Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Fatma Hassan Toufiq (25 total)

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwamba hadi sasa hivi katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma pesa ambayo imeidhinishwa mwaka 2014/2015 haijatolewa na pia ya 2015/2016 haijatolewa:-
(i) Je, ni lini pesa hizi zitatolewa ili kukamilisha ujenzi huo?
(ii)Je, Serikali haioni kwamba inaingia gharama za ziada inapochelewesha miradi na kuathiri mipango ya wale wakandarasi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini Serikali itakuwa tayari kutoa pesa hizo, jibu kwa ufupi ni kwamba pesa hizo kwa kuwa zipo kwenye bajeti, zitatolewa pindi Serikali itakapopata pesa za kutosha na ambazo zitakuwa tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu variation ambayo inatokana na kuchelewa kwa miradi, kwa bahati mbaya sana kuna gharama nyingine haziepukiki kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi wa nchi yetu. Nia thabiti ipo na utekelezaji utafanyika tu pale ambapo tutaweza kuwa na fedha hizo. Kwa bahati mbaya sana kama tutakuwa tumeshaingia gharama hatutakuwa na namna ya kuzikwepa kwa kuwa ndiyo hali halisi ya uchumi wetu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Serikali haijaanza kupokea maoni, je, imepangaje kushirikisha wanawake wengi zaidi katika kutoa maoni yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Wizara itaanza lini maandalizi ya kuchukua maoni hayo? Ahsante!
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara pamoja na Tume ya Kurekebisha Sheria imepanga kulifanya zoezi hili kama tulivyoelekezwa mwanzoni kwa kina na kwa kuwafikia wananchi wengi kadri iwezekanavyo na ndiyo sababu ya Baraza la Mawaziri kusema tusileta mabadiliko hapa bila kutumia utaratibu wa white paper ambao una lengo la kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo.
Kwa hiyo, tutahakikisha wanawake wengi iwezekanavyo tunawafikia na natoa wito kwa wananchi wote na wanawake wote Tanzania pale watakaposikia mchakato umeanza naomba wajitokeza kutoa maoni kuhusu sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu maandalizi yanaanza lini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Fatma Toufiq kwamba maandalizi yalishaanza na sasa hivi tunapitia nyaraka zote za mwanzo ziendane na hali halisi ya leo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Dodoma una mifugo mingi na kunahitajika kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo; Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kiwanda hicho katika Mkoa wa Dodoma?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Toufiq. Mpango wa Serikali ni kujenga viwanda vya kuchakata nyama, huu ni mkakati pamoja na faida ya zao hili la nyama, tunalenga kutumia njia hii kuwashawishi wafugaji waweze kutoa mifugo yao kwenye sehemu za hifadhi. Kwa hiyo Sekta binafsi inahamasishwa na tuna machinjio hapa, tunategemea kutengeneza Kongwa, Ruvu, na tunaimani kwamba kwa kuwa na Kongwa na machinjio ya Dodoma kiwanda kitaweza kutangamka. Lakini nichukue fursa hii kukuomba Mheshimiwa Mbunge, ukimuona Mwekezaji yeyote mwambie aje awekeze Dodoma, mimi ninazo ekari 200, kama anataka kuwekeza aje tushirikiane nitampa eneo, ajenge sehemu ya kuchakatia, machinjio tunayo ni sehemu ya kuchakatika nyama tu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Meshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, je, Mswada huu wa Sheria ya Makao Makuu utaletwa Bungeni mwaka huu?
Swali la pili, je, bajeti kwa ajili ya mchakato huu imetengwa katika kipindi hiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama Muswada huu utaletwa mwaka huu au la kwa kweli itategemea hasa na majibu yatakayotokana na kikao cha wataalam. Kwa hiyo, kama maoni yao hayatokuwa na marekebisho mengi ni wazi kwamba muswada huu utaletwa mapema. Lakini kama maoni yao yatasababisha marekebisho makubwa katika muswada huu, basi muda unaweza ukahitajika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kuhusu suala la bajeti ni wazi kwamba bajeti haiwezi ikawa imepangwa kipindi hiki, kwa sababu sheria hiyo bado haijapita, na kwa vyovyote vile sheria itakapopitishwa Bungeni, itaweka wazi muda wa kuanza utekelezaji wake na kwa wakati huo ndio bajeti itapangwa.
MHE. FATMA HASSAN TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeshakamilisha hatua za kuwasilisha muswada huu, je, ni lini muswada huu utawasilishwa Bungeni?
