Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Felister Aloyce Bura (7 total)

MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Eneo la Msalato lenye kilometa tisa katika ujenzi wa barabara ya Dodoma – Kondoa – Babati kwa kiwango cha lami bado halijakamilika.
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kipande hicho kilichobaki cha Dodoma – Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 8.65 cha eneo la Msalato ni sehemu ya barabara ya Dodoma – Kondoa hadi Babati yenye urefu wa kilometa 251. Barabara hii inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni barabara ya kutoka Dodoma mpaka Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65; sehemu ya pili, ni barabara ya kutoka Mayamaya mpaka Mela yenye urefu wa kilometa 99.35 na sehemu ya tatu, ni barabara ya kutoka Mela mpaka Bonga yenye urefu wa kilometa 88.8. Aidha, barabara ya kutoka Bonga hadi Babati yenye urefu wa kilometa 19.6 ilishajengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa sehemu ya Dodoma hadi Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65 unaendelea. Utekelezaji umefikia asilimia 80 ambapo jumla ya kilometa 35 zimeshawekwa lami na zimebakia kilometa 8.65 katika eneo la Msalato.
Mheshimiwa Spika, ujenzi ulikuwa umesimama kwa muda kutokana na Mkandarasi kutokulipwa kwa wakati. Kwa sasa Serikali inaendelea kulipa madai ya Wakandarasi akiwemo Mkandarasi anayejenga barabara hii ya Dodoma hadi Mayamaya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea malipo, Mkandarasi anayejenga barabara hii sasa yuko kwenye maandalizi ya kuanza ujenzi na kazi inatarajia kukamilika mwezi Desemba, 2016.
Kituo cha afya cha Chamwino Ikulu kinahudumia zaidi ya Kata 20 za Wilaya ya Chamwino na wanawake na watoto wa kata hizo wanategemea sana huduma za kituo hicho, lakini hakina vifaa tiba muhimu kama vile ultra sound:-
Je, ni lini Serikali itanunua ultra sound kwa ajili ya kituo hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kituo cha afya cha Chamwino hakina ultra sound kwa ajili ya huduma za mama na wajawazito na watoto. Kifaa hicho kinagharimu shilingi milioni 72.0 ambazo hazijawekwa kwenye bajeti ya Halmashauri kutokana na ukomo wa bajeti. Hata hivyo Halmashauri imewasilisha maombi ya mkopo wa shilingi milioni 72 katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kupata fedha zitakazowezesha kifaa hicho kununuliwa, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, wagonjwa wanao hitaji huduma hiyo kwa sasa, wanapewa Rufaa kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo huduma hiyo inapatikana.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Benki ya wanawake nchini ilianzishwa kwa nia ya kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa haraka na kwa riba nafuu.
Je, ni wanawake wangapi wameshanufaika na mikopo ya benki hiyo kwa Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) ilianzishwa mwaka 2009 katika misingi ya kujiendesha kibiashara ikiwa na jukumu mahsusi la kuwapatia wanawake mikopo yenye masharti nafuu na kwa haraka. Kimsingi benki hii inatoa huduma zake kwa wananchi wote bila ubaguzi na ndiyo maana tunasema hii ni benki pekee kwa wote. Benki ya Wanawake kwa Mkoa wa Dodoma ilianza kutoa huduma zake Disemba, 2012 ikiwa na vituo vinne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Septemba, 2016 benki kwa Mkoa wa Dodoma ilikuwa jumla ya vituo 18. Walionufaika na mikopo katika Benki ya Wanawake katika Mkoa wa Dodoma ni watu 19,740 kwa kipindi cha kuanzia Disemba, 2012 hadi Septemba, 2016; mikopo hii ina thamani ya shilingi 6,231,891,236. Kati ya hao wanawake waliopata mikopo hiyo ni 16,676 yenye thamani ya shilingi 5,063,765,641 sawa na asilimia 81 ya mikopo yote na wanaume wakiwa 3,064 ambao wamepata mikopo yenye thamani ya shilingi 1,168,125,595 sawa na asilimia 19.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo kwa lengo la kusaidia wakulima wakubwa na wadogo kupata mikopo ya pembejeo kwa haraka:-
