 jumla ya vijana 32,563 wamewezeshwa kupata mafunzo hayo katika fani mbalimbali.
(iv) Ni kuandaa na kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kuwezesha vijana kushiriki katika kilimo, hususan vijijini. Mkakati huu unalenga kuwawezesha vijana wa ngazi mbalimbali za elimu kushiriki kikamilifu katika kilimo na hivyo kuongeza fursa za vijana kupitia sekta ya kilimo vijijini.
Katika kutekeleza mkakati huu Serikali inaendesha mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa teknolojia ya kitalu nyumba kwa vijana na takribani vijana 18,800 wamepata mafunzo hayo katika Halmashauri zote.
(v) Kusimamia utekelezaji wa Azimio la Wakuu wa Mikoa mwezi Novemba, 2014 lililotoa maelekezo ya kila Halmashauri nchini kutenga maeneo ya vijana na kuyatumia kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali na biashara katika kila Halmashauri nchini.
(vi) Kutoa fursa za upendeleo kwa vikundi vya vijana wakiwemo wahitimu na wenye ulemavu ili kuwawezesha kupata fursa ya zabuni za Serikali kupitia sheria ya ununuzi wa umma.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Ndoa za utotoni ni tatizo kubwa katika jamii zetu hususan katika jamii zenye umaskini:-
Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa umma hasa katika maeneo ya vijijini ili wananchi wafahamu athari za kuozesha watoto katika umri mdogo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa umma katika kupambana na ndoa za utotoni ambazo zina madhara makubwa kwa watoto wa kike ambapo kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo TV, redio, magazeti na jarida imekuwa ikitoa elimu kwa umma kwa kuandaa ujumbe kuhusu madhara ya mimba za utotoni sambamba na kusisitiza wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kutoozesha watoto mapema. Aidha, mwaka 2017, Tarime Mkoani Mara, Serikali ilizindua kampeni ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ijulikanayo kama “Mimi Msichana Najitambua: Elimu Ndiyo Mpango Mzima”.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampeni hiyo ililenga kutoa elimu kwa watoto kuhusiana na mimba za utotoni na umuhimu wa kuelekeza muda wao mwingi katika elimu, kujitambua na kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki zao. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2018, jumla ya wananchi 13,234 walifikiwa na kampeni. Kati ya hao, wanafunzi 8,546, walimu 476, viongozi wa dini 110, wazee wa mila na wazee mashuhuri 90, ngariba 38, waendesha bodaboda 261, wazazi/walezi 3,600 na watendaji wa kijiji 113. Kampeni hii imefanyika katika Mikoa ya Shinyanga, Mara, Tabora, Lindi, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam na Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto. Sambamba na mpango huo, mwaka 2018, uliandaliwa Mdahalo wa Kitaifa ambao ulikuwa na lengo la kujadili vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo ndoa za utotoni. Mikoa yenye kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto ilijumuishwa katika utaratibu wa kuandaa Mpango wa Utekelezaji wa kampeni ambayo umeainisha jumbe za kipaumbele zitakazotumika na mikoa katika kuelimisha jamii katika mikoa husika kwa kuzingatia mazingira yao. Mikoa sita ilijumuishwa ikiwa ni pamoja na Shinyanga, Dodoma, Tabora, Mara, Katavi na Singida.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Elimu ya Afya ya Uzazi ni muhimu sana kwa vijana wa kike na kiume katika kuepuka mimba zisizo za lazima.