Swali la pili, je, Serikali ina mpango wowote wa kuandaa mtaala wa Wasaidizi wa Kisheria ili wote waweze kupata mafunzo kulingana na mtaala huo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Fatma Toufiq kwa maswali yanayogusa wananchi wa kawaida na hili suala kwa kweli hata sisi kama Wizara tunaona ni muhimu na ndiyo maana tumelifuatilia kwa karibu na Serikali imeridhia tuweze kuja na muswada huo ambao utajadiliwa na Bunge.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya taratibu kukamilika, muswada huu hautakuja moja kwa moja Bungeni hapa lakini utapitia katika Kamati, pia tutakuwa na mjadala wa muda mrefu kabla ya kuja na text ambayo Waheshimiwa Wabunge mtakuja kuijadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maandalizi ya kutosha tumeyafanya, kwa mfano, sasa hivi tuna mitaala kabisa iliyowekwa kwa ajili ya kuwafundisha hawa Wasaidizi wa Sheria. Ni kazi kubwa imefanywa na Chama cha Wanasheria Tanganyika na ninaomba nimhakikishie tu kwamba tumejiandaa vizuri sana kubeba hili jukumu.
Tunasema hivyo kwa sababu Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongelea kuhusu usawa mbele ya sheria. Tunaamini Muswada huu unatupeleka Watanzania karibu zaidi katika kukidhi mahitaji ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili uwepo usawa wa kutosha kabisa mbele ya sheria.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.
Je, Serikali imeandaa utaratibu wowote wa kuwakagua watoto ambao wapo chini ya umri wa miaka mitano katika kliniki au wasiohudhuria kliniki ili kuweza kupata takwimu sahihi za watoto ambao wamekeketwa chini ya miaka mitano ili kufahamu ukubwa wa tatizo ukoje? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba katika mfumo wa kutoa huduma za afya nchini watoto wote chini ya umri wa miaka mitano wanapaswa kuhudhuria kliniki ya RCH ili wapate chanjo mbalimbali lakini pia wazazi wao waweze kufikiwa na elimu mbali mbali ambazo zinatolewa kila siku kabla ya kuanza kwa kliniki hizo.
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na utaratibu huo watoto wote wachanga sasa hivi kuna mpango maalum chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa kuwaelimisha wauguzi wote nchini kufanya ukaguzi maalum wa watoto hususani wa kike kuhusiana na mambo ya ukeketaji ili tuweze kuwabaini wazazi ambao wamewapeleka watoto wao wachanga kufanyiwa ukeketaji.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo huduma hiyo sasa ipo na inaendelea kutolewa nchini. Nitoe onyo kwa wazazi wote ambao wanaendelea na vitendo hivi, kwamba wakikamatwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi utaratibu umehama badala ya kuwakeketa mabinti wakubwa, sasa hivi wazazi wamegundua kwamba wawakekete watoto wachanga. Jambo hili halikubaliki na tutachukua hatua kali, na ndiyo maana tumeweka sasa mkakati wa kutoa elimu kwa wauguzi wafanye ukaguzi maalum kwa watoto wa kike kama wamekeketwa ama la, kwa hiyo utaratibu upo.
MHE FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa
Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI na imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya mfuko huo, je, Serikali haioni umuhimu wa kutumia sehemu ya pesa za mfuko huo kwa kutoa ruzuku kwa kiwanda hicho?
Swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kuwa uzalishaji unaanza mapema zaidi ili kupunguza gharama za kuagiza dawa za ARV kutoka nje? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye Mfuko huu wa UKIMWI kwa mujibu wa sheria uko chini ya Ofisi hiyo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nijibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye ni mdau mkubwa tunayefanya naye kazi kwa pamoja kushughulikia masuala haya ya tatizo la UKIMWI nchini kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko huu ambao unashughulikia matatizo ya UKIMWI (ATF) umeanzishwa kwa mujibu wa sheria na sheria imeweka mamlaka kwa bodi inayosimamia mfuko huo kutoa miongozo na kuangalia ni kwa namna gani fedha zitakazopatikana kwenye mfuko
zitatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazoendana na tatizo la UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi imeshagawa utaratibu wa matumizi ya fedha hizo kwa asilimia 60 kutumika kwenye matibabu, dawa na vitendea kazi na asilimia nyingine 25 na 15 kwa kazi nyingine.