Je, ni lini Benki hiyo itaanza kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilianza rasmi shughuli zake mwishoni mwa mwaka 2015. Hadi kufikia Desemba 2016, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilikuwa imeshatoa mikopo ya jumla ya Sh. 6,489,521,120/= kwa miradi 20 ya kilimo katika Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga. Sambamba na utoaji wa mikopo, benki inatoa mafunzo kwa wakulima na hadi sasa imeshafanya mafunzo kwa vikundi 336 vya wakulima wadogo wadogo vyenye jumla ya wanachama 44,400 katika Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Dodoma, Benki imepata nafasi kwa ajili ya kufungua ofisi katika jengo jipya la PSPF ambapo inasubiri kukabidhiwa ofisi hiyo Julai, 2017, baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi. Aidha, benki imeshaanza kutafuta miradi ya kilimo ya wakulima wadogo wadogo yenye sifa za kukopesheka iliyopo katika Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha azma hii, benki imemwandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kumwomba aipatie miradi mizuri ya kilimo ambayo mkoa unapendekeza Benki iifikirie katika zoezi la kutoa mikopo. Pamoja na hayo, benki inaandaa utaratibu wa mafunzo yatakayotolewa kwa wakulima wadogo wadogo nchi nzima ikianzia na Mkoa wa Dodoma. Ni matumaini ya benki kuwa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo na wakati kwenye Mkoa wa Dodoma itaanza kutolewa mwishoni mwa mwaka 2017.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 aliyekuwa mgombea Urais kupitia tiketi ya CCM Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliwaahidi wananchi wa Kongwa na Mpwapwa kujenga barabara ya Mbande – Kongwa - Mpwapwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa yenye urefu wa kilometa 49.19 ilifanyiwa usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami na usanifu ulikamilika mwaka 2013. Baada ya kukamilika kwa usanifu Serikali imeanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu ambapo mwezi Julai, 2017 sehemu ya barabara yenye urefu wa kilometa 11.7 kutoka Mbande kuelekea Kongwa ilianza kujengwa. Hadi mwishoni wa mwezi Oktoba, 2017 kiasi cha kilometa tano za sehemu ya barabara ya Mbande - Kongwa zimekamilika kujenga hadi tabaka la juu (basic course). Mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Mkandarasi anayejenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino anaidai Serikali shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha jengo la Halmashauri.
Je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi huyo kiasi hicho cha fedha ili ujenzi huo uweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya Mkandarasi aliyejenga Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mpaka sasa ni shilingi milioni 758.2 yakiwemo madai yaliyohakikiwa ya shilingi milioni 368.0 na madai ambayo hayajahakikiwa ya shilingi milioni 390.2 ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/ 2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zinapaswa zitumike kulipa deni ambalo Mkandarasi anadai kabla ya kuendelea na kazi nyingine. Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo la Halmashauri unakamilika.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa maporomoko ya Ntomoko Wilayani Kondoa?
NAIBU WA WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Ntomoko ulilenga kutoa huduma katika vijiji 18 vya Wilaya ya Kondoa na Chemba lakini kutokana na uwezo mdogo wa chanzo kumesababisha kutokidhi mahitaji ya huduma ya maji katika vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi Novemba 2017 Wiraza kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI iliunda timu ya pamoja ya Wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa kina wa mradi huo pamoja na kutafuta chanzo kingine mbadala ili kuongeza wingi wa maji utakaokidhi mahitaji ya wananchi katika vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mapitio ya usanifu wa kina timu hiyo ilibaini kuwa chanzo cha Ntomoko hakina tena uwezo wa kuhudumia vijiji hivyo. Ili kukidhi mahitaji ya maji kwa vijiji hivyo, Serikali imepanga kukarabati miundombinu iliyoko pamoja na kujenga bwawa lenye mita za ujazo milioni 2.8 kwenye eneo la Kisangali katika kijiji cha Mwisanga litakalotoa huduma kwa vijiji vyote 18. Usanifu wa bwawa hilo pamoja na bomba kuu kutoka kwenye chanzo hadi makutano ya kijiji cha Lusangi umeshafanyika. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto zilizojitokea awali juu ya ukarabati wa miundombinu ya mradi huo, Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) kutekeleza ukarabati wa mradi huo badala ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.