Je, Serikali imejipangaje kuwahabarisha vijana ili kupunguza mimba zinazozuilika?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeaandaa mitaala ya kuwafundishia watumishi wa afya pamoja na vijana kuhusu afya ya uzazi kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kujitambua hasa kuhusu hatua za makuzi wakati wa kubalehe na namna ya kuhimili mihemko ili wasijihusishe na masuala ya ngono katika umri mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo haya huwajengea weledi na stadi za maisha vijana wetu hivyo kuwasaidia kuzingatia masomo zaidi na kujipanga vizuri ili kufikia ndoto zao za maisha. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau, mwaka 2018 ilizindua Jukwaa la Vijana la SITETEREKI lenye maudhui mahususi ya kumuelimisha kijana awe na mtazamo chanya wenye kumuwezesha kupata taarifa na huduma muhimu za uhakika kuhusu afya ya Uzazi kwa Vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine ikiwemo Wizara ya Elimu pamoja na Wadau wa maendeleo imeandaa Agenda ya Kitaifa ya Afya kwa Vijana na Uwekezaji (NAIA) yenye afua mtambuka zinazowahusu vijana hasa wenye umri wa miaka 10 hadi 19. Ajenda hiyo ilikuwa izinduliwe mwezi Machi mwaka huu, lakini kutokana na tishio la ugonjwa unaotokana na virusi vya Corona zoezi hilo limeahirisha kwa muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeona ni vema kuileta mikakati yote inalenga vijana pamoja na kuitengenezea ajenda moja. Ajenda hii imejikita katika maeneo sita ambayo ni eneo la kwanza ni Kuzuia maambukizi ya VVU, eneo la pili ni kuzuia mimba za utotoni na utoro wa shule, eneo la tatu ni Kuzuia unyanyasaji wa jinsia, kimwili na kisaikolojia, eneo la nne ni kuboresha lishe ya vijana; eneo la tano ni kuhakikisha wavulana na wasichana wanabaki shuleni na eneo la sita ni kuwajengea stadi za maisha kupambana na mazingira yanayowazunguka, ni Imani yangu kuwa, tukitekeleza kwa ufanisi afua zilizomo kwenye nguzo hizi tutakuwa tumemwezesha kijana wa Kitanzania kupata elimu ya afya ya uzazi kwa kiasi kikubwa hivyo kuwafanya kuwa rasilimali muhimu katika kuujenga uchumi wa nchi na kuweza kufikia lengo letu la kuwa nchi yenye uchumi wa kati.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wataalam wa zao la zabibu Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya 100 na wengine 68 kuhamia TARI kutoka Wizarani wakiwemo Maafisa Kilimo ambao watapelekwa katika vituo vya utafiti ikiwemo Kituo cha Uendelezaji wa Zao la Zabibu TARI Makutupora. Mkakati uliopo ni kuwajengea uwezo wa kutosha wataalamu waliopo kwa kuwapatia mafunzo mahsusi ya kilimo cha zabibu na kujifunza teknolojia mpya za kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la zabibu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Je, kuna wahanga wangapi wa vitendo vya ukatili nchini kuanzia mwaka 2019 hadi 2022?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za matukio ya vitendo vya ukatili nchini vilivyoripotiwa kwenye Vituo vya Polisi kuanzia mwaka 2019 hadi Machi, 2022 ni 27,838 kwa mchanganuo ufuatao: -
Matukio ya kubaka ni 19,726; kulawiti ni 3,260 ambao kati ya hao wanaume ni 3,077 na wanawake ni 183; kuunguzwa kwa moto ni 198 kati ya hao wanaume ni 73 na wanawake ni 125; kutupa watoto wachanga ni 443 kati yao wanaume ni 177 na wanawake ni 266; kipigo ni 4,211 ambao kati ya hao wanaume ni 16 na wanawake ni 4,195.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya kesi zilizofikishwa Mahakamani ni 21,063 na watuhumiwa ambao wamehukumiwa 14,278. Mashauri mengine yako kwenye hatua mbalimbali za upelelezi pamoja na Mahakamani. Aidha, Serikali inaendela kuiasa jamii kutumia vema taasisi za familia kaya, jumuiya za kidini kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa ili kudhibiti vitendo vya ukatili katika jamii.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuzuia matukio ya mauaji, kujiua na ukatili uliokithiri hasa kwa wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kuwakamata watu wote wanaotenda makosa yakiwemo ya mauaji na ukatili na kuwafikisha Mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaonesha kuwa matukio haya kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na watu kujichukulia sheria mkononi, imani za ushirikina, wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, migogoro kwenye ndoa, kugombania mirathi, ulevi na mmomonyoko wa maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kutekeleza mkakati wa kutoa elimu na mafunzo kwa jamii ili wananchi wafuate sheria za nchi katika kutatua migogoro inayojitokeza au wanapodai haki zao. Aidha, wananchi wanaombwa kuwashirikisha viongozi wa kijamii, kimila, kisiasa na kiserikali, wazee au watu maarufu wanaotambulika na kuheshimika ili kuwaasa ipasavyo na hivyo kuepuka kuvunja sheria za nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mafuta ya kula yanazalishwa kwa wingi nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza mkakati wa kuendeleza Sekta Ndogo ya Alizeti na Chikichi ambayo ndiyo mazao makubwa yanayoweza kuzalisha kwa tija mafuta ya kula hapa nchini kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa mkakati huo, viwanda vipya, kama Qstec na Jeolong vimeanzishwa. Upanuzi wa viwanda kama Mount Meru Millers, lakini pia, Serikali imeongeza nguvu katika taasisi za utafiti wa mbegu na hivyo kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za alizeti na michikichi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaelekeza nguvu zaidi kwenye kilimo cha kuzalisha mbegu bora, ili kukidhi mahitaji ya malighafi katika viwanda vyetu vya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatunga Sheria ya Uanzishwaji wa Baraza la Taaluma kwa Kada ya Ustawi wa Jamii?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na Uandaaji wa Sheria ya Taaluma ya Ustawi wa Jamii kwa kujumuisha maoni ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na ya wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Chama cha Wataalam wa Ustawi wa Jamii Tanzania na itakapokamilika Muswada wa Sheria utawasilishwa Bungeni.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa waajiri wanaowanyima safari watumishi wanaonyonyesha kwa kigezo cha kutumia fedha nyingi kujikimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 aya ya 5(1) ikisomwa pamoja na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 zinaelekeza watumishi wanaosafiri safari za kikazi wakiwemo wanaonyonyesha kupewe posho ya kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, Serikali inaelekeza tena na kusisitiza kwa waajiri wote wa watumishi wa umma kuwa watumishi wa umma wahudumiwe kwa usawa na haki kwa kuzingatia sera na kanuni zilizopo. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa treni ya mwendokasi kutoka Kaliua-Mpanda hadi Karema?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa njia ya reli ya Kaliua – Mpanda – Karema kwa kiwango cha Standard Gauge. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa reli hii.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Je, ni Wanawake wangapi wanaomiliki Migodi ya Madini nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima, kabla sijajibu hili swali, naomba sekunde 30 tu niweze kutoa pole kwa wananchi wangu wa Jimbo la Longido wanaoishi katika Tarafa ya Enduimet, Kata ya Olmolok ambao Shule yao ya Sekondari ya Enduimet iliungua moto jana na watoto wa kike 345 sasa hawana makazi na hawana chochote. Nawahakikishia kwamba, ninashirikiana na Serikali yetu sikivu kuanzia ngazi ya Wilaya na Mkoa, tutahakikisha huduma hizo muhimu za kupata mablanketi, vitanda na magodoro zinafanyiwa kazi ili waendelee kusoma kwa amani katika shule hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pole hizo sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, shughuli za madini zimekuwa zikifanyika kupitia watu binafsi na kampuni ambazo ndani yake kuna wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ilibainika kuwa, nchini kuna takribani wanawake milioni tatu wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa madini.
Mheshimiwa Spika, tafiti ndogo iliyofanywa na TAWOMA kwa kushirikiana na Shirika letu la STAMICO kwa wanawake 992 katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu, ilibainika kuwa, wanawake 17 sawa na asilimia 1.7 wanamiliki migodi, wanawake 67 sawa na asilimia 6.8 wanamiliki maeneo ya uchimbaji. Yaani maduara katika leseni za uchimbaji madini na wanawake 855 sawa na asilimia 86.2 wanajishughulisha na kazi zinazohusiana na uchimbaji pamoja na uchenjuaji wa madini huku wanawake 53 sawa na asilimia 5.3 wanatoa huduma maeneo ya uchimbaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwasimamia na kuwapatia leseni wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini ili kuongeza mchango wao kwenye sekta hii na kuimarisha uchumi wao. Wizara inaamini kuwa mwanamke akiwezeshwa, jamii nzima imewezeshwa. Ahsante sana.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Je, wanafunzi wangapi wamerudi shuleni baada ya kujifungua, tangu Serikali iruhusu wanafunzi hao kuendelea na masomo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitoa Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji shuleni wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali na mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya wanafunzi waliojiunga tena na shule baada ya kukatiza masomo walikuwa 22,844 ambapo kupitia mfumo rasmi ni 5,142 na mfumo usio rasmi ni 17,702.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa elimu kwa wanafunzi wa kike, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kusimamia utekelezaji wa Waraka tajwa, ili kuhakikisha kuwa wanafunzi waliopata ujauzito wanarejea shuleni na kutimiza ndoto zao za kielimu, ninakushukuru sana.