Kwa hiyo, kwa utaratibu ama ushauri ambao ameutoa Mheshimiwa Mbunge, tutarudi kuwasiliana na bodi kuona kama katika zile asilimia 60 zinaweza pia zikatumika katika kusaidia utengenezaji wa dawa kwenye nchi yetu ya Tanzania kama mfuko utakuwa umeshajitosheleza kwa kiasi kikubwa na kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kupokea ushauri wa kuboresha matumizi ya fedha ya mfuko huo kadiri inavyoonekana inafaa.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru
Mheshimiwa Jenista kwa kujibu sehemu ya kwanza ya swali hili, kati ya maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fatma Toufiq.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha tunawekeza katika uzalishaji
wa dawa za ARV nchini Tanzania? Nataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hadi sasa tuna viwanda
vitano, wawekezaji watano ambao wameonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uzalishaji wa viwanda vya dawa
nchini na wiki iliyopita tulikuwa pale Bagamoyo, Zinga Phamaceutical Company na moja ya dawa ambayo
watazalisha ni pamoja na dawa za kupunguza makali ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka tu kumthibitishia tunafanya kazi pia pamoja na Mheshimiwa
Charles Mwijage kuhakikisha kwamba tunazalisha dawa zetu zote ndani ya nchi badala ya kununua dawa nje ya nchi kama tunavyofanya sasa hivi.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa, Serikali imeona umuhimu wa kufufua na kurejesha majengo ya maendeleo ya jamii. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupata wataalam wa kutosha ili kuhudumu katika majengo hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, hali ya maisha imebadilika sana na wananchi wengi wana msongo wa mawazo na matatizo mbalimbali, mfano, masuala ya ukatili, hivyo wanahitaji wataalam wa unasihi na nasaha. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka muda maalum ili kuharakisha Halmashauri zote nchini zifufue majengo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya watumishi katika Sekta nzima ya Maendeleo ya Jamii na hivi sasa tuna upungufu wa asilimia takribani 61. Hata hivyo, Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili katika mafunzo ya watumishi katika sekta hii, mpaka sasa hivi tumeongeza udahili kwa kiasi kikubwa sana. Lengo ni kuhakikisha kwamba sasa huu upungufu tulionao tunaweza tukapata watumishi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba, kutokana na kuonekana kuna wananchi wengi sasa hivi wamekuwa na msongo wa mawazo, tunapokea ushauri huu nasi katika sekta ya afya tutaangalia njia nzuri zaidi ya kuweza kulifanyia kazi jambo hilo.(Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na tatizo la uwekaji kiholela wa matuta kwenye baadhi ya barabara za mitaani na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa vyombo vya moto na ikizingatiwa kwamba wananchi hawa hawana utalaam wowote. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kadhia hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokuwa namueleza Mheshimiwa Joseph Mhagama, ninatoa wito kwa Watanzania, barabara hizi zinajengwa kwa gharama kubwa sana ya pesa za Watanzania. Tunapoweka matuta bila vyombo vinavyohusika hasa TANROADS kufahamu tunaharibu barabara zetu ambazo tumezijenga kwa gharama kubwa sana. Kitu ambacho Serikali tunakifanya, tunapanga mkakati wa kuwasiliana na Wizara ya mambo ya ndani kitengo cha usalama barabarani kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi namna ya matumizi bora ya barabara bila kuleta ajali kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba sana Watanzania wasijichukulie maamuzi ya kuweka matuta barabarani hata kwa kugongwa kwa mbuzi tu isipokuwa wawasiliane na taasisi zinazohusika tusaidie kama kuna umuhimu wa kuweka matuta tutaweka, lakini kwa utaratibu ambao unaeleweka.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo lililopo katika jimbo la Kibiti linafanana na baadhi ya maeneo katika mji wa Dodoma, kwamba baadhi ya mitaa mfano Nkuhungu, Ilazo, Makole barabara zake za mitaa zipo katika hali duni sana. Je, Serikali itarekebisha lini barabara hizi ukizingatia kwamba sasa hivi Dodoma ni Makao Makuu? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu wazi hoja anayozungumza Mheshimiwa Fatma Toufiq kwamba ni kweli ni hoja halisia. Hii ni kwa sababu mji wetu wa Dodoma sasa hivi kwa maamuzi sahihi yaliyofanywa Serikali ni Makao Makuu yetu. Hata hivyo kupitia miradi yetu ambayo tunaendelea nayo hapa Dodoma, sawasawa na miradi ambayo tunaendelea nayo katika miji saba katika ile Strategic City Project; kazi hii inaendelea awamu kwa awamu. Wabunge nadhani mnakuwa ni mashahidi. Wabunge waliofika mwaka 2010 hapa Dodoma wakifanya ulinganifu na hali ilivyo hivi sasa ni tofauti sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tutaendelea kujenga miundombinu hii. Sasa hivi kuna ring road karibuni zitakuwa tatu. Kuna hii ambayo hata ukifika kule inakatisha, vilevile tuna barabara zetu za mitaa na wataalam wetu wanaendelea na kazi hiyo. Lengo letu ni kwamba tukifika mwaka 2020 Jiji la Dodoma litakuwa ni tofauti sana kwa sababu mpango wetu huo ambao unaenda mpaka mwaka 2020 utahakikisha mji wa Dodoma wote mitaa yake yote itakuwa na kiwango cha barabara za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo si lami peke yake isipokuwa tutapeleka na mataa pamoja na mifereji yote ya kuondoa maji kuhakikisha jiji hili linakuwa jiji la mfano ambao ndio mpango hasa wa Serikali yetu ilivyoamua.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hizi ajali za barabarani zinatokana na uzembe wa baadhi ya madereva na baadhi ya madereva kutumia simu wakati wakiwa wanatumia vyombo ya moto. Je, Serikali ina mkakati gani wa kurekebisha Sheria ya Usalama Barabarani ili kuwachukulia hatua kali zaidi hawa madereva ambao wamekuwa wakitumia simu wakati wakitumia vyombo vya moto? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kweli kuna kiwango kikubwa cha ajali zinatokea kutokana na uzembe. Ukiangalia hata kwenye kumbukumbu zaidi takribani ya matukio zaidi ya 1,500 yanatokana na uzembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kile alichokisema cha kurekebisha sheria na kuchukua hatua tunaendelea na utaratibu huo na tunasema tunakokwenda tutaanza hata kutumia taratibu ambazo nchi zingine wanatumia kwa ku- count down dereva ambaye anapatikana sana na makosa aweze kukosa sifa za kuendelea kumiliki leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunalifanyia kazi wazo lake na nimpongeze sana kwa kuguswa na jambo hili kwa sababu limekuwa likisababisha hasara sana kwa familia na kwa Taifa. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante. nashukuru sana kwa majibu ambayo yametolewa na Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mwekezaji aliyechukuwa DOWICO alizembea na kufunga kiwanda hicho, hivyo kusababisha uzalishaji mvinyo bora wa Dodoma kutokupatikana katika soko. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumpatia mwekezaji mwingine tofauti na huyu aliyepo ili aweze kukifufua kiwanda hicho?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imekuwa katika mpango wa kuwezesha uanzishwaji wa Kiwanda cha Kusindika mazao ya Zabibu katika Wilaya ya Chamwino kwa kushirikiana na mfuko wa GEPF. Je, ni hatua gani za haraka zilizochukuliwa na Serikali ili kuharakisha ujenzi wa kiwanda hiki ili wakulima wa zao la zabibu waweze kupata soko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU - K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza la kumtafuta mwekezaji mwingine, ndani ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Viwanda TIRDO na kwa kushirikiana pia na Ofisi ya Msajili wa Hazina tumeanzisha kitu kinaitwa Technical Audit na lengo lake kubwa ni kwenda kuvifuatilia viwanda hivi ambavyo vilibinafsishwa na havifanyi kazi na kuvifuatilia kuona namna gani vitaanza kufanya kazi kwa kupitia utaratibu huo wa utafiti ambao unafanyika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tunawasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi kwamba tayari ukarabati umeanza, kwa hiyo tutafanya hiyo technical audit ya kufuatilia kuona wanaanza lini kazi hii na baadaye tutatoa taarifa namna ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba jambo hili ni kubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma, hasa ukiangalia kwamba zabibu ndio zao pekee ambalo linategemewa sana hapa Dodoma na Dodoma ndio sehemu pekee duniani ambako kuna uwezo wa kuvuna zabibu hii mara mbili. Israel wamejaribu, Afrika Kusini wamejaribu imeshindikana, kwa hiyo tunafahamu umuhimu wa zao hili kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Spika, nimwondoa hofu Mheshimiwa Mbunge tu kwamba, hii pia ni Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwavutia wawekezaji wengi kujenga viwanda vikubwa hasa ukizingatia kwamba mpaka Machi, 2017 tayari tumeweza kuvutia viwanda vikubwa 393 ambavyo vimesajiliwa na tayari vimeshaweka kiasi cha shilingi trillion tano. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, hata hili nalo litafanyika
Mheshimiwa Spika, la pili ameuliza kuhusu Kiwanda cha Mvinyo pale Chamwino. Nafahamu wakulima wa Dodoma wanategemea sana viwanda hivi vikubwa kwa ajili ya soko la zabibu, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge katika utaratibu wa uwekezaji katika viwanda, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, iliamua kuingia moja kwa moja katika uwekezaji huu. Pale Chamwino Mfuko wa GEPF, WCEF pamoja na TIB kwa pamoja watafanya uwekezaji wa kiwanda cha mvinyo.
Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza hivi sasa tayari Bodi za Mifuko hii zimekwisha-approve kiasi cha shilingi bilioni 26 kwa ajili ya kwenda kuanza ujenzi wa kiwanda hiki. Niwaondoe hofu wananchi wa Mkoa wa Dodoma, watapata fursa ya masoko ya zabibu na ukiongozwa na wewe Mheshimiwa Spika, ambaye ni mkulima pia. (Makofi/Kicheko)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwaficha watoto ambao wamekuwa na ulemavu na hivyo kukosa haki za msingi kama afya na elimu. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu wazazi na walezi hawa ambao wanawakosesha hawa watoto? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kuhusiana na umuhimu wa kwamba kila mtoto mwenye ulemavu anawajibika ama ana fursa sawa na watoto wengine ambao hawana ulemavu. Kwa kuliona hilo hivi ninavyozungumza tayari kuna zoezi linaendelea la kuwatambua watoto wenye ulemavu kila mahali nchini ili kuona sasa ni jinsi ya kuhakikisha kwamba hawafichwi tena ndani na wanapatiwa huduma kama watoto wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili linafanyika. Hata hivyo niendelee kutoa rai kwa wazazi wote nchini pamoja na walezi kuhakikisha kwamba watoto wenye ulemavu wanawapatia fursa sawa na watoto ambao hawana ulemavu. Mtu mwenye ulemavu ni sawa na mtu mwingine ambaye hana ulemavu, akiwezeshwa anakuwa anaweza. Kwa hiyo, nitoe rai sana na niwaombe wazazi pamoja na walezi kulizingatia hilo kuona kwamba watu wenye ulemavu wako sawa pamoja na watu ambao hawana ulemavu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa ukosefu wa mabweni ni tatizo la nchi nzima na hasa katika shule za sekondari za kata, hivyo kufanya baadhi ya wanafunzi kupanga katika nyumba za watu binafsi; je, Serikali haioni umefikia wakati kuhamasisha wadau mbalimbali wa elimu kujenga hostel karibu na shule ili kuepuka kadhia hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalitambua sana tatizo la mabweni katika shule za sekondari za kata. Lengo la kujenga shule za sekondari za kata ilikuwa ni kuwawezesha watoto ambao wako ndani ya kata waweze kusoma, lakini tatizo ni kwamba kuna baadhi ya vijiji kweli viko mbali sana na Makao Makuu ya Kata au mbali sana na eneo ambalo ipo shule. Kwa hiyo, kuna tatizo kwamba wanafunzi wengi wamekuwa wakipanga nyumba kwa sababu hawawezi kutembea kilometa labda 15,20 kutoka nyumbani kwao kwenda katika shule kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo tatizo tunalielewa na ninaungana naye na tutaendelea kuhimiza wadau wajenge mabweni na hostel karibu na shule hizi ili kusudi ziweze kutoa huduma nzuri kwa watoto na hasa watoto wa kike waweze kuepuka matatizo mengine ambayo yanawapata kupanga katika nyumba za watu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa suala la ubakaji na ulawiti linazidi kuongezeka; je Serikali haioni imefika wakati wa kuwa na hotline maalum ya kutoa taarifa za ukatili kwa wale ambao wanapata tatizo hilo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeweka mpango mzuri wa kuwa na dawati la jinsia. Kwa nini Serikali isiweke utaratibu wataalam hawa wakaenda kutoa elimu katika shule zetu mbalimbali hapa nchini? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi maswali yake yote mawili ni kutoa ushauri na mapendekezo, nimhakikishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mapendekezo ambayo anayotoa, nitayafikisha Serikalini tuone namna ya kuyafanyia kazi. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la wahamiaji haramu kutoka Ethiopia linaongezeka, je, Serikali haioni imefikia wakati wa kulizungumza suala hili kidiplomasia kati ya Tanzania na Ethiopia ili kuweka utaratibu maalum kuepuka kuwaweka magerezani ambapo huligharimu Taifa? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu sahihi aliyoyatoa tangu mwanzo na niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa kulileta swali hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ijumaa na Jumamosi tulikuwa na vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vinavyoshughulikia masuala ya kiusalama ya kisekta na kwenye maazimio tuliyoyapitisha ni pamoja jambo hili kuwa jambo la mipaka yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tofauti na ilivyo sasa ambako nchi zingine zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwepo Kenya wanapopitia zaidi kwao wao hili jambo halikuwa kama tatizo walikuwa wanapita tu kama mtembeaji mwingine yeyote aliyeko ndani ya nchi husika. Kwa hiyo, kwa sasa tumesema hili ni jambo ambalo tutalioanisha na mambo mengine ambayo yanazuiwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ili hawa watu waweze kuanza kuzuiwa kwenye mipaka ya Kenya na Sudan Kusini tofauti na ilivyo sasa ambapo huwa wanapata kipingamizi wanapofika Tanzania na nchi zingine zote wanakuwa wameshapita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunalipokea na hilo jambo ambalo amelisemea la kuongea nanchi husika ambao wahamiaji hawa wanatoka ambapo ni Ethiopia, Eritrea pamoja na Somalia. Hiyo tutaifanya kwa kuanzia na Balozi zao zilizopo hapa ili jambo hilo liweze kuongewa pia katika nchi zao.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza mswali ya nyongeza, nina maswali mawili ya nyongeza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa Wizara haidhibiti kope bandia na kucha bandia lakini bado zina madhara makubwa sana kwa watumiaji hasa wanawake.
Je, Serikali haioni umefikia wakati kupitia Wizara ya Afya na TFDA kufanya utafiti ili kubaini ukubwa wa tatizo?(Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kuwa wagonjwa takribani 700 hupelekwa Muhimbili kutokana na athari za kujibadili rangi.
Je, Serikali haioni umefikia wakati kuwa na mpango kabambe wa kuihabarisha jamii na hasa wanawake kubaki na rangi zao za asili na kuepuka kutumia vipodozi vyenye madhara na hasa wanaume wawe ndiyo waelimishaji? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kufanya tafiti na kubaini madhara ya kucha na kope bandia na baada ya hapo sasa tutaanza kuwa na mfumo wa kuwa na takwimu mbalimbali kuhusiana na madhara haya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ameuliza je, Serikali hatuoni umuhimu wa kuhabarisha jamii kuhusiana na vipodozi ambavyo vinabadilisha rangi ya mwili. Naomba nitumie fursa hii kutoa elimu kidogo kwa Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu alituumba na hizi ngozi zetu hizi kwa makusudi yake mahsusi. Kwanza ngozi hizi ni moja ya kinga ya mionzi ya ultraviolets ambayo ngozi inatukinga dhidi yake, lakini pili, ngozi hii ni sehemu ya kinga za mwili ama kizuizi cha kinga ya mwili pale wadudu ama bakteria ama vijidudu vya aina yoyote vinapotaka kuingia katika miili yetu vinazuiliwa na ngozi zetu. Tunapokuwa tunajichubua ngozi zetu tunaziondoa kinga hizi na tunaondoa kinga hii dhidi ya miale hi ya ultraviolet, lakini tunaondoa kinga hii dhidi ya vimelea vya wadudu hatari.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mtu ambaye anafanya kujichubua ngozi anaingia katika madhara ya magonjwa ya ngozi, madhara ya kupata saratani ambayo inatokana na vimelea vilevile miale ya jua. Kwa hiyo, mimi naomba kutoa rai tu kwa Watanzania wote ambao wanatusikiliza na Waheshimiwa Wabunge ngozi zetu za asili ni urembo uliotosha, kama Wabunge tulizingatie hilo na wanaume tushiriki, rangi ya asili... naishia hapo (Makofi/Kicheko)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya shule za msingi zina vituo vya ufundi stadi, mfano, katika Wilaya ya Chamwino, vituo hivyo viko katika Shule ya Msingi Mvumi Mission na Shule ya Msingi Chamwino lakini hakuna vifaa wala walimu wa kutosha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvifufua vituo hivyo siyo kwa Wilaya ya Chamwino tu lakini katika shule zote za msingi ambazo ziko Tanzania hii? Ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLIJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Fatma Toufiq, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru kwa swali lake zuri kwa sababu ni kweli zile shule zipo lakini kwa kweli hali yake haijakaa vizuri, niliona nilipozitembelea. Kwa hiyo, tayari Serikali imeliona na kwa kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi hapa Nchini (ESPJ) ambao Wizara yangu inautekeleza kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, tutafanya tathmini ya shule hizo na kwa awamu tutaanza kuzifanyia maboresho kwa kuzipelekea vifaa.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa tatizo lililopo katika Mkoa wa Mtwara linafanana na kukatika kwa umeme katika eneo la Kigogo Mkoani Dar es Salaam tena bila taarifa; je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kadhia hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Toufiq amekuwa akifuatilia mara kwa mara suala hili la kukatika kwa umeme kwa maeneo ya Kigogo. Kupitia mpango wa Serikali na Shirika lake la TANESCO, tunajenga sub-station maeneo ya Mburahati ambapo sub-station hiyo itasaidia kumaliza kabisa tatizo la kukatika kwa umeme maeneo ya Kigogo. Nakushukuru.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa nami kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Chuo cha Ufundi VETA, Dodoma kilijengwa muda mrefu na kilikidhi kwa wakati ule na sasa hivi kuna ongezeko kubwa sana la vijana na miundombinu bado ni ile ile; je, Serikali haioni kwamba umefikia wakati wa kuongeza majengo na miundombinu ili kiendane na hadhi ya Jiji? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali ina mpango wa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika vyuo vyote nchini, na sio Vyuo vya Ufundi tu. Kwa hiyo, tutaendelea kuangalia vyuo vile ambavyo vinahitaji matengenezo na ukarabati pamoja na kuongezewa Majengo, ili tuweze kufanya hivyo kadiri bajeti itakavyoturuhusu.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu kwamba, hata Chuo cha Dodoma nacho ni moja kati ya vyuo tulivyonavyo na kwa vyovyote vile kulingana na upatikanaji wa fedha tutaangalia uwezekano wa kukipanua.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa soka la wanawake limekuwa likifanya vizuri sana hapa nchini na kimataifa, lakini soka hili halina wadhamini wa kulidhamini. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhamasisha wadau mbalimbali ili waweze kulidhamini soka hili la wanawake nchini? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Toufiq, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, soka la wanawake pamoja na kwamba limechelewa sana kupewa uzito stahili katika nchi yetu, tayari lina wadhamini. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Toufiq kwamba kila mwaka tunazidi kuongeza juhudi za kuwapata wadhamini. Moja ya nyenzo kuu ya kuwapata wadhamini wengi zaidi ni kuhakikisha kwamba tunaomba au tunaingia mikataba na kampuni mbalimbali za utangazaji ili soka hiyo iweze kuonyeshwa live katika luninga zetu na hata kutangazwa katika redio mbalimbali.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa maeneo ya uchimbaji madini (mining sites) katika Mkoa wa Dodoma yako zaidi ya 700 na kuna baadhi ya maeneo hayajaanza kuchimbwa kabisa madini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza kwa wawekezaji ili kusudi waweze kuja kuchimba katika Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, tuna maombi mengi sana ambayo wachimbaji wadogo na wakubwa wameomba katika Wizara yetu kupitia Tume ya Madini. Hapa Dodoma kuna wachimbaji wadogo wadogo wengi wameomba leseni hizo, kwa maana ya kwamba wanataka au wameonesha nia ya kuchimba. Sisi kama Serikali hivi karibuni ile Tume imeshaanza kufanya kazi na zile leseni tutazitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema toka mwanzo kwamba tunataka tuwawezeshe wachimbaji wadogo. Mradi katika Wizara yetu ambao ni mradi unaopata fedha kutoka Word Bank, yaani Mradi wa SMRP; mradi huu tunaangalia namna bora sasa ya kuwawezesha wachimbaji wadogo, kwa maana ya kuwasaidia kuwapa teknolojia, elimu na mitaji ili waweze kuchimba. Pia wachimbaji wa Mkoa wa Dodoma na wao wamo kwa sababu sisi tunafanya kazi nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa wachimbaji wadogo ambao wako katika Mkoa wa Dodoma, nipende tu kusema, walioonesha nia au walioomba maombi ya leseni, leseni zitatoka na wachimbaji ambao wanataka kuomba leseni sasa hivi Tume imeanza kufanya kazi walete maombi hayo katika Wizara yetu, tuweze kuwapa leseni, na tuangalie namna ya kuwasaidia ili waweze kuchimba na Wizara iko tayari na tunaendelea na kazi hiyo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Dodoma ni miongoni ya mikoa yenye mifugo mingi sana ikiwemo ng’ombe na kuna nyakati wafugaji wanakosa soko. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha wadau na wawekezaji mbalimbali ili waweze kujenga Kiwanda cha Maziwa na collection centre katika Mkoa wa Dodoma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Toufiq, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wetu ni kuhakikisha kwanza vile viwanda vyetu tulivyonavyo vinafanya kazi ya kuchakata mazao ya mifugo. Hapa Dodoma tunacho kiwanda kikubwa cha TMC ambacho hivi karibuni utendaji wake wa kazi haukuwa mzuri sana lakini Wizara tumeingilia kati tunahakikisha kwamba kiwanda chetu hiki kinafanya kazi nzuri ya uchakataji wa mazao ya mifugo kwa maana ya uchinjaji na hatimaye kutengeneza zile nyama kwa ajili hata ya kuuza nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake ni kujua namna tunavyoweza kuwavutia wawekezaji wa Kiwanda cha Maziwa hapa Dodoma. Nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wana Dodoma wote kwamba ombi hili la kuhakikisha tunakuwa na Kiwanda cha Maziwa hapa Dodoma tunalichukua na tutahakikisha kwamba Dodoma na yenyewe pia inakuwa centre nzuri ya kuhakikisha tunatengeneza mazao ya mifungo ikiwemo maziwa na kuyasambaza kote katika nchi yetu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza na namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake lakini nina maswali yangu mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wengi hawafahamu waende wapi pale matatizo wanapohitaji unasihi na hii imejidhihirisha hivi karibuni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza wanawake waliotelekezwa waende kwake, wamejitokeza wengi sana, sambamba na hilo na wanaume pia walijitokeza. Sasa nilitaka kufahamu je, Serikali haioni imefikia wakati wa kuhabarisha jamii kwamba huduma hizi zinatolewa ili waweze kupata huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii wako katika ngazi mbalimbali, je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga siku maalum walau siku mbili kwa wiki na kutenga maeneo maalum ili wananchi waweze kwenda kupata ushauri wa unasihi badala ya kusubiri kwenda kipindi cha muda wa kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kuhusiana na suala la uelewa wa wananchi, tunapokea ushauri wake na tutaufanyia kazi kwa lengo la kujengea uelewa na nitoe rai tu kwa wananchi kwamba huduma za ustawi wa jamii zipo katika Halmashauri zote na katika baadhi ya maeneo hadi katika ngazi ya kata. Wanapokuwa na changamoto zinahusiana na masuala ya migogoro ya familia masuala ya ustawi, watoto yatima, waende katika ofisi za Halmashauri ama za ngazi ya kata kuweza kupata huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili katika swali lake la nyongeza ameulizia kwamba kwa nini Serikali isitenge siku maalum na maeneo maalum ili huduma hii iweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Maafisa Ustawi wa Jamii ni waajiriwa wa Serikali na wapo muda wote kuweza kutoa huduma hizi kwa hiyo, huduma hizi zinatolewa siku zote za kazi katika muda wa masaa ya kazi katika maeneo husika ngazi ya Halmashauri, kata na mitaa ambapo Maafisa Ustawi wa Jamii wapo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Kijiji cha Kwahemu, Kata ya Haneti, kuna vikundi 16 ambavyo vina wachimbaji zaidi ya 200 lakini havina maeneo ya kuchimba madini licha ya kupeleka maombi Tume ya Madini. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kuwapa maeneo wachimbaji hawa wadogo ili waweze kujikimu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maeneo ya Kwahemu (Haneti), kuna uchimbaji mdogo mdogo wa madini ya vito. Katika eneo lile kuna leseni moja inamilikiwa na Bwana Dimitri, raia mmoja wa kigeni lakini kuna maeneo mengine ambayo yako katika utafiti kwa maana ya PL. Kama nilivyosema siku zilizopita ni kwamba tunafuatilia zile PL zote ambazo hazifanyiwi kazi tutazichukua na tutazifuta na tutawapa wachimbaji wadogo wadogo waweze kuchimba na waweze kujipatia riziki kama tulivyojipangia katika Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge watu wa Kwahemu maeneo ya Haneti tuna mpango kabambe wa kuwapa maeneo ya kuchimba. Wale wachimbaji walioko pale nilishafika na wakatoa kero zao na mimi kwa kweli naendelea kuzifuatilia kwa maana ya kuzitatua na tunahakikisha kwamba hawa watu wa Kwahemu watapata leseni na wataweza kupata nafasi ya kuchimba.